Monday, February 19, 2018

Fatma Samoura; Katibu Mkuu wa Fifa ni mwanamke wa shoka

 

Kwa mara ya kwanza, Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, limepata Katibu Mkuu mwanamke, Fatma Samoura baada ya uchaguzi uliowaingiza madarakani, Rais wa sasa Gianni Infantino mapema Februari mwaka juzi.

Mtandao wa hebdo.ch ulifanya mahojiano na Samoura ambaye ni raia wa Senegal aliyekuwa mtumishi wa Umoja wa Mataifa.

Samoura anasema ameingia Fifa lakini mpango wake ni kuijenga soka na kuifanyia mageuzi makubwa. Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Wewe ni mwanamke uliye nafasi ya juu katika medani za soka, unadhani tukutafsiri kama mtu wa mfano?

Samoura: Ndio unaweza kusema hivyo, mimi ni mtu wa mfano, lakini pia inatia moyo kuona wanawake wanaaminiwa katika nafasi kama hizi za juu za uongozi duniani.

Ukweli, mpango wa Fifa kwa sasa ni kuleta pamoja wanachama wake zaidi ya 200 kuibeba soka. Mipango yangu, ni kuyeyusha mawazo ya wanawake wengi kuwa mwanamke hawezi kujihusisha na soka, na ni kwa ajili ya wanaume.

Swali: Vipi, una mtoto wa kike anayecheza soka?

Samoura: Amekuwa akichezea timu ya shule, International School of Zurich. Amekuwa akinitumia video clip kunionyesha anachofanya. Hili ninaweza kusema ni kati ya machimbuko ya soka. Hata katika Afrika, kuna nchi ambazo wanawake wanacheza soka…wanakokota mpira na kucheza. Hii inapendeza na inaleta hamasa kwa jamii.

Mimi ninapenda mwanamke anayecheza soka kwa kuwa mwanamke anayecheza soka, hujichunga mwili wake, hujilinda na kujiepusha na mambo mengimengi.

Soka inampa nguvu. Nchini kwangu Senegal, wanawake wamejikita kwenye akademi mbalimbali wakicheza soka, na pia katika shule wapo na wakati mwingine wanacheza na wanaume.

Tatizo linakuja, wakati mwingine wanapata ujauzito na kushindwa kuendelea na kambi, utakuta wanaacha kucheza, wanaacha shule na kukosa mwelekeo.

Kwa wanaocheza soka, wengi hawana haja ya kuelezwa kwa sana kwa kuwa kila mmoja anafahamu, nini anakifanya. Wengine wanafahamu namna ya kusema hapana.

Swali: Umewezaje kuondokana au kuushinda mfumo dume ambao umechukua sehemu kubwa ya taifa la Senegal?

Samoura: Baba yangu alikuwa askari, tena ofisa, alikuwa mpigania uhuru wa Afrika. Mara zote alikuwa akisema: “Kama ukiona aibu, utaishia kufanya mambo ambayo wanaume hawataki yafanyike. Kwa hiyo mimi nikaondoa aibu.

Pia nilijifunza kuogelea, nilicheza basketball, nilicheza soka na kaka zangu. Mimi nilikuwa msichana pekee niliyekuwa nikicheza soka. Kingine nikuchekeshe, nilipokuwa shule nilikuwa ninaendesha pikipiki, kuja na kurudi nyumbani baada ya masomo.

Swali: Baada ya shule ukaja kuolewa, je mumeo unamuonaje? Anakubaliana na kila unachotaka kukifanya katika maisha yako?

Samoura: Mume wangu, ukweli tumekua pamoja mtaani tangu wadogo, tulisoma pamoja kwenye mji wa Lyon na tulifikia hatua tukaamua yetu kama baba na mama.

Unajua tulikaa chini tukaelezana kuwa hapa tunatafuta maisha ya kuwa kama ikitokea mmoja anapata kazi ya mbali, mmoja atalazimika kuangalia watoto. Ninafurahi nilipata bahati ya kuwa na mwanaume aliyekubaliana na hili, ninasafiri nakwenda mbali na yeye anabaki na watoto.

Swali: Mwaka 1995, ulijiunga na Umoja wa Mataifa, kitengo cha chakula, World Food Program. Nini hasa ulichokuwa unakifanya huko?

Samoura: Nilikuwa katika kitengo maalumu cha mpango wa chakula katika mataifa ya Liberia, Sierra Leone, Nigeria, Darfur, Afghanistan, Bangladesh, East Timor, Kosovo.

Kazi yangu ilikuwa kuandaa misafara ya kupeleka vyakula, kuandaa mazingira salama ya wasafishaji wa vyakula na misaada mingine ya kibinadamu, kuwaleta karibu wananchi katika maeneo salama, pamoja na kuanzisha mijadala na askari wanaoua askari walinda amani na watoa misaada.

Swali: Kipi kilikuwa kipindi chako kisichokuwa na presha na hofu?

Samoura: Hakuna kitu rahisi. Mimi naona kazi ilikuwa ngumu. Nchini Afghanistan kwa mfano, hali ilikuwa mbaya kama vile Kabul hatukutoka nje wala kutembea mitaani na sisi ilikuwa kusambaza chakula.

Mfano, mwaka 1996, nilikuwa Liberia katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Magari yetu ya misafara ya misaada kutoka mji mkuu Monrovia kwenda kwenye mpaka wa Sierra Leone, ilisimamishwa na watoto kati ya miaka, 12 na 14 walikuwa wamebeba bunduki aina ya AK-47.

Walitaka tupeleke misaada ya chakula makwao. Nilizungumza nao, nilizungumza nao hadi wakanielewa wale watoto, na baadaye wakaturuhusu wakaanza kupiga risasi hewani.

Tulisimamia kwenye misingi yetu. Kwa kuwa kila hali na mazingira yake, vilikuwa vinafanana: tulifanya kazi hiyo na kikubwa kuhakikisha misaada ya vyakula inawafikia walengwa.

Askari walikuwa wakitaka vyakula kwa nguvu na walikuwa wakiuza ili wapate fedha. Mazungumzo na majadiliano ya kuruhusu sisi kupita yalichukua takribani saa nzima. Bila mafanikio na misafara ilisita kuondoka. Ilikuwa wakati mmoja mbaya sana sitakaa kusahau maana mnapishana na risasi, mabomu na makombora.

Swali: Ulikuwa na kazi nzuri UN. Kwanini uliamua kuacha na kwenda Fifa?

Samoura: Nina miaka 55, ninafurahi sasa sisikii milio ya risasi. Ile kazi acha kabisa. Wewe unakuwa rafiki wa milio ya risasi na mabomu na machafuko, hayo ndiyo mazingira yako rafiki.

Swali: Wakati Rais wa Fifa, Gianni Infantino anakuteua mapema Mei mwaka juzi mara baada ya kuingia madarakani, tulisikia wewe ulikuwa mmoja wa vibaraka wake wa kampeni za chinichini na ndio sababu ya kukubeba?

Samoura: Mmh! Si kweli, mimi nilikuwa ninajisimamia, na kama isingekuwa hivyo, nisingekuwa UN kufanya kazi ya kusaidia maisha ya watu. Sikuwa mtu wake wala sikufanya kampeni.

Swali: Kazi yako ya miaka ya nyuma chini ya UN ni kubwa na soka ni kama kitu kidogo sana kwako?

Samoura: Fifa ni kama UN ya soka, iko pana duniani. Kuna matatizo yanayofanana. Katika soka kuna mengi na mpango wetu ni kuleta usawa kwa wanawake, kuondoa ubaguzi wa rangi, kupiga vita rushwa.

Haki za binadamu ni msingi mkubwa kwetu na mfano kama ilivyo kwa wafanyakazi wanaojenga viwanja vya Kombe la Dunia nchini Qatar. Tunapambana kila mahali. Soka inaweza kubadilika! Wanawake wanacheza kwa ari na nguvu, wanaume wanatakiwa kukaa chonjo. Ni somo tosha sana na ni kama UN.

Swali: Kumekuwa na kashfa mbalimbali ndani ya Fifa na inatajwa kuwa wahusika wa Fifa ni kama mafia zaidi ya Umoja wa Mataifa.

Samoura: Tunaendelea kuimarisha hilo. Kwa sasa matatizo mengi tumeyapunguza. Pamoja na hayo, bado tunaendelea na mchakato. Utaratibu mpya, utaratibu wa utawala, tunajaribu kuweka maeneo ya msingi kutengeneza mwongozo wa soka ambao tunautofautisha na zamani.

Changamoto za mabadiliko ziko katika utekelezaji wake kwenye vyama na mashirikisho ya soka. Kuna vyama na mashirikisho 23 hatuyapi misaada ama kwa kushindwa kutekeleza maagizo yetu au kwenda kinyume na utaratibu wa Fifa

Yote kwa yote, Fifa inapambana kupata fedha. Ikiwemo za matarajio ya Kombe la Dunia Russia. Kwa Russia ni mahala sahihi, hali yake kisiasa, kijiografia na kama hivi tulivyoandaa Kombe la Dunia.

Swali: Russia inaandaa Kombe la Dunia, halafu inaangusha mabomu Syria na ina mzozo na waasi wa Ukraine, mtaliepusha vipi kwa mashabiki?

Samoura: Hapa suala si Russia, Syria au Ukraine. Hili ni Kombe la Dunia, watu wanataka kuangalia Kombe la Dunia. Kombe la Dunia linaleta amani. Kama kuna kitu cha kulibadilisha Kombe la Dunia sijui, kwa kuwa Kombe la Dunia linaleta watu pamoja, mataifa pamoja na ndiyo maana hatutaki masuala ya soka yachanganywe na siasa na wala viongozi wa kisiasa kuingia mambo yetu.

Kombe la Dunia linaweza lisifanyike Russia kwa sababu ya mazingira, kwa Putin, ni kama Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi kwenye mji wa Sochi miaka mitatu iliyopita, soka ina nguvu ya kuhamasisha watu.

Kipindi ambacho Kombe la Dunia halikufanyika ni wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Tangu hapo, kumekuwa na vita kila mahali lakini Kombe la Dunia linachezwa. Hivyo ndivyo ilivyo. Hata Syria, kama hali itakaa sawa, tutaandaa mechi pale.

Pamoja na hali kuwa ngumu, watu wanaendelea na maisha Syria na wanataka kucheza soka. Soka ni burudani, ni kivutio, tunataka kuwapeleka wacheze mpira kule.

Swali: Sepp Blatter aliwahi kuzungumza hayo. Uliwahi kukutana naye?

Samoura: Hapana. Sijakutana naye.

Wakati wa utawala wake, Fifa ilikuwa ikiangalia sana fedha. Mrithi wake, Infantino, anataka kutengeneza faida zaidi, ameongeza timu kutoka 32 hadi 48. Hayo naweza kusema ni mafuriko ya timu.

Kwa upande mwingine, hii si habari ya faida. Kama tumedhamiria kuendeleza soka duniani, asilimia 30-40 ya wanachama wa Fifa, wanatakiwa kucheza Kombe la Dunia.

Tunataka kuhakikisha kuwa timu nyingi iwezekanavyo zinacheza Kombe la Dunia kutoka katika mabara. Ningependa kuona na nitafurahi mataifa mengine zaidi ya Ujerumani, Brazil, Hispania, Italia, Ufaransa au Argentina wanatwaa Kombe la Dunia. Itapendeza zaidi mataifa ya Afrika kutwaa Kombe la Dunia.

Mwaka 2002, Senegal iliingia robo fainali. Hatua za awali, tuliifunga Ufaransa waliokuwa mabingwa wa Ulaya na dunia. Tulikaribia kutimiza ndoto.

Ongezeko la timu kwenye Kombe la Dunia kuna maana kutakuwa na mechi nyingi.

Ujenzi wa viwanja na pia nchi italazimika kugharamika kwa ajili hiyo.

Pamoja na hayo, soka itabakia kama kiungo kikuu, ndiyo maana nchi zinaandaa pamoja na kingine ambacho tunaangalia, ni kuipa Afrika nafasi nyingine kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia.

Monday, February 19, 2018

Rais wa Fifa, CAF ndani ya Tanzania

 

Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka Tanzania, vigogo wa juu katika Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa na lile la Afrika, CAF watakuwa nchini kwa mkutano maalumu kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya soka.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino atashiriki katika mkutano huo maalumu uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia keshokutwa.

Mkutano huo utashirikisha nchi wanachama 19 za Fifa, utafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) unajulikana kwa jina la “Fifa Executive Football Summit” itawakilishwa na Rais na Katibu wake mkuu.

Tanzania ni nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyopewa heshima ya kuandaa mkutano huo ambao pia utajadili masuala ya soka la wanawake, vijana na mfumo wa usajili wa kielektroniki wa TMS ambao kwa sasa utakuwa chini ya Fifa wenyewe na si wakala.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkubwa wa Fifa kutembelea Tanzania na kubwa zaidi ni kupewa nafasi ya mkutano wa siku moja ambao viongozi wa mashirikisho ya soka katika nchi mbalimbali watashiriki.

Madhumuni hasa ya mkutano huo ni kuirejesha Fifa kwenye mpira wa miguu na mpira wa miguu kwa Fifa, kupanga mikakati ya maendeleo ya siku za usoni ikiwa ni pamoja na mataifa 12 duniani kupewa heshima ya kuandaa mikutano hiyo.

Mbali ya viongozi wa Fifa, pia viongozi wakuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) nao watakuwepo.

“Hii ni heshima na tumepewa nafasi kutokana na utawala bora ambao kwa kipindi cha miezi mitano tangu tuingie madarakani tumeonyesha,” anasema Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Wallace Karia.

Anasema kuwa kwa kipindi kifupi, wamerejesha heshima ya TFF katika ramani ya soka katika Afrika na Duniani bila kusahau Ukanda wa Cecafa ambao juzi ilimchagua kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji.

Miongoni mwa wajumbe 64 wanaoandamana na Infantino ni pamoja na makamu wake Mkuu, David Chung na viongozi wengine wakiwemo wa mabara, Salman Bin Ibrahim Al-Khalifa, Aleksander Ceferin, David Gill, Alejandro Dominguez, Victor Montagliani na Katibu Mkuu, Fatma Samoura.

Mataifa yatakayoshiriki mkutano huo ni Bahrain, Palestina, Saudi Arabia, United Arabs Emirates (UAE), Algeria, Burundi, Afrika ya Kati, Ivory Coast, Mali, Morocco, Niger, Tunisia, Bermuda, Monserrat, St. Lucia, Us Virgin, Maldives, Congo Brazzaville na wenyeji Tanzania.

Monday, February 19, 2018

Dk Mwakyembe: Tutawapa mapokezi makubwa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali imejipanga kuupa mapokezi mazuri msafara wa watu zaidi ya 64 wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, Gianni Infantino na kusema pia kuwa hiyo ni fursa ya Tanzania kujitangaza.

Infantino atakayeongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Ahmad Ahmad, Dk Mwakyembe alisema Serikali imeona ugeni huo ni mzito na haiwezi kuliachia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) peke yake kuratibu ziara hiyo.

“Kwa sababu hiyo tumeona tufanye kazi bega kwa bega na TFF ili kuhakikisha Infantino na msafara wake wanafurahi ziara hiyo.

“Tunataka kuionyesha Fifa kuwa Watanzania ni watu wa mpira, Watanzania wanapenda soka na ndiyo maana tunataka kuwapa heshima hata wakiondoka wakumbuke Tanzania,” alisema.

Waziri Mwakyembe alisema kama Serikali, watahakikisha msafara huo utakapokuwa nchini pamoja na ratiba zake, unapata fursa ya kukutana na Waandishi wa Habari.

Kuhusu kukutana na Rais John Magufuli, Dk Mwakyembe anasema Rais Magufuli ni mpenda michezo hivyo atafanya jitihada zake zote kuhakikisha anakutana na Rais Infantino atakapokuwa nchini.

‘’Kwakuwa Rais Magufuli ni mpenda michezo, lazima atapenda kuonana na Rais wa Fifa, Gianni Infantino, na mimi kama waziri mwenye dhamana ya michezo nitahakikisha hilo linawezekana,” anasema.

Monday, February 19, 2018

Kuna huu upande wa pili sasa…

 

By Charles Abel, Mwananchi

Wakati viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa na lile la Afrika, CAF wakiwasili nchini, kuna mengi yanaweza kuangazwa ambayo ninaweza kusema ni ya upande wa pili.

Kumekuwa na hoja za mambo yanayoendelea katika medani za soka, lakini tutaionyesha nini Fifa usafi wetu katika utawala bora wa soka Tanzania.

Kimsingi, tunasifia lakini kiukweli, hakuna ligi imara za mpira wa miguu kwa vijana na wanawake huku pia mfumo wa utawala bora unaozingatia weledi na uwazi ukiwa ni ndoto za alinacha.

Tangu Tanzania ilipoanza kupokea mamilioni ya fedha za kuendeshea na kusimamia miradi ya soka hadi leo hii, tuna jambo gani kubwa ambalo tunaweza kujivunia kama nchi tumefanikiwa zaidi kwenye mchezo wa soka kulinganisha na nchi nyingine kupitia fedha hizo?

Kama nchi, ni wazi tumeshindwa kuzalisha makocha bora ambao wangekuwa hata wanagombewa nje ya Tanzania. Mfano mzuru tunaiona nchi ndogo tu ya Burundi, makocha wametawanyika Afrika kwani hata kocha wa Gendarmerie ya Djibouti ni Mrundi, Issa Mvuyekure.

Mbali na kutawanyika nje ya Tanzania kufundisha, kwa ambao wangekuwepo, wangekuwa chachu ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya soka hasa kwa vijana wadogo.

Badala yake sasa, klabu zetu zimeendelea kupigana vikumbo kuajiri makocha wa kigeni kutokana na uwezo duni wa kundi kubwa la makocha wazawa.

Tumeshindwa kuandaa mipango imara ya kuhakikisha tunazalisha kundi kubwa la wachezaji bora ambao watakuwa msaada kwa timu yetu ya taifa na na hii inalazimisha viongozi wa klabu kuelekeza nguvu kwa wachezaji wa kigeni ambao wanaongeza gharama za klabu na wanachota mamilioni ya fedha ambazo zingelipwa kwa wachezaji wazawa.

Tunaweza kuandaa shughuli nyingi za kitalii na kiutamaduni kama sehemu ya burudani kwa msafara mzima wa Infantino na watu wake lakini ni lazima tukumbuke Fifa ipo kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.

Kwa kuwa wamekuwa wakitoa fedha kusaidia maendeleo hayo, furaha kubwa kwa jopo hilo linalokuja itakuwa ni pale watakapojiridhisha pasipo na shaka kwamba fedha wanazotoa zinatumika vizuri lakini pia maagizo ambayo wamekuwa wakiyatoa kwa ajili ya uendeshaji wa soka, yanafuatwa kikamilifu.

Soka ya wanawake, soka ya vijana wa rika mbalimbali na uimarishaji wa miundombinu ya soka kama viwanja, vifaa vya michezo, wataalamu kama madaktari wa michezo, wanasaikolojia na wakufunzi mbalimbali.

Pia utekelezaji wa maagizo ya Fifa kwa kuzingatia agizo la mkutano wa Bagamoyo.

Monday, February 19, 2018

Waafrika hawawezi kumsahau Sepp Blatter

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Pamoja na kupatwa na kashfa zilizomng’oa madarakani, kamwe Waafrika hawawezi kumsahau Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter ambaye alipambana kwa hali na mali tangu 2006, Afrika kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia.

Haikuwahi kutokea lakini Afrika ikaandaa. Afrika Kusini ilipewa kazi ya kujipanga na jukumu hilo lilifanyika tangu mwaka 2006.

Ukweli kulikuwa na fitna za mataifa yaliyoendelea, yaliona Afrika haiwezi kuwa mwenyeji lakini Blatter alisimama kidete na kusisitiza Afrika Kusini itaweza na Bara la Afrika litakuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia 2010.

Katika moja ya kauli zake alizozitoa kwenye mkutano uliofanyika kwa ajili ya kupata wenyeji wa Kombe la Dunia alisema kabla hajaondoka, anataka aone Afrika ikiandaa fainali hizo. Mataifa yaliyokuwa yakiwania Fainali za 2010 ni England, Afrika Kusini yenyewe, Ujerumani, Morocco na Brazil

Wafuatao ni marais ambao ama walikaimu au waliongoza Fifa kama marais wake. Infantino ni kiongozi wa 12 katika mlolongo wa watawala ndani ya Shirikisho la Kimataifa la Soka, Fifa.

1.Rais wa kwanza wa Fifa alikuwa Robert Guérin ambaye ni Mfaransa ambaye alizaliwa Juni 28, 1876 na alifariki Machi 19, 1952 (akiwa na miaka 75). Aliiongoza Fifa kwa miaka miwili, aliingia madarakani Mei 23, 1904 hadi Juni 4, 1906.

2.Daniel Burley Woolfall, raia wa Uingereza. Alizaliwa Juni 15, 1852 na alifariki Oktoba 24, 1918 (akiwa na miaka 66) Aliiongoza Fifa kuanzia Juni 4, 1906 hadi Oktoba 24, 1918.

3.Cornelis August Wilhelm Hirschman, raia wa Uholanzi. Alizaliwa Februari 16, 1877 na alifariki Juni 26, 1951 (akiwa na miaka 74). Aliingia madarakani Oktoba 24, 1918 (akikaimu) hadi mwaka 1920.

4.Jules Rimet Raia wa Ufaransa, alizaliwa Oktoba 14, 1873 na alifariki Oktoba 16, 1956 (akiwa na miaka 83). Aliongoza Fifa kuanza 1920 hadi Machi 1, 1921.

5.Rodolphe Seeldrayers, raia wa Ubelgiji, alizalia Desemba 16, 1876 na alifariki Oktoba 7, 1955 (akiwa na miaka 78). Aliingia madarakani Juni 21, 1954 hadi Oktoba 7, 1955.

6.Raia wa Uingereza, Arthur Drewry alizaliwa Machi 3, 1891 na alifariki Machi 25, 1961 (akiwa na miaka 70). Alikaimu nafasi Fifa kuanzia Oktoba 7, 1955 hadi Juni 9, 1956.

7.Ernst Thommen, raia wa Uswisi alizaliwa Januari 23, 1899 na alifariki Mei 14, 1967 (akiwa na miaka 68). Aliingia Fifa akikaimu Machi 25, 1961 hadi Septemba 28, 1961.

8.Raia wa Uingereza, Stanley Rous alizaliwa Aprili 25, 1895 na alifariki Julai 1986 (akiwa na miaka 91). Aliingia ofisini Septemba 28, 1961 hadi Mei 8, 1974.

9.João Havelange, Mbrazil aliyezaliwa Mei 8, 1916 na alifariki Agosti 16, 2016 (akiwa na miaka 100). Aliongoza Fifa kuanza Mei 8, 1974 hadi Juni 8, 1998.

10.Sepp Blatter, Raia wa Uswisi alizaliwa Machi 10, 1936 (ana miaka 81). Bado anaishi na aliiongoza Fifa kuanzia Juni 8, 1998 hadi Oktoba 2015 (alisimamishwa).

11.Issa Hayatou, raia wa Cameroon, alizaliwa Agosti, 9 1946 (ana miaka 71). Alikaimu urais Fifa, Oktoba 8, 2015 hadi Februari 26, 2016.

12.Gianni Infantino, raia wa Uswisi-Italia. Alizaliwa Machi 23, 1970 (ana miaka 47). Aliingia madarakani Februari 26, 2016 hadi sasa.

Monday, February 19, 2018

Hii ndiyo nafasi ya michezo na utalii

 

By Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Ni bahati na fursa ya kipekee ambayo Tanzania imepata kutokana na kupata nafasi ya kuandaa mkutano huo hasa ukizingatia ukweli kwamba imekuwa ni nadra kwa nchi za Afrika hasa zile za ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati kuandaa matukio makubwa ya kisoka kama mkutano huo.

Pengine wapo mashabiki na wadau wa soka ambao bado hadi sasa hawajapata ufahamu wa umuhimu wa tukio hilo kubwa ambalo linakwenda kufanyika hapa nchini siku chache zijazo.

Kwa kulitambua hilo, Spoti Mikiki linakuletea tathmini ya jinsi Tanzania inavyoweza kunufaika kutokana na Mkutano wa Mwaka wa Fifa ambao utafanyika hapa jijini, Februari 22.

Kukuza Utalii

Ujio huo wa Infantino utahusisha maofisa na viongozi wa vyama na mashirikisho ya soka kutoka nchi mbalimbali duniani ambao siku chache watakazokuwepo zinaweza kutumiwa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kama Mbuga na Hifadhi za Wanyama, maeneo ya kihistoria pamoja na utamaduni wa jamii mbalimbali za Kitanzania.

Fursa ya kiuchumi

Ni wazi pato la nchi litaongezeka kwa siku hizo chache ambazo ujumbe wa Fifa utakuwepo hapa nchini kwani ujio wao utaimarisha na kufungua fursa za kibiashara pamoja na kuongeza fedha za kigeni ambazo watazitumia katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali katika siku zote watakazokuwepo Tanzania.

Wafanyabiashara wa hoteli ndio wanaonekana watanufaika zaidi kupitia mkutano huo kwani wao ndio watalazimika kutoa huduma za malazi na vyakula kwa wageni hao.

Mtazamo chanya

Sekta ya michezo hasa mpira wa miguu imekuwa haipewi kipaumbele kikubwa hapa nchini tofauti na kwingineko ambako michezo inatazamwa kama moja ya sekta muhimu za kukuza uchumi na pato la nchi.

Pengine ujio huo wa Fifa na wajumbe wake unaweza kubadilisha mtazamo uliopo kwa sasa kwa sekta ya michezo na kufungua zama mpya za kuthamini na kuitazama nyanja hii kama miongoni mwa mambo yanayoweza kuleta maendeleo kwa Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangala alisema mbali ya kuongeza imani ya nchi mbalimbali kwa Tanzania pamoja na kuongeza fedha za kigeni, pia utasaidia kuitangaza nchi.

“Ujio wa ndugu zetu wa Fifa kuja kufanya mkutano mkuu wa kimataifa nchini maana yake tunafaidika kwa kiasi kikubwa sana kwenye sekta hii ya utalii. Faida kubwa ya kwanza ambayo tunaipata ni kwamba, ujio wa Fifa unaitangaza nchi yetu.

Tutafaidika na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa, wakiwa hapa watalala kwenye hoteli, watakula vyakula vya hapa lakini pia wanaweza wakatamani kwenda kwenye mbuga za wanyama na kadhalika.

Nimeona niwaalike kutembelea mbuga za wanyama na vivutio mbalimbali vya utalii kama fukwe na maeneo mbalimbali ya kumbukumbu na historia tuliyonayo hapa nchini maeneo ya utamaduni ili wakienda huko kwao wawe mabalozi kwa wenzao. Nitatengeneza ‘package’ maalumu kuwapa kama ofa endapo watapenda kwenda kutembea kwenye maeneo hayo ya utalii,” alisema Waziri Kigangwala.

Ushawishi kwa Fifa

FIFA imekuwa ikitoa fedha kwa mashirikisho na vyama vya mpira wa miguu kwa nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kusaidia maendeleo ya mchezo wa soka hasa ukizingatiwa na ukweli kwamba uendeshaji wa mchezo wa soka umekuwa ni wa gharama kubwa.

Mara kwa mara fedha hizo hutolewa kwa ajili ya kuendeshea miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundominu ya soka, soka la ufukweni, vijana na wanawake sambamba na kuimarisha masuala ya utawala kwenye mpira wa miguu.

Kadri FIFA inavyopata ripoti chanya za utekelezaji wa miradi ambayo imekuwa ikitoa fedha zake, ndipo inaposhawishika zaidi kuipatia nchi husika fedha nyingine kwa haraka zaidi pindi inapoomba.

Kama FIFA itapata nafasi ya kuona kwa macho miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa kutokana na fedha zake, kuna uwezekano mkubwa ikawa fursa muhimu kwa Tanzania kunufaika zaidi na fedha kutoka Fifa.

Monday, February 12, 2018

LIGI KUU BARA 2017/18-Simba ni bomu lililolipuka, wanatafutana

 

By Thomas Ng’itu, Mwananchi

Kwa waliokuwepo miaka kama sita, saba hivi wanakumbuka vizuri milipuko ya Mbagala na Gongo la Mboto. Iliumiza na kusababisha hekaheka nyingi. Hatutaki kukumbusha ya huko nyuma kwa kuwa yana maumivu mengi.

Lakini hayo yanaweza kuwa kama Simba ya sasa. Bomu likilipuka kila mtu anatafuta njia yake. Watu wanatafutana sasa. Hii ndivyo ilivyo kwa Simba. Kila timu zinatafutana sasa, wamtegee wapi Simba akwame.

Simba hii ni kama moto wa gesi, hauzimiki kirahisi. Simba imecheza mechi 17 imeshinda 12, sare tano na ina pointi 41. Hasimu wake Yanga wanafuatia kwa kuwa na pointi 34 wakati Azam wanaotingishatingisha wana pointi 33.

Wekundu hao wa Msimbazi wanaongoza ligi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam, kwa bao la Emmanuel Okwi ndilo lililoifanya timu hiyo kuzidi kujihakikishia nafasi ya ubingwa baada ya mechi hiyo ngumu. Mechi nyingine ambayo Simba imeshtua ni dhidi ya Singida United iliyoichapa mabao 4-0.

Kwa msimu huu kikosi cha Simba kinaonekana kubadilika aina yake ya uchezaji baada ya kuongezeka spidi na pasi nyingi za kusonga mbele, kupata mabao muhimu na kuifanya timu hiyo kusonga mbele.

BENCHI LA UFUNDI

Baada ya kipigo cha Green Warriors, uongozi wa Simba ulimtimua Joseph Omog na kumpa mikoba kocha Masoud Djuma, na kocha huyu alipotambulisha mfumo wake wa 3-5-2 watu wengi walikuwa wakimbeza katika Mapinduzi Cup. Lakini baada mfumo huo kuzoeleka hivi sasa watu wameanza kumuelewa kitu ambacho alikuwa anakitengeneza kwani mfumo huo, umekuwa ukiwafanya viungo wake kucheza kwa uhuru, huku viungo wa timu pinzani wakipata tabu.

Nyuma amekuwa akiwachezesha Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili na Asante kwasi, ambapo Kwasi ameonekana kuwa na msaada wa kutosha katika upande wa kushoto kutokana na spidi yake ya kupiga krosi pamoja na kupanda na kushuka kwa haraka.

Vile vile mfumo wa 4-4-2, katika kikosi hicho umekuwa na msaada katika kikosi hicho kwani nyuma wakicheza Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Shomari Kapombe na Asante Kwasi, huku katikati wakiwa Said Ndemla, James Kotei, Jonas Mkude na Shiza kichuya timu hiyo inakuwa bora zaidi. Mbele hupangwa John Bocco na Emmanuel Okwi.

Hata hivyo, baada ya kuja Pierre Lechantre, bado Simba wanaendelea na mifumo hiyo kutokana na Wafaransa wamekuwa wakifanana mifumo na Wanyarwanda, hivyo imekuwa wepesi makocha hao kufanya kazi kwa pamoja.

