KUTOKA LONDON : Jumuiya ya Waingereza na watanzania ilivyowakaribisha mabalozi wapya London

Muktasari:

  • Mmoja anasema alikuwa bwana mifugo enzi Mwalimu Nyerere akipigana kutekeleza Siasa ya Ujamaa Wilaya ya Mbulu. Kuna Mhindi aliyeitoroka Zanzibar kipindi marehemu Rais Sheikh Abeid Karume akilazimisha wasichana wa Kihindi na Kiarabu kuolewa na viongozi wa Serikali ya mapinduzi.

Chumba kimejazana watu utadhani senene.

Wazungu, Waafrika na Wahindi. Vijana kwa wazee. Baadhi ya vikongwe waliopitisha miaka themanini walifanya kazi zamani Tanzania.

Mmoja anasema alikuwa bwana mifugo enzi Mwalimu Nyerere akipigana kutekeleza Siasa ya Ujamaa Wilaya ya Mbulu. Kuna Mhindi aliyeitoroka Zanzibar kipindi marehemu Rais Sheikh Abeid Karume akilazimisha wasichana wa Kihindi na Kiarabu kuolewa na viongozi wa Serikali ya mapinduzi.

Ole wako Mtanzania usiyeijua sawasawa historia yetu. Tumepitia mambo ya ajabu ajabu. Mmoja wa hawa wasichana kaishi hapa London zaidi ya miaka arobaini. Walitishika. Si msichana tena huyu. Ni ajuza anayekimbilia miaka 70. Maisha yanakwenda. Tuko wapi lakini?

London hii.

Jumuiya ya Urafiki wa Waingereza na Watanzania (BTS) imekodisha chumba namba 116 cha chuo mashuhuri cha kusomea Lugha za Kiafrika na ukanda wa Mashariki ya dunia (Orient). Chuo hiki- kinachoitwa SOAS kwa kifupi- huhodhiwa kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma na kisiasa.

Leo tunawategemea watu maalumu.

Mabalozi watatu.

Mmoja ni Mtanzania.

Balozi mpya hapa Uingereza, Dk Asha- Rose Migiro.

Hebu niwaeleze kisa fulani kuhusu Dk Migiro.

Miaka kumi au zaidi iliyopita nilikuwa natafuta wasichana wa Kitanzania kucheza ngoma katika bendi yangu ya Kitoto. Kwa kuwa ni vigumu sana kupata wacheza ngoma (kupiga au kukatika )toka nyumbani, huwa nachukua wasanii wa nchi nyingine . Watanzania wanaocheza (au wanaopenda ) ngoma ni haba kabisa.

Hata kama wapo, Mtanzania yuko radhi kufanya kazi ya kupiga deki mahotelini au kukaa na wazee wagonjwa na walemavu kuliko akacheze ngoma. Ngoma Ulaya ni ajira rahisi na kubwa sana. Sasa katika tafuta tafuta zangu nikafuma vijana kadhaa ndiyo walikuwa wamewasili kusoma, London. Hapa wasomi wengi ( vyuo vikuu) ndiyo hucheza ngoma. Siku chache baadaye wakati wa kufanya fanya mazoezi mmoja wa wale kina dada akasema kaja kusomea uwakili. Akadai hata akicheza ngoma au akisota katika baridi siku moja anataka “kuwa kama Mheshimiwa Asha Rose Migiro.”

Huyo “mdada” alikuwa hayasemi hayo kwa masihara. Kwangu alifanana na mwewe au tai anapokuwa juu ya mti au ghorofa akimvizia kuku na vifaranga vyake. Hutazama kwa jicho la kuwinda, kuwania, kupania; kuweka imani.

“Namhusudu sana Mama Migiro...ananipa moyo!”

Enzi hizo Mheshimiwa Asha-Rose Migiro alikuwa bado hajateuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Bado waziri. Sasa fikiria siku alipoteuliwa kwenda Washington, Marekani, yule dogodogo alivyojisikia. Miaka imekwenda dada wa watu sikumwona tena. Nasikia aliolewa. Nimesikia siku hizi ana ofisi yake mwenyewe ya mambo ya uwakili. Keshahitimu na hutetea wanawake wenye matatizo ya kesi. Tena anaajiri watu. Alihamasishwa na nani vile?

