Saturday, December 16, 2017

Kazi kwenu Basata, TCRA, Bodi ya filamu kupambana na mavazi ya ovyoJulie Kulangwa

Julie Kulangwa 

By Julie Kulangwa

Ni kazi ngumu kumweleza msanii kuwa video yake haifai kuonyeshwa kwa kuwa ina maudhui yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania. Kila mmoja anajitetea kuwa hayo yamepitwa na wakati kwamba ili video au sinema ipendeze ni lazima iwe na wanawake wanaonyesha asilimia 95 ya miili yao.

Nakumbuka miezi miwili iliyopita nilihudhuria uzinduzi wa filamu moja pale Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Ilikuwa filamu nzuri iliyojaa ucheshi kiasi cha kuufanya ukumbi ule kuzizima kwa vicheko vya kila namna.

Lakini ghafla ni kama kila aliyekuwapo alipigwa ganzi baada ya kuonekana vipande vya wasanii wakiwa chumbani. Miguno ya kimahaba na vitendo katika filamu ile vilimfanya kila aliyekuwamo ndani ya ukumbi ule ajikute kashikwa na ganzi fulani hivi.

Bahati nzuri nilikaa karibu na mwigizaji wa kipande hicho, nilipomtazama naye nilimwona hana raha kama watazamaji wengine. Alishikwa na fadhaa. Hakika hakikuwa kipande kinachovutia kutazama. Sijui labda kingefaa kutazama ukiwa peke yako.

Kipande hicho ni sehemu tu ya uwakilishi wa filamu zetu na video za muziki. Sijawahi kuelewa ni kwa nini wasanii wanarekodi vipande hivyo vya mambo ya chumbani. Unapoona watu wazima wawili wanaingia chumbani, wakafunga mlango au labda kuzima taa, inatosha kujua kitakachoendelea.

Nakumbuka zamani tukitazama filamu za nje hasa Marekani na Ulaya lazima mkubwa wetu akae na rimoti tayari kusogeza mbele filamu pale kinapofika kipande cha watu wazima. Siyo utamaduni wetu, siyo mambo yetu na haifai kujilazimisha. Yanafadhaisha.

Ukija kwenye nyimbo za wasanii ndio utachoka. Asilimia kubwa ya video zinazoonyeshwa sasa zinahusisha wanawake wakitikisa makalio au kuonyesha asilimia 95 ya maungo yao. Kinachofunikwa ni sehemu tu ya mwili.

Rais John Magufuli amelizungumzia kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri wa burudani. Asingejua kama asingekuwa anawafuatilia wasanii wetu.

Huko mitandaoni ndio usiseme kwani wanawake wanashindana kukaa uchi na kuonyeshana neema walizojaaliwa. Wasanii wajiongeze tu wakaze buti ili wafike mbali na siyo kulazimisha kufanya udhalilishaji wa wanawake.

Wanawake nao wasikubali kutumika ovyo. Video wanazozirekodi sasa zinakwenda kukaa kwenye kumbukumbu za dunia hii. Je, miaka kumi ijayo watatamani kuwa walivyo leo?

Kazi kwenu Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na Bodi ya Filamu kushughulika na watu hawa.     

Saturday, December 16, 2017

Nchama The Best : Kutoka Mwanza mpaka Dar

 

By Jonathan Musa, Mwananchi jmusa@mwananchi.co.tz

       Nchama The Best, si jina geni haswa kwa wale wapenzi wa muziki wa Hip Hop. Jina lake halisi Nchama Anthony (23).

Amezaliwa jijini Mwanza katika Mtaa wa Bugarika. Ni mtaa ambao una sifa za kipekee, baadhi ya sifa zake ni upikaji wa Pombe haramu.

“Mimi ni mtoto wa pili kati ya sita kwenye familia ya Mzee Anthony Rocket. Kati yao, ni mimi tu ambaye imebarikiwa au mwenye kipaji cha sanaa ya uimbaji,” anasema.

Anasema kama wasanii wengine, amaepata taabu sana kabla ya kufika hapo alipo. Amefanya nyimbo nyingi tu ambazo hazikuweza kupata nafasi au kupendwa.

“Nimekuwa kwenye hii gemu miaka mingi. Ni bidii na kipaji changu ndiyo vigezo ambavyo vimeniweka hadi sasa hivi,” anasema Nchama.

Baadhi ya nyimbo zake ni pamoja na Kwa Ajili Yako, Soja, Nastrago na Waiter Leta.

Ilikuaje hadi ukaanza kuimba?

Anaeleza kwamba yeye amelelewa katika familia ya kipato cha chini na siku zote katika kile ambacho alikusudia kukifanya amekuwa akikifanya kwa bidii akikumbuka hali halisi ya maisha ya pale nyumbani.

Bugarika ni mtaa wa aina nyingi za maisha na hivyo mtu asipokuwa makini ni rahisi sana kujikuta angle nyingine kinyume na matarajio.

“Niliamua kuingilia fani hii, kwanza kama kipaji change lakini pia kutafuta riziki. Na namshukuru Mungu hali yangu ya maisha inaendelea kuimarika japo kwa mwendo wa wastani,” anaeleza Nchama.

Nchama kama vijana wengi wa Bugarika, aliwahi kuathirika na pombe kali maarufu kama ‘gongo’. Pombe hii ilimsababishia madhara kiafya maana kila alipoitumia, aliugua hususan tumbo.

“Kuna baadhi ya vitu mtu anajikuta amejiingiza pasipo hata yeye mwenyewe kujua. Nilikuwa mnywaji wa gongo kwa siku nyingi tu lakini namshukuru Mungu aliniepusha na hali hiyo na kwa sasa nipo shwari nakomaa,” anasema.

Alifanikiwa kuacha

Nchama The Best anasema kwamba licha ya kuwa na marafiki wengi wa kitaa ambao ni walevi na watumiaji wa dawa za kulevya, moyoni alitambua kwamba alikuwa na jukumu la kulitekeleza maishani… muziki.

“Haikuwa rahisi kuwakwepa ‘wanangu’ marafiki na kuanza kufanya mambo yangu kwa ajili ya manufaa yangu na jamii inayonizunguka,” Nchama.

Mwaka 2012 aliamua kutupia ndoano yake ili kuona kama angeambulia hata kidagaa tu.

“Sigara ya SM, waliandaa mashindano maalum ambayo waliyaita ‘Str8t Free Style Competion’, nilibahatika kuwa mshindi wa pili. Wlikuwa wameahidi kwamba mshindi wa kwanza na wa pili wangeweza kupata ufadhili wa kurekodi nyimbo kadhaa Dar Es Salaam ingawa haikuwezekana,” anabainisha.

Kampuni hiyo hiyo ilirejea mwaka uliofuata (2013), na kuandaa mashindano kama kawaida na kutoa ahadi zile zile. Awamu hiyo, Nchama The Best alifanikiwa kuibuka mshindi.

Mwaka 2016, Nchama The Best, aliweza kubahatika tena katika shindano la Super Nyota ambalo liliandaliwa na Clouds Media.

Ni hapa ambapo aliweza kudhihirisha uwezo wake wa kuchana na hivyo kuwa mmoja kati ya wasanii wa Mwanza waliokubalika kuwa sehemu ya burudani kwenye mzunguko wa Fiesta kwa udhamini wa Tigo.

“Hapa nilibahatika kwa mara ya kwanza kushiriki shoo ya watu wengi ambao iliofahamika kama Tigo Fiesta chini ya Clouds Media. Nilijiskia fahari sana na tangu hapo nilianza kuwa na ule ujasiri wa kupiga shoo kwa watu wengi,” Nchama.

Mwaka huu 2017, Nchama The Best pamoja na wasanii wachahche kutoka Mwanza, alibahatika kushiriki katika tamasha la Tigo Fiesta ambayo ilianzia mkoani Arusha na kufikia kikomo jijini Dar es salaam, siku chache zilizopita.

Anasema akiachilia mbali zile Ngoma zake za zamani, Nchama The Best kwa sasa anatamba na muziki wake ambao unapikwa na watu mbali mbali ambao ni wataalam wa siku nyingi katika kuhakikisha kwamba anakuwa sehemu nzuri.

Baadhi ya Ngoma zake kali ni pamoja na Tufanye Kesho ambayo amemshirikisha Dully Sykes, Kwa Muda na Wanangu.

Kwake yeye, kukacha utumiaji wa hgongo, ni mafanikio. Hakupelekwa ‘sober house’ kama wasanii wengine ila aliwahi kujitambua kwa kuzingatia mazingira ya nyumbani kwao, Bugarika.

“Kwa wale ambao waliwahi kuathirika na dawa za kulevya ikiwemo pombe, wanaelewa nnachoizungumzia. Kuacha tabia hizi ni kibarua kigumu sana, leo utaacha kesho utarudia. Lakini mimi niliamua na kusimama imara,” Nchama

Anasema licha ya kwamba hajafahamika kiviile, ni imani yake kwamba atatendelea kufanya vizuri ili muziki umlipe kama wenzake wakongwe wanavyofanya.

“Bidii na ari ya kutaka kufika mbali ndiyo silaha tu ya kufanya vizuri baada ya kujikita katika nidhamu,” anasema.     

Saturday, December 16, 2017

Wanamuziki wa kike vaeni nguo zenye staha

 

By Salim Said Salim

 Fikiria umekaa nyumbani kwako nyakati za jioni ukiangalia televisheni ukiwa na familia yako. Tena wanafamilia hao wamo mzazi wako au wa mke wako na shemeji yako. Baada ya sekunde chache tu kuifungua runinga watoto wako nao wanasogea karibu kuangalia.

Kipindi kilichokuwa kinarushwa hewani ni cha muziki uwe taarabu au dansi. Baaada ya kuona hivyo unaamua ujiliwaze kwa kujiburudisha kwa dakika chache huku ukingojea kuangalia taarifa ya habari ili kuelewa kilichotokea hapa nchini na kwengineko duniani.

Mara unaona kinaonyeshwa kikundi cha wasichana ambao wapo robo tatu uchi, wanacheza muziki na kukata viuno kama vile ni watu ambao hawana akili.

Kwa bahati mbaya, hiyo runninga yako haina kitufe (remote control) cha kuingoza ukiwa mbali kidogo na kwa hivyo inakubidi uondoke kwenye kiti chako haraka kwenda kuizima au kubadili kituo. Hali inakuwaje hapo?

Nimewahi kupata simulizi ya kuchekesha, lakini inayosikitisha juu ya mzee mmoja alikuwa anatoka kuoga akiwa amefunga taulo kiunoni. Alipotupa jicho ukumbuni akitaka kuingia chumbani kwake aliona wajukuu zake wa wakiangalia wanenguaji wakiwa nusu uchi.

