Friday, March 15, 2013

Mafuta ya nazi na uwezo wa kutibu ugonjwa wa kusahau

 

Kumekuwepo na taarifa kuhusu uwezo wa mafuta ya nazi kutibu ugonjwa wa kusahau unaowakumba wazee uitwao ‘Alzheimer’s disease’ wakati huohuo ikiripotiwa kuwa baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika kutibu ugonjwa huo hapo awali zinaonyesha kushindwa kufanya kazi inavyopaswa.

Hivi karibuni, kampuni kubwa ya dawa duniani , Pfizer  ilikiri kuwa dawa mpya aina ya dimebon ilionyesha kushindwa kutibu ugonjwa huo na huku ikifanya hali za wagonjwa kuzorota zaidi.

Wakati taarifa za kushindwa kwa dawa hizo zikiendelea kutolewa, madaktari na watafiti wameendelea kutafuta mbinu nyingine za kukabiliana na ugonjwa huu. Mojawapo ikiwa ni matumizi ya mafuta ya nazi.

Watafiti wanasemaje?

Hivi karibuni, jarida la kitafiti la European Journal of Internal Medicine limechapisha ripoti ya kitafiti inayozungumzia nafasi ya lishe katika kutibu ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer’s.

Watafiti waligundua kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya ukinzani dhidi ya utendaji kazi wa homoni ya insulin katika seli za ubongo na ugonjwa wa Alzheimers katika hatua zake za awali, hali iliyowafanya kufikiria kuwa pengine ugonjwa wa Alzheimers unafanana fanana na kisukari cha ubongo.

Wataalamu walikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa hata vyanzo vya awali vya ugonjwa huu yawezekana vikawa na uhusiano mkubwa na mfumo wa usafirishaji wa lehemu (cholesterol) kutoka kwenye damu mpaka kwenye seli za ubongo.

Aidha,  kuna ushahidi unaoonyesha  kuwa matatizo katika mfumo wa umeng’enyaji lehemu kwenye ubongo yanaweza kuchangia kusababisha ugonjwa wa Alzheimer.

Aidha, ilionekana pia kuwa wagonjwa wa Alzheimers walikuwa na kiasi kidogo sana cha lehemu kwenye bongo zao. Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu kwenye ubongo kuna uhusiano mkubwa na kuishi muda mrefu kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 80 na wengine wameonekana kuwa na uwezo mzuri wa kukumbuka mambo mbalimbali.

Utafiti mwingine uliofanyika mwishoni mwa miaka ya ‘80 ukitumia panya wenye mimba waliolishwa chakula chenye mafuta ya nazi na wengine chakula chenye aina nyingine za mafuta (unsaturated oil) ulioonyesha kuwa vitoto vya panya waliolishwa chakula chenye mafuta ya nazi walikuwa na maendeleo mazuri katika ukuaji wa ubongo wao ukilinganisha na wale waliozaliwa na panya waliokuwa wakilishwa chakula kilichowekwa aina nyingine za mafuta.

Hali hii imehusishwa na uwezo wa mafuta ya nazi kusaidia utendaji kazi wa tezi ya thyroid ambayo uhusika na ukuaji wa ubongo kwa watoto wadogo.

Mafuta ya nazi  na  kazi ya kutibu ugonjwa wa kusahau

Uzito wa ubongo ni asilimia mbili tu ya uzito wa mwili mzima, lakini seli zake zinachukua karibu robo ya lehemu yote iliyopo kwenye mwili wa binadamu.

Kazi ya lehemu katika ubongo ni kutengeneza viasili vinavyosaidia kuondoa sumu kwenye seli (antioxidants), kufunika seli za ubongo ili kuzuia kuvuja kwa madini (cellular ions leakage), na pia kuzipa seli umbo linalotakiwa.

Pia, husaidia kusafirisha vichocheo (neurotransmitters) vinavyopeleka taarifa kutoka sehemu moja ya ubongo mpaka sehemu nyingine, na kutengeneza na kuimarisha utendaji kazi wa sinapsi (synapses) au sehemu zinapokutana neva mbili kwa ajili ya kubadilishana taarifa.

Tofauti na aina nyingine, mafuta ya nazi yana kiasi kikubwa cha mafuta yajulikanayo kitaalamu kama saturated oils. Tofauti na unsaturated oils, saturated oils hayawezi kuvunjwa vunjwa kirahisi kutengeneza aina/zao nyingine.

Mafuta yenye sifa ya namna hii ni muhimu sana kwenye utendaji kazi wa ubongo kwa vile yanakuwa na uwezo wa kudumu muda mrefu bila kubadilishwa kwenda aina nyingine ya mafuta.

Faida nyingine ya mafuta ya nazi ni kuwa na uwezo wa kuupa ubongo chakula maalumu kinachofanya seli zake ziweze kujitengenezea nishati.

Uharibifu katika seli za ubongo unaotokana na ugonjwa wa Alzheimer’s husababisha seli hizo kushindwa kutumia sukari (glucose) kujitengenezea nishati na pia kuziwezesha zifanye kazi zake sawasawa.

Katika mazingira ambapo, glucose huwa kidogo mwilini, kwa mfano mtu unapofunga kula, au kufanya mazoezi makali kupita kiasi au kwa watoto wachanga waliozaliwa, ubongo hutumia vitu vinavyoitwa ketone bodies (ketones) kuzalisha nishati ili kuhuisha seli zake.

Kadhalika, mgonjwa wa Alzheimers, seli za ubongo wake nazo hutumia ketones moja kwa moja ili kujitengenezea nishati ya kuziwezesha kuishi kwa muda mrefu zaidi.

Mafuta ya nazi yana kiasi kikubwa sana cha viasili vinavyoitwa medium chain triglycerides. Unapokula mafuta ya nazi, mwili huvunja vunja mafuta hayo na kuzalisha ketone bodies kwa wingi, ambazo hatimaye hutumiwa na seli za ubongo.  

Changamoto zilizopo
Pamoja na kwamba kuna tafiti kadhaa zilizofanyika kujaribu kubainisha faida za mafuta ya nazi kiafya hususani ya ubongo, bado hakuna tafiti zilizoshirikisha idadi kubwa ya wagonjwa wa Alzheimers mpaka sasa kuchunguza ufanisi wa mafuta ya nazi kwa wagonjwa wa kusahau.

Hata hivyo, wanasayansi bado wanaendelea kuchunguza uwezo huu wa mafuta ya nazi na bila shaka jibu la uhakika litapatikana. 

-->