Kwa uhalifu huu Jeshi la Polisi lijitathmini

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Simon Sirro

Muktasari:

  • Tukio lililoanza kuleta mshtuko ni la ulipuaji wa ofisi za kampuni ya uwakili ya Immma iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, lakini kabla hilo halijapoa likatokea tukio kubwa zaidi la kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Siku za karibuni Taifa limeendelea kukabiliwa na matukio ya uhalifu yakiwamo ya kupigwa risasi watu mashuhuri, uvamizi na ulipuaji wa ofisi za mawakili na utekaji watoto.

Tukio lililoanza kuleta mshtuko ni la ulipuaji wa ofisi za kampuni ya uwakili ya Immma iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, lakini kabla hilo halijapoa likatokea tukio kubwa zaidi la kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Pia, kipindi hichohicho kulikuwa na tukio la utekaji watoto wanne mkoani Arusha, wawili walipatikana na wengine wawili waliuawa na kutupwa ndani ya shimo lenye maji.

Wiki hii yametokea matukio mengine mawili yaliyofuatana, kwanza ni kuvamiwa kwa ofisi nyingine za mawakili, hizi ni za Prime Attoneys zilizopo jengo la Prime House, Mtaa wa Tambaza, Upanga na lingine la kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali mstaafu, Vincent Mritaba na kuporwa fedha kiasi cha Sh5 milioni.

iku za karibuni Taifa limeendelea kukabiliwa na matukio ya uhalifu yakiwamo ya kupigwa risasi watu mashuhuri, uvamizi na ulipuaji wa ofisi za mawakili na utekaji watoto.

Tukio lililoanza kuleta mshtuko ni la ulipuaji wa ofisi za kampuni ya uwakili ya Immma iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, lakini kabla hilo halijapoa likatokea tukio kubwa zaidi la kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Pia, kipindi hichohicho kulikuwa na tukio la utekaji watoto wanne mkoani Arusha, wawili walipatikana na wengine wawili waliuawa na kutupwa ndani ya shimo lenye maji.

Wiki hii yametokea matukio mengine mawili yaliyofuatana, kwanza ni kuvamiwa kwa ofisi nyingine za mawakili, hizi ni za Prime Attoneys zilizopo jengo la Prime House, Mtaa wa Tambaza, Upanga na lingine la kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali mstaafu, Vincent Mritaba na kuporwa fedha kiasi cha Sh5 milioni.

Matukio haya ya kutisha yanayotokea mfululizo, yanatuonyesha kuna dosari eneo fulani katika suala zima la ulinzi wa raia na mali zao.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Simon Sirro alikutana na viongozi wastaafu wa jeshi hilo kubadilishana uzoefu, hasa kwa kuwa wao kwa sasa wako nje, wanayaona na kusikia mengi kuhusu utendaji wa polisi.

Sirro alitamka wazi kwamba wastaafu hao wameshauri mengi, lakini kubwa ni weledi wa askari polisi katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.

Haya yanayotokea kwa mfululizo yanaturejesha katika hoja hiyo ya weledi wa askari wetu ambao wastaafu hao waliudokeza.

Katika hilo la weledi, malalamiko yaliyopo kwa wananchi kuhusu utendaji wa askari polisi ni mengi kiasi kwamba kuna wanaoamini kuwa limefanikiwa zaidi katika kudhibiti wanasiasa kuliko uhalifu.

Miongoni mwa wanayolalamikia ni kwamba, askari badala ya kuwakamata washukiwa wa uhalifu au madai mengine kwa kufuata kanuni na sheria iliyounda jeshi hilo, katika baadhi ya matukio wamekuwa wakidai kwamba wanatekeleza amri kutoka juu.

Hayo na mengine mengi yamekuwa ni kero ya wananchi dhidi ya jeshi hilo. Ni vyema Jeshi la Polisi likajipa nafasi ya kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

Kinyume chake, kuongezeka kwa matukio haya ya uhalifu huku wananchi wakilalamikia utendaji wa jeshi hilo shutuma zitaendelea kuwaandama Polisi.

Zamani kulikuwa na malalamiko kwamba jeshi hilo halina vifaa vya kutosha kupambana na uhalifu hasa usafiri, lakini hivi sasa wamepewa pikipiki na magari kwa ajili ya vikosi vya kupambana na uhalifu.

Mbali na usafiri, polisi pia wamewezeshwa utaalamu wa kunasa mawasiliano na kupambana na uhalifu wa mtandaoni. Wananchi wanaona jeshi hili hata kama halijakamilishiwa vifaa vyote, lakini mafunzo waliyonayo na vyombo vya usafiri walivyopewa, uhalifu unaotokea sasa haukupaswa kuwapo.

Kuna jitihada nyingi zimefanywa na makamanda wa polisi waliopita, zikiwamo utii bila shuruti na ulinzi shirikishi, lakini kinachoshangaza matukio ya uhalifu hayawi historia.

Tunadhani kuna dosari mahala na jeshi hilo linapaswa kujitathmini zaidi na kuwasikiliza wadau kama lilivyoanza kwa kukutana na makamanda wake wastaafu.