Lini tutaanza kujifunza kutoka majuu? - 2

Muktasari:

  • Tofauti na hapa kwetu, uchaguzi, hasa wa Serikali za Mitaa ni kiini macho. Wenzetu wa Denmark kwao uchaguzi huo ni muhimu na mwisho wa siku utendaji wa Serikali za Mitaa huwa na tija ya lazima kwa Taifa.

Wiki iliyopita tuliangalia namna wenzetu wa Mji wa Horsholm na miji mingine ya Demark ikiwamo Copenhagen wanavyoshiriki katika demokrasia na wanavyojali umuhimu wa kupiga kura katika uchaguzi wao.

Tofauti na hapa kwetu, uchaguzi, hasa wa Serikali za Mitaa ni kiini macho. Wenzetu wa Denmark kwao uchaguzi huo ni muhimu na mwisho wa siku utendaji wa Serikali za Mitaa huwa na tija ya lazima kwa Taifa.

Tofauti ya uchaguzi wetu na wenzetu ni kwamba, sisi tunachagua viongozi wa Serikali za Mitaa ili wakasimamie mitaa yetu, vijiji na vitongoji vyetu kwa mambo ya kawaida.

Katika karatasi viongozi hawa wana dhamana kubwa, kwa mfano ukisoma Sheria ya Ardhi za Vijiji ya Tanzania ya mwaka 1999, utaona Serikali ya kijiji ilivyo na mamlaka makubwa katika kupanga, kutumia, kugawa na kuhuisha ardhi ya eneo lao.

Pamoja na mamlaka hayo makubwa, Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji hazina uwezo mzuri wa kiuchumi kuendeleza maeneo yao na miradi mikubwa ya vijiji.

Fedha zimewekwa kwa mtu wa kati ambaye ni halmashauri za wilaya zinazoongozwa kwa nguvu kubwa ya Serikali kuu.

Mfumo huu wa Tanzania haueleweki na unafanya uzito na dhamana ya Serikali za Mitaa kutoeleweka. Ilipaswa madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji wachaguliwe muda mmoja na wote jukumu lao liwe kusimamia maendeleo ya ngazi ya chini ya maeneo yao.

Kufanya uchaguzi wa madiwani mbali na kwa mfumo tofauti na ule wa vijiji, mitaa na vitongoji kunatengeneza ukuta wa utendaji kazi baina ya viongozi hawa na mwisho wa siku wanajiona wako tofauti au labda wao ni mabosi wa wale wa Serikali za Mitaa.

Ukweli halisi ni kuwa wote wanapaswa kuwahudumia wananchi katika ngazi hiyo ya chini na iliyo karibu zaidi na maisha ya kila siku ya wananchi. Mara nyingi madiwani wanafanya kazi zao kwa kuona wanawawakilisha wananchi kwa msingi mpana kuliko wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji.

Tofauti hizi kama nilivyosema zinaanzia kwenye uchaguzi. Ikiwa uchaguzi wa kada hizi za uongozi utafanywa pamoja na majukumu yakawekwa sambamba, nchi yetu itakuwa na Serikali za mitaa zenye nguvu.

Hii ni kwa sababu ya uwekwaji wa pamoja kwenye kapu moja kati ya madiwani na wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji na kwa hiyo, taarifa za mikakati ya kutafuta fedha, fedha zilivyopatikana na zilivyotumika vitakuwa vinafanywa na watu walioomba dhamana pamoja na hata kuahidi utekelezaji mbele ya wananchi katika kipindi kimoja.

Narudia tena kusisitiza kuwa nchini Denmark, uchaguzi wa Serikali za Mitaa unamaanisha madiwani na wajumbe wao pamoja na mameya. Hakuna Serikali za mitaa za aina mbili.

Hapa Tanzania zipo serikali za mitaa za aina mbili, ile ya madiwani na halmashauri zao na ile ya vijiji, mitaa na vitongoji na zote ‘zinajifanya’ kuwa ni Serikali za Mitaa za aina moja.

Mfumo huu usioeleweka umewekwa kimakusudi na Serikali nadhani ili kutimiza ile dhana ya ‘wagawe uwatawale’, siamini kuwa mfumo huu upo ili kurahisisha utendaji kazi.

Mfumo huu umewekwa ili kumzubaisha diwani kwamba ni mtu mzito na ana uhusiano wa karibu na serikali kuliko wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa huku akipewa rasilimali za kusimamia maendeleo.

Pia, ni mfumo unaomfanya kiongozi wa kijiji, mtaa au kitongoji ajione mkiwa na anayewajibika kwa wananchi moja kwa moja huku akiwa hana rasilimali za kufanya hivyo na akiwa hana uwezo wa kuhoji matumizi ya rasilimali zilizoko katika halmashauri yake.

Ni mfumo ambao unainufaisha Serikali Kuu na kuumiza wananchi wa kawaida, lazima sasa tutafute namna za kuhuisha mfumo huu.

