‘Bandari Dar ni nafuu zaidi kuliko Mombasa’

Muktasari:

Jambo hilo linachagizwa na baadhi ya wanasiasa na wasomi wakisema hiyo ni moja ya mambo ambayo yamesababisha kupungua kwa mizigo inayokwenda nje katika bandari ya Dar es Salaam.

Kumekuwa na malalamiko mengi ya wadau wa usafirishaji mizigo nchini wakidai kwamba tangu Serikali ilipotangaza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mizigo, gharama za huduma zimeongezeka.

Jambo hilo linachagizwa na baadhi ya wanasiasa na wasomi wakisema hiyo ni moja ya mambo ambayo yamesababisha kupungua kwa mizigo inayokwenda nje katika bandari ya Dar es Salaam.

Wanasema VAT kwenye mizigo imeongeza gharama za kusafirisha mizigo kutoka sehemu moja kwenda nje ya nchi. Hata hivyo, wadau hao hawajafafanua ni kwa kiwango gani wameathirika na kodi ya VAT.

Jambo hilo linakanushwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wakisema mizigo yote inayotoka nje ya nchi na kupita Tanzania, kwenda nchi nyingine haitozwi kodi kwa sababu walaji wake siyo Watanzania.

Mtafiti Mkuu wa TRA, Beldon Chaula anasema Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inasema mizigo yote inayopita Tanzania kwenda nje ya nchi haitozwi kodi.

Isipokuwa, anasema huduma nyingine ndogondogo zitakazotolewa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati mzigo unasafirishwa ndiyo zitakazotozwa kodi ya VAT kwa asilimia 18.

Anazitaja baadhi ya huduma hizo ndogondogo kuwa ni upakiaji na upakuaji wa mzigo, huduma za ukaguzi wa mzigo, huduma ya ulinzi wa mzigo husika na taratibu nyingine za forodha.

“Kwenye mfumo wa VAT kuna vitu vitatu vinavyotozwa kodi; bidhaa, huduma na nyumba mpya inapouzwa. Kwenye suala la usafirishaji wa mizigo ya kimataifa, sheria inasema mizigo hiyo ni zero-rated (haitozwi VAT),” anasisitiza Chaula.

Chaula anasema huduma au bidhaa zinazotozwa kodi ya VAT ya asilimia 18 ni pale zitakapotolewa au kutumika ndani ya nchi. Anasema kama bidhaa hizo zitatumika nje ya nchi basi hazitozwi kodi.

Kifungu cha 59 (3) cha sheria ya VAT kinaeleza wazi kwamba huduma za usafiri wa kimataifa zitatozwa asilimia sifuri ya kodi. Hata hivyo, sheria hiyo inabainisha kwamba hiyo haitajumuisha huduma nyingine ndogondogo zinazotolewa ndani ya nchi.

Anasisitiza kwamba huduma ndogondogo zinatozwa kodi ya VAT kwa sababu zinatolewa ndani ya Jamhuri. Mzigo unaokwenda nje ya nchi hautozwi kodi kabisa kwa sababu walaji wake si Watanzania na utalipiwa kodi huko uendako.

“Kumekuwa na upotoshaji mkubwa katika suala hili, naomba wafanyabiashara waelewe kwamba mzigo hautozwi kodi. Auxiliary services (huduma ndogondogo) kutozwa VAT haiwezi kuwa sababu ya watu kupunguza kusafirisha mizigo,” anafafanua mtafiti huyo.

Kuhusu kupungua kwa mizigo bandarini, Chaula anakiri kwamba mizigo katika bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa asilimia 15, lakini imepungua kwa asilimia 25 katika bandari ya Mombasa ambayo ndiyo mshindani mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam.

Anasema Kenya hawana sheria inayosema huduma ndogondogo zitozwe kodi ya VAT lakini wao ndiyo walioathirika zaidi. Kwa hiyo, kodi ya VAT kwenye huduma ndogondogo siyo sababu ya kupungua kwa kodi hiyo.

Chaula anasema sababu za kupungua kwa mizigo bandarini ni uchumi wa China kuyumba hasa kwenye uzalishaji wa chuma. Anasisitiza kwamba nchi hiyo ndiyo msafirishaji mkubwa, kwa hiyo akipunguza usafirishaji, bandari zote zinayumba.

“Kuna wasafirishaji wakubwa wa mizigo wasiozidi watatu katika bandari ya Dar es Salaam. Mmoja ambaye yuko Zambia anasema hawezi kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo kwa sababu randi ya Afrika Kusini imeshuka thamani, kwa hiyo ni nafuu kwake kibiashara,” anaeleza.

Kamishna wa Mapato ya Ndani - TRA, Elijah Mwandumbya anaendelea kufafanua kwamba suala kupungua kwa mizigo katika bandari hiyo, limetokana na usimamizi makini unaofanyika sasa ili kuhakikisha serikali inapata mapato.

Mwandumbya anasema waliokimbia ni wale ambao walikuwa wanapitisha mizigo kiujanja na kuifanya Serikali kukosa mapato. Hata hivyo, anasema sababu za kijiografia bado zinaipendelea bandari ya Dar es Salaam na wasafirishaji hao watarudi. “Mfanyabiashara wa Kongo hawezi kutumia bandari ya Mombasa eti kwa sababu anakwepa kodi ya VAT kwenye huduma ndogondogo. Tanzania iko karibu zaidi na Kongo, na bandari yetu ina gharama nafuu kuliko Mombasa,” anafafanua kamishna huyo.

“Mtu ambaye alizoea kukwepa kodi kwa kutoa rushwa, sasa hawezi kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa sababu serikali imedhibiti uendeshaji wa bandari. Jambo muhimu ni kuwa wazalendo ili kuisaidia Serikali kuongeza mapato.”

Kamishna huyo anabainisha kwamba badari ya Dar es Salaam ndiyo ina gharama nafuu katika kusafirisha kontena lenye urefu wa mita 20 na 40 ukilinganisha na bandari ya Mombasa ambayo inatoza VAT kwenye mizigo inayokwenda nje.