Huyu mzee, masikini alishituka na kuchanganyikiwa. Badala ya kuzima alivua taulo yake na kufunika kioo cha runinga na watoto kujikuta wanangalia maumbile ya babu yao. Masikini huyu mzee ….alitaka kuwalinda wajukuu zake na uchafu uiokuwepo kwenye rununinga na kumbe amefanya mabaya zaidi.

Hii ndio aina ya hali ambayo Rais John Magufuli hivi karibuni ameizungumzia kwa masikitiko makubwa na kuzungumzia kuporomoka kwa maadili ya Watanzania kunakoongezeka kwa kasi na kuonekanekana kukolezwa na baadhi ya wasanii wetu.

Dk Magufuli, kama walivyo Watanzania wengi, alihoji kama hali kama hiyo inakwenda sambamba na malezi, makuuzi na utamaduni wa Watanzania?

Jawabu lake haina haja ya kulisaka wala kulitafuta. Mwenendo huu haukubaliki katika maadili yetu ambayo hayataki hata mama na baba kupigana busu la mahaba hadharani kama wafanyavyo wazungu.

Mila, desturi na taratibu zetu za maisha zinaweka wazi mambo gani mtu anaweza kuyafanya hadharani na yepi sio mazuri kuyatenda mbele za watu, hasa watoto wadogo au wazee wako ambao unatarajiwa kuwaonyesha heshima na unyenyekevu.

Kwa kweli alichokieleza Rais kwa sauti ya masikitiko ndio kilio kikubwa kinachosikika sana siku hizi miongoni mwa Watanzania wengi ambao mwishowe hubaki kujiuliza: Taifa hili linaelekewa wapi?

Ukweli ni kwamba hali ilivyo siku hizi ni ya kusikitisha na kuisha na kama vile tumekuwa na jamii isiojuwa ilipotoka, haina heshima na maadili.

Haya hatuyaoni mitaani na makazini na zaidi miongoni mwa kizazi kipya, bali pia katika baadhi ya maneneo yanayotumika kwa burdani ya muziki, uwe wa taarab au dansi.

Fikiria inakuwaje katika jamii ya watu wanaojiita wastaarabu, waungwana na wenye kujiheshimu na wenye maadili kuwa na nyimbo zenye matusi na maneno machafu yanayotamkwa wazi wazi.

Kwa mfano, inakuwaje hata uwe na beti katika nyimbo isemayo tunacheza mechi bila ya jezi au panakuwepo maonyesho ya msichana anakata viuno ambavyo hata paka anapokuwa anafanya hivyo, hujificha juu ya dari ya nyumba au kwenye kichochoro na sio mbele ya watu.

Hapa tujiulize nani unawezakumwita mnyama, paka anayefanya mambo hayo kwa siri au binaadamu anayekata viuono hadharani?

Wakati umefika kwa Wtanzania kuitafakari hali waliokuwa nayo na kuifanyia marekebisho ya haraka ili kuiusu jamii ya hivi sasa na vizazi vijavyo.

Ipo haja ya kuwa na sheria zinazoeleweka na utaratibu mzuri wa kulinda heshima na maadili yetu. Vituo vyetu vya runinga vinapaswa kuacha kushabikia mwendo huu kwa kuonyesha muziki ambao wanenguaji wake wapo nusu au robo tatu uchi.

Nani kasema muziki haunogi mpaka mcheza dansi awe yupo nusu uchi au anafanya vitendo kuashiria kama vile tupo katika zoezi la kujamiiana?

Kwa upande mwengine, taasisi zinazosimamia masuala haya zinapaswa kupiga marufuku nyinbo au mitindo ya michezo ambayo inakiuka maadili ili kulinda heshima katika jamii.

Katika jamii nyingi masuala kama haya huwa na maeneo maalumu na wale wanaoshabikia huenda huko kuyafuata, sio mambo haya kuwafuata watu hata majumbani mwao wakiwa na familia zao, wakiwamo watoto.

Ni vizuri kila nyimbo ikapitiwa na kuangaliwa kama maneno yanayotumika sio ya matusi au hayatowi tafsiri chafu ambayo inakirihisha na masikio ya muungwana hayapendi kuyasikia.

Utaratibu huu pia utumike katika matangazo ya biashara kwa sababu baadhi ya matangazo badala ya kutangaza biashara yanahubiri lugha mbaya ambayo maeneno yake yanaposikika katika jamii watu hushindwa kuangaliana usoni.

Hivi karibuni, jamii imesikika ikilalamikia tangazo moja la kampuni ya simu za mkoni na watu wengi wamelieleza tangazo hilo kama ni matusi ya wazi kwa sababu maneno yaliotumika si ya kistaarabu,

Wasanii wetu wanaapswa wajipime na kujirekebisha na kuelewa vizuri mila, tamaduni na maadili ya Watanzania na kuhakikisha kwamba burudani wanayotoa inafurahisha na sio kukirihisha.

Kwa upande mwengie, siku hizi kumezuka mtindo wa kuonekana wasichana wanaotumika kufanya matangazo ya biashara kuzunguka mitaani katika magari yenye kupiga muziki kwa kelele na kukata viuno.

Wakati mwengine magari haya hufanya maonyesho yao yenye sura chafu katika maeneo yaliojaa watu warika tafauti kama vile karibu na shule, maofisi. masoko na hata pembezoni mwa nyumba za ibada.

Wakati mwengine huo muziki na ngoma ambazo wachezaji wake wapo nusu uchi hufanyika nyakati waumini wakiwa katika ibada kuomba maghfira kwa Mola wao.

Tusikubali kuigeuza jamii yetu kama vile ni nyumba ya ukahaba au danguro, tujaribu kwa uwezo wetu wote kurejea katika ustaarabu, uungwana, mila na desturi tulizorithi kizazi baada ya kizazi kutoka kwa wazazi wetu waliotutangulia.

Jamii hutakiwa kujivunia mambo mazuri na sio watu kwenda uchi au mambo yanayoshabikia ufuska na ukahaba.

Tujirekebishe haraka kabla ya kuja kujuta na kujiuliza kwa nini tuliamua kuweka kando ustaarabu, malezi, mila na utamaduni mzuri tuliorithishwa na wazazi wetu waiotutangulia.

Ni wajibu wa kila mmoja, awe kiongozi, mwandishi wa habari au msanii wakati wote kuhakikisha anachukua hatua muwafaka nyumbani kwake, mitaani na popote pale alipo kuendeleza mila, utamaduni na maadili mazuri na yenye kuvutia na kutunza heshia ya Mtanzania katika jamii yetu.

Tuseme basi na kuamua yaliopita si ndwele tugange yajayo. Tutafanikiwa kama tutafanya maamuzi ya hekima na busara.

Mungu ibariki na ilinde Tanzania na watu wake.     

Saturday, December 16, 2017

Dar es Salaam sasa ni Darinstagram

 

By Dk Levy

        Huku kwetu Uswahilini kila ukigonga mlango wa chumba cha mabinti. Utasikia subiri kwanza. Sijui huwa wanafanya nini wakiwa peke yako? Any way tuishie tu ‘kuimejini’ kila mtu kwa hisia zako.

Dunia ya Tanzania ya sasa. Kila kitu kiko Instagram. Ndo sehemu pekee inayohifadhi wapumbavu. Malaya. Matapeli na kila aina ya binadamu wenye ushetani ndani yake.

Ukiondoka Instagran huku mitaani nako kuna mambo yake. Tazama hili. Na hii ni kwa wadada. Ambao wamekuwa sehemu ya mtafaruku wa mishipa ya shingo na nyuso za wanaume huko mitaani.

Hii tabia inakera na inafurahisha kwa watu wenye mapepo ya ngono zembe. Kuvaa hayo madera yenu mitaani. Na kisha kuyashikilia na kuyanyanyua juu mpaka ngozi nyeupe inaonekana.

Mnawapa tabu na wakati mgumu sana baba na kaka zenu mitaani.Yaani ukimkuta mwanamke wa Temeke amevaa dera. Anachofanya ndo kile kile anachofanya wa Ilala. Kinondoni. Rufiji na kama siyo Kakola Geita huko.

Halafu kuna ile staili ya kulibana kwenye nguo ya ndani. Ni nini hasa mnatafuta? Hii tabia ipo kwenye maeneo ya wazi kama sokoni. Kwenye vituo vya mabasi. Madukani na mitaani. Unakuta mwanamama na msambwanda wake kavaa dera na kulibana ndani kwa ndani kwenye nguo ya ndani.

Hata kama mwanaume haoni anaishia kuhisi tu na kujikuta anapata mihemko. Wadada wenyewe wanatazama tu. Hawajui au makusudi kwamba hawaoni kama kikwazo kwa kaka na baba za jamani? Mkoje lakini na madera yenu hayo?

Hii tabu yote mnayopata kwa nini msiyakate ili yasiwape tabu namna hiyo. Kama kweli mnayabana na kuyashikilia kwa sababu ya kuburuza chini? Bora anayenyanyua kwa mbele basi. Kuliko yule anayechomekea ndani ya nguo ya ndani aisee. Mshindwe na mlegee. Sijui mkoje.

Lakini hiyo ndo raha yake kwa wakware na wapuuzi wa tabia za kipuuzi. Utasikia “Raha ya dera shurti linyanyuliwe kidogo mbele. Tukate ili liwe gauni? Hiyo ndo raha ya dera... likitosha sio dera tena kanzu hiyo.”

Hayo ndo majibu yao hawa wanaizaya waliokosa haya huku mitaani aiseee. Ningekuwa rais wa nchi hii ningeruhusu dera kuwa vazi rasmi la ofisini. Aidha kudumisha mila desturi na utaifa.

Pia kulinda wapuuzi wanaozurula tu mitaani badala ya kutulia maofisini. Maana uvaaji wa madera kwa dada na mama zetu siku hizi ni sehemu ya kivutio cha utalii wa ndani kwa kweli.

Tuachane na hayo. Tuangalie tatizo lingine ambalo ndo kubwa zaidi.

Mastaa wetu hasa wa kike wamekuwa na kautaratibu flani hivi, ambako neno sahihi kukatamka ni kautaratibu kakipuuzi, kipumbavu, hovyo kabisa.

Wakiwa kwenye uhusiano au kwenye ndoa kabisa, wana kawaida ya ‘shoo ofu’ mitandaoni. Kana kwamba wao ndo wa kwanza kuolewa au kumiliki mpenzi.

Watapamba kila picha nzuri mbele ya macho yao na mashabiki wao. Watawashirikisha mashabiki wao mpaka mambo ya faragha. Kifupi mitandaoni hasa Instagram watataka kutawala wao.