Wenzetu wa Denmark wamehakikisha kuwa Serikali zao za mitaa zina wataalamu wa kutosha, hawa wanashirikiana na mamlaka zilizopo kukusanya kodi na vipato vingine kwa ajili ya vipato vya halmashauri, wilaya au majimbo yao.

Baada ya makusanyo wanatumia fedha hizo kwa vipaumbele walivyojiwekea katika mitaa, vijiji na vitongoji.

Hapa Tanzania baraza la kata linaweza kujiamulia jambo hili kwa mujibu wa vipaumbele vyao, lakini baraza la madiwani la wilaya au katika halmashauri likakataa kipaumbele hicho na kujiwekea cha kwake.

Faida za mfumo wa Denmark

Uimarishaji wa ukusanyaji kodi kwa mfumo wa Serikali za Mitaa umeisaidia Denmark kukusanya mabilioni ya fedha kila mwezi.

Fedha hizi hutumika katika halmashauri husika kwa mujibu wa bajeti zao na halmashauri au miji inayokusanya fedha nyingi hupeleka mgao mkubwa kwenda Serikali Kuu na huko nako huzitumia fedha hizo kusawazisha upungufu wa bajeti kwa halmashauri zinazokusanya kidogo na kulifanya taifa zima liweze kwenda mbele kimaendeleo.

Mfumo wa Serikali za Mitaa Tanzania umefanywa kuwa tegemezi mno. Serikali hizo zinajiendesha kimaskini huku maeneo zilizopo kuna rasilimali za kutosha.

Ukitembelea maeneo yenye madini, mathalan utakuta fedha zinazopaswa kuchangwa na kampuni zinazochimba madini kwa ajili ya maendeleo ya vijiji au halmashauri walizopo hazieleweki.

Mfumo huu unawanufaisha wajanja wachache na haumnufaishi mwananchi wa kawaida, ifikie wakati fedha hizo ziwanufaishe wananchi na zaidi watambue fedha hizo ni shilingi ngapi, ziko wapi na zinatumikaje.

Utaratibu tulionao hivi sasa unafanya viongozi wa Serikali za Mitaa wasijue nini kinaendelea katika mikataba na manufaa mbalimbali.

Unaweza kukuta mgodi katika kijiji, lakini halmashauri ya kijiji, diwani na baraza la madiwani hawajui mambo yaliyomo katika mkataba huo.

Matokeo yake ni kuwa Serikali za Mitaa zinabaki kuwa majina huku wajanja wachache wakitokomea na manufaa ya fedha ambazo zimepatikana kutoka katika rasilimali za wananchi.

Askari wanasiasa

Jambo lililonitia moyo pale Horsholm ni kuwa, mji huo na miji yote ya Denmark katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hata uchaguzi mkuu watu wote wanaruhusiwa kushiriki katika siasa bila kujali kazi.

Nilikutana na askari Jeshi na Polisi kadhaa ambao ni wanachama wa vyama kadhaa na ni wagombea katika uchaguzi wa KV13.

Nilipouliza utaratibu ule unafanyaje kazi wakaniambia kwao inaruhusiwa, unatoka kazini na gwanda la jeshi unafika nyumbani unalivua unavaa sare za chama chako unakwenda kunadi sera na kupinga sera za wagombea wenzio.

Zaidi nikaambiwa hata ukichaguliwa kuwa diwani au mbunge unaendelea na kazi yako ya kulitumikia jeshi na ukitoka kazini unaenda ofisi za mbunge au diwani kuhudumia wananchi.

Yaani walinifundisha uwezo mkubwa walio nao wa kutenga mipaka ya kazi na siasa. Nikastaajabu mno!

Nilipomuuliza polisi mmoja anafanyaje kazi zote mbili maana yeye alikuwa diwani kipindi kilichopita na Novemba mwaka 2013 alikuwa anagombea kipindi cha pili, akaniambia ni jambo linalotekelezeka bila wasiwasi na wameshazoea.

Nilipouliza kama kumewahi kuwa na matukio ya polisi kupendelea chama chake katika shughuli za usimamizi wa utekelezaji wa sheria, wakaniambia kwao haliwezekani na kuwa polisi akifanya hivyo itagundulika mapema na ataishia kufukuzwa kazi na kwenda gerezani, wakasisitiza kuwa kila mmoja hataki hilo limtokee. Mfumo huu unaweza kumshangaza mtu yeyote yule.

Wizara ya Mambo

Kubwa kuliko yote, uchaguzi wa nchini Denmark unasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na siyo tume ya uchaguzi.

Nilipouliza ikiwa wizara inaweza kukipendelea chama kinachoongoza dola nikaambiwa hilo halikuwahi kutokea na halitatokea.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na mwanasheria simu; +255787536759/ barua pepe; [email protected]/ tovuti; juliusmtatiro.com.