Sunday, September 23, 2018

Uamuzi wa Chadema kususa uchaguzi, ni woga au ujasiri?

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

Ni uamuzi mgumu, ndivyo unavyoweza kuelezea hatua ya Chadema kutoshiriki chaguzi ndogo zinazotangazwa kila kukicha.

Ni uamuzi uliokuja wakati mezani kuna uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Liwale, Lindi na madiwani wa kata 37 utakaofanyika Oktoba 13, huku madiwani wengine wakiendelea kuacha kata zao wazi kwa kujitoa upinzani na kujiunga na CCM.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anataja sababu tatu za kutoshiriki chaguzi hizo.

Mosi, anasema hadi sasa wapigakura wapya hawajaandikishwa tangu 2015 kama sheria inavyotaka, pili, chama hicho kimekuwa kinafanyiwa hujuma za wazi, tatu, katika chaguzi hizo kumekuwa na matumizi makubwa ya nguvu za dola na wapigakura kutishwa.

Katika chaguzi ndogo tano, kuanzia ule wa Novemba 26, 2017 mpaka ule uliopita wa Septemba 15 mwaka huu, CCM imeshinda majimbo yote tisa ya ubunge na kata 86 zilizotokana na wawakilishi wake kuhama vyama na kujiunga na chama tawala. Chadema imeambulia kata moja ya Ibhigi mkoani Mbeya.

Matokeo hayo yameifanya historia mpya nchini katika uchaguzi kwa upinzani kupata matokeo mabaya ya uchaguzi katikati ya malalamiko.

Novemba 26, 2017, CCM ilitangazwa kushinda kata 42 kati ya 43 kupitia uchaguzi mdogo wa marudio nchini. Januari 14, CCM kilipata ushindi uchaguzi wa ubunge katika majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.

Katika chaguzi nne za mwaka huu, CCM imeshinda maeneo yote. Februari 17, CCM ilishinda jimbo la Kinondoni na Siha kabla ya Agosti 12, kushinda tena jimbo la Buyungu na kata 38.

Septemba 15 chama hicho tawala, kilishinda kata tatu na majimbo ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli na sasa kinajipanga kushiriki tena katika uchaguzi wa jimbo la Liwale na kata 37.

Katika chaguzi hizo, viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho wamekutana na changamoto ya kufunguliwa kesi mahakamani, kujeruhiwa na vifo kadhaa, hali ambayo imesababisha Chadema kutoa uamuzi wa kususia uchaguzi.

Uamuzi huo wa Chadema umekuwa mjadala mkubwa wa kisiasa. Wasomi na wanasiasa wana mawazo tofauti juu yake, baadhi wanasema ni mzuri na ulikuwa haukwepeki, lakini wengine wanasema kushiriki uchaguzi ni jukumu la chama cha siasa, bila kujali kitapata nini katika uchaguzi husika.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Joran Bashange, Katibu Mkuu wa NLD, Tozy Matwanga na Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi wa Vyama 11 vya siasa visivyokuwa na uwakilishi bungeni, Renatus Muhabhi ni miongoni mwa wanaunga mkono msimamo huo.

Kwa nyakati tofauti wanasema kuendelea kushiriki uchaguzi wenye kasoro za wazi na kuubeba upande mmoja kunahalalisha haramu dhidi ya vyama vya upinzani.

Hoja za viongozi hao zinaibuka juu ya malalamiko yasiyokoma ya mawakala wa vyama vya upinzani kunyimwa utambulisho wa kuwaruhusu kusimamia kura zao, hivyo kura kupigwa chini ya mawakala wa upande mmoja.

Chanzo cha tatizo

Hali imefikia hatua hiyo kutokana na malalamiko ya kila uchaguzi unaofanyika yanajitokeza ama kwa sura ileile. Ni suala la mawakala wa vyama vya upinzani, hasa Chadema, kukataliwa kwenye vituo vua kupigia kura.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikidai kwamba ama mawakala wake wananyimwa hati za viapo, au barua za utambulisho zinazotakiwa kuonyeshwa kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Mara nyingine hati hizo hucheleweshwa na kupatikana baadaye wakati uchaguzi unaendelea. Madai mengine ambayo hata hivyo yanakanushwa na mamlaka zinazohusika ni kuwa, mawakala wengine hukamatwa na polisi siku moja kabla au siku ya uchaguzi ili wasiwepo vituoni.

Mwisho wa matukio hayo ya kuzuiwa mawakala wa upinzani ni kituo cha kupigia kura kubaki na mawakala wa chama tawala pekee, wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Athumani Kihamia pamoja na kukiri kupokea malalamiko kuhusu kukataliwa kwa mawakala katika majimbo ya Monduli na Ukonga, alisema tatizo hilo si la jumla na limekuwa linasababishwa na wapinzani wenyewe kwa kuitaka kubadili mawakala na kuleta ambao hawajaapishwa.

“Hata huku Monduli niliko lilikuwapo, nimelifanyia kazi mimi mwenyewe na sasa kila kitu kinakwenda sawa.

Akizungumzia malalamiko ya Chadema, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage anasema “Kila chama kina hiari ya kushiriki na tume haiwezi kukilazimisha. Tume inaendelea kufanya tathmini ya uchaguzi baada ya kukamilisha itatoa taarifa.

“Kama uchaguzi ulifanyika kinyume cha sheria, wahusika walipaswa kufuata sheria kwa kwenda kutoa malalamiko yao kwenye vyombo husika badala ya kupeleka kwenye vyombo vya habari.”

Pamoja na uongozi wa NEC kuona malalamiko Chadema na upinzani si ya msingi, wachambuzi wa siasa na wanasiasa wanayatazama kwa jicho tofauti.

Profesa wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohammed Bakari anasema nafasi ya kupata ushindi kwa Chadema na upinzani kwa jumla imezidi kuwa finyu kutokana na mazingira ya kisheria, kikatiba pamoja na ya kisiasa.

Anasema uwezekano wa kushinda hata katika zile nafasi zenye matumaini umepotea.

“Sheria ni zilezile, Tume ni ileile, na huko nyuma kulikuwa na baadhi ya maeneo wangeweza kushinda lakini kwa sasa mazingira fulani ya kisiasa yaliyojitokeza, ambayo ukichanganya na udhaifu wa kisheria, kikatiba na muundo wa NEC, nafasi imekuwa finyu,” anasema Profesa Bakari.

Hata hivyo, msomi huyo wa masuala ya siasa, anafafanua kuwa pamoja na mazingira magumu kwa chama hicho kikuu cha upinzani, hoja ya kususia inatakiwa iendane na mikakati mingine mbadala, vinginevyo umaarufu na ushawishi wa chama hicho utaendelea kuporomoka zaidi.

“Uhai wa chama ni kushiriki kazi za siasa na chaguzi ni fursa kubwa ya chama kujitangaza na kuongeza ushawishi kwa maeneo mengi zaidi, sasa wanasusia chaguzi hizo wakati huo wamezuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa, kususia bila mbadala itavunja moyo, na inawezekana kabisa chama kikaendelea kupoteza umaarufu,” anasema Profesa Bakari.

Anasema nguvu ya chama huporomoka baada ya wafuasi na wanachama kuanza kukata tamaa ya kushiriki chaguzi.

“Wapiga kura wana tabia ya kufanya tathmini, je nikienda kushiriki kura yangu itakuwa na thamani? Au utamaduni ni uleule tu? Mtu anaona hakuna umuhimu wa kupiga kura, anakata tamaa ya kushiriki tena, ni dalili za kufanya vibaya zaidi kwa chama,” anasema.

Anasema kwa bahati mbaya zaidi, vyama vya upinzani vimezuiliwa kufanya mikutano ya hadhara huku chama kikiwa na wanachama waliojiandaa kuwa viongozi kupitia nafasi za uwakilishi wa wananchi.

Mbadala wa kususia chaguzi

Pamoja na mazingira hayo magumu kwa Chadema, baadhi ya wachambuzi wa duru za kisiasa wanahofia dalili za Taifa kurejea katika mazingira ya chama kimoja.

Hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi wa upinzani kuhamia CCM kisha kurejeshwa tena katika majimbo na kata zilezile, kuzuiliwa kufanya siasa za majukwaani, viongozi wa Chadema kufunguliwa kesi za uchochezi, madai ya dosari za kisheria, kikatiba na Tume ya Uchaguzi kupuuzwa.

Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anaonyesha wasiwasi wa nchi kuelekea kwenye mfumo wa chama kimoja. “Labda turudi kwenye chama kimoja na upinzani uwe ndani ya CCM kama tulivyokuwa awali. Tulikuwa na Tanu na ndani yake kulikuwa na upinzani,” anasema. Profesa Bakari anasema mahakama ni sehemu sahihi ya kutumika kudai mabadiliko ya kisheria, kikatiba na udhaifu unaoendelea lakini changamoto iliyopo ni mtazamo hasi uliojengwa na Chadema.

“Upinzani Kenya wamekuwa wakitumia vizuri mahakama na wanafanikiwa lakini hapa nchini wamejenga dhana potofu kwamba mahakama haziwatendei haki, sasa changamoto ni kwamba wanadai yawepo mabadiliko ya kikatiba, kisheria na CCM haiko tayari, pengine inategemea zaidi ushirikiano wa vyama na asasi za kiraia,” anasema.

Muhabhi anavitaka vyama vyote vya upinzani bila kujali tofauti zao, kuitisha mkutano wa kitaifa kwa ajili ya kupitisha tamko la pamoja kuhusu hali ya kisiasa na ushiriki wa chaguzi zijazo.

“Chadema wamechukua uamuzi sahihi kususia chaguzi hizi maana zimekuwa za kichefuchefu, kinachotakiwa ni kukutana vyama vyote, sisi tuna umoja wa vyama 11 visivyo na uwakilishi, bila kujali tofauti zetu wote upinzani tukutane na tuache unafiki, tutoe tamko la kususia chaguzi zote halafu tuone kama CCM wataingia peke yao kwenye uchaguzi,” anasema.

Muhabi anasema hatua hiyo itasaidia kuchochea mabadiliko ya kisheria, kikatiba na udhaifu unaotokana na muundo wa Tume ya Uchaguzi.

Tutarajie nini 2020

Profesa Shumbusho anasema hali haiwezi kubadilika hadi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020. “Kwa nini waendelee kuingia kwenye uchaguzi ambao wanajua hawatashinda? Nafikiri uamuzi wao ni sahihi, waache hadi hapo Katiba itakapobadilisha Tume ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi,” anasema.

Wachambuzi wengine wanasema tatizo kubwa ni viongozi wa NEC na wasimamizi wa uchaguzi wanateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama shindani.

Ushauri wa Lowassa,

Pamoja msimamo wa Chadema kama chama, mjumbe wake wa kamati kuu, Edward Lowassa anasema suluhisho la kuwa na uchaguzi huru ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi vinginevyo CCM itaendelea kutangazwa kushinda katika kila uchaguzi.

Anasema ili kufanya uchaguzi uwe wa huru na haki, ni lazima kuwe na sheria ambayo itafanya tume iwe inabanwa. “Lazima kuwe na chombo ambacho kinaibana tume, lakini sasa tume haiwezi kubanwa.”

Alisema jambo jingine ambalo linafanya uchaguzi huo kutokuwa huru ni kutokana na wakurugenzi na maofisa wanaosimamia uchaguzi kuwa wateule wa Rais.

“Wakurugenzi wengi walioteuliwa ni makada wa CCM ambao walianguka katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2015, Rais akawateua, usitarajie kama wapo huru hao,” alisema.

Sunday, September 23, 2018

Ukoloni Mamboleo na namna viongozi Afrika walivyonaswa

 

By Amani Njoka

Mwaka 1884-1885 ulifanyika mkutano wa mataifa ya Ulaya nchini Ujerumani kuhusu namna ya kuligawana bara Afrika. Mkutano huo ulisimamiwa na aliyekuwa Kansela wa Ujerumani kwa wakati huo, Otto Bismark na kufikia makubaliano ya kila nchi inayoweza kutawala sehemu yoyote ya Afrika na rasilimali zake, ichukue.

Ikumbukwe kwamba tangu karne ya 15 hadi karne ya 19 bara la Afrika lilikuwa sehemu muhimu pengine kuliko sehemu yoyote duniani kwa sababu ndilo lilikuwa mzalishaji mkuu wa malighafi kwa ajili ya mataifa ya Ulaya.

Historia inatuambia kwamba mataifa ya Denmark, Ufaransa, Urusi, Ureno, Italia, Hispania, Uturuki, Uholanzi yaligawiwa maeneo huku Ubelgiji na Marekani wakiwa kama wageni waalikwa.

Kweli mkutano huo ulileta mafanikio katika kile walichokidhamiria ikiwa ni pamoja na kuepusha migongano kati yao, kwani kila taifa lilikuwa na uchu wa rasilimali za bara hili.