Hii imekuwa ikiwatesa wengi wao pindi wanapoachana. Na kwa vile wengi wao ni magubegube wakomavu. La sivyo vifo vya kujitakia kukwepa aibu vingepatikana sana.

Kwa sababu mwanzo wa penzi lao walishirikiana na mashabiki wao. Basi mashabiki watataka kushirikishwa mpaka mwisho wao.

Kuna wale ambao wanaishia vibaya kwa kuibiana mabwana. Yaani staa huyu anamchukua bwana wa staa yule. Mitandaoni inakuwa ni matusi yasiyoelezeka.

Team ya huyu inamtukana nyakunyaku na team ya nyakunyaku inamkingia kifua kwa kujibu mapigo ya mitusi.

Katika hili mfano ulio hai ni wa Hamisa na Zari. Kwa sababu ya maisha yao kuyaanika sana mitandaoni yamezalisha haya yaliyotokea na kuendelea.

Tukio la hawa wawili limetengeneza matusi mapya. Yaani kuna watu wanatukana tusi ambalo halijawahi kutamkwa popote Duniani. Kisa Hamisa na Zari kuchukuliana bwana.

Ingawa wenyewe wamekuwa wakichukulia poa kwa sababu ya matukio haya kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine lakini ni mbaya sana.

Lazima mastaa wetu wajipime na maisha ya mitandaoni. Haya wanayoyafanya na mashabiki wao yamepita kwenye ustaarabu siyo tu wa Kiafrika bali wa kibinaadamu dunia nzima.

Mambo ya ajabu kabisa. Na kupitia hawa Mastaa wetu wawili ndipo utagundua kuwa Mange anachofanya kutukana watu mitandaoni ni asili yake.

Kumbe huku Bongo kuna kina Mange wengi kuliko idadi ya kura alizopata Lowassa 2015. Kifupi kila mtu anajua kutukana. Na kila mtu anajua kulipiza tusi kwa tusi. Inasikitisha sana.

Lakini yote haya ni sababu ya mizuka ya maisha ya mitandaoni. Zari anapenda maisha ya ‘shoo ofu’ na Hamisa naye anapenda hiyo kitu.

Na zaidi bwana wao ndo anapenda zaidi pamoja na familia yake yote mpaka majirani.Sasa nani wa kumshikia paka kengere? Hakuna.

Wanaishia kuacha dunia iende kama inavyokwenda. Hayo ndo madhara ya kuacha wazi mambo mitandaoni.

Achana na hao. Kama ulifuatilia siku chache zilizopita kabla ya mume wa Irene Uwoya Hamad Ndikumana hajafariki. Walikuwa wakilumbana kwa vijembe vingi mitandaoni. Ndikumana anasema hili Irene anajibu hili. Kila shabiki akajua kinachoendelea.

Hakuna wanandoa wasiogombana. Lakini kwa nini ugomvi wa wanandoa wenye mtoto mkubwa kabisa wafanyie mitandaoni? Kwa faida ya nani? Ili iweje?

Matokeo yake maneno ya mwisho katika ugomvi wao ambayo yalikuwa makali sana. Bado yapo mitandaoni.

Na mtoto atakuja kuyaona muda siyo mrefu hata Magufuli akiwa hajamaliza muhula wake wa kwanza. Mtoto anaachwa kwenye hali gani? Maneno ya baba yake ya mwisho kabla ya kufariki yatamuacha kwenye hali gani mtoto?

Wao walilumbana na kuapiana viapo kana kwamba hawana damu inayowaunganisha nyuma yao.

Mastaa wetu tukio la Uwoya kufiwa na mumewe huku wakiwa katikati ya malumbano makali mitandaoni. Liwe funzo kwenu. Akiba ya maneno kitu cha msingi.

Maneno ya Ndikumana yanaelea tu mitandaoni yakimsubiri mtoto aje kuyaona. Ajue kile alichokuwa nacho babaake moyoni juu ya mama yake. Inasikitisha sana.

Wekeni akiba ya maneno acheni kujitoa ufahamu mitandaoni. Imekuwa kama wendawazimu sasa kila staa kugeuza kurasa za Instagram kama guest house yake. Hotel yake. Chumba chake na bafu lake.     

Saturday, December 16, 2017

Akili nyingi mwisho wake uchiziGASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Kisa cha Tanzania kuitwa “Bongo” kipo wazi kabisa. Miaka ya 1980 baada ya vita vya Kagera, hali ya uchumi ilikuwa mbaya sana kiasi cha wananchi kutakiwa kufunga mikanda kwa muda wa miezi kumi na minane. Unga, mchele. Sukari, mafuta na sabuni zilikuwa bidhaa adimu zilizopatikana kwa mgawo katika maduka ya kaya.

Katika wakati huo kuku, samaki, nyama, mayai na maziwa zikawa bidhaa za anasa. Mtu aliyebeba mfuko wa matunda alipewa pole kwa maana kama hakuwa mgonjwa basi aliuguza. Wakati huo soda, bia na sigara hazikupata hata nafasi ya kuitwa bidhaa.

Mishahara mitupu haikuweza kukidhi mahitaji mama ya familia ya watoto wawili. Kizazi kilishagubikwa na maadui njaa na umasikini, na kulikuwa na hatari ya kuwa na kizazi kijacho kitakachotawaliwa na maadui hao ukijumlisha yule mbaya zaidi, adui ujinga.

Kwa nia njema kabisa Watanzania walilazimika kutafuta njia mbadala za kujikwamua. Waajiriwa waliongeza kulima bustani za mboga na kujenga magenge ya kuuza nyanya na vitunguu ili kuongeza tija. Siku za mapumziko ya mwisho wa juma na sikukuu zilitumika zaidi kwa shughuli za kujiajiri.

Hata hivyo vyuma havikulegea.

Vijana waliokuwa wakisubiri ajira za serikali na wale waliojiajiri wakabuni ya kwao. Waliwatazama wenzao waliotoka masomoni ng’ambo walivyo na ahueni ya maisha. walipowahoji wao walisema walikuwa wakijiongeza kwa vibarua vya kusafisha vyoo na kufagia barabara.

Majanki wakajiuliza kwa nini na wao wasiende huko kuhemea ili kuwasaidia wazazi majukumu ya familia. Lakini kwenda kulihitaji hati ya kusafiria iliyotolewa kwa mkono wa Umoja wa Vijana wa CCM, na nauli ambayo ilipaswa kutajwa kwa tahadhari kubwa kwani anayeombwa anaweza kupandwa na shinikizo la damu.

Katika kundi la vijana walioisaka fursa hiyo walikuwamo wale wenzangu na mie wasiosikia la muadhini wala la mnadi sala. Hawa walijiita “magangwe” ambao ukosefu wa bidhaa ilikuwa ni fursa moja kwao. Walijenga mtandao wa kupata na kuuza bidhaa adimu kwa mwendo wa kuruka au kulangua. Magangwe waliamua kudandia meli na kujificha katika kona zake. Kwa mujibu wa baadhi yao, wengine walijichimbia kwenye bomba la moshi na kuibuka katikati ya safari. Walikubali kuwa watumwa kama ada ya safari na wakafikishwa ughaibuni.

Huko nako walikuwa watumwa waliofanya kazi zote zilizokataliwa na wazawa, wakapata fedha na kuwanunulia wazazi na wadogo zao mahitaji. Ndio wakati tulioanza kuona “viwalo” vya “Jeans” na “raba mtoni” kwa wingi. Wengine waliweza kabisa kuinua ustawi wa familia zao. Na ni wakati huu ambao kauli mbiu ya “TZ akili kumkichwa” yaani “Tanzania mtaishi kwa akili vichwani mwenu” ilithibitika. Elimu ya darasani na kazi za kuajiriwa zisingeweza kukubeba katika maisha yako ya kila siku. Tanzania ikawa Bongo.

Lakini wakati mwingine akili nyingi hushusha maarifa. Vijana waliokwenda baadaye walianza kushindana anasa. Walishindana kurudi nyumbani na magari ya kifahari kama Buick, Cadillac na Ferrari. Wakawa wakitambiana utajiri kwenye kumbi za starehe.

Lakini walikuja kuharibu pale walipokuja kuwatambia Mawaziri waliokuja na Land Rover 109 kwenye sherehe za Kitaifa pale Uwanja wa Taifa. Magari yote ya mtumba yalipigwa marufuku ili kuwanusuru vijana walioelekea kuambukizwa kansa ya “Bongo akili kumichwa”.

Ubongo wa mtu anayewaza sana unaweza kuwasha taa kwa jinsi unavyofua umeme. Lakini ubongo wa Mtanzania wa wakati ule bila shaka ungeweza kuwasha mashine ya kusaga nafaka! Wenyewe walisema mbumbumbu anayeweza kuishi Tanzania hakuwa na tofauti na msomi mwenye digirii ya chuo kikuu.

Kwa kawaida binadamu ni wabunifu na wanaoweza kuyamudu mazingira yao. Lakini wabongo ukizingatia “waya” ulivyowasugua walikuwa wabunifu “plus”. Shida humfunza mtu mambo mengi sawasawa na vile anavyopambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Narudia kusema kuwa akili nyingi ni ukichaa kwa sababu Wabongo waliacha kubuni maendeleo na kuanza kutiana ujinga. Kwa mbali inafanana na mabaharia walivyoacha kuhudumia familia na kuanza kupiga misele. Mara wabunifu wakaanza kuchezea mita za umeme, namba za luku na kadhalika.

Wakaona haitoshi. Ni ukweli usiopingika kuwa maisha ya mwanadamu wa leo yanategemea kompyuta na simu za viganjani. Sanjari na hilo, tunategemea mitandao ya kijamii kupashana habari. Wajanja wakaamua kucheza na akili za watu mitandaoni. Utaona kichwa kisemacho: “Mkuu wa Mkoa abambwa uchochoroni”.

Kwa vile michezo ya kompyuta inaweza kumhamisha Mswahili kutoka Tandale hadi Hollywood. Utaona picha ya mheshimiwa akiwa kati ya machangudoa. Ukibonyeza kwa maana ya kutaka kuona kile kilichotukia unajikuta umefungua wimbo wa msanii mchanga anayelalamikia kuporwa mke. Na inaeleweka kuwa kila unapofungua ukurasa hata kama hukukusudia basi huwa unamchangia mwenyewe hela ya kubadilisha mboga. Juzi kati ndo nikasikia kubwa kuliko nyingi. Watu sasa wanaamua kuwafundisha uhuni binti zetu kwa kuwawekea nyenzo kwenye simu zao. Unampigia binti yako anakujibu kuwa yuko msibani. Na kweli unasikia sauti za vilio na kwaya za maombolezo. Lakini kumbe anakuwa amekusetia tu ili usigundue kuwa yupo klabu akila vichwa kama konda! Haki ya Mungu hizi akili nyingi zitatumaliza…     

Saturday, December 16, 2017

Tanzania ya Viwanda inahitaji ushiriki wa wasaniiAnko Kitime

Anko Kitime 

By Anko Kitime

Sanaa ni pana sana. Ukiangalia kila kinachokuzunguka, kina usanii ndani yake. Mpangilio wa habari katika gazeti hili, mpangilio wa lugha, mpangilio wa picha, halafu ukinyanyua macho na kuangalia vitu vilivyokuzunguka, majengo, mavazi, samani, vyombo vya usafiri, mpangilio wa rangi wa vitu hivyo au ukisikia sauti za muziki vyote ni kazi za aina mbalimbali za sanaa.

