Madhara ya kumtikisa, kumrusha juu mtoto mchanga kwa nguvu

Muktasari:

  • Njia hiyo ambayo ni ya kulia, huwawezesha kuwasilisha mahitaji yao kwa wazazi au walezi wao.

Tofauti na watu wazima, watoto wachanga huwa na njia moja ya mawasiliano.

Njia hiyo ambayo ni ya kulia, huwawezesha kuwasilisha mahitaji yao kwa wazazi au walezi wao.

Hata hivyo, madaktari wanasisitiza, kipindi ambacho wazazi wanatakiwa kuwa makini ni pale anapombmbeleza mtoto hasa mchanga anapolia.

Mtoto mchanga mara zote hupenda kulia ili kufikisha ujumbe kwa yule anayemlea, na wakati mwingine hulia sana kiasi cha kumfanya anayembembeleza kutumia njia mbalimbali za kumbembeleza kusudi anyamaze na hapo ndipo wengi hufanya makosa. Kwa sababu walezi wengine hujikuta wakipandwa na hasira na kushindwa kuvumilia kumuona mtoto akilia kwa mfululizo bila kunyamaza. Wengine huchukua uamuzi wa kuanza kumtikisa kwa nguvu au kumrusha rusha kwa nguvu bila kujua kuwa kitendo hicho kinamadhara makubwa kwa mtoto.

Wapo wengine pia hujikuta wakiwaangusha au kuwabamiza kichwa kwa bahati mbaya, kitendo hicho kina madhara makubwa kwa watoto hasa walio na miaka chini ya mitano.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha watoto wenye umri wa kuanzia wiki 6 hadi 8 hukumbwa sana na matatizo yatokanayo na kutikiswa au kubamizwa.

Kwa sababu watoto wengi wao walio katika umri huo hupenda kulia sana ukilinganisha na wa umri mwinginena wengi wao huwa wakiume.

Nini kisababishacho vilio hivyo?

Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mlezi au mzazi kumtikisa mtoto kwa nguvu.

Baadhi ni ile hali ya kuwa na msongo wa mawazo hasa wakati mlezi anakuwa na hasira. Mtoto akilia huamua kumtikisa kwa nguvu kusudi anyamaze, au wakati mwingine mtu huwa anakuwa amekula dawa za kulevya zikamtuma kufanya hivyo au anapokuwa amelewa pombe.

Lakini inaelezwa pia kuwa msongo wa mawazo kwa mlezi unaweza kuchangia au historia ya kuteswa na walezi wake angali akiwa mdogo. Watoto wengine walio katika hatari ya kukumbwa na tatizo hilo la kutikiswa kwa nguvu ni wale wanaolelewa mzazi mmoja.

Madhara ya kumtikisa mtoto

Baada ya kumtikisa mtoto kwa kukusudia au kutokukusudia anaweza kuonyesha dalili kuwa amepatwa na tatizo.

Hivyo kama mzazi au mtu mwingine amegundua hali hiyo, anatakiwa amuwahishe hospitali au kwa madaktari bingwa wa watoto.

Dalili hizo ni zipi?

Mtoto anapokumbwa na tatizo la kutikiswa ni pamoja na kupumua kwa shida, mapigo ya moyo kushuka, kushindwa kuona au kusikia vizuri hasa kwa ambaye hakuwa na tatizo hilo kabla.

Dalili nyingine ni mtoto kulala muda mrefu, hushindwa kula vizuri na kutapika mara kwa mara, ngozi yake huanza kupauka au kuwa rangi ya bluu au huweza kupatwa na degedege, kupooza na kupoteza fahamu.

Madhara yanayoweza kumpata mtoto aliye chini ya mwaka mmoja

Ubongo unaweza kuharibika na hakuna tiba mbadala, hivyo hali hiyo inaweza kumsababishia mtoto umauti.

Watoto wengine hupoteza uwezo wa kuona na kusikia, kitendo hiki pia huathiri hatua za ukuaji wa mtoto na tabia yake kwa ujumla.

Kwani anaweza akashindwa kuwa na uwezo wa kujifunza na kutafakari baada ya kufikia umri wa kuanza kwenda shule.

Wengine hukumbwa na degedege kila mara pamoja na tatizo kwenye kukaa na kutembea, madhara hayo wataalamu ‘Celebral palsy’. Hivyo basi, inawapasa wazazi au walezi kuepuka kubeba watoto wao hasa wanapokuwa wamelewa au wakiwa na msongo wa mawazo. Kwa wale wanaofanya kazi, wanashauriwa kuwapa maelekezo ya mara kwa mara dada zao wa kazi ya namna ya kumbembeleza mtoto.

Itapendeza zaidi mtoto kama atapata malezi kutoka kwa wazazi wote wawili pia kuelewa matatizo ya kudumu yanatokana na kubamiza vichwa au kutikiswa kwa nguvu

0759 775788