Jinsi ya kutafuta upendo halisi

Muktasari:

  • Swali kubwa wengi wanalojiuliza ni kuwa inawezekanaje mtu ajihisi mpweke na aliyetengwa wakati yuko katika mahusiano mazuri?

Kati ya kiu kubwa alizonazo mwanadamu aliyeumbwa ni kuwa na ukaribu na yule aliyempenda ili kuitosheleza kiu ya kupenda na hata kupendwa pia.

Swali kubwa wengi wanalojiuliza ni kuwa inawezekanaje mtu ajihisi mpweke na aliyetengwa wakati yuko katika mahusiano mazuri?

Daima tunahitaji kuwa karibu na watu kama vile tunavyohitaji chakula na maji. Lakini kama vile ilivyorahisi kwa sisi kujitafutia na kujichagulia chakula kizuri ni ngumu sana kwa wengi wetu kutengeneza na kuandaa mahusiano mazuri na wenzetu hasa na wale ambao tuna mapenzi nao.

Zipo sababu nyingi zinazoathiri thamani na ubora wa mahusiano tuliyonayo kwa wengine. Hali kadhalika zipo sababu nyingi pia zinazoathiri kiwango cha ukaribu tulionao katika mahusiano yetu. Maamuzi tofauti tunayoyafanya na tabia zetu kwa kila mmoja ni kati ya vitu vinavyofanya tuwe karibu zaidi ya kila mmoja wetu au kututenganisha mbali zaidi.

Maamuzi haya tunayoyafanya yote yapo chini ya utawala wetu sisi wenyewe. Uamuzi wa kwanza tunaoweza kufanya katika mahusiano ni uchaguzi wa nani awe rafiki au mpenzi. Mtu unayemchagua kuwanaye katika mahusiano ananafasi kubwa katika kiwango cha ukaribu(intimacy) mtakaokuwa nao. Kama utachagua vibaya ni wazi kabisa hutopenda muwe karibu zaidi, wakati kama ukichagua mtu unayempenda vizuri daima hamtapenda kutengana.

Ayala Malach Daktari katika idara ya sayansi ya tabia katika chuo kikuu cha Ben – Gurion Israel anasema mara nyingi tunachagua marafiki au wapenzi wale wanaotukumbusha watu wazuri na muhimu ambao tuliwahi kuwa nao katika utoto wetu, hasa wazazi wetu. Mioyo yetu inakuwa katika uhitaji wa mtu au watu watakotukumbusha mazuri na furaha tuliyokuwa nayo katika utoto kwenye familia zetu. Watu wawili wanapopendana kama mke na mume wametokea katika familia tofauti, mwanamke alipokea mapenzi ya baba yake kwa namna tofauti na mwanaume akapokea mapenzi yatofauti toka kwa mama yake.

Watu hawa watapata shida katika kuendana kwasababu kila mmoja hana nafasi ya kumkumbusha mwenzake asili ya mapenzi ya awali. Watu wa namna hii hutumia jitihada kubwa zaidi kuleta ukaribu baina yao. Mfano mmoja katika mapenzi (hasa mwanamke) atajitahidi kuvunja mipaka ya vile vinavyo watenga na kutafuta kuwa karibu zaidi na mwenzi wake wakati huo mwingine (hasa mwanaume) hujitahidi kujitenga na kutafuta kuwa pekeyake

Ili kushinda na kupata ukaribu baina yenu lazima wapenzi wote waishinde hofu inayowatenganisha, kila mmoja kutimiza nia yake. Lazima mjitahidi kuusahau utoto na maisha yenu ya awali ili mjenge ulimwengu wenu mpya pamoja, hii itakuwa uponyaji wa jumla wa uhusiano wenu.

Kama wapenzi watazishinda hofu zao na kufikia uwiano katika mahusiano yao basi hakutokuwepo na woga wala kuyumba katika kutafuta kuwa karibu zaidi, hali hii itayaweka mahusiano yenu katika hali nzuri.

Kila mmoja hatahisi kuumizwa hasa mnapojitahidi kuwa karibu kihisia.

Mwanamke anayekazana kuutafuata ukaribu na mumewe na asiye na uhakika kama hitaji lake hili atalipata huweza kuishia kuwa mpweke, aliyedhoofu, anayependa kujitenga na asiye na tumaini tena.

Wakati huu mumewe anaweza kufikiria kuwa mahusiano yao yamejengeka kwa maana malalamiko na lawama zimepungua au kuisha. Kumbe mwanamke ameamua kukata tamaa baada ya kuvunjika moyo. Hali kama hii ni hatari sana kwa ndoa.

Matokeo ya hali hii mwanamke hutafuta mbadala wa hamu yake kutimizwa na hivyo kuwa na uwezekano wa kwenda nje ya ndoa kimapenzi na mwisho wake hupelekea kutengana na hata talaka.

Mara tu mahusiano pembeni yanapoanza yanamong’onyoa ule ukaribu wenu kwa kasi sana. Kawaida ukaribu katika penzi unahitaji ukweli, uwazi na kila mmoja kujiachia kwa mwenzake. Mambo haya kamwe hayawezekani pale mmoja anapokuwa na mahusiano pembeni.

Hatari zaidi huwa pale ambapo mpenzi wa pembeni anakuwa ndio mwelezwa siri na matatizo ya nyumbani, hii inajenga ukuta mkubwa kwa maana uthamani na umuhimu wa huyu mpenzi wa nje unaongezeka, anakuwa sio tu kwa ajili ya kutimiza hitaji la ngono bali ni sehemu ya kutua mizigo ya moyoni mwa mwanandoa mmoja. Ikifika hali hii kumtoa huko au kumwachanisha ni kazi ngumu sana.

Anakuwa radhi akupoteze wewe mwanandoa mwenzake kuliko kumkosa huyo mwandani wake mpya aliyempata.

“chunga isifikie hapa”