Masuala yaliyoafikiwa katika mkutano huo yalikuwa ni kukomesha biashara ya utumwa, kueneza kile walichokiita ustaarabu na dini na kukomesha vita vya wenyewe vya wenyewe vilivyopiganwa na makabila na koo mbalimbali zilizokuwapo wakati huo. Hata hivyo, masuala haya hayakuwa mambo ya msingi sana kwao.

Hapo awali niligusia kwamba Afrika ilikuwa sehemu muhimu sana duniani kwa kuwa ilikuwa mahala pekee ambapo wangeweza kupata malighafi kwa ajili ya viwanda huko Ulaya na Marekani. Kila nchi wakati huo ilitamani kumiliki ardhi ya Afrika yenye rutuba, madini na kila nchi ilitamani iwatumie Waafrika kama nguvukazi katika mashamba yao. Kupitia mtifuano huo ndipo Bismarck akawaita wenzake mjini Berlin. Hapa ndipo historia inapotuambia kwamba Afrika ikakatwa vipandevipande, wakaingia kama mtu aliyeingia kwenye shamba ambalo alipanda yeye na kuvuma mazao yake. Wakakubaliana kwamba kila nchi miongoni mwao inaweza kuchukua koloni lolote kwa sharti tu la kuweza kutawala, hakuna taifa la Ulaya ambalo lingezuiwa kwa namna yoyote kufanya biashara katika bara la Afrika, hapakutakiwa kuwa na ongezeko la kodi kwa bidhaa yoyote kutoka au kuingia Afrika.

Vitabu vinaniambia madini yote na misitu minene ya mbao na magogo ya Kongo akapewa Mfalme Leopold II wa Ubelgiji, Uingereza ikachukua shaba ya Zambia, mafuta na ardhi yenye rutuba ya Nile huko Misri, Kenya, Sudan na dhahabu ya Kimberley, Afrika Kusini, Ghana na almasi ya Zimbabwe. Ufaransa ikapewa kila kitu kilichopatikana Jamhuri ya Afrika ya kati, Mauritania mpaka Gabon na Chad. Ureno akaambiwa ajichukulie Msumbiji na Angola. Italia ilichukua Somalia na sehemu za Ethiopia. Bahari, madini, mbuga za wanyama na ardhi nzuri ya Tanzania bara (Tanganyika kwa wakati huo) na Namibia alijichukulia Mjerumani.

Katika hayo yote Mwafrika hakuhusishwa, alikuwa hana hili wala lile mpaka alipokuja kujua kwamba yeye anapaswa kulima na kuchimba madini yake mwenyewe kisha awape hawa watu wapeleke kwao kisha watulete sigara, vioo, mafuta na nguo watuuzie, inauma sana.

Kwanini nimeanzia huko?

Huku ikiwa imepita miaka zaidi ya 50 tangu mataifa haya yaiache Afrika kwa kila kinachoitwa uhuru, mataifa haya yanaonekana kurudi tena kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Wakuu wa mataifa yaleyale yalikaa mwaka 1884-1885 yameanza kupishana kwa kasi ya ajabu katika anga la bara la Afrika. Wanakuja kwa njia ya makubaliano na mikataba ya kiuwekezaji.

Mifano ya hivi karibuni kabisa ni ujio wa waziri mkuu wa Uingereza, Kansela wa Ujerumani, marais wa China (Hu Jintao na Xi Jinping). Sambamba na hili kukawa na mkutano wa China na viongozi wa Afrika wa uliofanyika China, huko tuliahidiwa dola 60 bilioni.

China inaitaka Afrika huku ikifanikiwa kwa kiasi kikubwa Afrika ya Mashariki; Uingereza inakomaa na Kenya, Afrika Kusini na Nigeria na Ujerumani ikakomaa na Senegal, Ghana na Nigeria huku Ufaransa kupitia mkutano uliofanyika Mei mwaka huu mjini Paris, ikitangaza dhamira ya kuisaidia Afrika zaidi ya Euro 65 milioni.

Si hao tu, hata marais waliopita wa Marekani (Obama na Bush) wamefanya ziara Afrika, ikiwamo nchini mwetu na kuzungumzia mipango mbalimbali.

Tujiulize, kwa nini?

Katika makosa ambayo Afrika haipaswi kuyarudia ni kuacha mataifa haya yajichagulie cha kuchukua. Kwa sasa mataifa haya yanajua Afrika ina wasomi, wanaelewa wazi kwamba sasa hivi Afrika ina watu wenye uwezo wa kuchakata mambo, hivyo wanapaswa kutulia na kuja na mikakati inayoonekana kama pipi kumbe ndani shubiri.

Kwa sasa mataifa haya hayawezi kutumia mbinu waliyoitumia mwaka 1884-1885 au nyingine walizozitumia huko nyuma. Ni wakati wa kuwa makini.

Tusizubaishwe na mikopo yao ambayo huja kama neema kwa Afrika. Fikiri kuhusu Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia na mashirika mengine namna yanavyoinyemelea Afrika baada ya kushindwa kurejesha madeni. Suala la mikopo halijaanza leo, suala la mahusiano ya kibiashara hayajaanza leo, yalikuwepo tangu miaka ya 1,700 walipotudanganya kwa vioo, sigara, bunduki na nguo, kisha wakachukua rasilimali ambazo mpaka leo hazijulikani thamani yake kwa sababu nyingine hazipimiki.

Kwa sasa Afrika ina viongozi na wataalamu wenye ufahamu wa kutosha kabisa kugundua mitego na hila iliyoko katika mikataba yao. Kumbuka haya mataifa yanataka Afrika iendelee kuyategemea ili yenyewe yaendelee kunawiri, kwa hiyo yale yote yanayosemwa kwamba yanatoka kwao kutusaidia yachunguzwe mara nyingi iwezekanavyo. Kuna haja ya kuwa makini sana na hawa watu.

Hebu tuwatumie wataalamu tulionao hata kama ni wa kiwango kidogo lakini kwa manufaa yetu. Mataifa ya Kiafrika yanapaswa kuwaamini wasomi wake wa masuala mbalimbali kwa sababu hata wataalamu tunaowaamini kutoka mataifa ya nje ya Afrika walianza kama sisi tu, hawakuzaliwa wanaweza, walijifunza.

Afrika kwa sasa ina wataalamu karibu kila idara, watumike watatusaidia. Sisemi kwamba tusishirikiane wala kuwatumia wataalamu kutoka nje, tushirikiane nao huku tukiwekeza nguvu kubwa kwa hawa wetu, tufanye hivyo, lakini kwa umakini mkubwa kuliko umakini ambao tumewahi kuwa nao siku za nyuma.

Afrika isitegemee misaada

Hivi inakuaje bara kama Afrika lenye kila kitu tena kwa kiwango cha kutisha bado linaishi kwa kutegemea misaada? Ni ajabu lakini ni kweli kwamba Afrika inategemea misaada kutoka kwa watu ambao wanatutegemea sisi kupata wanachotuletea.

Ifike mahala tutambue na tuamini kuwa haya mataifa hayawezi kufanya chochote bila Afrika, yaani tuume meno na tukamate breki hata kama tutaumia lakini baadaye watatuheshimu.

Kuishi kwa kutegemea misaada kwa watu ambao wanatutegemea sisi kupata wanachotuletea ni kichekesho kinachoweza kumfanya mtu acheke karne nyingi, niamini mimi kwamba hata wao wanatung’ong’a. Tusiwe waoga, kuna baadhi ya mambo ambayo tunaambiwa tuyatekeleze ndipo tusaidiwe, lakini ukiangalia nyuma yake kuna madhara makubwa. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Afrika hukubali tu kusaini ili tupate misaada, lakini baadaye tunaingia kwenye mtego unaotulazimu kufia ndani.

Mfano, mataifa mengi yamekuwa yalikubali kuingia kwenye madeni ambayo yanakuwa matamu kwa nje, yaani kikitajwa kiasi cha hilo deni wanafikiri watanufaika lakini baadaye tunashindwa kulipa.

Tuziamini bidhaa za kiafrika pamoja na kuboresha uzalishaji wake. Ni ukweli usiopingika kwamba kuna baadhi ya sekta hasa kilimo bado zipo chini. Ukija sokoni unakuta bei ni ndogo, muda mwingine wakulima wanalanguliwa bidhaa zao.

Kutokana na hili unakuta uzalishaji unapungua, uzalishaji ukipungua maana yake tunajikuta tukitegemea bidhaa za vyakula kutoka nje. Sio hivyo tu, hata vile viwanda vilivyopo katika nchi za Afrika vinakufa kwa sababu bidhaa zake hazinunuliwi kwa sababu ya Waafrika hususani Watanzania kutokuviamini vya kwetu. Tujifunze kutumia vya nyumbani, licha ya kuamini kuwa vya nje vina ubora, vipo vingi pia vina ubora.

Serikali za kiafrika ziimarishe mifumo ya elimu. Kila kitu kinachofanyika kwa ufanisi katika ulimwengu huu kinategemea elimu. Ikiwa bidhaa zitakosa ubora, majengo yatakosa uimara, barabara hazitadumu, utawala utayumba, sekta za kilimo zitayumba, sekta ya fedha itayumba, sekta ya afya itayumba usiende mbali, chunguza elimu inayotolewa Afrika.

Elimu ikiwa mbovu hatuwezi kupata wataalamu wazuri wa masuala mbalimbali jambo ambalo litatufanya tuendelee kutegemea wataalamu wa afya, uchumi, wahandisi, wataalamu wa viwanda na madini ambao wakija wanaambatana na masharti kutoka nchi husika.

Elimu ikiwa mbovu mikataba mibovu hatuwezi kuikwepa, tutasaini tu kwa sababu hatuelewi. Zamani walituchukua, safari hii tusijipeleke wenyewe.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anafanya mazoezi kwa vitendo Mwananchi Communications Ltd na anapatikana kwa namba 0672395558

Sunday, September 23, 2018

Tutumie 2020 – 2025 kujenga mifumo imara (2)Julius Mtatiro

Julius Mtatiro 

By Julius Mtatiro

Jumapili iliyopita nilianzisha mjadala kuhusu jinsi ya kujenga mifumo imara ili mazuri yanayofanywa na Serikali yaendelezwe. Leo nahitimisha hoja hii na kufungua mjadala juu ya dhana hii.

Katika sehemu ya kwanza ya mjadala huu nilieleza namna uongozi wa awamu ya tano ulivyoweza kujipambanua na kutumia fedha za walipa kodi kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo ambayo italeta mchango mkubwa katika ustawi wa taifa letu.

Nikazungumzia namna uongozi wa Rais John Magufuli ulivyoweza kusimamia masuala sugu na kuifanya nchi inyooke, hayo ni yale ambayo kwa miongo kadhaa tuliyapigia kelele; rushwa na ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, nidhamu mbovu za watumishi wa umma, utendaji usio na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ubabe wa wenye fedha dhidi ya wananchi wanyonge na mengine mengi.

Nahitimisha hoja yangu leo kwa kuonyesha mwelekeo wa nchi yetu kuanzia mwaka 2020 – 2025 ambapo tunapaswa kuyatengenezea mkondo wa kudumu.

Mjadala wa yai na kuku

Mara zote, huwa nikitamka maneno “tujenge mifumo imara” watu wengi huhoji ikiwa mifumo imara inajijenga yenyewe au inajengwa na watu. Ukweli ni kwamba watu ndiyo hujenga mifumo, lakini mifumo imara hujengwa na watu imara, viongozi imara au viongozi wanaothubutu.

Kila nchi duniani, ilipofanikiwa kujenga mfumo fulani imara lazima walikuwako viongozi au kiongozi imara aliyeongoza ujenzi wa mifumo hiyo. Mfano; umoja, mshikamano na udugu walio nao Watanzania ni suala la kimfumo, si jambo la muda mfupi na halikushushwa tu.

Suala hili la kimfumo halikujileta lenyewe, lilijengwa kwa juhudi za viongozi imara waliowahi kuongoza taifa hili, wakiongozwa na Mwalimu Nyerere.

Afrika Kusini na Marekani

Nchini Afrika Kusini, baada ya mateso ya miongo mingi waliyopata Waafrika weusi kutoka kwa makaburu wa kizungu, isingelitegemewa taifa hilo likaendelea na maisha ya kawaida bila vita baina ya wazungu na watu weusi.

Suala la ustawi na uhusiano mzuri wa wazungu wa Afrika Kusini (makaburu) na weusi walio wengi (wenyeji) halikuja hivihivi, lilitokana na uthubutu na uimara wa viongozi wa ANC na Afrika Kusini, wakiongozwa na Nelson Mandela. Leo, maridhiano ya wazungu na weusi nchini Afrika Kusini yanaonekana yamo kwenye mfumo lakini hayakuanza tu yenyewe, yalijengwa na viongozi imara.

