‘Tume itamtangaza mshindi, si vinginevyo’

Muktasari:

  • Wakati siku zikihesabika kuelekea siku ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43, Tume imetembelea baadhi ya vyombo vya habari na kutoa elimu hiyo.

Uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni moja kati ya hoja zinazoulizwa mara kwa mara hasa pale watendaji wa Tume wanapokuwa katika jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura.

Wakati siku zikihesabika kuelekea siku ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43, Tume imetembelea baadhi ya vyombo vya habari na kutoa elimu hiyo.

Akizungumzia Uhuru wa Tume kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi cha Redio E FM, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani anataja majukumu ya Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasema ni kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura na kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano na uchaguzi wa madiwani kwa Tanzania Bara.

Majukumu mengine anayataja kuwa ni kuchunguza mipaka na kugawa majimbo, kutoa elimu ya mpiga kura na kuteua na kuwatangaza wabunge na madiwani wanawake wa Viti Maalum.

“Ibara ya 74 (11) ya Katiba, inasema katika kutelekeza majukumu hayo, Tume haitafuata amri au maelekezo ya mtu yeyote, idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote.

“Na kwenye ibara ya 74 (12), Tume ikishatekeleza majukumu yake, hakuna mahakama yoyote itakayohoji. Huo ndio uhuru wa Tume,” anasema Kailima.

Kailima anasema uhuru huo hauna mashaka ingawa wengi wanahoji uteuzi wa watendaji wa Tume.

Asema kuwa pamoja na mashaka hayo, hakuna shinikizo lolote Tume imewahi kupata katika kuteleza majukumu hayo.

Anabainisha kuwa majukumu yote ya Tume yaliyotajwa kwenye ibara za Katiba kuanzia ibara ya 5 hadi Ibara ya 98 na yote ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mita, yaliyotajwa kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Wilaya Namba 287, Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Miji Namba. 288, hakuna ambalo linasemwa na Tume haijalitekeleza.

“Dhana yao ni kusema nani kamteua nani. Hoja si nani kamteua nani, hoja mlipoteuliwa uhuru wenu ulioko kwenye Katiba mmeutekeleza?”

Alitolea mfano wa nchi za Ghana, Kenya na moja ya Ulaya na kueleza kuwa:

“Hakuna Tume ya Uchaguzi iliyokuwa inaaminiwa kama Tume ya Ghana kwa sababu haiteuliwi na Rais, lakini bado wanailalamikia. Kenya jirani zetu nadhani mmeona, iliyopo ni Tume ya pili baada ya Katiba Mpya ya Kenya, Rais wa Kenya hateui na mchakato uko wazi na watendaji wanasailiwa kila mtu anaona lakini wanailalamikia.

“Nimekwenda nchi moja ya Ulaya kuangalia uchaguzi wao karibu mwezi mmoja uliopita, Tume yao inateuliwa na wanaogombea, lakini ukiwauliza wanakwambia Tume yetu ni huru kwa sababu Katiba imesema tutekeleze haya na tunatekeleza majukumu hayo.

“Hapa kwetu kuna maeneo mengi tu hicho chama tawala kimekosa ushindi na tukakitangaza chama cha hao wanaolalamika, hata hicho chama tawala wanailalamikia Tume, kwamba mbona hapa hivi, tunawaambia ‘no’, ni kwa mujibu wa Sheria na Katiba tumetekeleza majukumu yetu.”

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi mdogo, Kailima anasema yanakwenda vizuri na wagombea 151 wakiwemo wanaume 140 na wanawake 11 kutoka vyama 12 ndio watakaopigiwa kura.

Anasema baadhi ya vifaa vya uchaguzi vimeshakwenda kwenye kata zinazofanya uchaguzi na vilivyobakia ni karatasi za kura ingawa karatasi za mfano za kura zimekwenda ili zitumike kuwanadi wagombea kwenye mikutano ya kampeni.

“Vyama vyote vimethibitisha usahihi wa karatasi kwa hiyo Tume inatarajia tarehe 23 karatasi za kura halisi na karatasi za matokeo zitasafirishwa” anasema Kailima.

Akizungumzia siku ya uchaguzi, Kailima anavishauri vyama vya siasa kuzingatia amani na utulivu kwa sababu vyama ni wadau wakuu wa uchaguzi.

Anaongeza kuwa uchaguzi utakuwa wa amani na utulivu iwapo vyama vitaamua vyenyewe kuwa na utulivu na namna ambavyo vitasimama kwenye mikutano ya kampeni na kuwashawishi wanachama wao wafanye nini itachangia utulivu wa hali ya juu.

“Tume tumejiandaa na tunategemea kutakuwa na uchaguzi wenye amani na utulivu na tunavisihi na kuvishauri vyama vya siasa viwashawishi wapenzi na wanachama wao wafuate utaratibu kwenye vituo vya kupigia kura na baada ya kupiga kura waenda nyumbani matokeo yatatoka,” anasema.

Kailima anakumbusha kuwa Tume imetoa fursa kwa ambao kadi zao zimepotea, zimeharibika au zimechakaa kutumia leseni za udereva, vitambulisho cha Taifa na hati za kusafiria.

“Watumie fursa hiyo wakapige kura lakini masharti ni lazima awe ameandikishwa, jina lake liwepo kwenye daftari na majina yafanane kwenye daftari na kwenye vitambulisho,” anasema.

Anaviasa vyama vya siasa vitumie kampeni kunadi sera zao na kuhamasisha wapenzi na wanachama wao kwenda kupiga kura na wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na wahudhurie kampeni zinazoendelea.

“Tume itatangaza yule ambaye atakuwa ameshinda kwa mujibu wa kifungu namba 70 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa na si vinginevyo,” anasema Kailima.

Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata 43 unatarajiwa kufanyika Novemba 26, 2017 na kampeni zinamalizika Novemba 25 mwaka huu.

Mwandishi ni Afisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa maswali na maoni tuma kwenda [email protected]