Lumbesa bado inatesa wakulima

Muktasari:

  • Hata hivyo, manung’uniko yake hayakuwa na maana kwani alilazimika kuuza kwa hasara ili apate mahitaji yake ya msingi aliyotarajia kununua baada ya kuuza viazi vyake.
  • Pia, kama asingeuza kwa ujazo huo angekosa mteja na badala yake viazi hivyo vingeozea ndani kwa sababu walanguzi wote wanataka ujazo wa lumbesa.

Mwanzoni mwa wiki hii nikiwa katika Kijiji cha Magoda mkoani Njombe, nilikutana na mkulima akiuza gunia 15 za viazi mviringo kwenye magunia yaliyojazwa kuzidi kiasi maarufu kwa jila la ‘lumbesa’huku akinung’unika kudhulumiwa.

Hata hivyo, manung’uniko yake hayakuwa na maana kwani alilazimika kuuza kwa hasara ili apate mahitaji yake ya msingi aliyotarajia kununua baada ya kuuza viazi vyake.

Pia, kama asingeuza kwa ujazo huo angekosa mteja na badala yake viazi hivyo vingeozea ndani kwa sababu walanguzi wote wanataka ujazo wa lumbesa.

Jioni ya siku hiyo wakati nikiangalia taarifa ya habari kwenye luninga, nikasikia tena malalamiko ya wakulima wa vitunguu, Ilula mkoani Iringa wakilia ugumu wa maisha baada ya kudhulumiwa mazao yao kutokana na ujazo usiozingatia vipimo.

Lumbesa kwa wakulima sio kilio cha jana wala juzi. Ni kilio sugu cha muda mrefu kwani kila mwaka wakulima wanapouza mazao yao huwa wanaishia kulanguliwa na wakati mwingine, huishia kupoteza hata mtaji waliotumia kwa ajii ya kilimo.

Lumbesa inamuweka mkulima kitanzini. Ni ukweli usiopingika kwamba, mkulima hana kauli kwenye mazao yake na wakati mwingi huwa analazimika kuuza hata kwa hasara ili asiumie zaidi.

Lumbesa ni kilio cha mkulima kisicho na msaidizi. Analima kwa gharama kubwa lakini mwisho anaishia kuwanufaisha wezi wa mazao yake ambao ni walanguzi.

Hii inaonyesha wazi kwamba sheria ya mizani na vipimo ya mwaka 1982, haijasimamiwa ipasavyo ndio maana wakulima wanaendelea kuteseka.

Kila siku wakulima wanalalamika na mikati yote ya kupambana na watu hawa inaishia kwenye taarifa za habari lakini huko vijijini, wakulima wanaendelea kudhulumiwa.

Kwenye suala hili wakulaumiwa ni Serikali kwa sababu inao uwezo wa kuwadhibiti wanunuzi hawa batili tangu shambani ambako mkulima ndio anauza mazao yake.

Nimeshuhudia kwa macho wakulima wakilia kuumizwa na wafanyabishara hawa ambao, sio kazi kubwa kabisa kuwadhibiti.

Tunajua upo uhusiano mkubwa baina ya viwanda na kilimo. Malighafi za viwanda lazima zitokane na kilimo.

Lengo hasa la mapinduzi ya viwanda ni kuinua uchumi wa Taifa na wananchi wakiwamo wakulima ambao hivi sasa wanalia.

Maana yake ni kwamba, lazima ziwepo jitihada za kuwakomboa wakulima kwenye lindi la manyanyaso ili matunda ya viwanda yawafikie.

Kama wafanyabishara wataendelea kuwalangua wakulima, sio rahisi kufikia lengo la mapinduzi ya viwanda kwa sababu havitawanufaisha wananchi kule vijijini.

Lazima sheria ifuatwe na wasimamizi wa sheria wasikae ofisini, waende mashambani waliko wakulima.

Kinachotokea ni kwamba, wakulima wanalazimika kuuza mazao yao hata kwa hasara wakihofia hasara kubwa zaidi kwa mazao yao kuoza.

Kwao sio rahisi kuungana na kupinga soko hilo haramu, kwa sababu kijiji kimoja wakigoma, mfanyabishara ataenda kununua kijiji kingine na mwisho wa siku, huyu mkulima aliyegoma atapata hasara.

Ijulikane tu kuwa wakulima wengi wanalima kwa gharama kubwa huku wakinunua pembejeo za gharama kubwa na kuishia kuuza kwa hasara na kuwanufaisha watu wengine kabisa.

Hatua kazi za kisheria zichukuliwe ili waache kuwaumiza wakulima.

Ni wakati muafaka wa kutupia jicho kwa mkulima ili kunusuru uchumi wa nchi ambao lazima uanzie kwa mkulima wa chini kabisa.