Pale Marekani, muungano wa mataifa mengi umeweza kujenga taifa moja imara, utumwa ukakomeshwa, serikali ya muungano ikaimarishwa hadi leo na uchumi wa nchi hiyo ukafanywa kuwa wa kisasa zaidi duniani. Mambo yote haya ambayo leo wanadamu wanayatazama kama mfano wa kuigwa ni mambo yaliyojengwa kimfumo, hayakushuka kama mvua kutoka mawinguni. Yalijengwa kwa juhudi kubwa, uimara na uthubutu wa viongozi imara na wenye kuthubutu wa wakati huo, wakiongozwa na Abraham Lincoln, rais wa 16 wa Marekani kati ya Machi 1861 hadi alipouawa Aprili 1865.

Watu imara hujenga mifumo imara

Ni wazi kuwa, na kwa kuzingatia mifano hiyo hapo juu, mifumo imara haijizai, hujengwa na watu, hujengwa na viongozi imara, wenye kuthubutu na maono, hujengwa na viongozi ambao wanayatazama mataifa yao kwa miaka 500 ijayo, vizazi na vizazi vya kesho kuliko leo. Ikiwa nchi yenu inabahatika kupata kiongozi ambaye mnakubaliana hadharani au sirini kuwa ni kiongozi imara, asiyeyumba, mwenye dira na maono – huo ni wakati mzuri wa kumsukuma na hata kusaidiana naye kujenga mifumo imara ndani ya nchi yenu.

Tanzania inaweza kutumia juhudi za sasa za Rais Magufuli, kuzichambua na kuchukua maeneo imara, ambayo ni mengi na kuyatumia kama mifano chanya ya kuiingiza kwenye kitabu cha kudumu cha mfumo wa uendeshaji wa nchi yetu.

Mbinu zinazotumiwa na uongozi wa awamu hii katika ubunifu, utekelezaji na usimamiaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, zingelitumiwa na kila awamu tangu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, leo hii tungelikuwa mbali sana.

Leo hii tusingelikuwa tunajenga reli wala kufufua shirika la ndege, maana hiyo kazi ingelifanywa wakati wa Mwinyi au Mkapa, leo hii tusingelikuwa tunatafuta umeme wa uhakika katika nchi yetu maana kazi hiyo ingelifanywa na awamu ya Mkapa au Kikwete.

Mchango wa marais wastaafu

Simaanishi kwamba Mwinyi, Mkapa na Kikwete hawakuwa viongozi imara, la hasha. Namaanisha kuwa, kama viongozi wa awamu hizo wangelitumika vizuri nyakati zao, masuala makubwa yakaibuliwa na kusimamiwa na kwamba utaratibu huo wa kuibua masuala hayo, kuyatekeleza na kuyasimamia ungelikuwa ni utaratibu wa kimfumo, leo tungelikuwa tunaulizana namna bora ya kufanya uwekezaji kuliko kutafuta umeme wa kudumu.

Kama hatukuwatumia watu imara kujenga mifumo imara wakati wa Mwinyi, Mkapa na Kikwete, hatuna budi kufanya hivyo hivi sasa ambapo hatupingani kwenye hoja kuwa nchi yetu inahitaji kujenga mifumo imara.

Kwa sababu tunakubaliana kuwa mifumo imara haishuki kutoka mbinguni, kwamba inajengwa na viongozi wenye maono, uthubutu na uimara, basi jambo hilo tunapaswa kulifanya hivi sasa, wakati ambapo nchi inaye kiongozi anayethubutu na mwenye uimara wa kutenda lolote lile ilimradi kiu yake ya kuona taifa lenye maendeleo inafikiwa.

Mifano dhahiri

Kwa mfano, mtindo wa utendaji wa sasa wa Serikali ambapo urasimu umepunguzwa, siyo jambo linalopaswa kuishia na uongozi wa JPM, linapaswa kuwa la kudumu, lizamishwe kwenye mfumo wa utendaji wa Serikali na kusiwepo na mkuu yeyote wa nchi ambaye atakuja kulivunja baada ya JPM, sanasana kila kiongozi ajaye baada ya JPM awe na kazi ya kukazia hapohapo au kuongeza utendaji wa Serikali isiyo na urasimu kupita kiasi.

Kwa mfano, mtindo wa sasa wa uibuaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo baadaye hugeuka kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kama ujenzi wa reli ya kisasa, ufufuaji ATCL, Mradi wa Umeme wa Stiegler na Ujenzi wa Bomba la Mafuta Uganda hadi Tanga – vinapaswa kuwa masuala ya kudumu. Yaani, utawala wa sasa wa JPM ubuni miradi mingine mikubwa na kuiwekea misingi ya utekelezaji ndani ya miaka mitano ijayo, kumi, ishirini, thelathini na zaidi ya hapo.

Mifumo imara na maono ya mbele

Maono ya sasa ya mahitaji ya taifa lenye maendeleo yaanze kujengewa misingi isiyofutika, akiondoka JPM madarakani, Rais ajaye na uongozi wake ajue ya kwamba yako masuala makubwa yanayopaswa kusimamiwa na utawala wake na kwamba masuala hayo ndiyo ajenda za kitaifa na vipaumbele vya maendeleo ya viongozi na uongozi wowote ujao.

Rais ajaye atakuwa na chaguo pia la kuanzisha masuala yake, lakini kwa vyovyote vile hataweza kutikisa ile miradi mikubwa ambayo ni vipaumbele vya taifa kwa wakati aliokabidhiwa nchi. Kwa mfano, tukiwa na mfumo imara itatusaidia ndani ya muda mfupi ujao tuwe na Reli nyingine za kisasa kutoka Kagera hadi Mara, Mara hadi Arusha, Arusha hadi Tanga, Tanga hadi Dar es Salaam, Dar res Salaam hadi Mtwara, Mtwara hadi Ruvuma hadi Mbeya, Mbeya hadi Iringa hadi Kagera.

Naam, kama leo tunaweza kujenga reli ya kisasa kutoka Dar hadi Mwanza na huenda Tabora hadi Kigoma, kwa nini awamu ijayo isiwe na malengo ya kutujengea reli nyingine ya kisasa kutoka mikoa kadhaa kwenda mikoa mingine? Lazima tuwe na mikakati endelevu katika taifa, lakini hatutaweza kujenga mikakati hiyo na kuitekeleza ikiwa hatutatumia faida ya kuwa na kiongozi imara kujenga mifumo imara wakati wake.

Shughuli endelevu

Suala la ujenzi wa mifumo imara siyo kazi ya utawala mmoja, walau mtawala mmoja na awamu yake hujenga msingi imara kwa baadhi ya masuala kama anavyofanya JPM kwenye maendeleo, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, matumizi mbaya ya fedha za umma na mambo kama hayo.

Utawala wa JPM ukiondoka, ukija utawala ambao hautakuwa umejengewa mipaka, tusishangae Tanzania ikarudi enzi za rushwa na ufisadi mkubwa, enzi za kusimamia miradi ya maendeleo ya kugusagusa, enzi za urasimu mkubwa kwenye sekta za umma na mengineyo.

Kwa kadri tunavyokosa muunganiko kati ya kiongozi imara, mifumo imara na uongozi unaofuatia baada yake ndivyo ambavyo tunazidi kuchanganyikiwa katika kuifanyia kazi dhana ya ujenzi wa mifumo imara.

Kwa kadri tutakavyoweza kujenga muunganiko kati ya viongozi imara tulionao kama JPM kwa kuwekeza matokeo ya uthubutu wao wa maendeleo kwenye mifumo yetu na kuiwekea kingo mifumo hiyo wakati tunakabidhi madaraka kwa viongozi wanaofuatia, ndivyo tutakavyoweza kutegua kitendawili cha ujenzi wa mifumo imara.

Ndiyo maana nikasema, kipindi cha 2020 – 2025 tuwekeze kwenye ujenzi wa mifumo imara. Mada hii inaweza kuwa ngumu sana, lakini hatukwepi kuijadili. Nilichofanya ni kuihitimisha kwa kufungua mjadala zaidi.

Julius Mtatiro ni mtafiti na mchambuzi wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mwanasheria, mfasiri na mtaalamu mshauri wa miradi, mtawala na mera. Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com)

Sunday, September 23, 2018

Kusahaulika vipaumbele muhimu vya bajeti kijinsiaTumaini Msowoya

Tumaini Msowoya 

Unapotaja neno ‘jinsia’ watu wengi huwa wanadhani ni suala la wanawake. Hata pale wanaharakati au wanasiasa wanapopiga kelele kuhusu upangaji wa bajeti yenye mtizamo wa kijinsia, bado fikra za watu wengi huwa zinawapeleka kwa ‘wanawake’.

Wachambuzi wa masuala ya kijinsia wanasema hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa kama upangaji wa bajeti hautaweza kuzingatia mlengo wa kijinsia, lakini hawamaanishi ‘mtazamo wa wanawake’.

“Hapa tunazungumzia makundi yote muhimu, yaani wanawake, wanaume, watoto, wenye ulemavu, wazee na vijana. Si wanawake peke yao,” anasema Mkuu wa Idara ya Maarifa, tafiti na uchambuzi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Happy Maruchu.

Mwanaharakati huyo wa masuala ya jinsia, anasema: “Ukipanga bajeti bila kujua mahitaji halisi ya makundi hayo, yaani kwa kuzingatia, tofauti za kimajukumu na kimahusiano ya makundi hayo, huwezi fikisha lengo.”

Uelewa mdogo kuhusu bajeti yenye mtazamo wa kijinsia ndiyo unaoilazimisha TGNP kuwakutanisha madiwani wa halmashauri mbalimbali za wilaya, manispaa na majiji nchini ili kuwanoa.

Baada ya kupata ujuzi huo, baadhi ya madiwani wanakiri kuwa walikuwa wanakosa uelewa mzuri kuhusu namna gani bajeti inaweza kuandalia kijinsia.

Wanasema dhana kwamba ‘bajeti inalenga wanawake peke yao’, ndiyo iliyokuwa inaleta ukakasi na kuwafanya wengi wasielewe.

Lakini, wale wanaoelewa kuhusu upangaji wa bajeti kwa mtizamo wa tofauti za makundi kimajukumu wanakiri kuwa imesaidia kuleta maendeleo chanya kwenye wilaya zao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anasema mipango ya maendeleo kwa nchi nyingi hasa zinazoendelea zinafuata mfumo dume ambao umekuwa ukitumiwa kuweka vipaumbele bila kufuata makundi maalumu, yakiwamo ya watu wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Diwani wa viti maalumu katika Manispaa ya Ilala, Sada Mandwanga anasema ‘bajeti yenye mtizamo wa kijinsia’ ni suala geni kwake, hivyo anahitaji kujifunza zaidi.

“Binafsi ndio najifunza sasa kuhusu hili jambo, zamani nilijua ukisema jinsia basi ni wanawake na wasichana peke yao,” anasema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mwalingo Kisemba baada ya kuanza kuzingatia usawa kijinsia katika uandaaji bajeti, wameweza kutafiti na kujua mahitaji ya msingi ya makundi maalumu na hivyo kuyapa kipaumbele.

“Kwetu shida ilikuwa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule za sekondari, tukagundua wanaoathirika zaidi ni wasichana. Wakati tunapanga bajeti, tulichukua jambo hilo kwa kipaumbele na tayari, tumejenga mabweni tisa katika shule tisa kati ya 28 zilizopo,” anasema Kisemba.

Maruchu anasema wameamua kuwanoa madiwani ili kuondoa dhana kwamba jinsia ni jambo linalohusu wanawake peke yao, pili, kuona wanao wajibu kushiriki kikamilifu kutafiti, kujua vipaumbele, kupanga na kupitisha bajeti zikiwa na mtizamo kijinsia.

“Bajeti yoyote lazima ianzie ngazi ya chini, tumewaita nyie madiwani kwa sababu mnatoka kwenye kata na mnaweza kufikia mitaa na vijiji. Kaanzieni kule kuandaa bajeti mkitizama haya makundi,” anasema.

Sababu za bajeti kijinsia

Maruchu anasema sababu za kuzingatia jinsia wakati wa kupanga bajeti za serikali ni pamoja na kuyapa makundi maalum fursa ya kupata huduma za afya, elimu na maji.

Ofisa huyo wa TGNP anasema kiuhalisia ni rahisi kupata maendeleo na kufikia uchumi ikiwa bajeti inayotengwa itazingatia makundi hayo.

“Kwa hiyo bajeti yoyote inayopangwa ni lazima iwe na mtizamo wa kijinsia, ianzie ngazi ya chini na nyie madiwani ndio viungo muhimu katika upangaji huo, hata hivyo hatua ambayo Tanzania tumefikia kwa sasa sio mbaya, tumeweza kuanza,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya bajeti, Geofrey Chambua anasema bajeti hiyo ndiyo inayolazimisha waandaaji kufanya tafiti ili kujua mahitaji ya jamii husika kabla ya kupanga vipaumbele.

