Friday, July 21, 2017

‘Hata kwenye wavu kuna mahasimu’

By Eliya Solomon, Mwananchi

Dar es Salaam.  Unapozungumzia  mahasimu wa soka la Tanzania  moja kwa moja  utagusia wakongwe  ambao ni Simba na Yanga, yote hiyo inatokana na historia kubwa iliyopo nyuma yao.

Kama ilivyo kwenye soka, basi hata kwenye mpira wa wavu na kwenyewe kuna miamba miwili ambayo ni Jeshi Stars na Magereza ‘Tanzania Prisons’.

Miaka ya nyuma, kulikuwa na timu kali za wavu na ilikuwa zikicheza, jiji zima linafahamu kuwa leo kuna kazi, ni timu moja ilikuwa inaitwa, Vyuma na tiomu ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Tipper.

Zilipokuwa zinacheza, mpira wa wavu ulitikisa anga za Tanzania wakati huo TAVA ikiwa chini ya mwenyekiti wake, Patrick Sombe. Kwa sasa timu hizo hazipo tena.

Ikutanapo miamba  hiyo, unaweza  dhani mpira utapasuka kutokana na mikwaju ya mashambulizi inavyoachiwa huku upande mwingine ukitumia nguvu nyingi kuzuia mikwaju hiyo.

Spoti Mikiki ilifanya utafiti mdogo kubaini uhasama wa timu hizo mbili moja ikiwa ya Jeshi na nyingine ya Magereza ulianzaje  pia tuliwafikia wadau wa mchezo huo ambao walitoa maneno yao juu ya upinzani wa timu hizo.

Chanzo cha Uhasama

Kocha wa Magereza, Edwin Masinga anasema uhasama wao umechangiwa na ubora wa timu zao  kwa nyakati hizo na upinzani ulikosekana kwa timu nyingine zilizokuwa zinachipukia.

“Sisi ni wakongwe nchini kwenye mchezo wa wavu, upinzani wetu nakumbuka ulianza rasmi mwaka 2003, upinzani wetu ni ndani ya uwanja mara baada ya mchezo huwa tunaendelea na urafiki  wetu.

“Kilichochangia upinzani ni ile shauku kwa kila timu kutaka kuwa juu ya mwenzake, ninakumbuka mechi yetu ya kwanza kukutana ilikuwa ni katika mashindano ya klabu bingwa ya Taifa.

“Mashindano hayo yalifanyaka Moshi, Kilimanjaro, ule mchezo ulikuwa wa piga nikupige maana ilikuwa tukishinda wanasawazisha na wakishinda tunasawazisha ile mechi ilibidi kwenda mpaka seti ya tano lakini tulishinda Magereza.” anasema.

Edwin aliongeza, kuanzia hapo upinzani uliongezeka zaidi kwa sababu Jeshi ilijawa na hasira za kutaka kulipa kisasi na ilikuwa kila wakikutana mchezo unakuwa wa kuvutia kutokana na upinzani wao.

Lengo la Uhasama

Kocha wa Jeshi Stars, Lameck Mashindano anasema lengo la upinzani wao ni kuleta msisimko kwenye mchezo huo ambao ulianza kuchezwa hapa nchini kwa miaka ya 1990.

“Upinzani wetu umezaa ushindani na tukikutana mchezo huwa na ushindani wa aina yake, kupitia ushindani huo watu huvutika na kuanza kuupenda mchezo wa mpira wa wavu.

“Tunashukuru Mungu kwa kiasi chake tumefanikiwa kupata mashabiki japo sio wengi sana lakini wamekuwa wakitoa sapoti kwa kutushangilia.

“Tunaheshimiana na tumekuwa hatuvunjiani heshima, tunawaheshimu kama  wapinzani wetu na wao nadhani wanatuheshimu ” anasema Lameck.

Wadau

Wadau wa  mchezo huo nao wamezungumza na kudai sio kazi nyepesi kutokomeza upinzani wa  timu mbili hata kama kutatokea timu nyingine bora zaidi yao.

Roggesern Joseph amesema upinzani wa timu hizo umeufanya mchezo huo kuwa na radha kama ilivyo kwenye soka upinzani wa Simba na Yanga.

“Wakutanapo Simba na Yanga muda mwingine huwa ni upinzani wa vurugu lakini kwetu huwa ni ushindani wa uwezo na sio vurugu.

“Kabla ya kutolewa kwenye Ligi ya mkoa timu ya Jeshi Stars kwa kosa la kukeuka kanuni, katika mechi zao nne ambazo wamekutana hivi karibuni, Jeshi kashinda 3 na Magereza akishinda 1.” anasema Joseph.

Naye Wasike Edwin amedai kuwa huwa wanainjoi michezo  baina ya timu hizo mbili na umekuwa ukiwafanya kujivunia walau Tanzania inatimu nzuri upande wa wavu.

“Japo kwa sasa kuna timu kama Chui, Makongo na nyinginezo zinazo fanya vizuri lakini upinzani wa hao jamaa hufanya baadhi ya shughuli za mji kusimama kwa ajili yao.

“Hakuna mdau ambaye yupo tayari kukosa mchezo  baina ya timu hizi,wanamakocha wenye uzoefu na hata wachezaji wenye viwango bora na nguvu za uchezaji.” anasema Wasike.

-->