JICHO LA MWALIMU : Shule inavyoweza kuchochea utalii

Muktasari:

  • Watanzania wamekuwa wakisemana vibaya kuwa hawana utamaduni wa kufanya utalii.
  • Sababu kadhaa zimekuwa zikitajwa kuwa kikwazo cha watu kufanya ziara za kitalii, ikiwamo umasikini, kutojengewa utamaduni huo tangu awali (shuleni/vyuoni, na katika familia).

Kumekuwapo  changamoto kubwa kwa wazawa katika kufanya utalii wa ndani ama wa nje ya nchi.
Watanzania wamekuwa wakisemana vibaya kuwa hawana utamaduni wa kufanya utalii.
Sababu kadhaa zimekuwa zikitajwa kuwa kikwazo cha watu kufanya ziara za kitalii, ikiwamo umasikini, kutojengewa utamaduni huo tangu awali (shuleni/vyuoni, na katika familia).
Nyingine ni gharama kubwa za viingilio na kutokuwa na taarifa za kutosha kama vile maeneo  yenye vivutio na namna ya ufikaji wake.
Utalii ni kitendo cha mtu kwenda kutembelea na kujifunza nchi na maumbile yake kijiografia.
Pia, utalii ni hali ya kusafiri huku na huko ili kuyafurahia mandhari.
Wengine husema kwamba hata kile kitendo cha wenyeji kusaidia au kushughulikia watalii na kuwahudumia nacho ni utalii.
Pia, utalii unahusisha kusoma desturi, tabia, utamaduni, miiko, matambiko na historia ya nchi au sehemu husika. Kuna aina mbalimbali za utalii kama vile  utalii wa kibiashara, kidini, mikutano, mapumziko, utamaduni,  historia na mazingira.
Utalii wa ndani ni kule kutembea kutoka mahali pamoja hadi pengine ndani ya nchi husika.
Tabia ya watu kuthamini na kufanya utalii wa ndani huweza kuchochewa sana kuanzia ngazi ya shule na vyuo.
Hii ni kwa sababu, shule ni wakala mkubwa wa mabadiliko na maendeleo endelevu. Mfano wa utalii rahisi kufanywa na jamii husika ni utalii wa baiskeli na wa kutembea kwa miguu.

Shule inawezaje kuwa wakala wa utalii wa ndani?
Ziara za mafunzo ni mbinu au njia mojawapo ya kujifunza na kufundishia shuleni au vyuoni.
Mwanafunzi hupata uelewa mkubwa anapotazama mazingira ya nchi kwa uhalisia. Madhumuni ya  utalii wa ndani hutofautiana kati ya sehemu moja ya utalii na nyingine.
Kuna uwezekano mkubwa wa shule kuandaa ziara za kimafunzo kwa madarasa tofauti katika kila kipindi cha likizo za masomo.
Kamati  za ziara za shuleni, hupaswa kuratibu maandalizi hayo kwa kutuma walimu kwenda kuona sehemu watakazopata malazi na chakula, watakazotembelea, na kama kuna shule wangependa kufanya nayo mtihani wa pamoja wa kujipima na kujua kiasi cha gharama.
Kama shule haziwezi kuandaa ziara hizi kupitia kamati maalumu za ziara, zinaweza kuomba huduma hiyo kutoka kampuni za utalii.
Kuna faida kadhaa za kutumia kampuni za utalii ili kufanikisha safari ya utalii au ziara za kimafunzo, ikiwamo kuokoa muda wa walimu kwenda kufanya mchakato wa maandalizi ya ziara husika.
 Aidha, kunapotokea dharura yoyote ile safarini, ni rahisi kampuni kushughulikia kwa kuwa kila siku wako katika michakato hiyo na ndiyo sehemu ya kazi zao.
Ikumbuke hata hivyo kuwa kutumia kamati za shule, pamoja na mambo mengine kunasaidia kupunguza gharama. Kampuni pamoja na kutoa huduma, bado zinafanya kazi hiyo kwa mrengo wa kibiashara unaolenga kupata faida.
Ni kwa vipi sasa  shule na vyuo zinaweza kuwa mabalozi wa utalii wa ndani? moja, kuwapa ufahamu na uelewa wanafunzi. Hii huwezesha jamii kufahamu kuhusu faida za utalii wa ndani na jinsi   wanavyoweza kuufanya.
Wanafunzi ni mabalozi wakubwa wa mabadiliko katika jamii. Wanapopata elimu huweza kuifikisha kwa wazazi na walezi kisha kwa jamii nzima.
Pia, wanafunzi ni wazazi wa kesho, watarithisha maarifa hayo kwa vizazi vijavyo.
Kwa kupitia shule na vyuo, tabia ya kupenda kufanya utalii wa ndani inaweza kukuzwa, kwa sababu ya uhamasishaji kutoka kwa wadau mbalimbali wenye uelewa wa utalii na kampuni zote zinazojishughulisha na utalii.
Mbili, mamlaka ya hifadhi za taifa huweza kutia chachu utalii wa ndani kwa kutoa punguzo za viingilio kwa wanafunzi na wanachuo, siyo tu katika kipindi cha sherehe za sabasaba na nanenane; ambapo wanufaika wengi huwa wale tu ambao walipata fursa ya kutembelea maonyesho hayo.
Tatu, shule kueleza fursa zinazoweza kuwanufaisha wanajamii ambao wameizunguka hifadhi ya taifa.
Kumekuwapo changamoto kadhaa kutoka kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi, ikiwamo kutoona  moja kwa moja  faida za utalii.
Hivyo, jamii hiyo huweza kusababisha mikwamo kwa watalii kama vile kutowapa ushirikiano stahili.
Nne, kupitia uhamasishaji kutoka vyombo vya habari na mawasiliano. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, vinaweza kuhamasisha utalii wa ndani.
Tano, mitalaa yetu ya elimu katika ngazi zote ziweke suala la utalii wa ndani kama suala mtambuka.
Ikiwezekana suala la utalii wa ndani lichopekwe katika masomo mbalimbali.
Mtaalamu wa masuala ya utalii na uhifadhi wa tamaduni, Ismail Swalehe, anaeleza kuwa sekta binafsi inayojishughulisha na utalii kama kampuni za utalii, bado hazijachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha jamii ya Kitanzania kufanya utalii wa ndani tofauti na wanavyofanya kwa watalii kutoka nje.
Anaeleza kuwa ni wakati sasa wa mamlaka husika kuziwezesha kampuni binafsi na vyama vya kijamii vinavyokuza utalii.
Shule nazo ziwajengee wanafunzi misingi ya kupenda na kuthamini utalii wa ndani tangu wakiwa watoto na vijana.
Siyo rahisi kwa mtu ambaye hakujengewa tabia ya kutumia kipindi cha likizo kwa kufanya ziara au utalii, akategemewa tu kuibuka ukubwani na kuanza kufanya.
Hata kama ana rasilimali na uwezo, bado hatoweza kufanya kwa sababu jambo hilo siyo sehemu ya utamaduni wake.
Hivyo, ni wajibu wa kila shule na chuo kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanapata fursa nyingi za kufanya utalii wa ndani mara nyingi iwezekanavyo.
Shule na vyuo zijenge tabia ya kutumia likizo kufanya ziara za kitalii. Kufanya hivi ni  kuchochea ari ya utalii wa ndani na kulinda na kuzithamini rasilimali zetu.