“Tunapotaja waandaaji madiwani ni watu muhimu, ndio wanaopitisha bajeti kwenye halmashauri na ndio wanajua wananchi wao kwenye kata wana shida gani,” anasisitiza Chambua.

Anasema bajeti yenye mlengo wa kijinsia ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yoyote ile kama wapangaji wataweza kujikita katika hiyo.

“Bajeti hii ndiyo inayotazama maeneo muhimu na namna ya kupanga vipaumbele, madiwani lazima wajue hali halisi ya makundi kwenye kata na ni nini hasa mahitaji yao ya msingi ili waweze kupanga bajeti.

Kuandaa bajeti kijinsia

Chambua anasema hatua ya kwanza ya kuandaa bajeti hiyo ni kwa waandaaji kujua mahitaji ya makundi maalumu yaliyo kwenye maeneo yao. “Ukishajua makundi na mahitaji yao utaangalia nini kipaumbele katika yote uliyojua,” anasema.

Anasema wakati vipaumbele vinapoangaliwa, ni muhimu kuoanisha na bajeti ya kipindi cha nyuma kujua utekelezaji wake hasa kwenye vipaumbele vilivyoibuka ulikuwaje.

“Ni jambo moja kutenga bajeti ya ujenzi wa bweni, lakini ni jambo la pili kujua bweni hilo limesaidia nini? Limepunguza tatizo lililokuwapo? Bajeti inayofuata iweje? Haya ni mambo muhimu mno,” anafafanua.

Wilaya zilizoweza

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo anasema katika utafiti wao walibaini kundi la vijana linahitaji upekee zaidi katika upangaji wa bajeti kutokana wengi kukosa ajira.

“Kwa hiyo tukakubaliana kuhakikisha sio tu kwamba wanapewa mikopo, bajeti watakayotengewa isaidie kuwaandalia mazingira mazuri ya kujikwamua kiuchumi,” anasema.

Anasema kwa kutumia asilimia nne inayotengwa na halmashauri kwa ajili ya vijana, walifanikiwa kutenga bajeti iliyoanza kuzaa matunda.

“Tumekwishatoa mikopo ya Sh160 milioni kwa makundi maalum wakiwemo vijana, tuna uhakika vijana wakiweza kuzalisha uchumi wao watainua maendeleo ya wilaya yetu,” anasema.

Halmashauri ya Morogoro haitofautiani na ile ya Mbeya ambako wanasema baada ya utafiti walibaini wanaweza kumaliza tatizo la mimba shuleni ikiwa yatajenga mabweni kwa ajili ya watoto wa kike.

Anasema walibaini pia wengi wanakatisha masomo kwa kutokana na umbali kutoka nyumbani hadi shule, waliamua kuandaa bajeti ya elimu kuzingatia jinsia.

Nini kifanyike

Akitoa mapendekezo ya nini kifanyike, Dk Sanga anasema jambo la msingi ni kuwajengea uelewa viongozi wa kuchaguliwa kwa sababu ndio wanaopewa rungu la kuongoza vikao vya bajeti.

“Kijijini anayesimama kuongoza kikao ni mwenyekiti wa kijiji, kata ni diwani na halmashauri ni mwanasiasa yuleyule wa kuchaguliwa ndiye kiongozi, bila wao kuelewa bajeti inayotengwa haiwezi kunufaisha makundi yote muhimu,” anasema.

Anasema mafunzo hayo lazima yafanyike kwenye mabaraza ya madiwani na kata ili kila mmoja wao ajue wapi anaweza kuanzia.

“Ukisema jinsia unaweza kupuuzia, lakini ikitokea mama akatumia saa nne kuchota maji kwa sababu ya umbali, sio tu umemuathiri yeye bali maendeleo ya kijiji, kata, wilaya na taifa,” anasisitiza.

Diwani Wa kata ya Kivule, Wilson Mollel anasema kama viongozi wa siasa watakuwa wanajengewa uelewa baada ya kuchagulia na kuanza kuingia vikao vya bajeti wataweza kufikia malengo ya mtizamo huo.

Wednesday, September 19, 2018

Uhusiano kati ya Mkurugenzi wa halmashauri, Mkuu wa wilaya

 

By Padri Privatus Karugendo.

Tumeshuhudia kutoelewana kati ya baadhi ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi wao. Pia, wakati mwingine kuna magomvi kati ya mwenyekiti wa halmashauri na wakuu wa wilaya au wakurugenzi. Ikitokea viongozi hawa wakawa wanatoka vyama vya siasa tofauti, hali inakuwa mbaya zaidi. Jambo hili tunaliacha kuendelea bila kulitolea ufumbuzi na ikitokea likawa miongoni mwa viongozi vijana: Sote tunajua kwamba taifa letu litajengwa na vijana; matumaini yetu yote na uhai wa taifa letu la leo, kesho na vizazi vijavyo yako mikononi mwa vijana wetu. Ni muhimu vijana hawa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya uongozi ili kuboresha uongozi wa taifa letu na kupanda matumaini mapya kwenye taifa letu.

Watoto wetu, wanaona yanayotendeka! Wakigombana mkuu wa wilaya na mkurugenzi na kurushwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, tunakuwa tunawafundisha nini watoto wetu. Ni kitu tunafundisha? Ni matumaini yapi tunayapandikiza miongoni mwa watoto wetu na taifa la kesho? Tusiwe wabinafsi, kwa kuangalia maisha yetu ya leo, ni muhimu pia kufikiria Tanzania ya kesho!

Katika ngazi ya wilaya, kuna viongozi watatu wazito. Mkuu wa wilaya, mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri. Na mara nyingi wananchi wanachanganyikiwa kutofautisha nafasi na umuhimu wa kila mmoja katika nafasi yake. Daima swali linakuwa ni nani kati yao mwenye madaraka makubwa zaidi ya mwingine na je, ni nani kati yao watatu anawajibika kwa nani? Je, hawa wanafanya kazi vipi bila migongano? Je, hawa wanaimarisha serikali za mitaa? Je, wananchi wanafahamu tofauti na umuhimu wa kila mmoja? Je, wao wanafahamu nafasi zao na wajibu zao bila kuingilia mwingine?

Serikali ya awamu wa nne, ilifanya jitihada kubwa kuendesha semina elekezi, ili kuondoa utata huu. Mfano, mwezi wa nane 2006, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kule Dodoma, iliendesha mafunzo ya awali ya wakurugenzi wapya wa halmashauri. Kati ya yale yaliyofundishwa ni uhusiano kati ya mkurugenzi wa halmashauri, mkuu wa wilaya na mwenyekiti/meya wa halmashauri. Bahati mbaya semina hizi zinafanyika kwa viongozi tu! Wananchi hawajapata mafunzo haya, ingawa ni muhimu pia na wao kufahamu mambo mbalimbali yanayohusu serikali za mitaa. Hivyo, lengo la makala hii ni kuwamegea wananchi baadhi ya mambo muhimu katika serikali zao za mitaa. Na leo ninawamegea uhusiano kati ya mkurugenzi wa halmashauri, mkuu wa wilaya na mwenyekiti/meya wa halmashauri. Ninabaki na matumaini kwamba siku za mbele Serikali itafanya mpango wa kuendesha semina kwa wananchi, hasa kwenye ngazi ya Vijiji na Mitaa, ili kuwaelimisha juu ya mambo mbalimbali ya serikali za mitaa.

Pia, ni matumaini yangu kwamba kwa vile sasa hivi migongano hii imejitokeza kwa nguvu. Kuna ulazima wa Serikali kurudi tena mfumo huu wa semina elekezi, kuwafundisha viongozi vijana juu ya mfumo wa utawala na uongozi katika ngazi ya wilaya. Kuna ngazi nyingi za utawala na uongozi, lakini leo nimeanzia kwenye wilaya, maana ngazi hii imeonyesha kuwa na migongano mingi. Ni ngazi ya utawala na uongozi ambayo viongozi na wananchi wanahitaji semina na mwongozo juu ya mfumo huu.

Majukumu ya msingi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na kudumisha amani na usalama baina ya raia wake, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kutoa huduma bora kwa wakazi wake. Na hili, kama anavyosema kila mara Rais John Magufuli, hayana vyama. Ni kwa Watanzania wote. Na hili lisisemwe tu kama wimbo, bali liingizwe kwenye matendo. Kwa kiasi kikubwa, jukumu la kuwaendeleza watu kiuchumi, kijamii na kuwapa huduma bora, limepewa Serikali za mitaa. Katika ngazi ya wilaya, ndiyo mahali ambapo sera na majukumu ya Serikali yanayolenga katika kuwahudumia wananchi zinatekelezwa. Kwa maana nyingine, ngazi hii ina umuhimu wa pekee katika kuhakikisha kuwa majukumu haya yanafanikiwa. Mkuu wa wilaya ndiye mwakilishi wa Rais na mtendaji mkuu wa Serikali kuu ambapo mtendaji mkuu katika halmashauri ni mkurugenzi wa halmashauri. Meya/ mwenyekiti wa halmashauri ni kiongozi wa kisiasa na kiungo cha wawakilishi wa wananchi.

Sheria za nchi zimebainisha majukumu ya Serikali kuu na yale ya Serikali za mitaa katika ngazi hii ya wilaya. Ni muhimu kila upande ukatoa ushirikiano ili kuiwezesha sheria kuchukua mkondo wake katika hali ya amani na ushirikiano. Mfano, uwezo wa mkuu wa wilaya kwa mujibu wa sheria za Serikali za mitaa, uko kwenye sheria Na.19 ya G.A. at District Level Part III (Pg 407), Sheria Na.8 ya 1982 kifungu Na. 78A na kanuni za kudumu za halmashauri.

Pia, kuna uhusiano kwa mujibu wa miongozo ya kiutawala. Kuna mwongozo wa namna ya kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wanaofanya kazi katika mamlaka za Serikali za mitaa (Barua Na. AB.110/112/01 ya tarehe 12.05.06).

Para 4.1.1 “ Pale halmashauri inapomtuhumu mtumishi anayefanya kazi katika halmashauri na ambaye mamlaka yake ya nidhamu sio halmashauri, mwenyekiti wa halmashauri anatakiwa kuwasilisha tuhuma hizo kwa mkuu wa wilaya ambamo halmashauri hiyo imo na mkuu wa wilaya atamjulisha mkuu wa mkoa haraka iwezekanavyo.”

Licha ya viongozi hawa wawili kuongozwa na sheria katika uhusiano wao, busara na hekima zinawataka kujenga ushirikiano mwema kati yao kwa vile malengo tarajiwa ya sehemu wanazoziongoza zinalenga wananchi walewale wa eneo wanalofanyia kazi. Na hapa neno la kuzingatia ni “ hekima na busara”. Uwazi na uwajibikaji kwa pande zote mbili ukiambatana na kuheshimiana utaweka mazingira mazuri kwa utekelezaji wa majukumu yao.

Maeneo ambayo yanaweza kusababisha uhusiano mbaya kati ya mkurugenzi wa halmashauri na mkuu wa wilaya ni pamoja na:-

-Serikali za mitaa zimepewa madaraka ya kujiamulia mambo yake wenyewe bila ya kuingiliwa ili mradi sheria na miongozo ya kitaifa inafuatwa. Eneo hili limekuwa likitafsiriwa vibaya na baadhi ya wakurugenzi kwa kufanya maamuzi ambayo hayana tija kwa halmashauri;

-Kwa upande wao wakuu wa wilaya wamekuwa na shauku kubwa kama wakuu wa Serikali na wawakilishi wa Rais ya kuhakikisha kwamba halmashauri zao zinafanikiwa katika kutekeleza majukumu yake;

-Serikali kuu kutopeleka fedha na vitendea kazi vya kutosha kwa wakuu wa wilaya na hivyo kuzifanya ofisi zao kuwa tegemezi/ombaomba kwa wakurugenzi wa halmashauri na hivyo kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao. Hali hii inashusha hadhi ya mkuu wa wilaya mbele ya mkurugenzi;

-Kukosekana kwa taratibu za wazi za kiutawala za maandishi zinazoongoza mahusiano baina ya viongozi hawa. Mara nyingi viongozi hawa wamekuwa wakiongozwa kwa njia ya muafaka ziadi kuliko taratibu zilizowekwa.

