Friday, January 19, 2018

Faini kwa uzembe yamaliza tatizo la utapiamlo, maambukizi ya VVU

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Katikati ya Mkoa wa Njombe wenye changamoto ya udumavu na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kuna kijiji kilichoweka rekodi ya aina yake kwa kufanikiwa kuwalinda watoto dhidi ya maradhi hayo.

Kijiji hicho cha Ikuna, hakina mtoto hata mmoja aliye chini ya umri wa miaka mitano mwenye tatizo la udumavu wala maambukizi ya VVU, japo wapo wazazi walio na maambukizi hayo.

Utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS), unaonyesha mkoa huo unashikilia nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 49.4 ya udumavu.

Lakini pia, Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika utafiti wake wa mwaka jana, unautaja Mkoa huo kuongoza kwa asilimia 11.4 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Wakati karibu kila kijiji tulichobahatika kutembelea kikiwa na kati ya watoto wawili hadi wanne wenye utapiamlo, Ikuna hakukuwa na mtoto hata mmoja.

Kijiji cha jirani cha Nyombo, chenye mazingira sawa na Ikuna wapo watoto chini ya umri wa miaka mitano wenye utapiamlo na maambukizi ya VVU.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuna, Ahazi Kihombo anasema si kwamba maambukizi ya VVU na utapiamlo kwa watoto hayakuwapo, laa. Yalikuwapo.

Anasema hayo yote yamewezekana kwa sababu ya umoja, ushirikiano na adhabu mbalimbali kwa familia zinazokiuka masharti ya malezi na lishe kwa watoto.

Muuguzi Mkunga wa Zahanati ya Ikuna, Anitha Mtitu anasema kati ya watoto zaidi ya 40 wa kijiji hicho waliofikishwa kliniki Desemba 22, 2017 hakuna aliyepatikana na utapiamlo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) lilisema mkakati wake ni kuhakikisha watoto hao wanapatiwa nafasi ya kuishi na kuziomba nchi hizo ikiwamo Tanzania, kuwekewa mazingira ya kuokoa vifo vya watoto hao kutokana na ukweli kwamba wengi hufariki dunia ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa. Kwa mujibu wa Unicef, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye viwango vya juu vya idadi ya vifo vya watoto wachanga duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Level & Trends in Child Mortality 2017, mwaka huo 2016, watoto wachanga 46,000 walifariki dunia nchini na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tisa kwa vifo hivyo.

Wakati Ikuna ikikosa mtoto mwenye utapiamlo, vijiji vya jirani kikiwamo cha Nyombo, wapo baadhi ya watoto wanaokabiliwa na hali hiyo licha ya kuwapo kwa chakula cha kutosha. “Watoto wote walikuwa kwenye rangi ya kijani kuonyesha afya zao ni nzuri, zamani hali haikuwa hivi. Ilikuwa mbaya sana,”anasema.

Waliwezaje kumaliza utapiamlo?

Hali mbaya ya utapiamlo na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto iliwafanya viongozi wa kijiji hicho kutafuta suluhu ya nini wafanye kuokoa maisha ya watoto hao.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Kihombo anasema njia rahisi ilikuwa kutengeneza ushirikiano wa karibu baina ya Serikali ya kijiji, wahudumu wa afya wa zahanati, wahudumu wa afya ya msingi na wananchi.

“Tulikubaliana kushirikiana, muuguzi akigundua mtoto ana utapiamlo, anatoa taarifa kwa mhudumu wa afya ya msingi, inakuja kijijini na sisi tunaenda kuitembelea hiyo familia,”anasema Kihombo.

Anasema Serikali ya kijiji ikipata taarifa ya kuwapo kwa familia yenye tatizo la lishe kwa mtoto, wanaenda kuitembelea kujiridhisha n akubaini sababu zinazowafanya wazazi washindwe kumpatia lishe bora mtoto wao

Anasema kama wakibaini sababu ni hali ngumu ya uchumi ndani ya familia, kijiji kinakubaliana kuchanga fedha au chakula kwa ajili ya kuisaidia.

“Kwa hiyo hapo mwenye chochote anatoa, tunakusanya na kuwapelekea walezi wa mtoto husika tukiwasisitiza kuhakikisha mtoto huyo anarejeshewa afya yake,” anasema.

Ikiwa watabaini sababu ni uzembe, familia husika inatozwa faini ya Sh20,000 na inapewa masharti ya kuhakikisha mtoto aliyepatwa na utapiamlo anarejea kwenye afya yake.

Kihombo anasema faini hiyo ilisaidia kila mzazi mwenye mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano kuona wajibu wa kusimamia na kuhakikisha anampa mwanawe lishe bora badala ya kuendekeza shughuli za kilimo na kuwasahau watoto.

Mhudumu wa fya ya msingi wa kijiji hicho, Jafeth Ngimbudzi anasema kihalisia hali ilikuwa mbaya na kama kijiji kisingesimama kidete, mambo yangekuwa mabaya zaidi.

“Kwa hiyo, kazi yangu kubwa ni kuwatembelea nyumbani watoto wenye shida, kuwashauri wazazi na kuhakikisha wanawapatia watoto wao chakula bora,” anasema.

Muuguzi Mtitu anasema kila watoto wanapoletwa kliniki, jukumu lake kubwa ni kutoa elimu ya lishe bora kwa wazazi.

Anasema wengi hawajui makundi bora ya chakula ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa mtoto kupata utapiamlo.

“Mzazi anamlisha mtoto uji asubuhi, ugali mchana na jioni kila siku, hapo anakuwa anamlisha chakula cha aina moja tu wakati uhakika wa kupata aina nyingine upo,” anasema.

Mratibu wa Lishe Mkoani Njombe, Ester Kibona anasema wanaendelea na hatua ya kuwahamasisha wazazi na walezi kufuga mifugo midogo kama bata, kuku na simbilisi kwa ajili ya kupata nyama na mayai kwa ajili ya lishe ya familia.

Hata hivyo, Unicef kupitia baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi chini ya Serikali, yamekuwa yakisaidiana na zahanati kuimarisha afya za watoto.

“Tunatamani kuiona Njombe isiyo na utapiamlo, hili litawezekana kama jamii yenyewe itakubali na kuona umuhimu wa kuwatunza watoto,” anasema.

Simulizi za udumavu kijijini

Baadhi ya wazazi na walezi waliowahi kupigwa faini au kusaidiwa wanasema bila sheria kijijini hapo pengine wangewapoteza watoto wao kwa uzembe.

Emiliana Lucheza mkazi wa Kijiji cha Ikunza anasema mtoto wake alizaliwa akiwa na kilo 3.5, lakini baadaye alipungua hadi kilo 1.5 kutokana na lishe duni jambo lililoufanya uongozi wa kijiji kuingilia kati.

“Mimi uchumi wangu ulikuwa tatizo, kwa hiyo nilichangiwa, nikapelekwa hospitali ambako mtoto alilazwa na kupewa dawa lishe. Hivi sasa nakazana kufanya kazi nipate chakula cha mtoto, sina tatizo tena,” anasema.

Naye Tumpe Ngimbudzi anasema mjukuu wake aliyekuwa na tatizo la utapiamlo anaendelea vizuri baada ya kupata lishe bora kutokana na jitihada za wauguzi na viongozi wa serikali ya kijiji.

Tulahega Magula anasema faini aliyotozwa kwa ajili ya uzembe wa kuwapa lishe bora wanawe ilimfanya ajitahidi kuwasimamia na kuhakikisha hawapati tena tatizo hilo.

Kuhusu maambukizi ya VVU

Mtitu anasema mkakati pekee waliojiwekea kuhakikisha hakuna maambukizi yanayowapata watoto ni kwa mama zao kuhudhuria kliniki na kujifungulia zahanati.

“Mama anapopata huduma za afya tangu wakati wa ujauzito anapata nafasi ya kuijua afya yake, kama atakuwa ameambukizwa anaweza kumlinda mtoto wake aliye tumboni kabla na baada ya kuzaliwa,”anasema.

Anasema kutokana na ukweli huo, wahudumu wa afya ya msingi wanasimamia kuhakikisha wajawazito wote kijijini hapo wanapima afya zao na kuwa makini kujilinda ili kuwalinda watoto wao tumboni.

“Hili pia tulifanikiwa. Hakuna mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano aliye na maambukizi japo wapo wazazi wenye watoto wadogo ambao wanayo maambukizi,” anasema.

Mwenyekiti huyo wa kijiji, Kihombo anasema sheria ya kwanza kwa wajawazito kijijini hapo ni kuhudhuria kliniki.

“Kujifungulia hospitali ni lazima, hii imetusaidia sana na tunamuomba Mungu tuendelee kuwasaidia watoto wetu,” anasema.

Mmoja wa akina mama ambaye mwanawe hana maambukizi anasema aliijua afya yake kuwa anamaambukizi ya VVU wakati wa ujauzito.

Anasema awali alishtuka, lakini baadaye aliiona ni hali ya kawaida kutokana na huduma aliyoipata kutoka kwa wahudumu wa zahanati.

“Kwa hiyo nilijifungua salama, nilimnyonyesha mwanangu miezi sita bila kumpa chochote na sasa nimemuachisha. Ana afya nzuri na ninamshukuru Mungu atakua salama,”anasema.

Mratibu wa Ukimwi mkoani Njombe, Dk Braine Burure anasema mkakati wa mkoa huo ni kupunguza au kumaliza kabisa maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo, anasema japo kukosekana kwa mashine ya kupima wingi wa virusi kwa maendeleo ya mtumiaji wa dawa za kufubaza VVU ni changamoto inayowafanya wengi kutofuatiliwa maendeleo ya tiba ipasavyo na huduma ya mama na mtoto inasimamiwa kwa umakini.

Anaitaja changamoto nyingine ni umbali kutoka makazi ya wananchi na vituo vya kutolea huduma za upimaji VVU na Ukimwi.

Lakini anasema tatizo hilo bado halijawa kikwazo kikubwa kwao, wanaendeleo kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala hilo ili kuona umuhimu wa kuwalinda watoto wao dhidi ya maambukizi ya VVU.

Mkakati wa Serikali

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka anasema msingi wa afya bora kwa jamii ni pamoja na kuzilinda zile za watoto na wajawazito.

Anasema ili kupunguza maambukizi ya VVU mkoani humo, mbali na kutoa elimu, lazima watoto wafanyiwe tohara ili kuua mila ya kutotahiriwa kwa baadhi ya jamii mkoani humo kwa madai inachangia kusambaza maambukizi.

Mratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Cocoda, Alatanga Nyagawa anasema Kijiji cha Ikuna ni cha mfano kwenye ulinzi wa mama na mtoto kwa sababu wametambua umuhimu wa kundi hilo.

“Ni kweli kijiji hiki ni waelewa hata sisi wakati tunakwenda kutekeleza miradi yetu wanatuelewa na kuitekeleza kwa makini hasa ile inayowahusu watoto,”anasema.

Nyagawa anasema kuzalisha chakula kwa wingi si sababu pekee ya jamii kuwa na afya bora.

“Kikubwa hapa ni usimamizi wa nini anachokula mtoto na kwa wakati gani,” anasema.     

Friday, January 19, 2018

Yanayosababisha kupasuka kwa chupa mapemaDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Wiki hii nitaelezea tukio ambalo si geni kulisikia kwa wajawazito na jamii.

Chupa kupasuka ni neno lililozoeleka katika jamii yetu likiwa na maana kitabibu kama ngozi au tando laini inayoyazunguka maji yanayomfanya mtoto aliye ndani ya nyumba ya uzazi kuelea, imepasuka na maji hayo kutoka.

Tando hii ya ngozi huweza kupasuka kiasili wakati au baada ya uchungu kuanza. Katika hatua hii si tatizo ni hali ya kawaida kujitokeza na kitabibu hujulikana spontaneous rupture of membrane.

Pia, tando hii inaweza kupasuliwa na mtoa huduma kwa baadhi ya wajawazito, kulingana na hali zao. Kwa mfano, mtoa huduma anaweza kumtathimini mjamzito, kama kuendelea kuwapo kwa ujauzito huo kunaweza kuhatarisha maisha ya mtoto tumboni.

Na kama chupa itapasuka kabla ya muda wake kufika, huenda ikawa ni tatizo la kiafya au madhara yatokanayo na hali ya ujauzito. Hivyo, leo nitalenga zaidi kwenye eneo hili.

Kupasuka kwa ngozi laini kabla ya mjamzito kupata uchungu halisi baada ya kukamilika kwa wiki 37 za umri wa mimba, kitabibu huitwa rupture of membrane (PROM) na kupasuka kwa chupa mapema kuliko kawaida kabla ya wiki ya 37 ya umri wa mimba, kwa neno la kitabibu huitwa preterm premature rupture of membrane(PPROM).

Inakadiriwa kati ya asilimia 8 hadi 10 ya wajawazito hupata PROM na asilimia mbili hupata PPROM. Hili ni moja ya tatizo linaloweza kuchangia kuzaliwa mtoto njiti.

Madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito yanaweza kuwapo kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Kutokea kwa tatizo hili kuna mhatarisha mjamzito na mtoto aliye ndani ya nyumba ya uzazi kupata matatizo likiwamo shambulizi kwenye ngozi laini inayomzunguko na maji maji ambayo mtoto huelea ambayo kitabibu yanaitwa Chorioamnionitis, kondo la nyumba kujipachika vibaya, kuumia kihisia, kupata matatizo wakati wa usisimuaji uchungu na kuchelewa kushikama kwa mama na mtoto.

Kwa upande wa mtoto, anaweza kuzaliwa baada ya siku saba tangu kutokea kwa PPROM, hii hutokea kwa asilimia 80 waliopata tatizo hilo.

Madhara anayoweza kupata mtoto ni pamoja na kuzaliwa njiti, kupata uambukizi mkali wa bakteria ambayo huambatana na homa kali, maji ya nyumba ya uzazi kuwa machache na kuzaliwa na kasoro usoni,

Matatizo mengine hujitokeza wakati wa kuzaliwa. Kwani anaweza kupata matatizo kwenye mapafu, kuzaliwa na miguu na mikono yenye ulemavu, kuathirika kwa ukuaji, kuchoropoka kwa kitovu na mishipa ya damu kuvujisha damu kwenye ubongo. Hali hiyo inayoweza kuchangia kupata jeraha la ubongo.

Wajawazito walio katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili ni pamoja na watumiaji wa sigara, watumiaji wa dawa za kulevya na wenye uambukizi wa viungo vya uzazi.

Dalili kubwa ni kutokwa au kuchuruzika ghafla kwa maji maji kwenye sehemu za siri za mjamzito ambayo yanaweza kusambaa mpaka katika maeneo ya mapajani.

Maji maji hayo yanaweza kutoka pale anapokohoa au kucheza kwa mtoto kunaweza kusababisha kuchoropoka kwa kitovu cha mtoto.

Sababu ya maambukizi inaweza kuwa mjamzito ameugua homa, anatokwa na maji maji yenye harufu kali ukeni na maumivu chini ya kitovu.     

Friday, January 19, 2018

Upungufu wa damu kwa mjamzito unaweza kuzuiwa

 

By Dk Kammu Keneth, Mwananchi

Wakati wa ujauzito mabadiliko ya kiafya husababisha upungufu wa kiwango cha damu kwa asilimia 20 hadi 30.

Hali hii husababisha uhitaji mkubwa wa madini ya chuma na virutubisho vya vitamini kwa ajili ya kutengeneza hemoglobin, moja ya vitu vinavyoiunda seli nyekundu kwenye damu.

Upungufu huu wa damu ujulikanao kitaalamu ‘Anemia’ hujidhihirisha kwa mjamzito pale kiwango cha madini ya chuma kinachohitajika kuwa kikubwa ikilinganishwa na kilichopo.

Hali hii husababisha usafilishaji wa oksijeni kwenda sehemu mbalimbali za mwili kuwa hafifu.

Kuna aina ngapi za anemia

Kuna aina kuu tatu za anemia ambazo huwakumba wanawake kipindi cha ujauzito. Ya kwanza ni ya upungufu wa madini ya chuma.

Utafiti unaonyesha takribani wajawazito asilimia 15 hadi 25 hupatwa na aina hii ya anemia. Na wataalamu ya afya ya mama na mtoto wanasema madini hayo ya chuma husaidia usafirishaji wa oksijeni kutoka kwenye mapafu kwenda sehemu mbali mbali za mwili pamoja na kwa mtoto aliyeko tumboni.

Aina ya pili ni ya upungufu wa virutubisho vya vitamini aina ya foleti. Foleti hupatikana katika mboga za majani, malimao, ndizi, parachichi, machungwa, mapapai, maharagwe na karoti.

Kirutubisho hiki ni muhimu kwani husaidia kuujenga uti wa mgongo imara kwa mtoto aliyeko tumboni.

Aina ya tatu ni ya upungufu wa vitamini B12, ambayo ni muhimu kwenye uzalishaji wa chembe nyekundu za damu zenye kazi ya kusafirisha oksijeni kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu.

Hata hivyo, tofauti na ukosekanaji wa aina hizo, kuna sababu nyingine huchangia upungufu wa damu.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na matatizo kwenye mfumo wa chakula unaosababisha kupoteza damu hasa kwa kipindi cha muda mrefu, nyingine ni maradhi kama malaria, Ukimwi, tatizo la seli mundu linalofahamika kwa jina la sikoseli, minyoo husabi ile inayonyonya damu katika mfumo wa chakula.

Je! Ni mambo gani yanayomuweka mjamzito katika hatari ya kupata upungufu wa damu?

Tunaambiwa miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha mjamzito kupata tatizo la upungufu wa damu ni pamoja na kubeba mimba zinazofuatana katika kipindi kifupi baada ya kujifungua, upungufu wa lishe yenye madini ya chuma, ujauzito wenye mapacha, kutokuwa na damu nyingi katika hedhi kabla ya ujauzito pamoja na kutapika sana wakati wa homa za asubuhi.

Namna unavyoweza kujitambua kuwa una tatizo hili

Tatizo hili la upungufu wa damu huambatana na dalili za maumivu ya kifua, kukabwa na pumzi, uchovu usio wa kawaida, maumivu ya kichwa hasa upande wa mbele, mapigo ya moyo kwenda haraka kwasababau katika kipindi hicho hemoglobin ya kusafirisha oksijeni mwilini huwa chache kutokana na upungufu wa madini ya chuma.

Hali hiyo husababisha moyo kupampu damu kwa haraka zaidi ili kuhakikisha oksijeni inasambaa katika sehemu mbalimbali za mwili kukidhi mahitaji, kupauka kwa ngozi na kucha, mikono na miguu kupatwa na ubadili, kutoweza kufikiria kwa makini, kwasababu ubongo unakuwa unahitaji oksijeni wakati wote.

Madhara yake

Madhara ya upungufu wa damu ni pamoja na kuongeza uwezekano wa kujifungua mtoto chini ya uzito wa kawaida, kuathiri ukuaji wa mtoto, matatizo katika ukuaji wa ubongo na uti wa mgongo, mimba kutoka kabla ya wakati, mtoto kupoteza maisha akiwa tumboni, uwezekano wa mama kupoteza maisha wakati wa kujifungua unaongezeka kama atapoteza damu nyingi wakati huo, husababisha pia matatizo ya moyo na mapafu na huongeza hatari ya kushambuliwa na maradhi mbalimbali.

Mambo ya kuzingatia kuepuka matatizo hayo

Wakati wa ujauzito ni muhimi kuhudhuria kliniki kwa ajili ya ushauri kutoka kwa daktari.

Kinga dhidi ya malaria ni ya muhimu kwani malaria ni moja ya chanzo cha anemia kwa wajawazito wengi. Pia kupata kinga dhidi ya minyoo, lishe bora inayojumuisha madini ya chuma ikiwamo nyama, kuku, samaki, mayai, maharagwe mboga za majani kama spinachi na vyakula vyenye vitamin C kama juisi ya machungwa inayosaidia unyonyaji wa madini ya chuma kutoka kwenye mfumo wa chakula kwenda kwenye damu.

Mjamzito anashauriwa anywe chai na kahawa ili kuzuia madini ya chuma kutoka kwenye mfumo wa chakula kwenda kwenye damu, hivyo inashauriwa asitumie kwa pamoja na vyakula vya madini ya chuma.

Dk Keneth ni daktari mwanafunzi anayepamba na kuepusha vifo vya mama na mtoto anapatikana kwa namba ya simu 0759 775788.     

Friday, January 19, 2018

Vitamini A ya kwenye kiazi inapunguza kasi ya kuzeeka

 

By Hadija Jumanne

Viazi vitamu ni miongoni mwa vyakula vya wanga vyenye faida mwilini kwa sababu vina viini lishe na dawa lishe zinazoweza kukinga na kutibu baadhi ya maradhi.

Viazi vitamu vinastawisha mwili hasa ngozi bila kujali ni ya mwanamke au mwanaume hasa vile visivyowekewa vinasaba kwa lengo la kuongeza kiwango chake cha vitamin A ya asili.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Dawa, Marekani (U.S. FDA) imebainisha kiazi kimoja kikubwa kinaweza kumpatia mtu asilimia 100 ya Vitamini A inayohitajika mwilini kila siku.

Unapokula viazi vitamu unapata vitamin A, C , B5, B6, C, E na unapata madini ya potasiumu, magneziamu, fosforasi, manganese, zinki, wanga, sukali ya asili, nyuzi lishe, beta- carotene na choline zinazosaidia kustawisha ngozi ya mwanadamu na kuifanya nzuri na husaidia mtu kupata usingizi mzuri.

Taasisi ya Afya ya Marekani (NIH) inasema Vitamini A inayopatikana kwenye viazi inasaidia kupunguza kasi ya kuzeeka na inaimarisha afya ya macho.

Hata hivyo, Daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Duke, Jill Koury anasema upunguvu wa Vitamini A unasababisha sehemu ya jicho inayopokea mwanga kuharibika na kusababisha uoni hafifu. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitivo cha Sayansi ya Lishe cha Harvard, Shule Kuu ya Afya ya Jamii (HSPH), beta-Carotene inapunguza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo na tezi dume.

Pia, dawa lishe aina ya beta-Carotene inayopatikana kwenye viazi husaidia kudhibiti maradhi ya moyo, pumu na kupunguza kasi ya mwili kuchakaa.

Utafiti huo pia ulibainisha dawa lishe hiyo huwasaidia wanawake kutengeneza vichocheo muhimu wakati wa ujauzito na kunyonyesha huku madini ya potasiamu yaliyopo ndani ya viazi hivyo inasaidia kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu.

Vinasaidia kuondoa madini yasiyohitajika mwilini, kuboresha ufanyaji kazi wa moyo, kuboresha mapafu, kuimarisha kinga ya mwili na ni chanzo kikubwa cha beta-carotene. Faida nyingine ni chanzo cha madini ya chuma, potassium na calcium,    

Friday, January 19, 2018

Taasisi ya Moi yazidi kuchanja mbuga katika matibabu ya kibingwa nchini

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Mapinduzi katika tiba za kibingwa nchini yanazidi kufanikiwa baada ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) kuanzisha matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu (Arthroscopy).

Tangu kuanzishwa kwa matibabu hayo miaka miwili iliyopita, mafanikio yameonekana baada ya kuwatibu zaidi ya wagonjwa 314 kupitia utaalamu huo.

Kufuatia kuanzisha huduma hiyo, Moi imefanikiwa kuokoa Sh2.8 bilioni ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.

Daktari bingwa wa mifupa aliyebobea katika upasuaji wa matundu, Felix Mrita anasema baada ya mafanikio waliyoyapata kutokana na upasuaji wa goti, hivi sasa wamefanya upasuaji wa bega kwa wagonjwa 10.

“Upasuaji huu unahusisha matumizi ya hadubini maalumu inayoingizwa kwenye goti la mgonjwa kwa njia ya matundu, hali inayomfanya daktari arekebishe misuli na mishipa yenye hitilafu kwa kufuatilia kile anachokifanya kwenye runinga maalumu,” anasema Dk Mrita.

Anasema ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida, aina hiyo ya matibabu huleta ufanisi mkubwa na kulifanya goti la mgonjwa kuwa salama na kupona kwa haraka.

“Kwa wanamichezo au mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huu anaweza kurejea katika hali yake ya kawaida na kushiriki michezo, kutembea au kukimbia bila tatizo ndani ya kipindi kifupi,” anasema Dk Mrita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface anasema gharama za upasuaji huo kwa hapa nchini zinagharimu Sh3 milioni ikilinganishwa na nje ya nchi gharama zake ni Sh12 milioni.

Dk Boniface anasema taasisi hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa asilimia 95 na asilimia 5 zilizobaki zinatarajiwa kumalizika kipindi kisichozidi miezi sita ijayo.

“Aina hii ya upasuaji inawanufaisha wanamichezo na watu wengine ambao kwa bahati mbaya hupata maumivu makali ya goti na kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilazimika kufuata matibabu hayo nje ya nchi kwa gharama kubwa,” anasema Dk Boniface.

Anasema uanzishwaji wa aina hiyo ya upasuaji umefanikiwa baada ya taasisi ya Moi kuwapeleka madaktari wake bingwa wa mifupa nchini Misri kujifunza katika kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja walikojifunza mbinu za upasuaji huo.

Namna upasuaji unavyofanyika

Dk Mrita ambaye ni daktari wa wanamichezo pia, anafafanua zaidi, mara nyingi wagonjwa wa michezo majeraha yao huwa ndani ya goti, hivyo kupitia matibabu hayo ni rahisi mgonjwa kupona kwa uharaka na kurejea uwanjani ndani ya mwezi mmoja.

“Zamani tulikuwa tunalifungua goti, lakini kutokana na teknolojia, tunatoboa mashimo matatu moja linaingizwa kamera na mengine vifaa kwa ajili ya upasuaji,” anasema.

Anasema walio wengi hupata majeraha katikati ya mkunjo wa goti kati ya mfupa wa paja na mguu hasa kukatika, hiyo husababisha mgonjwa kusikia maumivu kila akikunja goti na wakati mwingine akitembea huanguka.

Anasema mara nyingi mgonjwa akipimwa kwa kutumia kipimo cha X Ray hatagundulika ana tatizo gani hadi afanyiwe kipimo cha MRI.

“Tunapofanya upasuaji huu, tunaingiza hadubini na vifaa vingine viwili kwa ajili ya kufanya upasuaji ndani kwa ndani na kama pamekatika na inahitajika kupiga msasa tunafanya hivyo, mgonjwa anapona na anatembea kama kawaida baada ya muda mfupi,” anasema Dk Mrita.

Anasema wapo wagonjwa ambao hukatika misuli ya ndani, awali ilikuwa lazima kulifungua goti kwa ajili ya kuzitengeneza, matibabu hayo yaliwasababishia jeraha kubwa na kupona kwake ilichukua muda mrefe tofauti na sasa.

Dk Mrita anasema kwa upande wa vifaa, kila mgonjwa hutumia vyakwake, lakini si gharama kubwa kwa hapa nchini kwani iwapo ana bima hulipiwa.

“Tunasonga katika huduma hii na tangu mwaka jana tulianza kupasua bega, tumewafanyia wagonjwa 10 na wengi ni wacheza mpira wa mikono na wa kikapu na wagonjwa wa kisukari.

Moja kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo, mchezaji wa Timu ya Afya Club, Bakari Msongamwanja anasema baada ya kufanyiwa upasuaji huo Septemba mwaka jana, ilimchukua mwezi mmoja kurudi uwanjani.

“Baada ya upasuaji, nililazwa siku moja nikaruhusiwa nikawa nafanya mazoezi ya kuchezesha mguu, baadaye nilianza kukimbia taratibu na baada ya mwezi mmoja nimerudi uwanjani nacheza vizuri namba yangu ni 6,” anasema Msongamwanja.

Hemed Salehe mkazi wa Bagamoyo alipata tatizo la goti na baadaye alifanikiwa kufanyiwa upasuaji huo.

“Nilifanyiwa upasuaji na nilipta nafuu ndani ya siku mbili, nilirudi nyumbani nilikoendelea na mazoezi kwa siku kadhaa, lakini baada ya mwezi mmoja niliendelea na shughuli zangu kama kawaida.”     

Friday, January 19, 2018

Dalili hizi zinaweza kuashiria una tatizo la kiafyaDk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

        Kutokana na shughuli za kila siku na sababu zitokanazo na hali ya hewa, ni kawaida mtu kujikuta akipatwa na uchovu na maumivu ya aidha baadhi ya viungo au mwili mzima. Lakini hali hiyo mara nyingi huwa ni ya muda mfupi tu na baadaye hutoweka. Lakini ni vyema kuwa makini na uchovu na maumivu ya mwili yanayodumu kwa muda mrefu mwilini. Watu wengi wanatabia ya kupuuzia baadhi ya dalili zinazojitokeza kwenye afya zao bila kujua chanzo cha dalili hizo. Naoma ifahamike kuwa tabia hii ni hatari sana kwa sababu matatizo yote yote makubwa ya kiafya huwa yanaanza na dalili ndogo ndogo ambazo wengi wamekuwa wakizidharau. Leo kupitia safu hii nitaeleza baadhi ya dalili mbalimbali zinazojitokeza kwenye afya zetu japo zinaonekana ni ndogo lakini hupaswi kuzifumbia macho kwa sababu zinaashiria tatizo fulani kwenye mwenendo wa afya kwa ujumla.

Dalili ya kwanza ni udhaifu wa kwenye miguu na mikono kunakoambatana na ganzi.

Ikiwa sehemu za mikono na miguu zinadhohofika, zinakosa nguvu na kupata ganzi na hasa zikitokea hadi usoni, inaweza kuwa ni dalili ya kiharusi na hasa kama hali hii inatokea upande mmoja tu wa mwili.

Sambamba na dalili hizo, kiharusi pia huambatana na dalili ya kuishiwa nguvu unapotembea unapata kizungunzungu, na kushindwa kutembea vizuri.

Nikukumbushe tu msomaji kiharusi ni ugonjwa unaosababishwa na matatizo ya usambazwaji wa damu kwenye ubongo kutokana na kuziba au kupasuka kwa mirija inayosambaza damu kwenye ubongo na kusababisha chembechembe za damu kufa.

Kiharusi ni moja ya maradhi yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla kwa miaka ya hivi karibuni.

Hivyo pata msaada wa kitabibu haraka ikitokea unapatwa na dalili hizo pamoja na zingine kama kutoona vizuri, maumivu makali ya kichwa, kuhisi kuchanganyikiwa au kupata shida unapozungumza. Dalili nyingine ni maumivu ya kifua. Maumivu yoyote ya kifua na hasa yanayoambatana na joto kali na kutokwa na jasho, upumuaji wa shida, na hata kichefuchefu yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kitabibu haraka.

Maumivu ya kifua yadumuyo kwa muda mrefu yanaweza kuwa ishara ya maradhi ya moyo au shambulio la moyo na hasa yakitokea wakati wa kufanya mazoezi au hata shughuli yoyote inayofanya mwili utumike.

Lakini pia maumivu ya mara kwa mara ya kifua yanaweza kuashiria tatizo lingine tofauti na moyo, kama kuganda kwa damu kwenye mapafu au mzunguko wa damu kutokuwa sawa kwenye mapafu.

Ukibaini dalili hizo nenda kamuone haraka kwa ushauri wa kitabibu kama hali hiyo inajirudia mara kwa mara.

Lakini dalili nyingine ni mkojo unaoambatana na damu. Yapo matatizo mengi ambayo yamezoeleka yanayoweza kusababisha kutoa mkojo uliochanganyika na damu, kama maambukizi ya kwenye njia ya mkojo na ya baadhi ya maradhi ya zinaa kama yatakuwa yamedumu kwa muda mrefu bila tiba. Kama unatoa mkojo uliochanganyika na damu ikiambatana na maumivu ya mgongo au ya chini ya kitovu ni ishara unashambuliwa na baadhi ya maradhi ya figo na hasa uwapo wa mawe madogo kwenye figo ambayo kitaalamu yanaitwa kidney stones.

Tatizo hili hutokea wakati mawe hayo yanajitengeneza na kujikusanya kwenye figo baada ya mkojo kuchujwa. Yale mabaki ya mkojo hutengeneza mawe hayo yatokanayo na ile chumvi chumvi. Hulazimika kutoka kupitia njia ile inayotumika na mkojo kutoka kwenye figo ndani hadi kwenye njia ya mkojo ya nje iliyoambatana na via vya uzazi. Hivyo kupitia mchakato huu, wakati mwingine huchubua njia ya mkojo na kusababisha majeraha madogo kwenye njia ya mkojo. Ni vyema kumuona daktari ili kuangalia uwapo wa aina hii ya mawe kwenye figo.

Lakini tatizo lingine kubwa, mkojo uliochnganyika na damu mara nyingi huashiria saratani ya kibofu na hasa ikitokea hauambatani na maumivu yoyote hivyo ni vyema kuwahi kupata vipimo ili kuliwahi tatizo hili katika hatua zake za awali.     

Friday, January 19, 2018

Zijue faida muhimu za meno ya bandia kwa afya ya kinywa

 

By Dk Onesmo Mbagati, Mwananchi

Meno ya bandia kama yanavyoitwa ni mbadala wa meno asilia. Meno haya huwekewa watu ambao ama wamepoteza meno kadhaa ama yote kinywani. Unapoyavaa kinywani huonekana kama meno asilia na yamejipatia umaarufu miongoni mwa watu ambao kwa namna moja ama nyingine hawana meno kadhaa ama yote ya asili kwenye vinywa vyao.

Ni nini kinachosababisha mtu kufikia hatua ya kupoteza meno yake ya asili

Zifuatazo ni miongoni mwa sababu zinazoweza kumsababishia mtu kupoteza meno yake ya asili.

Kwa mfano, maradhi ya fizi, meno kutoboka, kuoza na kisha kung’olewa, ajali za barabarani au michezoni pamoja na ugomvi kati ya wanajamii kwa sababu mbalimbali, ni miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu akapoteza meno au jino lake la asili.

Lakini pia kuna sababu ya mtu kuanguka na kapigiza mdomo chini, husabnabisha pia kung’oka kwa jina la asili au kushambuliwa na kujeruhiwa na wahalifu.

Hata hivyo kuna baadhi ya watu wanapokuwa na upungufu wa meno kinywani huona si tatizo, lakini ukweli ni kwamba hilo ni tatizo.

Tatizo lenyewe likoje?

Tunaambiwa meno yanayokuwa yamebakia huanza kujivuta na kusogeleana ili kufunika sehemu ile ambayo jino limeng’olewa.

Hatua hii ni ya kawaida kwa mwili wa binadamu na ndiyo maana hata uking’oa jino kwenye taya la chini, utaona jino la juu la usawa huohuo linarefuka kwa kadiri muda unavyozidi kwenda.

Baada ya muda hali hii huathiri ukutanaji wa meno pale mtu anapotafuna chakula.

Kwani meno yaliyong’olewa husababisha taya na ufizi kusinyaa na kusababisha kubonyea kwa mashavu na hii husababisha mtu kuonekana mzee kuliko umri wake halisi.

Taya ambalo limepoteza meno huanza kupunguza uzito wake wa asili. Hii ni kwa sababu mizizi ya jino iliyojishika kwenye taya ambayo ni muhimu kwa ukuaji na udhibiti wa uzito wa taya inakua haipo tena.

Mizizi hiyo ya jino ndiyo huchochea ukuaji wa taya pamoja na kuhakikisha linakua na uzito stahiki.

Hivyo, ili kuhakikisha mtu unakua na meno imara na yenye afya, ni muhimu kulinda afya ya kinywa na mwili kwa ujumla.

Lakini katika nyakati hizi, ni kawaida kwa watu kuwa na meno ya bandia kama mbadala wa meno ya asili kutokana na sababu mbalimbali kuu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na tabasamu la uhakika mbele ya jamii zao.

Je kuna ina ngapi ya meno ya bandia

Meno ya bandia ambayo hutengenezwa ili yafanye kazi kama meno asili, yako ya aina mbalimbali.

Na mtu hutengenezwa kulingana na uhitaji, uwezo wa kifedha pamoja na hali yake ya kiafya baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake ya kinywa na wataalamu wa meno.

Mfano meno ya kuvaa

Haya ni yale ambao muhusika ana uwezo wa kuyavaa na kuyavua kwa ajili ya kuyafanyia usafi na huwa na uwezo wa kuyavua usiku kabla ya kulala.

Meno haya huweza pia kuwekwa kwa ajili ya meno ya mbele na hata ya nyuma, pamoja na watu waliopoteza meno yote kinywani.

Meno ya moja kwa moja

Haya ni meno ambayo mara yawekwapo hayawezi kutolewa na mtu aliyewekewa na daktari.

Mara nyingi hufanyika kwa meno ya mbele na kwa meno machache yaani tuseme jino moja mpaka matatu.

Hii ni kwa sababu kadiri yanavyozidi kuwa mengi, ndivyo uimara wake unavyopungua na uwezekano wa kuvunjika unavyoongezeka. Aina hii ya meno ya bandia haiwezekani kwa mtu ambaye hana meno kabisa kinywani.

Meno ya kupandikiza

Aina hii ya meno ndiyo yenye gharama kubwa kati ya meno yote ya bandia kutokana na hatua za utengenezwaji, dawa pamoja na vifaa vitumikavyo.

Meno haya hupandikizwa kwenye mfupa wa taya na huweza kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Je meno ya bandia huweza kutumika kwa muda gani?

Aina mbalimbali za meno ya bandia huweza kutumika kwa muda tofauti kulingana na aina au meno husika. Lakini kikubwa ni kuzingatia masharti ya utunzaji wa meno hayo.

Meno ya kuvaa na kuvua huweza kutumika kwa muda usiozidi miaka saba na baada ya muda huo inashauriwa kubadili kwani kitaalamu yanakuwa yameshachoka.

Meno ya Moja kwa moja na kupandikia haya huweza kukaa muda wa miaka kumi.

Maswali, maoni na Ushauri 0683-694771     

Friday, January 12, 2018

Watoto na tishio la kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Miaka ya zamani ilikuwa kawaida kuona wanafunzi wakikimbia mchakamchaka huku wakiimba nyimbo za kusifia, kukosoa, kujenga uzalendo na hata zile zilizokuwa zikimpinga Nduli Idd Amini.