MANULA KIBOKO

Nyanda wa Simba, Aishi Manula hivi sasa ndio kipa tegemeo katika kikosi cha Simba, baada ya kuondoka kwenda kufunga pingu za maisha na mpenzi wake, timu hiyo ilikuwa ikipata matokeo ndivyo sivyo hasa katika kombe la Mapinduzi.

Makipa Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja, bado hawajaonyesha upinzani wa kutosha kwa kipa huyo hali ambayo imeanza kuzua mjadala juu ya mbadala wake ikitokea Manula anapata majeraha au adhabu.

BEKI YAO BALAA

Usajili wa Asante Kwasi katika kikosi cha Simba ni kama umemfanya beki na mchezaji bora wa Simba msimu uliopita, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kukosa nafasi katika mzunguko huu wa pili kwa sababu kiwango cha Kwasi kimekuwa kikipanda kadri siku zinavyokwenda.

Kwasi ana uwezo mkubwa wa kupiga aina mbili za krosi, ana uwezo wa kupiga krosi za juu na mshambuliaji akafunga kwa kutumia kichwa, lakini vile vile ana uwezo wa kufosi na kuingia ndani ya dimba na kisha kutoa pasi kwa mshambuliaji na kupata bao kwa wepesi na lisipopatika bao basi kutatokea majanga yoyote akiwa ndani ya dimba.

Huku Tshabalala alikuwa na uwezo wa kupiga krosi za juu na kufanya timu ikapata mabao, lakini pia vile vile, mchezaji huyu alikuwa na uwezo wa kupanda na kushuka kwa wakati, lakini ujio wa Kwasi utamfanya awe katika wakati mgumu katika kikosi hicho cha Msimbazi.

Katika kiungo, mabeki wao Erasto Nyoni na Yusuph Mlipili, wameonekana kuelewana sana, inawezekana kwamba Simba walimsajili Mlipili wakimfanya kama nyongeza, lakini uwezo ambao beki huyu ameuonyesha hivi sasa ni mkubwa kuliko.

Licha ya kwamba Juuko Murshid na Salim Mbonde kuumia, Mlipili amejihakikishia namba katika kikosi hicho kutokana na uwezo ambao ameuonyesha, hasa katika mechi dhidi ya Singida United na Simba dhidi ya Azam, kwani alitulia na kuwatuliza vizuri washambuliaji wa Azam.

Lakini vile vile kwa upande wa beki Shomari Kapombe, ambaye alikuwa anaonekana kama ndio tayari ameshamaliza mpira wake, beki huyo amekuwa mwiba wa kuotea mbali katika upande wa kulia kutokana na spidi yake.

Kapombe kiwango chake kimerudi mara mbili yake baada ya kutoka majeruhi, kwasababu ameonekana kukomaa katika kupambana na mabeki wa timu pinzani, lakini vile vile uwezo wake wa kupiga krosi za uhakika na kiwango katika michezo aliyocheza tangu arejee katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar.

Spidi ya Kapombe na uwezo wake wa kupeleka mashambulizi, ukichanganya spidi ya Kwasi basi ndio wachezaji wa Simba ambao wanapeleka mashambulizi sikuhizi katika timu hiyo, mabao mengi huwa yanatokea katika upande wa wachezaji hawa.

MKUDE, NDEMLA, KOTEI USIPIME

Kiungo ndio kila kitu katika timu, Simba iliwahi kuwa na kiungo mkata umeme siku za nyuma Patrick Mafisango, lakini tayari ameshatangulia mbele za haki.

Hivi sasa Simba wameshaanza angalau kupoteza machungu ya awali ya kumkosa mchezaji huyo, baada ya kombinesheni ya hatari kutoka kwa Kotei, Mkude na Ndemla.

Viungo hawa wakiwa wanacheza kwa pamoja, hasa Kotei na Mkude humfanya Ndemla awe huru kufanya kazi yake kwasababu watu wa kumkabia na kumfanya awe huru wanakuwepo.

Mkude na Kotei wote kwa pamoja wanakaba vizuri vilivyo, hivyo wakikutana na timu ambayo inakuwa imeweka viungo wachache kivyovyote lazima wazidiwe na Simba kwasababu ya ujazo wa viungo ambao wanakuwa wamewekwa. Mkude ana uwezo wa kupiga pasi za mwisho na kukaba, lakini vile vile pia ana uwezo wa kupiga mashuti kama ilivyo kwa Ndemla, hivyo muda mwingine wanaweza wakashinda pia na sio kutengeneza.

Kotei yeye kazi yake ni moja tu kuhakikisha viungo wa timu pinzani hawafanyi vizuri katika dimba la katikati, huwa hana kazi nyingine yoyote zaidi ya hiyo kwa Mghana huyu akiwa yupo katika dimba lake.

Vile vile ana uwezo wa kumudu kucheza beki ya kati, hivyo anakuwa na msaada mkubwa akiwa katika kikosi cha Simba, hii ni sifa mojawapo ya wachezaji wa Simba msimu huu, kwani Kwasi,Nyoni, Kotei na Kapombe wote wana uwezo wa kucheza namba zaidi ya moja uwanjani.

KOMBINESHENI YA OKWI, BOCCO ACHA KABISA

Safari hii klabu ya Simba ina muunganiko mzuri wa washambuliaji wake, baada ya muunganiko wa John Bocco na Emmanuel Okwi kutoka Uganda.

Okwi hivi sasa ana mabao kumi na tisa, huku akiwa ndio mfungaji anayeongoza kwa mabao katika ligi kuu huku akifatia Chirwa, ambaye ana mabao kumi.

Hata hivyo Bocco naye pia ana mabao tisa hivyo inaonekana kabisa jinsi ambavyo wachezaji hawa wanavyoweza kufunga kwa pamoja, tofauti na vilabu vingine ambavyo unakuta mchezaji mmoja pekee ndio anafunga mabao mengi.

Kutokana na jinsi ambavyo wachezaji hawa wanashirikiana pale mbele katika kumi na nane kunawafanya waweze kutamba, kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.

Kitu kingine ambacho kinawasaidia Simba hivi sasa ni kwamba, kila aina ya bao wanalolitaka wanalipata, kwasababu Okwi ana uwezo wa kufunga kwa kutumia mguu na kichwa, pamoja na kupiga mipira ya adhabu vizuri na kuweka kimiani.

Vile vile Bocco naye ni mzuri katika mipira ya juu, lakini pia ana uwezo wa kumiliki mpira vizuri na kisha kuwatoka mabeki na kufunga, vilevile ana uwezo wa kuulinda mpira huo kama akiwa nasuguana na mabeki wengi, kisha kusubili mchezaji mwenzake aje na kumpa kisha kufunga.

WACHEZAJI WA AKIBA PIA MOTO

Hakika, hivi sasa kikosi cha Simba ni kipana, wakati ambapo wanafanya usajili wengi walikuwa wakiwaona kama wanasajili ovyo ovyo lakini hivi sasa ndio tunaona jinsi ambavyo wamjipanga.

Katika nafasi ya kiungo nje wana Mzamiru Yassin na Mwinyi Kazimoto, Mzamiru msimu uliopita alikuwa katika kiwango cha juu na kucheza mechi za mfululizo, hata hivi sasa anavyopumzishwa akiingia huwa anafanya maajabu vile vile.

Kazimoto naye amekuwa akibadilisha matokeo kila akipewa nafasi katika kikosi hicho na hii ni kutokana na uwezo wake wa kumiliki mipira na kujiamini vilivyo.

Hata kiungo, Nicholas Gyan, ambaye muda mwingine huchezeshwa kama beki wa kulia au winga, naye sio kama anakaa benchi kutokana na uwezo mdogo bali kutokana na upana wa kikosi uliopo katika kikosi hicho, lakini uwezo wake ni mkubwa.

Tshabalala ndio amejikuta katika wakati mgumu, kiwango cha Kwasi kimemuweka katika wakati mgumu kwenye kikosi cha Simba hivi sasa, lakini uwezo wake unajulikana kwamba ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.

Msimu uliopita alikuwa katika kiwango kizuri, alikuwa mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha timu ya Taifa, lakini hivi sasa atakuwa katika wakati mgumu kutokana na kutopata nafasi ya kucheza kutokana na ushindani.

Monday, February 12, 2018

Kane utampenda, apiga bao la maana Arsenal ikifa Wembley

 

Mauricio Pochettino, amesema hakuna mshambuliaji mahiri kama Harry Kane.

Kocha huyo amemtaja Kane ni mmoja wa washambuliaji hodari aliyewahi kumuona duniani.

Kauli ya kocha huyo imekuja muda mfupi, baada ya Kane kufunga bao maridadi la mpira wa kichwa dhidi ya Arsenal juzi usiku.

Tottenham Hotspurs ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Wembley, ilishinda bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Spurs inatumia uwanja huo kwa kuwa White Hart Lane upo katika matengenezo makubwa.

Mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya England, aliruka hewani baada ya kumzidi maarifa nahodha wa Arsenal, Laurent Koscielny kabla ya kumtungua kipa Petr Cech dakika ya 49.

Matokeo hayo yameisogeza Spurs hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England nyuma ya Manchester City na Manchester United.

Man City imezidi kujikita kileleni baada ya juzi usiku kuvuna pointi tatu kwa kuilaza Leicester City ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Etihad.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekubali bao la nahodha huyo wa timu ya Taifa ya England.

Wenger alisema mshambuliaji huyo alicheza kwa kiwango bora katika mchezo huo.

“Wakati mwingine inabidi ukubali kwa sababu ya kazi nzuri anayofanya. Lakini nataka nikwambie, narudia kwa uzoefu wangu ni mmoja wa wachezaji mahiri duniani,” alisema Pochettino.

Alisema Kane ni hazina ya sasa na baadaye kwa kuwa ana kipaji cha soka ambacho kimekuwa chachu ya mafanikio Spurs.

Kocha huyo raia wa Argentina, alisema anajivunia kuwa na mshambuliaji aina ya Kane ambaye ana uwezo mzuri wa kufunga mabao akiwa katika nafasi yoyote uwanjani.

“Kane ni mshambuliaji wa aina yake. Anafunga dhidi ya beki yeyote anayecheza naye,” alisema Pochettino.

Mshambuliaji huyo alisema ni faraja kwake kufunga bao katika mchezo mgumu uliokuwa na ushindani.

Bao la Kane linaweza kuzidisha shauku ya kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ambaye amekuwa akimmezea mate muda mrefu.

Real Madrid iliwahi kumtupia ndoano Kane katika usajili wa dirisha dogo kabla ya mpango huo kukwama. Zidane anasubiri usajili wa majira ya kiangazi.

Monday, February 12, 2018

Wadhamini wanavyozinogesha timu

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Juzi juzi, klabu ya Azam imeendeleza ushirikiano wake na Benki ya NMB baada ya kusaini rasmi mkataba mpya wa mwaka mmoja na benki hiyo kuidhamini kwenye mechi zake za Ligi Kuu na ikitokea kimataifa.

Hafla hiyo ya kusainiana mkataba ilifanyika Makao Makuu ya NMB na Azam FC iliwakilishwa na mmoja ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Yusuf Bakhresa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Azam Media Ltd, na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdul Mohamed huku Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, akitia saini kwa upande wa benki hiyo.

Mkataba huo unaendeleza ule wa misimu minne, tangu NMB ilipoanza kuidhamini 2014 ilipoibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambapo hii ni mara ya tatu wanarefusha ushirikiano huo na Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, Mohamed, aliishukuru NMB kwa kuendelea kuwadhamini na kuahidi kuendeleza moto wao wa kutwaa mataji chini ya udhamini wa benki hiyo baada ya kuanza na Mapinduzi Cup msimu huu.

Naye, Bussemaker, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo bora iliyoshamiri mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wao, ikiwemo minne ya kuidhamini. Hao ni Azam katika siku za karibuni.

Wadhamini wanaleta hamasa na msisimko, safari hii asilimia kubwa ya timu zina wadhamini wao kuanzia Simba na Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa.

Simba kwa nafasi yake na uwezo wake, ilitakiwa jezi kuchafuka kwa matangazo, lakini jezi zao ni safi zaidi ya matangazo ya SportPesa.

Yanga pia iliingia mkataba na kampuni ya Macron itakayowapa jezi pamoja na Afya.

Singida United imekuwa moto, lakini yote ni kutokana na nguvu ya Kampuni ya kutengeneza matairi ya Yara,Sportpesa,Benki ya KCB na Kampuni ya Puma.

Kwa upande wa Mbao FC, iko chini ya Kampuni ya kuuza matrekta ya GF Trucks pamoja na kampuni ya kuuza maziwa ya Cowbell ambao pia wanaidhamini Ruvu Shooting.

Wengine wanaotamba katika ligi kwa udhamini ni Mbeya City wanaojidai na udhamini wa Coca-Cola, Kapuni ya Binslum Tyre Company ambayo pia imetoa basi.

Ndanda imerahisishiwa maisha na Kampuni ya kutengeneza mabati ya Kiboko na Kampuni ya kutengeneza maji ya Ndanda Springs Water. Majimajiya Songea inacheza na sokabet.

Timu ambazo hazina wadhamini mpaka sasa ni Mtibwa Sugar, Prisons, Lipuli, Stand United, Mwadui, Kagera Sugar na Njombe Mji.

Timu zilizopanda Ligi Kuu

Mwaka huu, timu sita zimekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao. KMC na Lyon, JKT Tanzania, Biashara Mara, Coastal Union na Alliance Schools ya Mwanza.

Hata hivyo, kabla ya kuanza ligi hiyo ya timu 20, zinatakiwa kuanza kusaka wadhamini kwa ajili ya kuzisaidia timu zao angalau kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa gharama za uendeshaji ni kubwa.

Monday, February 12, 2018

Nchimbi hataki mambo mengi dimbani

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Ditram Nchimbi ni mshambuliaji hatari wa Njombe Mji anayetegemewa katika ufungaji mabao kwenye kikosi hicho ambacho kipo kwenye hatari ya kushuka daraja.

Katika michezo 17 ambayo Njombe Mji imecheza, imeshinda mara mbili, kufungwa mara nane na kutoka sare mara saba,jumla ya pointi walizokusanya ni 13.

Nchimbi amezungumza na Spoti Mikiki kuhusu mwenendo wa timu yake, safari yake ya soka ilipoanzia,changamoto na Malengo.

“Bado tuna nafasi ya kupigana ili tujinasue kwenye hatari ya kushuka daraja, ndiyo kwanza tumeanza mzunguko wa kwanza hivyo tuna kila sababu ya kuanza kuyabadili matokeo mabaya kuwa matokeo mazuri,” amesema.

Safari

“Kiujumla nimecheza ligi zote Bongo,kuanzia daraja la 4 ,3,2,1.Nilianza kucheza mpira huko Tunduru, Ruvuma timu inaitwa Tunduru Town Small Boys ili kuwa Ligi Daraja Nne. “Baadaye nikajiunga na Mbinga United ya daraja tatu, wakati huo ikiitwa Ligi ya Kanda, tukacheza la pili na haikuchukua muda nikasajiliwa na Majimaji ambayo ilikuwa daraja la kwanza.

“Nilikuwa sehemu ya wachezaji ambao waliipandisha daraja Majimaji kwa kufunga mabao 10 kwenye michezo ya Kundi letu A,” anasema Nchimbi. Baada ya kuipandisha daraja,mshambuliaji huyo hakudumu Majimaji na alijiunga na Mbeya City kwa mataba wa mwaka mmoja na nusu, ulipomalizika akahamia Njombe Mji.

Changamoto

“Changamoto ni nyingi sana kutokana na mazingira ya mpira wetu, ukisema uanze kuzizungumzia unaweza usimalize.Nilikuwa nazichukulia kama sehemu ya utafutaji,” anasema.

Malengo

“Kama nisipofikia hatua ya kucheza Ulaya basi ni bora nipate nafasi ya kucheza ligi ya Afrika Kusini na nyinginezo nje ya Tanzania,hilo ni lengo langu kuu” anasema.

Chakula na Mavazi

“Aiseeh!! Mimi Sio mtu wa mambo mengi kuanzia kwenye mavazi hata chakula, napenda kuvaa pensi na vesti.Chakula nachopenda kula sana ni Kitimoto na ndizi za kuchoma,” anasema.

Monday, February 12, 2018

Ninaifanya Kenya daraja la kuvuka kucheza kimataifa

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Kipa wa zamani wa Everton ya England, Timothy Matthew Howard ‘Tim Howard’ (38) ambaye anaichezea Colorado Rapids ya nyumbani kwao, Marekani aliwahi kusema kuwa ilikuwa ni ndoto yake kuwa mchezaji wa daraja la juu.

Kilichosemwa na kufanikishwa na Howard kinaendana na kile ambacho amekiazimia beki na kati wa zamani wa Majimaji ya Songea, Tumba Lui (26) ambaye amejiunga na Wazito F.C ya Kenya kwa makataba wa miaka miwili.

Wazito F.C ya Nairobi ambayo ipo chini ya kocha wao mkuu, Frank Ouna inashiriki Ligi Kuu Kenya msimu huu wa 2018/2019 kutokana na kupanda kwao daraja mwaka jana.

Leo katika mfululizo wa Makala zetu za ufuatiliaji, uvumbuzi wa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje, tunaye beki huyo mwenye ndoto pia ya kuitumikia Taifa Stars.

“Wakati naanza kucheza mpira wa mtaani, nilipenda sana siku moja kuja kuwa mchezaji wa kimataifa kwa kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi, sijawahi kukata tamaa kwa hata kuwaza kuachana na soka.

“Majimaji imekuwa sehemu ya kupiga kwangu hatua kwa kuonekana, unaweza ukajiulizaje ni kwa namna gani? Kwa sababu hatujashiriki mashindano yoyote ya kimataifa.

“Nilipokuwa nacheza Ligi Kuu Bara na Majimaji kumbe kulikuwa na kocha wa Wazito alikuwa anafuatilia mwenendo wangu kwa kipindi kirefu,” anasema beki huyo.

Anaendelea; “Safari hii ambayo wamenisajili, kocha alikuja maana tayari ilikuwa ameshaipandisha Wazito daraja na kuamua kufanya mawasiliano ya haraka ili kuona kama kuna uwezekano wa kunisajili.

“Sikuona kama kunatatizo la kufanya uamuzi kwa upande wangu kwa sababu niliona huo unaweza kuwa mwanzo wa kupiga hatua zaidi, mwanzoni kupata nafasi ya kucheza ligi kuu niliona ni hatua ya kwanza.”

Tumba anadai kuwa alifanya makubalino na Majimaji ili apate ruhusa ya kwenda kufungua ukurasa wake mpya wa utafutaji wa mafanikio upande wa soka la kimataifa.

“Japo haikuwa rahisi lakini nilipata barua ya kuniruhusu kujiunga na Wazito ambao nimeingia nao mkataba wa miaka miwili, na ninatarajia kuitumia Ligi Kuu Kenya kama daraja la kuvukia na kusonga mbele kama ilivyokuwa Majimaji.

Hata hivyo, Tumba hakuficha shauku aliyonayo ya kuichezea timu ya Taifa chini ya Salum Mayanga.

“Hakuna kitu ambacho nitaweza kujivunia kama kuwa shujaa kwa Taifa langu, unaweza kuwa shujaa ndani ya klabu fulani lakini ule uthamani wake ukawa mdogo.

“Taifa linaweza kuwakumbuka mashujaa wake.Nitakapo hitajika siwezi kusita kuja kuipigania Tanzania,nimelelewa na kukulia hapa kwa hiyo siwezi kuwa na chaguo la kuchezea Taifa lingine”anasema.

Anaendelea: “Matarajio yangu Kenya ni ushindani, nasikia kuna Watanzania wenzangu kule ambao wanacheza ligi hivyo sidhani kama nitakuwa mpweke.

Bado nipo Afrika Mashariki kwa hiyo siwezi kupata shida kwenye mazungumzo, vyakula na utamaduni mwingine, karibu nchi zote za Afrika Mashariki tunaingiliana kwenye mambo mbalimbali.”

Nyota wengine wa Kitanzania wanaocheza Ligi Kuu Kenya ni Abdul Hilal (Tusker), Aman Kyatta (Chemelil Sugar),Hamis Abdallah (SoNY Sugar) na David Naftar anayekipiga Nakumatt.

Katika mazungumzo hayo na Spoti Mikiki, Tumba hakuacha kutoa meneno yake kwa viongozi wa Majimaji, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa naye pamoja pindi akiichezea timu hiyo.

“Ninawashukuru sana viongozi na wachezaji wenzangu kwa nyakati mbaya na nzuri ambazo tumekuwa pamoja, nilijituma kuichezea Majimaji kwa nguvu na akiri zangu zote. Ninawatakia mwenendo mzuri kwenye ligi,” anasema.

Utekelezaji wa alichokisema Howard katika kuhitaji kuwa mchezaji wa daraja la juu, ulianza mwaka, 1997 kwa kuicheze North Jersey Imperials mara baada ya kulelewa na Central Jersey Cosmos.

Dhamira yake ya kweli miaka kadhaa baadaye ilimfanya kuwa mchezaji wa daraja la juu kwa kuichezea hata Manchester United kuanzia mwaka 2003 hadi 2007 na baadaye kuhamia Everton.

Howard mwenye miaka 38 soka lake limefikia ukingoni lakini Tumba ana nafasi ya kuendelea kupigania ndoto yake ya kuhitaji kuwa mchezaji wa daraja la juu.

Monday, February 12, 2018

Kops itabidi waipende tu ndoa ya Klopp na Fenway Group

 

Ikawa usiku na ikawa mchana, sekunde zikasogea na masaa yakaganda na wala siku hazikuweza kuganda, Liverpool imeweza kuishi kipindi cha miaka zaidi ya ishirini pasipo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza. Mpinzani Fulani mwenye roho ya korosho na anayeweza kutaka kuwatibua washabiki wa Liverpool anaweza kwenda mbali zaidi na kusema kuwa kuna binadamu wengi ambao wameweza kuingia kwenye ndoa na hawajawahi kuishuhudia Liverpool ikitwaa ubingwa huo wenye maana zaidi kwa Uingereza.

Huu ni uhalisia ambao unaweza kukupa sababu ya kuamini kuwa, kuna kitu hakijawahi kuwa sawa tangu miaka ya udhamini wa Carlsberg hadi leo Standard Chartered wakiwa kifuani.

Wapo wanaoweza kulileta suala hili na kuwa uongozi haujawahi kuwa makini na baadhi ya matajiri kama Tom Hicks na George Gillet ndio waliochangia kuipoteza Liverpool na kukaribia kuizamisha kwenye shimo la moto, yaani walikaribia kuiteketeza kabisa.

Hata hivyo, kumekuwepo na mwamko kwa misimu takribani miaka mitano iliyopita tangu klabu hiyo itwaliwe na wamarekani wanaomiliki kampuni ya FENWAY Group wakiongozwa na John Henry.

Liverpool imekuwa ikiongezeka thamani kila uchwao, wamekuwa na kiburi cha kuondoa makocha wa wastani mpaka leo wana Jurgen Klopp.

Pamoja na ubahiri wao wa hapo awali, walipata kocha ambaye aliwapa sababu ya kupata wachezaji kwa bei za kawaida kwenye soko kichaa la sasa na kuwapa nafasi ya kuweza kufanya usajili mkubwa walau mara moja kwa kila dirisha la usajili kwa sasa.

Kwa misimu inayoelekea kuwa mitatu sasa tangu atue klabuni hapo, Jurgen Klopp amesajili wachezaji ambao hawakuzidi Pauni 35 milioni kwa mchezaji mmoja na bado aliweza kuiweka Liverpool kwenye picha sahihi ya ushindani.

Kabla ya Virgil Van Djik, mchezaji ghali kwenye mikono ya Klopp alikuwa Oxlade Chamberlain pamoja na Mohamed Salah.

Kwa msimu uliopita Klopp aliirejesha Liverpool kwenye klabu bingwa Ulaya huku mchezaji wake ghali akiwa ni Sadio Mane ambaye hata hivyo aliumia kwa kipindi kirefu, thamani yake ilikuwa Pauni 30milioni.

Kipindi hiki chote, John Henry alikuwa Marekani na mkewe Linda Pizzuti Henry wakiwa wameegemeana begani wakitazama mchezo mwingine wa klabu ya baseball wanayoimiliki huko Marekani inayoitwa Boston Red Sox wakiamini sasa wamepata mtu atakayetuliza vichwa vyao anayeitwa Klopp.

Baseball ndo mchezo anaoupenda huyu mwanaume, pengine mkewe ni mfuatiliaji zaidi wa Liverpool kuliko yeye na ndio maana ni msumbufu Twitter kila Liverpool inaposhinda michezo mikubwa au wakati wa usajili akiwa shabiki mkubwa wa Marco Reus.

Baada ya kupandisha thamani ya klabu ya Liverpool kwenye mikono ya Klopp, kiburi kinaweza kuwa kimewapata sasa kutokana na ukweli kuwa wanaye mtu anayeendana na falsafa zao za “Moneyball”.

Moneyball tafsiri yake ni kutumia takwimu katika utendaji lakini pia kuhakikisha kuwa unanunua raslimali ambazo wengi wanaamini ni za bei ya kawaida na unauza zile ambazo wengi wanahisi zina thamani kubwa sokoni.

Kwenye mikono ya King Kenny Dalglish, walijaribu na usajili wa wachezaji kama Luis Enrique, Stewart Downing ulikuwa kwa ajili ya kuhakikisha mipira ya krosi inamshibisha Andy Carroll.

Kwa wakati huo, hawa ndio waliongoza kwa kupiga krosi nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England huku Carroll akiwa mshambuliaji aliyetumia mipira mingi zaidi ya krosi.

Jordan Henderson alikuwa mchezaji kinda zaidi aliyepiga pasi nyingi za uhakika na waliamini huyu atakuwa “project” ya muda mrefu.

Ni kipindi hiki ambacho kaka yangu Edo Kumwembe aliamini kuwa “Ghetto la Uingereza” lilikuwa limerejea na Liverpool ilikuwa itikise zaidi lakini alinacha alithibitika kuwepo kwenye ndoto hizi ambazo wengi tuliziamini.

Klabu ilitua kwenye mikono ya Brendan Rodgers ambaye alimpata Luis Suarez aliyekomaa na akajua kumtumia. Msimu ambao Rodgers hupewa lawama za kushindwa kujua namna ya kucheza michezo ya mwisho, na mashabiki wengi hawataki kukumbuka namna Gerrard alivyoteleza na kushindwa kuwapa ubingwa wake wa kwanza.

Ndoto pekee aliyoshindwa kuitimiza akiwa na Liverpool. Ni baada ya msimu huo na Brendan Rodgers alionekana kuvikwa shati kubwa linaloitwa Liverpool kwenye mwili wake mdogo.

Ni wakati huo ambao, Luis Suarez aliyeitwa “El Pistorelo” alikuwa ametua Barcelona na maisha hayakuwa tena sawa ndani ya Anfield, ukimya ulitawala, nyimbo ya You’ll Never Walk Alone ilififia kwa sababu washabiki walikosa miguu ya Suarez kwenye mwili wa Mario Balotelli, Ricky Lambert na baadae mchezaji aliyepingwa na kila mtu isipokuwa Brendan Rodgers mwenyewe, Christian Benteke.

Kulikuwa na akili moja tu iliyobaki baada ya wachezaji kuonekana kuchezeshwa nje ya nafasi zao na kitendo cha mchezaji Raheem Sterling kuonyesha wazi kuwa hataki kubaki Anfield kwa sababu hakuona “focus” na “future” kwa ajili ya maisha ya baadae.

Suala lilikuwa kupata kocha mwenye kariba ya kuvutia Liverpool na hakukuwa na wakati sahihi wa kumfukuza Rodgers kama ule ambao Klopp alipoamua kwenda likizo kuachana na soka.

Inawezekana Liverpool walifikiria kumbakisha Rodgers hadi mwisho wa msimu, lakini cheleachelea wangekuta mwana “Klopp” keshakuwa wa wengine. Na huu umekuwa uamuzi sahihi ambao haukuwarudisha haraka sokoni kusajili wachezaji wengi kwa mkupuo. Lallana aliyechokwa aligeuka lulu, Coutinho alipata kiwango chenye mwendelezo (consistency), Firmino alikuwa mwanaume wa shoka, Henderson akageuzwa kuwa mchezaji anayepiga pasi nyingi zaidi EPL na mashabiki wakakumbushwa kuna haja ya kuunga mkono klabu yao.

Hii ndio aina ya makocha wa ndoto ya uongozi wa John W Henry na mwenzake Tom Werner.

Moneyball ikaanza kufanikiwa, wakapatikana akina Wjinaldum kwa bei za kawaida kusukuma gurudumu huku akina Sakho wakiuzwa ghali, Benteke akiuzwa bei ya wizi, na Mane akipatikana kwa bei ambayo baada ya kucheza ndani ya jezi za Liverpool ilionekana bei ya kawaida. Maisha hayakubadilika mpaka kwa Salah ambaye inawezekana AS Roma wakawa wanajuta kumuuza kwa Pauni 32 milioni pekee.

Haya ni maisha yaliyokuwa ya ndoto za wamiliki hawa, wafanye vizuri kwa bajeti ndogo ya usajili na mishahara.

Ni katika kipindi hiki ambacho wamepata faida kubwa, lakini bado hawakuwa na muda wa kumimina fedha zao nyingi sokoni, wao humtuma Klopp atumie akili naye hawaangushi.

Wengi tulistuka namna gani Liverpool iliweza kutoa kiasi cha paundi milioni 75 kwa Van Djik, lakini ukweli ulipatikana kuwa walishapata paundi milioni 140 za Philippe Coutinho na bado wanaamini kuwa “TOP FOUR” ni halali yao. Hili ni tatizo kwa washabiki lakini sio tatizo kwa Klopp na wamiliki wanafurahia hilo.

Kuna kitu ni kigumu lakini itabidi mashabiki wa Liverpool wakielewe, na inawezekana itawapasa wakipende pia. Klopp anaamini anaweza kumbadili Chamberlain akatoa walau robo tatu ya Coutinho na maisha yakaendelea.

Kama ulikuwa hufahamu ni kuwa hata fedha za Keita Pauni45milioni zipo kwenye chenji ya Coutinho.

Sitoshangaa baada ya msimu mmoja Salah akauzwa Pauni150mil na maisha yakaendelea. Klopp kazi hii anaiweza na wao akina John Henry wanampenda kwa hili, ni kama Wenger na Arsenal yake.

Monday, February 5, 2018

Ronaldo aweka rehani kibarua cha Zidane Madrid

 

Mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo, ameshindwa kutuliza presha ya bosi wake Zinedine Zidane.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno, ndiye mfungaji bora wa Real Madrid katika mashindano mbalimbali.

Ronaldo, kinara wa kufunga mabao katika kikosi cha Real Madrid amegonga mwamba kuokoa kibarua cha Zidane.

Zidane amekalia kuti kavu baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri tangu kuanza msimu huu.

Real Madrid imeshindwa kufua dau mbele ya watani wake wa jadi Barcelona ambayo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Hispania.

Wakati Barcelona ikiwa kileleni kwa pointi 57, Real Madrid inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 39.

Jinamizi la matokeo mabaya limeendelea kuitesa Real Madrid, baada ya juzi usiku kupokwa tonge mdomoni dhidi ya Levante.

