Mabadiliko ya tabianchi yako dhahiri, tumejipangaje?

Muktasari:

  • Mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kuongezeka kwa joto duniani kwa sababu ya kuharibika kwa tabaka la ozoni.
  • Tabaka hilo hupunguza mionzi ya jua inayokuja duniani, lakini linaharibiwa na uharibifu wa mazingira hasa shughuli za binadamu.

Iwe kuna njaa au hakuna, ukweli ni kwamba nchi yetu imekumbwa na ukame kwa kiasi kikubwa. Hali hiyo imesababishwa na kukosekana kwa mvua za vuli za mwishoni mwa mwaka 2016.

Mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kuongezeka kwa joto duniani kwa sababu ya kuharibika kwa tabaka la ozoni.

Tabaka hilo hupunguza mionzi ya jua inayokuja duniani, lakini linaharibiwa na uharibifu wa mazingira hasa shughuli za binadamu.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zimejidhihirisha kwa zaidi ya miaka 50 sasa ambapo hali ya hewa duniani imekuwa ikibadilika, kwa sababu ya kuongezeka gesi chafu zinazozalishwa na mvuke wa maji, methane na hewa ya ukaa.

Gesi hizo zinatokana na kuungua kwa mafuta na makaa ya mawe, ukataji wa miti na shughuli nyingine za kibinadamu kama kilimo na uchimbaji wa madini na shughuli za viwandani.

Hali hiyo imesababisha wakulima wengi kujikuta katika wakati mgumu.

Siyo ajabu tena kusikia upungufu wa mvua au mvua kunyesha kupitiliza kiwango kinachotakiwa na kusababisha mafuriko.

Mbali na ukame unaojidhihirisha sasa, Tanzania imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji wakigombea maeneo ya malisho na kilimo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, katika mwaka 2013/14 ukame ulisababisha upungufu wa chakula kwa watu 828,063 katika wilaya 54 za mikoa 14 nchini na Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya Sh15.2 bilioni pamoja na Sh2.2 bilioni kwa ajili ya kusafirisha hadi kwa walengwa.

Mafuriko pia yametokea katika maeneo mengi hususani mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara na kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu.

Hatua mbalimbali zimeshachukuliwa kidunia kupitia mikutano mbalimbali, lakini hazijapunguza hali hiyo. Tatizo ni kwamba nchi zinazochangia uharibifu huo wa mazingira ni zilezile zilizoendelea zenye viwanda vingi, lakini hatua zinapochukuliwa, nchi zisizo na viwanda vingi nazo zinabebeshwa mzigo.

Hata hivyo, Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupitia kitengo cha maafa, ikiwa pamoja na kuendesha mafunzo ya kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa.

Serikali imesaidia na mashirika ya kimataifa kuimarisha utoaji wa taarifa za tahadhari zinazohusu mabadiliko ya tabia nchi, ili kuchukua hatua za ufuatiliaji, kufanya tathmini na mbinu mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo, Serikali inapaswa kwenda mbali zaidi hasa katika kilimo. Kwa kuwa sasa athari za ukame zimeanza kujidhihirisha nchini, basi ufanyike mkakati mahsusi.

Ni kweli Serikali imepanga kusambaza tani milioni 1.5 za chakula kwenye maeneo yenye upungufu, lakini Serikali ingeanza utaratibu wa kutoa ruzuku kwa wakulima walioathiriwa na ukame.

Ruzuku hiyo inaweza kuwa fedha au vitu kama mbegu za mazao yanayohimili ukame kama mtama, uwele na mengineyo.

Bado tunaikumbuka ile ahadi ya kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji, nadhani maboresho yanatakiwa kufanyika ili fedha hizo zitumike kuwakwamua wakulima.

Unapozungumzia wakulima katika nchi hii maana yake unazungumzia uhai wa nchi, kwani asilimia 75 ya Watanzania wameajiajiri au wanategemea moja kwa moja sekta hiyo.

Kwa hiyo, juhudi za makusudi zinatakiwa kufanyika kuiokoa sekta hii. Suala siyo kugawa tu chakula, lazima pia zifanyike juhudi za muda mrefu ili hata ukame ukiendelea, kuwepo na chakula cha kutosha.

Jitihada nyingine ni kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na kuwepo kwa ukame, bado kuna vyanzo vya kutosha vya maji vinavyoweza kutumika kwa kilimo.

Kwa mfano, Serikali ingejiwekea lengo la kufikisha asilimia 10 ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji kutoka asilimia 3 iliyopo. Tutafika mbali.

Juhudi nyingine ni kuongeza bajeti ya ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwa mujibu wa Azimio la Maputo la mwaka 2003, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zilikubaliana kutenga asilimia 10 ya bajeti zao kila mwaka kwenda kwenye kilimo.

Mpaka sasa bado Serikali haijaweza kutekeleza azimio hilo, matokeo yake kumekuwa na ukuaji hafifu wa kilimo hata kunapokuwapo mvua.

Miradi yote ya kilimo haiwezi kufanikiwa bila uwekezaji wa kibajeti, hivyo Serikali inapaswa kutoa kipaumbele kwa wizara hii.

Kwa kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi ziko dhahiri, hatupaswi kupambana nazo kwa dharura. Mipango ya muda mrefu lazima iwepo.

Elias Msuya ni mwandishi wa Mwananchi