Wapo waliodhani mchakamchaka ni kwa ajili ya kujifurahisha tu kumbe lah! Wanafunzi walikimbia ili kuimarisha afya zao na kujikinga na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Siku hizi hali imebadilika. Shule nyingi wanafunzi wake hawakimbii mchakamchaka wala hawafanyi mazoezi.

Mratibu wa maradhi yasiyo ya kuambukiza Mkoani Dar es Salaam, Dk Digna Riwa anasema aina ya maisha ya watoto wanayoishi siku hizi inawaweka kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi yasiyoambukiza.

Akizungumza katika uzinduzi wa mchakamchaka shuleni, uliofanyika katika Manispaa ya Ilala hivi karibuni, Dk Riwa anasema watoto wengi wanakosa muda wa kufanya mazoezi huku wakipatiwa vyakula vya mafuta, jambo linaloendelea kuhatarisha maisha yao.

“Lipo tishio kubwa kwa watoto kupata maradhi yasiyo ya kuambukizwa hasa ya moyo na pumu kwa sababu, hawana mazoezi ya afya,” anasema.

Watoto wengi wakiamka asubuhi hukutana na usafiri wa kuwapeleka shuleni, na kurejeshwa nyumbani, wanafungiwa huku wakila vyakula vingi vya mafuta hii ni hatari,” anasema daktari huyo.

Maradhi yasiyo ya kuambukiza ni yale ambayo hayasambai kwa mtu yeyote kwa kuwa hayana vimelea vinavyohusiana na maradhi hayo.

Maradhi hayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, athma (Pumu) na saratani.

Dk Riwa anasema ugonjwa wa pumu na moyo ni tishio zaidi kwa watoto.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya Kinga dhidi ya Magonjwa (CCP-Madicine Medical Centre), Dk Frank Manase, anasema maradhi hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha maumivi ya mwili, akili na kiroho kwa familia nyingi za Kitanzania.

“Kitendo cha kupoteza kiungo kimoja mfano mguu au jicho wakati bado unayahitaji, yaweza kuleta mateso yasiyovumilika kwa mtu yeyote,” anasema.

Anasema zipo familia nyingi zimeporomoka kiuchumi kwa sababu ya kuwa na mmoja wa wanafamilia mwenye moja ya maradhi sugu.

Kwa nini mchakamchaka kwa wanafunzi

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Nito Pallera anasema shule nyingi hazina utaratibu wa wanafunzi kukimbia mchaka mchaka jambo ambalo ni hatari kwa afya za watoto.

Dk Manasema anasema miezi sita iliyopita waliweka kambi ya upimaji afya wakitizama hasa maradhi ya moyo, seli mundu (sickle cell disease) afya ya akili, kinywa na meno, pua, koo na masikio.

Anasema matokeo waliyokutana nayo yaliwatisha kiasi cha kufikiria nini cha kufanya ili kuwasaidia watoto.

Walibaini wengi wao wanasumbuliwa na maradhi ya athma, moyo na mengine kwa sababu ya kutopimwa afya zao wala kufanya mazoezi.

“Kwetu sisi tafsiri ya mchakamchaka siyo michezo kama wengine wangesema, bali ni njia ya kupima afya, kutoa kinga ya afya na pia ni tiba kwa maradhi,” anasema Dk Manase.

Anasema kiuhalisia mtoto mwenye matatizo ya moyo, sickle cell, au pumu akiambiwa akimbie mchakamchaka na wenzake hataweza kumaliza nao kwa wakati mmoja.

Kwani atataka apumzike mara nyingi njiani na hataweza kumaliza kwa wakati kama wenzake.

“Hivyo kuna uhitaji wa kambi ya upimaji afya ili kuwabaini hawa watoto wenye maradhi, hivyo kupitia mchakamchaka, itakuwa kipimo tosha cha afya kwa upande mmoja,” anasema.

Anasema maradhi yasiyoambukiza huweza kusababisha vifo vya ghafla na mtoto mwenye pumu asipopata huduma ya haraka na sahihi, anaweza kupoteza maisha ndani ya dakika chache.

“Hivyo kumtambua mtoto mwenye pumu ni muhimu sana kuliko hata kuwa na wodi ya kumlaza inapombana,” anasema Dk Manase.

Hali ya maradhi kwa watoto

Wataalamu wa afya wanasema kutokana na hali ya maisha kubadilika na watu kubadili mienendo ya maisha kwa kula vyakula vya kisasa, vingi vikiwa ni vile vinavyozalishwa viwandani, maradhi yasiyo ya kuambukiza yameanza kubisha hodi kwa kasi kubwa kwa watoto na vijana.

Takwimu zilizotolewa na Baraza la Afya Duniani kupitia Mzunguko wa Malengo ya Lishe (2025), zinaonyesha katika kila watoto 25 walio chini ya umri wa miaka mitano Tanzania, watano kati yao wanakabiliwa na tatizo la uzito uliozidi kiasi jambo ambalo ni hatari.

Pia, takwimu za kituo cha maradhi ya kudhibiti uzito nchini Marekani zinaonyesha kati ya watoto watano, mmoja anauzito uliokithili au mkubwa.

Kwa mujibu wa Jarida la tiba la Uingereza, ‘The Lancet’, Volume 387, la Aprili 2, 2016, vifo vinavyotokana na kunenepa kupita kiasi ni mara tatu zaidi ya vifo vinavyosababishwa na kukosa chakula chenye lishe, ingawa bado nchi nyingi zinapambana na ukosefu wa chakula.

Wataalamu hao wanasema unene huyo ndiyo unawaweka watoto kwenye hatari ya kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Hali hiyo inawaweka katika hatari zaidi ya kupata maradhi hayo wakati wa kubalehe na ujana wao.

Wataalamu wa lishe kutoka Jukwaa la Lishe nchini (Panita), wanasema unene kupita kiasi ni ugonjwa wa utapiamlo utokanao na kula kupita kiasi.

Wataalamu hao wanasema matajiri na watu wenye kipato cha juu nchini ndiyo walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na kula vyakula vya gharama na visivyo na tija kwenye mwili.

“Kunenepa kupita kiasi maana yake ni mtu kuwa na uzito uliozidi wakati uzito wa mwili wake unakuwa mkubwa ukilinganishwa na mwili wake, huu ndiyo utapiamlo,” anasema Ofisa wa Panita, Lucy Maziku.

Maziku anasema utafiti unaonyesha matukio ya watu kunenepa kupita kiasi yanaongezeka jambo linaloongeza ukuaji wa tatizo la utapiamlo, sio tu kwa maradhi nyemelezi.

Hatua zinazochukuliwa

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Pallera anasema atasimama kuhakikisha wanafunzi wa manispaa hiyo wanatengewa muda wa kukimbia mchakamchaka kama njia ya kupambana na maradhi hayo.

Anasema hakuna ubishi kwamba njia pekee itakayowawezesha kutimiza malengo yao ni afya njema inayotokana na ufanyaji wa mazoezi, lishe bora na elimu nzuri.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anakiri kuwapo kwa tishio hilo na kuwataka wazazi kushiriki kuhakikisha watoto wao wanakuwa na afya bora kwa kuwafanyisha mazoezi badala ya kuwafungia ndani, huku wakitumia magari kwenda na kurudi shule.

Wanafunzi walonga ugumu wa mchakato

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi walisema itakuwa vigumu kwao kufanya mazoezi kutokana na baadhi ya shule kukosa maeneo ya michezo.

Ofisa Elimu, Ofisi ya Kamishna wa Elimu, Kenneth Konga anasema ipo haja kwa shule zote kuhakikisha zinatenga maeneo ya wazi kwaajili ya michezo kama sera inavyotaka.

Anasema changamoto pekee inayozikaba shule hizo ni kutokuwapo kwa maeneo hayo jambo ambalo linahatarisha afya za watoto.

Friday, January 12, 2018

Haya hapa madhara ya kuchelewa kuanza kliniki

 

By DK Kammu keneth, Mwananchi

Mwanamke anapopata ujauzito huwa na mawazo ni lini hasa anatakiwa aanze kuhudhuria kliniki ya afya ya uzazi.

Kwani wengi wao hawafahamu ni lini ndiyo muda muafaka wa kuanza kuhudhuria kliniki na wengi wao huchelewa kuanza kupata huduma hiyo.

Lakini wataalamu wa afya wanatuambia kliniki ya afya ya uzazi kwa mjamzito ni pale tu anapogundua kuwa ni mjamzito.

Wanasema ni vizuri hata kabla mwanamke hajashika ujauzito yeye na mwenzi wake wanaweza kuanza kuhudhuria kliniki.

Hii ni njia nyepesi inayoweza kuwafanya wazoee kuhudhuria kliniki hata wakati wa ujauzito.

Kliniki ya afya ya uzazi si kliniki ya wanawake pekee bali hata wanaume inawahusu.

Mara zote inashauriwa mjamzito anapoanza kliniki anatakiwa aende mwenza wake. Kuanza kliniki mapema kuna faida ikilinganishwa na mjamzito anayechelewa kuanza.

Kwani akiwahi kutamsaidia kupata huduma stahiki mapema na kuchelewa huweza kusababisha kukosa baadhi ya huduma katika kipindi cha ujauzito.

Naijulikane kwamba kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito kuna umuhimu mkubwa maana hili jambo limekuwa mara nyingine likichukuliwa kama ni la kawaida na halitiliwi mkazo na watu wengi.

Mahudhurio hafifu au kutohudhuria kliniki kunaweza kusababisha matatizo kwa mtoto au mama kabla au wakati wa kujifungua.

Kwanini jambo hili linatiliwa mkazo

Upimaji na matibabu ya maradhi ya zinaa, yakiwamo ya klamidia kisonono, kaswende, trikomonasi, UkimwiI na homa ya ini hupewa kipaumbele kutokana madhara yanayoweza kumkumba mama au mtoto katika kipindi cha ujauzitoa au wakati na baada ya kujifungua.

Maambukizi ya maradhi kama Ukimwi kama mjamzito atakuwa nayo, humsababishia mfumo wa kinga mwilini mwake dhidi ya maradhi kuwa hafifu.

Hali hali hiyo humuweka mjamzito katika hatari ya kushambuliwa na maradhi mbalimbali nyemelezi yanayoweza kuathiri ujauzito wake.

Pia utambuzi wa maambukizi ya VVU husaidia wauguzi kupanga namna sahihi ya kumzalisha mjamzito huyo ili kuepusha maambukizi kwa mtoto.

Kisonono hushambulia mfumo wa uzazi na mkojo.

Hali hii husababisha mfereji wa mkojo kuziba.

Mara nyingi mtoto huambukizwa ugonjwa huu mama anapojifungua na humsababishia mtoto kuugua maradhi ya meno.

Kaswende huwa na tabia ya kusambaa sehemu nyingine za mwili kama kwenye moyo na mifupa.

Na kama utashambulia mfumo wa fahamu, unaweza kusababisha homa ya uti wa mgongo inayoitwa kwa jina la kitaalamu meningitisi na hata mtoto aliyeko ndani ya mfuko wa uzazi anaweza pia asiumbike kikamilifu au anaweza kupoteza maisha.

Trikomatisi husababisha kupasuka kwa chupa mapema na kumfanya mjamzito ajifungue katika muda usio sahihi au mama anaweza kujifungua mtoto njiti.

Klamidia unaweza kusababisha uvimbe kwenye fupa nyonga, hivyo kuharibu tishu zinazohusiana na uzazi.

Hali hiyo humsababishia matatizo mjamzito hata wakati wa kujifungua na mara nyingine humsababishia kifo.

Kwa upande wa mtoto inaweza kumsababishia maambukizi kwenye njia ya hewa hasa kwenye mapafu na huweza pia kumsababishia upofu kama macho yatashambuliwa.

Mardhi ya Malaria kipindi cha ujauzito yanaweza kusababisha kujifungua kabla ya muda na huweza kusababisha mimba kutoka, maradhi ya anemia sugu, maradhi kwenye kondo la nyuma, kujifungua mtoto njiti, hivyo kumuweka katika hatari ya kupoteza maisha ndani ya siku 28 baada ya kuzaliwa.

Hivyo, ni muhimu kwa mjamzito kutumia chandarua chenye dawa wakati wa ujauzito na kuhudhuria kliniki kwa ajili ya kupatiwa dawa za kinga dhidi ya malaria.

Je tetenasi nayo inamadhara gani?

Tetenasi ni moja ya maradhi yanayoongoza kwa kusababisha vifo kwa wajamzito na watoto wachanga hasa katika nchi zinazoendelea. Hivyo, ni muhimu kukamilisha chanjo yake.

Kipindi cha ujauzito kuna uhitaji mkubwa wa damu katika mwili wa mjamzito ili kukidhi mahitaji ya mama na mtoto.

Kwa kutambua umuhimu huo, wajawazito hupatiwa dawa kwa ajili ya kuongeza kiwango cha damu kila waendapo kliniki.

Pia hupatiwa dawa za minyoo ili kuzuia maradhi ya kuhara. Mardahi hayo husababisha upungufu wa maji na damu kama mjamzito ataugua.

Maradhi mengine hatarishi ni UTI. Mama akienda kiliniki hupimwa na akigundulika kuugua, hupatiwa matibabu mapema kwa sababu yanaweza kusababisha mimba ikatoka au kujifungua mtoto njiti.

Kuhudhuria kliniki husadia pia kutambua maendeleo ya ukuaji wa mtoto aliyeko tumboni.

Kama una maswali wasiliana na Dk Kammu kwa simu namba 0759 775788

Friday, January 5, 2018

Njombe inavyokabiliwa na utapiamlo mkali licha ya chakula kedekede

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

“ Sijui kwa nini mtoto wangu anaumwa kiasi hiki wakati kila siku anakula mara tatu. Asubuhi, mchana na usiku. Hali yake ilikuwa mbaya na tulikata tamaa. Tusingepata ushauri wa madaktari na kuambiwa ni utapiamlo, mjukuu wetu angepoteza maisha.” Ndivyo anavyosema Josephine Mfumbilwa, mkazi wa Kitongoji cha Igominyi, mkoani Njombe akisimulia hali aliyonayo mjukuu wake.

Bibi huyu anaishi na mumewe Petro Mangula, pamoja na mjukuu wao wa miaka mitatu aliyedhoofu kutokana na ukosefu wa lishe bora. Licha ya kuwa na umri wa kutembea, mtoto huyo hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo hadi alipoanzishwa lishe maalum chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya ya msingi wa Kijiji cha Nyombo, Leonard Mfikwa. Nyumba ya Mfumbilwa imezungukwa na mashamba yenye viazi, mahindi, maharage na mboga za majani lakini bado mtoto huyo amedhoofika kwa udumavu. Familia ina ng’ombe na kuku wa kienyeji. Kadi yake ya kliniki ya mtoto huyo inaonyesha uzito wake ni kilo nane ingawa alipaswa kuwa na kilo zaidi ya kilo 15.

Baada ya kuhangaika naye sana, wazee hawa waliamini mjukuu wao amerogwa, kabla hawajagundua ni utapiamlo. Mfikwa anasema asingeingilia kati, huenda mtoto huyo angepoteza maisha. Utapiamlo si tatizo linaloitesa familia hiyo pekee. Ni ugonjwa unaowaumiza watoto wengi Njombe licha ya mkoa huo kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara.

Takwimu zinaonyesha Njombe ni kati ya mikoa vinara wa uzalishaji wa mazao ya chakula ingawa umo kwenye orodha ya iliyoathirika kwa watoto wenye udumavu kwa asilimia 49.4. Taarifa iliyosomwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) Septemba 2017, unakadiriwa kuvuna zaidi ya tani milioni 1.35 za mazao ya chakula na kuwa na ziada ya tani milioni 1.06 kwani mahitaji yake ni tani 171,771 tu.

Ofisa lishe wa mkoa huo, Ester Kibona, anasema kiwango cha udumavu kimepungua kutoka asilimia 52 iliyobainika mwaka 2010 mpaka silimia 34 kulingana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Takwimu za Baraza la Afya Duniani zinaonyesha katika kika watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano nchini, wawili wamedumaa. Ingawa kati ya mwaka 1992 hadi 2014 kiwango cha udumavu nchini kilipungua kwa asilimia 30, idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 2.4 hadi milioni 2.7 katika kipindi hicho. Shirika la Afya la Dunia (WHO) linaonyesha kila siku, zaidi ya watoto 270 wenye chini ya miaka mitano hupoteza maisha nchini kutokana sababu mbalimbali ikiwamo lishe duni. Sababu Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kipaumbele cha wazazi na walezi wengi wa Njombe ni kazi. Huwa na muda mfupi wa kuhudumia watoto na hawana uelewa wa kutosha wa chakula bora. Kukosekana kwa uelewa wa lishe kamili ni sababu kubwa ya mkoa huo kuongoza kwa udumavu.

Wazazi na walezi wengi wametingwa na shughuli za shamba na kuwasahau watoto.

Familia nyingi zina tatizo hilo ingawa zina akiba ya chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya makuzi ya watoto zilizonao.

Ofisa lishe huyo anasema kutozingatia lishe bora katika siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto tangu mimba inapotungwa mpaka mtoto anapofikisha miaka miwili inachangia kwa kiasi kikubwa mkoa huo kuwa na udumavu.

Anania Danda, mkazi wa Kata ya Kichiwa anasema mara nyingi, kipindi cha kilimo, hulazimika kuwaachia kiporo watoto wake kwa ajili ya chakula cha asubuhi na cha mchana ili amudu shughuli zake bila kupoteza muda.

“Huwa nawaachia kiporo cha ugali na maharage jikoni ninapojihimu shambani,” anasema Danda.

Muuguzi wa Zahanati ya Mlewela, Josephine Nyongole anasema kijiji hicho kina watoto wenye utapiamlo pia kutokana na sababu hizo. Wazazi hawajali lishe ya watoto.

Mganga wa Zahanati ya Nyombo, Leinisa Amulike, anasema utapiamlo ni hatari ikiwa wazazi wengi wataendelea kupuuzia lishe kwa watoto wao. “Wazazi wengi hawajali watoto, hawapangi ratiba kwa ajili ya chakula na wametingwa na kilimo. Hii ni hatari kwa makuzi ya watoto,” anasema.

Mtaalamu kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Lucy Maziku anasema udumavu ni sababu kubwa ya kuugua mara kwa mara kwa mtoto katika siku 1,000 tangu azaliwe.

Nyingine ni taratibu usiofaa wa kuwalisha watoto wachanga na wadogo ikiwamo kutowanyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa.

“Unapompa mtoto chakula kisicho na ubora, yaani virutubisho vinavyotakiwa, unamuweka kwenye hatari ya kupata udumavu,” anasema.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita kabla hajaanza kupewa chakula kingine chenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali.

Lucy anasema lishe duni ya wanawake kabla, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua inaweza kusababisha mtoto kupata udumavu.

Hali ya vijijini

Bibi Mfumbilwa hakutarajia katika umri wa zaidi ya miaka 70 atakuja kulea mtoto mwenye utapiamlo. “Kijana wangu anaishi Dar es Salaam. Alimpa mimba binti wa watu wakaja wote hapa. Tulilea mimba hadi alipojifungua. Matokeo yake walipoondoka, mama yake akamtelekeza mwanae na kukimbia,” anasema.

Baada ya kuachiwa mjukuu huyo, anasema hali ya mtoto ilianza kubadilika na hospitali wakaambiwa ana utapiamlo. “Kumbe hatukuwa tunamlisha vizuri,” anasema.

Emilia Lucheza, mkazi wa Kijiji cha Ikuna ambaye mtoto wake alizaliwa akiwa na kilo 3.5 lakini akapungua uzito hadi kilo 1.5 anasema hajui kwa nini mwanae alipata utapiamlo.

“Labda kwa sababu nilikuwa nashinda shambani ndiyo maana mtoto aliumwa, lakini nilikuwa namlisha,” anasema.

Anasema baada ya kupewa rufaa kutoka zahanati ya kijiji hadi Hospitali ya Mkoa wa Njombe na kupata matibabu, afya ya mwanae iliimarika. “Walinifundisha. Siku hizi namsimamia na ninahakikisha kwenye kila mlo nampa matunda,” anasema.

Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Ikuna, Safina Sanga, anasema hali ya mtoto huyo ilikuwa mbaya lakini baada ya usimamizi wao amepona.

Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Mlewela, January Nkinda anasema japo baadhi ya watoto wenye utapiamlo kijijini kwake, bado anajifunza namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Athari

Wataalam wa lishe na afya wanasema zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya watoto wenye utapiamlo hutokea katika mwezi wa kwanza wa maisha yao. Baraza la Afya Duniani linasema mtoto akidumaa hupata athari zisizoweza kurekebishika kwani hudumu katika maisha yake yote.

Miongoni mwa athari zinazotajwa kwenye kitabu cha baraza hilo cha mwaka 2015 ni udumavu wa akili jambo linaloweza kumfanya mtoto ashindwe kumudu masomo darasani.

“Ikiwa tatizo hili litaendelea kuwakumba watoto, linatishia kuwapo kwa wataalamu wa kutosha siku zijazo,” anasema mtaalamu mratibu wa Panita, Jane Msagati.

Watu wazima ambao walikuwa na udumavu utotoni hupungukiwa uwezo wa kufanya kazi hali inayosababisha kupungua kwa tija na mapato ya kiuchumi.

Ushauri

Miongoni mwa malengo ya Baraza la afya Duniani ni kupunguza idadi ya watoto waliodumaa kwa asilimia 40.

Ofisa lishe wa Njombe, Kibona anasema chini ya ufadhili wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) wanaendelea kupambana na udumavu ili kuokoa maisha ya watoto. Anasema Serikali imeamua kulivalia njuga suala hilo ili kuondokana na aibu ya kuwa juu kwa takwimu za utapiamlo.

Mhudumu wa afya Kijiji cha Ikuna, Japheth Ngimbudzi anasema kazi kubwa anayoifanya kijijini hapo ni kuzizungukia familia zenye watoto ili kutoa elimu ya namna ya kuwalisha.

Upo mkakati wa kutoa elimu ya chakula cha watoto, usafi wa mazingira na mwili, malezi na kuzingatia kanuni za afya kupambana na tatizo hilo.

“Wenye utapiamlo tunawasimamia wapate matibabu na tunapambana kuimarisha utoaji wa matone ya vitamini A, dawa za minyoo, upimaji wa hali ya lishe na kutoa rufaa kwa watoto wenye utapiamlo,” anasema.

Kingine kinachofanyika ni kuwafundisha wananchi umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto pamoja na kuwaelimisha kuhusu uzalishaji, uhifadhi na matumizi ya vyakula vyenye viinilishe vya kutosha kwenye mashamba darasa yaliyopo.

Friday, January 5, 2018

Kutoa mimba kadhaa hakuondoi uwezo wako kuzaaDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Karibuni wasomaji wa kona hii ya piramidi ya afya, leo nimeona nitumie nafasi hii kujibu moja ya swali ambalo linafanana na mengine yanayoulizwa.

Swali likuwa hivi (jina nimehifadhi) : Hivi mtu aliyewahi kutoa mimba mara mbili na mpaka dakika hii bado hajapata ujauzito, je hapo baadaye akipata ujauzito ataweza kuzaa vizuri bila kupata shida yoyote? Na je atawahi au atachelewa kuzaa?

Ni swali ambalo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara hasa na wanawake wengi ambao waliwahi kutoa mimba kwa makusudi au kwa sababu za kitabibu kama vile kuumwa au mimba kuharibika yenyewe.

Nitajibu swali kutokana na alivyouliza msomaji, kwakuwa umetumia neno kutoa mimba ina maana ilitolewa kwa kudhamiria yaani kinyume na sheria ambayo kwa lugha ya kitabibu tunaita illigeal abortion.

Kutoa mimba kinyume na sheria ni uondoaji wa kiumbe kilichotungwa kabla ya muda wa kuzaliwa haujafika pasipo sababu ya kitabibu.

Katika swali lako hukuweka umri wa mimba zilizotolewa wala muda gani uliokaa bila kushika ujauzito mwingine ila nitajibu. Ieleweke kuwa si lazima utolewaji wa mimba kuwa na muingiliano wa uwezo wa mwanamke kupata mimba, jambo la msingi ni utoaji uwe ni salama na usio na madhara yoyote.

Katika nchi ambazo kutoa mimba si uvunjaji wa sheria, wanawake wengi hutolewa mimba na kuwa salama bila kujitokeza kwa madhara yoyote na baadaye huweza kupata ujauzito mwingine wakiwa tayari kufanya kwa hilo.

Endapo mwanamke aliyetoa atajamiiana bila kinga yoyote anaweza kupata mimba nyingine ndani ya wiki mbili zitakazofuata baada ya yai lake la uzazi kupevuka.

Mtu anaweza kutoa mimba hata mara tano na akawa na uwezo wa kuzaa wakati wowote kama tu utoaji ulifanywa kwa kuzingatia utaratibu unaotakiwa na hakuna madhara yoyote yaliyojitokeza.

Madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutoa mimba nipamoja na maambukizi ya via vya uzazi, majeraha ya mlango wa uzazi na ndani ya mfuko wa uzazi ndiyo yanayoweza kusababisha mtu kushindwa kupata ujauzito hapo baadaye au akipata inatoka.

Utoaji wa mimba kila mara bila ushauri wa daktari unaweza kusababisha majeraha katika mlango wa uzazi na kuufanya kuwa dhaifu na wakati wakubaeba mimba zinaweza kutoka.

Maambukizi ya nyumba ya uzazi yanaweza yakatokea wakati au baada ya mimba kutolewa hivyo kutokea kwa maambukizi kwenye via vya uzazi ikiwamo mirija kuharibika.

Kuwahi au kuchelewa kuzaa hili litategemea kama hakuna madhara yoyote yalijitokeza na mizinguko ya hedhi kurudi kama kawaida.

Inashauriwa kitaalam, mwanamke aliyetoa mimba au mimba yake kuharibika na kusafishwa apumzike kwa kipindi kati ya miezi 6 mpaka 12 au mwaka mzima kabla ya kushika ujauzito mwingine.

Kufanya hivi ni kuupa mwili nafasi ya kujijenga upya na homoni kurudi katika utaratibu wake wa awali. Kumbuka, mimba inapotungwa kunatokea mabadiliko mengi mwilini ili kuandaa mazingira ya ukuaji wa mimba iliyotungwa.

Ni muhimu kuepukana na mimba zisizotarajiwa hasa kwa wasichana wanaosoma hii ni kutokana kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwamo kuachishwa masomo au kwenda zahanati za uchochoroni kutoa mimba hiyo.

Ikumbukwe kuwa mtaani watu hufanya pasipo kuwa na ujuzi wala kuzingatia usafi wa vifaa jambo ambalo linaongeza hatari ya kupata maambukizi ya maradhi mengine. Kwa watu wazima ni muhimu kutumia njia salama za kupanga uzazi.

Friday, January 5, 2018

Unaweza kuepuka, kutibu meno kuwa rangi ya kahawia

 

By Dk Onesmo Kapugi, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kwa kawaida, meno hutakiwa kuwa meupe lakini kutokana na sababu mbalimbali huweza kuwa na rangi nyingine.

Meno yaliyoharibika rangi humuathiri mhusika kisaikolojia. kwa mfano anaweza kujishtukia wakati wa kuzungumza. Hali hii husababisha kutojiamini anapokuwa na watu wenye meno meupe walau kuliko yeye katika shughuli mbalimbali.

Kwakuwa rangi ya meno itokanayo na kuzidi kwa madini ya floridi huwa haitoki kwa kupiga mswaki, wengi wa waathirika hudhani meno yao ni machafu hata baada ya kupiga mswaki

Hali hii ni matokeo ya tatizo linalotokea kwenye tabaka la nje la meno wakati wa utengenezwaji wa meno husika linalosababishwa na kuwapo kwa kiasi kikubwa cha madini ya floridi kuliko kiwango kinachohitajika.

Hali hii husababisha tabaka la nje la jino lililoathirika kuwa na madini mengine kwa kiwango kidogo wakati madini ya floridi yakiwa mengi kupita kiasi huku tabaka hilo likiwa na vitundu vidogo vidogo (porosity). Hivyo kuyafanya yasiweze kusafishika kwa kupiga mswaki.

Ukubwa wa tatizo hili kwa muhusika hutegemea vitu vingi kama vile umri ambao muathirika amekumbwa na madini hayo kwa wingi au namna mwili wake unavyoyapokea madini hayo. Sababu nyingine ni ukuaji wa mifupa, hali ya lishe kwa ujumla na matatizo ya figo.

Wakati tatizo la kuzidi kwa madini ya floridi huathiri mifupa yote mwilini, athari zinazotokea kwenye meno ya ukubwani ndio changamoto inayopewa kipaumbele zaidi na watu wengi kwani huathiri muonekano wao mzuri wa muhusika hivyo kumnyima uhuru sehemu nyingi anazokuwapo.

Maambukizi

Izingatiwe, kuzidi kwa madini ya floridi kupita kiasi kwenye meno huanza kwa watoto wakiwa wadogo wenye miezi 20 mpaka 30. Halikadhalika ni muhimu kujua kuwa umri mpaka miaka minne ya mtoto bado anakuwa katika kipindi hatarishi cha kuwa na meno yaliyoathiriwa na madini haya katika utu uzima wake. Hata hivyo kuanzia miaka minane na kuendelea, mtoto hawezi kuathirika tena.

Kiwango salama cha madini ya floridi kwa binadamu ni 0.05 to 0.07 mg F/Kg/kwa siku. Kiasi chochote juu ya kiwango hiki husababisha kuongezeka kwa uwezekano wa kuwa na meno yaliyoathirika.

Athari za kuzidi kwa madini ya floridi hivyo kuathiri rangi ya meno zinaweza kuepukwa kwa kudhibiti kiasi cha madini ya floridi ambayo mtoto anapewa mpaka umri usiopungua miaka sita.

Vyanzo vya floridi

Madini ya floridi hupatikana kwa wingi, japo kwa uchache, kwenye maji tunayotumia kwa shughuli mbalimbali kama vile kunywa au kupikia, magadi ambayo hutumia wakati wa kupika vyakula mbalimbali kama vile mrenda na maandazi au kwenye dawa za meno tunazotumia kupigia mswaki.

Madini ya floridi ni maarufu na hujulikana sana kwa uwezo wake wa kuzuia meno kutoboka. Kwa ujumla, madini haya husaidia sana kuimarisha mifupa yote katika mwili wa mwanadamu. Umuhimu wake huonekana zaidi linapokuja suala la uimara wa meno.

Utengenezwaji wa meno, kwa kiasi kikubwa, huhusisha muunganiko wa madini ya phosphorus na calcium ambapo kuongezeka kwa madini ya floridi hufanya muunganiko huo kuwa mgumu zaidi kuweza kuhimili shughuli zote zifanywazo na meno.

Kwa lugha nyepesi, kutokuwepo kwa madini haya mwilini huyafanya meno kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kutafuna, kung’ata au kingine chochote kinachoweza kufanywa na meno.

Madhara ya floridi

Kila kitu ikizidi mahali kinapopaswa kutumika huwa kunakuwa na madhara yanayojitokeza. Hata kuzidi kwa madini ya floridi kwenye meno nako kuna matokeo kam ahayo kutegemea wingi wa madini yaliyozidi.

Kwa kutambua kigezo hicho, tunaweza kwa ajili ya kueleweka kuyagawa katika makundi kulingana na mtazamo wa muhusika na jamii kwa ujumla.

Madhara kidogo. Kundi hili lina watu ambao meno yao yana weupe wa chaki. Hii inaweza kujitokeza kwa jino zima au sehemu ya jino, huenda ikawa kinywa kizima.

Wapo wenye madhara ya wastani. Hii ni kwa ile hali ambayo meno huwa na rangi ya kahawia kwa mbali. Hii husababisha aibu kwa baadhi ya wenye tatizo hilo kiasi cha kuwa wahanga wa kujihisi wenye kasoro kwenye jamii.

Baadhi ya waathirika huwekwa kwenye kundi la wenye madhara makubwa kwa kuwa ni watu ambao meno yao huweza kuvunjika ama kukatika hivyo kuwafanya wapate ganzi ama meno husika kuwa yanauma wakati wa kula ama kunywa. Mara nyingi kundi hili ndilo ambalo wengi wao, meno yao huvunjika vunjika na kutokuwa na sura nzuri. Hawa wanahitaji kuwa makini zaidi ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuvunjika au kukatika kwa meno yao.

Namna ya kuzuia hali hii ni kuepuka kutumia maji na vitu vingine vinavyoingiza mwilini ambavyo vina kiwango kikubwa cha madini ya floridi hasa kipindi cha utotoni ambapo meno huwa yanaota.

Ikumbukwe kwamba katika umri wa miezi 20 mpaka miezi 30 tangu mtoto kuzaliwa ndicho kipindi hatari zaidi kinachosababisha hali hii kama mtoto atalishwa vitu vyenye madini mengi ya floridi.

Friday, January 5, 2018

Usafi hupunguza fangasi kusambaa sikioni, kupunguza madhara mwilini

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi makala@mwananchi.com

Licha ya umuhimu wake, yasipotunzwa vizuri, masikio huweza kupata maambukizi ya yatokanayo na fangasi au bakteria. Mara nyingi maambukizi ya fangasi hufananishwa na yanayosababishwa na bakteria.

Leo tunaangalia maambukizi ya fangasi sikioni ambayo mara nyingi hutokea nje ya sikio. Hutokana na maambukizi ya fangasi. Vimelea vya fangasi vinavyosababisha maradhi haya kwa watu wengi huwa vinatoka kwenye jamii mbili ambazo ni aspergillus na candida.

Huweza pia kutoka kwenye jamii nyingine za fangasi kama vile actinomyces, phycomycetes na rhizopus. Jamii zote hizi hupatikana kwenye mazingira yaliyotuzunguka lakini kwa wengi huwa hawana madhara kwa sababu kinga ya kawaida ya mwili huwa na uwezo wa kukabiliana nao na kuwazuia wasilete tatizo lolote.

Fangasi hawa huweza kuleta madhara kwenye masikio pale inapotokea kinga ya mwili imeshindwa kuwazuia wasifanye hivyo. Mara nyingi maradhi haya hutibiwa kama yamesababishwa na vimelea aina ya bakteria kwa mgonjwa kupewa dawa aina ya antibiotiki ambazo hazina uwezo wa kukabiliana na vimelea aina ya fangasi. Matibabu sahihi hutolewa baada ya dawa za antibaiotiki kushindwa kutibu tatizo.

Walio hatarini

Ingaw akila mmoja anaweza kuugua mafangasi wa sikio, kuna walio kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya. Wanaooga au kuogelea kwenye maji yasiyo safi yaani maji machafu wanajiweka kwenye kundi hili. Yanaweza kuwa maji ya bwawa la kuogelea ambayo hayatibiwa au kubadilishwa siku nyingi au yaliyotuhama. Ikiwezekana, inashauriwa kuyaepuka.

Wengine ni wanaotumia dawa za kutibu maradhi mbalimbali kwa muda mrefu. Hii ni kwa sababu matumizi ya dawa kwa muda mrefu hushusha kinga za mwili hivyo kuufanya mwili usiweze kukabiliana na maradhi yatakayojitokeza.

Watoto wadogo wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maradhi haya kutokana na kutokua na kinga imara pamoja na kujihusisha kwao na michezo ambayo inawaweka kwenye mazingira yenye vimelea vingi vya maradhi haya.

Watu wenye umri mkubwa au wenye maradhi ya muda mrefu kama vile kisukari ambayo hushusha kinga ya mwili nao wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya fangasi wa sikio.

Dalili

Maumivu ya sikio hasa linapoguswa, muwasho na kuvimba ni miongoni mwa dalili za fangasi hawa. Baadhi ya wagonjwa hutoa usaha mweupe, mweusi au wenye rangi ya manjano sikioni.

Baadhi ya waathirika hushindwa kusikia vizuri kwenye sikio lenye tatizo, kama lililopata maambukizi ni moja, wengine hupata hisia kama kuna kitu kimekaa sikioni na wapo ambao sikio au masikio huziba.

Endapo mgonjwa atahisi moja ya dalili hizi inashauriwa aende hopitali kuonana na daktari ambaye atamfanyia vipimo maalum vya maabara.

Baada ya kujiridhisha kuwa ugonjwa unatokana na maambukizi ya fangasi daktari atatoa matibabu yanayostahili.

Matibabu

Kwanza kabisa ni vyema kusafisha sikio na kuondoa usaha au chochote kilichoko kwenye sikio. Hii husaidia kuondoa baadhi ya fangasi waliosababisha tatizo.

Utaratibu wa kusafisha sikio lililoathirika unatakiwa urudiwe mpaka pale atapopona. Usafishaji huu hufanywa kwa kutumia dawa ya hydrogen peroxide ambayo huondoa uchafu uliojishikiza kwenye kuta za mfereji wa sikio.

Kama maradhi yamesababisha ngoma ya sikio kuchanika basi ni vyema usafishaji huu ukafanywa na daktari bingwa wa masikio, koo na pua.

Zaidi ya kusafisha masikio yaliyoathirika, daktari atatoa dawa aina ya fangasi (antifungal agents) ambazo zina uwezo wa kukabiliana na fangasi. Kumbuka dawa za antibaiotiki (antibiotics) hazina uwezo wa kukabiliana na vimelea vya fangasi.

Dawa zinazotolewa huwa ni za matone ambayo mgonjwa ataweka kwenye masikio yake kwa kufuata maelekezo ya daktari. Haishauriwi kutoa dawa za kunywa kwa lengo la kutibu maradhi haya. Kama mgonjwa ni mtu mzima na kuna hatari ya maradhi kusambaa huwa inashauriwa kutibiwa kwa dawa za kunywa au zile zinazowekwa kwenye mishipa.

Hii ina lengo la kuzuia uwezekano wa vimelea vya fangasi kusambaa mpaka ndani ya sikio na mfupa wa fuvu na kusababisha madhara makubwazaidi.

