MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tujiepushe na makosa haya katika Kiswahili

Muktasari:

Miongoni mwa maneno ambayo watumiaji wa lugha wamekuwa wakiyatumia kwa makosa, ni pamoja na ‘pelekea’, ‘misamiati’, ‘agenda’, ‘makaratasi’, ‘mataa’, ‘tutakwenda ku...’ na mengineyo kama inavyofafanuliwa katika makala haya.

        Katika muktadha wa utumiaji wa Kiswahili, baadhi ya watumiaji hutumia maneno ya lugha visivyo kiasi cha maneno hayo kuzoeleka na kuonekana ni sahihi.

Miongoni mwa maneno ambayo watumiaji wa lugha wamekuwa wakiyatumia kwa makosa, ni pamoja na ‘pelekea’, ‘misamiati’, ‘agenda’, ‘makaratasi’, ‘mataa’, ‘tutakwenda ku...’ na mengineyo kama inavyofafanuliwa katika makala haya.

Watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili hupenda kulitumia neno ‘pelekea’. Kwa mfano, mtumiaji wa lugha huweza kusema, “Matumizi mabaya ya mali za umma yamepelekea Tanzania kuwa maskini.”

‘Pelekea’ si neno fasaha la Kiswahili linapotumika katika muktadha kama huo. Neno hili ni matokeo ya tafsiri sisisi kutokana na maneno ya Kiingereza ‘leading to’. Kisawe cha maneno hayo ni ‘sababisha’.

Kwa hivyo, sentensi hiyo ingepaswa kuwa; “Matumizi mabaya ya mali za umma yamesababisha Tanzania kuwa maskini.” Viongozi wengi hususan wa kisiasa hupenda kulitumia neno hilo.

Ifahamike kwamba neno hilo siyo fasaha katika Kiswahili badala yake neno ‘sababisha’ litumike.

Neno jingine linalotumiwa vibaya ni ‘msamiati’. Hili hutumiwa hivyo katika umoja na wingi. Kwa hiyo, mtumiaji wa lugha hapaswi kutamka ‘misamiati’ anapozungumzia dhana ya wingi. Makosa katika matumizi ya neno hili hufanywa na watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili.

Mathalani, mtumiaji wa lugha huweza kusema, “Kiswahili kina misamiati migumu” badala ya “Kiswahili kina msamiati mgumu.” Watumiaji wa Kiswahili wajue kwamba wingi wa neno ‘msamiati’ ni ‘msamiati’ na si vinginevyo.

Aidha, neno ‘agenda’ ni la Kiingereza ambalo hutumika zaidi katika miktadha ya vikao/mikutano. Kisawe cha neno hilo katika Kiswahili ni ‘ajenda’. Neno hilo lina maana ya ‘orodha ya mambo yatakayozungumzwa katika mkutano’. Hata hivyo, watumiaji wengi wa Kiswahili katika kutamka na kuandika, hutumia neno ‘agenda’ kimakosa badala ya neno linalotakiwa ambalo ni ‘ajenda’.

Pia, kuna matatizo ya matumizi ya neno katika ‘karatasi’. Wingi wa neno hilo ni ‘karatasi’ na siyo ‘makaratasi’ kama wengi wapendavyo kulitumia.

Kwa mfano, mtumiaji wa lugha huweza kusema; “Makaratasi ya kujibia mtihani yameisha” badala ya kusema “Karatasi za kujibia mtihani zimeisha.”

Vilevile, wingi wa neno ‘taa’ ni ‘taa’ na siyo ‘mataa’. Lakini katika miktadha mbalimbali ya utumiaji wa lugha, baadhi ya watumiaji wa lugha hutumia neno ‘mataa’ katika dhana ya wingi jambo ambalo ni makosa.

Siku za hivi karibuni kumezuka mtindo wa utumiaji wa Kiswahili ambao hauna mantiki. Matumizi ya maneno ‘tutakwenda ku...’ hasa katika mazingira ambayo uwasilishaji hufanyika mathalani katika miktadha ya mihadhara, utoaji wa mahubiri, matangazo studioni. Huku ni kufanya makosa.

Kwa mfano, mtangazaji wa kipindi studioni anaposema, “Katika kipindi hiki cha leo tutakwenda kujadili namna ugonjwa wa Ukimwi unavyoambukizwa.”

Swali linalokuja ni kwamba, ‘tutakwenda kujadili wapi ilhali tupo studioni?’ Hiyo ni kasoro kubwa. Badala yake mtangazaji angepaswa kusema, “Katika kipindi hiki tutajadili...” Matumizi hayo potofu ni athari ya tafsiri sisisi itokanayo na Kiingereza ‘Today we are going to...’

Watumiaji wa Kiswahili hatuna budi kutumia Kiswahili kwa ufasaha ili kila mmoja kwa nafasi yake aweze kuwa mwalimu kwa wanaotusikiliza na kujifunza kama lugha ya kigeni au lugha ya pili.

Tukiwa wabanangaji tutawapotosha wajifunzaji hao. Viongozi, wanahabari, wachungaji, walimu na watumiaji wengine, tufanye maandalizi tunapoandaa uwasilishaji wetu.