Tuesday, January 9, 2018

Mwandae hivi mwanao kwa mwaka mpya wa masomo

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Shule zimeanza kufunguliwa wiki hii na watoto wanaanza muhula mpya wa masomo baada ya mapumziko marefu ya mwisho wa mwaka.

Kuanza kwa muhula mpya wa masomo kunaweza kuleta changamoto fulani kwa watoto. Kwanza mtoto anatoka kwenye ratiba yenye kiasi fulani cha uhuru nyumbani na anarudi kwenye mazingira atakayolazimika kufuata ratiba isiyobadilika.

Lakini pia mtoto anaporudi shuleni, anaachana na watu wa karibu wa familia yake, ambao ndio hasa wanaomwelewa na pengine kumsikiliza vizuri zaidi na kwenda kukutana na watu ambao wakati mwingine hawana nafasi ya kujenga uhusiano wa karibu naye. Haya mawili yanaweza kumfanya mtoto asifurahie sana kurudi shule.

Kwa upande wa mzazi, hiki ni kipindi cha pilika nyingi za kuhakikisha mtoto anapata vifaa na mahitaji muhimu yanayohitajika shule ikiwa ni pamoja na sare mpya za shule, viatu, begi, madaftari, kalamu, vitabu na vifaa vinginevyo vya lazima shuleni.

Kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za maisha, hiki kinaweza kisiwe kipindi kizuri kwa wazazi wenye majukumu mengi ya kufanya.

Katika makala haya, nakusaidia kutazama namna gani unaweza kumwandaa mwanao kuanza mwaka mpya wa masomo hata katika mazingira magumu kiuchumi.

Unatambua uwezo wake?

Wajibu mkubwa ulionao mzazi ni kumfanya mtoto si tu atambue uwezo wake, lakini aweze kuukuza na kuuishi. Mtoto anayesoma tu bila kujua uwezo wake ni sawa na gari zuri lisilo na tatizo, lakini linaendeshwa na dereva asiyejua wapi anakwenda. Uwezekano wa kupata matatizo unakuwa mkubwa.

Ni muhimu mzazi kufanya jitihada za kujua uliko moyo wa mwanao. Jitahidi kadri unavyoweza kujaribu kumsaidia kujitambua mapema. Mtoto akiujua uwezo wake, atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufahamu afanye nini na elimu atakayoipata darasani.

Kuna namna nyingi za kumsaidia mtoto kujua uwezo wake. Mojawapo ni kumruhusu kushiriki shughuli mbalimbali zinazomfanya aguse vitu vingi vinavyohitaji ujuzi wa namna mbalimbali. Mtoto anaposhiriki shughuli hizi itakuwa rahisi kujua wapi ana uwezo zaidi na wapi moyo wake hauelekei.

Unaonyesha imani kwake?

Kama kuna jambo la msingi unaloweza kumfanyia mwanao ni kumfanya ajiamini. Mtoto asiyejiamini hawezi kufanya mambo mengi. Ndani yake kutakuwa na sauti inayomzomea muda mwingi na atakuwa na tabia ya kujisema maneno ya kujikatisha tamaa.

Maneno unayomwambia mara kwa mara ndiyo hasa yanayotengeneza sauti hii inayoweza kutoka ndani yake kumkatisha tamaa. Kama mzazi, shiriki kazi kubwa ya kutengeneza sauti chanya atakayoisikia mwanao. Mfanye ajiamini na kujisemea maneno yanayomwongezea hamasa ya kufanya mambo.

Kikubwa unachoweza kukifanya ni kumwonyesha mwanao kuwa una matarajio makubwa kwake. Hata katika mazingira ambayo hafanyi vizuri darasani kama unavyotaka, bado unaweza kuzungumza nae kwa namna inayotuma ujumbe kuwa unamwamini.

Usifanye kosa la kuonyesha umemkatia tamaa. Mtoto anahitaji kujua mzazi wake anamwamini.

Umemwekea mazingira mazuri?

Mazingira mazuri ya kujifunzia yana nafasi kubwa ya kusababisha mafanikio ya mtoto. Watoto wanapokutana na mazingira yanayowahamasisha kujifunza, wanakuwa na kazi nyepesi ya kufanya.

Tunapozungumzia mazingira mazuri tuna maana ya kuhakikisha anapata vifaa anavyovihitaji katika kujifunza; ushirikiano wa karibu kati yake na mzazi na kuona wanaomzunguka nao wanathamini kujifunza.

Hebu anza mwaka kwa kuhakikisha mtoto anajifunza bila wasiwasi. Kadri inavyowezekana, msaidie kujua unafuatilia masomo yake. Hakikisha amefanya kazi za shule anazorudi nazo nyumbani. Kagua madaftari yake mara kwa mara na pia jenga tabia ya kuulizia amejifunza nini shuleni.

Aidha, ni nyema kutengeneza mazingira rafiki nyumbani yatakayomhamasisha mtoto kujifunza. Msaidie kutengeneza ratiba ya siku anaporudi nyumbani ili ajue anapaswa kufanya nini kwa wakati gani.

Dhibiti matumizi ya televisheni lakini pia mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya mambo mengine nje ya masomo.

Umemsaidia kujua ndoto zake?

Ndani ya kila kichwa cha mtoto kuna matamanio ya kufanya kazi fulani. Mtoto anaona watu wazima wanaofanya kazi tofauti tofauti. Watu hawa kwa namna moja au nyingine wanamjengea ndoto fulani katika maisha.

Ukimuuliza mtoto yeyote anataka kuwa nani, hatokosa kukutajia kazi anazozifahamu kwenye mazingira yake. Hata hivyo, matamanio haya si lazima yawe ndoto zake. Wakati mwingine kazi anazosikia zina heshima katika jamii, ndizo zinazojenga matamanio yasiyoendana na uhalisia wake.

Mwaka huu jipange kumsaidia mtoto kujitambua. Mruhusu mtoto akacheze michezo mingi inayomfanya aigize shughuli mbalimbali anazoziona kwenye mazingira yake. Mkutanishe na watu maarufu wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya utaalamu.

Msimulie hadithi za watu waliowahi kufanya mambo makubwa katika maeneo yao ya utaalamu. Ikiwezekana, mpeleke mtoto kwenye maonyesho, maeneo ya kihistoria, maktaba na hata kutembelea vyuo vikuu.

Changamoto hata hivyo, wazazi wengi tuna tatizo la kutaka watoto wawe vile tunavyotaka sisi. Kwa maana nyingine, ni kama tunataka watoto wawe nakala ya maisha yetu badala ya kuwaruhusu kuwa vile walivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Mpe mtoto mwongozo unaomwezesha kuwa kile alichokusudiwa kuwa. Usijaribu kutimiza ndoto zako ulizoshindwa kuzitimiza kwa kumtumia mtoto.

Unamsaidia kuweka malengo?

Wajibu mwingine muhimu kwako kama mzazi ni kusaidia mtoto kujiwekea malengo yake ya kimasomo. Watoto wengi hushindwa kufanya vizuri darasani kwa sababu hawana malengo. Hawajui wanalenga kufikia hatua gani kwa mwaka husika.

Msaidie mwanao kujipanga mapema kipindi hiki anapoanza masomo. Kaa naye muweke malengo yanayolingana na hali halisi. Kwa mfano, kama mtoto anashika nafasi ya chini darasani, zungumzeni muone anaweza kupanda mpaka wapi kwa muhula huu wa kwanza.

Kosa unaloweza kulifanya mzazi ni kumwekea malengo ya juu mno yasiyoendana na uwezo na mazingira yake. Lakini pia ni muhimu kuelewa kuwa malengo yasiyopimika kila mara, hayana maana. Msaidie mtoto kuweka utaratibu mzuri wa kupima maendeleo yake kila mara.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Tuesday, January 9, 2018

Wadau: Kiswahili hazina ya Afrika na dunia

 

By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Kiswahili ni lugha adhimu na fahari ya bara la Afrika. Ni lugha ya pili inayozungumzwa na watu wengi Afrika baada ya Kiarabu.

Pia, ni lugha ya kwanza ya kibantu inayozungumzwa na watu wengi katika bara hili.

Lugha hii imeanza kutanua mawanda yake katika nchi nyingine duniani.

Inapendwa kwa sababu ya urahisi wake wa kujifunza na pia kama lugha ya kurahisisha mawasiliano na watu wengi zaidi hasa katika bara la Afrika.

Katika kongamano la kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu) lililofanyika Disemba mwaka jana, wadau mbalimbali kutoka nchi 13 duniani walikutana jijini Dar es Salaam kujadili mafanikio na mikakati ya kukuza lugha ya Kiswahili duniani.

Rais wa Chaukidu, Mahiri Mwita Anasema lugha hiyo ni rasilimali ambayo inaweza kuuzwa katika soko la utandawazi na kujipatia fedha za kigeni na kwamba ufundishaji wa lugha hiyo siyo suala la kitaaluma pekee bali inaweza kuwa fursa ya kibiashara.

Anasema kuna haja ya kukiweka Kiswahili katika namna mpya kwa ajili ya kupelekwa sokoni na kuuzwa kwa wageni.

Kufanya hivyo, anasema Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki zitapata fedha za kigeni kutokana na lugha hiyo.

“Taaluma ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ni taaluma mpya ambayo lazima tujiandae kwa ajili ya kuuza sokoni,” anasema.

Mwita ambaye anaishi Marekani, amewataka Watanzania na Afrika kwa ujumla kujivunia lugha ya kiswahili na kuitumia kama rasilimali ambayo ni kivutio cha utalii kwa wageni kutoka mataifa mengine hasa Ulaya na Marekani.

“Sisi ndiyo tunaofundisha Kiswahili, miaka ijayo watakuwa wanazungumza wengi. Lazima tujiulize tumejipangaje kukabiliana na wale ambao tunawafundisha, wasije wakatupiku siku zijazo,” anasema.

Kiswahili zawadi ya Afrika

Akizungumza katika kongamano hilo, Balozi wa Kiswahili Afrika, Salma Kikwete aliwataka Waafrika kukumbatia utamaduni wao, badala ya kutukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi kwa kutumia lugha zao na kuiacha lugha ya Kiswahili.

Anasema Waafrika wamepewa zawadi ya lugha ya Kiswahili na Mwenyezi Mungu, hivyo wasione haya kuitumia popote watakapokwenda.

“Tunapopata nafasi kwenye majukwaa ya kimataifa tusisite kukitumia Kiswahili, hiyo ndiyo njia moja wapo ya kukuza lugha yetu,” anasema balozi huyo na kusisitiza kwamba siku moja bara zima la Afrika litazungumza Kiswahili.

Anasema Kiswahili kinazidi kukua siku hadi siku na mataifa mengine yanaona umuhimu wa lugha hiyo.

Vyuo vya kimataifa vimeanza kufundisha Kiswahili, jambo linalosaidia kuongeza idadi ya wataalamu na watumiaji wa lugha hiyo.

Wamarekani wakichagua Kiswahili

Ilivyo ni kuwa Kiswahili kimeambatana na utamaduni wa watu na uchumi wao.

Watumiaji wa lugha ya hii wana utamaduni unaofanana na kupitia lugha hii watu wa mataifa mengine wanajifunza utamaduni wa watu wa pwani ya Afrika Mashariki ambako ndiyo asili yake.

Sababu hizo ndizo zilizoifanya Marekani kukichagua Kiswahili kuwa moja ya lugha 12 za kimkakati ambazo Taifa hilo kubwa duniani litazitumia kurahisisha mawasiliano yake na mataifa mengine duniani.

Mwita anasema Kiswahili kimechaguliwa kwa kuwa ni miongoni mwa lugha nyeti kwa ajili ya usalama na ustawi wa kiuchumi wan chi hiyo.

Anaeleza kuwa Wamarekani wamechagua lugha hizo ili waweze kuchangamana na watu wa mataifa mengine, hivyo wameona Kiswahili ndiyo lugha pekee itakayowawezesha kuchangamana na bara la Afrika.

Kiswahili kufundishwa kwa mabalozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Susan Kolimba, anasema Serikali imeandaa mpango wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mabalozi na wanadiplomasia waliopo hapa nchini.

Anasema mafunzo hayo ambayo yataanza kutolewa Februari mwaka huu ni hatua ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa kwa wizara yake, ili kuhakikisha Kiswahili kinakua na kuenea katika nchi zao.

Anasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kimechaguliwa kuratibu mafunzo hayo na sasa kinakamilisha taratibu kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo.

Dk Kolimba anasema Serikali inahimiza matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi, kwa sababu lugha hiyo ndiyo kielelezo cha Taifa hili na utamaduni wake.

“Zaidi ya watu milioni 200 duniani kote wanazungumza lugha ya Kiswahili; ni lugha ya pili baada ya Kiarabu kuzungumzwa na watu wengi Afrika, lakini ni lugha pekee ya Kibantu inayozungumzwa na watu wengi Afrika,” anaeleza.

Anasema Kiswahili ni lugha ya Taifa kwa nchi za Tanzania, Kenya na DRC; anatoa wito kwa nchi nyingine za Afrika kukifanya Kiswahili kuwa lugha yao ya Taifa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye anasema wanaendelea vizuri na mpango wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mabalozi na kwamba watatumia mfumo maalumu wa kuwafundisha.

Ili kukuza Kiswahili, anasema tayari chuo chake kimeanza kuitumia lugha hiyo katika vikao vyake vyote pamoja na utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali. Anasema hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

“Chuo chetu kina mchango mkubwa katika kukua kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu tunafundisha lugha hiyo kwa watu wa mataifa mbalimbali ambao nao wanakwenda kuitumia katika nchi zao,” anasema Profesa Anangisye ambaye amesimikwa rasmi kuongoza chuo hicho baada ya kustaafu kwa mtangulizi wake, Profesa Rwekaza Mukandala.

Tuesday, January 9, 2018

Mbinu za kukuza uwezo wa akili wa mtotoChristian Bwaya

Christian Bwaya 

Kwa muda mrefu wataalam wengi wa saikolojia ya elimu waliamini uwezo wa akili anaokuwa nao mtu unarithiwa na haubadiliki. Katika kuthibitisha kuwa akili za mtu haziwezi kubadilika, wapo wataalam, tena wengi tu, waliobuni kipimo cha akili za mtu kilichojulikana kama IQ. Kipimo hiki kilitumia mfululizo wa maswali anayoulizwa mtu kujua anawezaje kufikiri, kuelewa na kuchambua mambo.

Lakini kadri utaalam wa kupima utendaji wa ubongo ulivyoendelea kuongezeka, sasa tunaelewa akili za binadamu zinaweza kubadilishwa na mazingira anayokutana nayo mtu.

Mtazamo huu mpya unatupa faida mbili kubwa. Kwanza, unatusaidia kujua mambo yanayoweza kufanyika kubadili uwezo wa akili anazokuwa nazo mtu. Pili, unaongeza wajibu tulionao sisi kama wazazi katika kumwekea mtoto mazingira sahihi yanayoweza kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Katika makala haya tutazame mambo manne unayoweza kuyafanya kukuza uwezo wa mtoto kufikiri, kuelewa na kuhambua mambo.

Badili lugha anayojisemea mtoto

Kila mtu anayo lugha ya ndani anayoitumia kufikiri. Lugha hii ya ndani ina kazi kubwa ya kujenga vile unavyojichukulia. Unapofikiri jambo, kwa mfano, unaweza kusema maneno fulani yanayokuhamasisha, kukusifu, kukukosoa, kukutia wasiwasi, mashaka na hata kukukatisha tamaa.

Wataalam wanasema kuna uhusiano mkubwa kati ya mawazo ya mtu na kile anachokifanya. Kama mtoto, kwa mfano, atayaamini mawazo yanayomvunja moyo, matokeo yake yatakuwa ni kushindwa. Mtoto mwenye mawazo yanayomnyong’onyeza hawezi kuzidi mawazo hayo. Kukata tamaa, kujizomea, kujikosea kulikopitiliza, kunamnyima fursa ya kufikiri sawa sawa.

Mzazi jenga mazoea ya kumsemea mwanao maneno yanayomjenga. Tambua mazuri anayoyafanya na yaseme maneno chanya. Usiwe na tabia ya kumkosoa mno mtoto hata kama kweli hajafanya vizuri.

Fikiria mtoto amefanya vibaya darasani. Mzazi wa kwanza anamwambia, “Nikijua tu utafeli. Kwanza huna akili. Naona napoteza tu hela kukusomesha.”

Mzazi wa pili anamwambia, “Kwa namna ninavyokufahamu, uwezo wako ni mkubwa. Najua ukikazana, ukimsikiliza mwalimu na kujisomea, uwezo wa kufanya bidii kufikia uwezo wako halisi.”

Mzazi wa kwanza anaongea kwa hasira shauri ya matajiro makubwa aliyonayo kwa mwanae. Hachagui maneno ya kumwambia mwanae kwa sababu anaamini kufeli mtihani ni kukosa akili. Hajua athari ya maneno yake katika kujenga lugha ya ndani itakayoathiri uwezo wake wa kujituma.

Mzazi wa pili anaweza kuwa na hasira lakini anajua nguvu ya maneno yake. Anamtamkia mtoto maneno yanayomtia hamasa hata katika kufeli kwake. Maneno haya chanya yatajenga lugha chanya itakayokuwa hamasa ya kufanya vizuri zaidi.

Ongeza fursa za mawasiliano

Mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuongeza uwezo wa akili anaokuwa nao mtu. Kuzungumza na mwanao mara kwa mara kunakuza uwezo wake wa lugha, msamiati wake, na hata kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Unaweza kushangaa lakini ndivyo wataalam wanavyotuambia. Wazazi waongeaji wenye tabia ya kuzungumza na watoto huwasaidia kuwa na msamiati zaidi.

Lugha ina nafasi kubwa katika kujenga uwezo wa akili.

Bila kujali umri wake, jenga mazoea ya kujadiliana na wanao masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Wape nafasi ya kukusimulia yale wanayokutana nayo shuleni, kwenye michezo, mambo wanayoyasikia mitaani, matarajio waliyonayo na hata hofu wanazohitaji kupambana nazo. Fanya mazungumzo yawe utaratibu wa kawaida wa maisha ya hapo nyumbani.

Mfano, mwombe mwanao akuambie siku yake imekwendaje. Mwuulize maswali yanayomtaka ajieleze badala ya kujibu kirahisi ‘ndiyo’, ‘hapana’ na ‘sijui.’ Mruhusu mtoto akuulize maswali na jitahidi kuyajibu kadri unavyoweza.

Mara nyingi mtoto huuliza kutaka kuyaelewa mazingira yake, kuelewa mambo anayoyaona na kukutana nayo katika maisha. Kumbuka muhimu hapa sio majibu unayompa, bali uwezo wa kufikiri, kuelewa, na kuchambua mambo anayoyasikia.

Simulia hadithi

Tangu zamani utamaduni wetu ulitambua umuhimu wa masimulizi kwa watoto. Nyakati za jioni, wazazi walikuwa na utaratibu wa kukaa na watoto wao na kuwasimulia hadithi mbalimbali.

Hadithi hizi, mbali na kukuza ukaribu baina ya wazazi na watoto wao, zilikuza uwezo wa watoto kufikiri. Hadithi, mathalani, zinatumia wahusika wenye tabia na mikakati tofauti kwa kutumia madhari ya kufikirika. Haya yote humfanya mtoto alinganisha anayoyasikia na maisha yake ya kila siku.

Siku hizi desturi hii, hata hivyo, imeanza kupungua. Watoto wanatumia muda mwingi kufanya kazi za kitaaluma ambazo mara nyingine hazihusiani na maisha yao ya kila siku. Mbali na kufifiisha uwezo wao wa kuyaelewa mazingira yao, kazi hizi nyingi zinafunga fikra zao kwenye mambo fulani pekee.

Tunahitaji kufufua desturi ya hadithi kwa watoto. Mbali na kuwasimulia, tuwape nafasi wao wenyewe wabuni hadithi kuwasaidia kujua kuchagua wahusika, kupangilia matukio na kusema wanachokifikiri.

Hamasisha usomaji wa vitabu

Sambamba na masimulizi, mzazi una fursa ya kumhamasisha mtoto kusoma vitabu. Unaweza kuanza kwa kumsomea kitabu chenye hadithi zinazogusa mambo anayokutana nayo kwenye maisha.

Usomaji wa vitabu kwa watoto si tu unaimarisha uhusiano wenu, lakini unaongeza kumbukumbu, uzingativu na hata kukuza msamiati.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa huwezi kukuza tabia fulani kwa mtoto kama wewe mwenyewe huna. Lazima kwanza uanze wewe mwenyewe kupenda kusoma ili mwanao ajifunze.

Swali kwako mzazi, kwa mwaka 2017 ulisoma vitabu vingapi? Je, uliwahi kuonekana ukisoma hapo nyumbani au muda mwingi unautumia kutazama televisheni na kutumia simu?

Je, kuna vitabu vinaonekana kwenye mazingira ya nyumbani?

Lenga kumfundisha mwanao kwa vitendo. Onekana ukisoma ukiwa nyumbani. Kama huna vitabu au magazeti, unavyo vitabu vya dini. Anza na hivyo.

Pia, mnunulie vitabu kama zawadi yake na msomee nyakati za jioni anapojiandaa kulala. Watoto wanapenda sana fursa kama hizi. Kila inapowezekana, mpeleke kwenye maduka ya vitabu na maktaba kupanda mbegu ya mtoto kuwa na urafiki wa kudumu na maandishi.

INAENDELEA WIKI IJAYO

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Tuesday, January 2, 2018

Lishe shuleni inavyokuza ufaulu mkoani Njombe

Baadhi ya wanafunzi mkoani Njombe wakipata

Baadhi ya wanafunzi mkoani Njombe wakipata chakula cha mchana shuleni. Mkoa huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha wazazi kuchangia lishe kwa watoto wao wakiwa shuleni. Na Mpiga Picha Wetu  

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Je, unataka kupandisha ufaulu na kupunguza utoro shuleni mkoani kwako? Jaribu siri hii kutoka Mkoa wa Njombe.

Ofisa elimu taaluma wa mkoa huo,  Steven Bange, anasema siri iko katika kutambua umuhimu wa chakula kwa wanafunzi wakati wa masomo.

 Kwa ajili hiyo shule zote za Mkoa wa Njombe zinatoa huduma ya chakula.

“Ilikuwa unaweza kukuta mwanafunzi anasinzia darasani, ukimuuliza nini tatizo, anakuambia njaa! Kiuhalisia si rahisi kwa mtoto huyo kumuelewa mwalimu hata kidogo,” anasema na kuongeza:

“Tuligundua kwamba kumbe si rahisi kwa mtoto kushinda shule kwa saa nane bila chakula. Muda huu unatosha kudhoofisha afya yake na matokeo ni kushindwa kumudu masomo, kwa hiyo, dawa ilikuwa ni shule zote kuingia kwenye mpango wa lishe”.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Image, Shadrack Sodike, pamoja na kuunga mkono mpango wa chakula shuleni, anasema pia mpango huo unapaswa kuwa endelevu kwani licha ya kusaidia uelewa kwa wanafunzi, umepunguza utoro.

Kwa mujibu wa Bange, tangu Mkoa wa Njombe uanze kutoa chakula, ufaulu shuleni umeongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2017, baada ya shule zote 480 za msingi na 16 za sekondari kuanzisha huduma hiyo ya chakula.

Anasema kwa maana hiyo wanafunzi 240,987 wa shule za awali, msingi na sekondari tayari wanapata huduma ya chakula shuleni.

Njombe wanatekeleza mpango huo huku takwimu zikionyesha unakabiliwa na tatizo la udumavu na kushika nafasi ya pili kitaifa kwa kuwa na asilimia 49.4.

Wataalamu wa afya, likiwamo Jukwaa la Lishe nchini (Panita) linataja njaa kuwa kati ya sababu zinazoweza kukwamisha ufaulu kwa wanafunzi.

Mtoto anapokwenda shule na kushinda huko bila kupata chakula chochote, hupoteza uwezo wa kufikiri na hivyo kutoelewa darasani hata kama mwalimu atajitahidi  kufundisha.

Twaweza, taasisi ifanyayo tafiti nyingi za mambo ya kijamii inasema katika moja ya tafiti zake kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya matokeo ya watoto kujifunza na udumavu unaotokana na utapiamlo.

Utapiamlo ni matokeo ya mtoto kutokupata chakula cha kutosha na kisicho na virutubisho muhimu mwilini.

Mtaalamu wa lishe na mratibu wa miradi wa Panita, Jane Msagati, anasema uwezo wa kujifunza wa mtoto mwenye utapiamlo ni mdogo kulinganisha na mtoto mwenye afya njema.

Mkoa wa Njombe unatekeleza mpango wa chakula shuleni wakati pia zaidi ya wanafunzi 55,000 kutoka shule 48 za msingi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, wakitarajia kunufaika na mpango wa chakula shuleni unaolenga  kuinua kiwango cha ufaulu.

Njombe walianzaje?

Kimsingi, utoaji wa chakula ulianza mwaka 2012, japo kwa wakati huo shule chache zilikuwa zinafanya hivyo.

Bange anasema matokeo ya wanafunzi yalikuwa yanaonyesha kuwa pamoja na jitihada za walimu kufundisha, ufaulu katika shule zilizokuwa zinatoa huduma ya chakula ulikuwa mzuri zaidi.

Anasema ilibidi kukaa chini na kuona namna wanavyoweza kutekeleza azimio la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari  anapata chakula.

Anasema hawakuona haya kuwahusisha wadau wengine wakiwamo wanasiasa katika kutekeleza mpango wao.

Hata hivyo, anasema mpango huo ulisuasua baada ya kuja kwa mkakati wa elimu bure uliosababisha wazazi na walezi kuona kwamba hawahusiki katika kuhakikisha watoto wao wanapata chakula shuleni.

“Ilibidi tuanze kutoa elimu kwa wazazi wote na walezi waone ya kuwa jukumu la kuhakikisha watoto wanapewa chakula shuleni linawahusu. Walilipokea kwa mikono miwili na tumefanikiwa kwa asilimia 100,” anasema.

 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyombo, Ohidelis Gwivaha, anasema kijiji chao hakina wasiwasi kuhusu suala la watoto kupewa chakula.

“Unajua tuligundua hata kijiji chetu kina watoto wenye utapiamlo, sasa tulipoambiwa tuchangie wakati huo huo tukielezwa madhara ya njaa kwa watoto, hatukusita kabisa kufanya hivyo,” anasema.

Gwivaha anasema kazi ya serikali ya kijiji hicho ni kuhakikisha wazazi na walezi wote wanatoa chakula na hilo limefanikiwa.

  Anasema pia  wana mpango mahsusi kijijini hapo wa kutoa lishe maalumu kwa watoto wenye tatizo la utapiamlo na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).

“Haya yote tunayafanya baada ya kupata elimu ya uhakika ya masuala ya lishe kwa watoto. Hatupendi kuona watoto wetu wanapata utapiamlo, kwa sababu ya uzembe wetu wakati tunao uwezo wa kuhakikisha wanakula,” anasema.

Mkazi wa kijiji cha Ilimiwaha, Thabitha Ndendya, anasema hawalazimishwi kuchangia chakula shuleni baada ya kuelewa umuhimu wake.

“Walivyokuwa wamesema elimu bure tulijua hadi chakula watoto wetu watakula bure, ila sasa tumeelewa tunajitahidi bila kusukumwa,” anasema.

Hali tofauti Ludewa

   Kwa Wilaya ya Ludewa, hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa, utoaji wa chakula shule upo tofauti.

Bange anasema wamebuni mbinu ya wazazi wa mtaa mmoja kupeana zamu ya kupika na kuwapelekea chakula shuleni watoto wao, kwa kuwa si rahisi kukusanya muhogo na kuhifadhi shule.

   “Kule wanatumia muhogo, huwezi kuukusanya muhogo kwa wananchi na kuuhifadhi shule,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makula, Clemence Wihombe anasema shule yake haina wasiwasi katika kutekeleza mpango huo.

   Anasema walimu wamejipanga kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata chakula jambo lililosaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwenye shule hiyo.

Zaidi ya ufaulu, Bange anasema pia ya kuwa Njombe ni kati ya mikoa iliyofanikiwa kupambana na changamoto ya utoro kwa sababu ya utoaji wa chakula.

Mikakati  wa kupambana na uhaba wa walimu

Kwa mujibu wa Bange, chakula ni upande mmoja tu wa jitihada za mkoa huo kukuza elimu na kiwango cha ufaulu.

Anasema katika kupambana na uhaba wa walimu, wametafuta dawa ya kumaliza tatizo hilo kwa kuwatumia walimu wanaosubiri ajira.

Takwimu zinaonyesha mkoa huo unakabiliwa na upungufu wa walimu 670 wa elimu ya awali, 1991 wa shule za msingi na 446 wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari.

Anasema kutokana na uhaba huo wa walimu ilifika hatua baadhi ya shule zilibakiwa na walimu wawili, jambo lililotishia maendeleo ya elimu kwenye mkoa huo.

“Kukiwa na walimu wawili maana yake hawapaswi kuugua, mmoja akiugua kwa mwezi tu ni tatizo kubwa, maana yake watoto hawatafundishwa. Jambo hilo lilifanya tukae kutafakari njia za kupambana nalo,” anaeleza.

Anasema kimsingi mtaani wapo walimu wengi waliomaliza masomo yao lakini hawana kazi.

“Tulipogundua hawa wanaweza kutusaidia, ilibidi tuziagize kamati za shule zenye uhaba kuandaa utaratibu wa kuhakikisha walimu hawa wanapewa kazi ya kufundisha kwa ujira mdogo wakati wanasubiri ajira,” anaeleza.

Tuesday, January 2, 2018

Camfed lilivyomuokoa msichana Victoria

Victoria Fedelis, mmoja wa wanufaika wa mpango

Victoria Fedelis, mmoja wa wanufaika wa mpango wa asasi ya Camfed inayojihusisha na kusaidia kielimu watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Picha na Sharon Sauwa 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Victoria Fedelis mkazi wa kijiji cha Gongwe Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro,  ni miongoni mwa wasichana wanaoishi katika mazingira magumu ambao wamelazimika kuacha kujiendeleza kielimu ili kuwasaidia wadogo zake kutokana na kipato kidogo cha familia.

Kwa mujibu wa Shirika laUmoja wa Mataifa  la Kuhudumia Watoto (Unicef) inakadiriwa kuwa watoto 120 milioni wanaishi  mitaani na katika mazingira magumu duniani, huku bara la Afrika likiwa na watoto 30 milioni.

Tanzania inatajwa kuwa  miongoni mwa nchi zenye changamoto kubwa kwa kuwa na ongezeko la watoto hao kila kukicha.

“Baba yangu alimtelekeza mama yangu tukiwa wadogo, hivyo tulilelewa na mama ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza nyanya. Maisha yalikuwa magumu fedha iliyopatikana ilikuwa ni kwa ajili ya chakula, malazi na afya,”anasema.

Anasema alipofika darasa la saba alifaulu na kuchaguliwa kwenda kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Gondwe Wilaya ya Kilosa lakini kutokana na maisha aliyokuwa akiishi nyumbani, alikata tamaa  ya kuendelea na masomo.

 “Nilikata tamaa kabisa, niliona hakuna uwezekano wa kusoma tena baada ya kuona hali ya maisha tuliyokuwa tukiishi ingawa nilifaulu na kuchaguliwa kwenda sekondari,” anasema.

Anasema alikaa muda mrefu nyumbani akisubiri labda atatokea mtu wa kumfadhili ili aweze kuendelea na masomo yake ya sekondari.

Victoria anasema akiwa nyumbani ulipita usajili wa kuangalia watoto waliokuwa katika mazingira hatarishi na kubahatika kupata ufadhili wa kusomeshwa.

 “Nikiwa mazingira ya nyumbani alikuja mwalimu mkuu wa sekondari, kiongozi wa kijiji na mwalimu wa shule ya msingi, wakatuhoji jinsi gani mama alivyoshindwa kunisomesha mimi elimu ya sekondari. Mimi nilijieleza yote,”anasema.

Anasema baada ya mahojiano hayo,  waliitwa yeye na kaka yake  kusaini mkataba na shirika lilajihusisha na kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi la Camfed linalojihusisha na kusaidia watoto wanaoshi katika mazingira magumu.

“Ndoto yangu ilitimia nikaanza masomo yangu ya sekondari kwa kulipiwa ada ya shule na gharama nyingine za kuniwezesha kusoma na shirika hilo,”anasema.

Victoria anasema ingawa Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi wa msingi hadi sekondari lakini suala la ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi ni jambo la msingi,  ili kuwawezesha wanafunzi wa kike kuepuka changamoto wanazokutana nazo njiani na nyumbani.

“Kuna changamoto kwa mfano,  mtoto wa kike akirudi nyumbani ana shughuli za shamba inabidi amsaidie mzazi, kuna kupika na kuwasaidia wadogo zako unajikuta huna muda wa kusoma lakini ukikaa bweni unakuwa na muda mrefu wa kusoma,” anasema.

Anasema yeye alikuwa analazimika kutembea umbali wa kilomita 10 kwenda na kurudi shuleni kila siku na alikuwa anaamka saa 11 asubuhi ili awahi shule.

Anasema aliporudi nyumbani alikutana na shughuli za nyumbani ikiwa ni pamoja na kufanya usafi, kupika na kuwalea wadogo zake, jambo lililomkosesha muda wa kusoma.

“Watoto wa kiume mara nyingi wanapata muda wa kujisomea wakirudi nyumbani kwa sababu hawakutani na kazi, lakini kwa watoto wa kike inakuwa ngumu,”anasema.

Maisha kwa  sasa

Baada ya kumaliza shule, Victoria hakuchaguliwa kujiunga na masomo ya juu ya sekondari na hivyo alibakia nyumbani ingawa alikuwa na kiu ya kwenda chuoni.

Uamuzi wa kutohangaika  kutafuta elimu zaidi, ulitokana na wadogo zake wanaomfuatia kuhitaji msaada wake kimasomo na hivyo aliamua kujikita katika ujasiriamali.

“Nilianza kupika maandazi baada ya kupata mtaji kutoka katika kampuni ya Wachina ambayo nililipwa Sh15,000 kama ujira wa kufanya kazi ya kupanda mahindi katika shamba lao. Nilipopata fedha hizo nilizigawa nusu nikanunua debe la mahindi kwa ajili ya chakula nyumbani na zilizobaki nilianzisha mradi wa kupika maandazi,”anasema.

Anasema pia utaratibu wa Camfed baada ya kumaliza masomo chini ya ufadhili wa shirika hilo, ni mnufaika kuwasaidia wengine ikiwa ni kurudisha fadhila za kusomeshwa.

Harakati za Camfed

Mwenyekiti wa Bodi ya Camfed, Jeanne Ndyetabura anasema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2006,  miradi   inayotekelezwa kwa kushirikiana  na jamii imeweza kuwasaidia watoto 199,008 wa shule 675 za msingi na sekondari nchini.

Anasema watoto hao wamepata msaada wa ufadhili wa  shule kama vile ada, sare za shule, malazi na vifaa  vya usafiri.

“Ufaulu kwa wanafunzi wanaopata ufadhili umefikia asilimia 55.1 kwa mwaka 2016 kutokea asilimia 50.3 mwaka 2015. Na kwa shule zinazopata ufadhili, ufaulu umefikia asilimia 57.5 kwa mwaka 2016 kutoka asilimia 55.4  mwaka 2015,”anasema.

Jeanne anaomba wasichana wanaoishi katika mazingira magumu kupewa kipaumbele, pindi wanapoomba kujiunga  katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

“Kwa mfano tungetamani kuona wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu wanapatiwa asilimia 100 ya mikopo wa elimu ya juu pale wanapomba. Pia tunaomba kuwapo kwa  njia mbadala za kujifunzia hasa kwa wanafunzi  waliokwishatoka katika mfumo rasmi wa elimu,”anaeleza.

Tuesday, December 19, 2017

Utafiti; Motisha kwa walimu itaondoa mbumbumbu

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Kujua kusoma, kuhesabu na kuandika, hutegemea mwalimu.

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mwanafunzi anayeweza kuvuka darasa pasipo jitihada za mwalimu.

Ni mwalimu huyohuyo pia anaweza kusababisha wanafunzi wakahama madarasa na hatimaye kuhitimu elimu ya msingi wakiwa mbumbumbu.

Utafiti wa ‘Uwezo’ chini ya uratibu wa shirika la Twaweza, uliofanyika mwaka jana, unaonyesha kati ya wanafunzi 10 wanaomaliza darasa la saba, watatu hawawezi kufanya hesabu za darasa la pili, wakati nusu ya wanaomaliza elimu hiyo sawa na asilimia 49.1, hawawezi kusoma hadithi kwa Kiingereza.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Aidan Eyakuze anasema changamoto za wanafunzi kushindwa kujifunza,ndiyo iliyowasukuma kufanya utafiti mwingine wa namna ya kuboresha ufundishaji.

Japo upo usemi kwamba ualimu ni wito, bado ari ya walimu kufundisha inaweza kuongezeka mara dufu wanapothaminiwa ikiwamo kupewa motisha.

“Tunaitaka Tanzania ya viwanda, lakini ili tuifikie ni lazima kuhakikisha watoto wetu wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika. Mwalimu ndio chanzo cha uwezo na uelewa wa watoto wetu hivyo kukiwa na walimu bora watoto watajifunza,” anasema.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa ‘KiuFunza’, kuwalipa walimu motisha kunaongeza ari ya kufundisha na kuleta matokeo chanya ya wanafunzi kujifunza.

Katika utafiti huo, asilimia 91 ya walimu waliohojiwa wanakiri kuwa motisha ni dawa ya kuongeza kiu ya kufundisha na kufaulisha.

Eyakuze anasema utafiti wao unaonyesha kuwa walimu na uwajibikaji ni mambo ambayo yamekosekana shuleni na ndiyo yanayochangia kupunguza kiwango cha kujifunza.

INAENDELEA UK 16

INATOKA UK 15

“Motisha inaweza kuboresha matokeo ya kujifunza, japokuwa kujifunza kunachangiwa na mambo mengi. utafiti huu unaonyesha kuwa kuchanganya motisha na uwajibikaji kutaleta matokeo mazuri,” alisema.

Utafiti ulivyofanyika

Twaweza katika utafiti wao walitoa kati ya Sh8, 100 hadi Sh3.6 milioni kama motisha kwa walimu 788.

Awali fedha hiyo iliahidiwa kwa walimu mwanzo wa mwaka, kwamba mwisho wa mwaka wale watakaowawezeha wanafunzi wao kupata stadi za kujifunza, watapewa motisha.

Eyakuze anasema utafiti huo uliwalenga wanafunzi wa darasa la kwanza, pili na tatu na uliwahusisha wanafunzi 65,643 katika shule za msingi 135 za wilaya 21 nchini, katika kipindi cha miaka miwili.

Hata hivyo uwiano ulikuwa kati ya shule zilizo na walimu walipewa motisha na zile zisizo na walimu waliopewa motisha.

Mkurugenzi huyo wa Twaweza anasema wanafunzi 48,042 waliokuwa kwenye shule zilizopewa motisha waliweza kujifunza zaidi kuliko wenzao waliokuwa kwenye shule zisizo na walimu waliopewa motisha.

Kutokana na utafiti huo, watoto waliofunzishwa na walimu wenye motisha walikuwa na uwezo wa kujifunza zaidi na kuelewa zaidi stadi za kujifunza kuliko wenzao.

Kulingana na utafiti huo, mtoto aliyefundishwa na mwalimu aliyepewa motisha anauwezo wa kujifunza stadi kwa mwaka mmoja wakati mwingine, anatumia mwaka mmoja na nusu.