Kwa walio mbali na hospitali na ambao wanashindwa kwenda hospitali kuna namna nyingine za kutibu maradhi haya. Wanaweza kuhakikisha wanakausha sikio muda wote ili kuwanyima fangasi nafasi ya kushamiri kwani hufanya hivyo maeneo yenye joto na majimaji.

Kama utaweza kuhakikisha sikio ni kavu muda wote utasaidia kuzuia fangasi wasiongezeke. Jambo la tahadhari ni kutoingiza chochote sikioni kwani unaweza kukausha eneo la nje tu la sikio.

Ukiingiza kijiti cha kuondolea nta ya sikio utasaidia kuvisukumia ndani zaidi vimelea vya maradhi na kuhatarisha afya ya ngoma ya sikio.

Unaweza kuweka siki vilevile. Vimelea vya fangasi hushindwa kushamiri na kuongezeka kwenye mazingira yenye tindikali. Siki (vinegar) ina tindikali hivyo ukiiweka kwenye sikio basi huondoa mazingira rafiki kwao.

Madhara

Matumizi ya dawa sahihi dhidi ya vimelea vya fangasi huwa yana matokeo chanya. Hii ina maana kuwa dawa za kukabiliana na vimelea vya fangasi huwa zinafanya kazi.

Sababu ya maradhi ya fangasi kusumbua kwa muda mrefu huwa ni kutokana na uwepo wa vimelea hivi kwenye mazingira yanayotuzunguka hivyo mara tu baada ya kumaliza dozi ya dawa, vimelea hivyo hupata upenyo wa kurudi kwenye eneo vilipoleta madhara na kuendelea kuleta madhara.

Ili kuepuka kurejea tena kwa maradhi ni lazima kwa mgonjwa kuhakikisha anahakikisha masikio hayawi na majimaji na kuyaweka kwenye hali ya usafi muda wote.

Endapo mgonjwa hatopata dawa sahihi kwa wakati vimelea vya fangasi vinaweza kusambaa na kuingia ndani ya sikio na kwenye mfupa wa fuvu na kuleta madhara makubwa.

Ni vyema kwa mgonjwa kwenda hospitali mara tu anapohisi dalili za maradhi ya sikio. Hatua hii itawezesha matibabu kutolewa kwa wakati na kuzuia uwezekano wa maradhi kusambaa na kuleta madhara makubwa zaidi.

Friday, January 5, 2018

Upo uwezekano wa kupona kisukari ukibadili mfumo wa maisha

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Takwimu za Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF) zinaonyesha mtu mmoja kati ya kila 11, ana kisukari. Kuna zaidi ya watu wazima milioni 425 duniani kote wenye maradhi haya yasiyoambukiza.

Takwimu hizo pia, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana, zinabainisha kwamba mmoja kati ya wagonjwa wawili wa kisukari hafahamu kama anaugua maradhi hayo. hii ni sawa na nusu ya wagonjwa wote milioni 425 ambao ni takriban milioni 212.

Hata wajawazito nao hawako salama. Ripoti hiyo inaeleza, ugonjwa huo huathiri mjamzito mmoja kati ya sita duniani kote ambako kuna zaidi ya watoto milioni moja wenye kisukari aina ya kwanza.

Miongoni mwa watu wote wenye kisukari, ripoti inaonyesha theluthi mbili ya wagonjwa hao, sawa na milioni 279 wanaishi mjini ambako vyakula vya asili ama ni adimu au ghali zaidi hivyo kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi hayo.

Pamoja na ukweli huo, takwimu hizo zinaonyesha wagonjwa watatu katika kila wanne wanaishi kwenye nchi masikini au zenye kipato cha kati. Wawili kati ya watatu au theluthimbili ya wagonjwa hao ambao ni sawa na milioni 327 wana umri wa kufanyakazi wakiwa na umri kati ya miaka 20 mpaka 64.

Kutokana na ukweli huo, Serikali zinatumia gharam akubw akukabiliana na maradhi hayo. inaelezwa, asilimia 12 ya bajeti yote ya afya huelekezwa kukabiliana na kisukari. Mkuu wa Kitengo cha Kliniki ya Kisukari katika Hospitali ya M.P Shah ya jijini Nairobi, Dk Sairabanu Sokwalla anasema wagonjwa wengi bado hawajajigundua kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao.

“Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea. Takwimu zinaonyesha hali ilivyo huko Asia, Amerika na Ulaya kutokana na wananchi wake kuwa na utaratibu wa kupima. Barani Afrika, wengi hawajui kuhusu afya zao,” anasema.

Ukweli kuhusu hilo, unathibitishwa na Winnie Nginyo, mwanamke wa miaka 32 anayekiri: “Niliharibikiwa ujauzito wangu wa pili. Hapo ndipo nilihitaji uchunguzi ili kujua sababu, majibu yalibainisha kiwango kikubwa cha sukari mwilini mwangu.”

Mkenya huto anayeishi Mtaa wa Westlands, jijini Nairobi amefunguka na kuweka wazi kisa hicho na namna alivyoweza kupambana na kisukari mwilini mwake, kutoka 23mmol/1 mpaka kiwango cha kawaida, 6.2mmol/1.

Apona kisukari

Baada ya kugundulika miezi 18 iliyopita, jukumu kubwa kwake wakati huo lilikuwa ni namna ya kuepukana na kisukari kwa kuwa ipo historia katika familia yake, alijua ni ugonjwa wa kurithi.

Uzito wake kwa wakati huo ilikuwa kilogram 110: “Nimepunguza kilogram 21, haikuwa rahisi nilianza kunywa maji mengi, kula vyakula kwa kufuata mpangilio wa lishe hata kwa mume na mtoto wangu wa kiume mwenye miaka 10 pamoja na kufanya zaidi mazoezi.”

Hata hivyo Winnie anasema ni rahisi kuishi na kisukari ikiwa utazingatia matibabu na kuacha matumizi ya vyakula visivyofaa kwa mfano unywaji pombe uliokithiri na kutofanya mazoezi.

Yeye anafanya mazoezi mara tatu kwa wiki akitumia saa moja kuushughulisha mwili wake ili kupunguza mafuta. Kwa kuwa anaamini ulaji wa baadhi ya vyakula ikiwemo pipi, keki au chipsi kwa wingi huongeza tatizo, huviepuka.

“Inapaswa kuzingatia ulaji unaofaa, katika kila mlo nazingatia robo tangu kunakuwa na mbogamboga, matunda na wanga kwa kiasi kidogo sana, zaidi naepuka vyakula vyenye mafuta,” anasema.

Kupunguza madhara yamaradhi hayo, anashauri watu wawe na tabia ya kupima mara afya mara kwa mara kujua kama wana kisukari au la pamoja na kufuatilia matibabu kwa wenye maradhi hayo ili kuchukua hatua za kuudhibiti mapema. “Tabibu wangu aliniweka wazi kwamba nifuatilie matibabu inavyopaswa nitapona. Hivi sasa sukari yangu imeshuka na ni ya kawaida. Sasa nimeacha kutumia dawa nimepona,” anasema.

Winne mwenye mtoto mmoja, ana kiu ya kuwa na watoto watano hata hivyo anasema hajakata tamaa kwani madaktari wamemruhusu kuendelea kuzaa hivyo kuwa na uhakika wa kuongeza waliobaki.

Baada ya kugundulika kuwa na maradhi hayo, familia yake ilimuunga mkono kupambana na maradhi hayo. Anasema mumewe alihakikisha anakula vizuri na kufanya vitu vyote vinavyotakiwa.

“Tulipopoteza mtoto ilituuma sote hivyo tuliamua kubadili mtindo wa maisha. Tunaishi maisha mapya, nilikuwa na safari ndefu kupata mafanikio haya,” anasema Winnie. Ili kuhamasisha matibabu ya sukari, Winnie ameunda kundi la mtandao wa wa WhatsApp analolitumia kutoa elimu kwa wagonjwawalio katika matibabu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Dk Sokwalla anasema ugonjwa wa kisukari husababishwa na mtindo wa maisha na mara nyingi waathirika wakubwa ni wanawake. Anazitaja sababu kuu za kisukari kuwa ni uzito kupita kiasi na kutozingatia lishe na ulaji unaofaa huku akitahadharisha kukua kwa maradhi hayo kitakwimu.

Tanzania

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kwa bahati mbaya, watu wengi hawajitambui kuwa na ugonjwa huu na wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema.

Alisema katika nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika, Tanzania inashika nafasi ya nane na hadi mwanzoni mwa mwaka jana, zaidi ya watoto 2,000 wameingizwa kwenye rejista za watoto kwenye kliniki.

“Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari wapo kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Utafiti wa mwaka 2012 uliohusisha wilaya 50 nchini ulionyesha asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari,” alisema Ummy.

Friday, January 5, 2018

Tukisherehekea mwaka mpya tuielewe saratani ya shingo ya uzaziDk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Januari ya kila mwaka ni mwezi wa kuinua uelewa kuhusu saratani ya kizazi maarufu kama saratani ya shingo ya uzazi kutokana na kalenda ya magonjwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wadau na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala afya kote duniani huutumia mwezi huu kutathimini jitihada za kupambana na saratani ya shingo ya uzazi, ugonjwa unaoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine yeyote ya saratani.

Hapo awali, wanawake walikua wanapoteza maisha baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu tofauti na hali ilivyo sasa kwani idadi ya wanawake wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo imepungua kutokana na kampeni zilizofanyika kuongeza uelewa.

Wanawake hivi sasa hawana sababu ya kuendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huu ingawa bado wanaendelea kufa. Saratani ya shingo ya kizazi bado inaendelea kutishia maisha ya wanawake nchini. Ripoti za karibuni zilizotolewa na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani(CDC) zinaarifu kuwapo kwa maelfu ya wanawake walio hatarini kupatikana na saratani ya kizazi katika miaka michache ijayo huku sababu kubwa ikiwa ni kukosa taarifa na uelewa wa kutosha.

Saratani ya shingo ya kizazi ni ugonjwa ambayo huanzia na kukua kwenye mlango wa uzazi maarufu kama cervix ambayo ni sehemu nyembammba yenye uwazi inayoanzia ukeni hadi kwenye mfuko wa uzazi.

Saratani ya mfuko wa kizazi ndiyo inayoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine ya saratani ingawa ikigundulika mapema kuna kuwa na uwezekano mukubwa wa mgonjwa kupona.

Aidha, saratani ya shingo ya kizazi imethibitika kuwa ni saratani inayozuilika kirahisi kuliko nyingine zote. Njia pekee ya kuzuia na kujikinga na saratani hii ni kupata chanjo ya HPV; Human Pappiloma Viruses ambayo ni aina ya virusi vinavyosababisha saratani hii.

Saratani hii huwashambulia wanawake pekee hivyo kumaanisha hatari ya kwanza ni mwanamke mwenyewe. Mara nyingi hutokea katika umri wa kati. Zaidi ya nusu ya wanawake wanaopimwa na kukutwa na saratani hii huwa na umri kuanzia miaka 30 hadi 60 ingaw ahuwapata pia wenye wastani wa miaka 20, mara chache.

Inakadiriwa, asilimia 20 ya wanaopatikana ni wanawake kuanzia miaka 60 na kuendelea.

Sababu nyingine zinazomuweka mwanamke hatarini kupata ugonjwa huu ni uvutaji wa sigara na aina yeyote ya tumbaku, maambukizi ya Ukimwi au magonjwa mengine ya ngono na hasa yanayojirudia, uzito uliopitiliza, umasikini na sababu za kurithi zinazotokana na historia ya ugonjwa kwenye familia.

Mwanamke wakati wote anashauriwa kuwa makini na dalili kuu za ugonjwa huu kwani kupitia hizo zitampa msukumo wa kuwahi hospitali kuwaona wahudumu wa afya na kupata vipimo ili kuiwahi saratani hii ikiwa kwenye hatua za awali.

Dalili kuu za saratani ya shingo ya kizazi ambazo mwanamke hapaswi kuzifumbia macho ni pamoja na kutokwa na damu kusikoendana na ratiba ya mzunguko wake wa hedhi, kutokwa na damu wakati au baada ya tendo la ndoa au wakati wa kujisafisha na hedhi isiyokoma kwa mwanamke ambaye hawezi kushika mimba kutokana na umri.

Dalili nyingine ni ya mara kwa mara maumivu chini ya kitovu, kutokwa na uchafu wenye rangi ya maziwa au njano unaoambatana na harufu mbaya na maumivu wakati wa haja ndogo.

Friday, December 15, 2017

Watanzania asilimia 6.5 hawana vyoo kabisa

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Watanzania wengi hutumia vyoo visivyokuwa bora na hawaoshi mikono kwa maji safi na sabuni.Inaelezwa zaidi ya nusu yao hutumia vyoo vilivyo chini ya kiwango na moja ya kumi sawa na asilimia 6.5 hawatumii vyoo kabisa.

Matokeo ya haya yote, ni maradhi kwa maelfu ya watoto ambao hupoteza mai-sha kila mwaka kwa sababu ya maradhi yanayoweza kuzuilika ikiwamo kuhara na kipindupindu.Vyoo bora pamoja na kusafisha mikono ingeokoa nusu ya vifo hivi. Kwani hata wale waliona vyoo, suala la kunawa mikono kwa sabuni halizingatiwi kabisa wakati wa kutoka chooni na kabla ya kuanza kula chakula.Utafiti unaonyesha kutokutumia vyoo na kunasababisha uwapo wa nusu ya watoto waliodumaa kwenye jamii.

Tanzania inaelezewa kuwa na kiwango cha juu cha watoto wenye udumavu dun-iani, imeelezwa watoto milioni 2.7 wame-dumaa. Hawa ni watoto ambao wapo kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi na watakuwa na uwezo mdogo kiakili na matokeo mabaya ya kielimu, kadiri wana-vyokuwa. Wanapokuwa watu wazima, wanakuwa na uwezo mdogo kwa asilimia 20 chini ya wale ambao hawakudumaa.“Maendeleo yetu ya kiuchumi yanarudi nyuma.

Kutokuthamini usafi wa mazin-gira kunatugharimu zaidi ya Sh340 bilioni ikiwa ni katika muda uliopotea, afya isiy-okuwa bora na maendeleo duni,” anasema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jin-sia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.Anasema hiyo ni sawa na asilimia moja ya pato la taifa ambayo thamani yake inal-ingana na thamani ya umeme unaotumika nchini kote. Ummy anasema nchi kwa sasa inajikita katika kurekebisha hali hiyo mwaka hadi mwaka na ifikapo 2025, inakusudia kufikia uchumi wa kati au zaidi.“Wito wangu kwa wadau wa maendeleo, tunataka tuwe na kampeni moja nchini badala ya kuweka rasilimali fedha zetu sehemu mbalimbali, badala yake tuun-ganishe nguvu, tufanye kampeni moja ya usafi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchini,” anasema.Anatoa maagizo kwa maofisa afya kuz-ingatia hali za usafi wa mazingira kwani Tanzania haiwezi kuwa nchi yenye uchumi wa kati ikiwa usafi hautazingatiwa.“Awamu ya tano tunazungumzia kuokoa fedha za Serikali na kuzielekeza kwa jamii kwenye mambo yanayogusa wananchi moja kwa moja. “Huu ni uchambuzi wa Benki ya Dunia, tunapoteza Sh340 bilioni kila mwaka kuto-kana na kukosekana kwa hali ya usafi,” anasema Ummy.Hata hivyo, anasema mkakati mkubwa uliopo sasa ni kubadilisha mwamko na mtazamo wa wananchi kwanza, lakini pia kuweka sheria kali ili watu waone umuhimu wa kuwekeza katika usafi.Waziri huyo anasema imefika wakati sasa tathmini ifanyike kwa kila kijiji kuona matokeo ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012, ni wagonjwa wangapi wa matumbo na maradhi yatokanayo na ucha-fu wamepungua kiidadi.“Hatuwezi kuwa nchi yenye uchumi wa kati kama asilimia 40 tu ya kaya ndizo zenye vyoo bora huku kati ya shule 100 Tanzania, 28 pekee ndizo zenye vyoo bora,” anasema Ummy.

Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo anasema ofisi yake ipo tayari kuchukua kampeni hii ya usafi wa mazingira, kwa kuwa kila mkoa, wilaya, tarafa na kijiji ipo chini yake.

“Tutahakikisha kampeni hii inafanikiwa na watu wanabadili tabia zao, tuache kufanya kwa mazoea tungependa ujenzi wa vyoo bora uwe ni sehemu ya kipimo cha utendaji katika wilaya,” anasema.

Jafo anawaagiza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo awamu ya pili ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira.

Anasema wakurugenzi kutenga ikama za afya zina lengo la kupata watumishi wenye kada za afya kusimamia maeneo hayo muhimu katika kutekeleza kampeni hiyo kwa asilimia 100 ifikapo 2021.

Mratibu wa huduma za maji, afya na mazingira shuleni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teklnolojia, Teresia Kuiwite anasema wizara yake kwa kushirikiana na Tamisemi wameanzisha vilabu vya mazingira katika kila shule.

“Hilo linawafanya wanafunzi watakapokuwa, waelewe nini maana ya vyoo bora.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba anasema kampeni hiyo ni muhimu na iwapo Taifa likiamua kupima utendaji wa wakuu wa mikoa na wilaya katika ujenzi wa vyoo, watafanikiwa.

“Kama hawatafikia malengo basi wataondolewa kwenye nafasi zao. Hili ndilo azimio. Kama Njombe wameweza, hakuna sababu kwanini wengine washindwe.”

Awamu ya pili ya kampeni 2017/2021

Awamu ya pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira ilizinduliwa mjini Dodoma Desemba 7 na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan iliyowakutanisha mawaziri mbalimbali, wakurugenzi na makatibu.

“Hapa nchini asilimia 40.5 pekee ya kaya ndizo zenye vyoo bora wakati huo takwimu zinatuambia kaya laki sita hazina vyoo kabisa,” anasema hali hiyo inabainisha kiini cha kuendelea kushamiri kwa maradhi ya kuambukiza hususani kuhara na kipindupindu ambacho hadi sasa kinajitokeza katika baadhi ya mikoa na Halmashauri.

Samia Suluhu anasema madhara ya ukosefu wa miundombinu bora ya Usafi wa Mazingira hayaishii kusababisha maradhi na vifo, bali yanagusa sekta nyingine.

“Tanzania tunapoteza fedha nyingi kutokana na hali duni ya usafi hasa ukosefu wa huduma ya vyoo bora. Nchi yetu inaendelea kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambao hadi Novemba 12, 2017, watu 27,554 wameripotiwa kuugua na 432 walifariki dunia,” anasema.

Waziri wa Afya, Ummy anasema awamu ya kwanza ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira ilianza mwaka 2012/2016 ambayo ililenga ujenzi na matumizi bora ya vyoo, ikishirikisha halmashauri 163 tu.

“Kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza, jumla ya kaya 519,000 zilijenga vyoo bora na tulilenga kaya 600,000, vituo vya afya 441 vimejengewa vyoo bora kutoka malengo ya vituo 250, hivyo tumefanikiwa upande huo kwa asilimia 146,” anasema Ummy.

Anasema lengo la wizara ilikuwa ni kuzifikia kaya Milioni moja kutibu maji kwa kuweka dawa au kuyachemsha, lakini zilizofikiwa ni kaya 934,437 ambazo sasa zimeanza kutibu maji sawa na asilimia 93.

Mwongozo wa huduma za maji, vituo vya tiba

Wakati wa kuelekea utekelezaji wa awamu ya pili ya kampeni hiyo, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na vyoo katika vituo vya kutolea huduma za afya hasa maeneo ya vijijini bado ni changamoto.

Imeelezwa ni asilimia 44 pekee ya vituo vya afya vyenye huduma hizo. Kati ya hizo, asilimia 34 ya vituo hivyo vimebainika bado vinatumia maji kutoka vyanzo visivyosalama huku asilimia 56 zikikosa kabisa uwapo wa huduma hizo muhimu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa tathmini ya upatikanaji wa huduma muhimu katika vituo vya afya kwa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imezindua Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya.

Akizungumzia kuhusu mwongozo huo, Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima anasema umeandaliwa kwa makusudi ya kuboresha utoaji huduma katika vituo vyote vya afya nchini.

Anasema kupitia mwongozo huo wameelekeza jinsi ya kufanya ili kuweza kufikia lengo la kuwa na vyoo bora na huduma.

Mkurugenzi wa Uratibu wa Kisekta wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Andrew Komba anasema mwongozo huo utaisaidia Serikali na wadau wa maendeleo kusimamia na kutekeleza masuala ya usafi wa mazingira katika maeneo hayo.

“Mwongozo unatoa maelekezo stahiki wa namna vituo vya afya katika ngazi zote vinavyopaswa kufanya kwenye upangaji mipango na uandaaji wa bajeti zitakazotumika kusimamia usafi wa mazingira,” anasema.

Naye Mkurugenzi wa Mipango wa Shirika la WaterAid, Abel Deganga anasema kutokana na kukosekana kwa mwongozo kwa muda mrefu unaopima hali ya upatikanaji wa maji kwenye vituo vya afya nchini, utendaji kazi wa Serikali na wadau ambao ulikuwa unasuasua.

Friday, December 15, 2017

Nimonia ugonjwa unaokatisha maisha ya watoto wachanga

 

By Dk Kammu Keneth, Mwananchi

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti wake ilioufanya hivi karibuni, limebaini asilimia 16 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinasababishwa na nimonia.

Linasema takribani vifo 920,136 vilivyotokea mwaka 2015 kwa watoto, vinamechangiwa na nimonia.

Uchunguzi umeendelea kubaini kwamba moja kati ya vifo vitatu kwa watoto wachanga husababishwa na nimonia.

Mbali na hayo, nimonia ni moja ya maradhi 10 ya kwanza katika hospitali takribani zote nchini yanayowakumba watoto.

Chanzo cha maradhi hayo

Ugonjwa huu kwa asilimia kubwa husabishwa na bakteria, virusi pamoja na fangasi.

Bakteria aina ya Streptococcus pneumonia ameonekana kushika nafasi ya kwanza kwa kusabisha nimonia kwa watoto, akifuatiwa na Haemophilus influenzae type b (Hib).

Kwa upande wa virusi, kipo kinachojulikana kitaalamu kwa jina la respiratory syncytial virus.

Pia kuna fangasi aina ya Pneumocystis jiroveci wameonekana pia kuchangia robo ya vifo vya watoto wenye nimonia hasa wanaozaliwa wakiwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Pathofisiolojia Bakteria huweza kuingia kwenye mapafu kwa njia ya aspiresheni wanapofika kwenye mapafu.

Huko huvamia nafasi zilizo kati ya seli na kati ya alveoli, ambako makrofeji na nutrofili (seli nyeupe za damu zinazolinda) hujaribu kuwamaliza.

Nutrofili pia hutoa sitokini na kusababisha uamsho wa kijumla wa mfumo wa kingamwili.

Hii ndiyo inayosababisha mtoto kupata joto kali mwilini, kutetemeka na uchovu unaoshuhudiwa katika nimonia ya bakteria.

Nutrofili bakteria, na viowevu kutoka kwa mishipa ya damu iliyo karibu, hujaa katika alveoli na kusababisha konsolidesheni ionekanayo kwa eksirei ya kifua

Virusi vinafikaje kwenye mapafu

Virusi vinaweza kufika katika mapafu kwa njia mbali mbali ikiwamo ya kugusa kitu chenye virusi na kisha kushika pua. Maambukizi mengine ya virusi hutokana na matone kwenye hewa yaliyoambukizwa yakivutwa ndani hadi kwenye mapafu kupitia kinywani au puani.

Virusi vinapofika kwenye sehemu ya juu ya njia ya hewa, vinaweza kwenda hadi kwenye mapafu, huko huvamia seli zilizoko kwenye kuta za njia za hewa, alveoli au parenkaima za mapafu.

Virusi vingine kama vya ukambi na hepesi simpleksi, vinaweza kufika kwenye mapafu kupitia kwenye damu. Uvamizi wa virusi hivi kwenye mapafu unaweza kusababisha viwango tofauti vya vifo vya seli.

Kwani mfumo wa kingamwili ukijaribu kuitika kwa maambukizi haya, uharibifu zaidi wa mapafu unaweza kutokea.

Seli nyeupe za damu, hasa za mononuklea, kwa kawaida husababisha athari hiyo. Pamoja na kuharibu mapafu, virusi vingi huathiri ogani zingine wakati huohuo na kukatiza shughuli zingine za mwili. Virusi pia huufanya mwili kuwa mwepesi wa kuathiriwa na maambukizi ya bakteria; kwa njia hii, nimonia ya bakteria inaweza kutokea kama ugonjwa ambatani.

Namna ya kuitambua nimonia.

Shirika La Afya Duniani WHO limefafanua kiafya kuhusu nimonia ya watoto kwa msingi wa kikohozi au upumuaji mgumu na kiwango cha haraka cha kupumua, kujivuta ndani kwa kifua, au kiwango kilichopungua cha fahamu.

Kiwango cha haraka cha kupumua hufafanuliwa kama zaidi ya pumzi 60 kwa kila dakika kwa watoto chini ya umri wa miezi 2, pumzi 50 kwa dakika kwa watoto wa umri wa miezi 2 hadi mwaka 1, au zaidi ya pumzi 40 kwa dakika kwa watoto wa umri wa mwaka 1 hadi miaka 5. Kwa watoto, kiwango kilichoongezeka cha kupumua na kujivuta ndani kwa sehemu ya chini ya kifua ni vyepesi kuhisi kuliko kusikiliza milio ya kifua kwa stethoskopu.

Namna ya kuzuia nimonia

Uchanjaji huzuia nimonia za baadhi ya bakteria na za virusi kwa watoto na hata watu wazima.

Chanjo ya influenza ni bora dhidi ya influenza A na B.

Juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Udhibiti na Uzuiaji wa Maradhi, imependekeza uchanjaji wa kila mwaka kwa kila mtu aliye na umri wa miezi sita na zaidi.

Kuwapatia wahudumu wa afya kingamaradhi, hupunguza hatari ya nimonia ya virusi miongoni mwa wagonjwa wao. Chanjo dhidi ya streptokokasi nimonia na haemofilasi influenza, nazo zinaendelea kutolewa.

Kuwapatia watoto chanjo dhidi ya streptokokasi numoniae kumepelekea kupungua kwa visa vya maambukizi haya kwa watu wazima kwa sababu wengi wao hupata maambukizi kutoka kwa watoto. Chanjo zingine zinazokinga nimonia ni kifaduro, tetekuwanga na ukambi.

Mambo mengine ya kuzingatia ni kama vile kutibu maradhi fiche (yakiwamo ya VVU/Ukimwi na utapiamlo) ipasavyo, kunaweza kupunguza hatari ya nimonia.

Namna ya kuwakinga watoto wachanga

Kwa watoto wa chini ya miezi sita, inashauliwa kuwanyonyesha bila kuwapa chakula kingine ili kupunguza hatari na ukali wa ugonjwa.

Wajawazito inapendekezwa wachunguzwe Streptokokasi ya kundi B na Klamidia trakomatisi na kutoa matibabu kwa antibiotiki ikihitajika.

Hii husaidia kupunguza viwango vya nimonia kwa watoto wachanga.

Mbinu za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huenda ikafaa pia.

Dk Kammu keneth, 0759 775788 Katika jitihada za kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Friday, December 15, 2017

Njia rahisi ya kuboresha maisha ya mtoto mwenye maambukizi ya VVU

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Kuishi na mtoto mwenye maambukizi ya Virusi vya ukimwi ni jambo linalohitaji umakini ili kumeupusha na madhara ya maambukizi haya pamoja na maradhi nyemelezi.

Zipo njia rahisi ambazo mzazi au mlezi anapaswa kuzifuata ili kumuweza kuishi na mtoto mwenye VVU na kumsaidia kuboresha maisha yake ikiwamo kuishi maisha marefu na kufikia malengo yake.

Yafuatayo ni mambo ambayo kama yakifanyika yana tija kwa afya ya mtoto mwenye VVU, kwani humsaidia kuepukana na matatizo mbalimbali ya kiafya yatokanayo na maradhi sugu na nyemelezi.

Zingatia ushauri na matibabu

Mzazi au mlezi anapaswa kupata ushauri nasaha toka kwa wataalamu wa afya wenye mafunzo maalumu ya VVU na Ukimwi.

Hili ni jambo muhimu kwani itamfanya alifahamu tatizo na namna yakukabiliana nalo.

Mzazi au mlezi akipata elimu hiyo, ndiyo itamsaidia kuitumia kulinda afya ya mtoto mwenye maambukizi.

Kama mtoto mwenye VVU alishaanza matibabu ya dawa za kufubaza makali ya VVU na dawa za kuzuia maradhi nyemelezi, hakikisha mtoto anapata dawa bila kukosa.

Ikumbukwe, dawa hizi anapaswa kuzitumia katika maisha yake yote na ndizo zinazomwongezea muda wa kuishi na kadri anavyotumia ARV, ndivyo kinga ya mwili na afya yake huimarika.

Ushauri nasaha

Ushauri nasaha na kufahamu umuhimu wa dawa za ARV, inamsaidia mlezi au mzazi kufuatilia matibabu ya mtoto na kumjengea imani na dawa hizo tangu akiwa mtoto.

Kumjenga kitabia

Kumjenga kitabia mapema kuna faida kubwa kwani humfanya asiache kutumia dawa hata akiwa mkubwa.

Kwani akizoea kutumia dawa hizo, kutamfanya aishi maisha marefu.

Na hata inapobaini anaugua maradhi mengine, inakuwa rahisi kumuwahisha hospitali kupata huduma.

Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.

Watoto wenye VVU wapo katika hatari zaidi ya kushambuliwa na maradhi ukilinganisha na wengine.

Mlo kamili

Mlo kamili huwa na vyakula mchanganyiko yaani wanga, protini, mafuta, mboga za majani, matunda na unywaji wa maji yakutosha.

Vyakula hivi ndivyo vinavyotupa nguvu na joto pia kujenga mwili na kinga ya mwili.

Mlo kamili haimanishi ni mlo wenye gharama kubwa, jamii yetu imezungukwa na vyakula vyakiasili vinavyopatikana kirahisi. Mfano mboga za majani kama mchicha, matembele na karoti. Pia vyakula vya protini yakiwamo maharagwe ya soya, kunde, njegere na matunda ni maembe, machungwa na matikiti maji.

Matunda na mboga mboga zimesheheni virutubisho na madini mbalimbali yanayosaidia kujenga kinga ya mwili.

Hivyo ni jambo la msingi mzazi au mlezi kulima bustani za mboga na matunda na si vibaya kufuga kuku wakienyeji kwa ajili ya mayai na nyama (chanzo cha protini).

Mboga mboga, matunda, na protini ni muhimu sana katika ujenzi wa kinga ya mwili.

Ikumbukwe mtoto mwenye VVU ni rahisi kushambuliwa na maradhi kwa sababu kinga yake inakua dhaifu na bado ni mdogo.

Mtoto mwenye VVU ambaye tayari ni mkubwa, anahitaji kupata mapumziko yakutosha zaidi ya saa 8 kila siku, hii husaidia kinga ya mwili kuimarika.

Faida ya Michezo

Kwa watoto wenye umri wa miaka 2 na kuendelea, michezo ya kitoto na wenzake humfanya awe na mwili imara na mwenye furaha.

Furaha humpatia hisia chanya hivyo kumuepusha na matatizo ya kiakili.

Mpe mahitaji mbalimbali ikiwamo kumnunulia vifaa vya kuchezea kama mipira na midoli.

Kumjenga kisaikolojia

Ikianzia kwa mzazi kukubaliana na hali halisi baada ya kuelewa ushauri aliopewa ni jukumu lake kumjenga kiakili mtoto wake.

Mzazi au mlezi anapaswa kumkuza mtoto vizuri kwa kumuonyesha upendo na furaha.

Mfanye mtoto huyo asijione yuko tofauti, pale atakapofikia umri wa kuanza kutambua, ni vizuri akawa anaelimishwa mambo mbalimbali yenye tija na afya kwake.

Hapo baadaye ataweza kuelimika na kukubaliana na hali yake bila kupatwa na msongo wa mawazo au sonona.

Kwani uwapo wa mambo haya mawili huweza kumfanya asiwe na afya njema.

Haki ya kupata malezi bora

Watoto wenye VVU nao wanahitaji malezi bora kuanzia kwa wazazi au walezi mwishowe na jamii kiujumla.

Watoto hawa wanahitaji kulelewa kwa kuelekezwa na kufundishwa mambo mema.

Lengo la kufanya hayo ni kuwajenga kitabia na kupata hisia nzuri, kuzungumza nao na kuwaelekeza pasipo adhabu ni jambo la msingi.

Ni kawaida kwa watoto hawa kukasirika kirahisi na kupoteza hisia nzuri.

Ni vizuri kufahamu watoto hawa wana udhaifu mkubwa ukilinganisha na watoto wengine. Mfano ni rahisi kupata huzuni haraka, huwa na hasira na wakali.

Haki ya kupata elimu

Haki ya kupata elimu kwa watoto hawa huwa ni ya lazima kama watoto wengine, na itakapofikia muda wa kuanza shule ni vizuri nao wakapelekwa, tayari kuna sheria zinazowalinda watoto hawa kwa baadhi ya nchi.

Mtengenezee mazingira bora ya kuishi

Pale unapokuwa umemwekea mazingira bora ya ndani na nje ya nyumba, humfanya ajihisi mwenye utulivu wa kimwili na kiakili.

Weka mazingira safi ya mahali anapolala, anapotumia kwa ajili ya kupata chakula na anapocheza.

Hakikisha mtoto anakuwa msafi kimwili na nguo anazovaa. Hali hii itamfanya kuvutiwa na mazingira hayo na kuyapenda.

Uwazi wa tatizo

Ni vizuri kuweka wazi tatizo la mtoto wako kwa watu wa karibu katika hatua za awali na baadaye si vibaya kuwaeleza wanajamii muhimu kama viongozi wa mitaa na vijiji na shuleni kwa walimu wake, ingawa jambo hili huwawia vigumu.

Wengi huhisi wanaweza kutengwa na kunyanyapaliwa, lakini kutokana na elimu ya afya kuendelea kusambaa kwa kiasi fulani, jamii imeanza kuelewa na kuacha unyanyapaa na kuwatenga.

Ingawa bado inakubalika suala la kuweka wazi linabaki kuwa kwa mtoto, wazazi na walezi.

Ni muhimu kupata ushauri nasaha kuhusiana na jambo hili la kuweka wazi juu ya hali ya mtoto.

Kushirikiana na makundi muhimu

Kujenga uhusiano mwema na makundi kama ya wahudumu wa afya, kunasaidia kupata msaaada wa haraka na taarifa mpya, hivyo kujiongezea elimu ya afya ya namna ya kuishi na mtoto wako.

Kujenga urafiki mzuri na familia zingine ambazo nazo zimepata tatizo kama hilo, inasaidia kubadilishana mawazo, matumaini na faraja kwani hiyo ni moja ya nyenzo muhimu ya kupambana na unyanyapaa unaofanya na baadhi ya wanajamii wasio na uelewa na tatizo hili.

Ukaribu na watu kama walimu, maofisa ustawi wa jamii, washauri nasaa.

Hawa ni watu muhimu kwa malezi na husaidia kumjenga mtoto wako kisaikolojia.

Ikimbukwe mwalimu ndiye mlezi wake pale anapokuwa shuleni na ofisa ustawi wa jamii ni kiungo muhimu kati ya mtoto na jamii inayomzunguka.

Makundi mengine ni viongozi wa serikali za mitaani na viongozi wa dini, viongozi wa mtaa husaidia pia kuwaelewesha wanajamii tatizo mlilonalo na pia huwa na msada wa kupambana na unyanyapaa na kutengwa na jamii.

Kwakuwa jamii yetu huwa na imani zetu si vibaya kumjenga kiimani mtoto uliye naye ili aishi kwa matumaini.

Viongozi wa dini tayari wengi wana uelewa na wamepewa elimu juu ya mambo ya Ukimwi na wana msaada mkubwa katika maisha ya kila siku ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na wale wanaougua Ukimwi.

Friday, December 15, 2017

Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ina athari kisaikolojia

 

By Prosper Kaijage, Mwananchi

Kama ulifikiri kuandika au kutuma picha za kuelezea hisia zako katika mitandao ya kijamii ili upate amani ya moyo kwa kuwa umepitia magumu kwa kukerwa na watu, hiyo siyo njia sahihi wataalamu wa saikolojia wanasema.

Majibu ya uchunguzi uliofanywa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwamo ya kama Facebook, Instagram, snapchart na Whatsaap.

Imeonekana vijana na watu wengi ambao ni waumini wa mitandao hiyo huelezea mambo yao hasa zile yahusuyo faragha zao au za watu wa karibu yao.

Kwa mujibu wa mtandao wa Facebook, watu zaidi ya 1.28 bilioni wanautumia kila siku.

Hii imeelezwa baada ya ripoti iliyotolewa mapema Machi, mwaka huu.

Dunia sasa imehamia viganjani, ndiyo usemi unaotamalaki mitaani kwa sababu muda mwingi simu za watu zimekua msaada mkubwa kwa mawasiliano hasa katika ulimwengu wa mitandao ambao watu wanapata fursa za kubadilishana mawazo tofauti na awali, wengi walikuwa wakikutana kwa wauza kahawa na mafundi viatu.

Sufiani Rajabu (23), anasema amekuwa akitumia mitandao ya kijamii mara kadhaa na hasa wa facebook, kuandika na kuelezea hisia zake, akidai kuwa muda mwingi hushinda pekee yake akifanya shughuli zake.

“Kaka mimi nikiandika ndiyo naona kama napunguza jazba na pia najihisi kama nimetua mzigo wa matatizo, na maoni ninayoyapata mengine yananijenga lakini mengi ni yananiponda na kunisononesha,” anasema Rajabu.

Kijana mwingine, Mohamed Miraji anasema hafikirii kuanika mambo yake ya faragha kwenye mitandao kwani kufanya hivyo hakuwezi kumpatia mtu majibu sahihi ya kumaliza matatizo yanayomkabili.

“Kwa mfano mtu kama mwanaume , kuanika matatizo yako mitandaoni ni sawa na kujishushia heshima yake ya kiuanaume, waache,” anasema Miraji.