Zidane akiwa na matumaini ya kushusha presha katika mchezo huo, aliduwazwa dakika moja kabla ya mpira kumalizika kwa bao la kusawazisha.

Giampaolo Pazzini alipeleka kilio kwa Zidane kwa kufunga bao dakika moja kabla ya mpira kumalizika.

Real Madrid ilikuwa inaongoza mchezo huo hadi dakika ya 88 kabla ya Pazzini kufunga bao dakika ya 89.

Zidane, nahodha wa zamani wa timu ya Taifa y Ufaransa, aliondoka uwanjani akiwa amefura kwa hasira.

“Tulimiliki mpira vizuri hasa kipindi cha kwanza, lakini baada ya kufunga bao la pili hali ilikuwa tofauti, tulishindwa kujilinda kuepuka wapinzani wetu kusawazisha,” aling’aka Zidane.

Kocha huyo alisema mpira una njia zake, wamefanya makosa yaliyoigharimu timu katika mchezo aliodai walikuwa na nafasi kubwa ya kupata pointi tatu muhimu kwenye Ligi Kuu Hispania.

Licha ya kuwa na tofauti ya pointi 18 dhidi ya Barcelona, lakini hawezi kurusha taulo katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Hispania.

Monday, February 5, 2018

Yanga, Simba kuliamsha dude Afrika

 

By Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Miamba ya Tanzania Bara, Yanga na Simba, mwishoni mwa wiki hii zitaanza kibarua cha kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika kwa ngazi za klabu na zitakuwa nyumbani kwa mechi za hatua ya awali.

Yanga wanaoshiriki Ligi ya Mabingwa wataikaribisha St. Louis mabingwa wa Shelisheli, Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini wakati siku moja baadaye, Simba watapambana na Gendarmarie ya Djibout katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya wiki moja, Simba na Yanga zitakuwa ugenini kukamilisha vita ya kusaka tiketi ya kusonga mbele hadi raundi ya kwanza ambapo kama Yanga watafanikiwa kuitoa St. Louis, watakutana na mshindi wa michezo kati ya Township Rollers ya Botswana au El Merreikh ya Sudan, wakati Simba kama wakifanikiwa kusonga mbele, watakutana na timu itakayopita kati ya Al-Masry ya Misri au Green Buffaloes ya Zambia.

Wakati Yanga na Simba zikiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya kushiriki mashindano hayo, gazeti hili linakuletea dondoo fupi ya ushiriki wa timu hizo kwenye mashindano ya kimataifa.

Yanga

Ilijihakikishia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Yanga imekuwa na bahati ya kushiriki mashindano ya kimataifa mara kwa mara, lakini zaidi ya kufuzu mara mbili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati huo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mwaka 1998 na pia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016.

Inaingia kwenye mashindano ya mwaka huu huku zaidi ya wachezaji wake tisa waliokuwepo wakati wanafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016 wakiwa hawapo kikosini.

Simon Msuva ameuzwa Difaa el Jadidi ya Morocco, Haruna Niyonzima ametimkia Simba, Vicent Bossou ameachwa, wakati Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Amissi Tambwe, Kelvin Yondani wakiwa ni majeruhi na wameshindwa kurudi katika viwango vyao.

Msimu uliopita, Yanga ilitolewa na Zanaco ya Zambia kwenye hatua ya awali kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 jijini kabla ya kulazimishwa sare ya 0-0 ugenini na ilipoangukia kwenye Kombe la Shirikisho ilitolewa na MC Algers kwa matokeo ya jumla ya kufungwa 4-1.

Faida kubwa kwa Yanga ni kuanza na timu nyepesi katika kipindi ambacho msimu wa ligi huko Shelisheli umeshamalizika jambo linalofanya wapinzani wao wasipate maandalizi ya kutosha kuelekea mechi zitakazowakutanisha pia St. Louis wamekuwa hawana rekodi ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwani wameishia kwenye hatua za awali mara zote walizoshiriki.

Hii inaweza kuwasaidia Yanga kutotumia nguvu kubwa na kuanza kufanya maandalizi ya raundi ya kwanza ambayo wakifanikiwa kupenya, watafuzu kwenda hatua ya makundi.

Hata hivyo kiwango kilichoonyeshwa na Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara kwa sasa pamoja na matokeo ya Kombe la FA dhidi ya timu ya daraja la pili ya Ihefu FC kuna maswali juu ya utayari wao kwa mechi za kimataifa katika msimu huu.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema timu yake ina kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na lengo letu ni kufanya vizuri kwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mwaka huu kama tulivyofanya kwenye Kombe la Shirikisho miaka miwili iliyopita.

Tunaamini tuna kikosi kizuri ambacho kinaweza kupambana na timu yoyote hapa Afrika na kupata matokeo mazuri hivyo Wanayanga na Watanzania kwa ujumla wasiwe na hofu yoyote na tunawaomba watupe sapoti ya hali ya juu,” alisema Mkwasa.

Simba

Wamekuwa na rekodi tamu kwenye mashindano ya ngazi za klabu Afrika ikiwemo kufika hatua ya Fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993, kufuzu hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 pamoja na kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Mara ya mwisho kwao kushiriki mashindano ya kimataifa ilikuwa ni mwaka 2013 ambapo walitolewa kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Recreativo do Libolo kutoka Angola baada ya kuchapwa kipigo cha jumla cha mabao 5-0.

Walifungwa bao1-0, Dar es Salaam katika mechi ya kwanza kabla ya kwenda kupokea kibano cha mabao 4-0 ugenini huko Angola.

Wataanza na Gendarmarie ya Djibout ambayo haijulikani sana lakini kutokana na rekodi na kiwango cha soka la nchi hiyo, ni wazi kwamba wana kibarua chepesi cha kufuzu hatua inayofuata ingawa hawapaswi kuweka hata chembe ya dharau dhidi ya timu hiyo inayotoka nchi iliyo pembezoni mwa Bara la Afrika upande wa Kaskazini Mashariki.

Simba wapo kwenye kiwango bora kwa sasa, wakiongoza Ligi Kuu huku nguvu yao kubwa ikiwa kwenye safu yao ya ushambuliaji yenye nyota watatu wanaofukuzana kwa rekodi za kufumania nyavu, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.

Nguvu nyingine ya Simba ni kuwa na benchi imara la ufundi lenye uzoefu wa soka la Afrika likiongozwa na Mfaransa Pierre Lechantre anayesaidiwa na Masoud Djuma wote wanasifika kwa mbinu za kisasa na uwezo mkubwa wa kung’amua ubora wa timu pinzani.

Kingine kinachoibeba Simba ni upana wa kikosi chake ambacho kinaundwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye ubora na kiwango cha hali ya juu hivyo hawana presha kubwa hata wanapokumbana na tatizo la majeruhi au adhabu kwa wachezaji.

Changamoto kubwa ambayo inaonekana kuisumbua Simba kwenye mashindano ya kimataifa ni kukosa nidhamu ya mbinu pindi wanapokuwa ugenini, jambo ambalo limekuwa likiigharimu na kujikuta inaondolewa hata pale inapotangulia kuibuka na ushindi mnono nyumbani.

Mfano mwaka 2012, Simba ilitangulia kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Al-Ahly Shendi. Katika mchezo wa marudiano, Simba ilifanikiwa kuwabana vizuri Shendi hadi dakika ya 84 lakini ikajikuta ikiruhusu mabao matatu ya haraka ndani ya dakika sita za mwisho na walipofika hatua ya kupigiana penati, Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penati 9-8.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully alisema nadhani rekodi yetu katika mashindano ya kimataifa inajulikana na mara zote Simba inaposhiriki, imekuwa ikifanya vyema kulinganisha na timu nyingine pindi zinapopata nafasi.

“Tumerejea safari hii tukiwa na kikosi bora kinachofanya vizuri na kama uongozi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya mambo makubwa msimu huu.Wachezaji wanapata huduma sahihi na bora kwa wakati na kila ambacho kwa upande wetu tunapaswa kukifanya, tunakitekeleza ili tu tuweze kutimiza malengo yetu,” alisema Tully.

Klabu 59 zinashiriki Ligi ya Mabingwa huku klabu 54 zikitoana jasho katika Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.

Monday, February 5, 2018

Tanzania yasaka dhahabu madola baada ya miaka 20

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Tanzania inatarajiwa kushiriki kwa mara ya 14 michezo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kufanyika katika mji wa Gold Coast, Australia Aprili 4, mwaka huu.

Michezo ya Madola ina hadhi kwa kuwa inajumuisha wanamichezo mbalimbali duniani waliofuzu kwa kiwango bora.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimekuwa zikishiriki michezo ya Madola inayofanyika kila baada ya miaka minne.

Licha ya kupeleka wanamichezo kwenda kushindana, lakini Tanzania imeshindwa kutamba katika michezo hiyo kulinganisha na Kenya au Uganda.

Tanzania iliwahi kuwika kwenye michezo hiyo katika miaka ya 1970 hadi 1980 kwa kuwa ilikuwa na wanamichezo waliondaliwa vyema.

Baada ya kuondoka kizazi cha kina Timothy Kingu, aliyekuwa bondia nyota wa uzito wa juu, Tanzania imeshindwa kufanya vyema katika michezo ya Madola.

Ni miaka 20 imepita Tanzania imeshindwa kupata mafanikio katika ngumi baada ya mabondia wetu kutoka mikono mitupu.

Wakati mabondia wakiwa wamepoteza dira, kwa upande wa riadha ni miaka 12 sasa hakuna mwanariadha aliyevuna medali ya dhahabu baada ya Samson Ramadhani mwaka 2006.

Bondia Michael Yombayomba aliwatoa Watanzania kimasomaso mwaka 1998 kwa kutwaa medali ya dhahabu katika michezo hiyo iliyofanyika Australia na Malaysia.

Ushiriki wa Tanzania ulianza hivi

Tanzania ilisubiri hadi baada ya miaka minane kupata medali ya kwanza katika michezo ya Madola mwaka 1970.

Itakumbukwa Tanzania ilishiriki michezo ya Madola inayoshirikisha nchi zilizowahi kuwa koloni la Uingereza mwaka 1962.

Tanzania ilianza kushiriki kama Tanganyika, lakini baada ya Muungano na Zanzibar 1964, pande hizo mbili zimekuwa zikishiriki kama nchi moja. Tanganyika ilishindwa kung’ara kwenye michezo ya kwanza iliyofanyika Perth, Australia.

Miaka minne baadaye (mwaka 1966) ilishiriki michezo ya Madola iliyofanyika mji wa Kingston, Jamaica ambapo ilitoka mikono mitupu.

Ngumi yaweka historia Madola

Tanzania ilitakata katika michezo ya Madola mwaka 1970 baada ya kupata medali ya kwanza kupitia kwa bondia Titus Simba (marehemu) kuingia fainali katika uzani wa kati lakini alipigwa na John Conth wa England mjini Edinburgh, Scotland na kuambulia medali ya fedha.

“Ni rekodi nzuri kwenye ndondi, lakini tumeshindwa kuienzi na kushinda medali nyingi zaidi tangu 1998 Michael Yombayomba alipotwaa medali ya dhahabu, hakuna aliyefuata nyayo zake,” anasema bondia Hassani Matumla ambaye amewahi kushinda medali ya shaba ya michezo hiyo.

Wanamichezo wengine wa madola hawa hapa

Hadi sasa Tanzania ina medali 21 za madola ambazo ni dhahabu sita, fedha sita na shaba tisa.

Mbali na Simba, mwanariadha Filbert Bayi yeye amewahi kushinda dhahabu moja na fedha moja kwenye michezo hiyo kwa nyakati tofauti.

Wanariadha wengine walioshinda na aina ya medali kwenye mabano ni Claver Kamanya (shaba), Gidamis Shahanga (dhahabu mbili) Zacharia Barie (fedha), Juma Ikangaa (fedha) Zakayo Malekwa (shaba).

Wengine ni Simon Naali (shaba) Simon Mrashani (fedha), Andrea Suja (shaba), Francis Naali (dhahabu), John Yuda (shaba), Fabiano Joseph (shaba) na Samson Ramadhani aliyeshinda dhahabu. Kwa upande wa mabondia ni Michael Yombayomba ndiye pekee aliyeiletea nchi medali ya dhahabu ya madola.

Wengine ni Willy Isangura (shaba), Haji Ally (fedha), Bakari Mambeya (shaba) na Hassani Matumla (shaba).

Mwanzo wa Tanzania kupotea

Baada ya michezo ya 2006, Tanzania ilipoteza dira ya medali, kwenye michezo ya 2010 mjini New Delhi, India mwaka 2010 na 2014 Glasgow, Scotland, hakuna ilichoambulia.

“Kufanya kwetu vibaya naweza kusema kulichangizwa na kufutwa kwa michezo ya shule (Umitashumta na Umisseta), hata waliofanya vizuri kwenye michezo hiyo wengi wao ni matunda ya mashindano hayo.

“Kitendo cha michezo hiyo kufutwa kilitugharimu kwa asilimia kubwa,”anasema Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja.

Anasema ‘mzimu’ wa kufutwa michezo ya shule unaendelea kuitesa nchi hivi sasa katika ushindani wa kimataifa, lakini anasisitiza tangu imerejeshwa nchi imeanza kurejea upya kwenye ushindani wa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday, anasema mazingira ya wanamichezo miaka 10 iliyopita yalichangia kudorora katika sekta ya michezo nchini.

“Niliwahi kuwaita wanariadha na kuzungumza nao tatizo ni nini hadi tusifanye vizuri? walinieleza mambo mengi lakini kubwa walilosema hawana uzalendo kwa kuwa wanadhulumiwa stahiki zao.

“RT tuliwahakikishia kumaliza matatizo yote ndiyo sababu sasa riadha imerejea upya na niwahakikishie tu Watanzania, medali ya madola mwaka huu ipo,” anasema Gidabuday.

Katika michezo ya mwaka huu, Tanzania imepewa nafasi za wachezaji, viongozi, makocha 26 na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki (TOC), Filbert Bayi anasema idadi hiyo inaweza kupungua kutokana na wachezaji watakaofikia viwango.

“Utaratibu wa viwango ni mpya umeanza mwaka 2018, awali tulikuwa tunashiriki tu lakini sasa ili kushiriki lazima tufikie viwango, tumetoa nafasi kwa timu za ngumi, riadha, tenisi ya meza na kuogelea, bahati mbaya paralimpiki waliondoshwa kwa kutofikia viwango,” alisema Bayi.

Sikia kauli za wanamichezo wa madola

Wanariadha 10 waliofikia viwango, pia waogeleaji wanne, mabondia watano na wachezaji wa tenisi ya meza watatu wanatarajiwa kupeperusha bendera ya Tanzania.

Mwanariadha, Emmanuel Giniki ambaye anapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu anasema hana hofu ya ushindani na anaamini Tanzania itafanya vizuri.

“Tumejiandaa vizuri na tumekuwa na rekodi ya kumudu ushindani wa kimataifa, binafsi nakwenda kuleta medali msimu huu,”anasema Giniki.

Nahodha wa timu ya Taifa ya ngumi, Selemani Kidunda anasema juhudi binafsi za bondia ndizo zitakazoiletea nchi medali katika michezo ya Madola Australia.

“Tunajua ushindani ni mkubwa kwenye michezo hiyo, lakini mabondia tuko vizuri na huu ni mchezo wa mtu mmoja, hivyo inategemea siku hiyo umeamkaje tusubiri siku ifike,” anasema nguli huyo.

Muogeleaji wa timu ya Taifa, Celina Itatiro anasema wameanza kuboresha muda wao na wamejiandaa vyema kutwaa medali katika michezo hiyo.

Swali la kujiuliza je, wanamichezo wetu watarudi na medali kama walivyoahidi? tusubiri Aprili.

Monday, February 5, 2018

Jerome, kinda linalotembelea kivuli cha Cruyff

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Enzi za uhai wa Hendrik Johannes “Johan” Cruijff mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia (Ballon d’Or) mara tatu, amewahi kusema soka ni mchezo rahisi.

Maneno ya muasisi huyo wa mfumo wa ‘total football’ uliokuwa maarufu na timu ya Uholanzi ilitumia kwenye Kombe la Dunia mwaka, 1974.

Nguli huyo anafafanua kuwa ugumu mchezo wa soka ni matokeo ya mpira wa miguu kuwa rahisi tofauti na watu wanavyofikiri.

Maneno hayo yametawala akili ya mchezaji wa Kitanzania anayecheza soka ya kulipwa Kenya, Baraka Jerome kwenye timu ya Daraja la Kwanza Nakuru FC. Spoti Mikiki katika uvumbuzi na ufuatiliaji wa maendeleo ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje,tumefanikiwa kuzungumza na kiungo huyo mshambuliaji ambaye anategemea kwenda kufanya majaribio Ulaya.

“Maisha ya mpira ni magumu sana, kuna muda unaweza ukakata tamaa kama una roho nyepesi kwa sababu changamoto ni nyingi, nimeanza kuwaza kuhusu mpira nikiwa mdogo kwa kuanza kucheza mtaani.

“Kila jambo na wakati wake. Nilianza kwa kusuasua kucheza bila viatu na baadaye nikaanza kucheza kwa kutumia viatu kila hatua nilijipa kipimo kutaka kupiga hatua,”anasema Jerome.

Katika ukuaji wa soka nyota huyo wa Nakuru anasema alianza kuitumikia Zakhem iliyokuwa Daraja la Pili kabla kuitwa kwenye kikosi cha Copa Coca Cola.

“Nilicheza Temeke nakumbuka ilikuwa mwaka 2012, mashindano yalipomalizika viongozi wa African Lyon waliniona na kunichukua kwenye timu yao ya vijana.

“Maisha yangu ya kimpira hapo ndipo yalipoanza kuchukua sura nyingine, nilicheza African Lyon lakini kilifika kipindi kigumu cha ukata kwenye timu.

“Uzuri nilikuwa na uhusiano mzuri na kocha Aluko Simango ndiye aliyenifanyia mpango wa kuja Kenya kupata timu ya kucheza,” anasema mchezaji huyo wa Nakuru.

Jerome anadokeza uwezo wa soka haukujificha akiwa Nakuru alikutana na Asman Noor aliyevutiwa na kipaji chake kabla ya kuamua kuwa wakala wake.

“Sikuona kama ni tatizo kwa sababu niliona hiyo ni kama njia kwangu ya kuendelea kupiga hatua 2014 nilipata nafasi ya kwenda kufanya majaribio Serbia lakini mambo hayakwenda vizuri,” anaongeza Jerome.

Ingawa Jerome hakufanikiwa kucheza soka Serbia, anajiandaa tena kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Ulaya kwa mara nyingine.

Mchezaji huyo anasema wakala wake amemtaka kujiandaa kwa safari ya kwenda kufanya majaribio Oktoba kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.

“Kuna A,B na C za soka labla sikuwa nazo kipindi kile ni miaka minne imepita tangu nifanye majaribio mara ya mwisho, Mungu atanisaidia ili nifikie malengo yangu ya kucheza Ulaya,” amesema Jerome.

Hata hivyo, kiungo huyo anasema ana ndoto ya kuitumikia timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kaatika mashindano ya kimataifa.

“Kuhusu kuichezea Taifa Stars ni wajibu wangu kama itafika hatua nikihitajika, siwezi kugomea Taifa langu hata kidogo na moja ya vitu ninavyotamani ukiachilia mbali kucheza Ulaya ni kucheza pia Taifa Stars.

Anasema anavutiwa na nahodha Mbwana Samatta na Saimon Msuva kutokana na kazi nzuri wanayofanya ya kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Hakuna njia nyepesi kupata mafanikio katoka soka hilo ndilo alilomaliza nalo Jerome na kutufanya kurejea tena kwa alichowahi kusema Cruyff, kuwa mpira ni mwepesi lakini ugumu upo katika kuufanya mchezo uwe mwepesi.

Mfumo wa namna ya uchezaji inawezekana ndicho alichokuwa akikilenga, Crujff kwa Jerome ameutaja ugumu katika njia za utafutaji wa maisha ya soka.

Monday, February 5, 2018

Neymar mwenye picha ya Messi tusiyoifahamu

 

Ukifika Catalunya mji ilipo klabu ya Barcelona kuna binadamu mmoja maarufu kuliko wengi wa eneo hilo anaitwa Lionel Andres Messi.

Katika sura yake kuna upole umebebwa na historia yake kuwa alizaliwa akiwa na tatizo la kutokuwa na uwezo wa kukua hali iliyopelekea kupewa huduma maalumu ambayo ingechagiza ukuaji wake.

Uwezekaji ambao Barcelona walifanya wakitarajia kupata majibu au mavuno yenye ubora, lakini naamini hawakutegemea kuwa walikuwa wanalea huyu ‘jini’ anayezitesa timu anazokutana nazo.

Njaa yake inatibiwa na chakula ambacho ni mabao, pia pamoja na kuwa hakuzaliwa na miguu ya Ronaldinho Gaucho kwa maana ya kuwa na mbwembwe au ubunifu mwingi bado ameweza kukamilika katika uwezo wake na anaonekana kama hazuiliki.

Katika kinywa cha Wenger yaliwahi kutoka maneno ambayo yaliwakilisha fikra zake akiamini kuwa huyu hakuwa binadamu wa kawaida, huyu Messi alitengenezwa kucheza soka tu na siyo kazi nyingine duniani.

Wenger aliamini kuwa kuna tofauti ndogo kati ya mchezaji aliyekuwa kwenye “PS Game” na huyu ambaye viungo na mabeki wanakutana naye ndani ya uwanja. Hivyo ndivyo alivyozaliwa Messi, alibarikiwa na akaweza kutufanya tusijute kuona kipaji chake na kujifunza historia ya maisha yake kwa wale wanaopenda kukata tamaa.

Hata hivyo, kuna upande wa Messi ambao kwa kiasi kikubwa huwa tofauti na Cristiano Ronaldo linapokuja suala la vyombo vya habari na pia mashabiki.

Kutokana na maisha yao, Ronaldo huonekana kuwa mjivuni na mwenye kujisikia huku Messi akionekana kuwa kijana mstaarabu mpole na ambaye muda wote ungehisi anaonewa.

Kuna shutuma chache mtaani ambazo zinamhusisha Messi na kushindwa kwake kuendana na wachezaji wengine au kukorofishana na waamuzi na pia mashabiki kwa ujumla.

Kwa wapenzi wa soka huyu ni kama malaika ambaye mbawa zake kila mmoja hutaka kuziona zikipaa angani.

Lakini kuna watu wachache ambao hili sio jambo lililopo kichwani mwao. Binadamu wa kwanza anapatikana jijini Manchester kwa sasa kwenye klabu ya Manchester United, anaitwa Zlatan Ibrahimovic.

Kwenye moyo na akili ya Zlatan kuna jina moja ambalo huwa halivumiliki, Pep Guardiola. Zlatan anaishi katika ulimwengu wa giza alikojifungia na kuamini kuwa mtu pekee ambaye alihatarisha maisha yake ndani ya Barcelona alikuwa Guardiola kutokana na namna alivyomtaka acheze kwa kumsaidia Messi.

Kwa Ibrahimovic hili halikuwa tatizo kwake, lakini changamoto ilikuja wakati alipoambiwa kuwa anatakiwa atokee pembeni ili Messi acheze kwa uhuru zaidi kwenye eneo la ushambuliaji ikiwa ni moja kati ya nyakati chache ambazo “false 9” ilikuwa ni aina ya washambuliaji hatari.

Ibrahimovic anafahamu kuwa anaunafikia moyo wake kila siku, kutokana na udogo wa umri wa Messi pamoja na ubora aliokuwa nao, aliamini kuwa ile ilikuwa dharau kipindi.

Lakini, Guardiola angewezaje kuondoa furaha ya mchezaji ambaye alikuwa ameishika dunia, mchezaji ambaye alimpa kila kitu?

Ni wazi kuwa Guardiola aliamini Messi alianza kucheza kama winga na angeweza kuwatumia wote pamoja na Ibrahimovic, lakini Messi hakuwa tayari kukaa mbali na goli na nyota huyo wa Sweden alikuwa katika kipindi cha ubora wake ambao asingetaka kujifunza kitu kipya kwa maana ya uchezaji.

Lakini inawezekana kabisa Neymar akawa anatupa picha kamili ya namna gani Messi siye yule tunayeamini kuwa ndiye.

Hivi karibuni Real Madrid imehusika katika kutaka kuvunja rekodi ya usajili ili kumpata Neymar.

Ni wazi kuwa usajili wa Neymar kwenda Paris Saint Germain (PSG) ulimshitua kila mtu ambaye alikuwa muumini wa ‘MSN’ yaani Messi, Suarez na Neymar.

Hata hivyo, kulikuwa na jambo moja tu ambalo lilifanya muunganiko huu uvunjike, nalo ni Messi.

Neymar ni Ronaldo wa pili, anaamini ana mvuto na anaamini anatakiwa kupata biashara nyingi zinazotokana na kile anachofanya ndani ya uwanja.

Ndani ya akili ya Neymar anaamini kuwa kuna tofauti ndogo kati yake na hao wanaume wawili walioamua kufanya umiliki wa tuzo ya Ballon D’or kwa muongo mmoja uliopita.

Neymar anaamini ni bora zaidi akiwa na timu ya Taifa kuliko wote wawili na haoni inashindikana vipi kuwapa ushindani. Hizi ni tabia ambazo ni wazi pamoja na upole wa Messi, hajawahi kukubaliana nazo.

Hakuna mchezaji aliyewahi na atakayewahi kuwa mkubwa ndani ya Barcelona Messi akiwepo.

Katika timu ya Taifa, Messi alipata bahati mbaya kwani hakuwa na viungo nguli Xavi Hernandez, Andres Iniesta na hata Suarez ambao wapo tayari kumshika miguu na kumwambia kazi kwako fanya unavyoweza, sisi tunalainisha tu.

Huku Argentina kuanzia Carlos Tevez, Gonzalo Higuaini, Sergio Aguero, Diego Millito na pengine hata kina Dyabala wanaamini wao ni wanaume kwenye klabu wanayotokea na hawawezi kumsujudia Messi.

Neymar hana moyo wa Suarez ambaye ndoto zake alikuwa anakwenda kuzitimiza Barcelona akiwa amefikisha miaka 27 tayari.

Katika umri huo, Suarez alikuwa tayari kuwa nyuma kwa kila namna ili Messi awe Messi. Kwenye akili ya Neymar kuna roho tofauti, yeye anataka akiibeba Barcelona kwa kufanya maajabu dhidi ya PSG basi dunia isimame na kumwabudu.

Bahati mbaya ni kuwa dunia itasimama vipi wakati hata ndani ya klabu yako, haijawa suala kubwa kihivyo? Hii ilimkera kwa sababu mabao mawili ya Messi katika mchezo wa ligi unaofuata na usiokuwa na nguvu kubwa yangefunika kila kitu alichofanya wakati wake.

Barcelona inaamini Messi ni bora, Messi ana moyo unaomwambia kuwa yeye ni bora kupita wote na ndio maana wakati Iniesta akiwa anaomba mkataba amalizie maisha yake Catalunya, Messi alikuwa ameanza kulijaribu soko ili Barcelona watetemeke.

Naam namzungumzia Messi ambaye ametimiza miaka 30 akiwa bora na hakutaka kuambiwa kuhusu pensheni.

Kwao Brazil, Neymar anakimbiza mazimwi yaliyotangulia, ana rekodi bora ya ufungaji timu ya Taifa na anazungumzwa kama mchezaji bora duniani.

Neymar alipenda makombe lakini hakumpenda Messi na hakuvutiwa na ukweli kuwa alikuwa anatumika kama “greda” ili barabara ya wapinzani iwe nyepesi kwa Messi na Suarez kunufaika.

Neymar anaifahamu vyema sura ya Messi, anafahamu pamoja na upole wake haikuwa tayari kumkabidhi kijiti ili aanze kukimbiza mbio za Ballon D’Or.

Anafikisha umri wa miaka 26 mwezi Juni, huku Messi akiwa na miaka miwili au mitatu zaidi ya kuitaka tuzo hii. Neymar asingeweza kusubiri afikishe miaka 29 ili dunia impe heshima yake. Hajawahi kumpenda Messi na hatampenda kutokana na hili tu, ubinafsi wa Messi ambao wengi hatujawahi kuamini kama upo.

Neymar anaamini akiwafunika wote kombe la dunia, akachukua ligi ya Ufaransa na pia akifanya vyema Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuna wa kumzuia.

Baada ya msimu mmoja au miwili Ronaldo atakuwa tayari kumpisha pale Real Madrid, klabu ya ndoto yake.

Nakujuza tu, wakati Robinho anasajiliwa na Real Madrid, Neymar alikuwepo kwenye kufanya majaribio. Anaipenda hii timu na hampendi Messi kutokana na maisha aliyompa.

Achana na Ibrahimovic aliyeishia kumlaumu Pep Guardiola, Neymar anaifahamu picha halisi ya Messi ambayo wengi hatuitilii maanani.

Monday, February 5, 2018

Pombe inavyoathiri kiwango na utimamu wa wachezajiDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Kama ni mchezaji au mfanyaji wa mazoezi umewahi kujua kama unywaji pombe ni salama kwako kwa upande wa kiwango chako cha uchezaji na utimamu wa mwili wako?

Kama ulikuwa hujui, kiujumla unywaji pombe unaathiri kiwango cha mchezaji na utimamu wa mwili wake kwa njia mbili zifuatazo.

Njia ya kwanza ni kwasababu pombe huchochea figo kuruhusu maji kupotea kwa wingi kwa njia ya mkojo, hivyo unywaji wa pombe uliopitiliza unasababisha upungufu wa maji mwilini.

Kwa mfano mwanamichezo au mchezaji akanywa pombe kwa wingi na kisha akaingia katika zoezi au mechi, mchezaji huyu huwa katika hali mbaya zaidi kutokana na ukweli kuwa atapoteza maji mengi kwa njia ya jasho kwakuwa kadiri anavyocheza ndivyo joto la mwili hupanda na hivyo jasho hutoka kwa wingi.

Muunganiko wa kutokwa jasho na athari ya pombe ya kupoteza maji kwa njia ya mkojo huweza kuleta upungufu wa maji mkali kwa mchezaji.

Wakati wote mwanamichezo hutakiwa kuwa na kiasi cha maji ya kutosha mwilini ili kuwezesha mtawanyiko mzuri wa damu. Ikumbukwe kuwa damu ndiyo imebeba oksijeni na virutubisho muhimu kwa ajili ya misuli kukunjuka na kujikunja.

Hivyo basi upungufu wa maji mwilini huathiri utendaji wa misuli hivyo moja kwa moja huaathiri kiwango cha uchezaji na utimamu wa mwili kiujumla.

Hali ya upungufu wa maji mwilini huambatana na hali ya kubanwa misuli na kupata vijeraha vya misuli kirahisi. Vile vile kama kuna majeraha huchelewa kupona.

Njia ya pili ni kuwa pombe huingilia mfumo wa utengenezaji nishati ya mwili (glucose), ikumbukwe kuwa glucose ndiyo kama petroli ya mwili inayotumiwa na misuli ya mwili kufanya kazi yake.