“Watoto waliofundishwa na mwalimu aliyeahidiwa motisha anaelewa zaidi kuliko anayefundishwa na walimu asiye na motisha,” anasisitiza.

Mkurugenzi huyo wa Twaweza anasema ni ukweli usiopingika kwamba fedha ni kichocheo kikubwa cha mtu yeyote kufanya vizuri kwenye kile anachokifanya.

Hivyo fedha inaweza kutumika kama kichocheo cha motisha kwa walimu, na kuongeza ufaulu.

Walimu wazungumzia utafiti

Walimu waliofikiwa na utafiti huo wanakiri kuwa motisha inaongeza ari ya kazi.

Mwalimu wa shule ya Msingi Mtongani Jijini Dar es Salaam, Hellen Mbogo anasema motisha inaweza kumfanya mwalimu akapata mbinu nyingine mpya za kuhakikisha mwanafunzi anafanya vizuri ikiwamo, kumfuatilia kwa wazazi wake.

“Darasa langu lina wanafunzi 250 ambao huwa nawagawa kwenye makundi, hatuwezi kuwafundisha pamoja kwa sababu ya uwingi,”anasema.

Anasema kwenye shule yake, wameanzisha darasa maalum kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaojifunza polepole ili kuwanoa jambo lililosababisha ifanye vizuri wakati wa utafiti.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbweni jijini Dar es Salaam, Moses Amani anasema mfanyakazi yeyote anapopewa motisha kwenye kazi anayoifanya, anaongeza uwezo wa kuelewa na kufanya.

“Nilipata pia motisha kwenye huu utafiti, kwa kweli inaongeza ari ya kazi kwa sababu ilitufanya walimu kushirikiana na kufanya kazi pamoja,” anaeleza.

Mratibu wa utafiti huo Wilaya ya Kinondoni, Sofia Komba anasema awali walipowapelekea walimu suala la kupewa posho mwisho wa mwaka watakapofanya vizuri kiufundishaji, wengi walipuuza wakiona haiwezekani.

Lakini mwaka wa kwanza wa utafiti, walimu walioingia kwenye utafiti huo walipewa posho jambo lililosababisha wengine kuongezeka kwenye utafiti kwa mwaka wa pili.

Upo umihimu wa Serikali kutunza sera itakayoelezea masuala ya motisha, ikiwa kweli tunataka kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayeachwa nyumba kitaaluma.

Wachambuzi wazungumza

Baadhi ya wadau wa elimu wamekiri kwamba motisha inaweza kuongeza ari ya kufundisha na kufaulisha lakini wamekosoa utafiti huo kuwa sio motisha ya fedha (Bahshish) kwa walimu ndiyo kunaweza kunaweza kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Profesa Marjorie Mbilinyi anasema fedha sio motisha peke yake inayoweza kutumika kuwapima walimu, katika kuwaongezea ari ya kujifunza.

Anasema pamoja na fedha, Twaweza wangeweza kutizama aina nyingine ya motisha ambayo, walimu wanaweza kupatiwa katika kuongeza ari ya kufundisha shuleni.

Profesa Mbilinyi anaeleza kuwa mazingira mazuri ya kufundishia, sehemu nzuri za kuishi na uboreshaji wa mfumo wa ufundishaji vinaweza kuwa motosha kwa walimu.

Mshauri wa Elimu, Beatrice Omary anasema utafiti huo haukuweza kuonyesha jitihada zilizowahi kufanywa na Serikali au mashirika mengine katika kuboresha mazingira ya walimu.

Anasema kabla ya utafiti wao, walipaswa kuangalia kazi nyingine zilizofanywa ili kujua matokeo gani yalipatikana.

“Ili kujua kama kumpatia mwalimu pesa moja kwa moja kutasaidia basi zingeangaliwa jitihada nyingine zilizowahi kufanywa zimefanyaje,” anahoji.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Baraza la Mitihani nchini, Dk Alfred Mdimo anasema kwa sababu katika uwasilishaji wa utafiti huo walitoa takwimu zinazoonyesha asilimia 30 ya wanafunzi wanaofikia darasa la saba hawana stadi za kujifunzia za darasa la pili, wangekuja na suluhisho la kuondoa tatizo hilo.

“Utafiti wao ungeonyesha pia katika hao walimu walioahidiwa kupewa motisha, wangapi waliwezesha wanafunzi waliokuwa hawajui kusoma na kuandika kujua, na wale walioshindwa,” anaeleza.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), Audast Muhina anasema ni kweli kwamba motisha inaweza kuongeza ufaulu japo fedha sio njia peke yake ya kumpa motisha mwalimu.

Anasema huenda matumizi ya fedha yakawa makubwa zaidi ikiwa njia hiyo itatumika kwenye kumpa motisha mwalimu ili kumuongezea ari ya kufunzisha.

Tuesday, December 19, 2017

Ndoto ya ualimu ilivyopotea kwa Khalfani

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchi@co.tz

Pamoja na ulemavu wa macho alionao, hakuacha kuwa na ndoto ya kutaka kuwa mwalimu. Ni ndoto aliyokuwa nayo Khalfan Machaku, mkazi wa eneo la Songe Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga. Tangu utotoni alitaka kuwa mwalimu tena wa masomo ya sayansi.

“ Nilikuwa napenda ualimu tangu mdogo, ningependa kufundisha sayansi,” anasema.

Leo akiwa na umri uliojongea, anakiri kuwa ndoto hiyo ilishayeyuka. Khalfan hataki kusikia neno elimu na hata akipatikana wa kufadhili masomo, anasema hatokubali kusoma zaidi ya miaka mitatu.

“ Kwa sasa sitamani kusoma, muda umepita, kwa zamani nilitamani,”” anasema Khalfan ambaye jitihada za kujiendeleza zilikwama baada ya kukosa mtu wa kumuonyesha njia ya kujiendeleza.

Jitihada zake

Kipindi cha mwisho cha jitihada zake za kutaka kusoma anakumbuka kilikuwa miaka ya 1998,alipofuatwa na uongozi wa Serikali wilayani Korogwe kwa ajili ya kupatiwa nafasi ya kusoma Tanga Mjini.

Anasema kilichomkosesha kupata nafasi hiyo ni uwezo mdogo wa kifedha, kwa kuwa alitakiwa atoe anachokitaja kama ‘ kitu chochote’ ili apate fursa hiyo.

“ Niliitwa nikahojiwa wakasema watanitafuta, muda ulipofika hawakunitafuta, nikasikia nafasi zile zimejaa,” anasema na kuongeza:

“ Ilikuwa Serikali iliyokuwa ikitafuta walemavu na kwa Korogwe, aliyekuja alikuwa mkuu wa wilaya mwenyewe.

Pengine fursa hiyo ingebadilisha mwelekeo wa maisha aliyonayo sasa, maisha ya utegemezi kutoka kwa wengine.

Walemavu Kilindi

Khalfan anawakilisha watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kilindi, wanaokosa fursa ya elimu kwa kuwa wilaya haina shule kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona.

Sio Kilindi pekee, karibu wilaya zote mkoani Tanga hazina shule maalumu kwa ajili ya walemavu wa macho. Shule pekee ipo Tanga Mjini. Hali hii bila shaka inapeperusha ndoto za walemavu wengu akiwamo Khalfan, ambaye kama angebahatika kusoma, pengine leo angekuwa mwalimu.

Maisha yake

Kwa sasa Khalfan anajishughulisha na udalali wa mazao, kazi anayosema angalau inampatia fedha za kujikimu kimaisha.

Kinachomuuma ni kuwa akiwa Kilindi, hajawahi kufuatwa na kiongozi hata mmoja kujua mustakabali wa maisha yake.

“ Nikikutana na kiongozi yeyote kwa mfano mkuu wa wilaya au mkurugenzi wa halmashauri, nitamwambia anijengee nyumba. Jambo la pili, aniwezeshe kupata mtaji wa biashara.Naweza kufanya biashara za aina nyingi.” anaeleza.

Wito kwa Serikali

Khalfan anaisihi Serikali kuwa karibu na watu wenye ulemavu na kuwaendeleza.

“ Kwa wale ambao hawajasoma, Serikali iwasaidie kimaisha kwa namna inavyoweza,” anaeleza.

Pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kuhakikisha watu wenye ulemavu wananufaika na fursa za kielimu, changamoto za uchache wa shule kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu haina budi kufanyiwa kazi.

Ni udhaifu mkubwa kuona Mkoa mkubwa kama Tanga ukiwa na shule moja inayohudumia watoto wenye ulemavu wa macho. Hadithi ya Khalfan leo ingeweza kuwa nyingine kama angepata fursa ya kusoma ndani ya wilaya anamoishi.

Tuesday, December 12, 2017

Utoro unavyozalisha wanafunzi mbumbumbu wilayani Kilindi

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Majengo

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Majengo wakicheza katika viwanja vya shule. Walimu wanalalamika utoro mkubwa wa wanafunzi, jambo linalochangia wanafunzi wengi kutojua stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.  Picha na Abeid Poyo. 

By Abeid Poyo, Mwananchi aabukar@mwananchi.co.tz

Pongezi kwa Serikali kuhakikisha vitabu sio kitu adimu tena shuleni.

Hivi sasa katika shule nyingi nchini, uwiano wa wanafunzi na vitabu unakaribia 1:1, yaani mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.

Hiki ndicho kilichopo katika Shule ya Msingi Majengo iliyopo Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Wanafunzi wa darasa la pili shuleni hapo wapo darasani.

Juu ya madawati kumejaa vitabu vya somo la Kiswahili. Karibu kila mwanafunzi ana kitabu chake kilichoandikwa: Najifunza kuandika.

Wanafunzi hawa wamebakisha siku chache kuingia darasa la tatu, ngazi ya elimu ambayo inatarajiwa kila anayebahatika kuifikia awe tayari ameshazijua stadi muhimu za kusoma, kuandika, kuhesabu na hata kufanya hesabu rahisi.

Hata hivyo, hali haiko hivyo katika darasa hili la watoto 164. Naamua kuwapitia baadhi ya wanafunzi ili kupima uwezo wao wa kujua kusoma.

Namuonyesha mwanafunzi mmoja sentensi hii: ‘Nyumba inafanyiwa matengenezo’. Anayatazama maandishi kwa sekunde kadhaa, hakitoki kitu mdomoni mwake, na kadri muda unavyoyoyoma, nabaini kuwa sentensi hiyo imemshinda.

Mwingine namtaka anisomee sentensi: ‘Amina ni mwanafunzi’ Huyu hakusubiri kupoteza muda, kwa haraka akakiri kuwa hajui kusoma.

Kwa mujibu wa mwalimu wa darasa, Jenny Msigwa, hali hiyo sio jambo geni kwao, kwani katika darasa hilo la wanafunzi 164 wanaojua kusoma hawazidi 20.

Utoro unatajwa kama sababu kuu inayochangia maendeleo duni ya taaluma. Mwalimu Msigwa anasema karibu nusu ya wanafunzi wa darasa hilo ni watoro wa kudumu.

Kibaya zaidi kwa mujibu wa walimu, sio wazazi wala viongozi wa serikali ya kijiji wanaoonyesha dhamira ya dhati ya kuisaidia shule kupambana na hali hiyo.

‘’ Wazazi hawana ushirikiano, wanatukatisha tamaa, tumeamua kupambana na hali zetu. Ukiona anayejua kusoma basi ni yule anayekuja shule kila siku,’’ anasema mwalimu Msigwa anayelalamikia pia idadi kubwa ya wanafunzi, jambo linalompa wakati mgumu kumpitia kila mwanafunzi wakati wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mazingira yanavyochangia

Pamoja na utoro kutajwa kuwa sababu ya wanafunzi hao kutojua kusoma, mazingira ikiwamo miundombinu shuleni sio rafiki. Darasani wanafunzi wanasongamana.

Wanafunzi wanasema hawapati chakula cha mchana, licha ya walimu kusema kuwa wamekuwa wakiwapatia uji mchana.

Shule ina mashamba ya mazao kadhaa yakiwamo maharage na miembe. Wakati wa msimu, angalau embe hutumika kupunguza ukali wa njaa kwa wanafunzi.

Kwa maharage, mwalimu Ezekiel anasema mapato ya mavuno yake hutumika kugharimia baadhi ya masuala ya uendeshaji wa shule.

Mkakati wa shule

Mwalimu Mkuu, Joel Ezekiel, anasema wameamua kuushirikisha uongozi wa kijiji uwasaidie kuhusu kadhia hiyo kwa kupeleka majina ya wanafunzi watoro. Hata hivyo, analia ushirikiano mdogo wanaoupata walimu.

‘’ Tumechukua hatua ya kupeleka orodha ya wanafunzi watoro kwa hatua ya awali. Nasikitika bado hawajachukua hatua yoyote. Nilitaka nipeleke orodha nyingine lakini ile ya awali haijafanyiwa kazi na sijapewa jibu wamefikia wapi,’’ anasema.

Awali mwalimu Ezekiel anasema kwa kupitia vikao na wazazi waliamua kuweka adhabu ya Sh 1000 kwa kila siku ambayo mtoto atatoroka shule, suala analosema mwishowe halikuwa na tija.

Mmoja wa wazazi, Msekwa Mbotwe, anasema tangu mwaka 2017 uanze hajawahi kukanyaga shule iwe kwa kuhudhuria vikao au kufuatilia maendeleo ya mwanawe.

Kuhusu sababu ya kutofanya hivyo, anasema:’’ Sijawahi kuletewa barua ya kutakiwa kwenda shule.’’ Kwa Mbotwe, elimu ya mtoto wake ni mpaka aletewe barua kutoka kwa walimu!

Mwalimu Ezekiel anasema wanapoitisha mkutano katika shule hiyo yenye wanafunzi takriban 970, wazazi wanaohudhuria hawazidi 50!

Uongozi wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo anasema wanajitahidi kupunguza wimbi la wanafunzi kutoroka shule. Utoro uliopo sasa ni ule anaouita; ‘ utoro wa rejareja’ ambao pia wanaushughulikia.

‘’Hali ya utoro inapungua, bado upo utoro wa rejareja tunaoushughulikia. Kama Serikali tunaendelea kuwahamasisha. Nikienda katika vikao nawahamasisha kuhusu elimu kuwa ni wajibu wao,’’ anaeleza.

Mwamko mdogo wa elimu

Kilindi ni kati ya maeneo ambayo wakazi wake wengi bado hawajatambua thamani ya elimu kwa watoto wao.

Kwa Kilindi, uchunguzi mdogo wa Mwananchi, umebaini kuwa sio tukio geni kwa mzazi kumshtaki mwalimu au kumpa vitisho kwa kuwa tu amemrudi mwanawe mwenye matatizo ya kinidhamu.

Mwalimu mmoja (jina tunalihifadhi), anasema baadhi ya wazazi wamefikia hatua ya kujenga uadui na walimu.’’

‘’Kijijini kitu anachouziwa mwanakijiji mwingine kwa Sh 500 mimi mwalimu nauziwa kwa Sh 700, maji ya Sh 300 mimi napandishiwa bei,’’anasema mwalimu huyo.

Uchunguzi unaonyesha wakazi wengi wa wilaya hii iliyomegwa kutoka Wilaya ya Handeni, hawajasoma au wameishia darasa la saba.

Tatizo la kitaifa

Bila shaka wanafunzi wa Shule ya Msingi Majengo, ni kiashiria cha kuwapo kwa wanafunzi wengi nchini wanaovuka darasa la pili wakiwa hawana stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK.

Mfumo wa elimu nchini unamtarajia mwanafunzi wa darasa la pili awe na uelewa wa kutosha wa stadi hizo muhimu katika mchakato wa ujifunzaji na maisha kwa jumla.

Kisa cha shule hii kinashadadiwa na matokeo ya mara kwa mara ya tathmini za Uwezo zinazofanywa na asasi isiyo ya kiraia ya Twaweza.

Aghalabu, tathmini hizo zinazojumuisha watoto wenye umri kati ya miaka saba hadi 16, hubaini kuwapo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wakiwamo wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kwa mfano, matokeo ya tathmini ya mwaka 2015 iliyojumuisha watoto 32,694 kutoka kaya 16,013 na shule za msingi 1,309, yanaonyesha baadhi ya watoto wa darasa la saba walishindwa kufanya majaribio ya darasa la pili.

‘’Wanafunzi wanne kati ya 10 (sawa na asilimia 44) hawawezi kusoma hadithi ya Kingereza ya kiwango cha darasa la pili, wawili kati ya 10 (asilimia 16 ) hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili, na wawili kati ya 10 (asilimia 23 ) hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la pili,’’ inasema sehemu ya ripoti yab tathmini hiyo iitwayo; Je watoto wetu wanajifunza? Hali ya Elimu nchini Tanzania mwaka 2015.     

Tuesday, December 12, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Ninakwenda shule au ninakwenda shuleni?

 

By Erasto Duwe

 Imezoeleka kwa baadhi ya watumiaji wa Kiswahili kutumia tungo kama hizi: ‘Ninakwenda shule’, ‘Nipo chuo’, ‘Natoka hospitali’ na kadhalika.

Tungo zifuatazo kimuundo zinalingana na tungo tajwa juu. Ebu tuziangalie na kuzichunguza: (i). Ninakwenda ofisi* (ii). Nipo kanisa.* Kwa mtumiaji wa Kiswahili aliyezoea kutamka ‘Ninakwenda shule’ au ‘Nipo chuo’ anaweza kuona kwamba matumizi hayo ni sahihi. Kulingana na kanuni za lugha, tungo hizo si fasaha.

Maneno ‘shule’, ‘chuo’ na ‘hospitali’ ni nomino katika aina za maneno. Kulingana na taratibu za lugha, vitenzi ‘ninakwenda’, ‘nipo’ na ‘natoka’ katika muktadha huo havipaswi kufuatiwa na nomino kama ilivyo katika mifano hiyo hapo juu. Badala yake, vitenzi hivyo vinapaswa kufuatiwa na vielezi (vya mahali). Kwa sababu hiyo, tungo hizo zinapaswa kuwa ‘ninakwenda shuleni’, ‘nipo chuoni’ na ‘natoka hospitalini’.

Tukichunguza tungo namba (i) na namba (ii), tunaona kwamba tungo hizo zina makosa ya wazi ilhali zile za awali (ninakwenda shule, nipo chuo, nakwenda hospitali) ni vigumu kuona makosa hayo kwa kuwa watumiaji wengi wa Kiswahili wamekuwa wakizitumia na kuona kwamba ni sahihi. Kama ufasaha unavyokosekana katika tungo (i) na (ii) juu, ndivyo tungo hizi zinavyokosa ufasaha pia.

Sentensi (i) na (ii) kwa ufasaha zingepaswa kuwa: ‘Ninakwenda ofisini’ na ‘Nipo kanisani’.

Kulingana na uchunguzi mdogo uliofanywa na Mbalamwezi ya Kiswahili, watumiaji wengi wa lugha hususan wa maeneo ya mijini, hupenda kutumia lugha kwa namna hiyo (ninakwenda shule, nipo chuo na natoka hospitali), watumiaji wa Kiswahili wa Dar es Salaam na Pwani wakiongoza. Itambulike kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni za ufasaha wa lugha.

Aidha, kwa wale wanaotokea katika maeneo yasiyo ya mijini wao hawana shida katika hilo ingawaje wana namna yao ya kubananga katika muktadha huo. Kwa mfano, utasikia baadhi yao wakisema, “Nakwenda kanisanini”* badala ya “Nakwenda kanisani” au wengine husema “Nakwenda bustani”* badala ya “Nakwenda bustanini”. Jambo la msingi la kuzingatiwa katika muktadha kama huu ni kwamba mofimu ‘ni’ huongezwa kwenye nomino inayohusika ili kuunda kielezi kitakachoendana na kitenzi hicho.

Kwa hivyo, mwishoni mwa neno mathalani ‘bustani’ huongezwa ‘ni’ na kuwa ‘bustanini’. Aidha, kwa kuwa neno ‘kanisa’ ndiyo nomino, ‘ni’ huongezwa mbele ya nomino hiyo na kuunda neno ‘kanisani’ na siyo ‘kanisanini’ kama wengine walivyozoea kulitumia.

Pia, wapo watumiaji wengine wa lugha ambao badala ya kutumia ‘ni’ mwishoni mwa nomino husika, hutumia ‘kwa’ kwa lengo la kuonesha mahali ambapo tukio hutendeka. Kwa mfano, mtumiaji wa lugha huweza kusema, “Nakwenda kwa ofisi”. Matumizi ya ‘kwa’ katika muktadha huo hayaendani na taratibu za lugha. Mtumiaji huyu wa lugha kwa kuzingatia kanuni za lugha alipaswa kusema, “Nakwenda ofisini.” ‘Kwa’ hutumika ikiwa jina au cheo cha mtu kinahusika. Mathalani, “Nakwenda kwa mwalimu”

Aidha, yapo maneno ambayo watumiaji wa lugha huyatumia kwa makosa. Kwa mfano, neno ‘mchanga’ hutumika hivyo katika umoja na wingi. Baadhi ya watumiaji wa lugha wanapolitumia katika muktadha wa wingi hulitaja kama ‘michanga’. Utumiaji huo si fasaha. Maneno mengine yanayotumika visivyo ni ‘dazani’ badala ya ‘dazeni’ likiwa na maana ya ‘jumla ya vitu kumi na viwili’. Halikadhalika, neno ‘deksi’ hutumiwa kwa makosa badala ya ‘deski’likiwa na maana ya dawati.     

Tuesday, December 12, 2017

P4R; mpango uliobadilisha maisha ya wanafunzi Ukerewe

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pius Msekwa

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pius Msekwa iliyopo Ukerewe, Ally Yusuf akionyesha majengo ya vyoo vya kisasa, yaliyojengwa shuleni hapo.Na Mpigapicha Wetu 

By Oliva Kato

Elimu ni ufunguo wa maisha; Elimu ni bahari haina mwisho. Misemo hii inadhihirisha kuwa, ili binadamu aweze kuendesha maisha yake katika misingi inayokubalika, lazima awe ameelimika.

Ni kwa sababu hii jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya watu walioelimika. Katika jitihada hizo, upo mpango uitwao;: Lipa kulingana na Matokeo au kwa Kiingereza , Program for Results (P4R).

Huu ni mfumo mpya wa kufadhili sekta ya elimu ambao unatumiwa na Benki ya Dunia (WB), Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) na Wakala wa Maendeleo ya Kimataifa Sweden (SIDA).

Kupitia mfumo huu, fedha hutolewa kwa kukidhi vigezo vilivyokubalika baada ya kufanyiwa uhakiki na kuthibitika utekelezaji wake umefikiwa.

Huu pia ni mfumo wa ufuatiliaji ambao unahakikisha kuwa vipaumbele vya sekta ya elimu vinatekelezwa kwa kuzingatia mipango na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka husika.

Fedha zilizopatikana kupitia programu hii hutumika katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Kupitia programu hii Wizara imendelea kushirikiana na Tamisemi katika kuratibu uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.

Umekuwa ukitoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo, ofisi za walimu, uzio wa shule, visima, maktaba na maabara katika shule mbalimbali za umma zenye mahitaji makubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine chakavu katika shule hizo.

Hadi sasa ujenzi na ukarabati wa jumla ya madarasa 1,405, matundu ya vyoo 3,394, ofisi za walimu sita, mabweni 261, mabwalo tisa, nyumba za walimu 11, majengo ya utawala katika shule 13, maabara 3, uwekaji wa uzio katika shule 4, maktaba 2 na uwekaji wa umeme katika shule 2 upo katika hatua mbalimbali na hadi sasa halmashauri 129 zimenufaika kupitia mpango huu.

Ukerewe ilivyonufaika

Miongoni mwa halmshauri zilizonufaika ni pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe iliyopo mkoani Mwanza ambapo Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Frank Bahati anasema wilaya yake awali ilikuwa na shule za kidato cha kwanza mpaka cha nne kwa muda mrefu, lakini baada ya kupata fedha za P4R, halmashauri hiyo imeweza kujenga vyumba vya madarasa, mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano.

“Tulianza na miundombinu michache lakini Serikali ilisikia kilio chetu na tunaishukuru kwa kutambua umuhimu wa kuanzisha kidato cha tano wilayani humu, kwani tulikuwa na shule za kidato cha kwanza na nne tu, lakini sasa tuna kidato cha tano na sita. Aidha, wanafunzi wanakaa hapahapa shuleni kwa kuwa tayari tuna mabweni” anasema.

Bahati anasema wilaya yake imepatiwa kiasi cha fedha Sh518 milioni kutoka P4R ambazo zimeshatumika katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule za sekondari za Pius Msekwa na Bukongo zilizoanzisha mchepuo wa kidato cha Tano.

“Katika shule hizi mbili tumejenga mabweni mawili mawili, vyumba vya madarasa vinne, matundu ya vyoo 10 na ukarabati wa maabara katika shule. Katika shule ya Pius Msekwa wameongeza maabara ya Fizikia kwa ajili ya kidato cha tano na sita,’’ anasema na kuongeza:

‘’Ujenzi huo wa mabweni utawezesha wanafunzi wa kidato cha tano na sita kukaa na kusoma katika mazingira ya shuleni na kupunguza mwendo mrefu wanaotembea wanafunzi na kuacha kujiingiza katika makundi mbaya.’’

Wasaidia tatizo la mimba

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomih Chang’ah, anasema programu ya P4R ni mkombozi kwa wananchi wa Ukerewe, kwani pamoja na kuwezesha kuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita, lakini pia umeweza kusaidia katika mikakati ya kupunguza na kuondoa tatizo la mimba shuleni.

“Programu hii kwangu naona ilikuja kwa wakati mwafaka kwani imeweza kuifanya wilaya hii kwa mara ya kwanza kuwa na masomo ya kidato cha tano, lakini pia kuondoa tatizo la mimba kwani wanafunzi wote waliokuwa wanapanga mitaani watapata nafasi ya kukaa mabwenini,” anasema.

Oliva Kato ni Ofisa habari mwandamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.     

Tuesday, December 12, 2017

Sifa na faida za darasa linaloongeaJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

Darasa linaloongea ni lile lenye uwezo wa kumfanya mwanafunzi ajifunze kulingana na mahitaji yake hata asipokuwapo mwalimu.

Ni darasa  linaloongeza thamani, mtazamo chanya, furaha na amani ya akili ya mwanafunzi.

Zana mbalimbali zilizowekwa katika kona za darasa hilo na zilizobandikwa, humfanya mwanafunzi apende kujifunza zaidi na kuhudhuria shuleni bila kukosa.

Mkufunzi na mwezeshaji  kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Aisha Gguhiya anaeleza kuwa darasa linaloongea ni darasa  lililosheheni zana za kujifunzia na kufundishia.

Darasa hilo linaweza kutofautiana kulingana na muundo wa darasa na ubunifu wa walimu husika.

Zana zilizomo katika darasa hilo zinaweza kuwa katika mfumo wa picha za kuchorwa, picha za kubandikwa mbegu za nafaka, vitambaa, majani ya mimea mbalimbali au mchanga.

Zikiandaliwa hubandikwa katika kuta za darasa ili wanafunzi waweze kuona. Wakati mwingine hubandikwa hata juu ya dari kulingana na ubunifu wa walimu.

Darasa linaloongea huwa na kona mbalimbali za kujifunzia. Kwa mfano, kona za ujifunzaji,  kona ya hisabati (kuhesabu), kona ya uchoraji, kona ya kuandika, kona ya kusoma na kona ya baadhi ya vitu halisi ambavyo pia husababisha mvuto kwa watoto au wanafunzi.

Pia, kunaweza kuwa na kona ya toyi midoli inayotumika kulingana na uchaguzi wa mwanafunzi mwenyewe.

Katika hili mwalimu hawachagulii wanafunzi kona ya kujifunza, bali yeye atakuwa akisimamia namna kila mwanafunzi anavyojiamulia kona anayoipenda.

Darasa hili hutoa fursa kwa mwalimu kubaini vipaji mbalimbali vya wanafunzi wake na vitu wanavyopendelea.

Darasa hili huwa na mvuto na mara nyingi imezoeleka kutumiwa na walimu wanaofundisha hususani katika darasa la kwanza, la pili na la tatu.

Walimu wengi wamekiri kuwa darasa linaloongea limewasaidia kwa kiwango cha juu kuwawezesha wanafunzi wao kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa urahisi.

 

Faida za darasa hili

Darasa linaloongea huwa na faida nyingi kwa wanafunzi, walimu na shule. Baadhi ya faida hizi ni kama ifuatavyo:

Moja, huchangia kupunguza idadi kubwa ya utoro shuleni. Mvuto wa shule na madarasa huchangia kwa kiasi kikubwa  kuwafanya wanafunzi wapende kwenda shuleni bila shuruti.

Mazingira ya kuvutia ya darasani pia huongeza thamani ya shule na wanafunzi katika jamii.

Mbili, huhamasisha elimu jumuishi. Kwa sababu watoto wenye mahitaji mbambali huweza kulitumia darasa linaloongea bila ubaguzi.

Kwa mfano, wanafunzi wenye mahitaji maalumu wasioona na wasiosikia wote huweza kulitumia na kushirikiana na wanafunzi wengine.

Tatu, humfanya mwanafunzi kuwa mbunifu. Wanafunzi wanajengwa stadi za ubunifu na kujiamini kwa sababu hupewa fursa ya kwenda wenyewe kwa hiari yao kucheza au kujifunza katika kona ya ujifunzaji.

Nne, huleta ari ya kujifunza kwa mwanafunzi. Hamasa ya mwanafunzi kujifunza huchangiwa na namna walimu wanavyoweza kufanya madarasa yao kuwa yenye mvuto.

Darasa linaloongea humfanya mwanafunzi aweze kuhusianisha anayojifunza shuleni au darasani na maisha yake halisi.

Tano, humrahisishia mwalimu kazi ya ufundishaji na ujifunzaji kwa sababu kwa kiwango kikubwa hupunguza vurugu na kelele darasani. Darasa lenye wanafunzi watulivu na wasikivu husababisha mada kueleweka vizuri.

Pia, darasa hili ambalo limeandaliwa kwa kuwekwa zana bora za kufundishia na kujifunzia, lina uwezo wa kumshawishi mtoto kutaka kujifunza zaidi.

Sita, humfanya mwanafunzi kuwa mdadisi. Mwanafunzi anapokuwa mdadisi hii, anakuwa na tabia ya kutaka kujifunza  kutoka kwa wanafunzi wenzake.

Kuna wakati wanafunzi huulizana maswali juu ya picha zilizobandikwa katika darasa lao. Kwa kufanya hivyo hukuza kumbukumbu na kuendelea na tendo la kujifunza pasipo uwepo wa mwalimu.

Mwalimu Jackline Chaula wa Shule ya Msingi Chadulu iliyoko Dodoma Mjini, anaeleza kuwa mwanafunzi huendelea kujifunza kwa ziada.

Kwa mfano, inawezekana  mwalimu anayefundisha wanafunzi wa darasa la kwanza akawa amefundisha tarakimu mpaka namba tano katika kitabu, lakini katika kuta za darasani humo akawa amebandika picha zenye vitu kulingana na namba mpaka tarakimu ya namba 10 au 20.

 

Saba, hurahisisha upimaji wa mtoto katika hatua zake za kielimu darasani. Kwa mfano, ni jambo rahisi kwa  mwalimu kupata majibu ya haraka ya aina zote za upimaji kwa kumhoji mwanafunzi kulingana na picha anazoziona darasani kila siku.

Nane, humjengea mwanafunzi hali ya uzalendo. Mwanafunzi anayesomea katika darasa lenye sifa za kuwa darasa linaloongea, hujifunza pia moyo wa kulipenda, kulithamini, kulitunza na kulilinda darasa lake.

Mwanafunzi huyu anapokuwa amejengwa moyo na ufahamu wa kutunza vitu vyake binafsi, kutunza mali za shule, kutunza mali za wenzake, akiwa mkubwa atakuwa na uwezo wa kutunza, kulinda na kupigania maliasili za taifa lake popote pale.

Kwa hiyo, faida za kuwa na darasa linaloongea ni nyingi kwa mwanafunzi, mwalimu, wazazi, shule na taifa kwa jumla. Ni wajibu wa walimu hususani wanaoweka msingi wa elimu kwa watoto na vijana, kujitoa kutimiza wajibu wao sawasawa kiuweledi ili kuwapatia wanafunzi stahiki zao.

Walimu wanasisitizwa kuongoza vitendo vya ujifunzaji na ufundishaji kwa kutumia zana mbalimbali, ili kuweza kufikia malengo ya elimu.

Walimu wanaohisi hawana uwezo wa kufanya hivyo, ni vema wakachukua hatua ya kutembelea shule mbalimbali zilizo jirani kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.

 

Tuesday, December 12, 2017

Michezo inayoweza kudumaza uwezo wa mtotoChristian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Hivi karibuni, niliongea na mwalimu wa shule moja ya msingi mjini Moshi. Kwake, michezo na masomo ni vitu viwili visivyoweza kwenda pamoja. Mwalimu huyo alinieleza: “Ukiruhusu michezo shuleni, akili za watoto zitawaza michezo muda wote. Hawawezi kuzingatia masomo.”

Akaongeza: “Hapa shuleni kuna watoto wengi wanaopenda sana games (michezo ya kidijitali inayochezwa kwenye kompyuta na vifaa maalum vya kielektroniki.) Michezo kama hii imeathiri uwezo wao kufuatilia masomo wanaporudi nyumbani.”

Mwalimu ana hoja kwa upande mmoja. Pamoja na umuhimu wa michezo katika ukuaji wa watoto wetu, ipo haja ya kuangalia aina ya michezo inayomfaa mtoto.

Michezo ya kisasa

Teknolojia imebadili namna watoto wetu wanavyocheza. Wakati zamani tulikwenda viwanjani na kwenda nje ya nyumba tukifukuzana na kukimbia, leo watoto wa mjini wanacheza michezo karibu yote wakiwa sebuleni au kwenye vyumba vyao vya kulala.

Kama alivyosema mwalimu, michezo ya kisasa kama ‘games’ imekuwa maarufu kwa watoto. Mtoto anaweza kutumia kifaa kidogo cha kielektroniki kucheza mchezo wa kuunda maumbo mbalimbali, kuigiza hali ya kufikirika (simulation) kwa kupanga mikakati, mathalani, ya kumshinda mpinzani wake wakati mwingine kwa kumpiga risasi na mabomu.Pia, watoto wanaweza kucheza kwa mfumo wa kutazama kinachofanywa na watoto wenzake waliorekodiwa tayari, kama katuni zinazoonyeshwa kwenye video au vituo vya televisheni.

Katika michezo kama hii, mtoto hafanyi shughuli yoyote zaidi ya kukaa, kubofya vitufe kwenye kifaa vya kielektroniki, au kufikiri namna ya kupambana na ‘maadui’ wake wa kufikirika kwenye michezo.

Sambamba na michezo hii ya kiteknolojia, ipo michezo inayotumia vifaa vilivyotengenezwa tayari. Mtoto kwa mfano anaweza kununuliwa mwanaserere, midoli ya gari, nyumba, wanyama na kazi yake inabaki kujifunza namna ya kuitumia kwa mujibu wa waliotengeneza vifaa hivyo.

Uraibu

Michezo kama hii inayotumia teknolojia ina tabia ya kutengeneza tabia ya uraibu. Uraibu ni ile hali ya kuzoea kitu kiasi cha kutoweza kuachana nacho kirahisi.

Michezo hii imetengenezwa kwa kufuata mfumo wa kamari inayotengeneza shauku ya mtoto kuendelea kucheza ili kujua nini kitatokea.

Shauku hiyo, hujengwa, aghalabu, na motisha ya kushinda kwa kuwaua maadui wa kufikirika, kupata pongezi za sauti au alama za ushindi.

Michezo ya namna hii inaweza kumfanya mtoto akawa na aina fulani ya ulevi kwa kuuzoea mchezo kiasi cha kukosa utulivu asipocheza mchezo huo.

Ingawa ni kweli michezo hii huweza kukuza uwezo wa mtoto kufikiri kwa haraka kama ilivyo kwa michezo ya asili, changamoto yake ni kutegemea ubongo na vidole pekee.

Tukiongeza na uraibu, kwa hakika, michezo hii inaweza kuwa hatari si tu kwa malezi ya watoto, bali hata kwa maendeleo ya mtoto shuleni.

Kukosa uzingativu

Kuna malalamiko mengi kutoka kwa walimu kuwa watoto wa siku hizi, hasa mijini, hawana uzingativu darasani. Walimu wanasema kumpa mtoto kazi inayohitaji uzingativu wake kwa dakika kadhaa inaanza kuwa vigumu.

Sababu moja wapo inaweza kuwa ni mazoea ya aina fulani ya vitu anavyoviona kwenye michezo yake ya kiteknolojia isiyopatikana katika mazingira ya darasani.

Kwa mfano, mtoto aliyezoea tabiti kucheza michezo yake ya ‘kutafuta namna ya kutoroka kwenye kambi ya jeshi,’ hawezi kuona uwezekano wa kujifunza lolote kupitia maelezo yanayotolewa kwa kuchorachora ubaoni.

Umakini ni sifa muhimu katika masomo. Ili mwanafunzi afanikiwe lazima awe na uwezo wa kufuatilia kwa umakini kile kinachosemwa na mwalimu. Awe na uwezo wa kutumia macho na masikio yake kuchunguza wakati anapohitajika kufanya majaribio.

Mtoto asiyeweza kusikiliza maelezo ya mwalimu kwa sababu tu yanasemwa kwa namna isiyomvutia, anakuwa kwenye hatari ya kufanya vibaya kwenye masomo yake.

Kuiga tabia zisizofaa

Kuna visa vingi vya watoto kujifunza tabia za ajabu kupitia michezo inayopatikana kwenye ‘games.’ Ili kuifanya michezo hii ya kiteknolojia iwe na mvuto kwa watoto, wabunifu wake hutengeneza mazingira yanayoongeza msisimko.

Namna moja ya kuweka vionjo vya msisimko ni kumfanya mtoto apigane na maadui wakufikirika. Ili ashinde mchezo husika, mtoto hulazimika kutumia silaha kama bunduki na makombora kuwamaliza ‘wabaya’ wake.

Wakati mwingine, mtoto hutazama katuni zenye wahusika wanaoonyesha ukatili. Mara nyingi wahusika wenye ukatili na ubabe ndio wanaopendwa na watoto.

Albert Bandura, mwanasaikolojia maarufu wa karne ya 20, anasema michezo kama hii inawafundisha watoto kuiga tabia wanazoziona kupitia vifaa vya mawasiliano.

Siku hizi tunafahamu, mathalani, watoto wengi huwa wakorofi, wagomvi kwa wenzao. Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto hujifunza tabia hizi kupitia michezo wanayoicheza chini ya uangalizi wa wazazi wao.

Matatizo ya afya

Michezo mingi ya kisasa haimhitaji mtoto kutumia viungo vya mwili wake kama ilivyokuwa hapo zamani. Badala ya mtoto kwenda mtaani kurukaruka na wenzake, anabaki sebuleni akishikashika kifaa chake.

Mtoto huyu anaweza kucheza mchezo unaokuza uwezo wake wa kufikiri, lakini akajikuta muda mwingi hana anachofanya kinachoweza kutumia nguvu za mwili wake.

Hali kama hii kwa kiasi kikubwa huchangia matatizo mengi ya afya, ikiwamo kuongezeka kwa uzito kupita kiasi, maumivu ya mgongo, matatizo ya macho katika umri mdogo na changamoto nyingine za kiafya.