Joyce Michael, mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema simu zimesababisha kutokuwa karibu na watu, kitu ambacho kinasababisha wengi kuamua kutumia mitandao kusaka majibu ya matatizo yao, bila kujua kuwa wanajiathiri kisaikolojia.

Lakini dawa si hiyo, bali wengi wao ndiyo hujiongezea matatizo ya kupatwa msongo wa mawazo.

“Na hali hii tunaishuhudia zaidi kwa wale wanaojiona ni mastaa, hawa wameharibu utaratibu kwani kila wanachofanya wanaweka mitandaoni kitu ambacho vijana na watu wengi wanaiga kutoka kwao,”anasema Michael.

Mwanafunzi wa chuo cha Habari TSJ, ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema aliwahi kuandika jambo liloelezea hisia zake mtandaoni, lakini alijikuta akipoteza fursa ya ajira kwenye kampuni moja iliyokuwa ikimfuatilia kwa karibu kutaka kumuajiri.

“Sitorudia tena, sikuwa najua nini ninakifanya katika mitandao, ilikuwa mtu akinikwaza natumia mitandao kama njia ya kumjibu na kuandika chochote ninachojisikia bila kujua athari zake za baadaye,” anasema kijana huyo.

Wataalamu wa saikolojia wanasemaje kuhusiana na hatua hiyo?

Charles Nduku ni mtaalamu wa saikolojia, anasema mitandao ya kijamii inatumika kinyume na malengo yake.

Anasema badala ya watu kuitumia kwa ajili ya kupashana habari na taarifa mbalimbali za kujenga jamii, imegeuka kuwa uwanja wa matusi na mambo ya ajabu yanayofanywa na vijana wengi nchini.

Anasema mbali na kuanika mambo yake katika hadhara inayotumia mitandao hiyo yenye wafuasi wengi bado wanatamani vitu ambavyo wanavikuta suala ambalo linachangia kumomonyoka kwa maadili hasa jamii za kiafrika.

Nduku alienda mbali na kusema hata fursa za kazi na mambo mengine kwa vijana itabaki kuwa ndoto kutokana na kile ambacho mtu atakuwa amekituma au kuandika katika mitandao hiyo.

“Mtu hawezi kukupa fursa ya ajira au nafasi ya kufanya jambo lake mara atakapobaini ulichoandika katika ukurasa wa mtandao wako ni ukiukaji wa maadili.

Kwenye upande wa ajira, waajiri siku hizi huangalia tabia ya mtu pia kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii,” anasema.

Nduku anasema jamii inaweza kukupa heshima ila kupitia mambo ambayo hayastahili kuwekwa katika mitandao, inaweza kushusha heshima yako kwa sababu unatoa mwanya wa watu kukujadili kwa mema na mabaya.

Anasema matatizo ya kuelezea hisia hayawezi kutatuliwa katika mitandao, bali kwa kupitia wataalamu wa saikolojia ambao wanaweza kukupa msaada wa karibu.

Karoli Mabula, pia ni mtaalamu wa saikolojia anasema kuandika kitu ambacho kimekukwaza kwa namna yoyote ni moja ya tiba ya kutibu dukuduku ambalo linakusumbua, haijalishi ni katika mazingira gani.

Kwanini watu wanaamua kuanika siri zao kwenye mitandao?

Mabula anasema wengi wao hukosa watu waaminifu wanaoweza kuwaambia mambo yao na wakayatunza bila kuyatoa kwa mtu mwingine.

“Sasa hali hiyo inawafanya wengi waone suluhu ni kuandika kwenye kurasa zao za mitandao, jambo ambalo si ufumbuzi,” anasema.

Anasema maandiko yanayoandikwa kwenye kurasa wake na watu, mara nyingi hayamsaidii bali huchangia kumuingiza kwenye matatizo zaidi.

“Hakuna faida wala uhusiano wowote wa kuandika au kuelezea hisia zako mitandaoni na kutafuta suluhu ya tatizo hilo, na kumbuka si watu wote wanaweza kukuelewa kwa kile unachokifanya, lakini mtu akienda kwa washauri nasihi, watapata tiba ya matatizo yanayowasibu,” anasema Mabula na kuongeza: “Watu wengi wanaugua maradhi ya sonona, lakini badala ya kutafuta tiba kwa wataalamu, wanakimbilia kwenye mitandao ambako wanajikuta wakishusa thamani yao.

Tukumbuke thamani ya mtu inashuka kwa kitu kidogo sana, ndiyo maana vijana na watumiaji wa mitandao wanapaswa kuwa makini kwa wanachoandika kwani kuna wafuasi wengi ambao pia wanaweza kushusha heshima yao katika jamii.”

Lakini pia anasema si mitandao hiyo inalenga mambo hasi tu, wapo baadhi wanayoitumia kwa malengo chanya, wanafanikiwa kimaisha.

Friday, December 8, 2017

Vifo vya watoto njiti pasua kichwa Afrika Mashariki

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Wakati nchi zinazoendelea zikipambana na vifo vya wajawazito, makumi ya watoto njiti wanafariki kila siku katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo maeneo mbalimbali Tanzania, Uganda na nchini Kenya.

Ripoti iliyochapishwa 2012 na jopo la wataalamu wawakilishi wa mashirika makubwa ya kimataifa duniani, wasomi, taasisi za kitaaluma na mashirika ya Umoja wa Mataifa, makadirio yanaonyesha uzito wa tatizo la watoto njiti ni kubwa kuliko ilivyoripotiwa mwaka 2010.

Japokuwa vizazi kabla ya muda ni taswira ya tatizo la kidunia, lakini nchi zenye uchumi mdogo hasa zile za Afrika na za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinaelemewa na tatizo hilo.

Miongoni mwa nchi 11 zenye viwango vya juu vya kuzaliwa watoto njiti isipokuwa mbili tu, zipo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2010.

Tanzania

Nchini Tanzania takwimu zinaonyesha asilimia 13 ya watoto huzaliwa wakiwa na uzito pungufu ambao huchangia kwa asilimia 86 ya vifo vya wachanga.

Ripoti ihiyo inasema tatizo linalochangia kusababisha vifo vya watoto hao linalokadiriwa kufikia asilimia 27 ya vifo hivyo, ni pamoja na mtoto kuzaliwa njiti, maradhi ya vimelea vya bakteria, matatizo ya kupumua na kuvuja damu.

Kila mwaka, zaidi ya watoto 210,300 wanazaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito na kati yao, zaidi ya watoto 13,900 hufariki dunia. Kwa takwimu za mwaka 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee, inaonyesha idadi hiyo imeongezeka maradufu kutoka 30 mwaka 2012 hadi kufikia 1,500 mwaka 2016.

Mkuu wa Kitengo cha Watoto Njiti wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Edna Majaliwa anasema licha ya ukubwa wa tatizo, huduma ya Kangaroo imesaidia kwani ukaribu wa ngozi kwa ngozi baina ya mama na mtoto husaidia kupata joto asilia na lisilobadilika kirahisi.

Alisema husaidia pia kupunguza maambukizi ya maradhi kwa watoto, kuongeza hali ya kunyonyeshwa, kupunguza kupaliwa kwa maziwa kunakosababishwa na vifo vya ghafla na upatikanaji wa taarifa ya haraka pindi hali ya mtoto inapobadilika.

Hata hivyo, Dk Majaliwa anasema takwimu zinaonyesha vifo vya watoto njiti vimeendelea kupungua katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2012 hadi 2017 kwa Muhimbili.

“Hii inatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau wa afya ikiwamo kuanzishwa kwa huduma ya Kangaroo katika hospitali za mikoa na rufaa na upatikanaji wa huduma za dharura za kujifungua kwa wajawazito kwenye vituo vya afya (EmONC),” anasema.

Wanakabailiana vipi na changamoto

Hata hivyo anasema kuna changamoto kadhaa hasa ya ongezeko la watoto njiti linalosababisha kuwapo kwa ufinyu wa nafasi na huduma.

Kuhusu Incubator, Dk Majaliwa anasema Muhimbili ziko chache , lakini kutokana na uwapo wa watoto wengi wanaohitaji huduma hiyo, haziwezi kutumika, hivyo vyumba vya watoto njiti vimeongezwa joto kama la incubator ili kuweza kuwahudumia wote .

Kwa mujibu wa Msemaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Etty Kusiluka mashine za incubator hazihifadhiwi katika maghala ya bohari, bali MSD huziagiza kama kuna hospitali inazihitaji.

“Kuna baadhi ya vitu ni nadra kuvinunua hasa vifaa tiba kama incubator, hata hivyo bei yake inategemeana na mteja ambaye tunakwenda kununua kuna kampuni mbalimbali zinatengeneza, lakini katika rekodi yetu incubator ya mwisho ilinunuliwa kwa Sh3.37 milioni,” anasema Kusiluka.

Kenya

Nchini Kenya, takribani watoto njiti 26 wanazaliwa kila siku, wakati huohuo 8,303 kati yao hufariki dunia kabla ya mwezi mmoja wa maisha yao kila mwaka.

Mratibu Mwandamizi wa Afya wa Shirika la Save The Children la Jijini Nairobi, Joan Emoh aliliambia Mwananchi tatizo la watoto kuzaliwa njiti limeongezeka kwa muongo mmoja sasa.

Lakini anasema juhudi mbalimbali zinahitajika ili kutimiza malengo ya milenia ya mwaka 2030, yanayotaka kufikia watoto 12 kati ya 1,000 wanaozaliwa njiti wawe wanaishi.

Akizitaja takwimu za mwaka 2015, alisema watoto njiti 188,900 walizaliwa nchini humo, sawasawa na watoto wanane wanaozaliwa, mmoja wao ni njiti.

“Tunaposema mtoto njiti wametofautiana pia katika ukubwa wa tatizo, kitakwimu tukifuatilia, kati ya njiti 16, mmoja amezaliwa kabla ya wiki 10, wawili kabla ya wiki 6 mpaka 10 na 16 mara nyingi wanazaliwa kabla ya wiki moja mpaka sita,” anasema Joan.

Hata hivyo anasema kifo kimoja cha mtoto njiti kati ya vine, husababishwa na matatizo yatokanayo na kuzaliwa kabla ya wakati.

Joan anasema lazima ipatikane mbinu mbadala, ili kuepuka watoto wengi kutumia incubator moja, ambayo inaweza kusababisha maambukizi na vifo vingi vya watoto hao.

Kwa mujibu wa Dailymonitor la nchini Uganda, watoto njiti huchangia asilimia 25 ya watoto wote wanaofariki dunia baada ya kuzaliwa ambao ni sawa asilimia 13 ya watoto kwa kila vizazi hai 1,000.

Takwimu hizo zinaiweka nchi ya Uganda kwenye nafasi ya 28 kidunia zinazoongoza kwa vifo vya watoto njiti kwa mujibu wa ripoti ya Shirika linaloshughulikia watoto duniani (Unicef) iliyotolewa hivi karibuni. Ripoti hiyo inaeleza Uganda inapoteza watoto njiti 45,000 kila mwaka.

Teknolojia mpya

Teknolojia mpya ya kuwatunza watoto waliozaliwa kabla ya wakati kwa blanketi maalumu ‘incubator blanket’ imeelezwa itaokoa maelfu ya wanaozaliwa kabla ya wakati Afrika.

Ugunduzi huo umetambulishwa baada ya American firm Warmilu Inc iliyopo jijini Nairobi kubuni blanketi maalumu ambalo ni rahisi na rafiki kwa mama kumtunzia mtoto.

Teknolojia hiyo inayojulikana ‘IncuBlanket’, imeleta uvumbuzi katika utegemezi wa incubator za kutumia umeme na huduma ya Kangaroo ambayo hutolewa na mama (Kangaroo Mother Care). Imeelezwa huduma ya kifaa hicho itafanana na joto la mama.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Warmilu, Grace Hsia, teknolojia hiyo itaweza kuokoa maelfu ya maisha ya watoto njiti hususan maeneo ya vijijini kuliko na matatizo ya umeme na baadhi ya vituo vya afya visivyoweza kumudu gharama za incubator.

Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watoto milioni 20 wanazaliwa kila mwaka duniani, kati yao milioni 4 huzaliwa kabla ya muda wao ‘njiti’ na vifo vingi vimetajwa kutokea katika nchi zinazoendelea,c takribani milioni moja kati yao hufariki dunia kwa kukosa huduma muhimu.

Takwimu za Tanzania

Takwimu za tangu mwaka 2012 za watoto wachanga wanaolazwa Muhimbili, kati ya yao, asilimia hizo ni wale waliozaliwa kabla ya muda yaani ‘njiti’

Mwaka Takwimu

2012-2013 40.9%

2013-2014 29.4%

Friday, December 8, 2017

Zijue dalili za hatari kwa mtoto wakoDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Zipo dalili na viashiria ambavyo ni kielelezo vinavyoweza kuonyesha mtoto anaumwa sana na dalili hizi zimegawanywa katika sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni dalili za hatari na shemu ya pili ni ile ya dalili zinazohitaji kupewa kipaumbele.

Hata hivyo,baadhi ya wazazi au walezi wasio na ufahamu, wengi wao huchukulia dalili hizo ni za kawaida na huchelewa kufanya uamuzi wa kuwpeleka watoto hospitali mapema kufanyiwa uchunguzi sambamba na kupatiwa huduma za afya.

Inapotekea mtoto mwenye dalili za hatari akacheleweshwa kupatiwa huduma za afya, huweza kupoteza maisha au kupata madhara ya muda mrefu.

Hivyo, kuna umuhimu kwa wazazi na walezi kuzijua dalili hizo ili mara anapobaini kuwa zimejitokeza kwa watoto wao, wawahi kuwapeleka kwenye huduma za afya ili wahudumiwe kabla ya madhara makubwa hayajajitokeza.

Na akama itatokea mtoto akawa anashindwa kunyonya kabisa au kunywa chochote hata akilazimishwa inashindikana, hii ni moja ya kiashiria kwamba mtoto ana ugonjwa mkali.

Mtoto anapokuwa na ugonjwa wowote mkali ikiwamo wa maralia kali, nimonia kali au uti wa mgongo, mara nyingi dalili kama hizo hapo juu hujitokeza.

Kwa mfano ni kule kutapika kusiko kwa kawaida, huku akitoa kila kitu alichokula na hutumia nguvu nyingi na matapishi hutoka kwa msukumo mkubwa, hii ni moja ya dalili inayoashiria mwili kushambuliwa na ugonjwa mkali.

Unapoona ametapika kwa namna hiyo, mpeleke hospitali au kwenye vituo vya afya haraka.

Pia, kupatwa na degedege ni dalili inayoashiria uwapo wa ugonjwa mkali unaoathiri mfumo wa fahamu ikiwamo ubongo. Pale unapoona mtoto amepatwa na degedege, jua ni tatizo la kiafya na si vinginevyo.

Maradhi kama malaria, nimonia, jeraha la ubongo, uti wa mgongo, uwapo wa vimelea katika damu, upungufu wa sukari mwilini na chumvi, huwa na madhara ya kiafya yanayoweza kusababisha degedege.

Mtoto anaweza kukosa nguvu na kuwa mlegevu kupita kiasi na hufikia hatua ya kupoteza fahamu au kuweweseka.

Mambo yanayoweza kusababisha kupoteza fahamu ni pamoja na upungufu wa damu, kukosa hewa ya kutosha, sukari kushuka, upungufu wa maji na chumvi mwilini.

Matatizo hayo husababishwa na maradhi kama malaria, nimonia, uti wa mgongo na uwapo wa vimelea na taka sumu zake katika damu.

Tukiachana na dalili za hatari, dalili ambazo zinapewa kipaumbele kama viashiria vya uwapo wa tatizo la kiafya kwa watoto ambapo mzazi au mlezi atapaswa pia kuchukua hatua atakapoziona kwa watoto.

Dalili hizo ni joto la mwili kupanda, kukohoa mfululizo, kushindwa kupumua au kupumua haraka, mwili kubadilika rangi kuwa wa bluu au manjano, shingo kukakamaa, kuharisha zaidi ya mara tatu, maambukizi ya sikio, kulia mfululizo bila kunyamaza na kutokwa na vipele vingi mwilini.

Friday, December 8, 2017

UTI hatari kwa wajawazito, inaweza kuporomosha ujauzito

 

By Dk Kammu Keneth, Mwananchi

Utafiti wa kisayansi uliofanyika unadhihirisha wanawake hasa walio vunja ungo wapo katika hatari ya kupata maradhi ya UTI ukilinganisha na wanaume.

Inaelezwa mambo yanayochangia kuugua ugonjwa huo ni urethra kuwa fupi. Urethra ni mrija unaotoa mkojo kutoka kwenye kibofu kupeleka nje. Na mrija huo upo, karibu na njia ya haja kubwa, hal, ambayo hurahisisha uwezekano wa bakteria kuingia katika mfumo wa mkojo na kusababisha maradhi ya UTI.

Hatari ya UTI

UTI ni moja ya maradhi hatari hasa pale yanapowakumba wajawazito. utafiti unaonyesha takribani asilimia 40 ya wanawake wanaishi na UTI ambayo haijatibiwa na huwasababishia wapate matatizo mbalimbali yanayohatarisha maisha yao na ya mtoto wakati na hata baada ya ujauzito.

Sababu zinazomfanya mjamzito kuwa katika hatari ya kuugua UTI

Kutoweza au kupoteza uwezo wa kukamilisha haja ndogo kikamilifu, matatizo katika mirija ya mkojo yanatokana na mawe katika figo, kukunjamana kwa mirija ya urethra na ureta, mimba kugandamizwa ureta pamoja na matatizo katika mfumo wa fahamu, kushuka kwa nguvu kinga ya mwili, hali ambayo huuweka mwili katika hatari ya kushambuliwa na maradhi mbalimbali. Ugonjwa wa kisukari pamoja na vipimo vya hospitali visivyo salama anavyohudumiwa mjamzito huweza kuchangia maradhi hayo na kuvimba kwa kuta za urethra.

Mambo mengine yanayochangia ni pamoja na kushuka kwa kinga ya mwili, ujauzito kukandamiza mirija ya mkojo na kibofu. Bakteria wanaopanda kutoka kwenye mrija unaotoa mkojo nje, yaani urethra na kuingia kwenye kibofu kisha kuzaliana. Hali hii husababisha UTI kwenye kibofu.

Sababu nyingine ni pale bakteria wanapotoka kwenye mfumo damu na kuelekea kwenye figo.

Mfano wa bakteria hawa ni Escherichia coli, proteus, pseudomonas, Klebsiella na Staphylococcus hasa kwa wenye ugonjwa wa kisukari.

Sehemu za mfumo wa mkojo zinazoathiriwa na UTI.

Mrija unasafirisha mkojo kutoka kwenye kibofu kuelekea nje unapovimba, husababisha urethritis.

Kuvimba kwa kibofu husababisha cystisis. Kuvimba kwa mirija inayotoa mkojo kwenye figo kupeleka kwenye kibofu yaani ureters husababisha ureteritis na uvimba kwa figo husababisha pyelonephritis.

Namna ya kujitambua kuwa tayari una UTI.

Mtu aliye na maambukizi ya UTI mara nyingi huugua homa mara kwa mara na hupatwa na maumivu ya mgongo hasa eneo la kiuno, kujisikia kichefuchefu na kutapika hasa wakati bakteria wanapoanza kushambulia kwenye figo, kupata hamu ya kukojoa mara kwa mara, maumivu ya kichwa, uchovu wa mwili mzima, maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mkojo uliochangamana na damu na usio na harufu ya kawaida, maumivu wakati wa tendo la ndoa na maumivu sehemu za kibofu. Unapopatwa na dalili hizo, muone daktari mapema.

Matatizo yananayosababishwa na UTI wakati wa ujauzito.

Ugonjwa huo ni hatari kwa mjamzito kwani unaweza ukasababisha mimba kutoka kama hautatibiwa mapema.

Na wakati mwingine husababisha mjamzito akajifungua mtoto kabla muda na wengine hujikuta wakijifungua mtoto akiwa na uzito mdogo wa chini ya uzito wa kawaida wa kilo 2.5 yaani njiti.

Lakini wapo ambao pia huwasababishia motto akafia tumboni pamoja na kupungukiwa damu na maji.

Namna ya kujikinga na UTI.

Ili kujikinga na mhi hayo, madaktari wanashauri mtu anywe maji ya kutosha, kwa siku isiwe chini ya lita moja na nusu. Pia aepuka kula vyakula vyenye sukari nyingi ikiwamo kunywa pombe, chocolate na vyakula vyenye kahawa.

Inashauriwa kujenga tabia ya kukojoa mara ubanwapo na mkojo. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza uwnwa mkojo awahi kwenda kujisaidia badala ya kuubana ni hatari.

Inashauriwa kujenga tabia ya kuoga na kukojoa kabla na baada ya tendo la ndoa. Kufanya hivyo husaidia kuondoa bakteria walioko sehemu za siri.

“Epuka tendo la ndoa kama bado upo katika matibabu ya UTI na baada ya kukojoa usifute bali kausha sehemu zako siri ziweke safi na kavu muda wote na kama utazifuta hakikisha unafuta mbele kuelekea nyuma,” inaelekezwa.

Ni vizuri kuepuka kuvaa nguo za ndani zinazobana na hakikisha zile uzivaazo ni safi. Nguo za ndani aina ya kotoni zinapendekezwa zaidi kutumika sambamba na kula vyakula vyenye vitamini C kama matunda aina ya machungwa huwa na asidi ambayo husaidia kuondoa bakteria.

Dk kammu Keneth, anapatikana kwa namba 0759 775788.

Friday, December 8, 2017

Pera tunda lenye faida kubwa kwa wagonjwa wa kisukari

 

Pera ni miongoni mwa matunda yenye faida kubwa kwenye mwili wa binadamu kwa sababu vitamin C inayopatikana ndani ya tunda hilo, ni sawa na mara nne zaidi ya ile inayopatikana kwenye chungwa. Na kwa wagonjwa wa kisukari, wanashauriwa kulila mara kwa mara tunda hilo kwani lina kirutubisho chenye kinga dhidi ya sukari na hii ni kutokana kuwa na nyuzinyuzi (fibre).

Fibre ni muhimu katika kupunguza kiasi cha sukari kwenye damu na pia ni muhimu katika kuusafisha mfumo wa usagaji.

Pera ni zuri kwa wajawazito kwa sababu lina folic acid au vitamin B-9 ambayo husaidia kujenga mfumo wa fahamu kwa mtoto aliyopo tumboni pamoja na kuboresha uwezo wa kuona.

Pia tunda hili lina virutubisho mbalimbali ikiwemo vitamin B2, E na K pamoja na madini ya chuma, ‘copper’, ‘potassium’ na ‘manganese.’ Utafiti uliofanywa mwaka 1993 na kuchapishwa katika Jarida la Journal of Human Hypertension unaeleza kuwa pera hupunguza kiwango cha msukumo mkubwa wa damu ndani ya mwili kutokana na madini ya potassium na vitamin C ambayo husaidia kuweka sawa msukumo wa damu ndani ya mwili. Hata hivyo, madini yaitwayo Folate ambayo hupatikana katika tunda hili husaidia kurutubisha mayai ya uzazi na kuimarisha uwezo wa mtu kuona kama ilivyo kwa karoti ambayo insifika kwa kuwa na uwezo wa kuimarisha uwezo wa kuona. Vitamin B3, Vitamin B6 zilizopo ndani ya tunda la hili ni muhimu katika kuimarisha afya ya akili ya mwanadamu huku madini ya Potassium yaliyomo ndani ya mapera husaidia kurekebisha shinikizo la damu.

Mapera yana madini ya shaba ambayo ni mazuri katika kurekebisha utendaji wa kazi wa tezi ziitwazo thyroid na kwa kawaida tezi za thyroid zisipofanya kazi vizuri zinaweza kusabbisha matatizo ya afya kwa binadamu.

Wataalamu wa masuala ya lishe wanashauri kutumia kula pera baada ya kazi nzito na hiyo itasaidia katika kuufanya mwili na akili yako kupumzika.

Kwa wale wanaohitaji kuwa warembo, Pera huzuia kuzeeka kwa ngozi, kutoka na Vitamin zilizopo katika tunda hilo ambazo husaidia kuondoa sumu mwilini na kuikinga ngozi yako dhidi ya mikunjo na na kuchakaa.

(Hadija Jumanne)

Lakini majani ya mpera ni mazuri kwa kukuza nywele na kuzitibu zile zinazo katika, unachopaswa kufanya ni kuchukua majani ya mpera yanayojaa kiganja chako cha mkono kisha weka kwenye sufuria yenye lita moja ya maji, chemsha kwa muda wa dakika 15 mpaka 20.

Baada ya hapo, yaache yapoe kisha paka kwenye nywele zako kuanzia kwenye mzizi wa nywele mpaka mwisho na ukimaliza fanyia masaji nywele zako kama mtu anayepaka mafuta nywele zote, baada ya hapo unaweza kuacha kwa muda kama steaming kisha ukaosha.

Unaweza kufanya hivyo mara kwa mara, angalau mara tatu kwa wiki, kwa matokeo mazuri zaidi.

Friday, December 8, 2017

Upasuaji ubongo hospitali ya moi ulivyookoa maisha ya Lulu

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Magreth Mhagama (sio jina halisi) alikata tamaa kama kuna wakati mwanae Lulu aliyezaliwa akiwa na ubongo kwenye mfuko mkubwa nje ya kichwa kitaalamu ‘Occipital Encephacele’, atapona.

Tabasamu la mama huyo liliondoka usoni kila alipomuona mwanaye akishindwa kunyonya, kumeza, kupaliwa na kukohoa kutokana na maambukizi ya kifua ya mara kwa mara kutokana tatizo la ubongo.

Hata hivyo, saa nne za upasuaji mkubwa uliofanywa na jopo la Madaktari Bingwa wa Taasisi ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), zilirejesha upya tabasamu mama Lulu.

Uvimbe mkubwa uliohifadhi ubongo wake ulikuwa mkubwa mithili ya kichwa kingine.

“Sikuamini kama mwanangu atapona, nilikata tamaa. Nyumbani walinishauri niombe kurudi twende kwa waganga wa kienyeji wakiamini mtoto amechezewa kishirikina. Nawashukuru sana madaktari na manesi kwa kumsaidia mtoto wangu,” anasema mama huyo huku macho yake yakilenga machozi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo wa Moi, Nicephorus Rutabasibwa anasema haikuwa rahisi.

Anasema upasuaji wa ubongo unahitaji vifaa vya kisasa na umakini mkubwa kutokana na ukweli, hicho ni kiungo cha aina yake katika mwili wa binadamu.

Ubongo hutoa kila fikra, tendo, kumbukumbu, hisia na uzoefu wa kidunia.

Ubongo unapokuwa na hitilafu huathiri mfumo mzima wa fahamu wa mwanadamu.

Kwa mujibu wa jarida la New Scientist, Ubongo wa binadamu umetengenezwa na viungo laini vilivyo katika mfumo kama mafuta mazito yaliyoganda.

Dk Rutabasibwa anasema upasuaji huo wa kwanza kuwahi kufanyika nchini, uliwezekana kutokana na umakini mkubwa wa wataalamu sambamba na uwapo wa vifaa vya kisasa.

Mimba ilionekana kama mapacha walioungana

Mama wa mtoto anasema wakati wa ujauzito wake, alionekana kama ana watoto mapacha walioungana.

“Kwa hiyo nilijua ninamapacha kwa sababu, kulionekana vichwa viwili. Hivyo niliilea mimba yangu nikitegemea watoto wawili,”anasema.

Anasema alipopata uchungu, alienda kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro lakini kutokana na mkao wa mtoto tumboni alilazimika kufanyiwa upasuaji.

“Nilipojifungua nikaona mtoto anavichwa viwili, basi nilimpokea kwa sababu siwezi kumtupa wala kumnyanyapaa mwanangu. Nilianza kumlea kwa upendo tu,”anasema.

Siku nane baadae, mama huyo alipewa rufaa hadi Moi ambapo alipokelewa na madaktari bingwa.

“Nilipokelewa vizuri nikalazwa. Daktari akawa anakuja anamuangalia mtoto wanampima anaondoka. Aliniambia atapona tu lakini nilikuwa siamini,” anasema.

Mtoto afanyiwa utafiti

Wakati mama huyo amelazwa Moi, madaktari hao bingwa walikuwa wanafanya uchunguzi.

Dk Rutabasibwa anasema walitumia muda wa miezi miwili kufanya utafiti huo kuona namna ya kumfanyia upasuaji makini, utakaookoa uhai wa mtoto.

“Tathmini ya uchunguzi ilionyesha uvimbe au mfuko huo ulikuwa umefunika sehemyu kubwa ya ubongo na mishipa ya damu inayolisha ubongo, hivyo kuhatarisha maisha yake. Upasuaji ulihitaji umakini wa hali ya juu na vifaa vya kisasa,” anasema.

Mtoto hakuwa na uwezo wa kunyonya wala kumeza hali ilimfanya awe anapaliwa mara kwa mara na kupata maambukizi ya kifua (Aspiration Pneumonia).

Daktari huyo bingwa aliyeongoza jopo la madaktari wenzake anasema Lulu hakuwa na uwezo wa kulala vizuri hali ilimpa wakati mgumu mama yake.

Mama Lulu anasema hakuwa na uwezo wa kumbeba kwa sababu ya uvimbe mkubwa kuning’inia na kumfanya mtoto aonekane na vichwa viwili.

Siku ya upasuaji

Mama Lulu anasema siku moja kabla alipatiwa taarifa za mwanaye kufanyiwa upasuaji.

“Nilifurahi kwa sababu wenzangu wote watoto wao walikuwa wanafanyiwa ila mimi. Basi nilijiandaa kama nilivyoelekezwa ikiwamo, muda wa mwisho kumnyonyesha,” anasema.

Anasema siku hiyo aliamka mapema, akamuandaa mwanawe japo wakati wote hakuwa anaamini kama kweli atapona.

“Sikuwa na imani kabisa, nilimpeleka mtoto kwenye chumba cha upasuaji wakanipokea. Walinituma dawa nikaenda kununua, nikawaletea. Nikawa nakaa tu pale sielewi chochote,” anasema mama huyo.

Anasema alikaa tangu asubuhi hadi saa saba mchana bila kujua kinachoendelea japo wakati wote aliambiwa ni salama.

“Basi mara nikaambiwa niende ICU nikamuone mtoto, nikaenda nikaona ameondolewa uvimbe. Nilifurahi sana,” anasimulia.

Hali ilivyokuwa ndani ya chumba cha upasuaji

Rutabasibwa anasema changamoto kubwa waliyokumbana nayo wakati wa maandalizi ya upasuaji ilikuwa ni upatikanaji wa mishipa ya damu ya mtoto kwa kuwa ilikuwa midogo.

“Madaktari bingwa wa usingizi walipata changamoto kubwa ya kumpatia dawa ya usingizi mtoto Lulu kutokana na shingo yake kuwa fupi na maumbile ya shingo hiyo kuwa madogo,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface anasema upasuaji uliotumia saa nne ni upasuaji mkubwa.

Kama ungefanywa nje ungeweza kugharimu kati ya Sh25 hadi 30 milioni.

“upasuaji wa saa nne ni mkubwa, kama ungefanyika nje ya nchi pamoja na gharama zake zote za matibabu, ungegharimu fedha nyingi,” anasema Dk Boniface.

Anasema upasuaji huo umewezekana kutokana na umahiri wa madaktari wazalendo, chumba cha upasuaji chenye vifaa vya kisasa na huduma bora ya matibabu ikihusisha chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Anasema mkakati walionao ni kuhakikisha kesi zote kubwa zilizokuwa zinapelekwa nje, zinafanyia matibabu ndani ya nchi kwa sababu tayari wapo madaktari bingwa wanaoweza kufanya hivyo.

Hata hivyo, anasema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mwisho ya kutowasafirisha wagonjwa nje ya nchi, kutokana na kuwa na madaktari bingwa wa kutosha.

“Huu ni upasuaji mkubwa wa aina hii wa kwanza, tunao madaktari bingwa hapa kwetu na tuwahakikishie Watanzania kwamba safari za nje kwa ajili ya matibabu hazitakuwapo,”anaeleza.

Simulizi ya imani za kishirikina

Mama Lulu alipoambiwa huenda mwanawe amerogwa alianza kuamini.

Alipoambiwa aombe ruhusa kurejea kwao Morogoro, alitaka kufanya hivyo lakini alishauriwa asubiri matibabu.

“Nilipigiwa simu nikaambiwa kuna wenzangu wananizunguka, yaani wananichezea kishirikina wakasema niombe nirudi nyumbani,” anasema na kuongeza;

“Nilipomuuliza mwenzangu, aliniambia hayo ni mambo ya Mungu kwa hiyo tuvumilie matibabu. Hata hivyo, Daktari alikuwa ananipa moyo siku zote, nilidhani ananizungusha kumbe alikuwa akimchunguza mtoto,” anasema mama huyo.

Anasema kupona kwa mtoto wake ni kielelezo kwamba badala ya kutegemea waganga wa kienyeji na imani za kishirikina, huduma za afya zinatosha.

Ushauri wa Daktari

Dk Boniface anasema ni wakati wa jamii kubadili mtizamo wake kwa kuwapeleka watoto hospitali ili wahudumiwe kitaalamu.

“Waandishi wa habari iambieni jamii ni vizuri kutegemea utaalamu wa madaktari kuliko kuwapeleka watoto kwa waganga. Mtoto akiwa na tatizo, inabidi aletwe hspitali,” anasema.

Friday, December 8, 2017

Sio kila uvimbe kwenye mfuko wa uzazi ni sarataniDk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Moja ya dalili za saratani za aina nyingi huambata na uwapo wa uvimbe wa aina mbalimbali kwenye sehemu husika ya mwili kulingana na aina ya saratani.

Dhana hii imezua hofu kubwa kwa miongoni mwa wanawake wengi hasa inapotokea vipimo vikagundulika wana uvimbe ulioota kwenye mifuko yao uzazi.

Habari njema ni kwamba, uvimbe huo hautokani na ugonjwa wa saratani, bali husababishwa na sababu nyinginezo kama nitakavyoeleza, ila kwa kuwa hautokani na saratani, sio vyema kufumbia macho kwa sababu zina madhara mengine kwenye mfumo wa uzazi na afya.

Uvimbe huo huitwa uterine fibroids kwa kitaalamu,ni uvimbe usiotokana na saratani na mara zote huwa unaota na kukua kwenye ukuta au tabaka lililopo kwenye mfuko wa uzazi.

Uvimbe huu hutofautiana kwa ukubwa wa maumbile na wakati mwingine ukicheleweshwa unaweza kufikia hata ukubwa wa tikiti maji.

Pia, hutofautiana kwa idadi kati ya mwanamke mmoja na mwingine, mwanamke mmoja anaweza akaotwa na uvimbe zaidi ya mmoja kwenye mfuko wake wa uzazi, lakini mwanamke mwingine anaweza akaotwa na uvimbe mmoja tu kwenye mfuko wake na mara nyingi moja ya madhara yanayosababisha na uvumbe huo ni mkandamizo wa mfuko wa uzazi, huulazimisha kupanuka hadi kugusa kwenye viwambo vya mbavu na hapo ndipo matatizo mengine hujitokeza.

Hata hivyo, wanawake wengi hupatwa na tatizo hilo kwenye mifuko yao uzazi, lakini wengi wao hawatambui kama wanalo kwa sababu hauonyeshi dalili hadi unapokuwa mkubwa kupita kiasi na kuanza kuleta matatizo kiafya.

Nawashauri wanawake ni vyema wakajenga utamaduni wa kupata vipimo mara kwa mara ili kubaini ukiwa katika hatua za awali na kwa kufanya hivyo, watajiepusha na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na uvime huo.

Kama nilivyoeleza hapo juu, uvimbe huchukua muda hadi kuanza kuonyesha dalili zake, kama mwanamke mwenyewe hana utamaduni wa kupata vipimo mara kwa mara; au kama utakuwa umedumu kwa muda mrefu, anaweza kuziona dalili kama vile za hedhi iliyopitiliza ambayo baadaye inaweza kumsababishia kupata anemia, maumivu ya mgongo na kiuno. Pia anaweza kupata haja kubwa kwa shida, maumivu makali chini ya kitovu na hasa ikitokea uvimbe umeshakuwa mkubwa, kupata haja ndogo mara kwa mara kuliko kawaida na kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.

Ukiona dalili hizi, ni dhahiri una tatizo hilo na ni vyema kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo na mpango wa matibabu. Uvimbe unaoota kwenye mfuko wa uzazi japo hauwezi kusababisha saratani, lakini una madhara mengine makubwa kiafya ambayo ni pamoja na matatizo wakati wa kujifungua yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto hasa kama atakuwa alishika ujauzito akiwa tayari ana uvimbe. Lakini pia uvimbe huweza kusababisha mwanamke kukosa uwezo wa kushika mimba, mimba kutungwa nje ya uzazi na tatizo lingine kubwa ni mimba kuharibika mara kwa mara. Sababu kubwa zinazochangia tatizo hili ni mtatizo yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni.

Kisayansi, kwenye mwili wa mwanamke kuna homoni (vichocheo) za estrogen na progesterone, huwa zinafanya kazi ya kuchochea maendeleo ya ukuaji wa sehemu ya ndani ya mfuko wa uzazi kwenye kila mzunguko wa hedhi wa kila mwezi.

kwa ajili ya maandalizi ya urutubishwaji wa mayai na utungishwaji wa mimba, sasa wakati mwingine huwa inatokea homoni hizi hujichochea zaidi ya kiwango na hivyo kuanza kutengeneza vimbe ndogo ndogo kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi.

Lakini pia tatizo hili linahusishwa sana na sababu za kurithi. Ni vyema kwa mwanamke kuijua vizuri historia ya ukoo wake ili kutambua kama naye yupo kwenye hatari ya kurithi ugonjwa huu au la! Kwa sababu mara nyingi pia mtu anaweza kuupata ugonjwa huu kupitia vinasaba kutoka kwa watangulizi wake kwenye ukoo.

