MO apewe ushirikiano, siyo mizengwe

Muktasari:

  • Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji “Mo” alishinda zabuni baada ya kuwa mzabuni pekee aliyejitokeza akiwa ameweka dau la Sh20 bilioni.

Jumapili ya Desemba 2, klabu ya Simba iliandika historia baada ya wanachama kumtangaza mshindi wa zabuni ya kununua asilimia 50 ya hisa ili kuwa mmiliki mwenza.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji “Mo” alishinda zabuni baada ya kuwa mzabuni pekee aliyejitokeza akiwa ameweka dau la Sh20 bilioni.

Dewji, ambaye ni shabiki na mwanachama wa Simba, aliahidi makubwa kwa kuifanya klabu hiyo kongwe nchini kujiendesha kisasa na kibiashara baada ya mfumo huo kuanza rasmi.

Nampongeza Dewji kwa kushinda zabuni hiyo kwa kuthubutu kujitosa kufanya mabadiliko ya kimfumo katika uendeshaji wa soka nchini.

Hakuna shaka kwamba Dewji ni mtu makini ambaye ametumia muda mrefu kuipigania Simba akitaka kuipa mafanikio ndani na nje akiwa na dhamira ya kutaka kufuata nyayo za klabu bora Afrika zinazojiendesha kibiashara.

Bila shaka dhamira iliyomsukuma Dewji kuwekeza Simba ni kufuata nyayo za klabu nyingine barani Afrika zilizopata mafanikio kwa kutumia mfumo wa kisasa wa uwekezaji kama vile TP Mazembe Englebert, Esperance, Zamalek, Raja Casablanca, El Hilal, Al Ittihad na Kaizer Chiefs.

Klabu hizo zimepata mafanikio baada ya kutumia mfumo wa uendeshaji ambao umezifanya timu zao kuwa tishio katika soka Afrika.

Dewji aliahidi makubwa mbele ya wanachama 1,310 ambao walihudhuria mkutano mkuu uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya ahadi alizotoa katika mkutano huo ni ujenzi wa viwanja viwili vya mazoezi, kimoja cha nyasi bandia na kingine cha kawaida ambavyo vitatumika kulingana na mazingira.

Pia ameahidi ujenzi wa hosteli yenye vyumba 35 vya kisasa, mgahawa na eneo la kuburudika wachezaji, studio ya kuzalisha vipindi vya televisheni vya Simba, gym na shule za timu za vijana ili kuuza wachezaji ndani na nje ya nchi.

Kimsingi Dewji anaonekana ana dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi ya soka, hivyo anapaswa kuungwa mkono ili atimize ndoto yake ya muda mrefu.

Wadau namba moja wanaotakiwa kumuunga mkono Dewji ni wanachama ambao kwa mujibu wa sheria za Serikali, wanatakiwa kumiliki asilimia 51 za hisa tofauti na Katiba ya Simba inayowapa asilimia 50.

Kwa mujibu wa utaratibu, wanachama ndio wenye sauti kwa kuwa wanamiliki hisa nyingi, lakini kinadharia mfanyabiashara huyo atakuwa na nguvu kubwa ndani ya klabu hiyo.

Ingawa ‘anafungwa’ na kipengele cha kutokuongeza hisa alizopewa kwa mujibu wa mkataba, lakini Dewji atakuwa na nguvu zaidi kuliko wanachama kwa kuwa atatoa fedha zake kuwekeza.

Mfanyabiashara yeyote duniani anataka faida, hivyo siyo jambo geni kwa Dewji kutaka faida kwa mujibu wa mkataba alioingia na klabu hiyo na wanachama wanatakiwa kuheshimu makubaliano ya pande zote mbili.

Shida inaweza kuanzia hapo kutokana na utamaduni wetu wa muda mrefu tuliozoea katika uendeshaji wa soka kwamba mwanachama anataka “klabu kumfanyia kitu”, lakini si yeye kuifanyia klabu kitu.

Baadhi ya wanachama wenye nguvu na ushawishi ndani ya Simba na Yanga wamekuwa wakiishi kwa mizengwe ya kuzitegemea klabu hizo kupata ‘chochote’, hivyo mabadiliko ya kimfumo yatawatoa nje katika utaratibu wao wa kila siku.

Baada ya mfumo mpya kuanza hakutakuwa tena na makomandoo wanaoshinda klabuni kwa mizengwe, Dewji atakuja na watendaji wapya, bora wenye weledi wa kutosha katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji.

Kwa kuwa wanachama wamekubali mabadiliko, wanatakiwa kubadilika ili kuendana na mfumo mpya ambao utatoa fursa kwa watendaji wapya kufanya kazi kwa weledi kwa ajili ya manufaa ya klabu.

Katika mabadiliko ya sasa, hakutakuwa tena na viongozi wa kuchaguliwa, hawatamuona Evans Aveva au Geofrey Nyange ‘Kaburu’. Zitakuja sura mpya zilizobobea katika maeneo husika kulingana na nafasi zao za kiutendaji.

Mabadiliko yoyote yanakuja na faida na hasara zake kwa hiyo ni jukumu la wanachama kumpa nafasi Dewji kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba na makubaliano ya pande hizo.

Naamini wajumbe saba wa upande wa wanachama na wengine saba kutoka kwa Dewji, watafanya kazi kwa umakini kwa manufaa ya klabu ya Simba.

Nashauri vigogo wa Simba wajipange vyema kutoa elimu endelevu kwa wanachama kuhusu faida na hasara za uwekezaji ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.

Wapo baadhi ya wanachama wanaweza kuibua mzozo kwa kuwa hawakupata elimu ya kutosha kuhusu mfumo wa hisa, hivyo ni jukumu la viongozi kutoa elimu ya ufahamu.

Bila kutoa elimu ya kutosha, mfanyabiashara huyo anaweza kupata kikwazo cha kutimiza ndoto yake ya kuipa Simba mafanikio. Elimu ni jambo la msingi sana, ndiyo dawa ya kuepuka kuzalisha migogoro isiyokuwa na tija.