Ushauri

Pamoja na kukua kwa teknolojia inayobadili namna watoto wanavyoweza kushiriki michezo, wazazi tuna wajibu wa kuhakikisha muda unaotumiwa na watoto kucheza michezo hii unadhibitiwa.

Kila inapowezekana, mzazi afanye ukaguzi wa michezo anayocheza mtoto kujiridhisha kuwa hakuna chembechembe za tabia mbovu zinazoweza kuoteshwa kwenye ufahamu wa mtoto bila yeye kujua.     

Tuesday, December 5, 2017

Dawa ya elimu Tanzania ni zaidi ya kuwa na chombo cha kusimamia elimu

Mwalimu akiwajibika shuleni. Walimu ndio nguzo

Mwalimu akiwajibika shuleni. Walimu ndio nguzo kuu ya mafanikio ya elimu. Picha ya Maktaba 

By Mwalimu Ezekiah Oluoch

       Hivi karibuni, asasi isiyo ya kiserikali ya HakiElimu, iliandaa kongamano la kujadili hali ya elimu ya Tanzania Bara kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.

Katika jitihada za kufanya tukio hilo lipate watu na hadhi, waandaaji waliamua lifanyikie katika ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Huu ni ukumbi wa mapinduzi ya mawazo ya Kwame Nkurmah, aliyekuwa rais wa kwanza wa Ghana.

Katika Kongamano hilo ambalo nilitegemea wasomi wangezungumzia kwa mapana yake, dhana ya uboreshaji wa elimu katika nchi kwa kubeba dhana aliyokuwa nayo Nkurumah, wajumbe walijikita bila ya kujua katika koti la kubariki mtazamo wa siku nyingi wa HakiElimu.

Mtazamo huo ni ule utokanao na dhana kuwa ili elimu ya Tanzania iwe bora zaidi, kunatakiwa kuwapo kwa chombo cha kusimamia elimu pekee kama vile Kamishna wa Magereza anavyosimamia magereza nchini ndani ya Wizara ya mambo ya Ndani.

Makala haya yanajaribu kupitia kwa kifupi elimu ya Tanzania kwa sasa, changamoto zake na namna ya kukabiliana na changamoto hizo

Dhamira yangu ni kushauri mamlaka husika kuchukua hatua katika kurekebisha kasoro zilizopo ili kuifikisha elimu ya Tanzania mahali inapostahili.

Elimu ya Tanzania

Elimu ya Tanzania kama nchi ni elimu ambayo imesukwa vizuri katika kuandaa nini cha kuwafundisha watoto wetu. Ni elimu inayoheshimika ndani na nje ya Afrika.

Silabasi inayofundishwa hapa Tanzania kwa sehemu kubwa inakidhi mahitaji ya nchi isipokuwa kinachotakiwa ni kuboresha mbinu za ufundishaji, ili watoa elimu waweze kuwapa wanafunzi elimu inayowasaidia katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Silabasi ya Tanzania inaheshimiwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Hata mhitimu wa shahada ya kwanza nchini anapohitaji kusoma shahada ya uzamili katika vyuo katika baadhi ya nchi za Ulaya, haihitaji kufanyiwa usaili kama inavyofanyika kwa wanafunzi wa baadhi ya nchi barani Afrika.

Tunahitaji maboresho madogo madogo katika silabasi yetu, ili kukidhi mahitaji ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwanoa vizuri walimu wetu mara kwa mara ili wapate mbinu mpya.

Changamoto za elimu Tanzania

Changamoto kubwa kuliko zote katika elimu ya Tanzania, ni maslahi duni ya walimu katia ngazi zote. Wataalamu wanakubaliana kuwa ubora wa nchi hautegemei barabara, demokrasia iliyopo wala uchumi wa nchi hiyo.

Ubora wa nchi hupimwa kwa kuangalia ubora wa walimu wanaowafundisha watoto. Ili uwapate walimu bora lazima upitie hatua zifuatazo.

Kwanza, nchi ikubali kwamba utoaji wa elimu bora ni gharama kubwa na matokeo yake hayawezi kupimwa kwa Dola za Marekani. Watanzania watakapokubaliana kuwekeza kwenye elimu, watawasukuma wanasiasa kuhakikisha kuwa nchi inawekeza katika elimu kwa viwango vinavyokubalika.

Pili, nchi ikishawekeza kwenye elimu, walimu walipwe vizuri ili watekeleze majukumu yao kwa kuruhusu akili zao kumwaga ujuzi wote kwa watoto na kuweka mawazo yao yote kwa maendeleo ya watoto.

Tatu, usimamizi wa walimu haujawa mzuri kutokana na nchi kutokuwa na kanuni za kuwapata wasimamizi wa elimu. Viongozi wengi wa elimu katika ngazi zote huteuliwa kwa kujuana. Baadhi ya maofisa elimu wa wilaya wanawateua watu watakaowatii na kuwaweka kuwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu elimu kata

Kwa ngazi ya Wizara, hakuna utaratibu wa kuwapata maofisa elimu wa wilaya wenye ujuzi wa kusimamia elimu katika wilaya.

Usishangae kusikia kuwa hadi leo, kuna maofisa elimu wasio na shahada, lakini wanasimamia taaluma ambayo hutolewa na walimu wenye shahada.

Namna ya kukabiliana na changamoto hizi

Kwa kuwa Tanzania ina silabasi nzuri ya elimu katika ngazi zote, kipaumbele cha nchi kingeelekezwa katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza, mishahara ya walimu iwekwe kwa kiwango cha kuwavutia watu wenye ufaulu wa juu kupenda kazi ya ualimu. Kinachowavutia watu kujiunga na taaluma fulani ni maslahi watakayopata wakiwa kwenye taaluma hiyo.

Walimu wa Tanzania ni takribani asilimia 60 ya watumishi wote kwenye utumishi wa umma, lakini ukija kwenye mgawanyo wa mishahara, wanalipwa takribani asilimia 49 ya mishahara yote inayotengwa kwa ajili ya kuwalipa watumishi wa umma.

Kulipwa kwa mishahara ya walimu kuambatane na kulipwa kwa madeni yao, wapandishwe madaraja kwa wakati na kurekebishiwa mishahara kwa wakati na kupewa fedha za likizo.

Pili, Silabasi ya elimu yetu inapaswa kuangaliwa upya kwa kutoa uhuru kwa walimu kufundisha kulingana na sehemu husika. Kwa mfano, watoto wanaosoma kandokando ya Ziwa Tanganyika, wapewe elimu ya ziada juu ya uvuvi wa samaki.

Hii itakuwa kwa watu wote wanaokaa karibu na sehemu zenye uvuvi. Wanafunzi wanaoishi maeneo wanakolima ndizi wapate elimu zaidi juu ya utunzaji wa ndizi.

Walimu wakipewa uhuru huo wa kutoa elimu kulingana na sehemu walipo, mhitimu atakuwa na fursa nzuri ya kuchangia maendeleo kutokana na elimu aliyopata kutoka shuleni.

Tatu, usimamizi wa utoaji wa elimu uimarishwe kwa kuweka taasisi huru za kusimamia elimu kitaalamu bila ya kuingiliwa na wanasiasa. Elimu bora husimamiwa na taasisi tatu zilizo huru zinazoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Bunge.

Taasisi hizo ni ile inayopima ubora wa elimu (Baraza la Mitihani), ya pili ni ile inayotunga silabasi ya kufundishwa na walimu ( kwa Tanzania kuna Taasisi ya Elimu Tanzania).

Taasisi ya tatu ambayo haipo ni taasisi ya kukagua jinsi elimu inavyotolewa kama inakidhi matakwa ya silabasi. Taasisi hii imekuwa ikijulikana kama ukaguzi wa shule ambao kwa sasa huitwa udhibiti ubora wa shule.

Kwa mfumo wetu, bado Udhibiti ubora wa shule wizarani. Kiini cha matatizo ya ubora wa elimu ni kutokuwapo kwa taasisi hii. Natoa wito idara hii iwe wakala rasmi wa Serikali.

Aidha, kuna taasisi ya nne ambayo ni

ni bodi ya kusimamia taaluma ya ualimu. Ualimu ni taaluma na taaluma zote duniani zina bodi zake. Mpaka sasa uanzishwaji wa bodi hii umekuwa ukipigwa danadana.

Sio ajabu kuona kuwa hoja ya kuundwa kwa chombo hicho si kipaumbele cha wanasiasa, kwa kuwa hawajaona umuhimu wa walimu kuwa na bodi yao kudhibiti taaluma ya ualimu.

Ni maoni yangu kwamba hayo yakirekebishwa, elimu yetu itaendelea kuwa bora zaidi. Hatuhitaji kuwa na chombo cha kuratibu elimu nchini kama ilivyo kwa TCRA, Sumatra na nyinginezo. Kinachotakiwa ni kutumia mfumo ulioko kwa kuufanya kuwa imara katika kutoa elimu iliyo bora.

Mwalimu Ezekiah Oluoch anapatikana kwa barua pepe: Oluoch2009@yahoo.com     

Tuesday, December 5, 2017

Ghassani: Nilianza kutunga mashairi darasa la nne

Mohammed Ghassani (kushoto) akipokea tuzo

Mohammed Ghassani (kushoto) akipokea tuzo aliyoshinda mwaka 2015. Na Mpigapicha Wetu 

By Florence Majani, Mwananchi

       Ulikuwa ni usiku mmoja, katikati ya giza na baridi kali, akaamka katika kijichumba chake, akalia peke yake na huku akijiuliza maswali yasiyo na majibu. Kisha akaketi na kuchukua kalamu, na kuanza kuandika ubeti huu wa shairi.

``Nyumbani oo nyumbani, kwetu ninakukumbuka

Gizani humu gizani, machozi yamiminika

Kwa nini hivi kwa nini, kwetu miye nikauka? ``

Hiyo ni sehemu ya ubeti wa shairi la Mohammed Ghassani, katika kitabu chake cha ´Nna Kwetu: Sauti ya Mgeni ugenini´

Ghassani, ni Mtanzania na mtunzi wa mashairi, mkazi wa Bonn, Ujerumani, ambaye mapenzi yake katika utunzi wa mashairi yamempa mafanikio hadi kupata tuzo ya kimataifa ya kazi za Fasihi ya Kiafrika iitwayo Mabati Cornell.

Alishinda tuzo hiyo mwaka 2015 baada ya kupeleka shairi lake la ´Nna Kwetu´ lililozungumzia maisha yake ugenini. Tuzo hiyo iliambatana na zawadi nono ya dola za Marekani 5000.

Alivyoanza ushairi

Safari yake ya upenzi wa ushairi hadi kupata tuzo ya kimataifa ilianzia visiwani Pemba, Zanzibar miaka zaidi ya 20 iliyopita. Anasema alianza kuyanakili na kuyasoma akiwa mwanafunzi wa darasa la nne.

``Nilikuwa nayasoma mashairi yaliyokuwa yanachapishwa katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Mfanyakazi,`` anasema

Alipofika darasa la nne, akaanza kuandika mashairi yeye mwenyewe, akifuatilia na kusoma kazi za washairi nguli kama Juma Balo, Zuhura Salehe na wengineo.

Kabla ya kushinda tuzo hii aliwahi kuwa mshairi bora wa Wilaya ya Wete Kaskazini Pemba, baada ya kutunga shairi bora zaidi katika mashindano ya kiwilaya.

Ghassani, ambaye kwa sasa ni mtangazaji na mhariri wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, anasema mapenzi yake katika ushairi yalitokana na kupenda lugha.

``Nilijifunza Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza, na zaidi hasa napenda kujisomea riwaya za Kiswahili na ninapenda kutafsiri,``anasema na kuongeza:

``Jambo lolote likitokea na nikahisi napaswa kutuma ujumbe wangu au kutoa maoni yangu, naweza kuyatoa kwa njia ya ushairi na si lazima nichapishe kama kitabu, lakini naweza hata kuweka katika mitandao ya kijamii, ndicho ninachopenda.``

Mpaka sasa Ghassani ameandika mashairi zaidi ya 3000, lakini yaliyochapishwa na kuwekwa katika vitabu ni matano likiwamo lililompa tuz, Nna Kwetu, Andamo, Siwachi Kusema na Kalamu ya Mapinduzi lililozungumzia uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015.

Mashairi yake mengi ni ya kimapinduzi, siasa na kwa uchache masuala ya kijamii.

Anasema maudhui yake yanalenga kubadili fikra za watu katika siasa, kwa mfano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

``Ushairi wangu natamani kuwasilisha fikra zangu ili ziwe na maana katika jamii lakini isiwe kwa ubaya. Fikra zangu zidumu na ziache alama, `` anasema.

Diwani ya N’na Kwetu

Ukiisoma Diwani ya N´na Kwetu, utagundua kuwa Ghassani, ametumia Kiswahili fasaha. Licha ya kuwa baadhi ya misamiati ni migumu, lakini ameitafsiri,

Maudhui makuu katika diwani hiyo, ni maisha ya ukiwa ugenini lakini pia imeangazia safari yake kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere hadi Ujerumani. Maisha yake Ujerumani na hata simanzi aliyokuwa nayo kwa kuiacha familia yake.

Kwa mfano katika shairi hili anasema;

``Khadhira hii safari, leo hii niendayo,

Usidhani nahajiri, naselemeya machweyo,

Sienendi hiyari, nendea makadirio,

Basi kiri pendo kiri, niuke nina radhiyo.``

Wanaomjua Ghassani, akiwamo Faraji Said, aliyesoma naye Chuo Kikuu cha Tumaini, hawashangazwi na tuzo hiyo.

Saidi, anasema alikutana naye kwa mara ya kwanza chuoni, mwaka 2006.

``Hatukuwa wanafunzi wengi katika darasa letu ilikuwa rahisi kufahamiana kwa haraka. Wakati tunazoeana na huyu bwana niligundua anaongea Kiswahili kwa ufasaha mkubwa, ikiwamo kutumia msamiati mzito. Kuna wakati niliwahi kumtania na kumwambia anapaswa kutunga nyimbo au mashairi, `` anasema Saidi

Anasema, katika kipindi alichofahamiana na Ghasani, hakuwahi kujua kama ni mshairi.

``Kwa kweli anastahili tuzo,kwanza anajua lugha vizuri ya Kiswahili, pili ni msomi na mtafiti mzuri, tatu ni mtu mwenye fikra na uwezo mpana wa kuchambua na kudadavua mambo mbalimbali,`` anasema

Anaongeza: ``Naamini kwa kuchanganya kipawa na uwezo alionao, vimemsaidia kuwa mtunzi bora wa mashairi. Akiendelea kutunga basi ataendelea kupata tuzo nyingi siku zijazo.``

Akizungumzia utunzi wa mashairi au kazi za fasihi kwa ujumla, Saidi anasema utamaduni wa mashairi umekufa na kumekuwa na mwamko mdogo kwa vijana kuandika au kusoma mashairi.

Wasifu wake

Ghassani alisoma Shule ya Msingi Pandani, Pemba. Akajiunga na shule ya sekondari ya Utaani, baadaye akahamia shule ya Fidel Castro, hapo hapo Pemba. Alipata diploma ya lugha katika Taasisi ya Lugha, akijikita katika Kijerumani, Kiswahili na Kiingereza.

Baadaye, akapata shahada ya Sanaa ya Uandishi wa Habari.     

Tuesday, December 5, 2017

JICHO LA MWALIMU : Mwalimu ni mwanafunzi wa kudumuJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

Mwalimu ni mtu aliyepata ujuzi kupitia mfumo rasmi au usio rasmi, mwenye uwezo wa kumfundisha mwanafunzi maarifa au ujuzi.

Maarifa hayo mara nyingi hutegemewa yawe na manufaa kwa mwanafunzi na jamii inayowazunguka.

Katika kitabu cha Uhuru wa Wanawake kilichoandikwa na Mwalimu Julius  Nyerere, anaeleza kuwa:

“Wazungu ambao walifikiri kuwa Waafrika ni nusu watu sasa wameanza kuamini kuwa Waafrika ni watu kwa sababu katika mieleka ya mambo ya akili imeonyesha kuwa Mzungu anaweza kuangushwa na Mwafrika na Mwafrika anaweza kuangushwa na Mzungu.”

Nyerere alieleza hayo huku akikumbusha msingi wa maarifa kwamba katika masuala yanayohusu akili, binadamu wote wamejaaliwa tunu hiyo.

Tofauti hutokea pale  kila mmoja  kwa namna yake anavyotumia akili yake. Tukumbuke msemo: “akili ni nywele kila mtu ana zake”.

Mwalimu bora huambatana na sifa kadhaa  kama vile kupenda na kuithamini kazi yake, huku akiwa hayuko tayari kujiona duni wakati wote. Huyu ni mwalimu aliyejitambua kuwa ni mwalimu; ni lazima ataambukiza mambo mazuri kwa wanaomzunguka.

Katika hili mwalimu huweza kubadilishwa yeye binafsi kutokana na aina ya masomo anayofundisha. Kwa sababu watu huwa hivyo walivyo kutokana na namna wanavyofikiri, wanavyotenda na wanayozungumza. Kwa mfano, mtu akiendekeza upuuzi kila wakati huwa mpuuzi.

Pili, anayependa kujifunza mara zote. Mwalimu bora hufanya marudio, hujitafakarisha juu ya somo, maisha, uhusiano, maendeleo na masuala mengine katika nyanja mbalimbali ambazo humpatia uwezo mkubwa wa kuendelea kuwa mshauri katika jamii yake.

Kwa mfano, mwalimu anapotekeleza majukumu yake shuleni, huvaa kofia za kada mbalimbali kama vile  usuluhishi na kutoa adhabu (uhakimu na uanasheria), uuguzi pale mwanafunzi anapopata tatizo la afya akiwa shuleni

Pia, hutoa  ushauri wa masomo, tabia na usanii pale anapohamasisha utambuzi,  ukuzaji vipawa na vipaji mbalimbali vya wanafunzi wake.

Tatu, anayefahamu kuwa kujifunza ni tendo endelevu kwa maisha yote ya binadamu.

Mwalimu bora hufahamu vyanzo vipya vya maarifa katika fani yake au masomo anayofundisha na wakati mwingine hata asiyofundisha. 

Kwa kufanya hivyo, atakuwa na uwezo mkubwa wa kupewa changamoto na kuzitatua na kufaidika na mawazo kutoka kwa watu mbalimbali kupitia vitabu au kwa njia ya majadiliano na si mabishano.

Hii ni kwa sababu mwalimu bora hutambua kuwa mabishano yaliyo mengi huwa si chanzo cha maarifa na huendeleza ujinga badala ya hekima.

Nne, anayechukua hatua na  kutekeleza kwa vitendo yale anayojifunza. Mwalimu bora anapojifunza huchukua hatua za kutekeleza kwa vitendo ujuzi mpya alioupata kwa wanafunzi wake, jamii inayomzunguka na kwa maisha yake ya kila siku.

Kwa mfano, anapofahamu matumizi ya vifaa vya Tehama ni dhahiri huweza kutumia katika kurahisisha shughuli za ujifunzaji na ufundishaji na katika kukusanya, kuandaa na kuchakata taarifa mbalimbali shuleni na katika shughuli za maisha za kila siku.

Katika hili ni dhahiri mtu akimtazama mwalimu bora, atamuona mtu apendaye kuwa rafiki wa jamii, mtu afurahiaye kufanya shughuli kwa ushirikiano kama ilivyo kwa kada za wauguzi, wanasaikolojia, washauri na viongozi wa dini.

Tano, anayethubutu kukiri kuwa hafahamu au hajui ili aweze kufahamishwa. Mwalimu bora hupenda ukweli, huuishi ukweli na huwa na mawazo au akili yenye kujihoji katika masuala mbalimbali.

Kwa kuwa ni mwanafunzi wa kudumu kila siku hutamani kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa upande wa tatizo. Hii ni kwa  sababu hufahamu kuwa nguvu ya kuuliza hushinda nguvu ya ujinga.

Kwa kuuliza pale asipofahamu, mwalimu hujikuta akiwa na kiwango kikubwa cha kujiamini na kukuza upeo wake wa kuelewa mambo tofauti. Uwezo huo humsaidia kufikiri kwa kina, kufikiri kwa umakini na kwa usahihi. 

Sita, anayekubali kuomba radhi pale anapokosea kwani naye ni binadamu. Na kuomba radhi ni kitendo cha kiungwana na wala si cha kinyonge.

Mwalimu bora hufahamu namna ya kushughulika na hisia na udhaifu wake wa kibinadamu ili kupunguza au kuondoa upendeleo, ubaguzi na upuuzaji.

 Katika hili huwa na uwezo wa kumhudumia mtu yeyote pasipo kujali historia yake ya nyuma, rangi, jinsi, kabila, hali ya uwezo wa kiuchumi kama vile ambavyo yeye angependa kufanyiwa.

Saba, anayependa kufanya mambo sahihi kwa kiwango cha juu lakini kwa kutumia njia nyepesi.

Mwalimu bora huwa na uwezo wa kurahisisha mambo kwa ubora uleule tarajiwa, hivyo hutumia njia na mbinu za kujifundisha na kujifunzia zilizo rahisi kwa wanafunzi wake kumwelewa..  

Katika hili mwalimu huweza kujitofautisha na mtu asiye mwalimu; kwa sababu si kila mtu anaweza kufundisha.

Kufundisha si kusimama mbele darasani na kuandika ubaoni; kufundisha kunaambatana na maadili, kanuni, falsafa na uwezo wa kuwasilisha ujumbe stahiki kwa wakati stahiki.  

Hivyo, Mwalimu bora ni mwanafunzi wa kudumu kwa sababu kila siku katika maisha yake huendelea kujielimisha na kutafuta maarifa mapya na kuyatumia.

Vilevile katika kutafuta mambo mapya, hupata mbinu na njia mpya za kujifunzia na kufundishia, sambamba na kuibua namna ya kufaragua zana rahisi kwa kutumia malighafi zipatikanazo katika mazingira yake, zitakazokidhi mahitaji na uwezo wa kila mwanafunzi wake.

Ni wajibu wa jamii kuendelea kutengeneza mazingira rafiki na mazuri kwa wanafunzi na walimu ili waweze kufikia malengo ya maendeleo ya taifa kwa kupitia elimu.

Ili kuendelea kufurahia uhuru wa taifa, watu hawana budi kuwa na tabia ya kuwa wanafunzi wa kudumu katika maisha ili waweze kupata maarifa mapya na ujuzi wa kukabiliana na changamoto mpya za maisha. 

Tuesday, December 5, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tujiepushe na makosa haya katika Kiswahili

 

By Erasto Duwe

        Katika muktadha wa utumiaji wa Kiswahili, baadhi ya watumiaji hutumia maneno ya lugha visivyo kiasi cha maneno hayo kuzoeleka na kuonekana ni sahihi.

Miongoni mwa maneno ambayo watumiaji wa lugha wamekuwa wakiyatumia kwa makosa, ni pamoja na ‘pelekea’, ‘misamiati’, ‘agenda’, ‘makaratasi’, ‘mataa’, ‘tutakwenda ku...’ na mengineyo kama inavyofafanuliwa katika makala haya.

Watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili hupenda kulitumia neno ‘pelekea’. Kwa mfano, mtumiaji wa lugha huweza kusema, “Matumizi mabaya ya mali za umma yamepelekea Tanzania kuwa maskini.”

‘Pelekea’ si neno fasaha la Kiswahili linapotumika katika muktadha kama huo. Neno hili ni matokeo ya tafsiri sisisi kutokana na maneno ya Kiingereza ‘leading to’. Kisawe cha maneno hayo ni ‘sababisha’.

Kwa hivyo, sentensi hiyo ingepaswa kuwa; “Matumizi mabaya ya mali za umma yamesababisha Tanzania kuwa maskini.” Viongozi wengi hususan wa kisiasa hupenda kulitumia neno hilo.

Ifahamike kwamba neno hilo siyo fasaha katika Kiswahili badala yake neno ‘sababisha’ litumike.

Neno jingine linalotumiwa vibaya ni ‘msamiati’. Hili hutumiwa hivyo katika umoja na wingi. Kwa hiyo, mtumiaji wa lugha hapaswi kutamka ‘misamiati’ anapozungumzia dhana ya wingi. Makosa katika matumizi ya neno hili hufanywa na watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili.

Mathalani, mtumiaji wa lugha huweza kusema, “Kiswahili kina misamiati migumu” badala ya “Kiswahili kina msamiati mgumu.” Watumiaji wa Kiswahili wajue kwamba wingi wa neno ‘msamiati’ ni ‘msamiati’ na si vinginevyo.

Aidha, neno ‘agenda’ ni la Kiingereza ambalo hutumika zaidi katika miktadha ya vikao/mikutano. Kisawe cha neno hilo katika Kiswahili ni ‘ajenda’. Neno hilo lina maana ya ‘orodha ya mambo yatakayozungumzwa katika mkutano’. Hata hivyo, watumiaji wengi wa Kiswahili katika kutamka na kuandika, hutumia neno ‘agenda’ kimakosa badala ya neno linalotakiwa ambalo ni ‘ajenda’.

Pia, kuna matatizo ya matumizi ya neno katika ‘karatasi’. Wingi wa neno hilo ni ‘karatasi’ na siyo ‘makaratasi’ kama wengi wapendavyo kulitumia.

Kwa mfano, mtumiaji wa lugha huweza kusema; “Makaratasi ya kujibia mtihani yameisha” badala ya kusema “Karatasi za kujibia mtihani zimeisha.”

Vilevile, wingi wa neno ‘taa’ ni ‘taa’ na siyo ‘mataa’. Lakini katika miktadha mbalimbali ya utumiaji wa lugha, baadhi ya watumiaji wa lugha hutumia neno ‘mataa’ katika dhana ya wingi jambo ambalo ni makosa.

Siku za hivi karibuni kumezuka mtindo wa utumiaji wa Kiswahili ambao hauna mantiki. Matumizi ya maneno ‘tutakwenda ku...’ hasa katika mazingira ambayo uwasilishaji hufanyika mathalani katika miktadha ya mihadhara, utoaji wa mahubiri, matangazo studioni. Huku ni kufanya makosa.

Kwa mfano, mtangazaji wa kipindi studioni anaposema, “Katika kipindi hiki cha leo tutakwenda kujadili namna ugonjwa wa Ukimwi unavyoambukizwa.”

Swali linalokuja ni kwamba, ‘tutakwenda kujadili wapi ilhali tupo studioni?’ Hiyo ni kasoro kubwa. Badala yake mtangazaji angepaswa kusema, “Katika kipindi hiki tutajadili...” Matumizi hayo potofu ni athari ya tafsiri sisisi itokanayo na Kiingereza ‘Today we are going to...’

Watumiaji wa Kiswahili hatuna budi kutumia Kiswahili kwa ufasaha ili kila mmoja kwa nafasi yake aweze kuwa mwalimu kwa wanaotusikiliza na kujifunza kama lugha ya kigeni au lugha ya pili.

Tukiwa wabanangaji tutawapotosha wajifunzaji hao. Viongozi, wanahabari, wachungaji, walimu na watumiaji wengine, tufanye maandalizi tunapoandaa uwasilishaji wetu.     

Tuesday, December 5, 2017

ELIMU NA MALEZI : Michezo inavyokuza uwezo wa mtoto kiakili-1Christian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

        Imeanza kuaminika kuwa michezo na masomo haviwezi kwenda pamoja. Wazazi na walimu wanaichukulia michezo si tu kama upotevu wa muda wa mtoto, lakini pia inaathiri uzingatiaji katika masomo.

Katika kuhakikisha kwamba watoto wanaelekeza nguvu zao katika masomo, zipo shule huamua kupunguza au kuondoa kabisa michezo.

Itakumbukwa miaka ya nyuma kiongozi fulani, aliamua kufuta mashindano ya michezo katika ngazi za shule ya msingi na sekondari, kwa hoja kwamba michezo inawapotezea muda wanafunzi.

Vuguguvu hilo la kufuta michezo lilienda sambamba na msisitizo wa shule za msingi na sekondari kuongeza ufaulu. Ndio kusema wakubwa wa elimu waliamini kuwa kufuta mashindano hayo ya michezo shuleni kungepandisha taaluma katika shule zetu. Hata hivyo, baadaye uamuzi huo ulibatilishwa.

Michezo na ujifunzaji

Katika malezi na makuzi ya mtoto, umri wa mpaka miaka 12 hauwezi kutenganishwa na michezo. Karibu kila anachojifunza mtoto kuhusu mazingira yake, kinategemea na aina ya michezo anayoshiriki.

Ni kwa sababu hiyo, walimu wa ngazi za awali za elimu, wanafundishwa mbinu za kubuni michezo ya aina mbalimbali kuwasaidia watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu.

Katika makala haya, tunaichukulia michezo kama vitendo vinavyoshughulisha viungo vya mtoto kwa lengo la kumburudisha, kushindana na kujifunza mambo mapya.

Kwa mfano, mtoto anapotumia mikono na vidole vyake kurusha na kuudaka mdako, tunaweza kusema anashiriki michezo kwa sababu kwanza anashughulisha viungo vyake na pili analenga kufikia lengo la kumshinda mwenzake.

Mbali na kuboresha afya ya mtoto, tutazame namna michezo isivyoweza kutenganishwa na ujifunzaji wa mtoto.

Umakini

Michezo inaongeza umakini wa mtoto katika kufuatilia kile anachokifanya. Umakini ni ubora wa mawasiliano kati ya viungo vya mwili wake katika kufikia malengo ya mchezo husika.

Kwa mfano, mtoto anayecheza mchezo wa ‘rede’ inambidi kuwa na uwezo mzuri wa kuona na kufuatilia mwenzake mwenye mpira ataurusha wapi.

Bila uwezo mzuri wa kubashiri mwelekeo wa mpira, itakuwa vigumu kwake kuukwepa wakati huohuo akiendelea kujaza mchanga kwenye chupa inayotakiwa kujaa ili kumpa ushindi.

Umakini ni sifa muhimu katika masomo. Ili mwanafunzi afanikiwe lazima awe na uwezo wa kufuatilia kwa makini kile kinachosemwa na mwalimu; awe na uwezo wa kutumia macho na masikio yake kuchunguza wakati anapohitajika kufanya majaribio.

Kwa hiyo, utaona, mtoto anayepewa muda wa kucheza michezo inayokuza umakini wake anakuwa na nafasi ya kuwa makini darasani kuliko mwenzake asiyeshiriki michezo.

Ushirikiano

Michezo mingi inafanyika kwa ushirikiano wa watoto wengine. Mara nyingi lengo linakuwa kushindana kwa maana ya kujua nani anaweza kufanya vizuri zaidi ya mwingine.

Katika kucheza, mtoto atajifunza namna ya kupanga mikakati ya ushindi akiwa na wenzake. Katika kupanga mikakati, mtoto hujifunza mawazo mapya, hujifunza kukubali kwamba naye, kwa wakati mwingine, anahitaji kuachana na wazo lake na kufanyia kazi mawazo ya wengine.

Uwezo huu ni muhimu katika kujifunza. Ili mwanafunzi aelewe masomo yake vizuri, analazimika kusikiliza mawazo ya watu wengi. Bila uwezo wa kuvumilia mawazo asiyokubaliana nayo, itakuwa vigumu kwa mwanafunzi kufanya vizuri.

Lakini pia, katika kushindana na timu pinzani, mtoto hujifunza kwamba kuna kushinda na kushindwa. Maumivu ya kushindwa ni mtaji muhimu anaouhitaji mtoto katika maisha ya taaluma. Bila michezo, somo la kujifunza kushindwa linaweza kuwa gumu kueleweka.

Kufikiri kwa haraka

Kufikiri ni mtaji muhimu katika michezo. Ipo michezo mingi inayohitaji uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi kwa haraka na kwa wakati.

Kwa mfano, watoto wanapocheza mchezo wa mpira wa miguu, wanahitaji kufanya maamuzi muhimu kwa haraka. Lazima mtoto ajue mpinzani wake yuko wapi na anafikiri kufanya nini ili ajue cha kufanya kitakacholeta mafanikio kwa timu yake.

Vivyohivyo katika michezo mingine mingi. Bila uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka, mtoto hawezi kushinda.

Uwezo huu wa kufikiri kwa haraka unatumika darasani. Mtoto anayeweza kufanya maamuzi muhimu kwa wakati, mara nyingi ndiye anayefanikiwa zaidi.

Ubunifu

Michezo inahitaji ubunifu mkubwa. Wakati mwingine mtoto atahitaji kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yake na kuvigeuza vikidhi mahitaji ya mchezo unaokusudiwa.

Mathalani, katika mazingira ambayo watoto hawapati mipira iliyotengenezwa, watoto wanaweza kutumia mchanganyiko wa vipande vya godoro, nguo kuukuu na kamba kutengeneza mpira unaoweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

Pia, hata katika michezo mingine kama kuruka kamba, watoto wengi hutumia kamba za miti au zilizotengenezwa kwa kuunga vipande vya nguo kuukuu. Kazi hii ya kutengeneza kamba inakuza ubunifu kwa sababu mtoto anahitaji kutumia alichonacho kufikia lengo alilonalo.

Kwa hakika bila ubunifu, mtoto hawezi kufanya vizuri darasani. Mwalimu atampa maswali ambayo wakati mwingine hayana jibu linalofahamika waziwazi. Katika mazingira kama haya, mwanafunzi mwenye ubunifu anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi.

Lugha na kuhesabu

Katika michezo, watoto hulazimika kuwasiliana ili waweze kukubaliana sheria za mchezo na hata kupanga mikakati ya ushindi.

Lugha kama nyenzo ya mawasiliano, ndio kiini cha mawasiliano katika michezo ya watoto. Lengo la kupata ushindi humfanya mtoto si tu ajifunze namna ya kusema mawazo yake kwa lugha inayoelewa, lakini pia kuelewa kile wanachojaribu kukisema wenzake.

Kwa namna hii watoto wanaoshiriki michezo wana nafasi kubwa ya kuwa na msamiati zaidi kuliko watoto wanaonyimwa fursa hiyo muhimu.

Aidha, kupitia michezo watoto kujifunza kuhesabu. Mchezo kama mdako, kwa mfano, unamlazimu mtoto kujua idadi ya kete anazotumia, kuhesabu mitupo ya kete anayotakiwa kuidaka. Haya yote kwa pamoja yanamjengea mtoto uwezo wa kuhesabu wakati mwingine kabla hajakwenda shule. Itaendelea     

Tuesday, November 28, 2017

Sababu za wanafunzi kupungua madaraja mbalimbali ya elimu

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Miongoni mwa changamoto tete za sekta ya elimu nchini ni pamoja na mdondoko wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.

Hali ilivyo ni kuwa wanaobahatika kumaliza ngazi moja ya elimu, karibu nusu wanashindwa kuendelea na ngazi nyingine.

Kwa mfano, muhtasari wa takwimu za elimu kwa elimu awali, msingi na sekondari mwaka 2016 uliotolewa na Tamisemi unaonyesha wanafunzi waliokuwa wakisoma darasa la saba mwaka 2013 walikuwa 885,749.

Mwaka uliofuata (2014), wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza walikuwa 588,873. Miaka minne baadaye waliofanya mtihani wa kidato cha nne wakawa 385,938.

Unaposoma takwimu hizi, hukosi kugundua kuwa kadri wanafunzi wanavyopanda madaraja ndivyo wanavyopungua idadi yao.

Hali hii si kwa wanafunzi kuanzia mwaka 2013; ni ada ya miaka nenda rudi. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2012 walikuwa 894, 881, walioanza elim ya sekondari kati yao walikuwa 560,706.

Hata hivyo, miaka minne baadaye (2016) waliomaliza walikuwa 349,524 kati ya 560,706 walioanza kidato cha kwanza. Zaidi ya wanafunzi 211,182 hawakumaliza elimu ya sekondari ya kidato cha nne.

Hali hii ya upungufu wa wanafunzi inaendelea hadi madaraja ya juu ya elimu ya sekondari. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2014 walikuwa 297,488, lakini ni wanafunzi 73, 692 waliofanikiwa kufika kidato cha sita mwaka 2017. Wanafunzi 223,796 waliishia kidato cha nne. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Kwa nini wanapungua?

Mhadhiri wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joviter Katabalo ananasibisha hali hiyo na utoro anaosema unasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo mimba na ndoa za utotoni, biashara na wanafunzi kujiingiza katika makundi ya kihuni. ‘’Sababu kubwa ambazo zimeandikwa kitaalamu ni utoro mfano mwaka 2016 wanafunzi 61,488 waliacha shule,”anasema.

Anasema miaka 2016 kurudi nyuma utoro ulisababishwa na wazazi kushindwa kuwalipia watoto wao ada.

“Lakini kwa sasa Serikali imefuta suala la ulipaji ada kuanzia shule za msingi hadi sekondari, kwa hiyo hawa wanafunzi wanaoacha shule wanaamua tu kukaa nyumbani anasema na kuongeza:

“Mfano ukienda maeneo ya wafugaji utakuta vijana wengi wapo huko, pia kwenye madini, machimbo na biashara ndogondogo.

INAENDELEA UK.16

INATOKA UK.15

Mkurugenzi mkuu wa shirikisho la watoaji elimu wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara, Benjamin Nkonya, pamoja na kukiri sababu za utoro na mimba kwa wasichana, anasema usimamizi mbovu hasa shule za sekondari za Serikali unachangia mdondoko wa wanafunzi.

“Kwa jitihada hizi za elimu bure, hazina budi kwenda sambamba na usimamizi katika sekta hii, ili kuhakikisha elimu inakua na wanafunzi wanazidi kufanya vizuri,” anasema.

Mwamko mdogo wa wazazi unatajwa kuwa sababu kama anavyosema mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mpwapwa, Lukonge Mwiro

‘’Mzazi kutokuwa karibu na mwanawe kufuatilia maendeleo yake, inachangia mtoto kuyumba kielimu na kuamua kuacha shule kwani ni wanafunzi wachache ambao wazazi wao wapo karibu nao,’’ anaeleza.

Mazingira yasiyo rafiki

Mazingira yasiyo rafiki yanajumuisha ubovu na uduni wa miundombinu kama vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na tatizo la lugha. Hizi ni sababu zinazowakatisha tamaa wanafunzi na hatimaye baadhi wanajikuta wakiacha masomo.

“Unakuta mwanafunzi anakuja hapa hajui kabisa lugha inayotumika kufundishia kwa mtu huyu unawezaje kumsaidia?” Anahoji mwalimu Mwiro na kuongeza: “Tumejaribu kutoa ushauri kwa wanafunzi, kutengeneza mazingira ya wao kuzoea lugha lakini wengine wanaamua kuacha shule kwa madai kuwa hawaelewi.’’

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Saidi Mohammed anasema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha maendeleo ya watoto wao kielimu. Anasema wazazi ndiyo chanzo kwa mtoto kutomaliza masomo.

“Unakuta mtoto haendi shule lakini mzazi haulizi chochote na wengine wanaruhusu watoto wao kuingia kwenye biashara mbalimbali. Haiwezekani wanafunzi wanaanza wengi halafu mwisho wa safari wanabaki wachache, wazazi tuamke tusicheze na elimu,’’ anaeleza.

Kufeli mitihani

Sababu nyingine kubwa ya madaraja ya elimu kupungua wanafunzi, ni idadi kubwa ya wahitimu kufeli mitihani ya kumaliza madaraja husika.

Vijana wengi wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu hawafaulu mitihani yao ya mwisho. Wakati mwingine si makosa yao, shule nyingi hazina vitabu vya kutosha, na kwa hiyo inabidi wanafunzi kadhaa wachangie kitabu kimoja, inasema sehemu ya chapisho liitwalo Ujana Tanzania (2011).