Sababu zingine zinazocchangia kwa kiasi kikubwa sana tatizo hili ni pamoja na kupata hedhi katika umri mdogo zaidi, matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, uzito wa mwili kupitiliza, ukosefu wa vitamin D, na hata ulevi pia.

Friday, November 3, 2017

Saratani inavyotafuna uhai wa wanawake nchini

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Saratani ya matiti ni ugonjwa unaowapata wanawake na husababishwa na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake, hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo.

Ikiwa katika hatua za mwanzo, kwa kawaida huwa haina maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Na kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa sababu ugonjwa unaweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema na miongoni mwa dalili za saratani ya mititi ni uvimbe kwenye matiti ama makwapa. Titi kubadilika kiumbo, kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Dalili zingine ni rangi ya ngozi ya titi kubadilika na kuonekana kama ngozi ya nje ya chungwa na ile hali yake ya kuonekana kuwa na ngozi laini hutoweka.

Kwa hapa nchini, saratani hiyo natajwa kuwa ya pili kwa kusababisha vifo kwa wanawake na hali ya kuchelewa kupata ugunduzi na tiba haraka kumeelezewa kuchangia kwa kiwango kikubwa kuleta ugumu wa matibabu.

Takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) hivi karibuni, zimeainisha wagonjwa wapya wanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kwa wastani wa wagonjwa 206 mwaka 2005 hadi kufikia wagonjwa 816 mwaka jana.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi hiyo, Crispin Kahesa anasema hizo ni zile za wagonjwa wapya wanaofika kwenye taasisi hiyo pekee na haihusishi wagonjwa wa Tanzania nzima.

“Taasisi hii kwa kipindi cha miaka 10, imepokea wagonjwa wapya 5,867, hata hivyo asilimia 80 yao wamefika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa na hivyo kufanya matibabu yao kuwa magumu,” anasema Dk Kahesa.

Mratibu wa Programu ya Via vya Uzazi kutoka Wizara ya Afya, Dk Safina Yuma anasema saratani ya matiti ni ya pili kwa kuchochea vifo vinavyohusisha saratani kwa wanawake nchini na kuchelewa kupata ugunduzi na tiba ya haraka kukitajwa kuchangia kuleta ugumu wa matibabu.

INAENDELEA UK.16

“Asilimia 80 ya watu wakiugua hupona, lakini Afrika inaonekana ni asilimia 40 pekee mtu akiugua anaweza kupona. Inabidi kuweka mkakati maalumu wa kuhamasisha watu wauelewe ugonjwa huu,” anasema Dk Yuma.

Anasema tatizo la wagonjwa wengi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma katika hatua za mbele za ugonjwa, husababisha kushindwa kuishi kwa muda mrefu, wakigundulika baada ya mwaka mmoja au miwili, hufariki dunia.

Sababu za ugonjwa wa saratani ya matiti

Dk Yuma anasema sababu ya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mama asiponyonyesha mtoto maziwa, kuna homoni fulani lazima zitoke.

“Sasa asiponyonyesha anazizuia zile homoni ambazo zinaweza kufanya mabadiliko katika chembechembe za mwili na ikatokea saratani,” anasema Dk huyo na kuongeza

“Kidunia saratani ya matiti inaongoza lakini kwetu Tanzania ni ya pili katika takwimu kutoka ORCI, inaonyesha saratani inaongoza kuua na asilimia 11 ya wagonjwa wapya ni wa saratani ya matiti na takribani asilimia 10 ya vifo vinatokana na saratani hiyo,” anasema.

Dk Yuma anasema kila mwaka idadi inaongezeka kwa kuwa jamii haina uelewa na wengi hufika hospitali dalili zikiwa zimeshaonekana hata kwa macho.

Anasema ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya matiti na kizazi, wizara ilishaanzisha programu ya kusaidia kukinga saratani hizi kwa kuangalia dalili zake mapema ili kuwanusuru kina mama wengi kwa kuwapatia matibabu mapema na kukinga dalili za awali na kuandaa mwongozo na kutoa elimu kwa jamii ili ichukue hatua mapema.

“Saratani inapoanza huwezi kuona dalili na ukiona dalili ujue imefika mbali, kwahiyo, tunahimiza wanawake wengi wahudhurie kwenye vituo vya afya ili wachunguzwe mapema kusudi kuizuia na pia kupunguza gharama kwa Serikali,” anasema.

Nani yuko katika hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti

Dk Yuma anasema mwanamke yeyote yupo katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti ikilinganishwa na wanaume, kwani asilimia 99 ya wanaopata ni wanawake na asilimia 1 ni wanaume.

“Mtu akizaa watoto akiwa na zaidi ya miaka 35, hiyo pia huchangia kuugua ugonjwa huo, kwasababu vichocheo vyake vinakaa kwa muda mrefu katika mirija ya maziwa yake, sasa visipotoka, vinaweza kusababisha saratani ya matiti,” anafafanua.

Daktari bingwa wa maradhi ya saratani kutoka ORCI, Crispin Kahesa anasema saratani ya matiti huchukua asilimia 12 ambayo hata hivyo ni ya tatu kati ya zinazosumbua kwa takwimu za kitaifa huku wagonjwa 6,300 waliripoti mwaka 2016, idadi ambayo anasema ni kubwa na imekuwa ikiongezeka, kama hatua zisipochukuliwa, itaongezeka zaidi.

“Kinachokuza saratani hii pia ni umri wetu wa kuishi umeongezeka, kinamama wengi wamepata mafunzo ya kujichunguza wenyewe, lakini haya maradhi yanakuja wakiwa kwenye utu uzima na wengi huwa na wastani wa miaka 49 na wastani wa umri wa kuishi ni miaka 59.

“Lakini pia kuboreshwa kwa mfumo wa afya utakaowezesha kugundua na kuchunguza kampeni mbalimbali za awali,” anasema Dk Kahesa.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinasema kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hugundulika huku asilimia 26 pekee ndiyo hufika hospitalini kupata matibabu.

Na takwimu za ORCI zinaonyesha idadi ya wagonjwa wapya inazidi kuongezeka kutoka 2,416 kwa 2005 hadi kufikia 6,338 mwaka 2016.

Na aina nne za saratani zikionyesha kuchukua theluthi mbili za wagonjwa wote wa maradhi hayo.

Kutoka 2005 hadi 2016, asilimia 68 ya saratani zinazosumbua Tanzania ni ya matiti, ya ngozi ‘caposis sarcoma’, shingo ya kizazi na mfumo wa njia ya chakula, kwa kila wagonjwa 10, saba wanasumbuliwa na saratani hizo.

Rekodi hiyo ni kwa wale wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo pekee, ukiachana na hospitali zingine zinazotibu saratani nchini ikiwamo ya Bugando, KCMC, Mbeya na kwingineko.

Na inaelezwa saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa asilimia 34 sawa na mgonjwa mmoja kwa kila watatu wanaoumwa ugonjwa huo, nayo inapanda kutoka wagonjwa wapya 879 mwaka 2005 hadi kufikia 2,081 mwaka jana.

Dk Kahesa anasema saratani inayofuatia ni ya ngozi ‘caposis Sarcoma’ inayochukua asilimia 13 ya saratani zote, matiti asilimia 11 na ile ya mfumo wa njia ya chakula ni kwa asilimia 10.

Anazitaja saratani zingine zinazokuja kwa kasi hivi sasa kuwa ni ya shingo na kichwa inayochukua asilimia 7 ya wagonjwa wote, saratani ya matezi kwa asilimia 6 na ile ya damu kwa asilimia 4.

Saratani ya mfumo wa mkojo ina asilimia 3, saratani ya ngozi asilimia 3, jicho asilimia 2 na tezi dume ni asilimia 2 wakati huohuo aina zingine za saratani zikichukua asilimia 5.

Dk Kahesa anasema tangu 2005 mpaka sasa wagonjwa wapya wanaotibiwa katika taasisi hiyo wamefikia 129,075 na kwa wale wanaohudhuria kliniki ni 222,470.

“Waathirika wakuu wa saratani ni wanawake kutokana na aina ya zinazowashambulia wao pekee kuchukua asilimia 44, lakini carposis Sarcoma inaathiri wote hasa wale ambao mfumo wao wa kinga ya mwili umepungua, lakini madhara yake tunaweza kuyaona kwenye ngozi, mfumo wa chakula, hewa na sehemu zingine.

Serikali yaamua kupambana

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitoa Sh1 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, ili kupambana na ongezeko la wagonjwa wapya wa maradhi hayo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema mashine 100 za tiba mgando (cryotherapy) na mashine tisa za upasuaji mdogo (LEEP) pamoja na mitungi ya gesi 173 itakayowezesha mashine hizo kufanya kazi, tayari vimenunuliwa kupitia fedha hizo.

Ummy anasema mashine hizo zitatumika kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake watakaofanyiwa uchunguzi na kukutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Tumeshatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma ili kuweza kuhudumu bila vikwazo. Vifaa hivi vimekwishawasili nchini na vimesambazwa katika vituo vya Tiba 100 nchini kwa mikoa 10, Halmashauri 31 ambazo tumebaini zina vituo vichache vya kutolea huduma hizi ukilinganisha na Mikoa mingine.”

Anaitaja mikoa hiyo ni Mara, Singida, Geita, Dodoma, Tanga, Arusha, Manyara, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Anasema tangu 2008 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara imeshaanzisha vituo 459 kati ya hivyo, 343 ni vya Serikali na 116 vya mashirika na watu binafsi.

Kwa pamoja vinatoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa uzazi.

Friday, November 3, 2017

Itambue njaa iliyojificha na madhara yake kwa Watanzania

 

By Elias Msuya, Mwananchi

Japo Tanzania inajitosheleza kwa chakula kutokana na mavuno ya kilimo kila mwaka, bado Watanzania wanakabiliwa na njaa iliyojificha ya mlo kamili.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) inaonyesha Serikali hupoteza Sh800 sawa na asilimia 2.7 ya pato la Taifa (GDP) kwa mwaka, kwa sababu ya madhara ya upungufu wa virutubisho vya chakula vya chuma, vitamin A na tindikali ya foliki.

Mtaalamu wa Chakula na Lishe wa TFNC, Celestin Mgoba anasema mbali na fedha hizo, madhara mengine ni kupungua kwa nguvu kazi, watoto kushindwa kuelewa masomo darasani na kuongeza mzigo kwa Wizara ya Afya. “Mtu anahesabiwa ameshiba kama atapata mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamin na madini kila siku,” anasema Magoba na kuongeza:

“Kupata mlo kamili kunapunguza uwezekano wa mtu kuingia katika hatari ya kupata maradhi ya moyo, kisukari, mifupa na aina fulani za saratani.”

Akieleza maana ya utapiamlo, Magoba anasema ni upungufu wa virutubisho au ongezeko lake (kitambi).

“Upungufu wa virutubisho vya msingi ni njaa iliyojificha ambayo ni ukosefu wa madini na vitamin kwenye chakula. Madhara yake ni watoto kushindwa kukua, kukosa kinga ya mwili na afya kwa ujumla kwa watoto na kina mama walio katika umri wa kuzaa,” anasema Mgoba.

“Upungufu wa madini ya chuma husababisha watoto zaidi ya bilioni mbili duniani kupata mtindio wa ubongo na asilimia 25 ya vifo vya watoto kwa nchi zinazoendelea. Ukosefu wa madini ya iodine pia husababisha madhara kwenye ubongo wa mtoto,” anaongeza.

Mbali na madini, anasema ukosefu wa vitamin A huathiri asilimia 33 ya watoto na asilimia 37 nchini ikiwa ni pamoja na kupata upofu na vifo.

“Ukosefu wa folate (tindikali ya foliki na vitamin B9), husababisha vifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Ukosefu wa zinki hupunguza kinga ya mwili na kuongeza uwezekano wa maradhi ya kuhara hasa kwa watoto.

Anataja virutuibisho muhimu ni pamoja na zinc, folate, Niacin (B3), Cobalamin (B12), Thiamine (B1), Ribofalvin (B2), Pyrodoxine (B6) na Selenium akisema japo vinahitajika kwa kiwango kidogo (micro or milligrams) kwa siku, umuhimu wake ni mkubwa ikiwa ni pamoja na metabolizim, ukuaji na afya.

“Zinahitajika miligramu 18 za chuma, miligramu 11 za zinki na gramu 0.15 za iodine kwa siku. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, upungufu wa damu mwilini (anaemia) unasababishwa na upungufu wa madini ya chuma, ni tatizo sugu ambalo asilimia 40 ya watu duniani wanalo na kwa watoto ni asilimia 58.”

Hata hivyo, anasema kwa madini ya iodine wenye madhara ni asilimia 5 kwa kuwa upatikanaji wa chumvi yenye madini hayo ni kwa asilimia 90.

“Kwa Tanzania, asilimia 7 ya watu wana ugonjwa wa goita na wanaotumia chumvi yenye iodine ni asilimia 61,” anasema Mgoba.

Sababu za kukosa virutubisho

Akielezea sababu ya watu kukosa virutubisho licha ya kula na kushiba, Magoba anasema watu wengi wanakula vyakula visivyo na lishe ya kutosha kwa mfano nafaka, mbegu (legumes), mizizi ambayo kimsingi haina vitamin A, zink, chuma wala iodine.

“Wengi hawali vyakula vyenye virutubisho vya kutosha kama nyama, samaki, kuku, mayai, maziwa, matunda na mbogamboga. Hata ulaji wa vyakula vya mafuta ni mdogo. Mafuta husaidia ufyonzaji wa virutubisho mwilini,” anasema.

Anasema kutokana na ukosefu wa virutubisho hivyo, asilimia 34 ya watoto wa Tanzania hudumaa na asilimia 14 huwa na uzito mdogo.

“Kukosekana kwa Vitamin na madini mwilini hakusababishi njaa inayoonekana, bali isiyoonekana na matokeo yake watoto hubakiwa wakiwa na uzito mdogo, upungufu wa kinga, vipofu, kushindwa kuelewa masomo na maradhi ya akili,” anasema na kuongeza:

“Asilimia 17 ya watu wazima hushindwa kufanya kazi za uzalishaji kutokana na lishe duni.”

Anataja madhara mengine ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa neva za fahamu, matatizo ya uzazi, mfumo wa akili na utendaji kazi, ukuaji hafifu na mwisho kuwa mbilikimo, goita, matatizo ya kusikia na kuwa bubu.

Akieleza mbinu za kupambana na upungufu wa virutubisho, Mgoba anasema ni pamoja na kuongeza virutubisho (supplementation) na uimarishaji wa virutubisho (food fortification) na kuongeza virutubisho kwa njia za kilimo (crop biofortification).

Pia kuwapo kwa elimu ya lishe kwa jamii na kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Kwa upande wake, Mratibu mwandimizi wa mradi wa kuongeza virutubisho katika mfuko wa chakula (BNFB) Tanzania, Dk Richard Kasuga anasema tatizo la lishe ni sugu nchini, huku pia akitaja mikoa iliyoathirika zaidi.

“Mikoa yenye upungufu mkubwa kwa vitamin A ni Pemba Kaskazini asilimia 51, Kagera asilimia 47, Pwani asilimia 45, Manyara asilimia 44, Kigoma asilimia 39, Shinyanga asilimia 37 na Mtwara asilimia 36,” anasema Dk kasuga.

Anasema ili kuonyesha kuwa hiyo ni njaa iliyojificha, mikoa inayotajwa kwa uzalishaji mkubwa wa chakula nchini ndiyo inayoongoza kwa watoto wanaodumaa wakiwa chini ya miaka mitano.

Mikoa hiyo ni Rukwa asilimia 56, Ruvuma asilimia 44, Iringa asilimia 42, Kagera asilimia 42 na Geita asilimia 41.

Mikoa mingine ni Katavi, Mwanza na Tanga asilimia 39, Kigoma, Mbeya na Mtwara asilimia 38, Dodoma asilimia 37, Arusha na Manyara asilimia 36, Lindi asilimia 35 na Morogoro asilimia 33.

Mikoa yenye nafuu ni Pwani asilimia 30, Mara, Kilimanjaro na Singida asilimia 29, Tabora na Shinyanga asilimia 28 na Dar es Salaam asilimia 15.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunapunguza njaa isiyoonekana kwa watoto, kuonyesha jinsi ya kuongeza virutubisho kwenye mazao na kuimarisha nguvu za wadau na uwekezaji katika chakula,” anasema Dk Kasuga.

Friday, November 3, 2017

Nanasi linavyousaidia mwili kukabili maradhi

 

Mwili unapokosa kinga imara, huwa katika hatari ya kushambuliwa na kila aina ya maradhi. Ili kukabilina na hali hiyo, tunda la Nanasi linazosifa za kukabiliana tatizo hilo.

Nanasi ni miongoni mwa matunda yenye ladha nzuri mdomoni, lakini pia lina vitamini nyingi na virutubisho vyenye uwezo wa kuupa mwili nguvu na kuepuka kushambuliwa na maradhi.

Kwenye Nanasi kuna kirutubisho aina ya Bromelain kinachopatikana kwa wingi na virutubisho hivyo hulifanya tunda hilo kuwa na umuhimu kwa kujenga na kuimarisha kinga ya mwili wa binadamu.

Ulaji wa tunda hilo mara kwa mara unamsaidia mlaji kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kuvimba koo, baridi yabisi, gauti na hutibu matatizo ya tumbo na bandama.

Wataalamu wengi wa afya wanashauri ili binadamu upate kinga dhidi ya maradhi, anashauriwa kula tunda hilo kabla au baada ya mlo wake na wala asile nanasi na chakula kingine kwa wakati mmoja.

Usipofanya hivyo, virutubisho vilivyopo katika nanasi vitafanya kazi nyingine tofauti na ile iliyokusudiwa.

Nanasi lina virutubisho vya vitamin A,B na C na lina madini ya chuma, kopa na Phosphorous ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu.

Pia, tunda hilo hutibu matatizo ya ini, homa, vidonda vya mdomoni na husaidia kusafisha utumbo mwembamba.

Kwa wale wanaopoteza kumbukumbu, nanasi linao uwezo wa kutibu.

Linasaidia pia kutibu maradhi ya akili, kukosa mori, kutibu matatizo ya wanawake hasa ya upungufu wa hormoni na matatizo mengine ya sehemu za siri za mwanamke na husaidia kupata choo laini na kwa wakati.

Tatizo la upungufu wa damu pia linatatibiwa na nanasi ambalo pia husaidia kuongeza maziwa kwa wanawake wanaonyonyesha. (Hadija Jumanne)

Friday, November 3, 2017

Zitambue dalili za sonana na matibabu yakeDk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Mwanamke mmoja kati ya watano na mwanaume mmoja kati ya 10 wamewahi kuugua sonona katika maisha yao. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo hilo.

“depression” ni neno la kisayansi ambalo kwa tafsiri ya kawaida ndiyo tunaita sonona. Huu ni ugonjwa wa akili ambao mtu anaupata baada ya kupitia matatizo fulani na kumuacha kwenye huzuni au kusononeka kwa muda mrefu. lakini watu wengi bado hawajui kama hali hiyo ni ugonjwa kama yalivyo maradhi mengine.

Pamoja na sababu zinazochangia, lakini kitu kingine muhimu unachopaswa kukitambua ni dalili ugonjwa huo ni zipi.

Ninapotathimini sonona nikiwa na mgonjwa, hua namuuliza maswali haya; kwa kipindi cha siku chache zilizopita, umeshawahi kupatwa na hali iliyokufanya ujione kama hauna thamani na kupoteza matumaini? Au unakosa hisia kwenye vitu ambavyo awali vilikua vinakupa furaha na amani?

Kama jibu la maswali haya ni “ndiyo”, basi ni dhahiri mgonjwa huyo anakuwa anaugua sonona. Dalili nyinginezo zinazopaswa kufuatiliwa ni pamoja na kukosa hamu ya kula, kukosa usingizi wa kutosha (aidha kuchelewa kulala au hata kuwahi kuamka), kushindwa kutilia maanani mambo muhimu, kujiona kama huna uwezo wa kufanya jambo fulani na kila unapopaswa kufanya jambo hilo, unahisi uchovu, lakini pia wakati mwingine mtu anashawishika kujinyonga.

Ni dhahiri kwamba sonona ni tishio la maisha, kutokana na ukweli kwamba husabisha mtu kutofurahia maisha yake binafsi.

Katika kufuatilia ni kwa kiasi gani mgonjwa ameweza kuathirika na sonona, madaktari hutumia njia ya mahojiano kati yake na mgonjwa. Njia hiyo kitaalamu inajulikana PHQ-9(Patient health questionnaire).

Kupitia njia hiyo, daktari humuuliza mgonjwa maswali tisa maalum ambayo majibu ya mgonjwa yataonyesha ni kwa kiasi gani ameathirika na sonona kabla ya kumfanyia vipimo.

Cha kusikitisha ni kwamba, waathirika wengi wa tatizo hilo huwa hawaendi kupata ushauri wa daktari kwa dhana ya kuona aibu au kuona kuwa sonona sio tatizo la kulitilia maanani.

Sonona ni ugojwa kama yalivyo maradhi mengine ambayo yanahitaji msaada na yasipopatiwa tiba, yanaweza kuleta madhara makubwa kwa maisha ya kila siku. Kwa mfano, kama mtu ana vidonda vya tumbo na huamua kuyadharau maumivu yanayoambatana na vidonda hivyo bila kupatia tiba, ukingo wa utumbo mpana unakua hatarini zaidi kuathirika na kulazimika kufanyiwa upasuaji.

Na kwa sonona ipo hivyo. Daktari huenda asikuambie “jizuie na sonona ina madhara” kama hautoonyesha kuhitaji msaada wa daktari, sonona ni zaidi ya uifikiriavyo. Itakufanya upoteze hisia na kushindwa kufurahia mambo yote ya kijamii ambayo kwa kawaida yanaleta furaha katika maisha ya kila siku.

Ikiwa mgonjwa hajaathirika sana na sonona, ushauri wa kisaikolojia kwa mgonjwa namna ya kukabiliana na tatizo, utamsaidia. Aidha, kwa mgonjwa ambaye ameathirika zaidi na tatizo hilo, tiba ya dawa italazimika kutolewa kwake.

“Antidepressants” ni jina la kitaalamu ambalo linajumuisha makundi ya dawa za kutibu sonona.

Hata hivyo, dawa hizi pia huwa zinaleta matokeo mengine baada ya kutumiwa kama zilivyo dawa za aina nyingine. Matokeo kama ya uchovu, kuharisha au kukosa haja, mdomo kukauka ni baadhi tu ya matokeo ya kawaida ambayo mgonjwa anayapata baada ya kuzitumia dawa hizo.

Lakini matokeo haya yanatoweka baada ya siku chache. Mgonjwa anapaswa kutumia dawa hizo kwa muda hata zaidi wa miezi sita na hatakiwi kuacha kuzitumia hata kama akianza kupata afadhali ili kupunguza uwezekano wa ugonjwa kujirudia tena.

Pia, ukiwa na sonona ni rahisi sana kusikia hali ya uchovu na kukosa ari ya kufanya chochote, unashauriwa ufanye mazoezi kwani yanasaidia kusisimua vichocheo vinavyoleta hisia za kujisikia vizuri.

Hivyo ni muhimu kujilazimisha kufanya mazoezi hata kama unahisi uchovu.

Friday, November 3, 2017

Changamoto ya kutibu pumu

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Mara nyingi watu wengi hupenda kusikiliza na kuzingatia maelekezo mengi ambayo si sahihi wanayoelezwa na watu mitaani. Kwa mfano, mtu anaugua Pumu, badala ya kumpeleka hospitali, anashauriwa na watu ampatie dawa bila kupima au aende kwenye tiba za asili, mwisho wa siku mgonjwa anapoteza maisha au anazidi kuugua bila kupona. Wakati angempeleka kwa wataalamu wa afya, angeweza kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Pumu kitaalamu inaitwa Asthma ni ugonjwa hatari unaohitaji huduma za dharula, hatua stahiki zisipochukuliwa, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

Ugonjwa huu wenye tabia ya kusababisha mirija ya hewa kusinyaa, kukakamaa au wakati mwingine kuziba kabisa, huifanya hewa ishindwe kuingia na kutoka kwenye mapafu kutokana na njia hiyo kuwa nyembamba.

Ugonjwa wa pumu huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu kupitia mirija myembamba ya inayojulikana kitaalamu bronchioles.

Hali hiyo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje, hivyo kupumua kwa shida.

Tatizo hili linaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.

Mtu anayeugua pumu, hudumu nayo karibu kipindi chote cha maisha yake.

Aina ya pumu

Pumu imegawanyika katika makundi mawili; ipo ile ya ghafla inayoitwa kitabibu Acute asthma, mgonjwa aliye kwenye kundi hili hali yake huwa ya kawaida kwenye njia ya hewa isiyobadilika kati ya shambulizi moja na jingine.

Kundi lingine ni Pumu sugu (Chronic Asthma). Kundi hili huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya kuumwa, njia za hewa huzidi kuwa nyembamba na kusinyaa zaidi.

Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni:

Pumu inayobadilika (brittle asthma)

Kulingana na tabia ya kujirudia kwa matukio ya ugonjwa huo na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili, ambazo ni pamoja na ile inayobadilika ambayo ina tabia ya kujirudia kutokana na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.

Aina ya pili ni pumu inayobadilika ambayo mgonjwa anaweza kupata shambulizi la ghafla hata kama awali iliweza kuthibitiwa kwa matibabu.

Aina ya tatu ni Pumu hatari isiyobadilika. Pamoja na matumizi ya dawa kadhaa, zikiwamo za vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili (steroids), mgonjwa bado anaweza asipate nafuu ya haraka na anaweza kupoteza maisha.

Ipo pia pumu inayosababishwa na mazoezi (Exercise Induced Asthma)

Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya viungo.

Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia pua na mdomoni. Wakati mwingine inaweza kutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani na kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa.

Hali hii husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa.

Inashauriwa kwa watu wenye matatizo kama haya, kupasha moto misuli kwa mazoezi mepesi kabla ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu.

Ipo pia Pumu inayosababishwa na aina ya kazi. Mazingira ya kazi yanaweza kusababisha kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hilo.

Aina hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma, unga, mbao na nguo.

Pumu husababishwa na nini?

Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha shambulizi la pumu.

Mambo hayo ni pamoja na matatizo ya kinasaba.

Haya yanamhusisha mtu kwa karibu asilimia 90 hususani kipindi cha utoto.

Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.

Maendeleo ya kiuchumi

Ugonjwa wa pumu unaibuka sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ikilinganishwa na zenye maendeleo duni.

Magonjwa ya mapafu kama bronchitis, vyanzo vya mzio (allergens) ya vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya vyakula ni chanzo kimojawapo.

Uchafuzi wa mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali na kemikali kwenye maeneo ya kazi hasa ya viwanda yapo zaidi kwenye nchi zilizoendelea.

Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers ikiwamo propanolol, pia wapo katika hatari ya kupata shambulio la pumu.

Hatari ya ugonjwa wa pumu

Uwezekano wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu atakuwa na maradhi ya mzio, magonjwa ya ngozi au homa isababishwayo na aina fulani ya vumbi au kama atavuta chavu (pollen) kutoka kwenye maua au miti na kama atajihusisha na uvutaji sigara au kama ana historia ya ugonjwa wa pumu au mzio kwenye familia yao.

Dalili za ugonjwa wa pumu

Dalili za pumu ni pamoja na kuishiwa pumzi, kupumua kwa shida, kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing).

Kukohoa sana nyakati za usiku au asubuhi. Pia, kuwa na kikohozi kinachoambatana na kutoa makohozi mazito yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.

Mtu aliyepatwa na shambulizi kubwa la pumu (severe asthmatic attack) anaweza kushindwa kuzungumza na pia, anakuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa huku akitweta.

Vipimo na Uchunguzi

Pamoja na daktari kutaka kufahamu historia ya mgonjwa, anaweza pia kuamua kufanya vipimo ili kufahamu chanzo na madhara ya ugonjwa wa pumu kwa muathirika.

Matibabu ya Pumu

Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi au vyanzo vya mzio na matumizi ya dawa kwa walio na hali mbaya.

Kwa wagojwa wanaougua kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili.

Inashauriwa pia wenye tatizo hili kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea.

Pia, mgonjwa anashauriwa kuyaepuka mazingira ya baridi yanayoweza kuchochea kupata shambulio zaidi la ugonjwa huo.

aidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators).

Dawa za kuondoa mcharuko mwili kama vile cortisone ya drip (hasa wakati wa dharura) au nebulizer, na dawa za kuzuia mzio (antihistamine drugs).

Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri mgonjwa.

Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya (acute asthma) matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya oksijeni. Vilevile dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Aidha kwa vile mara nyingi shambulizi hili laweza kuwa la hatari sana, mgonjwa hulazwa hospitali na huongezewa hewa ya oksijeni, na kwa wagonjwa wasioweza kupumua kabisa, husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mashine maalum iitwayo (mechanical ventilator).

Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni kuepuka visababishi vya pumu na kuendelea na matumizi ya dawa zinazosaidia katika kutanua mirija ya hewa.

Kwa wagonjwa wanaopata mashambulzi ya mara kwa mara wanaweza kushauriwa na daktari kutumia dawa kadhaa zikiwemo zile zinazopunguza mcharuko mwili (mast cell inhibitors, inhaled steroids au oral steroids).

pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (muscle relaxants). Aidha ni vema pia kutibiwa na kuthibiti kutokea kwa magonjwa yote yahusuyo mfumo wa hewa.

Matumizi ya chanjo ya magonjwa kama influenza na pneumococcal pneumonia nayo husaidia sana katika uthibiti wa kutokea kwa pumu. Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu.

Friday, November 3, 2017

Pamoja programu yaja na mbadala wa kulinda kinywa

 

By Lilian Timbuka, Mwananchi

Ni kawaida kusikia uvumi miongoni mwa watu ambao si wataalamu wa afya wakiueneza kwa juhudi kubwa bila kujua au kujua wanapotosha umma.

Hivyo, ni vyema kujua kama mtu unatatizo la kiafya, unapaswa kwenda kuwaona wataalamu wa afya kwa ushauri zaidi.

Wapo watu wengi ambao hawafahamu ukweli juu ya umuhimu wa kutunza kinywa, na mara wapatapo maambukizi ya maradhi ya kinywa, hawafiki hospitali kwa ajili ya kupata tiba.

Kijana Ibrahimu Juma alisafiri kwenda kijijini kwao kwa ajili ya likizo, bahati mbaya aliugua jino, akamweleza bibi yake kuhusiana na hali hiyo.

Lakini badala ya bibi kumweleza mjukuu wake huyo aende hospitali akatibiwe, alikimbilia kwa jirani yake kuomba msaada wa tiba.

Kwa mujibu wa Ibrahimu, bibi alimletea kipande cha mavi ya ng’ombe yaliyokauka akamtaka akate kidogo na abandike kwenye jino linalomuuma, akidai ni tiba sahihi jambo ambalo si sahihi.

Huo ni mfano mmoja tu wa imani potofu iliyojengeka miongoni mwa watu kuhusiana na tiba sahihi ya kinywa ni ipi.

Lakini wapo watu hudai kupiga mswaki mara nyingi na kwa nguvu huzuia kuoza kwa meno.

Wataalamu wa tiba ya kinywa wanaonya kuwa kupiga mswaki mara nyingi na kwa kutumia nguvu, kunaweza kusababisha kukwangua sehemu ngumu ya nje ya jino, kulifanya laini na hatimaye kuuma au hata kuvunjika.

Kupiga mswaki mara mbili, taratibu na kwa njia sahihi ndicho kinachosaidia meno kuwa na afya

Wengine husema mtu hana haja ya kumuona daktari wa meno kama hajaugua.

Lakini kwa mujibu wa madaktari wa meno, kila mtu anatakiwa kuchunguzwa kinywa mara kwa mara.

Kwani siyo meno yote yanayoonekana mazuri na imara ni mazima, mengine yanaweza kuwa yameharibika hasa yale ambayo yako sehemu za ndani ambazo si rahisi kuonekana.

Hata hivyo, baada ya kubaini changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kuhusiana na tiba ya kinywa, hivi karibuni Chama cha Madaktari Wanafunzi wa Afya ya Kinywa Tanzania (Tanzania Dental Students Association-TDSA) wakishirikiana na Chama cha madaktari wanafunzi wa afya ya kinywa wa nchi za Ulaya (European Dental Students Association –EDSA) na Chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS) waliungana kutoa huduma za uchunguzi wa kinywa na matibabu kwa wanafunzi wa Shule za msingi za Uhuru Mchanganyiko, Buguruni na Shule ya Nyamata Academy, zote za Jijini Dar es Salaam.

Madaktari hawa wameanzisha program maalumu iitwayo ‘Pamoja’ ikilenga kutoa elimu na kutibu maradhi ya kinywa kwa wanafunzi.

Rais wa TDSA, Evarist Mulyahela anasema hii ni awamu ya tatu kufanyika tangu ilipoanzishwa mwaka 2015.

“Awamu hii ya tatu tuliianza Septemba 9 na tukaihitimisha Septemba 22, tuliwahudumia wanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ambayo ina wanafunzi walemavu pia, hivyo kufanya kuwa ya kipekee tukilinganisha na awamu mbili zilizopita za 2015 na 2016,” anasema Mulyahela na kuongeza: “Huduma hii tuliitolea Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili.”

Anasema zaidi ya wanafunzi 1,000 walipatiwa elimu ya afya ya kinywa kwa vitendo, namna sahihi ya kupiga mswaki kwa ufanisi.

Mulyahela anasema wanafunzi 838 walifanyiwa uchunguzi wa kinywa bure na kati yao asilimia 51 wasichana na asilimia 1.6 walemavu.

Wanafunzi 297 walipatiwa aina tofauti ya matibabu ya maradhi ya kinywa yaliyobainika.

“Matibabu tuliyoyatoa ni pamoja na kuziba meno, kusafisha na kung’oa yaliyobainika kuharika kwa kiwango kikubwa.

Licha ya kutoa huduma hiyo kwa wanafunzi, madakatri hao walitoa pia elimu kwa walimu wa shule hizo ili kurithisha elimu hiyo ya afya ya kinywa, ambayo pia wataweza kuwafundisha wanafunzi mara kwa mara kwenye vipindi vyao darasani.

Changamoto ya matibabu ya kinywa

Ofisa Programu wa Pamoja, Protus Musungu anasema bado kuna changamoto nyingi za kukabiliana na maradhi ya kinywa zinazowakumba madaktari na wataalamu wa afya ya kinywa.

Anataja changamoto mojwapo ni ukosefu wa vifaatiba kwenye maeneo wanayofika kutoa huduma.

Musungu anasema kulingana na muundo wa program wanayoifanya, wanauhaba wa viti vya matibabu vinavyohamishika pamoja na vifaatiba vya meno.

“Lakini pia tatizo la wakarimani kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia pia lilitupatia shida,” anasema Msungu.

Hata hivyo, anasema ili elimu ya kulinda afya ya kinywa iweze kufika kwa Watanzania wote, kuna haja kwa wadau mbalimbali wa afya nchini, kushirikiana na Serikali kuhamasisha kufanyika kwa uchunguzi wa afya ya kinywa kama yalivyo maradhi mengine kwa wananchi. Tunakaribisha wadau mbalimbali kuchangia “Pamoja kama tutasaidiwa upatikanaji wa vifaatiba vitakavyotuwezesha kuifanya kazi hii, tuko tayari muda wowote,” anasema ofisa huyo.

Msungu anasema umefika wakati wa kuongeza nguvu ya kuihamasisha jamii ijenge utamaduni wa kwenda hospitali kwa uchunguzi wa afya ikiwamo afya ya kinywa angalau mara moja kwa mwaka.

Anasema hiyo itasasidia kugundulika mapema kwa matatizo yoyote ya kiafya na kuwezesha utatuzi wa mapema kufanyika.

Wakati Msungu akitoa ushauri huo kwa jamii, wataalamu wa kinywa na meno wao pia wanaianisha namna ya kutunza meno ya watoto.

Dk Onesmo Sayo anasema wazazi wanapaswa kuanza kusafisha kinywa cha mtoto siku chache baada ya kuzaliwa kwa kufuta fizi zake kwa kitambaa safi kibichi.

Anasema mara tu meno yaanzapo kuonekana, hapohapo huweza kuanza kutoboka.

Dk Shayo anasema meno ya mbele ya utotoni huweza kujitokeza kinywani miezi sita baada ya kuzaliwa, ingawa baadhi ya watoto huweza kuchelewa kuota meno hadi anapofikisha miezi 12 au 14.

Hata hivyo, anasema ni vyema mzazi akajiridhisha mtoto wake anaweza kupiga mswaki mwenyewe kinyume cha hapo anashauri mzazi au mlezi aendelee kumpigisha mswaki mara mbili kwa siku kwa kutumia mswaki wa kitoto pamoja na dawa ya meno yenye madini ya floridi kiasi cha ukubwa wa punje ya maharage.

“Wakati mtoto anapokuwa na meno mawili yanayogusana tayari, anza kumzoesha kuflosi kila siku,” anasema daktari huyo.

Watoto Wa Umri Chini ya Miaka Mitatu

Kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 3, wazazi ama walezi lazima waanze kumpigisha mswaki mara tu meno yanapoanza kutokeza kinywani, mswaki huo uwe ni mdogo na dawa ya meno yenye madini ya floridi kidogo kiasi cha ukubwa wa punje ya mchele.

Ni lazima kupiga mswaki kwa umakini asubuhi baada ya kifungua kinywa na usiku kabla ya kulala. “Hakikisha mtoto hamezi dawa ya meno aliyotumia kupigia mswaki, badala yake ateme yote na kusukutua na maji,” anashauri.

Friday, November 3, 2017

Wasimulia vipodozi, rangi za midomo zilivyoathiri afya zao

 

By Lightness Mndeme na Jonathan Musa, Mwananchi

Kujiremba ni hulka ya wanawake wengi ambao mara nyingi unaweza kuwakuta wakitumia sehemu kubwa ya muda wao wa asubuhi kwa ajili ya kujiweka sawa na kujipendezesha.

Hata hivyo, pamoja na urembo kupendwa na wengi, lakini katika upande wa pili kuna jambo linalojitokeza, je vipodozi hivyo ni salama kiasi gani?

