Sekta binafsi yaipa Serikali mbinu kufikia uchumi wa viwanda

Muktasari:

  • Hayo yalielezwa juzi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kufua umeme ya Songas, Nigel Whittaker wakati wa mkutano uliowakutanisha maofisa watendaji wakuu wa kampuni binafsi nchini (CEOrt), kujadili namna Serikali inavyoweza kuingia ubia na kampuni binafsi katika utekelezaji wa miradi mikubwa na faida zake.

Dar es Salaam. Dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania nchi yenye uchumi wa kati itafanikiwa kwa haraka iwapo itashirikiana na sekta binafsi kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Hayo yalielezwa juzi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kufua umeme ya Songas, Nigel Whittaker wakati wa mkutano uliowakutanisha maofisa watendaji wakuu wa kampuni binafsi nchini (CEOrt), kujadili namna Serikali inavyoweza kuingia ubia na kampuni binafsi katika utekelezaji wa miradi mikubwa na faida zake.

Whittaker alisema ushirikiano unarahisisha upatikanaji huduma muhimu, ambazo si Serikali wala kampuni binafsi pekee ingeweza kufanikisha kwa ufanisi.

Naye ofisa mkuu wa fedha wa Songas, Anael Samwel alisema lengo la Serikali kuwa na uchumi wa viwanda, litafanikiwa iwapo sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu. “Tunaona Serikali inatamani kuwa na viwanda vingi na katika hivyo inahitaji umeme, tunatambua juhudi za Serikali kuhakikisha unakuwapo umeme wa kutosha kwa ajili ya hivyo viwanda,” alisema Samwel na kuongeza:

“Tunaamini Serikali inabidi kufanya kazi kwa ukaribu na mashirika binafsi ili ifanye kazi hiyo kikamilifu, Songas ipo tayari kushirikiana na Serikali.”