Pale unapokunywa pombe na inapoingia tumboni na kuvunjwa vunjwa au kusagwa huwa ini linashindwa kutengeneza kiasi cha kutosha cha nishati (glucose).

Hali hii ndiyo inayosababisha kuwa sukari ya mwili au nishati (glucose) katika damu kuwa chini. Mazoezi yoyote huitaji kiasi cha kutosha cha sukari/nishati ili kukupa nguvu.

Hivyo kwa mnywaji wa pombe ini lake hushindwa kutengeneza sukari/nishati hivyo mwili kukosa nguvu na hii huathiri kiwango cha mchezaji kwani atashindwa kucheza kwa nguvu.

Njia hizi mbili ndizo zina matokeo kama humsababishia mwanamichezo kukosa nguvu, misuli kuumwa na kuwa dhaifu, kuwa mchovu, kushindwa kuwa makini uwanjani, kukosa utulivu, kichwa kuuma, kubadilika tabia ikiwamo ukali au ukorofu na kuongezeka uzito kiholela.

Pia pombe inasababisha protini tunayoipata kwa kula vyakula kutonyonywa katika mfumo wa chakula. Kukosekana kwa kirutubisho hiki kwa mwanamichezo misuli yake haita jengeka na kuimarika.

Vile vile protini ndiyo inayochangia misuli kujikunja na kukunjuka, upungufu wa protini husababisha misuli kutofanya kazi yake kwa ufanisi hivyo mchezaji hukosa kasi anapokuwa uwanjani.

Pombe inachangia kushusha kiwango cha homoni ya kiume ijulikanayo kama Testosterone ambayo ndiyo inatuwezesha misuli kukua na kujikarabati, kwa mwanamichezo misuli imara ndio kila kitu.

Nihitimishe kwa kushauri wanamichezo kutokunywa pombe huku wanashiriki michezo, wakishindwa kuacha basi wanywe kwa kiasi. Lengo ni kulinda kiwango chao kisiporomoke na utimamu wa miili yao.

Monday, February 5, 2018

Vyama vya soka, klabu zitafute viongozi wenye weledi wa utawalaAllan Goshashi

Allan Goshashi 

Kufanikiwa kwa mtu ni kutegemea na malengo yake. Unaweza kufanikiwa kupata gari moja ukaona umefanikiwa, unaweza kujenga nyumba ukaona umefanikiwa, unaweza kujilimbikizia mali ambayo hata vitukuu hawatamaliza ukaona bado hujafanikiwa. Kufanikiwa kwa mtu ni malengo yake.

Kufanikiwa kwa mtu siyo fedha wala elimu tu. Kuna watu wana fedha nyingi na elimu kubwa lakini bado hawaoni kama wamefanikiwa. Wapo ambao kupata mtoto au mume au mke au cheo au pato zuri au elimu ya ngazi fulani au umaarufu wa kisiasa kwake ni mafanikio.

Kila binadamu ameumbwa na kiu ya kufanikiwa katika kila kitu anachofanya. Mafanikio ndio kilele cha mlima mkubwa wa maisha ambao umejengwa kwa misingi na ngazi za mihangaiko na mitihani ambayo unapaswa kuivuka ili upumzike kwenye kilele hicho.

Ni kwa muda mrefu sasa, Tanzania imekuwa ikitafuta mafanikio katika mchezo wa soka kimataifa, lakini hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana huku soka la Tanzania likizi kuporomoka.

Zipo sababu nyingi zinazoifanya Tanzania ishindwe kupata mafanikio katika mchezo wa soka kimataifa. Sababu kubwa ni kudharau msingi wa mchezo wa soka, yaani tumekuwa tukipandisha kuta za nyumba bila msingi!. Nyumba hii haiwezi kuwa imara kamwe, haiwezi kuleta mafanikio yoyote.

Hivyo ndivyo lilivyo soka la Tanzania, halijali msingi ambao ni soka la vijana, pamoja na soka kuchezwa katika ngazi ya grassroots.

Wachezaji wengi wa Tanzania wanaocheza Ligi Kuu hawajafundishwa mambo mengi ya msingi ya soka katika ngazi za chini, pia mashindano ya vijana nchini Tanzania yanafanyika ili kuhakikisha linatimizwa lengo la mashindano kufanyika, lakini siyo kwa lengo la kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mfumo thabiti ili kuibua vipaji ambavyo vitaendelezwa na kupewa mafunzo sahihi.

Katika hali ya kushangaza, shirikisho letu la soka nchini limeshindwa kabisa kuhakikisha tunakuwa na mpango utakaoleta mfumo thabiti kwa klabu kuwa na timu mbalimbali za vijana (ambazo ndiyo msingi wa soka letu) zitakazotusaidia kuwa na timu za vijana za Taifa imara.

Hebu tazama, mashindano ya Uhai yanayoshirikisha timu za vijana chini ya miaka 23 wa klabu za Ligi Kuu hayafanyiki siku hizi, pia zile mechi za timu za vijana zilizokuwa zinafanyika kabla ya kuanza kwa mechi za Ligi Kuu hazifanyiki!

Tukumbuke kwamba timu za Afrika Magharibi na Kaskazini zinafanya vizuri na kutusumbua katika soka la Afrika kwa sababu nchi nyingi za maeneo hayo zina mfumo wa kuandaa timu za vijana ambazo zinafika katika mashindano ya kimataifa hali inayowasaidia baadaye kupata wachezaji bora wa timu zao za taifa za wakubwa.

Ni lazima tuwe na timu nyingi za vijana mitaani na shirikisho la soka lizifuatilie na kuzijengea mfumo bora kabisa utakaosaidia vijana kuwa na walimu, viwanja,vifaa na mashindano mengi. Vijana wanatakiwa wacheze mechi nyingi za ushindani zisizopungua 22 mpaka 30 kwa mwaka katika mashindano yao na wanahitaji kufanya mazoezi yenye kiwango cha juu kila wiki.

Kama nilivyosema awali, zipo sababu nyingi zinazozuia Tanzania kupata mafanikio, ila hii ya kushindwa kuweka mfumo imara wa kuendeleza soka la vijana nchini ndiyo sababu kubwa zaidi nah ii inatokana na kuwa na viongozi katika mchezo wa soka ambao hawana maarifa ya kutosha katika utawala wa mchezo wa soka hali inayochangia kudumuza sekta hiyo.

Monday, February 5, 2018

Hatutarajii kuona ‘majamvi ya wageni’ Ligi KuuIbrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

Ligi Kuu ya soka Tanzania ndiyo ligi kubwa Tanzania kuliko ligi nyingine. Kila timu zinawania kucheza ligi hiyo, na ndiyo maana kuna madaraja ya pili, tatu na Daraja la Kwanza wote akili yao ni Ligi Kuu.

Kwa mtazamo wa haraka haraka, hata wachezaji wenyewe hamu yao kubwa ni kucheza Ligi Kuu. Kuna viwango vya uchezaji kwa hatua hiyo, lakini vilevile uwezo binafsi wa mchezaji unaweza kumtoa chini na kucheza Ligi Kuu.

Kuna baadhi ya timu; Coastal Union ya Tanga, JKT Tanzania, KMC ya Dar es Salaam, Ruvu JKT ni kati ya timu zilizojihakikishia kucheza ligi hiyo msimu ujao, baada ya kufanya vema katika mechi zao.

Timu sita zinasubiri kupanda baada ya TFF kutangaza kuwa ligi msimu ujao itakuwa na timu 20 badala ya 16 zilizozoeleka.

Sitaki kuzungumzia mlolongo mzima, kwanza nawapongeza wote waliofanya vizuri, lakini hapa nina mawili kwa hawa wanaokuja Ligi Kuu.

Kwanza; tuone ushindani ulioko huku Daraja la Kwanza ukihamia katika Ligi Kuu. Hatutarajii kuona timu zinakuwa jamvi la wageni au taulo la hotelini kwamba kila mmoja anajifutia.

Huwa inanipa tabu kidogo, kwamba huku Daraja la Kwanza timu inakuwa ngumu, haifungiki kirahisi lakini wakija Ligi Kuu ndiyo vibonde.

Sasa, sijui uwezo mdogo au wachezaji wanabadilishwa wote na kukosa muunganiko. Inashangaza kidogo.

Mfano mzuri, Coastal Union au JKT Tanzania ukiangalia matokeo yao, utaona kweli wachezaji wameiva, wanatumia kila aina ya uwezo kufanya vizuri na ndiyo maana wamepanda, sasa njoo kwenye Ligi Kuu uone kazi.

Kuwa jamvi la wageni kwa rundo la timu ndiko kulikoturudisha kuwa na timu 16 badala ya 20. Kumbuka Ligi Kuu ya Safari Lager ilikuwa na timu 20.

Ubovu au udhaifu wa timu, timu kushindwa kusafiri na mwisho wa siku kugawa pointi za chee kulipoozesha ligi, sasa wanaoikuja huku wanatakiwa kujipanga hasa.

Hatutarajii kuona mechi ngumu ya Simba na JKT Ruvu au Yanga na KMC lakini ikija KMC na Ndanda kwa mfano, wanawafunga kirahisi.

Hii hadi unajiuliza, hivi wakicheza hivi siku zote, chukulia Yanga na Mbao kwa mfano, Mbao ilishinda si ligi ingekuwa na ushindani kwa kiwango kile. Hatutaki kuona KMC na Yanga inakuwa mechi ya kufa mtu halafu KMC na Mbeya City hawa KMC wanapigwa kirahiisi, haipendezi hata kidogo.

Kingine ni miiko ya uwanjani. Kuna timu zilikuwa zinajifanyia inavyotaka huku Ligi Daraja la Kwanza na ndiyo maana kocha Fred Felix aliwahi kusema Ligi Kuu ni nyepesi kuliko Daraja la Kwanza.

Huku kuna nidhamu ya hali ya juu. Kama kuna timu zimezoea ama zimepanda kwa mbeleko, huku sasa ndiko kwenye kazi.

Makandokando ya Daraja la Kwanza yanawekwa kando na kucheza mechi za kusaka mwakilisha wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika.

Hatutarajii waamuzi kukunjwa, mashabiki kupigwa na vingine ambavyo kimsingi vinaweza kuipa Ligi Kuu sura nyingine. Nidhamu ya huku hailingani na Daraja la Kwanza, labda kwa waamuzi wasiosimamia Sheria 17 za soka.

Ninawapongeza waliopanda, lakini wajue kuna mengine zaidi ya hayo, lakini kikubwa hatutarajii kuona timu zinakuwa jamvi la wageni.

Monday, February 5, 2018

Pamoja na changamoto lukuki, mchezo wa kuogelea unachanja mbuga nchini

 

By Majuto Omary, Mwananchi

Mashindano ya kuogelea kwa waogeleaji chipukizi wenyeumri kati ya miaka saba na 14 yalimalizika wiki iliyopita kwenye bwawa la kuogelea lan Shule ya Haven of Peace iliyopo njia panda ya Kunduchi, Mbuyuni.

Mashindano haya yalishirikisha jumla ya waogeleaji 182 kutoka vilabu sita, ambavyo ni Wahoo kutoka Zanzibar, Shule ya Kimataifa ya Mwanza (MIS) na vine vya Tanzania Bara, Taliss, Bluefins, Champion Rise na wenyeji, Dar Swim Club (DSC).

Waogealeaji mbali mbali chipukizi walionyesha uwezo mkubwa katika mashindano hayo katika umbali tofauti wa mita 50, 100 na 200 katika staili tano ambazo ni butterfly, freestyle, Breaststroke, backstroke na Individual Medley (IM).

Waogeleaji hao pia walionyesha uwezo mkubwa katika kipengele cha kuogelea kwa kupokeza maarufu kwa jina la ‘relay’ kwa wavulana, wasichana na vile vike kwa waogealeaji mchanganyiko wa wanaume na wasichana.

Pamoja na waogeleaji wengi kuwa chipukizi, lakini waliweza kuvunja rekodi mbalimbali za mashindano hayo na kuto ishara ya maendeleo pamoja na changamoto mbalimbali ikiwa pamoja na ukosefu wa bwawa linalokidhi viwango vya kimataifa la mita 50 lenye vifaa mbalimbali vya kisasa.

WAOGELEAJI WALIOVUNJA REKODI

Jumla ya waogeleaji 25 waliweza kuvunja rekodi mbalimbali zilizowekwa katika mashindano yaliyopita ya chipukizi.

Kati ya hao, waogeleaji 15 ni raia wa Tanzania na 10 wanatoka mataifa mbalimbali ambao wanaishi nchini na kujishughulisha na mchezo huo kupitia klabu tofauti.

Waogeaji wa Watanzania kutoka klabu ya Bluefins ambao walivunja rekodi ni Lina Goyayi mwenye umri wa miaka nane (8) ambaye alivunja rekodi moja, Aliyana Kachra (miaka 9, rekodi moja) Aminaz Kachra (8, rekodi 4), Ralph Sereki (9, rekodi 3) ma William Sereki (7) ambaye alivunja rekodi tatu.

Katika orodha hiyo ya Watanzania ni Romeo Mihaly Asubisye (10) kutoka klabu ya Champion Rise ambaye alivunja rekodi saba ambapo waogealeaji kutoka klabu ya DSC ni Celina Itatiro (14) ambaye amevunja rekodi saba, Naaliyah Kweka (8, rekodi moja), Linnet Laiser (10, rekodi sita), Kalya Temba (14, rekodi 2) na Maia Tumiotto (13) aliyevunja rekodi sita.

Watanzania wengine waliovunja rekodi ni Khairaan Chunara (7) kutoka klabu Taliss ambaye amevunja rekodi mbili, Natalia Ladha (10, rekodi 7), Aravind Raghavendran (12, rekodi moja) na Rania Karume wa Wahoo aliyevunja rekodi tano.

Waogeleaji raia wa kigeni waliovunja rekodi ni Sebastian Carpintero (8, rekodi saba), Lisa DI Stefano (rekodi saba), Tele Sitoyo (10, rekodi moja). Waogeleaji wote hao wanatokea klabu ya DSC.

Pia wapo Zoey Detlefs (8) wa klabu ya Taliss alyevunja rekodi mbili, Kayla Gouws (12) aliyeibuka wa kwanza kwa kuvunja rekodi nyingi za mashindano hayp baada ya kuvunja rekodi tisa.

Pia yupo Lara Gouws (9) aliyevunja rekodi saba, Sydney Hardeman (10, rekodi tano), Aaron Hu (8, rekodi tano), Lucy Kiu (8, rekodi tatu) na Thea Muller (12, rekodi tatu).

CHANGAMOTO

Kocha maarufu wa mchezo wa kuogelea nchini, Alex Mwaipasi alisema kuwa kuongezeka kwa Watanzania wanaovunja rekodi katika mashindano hayo ni ishara tosha kuwa Tanzania inapata maendeleo makubwa katika mchezo huo.

Mwaipasi alisema kuwa awali hakukuwa na idadi kubwa ya waogeleaji wanaovunja rekodi huku raia wa kigeni wakitawala, lakini chipukizi wameonyesha uwezo mkubwa na kuvuna kile walichokipanda.

Muasisi na kocha wa klabu ya Bluefins, Rahim Alidina aliwapongeza waogeleaji wote waliofanya vizuri huku akiwapa moyo wale walioteleza kuwa bado wananafasi ya kufanya vyema katuja mashindano yajayo na kwa kuongeza bidii.

Alidina alisema kuwa waogeaji wa Tanzania wameonyesha maendeleo makubwa na kinachhotakiwa ni kuacha kubweteka ili kuendeleza mchezo huu na kutoa waogeleaji bora wa timu ya Taifa.

Kocha wa klabu ya DSC, Michael Livingstone alisema kuwa makocha wameonyesha kuwa kazi inafanyika na kinachotakiwa sasa ni kupata sapoti ili kuondoa changamoto mbalimbali.

Livingstone alisema kuwa Tanzania ina waogeleaji wenye vipaji vikubwa, lakini wanashindwa kujishughulisha na mchezo huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwa pamoja na bei kubwa ya vifaa.

“Tumeimba sana wimbo wa hakuna bwawa la kisasa la kuogelea kama ilivyo uwanja wa mpira wa Taifa, Uhuru na ule wa JKM Park, matokeo yake baadhi ya wazazi wenye uwezo ndiyo wanajishughulisha na mchezo, hao peke yao hawatoshi, tunahitaji bwawa la jumuiya kwa ajili ya kufundishia mchezo huu,”

“Wawekezaji kutoka Dubai walikuja hapa na kuomba kujenga bwawa la kisasa, ni zaidi ya mwaka sasa hakuna majibu, maeneo waliyopendekeza yamekataliwa, je unadhani watakuja hapa tena, naamini fursa hiyo watapewa nchi nyingine,” anasema Livingstone.

Katibu Mkuu wa DSC, Inviolata Itatiro alisema kuwa kuna waogeleaji wengi bora nchini, lakini wanakumbana na changamoto mbalimbali na wengine kuamua kuachana na mchezo, hivyo ametoa wito kwa wadau kusaidia.

Monday, February 5, 2018

Peter, chipukizi Azam aliyepiga ‘hat-trick’ ya ukweli

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Chipukizi wa Azam,Paul Peter (19) ameanza kuonekana atakuwa moto wa kuotea mbali baada ya kufunga, mabao matatu ‘hat-trick’ kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Shupavu.

Peter ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Mbaraka Yusuph kipindi cha pili katika mchezo wa raundi ya tatu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro alifunga mabao hayo dakika ya dakika ya 56, 77 na 87 huku Azam ikishinda kwa mabao 5-0.

“Hii ilikuwa ni hat-trick yangu ya kwanza katika mashindano ambayo yanatambuliwa na TFF, sikustaajabu hata kidogo na badala yake nilichukulia kawaida baada ya kufunga mabao yale kwa sababu ni kazi yangu kufunga.

“Nahitaji kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Azam, kocha amekuwa na imani na vijana na ndiyo maana amekuwa akitoa nafasi ya kuonyesha uwezo wetu,” amesema Peter.

Pamoja na Peter kuzungumzia hat-trick yake kwenye mazungumzo maalumu na Spoti Mikiki hakusita kuelezea changamoto, ndoto yake kwenye soka na nyota anayemkubali Azam.

Changamoto

Peter amedai amekuwa akizichukulia changamoto mbalimbali ambazo amekuwa akikutana nazo kama sehemu ya mafanikio kwa kuamini hakuna mafanikio bila hadithi ya maumivu.

“Huwa silalamiki kwa changamoto ambazo huwa nakutana nazo, nimekuwa nikimuomba sana Mungu anisaidie na muda mwingine nawashirikisha watu wangu wa karibu kwa ushauri,” amesema chipukizi huyo.

Ndoto

Akili ya Peter inawaza kucheza Ulaya, amedai hawezi kuzembea kwa kutizama maslahi zaidi kama ikitokea nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Nyota wake

Peter amemtaja chipukizi mwenzake, Yahya Zayd anamvutia kwenye kikosi cha Azam ambacho kipo chini ya kocha mkuu mwenye uraia wa Romania, Aristica Cioaba.

“Nampenda kwa sababu anaweza mpira, ana vitu vya mpira ambavyo mchezaji wa kiwango cha juu anatakiwa kuwa navyo,” amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Mugabe FC.

Monday, January 15, 2018

Mkenya apiga tatu La Liga

 

        Mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Michael Olunga amekuwa Mkenya wa kwanza kufunga mabao matatu kwenye mechi moja ya Ligi Kuu ya Hispania alipoiongoza timu yake ya Girona kuichakaza La Palmas kwa mabao 6-0.

Wakati Mkenya huyo akiweka historia, mabingwa wa Hispania wameendelea kuzama baada ya kufungwa bao 1-0 na Villareal, bao lililofungwa katika dakika ya nane na kuwafanya vigogo hao kuachwa kwa tofauti ya poiunti 19 na mahasimu wao wakubwa, Barcelona.

Olunga alifunga mabao hayo ndani ya dakika 22 katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Montilivi.

Mshambuliaji huyo ambaye anaichezea Girona kwa mkopo akitokea klabu ya Guizhou Zhicheng ya China, alifunga mabao hayo katika dakika za 57, 70 na 79 na kuw apia mchezaji wa kwanza wa Girona kufunga mabao matatu katika mechi moja ya Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga.

Ushindi huo pia ni mkubwa kwa Girona kwenye La Liga, ikiwa katika msimu wake wa kwanza katika daraja hilo na ushindi mkubwa iliowahi kuupata katika mashindano yote ndani ya miaka minne.

Bao lililofungwa kwa njia ya penati na Cristhian Stuani katikati ya kipindi cha kwanza ndio lilikuwa bao pekee katika kipindi hicho, lakini Girona ilicharuka katika kipindi cha pili na kufunga mabao hayo matano yanayoifanya La Palmas kupoteza mechi ya 14 kati ya 19 za ligi.

Mabao mengine yalifungwa na Borja Garcia na Cristian Portu.

Kilio kingine kilikuwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu ambako wageni, Villarreal walimuongezea presha kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane baada ya kushinda kwa bao 1-0.

Real ilifuzu kucheza robo fainali ya Kombe la Mfalme katikati ya wiki na itakutana na Leganes, lakini iliingia uwanjani juzi ikiwa nyuma ya Barcelona kwa tofauti ya pointi 16.

Na pengo hilom liliendelea kuwa kubwa baada ya Pablo Fornals kumalizia shambulizi la kushtukiza katika dakika ya 87 lililoanzishwa na Yellow Submarine.

Katika mechi nyingine, Atletico Madrid italazimika kumshukuru kipa Jan Oblak baada ya kuifikia Barcelona kwa pointi kutokana na ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Eibar.

Bao pekee la wageni lilifungwa na Antoine Griezman katika dakika ya 27.

Katika mechi zilizochezwa usiku Jumamosi, Valencia ilishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Deportivo La Coruna na sasa inaizidi Real Madrid kwa tofauti ya pointi nane.     

Monday, January 15, 2018

Kwa hili, Yanga ni kama wana ‘aleji’ na penalti

 

By Thomas Ng’itu Eliya Solomon

Yanga imetolewa katika hatua ya nusu fainali katika Kombe la Mapinduzi kwa mikwaju ya Penalti 5-4 dhidi ya watoza Ushuru wa Uganda URA, baada ya mchezo huo kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90.

Hii ni mara ya pili kwa Yanga kutolewa na URA katika hatua hii kama ilivyokuwa mwaka 2016, ilifungwa penati 4-3, huku Malimi Busungu na Geofrey Mwashiuya wakikosa penalti zao.

Spoti Mikiki limeangazia baadhi ya mechi zilizoihusu Yanga na ilipoteza kwa wachezaji wake kukosa penalti.

Klabu Bingwa Cecafa 1992

Katika fainali hii Simba iliifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-4 (ushindi wa jumla wa 6-5) baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwa muda wa dakika 120, mabao ambayo hata hivyo yalipatikana katika kipindi cha dakika 90 kwenye Uwanja huu wa Amaan, Zanzibar.

Mlinzi wa kulia wa Yanga, David Mwakalebela, ndiye aliyeikosesha timu yake penalti baada ya kupaisha hivyo Simba ikatwaa ubingwa.

Hiyo ilikuwa ni penalti ya nane ambapo Salum Kabunda ‘Ninja’, Said Mwamba ‘Kizota’ na Abubakar Salum ‘Sure Boy’ nao pia walikosa kwa Yanga, Kwa upande wa Simba, waliokosa ni Twaha Hamidu ‘Noriega’, Kassongo Athumani Mgaya na Damian Morisho Kimti.

Wafungaji wa penalti za Simba walikuwa George Masatu, Hamza Maneno, Fikiri Magosso, Issa Kihange na George Lucas ‘Gaza’ na walioifungia Yanga ni Said Mwaibambe ‘Zimbwe’, Issa Athumani Mgaya, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Hamisi Gaga ‘Gagarino’.

Kombe la Tusker, 2001

Mpambano ulikuwa wa fainali kati ya Yanga na Simba, ulimalizika dakika 90 suluhu.

Ilipokuja mikwaju ya penalti, Simba ilishinda kwa penalti 5-4, mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Nusu fainali ya Kombe la Tusker, Agosti 15, 2006 Simba ilitoka sare ya 1-1 dakika 90 kwa mabao ya Emanuel Gabriel na Credo Mwaipopo lakini katika mikwaju ya penalti, Simba ilishinda 7-6.

Nane Bora Ligi Kuu, 2007

Ilikuwa Julai 8, 2007, Yanga ilitoka sare ya 1-1 na Simba dakika 120 kwa mabao ya Moses Odhiambo (penalti dakika 2) na Said Maulid dakika 55. (Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4).

Ligi ya Mabingwa Afrika 2014

Yanga iliifunga Al Ahly bao 1-0 na kufanya mashabiki kuwa na imani ya kusonga mbele na mechi ya marudiano, Ahly ilishinda bao 1-0 na kuamuliwa mikwaju ya penalti.

Didier Kavumbagu, Nadir Haroub, Emmanuel Okwi, walipata penati zao lakini Oscar Joshua, Said Bahanuzi na Mbuyu Twite walipoteza penalti zao.

Yanga vs Azam (2015)

Mechi hii ilikuwa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) mwaka 2015. Yanga ilikutana na Azam katika hatua hiyo na mpira ukapigwa mpira mwingi. Hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyokuwa imeweza kupata bao.

Ilipokuja mikwajuya penalti, Yanga ikalala 5-3.

Ngao ya Jamii

Uzinduzi wa Ligi Kuu msimu wa 2015/16 Azam ikiwa na nyota wake Shomary Kapombe na John Bocco waliifunga Yanga kwa mikwaju ya penati 4-3, huku Hassan Kessy, Haruna Niyonzima wakikosa. Deogratius Munish ‘Dida’ pekee ndiye aliyefunga penati. Walioifungia Azam walikuwa Himid Mao, Kapombe na Kipre Balou.

Uzinduzi wa Ligi Kuu 2017/18, ulizikutanisha Simba na Yanga, mechi ya Ngao ya Jamii. Hadi dakika 120 matokeo yalikuwa suluhu.

Kwenye mikwaju ya penalti sasa, Yanga walilala kwa penalti 5-4. Kelvin Yondani na Juma Mahadhi walikosa wakati Thaban Kamusoko, Papy Tshishimbi, Ibrahim Ajib na Donald Ngoma walifunga.

Penalti za Simba zilifungwa na Method Mwanjali, Emmanuel Okwi, Haroun Niyonzima, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim ambaye alipiga penalti ya sita iliyokuwa ya ushindi. Baada penalti ya tano Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kukosa.

SportPesa 2017

Licha ya kufuzu nusu fainali baada kuifunga Tusker kwa mikwaju ya penalti 5-4, klabu hii pia ilikutana na changamoto baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-2 na kutolewa nje katika mashindano hayo na AFC Leopards ya Kenya.

Wachezaji wa Yanga Said Mussa na Said Makapu ndio walipeleka msiba Jangwani, baada ya kukosa penati lakini hata hivyo kipa Deogratius Munish ‘Dida’ , alipangua penati moja ya AFC Leopards lakini haikuweza kuwavusha.

Wachezaji wa Yanga waliofunga ni Nadir Haroub na Obrey Chirwa.

Kombe la Mapinduzi 2017

Simba na Yanga zilikutana kwenye nusu fainali mwaka jana.

Mechi hiyo ilimalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90 hivyo mikwaju ya penalti ikawa ndiyo njia pekee ya kumpata mshindi.

Simba ilipeleka kilio Jangwani baada ya kuibuka kidedea kwa kufunga penalti 4-2.

Mwaka huu, Yanga kama ilivyo ada, ilipoteza mechi yale kwa kufungwa penalti 5-4 na URA katika nusu fainali na kuiacha timu hiyo kuingia fainali.     

Monday, January 15, 2018

Siku 14 za Malimi ndani ya kijiji cha Manchester City

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Inawezekana ile ndoto ya kuwashuhudia wachezaji wa Kitanzania wakicheza, Ligi Kuu ya England ‘EPL’ ikatimia kwa miaka ya baadaye kutokana na uthubutu unaoendelea kwa wachezaji wa Tanzania.

Tatizo liko kwenye kanuni za England sasa. Hizi zinakinzana na hivi viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa, (Fifa).

Ilivyo, ili mchezaji wa kigeni apate kibali cha kucheza ni lazima nchi yake iwe nafasi ya kwanza hadi 70 kwenye ubora wa viwango vya Fifa pamoja na kulitumikia taifa lake kwa miaka miwili au mmoja kutokana na umri wake kwa kiwango fulani.

Nafasi ya upendeleo hutolewa kwa wachezaji ambao wameanzia kwenye ngazi ya chini kabisa ya soka nchini humo kwa maana ya akademi na pia wengine huchukuliwa kwa kupitia kwenye ligi za madaraja ya kati yenye ushindani,Ulaya au mchezaji awe na kitu cha ziada.

Wakati Mbwana Samatta wa KRC Genk akiongoza mapambano ya kupigania nafasi ya kucheza kwenye ligi za madaraja ya juu kama England kwa kupitia daraja la kati nchini Ubelgiji, kuna kijana wa Kitanzania ambaye hivi karibuni ametoka kufanya majaribio katika jijini Manchester akiwa na ndoto za kupaa katika Ligi Kuu England.

Spoti Mikiki imefanya mahojiano ya kina na kijana Malimi ambaye alikwenda kufanya majaribio ya siku 14 ya kujiunga na Manchester City ya England pamoja na baba yake ambaye ni Majaliwa Mbasa ambaye alisafiri naye kwa uangalizi kama mzazi.

Malimi (12) ambaye ni hazina ya baadaye kama kutakuwa na benki ya wachezaji kama hawa ndani ya TFF, anacheza nafasi ya ushambuliaji wa pembeni ‘winga’ pamoja na kipa, Daudi Damasi (12) walipata nafasi hizo kutokana na ushirikiano wa Tecno Mobile na asasi ya michezo ya Magnet.

“Matumaini yangu ni kupata nafasi ya kujiunga na Manchester City. Naupenda sana mpira na natamani siku moja kuwa mchezaji mkubwa ambaye nitalisaidia taifa langu la Tanzania.

Akizungumzia majaribio, anasema yalikwenda vizuri na sikuona tatizo lolote upande wangu, lugha iliyokua inatumika ni Kingereza ambacho sio kigeni kwangu, tulikutana wachezaji wa mataifa tofauti,” anasema Malimi ambaye alizaliwa 2005.

Hata hivyo kwenye majaribio hayo walipata nafasi ya kukaa pamoja na nyota kadhaa wa Manchester City ambao waliwaelekeza ni kwa namna gani wanaweza kuwa wachezaji wa kubwa.

“Nimefurahi wakati tunafundishwa darasani walikuja wachezaji wa Man City wakaanza kutuelekeza, alikuwepo Sergio Aguero, David Silva na Kevin De Bruyne, walitusisitiza kwenye kujituma na kufanya mazoezi kwa juhudi, hakuna kinachoweza kushindikana.

“Maneno yao nimeyashika na nitajitahidi kuyafanyia kazi kila wakati. Wachezaji hao nilikuwa nimewazoea kuwatumia kwenye gemu langu la mpira nyumbani nimefurahi kushikana nao mkono na wametufundisha mengi ya uwanjani,” anasema Malimi.