Uthibitisho kuhusu usalama wa vipodozi hivyo umejitokeza wakati mama mmoja mwenye miaka 54 aliyetambulika kwa jina la Mariam Said alipozungumza na gazeti hili na kukiri namna ngozi yake ilivyoharibika kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.

Anasema amekua akitumia vipodozi vya aina mbalimbali ikiwamo vile vya kung’arisha ngozi na vinginevyo. Lakini sasa ngozi yake inaonekana kama imeungua.

Hivi ni wapi Mariam alikosea?

Alianza kutumia vipodozi hivyo bila hata kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya urembo na mara zote alifanya hivyo kutokana na msukumo alioupata toka kwa marafiki zake akiamini itamwezesha kukata kiu yake.

Hata hivyo, mambo hayakuenda kama alivyotarajia, kwani kadiri siku zilivyokatika ndivyo ngozi yake ilivyozidi kuharibika. Alipoulizwa ni wapi alikuwa akinunua vipodozi hivyo, alisema; “Wakati mwingine nilinunua kutoka kwenye maduka madogo yaani vioski ambako walidai bidhaa zao walikuwa wakipata toka nje.”

Aliongeza: “Mara zote nilikuwa nikipuuzia kuzingatia yale yaliyoandikwa kwenye lebo maana mchanganyiko wa kemikali kwenye vipodozi hivyo sikuona kuwa na tatizo kwangu na jambo nililolitilia maanani zaidi ni kutaka kupata matokeo niliyokuwa nikiyatamani.” Haya ndiyo yanayowakumba waathirika kama kina Mariam ambao mara nyingi hushawishika kutumia vipodozi kutokana na matangazo ya vyombo vya habari na hata katika mazungumzo ya kawaida kwenye vijiwe na maeneo mengine.

Kwa nini ni muhimu kujua kile kilichomo kwenye kipodozi

Mmoja wa wataalamu wa afya, Dk Mwamvua Gugu aliwahi kuzungumzia juu ya vipodozi na kusema: “Baadhi ya vipodozi ambavyo havijathibitishwa ni hatari kwa sababu vinachanganywa na kemikali zenye madhara ya muda mrefu kwa ngozi ya binadamu na vinaweza kuchukua miaka mingi kuonyesha athari zake.”

Kwa mujibu wa Dk Gugu, vipodozi vya kung’arisha ngozi hutengenezwa na kemikali za zebaki, chloroquinone na hydroquinone; ambazo wataalamu wa afya wengi hawashauri zitumike.

Akielezea namna biolojia inavyofanya kazi katika kuharibu ngozi, Dk Gugu anasema, “Ngozi yetu imetengenezwa na kitu kinachojulikana melanin ambacho kinaifanya ionekane katika uasili wake. Kuwapo kwa kemikali zozote hatarishi, kunaweza kuifanya ngozi kupoteza nuru yake na hata kusababisha maradhi ya ngozi.

Kama watu wanayajua haya, kwani wanaendelea kununua vipodozi hivi?

Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini idadi kubwa ya vipodozi vinavyotumiwa na wanunuzi wengi ni vile vinavyouzwa mitaani na huuzwa kwa bei ya chini bila kuzingatia ubora wake.

Kwa mujibu wa Dk Sylvester Mathias ambaye ni ofisa mstaafu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), kuwapo kwa vitu vya kughushi vikiwamo vipodozi kunaweka afya za wananchi wengi hatarini achilia mbali suala la upotevu wa fedha.

Rangi za mdomo

Hili halina ubishi kabisa kuwa unapogusa mkebe wa mwanamke wenye vipodozi suala la kukutana na rangi za mdomo siyo kitu kigeni. Ni eneo muhimu sana kwao.

Mwanamke hawezi kuwa amekamilisha orodha yake ya vipodozi bila kuwa na urembo huo. Katika majiji makubwa likiwamo la Mwanza, kuna maduka maalumu yanayofahamika kama boutiques ambayo ni mahsusi kwa kuuza urembo wa kike.

Sophia Nyange (29) anayemiliki duka la vipodozi jijini Mwanza anasema hupata faida kutokana na biashara hiyo kwa vile sehemu kubwa ya wateja wake ni wanawake wafanyakazi.

“Kabla sijafungua biashara hii nilikuwa nikiuza nguo za watoto. Baadaye nikaja kugundua biashara hiyo ilikuwa haifanyi vizuri kama nilivyokuwa nikitaraji, hivyo rafiki yangu mmoja alinidokeza nifungue duka kwa ajili ya vipodozi vya wanawake,” anasema.

Sophia anasema huagiza bidhaa zake kutoka Nairobi Kenya, kila baada ya wiki moja. Wakati mwingine bidhaa zake za dukani huishi hata kabla ya mzigo mwingine haujaingia. “Natumia kama Sh2.5 milioni kuagiza mzigo mmoja kutoka Nairobi na hii hainipi kikwazo chochote hasa pale kunapokuwa na mahitaji makubwa kutoka kwa wateja hasa wale wa jumla ambao hulipa kabla ili wapate mzigo kama rangi za mdomo,” anasema.

Wakati kuna wale ambao kamwe hawawezi kutoka bila kwanza kujipaka rangi ya mdomo, poda sambamba na wanja, lakini wapo wanawake wengine huwa hawana tabia hiyo.

Pamela Juma (24) mkazi wa Geita, ameliambia gazeti hili kuwa amekatazwa kutumia rangi ya mdomo na daktari wake. “Miaka miwili iliyopita nilianza kutumia rangi za mdomo za aina mbalimbali, lakini hivi karibuni nilianza kutoka vipele mdomoni na ndipo dokta akanishauri kuacha kabisa kuzitumia,” anasema Pamela.

Hata hivyo, Pamela anakiri ushauri wa daktari wake. Anasema pamoja na kuacha kutumia urembo huo, midomo yake bado inapasuka na kutoa damu.

“Nadhani matumizi ya kupita kiasi yamenifanya midomo iwe dhaifu kwa vile kinga yake imepungua,” anasema mwana dada huyo.

Dhana inayotolewa na Pamela inafafanuliwa zaidi na Perpetua Hillary, mtaalamu wa ngozi mstaafu ambaye anasema rangi za mdomo mara nyingi huambatana na madhara yasiyokwepeka.

Wanawake kama Pamela huweka rangi ya mdomo mara nyingi wanapotaka kutoka nyumbani na wanaendelea na hali hiyo karibu siku nzima na hata wanapoingia kitandani.

“Kwa hali kama hii, lipustiki inaweza kukusababishia aleji, muwasho na mchubuko wa mdomo. Kiwango fulani cha kemikali yenye kuzulu pia inaweza kusababisha saratani,” anasema Dk Hillary.

Friday, November 3, 2017

Madhara wayapatayo wanaotoa mimba

 

Karibuni wasomaji wa kona hii ya piramidi ya afya, leo nimeona nitumie nafasi hii kujibu swali nililoulizwa hivi karibuni na msomaji.

Aliuliza mtu aliyewahi kutoa mimba mara mbili je! akiupata ataweza kujifungua salama?

Swali hili limekuwa likiulizwa kwa mara hasa na wanawake waliowahi kutoa mimba kwa makusudi au kwa sababu za kitabibu.

Nitajibu swali kutokana na alivyouliza msomaji, kwakuwa ametumia neno kutoa mimba, ina maana mimba hiyo ilitolewa kwa kudhamiria kinyume na sheria amabyo kwa lugha ya kitaalam tunaita Illigeal abortion.

Kutoa mimba kinyume na sheria maana yake ni uondoaji wa mimba iliyotungwa kabla ya kutimia muda wake wa kujifungua bila sababu ya kitabibu.

Hata hivyo, muuliza swali hakuweka umri wa mimba hizo zilizotolewa wala ni kwa muda gani amekaa bila kupata ujauzito.

Ila ieleweke si lazima utolewaji wa mimba uwe na muingiliano wa uwezo wa mwanamke kupata mimba. Jambo la msingi ni utoaji uwe salama usio na madhara yoyote.

Katika nchi ambazo kutoa mimba si uvunjaji wa sheria, inaonyesha wanawake wengi wanaotolewa hubaki salama bila kudurika na hata baadaye anaweza kubeba mimba tena.

Hii inamaanisha mwanamke aliyetoka kutoa mimba,akijamiiana bila kutumia kinga, anaweza kupata mimba ndani ya wiki mbili zitakazofuata ili mradi tu kiyai cha kiwe kimepevuka.

Mtu anaweza kutoa mimba hata mara tano lakini bado akawa na uwezo wa kubeba tena na akazaa iwapo tu utoaji huo utakuwa ulifanywa kwa kuzingatia utaratibu na haukuleta madhara yoyote.

Hata hivyo, wataalamu wanasema madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutoa mimba ni pamoja na maambukizi ya via vya uzazi, majeraha ya mlango wa uzazi na ndani ya mfuko wa uzazi ndiyo yanayoweza kusababisha mtu kushindwa kupata ujauzito baadaye au akapata lakini ikatoka.

Ila ikumbukwe, utoaji wa mimba bila utaalamu mara kwa mara unaweza kusababisha majeraha kwenye mlango wa uzazi na kuufanya uwe dhaifu na kila mimba ikitungwa inakuwa na uwezekano mkubwa wa kutoka.

Maambukizi ya nyumba ya uzazi yanaweza yakatokea wakati au baada ya mimba kutolewa, hivyo uambukizi huo ukasababisha via vya uzazi ikiwamo mirija kuharibika.

Kuhusu kuwahi au kuchelewa kuzaa

Suala hili litategemea pia kama hakuna madhara yaliyojitokeza na mzunguko wa hedhi wa muhusika kurudi katika hali yake ya kawaida.

Inashauriwa kitaalamu, mwanamke aliyetoa mimba au mimba kuharibika na akasafishwa, apumzike kwa miezi Sita hadi 12, ndipo abebe ujauzito mwingine.

Kwa kufanya hivyo, kutamsaidia kuupa mwili nafasi ya kujijenga upya na homoni kurudi katika utaratibu wake wa awali.

Ikumbukwe mimba inapotungwa hutokea mabadiliko mengi ya mwili yanayolenga kuandaa mazingira ya ukuaji wake.

Ni muhimu kuepuka mimba zisizo tarajiwa hasa kwa wasichana walio shuleni, kwani kunakuwa na madhara mengi ya kimwili na kimaisha. Kwani wengi hujikuta wakifukuzwa shule na wengine hudhurika kiafya kwa sababu ya kuzitoa kwa njia isiyosalama.

Ikumbukwe kuwa mtaani watu hufanya pasipo kuwa na ujuzi wala kuzingatia usafi wa vifaa, hivyo hatari ya kupata maambukizi ya maradhi mbalimbali ni kubwa. Kwa watu wazima ni muhimu kutumia njia salama za kupanga uzazi.

Friday, October 6, 2017

Afya ya ubongo inavyochochea maendeleo

 

By Maniza Zaman, Mwananchi

Wiki moja iliyopita nilikuwa Kigoma, moja ya mkoa maskini sana Tanzania. Niliwaona watoto wengi, wengine wakiwa wamebebwa mgongoni na mama zao, wengine wakiambatana na ndugu zao mtaani, wengine wamekaa chini kwenye mchanga mwekundu wakiwa katika dunia yao.

Nilijiuliza walikuwa wanafikiria nini, ni matunzo gani wanapata na kuna fursa gani katika maisha yao ya siku zijazo.

Nilijiuliza pia ni kinamama, kina baba na walezi wangapi wanafahamu namna siku za mwanzo za utoto zilivyo muhimu kwa maisha ya mtoto na namna gani tunaweza kufikisha ujumbe wa kisayansi juu ya umuhimu wa siku za utotoni katika nyumba na jamii zote nchini.

Tunao wajibu na dhamana ya kuufikisha ujumbe huu na kuzisaidia familia kulea familia zao, na hizi ndio sababu za kwanini lazima tutimize jukumu hili.

Wataalamu wanasema ubongo hukua kwa kasi kubwa katika siku 1,000 za mwanzo wa uhai wa binadamu. Hiki ni kipindi kinachoanzia kutungwa kwa mimba hadi umri wa miaka miwili.

Kila mara mama au baba anapocheza na kucheka, kusoma kitabu au kushiriki mchezo na mwanawe, ujue kuna maelfu ya hisia chanya zinazojengeka kwenye ubongo wa mtoto huyo mchanga, zinazojenga uwezo wake wa kujifunza, utendaji, kuendana na mabadiliko na hata kukabiliana na changamoto.

Utafiti uliodumu kwa miaka 20 na kuchapishwa katika jarida la Science, unaonyesha watoto wanaotoka katika kaya maskini na kupata uchocheaji bora wa kiwango cha juu katika utoto wao, walipata asilimia 25 zaidi ya kipato kwa wastani katika utu uzima wao kuliko wale ambao walikosa hatua hizo utotoni

Ripoti mpya ya ulimwengu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) iitwayo ‘Siku za Mwanzo za Maisha ya Kila Mtoto ni Muhimu (Early Moments Matter For Every Child).’ Inasema kipindi cha tangu kutungwa mimba hadi kuanza shule ni muhimu. Ni fursa adimu katika kuandaa vema ubongo wa mtoto. Huu ndiyo wakati wa kuujenga ubongo wake. Ikiwa watoto watalelewa kwa namna inayojenga vema akili zao, wataweza kujifunza vema, hivyo wataweza kuchangia na kupata kipato bora zaidi. Hii itawasaidia wao, familia zao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Watoto wanahitaji huduma bora za afya na lishe, kuchangamshwa, fursa za kujifunza utotoni na mazingira salama ili ubongo wao uweze kukua vema.

Kwa bahati mbaya duniani kote, mamilioni ya watoto wanakosa fursa hii. Watoto milioni 155 wamedumaa, watoto milioni 230 wanaishi katika mazingira yaliyoathiriwa na machafuko na wanakabiliwa na msongo wa mawazo; wengine milioni 300 wanaishi katika maeneo yaliyoathirwa na uharibifu wa mazingira, haya mambo yote yanaathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Tanzania pia ina maelfu ya watoto wanaokosa vichochezi hivyo vinavyolea ukuaji wa kiwango cha juu cha ubongo wao. Kwa mfano, lishe duni miongoni mwa watoto nchini imefanya asilimia 34 ya walio na chini ya miaka mitano kudumaa.

Wataalamu wanasema kudumaa humkosesha mtoto fursa ya kukua akiwa na afya bora, kumkosesha uwezo wa kujifunza kikamilifu na hata kupunguza nafasi ya kupata ajira akifikia umri wa kuajiriwa.

Ukatili dhidi ya watoto na kukua katika mazingira yanayomuweka katika hatari ya ukatili, inawasababishia msongo wa mawazo hivyo kuathiri ukuaji wa ubongo wao. Utafiti unaonyesha Tanzania inakabiliwa pia na tatizo la ukatili dhidi ya watoto. Tanzania iko katika kipindi muhimu cha historia yake. Katika miaka 10 hadi 15 ijayo, sehemu iliyo kubwa ya idadi ya watu wa taifa hili yaani vijana, wataingia katika umri wa miaka ya uzalishaji mali. Lakini, wakati nchi inakaribia kufikia hadhi ya kipato cha kati huku kukiwa na msukumo mkubwa wa kisiasa kuleta kwa haraka uchumi wa viwanda, sehemu kubwa ya nguvu kazi ijayo itakayosaidia kufikiwa kwa malengo haya, yaani, watoto wa leo, wanabaki katika hali ya unyonge pasipo matunzo yanayostahili.

Tunawezaje kubadili hali hii.

Ukosefu huu wa usawa si tu unahatarisha hatma ya watoto, lakini pia unahatarisha uwezekano wa Tanzania kufikia malengo yake.

Hii ina maana kwamba lazima uwekezaji mkubwa ufanywe kwa watoto.

Hesabu zimekwishafanyika, Ripoti mpya ya Unicef inaonyesha Dola 0.5 za Marekani zikiwekezwa kwa mtu mmoja, inawezekana kujumuisha mikakati ya malezi ya utotoni katika program za lishe na afya zilizopo.

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi ya Marekani (The US National Bureau of Economic Research) inasema kiwango cha faida ya kila mwaka kutokana na programu za uwekezaji katika makuzi ya mtoto (ECD) ni zaidi ya asilimia 13.7.

Manufaa yanaonekana kupitia matokeo bora kwenye elimu na afya, viwango vya chini vya uhalifu na vipato vya juu kwa mtu mmojammoja. Utafiti pia unathibitisha kuwekeza kwa kipindi hicho cha utotoni kuna manufaa makubwa kuliko kuwekeza kwenye hatua nyingine za ukuaji wa mtoto.

Wakati kuna jitihada zinaonekana sehemu mbalimbali duniani kukabiliana na changamoto za watoto, bado uwekezaji katika hatua hii ya awali ya ukuaji wake haijapewa kipaumbele.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), yanatoa fursa ya kuendeleza jitihada hizo. ‘Ripoti ya Siku za Mwanzo za Maisha ya Kila Mtoto ni Muhimu’ inasisitiza umuhimu wa kuitimiza ahadi hiyo. Wito wa Unicef kwa Serikali na asasi washirika, lazima tuwekeze kwa haraka katika huduma zinazowapa watoto hasa wale walionyimwa fursa kabisa, mwanzo bora wa maisha. Kwa mfano, kwa kutenga asilimia 10 ya bajeti za taifa za elimu kwa ajili ya elimu ya awali, kutaongeza idadi ya watoto waliopata fursa za mapema za kujifunza. Ili kuwafikia wengi na familia nyingi kwa gharama nafuu, serikali na washirika wanaweza kuunganisha hatua za kutatua matatizo ya utotoni katika huduma zilizopo, kama upimaji afya na matunzo ya watoto katika jamii. Sera rafiki kwa familia kama likizo ya uzazi yenye malipo na likizo ya kunyonyesha bila kuathiri kipato cha mama, ni lazima sasa ziwepo. Na ni lazima tupime maendeleo kwa kukusanya takwimu kuhusu viashiria muhimu.

Tanzania kuna programu zinazolenga malezi ya utotoni, lakini bado watoto wengi hawajafikiwa na programu hizo. Unicef inafanya kazi na serikali na wadau wengine kuweka kipaumbele kwa malezi ya utotoni na kufikisha ujumbe wa kisayansi kuhusu suala hilo. Mchango wa Unicef kwa serikali ni pamoja na kuisaidia kuweka msisitizo wa kumpa hamasa mtoto na malezi bora.

Wafanyakazi wa afya waliopatiwa mafunzo stahiki, wanafanya kazi kubwa vijijini kwa kutoa mafunzo kwa wazazi juu ya malezi bora na namna ya kuelewa tabia za watoto wachanga. Vikundi vya kina mama wanapewa mafunzo ya namna ya kutengeneza vifaa vya kuchezea vya watoto vya gharama nafuu kutokana na malighafi zinazopatikana katika mazingira yao.

Mambo yote haya yanasaidia kuboresha malezi ya watoto.

Hivyo basi, mara nyingine utakapopata fursa ya kumwangalia mtoto mchanga, tafadhali kumbuka kuwa ukuaji vema wa ubongo unahitaji lishe bora, huduma bora ya afya, mawasiliano chanya na mazingira salama. Inaweza kuonekana kuwa ni kitu kidogo, lakini maendeleo ya nchi yanategemea watu wenye uwezo kiakili. Inawezekana Tanzania kuwa na mamilioni ya watu wenye uwezo wa kiakili- wakiwamo wale watoto niliowaona mkoani Kigoma wiki iliyopita.

Maniza Zaman ni Mwakilishi wa Unicef Tanzania     

Friday, October 6, 2017

PIRAMIDI YA AFYA: kichefuchefu na kutapika kwa wajawazito

 

By Dk Shita Samwel

Kupata tatizo la kichefuchefu na kutapika katika hatua za awali za ujauzito hasa asubuhi, ni jambo la kawaida linaloweza kudumu mpaka wiki ya 14 ya ujauzito na kuisha lenyewe bila tiba.

Iwapo ujauzito unaweza kusababisha madhara ikiwamo kupata kichefuchefu na kutapika kulikopitiliza na kusababisha upungufu mkali wa maji na kupoteza uzito wa mwili.

Hali hiyo hujulikana kitabibu kama hyperemesis gravidarum, huwakabili wanawake 3 kwa kila wajawazito 1000 na huweza kuwapo mpaka wiki ya 20 na kuendelea.

Dalili zakeni mbaya na huambatana na madhara makubwa ukilinganisha na hali ya kujisikia vibaya katika hatua za awali za ujauzito hasa asubuhi, muda ambao hujulikana kama ‘morning sickness.’

Mara nyigi chanzo cha hali hiyo ni mabadiliko yanayotokana na hali ya ujauzito ikiwamo ya kiwango cha homoni mwilini.

Ingawa yako matatizo ya kiafya ambayo yanaweza kumsababishia mjamzito kutapika sana ikiwamo kuugua malaria, UTI, maradhi ya mfumo wa chakula na ujauzito pacha na kuwa na ujauzito uliokosa uhai unaoitwa Molar pregnancy.

Kutapika kulikopitiliza husababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini ambao husababisha madhara zaidi kama kutaambatana na upungufu wa chumvi chumvi, protini na sukari kuwa chini (utapiamlo) na vitamini mbalimbali.

Pia, ini linaweza kuathirika na kushindwa kufanya kazi, hali inayosababisha tatizo la mwili kuwa wa manjano (jaundice).

Hakuna madhara ya moja moja kwa mtoto aliye katika nyumba ya uzazi, isipokuwa huathirika kutokana na matokeo ya madhara aliyoyapata mama.

Dalili zake ni zipi

Dalili na viashiria ni pamoja na kutapika na kupatwa na kichefuchefu cha mara kwa mara, kuhisi hali ya kupoteza fahamu, kuishiwa nguvu, hali ya kuchanganyikiwa, mapigo ya moyo kuwa ya kasi, kupauka ngozi, midomo kuwa mikavu na ngozi kuwa ya njano (endapo ini likuwa limeathirika).

Nini kifanyike kudhibiti hali hiyo

Ili kudhibiti halihiyo, mjamzito anapaswa kwenda hospitali au katika kituo cha afya kuonana na wataalamu wa afya ya mama na mtoto mara tu anapopatwa na tatizo hilo.

Daktari atafanya uchunguzi wa vipimo ili kubaini chanzo cha tatizo ambalo mara nyingine husababishwa na maradhi.

kuyaweka kando maradhi yanayoweza kusababisha kutapika sana au kama atabaini ni kutapika kwa kawaida kutokana na ujauzito, atamshauri kula vyakula vikavu kidogo na maji kiasi ambayo anatakiwa kuyanywa mara amalizapo kula chakula.

Na maji hayo anatakiwa kuyanywa baada ya saa moja au mbili kupita baada ya mlo.

Pia, daktari atampatia mjamzito huyo dawa ya vitamini B au vitamini mchanganyiko kutokana na tatizo hilo kuambatana na upungufu wa vitamini mwilini.

Kama mgonjwa atabainika anatapika kupita kiasi na ana upungufu wa maji mwilini, atahitajika kulazwa ili kuongezewa maji kwa njia ya mshipa.

Mgonjwa huwekwa bila kula chochote kinywani Saa 24 na kupewa dawa za kuzuia kutapika mpaka hali itakapoimarika.

Mgonjwa hupewa ushauri nasaha na elimu ya afya ili kuelewa tatizo lake ili kumwezesha kuwa na utulivu wa kiakili.     

Friday, September 29, 2017

Asilimia 70 ya watu maskini hufariki dunia kwa saratani

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Kadiri dunia inavyopiga hatua za kiuchumi katika maeneo ya nchi zinazoendelea ndivyo pia magonjwa yasiyoambukiza yanavyozidi kujitokeza na kuipa hofu jamii.

Saratani ni moja ya janga hatari katika afya zetu kwani wengi wa wagonjwa hushindwa kupona na huugua kwa muda mrefu na kupata mateso makubwa kabla ya kufariki dunia.

Saratani kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama malignancy, cancer, neoplasm au tumour kwa lugha ya Kiingereza ni new growth. Pia kwa Kiswahili hujulikana uvimbe unaosambaa.

2008 peke yake watu milioni 7.6 walikufa kwa saratani duniani kote, hii ilikua ni sawa na asilimia 13 ya vifo vyote ndani ya mwaka huo.

Hata hivyo, utafiti umebaini asilimia 70 ya saratani zinatokea katika maeneo mengi wanayoishi watu wa hali ya chini katika nchi mbalimbali.

Pia, inaelezwa saratani inashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vingi kwa nchi zilizoendelea huko magharibi baada ya ugonjwa wa moyo.

Imefika mahali baadhi ya nchi duniani zimeamua kupitisha sheria inayoruhusu kumpa huduma ya kifo cha huruma, kifo kisicho na maumivu mtu anayeugua ugonjwa huyo.

Pamoja na kupingwa kwa huduma hizi kutokana na kutoendana na maadili ya tiba, lakini nchi hizo ziliamua kufanya hivyo baada yakuona mateso makali nay a muda mrefu wanayoyapata wagonjwa hawa.

Saratani inaanzaje

Ni hali inayojitokeza baada ya chembe hai za mwilini yaani seli kukua kiholela baada ya kutokea mparanganyika ndani ya chembe hai.

Saratani ni ugonjwa unaotokea baada ya chembe hai zisizo za kawaida kuzaliana na kuongezeka idadi pasipo kudhibitiwa, hivyo kuweza kuvamia sehemu nyingine za mwili na kuleta madhara.

Chembe hai za saratani huweza kusambaa maeneo mengine ya mwili kupitia mfumo wa damu na mfumo unaochuja vimelea vya maradhi unaoitwa lymph na tishu zilizo jirani ilipo saratani.

Ipo tofauti kubwa katika kupata saratani kwa upande wa umri, jinsia na mazingira tunayoishi.

Tofauti ya kiuchumi na kimaendeleo katika baadhi ya maeneo, huweza kuonekana katika kujitokeza kwa saratani mbalimbali.

Mojawapo ni ile ya uvimbe mgumu kama ya mapafu na matiti zinazojitokeza zaidi katika nchi zilizoendelea.

Hatari ya mtu kupata saratani ya mapafu ni mara nne zaidi kwa mtu anayeishi nchini Uingereza ukilinganisha na mtu aliyeishi India.

Tofauti nyingine ya kimaeneo ni ya saratani ya shingo ya uzazi.

Kwa nchi za Carribien, saratani hii inashika namba mbili kwa kusababisha vifo vya wanawake.

Kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, saratani ya mlango au shingo ya uzazi, Tanzania ndiyo inaongoza kwakuwa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Saratani si ugonjwa mmoja, bali ni maradhi zaidi ya moja kwani athari zake huibuka na dalili tofauti kadiri zinavyovamia mfumo mmoja kwenda mwingine.

Zipo takribani aina 100 za saratani, huweza kupewa jina kutokana na mahali iliposhambulia mwilini na aina ya chembe hai zilizoathirika.

Mfano saratani zinazoanzia kwa jina la chembe hai za ngozi ziitwazo melanocytes, huitwa melanoma wakati zile za utumbo mpana (colon) huitwa saratani coloni

Aina za saratani huweza kuainishwa katika makundi mbalimbali kutegemeana na mahali na aina ya tishi iliyoathiri.

Zifuatazo ni saratani na aina yake.

Carcinoma - saratani hii huanzia katika ngozi au tishu zinazofunika viungo vya ndani.

Sarcoma, hii ni saratani inayoanzia kwenye mifupa migumu, mifupa plastiki, misuli, sehemu zenye mafuta mengi na kwenye mishipa ya damu.

Leukemia, saratani hii huanzia katika tishu zinazotengeneza chembe hai, mfano (bone marrow) ute wa njano uliopo katikati ya mifupa, husababisha kutengeneza chembe hai zenye saratani na huingia moja kwa moja katika mfumo wa damu.

Lymphoma na myeloma saratani hizi huanzia katika chembe hai za mfumo wa kinga.

Mfumo wa fahamu ubongo na uti wa mgongo; saratani zilizoanzia katika chembe hai za ubongo ziitwazo neuroni.

Saratani inavyotokea katika mwili

Saratani zote huanzia ndani ya chembe hai. Hizo ndiyo muhimili mkuu wa kazi za kimwili. Ili kuweza kujua saratani inavyotokea, ni vema kujua nini kinatokea kwa chembe hai ya kawaida yenye afya na kubadilika na kuwa chembe hai iliyoathirika yenye saratani.

Mwili umeundwa kwa chembe hai tofauti ambazo huhitajika ili kuuweka mwili kwenye afya njema.

Chembe hai za mwili hujidhibiti katika ukuaji kimaumbile na kujiongeza idadi au kujigawanya.

Wakati seli zinapozeeka au kupata madhara, hufariki au kuuwawa na askari mwili, hivyo nafasi yake huchukuliwa na chembe hai mpya.

Seli hizi hupitia katika mizunguko mikuu miwili, yaani Meosis na Mitosisi. Mzunguko wa mitosis, seli moja hujigawa na kuwa seli mbili.

Pale inapotokea mparaganyiko wa vitu vya ndani ya seli vilivyobeba taarifa za kiurithi na maelekezo ya kimwili za vinasaba (DNA), huweza kuvurugwa na kukosa ufanisi.

Hali hii huleta matatizo katika mzunguko na kusababisha mtiririko usio wa kawaida. Pia, huleta matokeo mabaya ya ukuaji na ugawanyikaji wa seli kiholela usio wakawaida.

Basi hali hii ikitokea, seli hushindwa kufa pale inapohitajika ife na pia seli mpya huzalishwa pasipo mwili kuzihitaji.

Seli hizi za ziada zenye saratani kwa pamoja, hujirundika katika tishu na kuvimba, ndio huitwa Saratani.

Bado hakuna uthibitisha wa moja kwa moja kujua sababu hasa ya kisayansi kutokea kwa saratani, lakini kuna vitu au tabia hatarishi na vihatarishi vinavyoambatana na saratani mbalimbali kama dawa aina ya Cytotoxic huambatana na kujitokeza kwa saratani ya damu maarufu leukemia.

Maambukizi ya kichocho huambatana na saratani ya kibofu cha mkojo, kirusi cha papiloma namba 16 na 18, saratani ya shingo ya uzazi na siku za karibuni inahusishwa pia na saratani ya koo na bomba la chakula.

Jenetiki au chembe za kiurithi, inahusishwa na kujitokeza na saratani ya matiti na kokwa za mayai ya uzazi hasa kwa wanawake na utumbo mpana.

Mienendo na mitindo yakimaisha ni moja ya tabia na vitu hatarishi katika nchi za magharibi ambako watu hupata saratani kama ya matiti na utumbo mpana, lakini chanzo chake bado hakijajulikana.

Pia utumiaji wa tumbaku umeonekana kuwa sababu kubwa inayochochea karibu saratani zote ingawa zaidi ni kwa ya mapafu, kibofu, kichwa na shingo.

Unywaji wa pombe kupita kiasi husababisha saratani ya koo, sumu ya aflatoxin na saratani ya ini.

Mazingira yakufanyia kazi ikiwamo maeneo yenye mabati aina ya asbestos, husababisha saratani ya mesotholioma, kemikali ya aniline dyes yenyewe inasababisha saratani ya kibofu na mionzi ya jua husababisha saratani ya ngozi.

Vyakula vya wanyama na vyakusindika kama vya makopo vyenye kemikali za kuzuia kuharibika, vyakula vilivyo ambatana na uchafu, virusi vya HIV, kuwa na uzito au mwili wenye mafuta mengi, kutofanya mazoezi, matumizi ya dawa za kulevya, mazingira ya mwili kutokua safi, ngono zembe, majeraha sugu au ya mara kwa mara mwilini pia husababisha saratani.

Kuwa na historia yakifamilia ya kuugua saratani kwa zaidi ya mwaka mmoja na pia baadhi ya vichochezi vya mwili mfano oestrogeni vimeonekana kuambatana na saratani ya matiti.

Pamoja na kutaja sababu na mambo hatarishi, haimanishi kua kila mtu anayefanya hayo atapata saratani, kupata au kutopata hutegemeana na ubora na uwezo wa mwili wa mtu mwenyewe kupambana na maradhi.

Friday, September 29, 2017

Tambua namna uso unavyoweza kuainisha ubora wa afya yako

 

By Dk Christopher Peterson, Mwananchi

Uchovu, maumivu ya viungo sambamba na ya mwili mzima au maumivu ya tumbo na kichwa, ni baadhi tu ya dalili ambazo wengi tumezizoea.

Na kwa kupitia maumivu hayo, ndipo tunaanza kutambua kuwa afya zetu haziko sawa na huenda kuna baadhi ya maradhi ynaashiria kutushambulia, hivyo ni lazima kuchukua hatua ya kupata matibabu haraka kabla hali haijawa mbaya.

Lakini kila tunapojiangalia kwenye vioo, nyuso zetu pia zinasema mengi kuhusu afya zetu.

Baadhi ya maradhi mengi yanayoweza kuleta madhara makubwa kiafya yanaweza kutambuliwa kwa dalili zinazojitekeza kwenye uso wa binadamu.

Kujiangalia kwenye kioo ni jambo la kawaida ambalo twatu hulifanya karibu kila siku.

Lakini mtu anapojiangalia kwa makini, wakati mwingine anaweza kuyaona mabadiliko madogo yanayojitokeza usoni.

Mabadiliko haya yanaweza kudhani niwa ni ya kawaida, lakini ukweli ni kwamba hayapaswi kufumbiwa macho kwa sababu yanaashiria matatizo fulani ya kiafya.

Kwa mfano rangi ya ngozi na jicho kubadilika na kuwa ya njano.

Hii ni homa ya manjano. Inatokea pale mtu anapokuwa na uchafu mwingi mwilini au takamwili.

Hali hii huwa ni ya kawaida na isiyokuwa na madhara kwa watoto wachanga wenye umri wa wiki 38 hadi 40 kwa sababu maini yao bado hayajakomaa kama yanavyotakiwa.

Lakini kwa watu wazima, homa ya manjano inaweza kuashiria matatizo makubwa zaidi ya kiafya kama ya maambukizi ya aina mbalimbali ya virusi vinavyoshambulia ini (hepatitis) na maradhi ya ini ua matatizo ya kongosho au madhara yatokanayo na utumiaji wa vilevi.

Chunusi sugu:

Mara chache unaweza kupata chunusi au vipele vyeusi usoni. Hivi mara nyingi vinaashiria aleji ya chakula au matumizi ya baadhi ya sabuni za kuogea na mchafuko wa damu na baada ya muda hutoweka.

Lakini ni vema kufanya vipimo inapotokea chunusi hizo zinakuwa sugu. Kwa kufanya hivyo, kutasaidia kutambua dalili za maradhi mengine mapema hasa ya saratani ya ngozi.

Vidonda vinavyojitokeza pembeni ya mdomo mara nyingi vinasababishwa na baridi au na maambukizi ya ugonjwa wa zinaa unaotokana na kufanya ngono kwa njia ya mdomo au tabia ya kunyonya via vya uzazi wakati wa tendo la ndoa.

Maambukizi yanayopatikana kupitia njia hii yanasababishwa na aina fulani ya virusi kitaalamu vinaitwa herpes viruses.

Unapopata maambukizi ya virusi hivyo, vinabaki kwako na baada ya muda vinatengeneza vidonda na malengelenge mdomoni.

Wakati mwingine pia ni kawaida kutokwa na vidonda vidogo nje ya mdomo baada ya maumivu makali ya kichwa, uchovu kupita kiasi, homa, sababu za kisaikolojia na hasa kuwa na wasiwasi, na kupigwa na jua kwa muda mrefu.

Vidonda vinavyotokana na sababu kama hizo hutoweka vyenyewe baada ya muda, lakini kama vinajitokeza mara kwa mara na vinadumu kwa muda mrefu,ni vema kumuona daktari ili kupata tiba.

Mipasuko mdomoni:

Kila mmoja anapitia hali hiyo ya lipsi za mdomo kukauka na kutoa mipasuko midogo midogo kwa kipindi tofauti.

Mara nyingi husababishwa na hali ya hewa na hasa ya baridi, au kushuka kwa mfumo wa kinga mwilini kwa kipindi husika.

Tatizo hilo mara nyingi hudumu kwa muda mfupi na kutoweka. Lakini pia ni vema kutumia vilainishi vya kupaka mdomoni ili kuzuia lisiendelee.

Vilainishi vinapatikana kwenye maduka ya dawa na hata kwenye maduka ya vipodozi.

Japo tatizo hili hutoweka baada ya muda, lakini ni vema mtu akawa makini linapotokea mara kwa mara.

Kubabuka ngozi ya uso

Wakati mwingine kubabuka kwa sehemu ndogo ya uso hakuwezi kuleta tatizo kiafya na mara nyingi hutoweka baada ya muda.

Lakini mtu anapaswa kuwa makini anapoona hali hiyo imeenea sehemu kubwa ya uso. Tatizo hilo huwa si lakawaida. Kitaalamu linaitwa butterfly rash. Linapotokea usoni, ngozi hubabuka na sehemu iliyoathirika hutengeneza muonekano wa kipepeo.

Mara zote hiyo huwa ni ishara yakushambuliwa na ugonjwa unaoitwa “lupus”.

Huo ni ugonjwa unaotokea wakati mfumo wa kinga za mwili, badala ya kuulinda mwili dhidi ya maradhi nyemelezi, unageuka na kushambulia tishu na ogani za mwili.

Pamoja kupata ishara hiyo usoni, ugonjwa huo pia huambatana na ishara zingine kama za homa kali, sehemu za maungio kuhisi kukauka na kukaza, uchovu uliokithiri na joto la mwili kupanda kuliko kawaida.

Ukibaini hali hiyo, muone daktari haraka.

Kuota nywele sehemu ambazo sio za kwaida

Hali hiyo mara nyingi huwatokea wanaume kadiri wanavyozidi kukua na hasa sehemu za kuzunguka masikio na sehemu zinazokaribiana na macho. Na wananwake wao huota ndevu .

Wanawake wenye chini ya miaka 30 wanaoota nywele sehemu za usoni na hasa kidevuni, inaweza ikawa ni ishara ya ugonjwa unaoshambulia ovari na kitaalamu unaitwa polycystic ovary syndrome.