Katika zama hizi inashangaza kuwa matayarisho ya wasanii wa kuambatana na nchi ya viwanda haitiliwi mkazo, lakini bidhaa zote za viwanda zinahitaji usanii, kama ni kuchora nembo nzuri au kuweka tangazo zuri la mali au hata kutengeneza sura nzuri ya bidhaa zitakazozalishwa katika ‘nchi ya viwanda’ ni kazi ya sanaa.

Bila matayarisho ya wasanii bora tutakuwa na mali nzuri zisizo na sura ya kumvutia mlaji. Hakika mpaka leo naamini kuwa kama wasanii wangehusishwa katika kukamilisha lile gari lililotengenezwa Tanzania na kupewa jina ‘nyumbu’, mambo kadhaa yangekuwa tofauti, kwanza lingepatikana jina la kuvutia zaidi na pili gari lile lingebuniwa sura ya kuvutia zaidi.

Watu wengi hununua magari kutokana na mwonekano wa gari, bila hata kujiuliza mambo mengine ya kiufundi kuhusu gari husika.

Kama nilivyosema sanaa ni pana sana leo nizungumzie sanaa ya kutumia mdomo. Binadamu wote kwa kawaida tuna midomo na tunaweza kutoa sauti mbalimbali na mdomo huo. Mungu kawapa watu mbalimbali vipaji vya kuweza kutumia mdomo huo, kuna waimbaji wa staili, watambaji, waghani wa mashairi, wasimuliaji wa hadithi, watangazaji, wachekeshaji, wahubiri, wanasiasa, na wengine wengi wa aina yao.

Wote hawa wanafanya sanaa zao kwa kutumia mdomo, japokuwa katika hawa hawa wengine hujiona sanaa yao ni bora kuliko ya wengine na mara nyingi hukataa katakata kuitwa wasanii. Jambo moja lisilo pingika ni kuwa kila msanii hupenda kupata jukwaa la kuonyesha sanaa yake, na ndio maana kulibuniwa majukwaa, na hatimae majumba makubwa ya kuonyesha sanaa ambayo nayo huwa na majukwaa makubwa ya kupendeza. Wasanii hutayarisha shughuli zao na kisha hualika watazamaji au wasilikizaji.

Msanii aliyetayarisha au kutayarishiwa shughuli ni wazi ndie anayestahili kuweko jukwaa kuu kwani hata wanaokuja kumtazama wangetaka iwe hivyo ili wamuome na kumsikia vizuri.

Kwenye shughuli za wasanii ambao hutumia midomo yao kuhubiri siasa, mara nyingi huweza ikaonekana ni vizuri kualika wasanii wengine, kama vile wanamuziki au wacheza ngoma au wanamuziki wa bongofleva na kadhalika ili waje wafanye sanaa zao kuleta burudani au kutoa ujumbe wa siku hiyo, kabla msanii aliyetayarisha shughuli hajapanda jukwaani na kuhubiri siasa.

Katika shughuli za namna hii huwa hakuna utata sana kwani jukwaa kuu huanza kutumika na wanasiasa bila ya kuingilia. Lakini kuna tabia moja ambayo imejijenga hapa kwetu wakati shughuli inafanywa na wasanii wasio wanasiasa, ambao ili kufanikisha shughuli yao hualikwa wanasiasa, ni kawaida sana katika shughuli za namna hii ukakuta wanasiasa wamepangiwa viti kwenye jukwaa kuu na wenye shughuli kulazimika kujengewa jukwaa dogo pembeni, au kulazimika kufanya shughuli zao za sanaa kwenye sehemu ambayo hawaonekani.

Nitoe mfano, siku chache zilizopita kulikuwa na shughuli kubwa ambayo ilihusu wasanii kuhamasisha uzalendo, wasanii kutoka sehemu mbalimbali nchini walikusanyika Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo. Shughuli ilipangwa kufanyika katika ukumbi mzuri uliojengwa kitaalamu kwa shughuli kama hizi.

Na shughuli hiyo ilikuwa ikionyeshwa mubashara nchi nzima, hii iliwezesha ambao hawakuweza kuja Dodoma wafaidi na kuelewa yanayofanyika Dodoma bila wasiwasi. Siku hiyo ukumbi huu ‘ukaboreshwa’ kwa ajli ya shughuli, na jukwaa dogo lilitengenezwa pembeni, na hapo ndipo wasanii walipopangiwa kufanya shughuli zao, katika jukwaa kubwa vikapangwa viti vya kukalia viongozi watazamaji wa maonyesho ya sanaa.

Jengo hili lenye sehemu ya kukaa yenye zaidi ya viti mia tano, ikaachwa na viti vikapangwa kwenye jukwaa ambapo ndipo sehemu sahihi ya kuonyeshea kazi za sanaa. Ni nini kinasababisha ukumbi mzuri ule usitumike inavyotakiwa? Kwani viongozi wakikaa viti vya mbele na kuangalia sanaa zikiendelea jukwaani itakuwa wamedharauliwa?

Mkao huo unaleta utata mwingine mkubwa kwa wasanii wanaofanya onyesho, wanakuwa katika utata, je wanafanya onyesho kwa ajili ya hadhira hivyo wawape mgongo viongozi au wanafanya onyesho kwa ajili ya viongozi hivyo waipe hadhira mgongo? Kwa aliye angalia kupitia onyesho lile kupitia luninga, onyesho lilionekana ni la ovyo tu, wasanii wakionekana hawajui wanataka kufanya nini.     

Saturday, November 18, 2017

Jamii ilimuacha Lulu afike alipofikaElizabeth Michael

Elizabeth Michael 

By Dk Levy, Mwananchi

Huwezi kuwa Lulu bila kuwa Elizabeth Michael. Ana akili sana yule mtoto. Ngumu sana kumuelewa kama hujakaa naye wala kufanya naye kazi.
Ni fundi kweli kweli wa kupuuzia wapuuzi. Ukileta dharau kwake kuna bohari kuu ya dharau.
Ukileta mbwembwe kana mbwembwe mpaka mbwembwe zenyewe zinakaogopa.
Kiumbe bora uzao wa Eva anacheza kwenye kuta ndefu za gereza muda huu. Dunia ya Tanzania inakosa moja ya pambo bora kabisa mitaani mpaka miaka miwili itimie.
Makosa ya wazazi? Makosa ya jamii? Makosa ya tasnia ya filamu? Au ni makosa ya Lulu kukosa hofu?
Huu siyo muda sahihi wa kuzungumzia chanzo kilichopelekea mtoto yule mwenye urembo usiotiliwa shaka kwenda jela.
Kitu pekee ni kwa wapenzi wake kumuombea kwa Mungu. Kwenda kumuona gerezani mara kwa mara.
Kutunza kile alichofanya kabla ya matatizo haya. Ili akitoka gerezani asianze upya maisha.
Kila mtu anasema anavyojua yeye. Kila mtu kawa mshauri juu ya maisha ya Lulu.
Wapo waliofurahia eti adhabu ya kifungo inapunguza maumivu ya Mama Kanumba. Hakuna jambo lolote linaloweza kuondoka maumivu ya kuondokewa na mtoto wako wa pekee.
Maumivu yataondoka pale utakapokufa na wewe mzazi. Jaji hakutoa hukumu kwa ajili ya kumfariji mama Kanumba. Adhabu imetolewa kulingana na mazingira ya kesi yenyewe.
Wapo wanaosema adhabu aliyopata itamnyoosha maana amezidi sana mashauzi. Ndipo mtu unagundua kuwa mitandaoni hasa Instagram watu wengi wana matope vichwani na siyo ubongo. Instagram ‘majitu’ yasiyojielewa ni mengi sana. Kuna makopo mengi sana yanayojiita binadamu.
Wapo wanaosema hasa kuwa ni makosa ya mama yake yaliyopelekea Lulu kuanza upuuzi angali mtoto.
Malezi ya mtoto wa kike kwa mzazi mmoja wa kike yana tabu sana. Na hatuwezi kujua kwa nini waliachana na mumewe.
Itoshe tu kusema kuna maisha hayazuiliki kwa familia yenye makuzi ya upande mmoja wa mzazi.
Lakini pia wale waliomtumia kingono kwani hawakuwa kama wazazi wake? Kwa hiyo mtoto wa mtu ukimkuta barabarani amezidiwa utamuacha kwa sababu siyo mwanao?
Lulu alikuwa na kazi ndogo sana ya kumuaga mama na akaruhusiwa. Ambayo ni kwenda ‘Location’. Na kweli anayempigia simu ni Steven Kanumba mama ataacha kumruhusu mtoto atoke ikiwa akienda anarudi na chochote? Location hata wiki wanakaa mama hawezi kuwa na hofu. yuko na Kanumba wanacheza filamu.
Unamlaumu Mama Lulu kwa kuruhusu mwanaye kwenda kwa Kanumba. Wakati kuna wanaume waliwaruhusu wake zao kisa wamepigiwa simu na Kanumba kwenda kufanya naye filamu?
Alichoponzwa Lulu ni imani kubwa ya mama yake kwa watu waliomzunguka Lulu.
Sawa ni makosa ya wazazi ikiwa ni pamoja na wazazi wake waliomlea kisanaa. Walimuacha mtoto atende makubwa kuliko umri wake. Walimuacha mtoto atendewe mazito kuliko umri wake.
Na badala ya kumsaidia wakaamua kujisaidia wao wenyewe kwa tamaa za ngono.
Katoto kazuri kale aiseee. Mungu akalinde na mateso ya gereza.
Na kuna wanawake wakubwa kabisa kwenye sanaa ya filamu waliogeuka kuwa makuwadi kwa Lulu. Hawakuwa na hofu ya Mungu zaidi ya kuwaza kipato cha ukuwadi.
Leo hii ukimtazama Lulu ni sehemu ya wasichana wenye miili midogo. Pata picha miaka mitano iliyopita alikuwaje? Aliwezaje kuingia kwenye kumbi za starehe na kina Kanumba katika umri ule. Hili nalo la kumlaumu mama yake ambaye muda huo alikuwa anaamini mwanaye yuko Location na Kanumba kumbe wapo klabu wanakula vyombo.
Sasa hapo ni kosa la mama au la Kanumba kujitoa ufahamu? Na wale walinzi wa mageti ya kumbi za starehe kukosa haya na kuruhusu kitoto chenye akili za kitoto kuingia klabu usiku wa manane kikiwa na jibaba lenye mwili mkubwa kama makabati ya maktaba?
Jamii kwa ujumla wake iliacha huyu mtoto afikie hapo alipofikia. Uzuri wake ni kwamba amepata matatizo akiwa bado na umri mdogo sana. Ana muda mrefu wa kurekebisha alipokosea.
Kuwepo kwake gerezani kuna kitu kikubwa sanaa inakikosa  kuliko kile Lulu anachokosa kwa kutokuwepo kwake mtaani.
Kupitia matatizo ya Lulu liwe somo kwa wazazi kuwa makini na kina Lulu wao majumbani wasiaamini sana watu aina ya Kanumba.
Kuna kina Kanumba kwenye utangazaji. Uandishi. Makondakta. Mabodaboda. Mabajaji na wauza chips mitaani. Wapo.
Somo zuri kwa tukio la Lulu ni kwamba siyo tu anatumika kingono bila wazazi kujua. Bali hata jamii inayowazunguka wanaacha mtoto wa mtu atafunwe na mabazazi yaliyokosa soni. Utu. Hofu ya Mungu na roho mbaya iliyopitiliza.
Mchunge mwanao mwenyewe usisubiri jirani akuchungie.
Kinachotokea kwa Lulu. Binti mdogo kama yeye ni makubwa mno. Hayabebeki.
Kuna watu wanafurahia matatizo ya Lulu huku akiwa guest na mpenzi wake ambaye siyo mume/mke wala mchumba. Hajui kuwa naye lolote linaweza kumtokea huko chumba namba saba.
Lulu ni dhahabu. Dhahabu lazima ipite kwenye tanuru la moto mkali ili iwe dhahabu.
Atarudi mtaani atakuwa mpya. Atapiga pesa. Maisha yatandelea. Asante Mungu kwa kumfanya Lulu awe sehemu ya somo zito kwa wazazi na watu wengi sana mitaani.

