Wanakwenda wapi wakifeli kidato cha nne?

Furaha iliyoje kumaliza shule kama wanavyoonekana wanafunzi hawa. Lakini wanaishia wapi wanafunzi hawa pindi wanapomaliza kidato cha nne?

Muktasari:

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, watahiniwa 156,089  sawa na asilimia 46.41ya wahitimu wote walifeli mtihani huo kwa kupata daraja hilo la mwisho.

MWAKA 2011, nchi ilishuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wakifeli mtihani wa kidato cha nne kwa kupata daraja sifuri.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, watahiniwa 156,089  sawa na asilimia 46.41ya wahitimu wote walifeli mtihani huo kwa kupata daraja hilo la mwisho.

Katika mtihani huo wanafunzi 33,577 pekee sawa na asilimia 9.98 ndio waliopata kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, hivyo kuwa na uhakika wa kuendelea na kidato cha tano.

Kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, wanaopata daraja la nne, baadhi wako shakani kuendelea na daraja la sekondari ya juu. Katika matokeo hayo, hawa walikuwa 146,639 sawa na asilimia 43.60.

Ili kujiunga na kidato cha tano, wanafunzi hawa wanapaswa kuwa na alama C katika masomo yasiyopungua matatu.

Aidha, kwa waliopata daraja sifuri ni sawa na kusema miaka minne ya kuwa shule, wameambulia patupu, kwani kwa mfumo uliopo wa elimu hawawezi kuendelea kusoma, labda warudie mitihani au wajiunge na vyuo vinavyopokea wahitimu wa darasa la saba.

Bila shaka jeshi hili la vijana waliofeli ni kubwa, na kwa kuwa nchi haina utaratibu wa kuwaendeleza, swali kuu ni je, wahitimu hawa wanakwenda wapi, wana sifa ya kuajiriwa au hata kuwa na uwezo wa kujiajiri?

Ushuhuda wa hali ilivyo

Peter Mgaya alihitimu kidato cha nne mwaka 2011 mkoani Tanga na kuambulia alama ya mwisho ya daraja la nne.

Kwa kuwa kiwango hicho kisingempeleka kokote, anasema alibaki nyumbani akiwasaidia wazazi katika shughuli za kilimo.

Hata hivyo, anamshukuru shangazi yake ambaye baadaye alimtafutia kibarua cha kufanya usafi katika kampuni moja jijini Dar es Salaam.

“ Karibu darasa zima walipata sifuri, sijui wawili vile ndio waliopata division four (daraja la nne) ya alama za mwanzo mwanzo. Nilipomaliza sikuwa na la kufanya kijijini, wenzangu waliokuwa na ndugu Tanga mjini walikwenda wakasaidiwa kazi… Na mie nilimpigia siku aunt (shangazi) akanileta hapa Dar es Salaam, nashukuru siku zinakwenda,’’anasimulia Mgaya.

Akikumbuka kadhia ya kusoma bila walimu, Mgaya hana tena hamu ya kusoma. Anaitupia lawama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushindwa kuipatia walimu shule yao, jambo analoamini kuwa ndio sababu kubwa ya wao kufeli.

Hata hivyo, anasema kiasi kidogo cha fedha anachodunduliza katika kibarua chake kimerudisha imani ya kutimiza ndoto yake ya siku nyingi ya kusomea ufundi umeme.

Akifafanua anasema: “ Ndoto yangu kubwa shuleni nilitaka kuja kuwa fundi wa vifaa vya umeme. Baadaye napanga kwenda kusoma Veta.’’ Afadhali Mgaya amempata msitiri, sasa ana kibarua kinachomsaidia kusukuma gurudumu la maisha yake, na hata kutamani kurudi tena shuleni, lakini hali ikoje kwa vijana wa aina yake mijini na vijijini wasiokuwa na fursa ya kupata wasitiri?

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Ruth Meena hiki ni kipindi muhimu kwa Serikali kubaini sababu zinazochangia wanafunzi wengi kufanya vibaya katika mtihani wa kidato cha nne.

Anasema kuwa haiwezekani asilimia zaidi ya tisini ya watoto wanaofeli wakawa wajinga. Anaamini zipo sababu nje ya uwezo wa wanafunzi zinazochangia hali hiyo ya kusikitisha.

“Huwezi kusema watoto wote wanaofeli kwenye mitihani yao ni wajinga, kuna sababu zinawafanya wasifanye vizuri, lazima ziangaliwe na Serikali ili watoto waweze kufanya vyema kwenye masomo yao,” anaeleza.

Kwa mtazamo wake, Profesa Meena anataja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa walimu shuleni, uwepo wa walimu wasio na sifa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia.

Naye Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga anasema juhudi za Serikali kujenga shule nyingi za sekondari unakwazwa na kiwango duni cha elimu kinachotolewa katika shule hizo.

Hali hiyo ndiyo anayosema inachangia wahitimu wengi kukosa uwezo wa kushindana katika soko la ajira.

“Suala hili hatuwezi kuliacha kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi peke yake, lazima tushirikiane wote ili kuhakikisha elimu yetu inakuwa bora kwa manufaa ya vijana wetu,” anataja suluhu ya tatizo hilo.

Hali ya sasa na matokeo mabaya inakuja wakati Serikali ikiwa imejenga shule lukuki za kata ambazo zinatajwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli.

Shule nyingi za kata hasa zilizoko vijijini, hazina walimu wa kutosha jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kuhitimu kidato cha nne wakiwa hawajasoma baadhi ya masomo muhimu kama Hisabati.

Hata pale Serikali inapoajiri walimu na kuwapangia katika shule hizi, wengi hawaripoti na hata wakiripoti baada ya muda hukimbia vituo vyao na kuacha tatizo likiendelea kuwa kubwa.