Ili kuhakikisha kuwa kuna mahusiano mazuri kati ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri ni lazima kuzingatia yafuatayo :-

-Kila upande uhakikishe unatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa manufaa ya wananchi kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizopo;

-Serikali kuu iziimarishe Ofisi za Wakuu wa Wilaya kwa kuzipa fedha na nyenzo za kutosha ili kumwezesha mkuu wa wilaya kutekeleza majukumu yake ya kiserikali;

-Jitihada zifanywe za Kutoa miongozo ya maandishi inayobainisha nani afanye nini katika masuala ya kiutawala na

-Kila upande uweke mazingira mazuri ili kumwezesha mwenzake kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wa majukumu ya msingi ya mwenyekiti/meya ni kama ifuatavyo :- Yeye ndiye mwenyekiti wa baraza la madiwani. Kikao cha baraza la madiwani ni kikubwa kuliko vikao vyote katika halmashauri; Ni kiongozi mkuu wa kisiasa wa halmashauri; Ni kinara wa sherehe za halmashauri na yeye ndiye hutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa shughuli za halmashauri mwishoni mwa kila mwaka akionyesha shughuli zilizotekelezwa, mafanikio na matatizo yaliyojitokeza.

La kukumbuka ni kwamba meya/mwenyekiti si mfanyakazi wa halmashauri. Mfumo wa Serikali za mitaa uliopo hapa nchini hauruhusu meya/mwenyekiti wa halmashauri, wala diwani yeyote kuwa na madaraka ya kiutendaji (Tazama Kanuni za Maadili ya Madiwani aya ya 25 na 27). Ni watumishi na wala si madiwani wanaotekeleza.

Ili kudumisha uhusiano mwema kati ya meya/mwenyekiti na mkurugenzi wa halmashauri, meya/ mwenyekiti asijihusishe na shughuli za utendaji kazi wa kila siku. Ni kwa sababu hii na sababu nyinginezo za kiuchumi, wizara yenye dhamana ya Serikali za mitaa ilielekeza wenyeviti na mameya wawe ofisini siku mbili kwa wiki ili kupunguza migongano.

Uhusiano mzuri na thabiti kati ya viongozi hawa watatu (Mkuu wa wilaya, mwenyekiti/meya wa halmashauri na mkurugenzi wa halmashauri) ni nyenzo na hitaji muhimu siyo tu kwa amani na utulivu katika wilaya, bali kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wilaya na halmashauri husika. Hivyo ni muhimu kabisa kuwa na mahusiano mazuri kati yao.

Padri Privatus Karugendo.

+255754633122

pkarugendo@yahoo.com

Wednesday, September 19, 2018

Tume Huru ya Uchaguzi mwarobaini wa kuzuia mawakala wa upinzani

 

By Tausi Mbowe na Kalunde Jamal, Mwananchi

Ni malalamiko yasiyokoma. Kila uchaguzi yanajitokeza ama kwa sura ileile au kwa namna tofauti. Ni suala la mawakala wa vyama vya upinzani, hasa Chadema, kukataliwa kwenye vituo vua kupigia kura.

Lilianza kujitokeza zilipoanza chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Tatizo kubwa lilianza kuonekana katika uchaguzi wa jimbo la Kinondoni mkoani Dar es Salaam, limeendelea katika majimbo mengine na kata zilizofanya uchaguzi baadaye. Inavyoelekea ni malalamiko ambayo hayatokama leo wala kesho.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikidai kwamba ama mawakala wake wananyimwa hati za viapo, au barua za utambulisho zinazotakiwa kuonyeshwa kwa wasimamizi wa uchaguzi. Mara nyingine hati hizo hucheleweshwa na kupatikana baadaye wakati uchaguzi unaendelea.

Madai mengine ambayo hata hivyo yanakanushwa na mamlaka zinazohusika ni kuwa, mawakala wengine hukamatwa na polisi siku moja kabla au siku ya uchaguzi ili wasiwepo vituoni.

Katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita wilayani Monduli, yaliibuka mapya kwamba baadhi ya mawakala walitekwa na kushikiliwa kusikojulikana na gari la mbunge lililokuwa linasambaza wengine lilivamiwa na kutobolewa matairi kwa risasi. Polisi wanasema si risasi ni kitu chenye ncha kali kama kisu au bisibisi.

Mwisho wa matukio hayo ya kuzuiwa mawakala wa upinzani ni kituo cha kupigia kura kubaki na mawakala wa chama tawala pekee, wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Jambo linalowaliza wapinzani kuamini kwamba kura zao haziwezi kubaki salama bila zikiwa mikononi mwa washindani wao pekee.

Wakati Chadema na wapinzani wengine wakiendelea kulalamikia kwa kufanyiwa vitendo hivyo, wasomi na wanasiasa wameeleza kuwa sababu za matukio ni kutokuwapo Tume Huru ya Uchaguzi.

Sababu hiyo imeelezwa siku mbili baada ya uchaguzi uliofanyika Jumapili ukihusisha wabunge wa majimbo ya Ukonga, Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha na madiwani wa kata 23 na CCM imenyakua yote.

Kama ilivyokuwa kwa chaguzi zilizotangulia, Chadema imelalamikia vitendo vya mawakala wake kunyimwa fomu, hati za viapo pamoja na barua za watendaji.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Athumani Kihamia alipoulizwa jana kuhusu kujirudia kwa tatizo hilo na kwa nini linatokea tu kwa wapinzani, alisema “Niko hospitali, mtafute mwenyekiti wa Tume, Jaji Semistocles Kaijage, ambaye hata hivyo hakupatikana.

Hata hivyo, Akizungumza na Mwananchi Jumapili wakati uchaguzi unaendelea, Kihamia alikiri kupokea malalamiko kuhusu kukataliwa kwa mawakala katika majimbo ya Monduli na Ukonga na kuwa alikuwa ameyafanyia kazi.

“Hata huku Monduli niliko lilikuwapo, nimelifanyia kazi mimi mwenyewe na sasa kila kitu kinakwenda sawa. Hata hivyo, Mnyika hajarudi kwangu, kwa hiyo ni dhahiri hakuna tena tatizo, maana nilimweleza kama bado kuna shida anijulishe,” alisema Kihamia.

Hata hivyo, baadaye mchana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alipotembelea vituo vya uchaguzi katika Jimbo la Ukonga alikanusha madai kuwa mawakala wamezuiliwa kuingia vituoni huku akikiri kuwapo na idadi ndogo ya wapiga kura.

Alisema katika majimbo yote ya Monduli na Ukonga uchaguzi ulianza kwa wakati na ulikuwa unaendelea vizuri.

Alisema katika jimbo la Monduli lenye vituo 256 ni mawakala wanne tu walizuiliwa kuingia vituoni na ni kwa sababu za msingi.

“Hao mawakala wanne walizuiliwa kwa kuwa hawakutambuliwa na msimamizi, hawakuapishwa walikwenda kwa niaba ya wengine. Hizi habari zinazosambazwa kuwa mawakala wote Monduli wamezuiliwa si kweli watu wasisambaze taarifa ambazo hawana uhakika nazo. Naona kila kitu kinakwenda sawa hakuna wakala aliyezuiliwa na kama hajafika ni kwa utashi wake.”

Uzoefu wa Dk Bisimba

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi, Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema mara nyingi madai ya mawakala kunyimwa fomu, hati za viapo na barua za utambulisho kutoka kwa watendaji hutokea kwa vyama vya upinzani pekee kwa sababu hiyo ni mbinu chafu za kuharibu uchaguzi.

“Mara zote kunakuwa na hila za wazi katika vituo ili kuharibu uchaguzi na CCM ionekane imeshinda jambo ambalo si sahihi,” anasema Dk Bisimba.

Dk Bisimba anakumbushia tukio la mwaka 2017 alipokuwa mwangalizi wa uchaguzi mdogo Katika Jimbo la Kinondoni, kuwa vitendo hivyo vilikithiri.

“Bahati nzuri mimi nilishawahi kuwa mwangalizi wa hizi chaguzi ndogo, nilishuhudia figisufigisu nyingi ikiwamo hilo la mawakala kuwekewa vigingi. Nakumbuka nikiwa katika Kata ya Magomeni kituo cha kupiga kura cha Magomeni Kondoa mawakala wa Chadema walizuiliwa kuingia ndani mpaka saa 9:00 mchana kwa kisingizio cha kutokuwa na barua zilizopaswa kuwa nazo,” aliongeza.

“Lakini cha kushangaza ilipofika saa 9, alikuja mgombea wa Chadema, Salimu Mwalimu na kuomba kukagua barua walizokuwa nazo CCM, ndipo alipogundua hazikuwa na tofauti yoyote na zile walizokuwa nazo wenzao wakaruhusiwa kuingia lakini muda ulikuwa umeshaisha,” alisisitiza.

Dk Bisimba alisema alishuhudia kuna maeneo mengine wapinzani wakizuiliwa kuingia ndani na vituo, hawakujitokeza watu kupiga kura, lakini jioni wakati wa kuhesabu zilipatikana kura nyingi.

Dk Bisimba analaani vitendo hivyo na kusema kuwa havihashirii uwapo wa demokrasia ya kweli kwa kuwa havitoi haki sawa kwa vyama vyote.

Kufuatia hali hiyo Dk Bisimba anashauri wapinzani kutokaa kimya, badala yake wafuate taratibu za kisheria ikiwamo kwenda mahakamani.

“Bahati mbaya sasa nimeona Watanzania wamekata tamaa na matokeo yake wameamua kutojitokeza kupiga kura, hili halisaidii badala yake wapinzani wanatakiwa kuhakikisha wanadai haki hiyo kwa nguvu zote,” aliongeza.

Hata hivyo, Dk Bisimba anaonya kuwa vitendo hivyo endapo vitaendelea itasababisha mtafaruku mkubwa kwani ipo siku Watanzania watachoka na kuripuka.

Ukiacha ya Dk Bisimba, Wakili Peter Mshikilwa anasema vitendo hivyo vinafanywa kwa vyama vya upinzani kwa sababu hakuna Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itafanya kazi bila kuwa na wasiwasi wowote.

“Lazima utii mamlaka iliyokuchagua ndiyo kinachoonekana kwa Tume yetu ya uchaguzi, kukiwa na Tume huru kila kitu kitaenda sawa na haya hayatajitokeza,” alisisitiza Mshikilwa.

Wakili huyo alisema ili kuepukana na vitendo hivyo, kuna vitu vitatu ambavyo wapinzani wanaweza kuvifanya na kupata suluhisho la kudumu.

Mosi, anasema jambo la kwanza ni kwa wapinzani wanapaswa kulalamika mahakamani juu ya vitendo anavyofanyiwa na mahakama ikatoa tafsiri ya kisheria.

Pili, wapinzani wanaweza kutumia Mahakama kupinga matokeo hayo badala ya kuendelea kulalamika bila kuchukua hatua.

Tatu, ni kuwapo mpango wa muda mrefu wa kudai Tume huru ya uchaguzi.

“Sasa Tanzania hatuna Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na hili linaweza kupatikana kama wapinzani wakiamua kushinikiza

Ili kuhakikisha inapatikana kama ilivyo kwa jirani zetu Kenya ambako wameweza kupata suluhisho la kudumu,” alisisitiza.

Hata hivyo, CCM inasema suala la mawakala kupata matatizo si kwa wapinzani pekee bali pia mawakala wake hukumbwa na kadhia kama hiyo.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole anasema, “Ungekuwa umetaja maeneo maalumu ningeuwa kwenye nafasi nzuri ya kujibu, ukisema kwa ujumla si sawa, kwa sababu kuna mahali hata mawakala wa CCM walizuiliwa,” anasema Polepole.

Hoja tofauti ya Profesa Safari

Akizungumzia hilo Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari anasema vikwazo wanavyowekewa mawakala wa upinzani ni kwa sababu hakuna uchaguzi wa kweli.

Profesa Safari ambaye pia ni mwanasheria anasema kutokana na hali hiyo yeye haoni sababu za kwenda katika chaguzi hizo na badala yake wawaachie CCM pekee washiriki.

“Nilishawahi kusema kwamba msimamo wangu sioni sababu ya kuendelea kushiriki chaguzi hizi kwani ni fake (za kuigiza) na leo hii inadhihirisha kwamba chama tawala kinatumia kila njia kuhakikisha kinashinda kwa hila,” alisisitiza.

Alipoulizwa kwamba haoni kususia uchaguzi kunawanyima wapigakura kutumia haki yao kuchagua, makamu huyo mwenyekiti wa Chadema alisema haoni sababu ya kujidanganya kwamba wanapata haki yao ilhali hakuna usawa.

“Ni bora wakatulia nyumbani kuliko kushiriki kufanya maigizo,” anasema.

Akichangia mada hiyo, Waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema naye hali hiyo inatokana na kutokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

“Tunachofanya sasa ni maigizo tu, haiwezekani Mkurugenzi wa halmashauri kuwa ndiye msimamizi wa uchaguzi ukategemea kuwe na uchaguzi huru, hawa watu wanaripoti kwa Serikali kamwe hawezi kufanya vinginevyo,” anasisitiza Kasaka.

Kasaka anasema nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania wapinzani wamekuwa wakishindana na Serikali badala ya kushindana na chama tawala.