Saturday, November 18, 2017

Serikali, wasanii wawasaidie Mama Kanumba, Lulu

 

By Gaston Nunduma

Aprili 7, 2012 ni siku iliyobeba kumbukumbu nzito kwa msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael (Lulu). Ni siku aliyojikuta akiingia kwenye tuhuma za mauaji ya msanii mwenzie maarufu barani Afrika, Steven Kanumba. Lulu alifikishwa mahakamani na ilijiridhisha kuwa msanii huyo alikuwa na kesi ya kujibu.
Lulu alikiri mahakamani kuwa ni kweli alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Kanumba na kwamba siku ya tukio kulikuwa na ugomvi wa kimapenzi dakika kadhaa kabla ya kifo cha Kanumba. Alisema kuwa ilikuwa ni kawaida yake kumtembelea mpenziwe nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Habari hii imepokelewa kwa simanzi kubwa miongoni mwa wapenda sanaa, familia yake na watanzania kwa ujumla ukizingatia kuwa Lulu bado ni msichana mdogo aliyekuwa na mvuto wa aina yake kwenye tasnia.
Kama ilivyokuwa kwa wadau wengi wa sanaa, nimekuwa nikiifuatilia habari hii kwenye vyombo vya habari kuanzia tukio lilipotokea hadi hukumu ilipopitishwa. Mahakama ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya Serikali, hivyo basi hatuna shaka kabisa na busara ilizotumia kufikia hukumu hiyo.
Kwangu yote mawili; kufa kwa msanii na kufungwa kwa msanii ni mapigo makubwa. La kwanza ni kumpoteza moja kwa moja msanii Steven aliyefanya mapinduzi makubwa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya sanaa kimataifa. Lakini la pili pia naliona kuwa pigo kwa sababu tutamkosa msanii Lulu kwa muda mrefu. Kumkosa huku kunagubikwa na wasiwasi iwapo msanii huyu atarudi uraiani kama alivyoingia gerezani.
Hakuna asiyejua kuwa maisha ya jela si rafiki. Ni maisha mapya yenye sheria na kanuni zake zilizo tofauti kabisa na ya uraiani. Kwa kawaida mfungwa anakosa uhuru wa kujichagulia aina yake ya maisha kama chakula, mavazi, vinywaji, mawasiliano, burudani na kadhalika.
Huku anaanza akiwa na marafiki wapya kabisa. Ingawaje si wote walio gerezani walifanya makosa, lakini wapo wahalifu sugu ambao haiwezekani kujitenga nao kwani mtakula na kulala pamoja. Ni maisha yanayohitaji tahadhari kubwa na usaidizi wa karibu kwa watoto wadogo kama Lulu.
Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa miezi minane ya mwanzo wa kutumikia kifungo ndio wakati mgumu zaidi kwa mfungwa. Wakati huu ndio ambao mtu anahisi kupoteza ndoto zake za mafanikio alizoota tangu utotoni. Ni wakati ambao kama hatakuwa makini anaweza kumezwa na makundi mabaya.
Yawezekana Lulu na jamii wakadhani kuwa huo ndio mwanzo wa mwisho wa msanii huyo mdogo wa umri. Binafsi nadhani yeye mwenyewe ndiye mwenye kuibeba hatima yake. Anaweza kujiweka sawa kisaikolojia akakubaliana na hiki kilichotokea sasa. Bado maisha yanaendelea.
Lakini kwa upande mwingine, jela si jehanamu. Ni chuo cha mafunzo chenye kazi ya kurekebisha tabia. Tunaona watu wengi maarufu wakienda jela kwa makosa mbalimbali lakini bado wakiishi na fani zao katika kipindi chote cha adhabu. Pia kuna baadhi waliorudi uraiani na kufanya vizuri zaidi ya vile walivyoingia.
Mwaka 2005, Kimberly Denise Jones aliyejulikana kama Lil’ Kim alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani pamoja na kupigwa faini ya dola za Marekani 50,000 baada ya kuzidanganya mamlaka ili kuwaokoa marafiki waliofanya uhalifu. Hata hivyo mdada huyo alipunguziwa adhabu baada ya kuonesha utiifu akiwa kifungoni.
Mnamo mwaka 2013, mwimbaji na mwigizaji maarufu Lauryn Hill naye alitumikia kifungo baada ya kukutwa na hatia ya kushindwa kulipa kodi ya mapato kiasi cha dola za Marekani 1.8 milioni. Historia inaonyesha kuwa wadada hawa walifanya mapinduzi makubwa sana kisanii baada ya kutoka kifungoni.
Bado tunaamini kuwa Lulu angali na nafasi ya kufanya vizuri akiwa gerezani na hata baadaye. Kwa vyovyote vile  alikuwa na ndoto za kuleta mageuzi makubwa katika sanaa nchini. Mmoja wa walimu wangu wa uandishi alifanya kazi nzuri wakati akitumikia kifungo gerezani. Kwa maneno yake aliniambia kuwa yalikuwa ni matokeo ya kusimamia ndoto zake.
Kwa upande huu wanasaikolojia wanasema kuwa ukitaka kuzishinda sononi zako zigeuze kuwa mzaha. Zione kuwa changamoto inayokukumbusha jambo, na ukishalikumbuka yenyewe inapita zake. Nadhani hili linawezekana iwapo utakumbuka kuwa si kila mfungwa ametenda dhambi.
Ingawaje si rahisi kulisimamia hilo hasa kwa binti mdogo kama Lulu, lakini hayo yanawezekana kujijenga baada ya kukubaliana na hali halisi, baada ya kipindi kigumu cha mwanzoni. Ni muhimu kumtanguliza Mungu na kujipa moyo bila kusahau kudumisha nidhamu na utii kwa mamlaka.
Wito wangu kwa familia na wote walioguswa kwa karibu na matukio hayo ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Kila analolipanga huwa na makusudi kwetu. Moja kati ya makusudi ni kutupa mafundisho juu ya maisha yetu ya kila siku. Lakini lingine ni kutupima jinsi tunavyoweza kukabiliana na changamoto kama hizi.

Saturday, October 14, 2017

Wakitokea kina Rado watano tu Bongo Movie itasimamaJulie Kulangwa

Julie Kulangwa 

By Julie jkulangwa@mwananchi.co.tz

Ni kawaida yetu binadamu linapotokea tatizo kutafuta kichaka cha kujificha. Ni wachache ambao hurudi nyuma kuangalia wapi walijikwaa na kuanza upya.

Miaka miwili iliyopita soko la filamu za Bongo nchini lilikufa kabisa. Ray na wenzake waliokuwa wakitoa filamu kila mwezi wakatoweka kwenye shelfu za maduka ya filamu. Wakorea, Wazungu na Wahindi wakarudi kwenye chati.

Cha kustaajabisha kila mmoja alikuwa na sababu zake za kuporomoka kwa soko la filamu. Wengi waliwalaumu ‘Wahindi’ na wengine wachache wakatangaza kabisa kuwa hawatatoa tena filamu mpaka mdosi atakapokubaliana na matakwa yao.

Wengine walisema kilichowaangusha ni kujiingiza katika siasa hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi. Wasanii waligawanyika na wengine walihama toka kada moja kwenye nyingine kila dakika.

Wachache akiwamo nguli wa filamu za Kiswazi, Riyama Ally alikiri kuwa anguko la filamu ni ubora na si kitu kingine. Alisema mashabiki wamechoshwa kuibiwa kwa kuwahadaa kwa makava mazuri lakini ndani kilichowekwa ni utumbo mtupu.

Kwa kiasi kikubwa hicho ndicho kilichoangusha soko la filamu. Ubora! Mdosi alichangia kuangusha soko kwa sababu Bongo Movie wenyewe walimwacha awapangie nini cha kufanya. Mdosi alitoa fedha na maagizo ya majina ya watu anaowataka ndani ya filamu. Mwongozaji atajua atakachofanya lakini ahakikishe majina tajwa yamo ndani.

Wiki iliyopita mwigizaji Rado alizindua filamu yake Bei Kali. Ni filamu nzuri kwa kila kitu. Lakini kinachofanya niamini kuwa wakitokea kina Rado watano Bongo Movie itarudi kwenye mstari ni uthubutu wake.

Pamoja na changamoto na kubezwa amejifunga mkanda na kutoa filamu. Ni ujasiri wa kipekee. Wengine wamesusa na baadhi wamejificha nyuma ya kichaka cha kutengeneza tamthilia kwa maana wamekubali filamu ndiyo basi tena.

