Saturday, June 17, 2017

CASPER NYOVEST: ‘Mlokole’ anayetamba kwenye Hip Hop ya kidunia

Refiloe Maele Phoolo maarufu kwa jina la Casper

Refiloe Maele Phoolo maarufu kwa jina la Casper Nyovest 

Kinywele kimoja kinachoning’inia nyuma ya kichwa chake, swaga na aina ya maisha anaonekana mwana Hip Hop mgumu, lakini nyuma ya pazia ni ‘mlokole’ anayesali asubuhi na jioni na kutwa nzima husikiliza muziki wa Injili.

Huyu ni Casper Nyovest wa Afrika Kusini na Doc Shebeleza ni moja kati ya nyimbo zake nyingi zilizomtambulisha katika ramani ya muziki barani Afrika.

Ukiachana na Future, Diamond, Vanessa Mdee na Navy Kenzo Miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika Tamasha la Castle Light Unlocks Julai 22 mwaka huu ni Casper Nyovest.

Mwanamuziki huyu amefanya mahojiano na Mtandao wa Africa1 na kuzungumzia namna anavyoipigania imani yake katikati ya muziki wa Hip Hop.

Unawezaje kujieleza kwa sentensi tatu tu?

Nina malengo mengi ya kutimiza, siye mtu anayetabirika, nina badilika badilika.

Unawezaje kuishi katika dunia ya Hip Hop na ukabaki na imani yako?

Tunaishi kwenye dunia ambayo vijana wanaamini wanajua vitu vingi hasa kwa kuwa wanaweza kutafuta mtandaoni na kuvipata. Lakini, huwa kila siku ninajikumbusha wapi nilipotoka na kusudi la Mungu kwangu kuwapo duniani. Ninasali asubuhi na jioni kujikabidhi kwa Mungu.

Unasikiliza nyimbo gani siku hizi - unasikiliza nyimbo za kuabudu?

Mdogo wangu anacheza nyimbo za Hillsong muda wote. Kwa hiyo nalazimishwa kusikiliza nyimbo zao, lakini hata hivyo tumekua tukisikiza nyimbo za Hillsong tangu wadogo. Lakini, navutiwa zaidi na Mary Mary. Naweza kusema hao ndio ninaovutiwa nao zaidi.

Kitu gani kilikuvutia kuingia kwenye muziki?

Nilivutiwa na kaka yangu ambaye sasa ni marehemu, alikuwa shabiki wa muziki wa Hip Hop na kila mara nilimuona akiandika nyimbo. Nilianza kuandika kujifurahisha, lakini sasa ninaishi kwa kutegemea muziki wa Hip Hop.

Ulikutana na ugumu gani kabla ya kutoka?

Kupata mtu wa kuniamini na kucheza ngoma zangu. Tatizo kubwa lilikuwa unafanya kazi nzuri, lakini ukipeleka redioni naona wakati mwingine Dj alikuwa hata haisikilizi kazi yangu anaitupa kapuni. Nilijua siku moja nitaeleweka ndio maana sikukata tamaa. Niliendelea kupeleka kazi zangu.

Msanii gani anakuvutia?

Navutiwa zaidi na Kanye West, kwa hapa nyumbani navutiwa na HHP, halafu Drakes, Kendricks na J. Coles.

Ni yapi unahesabu kuwa mafanikio yako mpaka sasa?

Nadhani ni kuweza kuihudumia familia yangu. Ninachojivunia kingine ni kuweza kuujaza uwanja wa The Dome katika tamasha lililohudhuriwa na watu zaidi ya 20,000. Bado nina ndoto nyingi moja wapo ikiwa ni kumjengea jumba la kifahari mama yangu.

Sokoni kuna simu yenye jina lako hebu tueleze kidogo?

Ndio, nimeingiza sokoni simu yangu inayoitwa AG Hashtag. Ni simu nzuri na bei rahisi. Ninaomba Waafrika wainunue kwa sababu ni ya kwetu wote.     

-->