Bajeti isaidie kuchochea uchumi, kupunguza umaskini wa wananchi

Muktasari:

  • Mipango hii inapaswa kujumuisha, kuchochea na kusisimua uchumi.

Msimu wa mjadala ya bajeti bungeni ni fursa ya wadau mbalimbali kutoa mawazo yao kuhusu namna ya kuipata bajeti nzuri itakayoweza kutumika kukidhi malengo yanayotarajiwa.

Mipango hii inapaswa kujumuisha, kuchochea na kusisimua uchumi.

Kati ya mbinu za kiuchumi za kusisimua na kuchochea shughuli za uchumi ni matumizi ya Serikali. Matumizi hayo ni yale ya shughuli za maendeleo na kawaida.

Shughuli za kawaida ni pamoja uendeshaji wa ofisi wa kila siku, mishahara, semina na safari mbalimbali wakati zile za maendeleo ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kama vile barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege.

Kinachofanya kuwepo na kuchochewa kwa kusisimka kwa uchumi kupitia matumizi ya umma ni uingizaji wa fedha katika uchumi ambazo huongeza mzunguko.

Serikali ni mlaji mkubwa wa bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani na nje ya mipaka ya nchi. Kadri inavyozidi kutumia ndivyo inavyochochea na kusisimua uchumi kwa kuweka fedha katika mzunguko.

Sehemu ya fedha hizi ni zile zitokanazo na kodi. Serikali inapotumia, inalipa watu na kampuni mbalimbali ambazo hutumia fedha hizo katika ununuzi wa bidhaa na huduma tofauti kwa ajili ya kuziuza tena au matumizi binafsi.

Matumizi hayo ni muhimu kwa ustawi wa soko. Uhitaji huchochea uzalishaji na uzalishaji huchochea ajira. Matokeo ya ajira ni kipato kinachowezesha matumizi mapya.

Hivyo ni muhimu kwa Serikali kutumia kwa kuishirikisha sekta binafsi ili pamoja na mambo mengine ichochee na kusisimua uchumi.

Jambo la msingi ni kwamba fedha za matumizi ya Serikali zikitumika vizuri huweza kusisimua na kuchochea uchumi si Tanzania pekee, bali popote duniani.

Sekta binafsi

Matumizi ya sekta binafsi ni muhimu sana kuchochea na kusisimua uchumi. Sekta binafsi ni pana ikihusisha ile ya ndani na ya nje; rasmi na isiyo rasmi; ndogo kabisa, ndogo, ya kati na kubwa.

Matumizi ya sekta hii ni pamoja na uwekezaji katika sekta mbalimbali kama viwanda, kilimo, madini, usafirishaji na huduma za aina tofauti.

Matumizi katika uanzishaji na upanuzi wa vitega uchumi na uendeshaji wa siku hadi siku wa vitega uchumi hivi ni sehemu muhimu ya kuimarisha mzunguko wa fedha.

Pamoja na mambo mengine, matumizi hayo hulazimisha ajira kutokea katika minyororo mingi na mirefu ya thamani na mafundo yake.

Ajira hizi huleta kipato kinachochochea na kusisimua uchumi kutokana na matumizi ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazonunuliwa ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Hivyo ni muhimu bajeti zikapangwa kwa namna ambayo zitakuwa rafiki, wezeshi na kuvutia kwa sekta binafsi. Kwa upande wa kodi kwa mfano, lazima kupata mapato lakini yasiumize na kuifanya sekta binafsi isinyae. Pia matumizi ya kibajeti yakae kimkakati kwa namna ya kuichochea na kuiinua sekta binafsi.

Kipato binafsi

Matumizi ya kaya na mtu mmoja mmoja ni muhimu katika kuchochea na kusisimua uchumi kwa sababu matumizi huhusisha ununuzi wa bidhaa na huduma.

Huduma na bidhaa hizo ni pamoja na vyakula, vinywaji, mavazi, ujenzi na usafiri.

Matumizi hayo yanapofanyika fedha hubadilishana mikono kutoka kwa mnunuzi kwenda kwa muuzaji.

Wale wanaopokea fedha huzitumia katika matumizi mengine, hivyo kuendeleza uchochezi na usisimuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali. Kiwango cha matumizi ya kaya, mtu hata sekta binafsi kwa ujumla hutegemea kiasi cha fedha kinachobaki baada ya kulipa kodi.

Hivyo, ni muhimu kwa bajeti kuwezesha walaji katika ngazi ya kaya na mtu mmoja mmoja kuwa na kipato cha kutumia ili kuchangia kusisimua na kuchochea uchumi.

Sera za kodi

Aina, wingi na viwango vya kodi hutegemea sera za nchi. Sera za kupanua uchumi hujumuisha idadi ndogo na aina chache za kodi ambazo huchochea na kusisimua uchumi kwa sababu sera za aina hii hubakiza kiasi kikubwa cha fedha mikononi mwa walipakodi.

Kwa kadri fedha nyingi zinavyobaki mikononi mwa mwananchi kutokana na aina chache na viwango vya chini vya kodi, ndivyo uchumi unavyoweza kuchochewa na kusisimuliwa kwa haraka.

Kinyume cha sera pana za kikodi ni sera zinazominya uchumi ambazo pamoja na mambo mengine huwa na viwango vikubwa na aina nyingi za kodi.

Pamoja na kodi, ruzuku ni muhimu kama chombo cha kutekeleza sera za kodi kwa upana wake. Ruzuku ni fedha inayotolewa na Serikali ili kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho.

Ruzuku ni afya kwa uchochezi na usisimuaji wa uchumi, hivyo kama mamlaka zinataka kuchochea na kusisimua uchumi ni vyema bajeti zikapangwa kwa kuwa na sera za kupanua uchumi.

Sera za fedha

Kama ilivyo kwa sera za kodi, za fedha nazo ni muhimu katika kuchochea na kusisimua uchumi. Sera hizo huhusisha riba inayotozwa na benki za biashara na taasisi za fedha kwa wakopaji.

Sera pana za fedha huwa na riba ndogo kwa wakopaji hivyo kuwapa uhuru zaidi wa kukamilisha malengo yao kwa wakati. Riba inapokuwa chini huwezesha ukopaji, uwekezaji na matumizi.

Yote hayo ni afya kwa kuchochea na kusisimua uchumi, hivyo bajeti lazima zilenge kuwa na mazingira ya sera pana za fedha.