Mgodi wasafirisha tani 500 za graphite kwenda maabara Canada

Muktasari:

  • Katika uzinduzi wa usafirishaji huo ulioshuhudiwa na Balozi wa Australia nchini, Alison Chartres mwishoni mwa wiki iliyopita, kupitia kampuni tanzu yake ya Mahenge Resource Limited, ilisafirisha tani 530 za madini hayo kwenda kupimwa kubaini aina ya mitambo inayofaa kuyachakata.

Matokeo yaelezwa yatabainisha mitambo inayohitajika

Morogoro. Kampuni ya Black Rock Mining inayotafiti madini ya kinywe (graphite) wilayani Mahenge mkoani hapa, imeanza kutumia reli ya Tazara kusafirisha sampuli ya madini hayo kwenda Canada kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa vipimo vya kimaabara.

Katika uzinduzi wa usafirishaji huo ulioshuhudiwa na Balozi wa Australia nchini, Alison Chartres mwishoni mwa wiki iliyopita, kupitia kampuni tanzu yake ya Mahenge Resource Limited, ilisafirisha tani 530 za madini hayo kwenda kupimwa kubaini aina ya mitambo inayofaa kuyachakata.

Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko, mjiolojia wa Kanda ya Mashariki, Theresia Ntuke alisema vipimo hivyo vitasaidia kujua mitambo itakayofaa kuanzisha uchimbaji kinywe wilayani Mahenge.

“Kwa kuwa mradi huu unategemewa kuwa faida kubwa kwa nchi, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika,” alisema Ntuke.

Madini ya kinywe hutumika katika utengenezaji kaboni za penseli, betri, breki, gasketi za injini na mitambo mingine. Kampuni ya Mehenge Resource imegundua zaidi ya tani milioni 69.9 za madini hayo wilayani hapa.

Ntuke alisema mgodi huo unatarajiwa kuzalisha tani 80,000 ambazo zitaongezeka mpaka tani 250,000 na kuiingizia Serikali zaidi ya Dola 100 milioni za Marekani (zaidi ya Sh228 bilioni) kwa mwaka kutokana na kodi na tozo mbalimbali.

Ofisa mtendaji mkuu wa Black Rock Mining Limited na mwenyekiti wa Mahenge Resources, John de Vries alisema mradi wa Mahenge unakadiriwa kuwa wa nne kwa wingi wa madini ya kinywe duniani.

“Matumizi ya usafiri wa treni ni mazingira salama ya uwekezaji wetu na sekta ya madini kwa ujumla, kwa kuwa unapunguza gharama,” alisema.

Naye meneja wa Tazara (Tanzania), Fuad Abdallah alisema mradi huo utainufaisha kampuni hiyo na kuleta mabadiliko ya uchumi Ifakara na Mahenge kwa kuongeza ajira na ujenzi wa miundombinu.

Aliwataka wakazi wa Ifakara kujipanga kunufaika na mradi huo.