Kupenda kemia kunamsaidia katika mbio za ujasiriamali

Muktasari:

  • Biashara huweza kufanikiwa endapo mhusika ana ujuzi wa kutosha na akiifanya kwa weledi unaostahili anaweza kupata soko hata nje ya nchi bila ya kujali idadi ya wanaofanya shughuli kama yake.

Kila biashara inahitaji nia na bidii ya ziada kuifanikisha kwa kukwepa vikwazo vinavyojitokeza.

Biashara huweza kufanikiwa endapo mhusika ana ujuzi wa kutosha na akiifanya kwa weledi unaostahili anaweza kupata soko hata nje ya nchi bila ya kujali idadi ya wanaofanya shughuli kama yake.

Leah Ally (58), ni mtengenezaji wa sabuni anayekabiliana na ushindani uliopo. Kwa miaka minne sasa tangu alipopata mafunzo hayo kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), anaitegemea biashara hiyo kama chanzo kikuu cha mapato yake.

“Japo nilianza na mtaji mdogo, lakini nimeweza kusomesha watoto wangu hadi wamemaliza vyuo, kukuza mtaji wangu na kuimarisha biashara yangu,” anasema Leah.

Anasema alianza na mtaji wa Sh70,000 kutengeneza sabuni za mche kabla ya kubadili na kuhamia katika zile za maji baada ya kuona fursa zilizopo eneo hilo.

“Mpaka sasa mtaji wangu umefika Sh5 milioni. Nimeshajaribu vitu vingi lakini nilipenda sabuni ya maji kwa sababu ni rahisi na tangu zamani nilikuwa nikipenda somo la Kemia hasa katika kuchanganya kemikali maabara,” anasema.

Leah alianza na aina moja ya sabuni, lakini sasa hivi anatengeneza aina sita za maji tofauti ikiwamo ya kuondoa madoa, kusafishia sakafu, masinki, kuoshea vyombo, kufualia na kuoshea nywele.

Anasema bila kujali soko ana uwezo wa kutengeneza hadi lita 1,000 kwa siku na kuziweka katika vifungashio vya ujazo tofauti.

“Sabuni inayoweza kutumika sehemu yoyote huwa nauza Sh2,000 kwa lita moja na Sh,8000 kwa dumu la lita tano,” anasema Leah.

Anasema bei ya sabuni hupangwa kulingana na matumizi yake na kubainisha kuwa ile ya kusafishia sakafu hasa viwandani anaiuza kwa Sh3,000 kwa lita moja.

Anasema masoko ya sabuni za maji yako njenje na kuna wakati aliwahi kupata zabuni ya kutengeneza sabuni za kusafishia sakafu na kwa wiki moja na nusu aliingiza Sh11.5 milioni.

Soko lake kubwa ni kwa watumiaji wa majumbani na amekuwa akiuza hasa katika vikundi mbalimbali vya wanawake pindi wanapokutana kwenye vikao tofauti.

“Tukikutana katika vikao vyetu akina mama ninao uwezo wa kuuza hadi Sh300,000 kwa siku au zaidi ya hapo kwa sababu sabuni ni kitu ambacho hakikwepeki, usipokitumia katika kazi moja basi utatumia katika kazi nyingine,” anasema Leah.

Anasema daima soko kubwa linapopatikana huchochea ukuaji wa biashara yoyote duniani na anaamini pindi atakapoweza kuwafikia watu wengi zaidi ndivyo atakavyokua kibiashara.

Mjasiriamali huyo anayo ndoto ya kumiliki kiwanda kikubwa na kuajiri vijana wengi ili atengeneze urithi bora wa watoto na wajukuu zake.

“Hadi sasa nimeajiri watu wawili wanaonisaidia katika uzalishaji na ninategemea baada ya kukua zaidi wataongezeka kulingana na mahitaji ya wateja,” anasema Leah.