Uhamasishaji, udhibiti utasaidia kukuza sekta ya bima

Muktasari:

  • Changamoto iliyopo ni wengi kutoifahamu vyema sekta ya bima na kuzitumia huduma zake jambo linaloishawishi Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) kuelekeza nguvu nyingi kwenye eneo hilo.

Ni kawaida mtu anapougua kuulizwa kama anatumia Bima ya Afya au atalipa kwa fedha taslimu hivyo kuwafanya wananchi wengi kuifahamu bima hiyo.

Changamoto iliyopo ni wengi kutoifahamu vyema sekta ya bima na kuzitumia huduma zake jambo linaloishawishi Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) kuelekeza nguvu nyingi kwenye eneo hilo.

Hali hiyo inajitokeza ingawa, kwa miaka mitatu iliyopita, uchumi ulipokuwa unakua kwa wastani wa asilimia saba, sekta hiyo nayo ilishamiri kwa kiasi hicho. Licha ya kasi hiyo ya ukuaji, wananchi wengi hasa wa kipato cha chini hususan vijijini si wanufaika wakubwa wa sekta hiyo muhimu.

Vijijini ambako takwimu zinaonyesha ndiko kwenye wakazi wengi zaidi wanaojishughulisha na kilimo, elimu haijafika ya kutosha.

Kamishna wa Bima nchini, Dk Baghayo Saqware anasema Tira ni mamlaka inayowajibika kuweka mazingira wezeshi ya kukua kwa soko la bima, kwa sasa inakusanya taarifa za sekta ya kilimo ambazo zitawasaidia watoa huduma kupanga namna ya kufanya biashara.

“Data zilizopo sasa hivi si jumuishi lakini tunashirikiana na Wizara ya Kilimo kuandaa data zitakazowezesha kampuni za bima kujua hatari zilizopo katika zao fulani ili ziweze kupanga vizuri. Wengine wanaweka bima kutokana na mbegu lakini hiyo si ya kuaminika sana,” anasema Saqware.

Kutokana na data zinazoandaliwa, anasema kampuni za bima zitaweza kujua hasara inayoweza kujitokeza eneo fulani hivyo kuwa rahisi kupanga namna watakavyoona inafaa.

Mkakati

Alipokuwa akizindua mpango wa pili wa Taifa wa huduma jumuishi za fedha mwaka 2018 hadi 2022 mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mkakati uliopo ni kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia huduma za bima kutoka asilimia 45 waliokuwapo mwaka 2017 hadi asilimia 50 mwaka 2022.

Katika utekelezaji wa mkakati huo, mwezi uliopita, Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) ulitoa Sh407 milioni kusaidia kuhamasisha wananchi kutumia bima.

Ufadhili huo ulitolewa kwa Tira kwa lengo la kusaidia utoaji elimu kwa wananchi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.

Kamishna Saqware anasema changamoto kubwa inayowafanya wananchi kutotumia huduma za bima ni uelewa mdogo wa huduma hiyo.

Changamoto nyingine zinazochelewesha ukuaji wa sekta hiyo anasema ni kutokuwa na kiwango cha ukomo cha tozo ya bima (premium) kwa baadhi ya huduma na ukosefu wa ubunifu kuwa na bidhaa zitakazowafaa watu wenye kipato cha chini.

“Sekta ya bima imekua kwa asilimia saba kwa miaka mitatu iliyopita, changamoto zilizopo zikitatuliwa tutaweza kupiga hatua zaidi,” anasema Saqware.

Meneja wa kampuni ya bima ya Sanlam, Wilson Mnzava anasema uwepo wa bima mbadala kama vile Vicoba vinavyoruhusu wanachama wake kuchangia pindi mmoja kati yao anapokuwa na tatizo.

“Wananchi wana uelewa mdogo kuhusu huduma za bima,” anasema.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuna kampuni 31, madalali zaidi ya 150, mawakala zaidi ya 150 na wakadiria hasara za bima zaidi ya 50. Licha ya kuongeza watumiaji, mkakati unalenga kujenga uwezo wa wataalamu wa huduma hiyo pia.

Mmoja wa mawakala wa bima nchini, Salum Ramadhan anasema wapo Watanzania wanaonunua vitu vya thamani lakini hawavikatii bima.

