Sunday, April 28, 2013

Badili mwonekano wako kwa mitindo ya kusuka

 

Miongoni mwa mitindo ya wanawake ambayo  licha ya kuwepo kwa muda mrefu bado haipotezi uhalisia ni usukaji wa nywele kwa nakshi na mitindo tofauti unaosababisha mwonekano tofauti.

Licha ya kuwapo namna mbalimbali za utengenezaji wa nywele ikiwamo kushonea wiving, kuvaa wigi pamoja na kubandika nyewe za bandia ‘lace wig’ bado kusuka nywele katika mitindo tofauti itabaki kuwa aina ya urembo inayomtambulisha mwanamke wa kiafrika.

Siyo kwamba mitindo mingine ya nywele haimtambulishi mwanamke, bali tangu enzi, kusuka nywele ni mtindo usiopotea katika fikra za wanawake na kuonekana kuwa ni njia sahihi inayowatofautisha na wanaume, licha ya siku hizi kuwepo pia wanaume wanaosuka.

Mbali ya kumfanya mwanamke kuwa na mvuto wa aina yake, kusuka kunachangia kwa kiasi kikubwa pia kukuza nywele maradufu tofauti na zikiachwa bila kusuka.
Kusuka pia  kunaweza kumwepusha mwanamke asiweke kichwani kwake dawa zenye kemikali ili kulainisha nywele endapo ataamua kuziacha, ziendelee kuwa za asili zinazovutia.

Pia kunaweza kupunguza matumizi makubwa ya fedha katika kuzishughulikia nywele mara kwa mara kwa kuwa zikisukwa kwa utaalamu, zinaweza kumudu kukaa kichwani zaidi ya wiki mbili bila kuharibika.

Ipo mitindo ya usukaji maarufu inayojulikana na wengi kama vile yebo yebo, sangita, bob style, afro kink, dread, zigzag au mkeka pamoja na aina nyingine kadha wa kadha zinazooneka zaidi katika tasnia nzima ya mitindo na urembo.

Josephine Komba mtaalamu wa nywele katika saluni ya Shining hair dressing anaeleza kuwa usukaji wa nywele kwa mitindo tofauti, umekuwepo kwa miaka mingi licha ya kuibuka na kupotea, hali inayotokana na mitindo mipya au maboresho yanayofanywa kila kukicha.

“Siku hizi wasusi wamekuwa wabunifu wa hali ya juu na hata wengine tunajaribu kuangaalia nchi zingine wanafanya nini, ndipo tunaongeza utaalamu wetu lengo ni kuwafanya wanawake waendelee kuvutia na kubadilika kila siku wakiwa katika mitindo ya usukaji,anasema Komba

Anasema kuwa kwa sasa mtindo ambao umekuwa ukisukwa zaidi na wanawake ni mabutu ya rasta aina ya afro kink, ambazo baada hubanwa na kushonwa katika mtindo atakaopenda mhusika.

Imeandaliwa na Elizabeth Edward

-->