BIASHARA LEO : Wajasiriamali wajiandae fursa za uchumi wa viwanda

Muktasari:

  • Wajasiriamali wadogo na kati wanatakiwa kujiandaa vizuri kupokea ujio wa taifa hilo lenye fursa kemkem. Zipo athari nyingi chanya kwa biashara ndogo na kati kutokana na viwanda hivyo ambazo zitakuwa misingi mizuri ya kuimarisha miradi iliyopo.

Tukielekea kwenye uchumi wa viwanda kuna mambo mengi yanatarajiwa kutokea wakati wa kulipokea taifa jipya lenye uwekezaji wa aina yake kwenye sekta nyeti na muhimu ya viwanda.

Wajasiriamali wadogo na kati wanatakiwa kujiandaa vizuri kupokea ujio wa taifa hilo lenye fursa kemkem. Zipo athari nyingi chanya kwa biashara ndogo na kati kutokana na viwanda hivyo ambazo zitakuwa misingi mizuri ya kuimarisha miradi iliyopo.

Kutakuwa na urahisi wa kujifunza na kutumia teknolojia za kisasa kwenye uzalishaji kwa kipindi ambacho tutakuwa na viwanda vingi vya ndani ambazo zitapunguza gharama kwa wafanyabiashara watakaofungua macho.

Wajasiriamali wadogo wanapaswa kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kujifunza mbinu zinazotumika kwenye uzalishaji, usambazaji na kuona namna wanavyoweza kutumia teknolojia iliyopo kutanuka na kukuza biashara zao na kuzifanya kuwa bora zaidi.

Kuongezeka kwa ushindani sokoni kutokana na wingi wa bidhaa bila kujali kama zinafanana au la. Uwapo wa viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa tofauti utaongeza ushindani kwani wateja waliopo watatakiwa kutumia kipato chao kukidhi mahitaji.

Endapo bidhaa au huduma moja itatolewa na zaidi ya mzalishaji mmoja, ubora na huduma kwa wateja ni miongoni mwa sababu zitakazowavutia na zikiwa tofauti umuhimu utakuwa sababu ya msingi.

Viwanda hivi pia vinaweza vikatafuta mawakala au zikawa na ofisi za kuuza bidhaa zao moja kwa moja, hivyo kuongeza ushindani kwa wafanyabiashara wadogo ambao huuza kwa bei ya juu.

Kuimarika kwa bei za malighafi. Hii ni kutokana na ushawishi wa Serikali kuhamasisha matumizi ya malighafi za ndani huku ikizuia zile za nje. Wakulima na wafugaji wa mashambani watapata stahiki zao kulingana na jasho walilotoa kwa kipindi chote cha maandalizi mpaka mavuno ya mashamba yao.

Bidhaa na huduma zilizoongezwa thamani kwa ajili ya masoko yote mawili; ndani na kimataifa. Viwanda hivi tunatakiwa kuvitumia kama ngao muhimu ya kukuza na kuboresha bidhaa na huduma zetu kutokana na ukweli kwamba tutakuwa kwenye nafasi ya kujifunza na kukubali mabadiliko kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma. Hii itakuwa nguzo ya kutengeneza biashara zenye nguvu, masoko ya uhakika.

Kutanua masoko ya huduma na bidhaa za viwandani nje ya Tanzania. Viwanda hivi vitatanua masoko ya bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kuanza na ukanda wa Afrika Mashariki kabla ya kwenda mbali zaidi. Ni fursa kwa wajasiriamali kuangalia hili na kuanza kujiandaa na ujio wa viwanda hivi tangu vikiwa chini ili kukuza mtandao wa masoko nje ya Tanzania. Ni muhimu kujiandaa kuchangamkia fursa za masoko makubwa ndani na nje.

Kutanuka kwa huduma za taasisi za fedha kutokana na msukumo utakaokuwapo kutokana na shughuli za viwanda vitakavyojengwa kwa kuongeza mahitaji na mzunguko wa fehda.

Huduma za fedha zitakuwa muhimu kwa wafanyakazi na viwanda na watumiaji wa bidhaa zake. Hii itakuwa nafasi nzuri kwa biashara ndogo na kati kupata mitaji, kutanua na kukuza biashara kwa kuzingatia taasisi za fedha ni nguzo muhimu kwenye uwekezaji. Ujenzi wa viwanda utasaidia kuinua uzalishaji na malighafi nyingi zitahitajika huku soko likikua, hivyo muhimu kwa Watanzania kujiandaa kupokea mabadiliko haya yatakayokuwa na tija kwenye sekta ya kilimo, fedha na shughuli nyingine za ujasiriamali.