Friday, July 21, 2017

NDANI YA BOKSI : Kipaji na maisha ya hovyo ni kulwa na doto...

 

By Dk Levy

Ukijiongoza vyema katika dunia inayojaribu kila mara kukufanya uwe kitu kingine, hilo ndilo fanikio kubwa sana kwako.

Fanikio hili limewashinda mastaa wetu wengi kwenye sanaa, iwe muziki au filamu. Kipaji ni suala moja, kujiongoza kimaisha nje ya kipaji ni suala jingine kubwa na zito.

Unaweza kuwa na kipaji kikubwa lakini ukaishia kutumikia msemo wa wahenga wetu kuwa “Kipaji na maisha ya hovyo ni kulwa na doto”.

Ingawa wapo wengi wanaofurahia mtu kufeli kimaisha, kwa mtu mwenye utashi na akili za kibinadamu kamili hawezi kupendezwa nalo. Inaumiza.

Nani alikuwa kama Aisha Mbegu Madinda katika kunengua? Aliwafunika karibu kila kitu wenzake. Sura nzuri, umbile halisi la kibantu, ngozi laini ang’avu. Sharapova, Lilian Internet au Aunty Suzzy? Hapana! Na ukali wao wote, hapa walikuwa kimya.

Kuna maelfu ya watu waliifuatilia Twanga Pepeta ndani na nje ya Dar es Salaam. Siyo kwa sauti ya marehemu Banza au Choki. Siyo kwa tumba za marehemu MCD wala drums za marehemu Abou Semhando ‘Baba Diana’.

Ni kwa sababu ya uwepo wa kiumbe wa kike mwenye mvuto uliopitiliza, mnenguaji ambaye muda wote alitabasamu jukwaani na kumfanya shabiki kuona kama ananenguliwa na malaika mbele yake.

Marehemu Aisha Mbegu Madinda. Mungu ampumzike sehemu inayomstahili huko alipo. Hii ardhi imemeza watu wengi. Aisha alikuwa alama sahihi na nembo nzito kwa wanenguaji wa kike Tanzania.

Alikuwa hatari katika sekta hii. Alitisha kila mahali na hakuna aliyethubutu kubisha. Katika suala la kazi alikuwa ni zaidi ya hatari unayoijua. Kiuno laini, miguu matata stejini, na tabasamu murua usoni.

Kwa umaridadi huo na akili yake iliyotulia, akafanikiwa kuwa na nyumba, akamiliki saluni na mpaka akawa na usafiri wake. Kwa wanenguaji, nani alikuwa kama yeye? Wanamuziki wa Bongo Fleva walikuwa wanasubiri kwa Aisha. Uliza watu. Alikuwa daraja moja na marehemu Amina Chifupa kwa wakati ule.

Kwa binti kama yeye, mnenguaji kama alivyo, nini zaidi alihitaji zaidi ya hivyo katika maisha yake? Haikutosha hapo tu, jina lake lilikuwa juu usawa wa ndege na hewa.

Wengi walienda maonyesho ya Twanga wakiamini hatowaangusha kama kila siku alivyokuwa akifanya. Kwenye idara ya unenguaji jukwaani alikuwa ni bendi ndani ya bendi yenye bendi ndani yake. Acha kabisa. Si mpaka taarifa zikaja kuwa Mapedeshee wengi walikuwa wakienda Twanga wakisubiri mwisho wa shoo wasemezane naye.

Robo ya mashabiki wa kiume wa Twanga walimfuata Aisha wamtazame kisha wakalale na amani ya mioyo yao. Fundi wa kike kwenye jukwaa.

Kuna aina ya unenguaji wake kila msichana mnenguaji alimuiga. Kuna pozi zake ambazo ziliigwa awapo jukwaani. Tangu na tangu wakiwa na kundi lao la Bilbums pale Bilcanass, Aisha alikuwa mgodi. Alifanya kila kitu wenzake walichoshindwa, akafika kila mahali palipoonekana ni mbali kwake kufika. Mvuto wake jukwaani ulikuwa zaidi ya gitaa la Shakashia na kelele za Msafiri Diouf.

Aisha alikuwa nembo ya mafanikio kwa wanenguaji wote nchini. Aliijua kazi yake, akautunza mwili wake na hatimaye vikamletea mafanikio.

Ni kupitia Aisha, ndipo hata baadhi wakaona unenguaji unaweza kuwa kazi halali. Kama ambavyo Jide kawafanya wasichana wengi waamini kuna maisha nje ya ajira za digrii kwenye muziki.

Ndivyo ambavyo wasichana wengi waliamini kuwa kuna maisha nje ya kumiliki duka la vipodozi na kufanya kazi mahotelini kama utaweza kunengua vizuri. Aisha alikuwa taa ya wasichana wengi wa mjini kama kina Halima Kimwana. Mwisho nuru na ubora wa ngozi yake ukaanza kutoweka. Juhudi na ushupavu wake wa kunengua jukwaani ukayeyuka kama kipindi cha Afrika Bambata pale Clouds.

Dawa za kulevya alizozisogelea zilimkaribisha kwa shangwe na kumfanyia kila sherehe katika mwili wake. Yakamlea. Yakambembeleza. Naye akayakumbatia. Yakamnyang’anya mafanikio na afya yake nzuri, yakampora sifa yake nzuri na umaarufu wake uliovutia. Yakamuondolea kujiamini mbele za watu. Aisha akawa mnyonge bila sababu. Unga.