Chapisho linaongeza: “Majumbani mwao hakuna umeme na hivyo hawawezi kujisomea usiku. Shule nyingi hazina walimu wa kutosha, na kwa maana hiyo madarasa yana wanafunzi wengi kuliko idadi inayotakiwa.’’

Sababu maalumu kwa wasichana

Wanafunzi wa kike wana sababu na mianya zaidi ya kuacha shule kuliko wanafunzi wa kiume. Tafiti na uzoefu vinaonyesha wanafunzi wa kike wanaacha shule kwa sababu ya kupata mimba au kuolewa mapema, wazazi kuwalazimisha kukaa nyumbani kwa minajili ya kusaidia kazi za nyumbani.

Sababu nyingine ni ukosefu wa vyumba vya stara wanapokuwa katika mzunguko wa damu wa mwezi, uhaba wa vyoo na wasiwasi wa kudhuriwa wakati wakienda ama kurudi shule.

‘’Hadi kufikia mwaka wa mwisho wa elimu ya sekondari idadi ya wavulana na wasichana wanaosoma huwa sawa, lakini idadi yao wote huwa ni ndogo sana. Ni vijana wanne tu kati ya 100 wanaomaliza miaka sita ya elimu ya sekondari,’’ linaongeza kusema chapisho hilo lililotolewa kwa uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (Unicef).

Mkakati wa Serikali

Serikali inatambua kuwa mdondoko wa wanafunzi ni changamoto kubwa katika mfumo wa elimu. Mbinu, mipango na mikakati mbalimbali imekuwa ikibuniwa kuhakikisha tatizo hili linatafutiwa ufumbuzi.

Moja ya mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa mpango wa elimu bila ada kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari. Tangu kuanza kwa mpango huo ambao ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, wanafunzi zaidi wanaandikishwa shuleni.

Kwa mfano, takwimu za Tamisemi zinaonyesha kuwa watoto walioandikishwa darasa la awali na la kwanza mwaka 2017 walikuwa 3,188,149. Uandikishwaji huu ni sawa na ongezeko la wanafunzi 319,849 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi hao mwaka 2016.

Ili kuondokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaofika elimu ya sekondari, Serikali imeanzisha mfumo mpya wa elimumsingi ambapo wanafunzi watasoma kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne. Ni mpango unaolenga kuwaokoa maelfu ya watoto waliokuwa wakidondoka katika mtihani wa kumaliza darasa la saba.

Mikakati mingine ni pamoja na programu za utoaji chakula cha mchana na ujenzi wa miundombinu hasa mabweni kwa ajili ya wasichana ili kuwakinga na vishawishi vya kupata mimba.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anasema hadi Mei 2017, wizara yake ilisharatibu uboreshaji wa miundombinu katika shule 274 katika halmashauri 119. Uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 1081, vyoo 2802 pamoja na mabweni 200.

Nusura kwa wasichana

Kwa kuwa waathirika wakubwa wa mdondoko wa wanafunzi shuleni ni wasichana, wadau wamekuwa wakishauri pamoja na mambo megine wanafunzi wa kike kusoma katika shule zilizo jirani na maeneo wanamoishi.

Hii inaweza kusaidia wakaepukana na vishawishi na vikwazo ambavyo mwishowe huwaingiza kwenye janga la mimba za utotoni.

Mikakati mingine maalumu kwa ajili ya watoto wa kike hasa waliopevuka ni pamoja na kupewa elimu ya uzazi na makuzi kwa uwazi zaidi; kupunguziwa kazi za nyumbani na kaya masikini kuwezeshwa kwa kupewa mitaji ili kukimu ugumu wa maisha.     

Tuesday, November 28, 2017

Mabango ya Kiingereza Ubungo kwa ajili ya nani?

 

Nikiwa Ubungo, kandokando ya barabara ya Morogoro, eneo maarufu kama ‘Ubungo Mataa’, namwona mzee yapata umri wa miaka 70 hivi.

Akiwa amevalia miwani yake yenye lenzi nzito, anahangaika kusoma maandishi katika mabango yenye matangazo yanayohusiana na shughuli ya ujenzi wa barabara. Anaamua kumuuliza kijana anayepita karibu naye ili kupata ujumbe unaopatikana.

Kijana huyo anaangalia maandishi, midomo yake inashikana anaanza kugugumiza... halitoki neno!

Katika eneo tajwa, shughuli za ujenzi wa barabara zinaendelea. Kuna mabango mbalimbali ya kutoa hadhari kwa watumiaji wa barabara kama ilivyo ada. Hata hivyo, mabango mengi yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Asilimia kubwa ya Watanzania wanakijua vizuri Kiswahili. Mabango yaliyosimamishwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasaidia kuwa makini na hali ya eneo hilo si msaada kwao.

Mengi yameandikwa kwa Kiingereza ambacho wengi hawakijui kama mzee aliyetaka kupata ujumbe unaopatikana katika mabango hayo, lakini asifanikiwe kutokana na ugeni wa lugha iliyotumika.

Kiasi kikubwa cha mabango hayo yana ujumbe ambao hauna tafsiri ya Kiswahili isipokuwa machache. Baadhi ya mabango yanasomeka hivi: Caution Deep DANGER Excavation (hakuna tafsiri ya Kiswahili); Road Closed (hakuna tafsiri ya Kiswahili); Pass Right (yaliko maneno hayo hakuna tafsiri ya Kiswahili isipokuwa nyuma ya bango hilo); Pass Left (ni kama ilivyo katika Pass Right). Mengine yana maneno: Men at Work (yapo yenye tafsiri na yasiyo na tafsiri ya Kiswahili).

Halikadhalika, tatizo hili linajitokeza katika maeneo mengine mengi jijini Dar es Salaam yakiwamo ‘Simu 2000’, Kariakoo, Posta na kwingineko.

Ukiwa unaingia katika kituo cha mabasi cha Simu 2000, utalakiwa na bango kubwa la rangi ya buluu lenye maneno SINZA BUS TERMINAL bila tafsiri yake.

Aidha, katika kituo hicho eneo lenye huduma ya vyoo, kuna kibao kilichoandikwa TOILET. Nikiwa kituoni hapo siku moja, niliwahi kushuhudia watu kadhaa wake kwa waume wakiuliza vyoo vilipo, huku bango hilo likisomeka vizuri kutoka walipo.

Maneno mengine ya Kiingereza yanayopatikana kwenye mabango jijini ni kama vile ‘Don’t block the gate’, ‘Danger-dont sit here’, Male/Female; Men/Women (kwenye vyoo), Bus Stand, Humps ahead na mengineyo.

Maneno hayo hutumika katika baadhi ya maeneo bila tafsiri ya Kiswahili ambacho takriban asilimia 90 ya walengwa wa ujumbe huo wanakifahamu.

Mbalamwezi ya Kiswahili inajiuliza, ikiwa tumo ndani ya Tanzania ambamo wananchi wengi wanakijua Kiswahili, kwa nini kunawekwa mabango yenye lugha ya kigeni ambayo wengi hawaijui?

Sheria inaeleza kuwa, utoaji wa ujumbe kwa umma hauna budi kuzingatia kundi kubwa la watumiaji wa lugha ya mahali husika.

Kwa sababu hiyo, sehemu zote mabango yanapaswa kutumia lugha ya Kiswahili na kwa kuwa kuna wageni wachache ambao wengi wao hutumia Kiingereza, basi chini ya maneno ya Kiswahili, ujumbe huo ufasiriwe kwa Kiingereza na si kinyume chake.

Ujumbe unaotolewa katika mabango aghalabu ni muhimu. Ikiwa lugha iliyotumika haieleweki kwa walengwa basi ni kazi bure!

Katika maeneo ya Ubungo ambapo ujenzi wa barabara unaendelea, mtu anapaswa kuelewa ujumbe uliotolewa katika mabango hayo, ili aweze kuchukua hadhari.

Kwa hivyo, mamlaka husika ziwe makini pindi zinapoandaa matangazo hayo. Hazina budi kuzingatia kanuni za lugha katika uandaaji wa matangazo kwa umma.     

Tuesday, November 28, 2017

Dar yajipanga dhidi ya uhaba wa walimu wa sayansi

 

By Beatrice Moses, Mwananchi bkabojoka@mwananchi.co.tz

Wahenga waliwahi kusema: ‘ujuzi hauzeeki’. Kauli hii imewasukuma viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza ajira za muda kwa walimu wastaafu wa masomo ya sayansi.

Walimu hao licha ya kushika chaki kwa miaka zaidi ya 30 na kulipwa mafao yao na kiinua mgongo, bado ujuzi wao unahitajika kwa kuwa hauzeeki.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu wa masomo hayo ambao unazikabili shule nyingi za Serikali.

Ofisa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu anasema wamejipanga kukabiliana na tatizo hilo kwa njia mbili, ikiwamo ya kuwatumia wastaafu hao.

Njia nyingine anasema ni kuwatumia wahitimu wa masomo ya sayansi ya vyuo vikuuu pamoja na wahitimu wa kidato cha sita.

“Hii haimaanishi Serikali inatuachia jambo hili, bali wakati inaendelea kutuletea walimu wa sayansi na sisi tunaendelea kutafuta katika utaratibu tulioueleza hapo awali ili kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa ipasavyo,” anasema.

Lissu anasema walimu wastaafu hawahitaji kibali kutoka ofisi ya kamishna wa elimu, bali watawaunganisha na wakurugenzi wa wilaya na manispaa waingie mkataba ili waendelee kutumia ujuzi wao.

“Kwa hao wastaafu tutaangalia yule anayeweza kuongea maneno yakaeleweka vizuri, hana matatizo makubwa ya kiafya tumeshatoa maelekezo kwa maofisa elimu ngazi ya manispaa tushirikiane katika kufanikisha hili,” anasema.

Anasema kuhusu kuwatumia wahitimu hao, tayari wamewaombea kibali kutoka ofisi ya kamishna wa elimu ili wapate leseni za kufundishia.

Anasema hatua inayofuata baada ya kuwapata walimu hao ni kukutana na wakurugenzi wa manispaa zote za Dar es Salaam na kujadiliana nao jinsi ya kuwalipa.

“Walimu hawa wote watakuwa wanalipwa posho na wakurugenzi, hivyo hii sio kwamba ni ajira ya kudumu, ni kibali cha kufundisha kwa kupitia leseni za miaka miwili,”anasema.

Anasisitiza: “ Baada ya hapo mwalimu au mhitimu huyo kama atapenda kuendelea na kazi ya ualimu nasi tukawa tumeridhika naye, tutamfanyia mpango akosome kozi ya mwaka mmoja ya stadhahada ya uzamili wa ualimu.”

Walimu wajitokeza

Fortnatus Kagoro ni Ofisa elimu taaluma wa mkoa huo, anaeleza tayari walimu wastaafu 49 wameshajitokeza kuomba nafasi ya kufundisha kwa mkataba kwa awamu ya kwanza.

“Idadi ya wastaafu waliojitokeza ni ndogo ikilinganishwa na ile ya vijana waliosomea masomo ya sayansi ambapo waliotuma maombi jumla yao ni 352 kati yao 100 wamesomea ualimu ambao wanasubiri ajira.

Baada ya kuwachuja, anasema o wamepatikana 99 hata hivyo kati yao ni 75 ndiyo wanaotarajiwa kunolewa kwa mafunzo ya awali.

‘’ Kuna sekondari 138 wakati idadi ya walimu ni 2313; kuna upungufu wa walimu 1323 wa sayansi, wakati kwa upande wa masomo ya sanaa kuna ziada ya walimu kama 880,’’ anasema.

Hatua hiyo ya Mkoa wa Dar es Salaam inasukumwa na maono ya Serikali kuu, ambayo yalibainishwa bungeni Juni 2016 na aliyekuwa Naibu Wizara wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo.

Alilieleza kwamba kutokana na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na Hisabati, serikali inaangalia namna ya kuwatumia walimu wastaafu wa masomo hayo kwa mkataba maalumu ili kupunguza tatizo hilo.

“Katika bajeti ya mwaka 2015/16 tuliona kwamba tunapaswa kuajiri walimu, lakini tutaenda mbali zaidi kwa walimu wa sayansi. Wapo wale waliostaafu lakini wana uwezo mzuri wa kufundisha tutaangalia jinsi ya kuwapa mikataba ili waweze kutumika,” alisema.

Hali ya walimu nchini

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anataja takwimu za walimu waliopo nchini kwenye shule za sekondari za Serikali kuwa ni 88,999 ambapo kati yao 18,545 ni walimu wa sayansi na Hisabati. Anasema kuna upungufu wa walimu wa sayansi na Hisabati 22,460.

Pongezi za wadau

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Cathleen Sekwao anapongeza hatua hiyo, akieleza kuwa ukosefu wa walimu wa sayansi ni changamoto, licha ya Serikali kutoa kipaumbele ufadhili kwa walimu wanafunzi wa masomo ya sayansi.

Sekwao ambaye amewahi kuwa mwalimu wa ufundi kwa miaka 23, anaeleza kuwa kuna changamoto nyingi kuhusu walimu na kwa kiasi kikubwa zinaathiri zaidi mchepuo wa masomo ya sayansi ikilinganishwa na michepuo mingine.

“Kuna mambo yanawakamisha walimu ikiwamo mazingira duni ya kazi ya walimu yanayowavunja moyo kufundisha. Pia, uoga wa wasichana kusomea masomo ya sayansi nayo ni changamoto ya aina yake, licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kutoa upendeleo kwa wanafunzi wa sayansi,’’ anasema na kuongeza:

“Maneno kwamba walimu ndiyo wanalipwa mshahara mdogo pia yanasababisha vijana wahitimu wa ualimu kukimbia fani, ingawa ukweli ni kwamba kuna tofauti ndogo na watumishi hasa wa sekta ya afya.’’     

Tuesday, November 28, 2017

Mwanafunzi asifungwe na darasa kupata maarifaJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

       Kuna mijadala mingi kuhusiana na vyanzo vya mtu kujipatia maarifa, ujuzi au stadi mbalimbali za maisha.

Wengine wanahusianisha maarifa, elimu na majengo ya madarasa kuwa ndio chimbuko la maarifa. Wengine wanaeleza kuwa maarifa yanaweza kupatikana hata nje ya jengo la darasa ikiwamo kupitia maono na ndoto.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili ya Longhorn 2017, neno maarifa lina maana ya ujuzi aghalabu wa kuzaliwa nao, anaoutumia mtu kupambana na maisha yake kila siku; au mbinu; hekima na busara. Pia, maarifa ni elimu aipatayo mtu kutokana na kusoma, kusikia au kutenda; uzoefu au ustadi.

Vilevile, maarifa huweza kufasiliwa katika dhana mbalimbali za kifalsafa kama epistemolojia; kama mojawapo ya tawi la falsafa linalojihusisha na hali na upana (vikwazo) vya maarifa.

Hapa maswali kadhaa huhojiwa. Kwa mfano, maarifa ni nini; maarifa hupatikana wapi; je, watu hujua nini; na je hujua vipi kile ambacho wanajua?

Dhana hiyo imejikita katika uchambuzi wa hali ya maarifa na jinsi maarifa yanavyohusiana na dhana sawa kama vile imani, ukweli ama ushahidi. Pia, inahusu mbinu na uzalishaji wa maarifa na shaka kuhusu madai mbalimbali ya maarifa.

Mwanafunzi ni mtu anayepata mafunzo ya taaluma au stadi akiwa chini ya uangalizi wa mwalimu. Maswali ambayo watu wanaweza kujiuliza ni kwamba katika jamii yetu maarifa na ujuzi mbalimbali hupatikana katika shule pekee?

Nchi nyingi zilizoendelea zilifanya juhudi kubwa katika kuwekeza katika maarifa kwa watu; na maarifa hayo kuendelea kupatikana hata nje ya jengo la darasa. Kwa kufanya hivyo walijikuta wakivumbua vitu vingi vilivyo msaada kwa dunia yote.

Ni kweli kwamba uvumbuzi wao umerahisisha kazi na ni wajibu wetu kutafuta maarifa ya kutengeneza na kuongezea uwezo wa walivyovumbua.

Ni vema wanafunzi wetu wakafahamu kuwa uwekezaji unaofanyika kwao wa kupata maarifa, ndiyo utakaokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo yao binafsi, jamii na taifa kwa jumla.

Hivyo wapatapo fursa za kuwa shuleni wahakikishe wanapata maarifa stahiki kwa kadri inavyopaswa. Kwa mfano, nchi inapokuwa na maono ya kuwa taifa la uchumi wa kati kupitia mabadiliko makubwa ya uchumi wa viwanda, ni wajibu hata kwa walimu kusaidia kwa kubadilisha mtazamo wao. Na wanafunzi nao wawe tayari kupokea maarifa katika mtazamo huo wa uchangiaji katika sekta ya viwanda.

Kwa lugha nyingine ni pale jamii itakapoweza kuwekeza kwenye maarifa ya watu wake, basi maendeleo ya kweli na endelevu hayakosi kuwapo. Si rahisi kuendelea bila maarifa ya uzalishaji. Kujitegemea kutokane na juhudi za jamii na wasomi wenye maarifa ya kujizalishia vitua au kwa maendeleo yao na kwa biashara.

Shule zinaruhusu watu kupata maarifa nje ya darasa?

Mbinu za ujifunzaji na ufundishaji za mwalimu zichokoe kiu ya ndani ya mwanafunzi katika kujenga hali ya kujitegemea kufikiri na kutafuta maarifa mengine hata nje ya mipaka ya darasa. Wanafunzi wasifungwe na mipaka ya shule katika kupata maarifa au stadi zenye faida kwao na kwa jamii husika.

Kwa mfano; sehemu za wafugaji maarifa ya ufugaji bora utakaokuza uchumi na kubadilisha hali za maisha kuwa bora ni jambo la kuhamasisha.

Wengine wanaotoka katika maeneo ya uwindaji, uvuvi, kilimo, uchongaji na ususi, nao wanapaswa kupewa fursa ya kupata maarifa katika shule na mazingira yanayowazunguka ili elimu wanayoipata iweze kuleta maana na manufaa kwao.

Pia, wazazi wana mchango mkubwa katika kuhakikisha mtoto au mwanafunzi habanwi na ile dhana kuwa elimu hupatikana shuleni tu. Wao pia wanaweza kuwajengea watoto na vijana kuwa na nidhamu ya kazi na kupenda kufanya kazi tangu wakiwa nyumbani na kwenye jamii. Kwa sababu nidhamu, jitihada na nia ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa, hunyanyua taifa.

Walimu na jamii kwa pamoja wana kazi ya kujenga elimu ambayo haina malengo ya kibinafsi ila yenye malengo ya kuleta mapinduzi kwenye jamii na taifa kwa jumla. Hii ni elimu ambayo itasaidia kuinua jamii na siyo kuiangamiza; ambayo hujenga mwelekeo wa kitaifa na sio wa kibinafsi; na ambayo hujenga maadili ya watu kwa kujua kati ya usahihi na upotofu na hatimaye kufuata kilicho sahihi kwa faida ya taifa letu.

Mathalani, wapo watu ambao husoma lakini wanajiangalia wenyewe tu badala ya kusaidia jamii yao; jambo ambalo husababisha elimu yao kuwa na manufaa madogo katika kuleta mapinduzi kwenye jamii.

Watu hawa kimsingi wanapaswa kuleta mabadiliko kwenye jamii inayowazunguka, ili kukamilisha ile dhana ya thamani ya elimu.

Hivyo, maarifa yatokanayo na mbinu na njia mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji za walimu shuleni, zinapaswa kujenga misingi imara ya kimaadili. Jitihada za kutafuta maarifa na stadi stahiki zijengwe kwenye maadili ya jamii na taifa.

Hakuna taifa ambalo watu wake wameendelea bila kuwa na maarifa. Kwa hiyo ni muhimu kujifunza na kusoma bila kuchoka hata nje ya darasa rasmi na kutumia maarifa hayo kwa faida ya taifa na jamii kwa jumla.

Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha kuwa watoto na vijana wetu wanaosoma katika shuleni na vyuoni, hawabanwi na mawazo kwamba maarifa na stadi pekee hupatikana katika majengo ya shule.     

Tuesday, November 28, 2017

Umuhimu wa huduma ya unasihi kwa wanafunzi-2Christian Bwaya

Christian Bwaya 

        Tumeona jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na changamoto za kijamii zinazowakabili wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa nyakati tofauti, imekuwa ikitoa nyaraka zinazotoa maelekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na matatizo ya kijamii yanayoweza kuathiri maendeleo ya wanafunzi.

Katika makala yaliyopita, tuliona mifano kadhaa ya jitihada hizi. Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2000, mathalani, ulilenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujilinda na maambuzi ya Ukimwi.

Aidha, Waraka wa Elimu namba 11 wa mwaka 2002 ulianzisha huduma za malezi na ushauri nasaha kwenye taasisi za elimu.

Mpango huo hata hivyo, ulikabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa wataalamu wa unasihi shuleni na vyuoni na hivyo mpango huo haukuweza kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Utaratibu wa kuteua mwalimu mwenye majukumu mengine ya kufundisha, mwalimu asiye na mbinu na uzoefu wa unasihi na kumfanya kuwa mnasihi wa wanafunzi, ni kutarajia kisichowezekana.

Kwa kutambua upungufu huo, mwaka 2007, wizara kwa kushirikiana na mradi wa Kuzuia na Kuelimisha Wanafunzi kuhusu Virusi vya Ukimwi (PASHA), iliandaa mwongozo wa kuendeshea mafunzo ya unasihi kwa walimu shuleni.

Mwongozo huo, pamoja na malengo mengine, ulilenga kupanua uelewa wa walimu kuhusiana na mbinu za kufanya unasihi, afya ya uzazi, tabia hatarishi na elimu ya maisha kwa jumla.

Katika makala haya, tunaangazia maeneo muhimu ya maisha ya mwanafunzi yanayoweza kushughulikiwa kupitia huduma wa unasihi shuleni.

Kujitambua

Mwanafunzi anayejitambua anajua uwezo wake, anajua ndani yake kuna kitu gani, wajibu wake katika jamii ni upi. Kwa bahati mbaya, mitalaa yetu ya elimu, kwa jumla haishughulikii masuala haya ipasavyo.

Kupitia unasihi na ushauri, mwanafunzi huyu anaweza kusaidiwa kujitambua kwa maana ya kutambua wito wake maishani na kuelewa ndani yake kumelala nini kinachoweza kuamshwa.

Kuelewa wajibu wake

Malengo mapana ya elimu rasmi ni kumwezesha mwanafunzi kuelewa nafasi yake katika jamii. Hali halisi, hata hivyo, haionyeshi ni namna gani mfumo wetu wa elimu unawawezesha wanafunzi kutambua wajibu wao katika jamii.

Kutofikiwa kwa lengo hilo, kumefanya watu wetu wajifikirie wenyewe badala ya kujiuliza kile wanachoweza kukifanya kama mchango wao kwa jamii.

Kipimo cha mafanikio kimekuwa ni namna mtu binafsi anavyoweza kuwatumia watu wengine kutimiza mahitaji yake.

Unasihi unajaza ombwe hili. Kwanza, unasihi unamwezesha mwanafunzi kujitambua na hivyo kuwa na mtazamo mpana wa maisha.

Kupitia kujitambua, mwanafunzi anajengewa uwezo wa kuelewa ana kipi cha kufanya kinachoweza kuinufaisha jamii yake.

Mwongozo wa maamuzi

Maisha ya mwanafunzi kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote, ni mfululizo wa maamuzi. Mwanafunzi anahitaji kuamua kwa mfano, nani anafaa kuwa rafiki yake, ushauri upi wa kuzingatia na upi wa kupuuza.

Malezi katika familia nyingi, yamejenga ufa kati ya watoto na wazazi. Hali hii inafanya iwe vigumu kwa watoto kujengewa uwezo wa kufanya maamuzi yanayojitegemea.

Huduma ya unasihi inaweza kujaza ombwe hili kwa kumsaidia mwanafunzi kufanya maamuzi yanayoongozwa na uelewa. Pia, unasihi unaweza kumsaidia mwanafunzi kutengeneza vipaumbele.

Hakuna mafanikio yasiyotegemea uwezo wa kupangilia kipaumbele. Kujua kipi ni muhimu na kipi si muhimu, kifanyike wakati upi na kipi kingoje, ni baadhi ya mambo yanayoweza kumsaidia mwanafunzi.

Uelekeo wa kitaaluma

Nakumbuka wakati nasoma, hatukuwa na mtu wa kutusaidia kuelewa tunaelekea wapi. Tulitegemea vigezo kama ufaulu kuamua tufanye nini baada ya kumaliza masomo.

Matokeo yake wengi tulisoma fani zisizolingana na malengo na vitu vilivyokuwa ndani yetu. Tulipokwenda vyuoni, wakati mwingine, ilikuwa kawaida kuona watu wakihangaika kubadili fani walizokuwa wamezichagua awali.

Pamoja na ukweli kwamba wakati mwingine kuna sababu nyingi zilizo juu ya uwezo na mipaka ya mwanafunzi mwenyewe, mara nyingi, maamuzi hayo yanafanyika bila kuongozwa na uelewa.

Unasihi kwa mukhtadha huu, una nafasi kubwa ya kumwongoza mwanafunzi kujua afanye nini kwa ngazi ya elimu inayofuata. Badala ya kuongozwa na ufaulu na matarajio ya jamii pekee, mwanafunzi aongozwe na vipaji, uwezo na wito wa kipekee alionao ndani yake.

Changamoto

Shule zetu hazina walimu wengi wenye utaalamu wa unasihi. Ingawa walimu husoma unasihi kama sehemu ya mafunzo yao ya ualimu, ufundishaji kama tulivyoona kwa kweli haukidhi mahitaji halisi katika mazingira ya shule zetu.

Kwa mfano, wakufunzi na wahadhiri wengi wanaopewa kazi ya kufundisha unasihi vyuoni, mara nyingi huwa ni watu waliosoma ualimu wa jumla. Pamoja na kubobea kwenye ualimu, wahadhiri hawa hukosa uelewa wa kina wa unasihi kama somo linalojitegemea.

Lakini kwa kuwa imejengeka dhana potofu kwamba kila mhadhiri aliyesoma ualimu anaweza kufundisha unasihi, matokeo yake somo hili huishia kufundishwa kinadharia.

Changamoto hizi kwa kiasi kikubwa, zinatokana na ukweli kuwa saikolojia na unasihi, ni fani mpya ambazo bado hazijatambuliwa vya kutosha katika jamii yetu.

Tunavyo vyuo vichache hapa nchini, kwa mfano, vyenye programu za shahada za awali, umahiri na uzamivu katika saikolojia na unasihi. Vyuo vingine vilivyobaki vinafundisha saikolojia na unasihi kama sehemu ya programu nyingine.

Ushauri

Kwa kuwa tunakubaliana kuwa unasihi una nafasi muhimu kwa mafanikio ya mwanafunzi, ni muhimu basi kutazama namna tunavyoweza kufanya unasihi kuwa huduma ya lazima katika mazingira ya shule zetu.

Katika kulifanikisha hilo, kama taifa, tunazo sababu za kutosha kuanzisha na kuimarisha programu zinazoandaa wataalamu waliobobea katika saikolojia, ili waweze kusaidia malezi ya watoto wetu.     

Tuesday, November 21, 2017

Walianza shule 103 wakahitimu saba tu!

Hali halisi ya usafiri kwa wanafunzi wengi

Hali halisi ya usafiri kwa wanafunzi wengi wilayani Bahi ni kama hivi inavyoonekana kwa wanafuzi hawa wa Shule ya Sekondari Chikopelo. Kwa sababu ya umbali wanalazimika kutumia usafiri wa baiskeli. Picha na Tumaini Msowoya 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@wananchi.co.tz

       Kati ya wanafunzi 91 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Chikopelo, Wilayani Bahi, Dodoma mwaka 2014, ni 26 tu ndio wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

Taarifa rasmi katika shule hii zinaonyesha kuwa tatizo lilianza mara tu baada ya kuchaguliwa kwao, kwani wanafunzi 23 hawakuripoti hivyo walioanza kidato cha kwanza walikuwa 68 pekee.

Kutokana na “ugumu wa safari ya elimu”, zaidi ya nusu ya wale walioripoti waliishia njiani. Waliopo ni wanafunzi 26, huku 42 wakiwa wameacha masomo miaka minne iliyopita. Kati yao 14 ni wavulana na 12 ni wasichana.

Hata hivyo, mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Ahadi Mgando anasema hali hiyo siyo mpya shuleni hapo na kwamba idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu mwaka huu “ni kubwa” ikilinganishwa na miaka iliyopita!

Mgando anarejea takwimu za awali ambazo zinaonyesha kuwa mwaka 2011 walihitimu saba tu kati ya 103 walioingia kidato cha kwanza mwaka 2008, wakati mwaka 2013 walihitimu wanafunzi nane kati ya 42 walioandikishwa kidato cha kwanza mwaka 2010.

Mwaka 2014 walihitimu wanafunzi saba kati ya 36 walioandikishwa mwaka 2011 na mwaka jana kulikuwa na wahitumu wanafunzi 25 kati ya 256 waliojiunga na kidato cha kwanza 2013.

“Hii ni changamoto kubwa sana, shule yetu ina vyumba vya madarasa vingi lakini vingi vipo wazi kutokana na utoro wa wanafunzi,”anasema.

Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa kuwa suala la utoro linaonekana kuwagonganisha vichwa walimu na wazazi, ambao walishindwa kuelewana hata katika kikao kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili suala hilo.

“Kila siku wimbo ni utoro! utoro! Lini tutajadili masuala mengine? Mimi nadhani sisi tulio humu watoto wetu wapo tayari darasani, tumieni tu sheria kuwakamata wenye watoto watoro,”anasema mmoja wa wazazi, Charles Sales.

Shule hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 320, hivi sasa inao 192 lakini mkuu wake, Juma Idosa anasema ni wanafunzi 120 ambao wanahudhuria kikamilifu na kwamba waliobaki 72 wana mahudhurio hafifu.

Mwalimu Idosa anasema umaskini ndio sababu kubwa ya watoto wengi hasa wa kike kuacha shule. “…tumejitahidi kwa kila njia walau sasa hivi unaona kuna wanafunzi hao unaowaona,’’ anaeleza na kuongeza; Kwa kweli hali ni mbaya, ndio hapa nasukumana na wazazi tusaidiane ili wanafunzi hawa waweze wamalize shule.’’

Hali ilivyo Bahi

Utoro ni tatizo katika shule nyingi za Bahi. Katika Shule ya Sekondari Magaga, ni wasichana wawili tu ndio wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, kati ya saba walioanza kidato cha kwanza mwaka 2014.

“Tulikuwa saba darasani, wenzetu wengine waliishia njiani lakini sisi wawili tumesalimika. Sio kwamba hatukukutana na miiba, tulikutana nayo sana ila tunahitimu kwa neema ya Mungu,”anasema Mlekwa Matonya, mmoja wa wasichana hao.

Miba anayoizungumzia Mlekwa ni vishawishi kutoka kwa wanaume kwa sababu anakabiliwa na ugumu wa maisha, kutokana na kipato kidogo cha familia yake na wakati huo huo, amepanga chumba cha bei naafuu anakoishi peke yake.

Katika Shule ya Sekondari ya Bahi, kati ya wanafunzi 64 walioanza kidato cha kwanza miaka minne iliyopita ni 24 pekee ndio wanaotarajiwa kumaliza, huku 40 wakiwa wameishia njiani.

Tatizo la utoro liko hata katika shule za msingi. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifuduka, Daniel Mchomvu anasema kama isingekuwa ukali, madarasa ya shule hiyo yangekuwa matupu.

“Tulilazimika kuwa wakali, hatukuwa na mzaha kwenye suala la utoro hivyo wazazi wakaanza kuogopa na kulazimika kuleta watoto wao shuleni,” anasema.

Vifungu namba 35 (1), (2) na (3) vya Sheria ya Elimu ya 1978 na marekebisho yake vinawalazimisha wazazi kuwaandishikisha watoto wao darasa la kwanza, baada ya kufikisha miaka saba na kuhakikisha wanahudhuria masomo ya elimu ya msingi.

Sheria hiyo inampa wajibu mwanafunzi yeyote aliyeandikishwa kwa ajili ya masomo kuhakikisha anahudhuria shuleni bila kukosa hadi atakapohitimu elimu husika.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifuduka, Gasper Mhembano, anasema amekuwa akiwahimiza wazazi kusimamia mahudhurio ya watoto wao na kwamba wale wanaoonyesha ukaidi hushitakiwa.

Hata hivyo, anasema usimamizi wa sheria unakabiliwa na changamoto ya kutokuwapo kwa mahakama.

“Kutoka hapa hadi mjini ni kilometa 130 na usafiri ni duni hivyo wakati mwingine tunakosa jawabu,”anasema.

Ofisa elimu wa Sekondari Bahi, Hassan Mohamed anakiri kuwa utoro ni mzigo mkubwa kwa wilaya hiyo.

“Tulishawaagiza watendaji wa vijiji na kata kuchukua hatua kali za kisheria, ikiwamo kukamatwa na kupelekwa mahakamani wazazi wenye watoto watoro,”anasema.

Sababu za utoro

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inataja sababu za utoro kuwa ni umbali wa kutembea kwenda shuleni na kurudi, ujauzito, ndoa za utotoni, ajira za watoto, utoro, umaskini, kukosekana kwa mahitaji maalumu shuleni kwa baadhi ya wanafunzi na baadhi ya mila na desturi zinazokinzana na utoaji wa elimu kwa watoto wa kike.

Mkazi wa kijiji cha Zegere, Sebena Julius aliyeacha masomo kutokana na umbali kutoka kijijini kwake hadi shule ya sekondari ya Chikopelo alikokuwa akisoma anasema: “Nilikuwa natembea mbali na miguu inavimba, nikaamua kuacha shule nipo tu nyumbani”.

Mwingine ni Felista Martine wa kijiji cha Chali Igongo ambaye alisema umaskini ndio unaowasumbua wazazi wengi.

“Mwanangu alipofaulu niliugua kwa sababu sina kitu, nilihangaika nikapata mahitaji yake muhimu na japo anaendelea na shule, ila sijui kama atamaliza,”anasema Felista ambaye analea familia peke baada ya kutelekezwa na mumewe.

Mkazi wa Kijiji cha Isanga, Fadhil Wilfred aliitaja sababu nyingine ya utoro kuwa ni kukosekana kwa mwamko wa elimu miongoni mwa wananchi wa Bahi, akisema baadhi ya wazazi hufurahia watoto wao wa kike kuacha shule ili wapate mahari pale wanapoolewa.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu anasema moja ya kazi kubwa walizonayo ni kupambana na utoro.

“Kuna wakati tunatafuta vijana wasomi wa kuwaajiri kutoka kwenye hii wilaya tunashindwa, tatizo ni utoro. Kila siku huwa nawaambia mpaka lini watoto wenu watabaki bila elimu?”anasema.

Ni tatizo la kitaifa

Sio Bahi pekee, tatizo la utoro limetamalaki katika shule nyingi za umma nchini.

Kwa mfano, takwimu za msingi za elimu Tanzania (Best) zilizotolewa na Tamisemi Disemba 2016, zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 61,488 walioacha masomo, utoro unachukua asilimia 93.2 wakati mimba ni asilimia 5.6. Wanafunzi waliacha masomo kwa utoro asilimia 42.4 ni wasichana ikilinganishwa na wavulana ambao ni 51.5.     

Tuesday, November 21, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tunalisubiri kongamano la wadau wa Kiswahili

 

By Erasto Duwe

        Mikakati mingi ikiwa inaendelea kufanywa na Serikali na asasi zake kwa lengo la kukiendeleza Kiswahili.

Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), kimeandaa Kongamano kubwa la lugha ya Kiswahili litakalofanyika Novemba 23 hadi 24 katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili kutoka Afrika Mashariki na kwingineko.

CHAKAMA ni chama cha Kiswahili kilichoundwa mwaka 2002 kikihusisha nchi za Afrika ya Mashariki, na makao yake makuu yako jijini Arusha, Tanzania.

Lengo kubwa la CHAKAMA pamoja na malengo mengine ni kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti, ufundishaji na utumiaji wa Kiswahili katika Afrika Mashariki katika nyanja zake zote.

Shughuli kubwa zitakazofanywa katika siku hizo za kongamano ni uwasilishaji wa makala anuwai za kitaaluma zihusuzo lugha ya Kiswahili na majadiliano yatakayotawala mada husika.

Wawasilishaji watatoka miongoni mwa Wanachakama walioandaa makala hizo. Mada kuu katika Kongamano hilo ni “Kiswahili na Maendeleo ya Afrika Mashariki.”

Mada hii kuu ina mada ndogondogo ambazo zimefanyiwa tafiti na kuandikiwa makala zitakazowasilishwa katika kongamano hilo.

Miongoni mwa mada hizo ndogondogo ni pamoja na Kiswahili na Utandawazi, Kiswahili na Elimu, Hali ya Kiswahili katika mataifa ya Afrika Mashariki, na Kiswahili na Maendeleo ya Uchumi.

Nyingine ni Kiswahili na Siasa, Kiswahili na Uchapishaji, Kiswahili na Utafiti, Kiswahili na Usalama, na kadhalika.

Makala takriban 105 zitakazowasilishwa katika kongamano hilo na kufanyiwa majadiliano, zinahusiana na maeneo mbalimbali yaliyotajwa katika mada hizo ndogondogo.

Miongoni mwa mada hizo, zipo zile zinazohusu masuala motomoto ya kisasa yanayoibuka mathalani kuhusu maendeleo ya lugha na changamoto anuwai zinazokikabili Kiswahili.

Aidha, mada hizo zinahusiana na matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali kama mada hizo ndogondogo zinavyojipambanua.

Kiswahili kwa wakati huu, kimepewa hamasa kubwa kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kwa vitendo katika matukio ya kitaifa na kimataifa.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika moja ya vikao vya Bunge alionyesha bayana nia ya Serikali ya kukiendeleza Kiswahili kimataifa.

Alieleza kuwa, Serikali itawatuma wakalimani watakaofanya ukalimani wa hotuba za viongozi mbalimbali watakaoiwakilisha Tanzania katika mikutano ya kimataifa sehemu mbalimbali nje ya nchi.

Aidha, Bunge la Afrika Mashariki nalo tayari limekifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika vikao vyake.

Halikadhalika, idadi ya vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili huko ughaibuni, inazidi kuongezeka siku hadi siku na raghba ya wageni kujifunza Kiswahili imeongezeka maradufu.

Mwenyekiti wa CHAKAMA Afrika Mashariki, Dk Mussa Hans, anatoa wito kwa wanachama, wadau na wapenzi wote wa Kiswahili kushiriki kwa wingi katika kongamano hilo ili kuweza kujadili na kuzidi kukiimarishia Kiswahili misingi yake kama taaluma lakini vilevile kama lugha ya mawasiliano na utandawazi.     

Tuesday, November 21, 2017

Kilio cha shule ya msingi Pongwe

Sehemu ya wanafaunzi wenye mahitaji maalumu

Sehemu ya wanafaunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Pongwe iliyopo mkoani Tanga. Wanafunzi hawa pamoja na mambo mengine wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa chakula. Picha na Constantine Akitanda 

By Constantine Akitanda, Mwananchi

       Shule ya msingi Pongwe iliyoko katika kata ya Pongwe ndani ya jiji la Tanga ni miongoni mwa shule chache nchini zinazotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Shule hii iliyoanzishwa 1959 ikipokea wanafunzi wa darasa la tano hadi la nane, iko takribani kilomita 15 nje ya jiji hilo

Mwaka 1968, shule ilianzisha rasmi kitengo cha watu wenye ulemavu wa macho na ilipofika mwaka 2009 kitengo cha watu wenye ulemavu wa ngozi nacho kikaanzishwa na Serikali. Hii ilitokana na matukio kadhaa ya mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Shule ikapewa jukumu la kupokea wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, uamuzi huu ulifanynywa na Serikali kutokana na ukweli kwamba wenye ulemavu wa ngozi pia wanakabiliwa pia na tatizo la uoni hafifu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Yahya Mafita anasema kuendesha shule hiyo si jambo la mchezo, changamoto ni nyingi na ruzuku ya Serikali haitoshelezi katika kukabiliana na mambo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa chakula cha watoto wenye mahitaji maalumu shuleni hapo.