Anasema: “Katika siku 14, tulikuwa wakifundishwa darasani kisha tunakwenda kufanyia kazi uwanjani, tekniki na taktiki za mpira zote tumefundishwa na uzuri sikuwa na kasoro na wengi tulikuwa tuko vizuri.”

Katika mahojiano yetu, baba wa Malimi naye ameonekana kupigania mafanikio ya mwanae kwa kusema alianza kumjengea misingi ya mpira mwanae angali akiwa mdogo pamoja na kumkazania masomo hivyo amefuata nyayo zake.

Fundi wa kupiga mbizi

“Kipaji chake cha mwanzo kabisa kilikuwa ni kuogelea na wakati anasoma aliwahi kushinda tuzo tano mfululizo ila tatizo la aleji ya maji lilinifanya kumkataza kuendelea na mchezo huo, niliangaika sana na ilibaki kidogo niende naye nje kwa matibabu,” anasema Majaliwa.

Anaendelea; “Kupata nafasi ya kwenda kufanya majaribio nje hakika siwezi kusita kuwashukuru, Tippo Athumani, Juma Ndambile, Salehe Ali pamoja na Waziri wa habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.”

Hata hivyo, Majaliwa ambaye ni mnazi wa Simba, anasema ni wajibu wake kupigania ndoto za kijana wake hivyo wakati akiwa England alifanikiwa kuonana na mkuu wa kitengo cha usalama jijini humo ambaye ni Mtanzania aliyefurahishwa na ujio wa kijana wake.

“Tuliongea mengi na ametusaidia mawasiliano na timu za madaraja ya chini kama Coventry City na Milton Keynes Dons F.C, tunavuta subira ya majibu ila mambo yasipoenda sawa basi kijana wangu anaweza kwenda kujiunga na moja ya timu hizo, aanzie huku chini,” anasema Majaliwa.

Kama Malimi akifanikiwa kufuzu majaribio hayo na kujiunga na Manchester City Academy atakuwa Mtanzania wa pili kupitia kwenye akademi ya timu kubwa, awali ni Adam Nditi aliyekuwa Chelsea kabla ya kutemwa.

Hatua hiyo ya Malimi inaendelea kutoa mwanga kwa wachezaji wa Kitanzania kuwa ipo siku ile ndoto ya kuwashudia nyota wetu wa Kitanzania kucheza Epl itatimia kama ilivyo kwa Wakenya wanavyojivunia, Victor Wanyama wa Tottenham katika EPL.     

Monday, January 15, 2018

Kwaheri Coutinho; Ufalme hauna tija tena.

 

By Nicasius Agwanda

        Kabla ya kupewa jina la utani la Ronaldinho kutokana na ubunifu akiwa mwenye umbo ndogo na kijana mdogo zaidi kwenye klabu anavyochezea, alikuwa akitambulika kwa jina lake la asili ambalo ni Ronaldo de Assis Moreira, alilopewa na wazazi wake.

Kipindi chote hiki hakuna aliyewaza kuwa angekuwa mchezaji bora siku moja. Ndani ya kichwa cha Ronaldinho kulikuwa kuna fikra tofauti kabisa, wakati akiwa anamtizama kaka yake akicheza na ambaye alikuwa akitizamwa kama jicho la familia, yeye Ronaldinho alikuwa amechagua “role model” wake na ambaye angependa kuwa kama yeye siku moja.

Ronaldinho alikuwa akisikia habari za Roberto Rivellino, moja ya viungo bora kuwahi kucheza soka hasa katika kizazi cha Brazil kilichotwaa kombe la dunia mwaka 1970.

Huyu ndiye hasa aliyeleta uhai wa staili maarufu ya Flip Flap ama Elastico ambayo ilikuja kutumiwa na Ronaldinho kwenye kizazi cha sasa cha “Televisheni” akiwalaghai mabeki kwa kuwapoteza kama anakwenda upande mwingine kisha anaupeleka mpira kwingine na kukimbia.

Huyu ndiye aliyemzaa Ronaldinho kimpira ambaye alikuja kubadili mpira kuwa burudani yenye soka, gitaa, kinanda na matarumbeta ndani ya uwanja kwa wakati mmoja.

Aliufanya mpira utizamike na ufurahishe hasa kutokana na ukweli kuwa hata yeye aliufurahia na ndio maana hakuacha kuonyesha tabasamu lake.

Wakati Ronaldinho akielekea mwisho wa ubora wake kutokana na starehe zake, alikuwa pale nchini Italia akionyesha mbwembwe badala ya soka akiwa na klabu ya AC Milan.

Kuelekea msimu mpya wa mwaka 2010, kulikuwa na kinda mmoja aliyekua anatua kwenye klabu ya Inter Milan akitokea kwao Brazil kwenye klabu ya Vasco da Gama aliyeitwa Philipe Coutinho.

Ronaldinho haraka kabisa akihojiwa na vyombo vya habari aliweka bayana kuwa Italia ilikuwa imebarikiwa na kipaji kipya ndani ya kinda huyu aliyekuwa na umri wa miaka 18 tu kipindi hicho. Ronaldinho alikuwa akizungumza na jarida maarufu la michezo linalofahamika kama, La Gazzetta dello Sport na kauli yake ilikuwa “But watch out for another young talent, he’s just arrived but he’s destined to make his mark: Coutinho. The future is his.” Ronaldinho alimaanisha kuwa Lakini mtizame kuna kipaji kichanga, ndio kwanza kimefika na tutegemee akiacha alama, anaitwa Coutinho na wakati ujao utakuwa wake.

Ronaldinho alikuwa anafahamu kuwa anamzungumzia mchezaji ambaye alifahamu kuwa alikuwa anatizama kila anachokifanya kuanzia upigaji wa mipira ya adhabu, ubunifu, kuweza kucheza pembeni bila kasi na hata namna ya ushangiliaji.

Ronaldinho alimpenda Coutinho kwa sababu alifahamu kuna “Mini-Ronaldinho” ilizaliwa, na kama ambavyo yeye alikua akimtizama na kuiga aliyoyafanya Rivelino basi kuna mtoto ambaye alikuja kuonyesha yanayofanywa na Ronaldinho katika kizazi cha baadae.

Pengine bahati mbaya kwa Coutinho ilikuwa kuondoka kwa Benitez na kuja kwa makocha kama Leonardo na baadae Gasperini ambao walikuwa chini ya presha ya Massimo Morratti aliyetaka matokeo wa kila namna na kwa umri wake hakuwa tayari kuishi katika mazingira haya na maisha ya kutolewa kwa mkopo yakaanza.

Jicho la Liverpool lilikuwa lenye bahati wakati huu ambao hakuna aliyekumbuka maneno ya Ronaldinho tena na alibahatika kuja kwenye timu ambayo tayari ilikuwa na Luis Suarez ambaye alikuwa kiongozi kwenye eneo la ushambuliaji lakini pia alikuwepo Steven Gerrard ambaye alihakikisha kuna amiri jeshi kwenye eneo la kiungo.

Hapa Coutinho alikuwa na uhuru wa kukua taratibu kwa sababu kila mwenye macho alishagundua miguu yake ina jambo la muujiza ambalo lingeweza kutokea wakati wowote ule.

Mwendelezo wa kiwango chake ndio ulikuwa swali kubwa lakini hili lingekuja na wakati tu pale na angekubali kuwa mwanaume na kuacha uvulana.

Maisha yanayoongozwa na mshale wa saa huwa hayagandi, na Klopp ambaye alikuta wachezaji wengi wakiwa wanasuasua kutokana na nafasi wanazocheza alifanya kila mmoja awe lulu, lakini kati yao Coutinho akageuka kuwa Almasi inayong’ara zaidi ndani ya Anfield.

Wakati washabiki wakifurahia kuimba You’ll Never Walk Alone, muda ambao kumbukumbu za uchezaji wa Ronaldinho zikiwa zinarudi kwenye vichwa vya waliokuwa wengi na pia hamasa ya Liverpool yenye ushindani zikiwa zimerejea, kuna klabu ilikuwa inawaza namna ya maisha yatakavyokuwa baada ya msimu huu kumalizika, inaitwa Barcelona.

Ndani ya Barcelona Ronaldinho alimpisha Iniesta, na sasa dunia haikuwa na kiungo ambaye angeweza kupishwa na Iniesta na pengo lisiwe kubwa zaidi ya Philipe Coutinho.

Lakini kama hiyo haitoshi, Coutinho pia alikuwa anaona nafasi ya ndoto zake kuwa imefunguka, barabara yenye mito na mabonde mbele sasa ilikuwa tambarare na isiyokuwa na vikwazo zaidi ya maamuzi yake mwenyewe.

Coutinho alikuwa anaitizama jezi ambayo ilivaliwa na mtu aliyemhusudu, uwanja ambao ulifurahishwa na mtu aliyemzaa kimpira na pia uwanja ambao hauna ukame wa mataji na kubwa kuliko yote uwanja wa ndoto zake.

Kwa Coutinho, kusubiri mpaka majira ya kiangazi ilikuwa kupoteza muda kwa sababu majaaliwa ya msimu hayajulikani na kwa ligi ya England ndoto zinaweza kukwamia kwenye majeraha ambayo ameyapata mara kadhaa.

Lakini kuna ukweli mchungu usiozungumzwa pia kuwa Coutinho anaenda kwenye taifa ambalo ligi yake inatizamwa zaidi na watu wa Brazil na taifa ambalo kitabia nchi halina tofauti kubwa na Brazil, hivyo ni kama anaenda chumba cha pili cha nyumba yake.

Sababu kubwa nyingine ni kuwa, anaacha washabiki ambao pengine ni bora zaidi duniani, lakini anaenda kukutana na washabiki ambao hawana tofauti kubwa na wale wa Liverpool kwa maana ya kuwatukuza wachezaji hasa aina ya Coutinho. Lakini ni yupi asiyependa kupata pasi safi kutoka kwa Sergio Busquet, ni kichaa yupi asiyetaka kutoa pasi kwa Lionel Messi, Luis Suarez na Dembele?

Katika miaka 25 aliokuwa nao Coutinho, sio tu kuwa anatimiza ndoto yake mapema lakini pia anaenda kujifunza kwa mwanafunzi wa binadamu aliyempenda zaidi. Coutinho angependa kucheza jirani na Ronaldinho lakini sio tabu pale ambapo atakayemkuza kwa sasa ni Andres Iniesta.

Dunia imebadilika kwa sasa, ufalme ndani ya klabu sio tija tena. Coutinho hana moyo wa Roberto Firmino ambao ni aina ya mioyo ya Steven Gerrard ambao unakubali mapambano na kuhakikisha anakuwa sehemu ambayo jina lake litaimbwa daima.

Inawezekana kabisa hata Firmino akabadilika mbeleni lakini walau anafanania tabia hii. Coutinho anamfahamu Ronaldinho, ndoto yake haikuwa Liverpool ilikuwa pale ambapo Ronaldinho aliiweka dunia mikononi mwake.

Ufalme alioambiwa na Klopp haukuwa na maana kwake na hautokuwa na maana kwa wachezaji wa aina yake kwa sababu mapambano sio jadi yao. Kwaheri Philipe Coutinho, Kwaheri Wajina wangu, Liverpool watazoea na wana mtu sahihi ndani ya Klopp bahati nzuri umewapa fedha nzuri pia.     

Monday, January 15, 2018

Si kila jeraha la kuchanika msuli linahitaji upasuajiDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

        Tatizo la kuchanika misuli ni moja ya majeraha yanayowapata wanamichezo mara kwa mara. Ni tatizo ambalo lipo katika tano bora za majeraha yanayowapata wanamichezo duniani.

Leo nimeliongelea hili kutokana na mmoja wa wasomaji ambaye ni mchezaji wasoka kama alivyojitambulisha, aliniuliza kwanini baada ya kubainika amepata jeraha la kuchanika msuli wa paja hakufanyiwa upasuaji.

Si kila jeraha la kuchanika msuli linahitaji upasuaji, matibabu na muda wa kupona hutegemea zaidi ukubwa wa jeraha na uanishaji wake baada ya tathimini ya kitabibu kufanyika.

Kuchanika kwa msuli kitabibu hujulikana kama muscle strain au muscle pull na pia muscle tears. Tatizo la kuchanika msuli linaweza kuwa la kawaida linalopona na kuisha au likawa ni tatizo sugu linalojirudia mara kwa mara.

Jeraha linaweza kutokea sehemu fulani ya msuli bunda la nyuzi za misuli inayovutika au likaendana pamoja na kukwanyuka kwa nyuzi ngumu ijulikanayo kama Tendoni.

Tendoni ni muishilio wa msuli ulio kama nyuzi ngumu inayoupachika msuli katika mfupa na hivyo kuweza kufanya kazi yake ya kujikunja na kukunjuka ili kuleta mjongeo ikiwamo kutembea, kukimbia au kuruka.

Uanishaji wa jeraha la kuchanika kwa msuli ndiyo huwezesha namna mjeruhiwa atakavyotibiwa ikiwamo kufanyiwa upasuaji au matibabu ya kawaida bila upasuaji.

Kuna kuchanika kwa misuli daraja la kwanza ambayo majeraha yake huwa vimichubuko vidogo vya ndani ya msuli ambavyo havihitaji matibabu, hupona yenyewe kwa kupumzishwa kwa kipindi kifupi.

Kuna kuchanika msuli daraja la pili, hapa msuli unaweza kuwa umechanika pasipo kuachana pande mbili, majeraha haya huwa ni makubwa kiasi lakini nayo hayahitaji upasuaji.

Daraja la tatu ni majeraha makubwa, hapa msuli unakuwa umechanika na kuachana pande mbili na yanaweza kuambatana na kukwanyuka kwa nyuzi ngumu za Tendoni zinazojipachika katika mifupa.

Tendoni ya Msuli inaweza kukwanyuka na kutoka na kipande cha mfupa.

Majeraha ya daraja tatu huwapata zaidi wanamichezo wanaoshiriki michezo inayotumia nguvu na kasi ikiwamo mpira wa soka, riadha na mpira wa kikapu.

Ili kuweza kuanisha majeraha haya mjeruhiwa hufanyiwa uchunguzi wa kimwili, kubaini viashiria na kuthimini dalili alizonazo mgonjwa na vipimo mbalimbali. Vipimo ni pamoja na Picha ya xray ambayo hubaini endapo kuna ukwanyukaji wa nyuzi ngumu (Tendon) uliong’oa kipande cha mfupa mahala ilipojipachikia.

Kipimo cha picha ya MRI kufanyika ili kugundua majeraha ya tishu laini kwa ufasaha. Vile vile hata kipimo cha CT scan na Utrasound huweza hufanyika.

Aina zote za majeraha ya kuchanika misuli hutibika na mchezaji huweza kuendelea na michezo baada ya kupona.     

Monday, January 15, 2018

Mwaka huu tuandae walimu bora kwa shule za msingiAllan Goshashi

Allan Goshashi 

        Ni kweli michezo ni burudani, ila kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, michezo ni kipaumbele katika kutoa ajira pana, kukuza biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano.

Kwa mfano, nchi za wenzetu za Ulaya na Marekani, pia nchi za Afrika kama Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Tunisia, Morocco, Misri, Afrika Kusini na Algeria zinatumia kikamilifu nafasi hii ya michezo kujitangaza kisiasa na kiuchumi na kutengeneza ajira pana kwa raia wa nchi zao.

Katika hali ya kushangaza sisi Watanzania bado hatujaiona fursa hii pana ya ajira, kama tumeiona basi tunaidharau, maana hatuitendei haki hasa katika ngazi ya msingi, halafu tunatarajia kupata wanamichezo mahiri watakaoshindana kimataifa na michezo kuwa ajira yao.

Hii siyo sawa kabisa, hebu tazameni idadi ya walimu wa michezo waliopo katika shule za msingi za serikali na sekondari, tazameni na uwezo wa walimu hao wa kufundisha michezo, pia tazameni vifaa vinavyotumika pamoja na miundombinu iliyopo.

Ni wazi mkitazama mtaona kuna upungufu mkubwa wa walimu weledi wa michezo katika shule za msingi na sekondari, hali inayosababisha watoto wasipende michezo kwenye shule, hivyo walimu hao wachache na wale wasio na weledi kushindwa kuibua vipaji vya watoto kwenye shule.

Walimu hao wa michezo ambao hawana ueledi wameshindwa kuonyesha umahiri wao wa kuwabadilisha watoto kwa kuwapa mafunzo sahihi ya michezo kwa sababu kazi ya mwalimu siku zote ni kumbadilisha mwanafunzi kwa kumpa mafunzo sahihi.

Walimu wanaofundisha michezo katika shule za msingi wapo wachache, ila wapo kati yao wanaoonekana wana uwezo ila wengi wao wanahitaji kuendelezwa zaidi ili wawe na uwezo wa kutoa mafunzo mazuri kwa wanafunzi wao.

Wanahitajika walimu weledi wa michezo kufundisha michezo katika shule za msingi na sekondari kwa sababu walimu hao wanatakiwa kuwekeza muda wao na kuwa na uwezo wa kuwafundisha elimu ya viungo, nidhamu, aina ya vyakula wanavyotakiwa kula, kupanga ratiba za mazoezi, kupanga nini wanataka kuzifundisha timu zao, kuwafundisha saikolojia, mambo ya msingi ya kila mchezo husika na mengine mengi.

Ndiyo maana nahimiza umuhimu wa kuwapo kwa walimu weledi wa kutosha katika ngazi za chini, katika shule za msingi kwa sababu huko ndiyo msingi imara wa mchezaji unatakiwa kujengwa badala ya kusubiri mwanamichezo amekuwa mkubwa ndiyo apewe mafunzo sahihi na mwalimu mweledi.

Watoto wengi hujiunga na shule za msingi wakiwa na miaka sita hivyo akifika miaka 13 anamaliza elimu ya msingi, kipindi hiki mtoto akiwa shule ya msingi ndiyo kizuri cha kuendeleza kipaji cha mtoto.

Tusijidanganye kabisa kupata wanamichezo weledi ambao michezo kwao itakuwa ajira kama huku kwenye shule za msingi hakuna walimu weledi wanaoweza kutoa mafunzo sahihi kwa watoto ambao tunawategemea kuendeleza michezo mbalimbali.

Ninaamini serikali itahakikisha wanapatikana walimu wengi wa michezo katika shule za msingi kwa sababu suala hili lipo wazi, pia watawalipa vizuri walimu hao ili waweze kujenga msingi mzuri wa michezo nchini.

Pia, kurudishwa michezo kwenye shule, zoezi hilo lingeenda sambamba na kuandaa walimu wa kutosha wa kufundisha michezo hiyo.     

Monday, January 15, 2018

Hii ya Kamati ya Saa 72 inatengeneza maswaliIbrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

        L igi Kuu Tanzania Bara inaanza mikikimikiki yake baada ya kusimama kupisha Kombe la Mapinduzi.

Mashindano hayo yaliyofana mwaka huu, yamemalizika juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan kwa Azam kutwaa ubingwa kwa kuilaza URA kwa mikwaju ya penalti 5-3.

Lengo si kuyajadili mashindano hayo, lakini kikubwa ni kutaka kuangalia yaliyotukia hivi karibuni kwa TFF.

Ligi ikiwa imesimama, tulielezwa kuwa kuna baadhi ya matukio ambayo yalijiri tangu ligi hiyo ilipoanza Agosti mwaka jana ikiwamo vitendo vya utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukizigharimu timu pamoja na wachezaji, makocha na viongozi wa klabu.

Kwanza inashangaza kuona matukio haya kujirudiarudia, lakini pengine ni kutokana na presha za mechi husika.

Nataka kuiangalia Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ambayo kwa sehemu kubwa ndiyo wasimamizi wa ligi.

Kamati hiyo ndiyo inayotoa adhabu mbalimbali kwa klabu, makocha na wachezaji. Juzi hapa naweza kusema ilitoa mpya kwa kutoa adhabu kwa wachezaji, viongozi na timu, sasa shangaa ni kutokana na makosa yaliyofanyika muda mrefu, tofauti na ilivyokuwa inatarajiwa.

Iliziadhibu Mbao FC na kocha wao, Etienne Ndayiragije na wachezaji kadhaa wa timu mbalimbali akiwamo Obery Chirwa wa Yanga na Lambert Sabyanka wa Prisons kwa kuwasimamisha ama kupiga faini.

Kama nilivyosema kuwa inashangaza hali hii na pengine ni kutokana na tensheni ya mechi zao na ni wazi inadhihirisha kuwa kuna shida ya utovu wa nidhamu katika Ligi Kuu.

Ninachokiona hapa, si kwa timu hii, kuna tatizo la kinidhamu. Kwa mchezaji, kocha au viongozi, nidhamu ni msingi wa kila jambo .

Hata wachezaji wa soka kucheza bila ya nidhamu ni jambo linalowakwanza kufika mbali.

Inafahamika kwamba, klabu zisizo na nidhamu ni vigumu kufikia mafanikio ambayo wengi wanatamani kufika huko wanakokimbilia.

Nidhamu mbovu uharibu ladha ya mchezo kwa sababu inaweza kutokea kocha kufungiwa, kusimamishwa kitaifa ama kimataifa.

Klabu zinatakiwa kufahamu kuwa Ligi Kuu pamoja na wachezaji wote, makocha na hata viongozi wake kuwa ni vyema kujikita katika nidhamu, ili waweze kufika mbali na kusaidia kuinua soka letu.

Wakati mwingine, inawezekana TFF inashindwa kukemea suala hili kwa vile yenyewe inanufaika kwa faini inazozipiga timu, wachezaji, makocha na viongozi na kutunisha mifuko ya shirikisho hilo, lakini nidhamu mbovu ina athari kubwa kwa soka letu.

Hata kama suala la nidhamu nzuri ama mbovu ni suala linalomhusu mtu mmoja, lakini viongozi na makocha wanawajibu mkubwa wa kuwasaidia wachezaji wao kwa kuwaonya mapema na kuwataka kuingia viwanjani wakiwa na utulivu wa akili.

Kama kocha wa timu hana nidhamu wala kuwa na uwezo wa kuhimili presha za uwanjani na kufanya matendo ya ovyo na utovu wa nidhamu, ni vipi ataweza kuwahimili wachezaji wake. Kiongozi asiyeweza kuhimili vishindo vya uwanjani atawezaje kuanza kuwatuliza wachezaji wake pale wanapokuwa na munkari?

Cha msingi ni wachezaji kutofanya mambo yanayokwenda kinyume na soka lakini zaidi kwa TFF kutangaza adhabu kwa wakati.

Inapendeza kama mchezaji, kocha au timu akiadhibiwa palepale inapotokea amefanya makosa kuliko sasa kunaweza kuonekana kama dili kwa kuwafungia wachezaji muhimu baada ya kuona mchezo fulani unaelekea au unakaribia.     

Monday, January 15, 2018

Wametisha kombe la Mapinduzi

 

By Thobias Sebastian,Mwananchi

Kombe la Mapinduzi limemalizika mwisho wa wiki hii na kushuhudia baadhi ya wachezaji kutoka Azam, Simba na Yanga ambao hawapati nafasi za mara kwa mara kucheza kwenye ligi lakini kwenye mashindano hayo walitakata.

Kutakata kwa wachezaji hao kunaleta ugumu kwa makocha kufanya uamuzi katika upangaji wa vikosi kutokana na viwango bora vilivyoonyeshwa wao ambao si machaguo yao ya kwanza.

Makocha wa timu za Azam, Simba, Yanga na Singida United zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa upande mwingine huenda wakalazimika kupangua vikosi vyao vya kwanza ambavyo vimezoeleka ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Spoti Mikiki linakuletea wachezaji ambao wametamba katika michuano hiyo ambao kwenye ligi nafasi zao za kucheza ni finyu.

Jamal Mwambeleko, Simba

Katika mechi ya kwanza Simba dhidi ya Mwenge iliyomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, bao la Simba lilifungwa na Mwambeleko kipindi cha kwanza tena dakika ya pili lakini timu yake haikufika mbali kwenye mashindano hayo walitolewa katika hatua ya makundi.

Mwambeleko aliyesajiliwa kutoka Mbao FC, licha ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo lakini nafasi yake ya kucheza katika ligi anabanwa na Erasto Nyoni au Mohammed Hussein ‘Tshabalala ‘.

Ramadhani Kabwili, Yanga

Kipa wa Yanga ambaye amesajiliwa na timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano akitokea katika kikosi cha Serengeti Boys anaweza kuonesha kiwango katika mashindano hayo ya Mapinduzi.

Kabwili amecheza mechi mbili za makundi na kufungwa bao moja huku mechi zote Yanga ikiibuka na ushindi lakini licha ya kucheza vizuri katika mashindano hayo, hapati nafasi ya kucheza kwenye ligi

Mwinyi Kazimoto, Simba

Kiungo mkongwe wa Simba ambaye alionyesha kiwango safi katika mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya Mwenge na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi na alizawadiwa king’amuzi cha Azam.

Kazimoto ambaye ni fundi katika kuuchezea mpira, anastahili pongezi kwa kazi ambayo waliofanya lakini ni miongoni mwa wachezaji ambao wanakosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba ambacho kinaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Haji Mwinyi, Yanga

Aameonyesha kiwango bora kwenye mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Kenya mwishoni mwa mwaka jana na mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Kiwango chake ni kama salamu kwa Gadiel Michael ambaye ndiye aliyempoka namba. Uamuzi ni wa Lwandamina.

Moses Kitandu, Simba

Mshambuliaji wa Simba ambaye anacheza mechi zote nne za hatua ya makundi na kufunga goli moja katika mechi dhidi ya Jamhuri na kushinda 3-1.

Kitandu katika ligi hapati kabisa nafasi ya kucheza kwani nafasi yake kuna wakongwe John Bocco na Emmanuel Okwi ambaye anaongoza katika msimamo wa wafungaji wa Ligi Kuu akiwa ameshafunga magoli nane.

Peter Paul, JKU

Mpaka hatua ya makundi inakamilika alikuwa ameshafunga magoli matatu na kuwa katika vinara wanaongoza kufunga kwenye mashindano hayo akiwa sambamba na Ahmad Halika wa JKU.

Paul nafasi yake katika ligi ni ndogo, kwenye Kombe la Mapinduzi amefunga goli moja katika mechi chache alizocheza na licha ya kuingia katika muda wa nyongeza.

Maka Edward, Yanga

Kiungo fundi wa Yanga ambaye alimpandisha katika ligi kuu akitokea katika timu yao ya vijana amecheza mechi mbili za mwisho za Makundi ambazo walicheza dhidi ya Zimamoto na Singida United.

Maka alicheza katika Mapinduzi lakini kwenye ligi hajacheza hata mechi moja kwani nafasi yake huwa anacheza Raphael Daud na Kabamba Tshishimbi.

Emmanuel Mseja, Simba

Kipa ambaye wakicheza hata mechi moja katika ligi kutokana na nafasi yake kucheza kipa namba moja Tanzania Aishi Manula lakini katika mashindano hayo amecheza mechi zote.

Mseja hakuonyesha kiwango kizuri kwani katika mechi nne ambazo Simba wamecheza katika hatua ya makundi amefungwa magoli manne na pengine ni kutokana na kuzongwa na benchi tofauti na vile angekuwa anapangwa.

Mwidini Ali, Azam

Kipa mkongwe wa Azam yupo katika kikosi hiko kwa muda mrefu na alipata nafasi ya kucheza kwenye mechi kadhaa ingawa katika ligi hapati nafasi hiyo.

Azam katika ligi humtumia kipa wao mahiri, Razack Abarola ambaye hata katika mashindano hayo alitamba kwa kudaka vizuri mechi chache tu alizocheza dhidi ya Simba na Singida United.

Pato Ngonyani, Yanga

Beki wa kati wa Yanga ambaye kwenye ligi hana nafasi kabisa ya kucheza kutokana na nafasi yake kuzibwa na Kelvin Yondan na Vincent Andrew ‘Dante ‘.

Pato amecheza mechi mbili katika hatua ya makundi kama kiungo mkabaji na kuingia katika wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza kwenye kwenye ligi kuu ambayo itaendekea mwisho wa wiki hii.

Salum Kipaga, Singida

Mtihani kama huo unamkabili kocha wa Singida United, Hans Van der Pluijm atalazimika kumpanga Mudathir Yahya au Salum Kipaga kwenye nafasi ya kiungo mkabaji.

Mudathir alikuwa lulu kwenye Ligi Kuu na Mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Kenya mwaka jana lakini, Kipaga ametumia vyema fursa ya Kombe la Mapinduzi kujitangaza. Ameonyesha soka ya hali ya juu.

Said Makapu, Yanga

Kiungo mkabaji wa Yanga amecheza mechi zote katika mashindano hayo na katika mechi za mwanzo alikuwa akicheza kama kiungo mkabaji lakini alikuja kubadilishia namba.

Makapu amemaliza mechi tatu za mwisho katika hatua ya makundi akicheza kama beki wa kati baada ya Abdallah Shaibu na Kelvin Yondan kuumia na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi ya nusu fainali dhidi ya URA.

Matheo Anthony, Yanga

Straika wa Yanga ambaye alisajili misimu miwili iliyopita na Yanga baada ya kuonekana katika mashindano hayo ya mapinduzi amepewa nafasi ya kucheza safari hii.

Anthony kwenye ligi hajacheza hata mechi moja kwani nafasi yake huwa wanacheza Ajibu, Amiss Tambwe, Donald Ngoma na Obrey Chirwa ambao ambao ndio hupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Juma Mahadhi, Yanga

Winga wa Yanga mpaka mashindano yanamalizika alikiwa amefunga magoli mawili dhidi ya Mlandege katika mechi ya kwanza dhidi katika hatua ya makundi.

Mahadhi amecheza mechi nyingine nne hadi walipotolewa katoka hatua ya nusu fainali na URA lakini kwenye ligi nafasi yake ni ndogo na huishia benchi.

Said Mussa, Yanga

Winga machachari wa Yanga ambaye walimpandisha akitokea katika timu ya vijana msimu huu baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha Serengeti Boys amecheza mechi mbili za hatua ya makundi ingawa alikuja kuumia katika mechi ya mwisho.

Said hata katika wachezaji wa akiba wa Yanga kwenye ligi huwa akai lakini huku aliweza kupewa nafasi na kucheza.

Brayson Raphael, Azam

Kiungo wa Azam hana nafasi ya kucheza kabisa kwenye kikosi hicho katika mechi za ligi lakini amecheza vizuri katika mashindano ya Mapinduzi.

Raphael hupanda na kwa uwezo alionyesha katika mashindano hayo anapewa nafasi ya kucheza kwenye ligi kwani anastahili kuwepo katika wachezaji wa Azam ambao wanacheza kwenye ligi.

Yusuph Mhilu, Yanga

Winga wa Yanga alipandishwa na timu hiyo akitokea katika kikosi chao cha vijana na alikuwa akipata nafasi mara chache za kucheza na zikiwa zimebaki dakika za majeruhi japo soka yake inaonekana kuwa ya kiwango.

Mhilu amekuwa mchezaji wa kucheza mwanzo mwisho kwenye mashindano hayo akishirikiana na Ibrahim Ajib katika safu ya ushambuliaji.     