Kitendo cha kutoa filamu wakati Wadosi hawataki kuzinunua wakiamini haizuziki ni cha kishujaa na kinapaswa kuingiza kwenye kumbukumbu za tasnia hiyo.

Naamini soko la filamu bado lipo kubwa kwa sababu kiu ya Watanzania kuona kazi zinazowahusu haiwezi kukatwa na tamthilia na filamu za Wakorea na Wahindi. Kiu ya Mtanzania ni kuona filamu inayoakisi maisha ya mtu wa Tandale, Sinza au Mwanjelwa.

Rado aungwe mkono kwa kuwakomalia Wadosi kutotengeneza filamu wanazotaka wao bali walaji.

Saturday, October 14, 2017

Gosby : Rapa anayeamini katika elimu

 

By Frank Ngobile,Mwananchi

Wimbo Monifere alioimba akimshirikisha Vanessa Mdee katika kiitikio ulimtambulisha katika ramani ya Bongo Fleva lakini upekee wake ni aina ya muziki anaoimba.

Staili ya muziki aina ya trap ambayo imeibuka miaka ya karibuni imeonekana kushika kasi kwa kiasi kikubwa huku Bongo nao wasanii mbalimbali wa Rap wakiifanya japo imekuwa na mapokeo hafifu.

Moja ya wasanii wanaosifika kwa kufanya trap kali ni Gosby.

Alikoanzia

“Nilianza Muziki tangu nikiwa shule tena nilikuwa naimba kipindi hicho, lakini baadaye nilianza kurap na watu wakawa wanapenda zaidi sababu kwa kipindi hicho nilikuwa nafanya sana remix za wasanii wengine kwenye miaka ya 2007,”

“Wimbo wangu wa kwanza kupata mafanikio ulikuwa ni Everyday ambao niliutoa mwaka 2012 ulipendwa sana na baadaye zikaanza kuja na nyingine ambazo zilifanya poa pia kama BMS,” aliongeza.

Mgogoro na B Hitz

Kipindi fulani Gosby alikuwa akifanya kazi zake katika studio za B Hitz ambazo zinamilikiwa Hammy B chini ya mtayarishaji Pancho Latino.

Akizungumza uhusiano wao anasema kuwa wapo freshi “Mimi na B Hitz tuko freshi tofauti na watu wanavyofikiria na hakuna shida yoyote ile yale matatizo yaliyokuwepo mwanzo yalishaisha na maisha yanaendelea,” anafafanua

Mixtape yake

“Mixtape yangu inakuja mwezi Machi mwakani au pia inaweza kuwahi sababu kuna vitu tunaweka sawa,”

Wimbo wake na Izzo B

Kolabo yake na Izzo B inayokwenda kwa jina la Oh No anasema ilifanyikwa kama zali tu lakini imekuwa poa.

“Hii ngoma kuna watu walinizingua niliotaka kufanya nao, hivyo nilipodondoka kwa Izzo B yani fasta jamaa akanibariki na mashairi yake kwenye ngoma yangu,” alisema.

Elimu na muziki

“Mimi elimu yangu nimeishia chuo na nilianza muziki tangu nikiwa shule na sikuacha shule nimeweza kufanya yote na kwa ubora na kuna mambo naona kabisa elimu inachangia kwa namna muziki wangu ninavyofanya,”

“Nawashauri sana na bado nitaendelea kuwashauri rapa wengi, kamwe wasijaribu kuacha shule sababu ya muziki nawaambia unaweza kufanya vyote kwa wakati mmoja ni wewe kupanga muda vizuri basi,”

“Kwanza muziki ukiwa na elimu kidogo inasaidia katika mambo mengi hata uwasilishaji na ujuzi wako unakuwa vizuri sana,” aliongeza

Kimya kwenye gemu

“Nimekaa kimya kidogo kwenye gemu sababu nilikuwa nafanya mambo mengine ambayo yalikuwa yananibana kuweza kufanya muziki lakini kwa sasa nimeshapanga mambo yangu vizuri na ndio maana nimeachia dude hilo ambalo video yake inakuja baada ya kama wiki mbili,”

Saturday, October 14, 2017

Jini mkata kamba :Sababu tano kwa nini ndoa, uhusiano wa watu maarufu haudumu

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mara ngapi umeumia uliposikia wapendanao unaowakubali wametengana. Kuanzia Angelina Jolie na Brad Pitt, Heidi Klum na Seal, Vanessa Mdee na Jux, Lady Jady na Gadner G Habash. Inatokea mara kwa mara.

Watu maarufu ‘wanapambana’ na uhusiano wao kama wengine. Kwanza wao kuanzisha penzi na kubaki ndani ni ngumu zaidi. Siyo kwa sababu maisha yao yanamulikwa na kamera wakati wote, ni kwa sababu maisha yao yanaweza kuwafanya waishi tofauti ndani ya uhusiano. Mwanamuziki wa Marekani John Mayer anasema umaarufu unachangia uhusiano kutodumu. Mtaalamu wa Saikolojia nchini Uingereza, Donna Rockwell anasema umaarufu huwa unawasahaulisha. Wanazoea kuona kila mtu anawatazama wao, wanawake kwa wanaume wakijigonga kuwa karibu nao kiasi cha kusahau kuwa wanawajibu wa kutoa pia hasa wanapokuwa katika uhusiano.

Anasema ubongo hujenga mazoea ya kutaka kusikia kelele za watu wakimshangilia na huwa vigumu kuifunga sehemu hiyo. Msanii anapoasikia kelele za mashabiki au kufuatwa na mashabiki ubongo hutoa homoni ambazo humfanya ajisike akiwa ‘juu ya dunia’ lakini hajisikii hivyo akiwa na mpenzi wake.

“Mwanamuziki au mcheza filamu huyu anapoondoka ukumbini anaagwa na kundi la watu kila mmoja akijaribu kumshika mkono na wengine wakimwinda kupata japo usiku mmoja wa faragha naye, anarudi nyumbani na kukutana na mpenzi wake akimuuliza maswali magumu kutokana na ujumbe uliokutwa kwenye simu yake, ana ghadhibika haraka. Angetamani kunyenyekewa na si kuulizwa kwa ukali,”

Kupenda vichwa vya habari

Donna anasema iwapo itatokea mmoja katika uhusiano anapenda kuanika habari zake magazeti ya udaku huchangia uhusiano kufa kwa sababu hufukua mambo mapya kila siku ambayo yanaweza kumchosha mwenzi wake.

Anasema kuna uhusiano mkubwa wa uhusiano kuvunjika na mambo yanayoandikwa katika majarida ya udaku. Mfano hai ni uhusiano wa Kim Kardashian na Kris Humphries ambao ndoa yao ilidumu kwa siku 72 tu. Kwa Tanzania unaweza kuufananisha na uhusiano wa Wema Sepetu na Diamond Platnumz.

Kupishana sana umri

Ingawa anasisitiza kuwa umri siyo kigezo kikubwa lakini una nafasi katika kuufanya uhusiano udumu au ufe haraka.

Kuwa na ratiba tofauti

Mwanasaikolojia wa Marekani, Julia Flood anasema wasanii wengi wana ratiba ngumu ambazo huwaweka mbali na wapenzi wao na hii huchochea kutokuwa waaminifu. Anasema ubaya wake huchochewa na mazingira kwani watu hawa hufanya kazi na watu wengine wanaovutia kwa kila namna kwa hiyo anapokuwa mbali na mpenzi wake ni rahisi kushawishika.

Mahali walipokutana

Julia anasema mahali penzi linapoanzishwa panaweza kutoa jibu iwapo litadumu au la.

Anasema penzi linaloanzishwa kwa kukutana sehemu ya kurekodi filamu au video ya muziki na sehemu yoyote ya kazi huwa halidumu.

“Penzi la hivi huwa limeanzishwa kwa kuvutiwa na mwonekano wa nje, kadri wanavyokaa huanza kuujua mwonekano wa ndani na hivyo kupoteza hamu iwapo tabia haziendani,” anasema Julia.

Wivu, wivu wivu...

Kwa kawaida watu maarufu huzungukwa au kufanya kazi na watu wa jinsia tofauti.

Inawezekana mwenza akawa na wivu kwa kuunganisha matukio ambayo yanaweza kuwafanya wawe katika ugomvi mara kwa mara.\

Uhusiano ulitikiswa na jini mkata kamba

Kwa kipindi cha miezi miwili mastaa wa filamu na muziki nchini wameingia katika mtikisiko baada ya uhusiano wao kudaiwa kuingiliwa na ‘jini mkata kamba’. Alianza Diamond na Zari baada ya kudaiwa kuwa amezaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto. Ingawa baada ya kukiri watu waliamini hiyo ingekuwa dawa ya kurudisha mapenzi kwa mzazi mwenzake anayeishi nchini Afrika Kusini.Inavyoonekana kidonda cha usaliti moyoni mwa Zari kimekuwa kigumu kupona na jini mkata kamba amesimama kidete.

Hata hivyo inaonekana penzi hilo litaendelea kudumu hasa baada ya Zari kudai kuwa hajamwacha na hana mpango wa kuanchana na baba watoto wake wawili, Latiffah na Nillan.

Wolper na Brown

Moja kati ya couple nchini zilizoonekana zinaendelea kuwa Power Couple ni pamoja na ile kati ya mwigizaji Jackline Wolper na mpenzi wake aliyemtambulisha kwa jina moja la Brown. Hata hivyo wapenzi hao waliokuwa wakipendezana kwa mwonekano inasemekana wamepitiwa na jini mkata kamba.

Shamsa na Chid

Penzi la mwigizaji Shamsa Ford na mumewe Chid Mapenzi linadaiwa kunyemelewa na jinni mkata kamba kutokana na mwenendo wa maandiko ambayo amekuwa akibandika katika ukurasa wake wa Instagram. Mapema wiki hii aliandika: “Jamani sitokuja kumuacha mume wangu kwa ajili ya mwanamke hata siku moja labda afanye makubwa yasiyoeleweka kwenye jamii. ‘Amecheat’ Bili clinton sembuse Rashid wangu?” alihoji mwigizaji huyo maarufu aliyecheza filamu ya Chausiku.

Aunty Ezekiel na Mose Iyobo

Mwigizaji Aunty Ezekiel mwanzoni mwa wiki aliandika waraka mzito katika ukurasa wake wa Instagram akimkemea jini mkata kamba anayelinyemelea penzi lake kwa Mose Iyobo.

Alindika:… kwa uhandsom gani aliona huyu saa hizi mkajifanya kutwa kumtongoza kama sio tu ilimradi ‘umeshare’ na fulani sasa mimi sio mzungu ndugu yangu ntakukanyaga hutaamini kaulize yule …. wa china akupe habari yangu.”