“Nchi nyingi zimeshindwa kutengeneza mpaka wa Serikali na chama tawala, matokeo yake vyama vya upinzani vinajikuta vikipambana na Serikali badala ya chama tawala ndiyo maana unakuta Tume haitendi haki,” aliongeza.

Wednesday, September 19, 2018

Ziko wapi mbinu na sera za kudhibiti kisukari

Kifaa cha kupima kiwango cha sukari kwenye damu

Kifaa cha kupima kiwango cha sukari kwenye damu ya mgonjwa wa kisukari kwa lengo la kudibiti kwa haraka madhara ya ugonjwa huo kama kiwango cha sukari mwilini kitakuwa kikubwa.Picha ya maktaba 

By Salim Said Salim

Taarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa ugonjwa wa kisukari unakuwa kwa kasi na kwa hivi sasa ndio maradhi yanayoongoza kwa watu kupoteza maisha Zanzibar.

Unapokwenda katika vitengo vinavyohudumia watu wanaosumbuliwa na maradhi haya katika miji na vijiji vya Unguja na Pemba unapata mshituko.

Hapo unawakuta watu wengi, wakubwa, vijana na watoto wakisubiri kupatiwa huduma za vipimo, dawa au ushauri.

Utafiti wa mwaka 2001 ulionyesha asilimia 3.7 (watu 37 kwa kila 1,000) wa Zanzibar walikuwa wanasumbuliwa na ugonjwa huu na utafiti kama huo wa mwaka 2014 umeonyesha watu wanaougua maradhi haya imeongezeka kwa zaidi ya mara mbili na kufikia asilimia 7.9, kama wanane kwa kila watu 100.

Taarifa hiyo ya kutisha imeeleza kwamba wagonjwa wapya wapatao 40 hupokelewa katika hospitali sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba kila mwezi. Robo ya hao wagonjwa ni watoto wadogo.

Siku hizi utaona watu wengine walioathirika na ugonjwa wa kisukari wamekatwa miguu kunusuru maisha yao ili kuzuia ugonjwa huo usisambae zaidi mwilini.

Hii ni hatari kubwa na si ajabu ukifanyika utafiti mwingine katika miezi michache ijayo tukaambiwa sasa idadi ya wagonjwa wa kisukari ni asilimia 10.

Hili ni tatizo ambalo linapaswa kupewa umuhimu mkubwa kulipatia ufumbuzi na si tu kwa kuwapatia dawa wagonjwa, bali kwa kutafuta kiini chake cha ongezeko hili la kutisha la ugonjwa huu na kuchukua hatua zipasavyo kuudhibiti.

Ukiangalia kumbukumbu unakuta idadi ya watu waliokuwa wanasumbuliwa na maradhi haya visiwani miongo kama mitatu tu iliyopita utakuta walikuwa wanahesabika vidoleni na ilisemekana ulikuwa wa kurithi.

Lakini hii leo ni tafauti kabisa na unaweza kusema katika kila familia imeathirika kwa namna moja au nyingine na maradhi haya.

Wataalamu wameeleza mara nyingi kuwa miongoni mwa sababu kubwa ya kuwepo ongezeko la wagonjwa wa kisukari ni vyakula vilivyopita muda wake wa matumizi na vingine ambavyo ni vya viwango visiokubalika kwa matumizi ya binadamu.

Kwa muda mrefu hivi sasa tumesikia taarifa za mara kwa mara juu ya kuwapo kila aina ya vyakula vibovu, mchele, unga, maziwa na dawa hata za watoto wadogo zilizokwisha muda wake wa matumizi au feki.

Hazipiti wiki chache utasikia imezuiliwa shehena ya mchele mbovu bandarini au kukamatwa katika maghala unga au mafuta yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu.

Vitu hivi tumekuwa tukielezwa na wataalamu kuwa vimechangia sana kuwepo ongezo la wagonjwa wa kisukari.

Baadhi ya watu hawa wanaojifanya wajanja hubadili tarehe ya kumalizika matumizi ya dawa kwa kuweka tarehe mpya na kupelekea kuathiri afya za maelfu ya watu, wakiwamo watoto wadogo.

Lakini huoni watu wanaokamatwa na kushukiwa kushiriki katika uhalifu huu kubanwa sawasawa kisheria wala maduka yao kufungwa.

Baya zaidi ni kwamba hata wale wanaotarajiwa kusimamia mambo haya yasifanyike ndio wapo mstari wa mbele kushirikiana na wafanyabiashara wenye tabia ya kuathiri afya za watu wa Visiwani na wageni wanaotembelea Zanzibar.

Nadhani wakati umefika kwa sheria za kudhibiti vyakula vibovu na dawa feki ambazo nazo zimechangia kuongezeka kwa wagonjwa wa kisukari na maradhi mengine zipitiwe upya na kufanyiwa marekebisho.

Kwa mantiki hii wale wote wanaowasaidia au wanaoshirikiana na wafanyabiashara wenye mwendo huu mbaya wa kuhatarisha maisha ya watu kwa uroho wa kupata utajiri hawapaswi kuachiwa. Sheria lazima nayo iwabane kwa uhalifu walioutenda.

Ni kwa kupambana na waingizaji vyakula vibovu na dawa feki na kutoa elimu ya kinga nzuri tu ndio tutaweza kuidhibiti hali hii ya hatari ya kuongezeka kila siku idadi ya watu wanaougua kisukari Zanzibar.

Jamii inapaswa kuelimishwa kuwa hakuna sababu za msingi za kuwa na huruma na watu ambao hawawaonei huruma wengine, wanafanya mambo ya kinyama na kijahili.

Utajiri unaopatikana kwa kudhulumu maisha ya watu usipewe nafasi ya kustawi visiwani. Haya ni mapambano ambayo hayastahiki kuregezewa kamba.

Lazima tuwe na sheria kali ndipo tutakapoweza kuikoa jamii na maradhi mbalimbali, kupunguza kasi ya kupeleka watu wengi makaburini kila siku.

Tuache muhali na tuwe wakali. Raia mwema ni yule anayeheshimu na kuthamini maisha ya watu na sio yule ambaye anaua watu kimyakimya.

Wednesday, September 19, 2018

Serikali inafanyia kazi kero ya mafuriko?

 

By Ngollo John

Wiki iliyopita Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitangaza msimu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza Septemba hadi Oktoba mwaka huu.

Kwa mjibu wa Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi, mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi nchini.

Ongezeko la mvua hizo linatarajiwa katika mwezi Novemba na kuna uwezekano wa kutokea vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Zipo athari zinazoweza kutokea ikiwemo hali ya unyevunyevu wa udongo katika maeneo mengi yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani na juu ya wastani na kwamba shughuli za kawaida za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini zitaathiriwa.

Katika kipindi hicho vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na hivyo kuongeza uwezekano wa mafuriko hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Wakati utabiri huo unatolewa, Watanzania bado tuna kumbukumbu ya matukio ya mafuriko yaliyotokea katika msimu wa mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu ambazo zilisababisha mamia ya wakazi katika maeneo mbalimbali nchini kuathirika.

Miongoni mwa mikoa iliyokumbwa na mafuriko hayo ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza kwa uchache huku wakazi waliokuwa wanaishi mabondeni nyumba zao ziliingiliwa maji na hivyo kukosa sehemu za kuishi.

Nikitolea mifano jijini Mwanza watoto wawili wa familia moja walifariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na nyumba waliyokuwa wanaishi kutokana na mvua zilizokuwa zinanyesha jijini humo.

Matukio mengine ya namna hiyo yalitokea wilayani Kwimba ambako kwa mujibu wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri watu 13 walijeruhiwa na nyumba 479 zikiwemo vyumba viwili vya shule ya msingi Mangulumwa na maabara ya sekondari Igongwa ziliezuliwa na upepo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Wakati tukijipanga kwa msimu mwingine wa wa mvua tunapaswa kujiuliza, je, Serikali na wananchi wamefanyia kazi kwa kiwango gani changamoto hizo, ili kuhakikisha madhara na matukio kama hayo hayajitokezi?

Pamoja na changamoto ya watu kujenga na kuziba mifereji ya kupitishia maji, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha wanaoishi mabondeni wanatengenezewa mazingira salama ya kuishi ili kuwaepusha na athari kama hizo?

Ukiachilia mbali suala la watu kujenga kwenye mifereji lakini pia lipo tatizo la uharibifu wa mazingira ambalo kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikilipigia kelele na kuwahamasisha wananchi kupanda miti kuzuia uharibifu wa mazingira, lakini hakuna mrejesho kuhusu kiasi gani wamefanikiwa?

Huenda jibu likawa ndiyo kwa baadhi ya maeneo, hasa pale ambapo wamepanda miti ya kutosha kuzuia uharibifu wa mazingira hususani maeneo ya mjini lakini kwa vijijini ambako kuna waathirika zaidi suala hilo limefanikiwa kwa kiwango gani?

Kutokana na utabiri huu kunahitajika jitihada za ziada kuwaelimisha wananchi kuelewa madhara ya ukataji miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa ili kupunguza changamoto hizo.

Rai yangu ni kwamba kila mmoja kwa utashi wake asaidie kutatua changamoto za uharibifu wa mazingira ili kuepusha madhara kama hayo yaliyotukumba katika msimu uliopita.

Wednesday, September 19, 2018

Tofauti ya ukapa na ukufuli ni mfumuko wa bei kwa wananchi

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa sahihi kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa kwa mwezihivi karibuni. Kushoto ni Meneja wa Idara ya Ajiri na Bei, Ruth Minja. Picha ya Maktaba 

By Dk Levy

Juhudi zote zilizopita zimezidiwa na juhudi hizi za sasa, kiasi cha kuungwa mkono kuliko zote. Wenye juhudi mbadala wanafungasha virago huko waliko kwenye vyama vyao vya juhudi takataka na kujiunga na juhudi safi.

Juhudi hizi ndiyo pekee ambazo wafanyakazi mwaka wa tatu huu wanapandishiwa mishahara? Vijana wakimaliza tu vyuo wanakutana na ajira, na ajira zimetapakaa mitaani mpaka zingine zinachacha mitaroni? Au nakosea?

Wajanja wote wanaunga mkono juhudi. Sasa wewe endelea kubaki huko uliko. Utajikuta Tanzania nzima imekutenga, watu wako kwenye juhudi wewe ukisubiri huruma za posho za tripu na semina kama ndezi pori.

Imegundulika kuwa watu hawahami kwa hiari yao bali wanashawishiwa na juhudi. Ukitaka maisha bora au cheo kikubwa cha ghafla bin vuu, wewe unga juhudi iwe kwa kamba au gundi utajua wewe na Mungu wako.

Mimi siwezi kutoa jibu lolote kwa janga hili la kuhama kwenye juhudi na kujiunga na juhudi. Ili upate jibu sahihi na wewe zidisha juhudi ya kujiuliza au kujadili na wenzako kuliko kuponda ponda tu.

Kuna mpuuzi mmoja ambaye simuamini hata akinisalimia, eti anadai juhudi ni mpango wa kubadilisha maneno ya kitabu kitakatifu cha taifa, ili huko mbeleni wawaandae waunga juhudi wengi wa kuunga mkono juhudi zao.

Siyo tu kubadilisha maneno na kutupatia maneno mazuri zaidi, eti pia kuweka neno sahihi la mwenye juhudi abaki na juhudi zake milele amina. Ili aendelee kuungwa mkono kwa juhudi zake bila kushindanishwa na mwenye juhudi mwingine.

Akaendelea kuongea uongo wake kuwa wanatuandaa kisaikolojia huko mbeleni waungaji wa juhudi kutoka kwenye juhudi mbadala wapatikane wachache ikiwezekana Mungu akiwapenda zaidi wasiwepo kabisa ili awe mmoja tu.

Waungaji juhudi

Niliendelea kusikiliza uongo wake sikutaka kumuangusha, eti anadai waunga juhudi wanatutoa kwenye njia tusiende kupiga kura, maana hatutakuwa na imani na wenye juhudi mbadala, kwa hisia kuwa wataondoka tena kwenda kuunga juhudi za yuleyule.

Kuna watu waongo na huyu ni mmoja wapo. Ananiambia eti wanaoungwa juhudi hawataki vikundi vya wenye juhudi mbadala. Kwamba hata vikiwepo basi viwe ni vile vyenye kuendeshwa na wao. Lakini wenye vikundi juhudi mbadala halisi watawafuta wote.

Eti wajiandae kutowaona wenye juhudi machachari kutoka katika vikundi mbadala vya juhudi, maana wenye juhudi zao hawataki ushindani. Kama kuna mwenye juhudi mbadala wa kuingia mjengoni basi ni yule asiye na madhara kwao.