Anasema, Serikali iliamua kwa makusudi kuifanya Pongwe kuwa eneo maalumu na la kupigiwa mfano katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, lakini lengo hilo limegubikwa na changamoto.

Mojawapo ya changamoto hizo ni uhaba wa fedha kugharimia chakula kama anavyoeleza: “Chakula cha wanafunzi pekee kwa mwezi ni takribani Sh6 milioni, sisi tunapokea Sh3 milioni, hii ni changamoto kubwa ukizingatia kuwa hii ni shule maalumu na ina wanafunzi 79 wenye mahitaji maalumu wanaoishi hapa shuleni.”

‘’Elimu bila malipo ni jambo jema, lakini ni muhimu ruzuku ya Serikali iendane na uhalisia wa mahitaji ya kila shule. Ikumbukwe kwamba Shule ya Msingi Pongwe haihudumii wanafunzi wenye mahitaji maalumu pekee kutoka sehemu mbalimbali za nchi, bali pia hutumiwa na wanafunzi wenyeji wa eneo hili la Pongwe,’’ anaeleza.

Changamoto nyingine ni uhaba wa vyumba vya madarasa. Uhaba huu umesababisha darasa moja kuchukua wanafunzi hadi 120, hali inayosababisha wanafunzi kusongamana, lakini pia mwalimu kukosa udhibiti wa kutosha kwa wanafunzi na hasa namna bora ya kuwafundisha na kuwasimamia.

Kimsingi, idadi ya wanafunzi 120 kwa darasa inakinzana na sera ya elimu na miongozo mbalimbali inayotaka chumba kimoja cha kufundishia wanafunzi kisizidi idadi ya wanafunzi 40. Lakini hili limekuwa kinyume katika shule hii yenye mahitaji maalumu.

Mwanafunzi Marieta John mwenye ulemavu wa ngozi, anasema wanahitaji ulinzi wa kutosha katika jamii hasa kwa kuzingatia kuwa uzio uliokamilika, jambo linaloweza kusababisha wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kufanyiwa ukatili.

Shule haina uzio, uliopo umejengwa upande wa mbele pekee, eneo lote la nyuma ya shule liko wazi na huko ndiko kwenye pori, usalama wetu uko wapi? Kupafanya Pongwe kuwa shule yenye mahitaji maalumu lilikuwa ni jambo jema, lakini kuacha miundombinu ikiwa nusu ni hatari, tunaomba tusaidiwe kwa hili, anasema Marietha.

Ofisa elimumsingi wa jiji la Tanga, Khalifa Shemahonge anakiri kuzitambua changamoto za Pongwe na kwamba mahitaji ya wanafunzi maalumu kwa kawaida huwa ni gharama.

‘’Ni lazima Serikali tushirikiane na wadau wengine katika kusaidia kupunguza kama siyo kuzimaliza changamoto, ili tuweze kuwahudumia wanafunzi wetu. Tuwachangie watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwa watoto ni sehemu ya jamii, ’’anasema

CDTF yainusuru shule ya Pongwe

Mwalimu Mafita anatoa pongezi kwa taasisi ya ya Community Development Trust Fund (CDTF) ambayo ni miongoni mwa taasisi za kijamii iliyosikia kilio na kuitikia kwa haraka kutatua kero ya vyumba vya kulala wanafunzi wenye mahitaji maalumu sambamba na kutafuta gari.

‘’Gari hili sasa limerahisisha huduma kwa wanafunzi hasa kunapotokea suala la ugonjwa,’’ anaeleza.

CDTF ni moja ya mashirika yanayokusudia kuacha alama kwenye shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo baada ya kusikia kilio cha uongozi wa shule hiyo kupitia maombi maalumu, shirika likajielekeza kujionea uhalisia na kisha kuanza kutafuta fedha ili kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto badala ya kuiachia Serikali pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa CDTF Henry Mgingi anasema taasisi yake imebaini mahitaji kadhaa katika shule ya Pongwe, lakini imefanikiwa kuyatatua machache, miongoni mwa changamoto zilizopewa ufumbuzi ni pamoja na ununuzi wa gari moja kwa kushirikiana na Emirate Foundation

Ukiondoa kuwapatia wanafunzi bima ya afya, CDTF pia imefanikiwa kujenga nyumba ya kulala wanafunzi hao yenye uwezo wa kubeba zaidi ya wanafunzi 78 ambayo imegharimu jumla ya Sh98 milioni na kwamba jengo hilo la kisasa linatarajiwa kukabibiwa serikalini mwishoni mwa Novemba 2017.

‘’ Jamii na wadau wengine wote wakumbuke majukumu yao ya msingi katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu, kwa kuwa jamii ndiyo chombo kikubwa cha kujenga misingi ya kuwajenga watoto wetu,’’ anashauri.     

Tuesday, November 21, 2017

JICHO LA MWALIMU : Umuhimu wa zana za kufundishia kwa mwalimuJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

        Wakati mwingine baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kupata maarifa na ujuzi tarajiwa katika hatua fulani ya elimu.

Hii ni kwa sababu ya mbinu na njia za ufundishaji za baadhi ya walimu kushindwa kuwagusa.

Mathalani, maandalizi duni ya mwalimu kabla ya kufundisha na kutotumia zana mbalimbali za kujifunzia na kufundishia, zinaweza zikawa sababu mojawapo ya baadhi ya wanafunzi kushindwa kuelewa somo, hivyo kusababisha washindwe kufaulu majaribio na mitihani.

Zana za kufundishia na kujifunzia ni kitu chochote ambacho mwalimu hutayarisha, kwa lengo la kukitumia anapokuwa anafundisha ili kuinua kiwango cha uelewa na elimu kwa jumla.

Pia, zana za kujifunzia na kufundishia huwakilisha vifaa vyote ambavyo mwalimu hutayarisha na kutumia wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji, ili zimrahisishie ufundishaji wake na kuwafanya wanafunzi waelewe somo kirahisi zaidi.

Hivyo, zana za kufundishia na kujifunzia ni vifaa vinavyotumika katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji.

Makundi ya zana

Wataalamu wa saikolojia ya elimu na njia za ufundishaji, hugawa zana za kujifunzia na kufundishia katika makundi makubwa matano kama yanavyoainishwa hapo chini kwa kuzingatia umuhimu:

Moja, vitu halisi: Hivi ni bora kuliko zana nyingine kwa kutimiza lengo lake la kufundisha. Kwa mfano, vitu halisi vinaweza kuwa ni matunda, saa, simu, maji, chupa, samaki, mafuta na nyundo.

Mwalimu anapotumia vitu halisi katika somo lake, husababisha wanafunzi wake kujenga hali ya kuwa na uwezo wa kuchunguza, kuhoji (kudadisi), kugundua na kufurahia somo.

Zana zilizopo katika kundi hili la vitu halisi huzidi kuwapa fursa wanafunzi nafasi kubwa ya kujifunza kwa vitendo na kutumia milango mingi ya fahamu kwa wakati mmoja.

Mbili, zana bandia; wakati mwingine huitwa zana za maumbo au kwa lugha ya Kiingereza ‘model’ (modeli). Kundi hili la zana huchukua nafasi ya pili kwa ubora kutoka kundi la zana halisi.

Endapo hakuna uwezekano wa kupata kitu halisi, mwalimu anaweza kuchagua kutumia vitu bandia au vitu vilivyo mfano wa vitu halisi.

Kwa mfano; badala ya mwalimu kubeba kisu halisi au matunda halisi anaweza kuchukua kisu na matunda bandia (ya plastiki) yaliyotengenezwa mfano wa kitu halisi.

Faida za matumizi ya vitu au maumbo bandia huzidi zana za picha na chati kwa sababu vitu bandia hufanana na vitu halisi.

Tatu, runinga, video na sinema. Matumizi ya runinga, sinema na video kama zana za kujifunzia na kufundishia huwezesha wanafunzi kutazama na kuona vitu kama vilivyo katika uhalisia wake. Pia, wanafunzi huweza kuona na kusikia kinachofanyika katika picha jongefu.

Nne, picha na michoro: Kundi hili huwakilisha vifaa kama chati, grafu, ramani, mabango madogo na makubwa. Kundi hili la zana huzidiwa ubora na runinga kwa sababu huwawezesha wanafunzi kuona tu. Hivyo, zana hizi huhitaji uwezo wa uoni.

Tano, vinasa sauti, redio, cd na santuri. Kundi la zana hizi za kujifunzia na kufundishia humsaidia mwanafunzi kujifunza kwa kusikia.

Ni kazi ya mwalimu husika kutayarisha vipindi mbalimbali kwa kuvirekodi kupitia kinasa sauti. Zana hizi huweza pia kutumiwa na wanafunzi wanaosoma kwa njia ya masafa (learning distance).

Umuhimu wa kutumia zana

Matumizi ya zana za kujifunzia na kufundishia yana faida kwa pande zote mbili; humsaidia mwalimu kufikisha lengo au ujumbe kwa mwanafunzi.

Pia, mwalimu anapotumia zana, mwanafunzi hupata faida kwa kujifunza zaidi kwa kuona,kugusa, kuonja, kunusa, na kusikia (kwa kutumia milango yote ya fahamu)

Humsaidia kubadilisha mazingira ya kupatia maarifa na ujuzi; kumfanya afurahie somo hivyo kulipenda. Pia, kumpatia mwanafunzi maarifa na ujuzi kwa njia ya mkato na ujuzi wa maarifa hayo huwa vigumu kusahaulika upesi.

Kumuonyesha ukweli katika somo kwa sababu mwanafunzi huona vitu vya kweli au mifano yake; na kumsaidia kumfanya mwanafunzi ajifunze kwa njia ya kutenda na si kwa kusikiliza tu.

Sifa za zana zana za kufundishia

Zana zinazotumika kufundishia zinapaswa kuwa na uhusiano na mada inayofundishwa; nadhifu na zinazovutia; uhalisia; usahihi zisizoleta tafsiri mbaya kwa kundi fulani la imani ya dini; kubwa na zinazoweza kuonekana kwa darasa zima na zisizoleta madhara ya macho au masikio (zisiwe hatarishi). Pia, zana zinapaswa ziweze kuhamishika au kubebeeka kwa urahisi.

Umuhimu wa kuzijaribu zana kabla ya kutumika

Ni vizuri mwalimu akazijaribu zana au vielelezo vyake kabla ya kuvitumia darasani. Kwa kufanya hivyo, mwalimu hupata faida nyingi zikiwemo kuhakikisha kama zana/ vifaa hivyo vinafanya kazi kwa usahihi kama vilivyokusudiwa.

Kubaini kama kuna zana au vifaa vibovu ili viweze kutengenezwa au kutafuta vingine; kugundua udhaifu wa zana au vielelezo alivyopanga kuvitumia; kutambua haraka kama kuna madhara ya kiimani, yanayoweza kuletwa na vielelezo hivyo

Pia, kufahamu namna sahihi ya kutumia zana husika.

Matumizi ya zana au vifaa katika kujifunzia na kufundishia ni nyenzo muhimu kwa sababu husaidia katika ujenzi wa maana kwa kile mwanafunzi atakachojifunza. Vilevile, zana hurahisisha kazi ya mwalimu ya kufundisha.

Hivyo basi, zana za kujifunzia na kufundishia hupaswa zitumike kulingana na lengo la somo. Zitumike katika hatua yoyote ya somo kulingana na mpangilio wa mwalimu na lengo la zana husika.

Lengo hasa la kutumia zana katika kufundisha liwe kukuza na kuinua kiwango cha kujifunza cha mwanafunzi.

Ni vema na ni wajibu wa walimu kujifunza namna rahisi ya utengenezaji wa zana kwa kutumia malighafi zinaopatikana katika maeneo yao.     

Tuesday, November 21, 2017

ELIMU NA MALEZI : Umuhimu wa huduma ya unasihi kwa wanafunzi-1Christian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

        Unasihi si huduma iliyozoeleka katika mazingira yetu ya Kiafrika.

Mara nyingi tunaposikia maneno kama ‘ushauri nasaha’ mawazo yetu yanakwenda kwa watu wenye matatizo ya akili au waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Hata hivyo, huduma hii imekuwa sehemu ya maisha yetu kwa muda mrefu.

Tunafahamu, kwa mfano, tumekuwa na mila na desturi katika jamii zinazolenga kuwasaidia vijana wa umri fulani kujitambua na kutambua nafasi waliyonayo katika jamii.

Utaratibu huu wa wazee na watu wenye busara kuwaongoza vijana kujitambua, kimsingi ni aina ya unasihi.

Hata katika maisha yetu ya kila siku, tuna mazoea ya kutafuta ushauri kwa watu wanaoaminika tunapotaka kufanya maamuzi.

Ndiyo maana si ajabu kwa mfano, mtu anayefikiria kununua kiwanja mahali fulani, kutafuta watu anaoamini wanaweza kumsaidia.

Katika mazingira ya shule, unasihi hivi sasa una nafasi ya kipekee pengine kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.

Hii inatokana na ukweli kuwa mafanikio ya mwanafunzi darasani, kwa kiasi kikubwa yanategemea maisha yake ya kawaida nje ya darasa.

Kwa mfano, ili mwanafunzi aweze kusoma kwa utulivu, uhusiano wake na familia yake lazima uwe mzuri.

Mwanafunzi anayetoka kwenye familia yenye migogoro na misukosuko, anakuwa kwenye mazingira yanayoweza kuathiri uzingativu wake darasani.

Sambamba na hilo, kuna changamoto ya wazazi wengi kuwaachia walimu jukumu la kuwalea watoto wao.

Walimu nao wakati mwingine shauri ya idadi kubwa ya wanafunzi, hushindwa kupata nafasi ya kutosha kubeba jukumu hilo la malezi ipasavyo.

Mwanafunzi huyu anayesoma kwenye mazingira ya namna hiyo, hupita kwenye mabadiliko mengi ya kimwili yanayoweza kuathiri mtazamo na tabia yake kwa jumla. Bila kupata msaada mzuri, anaweza kupata shida kufanya vizuri darasani.

Jitihada za Serikali

Serikali imefanya jitihada kadhaa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada wa kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mfano, mwaka 2000, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ilianzisha mpango unaolenga kukabiliana na changamoto ya Ukimwi.

Waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2000 ulikuwa na madhumuni ya “kuwawezesha mwanafunzi wa shule na mfanyakazi wa wizara kufanya uamuzi wa busara, kuhusu tabia na mwenendo katika mahusiano ya ujinsi.”

Waraka huo uliolenga shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, ulikuwa na lengo kuu la “kuwaelimisha na kuwashauri wanafunzi na wafanyakazi, ili wajenge na wakuze tabia na mwenendo utakaozuia kuambukizwa na kuendea virusi vya Ukimwi na magonjwa ya zinaa kati yao na katika jamii.”

Kama inavyoonekana lengo hasa la wizara wakati huo lilikuwa kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi.

Wakuu wa shule na vyuo vya ualimu walielekezwa kuunda kamati ya malezi na elimu dhidi ya ugonjwa huo.

Pia, wizara iliziagiza shule na vyuo vya ualimu kutenga siku maalum kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi na jamii nzima ya shule kuhusu mambo yanayohusiana na maambukizi ya VVU.

Kazi kubwa ya kuwaelimisha wanafunzi ilifanywa na walimu na wakufunzi, ingawa wakati mwingine watalaamu wengine walikaribishwa kutoa mada.

Hii kwa hakika, ilikuwa hatua nzuri ya wizara katika kutambua ukweli kwamba maisha ya mwanafunzi nje ya darasa yanahusiana kwa karibu na maendeleo yake kitaaluma.

Mpango huo, hata hivyo, ulikuwa sehemu ya mpango wa mapambano ya kitaifa dhidi ya Ukimwi na haukulenga kukabiliana na changamoto nyingine zinazomkabili mwanafunzi.

Masuala kama mwanafunzi kujitambua, kutengeneza malengo yake ya ajira aipendayo, kukabiliana na mabadiliko yanayotokea mwilini mwake na hata kwenye jamii kwa ujumla hayakupewa uzito.

Matokeo yake nidhamu iliendelea kuwa changamoto kwenye shule zetu na vitendo vya wanafunzi kushiriki vitendo vya jinai na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, pombe na uasherati, viliendelea kushamiri.

Waraka wa elimu namba 11

Pengine kwa kutambua upungufu huo, Waraka wa elimu namba 11 wa mwaka 2002, ulianzisha huduma za malezi na ushauri nasaha katika taasisi za elimu.

Kupitia waraka huo uliosainiwa na Kaimu kamishna wa Elimu Mei 2, 2002, wakuu wa shule na vyuo vya ualimu walielekezwa kuanzisha kamati ya malezi na kuteua mwalimu mlezi na mshauri.

Kazi kubwa ya mwalimu mlezi zilizoainishwa kwenye waraka huo ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wote na kuzungumza na wanafunzi kuhusu ukuaji wao na mabadiliko wanayoyapata katika miili yao kabla na baada ya kupevuka.

Pia, kazi nyingine iliyoainishwa kwenye waraka huo ni, “kufanya mkutano na wanafunzi/wanachuo ili kujadiliana nao kuhusu matatizo wanayokabiliana nayo kielimu, kiafya na kijamii na kuwasaidia kupata mbinu za kukabiliana na matatizo hayo.”

Pamoja na nia njema ya mpango huo kutambua na kushughulikia matatizo mapana yanayomkabili mwanafunzi, changamoto ikawa kukosekana kwa wataalamu wa unasihi shuleni na vyuoni, ambao wangeweza kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi.

Sababu mojawapo ni vyuo vyetu kutokuwa na programu za shahada na stahahada zinazoandaa wataalamu waliobobea katika eneo la unasihi.

Ingawa unasihi na saikolojia ni sehemu ya mtalaa wa mafunzo ya jumla ya walimu kwa kila ngazi, bado ufanisi wake umekuwa na changamoto.

Katika vyuo vingi mathalani, somo hili hufundishwa na wakufunzi ambao wao wenyewe hawajawahi kufanya unasihi.

Katika mazingira kama haya, inakuwa vigumu kwa mwanafunzi wa ualimu kupata ujuzi madhubuti, utakaomsaidia kufanya kazi vizuri na wanafunzi wake.

Pengine kwa kuelewa kikwazo hicho, ilipofika mwaka 2007, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na mradi wa kuzuia na kuelimisha wanafunzi kuhusu masuala yanayohusiana na VVU/Ukimwi (PASHA), iliandaa mwongozo wa kuendeshea mafunzo ya unasihi kwa walimu shuleni.

Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, ulilenga kupanua uelewa wa walimu kuhusu mbinu za kufanya unasihi, afya ya uzazi na VVU/Ukimwi, tabia hatarishi na elimu ya maisha. Itaendelea wiki ijayo     

Tuesday, November 14, 2017

Watoto yatima wanavyofaidi fursa za elimu

Watoto wengi yatima wamekuwa wakinufaika na

Watoto wengi yatima wamekuwa wakinufaika na fursa za elimu katika shule mbalimbali nchini. Picha ya Maktaba 

By Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Katika kipindi ambacho baadhi ya watoto wenye wazazi wote wakideka na kupata mahitaji yote ya kifamilia na fursa za elimu, kuna watoto yatima zaidi ya 700,000 wanaosoma shule za msingi nchini wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma za msingi.

Uchambuzi wa takwimu za msingi za elimu Tanzania mwaka 2016 (Best 2016) uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa Tanzania ina watoto yatima 731,536 ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili ikiwa ni sawa na watoto takriban tisa kwa kila 100 wa darasa la kwanza hadi la saba.

Mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto yatima nchini ni Iringa yenye watoto 14 kwa kila 100 (asilimia 14.4) ikifuatiwa na Njombe watoto 13 (asilimia 12.7), Mbeya watoto 11 na Pwani watoto 10 kwa 100 ambayo ni sawa na asilimia 10.4.

Hata hivyo, ipo baadhi ya mikoa yenye kiwango kidogo cha wanafunzi yatima ikiwa ni chini ya wastani wa kitaifa wa watoto tisa kwa kila 100 (asilimia 8.5). Mikoa hiyo ni pamoja na Manyara, Kigoma, Singida, Mtwara na Lindi.

Katika kundi hilo la wanafunzi yatima, takriban robo au asilimia 23 wamepoteza wazazi wote wawili, hivyo kutegemea zaidi msaada wa walezi au wasamaria wema.

Mbali na yatima wa darasa la kwanza hadi la saba, kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa mapema mwaka huu kuna wanafunzi wa elimu ya awali 125,141 ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili, huku zaidi ya theluthi mbili wakiwa ni wale wenye mzazi mmoja.

Mwanza inaongoza kwa kuwa na yatima wengi katika elimu ya awali kwa kuwa na watoto 10,848 ikilinganishwa na Katavi yenye wanafunzi yatima 1,168.

Wadau wa malezi na haki za watoto, wanaeleza kuwa yatima ni miongoni mwa makundi ya watoto walio hatarini kutengwa katika jamii na kukosa fursa muhimu katika maisha zikiwemo za kielimu, kijamii na kiafya.

Asasi ya kiraia ya Save the Children inaeleza kuwa pamoja na kwamba hawajafanya utafiti kujua chanzo halisi kilichosababisha baadhi ya mikoa kuwa na yatima wengi, tafiti nyingine zilizowahi kufanywa zinaonyesha vyanzo vikuu ni umaskini, magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu na malaria, vifo vya kinamama wakati wa kujifungua na mifarakano katika ndoa.

Japo huenda kuna sababu lukuki zinazobabisha baadhi ya mikoa kuwa na yatima wengi, Mwananchi limebaini kuwa mikoa mitatu inayoongoza kuwa na yatima wengi katika shule za msingi ya Iringa,

Njombe na Mbeya pia inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa viashiria vya Ukimwi na Malaria (THMIS) wa mwaka 2011/12.

Njombe inaongoza kwa kuwa na watu wengi wenye virusi vya ukimwi kwa kuwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa asilimia tisa. Ikumbukwe kuwa wakati huo, wastani wa kitaifa wa watu wenye VVU ulikuwa ni asilimia 5.1.

Changamoto za wanafunzi yatima

Tofauti na watoto wenye wazazi wote, yatima hukabiliwa na changamoto lukuki kutokana na baadhi kukosa walezi imara na wenye mapenzi mema, jambo linalofanya wakose haki zao na fursa nyingi za kujiendeleza.

“Tafiti zinaonyesha kuwa yatima huwa na changamoto za kifedha na vikwazo vingine vya kupata elimu, hivyo huwa katika hatihati ya kukosa elimu bora ambayo ingewapa fursa ya kujikita kwenye taaluma zinazohitaji ujuzi wa juu na kupata ajira zinazolipa zaidi,” anasema mtafiti wa Save the Children, Anitha Martine.

Mbali na elimu, anasema yatima wapo hatarini kupata msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia kutokana na kukosa malezi kikamilifu, hasa wale wasiokuwa na walezi wa uhakika na kufanya watoto hao washindwe kufurahia utoto wao na kuishi kwa afya.

Martine ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya watoto, anasema yatima pia hukumbana na changamoto ya ulinzi katika familia na jamii, jambo linalowafanya wawe waathirika wakubwa wa mimba na ndoa za utotoni ambazo huwakosesha pia fursa za kimasomo.

Hata hivyo, watoto hawa wanaweza kulelewa katika mazingira mazuri ambayo yatawafanya wapate fursa nyingi kama wenye wazazi wote wawili.

Mkurugenzi wa huduma za watoto wa shirika lisilo la kiserikali la C-Sema, Emmanuel Michael anasema kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu wa haki na ustawi kwa watoto yatima na namna ya kuwalea kama watoto wengine.

“Hii itasaidia watoto hawa waweze kukua na kutimiza ndoto zao na kujenga jamii yenye usawa,” anasema.

Hata hivyo, anasema jamii pekee haitafanikiwa kama hakutakuwa na utekelezwaji wa sheria, sera na miongozo mingineyo inayohusu maslahi na ustawi wa watoto kama vile sheria ya mtoto.

“Ni lazima kurekebisha sheria hasa zile ambazo zinamkandamiza mtoto kama vile sheria ya ndoa, ambayo kwa namna moja inaweza kuchangia kwa watoto yatima hasa wale wa jinsia ya kike kujikuta wakikumbwa na janga la ndoa na mimba za utotoni,” anasema.

Ili kuwasaidia watoto wakiwamo yatima iwapo wamekumbwa na masaibu ya kuvunjiwa haki wakiwa shule au maeneo mengine, Michael anawaomba wananchi kupiga simu namba 116 ambayo ni ya bure.

Yatima na elimu

Serikali katika ngazi mbalimbali imesema inachukua hatua ya kuwatambua na kuwalinda yatima, ikiwamo njia mahususi ya kuwatambua iliyosaidia hadi kupatikana kwa takwimu za wanafunzi yatima shuleni.

Katika mkoa wa Mbeya ambao ni wa tatu kwa kuwa na yatima wengi katika shule ya msingi, kuna mpango wa kuanzisha mfuko wa elimu wa mkoa unaolenga kuwawezesha wanafunzi wote wanaosoma katika mazingira magumu hususan yatima.

Mkoa huo ulikuwa na yatima 41,956 mwaka jana kati ya wanafunzi 181,845 ambao ni sawa na asilimia 12.7 ikiwa ni mara moja na nusu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 8.5 ya yatima waliopo katika shule za msingi za umma na zile zisizo za Serikali.

Ofisa elimu wa Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza, anasema yatima ni wengi katika mkoa huo kiwango ambacho huenda kikazidi hata takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Rais-Tamisemi mapema mwaka huu, jambo lililofanya watafute njia ya haraka kuwasaidia.

Hadi sasa, Ndigeza anasema kuna utaratibu wa kuwasaidia watoto yatima kupitia halmashauri ambazo huwatambua waliopo na kuwawezesha, ili waweze kuendelea kimasomo na kupata fursa nyingine muhimu za kimaisha.

Hata hivyo, mamlaka za Serikali za Mitaa pekee haziwezi kutatua changamoto zinazowakabili, ili kuwafanya yatima wapate fursa sawa na wale wenye wazazi wote wawili.

Ili kuwalinda na kuwawezesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Serikali mwaka huu imeanza kutekeleza mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto utakaotekelezwa kwa miaka mitano.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Erasto Ching’oro anasema malezi ya watoto yatima ni mtambuka kwa kuwa yanahusisha taasisi na watu mbalimbali wakiwamo wanajamii, jambo ambalo linasisitizwa na mpango huo ulioanza Julai.

Ching’oro anasema halmashauri hufanya utambuzi wa yatima wote waliopo shule na wasiokuwepo, familia wanazotokea na mahitaji yao ili kuona namna inavyoweza kuwasaidia ikiwamo katika masuala ya kielimu na pia kuwaunganisha na wadau wengine kama asasi za kiraia wapate misaada zaidi.

“Katika haki tano za msingi kwa watoto, elimu ni moja wapo, ndiyo maana huwa tunafanya utambuzi katika kila familia ili tujue mahitaji yao na kuangalia namna ya kuwasaidia, ‘’ anasema na kuongeza:

“Nakiri huenda kuna upungufu katika utoaji taarifa za upatikanaji wa huduma zinazotolewa kwa watoto hao kwa wananchi, lakini tunajitahidi kushirikiana na taasisi mbalimbali kuwapatia huduma muhimu wanazohitaji.’’

Tuesday, November 14, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tunahitaji kuwa wazalendo katika Kiswahili

 

By Erasto Duwe

Uzalendo ni dhana inayofafanuliwa katika ‘Kamusi ya Kiswahili Sanifu’ kuwa ni hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake.

Katika makala haya uzalendo unachukuliwa kuwa ni hali ya mtu kuwa na mapenzi katika lugha ya Kiswahili na kuwa tayari kuitumia katika mazingira mbalimbali, hata yale ambayo isingekuwa rahisi kufanya hivyo.

Kutokana na ukweli kwamba Wakoloni walifanikiwa kutusadikisha kuwa kila kitu chetu ni cha kishenzi, jambo hilo limeendelea kutuathiri hadi leo hii. Athari hiyo imeiathiri jamii yetu kwa miongo kadhaa hadi sasa.

Tunu zetu bora za utamaduni kama vile mila, desturi, lugha kwa kuzitaja kwa uchache, zimekuwa zikionekana kuwa za kishenzi.

Kinyume chake jambo lolote linalohusiana na Wakoloni hao hata kama halina maana yoyote kwetu, limekuwa likitukuzwa na kupewa thamani ya pekee. Hiyo ni kasoro kubwa ambayo lazima tuikiri wazi.

Kwa upande wa lugha adhimu ya Kiswahili, kumekuwa na mitazamo kadhaa miongoni mwa wanajamii. Lipo kundi la wasomi linaloshadidia Kiswahili kuenziwa na kutumiwa katika nyanja mbalimbali muhimu katika jamii yetu.

Aidha, kuna kundi jingine la wasomi ambalo linaweka ukinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya Kiswahili katika maeneo hayo mbalimbali muhimu. Mvutano wa makundi ya wasomi umekuwa na athari pia katika kuwaathiri Watanzania wengine ambao hawaingii katika makundi hayo tajwa ya wasomi.

Wapo wanaoamini kwamba Kiswahili hakina thamani kama zilivyo lugha za kigeni hususan Kiingereza.

Watu hao nao wamekuwa wakishadidia thamani na umuhimu wa lugha za kigeni kwa kukibeza Kiswahili hata kama lugha hizo za kigeni hawazijui huku wakitumia Kiswahili katika mawasiliano yao yote.

Aidha, lipo kundi linalokithamini Kiswahili kwa kuunga mkono kauli za wasomi wanaokishadidia Kiswahili. Hao wanatamani pia kuwa Kiswahili kipewe majukumu makubwa zaidi ikiwamo kutumika kufundishia katika nyanja zote za elimu.

Ikumbukwe kwamba ‘Kiswahili ni chetu, lugha za kigeni ni zao.’ Hata siku moja lugha hizo za kigeni hazitarejelewa kwamba asili yake ni Tanzania au Afrika Mashariki.

Dunia nzima inatambua kwamba, kitovu cha Kiswahili ni Tanzania ama Afrika Mashariki. Kwa hivyo, hilo ni jambo la kujivunia, na kwa sababu hiyo tunapaswa kukienzi Kiswahili, kukitoa kilipo na kukipeleka mbele zaidi ili kwamba ile dhana ‘sisi ni kitovu cha Kiswahili duniani’ idhihirike.

Hakuna lugha iliyo bora zaidi kushinda nyingine. Kila lugha ni bora kwa watumiaji wake kwa kuwa inawawezesha kukidhi mahitaji yao.

Wenye mtazamo kwamba Kiswahili kipo nyuma bado, wamekosa taarifa za sasa mintarafu nafasi na hadhi ya Kiswahili duniani.

Hata hivyo, kukiongelea vibaya kilicho chako badala ya kutafuta nafasi ya kukikwamua ni kukosa uzalendo na ni utumwa wa kimawazo.

Wakati baadhi yetu wakiwa na mawazo dufu dhidi ya Kiswahili, wageni kutoka mabara mbalimbali wanakisaka kwa udi na uvumba kutokana na umuhimu wake.

Viongozi wetu wa nchi wamekuwa mfano wa kuigwa katika hili. Rais wetu, John Magufuli ameonyesha uzalendo wa hali ya juu.

Tofauti na ilivyokuwa imezoeleka awali, sasa tunashuhudia Rais wetu akitumia Kiswahili mbele ya wageni wa kimataifa wasiokijua Kiswahili. Kufanya hivyo kuna mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha yenyewe. Kiswahili kinazidi kupanda hadhi na kinazidi kutangazwa kote duniani. Uzalendo huu ndio unaohitajika.

Kila mmoja akiwa na mapenzi ya namna hii, Kiswahili kitazidi kutukuka. Tuige mfano wa uzalendo katika Kiswahili kutoka kwa Rais wetu, shime!

Tuesday, November 14, 2017

Fundi ujenzi alivyokatisha ndoto za Secelela

Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanae

Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanae aliyezaa na mwanaume aliyekuwa na uhusiano nae wakati akisoma sekondari. Picha na Habel Chidawali 

By Habel Chidawali,Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

“Sijawahi kuwaza kitu kingine zaidi ya kazi mbili hadi leo, moja ni udereva wa magari makubwa na kazi ya pili ni kuwa muuguzi katika hospitali zenye wagonjwa wengi kutoka vijijini, lakini ndiyo basi tena,”

Ni simulizi ndefu ya msichana Secelela Juma (17) binti ambaye anashuhudia ndoto yake ikiyeyuka kwa sasa, licha ya kujitia moyo kuwa suala la udereva anaweza kupambana hadi alifikie.

Secelela ambaye kwa sasa anaitwa mama John, anaanza kutaja sababu za kupotea kwa ndoto yake ni fundi ujenzi ambaye alikutana naye Julai 2015 wakati akiwahi shuleni. Alikuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ihala ya mjini Mpwapwa.

Anasema umbali wa shule ulimfanya apatiwe msaada wa usafiri wa pikipiki ili kumwahisha na ilifanyika hivyo lakini wakiwa njiani, mtoa msaada alibadil mazungumzo na kuanza kumtaka kimapenzi, huku akiahidi kuendelea kumpa lifti ya kuwahi shule wakati wowote.

“Siku ya kwanza nilipata ukakasi kidogo kumjibu, siku iliyofuata niliamua kumkubalia na siku hiyo hiyo jioni tulianza uhusiano wetu,” anasema.

Msichana huyo ni miongoni mwa wasichana waliotoa ushuhuda kwenye mafunzo ya kujitambua ambayo yaliendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Utu wa mtoto (CBF) kwa wasichana walioolewa au kuzaa chini ya umri. Alionyesha ujasiri mkubwa wa kuwafundisha wenzake 25 mbinu za kujikinga na wanaume wakware.

Katika simulizi yake anasema hakuwahi kuwaza kujifunza kitu kinachoitwa mapenzi na hakutarajia kufanya katika umri wake, lakini alijikuta akitumbukia kwa sababu ya lifti.

Nini kilitokea

Secelela anasema, alipomaliza masomo ya msingi, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Ihala wakati yeye akiishi kwa wazazi wake mtaa wa Igovu mjini Mpwapwa ambako ni mbali na shule aliyopangiwa.

Anasema umbali huo ulikuwa ni changamoto ya kumfanya akutane na vishawishi vingi kutoka kwa wavulana wa mtaani na hata watu wazima. Kila alipokwenda shule au aliporudi nyumbani, hakukosa kukutana na mtu aliyemweleza habari za uhusiano ya kimapenzi.

Kwa maelezo yake, alijitahidi kuwa mvumilivu na mtu mwenye misimamo lakini mwishoni akajikuta ametumbukia kwenye shimo ambalo liliharibu maisha yake kwa jumla.

Anaeleza kukutana na mvulana ambaye alizoea kumuona mtaani hapo, ingawa kwa sasa ana muda mrefu hajamwona zaidi ya kuwasiliana kwenye mitandao. Alianza kama mtu mwema kabla ya kumgeukia na kuwa mpenzi wake kwa muda mrefu.

Aacha shule

Secelela alikwenda shuleni hadi novemba Mwaka 2015 alipofanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kisha wakafunga shule, huku wakingoja matokea ya kuingia kidato cha tatu.

Hata hivyo, hakuwahi kukanyaga kidato cha tatu kwani walipofungua shule, aliona aibu kwenda kuungana nao kwa kuwa alishakuwa na mimba kubwa.

“Yaani kabla hatujaitwa kwenda kupimwa shuleni, mimi nilikuwa wa kwanza kujiondoa mwenyewe ingawa matokeo nilisikia kuwa nilikuwa nimefaulu na kutakiwa niendelee na kidato cha tatu, ‘’ anasema na kuongeza:

“..nilivyoanza kuhudhuria kliniki nikawa nakutana na wenzangu wengi ambao tulikuwa darasa moja ama walikua na watoto au wana mimba .”

Maisha baada ya kuacha shule

Hali ilikuwa shubiri nyumbani baada ya wazazi wake kuanza kumsimanga kila wakati kuwa amewatia aibu akiwa ni mtoto wao wa mwisho kati ya watoto watano, jambo lililomfanya awaze hata kujidhuru kabla ya kutoroka nyumbani na kwenda kuishi kwa kwa ndugu.

Aliishi nje ya familia yao kwa miezi mitatu lakini mimba ilipofikia miezi 8 aliamua kurudi kwa wazazi wake na kuomba msamaha.

Mwisho wa ndoto yake

Secelela anasema giza nene katika maisha yake lilianzia hapo na kufifisha ndoto yake aliyoanza kuiwaza tangu shule ya msingi kwamba wakati mmoja aje kumiliki leseni ya kuendesha magari makubwa ndani na nje ya nchi.

Licha ya kujipa moyo kuhusu udereva kwamba anaweza kutumia elimu yake ya kidato cha pili na kujifunza, anasikitika kuwa pengine magari atakayoendesha ni ya ndani ya nchi na siyo nje ya nchi.

Kuhusu ndoto ya uuguzi, anasema: ‘’ Ndoto hiyo ni kama imekufa kifo cha aibu kwa kuwa siwezi tena kufikia hatua ya kuwa muuguzi katika zanahati zinazokusanya kinamama wa vijijini ambao nilitamani kuwahudumia. Sasa nawaza kumiliki mgahawa au duka la vyakula ambavyo vinahitaji mtaji.’’

Hatari kwa wasichana wadogo

Selelela anasema kuwa, wasichana kati ya miaka 15 hadi 17 ndiyo kundi linalodanganywa kwa sehemu kubwa na wanaume, kwani bado hawana uwezo mkubwa katika kujibu mashambulizi ya kuepuka vishawishi pale wanapodanganywa.

Sababu nyingine anatajwa ni kuwa wanaume hawaoni tabu kugharimia wasichana wadogo ambao kimsingi hawana mahitaji mengi. Ndiyo maana hata wavulana wadogo nao wamekuwa wakiwarubuni.

“Msichana anatamani chipsi, wakati mwingine kiwi ya viatu tu au nauli au nguo ambavyo wavulana wenye vipato vya chini pia wanaweza kumudu kuvipata,” anaeleza.

