MAONI-Kweli ipo haja ya kubadili mfumo wa kilimo

Muktasari:

  • Hii inatokana na umuhimu na mahitaji ya mazao yanayotokana na kilimo hai katika dunia ya sasa kama waziri wa biashara, viwanda na masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alivyokaririwa jana na gazeti hili akisema, “Watalii ni watu wasiopenda vyakula vyenye kemikali, hivyo tukianza kutumia kilimo hai tutazidi kuwavutia kwa sababu wataamini mboga zetu za majani, matunda na hata viungo.”

Kauli ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba ina mpango wa kubadili mfumo wake wa kilimo kutoka ule unaotegemea mbolea zenye kemikali hadi kilimo hai inafikirisha.

Hii inatokana na umuhimu na mahitaji ya mazao yanayotokana na kilimo hai katika dunia ya sasa kama waziri wa biashara, viwanda na masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alivyokaririwa jana na gazeti hili akisema, “Watalii ni watu wasiopenda vyakula vyenye kemikali, hivyo tukianza kutumia kilimo hai tutazidi kuwavutia kwa sababu wataamini mboga zetu za majani, matunda na hata viungo.”

Nukuu hiyo inatuma ujumbe wa afya, kwamba watalii hawapendi vyakula ambavyo mazao yake yamezalishwa kwa kutumia mbolea za viwandani kutokana na changamoto zake za kiafya.

Kwa maana hiyo, kwa kuwa Zanzibar inategemea utalii kwa ajili ya mapato kupitia kodi na tozo mbalimbali na pia kwa kuwa sekta hiyo inanufaisha wakazi wengi iwe katika vikundi au mtu mmojammoja, hivyo kuzingatia matakwa ya watalii ni moja ya vigezo vya kuwavutia na kuwafanya waongezeke.

Lakini kama tulivyosema kwamba kauli hiyo inafikirisha hasa pale tunapojiuliza kwamba hivi wanaohitaji aina hii ya mazao ni watalii tu, sisi wenyewe je? Ukweli ni kwamba hata sisi ni wahitaji.

Hivyo basi, tunatoa wito si kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pekee, bali haya ya Muungano kulichukua suala hili kama fursa ya kujiongezea soko lakini pia kulinda afya za watu wake.

Kama katibu mkuu wa wizara ya biashara, viwanda na masoko wa Zanzibar, Juma Ally Juma alivyokaririwa pia na gazeti hili toleo la jana akisema sera za Tanzania hazitilii suala la kilimo ndiyo maana hakiwanufaishi Watanzania kwa kiasi kinachostahili.

Alisema kuna fursa nyingi ambazo wakulima wanapaswa kuzitambua akitoa mfano wa mfanyabiashara mmoja wa Ujerumani ambaye alisema hununua tani 500 za viungo kwa mwaka kutoka nchi mbalimbali lakini akisema vya kutoka Tanzania hupata wastani wa tani 10 tu.

Tunawataka wenye dhamana ya kusimamia kilimo, masoko na viwanda kukutana kuandaa mpango mkakati wa kuimarisha kilimo cha mazao ambayo masoko yake ni makubwa hususan baada ya kuchakatwa tukiamini kwamba kwa kufanya hivyo, uchumi wetu utakuwa katika ngazi zote; mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.

Mathalan, wataalamu wa kilimo wakiandaa mkakati kabambe wa kilimo hai ni dhahiri kwamba tutapata soko la ndani na nje kutoka kwa watalii wanaokuja nchini mpaka watu wetu wenyewe na kwa kuwa watu wa masoko watakuwa wameshaonyesha milango; hakuna mkulima atakayevuta shuka wakati akifahamu fika kwamba sasa kinalipa.

Hiyo ikienda sambamba na mkakati wa kuchakata mazao tena kwa kutumia mashine nyepesi na kuzifungasha vyema, hakika tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika suala zima la kuinua kipato.

Tunaamini kwamba ikiwa moja ya vipaumbele vyetu vitakuwa ni kilimo kwa mtazamo huo, asilimia 80 ya Watanzania wanaoelezwa kwamba wanakitegemea watakuwa wameuaga umaskini na hiyo maana yake itakuwa ni taifa zima.

Kadhalika, tukifanya hivi ile dhana ya kuwakatisha tamaa wakulima na kukifanya kilimo kama adhabu ya ‘kama kazi imekushinda mjini rudi kijijini ukalime’ itakoma kwani kilimo ndicho kitakachokuwa mkombozi na alama ya utajiri wa wananchi walio wengi. Kupanga ni kuchagua.