Friday, July 21, 2017

Diamond kuongoza mashambulizi

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Ikiwa imebaki wiki moja kuelekea ile sikukuu ya aina yake, Kampeni ya Castle Lite Unlocks, Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza atatumbuiza nyimbo zake tatu alizoziachia hivi karibuni.

Diamond anatamba na nyimbo zake mpya ambazo ni I Miss You, Fire na Eneka alioutoa kimya kimya mapema wiki hii.

Wasanii wakubwa wanaotamba ulimwenguni watalipamba jukwaa katika Tamasha hilo litakalofanyika katika Viwanja vya Leaders, Julai 22 mwaka huu.

Wasanii hao ni Future kutoka Marekani na Casper Nyovest wa Afrika Kusini. Wengine kutoka hapa nyumbani ni Vanessa Mdee, kundi la Weusi na Navy Kenzo. Meneja uhusiano wa wateja wa kampuni ya Tanzania Brewaries Limited (TBL) kwa Afrika Mashariki, George kavishe anasema ili mashabiki wafurahie siku hiyo waanze kununua tiketi mapema au kushiriki katika bahati nasibu zinazoendelea.

“Kwa mara nyingine tena tunawakumbusha wapenzi wa muziki, hasa walioko katika Jiji la Dar es salaam na maeneo ya karibu kujiandikisha kwa wingi kwani tukio hilo la aina yake linakaribia” alisema Kavishe.

Akitangaza washirika wa tamasha hilo, Kavishe alipongeza mchango wao akisema kwamba wametekeleza jukumu kubwa katika mafanikio ambayo kampeni hiyo imefikia mpaka sasa.

Alitaja wadhamini hao kuwa ni Tigo Tanzania, Clouds FM, CFAO Motors, Marlboro na Serena Hotel Dar es Salaam.

“Tunawashukuru washirika wetu kwa kukamilisha juhudi zetu katika kuelekea kwenye tamasha la nne la muziki ambalo nina hakika kuwa litakuwa ni chanzo cha mabadiliko makubwa katika tasnia ya muziki wa ndani”, amesema Kavishe.

Jinsi ya kununua tiketi

Kavishe amewashauri wapenzi wa muziki kununua tiketi kupitia Tigo Pesa kwa namba namba 0674 444 444 na kwenda kuzichukua katika Tigo Shop yoyote katika Jiji la Dar es salaam.

Amesema watumiaji wa mitandao mingine ya simu wanaweza kununua tiketi kwa kuchagua “mitandao mingine” katika menyu ya simu pesa zao na kununua kwa kupitia namba hiyo hiyo ya malipo.

“Manunuzi ya tiketi yanaenda kwa kasi sana kwa hiyo ninawasisitiza watu wote kununua tiketi zao sasa kwa sababu hili ni tukio ambalo haupaswi kukosa.

Alisema mashabiki wategemee burudani ambayo haijawahi kutokea hapa Tanzania: “Tumeandaa tamasha hili katika viwango vya hali ya juu, . Usalama na mpangilio utakuwa wa kipekee,” anasema.

a Kavishe.

“Gharama ya tiketi ni Tshs 20,000 lakini wateja watakaolipa kwa Tigo Pesa watafurahia punguzo la bei la Sh5,000,” alisema Kavishe, huku akiongeza kwamba kwamba wateja wataweza kujipatia tiketi zao kutoka katika maduka ya huduma kwa wateja ya Tigo (Tigo shop) yaliyopo karibu nao.

Alizitaja sehemu ambalko wanaweza kwenda kuchukua tiketi zao kuwa ni pamoja na: Mlimani City-Mlimani City Mall, Makumbusho (mkabala), Palm Beach Residence-Ocean Road, Nkurumah- Nyerere Road- Gold Star, Buguruni-Rozana, Quality Center-Quality Center Mall, JM Wall- Hotel Harbor View, Masaki- Haille Selassie Road, Kariakoo-Msimabazi/Pemba Street, Manzese Darajani, Kigamboni-Ferry, Tegeta-Kibo Complex na Mbagala- Oil Com Gas Station.

Friday, July 21, 2017

HEKAYA YA MLEVI : Unajua hadi vumbi linauzwa?GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Niliwahi kuulizwa na rafiki wa Kijerumani: “kinywaji chenu asilia ni kipi?” Nikamjibu “viko vingi: togwa, kosha, dafu…” Nilipomtupia jicho nikamwona naye ashanitupia la kwake. Haraka nilimuita muuza madafu. “Kata mawili laini, maji mengi”. Muuza dafu alitomasa madafu, akayatikisa na kukata.

Tulipata madafu laini kama tulivyoagiza hadi mgeni alishangaa. Na mimi nikajigamba kuwa Mswahili hasahau asili. Alilifurahia lile dafu kiasi mchana ulipoingia aliomba chakula cha asili. Nilimpeleka kwa mama lishe na kumuagizia dona kwa perege chukuchuku, miksa kisamvu na kauzu.

Alisuuzika kwelikweli. Lakini baada ya msosi alitaka kushushia soda ya kikwao iliyoitwa “Schweppes”. Nikamwambia kuwa hapa hiyo ni picha ya Kilatino. Labda tusogee pale Motel Agip ndo watamwelewa. Tulikwenda na tukaipata.

Nikamsoma vizuri Mdachi huyu. Alipiga vazi la “lederhosen”, gari yake ilikuwa “Volkswagen Audi”, alipoteremka akachomoa pakiti ya sigara ya “Reemtsma Imperior” na kibiriti cha “Erdgas”. Kila kitu kilitengenezwa nchini mwao. Bila shaka huyu mtu alikuwa akitembea na Taifa lake.

Wakati wote alikuwa akiusifu urafiki wa Ujerumani na Tanzania. Alisema kuwa huu ni mfano wa kuigwa kwa sababu marafiki wote wamekaza kwenye mapinduzi ya viwanda. Akatoa mifano ya jinsi Schweppes ilivyoendelezwa kutoka togwa hadi kinywaji cha biashara kimataifa.

Kwa upande mmoja yalikuwa madongo mazito kwangu. Sikujua nami ningeanzaje kujigamba jinsi tulivyoendeleza bidhaa asilia kwenye uwanja wa biashara. Ni kweli tulishawahi kusindika machicha ya nazi tukapata mafuta ya nywele, vifuu vya nazi kuwa sumu ya mbu na miti kuwa karatasi. Lakini ni lini?

Sikukubali kiurahisi. Pale Hotelini niliagiza soda ya Fahari. Hiyo ingetosha kufagilia kinywaji cha ridhaa cha maji ya machungwa kwenda kibiashara. Mhudumu aliniangalia mara mbili, kisha kwa kuwa niliambatana na mzungu alikwenda kumuuliza meneja. Nikajua mambo yashaharibika.

Aliporudi kunieleza kuwa hata yeye hakuwahi kukijua kinywaji hicho, niliagiza Schweppes kwa madai ya kuonja ladha asilia za wenzetu. Hata yeye si kaonjeshwa dona kwa kisamvu? Ngoma droo!

Lakini nilipigia mstari jambo hili; Moja ya njia za uhakika za kulipa kodi ni matumizi ya bidhaa mnazozalisha. Na hakuna nchi iliyoendelea bila uzalishaji. Na huwezi kuzalisha bila viwanda. Hata mzalishe tani trilioni za chakula, mafuta na madini, mkiuza ghafi ni kazi bure. Mkiuza ufuta bado mtalazimika kununua mafuta ya kula kulekule kwa bei ya kutisha pamoja na kodi.

Kwa hiyo mkigundua gesi nchini kwenu, harakisheni ujenzi wa viwanda vya gesi. Mtakapoiingiza mtamboni kuichuja mtaipata ikiwa na madaraja yake yote. Kwenye uchafu wa gesi mtavuna petroli, kisha mafuta ya taa, halafu dizeli. Bado utamu unakuja: baada ya dizeli mnapata oili, grisi na lami. Hadi uchafu unauzwa. La kwanza mtatumia mazao yenu kwa gharama nafuu sana. Ebu fikiria longolongo ya mafuta yanayotoka Arabuni kuuzwa bei nafuu Zambia kuliko hapa. Mafuta haya yanashukia kwenye bandari yetu na tunayasafirisha wenyewe kwa bomba la TAZAMA. Nina maana kuwa bidhaa mnayozalisha wenyewe hainaga longolongo.

La pili mtauza kila kitu kitokacho kwenye zao hilo. Mtakuwa na pato la uhakika kutoka kwenye kila kitu kama kilivyo. Kila zao linaposindikwa kunatoka kitu na kunabakia kitu. Hamtakimbizana na makirikiri… sijui nini… Unapokoboa mahindi unabaki na pumba ambayo ni malighafi katika kutengeneza Kangara. Upo hapo?

La tatu mtakuwa kwenye chati ya walalao hai kwa sababu ajira zitakuwa wazi kwa watu wenu. Mtafikia mahala hadi mtatangaza zawadi nono kwa wanaosapoti rasilimali watu. Tuzo kwa wazaao watoto zaidi ya kumi na tano, tofauti na hivi sasa ukizaa nane tu unaonekana mwanga!

Kutokea hapo Mtanzania ataweza kuota analishwa doriyani na watumishi bora kumi na wawili. Zile ndoto za kuzungukwa na mapaka meusi yenye macho mekundu zitatoweka. Hutayaota tena mazombi wanaokudai wakija na misumeno kugawana maini yako.

Mwendo wa kutoka kwenye kununua embe hadi kufika kwenye kuzalisha maembe si mwepesi. Lakini kama wewe ni mlaji haukosi kuwa na kokwa. Badala ya gharama za kutafuta na kununua kokwa, unaweza kupambana na jitihada tu na ukafanikisha.

Hivi sasa tunao wajasiriamali kwenye kila kona nchini. Kuna wauza lishe, sabuni, juisi, vipodozi na mahitaji mengi sana ambayo pale mwanzoni tuliagiza Ulaya. Lakini leo wauzaji hawa wanapata bidhaa hizi kutoka kwa wajasiriamali wanaozalisha bila mitaji mikubwa.

Serikali, wadau na taasisi za fedha wanaunga mkono jitihada hizi. Lakini kwa mshangao wanawapa mikopo midogo yenye riba kubwa kiasi cha kuwafanya kuwa watumishi wao. Hadithi kubwa ni rejesho: Umekopeshwa milioni mbili urejeshe laki tano kila mwezi kwa miezi minane! Sasa huu ni mkopo au mauaji?

Kama kweli tunataka Tanzania ya viwanda tuanze na hawa. Badala ya kuwakopesha fedha kiduchu kwa riba kibwena, tuwakopeshe viwanda vidogo na vitendea kazi bila riba. Kwani riba kitu gani bwana? Tunataka nchi iendelee au tunapenda kuhesabu vifaranga wakati koo angali mtamizi?

