JICHO LA MWALIMU : Sifa ya mwanafunzi ni taaluma na nidhamu

Muktasari:

  • Wengi wamekuwa wakifanya uchaguzi wa shule kwa ajili ya watoto wai kutokana na kutazama ufaulu katika matokeo ya mitihani ya taifa.

Licha ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya shule na vyuo nchini,  kumekuwapo na changamoto kwa jamii kubaini ipi ni shule ama chuo kilicho bora.
Wengi wamekuwa wakifanya uchaguzi wa shule kwa ajili ya watoto wai kutokana na kutazama ufaulu katika matokeo ya mitihani ya taifa.
Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili, taaluma ni ujuzi au maarifa yanayopatikana kwa kusoma au kufundishwa darasani.
Wakati mwingine taaluma hutafsiriwa kwa kufananishwa na elimu.
Elimu ni jambo lolote analoambiwa mtu au jamii kwa lengo la kuelimishwa na kuelewa.
Mtu huweza kupata elimu kutoka sehemu mbalimbali ambazo zipo katika mfumo ulio rasmi au usio rasmi.
Nidhamu ni staha, heshima, taadhima au tabia njema aliyonayo mtu mbele ya watu katika jamii anayoishi.
Pia, nidhamu ni utaratibu wa kuendesha jambo kulingana na maelezo au maelekezo yaliyotolewa.
Kwa mwanafunzi au mwanachuo, taaluma na nidhamu haviwezi kutenganishika; ni kama chanda na pete.
Ili mwanafunzi aendelee kufanya vizuri kitaaluma na katika maisha yake ya baadaye, anapaswa kuwa na nidhamu.
Nidhamu humwezesha kushirikiana na watu wengine bila tatizo; humsaidia katika kazi  na kuwa raia mwema mwenye mchango kwa maendeleo endelevu ya taifa lake.
Sifa za mwanafunzi bora
Mwanafunzi bora anapaswa  kuwa na nidhamu; kuwa mdadisi na mbunifu; kuwa na ushirikiano na wenzake na kuwa na mazoea ya kuwahi shuleni.
Nidhamu siyo tu kwamba huhitajika  kwa mwanafunzi awapo shuleni tu,  la hasha. Nidhamu inapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtu.
Kimsingi, mtu hawezi kutenganisha mafanikio yoyote na nidhamu, kwani ni kiini cha utiifu katika kukamilisha mipango ambayo mtu amejiwekea.
Mwanafunzi anapokuwa shuleni au chuoni kuna mambo mengi anayopaswa kuyakamilisha kabla ya muhula, mwaka au miaka kuisha.
Watunga mitalaa huandaa idadi ya masomo au kozi kulingana na muda, hivyo wanafunzi hawana budi kutambua kuwa kila sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi au mwaka ni muhimu vikatumika kinidhamu ili kuweza kukamilisha malengo yao ya kitaaluma.
Wapo baadhi ya wanafunzi wanaozembea katika miaka ya mwanzo kabla ya kufikia mwaka ule wa kufanya mitihani wa mwisho au wa taifa.
Ni vizuri wakafahamu kwamba mafanikio yao ya kitaaluma hujengwa kwa jitihada ndogondogo za muda mrefu na sio kungojea mtihani ndio wachukue hatua za maandalizi.
Watu wengi waliofanikiwa na wanaoendelea kufanikiwa kama viongozi au wafanyabiashara mashuhuri, wote  huwa na nidhamu katika utendaji wao wa kazi.  Hawa aghalabu wana nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha zao au nidhamu ya kufuata miiko na maadili ya taifa.
Watu wengi huwa na ndoto za kufanya mambo makubwa maishani, lakini, huishia kutekeleza kwa kiwango cha asilimia 50. Ni   nidhamu pekee ya kuamini kile wanachofanya kwa usahihi kwa wakati sahihi, ndio huwasukuma kuendelea kuzisogelea ndoto zao mpaka wanapozitimiza.
Kwa mfano, kama ambavyo inafahamika kuna wakati wanafunzi hupaswa kuelekezwa na kufuatiliwa na walimu wao ili waweze kutimiza lengo la kuwapo shuleni kupata elimu bora.
Shule ni kama mfereji wa maji uliounganishwa kutoka mtoni au katika bomba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mkulima alichimba mfereji wa maji kwa kuwa ana lengo ambalo ndilo humuongoza kutafuta maji hata kama ni kutoka umbali kiasi gani. Lengo lake ni kupata mazao bora.
Vivyo hivyo, jengo la shule huwaelekeza wanafunzi katika lengo la maisha bora. Wanafunzi wapate maarifa na kukua kimwili, kiakili, kijamii na kiroho. Hapo ndipo nidhamu yao pia huingia.
Kwa asili, maji husafiri kutokana na kani ya uvutani ya dunia (gravitation force) itakapoyataka yaende kama hakuna mfereji wa kuyaelekeza.
Vivyo hivyo, akili ya mwanafunzi hupenda  kujaribu kila jambo kwenda kila upande; hapo ndipo nidhamu huhitajika ili kumpa njia ipasayo kufuata kama ilivyo kwa mfereji wa maji.
Kuchimba mfereji na kulinda nidhamu shuleni si jambo rahisi. Kwani maji katika mfereji na wanafunzi shuleni au vyuoni, hujaribu kukwepa kuongozwa.
Maji yatajaribu kuvuja sehemu yenye ufa katika mfereji au kupanda kuta za mfereji huo kama hazina urefu wa kuyazuia. Wanafunzi nao watajaribu kukwepa maelekezo na sheria kama nidhamu haitawekewa mkazo ipasavyo.
Mwanafunzi ni kama maji na nidhamu shuleni ni kama kuta za mfereji wa maji. Maji yataenda vizuri na kwa matumizi yaliyokusudiwa, endapo yatafuata mfereji ulio imara na madhubuti.
Vivyo hivyo mwanafunzi atafanya vizuri katika masomo na maisha yake kama nidhamu itatiliwa mkazo shuleni.
Wanafunzi wana wajibu mkubwa katika kujenga maadili mema wakiwa shuleni. Na maadili haya yawe mazuri na yaliyojikita katika taratibu zinazokubalika na jamii nzima kwa faida ya taifa na vizazi vijavyo.
Mwanafunzi bora mwenye maadili mema hana budi kujenga utamaduni wa kujitegemea hasa katika masomo. Hili  husaidia kujenga moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Mafanikio ya shule kuwa na nidhamu huchagizwa pia kutokana na uhusiano mzuri baina ya wazazi na walimu.
Wapo baadhi ya wazazi wanaolaumu na kuvunja moyo juhudi za walimu za kupambana na utovu wa nidhamu shuleni.
Wazazi hawa ama huwajia  juu walimu kukataa kuitikia  wito wanapoombwa kufika shuleni na kuelezwa tabia za watoto wao.  Wapo wanaofikia hatua ya kuwafanyia vitendo vya ubabe walimu, ikiwamo kuwadhuru.
Ni vema jamii kwa pamoja ikaendelea kuweka mkazo  kwamba taaluma inapaswa kuendana sambamba na nidhamu.
Hii itasaidia  kuwa na taifa lenye watu wachapa kazi, wabunifu, wenye mtazamo chanya na wenye nidhamu ya kulinda rasilimali za taifa kwa faida ya vizazi vijavyo.