Tatizo hilo linaweza kumfanya mwanamke apoteze uwezo wa kushika mimba na kuzaa.

Madoa ya rangi ya pinki usoni

Tatizo hili linaitwa melasma. Ugonjwa wa ngozi ya uso ambao unasababisha madoa yenye rangi ya pinki kwenye ngoi ya uso.

Mara nyingi unasababishwa na ujauzito, au matumizi ya baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango.

Kutokana na sababu za ujauzito au matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango, melasma hutoweka baada ya mtoto kuzaliwa au mwanamke kuacha kutumia vidonge vya kupangilia uzazi.

Lakini pia melasma inaweza kudumu kwa kipindi kinachozidi hadi mwaka.

Na ikitokea imedumu kwa kipindi kirefu ni vyema kumuona daktari, ili kuppata tiba na inatibika.

Mwandishi wa makala haya ni daktari anapatikana kwa namba ya simu 0658 060 788

Friday, September 29, 2017

Juisi ya stafeli hutibu mfumo wa fahamu

 

By Hadija Jumanne

Hivi ulishawahi kujiuliza matunda yapi yawe rafiki kwako na familia yako? Jibu usinipe ila bado hujachelewa naomba uanze sasa kwa kula Stafeli kwani ni tunda lenye faida nyingi mwilini kama yalivyomatunda mengine. Asilimia 12 ya tunda hilo lina sukari ya asili ambayo ni salama kwa mlaji na kwamba ni chanzo kikuu cha Vitamini C, madini ya chuma na Niacin Riboflavin.

Stafeli hustawi katika ukanda wa kitropiki na tunda hilo hufanana kidogo na tunda la topetope ambalo nalo lina kiasi kikubwa cha sukari ya asili.

Tunda hili hutibu matatizo ya mfumo wa fahamu, shinikizo la damu, msongo wa mawazo na saratani.

Utafiti uliowahi kufanyika unaonyesha juisi yake pia hutibu saratani kwa haraka, kwa sababu inanguvu mara 10,000 zaidi ya tiba ya mionzi katika kuzuia seli za saratani.

Hata hivyo, wagonjwa wa saratani wanapokuwa katika tiba ya hospitalini wanashauriwa kula tunda hilo kwa ajili ya kupunguza makali ya dawa za saratani anazotumia pamoja na maumivu.

Stafeli linakirutubisho aina ya Annona Muricata kinachoweza kukabiliana na maradhi ya saratani katika mwili wa binadamu.

Mbali ya kuwa ni chanzo kikubwa cha vitamini, tunda hilo hutibu maumivu ya nyama za mgongo, hurekebisha usawa wa kiasi cha damu na sukari mwilini na huongeza kinga ya mwili.

Faida nyingine hudhibiti ukuaji wa bakteria, virusi, vijidudu nyemelezi na hutibu majipu na uvimbe, huongeza stamina ya mwili na kurahisisha kupona haraka na hufukuza chawa.

Majani yake hutumika kama chai.

Majani hayo hutibu pia kuharisha damu, mafua na husaidia mfumo wa umeng’enyaji wa chakula.

yanatumika pia kutibu maumivu ya mishipa. Mtumiaji unatakiwa kuyasaga mpaka yalainike kisha yapashe jikoni na kupaka katika eneo la mshipa wenye maumivu.

(Hadija Jumanne)

Friday, September 29, 2017

Miongoni mwa sababu zinazowafanya wanawake kushindwa kubeba ujauzito

 

By Dk Christopher Peterson, Mwananchi

Siku chache zilizopita nilieleza kuhusu sababu kubwa zinazowafanya wanaume wengi kupoteza uwezo wa kutungisha mimba hata kama nguvu zao za jinsi zipo sawa.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa hivi sasa asilimia kubwa ya wanaume husumbuliwa na tatizo hilo bila wao kujijua.

Lakini kutokana na maswali mengi niliyoyapokea, nawapongeza wasomaji wetu kwa mapokeo ya somo lile lililosababisha niandike makala haya.

Ni ukweli usiopingika kuwa tatizo la kupoteza uwezo wa kuzaa linawaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake kuliko wanaume.

Wanawake wengi ndiyo waathirika wakubwa kuliko wanaume inapofikia suala zima la afya ya uzazi na matatizo yake kwa ujumla.

Dalili kubwa inayoonyesha mwanamke hana uwezo wa kuzaa inaanzia pale anapopoteza uwezo wa kushika mimba baada ya kujaribu kwa kipindi cha miezi 6 na kuendelea.

Kupata hedhi inayozidi siku 35 na kuendelea na kupata pia hedhi iliyo chini ya mzunguko (chini ya siku 21), kuyumba kwa tarehe za hedhi au kutopata hedhi kwa baadhi ya miezi, kuna tafsiri kwamba mwanamke anakosa urutubishwaji wa mayai yake.

Wanawake wengi wamejikuta wanaangukia kwenye matatizo haya kutokana na sababu mbalimbali ambazo wakati mwingine zinachangiwa na aina ya maisha wanayoishi au hata matatizo ya kurithi na kupatwa na aina nyingine ya magonjwa ambayo yanaenda kuathiri mfumo wa uzazi moja mkwa moja.

Sababu zinazowafanya kutoshika mimba

Sababu ya kwanza ni matatizo katika urutubishwaji wa mayai. Matatizo katika urubishwaji wa mayai yanajitokeza baada ya mayai yanayokua hayajakomaa kwenye ovari zake au ovari zenyewe zinashindwa kuachia mayai yaliyokomaa hadi tarehe ambazo mwanamke zinamruhusu kushika mimba. Kitaalamu, tatizo hili linaitwa premature ovarian failure.

Tatizo hili huwa linawapata wanawake wengi na ni vigumu kwao kushika mimba.

Dalili za tatizo

Zipo dalili zinazoashiria kuwa mwanamke ana tatizo hilo ambazo ni pamoja na kukosa baadhi ya mizunguko yake ya hedhi.

Nyingine ni pale anapokaribia kupata hedhi, hujisikia maumivu ya kawaida ya tumbo au maumivu ya kawaida au muwasho kwenye matiti na maumivu ya kiuno.

Sababu nyingine ni baadhi ya matatizo yanayojitokeza kwenye mfuko wa uzazi.

Hata hivyo, wataalamu wa magonjwa ya wanawake wanasema wakati mwingine tatizo la kutopata ujauzito husababishwa na mwanamke mwenyewe.

Kwani baadhi yao wana tabia ya kutoa mimba kiholela bila kujua kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasababishia matatizo kwenye mfumo wa uzazi.

Kwani wengi wao hutoa mimba bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Tatizo hilo linapaswa kufahamika kwa wanawake wenyewe kuwa utoaji wa mimba na hasa mara kwa mara bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya au madaktari husababisha kuacha baadhi ya mabaki ya uchafu wa mimba zilizoharibiwa kwenye mfuko wa uzazi bila wao kujua.

Hivyo, si ajabu kwa mwanamke huyu akashindwa kushika ujauzito hapo baadaye atakapoamua kuzaa, kutokana na mfuko wake wa uzazi kuvurugika.

Lakini pia baadhi ya matatizo mengine yanayojitokeza kwenye mfuko wa uzazi ni uwapo wa uvimbe ambao kitaalamu huitwa fibroids.

Na wakati mwingine nje ya ukuta wa mfuko wa uzazi kunaweza kujitokeza baadhi ya tishu zinazojijenga kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi.

Tishu hizo zikikua na kuongezeka zinaweza kumletea mwanamke tatizo la kushindwa kubeba ujauzito.

Tatizo hilo kwa jina la kitaalaamu linaitwa endometriosis na ni muhimu kupata ushauri wa daktari ili kuchunguza uwezekano wa kuwapo kwa tatizo hilo.

Endometriosis mara zote huambatana na dalili za maumivu makali wakati wa hedhi au wakatiwa tendo la ndoa au kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi ikiambatana na mabonge mazito na maumivu kwenye mfumo wa uzazi hadi kwenye kiuno.

Ni vema kuwaona watoa huduma za afya ukiona dalili hizi mara moja.

Tatizo lingine ni mabadiliko yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni.

Wanawake wengi wanasumbuliwa na tatizo hilo bila kujijua. Kuyumba kwa uwiano wa mfumo wa homoni mwilini ni tatizo lingine ambalo kwa asilimia kubwa pia huwakumba wanawake.

Kisayansi, imethibitika kuwa kuyumba kwa mfumo wa homoni ni moja ya matatizo makubwa yanayowafanya wanawake washindwe kushika mimba.

Mchakato mzima wa upevushwaji na urutubishwaji wa mayai kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke kisayansi, unaratibiwa na mfumo wa homoni.

Hivyo, kuyumba kwa mfumo huo huathiri moja kwa moja mchakato mzima wa utungishwaji mimba.

Ni vema kumuona daktari kwa ajili ya vipimo kama ikitokea mwanamke anashindwa kupata ujauzito ili kubaini kinachosababisha tatizo hilo.

Sababu nilizozieleza ni chache kati ya nyingi zinazosababisha matatizo haya. Ushauri wangu ni kujenga ukaribu na watoa huduma za afya kwa ajili ya msaada wa uchunguzi na matibabu.

Friday, September 22, 2017

Unavyoweza kukabiliana na hofu kabla ya kupima afya

Wakazi wa kisiwa cha Juma kilichopo wilayani

Wakazi wa kisiwa cha Juma kilichopo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kuchunguzwa afya zao na kupewa matibabu bure kisiwani hapo juzi, matibabu hayo yalitolewa na Shirika la Christian Life World Mission Frontiers la Nchini Korea. Picha na Maktaba 

By Colnely Joseph, Mwananchi

Tangu ugonjwa wa Ukimwi ulipogundulika, licha ya kusababisha vifo vya maelfu ya watu, umendelea kuibua hofu kwa watu na miongoni mwa vitu vinavyoogopwa sana kuhusu ugonjwa huo ni suala la kupima afya ilikubaini kama mtu anamaambukizi ama laa.

Licha ya kuwapo kwa elimu na jitihada kubwa za Serikali na mashirika mbalimbali kuhusiana na vita dhidi ya ugonjwa huo, bado kuna ukakasi mkubwa kwa mtu kufanya uamuzi wa kujitokeza kupima afya ili kujua usalama wao ukoje.

Kama kunasababu kubwa inayosababisha vita dhidi ya ugonjwa huo kuwa ngumu ni pamoja na suala la watu kutofanya uamuzi wa kupima afya zao ili taratibu nyingine za kiafya ziweze kufuata.

Lakini wataalamu wa saikolojia wanasema kadiri mtu anavyokuwa na uelewa wa jambo fulani kwa kina, ndivyo hofi nayo hutoweka.

Kwa maana hiyo, watu ambao wanahofu ya kupima afya zao au kukimbia majibu baada ya kupima virusi vya ukimwi, hawajaelewa vizuri umuhimu wa kupambana na ugonjwa huo kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.

Umuhimu wa kujua afya yako

Kuna faida lukuki za mtu kutambua afya yake kwani njia pekee ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kwa upande wa kuambukiza au kuambukizwa, ni mtu kujitambua yupo upande gani.

Kuzuia maambukizi mapya, kupima afya na kuchukua majibu yako, kunamuwezesha mtu kubadili mfumo wa maisha yake. Kwani akishatambua hauna maambukizi, kwa vyovyote atakua makini katika kujilinda aidha kwa kuwa mwangalifu sanjari nakupunguza mambo hatarishi.

Pia, itamsaidia kama anamaambukizi ya virusi amkinge mwenzake na yeye pia asipate maambukizi mapya yanyoweza kinga zake za mwili kushambuliwa kwa kasi zaidi.

Watu wanaamini kupima afya ilikujua upande waliopo ni jambo la kuogofya, lakini ukweli kukaa bila kujua afya yako ni jambo la kutisha zaidi kuliko kujitambua kuwa tayari una maambukizi.

Kwani mtu akishajitambua atachukua tahadhari kwa kuanza kuchukua hatua sahihi za kujitibu.

Wanasaikolojia wanaamini kuwa kujua tatizo ni njia sahihi ya kulitafutia ufumbuzi hata kama hakuna ufumbuzi wa kudumu kuhusu suala husika.

Baada ya kupima

Wanasaikolojia wanasema mtu akishapima afya yake na kujitambua, ni rahisi kushawishi hata wengine kufanua hivyo.

“Lakini wapo ambao huwa wepesi kwenda kupima lakini kwenye kupokea majibu ni shughuli.”

Japo inaweza kukuchukua muda kukubaliabna na hali hiyo kutokana na uasili wa binadamu hususan katika kupokea taarifa za kushtua, lakini ni jambo zuri kuhakikisha unaikabili hofu na kupata ukweli kuhusu afya yako.

Wasemavyo wataalamu wa afya Anaeleza Daktari Stanley Binagi wa hospitali ya Amana kuwa kupima afya hakumaanishi mtu huyo anaweza kufa leo. Pia anasema mtu kwenda kupima afya yake haimaanishi kuwa atakutwa na virusi vya Ukimwi la, la hasha.

Dk Binagi anasema kupima ni njia mwafaka ya kusaidia kujua mwenendo wa afya ya mtu kwa ujumla.

Anasema na hata wale wanakutwa na maambukizi ya virusi, inasaidia kujua viko katika hatua gani ili aanze kupatiwa matibabu.

“Kupima kunaweza kumsadia muathirika na watu wanaomzunguka hasa kama yuko katika uhusiano na mtu mwingine au kwenye ndo,” anafafanua daktari huyo.

Anasema watu wasiogope kujitokeza kupima afya zao kila mara kwani itamsaidia hata kubaini matatizo mengine ya kiafya kama anayo.

Lakini pia kwa wale ambao wanawapenzi, itawasaidia kuwakinga wapenzi wao kwani wataweza kutumia kinga.

“Hii ni kama ilivyo dozi, ili iweze kutibu ugonjwa lazima itumike kwa kiwango stahili. Sasa ukiwa na virusi vichache mwilini unaweza kuwapiga na kinga za mwili ukawa sawa.” anasema.

Hakuna sababu ya watu kuwa na hofu kuhusu kupima afya zao kwani mtu akishajitambua mapema, pia ni kinga kwake.

Kwasababu inamuwezesha kuishi miaka hata 30 na zaidi kwa kujua tu ukweli wa afya yake.

Anasema lazima muathirike atambue hakuna binadamu aliye na uhakika wa kuishi zaidi ya siku moja, kwani katika maisha kifo kipo kila mahali na wakati wowote kinaweza kikatokea. Hivyo kupima na kujua afya yako ni miongoni mwa mambo muhimu kwa mtu kuyaamua.

Dk Binagi anasema hakuna sehemu ilioandikwa mtu atakufa lini, bali ni Mungu pekee ndiye mwenye siri hiyo.

Hivyo, mtu anaweza kukumbwa na mauti kwa sababu mbalimbali, ikiwano kuugua shinikizo la damu, kisukari, moyo na maradhi mengine ambayo kama yangegubdulika mapema, huenda yangetibiwa na mtu akajiongezea siku za kuishi.

Binagi anaongeza kuwa kwa waathirika wa Ukimwi hawapaswi kuwa na hofu, kwani hali imebadilika.

Anasema mtu akishabainika kuwa anamaambukizi ya virusi, madaktari humuanzishia tiba mara oja, tofauti na awali, ilipokuwa inasubiriwa hadi kinga zake za mwili za mwili kushuka.

Anasema matibabu hayo yamewasaidia wengi kuendelea kuishi wakiwa na afya njema.

Asemavyo mwanasaikolojia

Mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Christom Solution, Charles Nduku anasema hofu ya kupima inasababishwa na ukosefu wa elimu juu ya kujikinga na madhara ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Anasema licha ya Serikali na wadau mbalimbali wa afya kuendelea kutoa elimu hiyo nchini, lakini inaonekana bado haijajitosheleza.

Nduku anasema kama elimu ingekuwa imetolkewa kwa kiwango kikubwa, watu wasingekuwa na hofu ya kupima afya zao.

“Hali hii inatukumbusha kuwa bado hatujafika lengo la kuwashawishi Watanzania watambue umuhimu wa kupima afya zao, tuongeze juhudi,” anasema Nduku.

Hata hivyo anasema; kuishinda hofu ya kupima na kujua afya yako, ni miongoni mwa mambo muhimu katika maisha japo kumekuwa na hofu kubwa kuhusu suala hilo.

Anasema Watanzania wakumbuke ni heri nusu shari kuliko shari kamili, waondoe hofu, wajitokeze kwa wingi kwenda kupima afya zao bila kusubiri shuruti.

Friday, September 22, 2017

Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Moyo wenye afya njema huweza kutoa mapigo yake katika mpangilio sawa ukiratibiwa na uwapo wa mpitisho wa nguvu wa msukumo wa umeme wa moyo.

Umeme huo wenye tabia ya kipekee, huweza kutolewa katika kiwango maalumu kinachowezesha misuli ya moyo kudunda na kutoa mapigo yenye mpangilio sawa na yenye ufanisi pasipo kudunda ovyo ovyo.

Mapigo ya moyo kwenda bila mpangilio na uwapo wa dosari ya upitishwaji wa umeme wa moyo, husababishwa na tatizo la uzalishaji au upitishawaji wa umeme huo.

Hata hivyo, kukua kwa maendeleo ya kisayansi katika fani ya tiba kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa wagonjwa wanaougua maradhi ya moyo, ikiwamo kasoro ya mapigo ya moyo ambayo kitabibu hujulikana Arryhthmia.

Maendeleo hayo ndiyo yamechangia kutengenezwa kwa mashine iitwayo Pacemaker inayopandikizwa mwilini kusaidia kuzalisha umeme wa moyo.

Uzalishaji wa umeme huo husaidia kurekebisha athari ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mtu maarufu ambaye amepachikwa mashine hiyo ya pacemaker kifuani kwa zaidi ya miaka 10 sasa, ni kocha aliyewahi kuifundisha klabu ya soka ya nchini Uingereza, Manchester United, Sir Alex Furgerson.

Mashine hii ndiyo inamfanya kuendelea kuishi bila kupata mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.

Mashine hii pia ndiyo mbadala wa kituo cha uzalishaji umeme wa moyo kwa ajili ya kuwezesha kuwapo kwa mapigo ya moyo yasiyo na hitilafu.

Umeme wa moyo

Moyo umeumbwa ukiwa na umeme wake wa asilia unaopita kwenye nyaya maalumu ambazo zimejitandaza kwenye misuli ya chemba za moyo.

Mfumo huu wa umeme ndiyo unauwezesha kudunda na kutoa mapigo yanayosukuma damu kwenda maeneo mbalimbali mwilini.

Chanzo cha Tatizo la mapigo ya moyo

Tatizo lolote katika mfumo wa umeme wa moyo na misuli ya chemba zake inayoletwa na maradhi mbalimbali ya moyo, huweza kuathiri udundaji wa mapigo yake.

Sababu kubwa ya kutokea tatizo hilo ni kuingiliwa na mfumo mzima wa usambazaji wa umeme wa moyo. Maradhi yanayoweza kusababisha hali hiyo kutokea ni pamoja na ya misuli ya moyo, mtu kuzaliwa akiwa na ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, homa, matumizi ya tumbaku, ulevi wa kupindukia, shambulizi la moyo au kama mtu alishafanyiwa upasuaji wa moyo.

Mambo mengine yanayoweza kuchangia ni utumiaji wa vinywaji vyenye caffein, matibabu ya dawa kama kwinini na za pumu aina ya Aminophiline na kutowiana kwa chumvichumvi na maji mwilini.

Vile vile, utumiaji wa dawa za kulevya na matatizo ya tezi inayozalisha homoni zinazochangia ukuaji wa mwili. Wakati mwingine chanzo cha tatizo kinaweza kisugundulike moja kwa moja. Tatizo la mapigo ya moyo linaweza pia kusababisha mapigo yake kuwa na kasi ya juu, au kuwa na kasi ndogo au kutolewa bila mpangilio.

Moyo una misuli inayofanya kazi ya kujikunja na kukunjuka ili kusukuma damu mwilini. Kila pigo moja la moyo huzalisha mtiririko wa haraka wa mapigo makuu mawili ya misuli ya chemba za moyo.

Kwa kawaida moyo una chemba nne, juu ziko mbili na chini mbili, chemba hizi, misuli yake ndiyo hutoa mapigo kwa ajili yakusukuma damu.

Pigo la kwanza la moyo hutokea kwenye chemba za juu, yaani Atria, wakatika pigo la pili kusukuma damu hutokea katika chemba za chini ziitwazo ventricles.

Chemba za juu hupokea damu inayoingia kwenye moyo na kuisukuma kwenda chemba za chini zinazopokea damu hiyo na kuisukuma kutoka ndani ya moyo kwenda kwenye mapafu na sehemu nyingine mwilini.

Kwa kawaida, mapigo ya moyo hudhibitiwa na nguvu ya msukumo wa umeme. Katika hali ya kawaida, nguvu ya msukumo wenye umeme hutolewa na kitu kilichopo kiasili kwenye moyo kiitwacho Sinus node, kilichopo upande wa kulia wa moyo kwenye chemba ya juu.

Sinus node ni sawa na mashine ya Pacemaker ambacho mwanadamu amekitengeneza kutatua tatizo la mfumo wa umeme wa moyo. Mawimbi yenye nguvu ya msukumo wa umeme huzalishwa kwa kila pigo la moyo katika Sinus node na mawimbi hayo ndiyo yanawezesha kutoa ishara kutokea kwa mkunjuko wa misuli ya moyo.

Baada ya mawimbi, msukumo wa kuwezesha kutoa mapigo katika chemba za juu, husafirishwa na huweza kufika na kutulia kwa muda mfupi katika kituo kingine cha moyo kiitwacho AV node, kilichopo sehemu ya juu ya ukuta unaotenganisha chemba mbili za chini.

Kutulia huko ndiko kunatoa nafasi kwa damu kumiminika kutoka chemba za juu kwenda chemba za chini.

Hivyo basi, mawimbi ya nguvu ya msukumo huweza kwenda chini kwenye chemba mbili za chini na kusababisha zao la mkunjuko wa misuli ya chemba za chini, hivyo msukumo wa pili hutokea na damu husukumwa kutoka kwenye vyumba hivyo.

Madhara gani yanaweza kutokea

Mapigo ya moyo yanapoenda kwa kasi isiyo ya kawaida, inaweza kusababisha damu kutosukumwa kwa ufanisi katika maeneo ya mwili mzima.

Hali hii inaweza kuchangia ogani na tishu za mwilini kukosa hewa ya oksijeni ikiwamo sehemu nyeti za mwili, misuli ya moyo na ubongo kukosa damu.

Hivyo kusababisha maeneo hayo kushindwa kufanya kazi. Madhara makubwa yanayoweza kujitokeza ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, shambulizi la moyo, kiharusi na kifo cha ghafla.

Halii hii inaweza kuleta dalili mbalimbali ikiwamo kizunguzungu, kukatika pumzi au kupumua kwa shida, kichwa kuuma na kuona nyota nyota, kuhisi mapigo ya moyo yako juu na kudunda vibaya, kifua kuuma na kupoteza fahamu.

Ingawa si mara zote wenye tatizo la mapigo ya moyo huwa na dalili za wazi, mara zingine hugundulika na matatizo haya pale anapokuwa katika uchunguzi wa kawaida.

Nini cha kufanya

Tatizo linapopata matibabu ya uhakika, mara chache linaweza kuhatarisha maisha. Hata madhara yake pamoja kuwa ni makali, lakini yanazuilika kwa matibabu.

Vipimo muhimu ambavyo hufanyika ni pamoja na cha ECG na ECHO ambavyo huweza kubaini matatizo mbalimbali ya moyo.

Matibabu hutegemeana na bainisho la aina ya mapigo ya moyo yasiyo yakawaida. Mgonjwa anaweza kutohitaji kutumia dawa au kutumia dawa za kurekebisha dosari ya mapigo yasiyo kuwa ya kawaida, njia ya upasuaji na kubadili mitindo na mienendo ya kimaisha.

Kwa upande wa matibabu ya hitilafu ya uzalishaji umeme, mashine ya pacemaker inaweza kupandikizwa kwa njia ya upasuaji chini ya ngozi maeneo ya kifuani au tumboni ili kusaidia kurekebisha hitilafu ya umeme katika moyo.

Mashine hii inatoa umeme mdogo usio na nguvu kubwa pale inapohisi umeme au mapigo ya moyo hayako sawa. Mashine hii hupendekezwa na madaktari wa moyo kuwekewa mtu mwenye tatizo la kutoa mapigo ya moyo yenye kasi ndogo, kwa kawaida kasi ya mapigo kwa mtu aliyetulia ni kati ya 60-100 kwa dakika.

Pia, inapendekezwa kutumika kwa mgonjwa mwenye kizuizi cha mpitisho wa umeme wa moyo, tatizo linalotokana na kuingiliwa utiririkaji wa umeme wakati unaposambaa au umeme kuwa mdogo. Kuna aina nyingine ya mashine inayopandikizwa kwa upasuaji ijulikanayo kama Implantable Cardioverter defibrillator(ICD) inayotumika kutatua aina ya mapigo yasiyoyakawaida na ni hatari.

Aina hiyo ya mapigo yasiyo yakawaida husababisha chemba za chini kutoa mapigo ya kasi. Mashine ya ICD huweza kubaini tatizo na kutoa shoti ya umeme katika misuli ya moyo ya chemba za chini na kusahihisha tatizo hilo na mapigo kurudi katika hali yake ya kawaida.

Matibabu mengine ili kurekebisha hitilifu ya mapigo ya moyo ni pamoja na Catheter Ablation inayotumika kutatua aina ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida kwenye chemba za juu.

Njia hii huwa na mrija ulio kama waya huingizwa kwenye mishipa ya damu ya miguuni na kufika katika moyo ambao hutoa mawimbi yenye nguvu ya umeme ili kurekebisha hitilafu ya mapigo ya moyo. Ili kuzuia matatizo haya, inashauriwa kuepuka mambo hatarishi yanayochangia kutokea kwa magonjwa ya moyo ikiwamo udhibiti wa uzito wa mwili, matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi na matumizi ya dawa za kulevya.

Zingatia kula vyakula visivyo na mafuta mabaya, kula zaidi mboga za majani, matunda na wanga isiyokobolewa na fanya mazoezi mara kwa mara. Inashauriwa kufanya uchunguzi wa afya ya moyo mara kwa mara angalau mara moja baada ya miezi sita ili kubaini matatizo mapema kabla ya kuleta madhara.

Friday, September 22, 2017

Hata mwanamke hupatwa na ngiriDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

By Dk Shita Samwel

Karibuni wasomaji wa kona hii, leo nizungumzia tatizo la kiafya la ngiri, kitabibu huitwa hernia.

Ngiri maana yake ni kuhama kwa sehemu ya utumbo ama nyamanyama zinazoshikamana na utumbo kutoka katika pango lake na kwenda kujipenyeza na kujihifadhi katika pango la sehemu nyingine mwilini kulikona tishu dhaifu.

Wasomaji wengi hunitumia maswali yanayoonyesha kuchanganya kati ya ngiri na busha.

Busha au kwa kiswahili fasahan ngirimaji, husababishwa na uwapo wa mrundikano wa maji kwenye mfuko wa korodani katika nafasi ya tabaka mbili zinazounda mfuko wa korodani.

Hii hutokana na kuzibwa kwa mfumo wa usafirishaji majimaji kwenye korodani na minyoo midogo ambayo huenezwa na mbu.

Zipo aina mbalimbali za ngiri zinazowapata wanadamu. Ipo ya mfereji wa ndani kwenye nyonga ambayo mara nyingi huwapata wanaume na kitabibu huitwa inguinal hernia.

Huwapata wanaume kutokana na nyama nyama za eneo hilo la mfereji wa nyonga kuwa na udhaifu wakiasili, hivyo kuruhusu tishu za tumboni kujipenyeza.

Aina hii ndiyo huwachanganya watu wakidhani ni busha. Hii ni kutokana na umbile lake baada ya sehemu ya utumbo kujipenyeza katika mfereji wa nyonga unaopitisha vitu vinavyoenda katika korodani.

Aina ya pili ya ngiri ni ile inayojitokeza pia kwenye nyonga, lakini inakuwa ipo nje ya mfereji wa nyonga, ngiri hii hujulikana kitabibu ni femoral hernia.

Aina hii huwapata zaidi wajawazito na wanawake wanene. Tishu za tumboni hujipenyeza kwenye uwazi unaopitisha mshipa mkubwa wa damu unaopeleka kwenye miguu.

Aina ya tatu ya ngiri hujulikana kama ngiri ya kitovu. Nayo hujitokeza eneo la kitovu kutokana na udhaifu wa tishu za kitovuni.

Aina ya nne ni ngiri inayojitokeza baada ya sehemu ya juu ya tishu ya mfuko wa kuhifadhia chakula kwenda kujipenyeza katika uwazi uliopo katika kifua, kitabibu inaitwa hiatus hernia.

Aina nyingine ni ile inayojitokeza baada ya kufanyiwa upasuaji maeneo ya tumboni na hujitokeza baada ya jeraha kupona. Sehemu ya utumbo huweza kuhama katika pango lake na kwenda kujipenyeza kwenye uwazi uliojitengeneza baada ya jeraha kuunga.

Aina hii kitabibu inaitwa Incisional hernia na hujitokeza pia baada ya upasuaji uzazi. Aina hii huwapata zaidi watu wanene na wenye umri mkubwa.

Lakini pia kuna aina nyingine ambazo hutokea kwa uchache mwilini ikiwamo ngiri inayotokea maeneo ya mgongoni.

Takribani vihatarishi vya kupata ngiri huwa ni vile vile, ila sababu kubwa ni kuwapo kwa sababu yoyote ile inayochangia kutokea kwa shinikizo kubwa tumboni na uwapo wa pango ambalo lina tishu dhaifu.

Kuongezeka kwa shinikizo kunachangia kusukuma tishu za tumboni kwenda katika pango jingine ambalo lina tishu dhaifu hivyo kuruhusu upenyaji wa tishu zingine.

Vile vile, uwapo wa dosari au kuzaliwa na maumbile yasiyotimilifu kwa watoto wakiume.

Baada ya kuzaliwa huwa na udhaifu wa tishu za maeneo ya mfereji wa nyonga na kusababisha augue maradhi hayo.

Zipo sababu mbalimbali zingine zinazochangia mtu kupata ngiri, usikose kusoma jarida hili la afya ili ujifunze kwa undani zaidi.

Friday, September 22, 2017

Siyo kila uvimbe kwenye mfuko wa uzazi ni sarataniDk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

By Dk Christopher Peterson

Ni dhahiri kuwa moja ya dalili ya saratani huambata na uvimbe kwenye sehemu husika ya mwili kulingana na aina yake. Dhana hii imezua hofu miongoni mwa wanawake wengi, hasa inapotokea baada ya vipimo kugundulika kuwa wana uvimbe kwenye mifuko yao ya uzazi.

Lakini wataalamu wa afya wanasema si kila uvimbe hutokana na ugonjwa wa saratani, bali mwingine husababishwa na mambo mengine, ila haupaswi kupuuzwa kwani huenda ukawa na madhara ya aina nyingine kwenye mfuko wa uzazi.

Kuna uvimbe unaoitwa kitaalamu uterine fibroids, huu hautokani na saratani na mara nyingi huota na kukua kwenye ukuta au tabaka lililopo kwenye mfuko wa uzazi.

Uvimbe huo hautofautiana kwa ukubwa wa maumbile na wakati mwingine ukicheleweshwa unaweza kukukua kwa ukubwa wa tikiti maji.

Pia, hautofautiana kwa idadi kati ya uliomuota mwanamke mmoja na mwingine, kwani mmoja unaweza ukaota zaidi ya mmoja kwenye mfuko wake wa uzazi, lakini mwanamke mwingine unaweza ukaota mmoja tu.

Mara nyingi uvimbe unaota mmoja, madhara pindi unapokuwa na kuonezeka, huukandamiza mfuko wa uzazi na kuulazimisha upanuke hadi kugusa kwenye viwambo vya mbavu, hapo ndipo matatizo mengine yanapoanza.

Wanawake wengi wanakuwa hupatwa na uvimbe huu, lakini hawatambui kama wanao kwa sababu mara nyingi hauonyeshi dalili hadi pale unapokuwa mkubwa kupita kiasi na kuanza kuleta matatizo kiafya.

Hivyo, wanawake wanawashauri kujenga utamaduni wa kupima mara kwa mara ili kuubaini kabla ya haujaleta madhara makubwa.

Kama nilivyoeleza hapo juu, uvimbe huu huchukua muda hadi kuanza kuonyesha dalili zake, lakini kama mtu ana utamaduni kupima mara kwa mara anaweza kubaini dalili zake ambazo ni pamoja na kupata hedhi iliyopitiliza. Hali hiyo inaweza kusababisha mtu kupata anemia, maumivu ya mgongo na kiuno, haja kubwa kwa shida, maumivu makali chini ya kitovu na hasa ikitokea uvimbe umeshakuwa mkubwa.

Pia anaweza akawa anaenda haja ndogo mara kwa mara kuliko kawaida na kujisikia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.

Ukiona dalili hizo, ni dhahiri una tatizo hilo na ni vema kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo na mpango wa matibabu.

Uvimbe unaoota kwenye mfuko wa uzazi japo hauwezi kusababisha saratani, lakini una madhara mengine makubwa kiafya.

Madhara hayo ni pamoja na matatizo wakati wa kujifungua, yanaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto kama mama alishika ujauzito wakati tayari ana huo uvimbe. Lakini, unaweza pia kusababisha kutobeba ujauzito au kutungwa nje mfuko wa uzazi na tatizo lingine kubwa, ni mimba kuharibika mara kwa mara.

Sababu kubwa zinazochangia tatizo hili ni matatizo yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni. kisayansi, kwenye mwili wa mwanamke kuna homoni (vichocheo) za estrogen na progesterone. Homoni hizi mbili zinafanya kazi ya kuchochea maendeleo ya ukuaji wa sehemu ya ndani ya mfuko wa uzazi kwenye kila mzunguko wa hedhi wa kila mwezi, kwa ajili ya maandalizi ya urutubishwaji wa mayai na utungishwaji wa mimba, sasa wakati mwingine huwa inatokea homoni hizo hujichochea zaidi ya kiwango hivyo kuanza kutengeneza uvimbe mdogo mdogo kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi.

Lakini pia tatizo hili linahusishwa na sababu za kurithi. Ni vema kwa mwanamke kuijua vizuri historia ya ukoo wake ili kutambua kama naye yupo kwenye hatari ya kurithi ugonjwa huo au la!

Kwa sababu mara nyingi mtu anaweza kuupata ugonjwa huo kupitia vinasaba vitokavyo kwa watangulizi wake wa ukoo. Sababu zingine zinazochangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo ni pamoja na kupata hedhi katika umri mdogo, matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, uzito wa mkubwa wa mwili, ukosefu wa vitamin D na ulevi pia.

Friday, September 15, 2017

Maajabu ya bangili ya shaba na tiba ya ndani kwa mwili wa binadamu

 

By Dk John Haule, Mwananchi

Binadamu ameumbwa kwa namna ya ajabu, anapopatwa na maradhi huhitaji tiba za aina nyingi ikiwamo ya maji (Hydrotherapy), ya kupakwa matope (Mudtherapy) na nyinginezo nyingi ikiwamo ya kuvaa bangili ya shaba (copper bracelet).

Bangili hii inamfanya binadamu kujitibu maradhi mengi. Lakini leo nitayadadavua maradhi matano.

Historia yake

Uvaaji wa bangili ya shaba uligunduliwa ni tiba kwa mvaaji toka enzi za kustaarabika kwa watu wa Misri ambao wanasadikika ndiyo waliosambaza ustaarabu huo duniani kote.

Kwa muda mrefu imani hiyo imeendelea kutumika duniani na mpaka sasa sayansi bado inakiri kuwa bangili hiyo ina tiba zisizoonekana zenye uwezo wa kuponya taratibu maumivu ya misuli na viungo kwa ujumla. Ukiacha hilo, bangili hiyo huimarisha kinga ya mwili na kuongeza kiasi cha nguvu za mwili wa mvaaji kimaajabu.

Kukakamaa na maumivu ya viungo

Sote tumewaona wanawake wa kimasai huvaa bangili hizo na ni aghalabu kuwakuta wakiugua maumivu ya viungo. Ni wanawake imara wanaomudu kuchunga makundi ya ng’ombe wakitembea kwa muda mrefu. Kwa taarifa, gari liitwalo Land Cruiser VX lilipewa jina la ‘Shangingi’ ikimaanishwa ni mwanamke wa kimasai yaani ‘Sangiki’ kutokana na uimara, umadhubuti na uzuri wa gari hilo.

Kinadharia, imebainika kuwa madini anayopata mvaaji wa bracelet hufyonzwa vizuri zaidi ya madini ayapatayo mtu anayemeza vidonge vya lishe kwa kuwa huenda moja kwa moja katika mfumo wa damu bila kupitia katika ini. Sote tumeshuhudia wavaaji wa copper bracelets ni wenye nguvu, afya njema, wasio na woga na hujiamini sana. Hii ndio nguvu isiyoonekana ya copper bracelet.

Kuimarisha afya ya mishipa na moyo

Binadamu anapopungukiwa na madini ya shaba na mazao yake huwa hatarini kuugua magonjwa yanaohusisha moyo na mishipa yitwao ‘Aortic aneurysms’ Sio siri, tafiti nyingi duniani zimeunyesha kuwa mtu akipungukiwa na madini ya shaba huvuruga mtiririko wa damu mwilini na hata kupandisha kiwango cha kolestro katika damu na kusababisha uharibifu kwenye moyo na njia za damu mwilini. Madini ya shaba mwilini hudhibiti na kuratibu fibers, collagen, na elastin hivyo kumlinda mtu na shambulizi dhidi ya Aortic aneurysms. Hapo utagundua kuwa kuvaa copper bracelet ni rahisi lakini kunaweza kukukinga na maradhi makubwa sana hasa kupooza ambayo ni magonjwa yanaotuua kwa kasi sana siku hizi. Ni aghalabu sana kumkuta mtu anayevaa copper bracelet kuugua maradhi ya moyo.