Tuesday, November 14, 2017

JICHO LA MWALIMU : Sifa ya mwanafunzi ni taaluma na nidhamuJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

Licha ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya shule na vyuo nchini,  kumekuwapo na changamoto kwa jamii kubaini ipi ni shule ama chuo kilicho bora.
Wengi wamekuwa wakifanya uchaguzi wa shule kwa ajili ya watoto wai kutokana na kutazama ufaulu katika matokeo ya mitihani ya taifa.
Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili, taaluma ni ujuzi au maarifa yanayopatikana kwa kusoma au kufundishwa darasani.
Wakati mwingine taaluma hutafsiriwa kwa kufananishwa na elimu.
Elimu ni jambo lolote analoambiwa mtu au jamii kwa lengo la kuelimishwa na kuelewa.
Mtu huweza kupata elimu kutoka sehemu mbalimbali ambazo zipo katika mfumo ulio rasmi au usio rasmi.
Nidhamu ni staha, heshima, taadhima au tabia njema aliyonayo mtu mbele ya watu katika jamii anayoishi.
Pia, nidhamu ni utaratibu wa kuendesha jambo kulingana na maelezo au maelekezo yaliyotolewa.
Kwa mwanafunzi au mwanachuo, taaluma na nidhamu haviwezi kutenganishika; ni kama chanda na pete.
Ili mwanafunzi aendelee kufanya vizuri kitaaluma na katika maisha yake ya baadaye, anapaswa kuwa na nidhamu.
Nidhamu humwezesha kushirikiana na watu wengine bila tatizo; humsaidia katika kazi  na kuwa raia mwema mwenye mchango kwa maendeleo endelevu ya taifa lake.
Sifa za mwanafunzi bora
Mwanafunzi bora anapaswa  kuwa na nidhamu; kuwa mdadisi na mbunifu; kuwa na ushirikiano na wenzake na kuwa na mazoea ya kuwahi shuleni.
Nidhamu siyo tu kwamba huhitajika  kwa mwanafunzi awapo shuleni tu,  la hasha. Nidhamu inapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtu.
Kimsingi, mtu hawezi kutenganisha mafanikio yoyote na nidhamu, kwani ni kiini cha utiifu katika kukamilisha mipango ambayo mtu amejiwekea.
Mwanafunzi anapokuwa shuleni au chuoni kuna mambo mengi anayopaswa kuyakamilisha kabla ya muhula, mwaka au miaka kuisha.
Watunga mitalaa huandaa idadi ya masomo au kozi kulingana na muda, hivyo wanafunzi hawana budi kutambua kuwa kila sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi au mwaka ni muhimu vikatumika kinidhamu ili kuweza kukamilisha malengo yao ya kitaaluma.
Wapo baadhi ya wanafunzi wanaozembea katika miaka ya mwanzo kabla ya kufikia mwaka ule wa kufanya mitihani wa mwisho au wa taifa.
Ni vizuri wakafahamu kwamba mafanikio yao ya kitaaluma hujengwa kwa jitihada ndogondogo za muda mrefu na sio kungojea mtihani ndio wachukue hatua za maandalizi.
Watu wengi waliofanikiwa na wanaoendelea kufanikiwa kama viongozi au wafanyabiashara mashuhuri, wote  huwa na nidhamu katika utendaji wao wa kazi.  Hawa aghalabu wana nidhamu ya matumizi mazuri ya fedha zao au nidhamu ya kufuata miiko na maadili ya taifa.
Watu wengi huwa na ndoto za kufanya mambo makubwa maishani, lakini, huishia kutekeleza kwa kiwango cha asilimia 50. Ni   nidhamu pekee ya kuamini kile wanachofanya kwa usahihi kwa wakati sahihi, ndio huwasukuma kuendelea kuzisogelea ndoto zao mpaka wanapozitimiza.
Kwa mfano, kama ambavyo inafahamika kuna wakati wanafunzi hupaswa kuelekezwa na kufuatiliwa na walimu wao ili waweze kutimiza lengo la kuwapo shuleni kupata elimu bora.
Shule ni kama mfereji wa maji uliounganishwa kutoka mtoni au katika bomba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mkulima alichimba mfereji wa maji kwa kuwa ana lengo ambalo ndilo humuongoza kutafuta maji hata kama ni kutoka umbali kiasi gani. Lengo lake ni kupata mazao bora.
Vivyo hivyo, jengo la shule huwaelekeza wanafunzi katika lengo la maisha bora. Wanafunzi wapate maarifa na kukua kimwili, kiakili, kijamii na kiroho. Hapo ndipo nidhamu yao pia huingia.
Kwa asili, maji husafiri kutokana na kani ya uvutani ya dunia (gravitation force) itakapoyataka yaende kama hakuna mfereji wa kuyaelekeza.
Vivyo hivyo, akili ya mwanafunzi hupenda  kujaribu kila jambo kwenda kila upande; hapo ndipo nidhamu huhitajika ili kumpa njia ipasayo kufuata kama ilivyo kwa mfereji wa maji.
Kuchimba mfereji na kulinda nidhamu shuleni si jambo rahisi. Kwani maji katika mfereji na wanafunzi shuleni au vyuoni, hujaribu kukwepa kuongozwa.
Maji yatajaribu kuvuja sehemu yenye ufa katika mfereji au kupanda kuta za mfereji huo kama hazina urefu wa kuyazuia. Wanafunzi nao watajaribu kukwepa maelekezo na sheria kama nidhamu haitawekewa mkazo ipasavyo.
Mwanafunzi ni kama maji na nidhamu shuleni ni kama kuta za mfereji wa maji. Maji yataenda vizuri na kwa matumizi yaliyokusudiwa, endapo yatafuata mfereji ulio imara na madhubuti.
Vivyo hivyo mwanafunzi atafanya vizuri katika masomo na maisha yake kama nidhamu itatiliwa mkazo shuleni.
Wanafunzi wana wajibu mkubwa katika kujenga maadili mema wakiwa shuleni. Na maadili haya yawe mazuri na yaliyojikita katika taratibu zinazokubalika na jamii nzima kwa faida ya taifa na vizazi vijavyo.
Mwanafunzi bora mwenye maadili mema hana budi kujenga utamaduni wa kujitegemea hasa katika masomo. Hili  husaidia kujenga moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Mafanikio ya shule kuwa na nidhamu huchagizwa pia kutokana na uhusiano mzuri baina ya wazazi na walimu.
Wapo baadhi ya wazazi wanaolaumu na kuvunja moyo juhudi za walimu za kupambana na utovu wa nidhamu shuleni.
Wazazi hawa ama huwajia  juu walimu kukataa kuitikia  wito wanapoombwa kufika shuleni na kuelezwa tabia za watoto wao.  Wapo wanaofikia hatua ya kuwafanyia vitendo vya ubabe walimu, ikiwamo kuwadhuru.
Ni vema jamii kwa pamoja ikaendelea kuweka mkazo  kwamba taaluma inapaswa kuendana sambamba na nidhamu.
Hii itasaidia  kuwa na taifa lenye watu wachapa kazi, wabunifu, wenye mtazamo chanya na wenye nidhamu ya kulinda rasilimali za taifa kwa faida ya vizazi vijavyo.

Tuesday, November 14, 2017

ELIMU NA MALEZI : Elimu bora ilenge kuwawezesha wanafunzi kujitambuaChristian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Bila shaka umewahi kukutana na mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu lakini anafanya mambo yasiyofanana na elimu aliyonayo.

Wakati mwingine kitu kilekile kingefanywa na mtu unayejua hajaenda shule hakishangazi.

Lakini kwa kuwa aliyekifanya ni ‘msomi’ basi swali linakuwa, “Hivi huyu naye amesoma? Kama kusoma kwenyewe ndio huku, kuna haja gani ya kusoma?”

Jamii kwa kawaida ina matarajio makubwa kwa mtu aliyekwenda shule. Kiwango cha elimu anachokuwa nacho, mtu kinaijengea jamii matarajio fulani kwake.

Elimu inachukuliwa kama chombo chenye uwezo wa kubadili maisha ya mtu katika ujumla wake.

Tabia ya mtu aliyesoma inatarajiwa kuwa bora zaidi ya mtu asiyesoma. Hapa tunazungumzia mambo madogo, lakini yenye umuhimu kama vile heshima kwa watu.

Mengine ni uwezo wa kuvumilia mawazo tofauti na namna anavyoweza kuwasilisha mawazo yake.

Jamii inayachukulia mambo haya kama kiashiria cha kupima ‘usomi’ wa mtu.

Ingawa ni kweli ubora wa elimu ya mtu unaweza kupimwa kwa upeo wake wa kuona na kutatua matatizo yanayoikabili jamii, mara nyingi jamii haishii hapo. Jamii huyapa uzito mkubwa mambo ya kawaida yanayogusa utu wa watu.

Watu mathalani, wanataka kuona namna gani elimu aliyonayo mtu imemjengea tunu muhimu za maisha kama uadilifu, uaminifu, kusema kweli na unyenyekevu.

Tunu hizi ndizo zinazochukuliwa kwa uzito mkubwa wakati mwingine kuliko utaalamu alionao mtu.

Inapotokea mtu amesoma na bado akawa mwizi, tapeli, mlaghai, mwenye majigambo, mlevi, mzinzi, kwa kawaida watu huanza kuwa na wasiwasi na elimu yake.

Mara zote mtu anapoonyesha tabia hizi, watu watajiuliza, “Elimu ina faida gani kama mtu anafanya mambo ya kijinga kama haya?”

Katika muktadha huu, mabadiliko ya maisha huchukuliwa kama kipimo muhimu cha ubora wa elimu aliyoipata mtu.

Pia, jamii inaamini mtu aliyesoma lazima aweze kumudu maisha yake. Usomi wake ni lazima uende sambamba na kuboresha mtindo wake wa maisha.

Huwezi kwa mfano, kusema umeelimika na bado ukabaki kuwa masikini.

Katika macho ya jamii, umasikini ni kiashiria cha mtu aliyeshindwa kuelimika.

Elimu inatarajiwa ikusaidie kutumia maarifa yako kujipatia au kujiongezea kipato.

Inapotokea mtu anakuwa na elimu kubwa lakini hana uwezo wa kubadili changamoto zilizopo kwenye jamii kuwa fursa, watu wanakuwa na wasiwasi naye.

Wakati mwingine, hali hiyo huifanya jamii iwabeze wasomi kwamba wamepoteza muda mwingi kujifunza mambo ambayo yameshindwa kuwasaidia wao wenyewe kuboresha maisha yao wenyewe.

Kwa mujibu wa jamii, kushindwa kumudu maisha yako ni kiashiria cha elimu isiyokidhi haja anayoweza kuwa nayo mtu.

Inawezekana mitazamo hii inawakilisha mtazamo hasi wa jamii dhidi ya elimu.

Tunafahamu kwa mfano, lipo wimbi la kujaribu kuifanya fedha iwe ndio kipimo cha heshima ya mtu.

Lakini ni kweli pia kwamba wasomi wenyewe kwa namna wanavyoonekana kupitia mchango walionao kwa jamii, ndio waliochangia kukuza mtazamo hasi uliopo kwa jamii dhidi ya elimu.

Lakini kwa kuwa matokeo ya elimu ni sharti yaiguse jamii ambayo ndiyo mnufaika wake mkuu, ni dhahiri jamii isipoguswa na matokeo hayo, maana yake ni kwamba wasomi wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwa jamii.

Zipo sababu nyingi zinazochangia kuifanya elimu ishindwe kuwa na manufaa kwa watu na jamii kwa jumla. Mojawapo ya sababu hizo ni msisitizo wake kwenye eneo moja tu la taaluma.

Tangu mwanafunzi anapoanza darasa la kwanza mpaka chuo kikuu anatarajiwa ‘kuelimika’ kwa kipimo cha kufaulu mitihani.

Mzazi anategemea mtoto arudi nyumbani na cheti chenye alama za juu. Wakuu wa elimu wanapozungumzia kupandisha kiwango cha elimu, wanafikiria ufaulu wa mitihani.

Mtazamo huo wa kutukuza taaluma dhidi ya maeneo mengine ya kimaisha unashushwa kwa mwalimu ambaye naye kwa nafasi yake, anakuwa hana namna nyingi zaidi ya kufanya kazi ya ziada kufikia matarajio hayo kwa kuhakikisha mwanafunzi anafaulu kwa kiwango cha juu.

Mwalimu anakuwa hana muda wa kusikiliza shida za mwanafunzi, kumsaidia mwanafunzi kujenga tabia njema, kwa sababu jitihada zake zote zinalenga kukuza eneo moja tu la maarifa.

Hata hivyo, hili si kosa la mwalimu pekee. Jamii yetu kwa ujumla wake, inaamini elimu ni uwezo wa kiakili unaomfanya mwenye akili aonekane kuwa bora kuliko mwenzake ‘asiye na akili’ za darasani.

Matokeo ya mtazamo huu finyu wa elimu, ni kudumaza maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya binadamu. Kwa mfano, siha zinazokuza utu na utimamu wa binadamu kama vile nidhamu, maadili, bidii ya kazi, uaminifu, afya ya akili na mwili, stadi za maisha na ukuaji wa kiroho hazipewi nafasi inayostahili.

Hali iko hivyo kwa sababu mitalaa yetu imebaki kuwa na kazi moja kubwa. Kupanua ufahamu wa mtu na kukuza uwezo wake katika kudadisi mambo wakati mwingine kuliko kujielewa na kuwa binadamu timamu.

Tunatumia muda mwingi kuyaelewa mambo yanayotuzunguka lakini tunasahau kumfanya ‘msomi’ huyu aingie ndani yake na kujitafakari yeye ni nani na nafasi yake ni ipi katika jamii.

Matokeo yake wanafunzi hukazana kupata alama A darasani lakini wanadumaa kwenye maeneo mengine muhimu yatakayowasaidia kufanikiwa kwenye maisha.

Ni vyema tukatambua kwamba ufaulu mzuri usiokwenda sambamba na kujengwa kitabia hauwezi kuwa na manufaa ya maana.

Tunahitaji kuweka msisitizo katika kukuza maeneo yote muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi.

Tujenge mfumo thabiti ulio rasmi utakaosaidia kuwalea vijana kimaadili na kiroho ili maarifa wanayoyapata yawasaidie kuwa binadamu wenye tija kwa jamii.

Sera zetu za elimu hali kadhalika, zisiishie kuelimisha akili za vijana wetu na kuwaacha hawajitambui wao ni nani na nafasi yao katika jamii.

Vinginevyo, elimu itabaki na kazi ya kumwandaa mtu atakayesubiri kuajiriwa ili apate fursa ya kutumia maarifa yake kuiba na kujiletea manufaa yake binafsi.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Tuesday, October 31, 2017

Maajabu ya biashara ya maandazi, vitumbua darasani

 

By Beatrice Moses Mwananchi bkabojoka@mwananchi.co.tz

Kwa Adelina Stephano, mkazi wa Bukoba vijijini mkoani Kagera, upishi wa maandazi na vitumbua na wakati mwingine kuchoma mahindi, ndizo biashara zinazomwingizia kipato cha kila siku.

Japo biashara hizo ndizo anazotegemea kimaisha, lakini hafurahishwi nazo, kwani anaamini kama angepata fursa ya kusoma hadi chuo kikuu, pengine leo hii asingekuwa muuza maandazi na vitumbua.

“ Elimu yangu ni darasa la saba siyo kwamba sikupenda kuendelea na masomo lakini wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunilipia ada, hivyo nimejikuta naishia kumudu shughuli hizi ndogo ndogo,” anasema.

Uzoefu wa maisha aliopitia Adelina ambaye pia ni maarufu kwa jina la Kokushubila, umempa hamasa ya kuwekeza katika elimu ya watoto wake watatu.

Unaweza kushangaa biashara anazofanya, lakini ari na hamasa ya kuwekeza kwenye elimu, vimemfanya awe tayari kulipa ada ya Sh1,612,000 kwa mwaka ili mwanawe Derick Mbezi asome katika shule anayosema inafanya vizuri kitaaluma.

Alifikia uamuzi huo baada ya kutambua kuwa elimu ni mtaji, hivyo amekuwa akihangaika kusaka ada kupitia shughuli zake za biashara ndogondogo.

Matokeo yampa furaha

Kama Wahenga wanavyosema; “penye nia pana njia” ndivyo ilivyotokea kwa Adelina, kwani nia yake imeanza kufanikiwa. Sasa ana furaha baada ya mwanawe huyo anayesoma katika Shule ya Msingi Rweikiza kupata wastani wa alama A.

Shule hii ni miongoni mwa shule 10 bora kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

“ Mwanangu alikuwa anasoma Shule ya Msingi Makonge ya Serikali, iliyopo kata ya Kanyangereko wilayani Bukoba. Wakati huo shule hizo waliziita yeboyebo, hazikuwa na matokeo mazuri kwenye mitihani ya taifa hivyo niliamua kumhamishia shule binafsi ya Rweikiza,” anaeleza.

Anasema kuwa uamuzi wa kumhamisha ulisababishwa na mambo kadhaa, ikiwamo ufaulu mzuri katika shule binafsi.

Anasema pia alibaini kuwa mazingira ya shule hiyo aliyokuwa akisoma mwanaye awali, ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, ambao ulisababisha watoto kutojifunza vyema hivyo kushindwa kumudu ushindani wa kimasomo na wenzao kutoka shule binafsi.

“Kufeli kwa wanafunzi wengi wanaosoma kwenye shule za serikali, hakumaanishi kwamba wao ni bongo lala, bali wamekosa fursa za kujifunza vyema ikilinganishwa na wenzao,” anasema mama huyo.

Kwake anaona ni vigumu kwa shule za Serikali kutatuliwa changamoto zinazozikabili, kwa sababu viongozi ambao wangepaswa kuzisimamia wengi wanasomesha watoto wao kwenye shule binafsi, hivyo hakuona matumaini kama shule hizo zitaboresha.

Jinsi alivyomudu kulipa ada

Anasimulia kuwa mwanzoni, alikusanya kiasi cha Sh500,000 kama mtaji wa kufanya biashara kubwa. Hata hivyo, akabadili uamuzi na kuamua kuzitumia fedha hizo kulipa ada ya mwanawe.

“Bahati nzuri utaratibu wa ulipaji wa ada uliopo katika shule hii ni mzuri, kwa sababu wanaruhusu kulipa kwa awamu nne; unaruhusiwa kulipa Sh403,000. Lakini kama wangetaka za mkupuo naamini isingewekana maana kulipa Sh 1,612,000 sio jambo jepesi kwangu,” anaeleza.

Huo ukawa mwanzo wa kumsomesha mtoto wake katika shule aliyoiamini kuwa ni bora kwa taaluma. Anasema kwa kupitia biashara ndogondogo anazofanya na mikopo kutoka vikundi vya vikoba, akajiwekea utaraibu wa kutunza fedha kwa ajili ya ada kila muhula unapofika.

Anavyojiandaa kumsomesha elimu ya sekondari

Pamoja na kuwa na furaha ya ufaulu mkubwa wa mwanawe, Adelina anaomba mwanawe achaguliwe kujiunga na shule bora ya Serikali, shule anayosema itamwepushia na mzigo wa kulipa ada kubwa kama ilivyokuwa awali.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, inatamka kuwa Serikali itahakikisha elimu ya awali hadi kidato cha nne inakuwa ya lazima na ya bure katika shule za umma. Kwa Adelina, sera hii inampa ahueni kuwa angalau mzigo wa ada kubwa sasa hautomwelemea.

“Kwa kweli asipochaguliwa huko alipoomba nitaumia, kwa sababu sasa nimeyumba kibiashara. Niliugua uvimbe gharama za matibabu zikala sehemu ya mtaji wangu, nitashindwa kumudu kumlipia ada,”anaeleza.

Anasema hali ilipokuwa ngumu alilazimika kumtoa mwanaye bweni na kuingia kutwa shule akitembea umbali mrefu, hivyo anashukuru mwanaye alimuelewa na amefanya vyema kama wenzie.

Adelina Stephano akiwa nan mwanawe Derick Mbezi

Adelina Stephano akiwa nan mwanawe Derick Mbezi aliyepata wastani wa A katika mtihani wa darasa saba. Na Mpigapicha Wetu

Mwanawe azungumza

Derick anasema ndoto yake ni kuwa rubani na ameomba kuchaguliwa katika shule za sekondari za wavulana Ilboru, Mzumbe na Mpwapwa, kuendeleza safari ya ndoto yake hiyo.

“Nashukuru nimefaulu sikumbuki kukwazwa na chochote nilipokuwa shuleni,’’ anasema mwanafunzi huyo.

Maendeleo ya taaluma Shule ya Msingi Rweikiza

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rweikiza, Baraka Mwambinga anaeleza kuwa wamefanikiwa kushika nafasi ya tisa kitaifa, kwa sababu ya mambo mengi ikiwamo walimu kujituma ipasavyo.

Anasema walimu walikuwa na ari kwa kuwa walijengewa mazingira mazuri ya kazi kama maslahi bora, hatua ambayo imeiwezesha shule hiyo kuwa ya kwanza katika Wilaya ya Bukoba Vijijini na ya nne kimkoa.

Kwa upande wa wanafunzi, anasema walijawa na utayari wa kujifunza, huku wakipata huduma ya mahitaji yote muhimu.

“ Hii ni shule ya bweni, hivyo tulikuwa huru kuwapanga wanafunzi kujisomea na kufanya mitihani kila wiki,’’ anasema.

Tuesday, October 31, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Athari ya Mwalimu Nyerere na Karume katika Kiswahili

 

By Erasto Duwe

Viongozi mbalimbali hususan wa kisiasa, wana mchango mkubwa katika kustawi au kuporomoka kwa utamaduni wa jamii.

Hii inatokana na misimamo, sera, sheria na miongozo mbalimbali wanayoiweka. Ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania tunaoushuhudia leo hii ni matokeo ya jitihada za viongozi waasisi wa Taifa hili.

Tukiwa katika mwezi wa kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, miongoni mwa mengi aliyoyafanya, suala la kuweka misingi imara ya Kiswahili kamwe halitasahaulika. Pamoja naye ni kiongozi mwasisi-mwenza Sheikh Abeid Amani Karume.

Ikumbukwe kwamba nchi nyingi za Kiafrika ambazo zilitawaliwa na wageni, ziliathirika vikubwa kiutamaduni hususan katika kipengele cha lugha.

Aidha, urithi ulioachwa na wakoloni pamoja na wageni hao umekuwa kama kilevi ambacho athari yake huonekana hata leo hii.

Mathalani, zipo baadhi ya nchi ambazo wageni hao wameacha lugha zao zikitumika na wenyeji walioachiwa lugha hizo, huzionea fahari na kuzikumbatia hata kubeza jitihada zifanywazo kuzienzi lugha za Kiafrika.

Historia ya Tanzania kwa upande wa lugha ni tofauti kidogo. Hii ni kwa sababu ya misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume, kama viongozi Tanzania.

Kiswahili ndiyo lugha iliyotumika kuyaunganisha makabila zaidi ya 120 katika harakati za kudai uhuru. Hata hivyo, Kiswahili kiliendelea kuenziwa na waasisi hao kwa kukipa nafasi muhimu kitaifa baada ya uhuru.

Nchini Uganda kwa mfano, Kiswahili kilijengewa dhana tofauti hivyo kutopewa kiapaumbele. Kiingereza kinakumbatiwa na kuchukuliwa kama lugha azizi mpaka leo hii.

Aidha, baadhi ya nchi za Kiafrika lugha zake za taifa ni zile zilizoachwa na wakoloni.

Tanzania hurejelewa kama kitovu cha Kiswahili duniani kwa sababu ya misingi iliyowekwa na Nyerere na Karume.

Viongozi hawa walifanya hivyo wakizingatia kwamba nchi haina budi kuwa na utamaduni wake yenyewe. Utamaduni unahusisha mambo mbalimbali, moja kati ya hayo ni lugha. Nyerere na Karume kwa kulitambua hilo, waliweka mkazo na uzito mkubwa katika utamaduni.

Yapo mambo mengi yaliyofanywa na waasisi hawa na hata kuifanya lugha ya Kiswahili leo hii iwe na sura iliyonayo.

Miongoni mwa hayo ni: Mwalimu Nyerere kuanzisha sera ya lugha ambayo haikuwa katika maandishi iliyotoa dira kwamba; ‘Kiswahili ni lugha ya Taifa na mojawapo ya lugha rasmi za Tanzania, na Kiingereza ni lugha kuu ya kigeni na lugha rasmi ya pili Tanzania.

Profesa Mugyabuso Mulokozi anatanabahisha kuwa, sera hii ilitekelezwa kwa vitendo na hatua kadhaa zilichukuliwa kutokana nayo.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kukitangaza Kiswahili kuwa lugha ya Taifa (1962); kuanzishwa kwa Wizara ya Utamaduni (1962); TUKI (1964); Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (1964); Bakita (1967); Kiswahili lugha ya kufundishia shule ya msingi (1968); Elimu ya Msingi kwa Wote (1972); Elimu ya Watu Wazima (1972-1985) na hatua nyingine nyingi.

Profesa Mulokozi anasema; “Matokeo ya sera hizi ni ukuaji wa lugha yenyewe ya Kiswahili kutokana na matumizi mapya na mapana zaidi. Kwa mfano, maneno mapya ya siasa na utawala kama vile kata, tarafa, ujamaa... yaliibuka.”

Aidha, anaongeza kuwa, maneno kama sayansi na teknolojia, elimu, uchumi na mengineyo yaliibuka na kupanuka kimatumizi.

Viongozi waige mfano wa Nyerere na Karume katika kukiendeleza Kiswahili kutokana na nafasi zao. Nasi raia tuzienzi jitihada za waasisi hawa kwa kukitendea haki Kiswahili.

Tuesday, October 31, 2017

Klabu za usalama shuleni kinga ajali za wanafunzi

Wanafunzi wakivuka barabara ya Kawawa jijini

Wanafunzi wakivuka barabara ya Kawawa jijini Dar es Salaam. Kuwapo kwa klabu za usalama kwa wanafunzi shuleni, kunaelezwa kama chachu ya kupunguza ajali zinazowakabili wanafunzi barabarani. Picha na Beatrice Moses 

By Beatrice Moses, Mwananchi bkabojoka@mwananchi.co.tz

Ajali iliyosabisha vifo vya wanafunzi 32 na walimu wao wawili wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha mwanzoni mwa Mei mwaka huu ilishtua na kuhuzunisha wengi.

Wanafunzi hao waliokuwa wanakwenda kufanya mtihani katika shule ya Tumaini Junior ya Karatu, walifariki dunia wakiwa wamebakiza miezi minne kumaliza darasa la saba.

Mengi yalisemwa kuhusu chanzo cha ajali hiyo, ikiwamo mwendo kasi wa dereva na hali mbaya ya hewa. Wengine walidai kuwa breki za gari zilishindwa kufanya kazi.

Takwimu za ajali kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, zinaonyesha kuwa mwaka 2015 jumla ya watoto 135 wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 19 walikufa kwa ajali.

Kati ya hao wavulana walikuwa ni 88 na wasichana 47. Waliojeruhiwa walikuwa ni 351 ambapo wavulana walikuwa ni 131 na wasichana 120.

Mwaka 2016, taarifa inaonyesha kuanzia Januari hadi Septemba watoto 99 wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 19 walikufa kwa ajali wavulana wakiwa 61 na wasichana 38. Waliojeruhiwa ni 229 wasichana 69 na wavulana 160.

Inawezekana ni kweli ajali haizuiliki lakini chanzo cha ajali kinaweza kuzuilika iwapo umakini utaongezeka kwa watumiaji wote wa vyombo vya moto.

Ni kwa sababu hiyo, tangu mwaka 2014 Baraza la ushauri la watumiaji wa Mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na Majini (Sumatra CCC), limekuwa likisimamia klabu za usalama shuleni ili kutengeneza wajumbe wa kujitolea kutoa elimu hiyo kwa jamii.

Ofisa elimu kwa umma wa Sumatra CCC, Nicholous Kinyariri anasema klabu hizo zinashirikisha wanafunzi ambao wanasaidia kufikisha ujumbe kwa njia rahisi kwa wazazi wao, wanafunzi wenzao, ndugu jamaa na marafiki.

Anasema kuwa tayari klabu zimeanza kuonyesha mafanikio kwa kuwa wanafunzi wanachama wamekuwa, wakiongoza kwa kutoa taarifa zinazosaidia magari yanayooendeshwa kwa kuhatarisha maisha, kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

“ Pamoja na kwamba wengi wao hawamiliki simu, lakini wamekuwa wakitumia njia ya kuomba walezi waliopo kwenye shule zao au wazazi na wasafiri wengine kuhakikisha ujumbe unafika haraka mahali husika kwa hatua mara wanapoona viashiria hatarishi vya safari,” anasema Kinyariri.

Mpaka sasa anasema kuna wanachama 2,550 katika mikoa tisa, huku mpango uliopo ukiwa ni kuongeza mkoa mwingine hivi karibuni.

Anasema klabu hizo zinakuwa na wanafunzi 50 katika kila shule iliyochaguliwa kuwa kwenye mpango huo. Wanachukua idadi hiyo ili kuhakikisha wanafikisha elimu husika kwa kiwango cha uelewa uliokusudiwa.

“Kuna gharama katika kuanzisha klabu hizi ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo husika, kugharimia shughuli zinazofanywa ikiwamo kurekodi nyimbo za kuelimisha jamii zinazopigwa kwenye radio. Lakini sisi hatujali gharama hizo, tunachotaka ni kuona elimu hii inasaidia jamii,’’ anasema.

Anabainisha mwaka jana wanafunzi wanachama 700 walihitimu masomo yao, mwaka huu watahitimu 666. Ni wanafunzi anaosema watakuwa na muda mzuri wa kuelimisha jamii.

“ Tumekusudia pia wakati wa likizo kila mwanafunzi mwanachama atoe elimu na kipeperushi kwa watu 10 na atuletee namba za simu za aliozungumza nao. Hapo unaweza kuona tutakuwa tumefikia watu wengi,” anaeleza.

Matokeo chanya

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim akizungumzia kuhusu vilabu hivyo, anasema vinasaidia katika kutoa elimu ambayo inachangia katika kupunguza ajali ambazo zimesababisha wananchi wengi kupoteza maisha, huku wengine wakipata ulemavu na hivyo kuongeza idadi ya watu tegemezi.

Anasema kikosi chake kinaendelea kujiimarisha kwa kupambana na kuwadhibiti kwa mujibu wa sheria, madereva wazembe na wanaoendesha magari mabovu.

Mkaguzi wa magari na madereva, Inspekta Yohana Mjema,anasema klabu hizo ni suala jema kwa kuwa linasaidia wanafunzi kuwa makini wanapotembea kwa miguu au wakiwa ndani ya vyombo vya usafiri.

“ Nikiwa mmoja wa askari wa kikosi cha usalama barabarani, natambua kuna maeneo ambayo ni changamoto kwa watoto hasa katika kuvuka, maana mengine bado hayajawekwa alama,” anasema na kuongeza:.

“ Hali hiyo ni hatari kwa sababu kuna madereva wazembe wanaendesha bila tahadhari yoyote hata kwenye maeneo ya shule, hivyo kugonga wanafunzi. ‘’

Othman Juma ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shuke ya Sekondari ya Benjamini Mkapa ambaye ni miongoni mwa wanachama wa klabu ya usalama wa barabarani. Anaeleza kuwa vinawasaidia kujengea uelewa mzuri wa alama za barabarani na haki za msingi za vyombo vya moto.

“ Ajali zimezima ndoto za wanafunzi wenzetu wengi kwa kuwasababishia vifo na wengine ulemavu, Nani ajuae wangeendelea kuishi wangekuwa kina nani na wangesaidia kwa namna gani maendeleo ya Taifa letu,”anasema.

Juma anasema kuwa amewahi kushuhudia ajali iliyosababisha kifo cha mwanafunzi katika eneo la Mbagala Mission aliyekuwa anavuka kwenye kivuko chenye cha pundamilia. Dereva alipita kwa kasi bila tahadhari na kusababisha ajali.

Tuesday, October 31, 2017

JICHO LA MWALIMU : Haiba ya mwalimu inavyochochea ujifunzajiJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

Watu wengi wamekuwa wakichukulia haiba kuwa ni ule mwonekano wa kimavazi wa mtu.
Kwa mujibu wa kamusi mbalimbali za Kiswahili, haiba ni tabia nzuri, mwenendo wa kupendeza; haiba ni hali katika mtu inayofanya wengine wavutike naye ama mvuto wa heshima.
 Pia, haiba ni zile tabia zote za mtu ambazo huweza kumfananisha au kumtofautisha na mwingine.
Mtaalamu wa saikolojia, Christian Bwaya anaeleza kuwa haiba ni jumla ya tabia za mtu zinazotokana na kile anachofikiri, anachopenda, anavyojichukulia yeye mwenyewe, anavyowachukulia watu wengine na kadhalika.
Haya yote hujenga mwonekano wa mtu unaopimika (tabia) kama vile anavyoongea na watu, anavyodhibiti hasira zake, anavyovaa, anavyofanya maamuzi, anavyoweza kuwa mwaminifu, anavyoweza kutunza siri moyoni, anavyoweza kukabiliana na changamoto.
Kwa muktadha huo, haiba hujumuisha zaidi ya mwonekano wa nje; haiba ni mwonekano wa mtu kitabia, kimatendo, kimavazi na kimaongezi.  
Haiba huweza kubadilika kutokana na umri, mazingira na jinsi ambavyo mtu alilelewa na makuzi yake. Kuna mambo ambayo hufanya watu wakafanana haiba zao kama kuishi pamoja, mila na desturi, uhusiano wa familia na hata kusoma pamoja.
Pia, yapo mambo ambayo huweza kutengeneza haiba tofauti kama motisha anayopata mtu, mtazamo, uwezo wa akili wa kutafakari.
Haiba na ufundishaji
Mwalimu ana nafasi kubwa ya kuambukiza haiba yake kwa wanafunzi wake. Hivyo, haiba ya mwalimu huweza kuathiri tendo la ufundishaji na ujifunzaji darasani. Mwalimu anapokuwa na sifa zinazowavutia wanafunzi kama umahiri katika kufundisha somo lake, husababisha wanafunzi kupenda hilo somo na hivyo kulifanya vizuri katika mitihani.
Mwalimu mwenye utulivu wa mawazo na mwonekano mzuri, huzalisha wanafunzi wenye usawazo. Kinyume chake huambukiza na kuzalisha wanafunzi wasio na utulivu wa kifikra na mtazamo. Mojawapo ya kazi ya mwalimu ni kuhamasisha haiba zinazokubalika katika jamii kwa wanafunzi wake.
Tabia hujenga haiba ya mtu. Kwa mfano, mwalimu anayenyoa kiduku au anayevalia suruali kwa staili ya ‘mlegezo’ mbele ya wanafunzi wake huweza kuambukiza tabia hiyo kwa wanafunzi wake, ambao pia wakiunganisha na mbwembwe zao hali ya uvaaji shuleni na mitaani huwa tete zaidi. Pia, mwalimu anapotumia lugha ya staha huambukiza wanafunzi wake tabia inayofaa.
Kuna makundi mbalimbali katika jamii yanayopishana juu ya dhana ya umuhimu wa haiba katika taaluma ya ualimu.
Mathalani, wapo wanaodhani kwamba haiba haina umuhimu kama mwalimu anatekeleza tu jukumu lake la kuingia darasani na kufundisha na kuondoka. Tabia yake na mavazi yake hayana umuhimu.
Pia, lipo kundi la watu wengine ambao huona siyo vema kwa mwalimu kukosa haiba ya kiualimu. Hii ni kwa sababu haiba ya mwalimu husababisha mabadiliko chanya katika tabia ya mwanafunzi ambayo ndiyo lengo kuu la kujifunza.
Hivyo, ni vema walimu wakawa na tabia njema za kuigwa kuanzia wanavyoongea, wanavyotembea, wanavyowajibika na namna wanavyovaa yaani ule mwonekano wao wa nje.  Ikumbukwe kuwa  wapo wanafunzi ambao hujifunza hekima na utulivu wa akili kutokana na kile wanachokiona, kukigusa na kukisikia.
Umuhimu wa haiba ya mwalimu unabaki kuwa  muhimu bila kujali anafundisha ngazi ipi ya elimu. Kwa mfano, kuliwahi kutokea mhadhiri mmoja wa kike katika chuo kikuu kimoja ambapo mavazi yake hayakuwa ya staha kwa maadili ya Kitanzania na chuo kikuu hicho kiasi cha kusababisha hata wahadhiri wenzake kulalamika kuhusu mavazi yake.
 Cha ajabu alipoitwa na mkuu wa chuo na kuonywa kuhusu uvaaji wake huo, alimjibu kwamba yeye alikuwa ameingia mkataba na chuo wa kufundisha na si kumuamulia mavazi gani avae au asivae. Hili lilisababisha chuo  kuongeza kipengele cha haiba katika mkataba wao wa ajira.
Baadhi ya walimu wanaeleza kuwa baadhi ya changamoto wanazokutana nazo na kufanya kazi hiyo ionekane ngumu kwao na kutokuwa na mvuto, ni mazingira magumu na duni ya kufanyia kazi na idadi kubwa ya wanafunzi darasani.
Pia kuna tatizo la baadhi ya watu wasio na sifa ya ualimu kusomea fani hiyo, hawa wakisukumwa zaidi na sababu za kiajira.
Haiba pia huendana na  mtu kujitambua. Kujitambua ni hali halisi ya kuelewa kuwa mtu anaishi kama mtu binafsi na tofauti na mtu mwingine.
Kujitambua kunahitaji ukweli na uthubutu kuhusu mtu anavyofikiri, anavyohisi na kukubali ukweli anaouona kuhusu yeye.
Mwanzo wa kujitambua ni mtu kuelewa kuwa yeye ni mtu binafsi na tofauti, na kufahamu jinsi anavyohusiana na watu wengine pamoja na mazingira yake.
Kujitambua hutegemea jinsi mtu anavyojibu kwa uhakika maswali kama, “Mimi ni nani, niko wapi na  ninataka kwenda wapi maishani?”
Majibu sahihi na ya wazi kwa maswali hayo humwezesha mtu kupanga kwa urahisi mwelekeo wa maisha yake na kutambua uwezo alionao. Ni mtaji wa kumfikisha mtu katika mafanikio yake.
Mwanafunzi aliyejitambua hufahamu mwelekeo wa maisha yake na kuwa na dira ya kufikia malengo yake.  Hawi mtu dhaifu, na asiye na thamani. Hujitunza, hujiheshimu na kuheshimu wengine. Kutojitambua husababisha mtu kutokuwa na msimamo.
Hivyo, ni wajibu wa mzazi na mwalimu kumsaidia mwanafunzi ili ajitambue yeye ni nani, ameumbwa kwa makusudi gani na ana thamani gani?
Atambue kwamba yeye ni mtu wa pekee na wa thamani  machoni mwa Mungu; na hakuna binadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya, wala aliyelazimisha azaliwe na wazazi waliomzaa.
 Kitaaluma, mwalimu anawajibika kukuza haiba za wanafunzi wake kwa kuwajali na kukuza uhusiano mkubwa baina yake na wanafunzi, wazazi, familia, jamii na kada nyingine.

Tuesday, October 24, 2017

Anna : Hata sijui nilivyofaulu darasa la saba!

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

“Nikuulize swali mwenyewe. Hivi kwani mimi nilifauluje? Najiulizaga kila siku ila hata sipati jibu, sijui nilifauluje”.

Achana na makosa ya kisarufi ya maneno nilifauluje (nilifaulu vipi) na naulizaga (nauliza), kimsingi, swali lenyewe halikuwa rahisi kulijibu.

Ni swali aliloniuliza Anna Matonya (16), ambaye alipaswa kuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Magaga iliyopo wilayani Bahi katika Mkoa wa Dodoma.

Imepita takriban miezi miwili tangu aamue kuacha shule, anataka kufahamu namna alivyoweza kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana baada ya kuhitimu katika Shule ya Msingi Chifutuka.

Hatua yake ya kuamua kuacha masomo inatokana na madai yake kwamba akiwa shuleni hakuwa akielewa chochote darasani.

Siyo kwamba hajui kusoma na kuandika, La hasha! isipokuwa analalamika aliwezaje kufaulu darasa la saba kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuyamudu masomo.

Lakini akiwa sekondari mzigo ukazidi kumwelemea hasa pale lugha ya Kiingereza ilipokuwa ikitumika kufundishia. Anasema haelewi.

