ELIMU NA MALEZI : Umuhimu wa kumpunguzia mtoto shinikizo la kufaulu

Muktasari:

  • Shule zetu hazina namna nyingine ya kumwelimisha mtoto zaidi ya kumtaka akusanye, akumbuke na kutumia maarifa aliyonayo kujibu maswali ya mtihani.

Ufaulu wa mitihani umepewa nafasi ya pekee katika mfumo wetu wa elimu.

Shule zetu hazina namna nyingine ya kumwelimisha mtoto zaidi ya kumtaka akusanye, akumbuke na kutumia maarifa aliyonayo kujibu maswali ya mtihani.

Ingawa ustawi wa jumla wa binadamu hautegemei eneo hilo moja la ukusanyaji na utumiaji wa maarifa, shule zetu zinaonekana kuamini kuwa pasipo mtu kuwa na maarifa mengi, hawezi kufanikiwa.

Kasumba hii imetuathiri hata sisi wazazi. Tunafikiri, kwa mfano, ni lazima mtoto afaulu masomo kwa kiwango cha juu ili afanikiwe. Matarajio haya makubwa yanatufanya tuwaweke watoto kwenye shinikizo kubwa mno la kufaulu, tukiamini ufaulu ndio kigezo cha ustawi wao katika maisha.

Matokeo yake, tangu mtoto anapoingia shuleni mpaka anamaliza, anajikuta katika mazingira ambayo kimsingi hana kazi nyingine zaidi ya kumridhisha mwalimu na mzazi wake.

Wazazi tunataka kuona mtoto ana uwezo wa kukusanya na kukumbuka maarifa. Mazoea haya yanaibua changamoto kadhaa za kimalezi kwa watoto.

Kulea tabia ya ushindani

Shule zetu zinathamini wanafunzi wanaofanya vizuri na kudhihaki wale wanaoonekana dhaifu. Mtoto anayefanya vizuri darasani, kwa mfano, ndiye anayependwa na walimu, ndiye anakuwa maarufu, na ndiye anayepata zawadi ya kuwa bora kuliko wengine. Hili ni tatizo na nitaeleza kwa nini.

Kwa muda mrefu, tuliamini kumzawadia mtoto mdogo aliyefanya vizuri kuliko wenzake ingekuwa si tu motisha kwake kuongeza jitihada za kufanya vizuri kwa mara mwingine tena, lakini pia ingewafanya watoto wengine kuweka bidii zaidi kwa matarajio ya kupata zawadi kama aliyopewa mwenzao.

Hata hivyo, tafiti nyingi zikiwamo za Profesa Carol Dweck wa Chuo Kikuu cha Stanford, zinaonyesha utamaduni huu wa kuwapongeza watoto kwa namna inayobagua uwezo wao, una kasoro nyingi zinazoweza kukuza mitazamo mibovu kwa watoto.

Kwa mfano, mtoto aliyezoea kuongoza darasani na kusifiwa anaweza kugeuka kuwa mtumwa wa sifa.

Utumwa huu wa sifa unamweka kwenye hatari ya kuwa na tabia ya kuelekeza nguvu kwenye eneo linalomfanya ajione bora na hivyo kukwepa maeneo mengine ambayo, pengine yanaweza kuwa muhimu katika maisha. Ikiwa mathalani, mtoto anajua walimu na wazazi humsifia kwa kufaulu vizuri, mtoto huyu anaweza kukwepa kushiriki kazi za ndani ambazo anajua haziwezi kumgusa mzazi wake.

Pia, kupongezwa kwa kuwazidi wengine kunaweza kumkatisha tamaa mtoto hasa pale inapotokea ama anafanya vizuri, lakini hakuna mtu anayejali au kuna mtoto mwingine anayeonekana kumzidi kinyume na vile alivyozoea.

Lakini vile vile, kwa upande wa watoto wanaoshuhudia mwenzao akizawadiwa kwa kuwazidi mara kwa mara, wengi hunyong’onyea na kuanza kujiona kama watu duni wasio na uwezo wa kufanya vizuri kama wenzao.

