Kwa hili, nalipongeza shirika la Twaweza

Muktasari:

  • Haikuwa kama ziara za watafiti kuuliza kero za wananchi na kuondoka na baadaye kutoa mrejesho kama ilivyozoeleka kwa makundi mengi ya kitafiti.

Mwishoni mwa Mei, nilikuwa sehemu ya timu ya Twaweza iliyofanya ziara ya siku tatu katika baadhi ya vijiji vya wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Haikuwa kama ziara za watafiti kuuliza kero za wananchi na kuondoka na baadaye kutoa mrejesho kama ilivyozoeleka kwa makundi mengi ya kitafiti.

Katika ziara hii, tulikwenda kuishi na wananchi, hatukufikia kwenye nyumba za wageni. Tulienda wanapoishi wananchi, tuliishi kama wanavyoishi, tulikula wanachokula hata kujilazimisha kufikiri wanachofikiri kuhusu maisha.

Tulikuwa sehemu ya familia maskini kabisa ambazo pengine zingetarajia sisi kama wageni kuwa watoa mawazo kuhusu maendeleo na maisha. Tulijishusha na kuwa wasikilizaji wa kile wanachokifikiri kuhusu ustawi wao na maendeleo ya nchi kwa jumla.

Huu ulikuwa uzoefu mpya katika maisha yangu, ulionifanya nitafakari ni taasisi au watu wangapi wanaoweza kufanya hiki walichofanya Twaweza, asasi iliyojikita katika kufanya tafiti mbalimbali za kimaendeleo.

Nilijipa jukumu la kutafakari kwa kuwa uzoefu unaonyesha wananchi vijijini hasa wa kada za chini, wamedharauliwa. Tunafikiri wananchi hawa hawawezi kufikiri hivyo kuhitaji maagizo pekee kwa ajili ya utekelezaji.

Kuna ushahidi mwingi katika maeneo mbalimbali nchini, wananchi wanalalamika kuwa hawashirikishwi katika utoaji wa mawazo ya kimaendeleo. Pengine ushiriki wao ni pale wanapotumiwa na watafiti kama sampuli za wachache kufanya utafiti huku mwingi ukiwa unaowanufaisha watafiti.

Nitatoa mifano kadhaa kuonyesha namna watu wa chini hasa katika sekta ya elimu wakiwamo walimu, wanafunzi na wazazi wasivyoshirikishwa katika masuala mbalimbali. Na haya wamekuwa wakiyasema walimu wenyewe katika majukwaa yao mbalimbali.

Mfano mzuri ni utungaji wa sera, miongozo ya elimu na ubadilishwaji wa mara kwa mara wa mitalaa ya elimu nchini. Kwa hili la mitalaa, japo wataalamu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wenye jukumu la kuisimamia kudai wanawashirikisha walimu, wengi wanadai hilo halina ukweli.

Aghalabu wamekuwa wakipewa maelekezo ya kutumia mtalaa mpya bila ya kupata mwongozo wa kuutumia hivyo kuwa sababu ya wanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani.

Katika ngazi ya wizara hali ni hiyohiyo, watunga sera wamekuwa wakijifungia ofisini na kuibuka na matamko ya kisera na miongozo, pasipo kufanya utafiti wa kina unaowashirikisha wadau wengine katika ngazi za chini kabisa.

Siyo kwenye elimu pekee, hali hii imetamalaki karibu kila sekta nchini. Wananchi wamekuwa wakipokea maagizo badala ya kuwa sehemu ya kuyatatua. Matokeo yake ni kusuasua kwa maendeleo kwa kuwa wananchi wanaamini wanasukumwa kama punda asiyejua thamani ya mzigo alioubeba.

Kamwe hatuwezi kupata maendeleo ya walio wengi ikiwa wachache wanajipa jukumu la kufikiri kwa niaba ya wengine. Watanzania siyo wajinga, hata huko vijijini kunakodharauliwa, wapo watu wana mawazo mazuri yanayoweza kuipeleka mbali nchi hii kimaendeleo. Tunayapataje mawazo yao kama tunawapa kisogo?

Ndiyo maana nasema kitendo cha watumishi wa Twaweza kwenda vijijini na kujifunza kutoka kwa wananchi, kinapaswa kuigwa na kila mtu au taasisi inayoshughulika na ustawi wa watu.

Serikali ndiyo taasisi ya kwanza na kubwa inayosimamia ustawi wa Watanzania, lazima tukubali kuwashirikisha wananchi katika kuiendeleza nchi. Si jukumu la wachache kwa niaba ya wengi.

Tuwasiliane: 0754 990 083