Anasema anaumizwa kushika mkia katika matokeo ya mitihani yake na kusababisha kupewa adhabu huku akichekwa na wanafunzi wenzake.

“Afadhali shule ya msingi nilijifunza kwa Kiswahili na sio sekondari, maana nikienda darasani siambulii kitu,”anasema na kuongeza:

“Kila siku nakuwa wa mwisho, walimu wakifundisha sielewi hata kidogo. Wakiongea Kiingereza ndio kabisa kama napotea, ndio maana nimeamua kukimbia shule”.

Anna anasisitiza kwamba haelewi ilikuwaje jina lake likawa miongoni mwa majina 31 ya wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka huu.

“Tupo 31 darasani, kila tukifanya mitihani nakuwa wa mwisho na kuchapwa viboko, kwa hiyo sitaki tena kusoma bora nimsaidie mama kazi za nyumbani,” anasema.

Anasema amejitahidi kusoma kwa bidii ili walau aendane na wenzake, lakini bado aliambulia nafasi ya mwisho jambo lililomkatisha tamaa ya kuendelea na masomo.

Anasimulia kwamba alijaribu kuwaambia wazazi wake kuhusu mwenendo wake kielimu, lakini hawakumwelewa na badala yake walimsihi aendelee na shule kwa kuwa ndio msingi pekee wa maisha yake.

“Hakuna aliyenisikiliza, baba na mama wote wanataka niendelee kusoma sekondari, sasa nitasomaje wakati sielewi chochote? Mimi sitaenda tena ila ningekuwa naelewa ningeendelea,”anasema na kuongeza:

“Nilienda porini, sikuogopa chochote kwa sababu nimechoka kuchekwa kwa kuwa wa mwisho darasani”.

Muundo wa mtihani wakosolewa

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifutuka, Daniel Mchomvu anasema muundo wa maswali ya kuchagua unaotumika sasa katika mtihani wa taifa wa darasa la saba, ndio unaosababisha wanafunzi wengi wasio na uwezo kufaulu akiwamo Anna.

“Unaweza kumkuta mtoto anabuni jibu na kufaulu, ndio maana wanaokwenda sekondari wengi hawana uwezo kama binti huyu amejikuta haendani na wenzake,”anasema.

Wadau mbalimbali wa elimu wanasema mabadiliko ya muundo wa mtihani huo, ndio unaosababisha kuwapo kwa wanafunzi wanaochaguliwa sekondari huku baadhi wakiwa hawajui stadi za msingi za kusoma na kuandika.

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati nchini (MAT/CHAHITA, Dk Said Sima anasema, Serikali ifanyie kazi maoni ya wadau ya kubadilisha mfumo huo kwa sababu unaua taaluma ikiwamo somo la Hisabati kwa sababu wengi wanaofaulu hawana uwezo.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Frank John anasema kilichosababisha mfumo huo kuanza kutumika ni matumizi ya mashine wakati wa kusahihisha. Ni mfumo uliowekwa makusudi kwa ajili ya kurahisisha kazi ya usahihishaji

Anasema: “Ni mfumo mbaya usiomuandaa mtoto. Hii ni hatari kwa Taifa.’’

Hata hivyo, Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Bahi, Hassan Mohamed anatetea muundo wa mitihani hiyo kwamba haina ubaya wowote. “Asiyejua kusoma na kuandika hawezi kujibu. Nchi zaidi ya 13 zinatumia utaratibu huu kwa hiyo sio muundo mbaya,”anasema.

Wazazi wasononeka

Akiwa miongoni mwa wanafunzi wasichana waliopangiwa vyumba mtaani katika kijiji cha Magaga, wazazi wake wanasema wamekuwa wakimpatia binti yao mahitaji yote.

“Mwanangu ananisikitisha sana, huyu ndiye niliyemtegemea walau, nilijua akisoma atawasaidia wadogo zake lakini ndio kama unavyosikia,” anasema baba yake Julius Matonya, mkazi wa kijiji cha Chikopelo.

Ilimlazimu Matonya kuwaomba walimu, viongozi wa serikali ya kijiji na majirani zake waongee na binti yake ili aendelee na masomo lakini haikuwezekana.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifutuka, Gasper Mhembano anakiri kushiriki katika kumashwishi Anna aendelee na masomo, lakini anasema ushauri wake pia uligonga mwamba kwani alikataa kata kata.

Baada ya kuona analazimishwa kuendelea na masomo, Anna aliamua kukimbilia porini ambako alikaa huko siku mbili kuepuka karaha ya kutakiwa aende shule.

Wapita njia ndio waliomuona Anna akiwa amejilaza porini. Walimfuata na kumbembeleza arudi nyumbani, akakubali.

Mama mzazi wa Anna, Peris Matonya anasema jamii inayowazunguka iliamini kwamba binti yake huyo ameacha masomo ili aolewe na kwamba alipotoroka wengi walidhani kwamba amekimbilia kwa wanaume.

Hata hivyo Anna mwenyewe anasema: “Sitaki kuolewa mimi ila pia sitaki shule maana sielewi darasani”.

Mama huyo anasema kazi pekee anayoweza kuifanya mwanawe baada ya kuacha masomo ni kupika pombe. “Mimi napika pombe kama unavyoniona, amerudi nyumbani hakuna namna atanisaidia hii kazi tu,”anasema.

Kwa upande wake, Anna anaona bora akasome shule ya fundi, lakini wazazi wake wanasema kwa sasa hawana fedha za kumsomesha kwa kuwa waliwekeza kwenye elimu yake ya sekondari hivyo asubiri hadi watakapopata fedha.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Daudi Gingi anasema sio Anna peke yake, baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaopelekwa baada ya kufaulu huwa hawana uwezo.

Matonya anakiri kuwa maendeleo ya binti yake shule ya msingi hayakuwa mazuri, lakini matokeo ya kufaulu mtihani wa darasa la saba yalimtia moyo kwamba huenda alibadilika.

“Nilijua atafeli kwa sababu alikuwa anapata 10 au 20…alipofaulu nilimshukuru Mungu nikawekeza akili zangu kwenye shule yake matokeo yake anatuambia kwamba haelewi,”anasema.

Necta yatoa neno

Ofisa mitihani mwandamizi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Yustine Balyuha anasema mfumo huo unapitiwa upya ili kuona namna ya kuubadilisha.

“Tunapitia upya kuona namna tunavyoweza kubadili mfumo huu, japo sio rahisi kwa mtoto asiyejua kufaulu kama inavyosemekana,”alisema katika mkutano wa wadau wa hesabu uliofanyika hivi karibuni.

Tuesday, October 24, 2017

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Fasihi ya Kiswahili na ajira kwa wasomi

 

By Erasto Duwe

Kazi ni kazi ilimradi mkono uende kinywani,” ni msemo wa Kiswahili unaosisitiza watu kufanya kazi yoyote halali ili kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji yao muhimu maishani. Kumekuwa na tabia ya kulalamika miongoni mwa wanajamii kuhusu kukosekana kwa ajira hususan kwa vijana waliohitimu masomo yao katika vyuo na vyuo vikuu.

Vijana wengi wa kileo wanapokuwa vyuoni huwa na ndoto nyingi. Huwaza kupata kazi nzuri mara baada ya kuhitimu masomo yao.

Aidha, wengi huwaza kumiliki nyumba za kisasa, magari mazuri na fedha nyingi.

Kwa jumla, huwaza kuwa na maisha ya kifahari kupitia elimu yao. Pamoja na fikra hizo zote, chanzo cha fedha wanachokitegemea ni kuajiriwa.

Ni wachache miongoni mwao wanaowaza kujiajiri. Baada ya kuhitimu, ajira zinapokosekana, vijana hubaki wakiilaumu Serikali.

Riwaya ya Utubora Mkulima iliyoandikwa na Shaaban Robert na kuchapishwa mwaka 1968 inatubungua bongo tuwe na mtazamo tofauti.

Katika riwaya hii msanii anamchora mhusika Utubora kuwa kijana mwenye elimu ya chuo kikuu, aliyekuwa karani kwa bwana Ahmed.

Kijana huyu anachorwa kuwa mchapakazi hodari aliyependwa sana na tajiri wake. Hata hivyo, Utubora hakuona kuwa ajira hiyo ni jambo la kuling’ang’ania. Tamaa yake kubwa ilikuwa kujiajiri mwenyewe na kujipatia kipato kitokanacho na kazi ya ubunifu wa akili yake.

Utubora alikata shauri la kwenda kuishi Mrima (kijijini) akakae shambani karibu na pahali alipokuwa akikaa mama yake. Akiwa huko alijishughulisha na kilimo. Alilima na kufuga mifugo mbalimbali. Moyo wake ulikuwa radhi na wenye furaha katika shughuli zake za kilimo alizokuwa akizifanya. Pamoja na hilo, alifanikiwa kujenga uhusiano mzuri na kila mmoja.

Tumetumia mfano wa kitabu hiki ili kuonyesha kuwa licha ya kuwako kwa ajira za kuajiriwa kuna upande wa pili wa ajira. Kama tulivyokwisha kueleza hapo awali, vijana wengi siku hizi huwaza kuajiriwa.

Ikiwa hawapati ajira hizo, huendelea kubaki mtaani wakisubiri ajira zitoke hata kwa miaka kadhaa. Kilimo kwa baadhi ya vijana huonekana kama ni shughuli ya watu wa tabaka fulani lisilowafaa wao.

Ipo haja ya vijana wasomi kujifunza kutoka kwa msomi mwenzao Utubora (mkulima). Kijana huyu hakuwa na tatizo la ajira lakini pamoja na sababu nyingine za kurudi Mrima, yeye alipenda zaidi kujiajiri mwenyewe. Maisha ya mjini hayakuwa na la pekee kwake.

Alifurahi kuitumia elimu yake ya darasani katika kile alichojipangia mwenyewe yaani kujishughulisha na kilimo. Laiti vijana wangalikuwa na ubunifu wa kutumia elimu yao kubuni ajira binafsi huenda leo hii maisha ya vijana wasomi yangalikuwa na sura tofauti.

Ile hali ya kusubiri ajira za ofisini kwa miaka kadhaa na kulalamika ingepungua. Vijana wanaohitimu ‘wajenge ofisi’ zao katika shughuli za kujitegemea wenyewe kama vile kilimo cha kisasa na viwanda vidogovidogo na hivyo kutoa nafasi za ajira kwa wengine.

Vijana wanaokimbilia mijini kutoka vijijini nao wanalo la kujifunza kutoka kwa Utubora. Mijini ambako vijana wengi hufikiri kuwa maisha ni rahisi, hali ni kinyume chake!

Kila kitu hutegemea fedha. Kutokuwa na fedha husababisha vijana wengi kujiingiza katika wizi na kufanya shughuli haramu hivyo kuhatarisha maisha yao. Msanii Shaaban Robert kwa kumtumia Utubora anataka kuieleza jamii kuwa shughuli za uzalishaji au ujenzi wa jamii kiuchumi, huweza kufanyika kwa namna yoyote halali na popote si lazima iwe mjini.

Tuesday, October 24, 2017

Ndoto ya Chiswanu kumiliki kiwanda cha viti vya walemavu

Erasto Chiswanu akionyesha kiti kinachotumia

Erasto Chiswanu akionyesha kiti kinachotumia umeme, alichokitengeneza kwa ajili ya matumizi ya walemavu wa miguu. Picha na Asna Kaniki 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Hivi sasa ubunifu ndiyo njia pekee inayoweza kumkomboa kijana aliyemaliza masomo yake.

Kwa vijana waliomaliza elimu ya juu hawahitaji tena kuajiriwa kwani, ubunifu kwao ni ajira pekee.

Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia ubunifu, unatajwa kama chachu ya watu hasa vijana katika kujipatia ajira.

Erasto Chiswanu aliyemaliza masomo ya uhandisi wa umeme katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, (DIT) anasema ubunifu kwake ni ajira tosha.

Kijana huyu ameunda kiti cha walemavu kinachotumia umeme. Anasema kiti hicho hakihitaji kusukumwa bali hujisukuma chenyewe kwa kutumia mfumo huo wa umeme.

Anasema kiti hicho alichokitengenezwa mwaka huu, kimemgharimu kiasi cha Sh 2.7 milioni kuanzia maandalizi hadi kukamilika kwake.

Anasema lengo la kubuni kiti hicho ni baada ya kuona kuwa watu wenye ulemevu wanapata shida kutafuta msaada wa kusukuma kiti wanapohitaji kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kiti hicho kinatumia betri na kina uwezo wa kutembea umbali wa kilometa tano hadi saba kwa saa.

“Kwa matumizi ya hapa mjini mgonjwa anaweza kukitumia kwa muda mrefu bila kuisha chaji, lakini hata kama kitatumika kwa umbali mrefu ikitokea kikazimika betri inaweza kuchajiwa tena na kuendelea kufanya kazi” anasema. Anasema ubunifu huo ambao kwake ulikuwa mgumu, umekuja baada ya kuona karibu kila kitu kimeshabuniwa, hivyo alitaka kuwa tofauti na wengine.

“Nilijiandaa mapema kuwa nitatengeneza kitu cha aina yake. Nilipokuwa mwaka wa tatu fikra zangu zililenga kubuni kiti hiki maalumu na cha kisasa kwa ajili ya walemavu” anasema na kuongeza’

“Kwanza nilifikiria kuhusu walemavu, wazee na wagonjwa wanavyoshindwa kutembea sehemu mbalimbali kwa kukosa kitu cha kumsaidia.”

Baada ya kupata wazo hilo, anasema alipeleka mapendekezo yake kwa mwalimu juu ya utengenezaji wa kiti hicho.

Kazi na jasho

Haikuwa kazi rahisi kwa Chiswanu kukamilisha kiti hicho, kwani anasema kila mara aliwaza kiti hicho kiwe katika mfumo upi.

“Mwaka jana Novemba, nilianza kuwaza, kwamba sawa kiti kitajiendesha kwa kutumia umeme, lakini wasiwasi wangu ni jinsi ya kukikamilisha, maana kiti hiki ndiyo mara ya kwanza kubuniwa hapa nchini vingine vinapatikana Afrika ya Kusini na India.

“Nilianza kufikiria kichwani ni namna gani hicho kiti kinaweza kutumika, nikawaza vifaa gani nitumie, kiwe cha aina gani, kiwe na muonekano gani” anasema.

Changamoto

Chiswanu anasema kama sio kujipa moyo na kuonyesha jitihada zake asingeweza kukamilisha mradi wake kwani hata walimu iliwachukua muda kuelewa alivyowapelekea pendekezo lake. Anasema changamoto kubwa aliyokumbana nayo ni mtaji.

“Vifaa vinauzwa kwa bei ghali na ndiyo maana vingine nimetumia vya kawaida kwa kuwa nilikosa mtaji,’’anasema.

Matatizo ya kiufundi nayo yalichangia kukwamisha umalizaji wa haraka wa kiti hicho, kwani anasema alilazimika kurudia mara nne hadi kukamilika.

Akatishwa tamaa

Chiswanu anasema changamoto nyingine aliyokumbana nayo ni baadhi ya wanafunzi wenzake kumkatisha tamaa.

“Wakati nahangaika, wanafunzi wenzangu walishauri niachane na hicho kiti kwani kitanigharimu kiasi kikubwa cha fedha. Mimi niliichukulia kama changamoto kwani nilitegemea wao waniunge mkono na kunitia moyo” anasema.

Kuhusu mafanikio, anasema: “Nimeweza kujulikana kupitia ubunifu wangu, hasa tunapokwenda katika maonyesho mbalimbali kila mtu amefurahia ubunifu wangu,”.

Matarajio

Chiswanu ana ndoto ya kuwa na kiwanda kikubwa, ili aweze kutengeneza viti vingi ambavyo atasambaza katika maeneo tofauti.

“Sio siri uhandisi upo kwenye damu na lengo langu ni kusaidia wasiojiweza, kwani wazee, wagonjwa na walemavu wanashindwa kutembea maeneo mbalimbali kwa kukosa mtu wa kusukuma viti vyao” anasema.

Kwake dhamira siyo kutengeneza viti hivyo, bali pia kutoa mafunzo kwa vijana wengine.

Wito kwa Serikali

Anatoa rai kwa Serikali kuwawezesha wanafunzi wabunifu, kwa kuwawezesha rasilimali fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiubunifu

“Mimi naamini endapo Serikali itatushika mkono kwa kutenga bajeti kwa ajili ya ubunifu tutafika mbali na vijana hatutohangaika kutafuta ajira baada ya masomo” anasema na kuongeza:

“Nchi nyingi zinafanya ubunifu na kwa kiasi kikubwa zinanufaika kwa ubunifu huo, hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele kwa kutumia teknolojia mbalimbali kama hii niliyofanya.”

Tuesday, October 24, 2017

JICHO LA MWALIMU : Shule inavyoweza kuchochea utaliiJoseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

Kumekuwapo  changamoto kubwa kwa wazawa katika kufanya utalii wa ndani ama wa nje ya nchi.
Watanzania wamekuwa wakisemana vibaya kuwa hawana utamaduni wa kufanya utalii.
Sababu kadhaa zimekuwa zikitajwa kuwa kikwazo cha watu kufanya ziara za kitalii, ikiwamo umasikini, kutojengewa utamaduni huo tangu awali (shuleni/vyuoni, na katika familia).
Nyingine ni gharama kubwa za viingilio na kutokuwa na taarifa za kutosha kama vile maeneo  yenye vivutio na namna ya ufikaji wake.
Utalii ni kitendo cha mtu kwenda kutembelea na kujifunza nchi na maumbile yake kijiografia.
Pia, utalii ni hali ya kusafiri huku na huko ili kuyafurahia mandhari.
Wengine husema kwamba hata kile kitendo cha wenyeji kusaidia au kushughulikia watalii na kuwahudumia nacho ni utalii.
Pia, utalii unahusisha kusoma desturi, tabia, utamaduni, miiko, matambiko na historia ya nchi au sehemu husika. Kuna aina mbalimbali za utalii kama vile  utalii wa kibiashara, kidini, mikutano, mapumziko, utamaduni,  historia na mazingira.
Utalii wa ndani ni kule kutembea kutoka mahali pamoja hadi pengine ndani ya nchi husika.
Tabia ya watu kuthamini na kufanya utalii wa ndani huweza kuchochewa sana kuanzia ngazi ya shule na vyuo.
Hii ni kwa sababu, shule ni wakala mkubwa wa mabadiliko na maendeleo endelevu. Mfano wa utalii rahisi kufanywa na jamii husika ni utalii wa baiskeli na wa kutembea kwa miguu.

Shule inawezaje kuwa wakala wa utalii wa ndani?
Ziara za mafunzo ni mbinu au njia mojawapo ya kujifunza na kufundishia shuleni au vyuoni.
Mwanafunzi hupata uelewa mkubwa anapotazama mazingira ya nchi kwa uhalisia. Madhumuni ya  utalii wa ndani hutofautiana kati ya sehemu moja ya utalii na nyingine.
Kuna uwezekano mkubwa wa shule kuandaa ziara za kimafunzo kwa madarasa tofauti katika kila kipindi cha likizo za masomo.
Kamati  za ziara za shuleni, hupaswa kuratibu maandalizi hayo kwa kutuma walimu kwenda kuona sehemu watakazopata malazi na chakula, watakazotembelea, na kama kuna shule wangependa kufanya nayo mtihani wa pamoja wa kujipima na kujua kiasi cha gharama.
Kama shule haziwezi kuandaa ziara hizi kupitia kamati maalumu za ziara, zinaweza kuomba huduma hiyo kutoka kampuni za utalii.
Kuna faida kadhaa za kutumia kampuni za utalii ili kufanikisha safari ya utalii au ziara za kimafunzo, ikiwamo kuokoa muda wa walimu kwenda kufanya mchakato wa maandalizi ya ziara husika.
 Aidha, kunapotokea dharura yoyote ile safarini, ni rahisi kampuni kushughulikia kwa kuwa kila siku wako katika michakato hiyo na ndiyo sehemu ya kazi zao.
Ikumbuke hata hivyo kuwa kutumia kamati za shule, pamoja na mambo mengine kunasaidia kupunguza gharama. Kampuni pamoja na kutoa huduma, bado zinafanya kazi hiyo kwa mrengo wa kibiashara unaolenga kupata faida.
Ni kwa vipi sasa  shule na vyuo zinaweza kuwa mabalozi wa utalii wa ndani? moja, kuwapa ufahamu na uelewa wanafunzi. Hii huwezesha jamii kufahamu kuhusu faida za utalii wa ndani na jinsi   wanavyoweza kuufanya.
Wanafunzi ni mabalozi wakubwa wa mabadiliko katika jamii. Wanapopata elimu huweza kuifikisha kwa wazazi na walezi kisha kwa jamii nzima.
Pia, wanafunzi ni wazazi wa kesho, watarithisha maarifa hayo kwa vizazi vijavyo.
Kwa kupitia shule na vyuo, tabia ya kupenda kufanya utalii wa ndani inaweza kukuzwa, kwa sababu ya uhamasishaji kutoka kwa wadau mbalimbali wenye uelewa wa utalii na kampuni zote zinazojishughulisha na utalii.
Mbili, mamlaka ya hifadhi za taifa huweza kutia chachu utalii wa ndani kwa kutoa punguzo za viingilio kwa wanafunzi na wanachuo, siyo tu katika kipindi cha sherehe za sabasaba na nanenane; ambapo wanufaika wengi huwa wale tu ambao walipata fursa ya kutembelea maonyesho hayo.
Tatu, shule kueleza fursa zinazoweza kuwanufaisha wanajamii ambao wameizunguka hifadhi ya taifa.
Kumekuwapo changamoto kadhaa kutoka kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi, ikiwamo kutoona  moja kwa moja  faida za utalii.
Hivyo, jamii hiyo huweza kusababisha mikwamo kwa watalii kama vile kutowapa ushirikiano stahili.
Nne, kupitia uhamasishaji kutoka vyombo vya habari na mawasiliano. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, vinaweza kuhamasisha utalii wa ndani.
Tano, mitalaa yetu ya elimu katika ngazi zote ziweke suala la utalii wa ndani kama suala mtambuka.
Ikiwezekana suala la utalii wa ndani lichopekwe katika masomo mbalimbali.
Mtaalamu wa masuala ya utalii na uhifadhi wa tamaduni, Ismail Swalehe, anaeleza kuwa sekta binafsi inayojishughulisha na utalii kama kampuni za utalii, bado hazijachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha jamii ya Kitanzania kufanya utalii wa ndani tofauti na wanavyofanya kwa watalii kutoka nje.
Anaeleza kuwa ni wakati sasa wa mamlaka husika kuziwezesha kampuni binafsi na vyama vya kijamii vinavyokuza utalii.
Shule nazo ziwajengee wanafunzi misingi ya kupenda na kuthamini utalii wa ndani tangu wakiwa watoto na vijana.
Siyo rahisi kwa mtu ambaye hakujengewa tabia ya kutumia kipindi cha likizo kwa kufanya ziara au utalii, akategemewa tu kuibuka ukubwani na kuanza kufanya.
Hata kama ana rasilimali na uwezo, bado hatoweza kufanya kwa sababu jambo hilo siyo sehemu ya utamaduni wake.
Hivyo, ni wajibu wa kila shule na chuo kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanapata fursa nyingi za kufanya utalii wa ndani mara nyingi iwezekanavyo.
Shule na vyuo zijenge tabia ya kutumia likizo kufanya ziara za kitalii. Kufanya hivi ni  kuchochea ari ya utalii wa ndani na kulinda na kuzithamini rasilimali zetu.

Tuesday, October 24, 2017

ELIMU NA MALEZI : Umuhimu wa kumpunguzia mtoto shinikizo la kufauluChristian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Ufaulu wa mitihani umepewa nafasi ya pekee katika mfumo wetu wa elimu.

Shule zetu hazina namna nyingine ya kumwelimisha mtoto zaidi ya kumtaka akusanye, akumbuke na kutumia maarifa aliyonayo kujibu maswali ya mtihani.

Ingawa ustawi wa jumla wa binadamu hautegemei eneo hilo moja la ukusanyaji na utumiaji wa maarifa, shule zetu zinaonekana kuamini kuwa pasipo mtu kuwa na maarifa mengi, hawezi kufanikiwa.

Kasumba hii imetuathiri hata sisi wazazi. Tunafikiri, kwa mfano, ni lazima mtoto afaulu masomo kwa kiwango cha juu ili afanikiwe. Matarajio haya makubwa yanatufanya tuwaweke watoto kwenye shinikizo kubwa mno la kufaulu, tukiamini ufaulu ndio kigezo cha ustawi wao katika maisha.

Matokeo yake, tangu mtoto anapoingia shuleni mpaka anamaliza, anajikuta katika mazingira ambayo kimsingi hana kazi nyingine zaidi ya kumridhisha mwalimu na mzazi wake.

Wazazi tunataka kuona mtoto ana uwezo wa kukusanya na kukumbuka maarifa. Mazoea haya yanaibua changamoto kadhaa za kimalezi kwa watoto.

Kulea tabia ya ushindani

Shule zetu zinathamini wanafunzi wanaofanya vizuri na kudhihaki wale wanaoonekana dhaifu. Mtoto anayefanya vizuri darasani, kwa mfano, ndiye anayependwa na walimu, ndiye anakuwa maarufu, na ndiye anayepata zawadi ya kuwa bora kuliko wengine. Hili ni tatizo na nitaeleza kwa nini.

Kwa muda mrefu, tuliamini kumzawadia mtoto mdogo aliyefanya vizuri kuliko wenzake ingekuwa si tu motisha kwake kuongeza jitihada za kufanya vizuri kwa mara mwingine tena, lakini pia ingewafanya watoto wengine kuweka bidii zaidi kwa matarajio ya kupata zawadi kama aliyopewa mwenzao.

Hata hivyo, tafiti nyingi zikiwamo za Profesa Carol Dweck wa Chuo Kikuu cha Stanford, zinaonyesha utamaduni huu wa kuwapongeza watoto kwa namna inayobagua uwezo wao, una kasoro nyingi zinazoweza kukuza mitazamo mibovu kwa watoto.

Kwa mfano, mtoto aliyezoea kuongoza darasani na kusifiwa anaweza kugeuka kuwa mtumwa wa sifa.

Utumwa huu wa sifa unamweka kwenye hatari ya kuwa na tabia ya kuelekeza nguvu kwenye eneo linalomfanya ajione bora na hivyo kukwepa maeneo mengine ambayo, pengine yanaweza kuwa muhimu katika maisha. Ikiwa mathalani, mtoto anajua walimu na wazazi humsifia kwa kufaulu vizuri, mtoto huyu anaweza kukwepa kushiriki kazi za ndani ambazo anajua haziwezi kumgusa mzazi wake.

Pia, kupongezwa kwa kuwazidi wengine kunaweza kumkatisha tamaa mtoto hasa pale inapotokea ama anafanya vizuri, lakini hakuna mtu anayejali au kuna mtoto mwingine anayeonekana kumzidi kinyume na vile alivyozoea.

Lakini vile vile, kwa upande wa watoto wanaoshuhudia mwenzao akizawadiwa kwa kuwazidi mara kwa mara, wengi hunyong’onyea na kuanza kujiona kama watu duni wasio na uwezo wa kufanya vizuri kama wenzao.

Tafsiri yake ni kwamba, kwa watoto wadogo, hakuna sababu ya msingi ya kuwawekea mazingira ya kuwashindanisha kiuwezo, hali inayoweza kuwaingizia dhana ya kushindana hata katika mazingira ambayo hakuna sababu yoyote ya ushindani.

Kudumaza vipaji

Changamoto ya pili ya shinikizo hili kubwa la taaluma kwa watoto, ni kudumaza vipaji ambavyo kimsingi hakuna namna ya kuvipima kwa kutumia mitihani.

Kwa kuwa shughuli karibu zote zinazoendelea darasani zinalenga kujenga eneo moja tu la kukusanya na kukumbuka maarifa, mtoto hawezi kuwa na motisha ya kufanya vitu vingine visivyohusiana na masomo.

Matokeo yake mtoto anapokuwa shuleni anakuwa hana kazi nyingine zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Anaporudi nyumbani, hali kadhalika, anakutana na mzazi anayeamini kazi ya msingi ya kufanya kwa mwanae ni kuzingatia masomo.

Mtoto anayeishi kwenye shinikizo la namna hii anapojaribu ‘kuchepuka’ kidogo ili kukuza vipaji visivyotambuliwa na mitihani rasmi ya darasani, anajikuta kwenye mgogoro na mwalimu na mzazi.

Kwa sababu hii, watoto wetu wengi ambao pengine wangeweza kuwa na vipaji vya kila aina, wanaishia kufanya vitu ambavyo mara nyingine havifanani navyo.

Kudumaza ukuaji

Shinikizo hili kubwa la kufaulu masomo pia linaathiri mtindo wa kawaida wa maisha ya mtoto. Kwa mfano, shule inayotaka mtoto awe bora kitaaluma, kwa kawaida itamnyima fursa ya kushiriki shughuli zisizo za kimasomo, lakini ambazo kimsingi zingeweza kuwa muhimu katika makuzi.

Kwa sababu ya kusoma kwenye shule inayotaka kuongoza kwenye mitihani, mtoto huyu mdogo, hatopata mtu wa kumfundisha kujifanyia usafi wake binafsi, kufagia, kushiriki kazi za mikono kwa sababu tu mitihani ambayo ndio kipimo cha ubora wa shule haina vipengele vinavyopima utu wa mtoto na hata ushiriki wake kwenye kazi za mikono.

Pamoja na uzuri wa kufaulu masomo, mtoto mdogo wa shule ya msingi, kwa hakika anahitaji kufaulu pia hata kwenye maeneo mengine yenye nafasi muhimu ya kumsaidia kupata mafanikio katika maisha.

Mbali na kupata alama 95 darasani, kwa mfano, mtoto huyu anahitaji kujifunza umuhimu wa kujali hisia na mahitaji ya wengine, tabia ambayo angeweza kujifunza vizuri zaidi kupitia michezo kuliko vitabu vilivyotajwa kwenye mtalaa.

Kasoro hii ya mfumo wa elimu kutilia mkazo eneo la ufahamu na maarifa kuliko maeneo mengine, imefanya watoto wengi wakose fursa pana ya kujengwa kiroho, kimaadili na hata kupata stadi nyingine muhimu za kimaisha.

Ushauri

Natambua shauku kubwa waliyonayo wazazi kuona watoto wanashika nafasi ya kwanza darasani. Hata hivyo, kama tulivyoona kwa ufupi, shauku hiyo ya kuwa na watoto wenye ‘akili’ isiwafanye watoto wakajikuta wakibanwa mno na hivyo kukosa muda wa kujifunza stadi nyingine za maisha.

Aidha, tunazo sababu za kutosha kuvumilia hata pale tunapoona watoto wetu hawafanyi vizuri darasani. Hakuna ushahidi wa kitafiti unaothibitisha kuwa ufaulu wa sekondari na vyuoni unategemea ufaulu mkubwa wa ngazi za chini.

Miaka ya awali ina umuhimu mkubwa katika kujenga sura ya maisha atakayoishi mtoto. Tunahitaji kuweka msisitizo mkubwa kwenye kujenga utu, kuwakuza kiroho na kuwafundisha stadi za maisha, kwa sababu hayo ndiyo maeneo yatakayoamua mustakabali wao.

Tuesday, October 17, 2017

Simulizi ya msomi aliyerudia mtihani wa kidato cha nne mara nne

 

By Abeid Poyo aabubakar@mwananchi.co.tz

Hebu pata picha ya mtu anayejikwaa barabarani tena sehemu ileile aliyoumia jana na juzi, lakini bado yumo; haoni shida wala kukata tamaa au kufikiria kuchepukia barabara nyingine.

Kila anapojikwaa, hujizoazoa na kuamka. Ujasiri wa kupambana na hali yake hadi kuzishinda changamoto zilizoelekea kuwa kikwazo katika maisha yake, umemfanya kuwa mmoja wa watu wa kupigiwa mfano.

Mtu aliyejikwaa mara kadhaa na hatimaye kupata ufumbuzi, ni Clement Fumbuka ambaye sasa ni mtaalamu wa ufugaji kwa ngazi ya elimu ya juu. Na ili watu wajue kukata tamaa katika maisha ni kosa kubwa, Fumbuka ametunga kitabu kiitwacho “Jijenge kimawazo: Anguka mara 7 simama mara 8”.

Kitabu hiki kinaakisi maisha yake; maisha ya kutokata tamaa maishani. Laiti angekuwa na aibu ya kusimulia yaliyomtokea miaka 13 iliyopita au angekuwa mchoyo, angeinyima jamii ya Kitanzania siri ya mafanikio ya kielimu aliyo nayo.

Fumbuka anatudhihirishia kuwa maisha ni mapambano, hakuna kukata tamaa maishani. Mikasa aliyokutana nayo katika safari yake kielimu leo inatumika kwa wengi kama funzo lenye kushibisha.

Kufikia kuwa mtu mwenye elimu ya chuo kikuu na kipaji cha uandishi wa vitabu, Fumbuka “alianguka chini mara nne, na akasimama”. Hapana, hakuanguka chini bali alishindwa mtihani wa kidato cha nne mara nne na bado alirudia kwa bidii hadi akafaulu.

Kitabu cha hamasa

Unaweza kukiita kitabu chenye mafundisho ya hamasa kuhusu harakati za kuzikabili changamoto za maisha. Ametumia saikolojia, mafundisho ya kidini, ufundi wa lugha na mifano kadhaa kuelezea kwa nini binadamu hapaswi kukata tamaa.

Mbali ya kitabu “Jijenge kimawazo: Anguka mara 7 simama mara 8” kinachosimulia harakati za maisha, pia ametunga vitabu vingine kama “Hujashindwa ndoto yako” (2015), “Mtunze kuku akutunze”(2016) kinachozungumzia ufugaji wa kuku.

Safari yake kielimu

Kitabu chake kinasadifu maisha binafsi. Hakuandika kitabu mithili ya riwaya za kufikrisha, bali kudhihirisha kwamba mtu anaweza kuanguka mara saba na akasimama mara nane kwa ujasiri na sasa ni mtaalamu wa mifugo, elimu aliyoyapata kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Mwaka 2004 kwa mara ya kwanza alifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Geita na kujikuta akifutiwa matokeo kwa sababu anazosema hakuzifahamu.

“Sikujua kama nilifaulu au la. Kutokana na sababu za kiuchumi, sikuweza kufuatilia chanzo cha kufutiwa, kwani wazazi hawakuweza kugharimia ufuatiliaji,” anasema

Huu ukawa kama mwanzo wa kinachoweza kusemwa kama nuksi. Baada ya hapo alijaribu mara kadhaa kurudia mtihani huo lakini hakufanikiwa.

“Niliamua kujisajili katika kituo cha kujiendeleza watumishi walioko kazini na elimu ya watu wazima (Klasta)). Hapo nilifanya mtihani kama mtahiniwa binafsi. Mazingira hayakunipa nafasi nzuri kujisomea na kujiandaa vema kama ilivyo kwa mtahiniwa wa shule,” anasema.

“Sikuwa na tatizo lolote niwapo kwenye chumba cha mtihani. Changamoto za kawaida wakati mwingine zilijitokeza lakini hazikuwa tatizo kubwa kunikatisha tamaa. Nakumbuka mara ya kwanza kufanya mtihani katika kituo cha Klasta, msimamizi wa mtihani alinipa mtihani wa Engineering Physics badala ya Basic physics. Baada ya saa moja na nusu tangu mtihani uanze, msimamizi alishtuka na kunifuata. Alifika na kunitaka radhi kuwa mtihani alionipa siyo wangu, bali amekosea kunipa mtihani wa mtu mwingine ambaye alikuwa anafanya mtihani wa somo hilo,” anasimulia.

Anasema wakati wote wa kurudia mitihani mwaka hadi mwaka, ndugu, jamaa na marafiki waliungana naye mwanzoni, lakini mwishowe walimchoka wakiamini ni sawa na mtu anayetwanga maji kwenye kinu au alikuwa fungu la kukosa.

“Marafiki wengi walianza kuniambia niachane na shule kwani maisha si lazima niwe nimesoma tu. Ndugu zangu walianza kunishauri nifanye biashara. Kaka yangu mmoja alijitokeza na kutaka kunipa mtaji nianze biashara. Wazo lake sikulikataa lakini nilimwambia anitunzie mtaji nikishindwa kabisa ndipo anipe mtaji huo. Niliendelea tena kulipia mtihani kila mwaka hadi nilipofaulu na kupata vigezo vya kuendelea na kidato cha tano,” anaeleza.

Fumbuka anakumbuka mtihani wake wa kwanza alipoanza kurudia matokeo yalikuwa; Kemia (B), Biolojia (D), Fizikia (D), Jiografia (D), Kiswahili (D), Uraia (D), Kiingereza (D), Hisabati (D) na Historia (F).

Ndoto yake anasema ilikuwa kusoma tahasusi za PCB au PCM, hivyo kwa matokeo hayo akawa na deni la kutafuta angalau alama C katika masomo ya Fizikia na Biolojia.

Mwaka 2006 akarudia masomo matatu: Fizikia, Hisabati na Biolojia. Matokeo yakawa Biolojia (C), Fizikia (D) na Hisabati (D) hivyo bado akawa anadaiwa angalau C moja ya kumpa sifa ya kujiunga na kidato cha tano.

“Baada ya matokeo hayo nilipata matumaini mengine, nikaamua kwenda kusoma ‘Pre-form five’ (masomo ya kujiandaa kwa kidato cha tano) katika sekondari ya Buluba iliyopo Shinyanga, huku najipanga kurudia tena kusafisha matokeo yangu.

‘’Shule niliyokwenda kusoma, haikuwa na tahasusi za PCB na PCM, badala yake kulikuwa na CBG (Kemia, Biolojia na Jiografia). Niliamua kusoma CBG mwaka 2007 na wakati huohuo nililipia tena mtihani wa kidato cha nne na kufanikiwa kupata C ya Jiografia. Alama hii ikanipa sifa ya kusomea CBG na hivyo nikawa na ruhusa ya kwenda kidato cha sita,” anaeleza.

Huo ukawa mwanzo wa safari ya kuelekea kuipata shahada ya kwanza aliyonayo sasa. Baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo mwaka 2009.

Fumbuka ambaye sasa ni mfanyakazi katika Chuo cha Kilimo na Mifugo cha Kilacha mkoani Kilimanjaro anasema, jinamizi la kufeli halikumwandama hadi alipofanikiwa kuhitimu masomo mwaka 2012.

Tena chuoni alikuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wenzake. “Kutokana na uwezo wa kueleza kitu mpaka mtu akaelewa haraka, wanafunzi wenzangu walipenda niwafundishe na pengine waliniomba niende chuoni kuwasaidia kipindi cha likizo, walipokuwa wakirudia mitihani,” anasema

Moyo wa kutokata tamaa

Siku zote anasema aliamini kuwa angefanikiwa kufikia kiwango cha elimu alichokitamani ndiyo maana matokeo mabaya katika mitihani hayakuwa sababu ya kumkatisha malengo yake.

“Kila matokeo ya mtihani yalipotoka yalinipa akili mpya kurudi tena darasani kuendelea na mapambano, huku akilini nikiwa na msemo; ‘Mapambano ni sehemu ya maisha, kushindwa au kushinda kupo kwenye mikono ya Mungu),” anaeleza.

Moja ya vitu vilivyomsukuma kutokata tamaa katika safari yake ya elimu ni kuchukia maisha duni na kutaka kutafuta suluhisho la kuwa na maisha bora nyumbani. Sababu nyingine anasema ni nguvu iliyomvuta kutimiza malengo yake kama vile kuona watu waliofanikiwa kupitia ndoto yake na kumtia moyo kuwa atafanikiwa kama wao.