Kuimarisha mfumo wa kinga

Shaba ikivaliwa mwilini mwa binadamu hufyonzwa taratibu na kwa kiwango sahihi kabisa ambacho hungia katika mfumo wa damu, hivyo kumfanya mvaaji awe na uwiano sawa kati ya mwili na saikolojia yake. Hii hutokea kwa kuwa shaba huharakisha utoaji wa sumu na taka mwili na kuufanya mwili wa binadamu uzalishe ‘enzymes’ zinazotengeneza ‘Hemoglobin’ nyingi na kwa haraka inavyotakiwa. Hii ndio sababu ulipokutana na mtu aliyevaa copper bracelet ulimuona ni mwenye furaha na anayejiamini kwa lolote mbele yake. Jiulize, kwanini Ukihitaji kuunganishiwa umeme ni lazima ufunge nondo ya shaba na uichimbie ardhini ndipo utaunganishiwa huduma hiyo? Ni kwamba itasaidia kupambana na nguvu za umeme za ziada na kama ukikatika kila kitu cha umeme ndani ya nyumba kikiguswa huwa na shoti ya umeme.

Hupunguza uzee (Anti-aging)

Shaba ikivaliwa hutoa aina ya viuasumu viitwavyo ‘anti-oxidant properties’ ambavyo huzuia taka na sumu za mwili kuharibu seli za mwili na kuzilinda pia.

Kwa kudhibiti na kuratibu uzito wa collagen na elastic pamoja na fiber, shaba huweza kuzuia mwili wa mvaaji kuzeeka haraka na hivyo tumewashuhudia wavaaji wakionekana bado vijana wakati umri wao umeenda.

Hizi ni baadhi tu ya faida za kuvaa copper bracelet iwe kwa wanaume au hata wanawake.

Kwa kawaida huwezi kuona utendaji kazi wake kama miujiza ya kulala na kuamka ukakuta mabadiliko bali huchukua miezi miwili hadi mitatu mvaaji kugundua kuwa mwili wake umepata mabadiliko kiafya na toka hapo ataendelea kufaidi hasa kutougua mara kwa mara.

Upatikanaji:

Upatikanaji wa Copper Bracelets si mgumu na bei zake siyo ghali pia.

Wamasai hutembeza barabarani wakiziuza katika maeneo mengi ya mijini na hasa Jijini Dar es Salaam.

Ukiacha hao, unaweza ukaingia kwa sonara akakutengenezea na haitakuwa ghali kama dhahabu kwa kuwa madini ya shaba bei yake ni rahisi.

Ningependa kusikia toka kwenu wasomaji kutokana na sababu hizi tano tu tulizoziona leo hapa na kugundua kuwa vazi hili ni tiba, bado tu hatuna sababu ya kuidhinisha Copper Bracelet kuwa vazi letu la taifa? Tuonane wiki ijayo.

Dk John Haule (Dietition)

+255 768 215 956

Facebook/john.haule4

Friday, September 15, 2017

Hasira huchangia kupungua kwa kinga ya mwili ya binadamu

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi

Kinga  ya mwili huongezeka au kupungua kila siku kutegemeana na mtu amekula nini, amekunywa nini au hali ya ubongo wake ikoje kwa sababu kama mtu atakuwa na hasira siku nzima, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kupungua kinga yake ya mwili.

Watalaamu wa masuala ya lishe wanasema hakuna dawa au chakula cha kula siku moja cha kuponya tatizo la kushuka kwa kinga ya mwili, badala yake jamii inatakiwa kula mlo wenye mpangilio unaokubalika.

Wanabainisha kuwa njia nzuri ya kukabiliana na tatizo hilo ni kula matunda, mboga za majani, vyakula vya nafaka na maji ya kunywa ya kutosha.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa anasema kila chakula kina umuhimu na mchango wake katika kujenga na kuupa mwili nguvu.

Anasema  baadhi ya vyakula vinasaidia kupunguza kemikali zinazosababisha saratani.

“Saratani ni ukuaji wa chembechembe hai zinazokuwa bila mpangilio, hata hivyo mwili wetu  unaanza kujengwa na chembechembe hai moja na baadaye zinaunganika na kuwa nyingi na hatimaye kuwa chembechembe hai zinazotengeneza tishu zenye baadhi ya  viungo (organs),” anasema Dk Kahesa.

Anavitaja baadhi ya vyakula  vyenye uwezo wa kupambana na saratani  kuwa ni vyote vyenye vitamini na vina mchango mkubwa katika kuzuia saratani.

Anasema kuna baadhi ya vyakula vinajenga kinga ya mwili na kuna vingine vinachochea saratani kutokea kutokana na mazingira.

Wakati Dk Kahesa akisema hayo, Muuguzi kutoka Shirika la Watawa la Mabinti wa Maria Immakulata (DMI),  Farida Mathola anavitaja baadhi ya vyakula na matunda yanayopambana na kuzuia saratani kuwa ni maboga, karoti, viazi vitamu, pilipili nyekundu na zile za njano.

Vingine ni  Bilinganya, Binzari, Broccoli, Nyanya, majani ya ngano huku kitunguu saumu kikionyesha  uwezo wa kuondoa hatari ya kupatwa na saratani ya tumbo, koo na matiti kwa mtu anayetumia mara kwa mara.

Farida anasema  mboga za majani zenye rangi ya kijani zinauwezo mkubwa wa kupambana na Saratani huku Spinachi ikiwa inaongoza kwa sababu ina uwezo mkubwa wa kutoa kinga mwilini au kuondoa hatari ya kupatwa na saratani ya ini, kizazi, utumbo mpana na kibofu cha mkojo.

“Kutokana na hali hiyo, jamii inaweza kuziweka mboga hizi katika orodha ya vyakula vya kila siku, hasa ukizingatia umuhimu wake wa kupambana dhidi ya magonjwa ya kansa na kuwapo kwa kiwango kingi cha Vitamin E, ambayo nayo ni muhimu kwa kinga ya mwili,” anasema Farida.

Anafafanua kwa upande wa matunda , Stafeli, Barungi , Tufani, machungwa na Nanasi ni miongoni mwa yanayotajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na saratani huku nanasi likiwa na kimeng’enyo cha aina ya ‘bromelain’, ambacho ni muhimu  kwa kinga dhidi ya saratani ya matiti na mapafu na pia, lina vitamin C inayoongeza kinga mwilini.

Pia, Tufani (Apple) lina kirutubisho muhimu kiitwacho ‘quercetin’ kilichoonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kupunguza hatari ya mtu kupatwa na saratani ya mapafu na ina . Pia, uwezo wa kupunguza kasi ya kukua kwa seli za kansa ya kibofu. Muuguzi huyo anaelezea  kwa ufupi baadhi ya faida zilizopo kwenye vyakula na matunda yanayozuia Saratani kwa binadamu.

Kuwa moja ni pamoja na majani ya ngano, sharubati (juisi) ya majani ya ngano nayo husaidia kuimarisha protini kwenye seli nyekundu za damu na kuimarisha kinga ya mwili na mfumo wa kusaga chakula na kuondoa lehemu.

Pia, majani hayo huimarisha mfumo wa sukari mwilini na kutibu wenye matatizo ya kisukari. Huimarisha na kutibu matatizo ya ini, figo na kuondoa sumu mwilini.

Barungi lina wingi wa asidi ya citric, potassium na calcium na mtu anapokula tunda hilo usiku wakati wa kwenda kulala humfanya apate usingizi mzuri.

Lakini unywaji wa juisi ya tunda hilo asubuhi kabla ya kula chakula kingine, huondoa tatizo la kukosa haja kubwa na kuongeza hamu ya kula pamoja na kusaidia uyeyushaji wa chakula mwilini, lakini pia hupunguza homa itokanayo na mafua makali.

Barungi hutibu pia magonjwa ya kiharusi, hupunguza rehemu, unene, kukarabati mishipa ya damu na kuipa damu uwezo wa kutembea mwilini.

Binzari au manjano (Turmeric)

Licha ya watu wengi kutumia binzari kama kiungo, lakini kina faida nyingi mwilini ikiwamo ya kuzuia hatari ya kupata saratani.

Ulaji wa binzari mara kwa  mara huimarisha afya ya macho, viungo vya mwili na utendaji kazi wa ini. Lakini pia huimarisha chembe hai za mwili na mfumo wa uzalishaji mbegu za uzazi.

Tikitimaji chungu

Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa kwenye Jarida  la Utafiti wa Kansa, majimaji yanayotolewa katika tikitimaji chungu yanayojulikana kama ‘karela’ kwa kihindi, hupunguza kasi ya kukua kwa seli za sarataniya matiti.

 Utafiti huo ulioongozwa na mtafiti  Ratna Ray, unaeleza  tikitimaji chungu lina uwezo wa kuzuia saratani ya matiti, lakini bado haijathibitika kama majani yake yanauwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Kitunguu Saumu

Licha ya kutibu magonjwa zaidi ya 30, kitunguu swaumu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini kikielezewa kuwa na faida katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria, matatizo kwenye mapafu, mfumo wa umeng’enyaji chakula na matatizo ya kuishiwa nguvu.

Ulaji wa mara kwa mara wa kiungo hicho huondoa sumu mwilini, husafisha tumbo, huyeyusha mafuta mwilini, husafisha njia ya mkojo na hutibu UTI na kuondoa amoeba, minyoo na bakteri wengine.

Lakini pia kiungo hicho kina uwezo wa kuongeza nguvu za kiume na hutibu matatizo ya kukosa nguvu za kiume.

Brokoli (Broccoli)

Miongoni mwa faida iliyopo katika mboga hiyo ni kuzuia mwili kupatwa na saratani. Kwa sababu ina glucoraphanin ambayo hubadilishwa mwilini na kuwa sulforaphane inayozuia saratani.

Pia, broccoli husaidia mfumo mzima wa neva na ubongo kufanya kazi inavyotakiwa, huipatia misuli nguvu, lakini pia  huimarisha msukumo wa damu na hupunguza sumu mwilini kwa kusafisha uchafu

Bilinganya

Ni aina ya mboga inayopatikana katika kundi la mbogamboga, lakini pia inaweza kutengenezwa juisi ambayo husaidia kutoa taka mwili kwa njia ya haja ndogo.

Virutubisho vilivyopo katika mboga hiyo husaidia kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo na kiharusi na ngozi ya bilinganya inaambatana na miseto iitwayo terpenes inayosaidia kupunguza lehemu mwilini.

Stafeli

Asilimia 12 ya tunda hilo lina sukari ya asili na ni salama kwa mlaji na ni chanzo kikuu cha vitamini C, madini ya chuma na Niacin  Riboflavin huku likiwa na kirutubisho aina ya Annona Muricata chenye uwezo wa  kukabiliana na maradhi ya saratani. Tunda hilo huzuia matatizo ya mfumo wa fahamu, shinikizo la damu, msongo wa mawazo, hudhibiti ukuaji wa bakteria, virusi, vijidudu nyemelezi, hutibu majipu na uvimbe, huongeza stamina ya mwili na kurahisisha kupona haraka, hufukuza chawa na kuzuia magonjwa yasaratani.

Utafiti  uliowahi kufanyika, unaonyesha juisi ya stafeli hutibu saratani kwa haraka kwa sababu inanguvu mara 10,000 zaidi ya tiba ya mionzi katika kuzia seli za saratani.

Nyanya:

Moja kati ya faida ya nyanya katika mwili wa binadamu ni kulinda uharibifu wa DNA kutokana na wingi wa antioxidants, vitamin  C na A ambazo kwa pamoja hufanya kazi ya kulinda DNA isishambuliwe, lakini nyanya hiyo husaidia kukinga mwili dhidi ya ugonjwa wa kisukari.

Nyanya huzuia saratani ya tumbo, mapafu, koo na saratani ya kizazi, lakini ulaji wa nyanya kwa wingi huzuia saratani  ya tezi dume na hupunguza kiwango cha sukari mwenye damu, husaidia kusafisha ngozi, husaidia macho kuona vizuri hasa nyakati za usiku. 

Nini kifanyike

Luitfrid Nnally ni mtaalamu wa Masuala ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini ( TFNC), anasema ili kukabiliana na tatizo la saratani, ni lazima kuwapo na maandalizi bora ya chakula kabla ya kupikwa ili virutubisho vilivyopo visiweze kupotea.

Dk Kahesa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya Saratani anasisitiza ili jamii iweze kukabiliana na saratani na magonja menginie, inatakiwa kula vyakula hai na halisi badala ya vilivyosindikwa. “Kuna baadhi ya watu wanaondoa virutubisho bila kujua, mfano unatenegeza juisi ya embe halafu unaongeza radha, unakuwa umeweka kemikali na unaua baadhi ya virutubisho hai vilivvyokuwapo kwenye tunda lako,” anasema Dk Kahesa.

Idadi ya wagonjwa wa saratani wanaogunduliwa nchini

Mtaalamu wa Kliniki ya Saratani  kutoka ORCI, Khamza Maunda anasema wagonjwa 50,000 hugundulika kuwa na saratani kila mwaka huku taasisi hiyo ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 5,000 sawa na asilimia 10 ya idadi ya kitaifa.

Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini, Profesa Ayoub Magimba anasema katika miongo miwili iliyopita, magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo saratani yamekuwa kwa kasi na kutishia  afya za Watanzania.

Profesa Magimba anasema juhudi za haraka zinapaswa kuchukuliwa  na Serikali ili kukabiliana na  hali hiyo kwa sababu  watu wengi wapo hatarini kupata magonjwa hayo kwa kukosa uelewa wa namna ya kukabiliana na magonjwa  hayo.

Friday, September 15, 2017

PIRAMIDI YA AFYA: Wasiotahiriwa wako hatariniDk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

By Dk Shita Samwel

Hivi karibuni tuliona umuhimu wa tohara kwa wanaume, leo nitazumgumzia saratani ya sehemu za siri za mwanaume.

Pale tishu za sehemu hizo  zinapovamiwa na seli zenye saratani zinazoweza kukua bila mpangilio, ndipo hujitokeza.

Muathirika humchukua miaka miwili kupoteza maisha kama hatua za tiba hazitachukuliwa.

Maambukizi ya virusi vya Papilloma kwa mwanaume asiyetahiriwa humweka zaidi kwenye hatari ya kupata saratani hiyo.

Saratani ya sehemu za siri ya mwanaume huwatokea mara chache ukilinganisha na saratani ya tezi dume inayoongoza kuwapata wanaume wengi na huwasababishia vifo.

Wanaume wenye umri mkubwa wasio wasafi wa mwili ndiyo wanapatwa zaidi na saratani hii.

Saratani yoyote inapompata mwanadamu na ikapiga hatua za mbeleni huwezi kuwa na madhara makubwa ikiwamo kusambaa katika maeneo mbalimbali mwilini na kusababisha vifo.

Vihatarishi vya kupata saratani hiyo ni pamoja na kutofanyiwa tohara, maambukizi ya virusi vya papiloma ambayo huwapata zaidi wasiotahiriwa, kujamiana bila kinga na kuwa na wapenzi wengi.

Mambo mengine ni pamoja na utumiaji wa tumbaku, watu wenye zaidi ya miaka 60, kuwa na tatizo la kuzaliwa na ngozi ya mbele (govi) kushindwa kurudi nyuma (kufeduka), kitabibu hujulikana phimosis, kutokuwa msafi wa mwili na kuugua magonjwa ya zinaa.

Haimaanishi kuwa mwanaume akiwa na vihatarishi hivyo ndiyo lazima apate saratani hiyo, na pia, haimaanishi kuwa asiye na vihatarishi hivyo hawezi kuugua saratani hiyo.

Dalili na viashiria ni pamoja na kuwashwa au kukereketwa eneo la uume, tishu eneo la uume kuwa jekundu, kuwa na uvimbe, uwapo wa kakidonda katika uume, kutoa uchafu kama majimaji na kuvuja damu katika eneo lenye kidonda.

Pale saratani inaposambaa maeneo jirani ikiwamo kiunoni na eneo la njia ya haja kubwa na yale ya mbali kama ini na mapafu, dalili itategemea na mahali ilipovamia.

Dalili za baadaye katika hatua za mwishoni za ugonjwa huo ni pamoja na uzito wa mwili kupungua, kukonda sana, kupungukiwa na damu, kuchanganyikiwa na kupata sonona (depression).

Matibabu ya saratani hiyo hutegemea na hatua iliyofikia. Hivyo, hapa ndipo hatua ya kunyofoa sampuli ya tishu kwa ajili ya uchunguzi wakimaabara ili kujua hatua ya saratani ilipofikia.

Inapobainika iko katika hatua za awali, huweza kutibika kwa upasuaji kwa kuondoa sehemu ya ngozi au sehemu ya uume.

Katika hatua za mbeleni yaani hatua ya tatu kuendelea, matibabu huwa ni kwa tiba ya mionzi na dawa za kemikalitiba.

Endapo itabainika imeisha sambaa maeneo mbalimbali mwilini na ni vigumu kutibika, mgonjwa hupewa matibabu maalumu kwa ajili ya kumpunguzia maumivu, kumwongezea damu na lishe maalumu. Hapo ndipo mgonjwa hupatiwa pia ushauri maalumu kwa ajili ya kumwezesha kukubaliana na hali hiyo. Ndugu pia hupatiwa elimu ya namna ya kuishi na mgonjwa wao kwa lengo la kumsaidia na kumpatia faraja.

Nihitimishe kwa kuwashauri wale wote ambao hawajafanyiwa tohara, kufika katika huduma za afya kwa ajili ya kufanyiwa tohara.

Wajitokeze pia katika kliniki maalumu za madaktari wanaotembelea mikoani ambao huwafanyiwa tohara bure. Hakikisha unaepuka vihatarishi nilivyoorodhesha hapo juu.

Fika katika huduma za afya mapema pale unapoona dalili.

0763-296752

Friday, September 8, 2017

Hedhi mzigo mzito kwa wanafunzi wengi wa kike

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bahi,

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bahi, Srella Suleiman akizungumza na wanafunzi wa kike wanaoishi hoteli.​ 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Saa 5.30 asubuhi, niko ofisini kwa Mwalimu Grace Mbega. Huyu ni mwalimu wa afya wa Shule ya Msingi Chifuduka, wilayani Bahi katika Mkoa wa Dodoma.

Mara anaingia mwanafunzi wa kike. Baada ya kutuamkia anasema: “Mwalimu naomba kile kitu, naumwa.” Mwalimu Grace akacheka na kumuuliza kwani hujui kutengeneza za kienyeji?

Yule mwanafunzi alisema anajua isipokuwa amesahau na hata kama angekumbuka namna ya kutengeneza, asingeichukua kwani hakujua kama angekuwa katika hali hiyo kwa siku hiyo.

Baadaye nilikuja kubaini kwamba binti huyo mdogo alikuwa akiomba taulo ya kike (pedi) baada ya kuingia ghafla katika mzunguko wake wa hedhi akiwa tayari amefika shuleni.

Mwalimu Grace alifungua droo yake, akachukua kitambaa kigumu, mkasi, pamba na uzi. Huku akimuelekeza, alianza  kutengeneza taulo ya kike ya asili kwa kukata kitambaa kwa mtindo wa duara. “Ukishakata kitambaa chako, unaanza kukifuma vizuri pembeni,” alisema Grace huku akifuma kitambaa hicho na wakati huo akimuelekeza mwanafunzi huyo aliyekuwa amesimama pembeni yake.

Alitengeneza vishikio viwili alichukua pamba na gozi, kisha akapachika pamba iliyowekwa kwenye gozi vizuri. Baada ya hapo alimuelekeza namna ya kuitumia na kumkabidhi.

Msichana huyo aliondoka ofisini kwa mwalimu wake huku akifurahi. “Nilishawafundisha, nikaa nao kiurafiki, wale walio kwenye umri wa kupevuka na waliopevuka wanaelewa namna ya kutengeneza,” anasema mwalimu huyo.

Hata hivyo, Mwalimu Grace anasema huwa anawasaidia taulo za dharura tu, na kwamba, mabinti wengi hutumia zaidi vitambaa kwa sababu hawamudu gharama za kununua pedi. “Hata hizi za asili tunazotengeneza hapa shuleni zinagharama japo ni kidogo,” anasema.

Hedhi ni kati ya vikwazo vinavyowafanya wanafunzi wengi wa kike kukatisha masomo yao hasa wale wanaosoma maeneo ya vijijini.

Taasisi ya Uangalizi wa Haki za Binadamu ya Human Rights Watch (HRW) katika ripoti yake ya mwaka huu kuhusu hali ya utoaji wa elimu ya sekondari nchini, inasema mazingira ya shule nyingi si rafiki kwa mwanafunzi wa kike hasa akiwa katika hedhi.

Ripoti hiyo inasema usimamizi mzuri wa usafi wa hedhi unahitaji maji ya kutosha, mazingira safi na faragha ili kuruhusu wasichana kubadili au kutupa kwa ustaarabu taulo au pedi wakiwa shuleni.

Utafiti uliofanywa na Shirila la Maendeleo la Uholanzi la SNV katika wilaya nane nchini, unabainisha asilimia 98 ya shule za wilaya hizo hazina miundombinu rafiki kwa wasichana wanapokuwa kwenye hedhi.

Mwalimu wa afya wa shule ya Sekondari ya Magaga, Wende Mbuna anasema kwenye shule hiyo wanafunzi wengi wa kike huwa hawagusi shule wakati wanapokuwa hedhi.

“Pedi za ziada zipo lakini anapewa moja tu, akija kuomba akati inapomtokea dharura. Umaskini ni tatizo kubwa hivyo, vifaa duni vya kujisitiri huwafanya waamua kukaa nyumbani,”anasema Mbuna.

Ilibainika kuwa wanafunzi wengi hawamudu gharama za taulo za kike ambazo ni kati ya Sh2,500 hadi 3,500 kwa paketi moja.

“Natumia vitambaa na huwa nahofia kama nikibaki darasani naweza kuchafuka kwa kupata madoa kwenye sketi yangu ya shule halafu nichekwe, ndio maana naona bora nibaki nyumbani,” anasema mmoja wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Chonama.

Msichana huyo (jina linahifadhiwa) huwa anatumia kati ya siku nne hadi tano kila mwezi kwa hedhi na anasema katika siku hizo huwa haendi shule.

Anasema hajawahi kubahatika kutumia taulo ya kike (pedi) ya dukani tangu alipopevuka miaka miwili iliyopita.

Msichana mwingine wa  darasa la saba katika shule ya msingi Chifuduka anasema pia hajawahi kutumia taulo za dukani na kwamba mama yake amekuwa akisema hawezi kumnunulia kwasababu hana fedha.

“Natamani sana kutumia za dukani kwa sababu nitakuwa na uhakika wa kutochafuka nikiwa darasani. Hizi za vitambaa inabidi ubadilishe kila mara, na kwa kubadilishia hakuna labda chooni nako kuna harufu kali,”anasema.

Anasema kukuwa hakuna mitihani darasani kwao, kipindi cha hedhi huwa haendi shule. “Huwa nakaa kimya simwambiagi mama wala baba. Huwa nasema kichwa kinauma basi nabaki nyumbani,”anasema msichana mwingine.

Mganga mfawidhi wa Hospitali Teule wa Hospitali ya Kigoma Ujiji, Dk Kilawa Shindo alisema zipo athari nyingi za watoto wa kike au wanawake kutumia vitambaa wakati wa hedhi.

Dk Kilawa anasema mwanamke anayetumia vifaa hivyo ni rahisi kupata maambukizi  kwenye kizazi ‘Pelvic Inflamatory Desease)  na  kwenye njia ya mkojo  endapo kitambaa hicho kitakuwa na vimelea vya wadudu kama bacteria na fungus.

“Pia mavitambaa ni rahisi kuloa hali inayoweka eneo la ukwe kuwa na unyevu na kuhatarisha mwanamke kupata fungus kisha kuwashwa sehemu zake za siri,” anasema.

Anasema kuwa inashauriwa ikiwa mwanamke atatumia vitambaa badala ya pedi ni sharti kifuliwe kwa maji safi, kikauke na kupigwa pasi ili kuua vimelea vyote vinavyoweza kuzalisha wadudu.

Kuhusu maumivu makali ya tumbo, Dk Kilawa anasema kitaalamu inaitwa Dysmenorrhea, hali hii inatokana na misuli ya ukuta wa uzazi kujiminya wakati wa kuuvunja ukuta uliokuwa umeandaliwa kupokea kijusi endapo mwanamke angekutana na mwanaume.

Afisa Afya wa tarafa ya Bahi Sokoni, Mudila Mundeli anasema yapo yapo magonjwa yanayoweza kuwapata watoto wa kike kutokana na matumizi ya vifaa vya hedhi vizivyo salama.

“Magonjwa yanawakumba sana kwa sababu maji na vifaa wanavyotumia wengi sio salama hii ni hatari pia,” anasema.

Anasema hata wakitoa elimu kwa watoto na wazazi wao, ugumu unabaki kwenye hali ya uchumi kwa kuwa wengi hawamudu gharama.

“Ndio maana tunasisitiza kila shule iwe na kitengo cha afya kwa sababu hiki kinasaidia walau wanafunzi hasa wa kike kupata elimu inayowahusu,”anasema.

Ni suala la kawaida

March 8 mwaka jana Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya hedhi ili kuelimisha jamii kwamba jambo hilo ni la kawaida katika mfumo wa maisha ya jinsia ya kike, na hutokea kila baada ya siku 28.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifuduka, Daniel Mchomvu anasema hedhi sio siri tena shuleni kwake. “Hata hiyo mtoto mdogo muulize kuhusu hedhi anajua. Tumeamua kuwafundisha ukweli wajitambue tangu wadogo. Wasione ajabu,” anasema na kuongeza:

“Tulimteua mwalimu wa kike, kazi yake kubwa ni kukaa na mabinti hapa shuleni ili  waliopevuka awasaidie elimu ya afya na wanapokuwa hedhi waone ni kawaida, wasiache masomo”.

Kwa upande wake Mwalimu Grace anasema katika jitihada za kutoa elimu kwa jamii, waliitisha kikao cha wazazi ili wajadili suala la hedhi kwa watoto wao na namna wanavyoweza kuwasaidia, wahudhurie masomo.

“Baba au mama yeyote anaweza kuzungumza na mwanae wa kike, hedhi sio siri tena,”anasema.

Mzazi, Jeremia Matonya anasema hajawahi kujua siku za hedhi za binti yake. Hata hivyo anakiri kuwa kila mwezi kuna siku binti yake huwa huwa haendi shule.

“Naanzaje kumuuliza eti upo mwezini? Hiyo ni kazi ya mama yake. Akilala ndani najua anauma,”anasema Matonya akiona ajabu kwa namna anavyoelimishwa kwamba, hedhi ni kitu cha kawaida.

Anasema hajawahi kutoa fedha yoyote kwa ajili ya kumnunulia taulo binti yake, japo ni mwaka wa pili tangu apevuke.

Mwalimu Grace analazimika kutumia muda mrefu, kuwalekeza namna ya kuwajali mabinti zao japo ukweli unabaki palepale, gharama za kumudu.

Ofisa elimu wa Sekondari Wialaya ya Bahi, Hassan Mohamed anasema walimu wakiume na wakike kwenye wilaya hiyo wameshafundishwa namna ya kuwasaidia wasichana wanapokuwa hedhi.

Mtandao wa maji na mfumo wa majitaka nchini (TAWASANET) katika mapendekezo yake yaliyotokana na utafiti wake kuhusu miudombinu katika shule kwa ajili ya manbinti wakati wa hedhi, unapendekeza kutungwa kwa sera zitakazolazimisha ujenzi wa shule kuzingatia mahitaji hayo.

Kadhalika Tawasanet wanapendekeza kuwapo kwa mfumo rasmi wa masuala ya hedhi kuzungumzwa kwa uwazi katika utoaji wa elimu, ili kuvinja ukimya ambao umekuwa sababu ya ‘mateso’ kwa wanafunzi wa kike.

Ofisa elimu wa Sekondari Wilaya ya Bahi, Hassan Mohamed anasema walimu wakiume na wakike kwenye wilaya hiyo wameshafundishwa namna ya kuwasaidia wasichana wanapokuwa hedhi ikiwa ni hatua ya kwanza ya utekelezaji.

Hata hivyo, wakati wa maashimisho ya Tamasha la Jinsia, halmashauri za Wilaya ya Kishapu na Kisarawe zilipata tuzo baada ya kuweza kutenga bajeti na kuanza kutoa bure pedi kwa wasichana wote waliopevuka shuleni.

Friday, September 8, 2017

Kati ya watoto 1500 wanaozaliwa mmoja ana tatizo la kijinsia

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Unapokutana na pasi ya kusafiria ya raia kutoka nchi kama Australia kwa asiyefahamu anaweza kustaajabu kwani zimeachwa sehemu tatu za kujaza jinsi ya msafiri. Na hii ipo wazi, kwasababu mtu anatakiwa ajaze kama yeye jinsi yake ni kike,  kiume au ya kike na kiume.

Hilo siyo jambo la kushangaza, kwani sehemu ya kujaza jinsi kama mtu anazo zote ya kike na kiume iliongezwa baada ya nchi hiyo kubaini matatizo ya kiafya yanayoweza kumpata binadamu.

Kama tulivyoshuhudia mpambano wa kupatikana katiba mpya ambayo ndiyo itakua ikiongoza maisha ya Watanzania, vivyo hivyo hata mwili wa mwanadamu huwa na katiba yake na inapovurugwa au kubadilishwa kiholela, huwa na matokeo mabaya.

Katiba ya mwili wa binadamu imo ndani ya vinasaba, kitabibu ni Genes.

Chembe hizo ndizo hubeba taarifa za kiurithi za binadamu zenye maelekezo ya shughuli zote pamoja na maumbile yake yatakavyokuwa.

Wataalamu wanasema kuvurugika kwa taarifa hizo, husababisha matatizo ya kimwili ambayo binadamu anapozaliwa hujikuta akiwa na maumbile tofauti na ilivyo kawaida kama mtu kuzaliwa akiwa na jinsi mbili.

Inaelezwa kuwa uwapo wa jinsi mbili mwilini na huku zikikaribiana kiutendaji kwa muathirika, ni mojaya matokeo ya kuvurugika kwa chembe za urithi.

Unawezaje kumtambua mtu mwenye jinsi mbili

Machoni unaweza ukamtambua mtu kwa mwonekano wa kiume, lakini akawa mwilini mwake ana chembe za urithi za kiume. Vivyo kwa kwa upande wa mwanamke.

Katika jamii matatizo kama hayo hupokelewa tofauti kutokana na watu kutokuwa na uelewa wa tatizo.

Hali hiyo huwafanya waathirika kutokuwa wawazi na uhofia hata kwenda katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata ushauri nasaha wa kitabia au hata kupata matibabu mengine.

Taarifa za jumla za tatizo hilo

Tatizo la mtu kuwa na jinsi mbili au zisizo za kawaida kwa lugha ya kitabibu hujulikana kwa jina la intersex.

Kitabibu maana yake nikuzaliwa na upungufu kwenye maeneo ya viungo vya uzazi na mfumo mzima sehemu za ndani, yaani kwenye kokwa ya kike au yakiume na sehemu za nje yaani kwenye uke, uume na sehemu zingine za siri.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kwa kila watoto 1,500 hadi 2,000 wanaozaliwa, mmoja huwa na tatizo hilo lakimaumbile ambalo huonekana kwa macho.

Moja ya changamoto kubwa ambayo waaathirika hawa hukumbana nayo ni uhusiano wa kimapenzi, kijamii na binafsi.

Watu hawa hukumbana na hali ya kuwa na aibu na wengine hutengwa na kunyanyapaliwa.

Jambo kama hili huwafanya waathirike kisaikologia na kujitenga na jamii.

Nini kinatokea mwilini na kusababisha tatizo hili?

Kwa kawaida, mwanadamu huwa na mgawanyiko wa chembe hai za urithi nusu toka kwa mzazi wa kike na nusu kutoka kwa mzazi wakiume, pale yai la kike na kiume yakikutana hupatikana mtoto aliye na chembe za urithi toka kwa wazazi wake.

Taarifa hizi hubebwa na chembe zilizo kama utepe na umbile kama la herefu X na huwa na kifundo katikati.

Chembe hizi kitabibu huitwa chromosome ndizo zinabeba taarifa za urithi kwa kila kitu mwilini kuanzia urefu wa mtoto anayezaliwa hadi rangi ya macho anayotakiwa kuwa nayo.

Chembe hizi huwa na protini maalum na molekyuli moja ya DNA (vinasaba) ambavyo vimo ndani ya seli ambayo hubeba taarifa nyeti.

Hiyo sasa ndiyo huwa kama katiba yenye maelekezo yote yanayotakiwa kufanywa na mwili.

Kuanzia wanadamu, wanyama na mimea, chembe za urithi za chromosomes zipo katika mtindo wa jozi.

Zipo jozi 22 ambazo huitwa autosom na nyingine ni jozi ya ziada ambayo inahusika na mustakabali wa jinsi ya mwanadamu itakavyokuwa, ambayo kitabibu huitwa sex chromosome.

Hii ndiyo inafanya jumla yake kuwa  jozi 23 au kwa maana nyingine, ni seli huwa na chromosomes 46 jumla.

Sex chromosomes ndizo  zinazohusika kutoa mustakabali wa jinsi ya mtu katika maumbile ya nje na ya ndani, chembe za aina hii huwa na chembe ya chromosome X na Y.

Inapotokea muunganiko wa jozi ya XX huyo ni mwanamke na jozi XY ni mwanamume, sehemu ya nje ya jinsi huwa na sehemu za siri za nje na sehemu za ndani huwa ni korodani na kokwa ya kike kitaalam ovary.

Sehemu za ndani ndiyo tezi zinazozalisha vichochezi vya kike kwa mwanamke na kwa mwanaume ni mbegu za kiume na kichochezi cha kiume.

Vichochezi hivi ndivyo hutoa tabia za kijinsia za kike na kiume na humsababisha mtu aonekane mke au mme.

Mbegu ya kiume na yai lakike baada ya mizunguko ya seli huwa na malighafi za urithi nusu ambazo ndiyo chromosomes, yaani hujigawa kutoka chembe 46 nakuwa nusu yake ambayo ni 23.

Mimba inapotungishwa ndipo nusu ya chembe za chromosome 23 huunganika na kutengenezwa kiumbe ambacho huwa na chembe 23 toka kwa baba na 23 toka kwa mama.

Lakini panapotekea upungufu kwenye chembe za urithi kitaalamu huitwa gene mutation.

Katika chembe hizo za urithi ndipo mabadiliko ya kimaumbile yanapotokea ya nje na ya ndani.

Wapo watu wenye muonekana wa mwanamke, ambao huwa na korodani na uume, lakini na wana chromosomes XY ndani ya mwili ambayo humthibitsha kuwa ni jinsi ya kiume.

kazi ya korodani kutengeneza homoni itwayo testosterone.

Homoni hii ndiyo inakazi ya kumfanya mtu awe na tabia za kiume pamoja na maumbile yake.

Homoni hii huwa na kazi yakumfanya mwanaume kipindi anabalehe kuwa na sauti nzito, misuli mikakamavu na mikubwa, utawanyikaji wa nywele kama vile ndevu.

Lakini miili ya wanawake huwa inashindwa kuipokea homoni hiyo ili iweze kufanya kazi yake, tatizo hilo kitabibu huitwa Androgen Insensitivity syndrome.

Watu wenye tatizo hilo hungeliweza kuwajua kwakuwa wanapozaliwa huwa na sehemu zakike katika seheme zao za siri.

Na hata wazazi na wahudumu wa afya hupewa taarifa kuwa umejifungua mtoto wa kike na cheti cha kuzaliwa pia hujazwa mtoto wa jinsi yake ni ya kike.

Lakini kadiri mtoto huyo anavyozidi kukua, dalili za uwapo wa jinsi mbili huonekana.

Miaka ya nyuma wataalamu wa upasuaji walikua wakifanya marekebisho na kuangalia jinsi ipi iko imara walikuwa wakiiacha na kuiondoa ile dhaifu.

Lakini kumbe ilikua ni makosa kwani wale waliopasuliwa walipofikia umri wa utu uzima, walijikuta wameondolewa jinsi ya kiume, lakini ana muonekano wa kike ukubwani.

Na walipopimwa walikutwa na chembe zao za urithi ni XY yaani mwanaume. Mwingine katiba ya mwili wake ni ya kike, yaani ana chembe XX, hivyo anakuwa na maumbile ya kiume na jinsi yake ni yakiume.

Ushahidi wa kiuchunguzi wa kutumia uchambuzi wa kina wa chembe hai ndiyo unatoa uthibitisho kuwa mwanadamu huyo ni mwenye katiba ya chembe za urithi za kike au za kiume.

Kwa wenzetu walioendelea wamekuwa na watu wenye tatizo hili, hivyo wakaamua kuwajali kwakuwapa uhuru wakuamua baada ya kupatiwa ushauri.

Taarifa iliyotolewa Juni 14 na Shirika la Habari la CNN, ilisema kuna ushuhuda wa baadhi ya waaathirika wa tatizo hilo walioanzisha umoja wao na walitoa ushahidi wa wazi kuwa unapomtazama usoni, hufanana kwa kila kitu na mwanaume. Shuhuda mmoja alisema alianzisha uhusiano na mwanaumke, lakini ilikua ikimnyima raha kwakuwa alikua na muonekana wa kiume ila ana jinsi ya kike.

Vivyo hivyo kwa mwanadada……ambaye alikua na uhusiano ambao haulufikia katika mapenzi.

Anasema kila alipofikiria jambo hilo, ilimuwia ugumu kwa sababu ya maumbile yake.

Uanishwaji wa tatizo la muingiliano wa jinsi

Kuna aina 4 za muingiliano wa jinsi yaani 46xy, 46xx, muingiliano jinsi wenye kokwa moja au zote mbili na muingiliano jinsi wakutatanisha.

Sehemu ya pili ya makala haya itaeleza aina hizo zilivyo na kama tatizo hili linatatulika.