Akaanza uvivu wa kunengua na kupaka poda usoni. Taratibu akaanza kutoweka katika majukwaa ya Twanga. Yakampunguzia kumbukumbu na kusahau ratiba za shoo. Akawa anachelewa jukwaani na kukwepa baadhi ya shoo. Asha Baraka akalia peke yake.

Dawa hizo ambazo zingine zinaingizwa na watoto wa vigogo pamoja na baadhi ya wasanii, zikamfanya asiwe na thamani na hadhi kama ilivyokuwa zamani.

Aisha Madinda hakumshitua mtu yeyote tena kwa sura na tabasamu lake. Hata akili yake pia kuna mahali ikapoa na haikuwa na ule moto wa zamani. Tumuache Aisha apumzike. Tuzidi kumuombea.

Unawakumbuka Nako 2 Nako? Kikosi cha Mizinga waliwahi kusema miongoni mwa wanamuziki wa kundi hili wanatumia dawa za kulevya.

Kwa kudhani ni tambo za kisanii na kwa kuwa makundi hayo kama yalikuwa hasimu, wengi wakapuuzia.

Alianza kuvumishwa Ibra da Hustler. Kwa kumuangalia ni kama ilikuwa kweli. Ila pia kwa kumuangalia tena ni kama ilikuwa hapana. Siku zikaenda.

Kila kona Nako 2 Nako ikawa inashika. Watu wakaanza kuyapotezea baadhi ya makundi na kuanza kuwashabikia wao kwa kasi. Mara likavunjika.

Ibra akajitenga na wengine wakabaki. Japo pengo la jamaa lilikuwa dhahiri, ila kwa kuwa waliobaki pia walikuwa vichwa na wenye kujielewa, kila kitu kikaenda poa.

Haikuwahi kutajwa Nako 2 Nako bila Lord Eyes. Utapigwa na mashabiki. Kila mmoja aliona ndiye aliyebeba ufalme wa kundi lile. Mwanzo kutoka Arusha alikuwa akihusudiwa Joh Makini na Watengwa, ila baada ya ujio wa ngoma kali kali za Nako, kila mmoja aliwaona ndiyo hasa mastaa wa Arusha huku Lord Eyes akionekana kama ndiye mfalme halisi.

Unakumbuka ngoma kama Hawatuwezi, Ndiyo Zetu, Bang na Mchizi Wangu. Hizo ngoma na nyingine nyingi zilizidi kudhihirisha akili komavu ya akina Lord Eyes. Mara kikosi cha Mizinga wakaja na kampeni yao ya “Hip Hop Bila Madawa inawezekana”, na katika mabango yao wakamtaja Lord Eyes kuwa anatumia dawa za kulevya. Nani aliwaamini?

Mara Nako 2 Nako wakaanza kuchuja. Lord Eyes akachuja zaidi na ufalme wake ukahama na kwenda kwa G Nako. Bado watu hawakushtuka.

Taarifa zikaja za unga, tukataka kukataa ila uraibu wa Ray C ukawashawishi wakubali. Lord anaingia kwenye kundi la vijana wenye vipaji walioshindwa kuongozwa na kujiongoza. Inaumiza. Na kwa mwendo huu ni dhahiri jamii ya muziki inapungukiwa kitu. Weusi wako juu vile, lakini mtu mrefu mwenye mbavu nene haonekani kando yao.

Kila siku huwa tunalia na dawa za kulevya. Kama bila dawa unadhani ni wapi angekuwapo Lord Eyes? Hii dunia ya muziki ingekuwa chini ya soksi zake ikimuabudu Chalii huyu wa Arachuga.

Ni nyimbo ngapi za thamani na kiwango zingekuwa zimetengenezwa na Ray C pamoja na marehemu Langa na Mark II B. Ni mali ngapi angechuma Aisha Mbegu Madinda kwa kipaji na uwezo wake?

Kuwaonea huruma walioko magerezani iwe China au Tanzania, kwa sababu ya biashara za dawa za kulevya ni sehemu ya ushetani kama ushetani mwingine.

Sioni sababu ya kuwaonea huruma wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Ni sehemu ya Ibilisi tunaoishi nao hapa duniani huku tukiwaona mashujaa kwa mali wanazomiliki kupitia biashara ya kuua nguvu kazi ya Taifa.

Bila tamaa yenu ya fedha na utajiri wa haraka, leo Aisha Madinda huenda angekuwa na bendi yake, mgahawa wake au hata chuo chake cha unenguaji.

Wako wengi sana waliotoweka kwenye sanaa kwa sababu ya unga. Unapomtazama Profesa Jay leo, kuna mkali aliyemuhusudu hata kudiriki kupita kwenye njia zake za kuchana mistari Terry Fanani. Unga ulimchelewesha kupanda basi la mshahara.

Achana na unga, wasanii wengi wa filamu pamoja na kuigiza mapenzi kila siku kwenye filamu zao. Lakini, wameshindwa kujiongoza kwenye mapenzi katika maisha halisi. Wengi wanayumbishwa kisanaa katika daraja lile lile kama wala unga lakini wao ni kwa sababu ya mapenzi. Kipaji ni suala moja, kujiongoza ni suala lingine zito. Linahitaji akili kubwa zaidi ya kukaa location.

Ushindi wetu mkubwa siyo kukwepa kuanguka, bali kusimama kila wakati tukianguka.

-->