Thursday, May 17, 2018

Usikopeshe kumfurahisha mkopaji, utapoteza fedha

 

By Wakili Jastine Kaleb

Kitendo cha kumpa mtu kiasi chochote cha fedha au mali kwa makubaliano ya kuzirejesha baada ya muda kinapaswa kufanywa kwa umakini.

Kukopesha huwa kwa mafanikio endapo wanaokopeshwa wanakuwa waaminifu. Ikiwa hivyo tu, kukopesha hukuza mtaji na huongeza mzunguko wa fedha na kukuza uchumi.

Mchakato huu huwasaidia wakopeshaji kukuza mtaji na kuvutia faida. Kutorejeshwa kwa mkopo ndani ya muda wa makubaliano huwa ishara ya ama kutolipwa kabisa au kulipwa nje ya muda.

Kutorejeshwa kwa mkopo husababisha hasara, huchelewesha kutimia kwa malengo ya mkopeshaji, huvunja uhusiano mzuri wa kibiashara uliojengwa kwa muda mrefu, na mkopeshaji asipokuwa mwangalifu anaweza kufilisika.

Sheria ya madai inaeleza kuwa, mdaiwa anaweza kufungwa endapo atashindwa kulipa deni na ikiwa mdai ataiomba mahakama imfunge mdaiwa na atakuwa tayari kugharimia mahitaji yake awapo gerezani. Hivyo mahakama baada ya kujiridhisha inaweza kuamuru mdaiwa akamatwe na afungwe.

Usipokuwa makini kabla ya kukopesha unaweza kugombana na watu, undugu unaingia shakani na urafiki uliodumu kwa muda mrefu unavunjika kwa kushindwa kujenga mazingira mazuri ya uwajibikaji kisheria kati yako na unayemkopesha. Hii haijalishi unamkopesha nani na kiasi gani unampa.

Ukishindwa kuweka kumbukumbu zako vizuri utapoteza fedha pasipo kujua hatimaye kufilisika. Fedha haina undugu, kujuana wala urafiki. Ukitaka kufanikiwa na kudumisha mafanikio yako lazima ujenge misingi ya kisheria itakayolinda fedha zako na masilahi ya vizazi vijavyo.

Kwa kuzingatia ukweli huo, usikopeshe kwa kuangalia leo bali kesho. Uwe na maono ya kuona miaka mingi ijayo na kuchukua tahadhari mapema iwezekanavyo.

Kwanza hakikisha una mkataba wa maandishi kati yako na unayemkopesha. Usimkopeshe mtu kwa makubaliano ya mdomo, haijalishi unamuamini kiasi gani.

Vilevile, mkataba huo unapaswa kushuhudiwa na wakili, hakimu au shahidi mwingine yeyote. Hata kama hawatakuwa miongoni mwa hao, ni muhimu kuwa na mtu wa tatu kama shahidi katika mkataba wenu atakayesaidia kuutetea.

Hakikisha mtu unayeingia naye mkataba ana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo na ndiye atakayewajibika katika urejeshwaji wa mkopo huo. Usije ukaingia mkataba na mtu mwingine na ukatarajia ulipwe na mtu mwingine, utakwama.

Fahamu anwani ya unayemkopesha, anapoishi, ofisi yake, mawasiliano na mambo mengineyo muhimu yanayomhusu. Usimkopeshe mtu mliyekutana barabarani, kanisani au msikitini.

Jiridhishe kama mkopaji ana uwezo wa kulipa ndani ya muda mliokubaliana. Usimkopeshe mtu kwa kumhurumia ili atatue shida zake bali kwa maslahi ya kibiashara. Kama unajua hana uwezo wa kulipa, usimkopeshe.

Angalia kama ana dhamana yoyote au kuna mtu amejitolea kumdhamini kulipa deni hilo. Kukosekana kwa dhamana ni kuhatarisha usalama wa fedha zako.

Tathmini utakavyopata fedha zako endapo mtu huyo atafariki dunia, akipata ulemavu wa kudumu au tatizo lingine lolote. Ukiona hupati majibu, tafakari mara mbilimbili kabla hujakopesha.

Ukiona huna majibu sahihi ya vigezo hivyo usithubutu kumkopesha mtu. Ili muendelee kuwa na uhusiano mzuri watu wengine unatakiwa usiwakopeshe.

Kwa taasisi zinazotoa mikopo ni muhimu kupata vibali vya kufanya hivyo na kulinda haki zako na za mteja kisheria kwa kutomdharirisha, kumnyanyasa au kumfanyia fujo kwa kushindwa kurejesha mkopo.

-->