Sababu ya tatu anaeleza ni; “Nguvu ya ndani ya nafsi. Nguvu hii ilikuwa kubwa kuliko sababu zote zilizonifanya kuendelea kurudia mitihani. Nguvu hii haikukauka moyoni, kila mara nilisikia mahojiano ya nafsi mbili moyoni.”

Anasema nafsi moja aliisikia ikilalamika kwa mateso mengi na kutaka kukata tamaa na nafsi nyingine ilikuwa inahoji kama ataamua kukata tamaa kusoma, je hatakuja kujutia maamuzi hayo hapo baadae? Na kama anaamini tangu mwanzo kuwa elimu ndiyo silaha muhimu kuliko chochote katika maisha yake, je atatumia silaha gani kuyakabili maisha?

“Watu wengi walitokea kunikejeli na kunibeza lakini sikuona majibu ya maswali haya tofauti na kuhakikisha nimefikia elimu ninayoitaka.’’

Mazingira ya nyumbani

Kama ilivyo kwa jamii nyingi za Kitanzania mazingira ya nyumbani kwao katika kijiji cha Nkungulu wilayani Kwimba hayakuwa rafiki kwake.

Kila siku alikwenda shambani lakini alihakikisha kila ifikapo jioni anakwenda kulala Kwimba mjini ambako ni umbali wa kilomita nane kutoka kijijini. Alifanya hivyo kutunza akili ya kutobadili fikra za kusoma.

Changamoto nyingine iliyomkabili ni ya kukosa fedha za kugharimia masomo yake, hali iliyomlazimisha kufanya shughuli kama kuchoma mkaa na kukata kuni.

Wito wake kwa Watanzania

Fumbuka anawasihi Watanzania kufanya maamuzi na kusimamia ndoto ya malengo wanayojiwekea.

“Binafsi pamoja na kupanga kufanya mambo mengi, mengi yalichelewa kufanikiwa, lakini hakuna jambo ambalo nilipanga na kulisimamia likaja tofauti. Nimekuwa mtu wa kumshukuru Mungu kwa kutimiza ndoto zangu na malengo mbalimbali ambayo nilijiwekea. Subira, uvumilivu na kujituma katika mipango ni mambo matatu ambayo kwangu yamenifanya nifikie malengo,” anasema.

Wasifu na familia

Anasema, “Nyumbani tulizaliwa watoto 14 tukiwa wote ni watoto wa baba mmoja na mama mmoja. Hadi sasa tulio hai ni watoto 13, mimi ni mtoto wa 12. Katika watoto wote, mimi pekee nimefanikiwa kufika elimu ya juu. Wawili walifanikiwa kuhitimu kidato cha nne lakini hawakuendelea, wengine 10 waliishia darasa la saba.”     

Tuesday, October 17, 2017

Ubunifu wa kuvutia wa wanafunzi shule ya kata

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Kwa kawaida, mwanafunzi anayejitambua hategemei anachofundishwa na mwalimu pekee, bali kujiongeza kwa kuwa mbunifu.

Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia, ubunifu unaweza kumsaidia katika soko la ajira pindi anapohitimu.

Wanafunzi Naimah Mohammed na Stephano Chacha kutoka Shule ya Sekondari Vingunguti, wameamua kuishi kwenye uhalisia huu.

Pamoja na umri wao mdogo, vichwa vyao vinachemka baada ya kubuni mashine ya kupalilia inayotumia nishati ya jua.

Ubunifu wao unaweza kutajwa kama kielelezo cha umuhimu wa shule za kata zilizosambaa kila kona ya nchi. Wamewatoa kimasomaso wanafunzi wenzao, hasa dhidi ya baadhi ya watu wanaozitazama shule za kata kwa jicho la pembeni.

Wanafunzi hawa wenye ndoto ya kuja kuwa wahandisi baadaye, walitengeneza mashine hiyo Mei mwaka huu kwa lengo la kuwarahisishia wakulima na kutatua changamoto za kilimo zinazowakabili wakulima nchini.

“Kabla ya hapo tulifikiria kitu gani tutengeneze, tukakubaliana kubuni kitu ambacho kama kitaungwa mkono kitakuwa na manufaa katika jamii,”anasema Naimah.

Baada ya kubaini kuwa changamoto inayowakabili wakulima wengi nchini, ni kulima kilimo cha kizamani hasa kutumia jembe la mkono, fikra ikawa ni kutengeneza mashine rahisi ya kupalilia.

Kifaa hicho kimetengenezwa kwa vifaa vitano ambavyo ni paneli ya nguvu ya jua, swichi, mota na betri. Kinatumia jembe lenye meno mithili ya msumeno sehemu ya kulimia.

“Hili jembe lina mfumo wa kifaa ambacho kinabebwa mgongoni kama begi. Kifaa hiki kinabeba vifaa vyote vinavyotumia nishati ya jua, sehemu ya pili ni jembe,’’ anasema na kuongeza;

‘Ni jembe la kawaida lakini lina meno sehemu ya kulimia na mpini wake kwa juu tunaweka swichi ambayo ikibonyezwa jembe linapalilia; kazi ya mkulima ni kushikilia tu.’’

Wanasema mashine hiyo ina uwezo wa kupalilia eneo la ekari moja kwa siku mbili au tatu. Aidha. inaweza kutumika kujaza udongo kwenye mashina ya mazao kama vile karanga.

Naimah ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo iliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam,anasema jembe la mkono lina athari kwa wakulima, hivyo wanapaswa kubadilika na kuanza kutumia vifaa vya kisasa.

“Mkulima anapotumia jembe la kawaida itamlazimu kuinama, katika hali ya kawaida mtu anapoinama kwa muda mrefu lazima atapata maumivu ya mgongo, hivyo hata uzalishaji unapungua kwa kuwa atatumia muda mrefu kupalilia shamba” anasema.

Kubuni mashine hiyo siyo mwisho wa safari yao, kwani wanasema wanatarajia kubuni kitu kingine kikubwa ikiwa watawezeshwa.

Chacha anasema baada ya ubunifu wao huo kushinda katika mashindano ya wanasayansi bora chipukizi yaliyofanyika Agosti mwaka huu, huo ni mwanzo mzuri wa kutangaza kifaa chao.

Wito kwa Serikali

Chacha anatoa rai kwa Serikali kuwaunga mkono kwa kuufanyia kazi ubunifu wao na hata kuwawezesha kifedha.

“ Jembe hili linaweza kumsaidia mkulima moja kwa moja, kwa hiyo ubunifu unaongeza maendeleo ya nchi,”anaeleza.

Anasema kupitia jembe hilo ambalo ni rahisi kutumia na lisilotumia gharama yoyote zaidi ya nishati ya jua, wananchi wataongeza kipato kwa kulima mazao mengi, na jamii nzima itanufaika.

“Mashine hii tuliyoigundua ni mbadala wa kutumia jembe la mkono, nchi za wenzetu wanatumia hizi teknolojia kwa ajili ya kilimo, hivyo hata sisi mashine hii kama itapewa kipaumbele inaweza kuwa suluhisho katika sekta ya kilimo,” anasema.

Benitho Sutta ni mwalimu wa somo la Fizikia shuleni hapo. Anasema baada ya kupokea wazo kutoka kwa Naomi na Chacha, aliahidi kutoa ushirikiano ili kufanikisha wazo lao la kutengeneza kifaa cha kipekee nchini.

Anasema wazo lao ni la kipekee kwani limejikita kutatua changamoto katika sekta ya kilimo nchini.

“Wanafunzi wengi wanakimbilia masomo ya sanaa na hicho ndicho kinachowakwamisha wengi kwa kigezo kuwa masomo hayo ni mepesi, lakini ukweli ni kwamba masomo ya sayansi yanaweza kumweka mwanafunzi katika nafasi nzuri ya kujiajiri kupitia ubunifu,” anasema.

“Nimegundua kuwa wanafunzi wengi ni wabunifu; wana mawazo mengi kichwani lakini yanakuwa kama michezo ya kuigiza kwa sababu namna ya kuyaleta katika hali halisi inakuwa ngumu kuyatekeleza,”anasema na kuongeza:

“Mfano jembe hili limegharimu kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali na kupeleka kwa fundi kuchomelea, kwa hiyo kiasi kikubwa cha fedha kimetumika.

Chacha na Naimah wanalia kutotembelewa na kiongozi yeyote wa kuwapa moyo au kuwasaidia kuhusu ubunfu wao.

Mwalimu wao anasema kama wangepata msaada wangefanya vizuri zaidi katika ubunifu na kutengeneza mashine nyingi zinazoweza kutumika nchi nzima.     

Wednesday, October 18, 2017

‘Homework’ zinavyodumaza ukuaji wa watoto

 

        Ukiwauliza wazazi kitu gani wanafikiri kikisitizwa mapema zaidi kwa watoto kitawasaidia kufanikiwa, wengi watakwambia elimu.

Ni kwa kwa sababu hiyo, wazazi hasa wasomi wanaharakisha kuwapeleka shule watoto wenye umri mdogo.

Ninawafahamu watoto wengi wa miaka minne wanaosoma darasa la kwanza. Wazazi wao wanafanya hivyo, wakiamini mtoto akisoma mapema, maana yake uwezekano wa kufanikiwa maishani unakuwa mkubwa.

Shuleni pia, watoto hawa wanakutana na walimu wanaofanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafaulishwa mitihani.

Mbali na mtoto kufundishwa mambo mengi yanayomzidi umri wake, kuna hili la walimu kuwapa watoto kazi nyingi wanazotakiwa kuzikamilisha baada ya muda wa masomo (home work).

Faida ya kazi za nyumbani

Kazi za nyumbani zina nafasi ya kutengeneza daraja kati ya mazingira ya shule na nyumbani. Kimsingi, mwalimu anatarajia kumfanya mzazi awajibike kutengeneza mazingira ya kitaaluma nyumbani.

Kufanya hivi kunamlazimisha mzazi kujenga tabia ya kufuatilia maendeleo ya mwanawe kimasomo, na hivyo kutilia mkazo kile ambacho mwalimu amekifundisha darasani.

Hoja nyingine ya watetezi wa kazi hizi, ni kumfundisha mtoto tabia ya kuwajibika.

Inaeleweka kwamba mtoto anaporudi nyumbani na kazi, akili yake inakuwa na kazi ya kuhakikisha wajibu aliopewa na mwalimu shuleni unakamilika.

Profesa Harris Cooper, wa Chuo Kikuu cha Duke amefanya tafiti nyingi kuhusiana na utamaduni huu. Anasema; “Kazi za nyumbani ni utaratibu mzuri wa kujifunza. Kuna faida kadhaa, lakini faida hizo zinategemea umri wa mtoto.”

Kwa watoto wa madarasa ya awali (yaani shule ya awali na msingi), anafikiri inatosha shughuli ya mtoto kujifunza iishie darasani.

Mwalimu akitumia muda wake vizuri darasani, hana sababu yoyote ya kumpa mtoto kazi za ziada, kwa sababu hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya wingi wa kazi za nyumbani na mafanikio ya mtoto kitaaluma.

Nikijitolea mfano mimi mwenyewe, sikumbuki ni lini niliwahi kukaa nyumbani nikifanya kazi za shule nikiwa nasoma shule ya msingi. Baada ya masomo, ratiba ya nyumbani ilikuwa ni kumsaidia mama kufanya kazi.

Baadaye nilipata muda wa kucheza na kwa kuwa nilitumia muda wa shule vizuri, hatimaye nilifanikiwa kitaaluma.

Tafiti tofauti

Etta Kralovec, ambaye ni profesa wa elimu katika Chuo Kikuu cha Arizona anasema; “Utafiti uko wazi kabisa kwamba saa mbili za kufanya kazi za shule baada ya muda wa shule, zinatosha kwa mtoto mkubwa (wa sekondari.) Lakini kwa mtoto mdogo (shule ya msingi), kazi za nyumbani hazina faida ya maana.”

Binafsi nimekuwa nikifuatilia kazi ambazo watoto wengi wa madarasa ya chini wanapewa kuzikamilisha nyumbani. Nyingi, kwa kadri ninavyoziona, hazina ulazima wowote zaidi ya kujaribu kumwaminisha mzazi kwamba kuna kitu kinafanyika shuleni.

Kwa mfano, kazi nyingi ni za kukariri kwenye vitabu, ambavyo mara nyingi havijapitiwa kwa makini na wataalam kujiridhisha ikiwa vinafaa kwa watoto wadogo.

Baadhi ya vitabu vina masimulizi yenye maudhui yasiyolingana na umri wala utamaduni wetu, lakini ndio vitabu ambavyo watoto wetu wanatumia muda mwingi kuhangaika navyo kukamilisha kazi za nyumbani.

Athari kwa ukuaji

Mtoto anayeanza shule, anahitaji kusaidiwa kupenda kujifunza na kuona shule ni mahali pazuri. Utamaduni huu wa kuwapa watoto kazi nyingi, hata hivyo, unawafanya watoto hawa waanze kuchoka shule.

Fikiria mtoto wa miaka mitatu anayehitaji kucheza, anajikuta kwenye mazingira ambayo kuna mtu anamlazimisha kujua kujumlisha na kutoa.

Ingawa ni kweli mtoto anaweza kujifunza kwa lazima, lakini kufanya hivyo kunaweza kumdumaza mtoto kwenye maeneo mengine muhimu ya ukuaji. Mfano mdogo, watoto wengi hujikuta kwenye migororo mikubwa na wazazi wao kwa sababu tu hawajafanya kazi za shule.

Badala ya kukaa na kuwafundisha watoto wao maadili, tunu za maisha na kuwakuza kiroho na hata kujenga mawasiliano ya karibu, wazazi wengi wanaishia kufokeana na watoto kwa sababu tu hawajakamilisha kazi.

Mara nyingi watoto hawafanyi kazi hizi si kwa sababu ni wavivu, jeuri au si wasikivu. La hasha! Mara nyingi sababu ni ukweli kwamba tumewaingiza kwenye mduara wa shinikizo la kitaaluma mapema zaidi kuliko umri wao.

Kujenga utegemezi

Fikiria mtoto ameshindwa kufanya kazi alizotakiwa kuzifanya kwa uzembe. Katika mazingira kama haya, mzazi anageuka kuwa afande anayehakikisha kazi zote zimefanyika hata kama mtoto mwenyewe kimsingi haoni maana ya kile anachotakiwa kukifanya.

Inapotokea mtoto hana uwezo wa kuzifanya, badala ya mzazi kubeba wajibu wa kukazia yale ambayo mtoto alijifunza shuleni, mzazi anaamua kuzifanya mwenyewe kwa niaba ya mtoto, ili mwalimu shuleni asione mtoto hana mtu wa kumsaidia anaporudi nyumbani.

Hapa tunatengeneza tatizo jingine la mtoto kujenga utegemezi kwa watu wazima na kumnyang’anya mtoto tabia ya kuwajibika kwa mambo yanayohusu.

Ingawa kumsaidia mtoto kukamilisha kazi zake inaweza kuonekana kama mchango chanya wa mzazi kwa mtoto, tabia hii inaweza kupanda mbegu ya kuwategemea watu wengine hata atakapokuwa mtu mzima.

Ushauri

Shughuli zisizo za kitaaluma moja kwa moja zina nafasi kubwa ya kumfundisha mtoto vizuri zaidi kuliko kazi za nyumbani.

Kwa mfano, kuwasomea na kuwasimulia watoto hadithi ni namna bora zaidi ya kuwafundisha watoto mambo wanayoyahitaji katika maisha yao ya kila siku. ada ya shughuli ya kujifunza shuleni, ni vyema nyumbani pawe sehemu ya kumfanya mtoto ashiriki shughuli nyingine akiwa na familia yake.

Pia, tuweke mazingira ya mtoto kutumia akili yake katika kuyachunguza mazingira yake kupitia michezo na kazi za mikono.

Shughuli hizi tunazoziona hazina maana, zina nafasi kubwa ya kukuza uwezo wa mtoto kukumbuka, kuzingatia, kufikiri kwa haraka, kukaa na wenzake na hata kuvumbua vipaji vyake ambavyo wakati mwingine hatuvigundui kwa sababu muda wote tunataka afanye hesabu, asome na aandike.     

Tuesday, October 10, 2017

Safari ya miaka 35 ya Mukoba katika ualimu

 

By Phiinias Bashaya, Mwananchi pbashaya@mwananchi.co.tz

Alianza kama mwalimu wa shule ya msingi, akastaafu akiwa na kumbukumbu ya kuwa kiongozi wa juu wa wa shirikisho la wafanyakazi nchini.

Haikuwa kazi rahisi kufika hapa alipo. Maisha ya ualimu wa Gratian Mukoba aliyestaafu hivi karibuni yalianza mwaka 1982 katika Shule ya Msingi Mwavile, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Alijipambanua kama mtetezi wa haki na hata kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Walimu nchini(CWT) na baadaye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Katika maisha yake ya kazi Mukoba, amefundisha jumla ya shule saba katika mikoa ya Mwanza, Kagera na safari yake kuishia katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ya jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wetu Phinias Bashaya, amefanya mahojiano naye kuhusu safari yake ya miaka 35 akiwa mwalimu na kiongozi wa walimu nchini.

Swali: Kipi umejifunza kama mwalimu miaka yote ya utumishi wako?

Jibu: Nimejifunza kuwa elimu haithaminiwi kwa kiwango kinachotakiwa. Mazingira ya kujifunzia na kufundishia yamekuwa sio rafiki kwa watoto na walimu wao. Walimu wanakabiliwa na ukosefu wa nyumba, vifaa vya kutolea elimu, kutopandishwa vyeo, kutopandishwa mshahara, kutorekebishiwa mshahara mara wanapopanda madaraja, kutolipwa madeni yao kwa wakati na mengineyo.

Swali: unaridhika na hadhi waliyonayo walimu wa Tanzania?

Jibu: Siridhiki na hadhi ya walimu kwa sababu miaka ya 1960, walimu waliheshimika. Walilipwa mishahara mizuri hivyo walimiliki magari, wakajenga nyumba bora na kusomesha watoto wao. Wananchi au jamii ilikuwa ikiwaheshimu walimu. Na wao walitumikia wito wao kwa moyo mmoja huku wakijibeba na kujielewa. Waliendelea kujinoa ili wawe imara kitaaluma, lakini kwa sasa ualimu umepoteza heshima yake.

Swali.Walimu wanachukuliwa kama kundi la watumishi waoga wanaolalamika tu badala ya kuchukua hatua; jambo hilo lina uhalisia wowote?

Jibu.Hili lina ukweli fulani kwani hata pale tulipofuata sheria zote za nchi tukafikia hatua ya kufanya mgomo baada ya milango ya mazungumzo kufungwa, bado wanachama wengi waliogopa vitisho vya mwajiri wakaenda kazini. Bado kunatakiwa kujengwa moyo wa kujiamini kwa walimu na hili litatokana na kiwango cha kujielewa na kujua thamani halisi ya kazi yao.

Swali. Ni kitu gani kilikusukuma kuwania nafasi za uongozi kwenye Chama cha Walimu

Jibu. Tangu utoto wangu nachukia uonevu au haki kupotea. Msukumo huu umo ndani yangu, nahisi ndio umekuwa nguvu nyuma ya harakati zangu za kuipigania kila siku.

Swali. Walimu walikuamini na kukuchagua kuwa Rais wao, unadhani matarajio yao kwako yametimia?

Jibu. Kuongoza walimu kulitokana na jinsi nilivyojipambanua kupigania haki kuanzia shuleni Kahororo wilaya ya Bukoba na shule nyinginezo. Baada ya kuongoza sehemu hizo, walimu wa nchi nzima waliniamini na kunichagua kwa mara ya kwanza mwaka 2002 kuwa makamu wa Rais wa CWT na 2007 kuniamini zaidi na kunichagua kuwa Rais wa CWT na 2014 wafanyakazi wote kunichagua kuwa Rais wa TUCTA (Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania).

Swali.Ni mambo gani mapya yamefanyika katika uongozi wako ambayo ungependa yakumbukwe na kuendelezwa?

Jibu. Katika uongozi wangu yamefanyika mengi. Siwezi kusema kuwa ni mimi mwenyewe kwani taasisi huongozwa na timu. Nishukuru Mungu kwa kunikutanisha na timu nzuri niliyofanya nayo kazi na kuweza kupata mafanikio yaliyoipambanua CWT kama chama kikubwa na chenye nguvu kulinganisha na vingine.

Mambo makubwa ni ujenzi wa ofisi za mikoa na wilaya, ujenzi wa jengo la uwekezaji la Mwalimu House, ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi kama magari na samani za ofisi. Pia, nimeacha wigo wa madaraja ya walimu umepanuliwa kwa madaraja mawili zaidi kwa kila ngazi.

Swali.Umewahi kuongoza mgomo wa walimu nchi nzima kudai masilahi yao, unadhani ulifanikiwa kushinikiza kile mlichokidai?

Jibu. Niliongoza migomo miwili mwaka 2008 na 2012, tulifanikiwa kiasi kwani kila mgomo ulipoisha walioshiriki kikamilifu waliongeza ujasiri na wale walioogopa kushiriki waliona kuwa inawezekana.

Hatukupata kile tulichokidai kwa ukamilifu, kwani mwajiri mara zote aliumaliza mgomo wetu kwa kutumia mahakama ambayo haikutupatia kile tulichokuwa tunadai, hivyo kuacha hali isiyo njema kwa upande wetu.

Swali. Mliwezaje kukaa meza moja na Serikali kumaliza mgomo?

Jibu. Hatujawahi kukaa mezani na Serikali kumaliza mgomo, migomo mitatu ya 1993, 2008 na 2012 yote iliisha kwa vitisho na walimu kurudi kazini huku wameinamisha vichwa chini.

Swali. Nini chanzo cha kuwapo kwa makundi yenye mtizamo tofauti kwenye chama yaliyokuwa yanashinikiza kujitenga na kuanzisha chama kipya cha walimu?

Jibu. Chanzo cha makundi ndani ya chama ni sheria inayoruhusu uanzishwaji wa vyama, vingine ni yale niliyoyaeleza hapo juu ya kuwa na waajiri tofauti. Pia, ipo hali ya ubinadamu; kuna mtu anaona akianzisha chama atapata uongozi hasa baada ya kugombea na kushindwa.

Swali. Hadi unaondoka kwenye uongozi wa CWT, kundi linalotaka kujitenga bado lipo au changamoto hiyo imetatuliwa?

Jibu. Bado lipo na linajinasibu kwa kueleza kuwa nchi nyingine zina vyama vinane hata zaidi. Mimi nimekwenda nchi nyingi, pale penye utitiri wa vyama na mashirikisho sikuwahi kusikia faida kwa wafanyakazi zaidi ya malalamiko na sehemu nyingi vyama vimekuwa vikiungana na kuacha kugawana nguvu ili viweze kumkabili mwajiri kwa nguvu moja na sauti moja.

Swali. Kwa nini CWT iliamua kuanzisha benki ya walimu?

Jibu. Katika dira yetu mwanzoni tulijiwekea malengo makuu matano likiwamo la kupigania hali bora ya uchumi wa wanachama hao

Sasa uanzishwaji wa benki ni kutekeleza lengo hili la kuwaimarisha wanachama kiuchumi. Hii inatatua pia tatizo la riba zisizo rafiki zinazotolewa na taasisi za fedha ambazo kwa kiwango kikubwa zimejinufaisha kwa kuwakopesha walimu na kuwatoza riba kubwa hadi asilimia 300.

Swali. Unalizungumziaje suala la elimu bure kwa wanafunzi na mazingira ya walimu kufundisha nchini?

Jibu. Suala la elimu bure kwa wanafunzi ni zuri, linaondoa kumfungia milango mtoto aliyezaliwa kwenye familia masikini ambazo zingeshindwa kumudu karo na mahitaji mengine ya shule. Hata hivyo, utaratibu huu umeleta changamoto kwani madarasa mengi yanajaa mno, huku ni kumweka majaribuni mwalimu ambaye kwanza hana motisha.

Labda nieleze hapa kuwa siku zinavyokwenda ndivyo binadamu anavyopaswa kutayarishwa kwa ubora zaidi. Kinachobeba uzito siyo idadi ya watu waliopo duniani kwa wakati fulani bali ubora wao. Uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa unatokana na upungufu wa watu bora unakwenda kuleta madhara makubwa mno.

Ni bahati mbaya kwamba gharama ya vita duniani kwa mwaka ni mara nane ya gharama ya kutolea elimu. Kama mataifa na Tanzania ikiwamo yatashindwa kubadilisha mizani hiyo hapo juu, dunia itaendelea kujiandalia angamizo lake.

Swali: Ni mambo gani katika elimu ungetamani yawe na msingi wa kudumu badala ya kutegemea utashi na matamko ya wanasiasa?

Jibu: Ningetamani kuufanya ualimu uwe kazi ya heshima namba moja kama ilivyo katika za Ujerumani na Finland. Kwa kufanya hivyo ualimu utavutia vijana wenye uwezo wa kutayarisha watoto kwa ubora unaotakikikana.

Ningetamani mazingira ya kufanyia kazi ya ualimu yaboreshwe ili wote wafundishaji na wajifunzaji waweze kutimiza kwa ukamilifu malengo ya kuelimisha na kuelimika.

Tuesday, October 10, 2017

Emmanuel na ndoto ya kuongoza mtihani wa Taifa

Emmanuel John akiwa na baba yake John Buseme,

Emmanuel John akiwa na baba yake John Buseme, baada ya kuibuka mwanafunzi bora katika mahafali ya kuhitimu darasa la saba Shule ya Kwema Modern ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Shija Felician 

By Tausi Mbowe, Mwananchi tmbowe@mwananchi.co.tz

Kila aliyekuwapo katika hafla ya mahafali ya miaka 16 Shule ya Msingi Kwema Morden iliyopo mjini Kahama, Shinyanga alitamani kumuangalia pale jina lake lilipokuwa likitajwa mara kwa mara.

Mbele ya umati wa wazazi, walimu na wageni waalikwa waliofika shuleni hapo kwa ajili ya mahafali hayo, jina la Emmanuel John lilisikika kwa zaidi ya mara tano.

Awali mwanafunzi huyo aliitwa kwa ajili ya kupokea zawadi baada ya kuongoza katika somo la Hisabati kisha ikafuata Maarifa ya jamii, Kiswahili na masomo mengine. Mwishowe akaibuka mshindi wa jumla katika masomo yote.

Haikuishia hapo hata ilipotajwa zawadi ya mwanafunzi bora aliyefanya vizuri katika michezo, jina lake likachomoza tena na kuitwa jukwaani baada ya kushika nafasi ya kwanza.

Wakati sherehe hizo zikiendelea, nilishangazwa na kipaji cha mwanafunzi huyo ambaye wakati huu tena alipanda jukwani na kucheza ngoma nzuri akishirikiana na wanafunzi wenzake.

Ngoma hiyo ya Kisukuma maarufu kwa jina la gobogobo ilitoa burudani nzuri, lakini kivutio kikubwa ilikuwa ni kwa Emmanuel ambaye alionekana kucheza kwa ustadi mkubwa.

Jambo hilo lilinusukuma na kutaka kujua historia ya mwanafunzi huyo kwa undani, lakini pia anawezaje kufanya vizuri katika masomo na hata masuala nje ya taaluma.

Kwake, siri ni hii: ‘’… siri ya kukufanya vizuri ni kufanya kila kitu kwa kikamilifu na kutopuuzia ninachojifunza. Lakini kubwa zaidi ni kumtanguliza Mungu katika kila kitu,’’ anasema mwanafunzi huyo kwa uso wa bashasha.

Lakini Emmanuel anasema jambo lingine linalosababisha kufanya vizuri ni uwepo wa miundombinu bora ya kujisomea shuleni hapo, huku walimu ambao wamekuwa msaada mkubwa kwake wakichochea mafanikio hayo.

“Hapa shuleni mazingira ni rafiki , walimu wapo wa kutosha, lakini wamekuwa wakitufundisha kwa upole na urafiki mkubwa jambo linalotuongezea hamasa ya kupenda shule.

Akizungumzia historia yake, Emmanuel anasema tangu alipoanza masomo ya chekechea amekuwa akishika nafasi ya kwanza na mara moja tu alianguka na kushika nafasi ya pili jambo lilomkosesha furaha.

“Nakumbuka nilikuwa darasa la tatu baada ya matokeo nikajikuta nimeshika nafasi ya pili, roho iliniuma sana sikuwa na amani hata kidogo na wakati wote nilikua mnyonge nikitafakari namna ya kurudi katika nafasi yangu.”

Anakiri kwamba kufanya kwake vibaya kwa mwaka huo ni matokeo ya kutozingatia masomo na baada ya kugundua hilo alihaidi kubadilika mpaka atakapo maliza elimu yake.

“Lengo langu ni kuongoza katika mtihani wa kitaifa na naamini kwa uwezo wa Mungu nitafanikisha kwani ni jitihada na nimejiandaa vyema kwa hilo,”anasisitiza.

Baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Jonh Buseme anasema anaamini palipo na nia pana njia na kwamba anachofanya kwa sasa kumuombea kwa Mungu ili ndoto za mwanawe zitimie.

“Siku zote amekuwa akiamini katika kufanya vizuri, lengo lake ni kuongoza kitaifa ndiyo maana anafanya juhudi ili kufanikisha hilo.”

Hata hivyo, Buseme anasema Emmanel ambaye ni mtoto wake wa pili ni tofauti na watoto wake wengine wanne. Huyu amekuwa na tabia tofauti za kupenda kusoma na kusali sana.

“Huyu bwana kabla hajaanza kufanya chochote ni lazima asali, nafurahishwa na tabia yake ya kupenda kumtanguliza Mungu kabla ya kitu chochote na ndiyo maana naamini atafanikisha ndoto zake.”

Ratiba yake ya kila siku

Kutumia ratiba kwa usahihi ni siri nyingine ya mafanikio kwenye masomo yake darasani. Anasema kila siku huamka saa 11.00 asubuhi.

“Nikiamka tu jambo la kwanza ni kusali ili kumshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kumuomba aniongoze siku nzima kisha najiandaa na ikifika saa 11.30 naingia darasani kusoma kwa muda mchache kabla ya kuungana na wenzangu kufanya usafi wa kawaida wa asubuhi,”anaelezea.

Awapo darasani, anasema humsikiliza mwalimu na kufanya kazi zote anazoachiwa kufanya.

Hajawahi kumiliki simu

Kwake Emmanuel simu na mitandao ya kijamii ni adui mkubwa wa maendeleo yake na kwamba hatarajii kuimiliki mpaka pale atakapofikisha umri wa utu uzima.

‘’Unajua wanafunzi wengi wanashindwa kufanya vizuri kutokana na kumiliki simu za mikononi, hivyo muda mwingi badala ya kuutumia kusoma wanautumia katika mitandao ya kijamii na kujikuta wakipotea,”anasema na kuongeza:

“Mitandao ya kijamii ina faida, lakini pia ina hasara kubwa kwa wanafunzi maana wengi hawajui jinsi ya kuitumia na kujikuta wakitumbukia katika masuala ya kuiga mambo yasiyofaa.’’

Mkurugenzi ataja siri ya mafanikio

Mkurugenzi wa Shule hiyo, Paulini Mathayo anasema siri kubwa ya kufanya vizuri kwa shule yake ni uwepo wa miundombinu bora ya kufundishia. Lakini pia mwanafunzi anapougua, hupata huduma bora.

“Niliamua kujenga kituo cha afya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanafunzi wangu, lakini pia motisha kwa walimu na wanafunzi wangu ni jambo la msingi,’’ anaeleza.

Anatoa mfano wa matokeo ya mwaka jana ambapo shule hiyo ilitoa wanafunzi wanane kati ya 10 walioingia katika 10 bora kitaifa.

Tuesday, October 10, 2017

Kuharakisha kumpeleka shule mtoto kunaweza kumdumazaChristian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Mwanzoni mwaka huu, niliamua kumpeleka mwanangu wa miaka mitatu shuleni.

Katika umri huo mdogo, kwa kweli tulitamani mtoto angebaki nyumbani. Lakini kwa kuwa mimi na mke wangu tunalazimika kwenda kazini asubuhi, tuliona ni vyema mtoto akapata mahali salama pa uangalizi.

Hata hivyo, hatukutarajia mtoto mdogo kiasi hicho akajifunze kusoma, kuandika wala kuhesabu. Tuliichukulia shule kama sehemu salama zaidi ya malezi kwa mtoto kuliko kumwacha nyumbani na msichana wa kazi.

Kutofurahia shule

Siku chache baada ya mtoto kuanza kuhudhuria shule, tulianza kuona mabadiliko. Kwanza, mtoto alirudi nyumbani akiwa amechoka na hivyo alilala mapema zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Hatukupata wasiwasi kwa sababu usingizi wa kutosha ni mojawapo ya mahitaji muhimu kwa afya ya mtoto.

Tulianza kupata wasiwasi mtoto alipoonekana kukosa shauku ya kwenda shule. Kama wazazi tulifikiri shule ni mahali pa furaha zaidi kwake hasa kwa sababu anakutana na wenzake wa umri wake.

Kingine tulifikiri kwa sababu shuleni angepata muda wa kucheza michezo mingi isiyopatikana katika mazingira ya nyumbani, hivyo kwa vyovyote angekuwa na msisimko wa kwenda.

Kwa hiyo hali hiyo isiyotarajiwa ya mtoto kutofurahia shule ilitustua kidogo kama wazazi hasa kwa sababu wakati mwingine aligoma kabisa. Fahari ya kuvaa nguo za shule, kubeba begi kama dada yake haikutosha kumpa sababu ya kutamani kwenda shule. Wakati mwingine ilibidi kufanya kazi ya ziada kumshawishi.

Mzigo wa masomo

Niliamua kufanya uchunguzi mdogo kubaini kitu gani hasa kilisababisha yote hayo. Nikagundua mambo kadhaa. Kwanza, ugeni wa mazingira. Kama ambavyo baadhi ya sisi watu wazima huhitaji muda kuzoea mazingira mageni, ndivyo inavyotokea kwa watoto wadogo.

Kitendo cha kuondoka nyumbani, mahali anapopachukulia kuwa salama zaidi kwake, na kwenda kukaa saa nyingi mahali pengine akiwa na watu asiowafahamu vizuri, kinaweza kumfanya asifurahie. Hata hivyo, nilitarajia angezoea mazingira yale baada ya muda kwa sababu si tu walezi wake shuleni walikuwa wachangamfu kwa watoto, lakini pia wingi wa watoto wa umri wake sambamba na upatikanaji wa vifaa vya michezo, ungemsaidia kufurahia vitu vingi zaidi kuliko kama angebaki nyumbani.

Baadaye nikagundua utaratibu wa malezi katika kituo hicho ulikuwa na kasoro. Watoto wale wadogo walifundishwa masomo ambayo, kwa hali ya kawaida, hufundishwa kwa watoto wa darasa la kwanza wenye miaka kati ya sita na saba.

Mtoto wa miaka mitatu, kama huyu wa kwangu, alilazimika kuanza kujifunza ‘alfabeti’, ‘tarakimu za Hisabati’ na hata kuanza kukariri baadhi ya maneno kwa lugha ya Kiingereza. Malezi yalitilia mkazo zaidi kwenye taaluma kuliko michezo.

Matarajio ya sisi wazazi

Nilimuuliza mkuu wa kituo hicho kujua mtazamo wake kuhusu jambo hilo. Akajibu:, ‘Hapa tunawaandaa vizuri ili watakapokwenda darasa la awali wasipate shida. Kwa hiyo tunahakikisha wanapotoka hapa wawe wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu. Vilevile, tunawafundisha lugha ya Kiingereza ambayo ni muhimu kwa masomo ya darasa la kwanza.’

Mwalimu huyu, kwa jinsi alivyoongea, alionekana kuamini kuwa msisitizo mkubwa kwenye masomo una manufaa kwa watoto kwa sababu uliwaandaa kufanya vizuri katika ngazi za juu. Nikataka kujua kwa nini wasingesubiri watoto wafike ngazi husika ili wajifunze kile wanachotarajiwa kujifunza.

Hakunificha sababu, kwani alisema: ‘Nyinyi wazazi ndio wateja wetu na hicho ndicho mnachotaka. Ukimleta mtoto wako hapa, unatarajia ajue kuongea Kiingereza, asome na aweze kuandika na kufanya hesabu. Vyote hivyo ndani ya muda mfupi.’

Nikakumbuka wakati ninatafuta nafasi ya darasa la kwanza kwa binti yangu wa kwanza. Haikuwa kazi rahisi. Watoto wanaotarajia kuanza darasa la kwanza ilibidi wafanye mtihani wa kupima uwezo wao wa kusoma, kuandika kwa Kiingereza na walipaswa kuwa na uwezo wa kufanya mahesabu.

Kimsingi, walimu wa darasa la kwanza waliopaswa kuwa na kazi ya kufundisha mambo hayo matatu, nao walitarajia kuletewa watoto ambao tayari wameshajifunza yale wanayopaswa kuwafundisha baada ya kuwapokea shuleni.

Kwa hiyo nikaona mwalimu alikuwa sahihi. Matarajio makubwa ya wazazi yanachochea jitihada kubwa za walimu kukidhi matarajio hayo. Kwa bahati mbaya hali kama hiyo inachangia kumlazimisha mtoto mdogo wa miaka miwili au mitatu kujifunza mambo ambayo wakati mwingine hayalingani na umri wake.

Makuzi yanayosahaulika

Nikirudi kwa mtoto wangu huyu wa miaka mitatu, mara nyingi alirudi nyumbani akiwa na ‘kazi nyingi za nyumbani.’ Walezi wake shuleni walifanya hivyo kwa nia njema ya kuturidhisha sisi wazazi walioamini tunataka kuona matokeo mazuri ya fedha tunazolipa kama ada ya ‘masomo.’

Kazi hizi, pamoja na nia njema ya waliozitoa, zilikuwa na mchango mkubwa katika kumchosha akili. Kazi hizi kwa kweli hazikuzingatia uwezo wa mtoto. Katika umri wake wa miaka mitatu, shughuli ya maana anayoihitaji zaidi ingekuwa michezo.

Kupitia kucheza, mtoto angejifunza mambo ambayo yangekuwa msingi wa maisha yake kuliko kukazaniwa kushika masomo. Michezo, mathalani, ingemfundisha umuhimu wa kushirikiana na wenzake, kuelewa wenzake wanafikiri nini, kuchangamsha ufahamu wake na kwa ujumla, kufurahia utoto wake.

Lakini kwa sababu ya ‘fikra za maendeleo’ watoto hawa wamenyimwa fursa ya kuuishi utoto wao na badala yake wanakabiliwa na shinikizo la kufanikiwa kupitia ‘ufaulu.’

Sisi wazazi wenye ‘fikra za kimaendeleo’ kwa kweli hatutarajii mtoto acheze, akosee, afeli, ajifunze. Kilicho muhimu kwetu ni mtoto ‘kushika masomo’ na kujua Kiingereza.

Matokeo yake watoto wanajikuta wakitumia muda mwingi kwenye kazi ambazo wakati mwingine zinawazidi umri. Haya yote yanafanywa kwa gharama ya maeneo mengine muhimu ya ukuaji wa mtoto.

Kwa kuwa nilishaanza kuona matokeo ya mtazamo huo wa kumharakisha mno ‘masomo’ mwanangu, nilimwambia mwalimu nimempeleka mwanangu pale ili apate nafasi ya kucheza. Mwalimu alinishangaa.Itaendelea

Blogu: http://bwaya.blogspot.com