Tafsiri yake ni kwamba, kwa watoto wadogo, hakuna sababu ya msingi ya kuwawekea mazingira ya kuwashindanisha kiuwezo, hali inayoweza kuwaingizia dhana ya kushindana hata katika mazingira ambayo hakuna sababu yoyote ya ushindani.

Kudumaza vipaji

Changamoto ya pili ya shinikizo hili kubwa la taaluma kwa watoto, ni kudumaza vipaji ambavyo kimsingi hakuna namna ya kuvipima kwa kutumia mitihani.

Kwa kuwa shughuli karibu zote zinazoendelea darasani zinalenga kujenga eneo moja tu la kukusanya na kukumbuka maarifa, mtoto hawezi kuwa na motisha ya kufanya vitu vingine visivyohusiana na masomo.

Matokeo yake mtoto anapokuwa shuleni anakuwa hana kazi nyingine zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Anaporudi nyumbani, hali kadhalika, anakutana na mzazi anayeamini kazi ya msingi ya kufanya kwa mwanae ni kuzingatia masomo.

Mtoto anayeishi kwenye shinikizo la namna hii anapojaribu ‘kuchepuka’ kidogo ili kukuza vipaji visivyotambuliwa na mitihani rasmi ya darasani, anajikuta kwenye mgogoro na mwalimu na mzazi.

Kwa sababu hii, watoto wetu wengi ambao pengine wangeweza kuwa na vipaji vya kila aina, wanaishia kufanya vitu ambavyo mara nyingine havifanani navyo.

Kudumaza ukuaji

Shinikizo hili kubwa la kufaulu masomo pia linaathiri mtindo wa kawaida wa maisha ya mtoto. Kwa mfano, shule inayotaka mtoto awe bora kitaaluma, kwa kawaida itamnyima fursa ya kushiriki shughuli zisizo za kimasomo, lakini ambazo kimsingi zingeweza kuwa muhimu katika makuzi.

Kwa sababu ya kusoma kwenye shule inayotaka kuongoza kwenye mitihani, mtoto huyu mdogo, hatopata mtu wa kumfundisha kujifanyia usafi wake binafsi, kufagia, kushiriki kazi za mikono kwa sababu tu mitihani ambayo ndio kipimo cha ubora wa shule haina vipengele vinavyopima utu wa mtoto na hata ushiriki wake kwenye kazi za mikono.

Pamoja na uzuri wa kufaulu masomo, mtoto mdogo wa shule ya msingi, kwa hakika anahitaji kufaulu pia hata kwenye maeneo mengine yenye nafasi muhimu ya kumsaidia kupata mafanikio katika maisha.

Mbali na kupata alama 95 darasani, kwa mfano, mtoto huyu anahitaji kujifunza umuhimu wa kujali hisia na mahitaji ya wengine, tabia ambayo angeweza kujifunza vizuri zaidi kupitia michezo kuliko vitabu vilivyotajwa kwenye mtalaa.

Kasoro hii ya mfumo wa elimu kutilia mkazo eneo la ufahamu na maarifa kuliko maeneo mengine, imefanya watoto wengi wakose fursa pana ya kujengwa kiroho, kimaadili na hata kupata stadi nyingine muhimu za kimaisha.

Ushauri

Natambua shauku kubwa waliyonayo wazazi kuona watoto wanashika nafasi ya kwanza darasani. Hata hivyo, kama tulivyoona kwa ufupi, shauku hiyo ya kuwa na watoto wenye ‘akili’ isiwafanye watoto wakajikuta wakibanwa mno na hivyo kukosa muda wa kujifunza stadi nyingine za maisha.

Aidha, tunazo sababu za kutosha kuvumilia hata pale tunapoona watoto wetu hawafanyi vizuri darasani. Hakuna ushahidi wa kitafiti unaothibitisha kuwa ufaulu wa sekondari na vyuoni unategemea ufaulu mkubwa wa ngazi za chini.

Miaka ya awali ina umuhimu mkubwa katika kujenga sura ya maisha atakayoishi mtoto. Tunahitaji kuweka msisitizo mkubwa kwenye kujenga utu, kuwakuza kiroho na kuwafundisha stadi za maisha, kwa sababu hayo ndiyo maeneo yatakayoamua mustakabali wao.