Monday, January 15, 2018

Issa Juma anavyozitamani ligi za barani Ulaya

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Mtibwa Sugar inajivunia kiungo wake, Issa Juma ambaye licha ya kucheza eneo la kiungo wa kati pia ana uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji (10) na hata kwenye eneo la ushambuliaji wa mwisho.

Kiungo huyo aliitwa kwenye ule mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi na kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga ili kuziba nafasi ya Orgeness Mollel wa FC Famalicao ya Ureno ambaye alishindwa kuwasili.

Issa mwenye asili ya Zanzibar amezungumza na Spoti Mikiki na kuelezea mambo kadhaa ambayo wadau wengi wa soka hawafahamu kuhusu yeye hasa alipoanzia kucheza soka na tabia yake kwa ujumla.

“Kuna timu moja ya mtaani inaitwa Jamaica ya Zanzibar hiyo ndiyo nilianza kuichezea wakati nikiwa mdogo, 2010 hadi 2013 na ndipo nilipoanza sasa kuangaikia kwa kutafuta timu kubwa ya kuichezea,” anasema Issa.

Changamoto

“Nimepitia mengi sana lakini kikubwa ni changamoto ya kutokuwa na jina kubwa, ilinifanya kuwa na wakati mgumu sana, hakuna aliyekuwa anajali kuhusu mimi mpaka pale atakaponiona nacheza. “Mtibwa nilifanya majaribio na kufuzu ila ilibidi kuanza kuonyesha kwa nguvu zote ili nianze kujijengea jina, kwa kiasi chake nimefanikiwa, ukiwa haufahamiki ningumu sana kwenda sehemu na kupata nafasi moja kwa moja,” anasema.

Mavazi

“Sio mtu wa mambo mengi kwenye mawazi, mara kwa mara navaa tisheti na jinzi ila sio kwamba ndiyo nguo ninazo zipenda, huwa napenda sana kuvaa suti ila tatizo lile ni vazi ambalo huwezi kulivaa kila wakati,” anasema Issa.

Malengo

“Wachezaji wengi wa hapa nyumbani maisha yao ya mpira huishia Yanga na Simba, sipendi na kwangu iwe hivyo natamani sana kama nitashindwa kufika Ulaya basi nicheze hata Ligi ya Afrika Kusini,” anasema Issa.     

Monday, January 8, 2018

Msuva: Akili yangu ni kucheza Ulaya tu

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

 Baada ya kumalizika kwa duru la kwanza la Ligi Kuu Morocco,Saimon Msuva ameona ni bora kurejea nyumbani kwa mapumziko mafupi kabla ya kuanza kwa duru la mwisho la ligi hiyo ambayo ni maarufu kama Batola Pro.

Julai, 29 mwaka uliopita wa 2017 ni siku ambayo hakika itasalia kwenye kumbukumbu za Msuva ambaye alitambulishwa rasmi kama mchezaji wa Difaa chini ya usimamizi wa Dk. Jonas Tiboroha akitokea Yanga.

Difaa ambayo ilianzishwa mnamo,1956 haijawahi kushinda taji hata moja la Batola Pro na badala yake wamekuwa wakiambulia kushika nafasi za pili kwa misimu kadhaa.

Historia inaonyesha wamewahi kutwaa Kombe la Mfalme ‘Coupe du Trône’mara moja,2013.

“Nyumbani ni nyumbani.Sikuona sababu ya kunifanya nisirejee kipindi hiki ambacho nimekaa mbali na familia yangu kwa miezi kadhaa,japo nitakuwa hapa kwa kipindi kifupi cha kama wiki moja na siku kadhaa,” anasema Msuva.

Msuva alitua nchini,Januari 4 na kupokewa na ndugu, jamaa na marafiki waandishi wa habari ambao walifanya naye mahojiano kabla ya mtu wake wa karibu kumpokea mizigo yake na kuelekea naye nyumbani kwao.

“Wazazi walifurahi sana kuona kijana wao nimerejea tena,hata kama nilikuwa nafanya nao mawasiliano nikiwa kule kunikumbuka kwao kuwepo pale kuna

utofauti wa kuongea nao na kuniona macho kwa macho,” anasema Msuva.

Mara baada ya kuwasili,Msuva aliamua kujumuika na nyota wengine wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ajili ya kwenda kwenye msiba wa mama yake na kiungo wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy.

“Nilipokea taarifa za msiba kwa mstuko kwa sababu natambua umuhimu wa wazazi.Namwombea Sure Boy, Mungu amwongoze kwenye kipindi hiki kigumu,” anasema.

Baada ya mazungumzo ya awali, Spoti Mikiki ilimdodosa mawili, matatu:

Swali: Tangu uatue Difaa, unaonekana kubadilika na kuwa na umakini mkubwa, nini hasa kimekubadilisha

Msuva: Ni mabadiliko ya nafasi ninayocheza...kasi niliyo nayo kocha aliona ninafaa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho na muda mwingine amekuwa akitaka tucheze pacha katika nafasi hiyo ya ushambuliaji na mwenzangu,

Hamid Ahaddad ambaye ndiye mashambuliaji halisi anayetegemewa kwenye kikosi cha kwanza.

Swali: Ulipata shida zipi baada ya kutua kwenye timu yako na namba unayocheza?

Msuva: Sikuwa napata sana shida kwenye nafasi hiyo mpya kwa sababu kipindi nacheza soka la utotoni nilikuwa nacheza kwenye nafasi hiyo, bahati nzuri kocha akaona ninafiti kwenye hiyo nafasi na kuamua kuwa ananitumia mara kwa mara.

Swali: Mara zote anakupanga kwenye nafasi hiyo tu?

Msuva: Inategemea maana kuna muda ninatokea pembeni ila sio sehemu ambayo natumika sana.

Swali: Umeimarika sana katika kupiga mabao, nini siri Msuva?

Msuva: Aaa! Kidogo, lakini niseme tu ni umakini wa ufungaji niliokuwa nao na kujiamini zaidi kumenifanya kuwa hivi ila cha ziada ni kuwa nacheza mbele zaidi hivyo kuna uwezekano wa kuendelea kufunga.

Swali: Nini umejifunza kutoka kwa wenzako ikilinganisha na soka ya Tanzania?

Msuva: Nimejifunza mengi na ofcourse, nimekuwa mtu wa kujifunza kila siku kutoka kwa wenzangu, kujifunza kwangu kumenipa maarifa zaidi katika uchezaji wangu.

Swali: Vipi, tofauti gani umeona soka ya Tanzania na huko Morocco?

Msuva: Soka lao ni tofauti sana na letu hivyo nimekuwa nikijipa muda wa kuchota ujuzi taratibu. Wenzetu wanatumia nguvu kidogo lakini akili nyingi. Lazima uwe na maarifa ya kutosha kucheza soka kule.

Swali: Wakati unatua sasa Morocco, ilikuwaje katika soka, mambo gani makubwa umefanya?

Msuva: Wakati ninajiunga na Difaa nilicheza michezo 13 ya kirafiki na katika michezo hiyo nikiwa kwenye nafasi yangu hiyo mpya nilifunga mabao tisa na mara baada ya kuanza kwa msimu mpaka sasa nina jumla ya mabao sita katika mashindano yote.

Swali: Katika ligi hali ya ufungaji ikoje?

Msuva: Nashukuru Mungu sipo nyuma. Nimo kwenye orodha ya wafungaji wa Batola Pro nikiwa na mabao matano, nipo nafasi ya nane na nimezidiwa mabao matatu na kinara wa mabao Mehdi Neghmi wa Ittihad Tanger, ana mabao nane.

Swali: Nimesikia uliingia kwenye kikosi bora cha Novemba, hii ikoje?

Msuva: Ni kweli, niliingia mara moja kwenye kikosi bora cha mwezi, Novemba mwaka jana kwa kufunga mabao mawili na kutengeneza mengine matatu ndani ya mwezi huo.

Swali: Umeshawahi kufikiria kuhama timu hiyo?

Msuva: Nimekuwa nikifikiria kuondoka kwenye klabu hiyo na kutimkia zangu Ulaya ambako ninapataka tangu nikiwa Yanga. Kabla ya hata kujiunga na Difaa nilikuwa nina mawazo ya kucheza Ulaya ila isingekuwa rahisi kutoka moja kwa moja Yanga hadi Ulaya ndiyo maana ziliponifikia ofa tofauti kwa usaidizi na wasimamizi wangu tulifanya mchanganuo.

“Lengo la kwanza lilikuwa kuitumia timu hiyo kama njia, napambana kila kukicha ili nipite kama ninavyohitaji,naomba hata mwaka huu usiishe niwe nimepata nafasi sehemu nyingine.

Swali: Kuna timu zimeonyesha nia na wewe:

Msuva: Ndiyo, kuna timu ambazo zimeonyesha kunihitaji ila siwezi kuziweka wazi kwa sababu mambo bado ila watu waniombee.

Swali: Nasikia wanakuita Sadio Mane yule straika wa Liverpool, imekuwaje hadi ikawa hivyo?

Msuva: Ni mapenzi yao juu yangu. Labla tumekuwa tukifanana uchezaji maana wamekuwa wakinifananisha naye, sikuwahi kuwauliza kwa nini wameamua kunipa ilo jina ila nimekuwa na mahusiano nao mazuri licha ya kuwepo kwa changamoto ya kimawasiliano.     

Monday, January 8, 2018

Danstan: Trans Camp haishuki la pili

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Licha ya Trans Camp ya Daraja la Kwanza (FDL) kutokuwa na nafasi ya kupanda daraja, kiungo wa timu hiyo, Abdallah Danstan (22) anasema ni bora wasalie kwenye daraja hilo kuliko kushuka.

Dastan ni mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha maafande hao ambao kama sio mipango yao kwenda ovyo walikuwa na hesabu za kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu ujao.

Spoti Mikiki imefanya mazungumzo na kiungo huyo ambaye alishiriki kuipandisha timu hiyo kutoka daraja la pili kwenda la kwanza na kusema kiu yake ni kucheza VPL.

“Ngazi ya juu kwenye mpira wetu wa Tanzania ni kucheza Ligi Kuu, tumejitahidi kuhakikisha timu inapanda ila mambo sio mazuri,” anasema kiungo huyo.

Dastan amefichua kuwa alipitia Simba B wakati akichipukia kwenye soka na baadaye akajiunga na JKT Oljoro ambapo na kwenye hakudumu kwa kipindi kirefu,2016 akahamia Trans Camp.

“Simba nimecheza mpira ila kilikuwa kikosi cha vijana,niliona pale panaweza kunichukua muda kupata nafasi kikosi cha kwanza na ndiyo maana nilifanya uamuzi wa kujiunga na Oljoro.

“Hapakuwa na tatizo Oljoro na baada ya kufanya vizuri hapo nikasajiliwa na Trans ambao walikuwa Daraja la pili,” anasema Dastan.

Akizungumzia uwezekano wa kurejea Simba kwa siku za usoni kama atahitajika, Dastan anasema kuwa atakachotazama ni maslahi yake na wala hatotoa nafasi ya upendeleo kwa kuwa amelelewa hapo.

“Heshima yangu kwa Simba ni kubwa ila katika hilo tutasamehana kidogo na sio Simba pekee ni kwenye timu yoyote itakayonihitaji,” anasema.

Hata hivyo, Dastan anadai ni kama amekuwa na bahati kwenye uchezaji wake mpira kwa kuwa hajawahi kupata changamoto yoyote kubwa.

“Kuna majeraha ya kawaida ambayo huwa yanatokea ila sijawahi hata siku moja kupata changamoto ambayo ikanifanya labda kufikiria hata kuachana na soka, bado ninaendelea kujihusisha na mpira kwa hiyo lolote linaweza kutokea ila naomba Mungu aendelee kuniepusha na majanga,” anasema Dastan.     

Monday, January 8, 2018

Mkwawa umenena, kuna vyama vya michezo na vijiweIbrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

Katikati ya wiki iliyopita, Serikali kupitia kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini, Ibrahim Mkwawa amesema vyama visivyokuwa na ofisi atavifuta mara moja. Hiyo ilikuwa mahojiano maalumu na gazeti hili.

Mkwawa alisema kuwa pamoja na Tanzania kuwa na vyama vya michezo visivyopungua 58, asilimia kubwa ya vyama hivyo vimekosa sifa kwa kutokuwa na ofisi na watendaji wake wanaendesha shughuli zao ama kwa kutumia ofisi zao za kazi walizo ajiriwa, ofisi zao binafsi na wengine kutumia simu za mkononi au wanatumia briefcase kama ofisi na nyaraka zote ziko humo.

Ukweli hii ni kinyume na sheria za usajili chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na zinaelekeza kuwa kila chama kinatakiwa kuwa na ofisi.

Nimeipenda hii aliyosema kwamba ofisi yake itafanya uhakiki wa vyama hivyo na baadaye kuchukua hatua stahiki ikiwa pamoja na kufutiwa usajili wake.

Hili liko wazi kwamba si jambo la ajabu wala aibu kwa vyama vikubwa hapa nchini kutokuwa na ofisi za kufanyia kazi, wengi wanafanyia kupitia ofisi zao binafsi au sehemu wanayofanyia kazi na wengine kutumia simu za mkononi, hii haiwezi kuleta maendeleo ya michezo nchini.

Kinachonishangaza, baadhi ya vyama au mashirikisho yanapokea fedha za maendeleo ya mchezo husika kila mwaka, lakini wanashindwa kujipanga kujenga ofisi! Kama fedha zinaletwa kwa maendeleo, basi wachangishane viongozi na wanachama kupatikane ofisi. Hii ni aibu iliyoje.

Halafu unajiuliza, wazungu wameleta fedha zao, sasa wakitaka kuona ofisi na hicho kinachotumwa, si itakuwa aibu kubwa

Ninadhani itapendeza kama Mkwawa akianza kufanya sensa ya vyama na kufanya uhakiki wa kila chama cha michezo.

Kwa mujibu wa Mkwawa, serikali inataka kuona maendeleo ya ukweli katika sekta ya michezo tofauti na hali ilivyo sasa.

Kama tulivyoona, Tanzania kuna vyama vya michezo 58, lakini vyama ambavyo vina ofisi eneo la Changamani ni Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT) na kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBC). Vyama ambavyo vina ofisi ni pamoja na TFF, TGU (gofu), TCA (Kriketi) na Chama cha Baiskeli (Chabata).

Hapa kuna kazi. Ni vizuri msajili kufanya kazi ya kuhakikisha kila chama kina ofisi ya kufanyia shughuli zake.

Kingine ambacho kinakwenda sanjari na hiki ni kufanyia sensa. Nimesema hapo juu kwamba ifanyike sensa na uhakiki. Tunaona kati ya vyama hivyo vyenye ofisi na viosivyo na ofisi hata robo yake havifiki katika michezo.

Tunaisikia TFF, tunawasikia riadha, netiboli, ngumi, wavu, kikapu na kuogelea.

Ninasema sensa kwa maana ipi, ifahamike kuwa vyama viko kweli Tanzania nzima au vya Dar es Salaam pekee?

Wana wanachama? Katiba zikoje?

Kwa vyama 58, Tanzania ingekuwa inapeleka kundi la la wanamichezo walioiva kwenye Michezo ya Olimpiki, Madola na Afrika, lakini unajiuliza wanafanya nini?

Hawa jamaa ninaamini wanatumia vyama vya michezo kama vichaka vya kupigia fedha za mashirikisho ya kimataifa lakini hakuna kinachofanyika.

Wataandaa visemina, watapiga mapicha na kutoa vyeti, na watazituma kwa wazungu kuwalainisha watoe fedha zaidi, na kwa kuwa wanataka maendeleo wanamwaga fedha kumbe watu wanapiga.

Nampongeza Mkwawa kwa kuliona hili jipu la aina yake na isiishie kutoa tamko, afuatilie.     

Monday, January 8, 2018

Kipaji cha mwanamichezo ni fursa muhimu ya maishaAllan Goshashi

Allan Goshashi 

        Uzuri uko kwenye macho ya yule anayeuona. Sasa unaweza kujiuliza, je, anayeuona ni nani?, Je, ni mwenyewe muhusika au ni watu wengine. Wenye kuuona uzuri ni wengi na kila mtu ana haki ya kuamua kama anachokiona machoni mwake ni kizuri au la.

Binafsi, naiona michezo kama ni kitu kizuri kwa sababu sehemu yoyote utakayokwenda duniani, huwezi kuikimbia michezo, lazima utakutana nayo isipokuwa kama; huitaki , hauipendi, hujui maana yake, unafanya makusudi kuikataa au huoni faida yake.

Michezo pia inatufundisha ushindani wa kistaarabu, ushindani unaozingatia sheria na kanuni, ushindani unaojenga urafiki badala ya uhasama; ushindani unaoleta upendo badala ya chuki na ushindani unaoleta amani badala ya shari.

Vilevile, michezo husaidia kujenga na kuimarisha afya, hujenga moyo wa kishujaa, kujihami, ukakamavu, kujiamini na humjenga mwanamichezo kimwili, kiakili na kiroho na hutoa ajira na burudani.

Zamani michezo ilikuwa ikionekana kama ni burudani , lakini hivi sasa michezo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo kwa upana wake, yaani maendeleo kiuchumi, kiafya, kielimu vyote vinasukumwa na michezo.

Mamilioni ya watu duniani wanategemea michezo kuendesha maisha yao, hata hapa nchini kuna watu wengi wanaotegemea michezo ili kuendesha maisha yao, kwa hiyo michezo siyo jambo dogo. Michezo ni shughuli muhimu ambayo inatakiwa kuandaliwa. Ndiyo maana siku zote ninapoona watu waliopewa dhamana ya kuongoza michezo nchini hawaithamini michezo ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Wanafunzi wa Shule za Sekondari (Umisseta) na ile ya shule za msingi (Umitashumta) huwa ninashangaa sana.

Michezo hii ya shule za msingi, sekondari pamoja na ile ya vyuo vikuu ni muhimu sana katika kuibua na kuviendeleza katika mfumo rasmi kwa manufaa makubwa ya taifa.

Ninasema hivyo kwa sababu nilibahatika kushiriki katika michezo ya Umisseta na kushuhudia wanamichezo wengi wenye vipaji ambao hivi sasa wameishia kuajiriwa katika mashirika mbalimbali ya umma na binafsi.

Hali hii inaashiria nini? Hii inaonyesha kwamba taifa letu haliamini katika kuwawezesha watu kuishi kwa kutumia vipaji vyao badala yake linahamasisha watu kuajiriwa na ndiyo maana inakuwa ni vigumu pia kwa vijana kujiajiri.

Hili ni tatizo kwa Taifa na linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka kwani madhara yake ni kuikosesha nchi vipaji bora, ajira, mapato makubwa na mambo mengine mengi muhimu yanayotokana na kipaji cha mwanamichezo.

Kipaji cha mwanamichezo kikiandaliwa na kuendelezwa vizuri huwa kina uwezo wa kutoa ajira nyingi kama lilivyo kampuni. Ndiyo, kipaji cha mwanamichezo kinazungukwa na kutoa fursa kwa walimu, waamuzi, madaktari, makamisaa, mawakala, watendaji, wanasheria, wakata majani wa uwanja, watu wa usafi, wapishi, walinzi, wakufunzi na wataalamu wa taaluma nyingine nyingi.

Sasa huwa ninajiuliza, je, kwa hapa nchini bila ya kuendeleza michezo ya Umisseta, Umitashumta na ile ya vyuo vikuu tutawapata wanamichezo watakaoweza kuendesha maisha yao na kutoa fursa za ajira? Au ndiyo maana watu waliopewa dhamana ya kuiongoza michezo hawaoni umuhimu wa michezo?

Ni wazi suala la kuendeleza michezo linapigiwa kelele na waandishi wa habari pamoja na wadau wengine.     

Monday, January 8, 2018

Je, unayafahamu mazoezi yanayosaidia kujenja mwili?Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

        Mwanadamu wa kawadia na wanamichezo wanahitaji mazoezi bora ambayo yataujenga mwili wake na kuufanya uwe imara na afya njema, mazoezi yanakuepusha na uzito mkubwa na unene uliokithiri.

Mwanadamu hasa kwa mwanaume kuwa na mwili wenye mwonekano mzuri ulio na misuli imara na iliyojengeka ni jambo ambalo linapendwa lakini si kila zoezi linaweza kuujenga mwili wote.

Inawezekana unahangaika kubeba vyuma vizito ili kuujenga mwili pasipo kufahamu ni aina gani ya mazoezi yanayoongoza kujenga mwili.

Yapo mazoezi ambayo yanakubalika na wataalamu wa tiba za michezo na mazoezi ya viungo kuwa ndio yanakufanya kujenga mwili wote kutokana na uwezo wa kushughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi haya endapo mwanadamu atayafanya mara kwa mara humfanya kuwa na mwili imara uliojijenga.

Zoezi linaloshika namba moja kwa kujenga mwili huwa ni kuogelea, zoezi hili linaujenga mwili kwani kuogelea kunahusisha misuli mingi zaidi kuanzia miguu, kiwili wili, mikono na kichwa.

Jaribu kuwatazama wavuvi, wapiga mbizi, wanamichezo waogeleaji utagundua wamejengea mwili mzima.

Zoezi la pili ambalo linashika nafasi ya pili kwa kujenga mwili huwa ni kucheza mziki, lakini sio muziki laini kama ilivyo bluzi au taarabu asilia. Muziki kama wa dansi, house, hot fanky, pop na ngoma za kitamaduni inahusisha kuchezesha misuli mingi mwilini hivyo kumfanya mcheza dansi kuwa na misuli imara.

Zoezi linaloshika namba tatu huwa ni kukimbia, mwanadamu anapokimbia uhusisha misuli ya mwili mzima. Ukiwatazama wanariadha wengi duniani, wana miili imara yenye misuli iliyojijenga vyema.

Michezo kama sarakasi, karate, soka, mpira wa kikapu, mchezo wa ragga yenyewe ndio inashika namba nne kwa kujenga misuli na kumfanya mwanadamu kuwa imara kimwili na kiafya.

Zoezi namba tano huwa ni kutembea nako ni mojawapo ya zoezi ambalo linahusisha misuli mingi ya mwilini, kutembea umbali mrefu ndiko haswa kunakojenga mwili.

Mtindo huu ndio unaowafaa watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kujenga mwili wenye afya njema, utahitajika kutembea umbali wa wastani huku ukitembea na kutupa mwili na mikono ili kuishughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi ndio chanzo cha kuwa na mwili imara wenye afya njema hivyo kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ikiwamo kisukari cha aina ya pili, maradhi ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Jipangie ratiba ya kufanya mazoezi haya kwani mazoezi ni afya, ni vizuri pia kabla ya kujiingiza katika mazoezi haya uwe umefanya uchunguzi wa afya yako kwa ujumla.

Bado nasisitiza kwamba jipime uzito na ufahamu ni aina gani ya mazoezi unayotaka kufanya na usifanye mazoezi magumu kiasi cha kukuhatarishia afya yako..     

Monday, January 8, 2018

Liver pool walihifadhi fedha kwenye ‘kibubu’ katika Usajili Virgil Van Dijk

 

Maisha hayakuwahi kuwa hivi, hatukuwahi kuyazoea katika hali hii, hatukufikiria hii siku itakuja, ni jambo geni kwenye mboni za macho yetu na wala hakuna aliyetarajia hili jambo kulitokea lakini wote tunalishuhudia na pengine ni kheri kama tukishuhudia historia ambao tunaweza kuja kusimulia vizazi vyetu vijavyo. Hizi ni fikra ndani ya shabiki na mfuasi yeyote Yule wa ligi pendwa duniani ya England.

Hakuna ambaye hashangazwi na kasi waliyokuwa nayo klabu ya Manchester City, hatokuwepo ambaye atashangaa ubora aliozalisha Pep Guardiola msimu huu na inawezekana wasioamini katika uwezo wake wakasema anabahatisha lakini bado wote tutakuwa tumebaki kwenye neno moja tu, “mshangao wa msimu huu”.

Wakati tukiwa tunastaajabu ya Mussa aliyekuwepo pale Manchester City anayejaribu kuivusha klabu hiyo kwa kasi kwenye bahari ya shamu, huku tunaona mapya ya Jurgen Klopp. Naam moja ya makocha bora kabisa kwenye Ligi Kuu England na ambaye ameifanya Liverpool irejee kwenye kilele chake cha ushindani na walau kuwa na wachezaji wenye ushindani na kuvutia majina makubwa tofauti na ilivyokuwa chini ya Roy Hodgson, kisha Kenny Dalglish na baadaye, Brendan Rodgers ambaye alikuwa na msimu bora wa Suarez kisha mingine ikaenda kombo.

Klopp amerejesha soka linalovutia ndani ya Liverpool, amerejesha ubora wa wachezaji wengi waliionekana wa kawaida chini ya makocha wengine na kuwafanya waonekane wanaofaa. Bahati nzuri ni kuwa aliweza kufanya kazi chini ya bajeti ndogo ya kutokusajili kwa zaidi ya Pauni40milioni na akapata wachezaji bora wenye majina ya Matip, Mane, Wjinaldum pamoja na Salah kisha Chamberlain anayeonekana anakuja vyema kwa sasa.

Akiwa ametulia kabisa kwenye nafasi bora tangu alipofika Liverpool na akiendelea kuleta mabadiliko kwenye kikosi ikiwemo kuwa na safu ya ushambuliaji inayoonekana kuwa hatari zaidi kwenye Ligi Kuu England na moja ya safu bora barani Ulaya nyuma ya Paris St Germain, Klopp kuna jambo moja alilohubiri msimu wa mwaka 2016-2017.

Akiwa ameketi kwenye kiti chake, mbele ya waandishi wa habari alikuwa anaponda kiwango cha fedha alizonunuliwa nazo mchezaji Paul Pogba.

Klopp alipinga hoja ya kusajili mchezaji kwa kiwango kinachokaribia Pauni 100milioni, huku akiweka bayana kuwa apo akiumia basi inakuwa maumivu kwa timu nzima.

Yeye aliamini kuwa mafanikio yanakuja kwa kuunganisha wachezaji pamoja lakini hawezi kwenda kufanya manunuzi makubwa ya wachezaji kwani sivyo alivyo na iwapo klabu vingine vinafanya basi yeye hana tatizo lakini haamini kama ndicho ambacho soka linahitaji na katika hili hakutofautiana kwa kiwango kikubwa na Wenger kwa sababu wote ni wachumi na walitazama thamani ya fedha ya kizamani. Hawakukumbuka kuwa kwa sasa soko limewewuka na bei ya kondoo wananunuliwa kuku.Wakati Wenger akianza kubadilika tabia kwa Alexander Lacazette na Pauni50milioni alizotoa, ilikuwa inasubiriwa sauti ya Klopp ipae mawinguni kwa kiwango kikubwa cha fedha ambacho angetoa. Inawezekana alianza kuonyesha makucha kwa kumsajili Ox Chamberlain kwa kiwango cha Pauni35milioni ambazo zingefika 40 kutokana na kiwango chake lakini bado haikuwa “story” kubwa hadi hapo ilipofika Desemba 27, 2017.

Liverpool ilikuwa inavunja rekodi ya usajili wa dunia kwa beki. Walikuwa wanatoa fedha ambazo Mourinho anaziita za mastraika kwa beki wa kati. Pauni 75milioni sawa na Lukaku zilikuwa zinatoka kwenda Southampton kumsajili beki Virgil van Dijk, ajabu lakini ni kweli aliyemsajili ni Jurgen Klopp. Ni wazi sio thamani inayomstahili mchezaji huyu, lakini swali lingine ni kuwa kwanini Liverpool wapate kifua cha kusajili mchezaji kwa kiwango kikubwa hivi cha fedha? Kwenye uchumi kuna somo zuri ambalo nikiwa pale Umbwe, mwalimu mmoja maarfu wa Uchumi anayefahamika kama Mafikiri aliwahi kulitoa. Mafikiri alikuwa anatueleza “Value For Money” yaani kwa tafsiri thamani fedha.

Thamani ya fedha hutizamwa kulingana na uchumi inakofanyia manunuzi lakini pia ikilinganishwa na bidhaa inayonunuliwa na kiwango cha mtoaji katika manunuzi hayo. Kwa Liverpool wamehifadhi fedha hii kwa kipindi kirefu kuliko klabu nyingine zote. Wakati Manchester United ikisuka kikosi chake kwa kutoa Pauni 90 milioni kwa Pogba, 75+ kwa Lukaku, 40+ kwa Matic na fedha nyingi kwa wachezaji kama Bailly, Lindelof na wengine, Liverpool haikuwa inamwaga fedha hizi. Manchester City wao walianza kitambo kwa Kevin De Bryune, Raheem Sterling, Mangala mpaka leo kwa Mendy, Kyle Walker na John Stones ambao wote walikaribia au kuvuka Pauni50 milioni kwenye manunuzi.

Na hata wakati Chelsea wakitoa zaidi ya Pauni 60milioni kwa Morata, 40 kwa Bakayoko na 35 kwa Rudiger na ile milioni 40 kumrejesha David Luiz wao Liverpool hawakuwa na misuli hii. Bahati mbaya hata wakati Arsenal ikivunja rekodi kwa Lacazette na Tottenham wakitoa karibu paundi milioni 45 kwa beki Davinson Sanchez, Liverpool bado walikuwa wanatoa macho.

Lakini ni wazi uongozi wa Fenway Group ulimtaka Klopp kufanya usajili na kutumia vyema wachezaji wa gharama ya kawaida ili waje kumwaga fedha kwa wachezaji wakiwa wametulia. Ndio maana sio ajabu kuona thamani za wachezaji wa Liverpool kuanzia eneo la kiungo mpaka ushambuliaji likiwa halina Paundi40milioni hata moja.

Baada ya kuwa na safu bora ya ushambuliaji kwa gharama kiduchu, Roberto Firmino (£29million), Sadio Mane (£30million), Mohamed Salah (£35 million), Chamberlain (35 million),

Coutinho (8 milioni), Liverpool walitaka kupata kupaza sauti kuwa wanaweza kufanya makubwa kwenye soko la usajili. Van Djik ni mchezaji mwenye asiyezidi thamani ya Pauni 60milioni, lakini kwa sababu Barcelona, Manchester City na Chelsea tayari zilishamtizama Liverpool walitakiwa wapige kifua kumpata.

Na kumpata huku kulimaanisha walipe fedha ambayo hawa wengine wangekaa kando. Haya yalikuwa mahesabu sahihi ya Liverpool, lakini yanakuja baada ya uwekezaji wa uvumulivu kupata hicho walichonacho kwenye safu ya ushambuliaji kwa bei nafuu ya mabeki. Hii inawapa uhuru wa kuifanya thamani ya fedha waliyomnunulia Van Djik kuwa na maana. Kwa lugha nyingine ni kuwa Liverpool walisajili kwenye eneo la ushambuliaji kwa fedha kiduchu huku nyingine wakitunza kwenye “kibubu” mpaka zijae ndipo wazitumie pale itakapowalazimu.

Wakiwa wanakaribia kumpoteza Coutinho, ilikuwa ni lazima wafanya jambo ili huyu aweze kujiuliza mara mbili kama klabu hii ina maono ya ubingwa.

Wameruhusu zaidi ya mabao 23 mpaka sasa, mengi zaidi kwa timu zilizokuwa nafasi 5 za juu hivyo walihitaji beki. Hii itawasaidia pia kupata wachezaji wengine wazuri, hasa kwa sababu wanaye Naby Keita atakayekuja msimu ujao pia.