Miaka imekwenda ndiyo....

Dk Migiro alikaa Marekani, akarejea Tanzania, akaendelea na shughuli za taifa hadi alipoteuliwa kuwa Balozi hivi karibuni. Majuma matatu yamekwisha toka alipowasili. Leo kakaribishwa na mtayarishaji wa hafla hii ndogo, Dk Andrew Coulson. Dk Coulson ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Birmigham. Zamani aliwahi kufundisha chuo kikuu cha Dar es Salaam. Hawa ni watu wasiochuja mapenzi yao kwa taifa letu ...wanawapenda Watanzania, wanaipenda bado nchi na kuililia...ingawa weupe.

Kumbukumbu nzito.

Dk Coulson anamkaribisha Mheshimiwa Migiro.

Dk Migiro anatoa hotuba fupi akisema yuko tayari kukutana na watu mbalimbali na kujenga mahusiano ya kirafiki kati ya Tanzania na Uingereza.

Lakini mgeni siyo yeye tu.

Balozi mpya aliyeteuliwa kuiwakilisha Uingereza Tanzania ni Sarah Cooke. Mrefu, mtaratibu, kavalia miwani ; akijaribu maneno mawili matatu ya Kiswahili. Wa tatu ni balozi wa zamani huko anakokwenda Cooke yaani Dianna Melrose. Wakati mheshimiwa Melrose akiondoka London kulekea Tanzania, safu hii iliandika habari zake, mwaka 2013.

Tulimchangamkia shauri aliwahi kuwa balozi Cuba. Cuba ni rafiki mkubwa wa nchi za Kiafrika, hususan Tanzania. Kwa miaka tele, Cuba iliisaidia Afrika kihali na mali. Ilituma madaktari wake lukuki Afrika ikiwamo Tanzania. Waganga hawa wana bidii sana. Wana bidii kiasi ambacho miaka michache iliyopita wametumwa kufanya kazi Brazil, taifa kubwa na tajiri zaidi ya Cuba. Cuba chini ya Fidel Castro, ilijitolea askari wake kusaidia wananchi wa Angola kupambana na majeshi ya makaburu wa Afrika Kusini yalipoivamia mwaka 1977.

Naam.

Balozi Melrose anayeongea Kispanyola aliwahi kuishi Cuba kabla ya kuja Tanzania. Sasa hivi anakimudu Kiswahili cha kuombea maji. Mwingine ni balozi aliyemtangulia, Philip Parham- huyu alikuwa Tanzania kati ya 2006 na 2009.

Katika maongezi ya mapokezi, mhadhiri Dk Coulson anakumbusha kuwa huu ni msimu wa kuvutia na maendeleo ya viongozi wanawake. Siyo ajabu maana Waziri Mkuu mpya Uingereza ni Theresa May wa chama cha Conservative.

Hotuba zinapomalizika ni muda wa porojo, biashara, kujuana na vinywaji baridi. Wakati nikipiga piga picha nakumbushwa na Coulson kuwa wapo watu wa maana sana hapa, lakini hawajulikani. Mmoja mathalan ni aliyekuwa askari wakati wa vita vya dunia vya 1939-1945. Kapteni David Nichol ambaye keshafikisha miaka 95. Alikuwa Tanzania karibuni. Wakati wa vita hivyo vikuu alipigana Burma, Madagscar na Afrika Mashariki. Baadaye alifanywa mkuu wa mkoa mmoja wa Tanganyika chini ya Serikali ya kikoloni. Matembezi ya Tanzania yamekuwa kila mwaka. Karibuni aliweka taji la maua katika mnara wa askari , Dar es Salaam, kama heshima kwa askari wenzake waliompigania malkia na himaya nzima ya taifa hili tunaloendelea kuhusiana nalo, kilugha, kisiasa na kiuchumi.

Tovuti : www.freddymacha.com