MAGONJWA NA TIBA: Matumizi ya vidonge vya uzazi yana madhara?

 Wiki iliyopita nilieleza kuhusu matatizo ya kutopata hedhi ambayo yamekuwa yakiwapata wanawake wengi na pia, nilieleza moja ya sababu kubwa zinazochangia kukosa, kubadilika kwa tarehe za mizunguko ya hedhi ni pamoja na matumizi ya njia mbali mbali za kupanga uzazi ikiwamo ile ya kutumia vidonge.

Suala la afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa ujumla, ni suala linalotakiwa kupewa uzito na kuhitaji ushauri na uangalizi kutoka kwa watoa huduma za afya kama yalivyo masuala mengine ya kiafya.

Hivyo, siyo vema kutumia njia yoyote ya uzazi wa mpango bila kupata ushauri kutoka kwa watoa huduma wa afya ili kukabiliana na matokeo hasi ya matumizi ya njia hizi.

Matumizi ya njia za uzazi wa mpango hasa ya vidonge, ni moja ya njia salama na nafuu zaidi lakini usalama huu utaimarika zaidi iwapo itatumika chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya, hata hivyo, ni dhahiri kuwa wakati wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango, mwanamke atapitia matatizo madogo madogo ya kiafya ambayo kupitia hayo, yanaweza kumfanya kushindwa kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Kwa hiyo, naomba ieleweke kuwa ni kweli matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango yanaweza kusababisha matatizo madogo madogo ya kiafya japo sio kwa wote. Lakini kwa walio wengi huyapata na kwa msaada wa watoa huduma za afya, matatizo haya hutatuliwa.

Mwanamke anaweza akawa anapata kichefuchefu mara kwa mara na kuhisi kama ana homa, baada ya kuanza kutumia vidonge hivi. Lakini dalili hizi hupungua taratibu baada ya muda fulani.

 Kwa kipindi hiki mwanamke anashauriwa kunywa vidonge hivi wakati wa usiku anapotaka kwenda kulala ili kupunguza kichefuchefu na uchovu. Aidha, iwapo dalili hizi zitadumu kwa muda mrefu, ni vema kupata ushauri wa daktari.

Mabadiliko yanayojitokeza kwenye matiti pia ni madhara mengine madogo yatokanayo na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango. Katika kipindi hiki, mwanamke anaweza kuyaona mabadiliko kwenye matiti kama ya kuonekana kama yamevima na kuongezeka ukubwa na kupata maumivu. Mabadiliko haya hujitokeza wiki chache baada ya kuanza kutumia vidonge.

Naomba niwatoe hofu kuwa mabadiliko hayo  yanasababishwa na mabadiliko yaliyojitokeza kwenye mfumo wa homoni baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo na wala hayana uhusiano na saratani ya matiti. Lakini ni vizuri kumuona daktari haraka kama mabadiliko haya yatadumu kwa wiki kadhaa.

Madhara mengine yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango ni sehemu za siri kutokwa na ute usio wa kawaida.

Baadhi ya wanawake wanapatwa na hali hii wakati wa matumizi ya vidonge hivi. Hii ni kutokana na maadiliko ya mfumo wa homoni, hivyo, matumizi ya vidonge hivyo husababisha mfumo wa homoni kuyumba na kufanya mabadiliko fulani kwenye mfumo wa uzazi.

Matatizo mengine yatokanayo na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo wanawake wengi huyapata ni kuongezeka kwa uzito wa mwili kwa kasi kutokana na vidonge kuchochea  homoni za kike, mabadiliko ya kihisia, kukosa hedhi kwa baadhi ya miezi na hata maumivu ya kichwa ya mara kwa mara ambayo baada ya muda hutoweka.