Hii itawafanya wachezaji waliokuwa na mpango wa kuondoka kuvutiwa na “project” hii huku wakiamini mipango ya timu yao. “Value for Money” kwa Liverpool hapa imekubali lakini kwa washabiki haiwezi kuonekana. Fedha hii waliituzna kwa muda mrefu, si unaona Salah wa bei nafuu ndo mchezaji bora EPL?     

Monday, January 8, 2018

Hakika Mandawa ni sawa na nabii asiyekubalika kwao

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Ule usemi wa nabii hakubaliki kwao unaweza kutumika kwa mshambuliaji wa Kitanzania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana inayocheza Ligi Kuu ya nchi hiyo.

BDF XI iliwahi kucheza na Simba na Yanga katika mashindano ya klabu Afrika kwa nyakati tofauti na timu hizo kushinda mechi zote.

Kwa upande mwingine Mandawa alionekana kama mwisho wake umefika baada ya kufanya vizuri akiwa na Kagera Sugar, Mwadui na Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti amekuwa moto wa kuotea mbali nchini Botswana.

Mbali na kuvumbua kwetu vipaji vya wachezaji wa Kitanzania wanaofanya vizuri nje ya mipaka ya Tanzania na hata wale wanaochipukia kwenye vituo mbalimbali vya soka pia tupo mstari wambele kufuatilia na hata nyota wa Kitanzania ambao wanafahamika na wanafanya vizuri nje ya nchi kama ilivyo kwa Mandawa.

Wiki iliyopita, tulikuwa na mchezaji kinda wa Kitanzania, Julian Amani (18) anayechipukia kwenye kituo cha Kuala Lumpur Youth Soccer (KLYS) nchini Malaysia ambako alizungumzia anavyotamani kufanya vizuri kwenye soka la ushindani hapo baadaye.

Tukiachana na Julian, Mandawa anayetamba nchini Botswana na BDF XI anasema hana papara za kuitwa timu ya Taifa japo shauku yake ni kuendelea kukichezea kikosi hicho cha Salum Mayanga.

Mandawa ambaye amekuwa akitegemewa kwenye kikosi hicho, amefunga jumla ya mabao sita na kutengeneza mengine matatu katika michezo 13.

“Uzuri ninapata muda mzuri wa kucheza hivyo maendeleo yangu muhimu yatakuwa yanapatikana,ninachoomba ni uzima ili niendelee kuonyesha,najiona nina nguvu za kuendelea kupambana na kinachonipo moyo zaidi ni namna ambavyo nina aminika kwenye kikosi changu.

“Huku napewa heshima yangu kama ilivyo kwa Tanzania ambapo kumekuwa na utamaduni wa kumpa heshima yake mchezaji wa kigeni,mwanzoni nilijiuliza kipindi chote nilikuwa wapi maana nilijiona ni kama nilitakiwa kujiunga nao miaka kadhaa nyuma.

“Jamaa walikuwa wakinifuatilia kwa kipindi kirefu,haikuwa ghafla wao kunisajili,inaweza kuwa imechukua hata zaidi ya miaka miwili,” anasema Mandawa.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo, aliweka wazi kuwa kubadilisha kwake mazingira kumemfanya kurudi kwenye makali yake ya ufungaji.

“Ni kweli mazingira ya kuwa ugenini yamenifanya kujituma zaidi,itakuwa aibu timu kumlipa mshahara mchezaji mvivu na katika nafasi yangu ili watu wanikubali ni lazima niwe na funga mabao.

“Muda wote ambao nimekuwa kule sijapata tatizo lolote,Wabotswana hawana tofauti sana wa Watanzania,”amesema mshambuliaji huyo ambaye kabla ya kuondoka Mtibwa aliifungia mabao nane kwenye msimu wake wa mwisho.

Akizungumzia safari yake ya kutua kwenye timu hiyo ilivyokua, Mandawa anasema hesabu zake zilikuwa ni kujiunga na Township Rollers lakini mara baada ya kufanya majaribio hakufanikiwa kupata nafasi ya kujiunga na timu hiyo.

“Nilienda Botswana kufanya majaribio lakini sikufanikiwa kujiunga na timu ambavyo niliilenga ila ilitokea hii timu ninayoichezea na tukafanya makubaliano ya kujiunga nayo,hawakuwa na shida kabisa juu ya uwezo wangu.

“Muda umeongea na uzuri wa mpira kila kitu kinaonekana uwanjani,mabosi wamekuwa wakifurahishwa na uwezo wangu.Siwezi kusema kuwa ile timu ya mwanzo kama ikinihitaji sintojiunga nayo tena itategemeana na mazungumzo yatakavyokuwa kuwa baina yao.

“Nina mkataba bado na BDF XI hivyo siwezi kufanya makubaliano ya aina yoyote na timu yoyote,ukweli ni kwamba nina furaha na pia nina maelewano mazuri na wachezaji,viongozi wa timu yangu haitokuwa rahisi kuondoka kwa sababu nawaheshimu waajiri wangu,” amesema Mandawa.

Timu hiyo ya Mandawa imetwaa kombe la ligi kuu nchini humo mara saba ambapo ni kwenye miaka ya 1981, 1988, 1989, 1991, 1997, 2002, 2004 na kwa upande wa kombe lao la Chalenji ni mara tatu katika miaka ya 1989, 1998 na 2004.

Hata hivyo Mandawa ameweka wazi kuwa lengo lake ni kuisaidia timu yake hiyo ili kuchukua ubingwa wa ligi ambo utawapa nafasafi ya kushiriki mashindano ya Kimataifa msimu ujao.

BDF XI imewahi kushiri mara mbili kwenye Ligi ya mabingwa Afrika kwenye miaka ya 1998 na 2012 ambapo waliishia kwenye hatua za awali na katika shirikisho na kwenyewe ni mara mbili tangu timu hiyo ianzishwe 1978.

“Hakuna kinachoshindikana.Mkazo uliopo unaweza kutusaidia kwa sababu bado tupo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo,” amesema.     

Monday, January 8, 2018

Kufunga bao kunakotengeneza kilio kwa mchezaji

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Mario Balotel aliwahi kuibuka na staili yake ya kushangilia baada ya kufunga bao akiwaonyesha mashabiki maandishi aliyoandika kifuani kwake ‘Why Always Me’ hiyo ilikuwa staili yake lakini akitumia njia hiyo pia kufikisha ujumbe waswahili wanasema ‘meseji senti’.

Kila mchezaji ana staili yake ya kushangilia pale anapofunga hasa kwenye soka, wapo wanaoshangilia kwa mtindo wa kujisareresha kkwa magoti, lakini viwanja vya wenzetu, wapo wanaovua jezi, lakini pia wapo wale wanaoshangilia na wakipongezwa, humwaga machozi.

Staili hiyo ya kushangilia huku mfungaji akilia machozi imekuwa ikiwafikirisha wengi, wapo wanaoamini mchezaji anajifanyisha, wapo wanaomchukulia kuwa mzalendo kupitiliza kwenye timu yake lakini kumbe sivyo. Baadhi ya wachezaji, makocha, wanasaikolojia wamezungumzia hali hiyo kuwa inasababishwa na mambo mengi. Nini kinaliza wachezaji? Siri ya kilio hicho hii hapa.

Amiss Tambwe

Straika wa Yanga, Raia wa Burundi anasema hali ya mchezaji kushangilia bao hadi kumwaga machozi akimtolea mfano winga wa Simba, Shiza Kichuya kuwa aliwahi kumshuhudia akilia baada ya kufunga.

“Binafsi sijawahi kushangilia hadi nikalia, lakini nimewahi kumshuhudia Kichuya akilia baada ya kutufunga kwenye mechi ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 Simba wakisawazisha kwa mpira wa kona uliopigwa na yeye mwenyewe,” anasimulia Tambwe.

Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Burundi anasema kitendo cha mchezaji kufunga bao na kisha kuanza kushangilia huku akilia kinatokana na kuwa katika hali ya furaha iliyopitiliza, hasa kwa kutotarajia kama kitu hicho kingetokea.

“Lakini pia unaweza kupewa nafasi na kocha, lakini mashabiki wasikuamini kabisa na ghafla umeingia kwenye mechi ikakukubali na kujikuta umefunga bao muhimu tena mechi yenye ushindani kweli kweli na goli lako ndiyo likawapa ubingwa hivyo unajikuta unalia bila kutarajia.

Shiza Kichuya

Winga huyu wa Simba ndiye ametajwa na Tambwe kwamba aliwahi kulia baada ya kuisawazishia timu yake dakika za lala salama na kuifanya Simba kutoka sare ya bao 1-1, mwenyewe anasema hakumbuki kama alishangilia hadi kulia machozi kwenye mchezo huo lakini kitendo cha mchezaji kushangilia hadi kulia machozi kinatokana na namna alivyolichukulia goli alilofunga.

“Kuna mechi zinakuwa ngumu sana, sasa inapotokea labda wewe ni mchezaji ambaye huaminiki au hupewi nafasi lakini kwenye mechi hiyo kocha amekupanga na ukafanya vizuri tena magoli au goli lako ndilo likaisaidia timu yako kutwaa ubingwa ile furaha unayokuwa nayo kama una machozi ya karibu lazima ulie,” anasema Kichuya.

Peter Tino

Mwenyewe anapenda kujiita staa ambaye aling’ara akiwa mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars, Peter Tino anasema haijawahi kumtokea akashangilia goli hadi kulia lakini kulia baada ya kufungwa ni kitu cha kawaida.

“Unajua yale mapenzi unayokuwa nayo kwenye timu ndiyo yanasababisha mtu alie aidha kwa furaha au kwa huzuni, sina kumbukumbu kama kuna mchezaji mwenzangu enzi nacheza aliwahi kulia baada ya kufunga.

“Ila kulia baada ya kufungwa ilikuwa ni kitu cha kawaida, unajua zamani ulikuwa ukipewa heshima ya kuvaa jezi ya timu ya taifa, ile nembo unayoivaa inakupa uchungu kweli kweli hata jezi ya Simba na Yanga, ilikuwa ina thamani kubwa ambayo ikitokea umefungwa unajikuta tu unalia.

“Binafsi niliwahi kulia uwanjani, sio kwa kufunga bao lakini kwa kufungwa, kinachokufanya ulie ni ile thamani ya jezi ya timu yako, lakini wachezaji wetu wa siku hizi Kibongo bongo hata wakifungwa wao wanacheka tu, hawaumwi na kufungwa,” anasema Peter Tino.

Mbaraka Yusufu

Straika wa Azam FC aliyetokea Kagera Sugar anasema: “Kushangilia hadi kulia ni kitu cha kawaida kwa mchezaji hasa kutokana na mapenzi yake na timu, kwa mfungaji kulia kwanza ni furaha iliyopitiliza.

“Kitu kingine ni kutokana na alivyoisaidia timu yako katika mchezo huo kupata matokeo na huwa inatokea sana kwenye mechi ngumu na zenye ushindani au mchezo wa fainali, unapambana na kupata bao ukiamini hawa hawawezi kurudisha na kila mmoja anakupongeza.”

Wasikie makocha

Kaimu kocha Mkuu wa Simba, Djuma Masoud anasema kuna vitu vingi ambavyo vinasababisha mchezaji kufunga bao, kushangilia hadi kulia na kutoa machozi.

“Inaweza kuwa mchezaji huyo amepangwa kuchezwa lakini kishakashaka kila mtu hamuamini ila kocha akamtia moyo na kuwambia acheze anaweza, sasa ikitokea amefunga akikumbuka hayo, mwingine anajikuta analia kwamba kumbe anaweza,” anasema Masoud.

Mrage Kabange kocha wa Njombe Mji anasema katika historia yake ya soka amewashuhudia wachezaji wengi tu wakishangilia huku wakilia machozi.

“Wengi naamini huwa kuna kumbukumbu inawajia ndiyo sababu wanajikuta wakilia machozi baada ya kufunga, pengine hajawahi kufunga muda mrefu au ndiyo bao lake la kwanza katika maisha yake ya soka hivyo anaona kama ametoa gundu,” alisema Kabange.

Zuber Katwila kocha mkuu wa Mtibwa Sugar anasema kwa hapa nchini wengi wanashangilia kwa staili ya kulia kama utani lakini kwa wale ambao huwa wanalia kweli kweli wanapofunga huwa wana onyesha furaha iliyopitiliza.

“Sijawahi kumuona mchezaji akilia kwelikweli hapa nyumbani, wengi wanafanya kama utani wanaweka mikono usoni kama ishara ya kujifuta machozi, wale wanaolia kweli uwa wanafurahi kupitiliza.

“Unajua kuna wachezaji anasema nikifunga nitafanya kitu fulani, au anaenda uwanjani na fulana kavalia ndani imeandikwa hivyo anapambana ili afunge afunue fulana maandishi yaonekane, kila mtu anakuwa na malengo yake hivyo ikitokea amefanikiwa wengine ndiyo inawafanya kulia machozi.

Kauli ya wanasaikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Modesta Kimonga ambaye ni mwalimu wa Chuo cha Ualimu Patandi tawi la Sahare, Tanga anasema mchezaji anapokuwa akicheza uwanjani kuna homoni inafanya kazi sana ambayo ndiyo husababisha wengine kuwa na hasira.

“Homoni hiyo huwasababishia wengi wao ‘ku-react’ kwa namna ambazo sio nzuri, zile shuluba ambazo wanapata uwanjani inapotokea wameshinda ndiyo baadhi yao hujikuta wakishangilia hadi kulia,” anasema Kimonga.

Dk Frank Masao ambaye pia ni mtaalamu wa saikolojia Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema kinachosababisha baadhi ya wachezaji kushangilia hadi kulia machozi ni furaha ambayo inaendana na kumbukumbu ya tukio fulani ndani ya akili yake.

“Sio wachezaji tu, kuna watu wa aina hiyo pale anapopata kitu ambacho hawakukitarajia hulia. Msichana nafahamu kuwa anavalishwa pete ya uchumba, lakini atalia kitendo kikifanyika, kwmaba haamini tukio lile.

“Kwa mchezaji huwa anakumbuka shuluba alizopitia sasa pale inapotokea amefunga goli baadhi yao huangua kilio,” anasema.

Mtaalamu mwingine wa saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chriss Mauki anasema furaha iliyopitiliza ndiyo inasababisha mchezaji kutokewa na hali ya kushangilia hadi kulia.     

Monday, January 8, 2018

Ndoto ya Coutinho yatimia, atua Barca

 

Usajili wakati wa dirisha kubwa majira ya joto, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alikuwa mkali kwa Phillipe Coutinho. Alikuwa hataki mtu amsogelee hata aje na fungu kiasi gani.

Barcelona wakasema anatania huyu, wakamletea fedha Pauni 50mil akatataa

wakapanda hadi Pauni zaidi ya 80mil akagoma, wakaenda Pauni130m akagoma na hakumruhusu.

Ilimuumiza sana Coutinho, lakini akawa na akili ya kiutu uzima, akasema siku hazigandi. Akacheza mpira na hata kufunga mabao muhimu kwa timu yake.

Waandishi wa habari hawakuacha kumchokonoa, wakamuuliza, anaona vipi hilo la kucheza na alitaka kuondoka, akasema yeye ni Liverpool na anacheza mpira Liverpool.

Alhamisi iliyopita, usiku sasa, kabla ya mechi ya Everton Kombe la FA akasema kama kucheza, atacheza mechi yake ya mwisho kisha anasepa zake Barcelona.

Barcelona wakaja jumla. Liverpool waliwapandishia dau hadi kufikia Pauni 140mil, wanaume walikuwa wamedhamiria kweli. Wakaja na kianzio cha Pauni107mil kwa ajili ya kuinasa saini yake.

Alipohojiwa juzi akiwa mwenye furaha, Coutinho alisema: “Nimeshaaga washkaji zangu, marafiki wote wanafahamu naondoka.

Coutinho alitarajiwa kutambulishwa kwenye mchezo kati ya timu yake mpya na Levante kabla ya kufanya ziara ya kwenda Falme za Kiarabu Abu Dhabi.

Kiungo Coutinho kwenda Hispania, kutamfanya kuwa mchezaji wa pili ghali baada ya Neymar lakini pia ni rekodi kwa Liverpool. Liverpool ilipoipiga Everton 2-1 Kombe la FA kwenye Uwnaja wa Anfield, Coutinho aliwekwa benchi huku Virgil van Dijk akicheza kwa mara ya kwanza baada ya kumchukua kwa Pauni75m akitokea Southampton.     

Monday, December 11, 2017

MO aanza na KIUNGO mzambia

 

By Thobias Sebastian, Mwananchi

Kama ulidhani Mohamed Dewji “MO” anatania, basi umeula wa chuya; ameliamsha dude.

Juzi Mo alitangazwa kuwa mshindi wa zabuni ya hisa za kuwa mmiliki mwenza wa klabu ya Simba akimiliki asilimia 50 na hivyo kuwa na haki ya kuingiza wajumbe saba kati ya 14 kwenye bodi ya uendeshaji klabu. Saba wengine wanawakilisha wanachama. Hiyo ndiyo Simba.

MO anataka kuifanya Simba kuwa klabu kubwa, tajiri na yenye kukusanya mataji. Wanaokusanya mataji ni wachezaji na Mo ameanza kwa kumtazama Jonas Sakuhawa kutoka Zambia.

Simba mwakani watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukosekana kwa takriban miaka mitano baada ya mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa 2012.

Lakini msimu huu wameanza kujipanga mapema kwa kusajili wachezaji ili kuboresha kikosi chao ambacho kitakwenda kwenye michuano hiyo kwa kutaka kusajili wachezaji wa maana ambao wanatajwa.

Majaribio

Simba imemleta winga Mzambia Jonas Sakuhawa ambaye yupo katika majaribio kwenye kikosi cha Joseph Omog ambacho hakijaonja ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka mitano.

Sakuhawa alizaliwa Julai 22, 1983 Kafue Zambia anacheza kama mshambuliaji wa kati au pembeni na amecheza timu kubwa Afrika na hata Ulaya pia.

Alianzia klabu ya Zesco United 2006-09, baadaye alikwenda Lorient ya Ufaransa ambako alicheza mechi 14 kati ya 2009-10 bila kufunga na mwisho wa msimu huo alikwenda kwa mkopo Le Havre pia ya Ufaransa.

Alijiunga na Al-Merreikh ya Sudan msimu wa 2011-12, kabla ya kutimkia zake TP Mazembe msimu wa 2013-14 na mwaka 2015 alirudi kwao Zambia na kujiunga na Zesco na sasa ametua Simba kwa majaribio.

Mkali wa mabao

Akiwa kikosi cha Al-Merreikh alicheza mechi 33 na kufunga magoli 22 na alipokuwa TP Mazembe alicheza mechi 29 na kufunga magoli 14. Kwa ujumla amecheza mechi 62 na kufunga magoli 36.

Sakuhawa ana wastani wa kufunga goli kila baada ya mechi mbili ambazo amecheza kwahiyo kama atakuwa na uwezo kama huo anaweza kuisaidia Simba yenye shida ya wafungaji.

Anavyocheza

Tangu atue Simba takriban wiki moja iliyopita, Sakuhawa amefanya mazoezi chini ya kocha msaidizi Mrundi Masoud Djuma aliyeshika nafasi ya Omog ambaye hayupo.

Muda wote aliokuwepo hapa nchini, Sakuhawa amefanya mazoezi vizuri na Simba kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini na alikuwa anaonyesha ana kitu cha ziada.

Sakuhawa amefanya mazoezi na Simba siku tano lakini ameonyesha utulivu, umakini uzoefu na amekuwa akifunga mara kwa mara katika mazoezi ya kufunga ambayo anapewa na Djuma.

Kiwanja chamzingua

Sakuhawa anasema amekuja moja ya timu kubwa barani Afrika kwa kuwa alikuwa akiisikia Simba. Lakini amekutana na changamoto ya uwanja ambao wanatumia kufanyia mazoezi. “Uwanja si mzuri hasa eneo la kucheza kama huko ambako nimetoka, lakini nitajitahidi kuonyesha kile ambacho ninacho katika siku zote ambazo nitakuwa nafanya majaribio hapa na kocha naimani anaweza kuona uwezo wangu licha ya changamoto hiyo,” anasema.

“Kama nikipata nafasi ya kucheza katika kiwanja ambacho kinaeneo zuri la kuchezea ninaimani nitaonyesha zaidi uwezo niliokuwa nao,” aliongezea Sakuhawa ambaye yuko katika wiki ya mwisho ya majaribio yake.

Liuzio awashtua Simba

Straika wa Simba Juma Liuzio, ambaye amekuwa na nafasi finyu ya kucheza mara kwa mara katika kikosi hicho msimu huu, alisema Sakuhawa ni mchezaji mzuri ambaye alishawahi kucheza naye Zesco United.

Liuzio anasema Sakuhawa ni mzoefu na alikuwa akicheza vizuri katika kikosi cha Zesco ambacho kilikuwa chini ya kocha George Lwandamina ambaye kwa sasa anainoa Yanga.

“Sakuhawa alikuwepo wakati Zesco inafika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na Mamelod Sundowns, kwa hiyo si mchezaji wa kumbeza ingawa sijamuona siku nyingi tangu mimi nilipoondoka Zambia,” anasema Liuzio.

Monday, December 11, 2017

Eliuter: Viongozi Friends waliniwekea mizengwe

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Mshambuliaji Eliuter Mpepo amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Tanzania Prisons na ameonekana kutolewa macho na vigogo wa soka kutokana na uwezo wake katika ushambuliaji.

Mpepo (20) ameichezea Prisons mechi saba na kufunga mabao matatu, likiwemo bao maarufu alilomfunga kipa wa Yanga, Youth Rostand wakati timu hizo zilipofungana bao 1-1.

Kabla ya kutua Tanzania Prisons, mshambuliaji huyo amezichezea Kinyerezi United, Friends Rangers na Mbeya Kwanza.

Hata hivyo, Mpepo anasema hawezi kusahau mazingira aliyopitia akiwa Friends Rangers.

“Ulifika wakati nikaanza kuwaza kuachana na soka. Nilivyojiunga na Friends kuna baadhi ya viongozi walikuwa hawanipendi kabisa hivyo walinitengenezea zengwe kwa hata kupandikiza chuki kwa mashabiki,” anasema Mpepo..

“Kwa kweli walifanikiwa maana kila nilipokuwa ninaingia uwanjani nilikuwa ninazomewa. Nilishindwa kumudu hali ya kuzomewa hadi ikaanza kuathiri uwezo wangu wa kawaida uwanjani. Nilipiga moyo konde na kuushinda ule mtiani.”

Pamoja na kuonekana kuwa mmoja wa washambuliaji hatari kwa sasa, Mpepo anasema hana tatizo wala mapenzi kati ya Simba na Yanga kama ukitokea upande wowote kumwitaji atakuwa tayari kuusikiliza.

“Ninafanya kazi popote bila ya kuhofia chochote,” anasema.

“Ninaweza kucheza Simba na hata Yanga kama wakinihitaji. Ninamshukuru sana kocha wangu wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohammed kwa kuniamini na kunipa nafasi.”

Mbali na kocha wake, Mpepo aliwataja watu wengine ambao wamechangia kukua kwake kisoka ambao ni Kivunje, Olenjo, Mwenjala na Henry Mzozo.

“Kivunje alinifundisha mpira Kinyerezi pia nilikuwa nikipewa sana moyo wakati napitia magumu na familia ya Mr Mwambete, Nguvumali, Shiraz Batchu na kaka yangu Justin, bila hao ingekuwa ngumu kufika hapa nilipo,” anasema.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji, alisema kama si soka anaamini kuwa kazi ya ununuzi na ugavi ingemtoa kimaisha kwa sababu ni kazi ambayo ameisomea.

Monday, December 11, 2017

Msuva, utafika tu muda wa WEWE kujidai

 

Mchana mmoja kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa picha zikimwonyesha Saimon Msuva akiwa eneo la hoteli ya kisasa. Msuva anaonekana amevalia suti nadhifu mithili ya kijana anayeelekea kutoa posa kwenye nyumba ya kifalme.

Bandiko hili liliambatana na maneno kuwa Msuva alikuwa kwenye harakati za majaribio na klabu moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania yaani La Liga.

Haikuteka akili yangu kwa kiasi kikubwa kwa sababu mawazo yangu yaliniambia pengine ilikuwa mapema kupita kiasi kwa suala lile kutokea huku nikiamini Msuva alikuwa bado na muda wa kufanya makubwa na klabu yake mpya ya Difaa El Jadidi, hivyo isingeweza kumruhusu mapema kiasi hiki kuondoka wakati akiwa ndio kwanza ameanza kuingia kwenye mfumo wao.

Bahati nzuri sikuwa mbali na taarifa zinazomuhusu hivyo nikafanya jitihada kupata ukweli wa mambo na kupitia vyanzo vinavyoaminika, kijana huyu wa Kitanzania ambaye alikacha fani ya “Mosses Iyobo wa WCB” na kuamua kutumia miguu yake kutafuta unga, alikanusha taarifa hiyo na kuweka bayana kuwa bado alikuwa na kazi ya kufanya pale Morocco. Ndio alikuwa bado na kazi ya kumfanya kocha Abderrahim Taleb kuamini katika miguu yake zaidi ya ilivyokuwa kawaida.

Ndani ya kikosi cha El Jadidi ama El Jadida kama wengine wanavyoita kutokana na eneo inapotokea, Msuva anasimama kama moja ya wachezaji muhimu kwa sasa, jambo ambalo hakuna aliyetarajia lingetokea kwa haraka kiasi hiki. Ndani ya ubongo wowote unaowaza vyema basi utagundua kuwa kuna vipaji vingi Tanzania ambavyo iwapo vikipata macho basi vitaona malisho mengi na ardhi zenye rutuba nje ya hii inayoitwa Tanzania.

Safari ya Msuva ambayo wengi hatutaki iwe na kugota, inatakiwa iwe mfano kwa wengi ambao walihisi Mbwana Samatta alikuwa na “bahati ya maisha.”

Kwenye karatasi yoyote ambayo utaandika vikosi ama majina ya wachezaji wa Tanzania, ni wazi kuwa utapata majina kama Ibrahim Ajib, Mo Ibrahim, Said Ndemla, Shaban Idd, Ramadhani Singano, Shiza Kichuya, Raphael Daudi na wengine wengi kuwa wana vipaji vya asili kuliko Msuva, lakini mwenzao huyu ana Baraka moja ambayo hawa wameshindwa kuishughulikia nayo; kujituma na kufahamu wanachotaka.

Inawezekana katika kundi hili bado wengi wana nafasi ya kufanya makubwa, lakini maisha ya Msuva ndani ya Ligi Kuu ya Vodacom na upinzani aliowahi kupata inakupa picha ni moyo wa aina ipi aliokuwa nao.

Kwenye michezo na hata maisha si kila binadamu huzaliwa na hulka ya kuwa mshindi au kuwa na roho ngumu na ndio maana si ajabu kwenye mpira wa kikapu kusikia kauli inayomsema Lebron James kuwa hakuzaliwa na roho ya kikatili ndani ya uwanja kama Michael Jordan au Kobe Bryant ambao waliweza kusaka ushindi vyovyote vile.

Lebron ilibidi ajifunze hili kwa kuishi jirani na washindi kama Dwayne Wade alipokwenda Miami Heat. Hivyo inawezakana pia Ajib asiwe na roho ya Msuva, lakini akawa na nafasi ya kujifunza. Swali pekee linabaki kuwa yupo tayari?

Moyoni mwangu na roho yangu ya Kizalendo ninaona kabisa maisha yetu kwa maana ya idadi na majaaliwa ya vipaji yapo katika sehemu na mlengo mzuri. Wachezaji wameanza kupata tamaa na msukumo wa kufika mbali na kufanya makubwa.

Huku kukiwa na taarifa za Himid Mao kutakiwa na Afrika Kusini ambako ataungana na Abdi Banda, idadi ya “maprofeshino” itapendeza zaidi pale majina ya Said Ndemla na Kichuya yakitoka kama inavyoendelea kutajwa ili kuendelea kufumbua macho ya wachezaji kama Mbaraka Yusuph ambaye ana nukuu ya kusikitisha ya kutoona umuhimu wa ligi za nje.

Nikiwa katika furaha na nikiwa na kusudio la kuonyesha umuhimu wa kuendelea “kuwafungulia njia” vijana wetu pale tunapopata nafasi, mikono yangu ilikuwa kwenye mtandao na nilikuwa natazama namna ligi ya Morocco inavyoendelea, Simon Msuva amenifanya niwe shabiki wao.

Hakuna sababu ya kuchambua umuhimu wa Mohamed Salah ndani ya Liverpool bila kutaka kufahamu ni kwanini Msuva ameanza kufanya makubwa kila akiitwa Taifa Stars.

Mpaka makala haya yanaenda kuchapishwa, kikosi anachochezea Msuva cha Difaa El Jadida kilikuwa kwenye nafasi ya tatu Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kwa jina la Botola.

Ikiwa na pointi 14, El Jadida ilikuwa imefunga mabao 14, huku matano yakiwa yamefungwa na mchezaji wao Bilal El Megri na Msuva akiwa miongoni mwa wachezaji watatu waliofunga mabao mawili kila mmoja.

Kwa tafsiri nyingine ni kuwa Msuva ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemewa katika kikosi cha kocha Abderrahim Talib.

Ukitazama namna ya mgawanyo wa mabao mpaka hapo maana yake ni kuwa kikosi chao kina mfumo ambao ni “free flowing” yaani mfumo huru ambao unatoa nafasi kwa wachezaji wengi kufunga mabao mengi.

Mfumo huu unarahisisha wachezaji kama Msuva wanaopenda kufunga wakitokea pembeni kupata faida na kuendelea kukomaa zaidi na hii inaweza kuwa faida kubwa kwa Msuva ambaye alipewa majukumu haya toka akiwa na kikosi cha Yanga, hii ni baraka kwake.

Si muda mrefu sasa tutakuwa tunaita kikosi cha Taifa Stars na majina mengi yakiwa ni yale yanayocheza nje ya ligi yetu. Ukomavu wa Banda unakupa sababu ya kwanini wachezaji hawatakiwi kuwa ndani, huku ufungaji wa Msuva ndani ya Taifa ni mabadiliko ya muda mfupi ambayo tunaombea yaendelee kuongezeka afike League One pale Ufaransa, ambako kutokea Morocco ni rahisi zaidi.

Naamini moyo wa Msuva ni wa kupigana. Naamini ni mshindi na ninaamini ni mwanaume wa shoka. Alikuwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa, zimetimia. Sasa nataka arudi kitandani aweze kuanza kuota ligi kubwa zaidi kwam kuwa Ufaransa na La Liga kunafikika.

Hongera Msuva. Wenzio waanze kukutamani kila ukipiga hatua maana itasaidia Taifa kwa ujumla.

Monday, December 11, 2017

Yuko akademi Marekani lakini ndoto yake ni Taifa Stars

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

jambo ambalo linaweza kuwa linamrahisishia kazi kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga utayari wa wachezaji wanaosakata soka nje ya nchi kuja kulitumikia taifa lao.