Alipomaliza kuongea uongo wake mimi nikasema kuwa tulipofikia ni bora itangazwe kuwa tuna mfumo mmoja wa juhudi, kwani sioni maana na uwepo wa juhudi mbadala kama utaratibu ndio huu wa kuchagua watu na kuhama kisha kuchagua tena.

Baada ya kumwambia hivyo naye akaja juu akasema pengine ni lengo ni juhudi mbadala kupandikiza mamluki ndani ya juhudi mkuu. Ili wakiingia kwenye maeneo nyeti ya juhudi mkuu watibue. Hii ikawa kichekesho ndani ya kichekesho cha kupuuzwa.

Binafsi niliyapuuza maoni hayo maana naona huu ni upigaji tu kama upigaji mwingine. Sema huu unaendesha kisomi zaidi baada ya kugundua udhaifu wa rubani wa juhudi. Ukitumia mwavuli wa chama utapiga pesa mpaka uchoke bila kuguswa.

Ila nawaonya wanaokubali mchezo huu wa kuunga juhudi wakikengeuka mbele ya safari huku faranga nyingi zimetumika kwa ajili yao, watakiona cha moto kutoka kwa wamiliki wa juhudi ndani ya taifa hili. Wasithubutu.

Kuna watu najua hawaelewi au hawakubaliani na hili. Kwamba kazi ya kupata mwenye juhudi safari hii ni mgumu kuliko. Mwenye juhudi na muunga juhudi wote watapata taabu sana. Juhudi zitabaki kuwa juhudi kama juhudi za kuchagua mwenye juhudi halisi.

Kwanza samahani, nilianza moja kwa moja na maneno mengi bila salamu. Kwa wale ambao mambo ya kiafya hayako sawa na kukaa tenge poleni sana. Lakini vipi jamani mnaonaje mfumuko wa bei?

Ujanjaujanja watiwa kufuli

Maana toka 2005 vitu bei iko juu mpaka leo halafu cha kushangaza mishahara imeganda palepale kama sanamu la askari pale posta katikati ya Dar es Salaam. Au ndo maana mpango mzima ni kuunga juhudi?

Maana kuniongezea elfu mbili katika mshahara wangu naona unazingua tu. Ni kuchezeana akili. Unaongeza elfu mbili halafu kila kitu bei juu kama minara ya simu maana yake nini? Kama si kunisanifu tu.

Ni kweli pesa za ujanjaujanja zimebanwa. Lakini ubanaji uende sambamba na udhibiti wa mfumuko wa bei. Muigeni Mzee Mkapa ambaye katika utawala wake alibana kila kitu mpaka neno la Ukapa likazaliwa, lakini alidhibiti mfumuko wa bei.

Awamu hii siyo Ukapa tena, bali milango ya pesa za ujanjaujanja wizi na ufisadi imetiwa kufuli. Lakini wamesahau kuweka kufuli katika mlango wa mfumuko wa bei. Hapa kubana ni sawa na kujaza maji kwenye pakacha.

Jamani huu wa wimbo wa amani msitegemee utaendelea kutufurahisha. Wakati tunawaona nyinyi pekee ndiyo mnafaidika zaidi na amani hii. Kuna kitu tunakiona baina yenu na sisi. Tofauti kubwa sana ya kimaisha.

Wakati nyinyi mkipata nafasi ya kuunga na kuungwa kijuhudi, sisi ndoto ya juhudi hatujui tutaota lini. Fanyeni hima mambo yakae sawa kabla ule msemo wa kama mbwai na iwe mbwai haujaingia katika vichwa vya wengi.

Watu wanataka unafuu wa maisha, hizo propaganda za juhudi na matamko yatosha.

Hii ni karne ya ishirini na moja, hakuna Mtanzania mjinga. Siku itafika ya mtu wa Masaki na Tandale wote kupita njia moja.

Wednesday, September 19, 2018

Filamu ya Balozi Kagasheki, Dk Amani kurudi kivingine

 

By Phinias Bashaya, Mwananchi pbashaya@mwananchi.co.tz

Mvutano wa kisiasa kati ya wanasiasa wawili, Mbunge wa zamani wa Bukoba, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa zamani wa Manispaa ya Bukoba Dk Anatory Amani unafanana na filamu iliyowachosha watazamaji baada ya kuendelea kwa muda mrefu bila mshindi kupatikana.

Viongozi hao walitofautiana kwa hoja na hivyo kuwagawa watazamaji ambao waliunda vikundi vya upambe na kuanzisha mashambulizi ya maneno kwenye vijiwe vya kahawa kwa kudandia hoja za wanasiasa hao.

Hatimaye Dk Amani alihama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi mwaka 2015 na kutetea nafasi yake ya udiwani katika Kata ya Kagondo lakini akashindwa kurejea katika umeya; Kwa upande wa pili, Balozi Kagasheki akapoteza jimbo la Bukoba Mjini dhidi ya mgombe wa Chadema, Wilfred Lwakatare.

Baada ya kutangaza kurejea CCM hivi karibuni, Dk Amani ametangaza kuwasamehe maadui wake wote, miongoni mwao wakiwamo saba ambao alikuwa tayari amewasajili katika kundi la ‘adui namba moja’.

Katika mkutano wa ‘ndani’ uliofurika mamia ya wanachama wa Kata ya Hamugembe, hivi karibuni, Katibu wa CCM katika Manispaa ya Bukoba, amefanya upatanisho usio rasmi akimtaka Kagasheki kurejea ulingoni kuwanadi wagombea wa CCM pindi kampeni za uchaguzi mdogo zitakapoanza.

Wakati mkutano ukiendelea katibu huyo anatoa taarifa ya kupokea ujumbe aliotumiwa na Kagasheki kwa njia ya simu, akikubali kushiriki hatua zote za kampeni za wagombea wa CCM katika kata za Hamugembe na Kagondo ambako madiwani wamejiuzulu.

Kama ilivyofanyika katika kata zote ambazo madiwani wa upinzani wamerejea CCM, hata jina la Dk Amani linatarajiwa litapita bila kupingwa kuwania tena udiwani katika Kata ya Kagondo na pengine Balozi Kagasheki ataongoza timu ya ushindi.

Kosa la kwanza

Pamoja na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza kuanza kwa kampeni katika kata za Hamugembe na Kagondo, wagombea wa CCM tayari wanajulikana na viongozi wamekwishawaombea kura katika mkutano huo wa kuwakaribisha.

Katibu wa CCM Manispaa ya Bukoba, Mohamed Ali anatoa onyo kwa mwanachama atakayeonyesha nia ya kugombea katika kata hizo kuwa atachukuliwa hatua za kinidhamu na uchunguzi utafanyika dhidi yake.

Anaomba wanachama ambao tayari wameunda mitandao kwa maandalizi ya kugombea nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 waunganishe nguvu kukomboa kata hizo kwanza ambazo zilikuwa zinaongozwa na upinzani.

Hata hivyo, lawama na karipio dhidi ya baadhi ya viongozi wa ngazi ya wilaya ambao waling’oka au kung’olewa, kwa tuhuma kuwa walishiriki kukiangusha chama na kukifikisha hapo kilipo, ni shambulizi ambalo halikutakiwa kufanyika hadharani.

Baadhi yao bado wana nguvu ya ushawishi kwenye siasa ndani na nje ya chama. Hata kama hawahitajiki katika uchaguzi mdogo wa madiwani, nguvu yao inaweza kujitafsiri kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na nyingine zijazo.

Katika kusanyiko hilo kilichosahaulika ni kuwa kilichowafikisha hapo walipo ni viongozi kukosoana hadharani, jambo ambalo huchochea mgawanyiko zaidi na kuwa na chanzo cha kuibuka kwa makundi yanayoanzisha hoja za utetezi dhidi ya mashambulizi yanayofanyika hadharani.

Ugumu wa Hamugembe

Kata ya Hamugembe ni miongoni mwa kata 14 za Manispaa ya Bukoba ambayo matukio ya kihistoria kwenye majukwaa ya kisiasa yanaifanya itofautiane na kata nyingine. Imewahi kuongozwa na madiwani wa vyama vya CCM, CUF na Chadema kwa vipindi tofauti.

Wapiga kura wa kata hiyo kilio chao hakijawahi kubadilika kwenye suala la ubovu wa miundombinu ya barabara na maji, ambapo hata madiwani wa vyama tofauti waliotangulia walitoa ahadi ambazo hazikutekelezeka.

Kero hizi na nyinginezo ndizo zimechangia wananchi kujikuta wanabadili madiwani kwa vipindi tofauti na vyama vyao kama njia ya kutafuta majibu ya changamoto zao, hivyo wana uzoefu wa kutosha na lugha tamu za madiwani.

Uchaguzi wa kata ya Hamugembe pia utabeba mvuto wa kijimbo, ikitegemewa wapambe wa wagombea wa vyama watakaopitishwa watasafiri kutoka katika kata zao na kwenda kuongeza idadi kwenye mikutano ya kampeni.

Pamoja na kuwa Dk Amani anategemewa kuwa katika kibarua cha kurudisha udiwani wake katika kata ya Kagondo, pia inatarajiwa ataonekana mara nyingi kwenye jukwaa moja na Balozi Kagasheki wakimnadi Muhaji Kachwamba aliyerejea CCM akitokea Chadema.

Wanasiasa hao wanatarajiwa kutangaza mbele ya umma wakati wa kampeni hizo kuwa wamezika tofauti zao, huku kila mmoja akionyesha umahiri wake wa kuumba maneno wakati akijitetea kwa mambo yaliyopita.

Ajenda ya tetemeko

Kwa vyovyote vile ajenda ya tetemeko la ardhi inatarajiwa kukoleza uzito wa kampeni za udiwani katika Kata ya Hamugembe. Kwa kuwa bado kuna makovu ya tukio hilo wagombea wanatakiwa kuchagua maneno ya kuongea hasa wakati wa kutafuta kura nyumba kwa nyumba.

Hii ndiyo kata ambayo katika tukio hilo la Septemba 10, 2016 watu wanane katika mtaa wa Omukishenye walipoteza maisha. Hivyo suala la msiba ulioikumba kata hiyo halikwepeki wakati wanasiasa na wapambe wao watakapokuwa majukwaani wakiomba kura.

Mtaa wa Omukishenye ulitembelewa zaidi na viongozi tofauti kujionea maafa ya tetemeko na baadhi yao wanatarajiwa kuonekana tena wakati wa kampeni wakiomba kura na kuwaeleza waathirika jinsi walivyoshughulikia janga lililowapata.

Kampeni za nyumba kwa nyumba zinaweza kuwa ngumu zaidi katika mtaa huu kwa kuwa baadhi ya familia ziko kwenye mahema baada ya kushindwa kujimudu tena. Katika kuomba kura katika familia hizi mgombea anahitaji ujasiri wa ziada.

Kwa wanasiasa ambao hawakufika kutoa pole wakati wa janga hilo ujio wao wakati wa kampeni unaweza kukoleza mijadala ya wapambe kwenye vijiwe vya kahawa kuhusu thamani ya mpiga kura wakati wa shida na umuhimu wake wakati wa uchaguzi.

Upinzani washtuka

Kuondoka kwa madiwani wa Hamugembe na Kagondo na kurejea CCM, ulikuwa mwanzo wa kutimua vumbi kwenye kambi ya upinzani na kusababisha baadhi ya madiwani kutiliwa shaka kuwa nao wako njiani kuondoka.

Uvumi huo ulizimwa na diwani wa Kashai, Nuruhuda Kabaju aliyejitokeza hadharani na kukanusha madai ya kupokea gharama za uhamisho, huku akikubali kuwa miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wanawindwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari, diwani huyo alishauri kama kuna fungu limeandaliwa kwa ajili ya kufanikisha mipango ya kumhamisha ni bora likaelekezwa kwenye huduma nyingine za kijamii kama barabara, maji na umeme.

Hata hivyo, shutuma za madiwani kurubuniwa kwa fedha na ahadi nyingine zinakanushwa mara zote na viongozi wa CCM wanaodai wimbi la madiwani na wabunge kuukimbia upinzani ni baada ya chama hicho kupata mvuto mpya unaotokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

Utekelezaji wa ilani ya chama hicho pia umesisitizwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo ambaye hivi karibuni amewataka wananchi kujitenga na uvumi kuwa miradi yao inakwamishwa na Serikali makusudi.

Anasema kuwa kituo cha Afya cha Zamzam kimeboreshwa kwa gharama kubwa kama sehemu ya miradi iliyotekelezwa na Serikali kwa ajili ya wananchi na kuwa kama ingekuwa ni kukwamisha miradi kituo hicho kisingeboreshwa.

Wednesday, September 12, 2018

Bashe: Hata mimi naweza kuhama CCM kama hakitakuwa na tija kwa wananchi

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe akizungumza

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe akizungumza katika mkutano wa kampeni za mgombea Ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwanagati Kitunda, jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Said Khamis 

By Cledo Michael, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema zipo sababu za kwa nini aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kuhama chama hicho na kujiunga CCM kwa kuwa ni haki ya kisheria.

