Matumizi duni ya pembejeo kushusha uzalishaji kahawa

Muktasari:

  • Mbali na kupungua kwa uzalishaji mwaka huu, hali ilikuwa hivyo mwaka jana uliposhuka kwa asilimia 30 kutoka tani 60,880 zilizopatikana mwaka 2016.

Dar es Salaam. Uzalishaji wa kahawa unatarajiwa kushuka kwa asilimia 8.43 kutoka tani 46,963.5 zilizopatikana mwaka 2017 hadi tani 43,000 mwaka 2018, ripoti ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) inaeleza.

Mbali na kupungua kwa uzalishaji mwaka huu, hali ilikuwa hivyo mwaka jana uliposhuka kwa asilimia 30 kutoka tani 60,880 zilizopatikana mwaka 2016.

Kupungua kwa uzalishaji huo, kumefanya lengo lililowekwa na TCB la kuzalisha tani 80,000 mwaka 2017 kutofikiwa kwa asilimia 41.29.

Ripoti inaeleza miongoni mwa changamoto zilizochangia kushuka kwa uzalishaji ni matumizi madogo ya pembejeo, hususan mbolea na mabadiliko ya hali ya hewa.

Pia, mambo hayo yamechangia kuwapo kwa uzalishaji duni katika mikoa ya Kagera, Ruvuma na Songwe ambayo inaongoza.

“Katika Mkoa wa Songwe uzalishaji ulipungua kwa asilimia 39.21, Ruvuma (20.72) na Kagera (18.08),” ripoti inabainisha.

Kuyumba kwa uzalishaji huo na ubora wa kahawa kuliweza kuathiri bei ya mkulima na kusababisha soko la mnada kumilikiwa na kampuni chache za nje.

Mkurugenzi mkuu wa TCB, Adolf Kumburu alisema wanajitahidi kukwamua wakulima na vyama vyao na kuongeza thamani ya zao ili waweze kuona fursa katika uzalishaji.

“Hata katika ile mikakati iliyokuwa imewekwa awali tunaifanyia marejeo ya muda wa kati na taarifa ya mshauri mwelekezi itawasilishwa ili kujua ni wapi tulijikwaa na tujipange upya,” alisema Kumburu.