Mandhari za usafiri majuu na nchi zilizoendelea

Muktasari:

  • Nikiwa sekondari, miaka 45 iliyopita, usafiri wa matreni ulikuwa kawaida. Safari ziliunganisha miji mikubwa ya Tanga, Arusha, Moshi, Kigoma, Mwanza, Morogoro; ajali hazikuwa nyingi kama yalivyo mabasi leo.

Tumalize mada kwa kuangalia magari moshi.

Nikiwa sekondari, miaka 45 iliyopita, usafiri wa matreni ulikuwa kawaida. Safari ziliunganisha miji mikubwa ya Tanga, Arusha, Moshi, Kigoma, Mwanza, Morogoro; ajali hazikuwa nyingi kama yalivyo mabasi leo.

Huku Majuu usafiri wa mabasi ndiyo salama kuzidi yote. Kama tulivyoona wiki jana ni kutokana na utaratibu uliowekwa kuhakikisha usalama, kutokwenda mbio, madereva kupewa elimu na hapo hapo wao kulindwa .

Usafiri wa magari moshi lakini ulikuwepo Uzunguni kabla ya mabasi.

Yamegawanyika. Ya ardhini na chini. Yote huenda kasi , na uvumbuzi unaondelea Japani sasa hivi umeainisha matreni yanayopaa mwendo wa sauti.

Ajali za matreni ni nadra sana – hutokea ndiyo- lakini si kama magari. Kwanza kwa vile magari moshi hayatumii barabara, hivyo hakuna ushindani na misongamano. Pili, hayachafui mazingira kwa moshi kama magari na ndege Ulaya. Tatu, matreni hubeba abiria wengi kuliko magari na mabasi.

Usafiri wa ardhini (Underground, Subway, Metro au Tubes), ulianzia Uingereza mwaka 1863.

Baadhi ya njia zilizojengwa London zingalipo hadi leo, na karabati huendelea kila siku. Inasadikiwa kiasi cha mapanya nusu milioni wanaishi ndani ya njia hizi zenye umri zaidi ya miaka 150. Usafiri huu ulioleta mapinduzi makubwa ya mwanadamu uliigwa na leo nchi zote zilizoendelea zina usafiri wa magari moshi ya ardhini.Vituo vingi vya magari moshi vilitumiwa kuwaficha wananchi wakati mabomu yakiangushwa London, vita vikuu vya pili vya dunia – 1939-45..

Nimeishi London miaka 20 na sijawahi kusikia magari moshi ya ardhini yakigongana au kufanya ajali. Ajali zinazotokea huwa ama zimesababishwa na magaidi au magari moshi juu ya ardhi ambapo dereva ama alikosea jambo au reli zilikuwa na mushkeli. Ni usafiri mzuri sana. Wastani wa mwendo ni kiasi cha kilometa 32 na kasi ni 96.

Nikiishi Brazil walijenga reli moja tu ardhini (Metro), mjini Rio De Janeiro. Wakazi walihisi salama zaidi kusafiri ardhini, kwa sababu, ni rahisi askari kuzuia milango na kushika majambazi.

Jambo jingine linaloofanya magari moshi kupendwa ni mwendo wake wa kasi.

Kiwastani London, ukitaka kwenda katikati ya jiji, ni rahisi zaidi kuchukua gari moshi kuliko basi au gari. Njia za matreni haya zimegawanywa vituo 270 – njia 11- , vinavyosafirisha wakazi milioni tano kila siku. Idadi ya wakazi jijini ni milioni nane. Hii ina maana robo tatu ya wananchi hutumia magari moshi kila siku. Penye abiria wengi zaidi ni Waterloo (milioni 95 mwaka 2015), Oxford Circus ( eneo la biashara na maduka), Kings Cross na Victoria (kusini ya jiji). Hairuhusiwi kuvuta sigara au kunywa pombe ndani ya vyombo vya usafiri , Uingereza.

Mwaka 2012, aliyekuwa Waziri wa Usafiri, Dk Harrison Mwakyembe alijitahidi kujenga reli iliyounganisha Dar es Salaam. Kitendo kilichangia sana kupunguza msongamano. Hadi sasa ni njia mbili tu za magari haya moshi. Tujiulize na sisi tungekuwa na hata nusu ya matreni yaliyojengwa nchi za wenzetu ingewafaa vipi wananchi ? Usafiri mzuri huhakikisha wananchi wanafanya kazi vyema na kuishi maisha ya furaha.

Hiyo ni tija na manufaa kwa taifa zima.