Na Spoti Mikiki imechangia kuonyesha baadhi ya wachezaji walio nje, hasa Hamis Abdallah (Sony Sugar),Abdul Hilal (Tusker) na Aman Kyata (Chemelil) za Kenya ambao wameanza kuitwa kulitumikia taifa lao kwenye kikosi cha timu ya Taifa.

Wiki iliyopita tuliona safari ya Yusuf Juma ambaye anaichezea Monroe SC, tangu ilivyoanzia mkoani Kigoma hadi Marekani ambako nako yuko mbioni kuondoka kutokana na kuhitaji sana kwake kucheza barani Ulaya akizipigia hesabu Arsenal na Chelsea.

Wiki hii tunaye mdogo wake, Abdallah Juma (16) ambaye yupo kwenye kituo cha New England Revolution akipatiwa misingi ya mpira kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani.

Abdallah anakaribia kutimiza miaka 16 hivi karibuni ameongea na gazeti hili kutoka kwenye kambi ya kituo hicho iliyopo Florida, Marekani na kusema japo amekulia Marekani lakini anatamani kuanza kuzichezea timu za vijana za nchi yake ya Tanzania.

“Kucheza timu za vijana kuna umuhimu wake, inategemea na mipango ya makocha husika ambao nadhani wamekuwa wakiita wachezaji kutokana na mahitaji yao, nipo kwenye hiki kituo ila natamani kuzichezea timu za vijana za Tanzania.

“Nilitoka Tanzania na kuja huku Marekani na familia yangu nikiwa mdogo sana, sina kumbukumbu nyingi kuhusu nchi yangu ila ninachojua, mimi ni Mtanzania, kukulia kwangu Marekani hakunifanyi niwe na uamuzi wa kuwa raia wa huku.

“Ndoto yangu ni kuwa mchezaji mkubwa ili nilisaidie pia Taifa langu la Tanzania kwenye ngazi tofauti za timu za Taifa,hata kama ikitokea nimeshawishiwa kuachana na Tanzania na kuichezea Marekani sintokuwa tayari,” anasema Abdallah.

Ameendelea.”Ujinga ni kuisaliti nchi yako, hakuna sababu ya kunifanya niisaliti Tanzania na natamani sana siku nikipata nafasi nirudi ili nilione vizuri Taifa langu, maana nasikia kwanza lina vivutio vingi vya Utalii,”

Abdallah ambaye anamudu kucheza kwenye nafasi ya kiungo mshambuliaji, amesema namna soka la kufundishwa linavyoweza kumfanya mchezaji kuwa bora zaidi.

“Kila siku tunausoma mpira ambao unamambo mengi, sio kuucheza tu uwanjani, mchezaji kwenye kituo chochote cha soka huwa anaandaliwa kuja kuwa mchezaji wa kulipwa hivyo kuna vitu vya ziada anavipata ikiwemo kucheza kwa nidhamu.

“Ukikizoea kitu basi utakuwa unakifanya kwa umakini, kadri unavyosisitiziwa nidhamu na kuifanyia kazi kila siku inakujenga mchezaji, sio nidhamu pekee pia kuna mbinu mbalimbali za mpira na mengineyo mengi ambayo mchezaji binafsi anatakiwa kuwa nayo.

“Mwenye kipaji halisia akiongezea na maarifa ya kwenye kituo cha mpira basi ni wazi huyo mchezaji atakuwa na uwezo mara mbili, yule ambaye anakipaji na hata hajapitia kwenye kituo atakuwa na uwezo mara moja labla kipaji chake kiwe cha hali ya juu,” anasema.

Mdogo huyo wa Yusuf,amesema kuwa anasimamiwa na kaka yake hivyo suala la wapi anategemea kucheza kama akipevuka kwenye kituo hicho alishindwa kutoa jibu la moja kwa moja na mwishowe kumsukumia Hamis ambaye ni kaka yake mkubwa.

“Kaka Hamis ndiyo anaweza kuzungumzia hilo vizuri, nipo kwenye hiki kituo yeye ndiye anafanya mipango nje ya kutusimamia pamoja na kaka yangu mwingine Yusuf hivyo siwezi kulizungumzia hilo sana.

“Ila natamani zaidi kucheza Ulaya, soka la Ulaya linamvuto zaidi na hata ushindani wake ni mkubwa kama utalinganisha na huku,” anasema kiungo huyo mchezeshaji.

Hamis, akimzungumzia mdogo wake, Abdallah anaeleza namna ambavyo anaweza kumudu kuwasimamia wadogo zake pamoja na mipango yake kwa ujumla ilivyo.

“Soko la mpira wa Ulaya linalipa hivyo nimeopanga kujikita zaidi na Ulaya, Yusuf nimeshafanya mpango kwa kuzungumza na timu kadhaa ambazo atakwenda kufanya majaribio mwenzi,Januari.

“Abdallah yupo kwenye kituo sina haraka naye maana anamuda wa kuendelea kujifunza, atakapomaliza mafunzo yake tutaangalia ni wapi patakuwa sehemu sahihi kwake, kinachonipa faraja ni kuwa wote wawili wanauwezo mkubwa.

“Kama misingi ya mpira wanayo kwa hiyo hata kwenye kufanya majaribio hawawezi kukwama kabisa kwa kukosa timu za kuzichezea, kikubwa tuombe uzima,” anasema kaka huyo.

Monday, December 11, 2017

BAADA YA BAO Tino: Joel Bendera alinibeba mgongoni Zambia

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Kocha Joel Bendera ametangulia na jana Jumapili alipumzishwa katika nyumba yake ya milele wilayani Korogwe, lakini ameondoka na historia yake tamu ambayo nyota wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino anasema kama sio Bendera, Taanzania isingecheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1980.

Bendera alifariki Alhamisi iliyopita akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa nne tu tangu alipopokewa akitokea mjini Bagamoyo.

Mchezaji wa zamani wa Pan African, Peter Tino hatasauliwa kutokana na kufunga bao lililoiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini mshambuliaji huyo anasema wa kukumbukwa zaidi ni Bendera.

“Asikwambie mtu, wachezaji tulifuraji lakini bendera alifurahi zaidi tulipofunga bao la kusawazisha kwenye mechi na Zambia tena mbele ya rais wao, Kenneth Kaunda kwenye uwanja wa Ndola,” Tino anasimulia alipofuatwa na Spoti Mikiki.

“Baada ya filimbi ya mwisho, Bendera alinikimbilia na kunibeba mgongoni. Ilikuwa ni furaha ya Watanzania wachache waliokuwa pale uwanjani.”

Anasema ushindi haukuanzia uwanjani, bali maneno ya Bendera walipopokelewa ubalozini.

“Tulipofika Lusaka, timu yetu ilikwenda kumtembelea balozi kabla ya kwenda Ndola. Tukiwa pale (ubalozini) tulionyeshwa magazeti ya Zambia, rais wao akiwa ameshika funguo za gari na kutamka kwamba kila mchezaji atapewa gari na nyumba kama wataifunga Tanzania,” anasema.

“Yale maneno yalimuumiza mno Bendera. Alituambia, ninyi hamjaahidiwa chochote, lakini ninyi ndiyo mnatakiwa mtoe zawadi kwa Watanzania. Msitumike kama mgongo wa watu kupewa nyumba na gari. Bendera alizungumza kwa ujasiri mno na maneno yake yalitusisimua na tuliwaahidi kufia uwanjani.

“Kwenye mechi ilikuwa hakuna bahati mbaya. Hadi mapumziko tulikuwa tumeshafungwa bao 1-0. Tukiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kocha mzungu alizungumza akamaliza, ikafika zamu ya Bendera sasa, alizungumza kwa hisia akasema maneno yangu ni yale yale.

“Tusikubali watu wapewe nyumba na gari kwa mgongo wetu, Serikali haijatoa ahadi yoyote kwetu, lakini sisi tutoe ahadi kwa Watanzainia, wao wanaongoza na bila shaka sasa hawana nguvu hivyo sisi twendeni tukawafunge, Bendera alipomaliza kutamka hivyo, mimi niliitikia sawaa tena kwa sauti ya juu,” anasimulia Peter Tino. “Wakati tunacheza, pale Uwanjani kulikuwa na Watanzania kama 30 hivi au 40 ambao walikuwa wakitushangilia mwanzo mwisho kwani kitendo cha kufungwa bao moja hadi mapumziko wao waliona cha kishujaa kwetu kwani walijua tutapigwa nne au tano hadi mapumziko.

“Baada ya bao letu mpira ukaisha kwa sare ya bao 1-1, Bendera alikuja spidi hata sikumbuki alinibebaje mgongoni. Nilijikuta niko tayari mgongo kwake huku akiimba ndoto yangu imetimiaaa! Ilikuwa ni furaha isiyopimika kwani matokeo yale yalitupeleka AFCON kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya kuibika na ushindi wa bao 1-0,” anasema.

Jinsi bao lililovyofungwa

Tino alifunga bao hilo wakati Stars iliporudiana na Zambia jijini Ndola Agosti 26,1979 wakati huo wenyeji wakijulikana kwa jina la KK Eleven, kumaanisha rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.

Iko hivi, Taifa Stars wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Slowmir Wolk kutoka Poland, akisaidiwa na Bendera na Ray Gama ambaye naye ni marehemu, ilikata tiketi ya kushiriki Fainali hizo za Afrika.

Katika pambano hilo la agosti 26, 1979, Taifa Stars ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili ifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.

Timu hizo zilikuwa zinarudiana baada ya Stars kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizotangulia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), bao pekee likiwa limefungwa na kiungo, Mohammed Rishard Adolph.

Katika mchezo huo wa marudiano, KK walipata bao la mapema katika mchezo huo ambalo lilidumu hadi dakika ya 85.

Dakika tano za mwisho, Peter Tino alisawazisha bao na kunyamazisha umati wa mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Ndola.

Ilipigwa kona kuelekea lango la Stars na kipa Juma Pondamali “Mensar” akaupangua kwa ngumi, ukamkuta beki wa kati, Leodegar Chilla Tenga ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Hussein Ngulungu. Kiungo huyo akamgongea Tino.

Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino aliwazidi ujanja akiwa nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia na kupiga kombora la mguu wa kulia, lililompita kipa wa Zambia aliyekuwa kikwazo, John Shileshi.

Katika mchezo huo, Tanzania iliwakilishwa na; Juma Pondamali ‘Mensar’, Leopard Tasso Mukebezi, Mohammed Kajole Machela/ Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Chilla Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein ‘Keegan’, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.

Nahodha Leodegar Tenga

Leodegar Tenga, aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka 10, aliiongoza timu hiyo uwanjani na kufanya vizuri hata kufika fainali hizo.

Akimzungumza na Spoti Mikiki Hospitali ya Lugalo wakati wa kuuaga mwili wa Bendera, Tenga anasema: “Mwalimu Bendera alikuwa na uwezo mzuri wa kuongea na wachezaji kabla na hata wakati wa mchezo.

“Tulikuwa tukijisikia furaha tukiwa naye. Kila mmoja wetu alijiona ni mwana familia, hakika hili ni pigo kwenye familia ya mpira na daima atabaki kukumbukwa kama mtu mbaye amelifanyia Taifa makubwa.”

Hata hivyo, Tenga anasema kuwa mafanikio yao hayakuja kirahisi kwani waliandaliwa kwa miaka minne kuanzia mwaka 1976.

Kiraka Adolf Rishard

Jina la timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars lilizinduliwa katika mchezo ambao Tanzania iliongozwa na Bendera, kwa mujibu wa Adolf Rishard, mchezaji mwingine aliyewahi kuwa chini ya mkufunzi huyo.

Rishard, ambaye pia alifunga bao katika mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Zambia nyumbani, anasema Bendera alikuwa ni kocha mwenye maono.

“Mimi niliitwa Stars 1976 kwenye mechi na Kenya kwa ajili ya kuzindua jina la Harambee Stars. Alikuwa pamoja na marehemu Gama mwaka 1977 hatukucheza Chalenji kutokana na vita ya Uganda, lakini mwaka 1978 tulikwenda kuweka kambi Lushoto kwa ajili ya Chalenji na 1979 tulikuwa wa tatu kwenye Chalenji Nairobi .

“Wakati huo ndio tulikuwa katika harakati za kufuzu tukiwa naye hadi 1980 kwenye AFCON. Lakini baada ya AFCON aliondoka na kocha wa Stars akawa Msomari, japo sikumbuki Bendera aliondokaje ondokaje Stars wakati ule,” anasema Rishard.

“Ninamkumbuka Bendera alikuwa na kipawa cha hamasa, alitupa hamasa sana kiasi cha kufanya vizuri mechi zetu.”

SAFARI YA KOROGWE

Bendera alifariki Desemba 6 jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Brass Kiondo ndugu yao alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupumua ambalo lilimuanza Desemba 3 na alikuwa anatibiwa Hospitali ya Korogwe na baada ya hali yake kuimarika, akapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini hali ilibadilika ghafla hadi mauti yalipomkuta akiwa Muhimbili.

Bendera aliagwa juzi jijini Dar es Salaam na ndugu, jamaa na marafiki na wanamichezo, hasa wachezaji aliowafundisha akiwemo Tenga na Tino.

Watu wengine waliohudhuria ni pamoja na mkurugenzi wa ufundi wa TFF ambaye pia ni kocha, Salum Madadi na mtangazaji mkongwe, Tido Muhando.

Wengine ni mbunge wa Muheza, Adadi Rajab.

Bendera aliwahi kuwa mbunge wa Korogwe Mjini, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkuu wa mikoa ya Morogoro na Manyara.

Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26, Bendera alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa waliostaafu na nafasi yake imechukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kutoka kuwa mkuu wa Wilaya ya Arumeru.

Mapema baada ya kushindwa ubunge, aliteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro.

Monday, December 4, 2017

Najua tu naonekana mgeni

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimteua Dk Mshindo Msolla kuinoa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Dk Msolla akaita wachezaji wake, kati ya aliowaita alikuwemo Ammy Ninje. Watu wakawa wanajiuliza “huyu Ammy Ninje ni nani? Katokea wapi” Mbona hatukuwahi kumsikia?”.

Akamtetea,akisema anamfahamu na alikuwa anamfuatilia huko England. Itakumbukwa hakucheza mechi nyingi kwa kuwa alibanwa na majukumu ya timu yake huko nje.

Juzi juzi, TFF ilimtangaza Ninje kuwa kocha wa Kilimanjaro Stars iliyoko Kenya kushiriki Kombe la Chalenji, na jana ilicheza na Libya.

Lakini bado wadau wanajiuliza “huyu Ninje ni nani hasa? Asili yake ni wapi” kwa kuwa anaonekana kama ni mgeni kwenye kikosi hicho cha Tanzania Bara.

SI MGENI TANZANIA

Kwanza Ninje anasema yeye si mgeni kwani ni msaidizi wa kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga tangu alipoteuliwa.

Amekuwa na timu kipindi chote na zaidi ndiye msimamizi wa timu na Mayanga ni kama anaratibu. Kimsingi anasema kuwa anaonekana mgeni kwa kuwa hafundishi timu yoyote ya Ligi Kuu kama ilivyo makocha wengine wazawa.

“Ninasaidiana na Mayanga Taifa Stars hivyo mimi si mgeni kama wengi wanavyodhani,” anasema Ninje katika mahojiano na Spoti Mikiki.

“Nina ujuzi wa kutosha ambao nimetoka nao Uingereza ambako ndiko nilipojipatia elimu ya ukocha na uzoefu kwa kukaa chini ya makocha kadhaa Uingereza na Tanzania.”

CHALENJI

Ninje anaipeleka Tanzania kwenye michuano ambayo haina rekodi nzuri ya mafanikio, lakini haonekani kuwa na hofu nayo.

“Nimejipanga, ninafahamu Chalenji haina mabadiliko sana,” anasema.

“Haya ni mashindano ambayo kila mchezo una umuhimu wake, itatulazimu kupata matokeo ya ushindi kwenye kila mchezo utakaokuwa mbele yetu. Ninafurahia kuwa na kikosi kizuri chenye wachezaji wepesi kushika maelekezo.

“Kikubwa ni Watanzania kuniunga mkono, mengine watajionea wao wenyewe uzuri. Hayo mashindano huenda yakaonyeshwa hivyo wataiona timu yao itakavyokuwa ikipambana.”

Kabla ya kuondoka nchini Kili Stars ilijikita hasa kwenye mazoezi na kufanyia kazi mfumo wa namna ya uchezaji kwa kuanzia eneo lake la nyuma. Mara nyingi katika mazoezi, Ninje alionekana kutaka timu yake ianzishe mashambulizi kutokea kwenye ngome; mabeki wa kati au pembeni kulingana na hali ya mchezo.

KUNDI A

Katika mashindano ya Kombe la Chalenji, ambayo hushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na majirani pamoja na kualika timu za nje ya ukanda, Tanzania Bara imepangwa Kundi A pamoja na Kenya, Libya, Zanzibar.

Ninje anakubali kuwa hilo si kundi jepesi, lakini ana matumaini ya kufanya vizuri.

“Tumejiandaa vizuri hivyo hatuna cha kuhofia. Timu zote tunazichukulia kwenye daraja moja,” anasema.

“Katu hatuwezi kuibeza timu yoyote kwa sababu kwenye soka ile ambayo hauipi nafasi, inaweza kuonyesha maaajabu ambayo husababishwa na uzembe.

“Dharau inasababisha kutofanya kitu kwa ufasini, ndiyo maana ninasema tumejipanga.”

Monday, December 4, 2017

Kombe la Chalenji 1981-Ilikuwa akiingia Mogella tu, kapiga bao

 

By Ibrahim Bakari, Mwananchi

Achana na mwaka 2010 Tanzania Bara ilipotwaa ubingwa wa Chalenji kwa bao la beki wake, Shadrack Nsajigwa, shughuli ilikuwa mwaka 1981.

Iko hivi, kulifanyika mashindano mengi, Tanzania Bara ikawa mwenyeji baada ya 1981, mwaka 1992, 2002, 2007, 2010 na 2011. Hata mwaka 2010 wakati inatwaa ubingwa, moto wake haukuwa kama ilivyokuwa mwaka 1981.

Kuna mchezaji anaitwa Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ anasema: “Nilipewa hilo jina mwaka 1981 nikiwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye mechi za Chalenji na ilikuwa zaidi dhidi ya Malawi.

“Tulikuwa tumefungwa magoli 2-1 katika ile mechi na Malawi, niliingia dakika ya 75, zikiwa zimesalia dakika mbili mpira kwisha, nilifunga goli la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa sare ya 2-2.

“Pale ndipo nikapewa jina la Golden Boy, ilifikia mahali nikawaaminisha mashabiki kutokana na uwezo wangu kwamba, nikiingia tu lazima nifunge na kweli ilikuwa hivyo kutokana na kujitunza na kulinda kiwango changu hadi nilipostaafu,” anasimulia.

Tanzania Bara wakati huo ikiwa chini ya kocha Mjerumani, Rudi Gutendorf, na kati ya wachezaji wake, alikuwa Zamoyoni Mogella. Tanzania ikifungwa, akiingia tu lazima atikise nyavu, licha ya kuwa Wakenya walimbana tukalala 1-0 katika fainali.

Ilikuwa dakika kama 10 au 15 kabla mpira kwisha, Gutendorf alikuwa anamwinua Mogella basi uwanja mzima kelele.

Mashindano yale yalikuwa na msisimko wa aina yake, kila mmoja alikuwa nyuma ya timu ya Tanzania Bara hadi fainali dhidi ya Kenya tuliyolala kwa bao la Ouma.

Hata hivyo, mwendo wa mashindano haya umekuwa wa kusuasua kutokana na udhamini, lakini sasa kuanzia jana Desemba 3 hadi 17, mwaka huu Kenya ndiye mwenyeji wake na Tanzania Bara imepangwa Kundi A pamoja na Zanzibar, Libya, Kenya na Rwanda.

Bara jana ilikuwa ikicheza na Libya mechi ya ufunguzi wakati Kenya ilikuwa ikikwaruzana na Rwanda.

Lilikoanzia Kombe la Chalenji

Hicho kilikuwa kibwagizo cha 1981, lakini Chalenji ilianzia wapi hasa?

Tunaelezwa katika historia kuwa hii ndiyo michuano mikongwe Afrika. Ilianza mwaka 1926 wakati huo ikiitwa Gossage ambayo sasa inatimiza miaka 91.

Gossage lilikuwa jina la tajiri mmoja akimiliki kiwanda cha sabuni na ndiye alikuwa mdhamini na alikuwa akipenda soka.

Baada ya kumaliza kuizunguka Afrika Mashariki kwa usafiri wa reli enzi hizo ikiitwa, Uganda-Kenya Railways mwanzoni mwa miaka ya 1900, katika safari yake alikuwa akikutana na makundi ya watu waliokuwa wakikaakaa bila kujishughulisha baada ya kumaliza kujenga reli na shughuli nyingine.

Wengi wao walikuwa Waafrika, Waasia na Wanubi ambao ndiyo waliokuwa wakijenga reli. Gossage aliona kwamba njia pekee ya kuwafanya wafurahi ni kuwawekea michezo (mashindano).

Kwa hiyo, mwaka 1927, alianzisha michuano iliyoshirikisha mataifa ya Kenya na Uganda na alianzisha Kombe lililoitwa Gossage. Mashindano yalishindaniwa katika miji ya Kampala na Nairobi kwa miaka mingi na kuwa moja ya mashindano maarufu.

Tanganyika (sasa Tanzania) ilijiunga 1944 na kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza kuanzia 1945.

Kwa upande wa Zanzibar, iliyokuwa chini ya utawala wa Waarabu, mwaka 1948 baadaye iliingizwa na kufanya mashindano ya mataifa manne.

Mashindano yaliendelea na jina la Gossage hadi mwaka 1963 na kubadilishwa jina na kuitwa Mashindano ya Chalenji Afrika Mashariki.

Mataifa hayo manne yalishindana hadi 1973 walipokaribisha mataifa mengine.

Katika mkutano maalum uliofanyika Nairobi, Kenya wanachama hao walikubaliana kuiingiza Somalia, Zambia na Ethiopia na wakati huo sasa ndipo Cecafa ikazaliwa.

Sasa kuna mataifa saba yaliyoingia. Wakati huo na Makao Makuu ya Cecafa yalikuwa Mogadishu, Somalia kabla ya kuhamishiwa Nairobi. Michuano hiyo inaitwa Kombe la Cecafa.

Mwaka 1974, nchi wanachama walianzisha mashindano mengine, lakini haya yalikuwa katika ngazi ya klabu, uzinduzi ulifanyika Dar es Salaam na ndiyo hiyo Kombe la Kagame.

Sudan na Malawi zilijiunga Cecafa mwaka 1975. Baadaye 1981, Zimbabwe, baada ya kupata uhuru wake 1980, ikajiunga na familia ya Cecafa.

Hata hivyo, 1994 baada ya kuanguka utawala wa kidhalimu Afrika Kusini, kulianzishwa Baraza kama Cecafa la Cosafa lililokuwa likiunganisha mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Kutokana na hali hiyo, mataifa ya Malawi, Zambia na Zimbabwe yakajiondoa Cecafa na kuanza maisha mapya ya Cosafa.

Kuondoka kwa mataifa hayo, kulifungua mlango kwa Rwanda, Burundi na Eritrea, pamoja na Djibouti kuingia Cecafa mwaka 1995.

Hiyo ilifanya mataifa ya Cecafa kufikia 11 ambayo ni: Kenya, Sudan, Uganda, Tanzania, Ethiopia, Eritrea, Zanzibar, Somalia, Rwanda, Djibouti na Burundi.

Waliotwaa mara nyingi

Mpaka sasa, Uganda Cranes imetwaa mara nyingi, 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009, 2011, 2012 na 2015.

Kenya inafuatia, 1975, 1981, 1982, 1983, 2002 na 2013 wakati Tanzania Bara imetwaa mara tatu, 1974, 1994 na 2010 sawa na Malawi 1978, 1979, na 1988 na Sudan 1980, 2006 na 2007.

Monday, December 4, 2017

Makundi ya Morocco, Nigeria na Tunisia siyo ya kitoto!

 

Kuna kitu hakijawahi kufanyika Afrika lakini juzi Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Ahmad Ahmad alifanya, alizipa nchi zilizofuzu Fainali za Kombe la Dunia, kila mmoja Dola 500,000 za maandalizi.

Unaambiwa Rais wa CAF aliyepita, Issa Hayatou, tangu aingie madarakani Lionel Messi akiwa na mwaka mmoja, hajawahi kufanya. Hayatou alimwagwa kwenye uchaguzi wa CAF uliofanyika Addis Ababa Machi 16, mwaka huu.

Achana na Hayatou, Ahmad Ahmad anataka kuiweka Afrika karibu kwa kila mmoja, ametoa nafasi kwa timu kujiandaa, anaziandalia mechi za majaribio lakini pia amesogeza mechi za kuwania kucheza Afcon 2019 zilizokuwa zichezwe Machi mwakani akazipeleka Oktoba mwakani.

Mataifa matano ya Afrika yatakayokwenda Moscow, Russia kwenye Fainali za Kombe la Dunia ni Nigeria, Morocco, Tunisia, Misri na Senegal.

Ijumaa jioni, wenyeji wa fainali hizo waliandaa hafla kubwa ya kupanga ratiba na makundi ya fainali hizo zikiwemo nchi hizo za Afrika.

Ukiangalia droo hiyo, mataifa ya Morocco na Nigeria yatakuwa na kibarua pevu katika makundi yao.

Nigeria imepangwa na mabingwa wa zamani Argentina. Super

Eagles inaweza kugeuziwa kibao licha ya kuifunga mabao 4 – 2 katika mchezo ya kirafiki hivi karibuni. Mbali na Argentina,

Nigeria itakutana na Croatia na Iceland katika Kundi D.

Kundi B, Morocco watakuwa na shughuli pevu watakapokutana na kasi ya Cristiano Ronaldo na mastaa wengine wa Ureno. Timu hiyo pia ni bingwa wa Ulaya.

Shughuli nyingine watakayokutana nayo Morocco ni kwa wakali wa Hispania na timu isiyotabirika ya Iran.

Wawakilishi wengine wa Afrika, Tunisia watakutana na mziki wa Ubelgiji utakaokuwa ukiongozwa na Romelu Lukaku katika Kundi G. Nchi nyingine katika kundi hilo ni England na wageni wa fainali hizo, Panama.

Misri walioko Kundi A itawalazimika kuweka pembeni masuala yao ya kidiplomasia na kuingiliana na Saudi Arabia.

Pia watakumbana na joto la wenyeji, Russia. Timu nyingine watakayokumbana na nayo ni wataalamu wa rafu, Uruguay.

Senegal walioingia robo fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 Korea Kusini na Japan wanaonekana kutokuwa na kazi ngumu, lakini shughuli watakutana nayo kwa Poland, Colombia na Japan na jina la Sadio Mane tayari limeanza kuonekana kama litakuwa tishia katika Kundi hilo kutoka Senegal.

Rekodi za Wawakilishi wa Afrika

1. MISRI – ‘Pharaohs’ ilicheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza nchini Italia 1990

2. MOROCCO – ‘Simba wa Atlas’ walifuzu wakiwa na rekodi nzuri Afrika.

3. NIGERIA – ‘Super Eagles’ wamekosa Fainali moja tangu walipocheza Fainali za Kombe la Dunia Marekani 1994

4. SENEGAL – Waliingia kwa mara ya kwanza Korea/Japan 2002, Simba wa Teranga wakaingia robo fainali.

5. TUNISIA – walicheza Fainali za Argentina 1978, ‘Tai wa Carthage’ ilikuwa timu ya kwanza kushinda mechi ya Kombe la Dunia.

FAINALI ZA 2014 VS 2018

Mwaka 2014 timu za Afrika zilizofuzu ni Ghana, Cameroon, Ivory Coast, Nigeria na Algeria. Moja ya Afrika Kaskazini na nne kutoka sub Sahara.

Miaka minne baadaye, ni Nigeria pekee ikarudi kwenye fainali. wakati huo sasa ikawa na timu nyingine ya Afrika Magharibi, Senegal.

Timu nyingine ni kutoka Afrika Kaskazini – Misri (mabingwa mara nyingi wa Afcon), Morocco na Tunisia.

Timu kutoka mataifa mengine

UKANDA WA UEFA – ULAYA

UBELGIJI – Walifuzu wakitokea Kundi H na hawakupoteza mechi hata moja.

CROATIA – Wazoefu, walikuwa watatu Fainali za Ufaransa 1998

DENMARK – Walifuzu kiulaini kwa kuifunga Jamhuri ya Ireland.

ENGLAND – ‘The Three Lions’ wameingia mara ya 14 kati ya 16 walizoshiriki.

UFARANSA – ‘Les Bleus’ wanacheza mara ya sita mfululizo.

UJERUMANI – Waliingia wakijiamini kwa ushindi wa asilimia 100.

ICELAND – Taifa lenye idadi ndogo ya watu kuwahi kufuzu.

POLAND – ‘The Poles’ walikuwa wa tatu Fainali za Ujerumani mwaka 1974 na Hispania 1982

URENO – ‘Seleção das Quinas’ Fainali za tano mfululizo.

RUSSIA – Kama Soviet Union, walikuwa wanne Fainali za England 1966

SERBIA – ‘The Serbs’ilifuzu kutokea Ukanda wa UEFA Kundi D ikipoteza mechi moja.

HISPANIA – Mabingwa 2010, ilianza kucheza Fainali za Italia 1934.

SWEDEN – Walimaliza wa pili Fainali za Kombe la Dunia 1958.

USWISI – Mara tatu wamemaliza nafasi ya tatu Kombe la Dunia.

CONMEBOL – AMERIKA KUSINI

ARGENTINA – Mabingwa mara mbili. Walikuwa kwenye uzindizi wa Kombe la Dunia mara ya kwanza nchini Uruguay 1930

BRAZIL – ‘Seleção’ ilikuwa ya kwanza kufuzu fainali za mwakani ukiacha wenyeji Russia.

COLOMBIA – ‘Los Cafeteros’ ilikuwa chini ya kocha, Jose Pekerman raia wa Argentina Fainali za Ujerumani mwaka 2006.

PERU – Imerudi Fainali za 2018 baada ya miaka 36.

URUGUAY – ‘La Celeste’ walitwaa ubingwa 1930 na Fainali za Brazil 1950

CONCACAF – AMERICA KASKAZINI

COSTA RICA – ‘Los Ticos’ ilionyesha soka yake Brazil 2014, na kuingia robo fainali.

MEXICO – ‘The Mexicans’ ilipoteza mechi moja ikiwani kufuzu Russia 2018

PANAMA – Imetokea Amerika ya Kati, imefuzu kwa mara ya kwanza Russia.

UKANDA WA AFC – ASIA

AUSTRALIA – ‘Socceroos’ Inaingia mara ya tano Kombe la Dunia.

IRAN – ‘Team Melli’ timu ya kwanza Asia kwenda Russia 2018

JAPAN – Mara ya 16 kuingia fainali.

JAMHURI YA KOREA – ‘The Taeguk Warriors’ Haikuwahi kucheza Kombe la Dunia tangu 1986

SAUDI ARABIA – Ilianza kucheza Fainali za Kombe la Dunia 1994 nchini Marekani.