Kwa mujibu wa Bashe, hata yeye anaweza kuhama endapo chama chake cha CCM hakitakuwa na tija kwa wananchi.

Bashe ambaye alikuwa akizungumza katika kampeni za kumnadi mgombea huyo wa ubunge Jimbo la Ukonga kupitia CCM alisema ipo hoja inayosemwa kwamba Waitara amenunuliwa, hilo si kweli na kwamba anamfahamu kiongozi huyo tangu wakiwa pamoja Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

“Mwanasiasa yoyote anapoamua kuwatumikia wananchi anapanda basi, vyama vya siasa ni sawa na basi, ukiona basi hilo dereva, kondakta hamuelewani unaweza kushuka kwenye basi hilo,” alisisitiza Bashe.

“Aliondoka mzee (Augustine) Mrema mwaka 1995, Maalim Seif naye akaondola hadi mzee wangu (Edward)Lowassa alifanya hivyo, hatujawahi kutuhumu kama mtu amenunuliwa,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Bashe, hiyo ni hoja dhaifu inayotolewa na wanasiasa walioshindwa kufikiri; “wanaosema tulimnunua Waitara wao watuambie walimnunua kwa shilinga ngapi mwaka 2008,” aliongeza.

“Hakuna jambo linanisikitisha mimi kama kijana eti kwamba mwanasiasa anapohama chama anatuhumiwa amenunuliwa. Hata sisi wana CCM chama chetu kinaposhindwa kusimamia masilahi, au kutatua matatizo ya watu ukiona mimi nimebaki CCM jua tunalinda matumbo yetu,” alisema.

Mbunge huyo amevitaka vyama vya upinzani nchini kujitathmini ndani ya vyama vyao na kuacha kuituhumu CCM kwamba inanunua wabunge na madiwani wao.

Kutokana na tuhuma kwamba CCM imepanga kumteka mgombea wa Chadema, Asia Msangi, Bashe alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama vimpe ulinzi wa kutosha mbunge huyo.

“Naviomba Vyombo vya ulinzi na usalama vimpe ulinzi, tulipuuza puuza maneno yakatokea maafa uchaguzi wa Kinondoni. Kama wanasema mgombea wao atatekwa wamuwekee ulinzi nyumbani kwenye gari na kila sehemu,” alisema Bashe.

Kuhusu gharama za uchaguzi kuwa kubwa kutokana na kurudiwa, Bashe alisema hakuna jambo lisilokuwa na gharama hata kwenda peponi kwa Mungu kuna gharama lazima usali, utoe sadaka, utoe zake na lazima ufe.

“Wanasiasa wanaosema chaguzi ndogo ni gharama leteni muswada bungeni tubadilishe sheria ili mtu akihama ahame na ubunge wake,” alisisitiza.

Awali mwenyekiti wa CCM Kata ya Tandale, Tamim Omari Tamim alisema vyama vya upinzani vimekufa ndiyo maana wanachama wake wanahamia chama hicho tawala.

“Vyama vya upinzani vimekufa. Ukisia CUF, sijui Chadema na wewe ukaingia kichwa kichwa basi akili huna,” alisisitiza mwenyekiti huyo.

Alisema wananchi wakimchagua Waitara atakuwa mkombozi wao kwa kuwa wakazi wengi ni kabila lake hivyo hawezi kuwaangusha.

“Nimesikia eti hapa kuna wapinzani, mimi nataka niwambie kama kulikiwa na mpinzani mkubwa kwenye nchi hii basi nikuwa mimi. Nilikuwa CUF tangu 1992 kabla ya Katibu Mkuu wa chama hicho taifa Maalim Seif Hamad na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba,” aliongeza.

Kwa upande wake mbunge wa Mtera, Livinstone Lusinde alisema mawaziri wakuu wastaafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa baada ya kujiunga na vyama vya upinzani wamekuwa wanafiki kwa kuwa wanayo yaahidi hawawezi kutekeleza.

“Suala la kuja CCM sio suala la dharura..Kinachowasumbua ni kwamba wanafahamu nguvu zangu ni kubwa sana ni jeshi la mtu mmoja.”

Wednesday, September 12, 2018

Nani ni nani kati ya China na Afrika?

 

By Amani Njoka

Tangu miaka ya 1960 China imekuwa ikiwekeza kwa wingi barani Afrika hususan kwenye miundombinu ya barabara, reli na majengo. Zipo kampuni nyingi za kichina barani Afrika, ikiwamo Tanzania, ambazo zimewekeza na kufanya shughuli zake nchini katika uwekezaji huo.

Miradi mikubwa Kiwanda cha Urafiki pamoja na reli ya Tazara ni moja ya miradi mikubwa iliyofanywa na serikali ya China barani Afrika.

Taarifa kutoka katika kituo cha utafiti wa masuala ya uhusiano wa China na Afrika kipo katika Chuo Kikuu cha Hopkins, Marekani zinasema kuwa kipindi cha mwaka 2000 hadi 2016 China imewekeza kiasi cha zaidi ya Dola125 bilioni katika bara la Afrika.

Hata hivyo, katika mkutano uliofanyika mapema wiki hii, China imesema itaendelea kuisaidia Afrika katika ujenzi wa miundombinu pamoja na masuala ya ulinzi na kiusalama.

Serikali ya China ilifadhili mradi wa ujenzi wa reli kutoka Nairobi mpaka bandari ya Mombasa nchini Kenya uliogharimu kiasi dola 3.2 bilioni. Mradi wa reli hiyo iliyotegemewa kuunganisha nchi za Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Ethiopia, umeonekana kusuasua baada ya kubainika kutia hasara ya zaidi ya Dola100 bilioni katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kukamilika kwake.

Mkutano uliofanyika Beijing, wiki iliyopita Serikali ya China ilisema itatoa Dola60 bilioni ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Ndoa ya China na Afrika

Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping alisema China haiwekezi katika miradi isiyo na maana, bali inalenga kulisaidia bara la Afrika kujenga miundombinu na kuifanya nchi hiyo kuwa pekee inayowekeza kiasi kikubwa cha fedha barani Afrika.

Pamoja na hayo, wakosoaji wameonya kwamba mataifa ya Afrika yamejikuta yakiingia katika madeni isiyoweza kumudu kutoka kwa nchi hiyo kubwa barani Asia. Akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais Jinping aliwaambia viongozi na wafanyabiashara kutoka Afrika kuwa ushirikiano wa China na bara hilo umelenga kuiletea Afrika maendeleo.

“Rasilimali zinazotokana na ushirika wetu hazipaswi kutumika katika miradi hewa bali katika miradi inayoonekana na yenye tija kubwa,” alidokeza.

Msomamo huo uliungwa mkono huku Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akieleza wazi kuwa hakubaliani na wale wanaotaka kuwaaminisha kwamba hii ni aina mpya ya ukoloni inayotaka kulikumba bara la Afrika. Mataifa yote ya Afrika yalikuwa na uwakilishi katika mkutano huo isipokuwa Swaziland ambayo ina ushirika na Taiwan. Wakati huohuo China inadai Taiwan ni sehemu ya nchi yake, hivyo kufungamana na Taiwan ni kama kuisaliti China, hivyo Swaziland isingeweza kuwa na ushirika na China na Taiwan kwa wakati mmoja.

Licha ya ukosoaji mkubwa unaelekezwa katika ushirika huo, Rais Jinping aliendelea kusisitiza kuwa uhusiano huu hauna mahusiano yoyote ya kisiasa bali ni nia ya dhati kabisa ya kuisaidia Afrika katika ujenzi wa miundombinu yake bila masharti yoyote.

Kiasi hicho cha fedha kitakuwa kama mkopo na msaada ikijumuisha ujenzi wa miundombinu na ufadhili wa masomo.

Kwa hakika ushirikiano huu umeonekana msaada mkubwa kwa Afrika ukilinganisha na vile ambavyo hali ingekuwa bila msaada wa China.

Hata hivyo, katika hili kuna mambo ya kutazama kwa kina kabla hujashangilia au kuukosoa ushirikiano na makubaliano haya. Ili uweze kufanya hivyo haupaswi kuwa upande wowote.

Wakosoaji wengi wamekosoa kwa kuwa pengine watakosa fursa za mataifa yao kuwekeza barani Afrika au pengine wamekwishaathirika kwa kiwango kikubwa na madeni haya au kinyume chake.

Lakini, ukikaa nje ya makubaliano haya na utazame kama hakimu asiyemfahamu mtu yeyote katika kesi, kisha usikilize maelezo ya pande zote mbili kwa weledi, upokee ushahidi halafu utoe maamuzi utaweza kutoa maamuzi sahihi.

Hata hivyo, hii sio kesi ya kuamua ni jambo ambalo linakupasa utazame hali halisi ya Afrika na China halafu uone ni yupi ananufaika zaidi, hasa kwa kuwa kimsingi pande zote zinanufaika.

Ni kweli usiopingika kuwa kwa kipindi kirefu China imeisaidia Afrika kwa mikopo na misaada mbalimbali, lakini katika hili sioni nchi kama China iliyo tayari kuwekeza kwa hasara, ninaiona China ikipanda punje moja ya mhindi kisha ivune punje nyingine hamsini.

Kama ni kweli China imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuiendeleza Afrika, ni vipi nchi hizi zimeshindwa kuendelea huku yenyewe ikizidi kunawiri katika uchumi wake?

Hivi majuzi bidhaa za China zimeongezewa kodi nchini Marekani, China nayo ikajibu kwa kuongeza kodi katika bidhaa za Marekani nchini mwake. Ulaya nako hakueleweki ndio kwanza (Waziri Mkuu) Theresa May wa Uingereza na (Kansela) Angela Merkel wa Ujerumani wanapishana angani. Unafikiri China itauza wapi bidhaa zake, unafikiri ataungwa mkono na nani kama si Afrika? Kwa hali hii China haiwezi kupoteza fedha na rasilimali zake bure. Katika hili fikiria vyema kisha jijibu bila kupepesa macho.

Keti chini kisha tulia halafu tazama vyema utaona nchi mbili kubwa (China na Marekani) zikikimbizana katika chati ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani, kisha geuka tazama mzozo wa kibiashara unaoendelea kati ya nchi hizo mbili. Baada ya kutazama kwa makini utapata jibu lako, lakini mimi nikitazama sioni kama kuna nchini yoyote kati ya hizi (China na Marekani) inataka kushindwa kirahisi, sioni kama kuna nchi iliyo tayari kupoteza ubabe wake kiuchumi kwa kutapanya fedha na kupoteza muda zaidi, bali itataka kujiimarisha. Vilevile sioni kama kuna nchi iliyoko tayari kusinzia ipigwe kikumbo.

Baada ya kutazama uwekezaji wa China kwa Afrika, ninageuka upande mwingine na kuiona Afrika isiyo na teknolojia na miundombinu ya kutosha na kuiona China kama msaada mkubwa.

Ukiachilia mbali reli ya Nairobi kwenda Mombasa, barabara, madaraja, viwanda na viwanja vya ndege vilivyopo katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, ninawatazama wanafunzi wengi kutoka Afrika wakipewa ufadhili kwenda kusoma China katika fani mbalimbali ikiwemo uhandisi na afya, ninakiri kwamba kama sio China haya yasingekuwepo. Lakini, inakuwa vigumu kuamini kama wanafanya haya bila ya wao kupata faida yoyote.

Nazifikiria fursa za kibiashara, kiafya na kielimu zilizopo baina ya China na Afrika ninaona kwa kiasi fulani China imetutoa mahala ambapo tulikuwa na kutuweka mahala tulipo kwa sasa. Ninatazama miundombinu ya usafiri iliyopo katika majiji mbalimbali, ninaiona kama mkombozi kwa kiwango chake. Hata hivyo, ni vipi China inaweza kufanya yote haya bila yenyewe kufaidika?

Soko la bidhaa za China

Soko la bidhaa za China, ni mara kadhaa tumekuwa tukisikia malalamiko kwamba bidhaa za nchi hiyo hazina ubora bila, zipo bidhaa zinazokuja kulingana na thamani ya soko lililopo.

Kwa sasa China inaitazama Afrika kama mnunuzi mkubwa wa bidhaa zake. Inakuja kama mwekezaji ili kufungua milango ya bidhaa zake kuuzwa kwa wingi Afrika. China inatupatia mikopo kisha itaingiza bidhaa zake na kuvuna fedha, itakusanya mikopo yake na kuondoka sisi tukifurahia barabara na reli ambazo uendeshaji wake unatugharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Mwandishi ni Mwanafunzi wa Shahada ya awali ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anafanya mazoezi kwa vitendo Mwananchi Communications Ltd.

0762395558

Wednesday, September 12, 2018

Joto la kampeni laongezeka Monduli, Ukonga