Ukarabati Jangwani Yanga mpya inakuja na kuondoka

Monday October 23 2017

 

By Thobias Sebastian, Mwananchi

Desemba 2010, aliyekuwa mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji alianza ukarabati wa jengo ikiwamo kupakwa rangi ili liendane na hadhi yake na baada ya hapo, aligeukia ukarabati wa Uwanja wa Kaunda.

Manji alisema, anataka kuifanya klabu kuwa ya kisasa kwa gharama ya zaidi ya Sh900m. Klabu hiyo chini ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Imani Madega, anasema uwanja wa Kaunda, hadi kukamilika kwake ulitakiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 15, 000 waliokaa.

Itakumbukwa Madega alisema baadhi ya mechi za Ligi Kuu kuanzia mzunguko wa pili wa msimu huu zichezewe Uwanja wa Kaunda.

Vilevile, ikumbukwe kuwa mwishoni mwa Novemba 2010, Manji aliwahi kutishia kujitoa kuifadhili klabu hiyo huku akiwalalamikia watendaji wa Yanga wamekuwa wazito katika kuchangamkia vitu vya maendeleo akitolea mfano duka la klabu hiyo ambalo ni wazi hadi leo halijapangishwa.

Kuliundwa kamati ya kuhakikisha watu waliovamia kiwanja cha Yanga, Mitaa ya Twiga na Jangwani wanaondolewa ili ujenzi wa uwanja uanze mara moja, lakini watu hao wamekuwa wazito kitu ambacho kinamkatisha tamaa.

Awamu mpya

Ikaja awamu nyingine. Mwaka 2013/14 Yanga ikaja na mpango mkakati wa kuitengeneza Jangwani mpya. Ilikuwa ianze kwenye jengo.

Mkakati ukaandaliwa na wazee wa Yanga, walipanga kufanya maandamano kwenda Ikulu kukutana na Rrais Jakaya Kikwete iwapo ofisi ya Meya ya Manispaa ya Ilala itashindwa kuwajibu ombi lao la kuongezewa eneo ili wajenge Uwanja wa kisasa wa michezo katika eneo la Jangwani pembeni ya klabu yao.

Katika kuonyesha imedhamiria kufanya mabadiliko, wazee waliandaa maandamanao na uongozi wa Yanga uliiandikia Polisi barua kuomba kibali ili wafanye maandamano hayo leo.

Itakumbukwa barua hiyo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu ilisema kuwa uamuzi wa kuitisha maandamano hayo umetokana na Manispaa ya Ilala kuchelewesha maombi yao ya kuongezewa eneo la ujenzi wa Uwanja, hivyo wao wameamua kuandamana kisheria.

Aliyekuwa Meya wa Ilala wakati huo, Jerry Slaa akilizungumzia suala hilo la Yanga kushindwa kuongezewa eneo ili wajenge uwanja, alisema suala la uwanja wa Yanga lina wadau wengi likiwamo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Ardhi, kwani yeye binafsi ana nia ya dhati kuhakikisha jambo hilo linakwisha, lakini hawezi kufanya bila ya kufuata taratibu.

Alisema moja ya taratibu ni kujadiliana na viongozi wa Yanga, pia uongozi wa Manispaa ya Ilala kufanya ziara Jangwani kukagua eneo ambalo Yanga wanataka waongezewe na kutoa uamuzi.

Uongozi wa Manispaaa ya Ilala unataka kukagua eneo hilo la Jangwani kwa sababu unataka kujua eneo ni lipi, lina ukubwa gani, linaathiri nani, uwanja wa aina gani na mengine mengi.

Desemba mwaka 2011, uongozi wa Yanga ulitoa ahadi ya kujenga uwanja wa kisasa eneo la Jangwani huku ikimtangaza mkandarasi, Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwamba ndiye atakayejenga uwanja huo mpya.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ujenzi huo wa uwanja unatakiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000, lakini hadi sasa hakuna hata dalili za kuanza huku viongozi wa Yanga wakisema Serikali inawanyima eneo la nyongeza kwa sababu eneo la sasa ni dogo.

Ukiacha uwanja wa mpira wenye viti 40,000, Yanga pia wanadai wanataka kujenga katika eneo hilo hosteli, ya wachezaji na shule/akademia ya soka, viwanja vya mazoezi, eneo la kuegesha magari, hoteli na sehemu ya makazi, ukumbi wa mikutano, maofisi, benki, zahanati, maduka makubwa, ukumbi wa sinema na sehemu za kupumzikia.

Mipango hiyo ni kama imekufa na sasa Yanga inakuja na mipango mingine. Hebu fuatilia.