“Kama ilivyo kwenye afya, baadhi ya huduma inatakiwa iwe lazima kuwa na bima. Hamasa iongezwe ili wananchi watambue na kuwa tayari kujiunga,” anasema.

Marekebisho ya sheria mbalimbali za maliasili za nchi yaliyofanyika mwaka jana inawataka wawekezaji kutumia bima za nchini kwenye shughuli zao zote.

Tira inao mfumo wa unaoratibu bidhaa zinazoingia nchini ambazo zimekatiwa bima kwenye kampuni za ndani (Tanzania Imports Insurance Portal).

Mfumo huo wa kimtandao ulianzishwa Januari Mosi ili kutoa fursa kwa waagizaji kukata na kulipia bima za bidhaa zao na mpaka sasa watoa huduma hao wamefanya biashara yenye thamani ya Sh409 milioni.

“Kwa miezi mitano tangu kuanza kwa mfumo huo kampuni zilizosajiliwa zimeingiza Sh409 milioni. Ni soko ambalo liko wazi, watu wachangamkie fursa,” anasema Saqware.

Kwa kampuni ambazo hazijasajiliwa, anasema zinaisababishai Serikali hasara ya Sh84 bilioni kutokana na kutojiunga na mfumo wa uhakiki wa bima kielektroniki (Tira-Mis) ulioanzishwa mwaka mmoja uliopita.

Kutokana na kutosajiliwa, baadhi ya kampuni hazipati taarifa zao katika mtandao hivyo kusababisha watu kuendelea kuuziana stika bandia ambazo kama zingeuzwa kihalali zingesaidia kukuza sekta.

Watoa huduma

Mwenyekiti wa chama cha madalali wa bima Tanzania (Tiba), Mohammed Jaffer anashauri kampuni za bima kufungua matawi vijijini kuhakikisha huduma hiyo inapatikana maeneo yote sanjari na kutoa elimu.

“Serikali inapaswa kuja na mpango mkakati utakaoziwezesha benki kuuza bima kwa watu binafsi jambo litakalosaidia kukuza sekta hiyo hususan maeneo ya vijijini tofauti na mjini ambako kuna mawakala na madalali wengi wa bima,” anasema.

Vilevile, anasema Serikali iweke mazingira rahisi kwa soko la kati ili kuruhusu madalali na mawakala wengi zaidi kushiriki katika mauzo ya bidhaa za bima kwa wingi ndani ya nchi.

Kampuni za ndani

Pamoja na kuwapo kwa kampuni nyingi nchini, takwimu zinaonyesha huwa zinakosa takribani Sh300 bilioni kila mwaka kutokana na kutokuwa na mtaji mkubwa kutoa huduma kwa miradi ya fedha nyingi.

Mapema Januari, Tira iliidhinisha waraka unaokusudia kuimarisha ustawi wa kampuni za ndani ikiwa ni jitihada za kupunguza wimbi la kampuni za nje kutawala biashara hiyo nchini hata pale ambapo kampuni za ndani zina uwezo wa kufanya hivyo.

Dk Saqware anasema kwa sasa kampuni za ndani zinahudumia soko kwa asilimia 57 tu na asilimia 43 zinazobaki zinahudumiwa na kampuni za nje kupitia bima mtawanyo ambako zaidi ya Sh300 bilioni huelekezwa huko.

Anasema shughuli za bima zikifanywa zaidi na kampuni za ndani zitaongeza mzunguko wa fedha katika taasisi za fedha na benki za biashara nchini hivyo kukuza mtaji wa wajasiriamali na uchumi kwa ujumla.

Changamoto zilizopo kwenye bima mtawanyo, anasema ni ushiriki hafifu wa kampuni za ndani katika kutoa bima za majanga makubwa. Vilevile, kampuni za ndani, anasema zinatoa upendeleo kwa kushirikisha kampuni za nje zaidi kuliko za ndani.

“Baadhi ya kampuni hufanya biashara na kampuni za nje zisizo na viwango, kukosekana kwa uwazi katika biashara hiyo na baadhi ya kampuni kupeleka nje biashara ambazo muda wake umeisha ni miongoni mwa mapungufu yanayotakiwa kufanyiwa kazi haraka,” anasema Dk Saqware.