Mikakati inayoendelea

Unaweza kusema ni habari zinazotia matumaini japo mwanga wake uko mbali. Hakuna mkakati hasa unaounganisha mkandarasi na fedha za ujenzi wa uwanja wa kisasa kama ilivyotajwa kwenye mkakati wa pili uliokwama.

Kwa sasa viongozi wa timu hiyo wameamua kujitoa kipaumbele katika kusimamamia matengenezo ya Uwanja wa Kaunda ambao upo katika makao makuu ya klabu hiyo.

Gazeti hili lilitembelea makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani ambapo ndipo unapatika uwanja huo na viongozi wa mabingwa hao wa kihistoria wa ligi kuu Bara, walifunguka kuhusu uwanja pamoja na jengo la makao makuu ya klabu.

Kila kiongozi alifunguka kwa nafasi yake na kueleza matengenezo ya uwanja na jengo hilo ambalo miaka ya nyuma lilikuwa likitumika na wachezaji kwa kuweka kambi na shughuli nyingine nyingi kwa manufaa ya klabu.

Kauli za viongozi kwa sasa, Clement Sanga, Kaimu Mwenyekiti wa Yanga anasema kuna makundi zaidi ya 400, ya mashabiki wa Yanga wanataka kutumia mashabiki hao ili kubadili klabu ambao wapo tayari kujitolea kuisaidia klabu yao kwa hali na mali.

Ukarabati wa uwanja unaendelea na upo katika hatua za awali kuhakikisha tunakuwa na kiwanja chetu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma lakini licha ya kuwa na marekebisho ya uwanja kuna marekebisho mengine ya jengo tunayafanya.

“Mashabiki wa Yanga wakae mkao wa kula mambo mazuri yanakuja juu yao ila wanatakiwa kuwa sambamba na klabu ili kuhakikisha wanajitoa na kukamilisha zoezi la kujenga uwanja wa Kaunda na jengo la makao makuu ya klabu,” anasema Sanga.

Charles Boniface Mkwasa, Katibu mkuu wa Yanga anasema kila kitu kinakwenda sawa katika kuhakikisha Uwanja wa Kaunda unakamilika na kuwa moja ya viwanja vidogo vya kisasa ambacho kitakuwa chanzo cha mapato kwa klabu.

Mkwasa anasema: “Tumewekeza nguvu ili kuhakikisha uwanja wetu unakamilika ambao utatupunguzia gharama za kulipia viwanja vya watu ili kufanya mazoezi lakini itakuwa kitega uchumi kwa wale ambao watakuwa wanataka kutumia uwanja huu.

“Tukiwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha uwanja unakamilika tuna malengo mengine ya kuhakikisha jengo la klabu linabadilika na kuwa la kisasa,” anasema Mkwasa.

Naye Ofisa habari wa Yanga, Dismas Ten anasema ili uwanja wa Kaunda ukae levo, vinahitajika kuingia vifusi lori 2,250, na mpaka sasa wameshamwaga robo ya uwanja huo kwahiyo wanaomba wapenzi na mashabiki wa soka kujitokeza ili kuongeza nguvu katika jambo hilo la kimaendeleo.

Ten anasema mipango iliyokuwa katika uongozi wa Yanga ni kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa Uwanja huo kabla ya msimu ujao kuanza ili kutumia uwanja huo katika mazoezi msimu unaokuja.

“Baada ya kukamilisha kuweka vifusi, kwanza tunataka kulikamilisha kabla ya Desemba na kuingia Junuari inakuwa kazi ya kuotesha nyasi na kukamilisha mambo mengine ya muhimu kama majukwaa,” anasema.

“Si jambo rahisi ila tumeamua kuteua kamati ya ujenzi ambayo itasimamia uwanja jinsi gani ya kumwaga vifusi na kuusimamia mpaka hatua ya mwisho utakapokamilika lakini kamati hiyo itasimama pia kurekebisha jengo la klabu kuwa la kisasa,” alisema.

“Gharama rasmi mpaka uwanja unakamilika hatutakuwa nayo kwani hili zoezi la vifusi kuna watu wengine wanatupatia bure na wengine tanawapoza kwahiyo gharama rasmi haijajulikana bado.

“Kamati ya ujenzi itakuwa na wahandisi ambao ndio watatoa gharama kamili ya ujenzi wa uwanja pamoja na jengo ila kwa sasa hakuna hesabu yoyote iliyokuwa kamili ya kipesa ambayo tumeitumia au tutaitumia.

“Si vizuri kutaja idadi ya wanachama ila tunaomba wanachama na wale ambao siyo wanachama kuja kuisaidi Yanga katika jambo kama hili la kimaendeleo katika soka la nchi hii,” anasema Ten.

Advertisement