Kwa hili Serikali inaweza. Basi tu.

Friday, July 21, 2017

Ishi kidigitali lakini mambo ya ndani yabaki katika ulimwengu wa analogiaJulie Kulangwa

Julie Kulangwa 

By Julie jkulangwa@mwananchi.co.tz

Wakati digitali inaanza kushika kasi miaka ya 2005- 2006 hata usomaji vitabu ulibadilika kwani wengi walidownload katika mitandao. Ndio wakati matumizi ya tablets na kindle yaliposhika kasi .

Ilikuwa ni fasheni kuwaona watu katika vyombo vya usafiri, majumba ya starehe na bustani wakiwa wameinamia vifaa vyao hivyo wakisoma vitabu. Mauzo ya vitabu mtandaoni yalikua kwa kasi kama moto nyikani.

Miaka 10 baadaye mauzo ya vitabu mtandaoni yameshuka. Mauzo ya vitabu vilivyochapishwa yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia saba tangu wakati huo. Utafiti uliofanywa mwaka jana umeonyesha asilimia 64 ya vijana wa kati ya miaka 16-35 wanapendelea kusoma vitabu vilivyochapishwa.

Kwa nini mfano huu wa vitabu katika mada hii? Ni kwa sababu utafiti uliwahusisha vijana ambao inaaminika digitali imewakumba na kuwazoa wazima wazima. Maana yake ni nini sasa? Kumbe analogia ina utamu wa aina yake ambao hauwezi kubatilishwa na digitali.

Basi hata katika maisha kuna mambo inabidi yanabaki katika analogia. Sasa hivi kila kitu kinaanzia kwenye mitandao ya kijamii na kwa sababu kuna deni kwa watazamaji inabidi kila kitu kianikwe huko ili kuuaminisha umma kuwa mambo yapo vizuri.

Ubaya katika hilo ni kwamba watu wanayafukua hata ambayo hayakustahili lakini wanafanya hivyo kwa kuwa mwenyewe umeamua kuishi hivyo. Kubaki analogia kuna saidia pia kuepusha maumivu na udhalilishaji.

Wema Sepetu miaka yote huwa anaitwa mgumba kwa kuwa hajazaa mpaka sasa lakini siyo Jokate Mwegelo, Flaviana Matata au Jackline Wolper ambao wamemzidi umri. Anasemwa hivi kwa kuwa mwenyewe ameamua kuipeleka ishu hiyo katika ulimwengu wa kidigitali.

Uzuri wa analogia unakufanya uwe na umiliki na siyo vya umma. Ni sawa na unapokuwa na kitabu chako katika kabati ni tofauti na kile kilichopo katika tablet. Mgeni akifika nyumbani kwako anakiona kikipendezesha nyumba na kumuonyesha kuwa ameingia katika nyumba ya msomi.

Siyo kwamba watu hawafanyi mambo mabaya katika maisha yao lakini wameamua maisha yao kuyaacha katika analogia na hiyo inawasaidia kuficha aibu zao. Kila mtu kuna wakati huteleza na ndio ubinadamu lakini ni chaguo binafsi kuyaacha analogia au digitali. Ni muhimu maisha binafsi yabaki katika analogia.

Friday, July 21, 2017

NDANI YA BOKSI : Kipaji na maisha ya hovyo ni kulwa na doto...

 

By Dk Levy

Ukijiongoza vyema katika dunia inayojaribu kila mara kukufanya uwe kitu kingine, hilo ndilo fanikio kubwa sana kwako.

Fanikio hili limewashinda mastaa wetu wengi kwenye sanaa, iwe muziki au filamu. Kipaji ni suala moja, kujiongoza kimaisha nje ya kipaji ni suala jingine kubwa na zito.

Unaweza kuwa na kipaji kikubwa lakini ukaishia kutumikia msemo wa wahenga wetu kuwa “Kipaji na maisha ya hovyo ni kulwa na doto”.

Ingawa wapo wengi wanaofurahia mtu kufeli kimaisha, kwa mtu mwenye utashi na akili za kibinadamu kamili hawezi kupendezwa nalo. Inaumiza.

Nani alikuwa kama Aisha Mbegu Madinda katika kunengua? Aliwafunika karibu kila kitu wenzake. Sura nzuri, umbile halisi la kibantu, ngozi laini ang’avu. Sharapova, Lilian Internet au Aunty Suzzy? Hapana! Na ukali wao wote, hapa walikuwa kimya.

Kuna maelfu ya watu waliifuatilia Twanga Pepeta ndani na nje ya Dar es Salaam. Siyo kwa sauti ya marehemu Banza au Choki. Siyo kwa tumba za marehemu MCD wala drums za marehemu Abou Semhando ‘Baba Diana’.

Ni kwa sababu ya uwepo wa kiumbe wa kike mwenye mvuto uliopitiliza, mnenguaji ambaye muda wote alitabasamu jukwaani na kumfanya shabiki kuona kama ananenguliwa na malaika mbele yake.

Marehemu Aisha Mbegu Madinda. Mungu ampumzike sehemu inayomstahili huko alipo. Hii ardhi imemeza watu wengi. Aisha alikuwa alama sahihi na nembo nzito kwa wanenguaji wa kike Tanzania.

Alikuwa hatari katika sekta hii. Alitisha kila mahali na hakuna aliyethubutu kubisha. Katika suala la kazi alikuwa ni zaidi ya hatari unayoijua. Kiuno laini, miguu matata stejini, na tabasamu murua usoni.

Kwa umaridadi huo na akili yake iliyotulia, akafanikiwa kuwa na nyumba, akamiliki saluni na mpaka akawa na usafiri wake. Kwa wanenguaji, nani alikuwa kama yeye? Wanamuziki wa Bongo Fleva walikuwa wanasubiri kwa Aisha. Uliza watu. Alikuwa daraja moja na marehemu Amina Chifupa kwa wakati ule.

Kwa binti kama yeye, mnenguaji kama alivyo, nini zaidi alihitaji zaidi ya hivyo katika maisha yake? Haikutosha hapo tu, jina lake lilikuwa juu usawa wa ndege na hewa.

Wengi walienda maonyesho ya Twanga wakiamini hatowaangusha kama kila siku alivyokuwa akifanya. Kwenye idara ya unenguaji jukwaani alikuwa ni bendi ndani ya bendi yenye bendi ndani yake. Acha kabisa. Si mpaka taarifa zikaja kuwa Mapedeshee wengi walikuwa wakienda Twanga wakisubiri mwisho wa shoo wasemezane naye.

Robo ya mashabiki wa kiume wa Twanga walimfuata Aisha wamtazame kisha wakalale na amani ya mioyo yao. Fundi wa kike kwenye jukwaa.

Kuna aina ya unenguaji wake kila msichana mnenguaji alimuiga. Kuna pozi zake ambazo ziliigwa awapo jukwaani. Tangu na tangu wakiwa na kundi lao la Bilbums pale Bilcanass, Aisha alikuwa mgodi. Alifanya kila kitu wenzake walichoshindwa, akafika kila mahali palipoonekana ni mbali kwake kufika. Mvuto wake jukwaani ulikuwa zaidi ya gitaa la Shakashia na kelele za Msafiri Diouf.

Aisha alikuwa nembo ya mafanikio kwa wanenguaji wote nchini. Aliijua kazi yake, akautunza mwili wake na hatimaye vikamletea mafanikio.

Ni kupitia Aisha, ndipo hata baadhi wakaona unenguaji unaweza kuwa kazi halali. Kama ambavyo Jide kawafanya wasichana wengi waamini kuna maisha nje ya ajira za digrii kwenye muziki.

Ndivyo ambavyo wasichana wengi waliamini kuwa kuna maisha nje ya kumiliki duka la vipodozi na kufanya kazi mahotelini kama utaweza kunengua vizuri. Aisha alikuwa taa ya wasichana wengi wa mjini kama kina Halima Kimwana. Mwisho nuru na ubora wa ngozi yake ukaanza kutoweka. Juhudi na ushupavu wake wa kunengua jukwaani ukayeyuka kama kipindi cha Afrika Bambata pale Clouds.

Dawa za kulevya alizozisogelea zilimkaribisha kwa shangwe na kumfanyia kila sherehe katika mwili wake. Yakamlea. Yakambembeleza. Naye akayakumbatia. Yakamnyang’anya mafanikio na afya yake nzuri, yakampora sifa yake nzuri na umaarufu wake uliovutia. Yakamuondolea kujiamini mbele za watu. Aisha akawa mnyonge bila sababu. Unga.

Akaanza uvivu wa kunengua na kupaka poda usoni. Taratibu akaanza kutoweka katika majukwaa ya Twanga. Yakampunguzia kumbukumbu na kusahau ratiba za shoo. Akawa anachelewa jukwaani na kukwepa baadhi ya shoo. Asha Baraka akalia peke yake.

Dawa hizo ambazo zingine zinaingizwa na watoto wa vigogo pamoja na baadhi ya wasanii, zikamfanya asiwe na thamani na hadhi kama ilivyokuwa zamani.

Aisha Madinda hakumshitua mtu yeyote tena kwa sura na tabasamu lake. Hata akili yake pia kuna mahali ikapoa na haikuwa na ule moto wa zamani. Tumuache Aisha apumzike. Tuzidi kumuombea.

Unawakumbuka Nako 2 Nako? Kikosi cha Mizinga waliwahi kusema miongoni mwa wanamuziki wa kundi hili wanatumia dawa za kulevya.

Kwa kudhani ni tambo za kisanii na kwa kuwa makundi hayo kama yalikuwa hasimu, wengi wakapuuzia.

Alianza kuvumishwa Ibra da Hustler. Kwa kumuangalia ni kama ilikuwa kweli. Ila pia kwa kumuangalia tena ni kama ilikuwa hapana. Siku zikaenda.

Kila kona Nako 2 Nako ikawa inashika. Watu wakaanza kuyapotezea baadhi ya makundi na kuanza kuwashabikia wao kwa kasi. Mara likavunjika.

Ibra akajitenga na wengine wakabaki. Japo pengo la jamaa lilikuwa dhahiri, ila kwa kuwa waliobaki pia walikuwa vichwa na wenye kujielewa, kila kitu kikaenda poa.

Haikuwahi kutajwa Nako 2 Nako bila Lord Eyes. Utapigwa na mashabiki. Kila mmoja aliona ndiye aliyebeba ufalme wa kundi lile. Mwanzo kutoka Arusha alikuwa akihusudiwa Joh Makini na Watengwa, ila baada ya ujio wa ngoma kali kali za Nako, kila mmoja aliwaona ndiyo hasa mastaa wa Arusha huku Lord Eyes akionekana kama ndiye mfalme halisi.

Unakumbuka ngoma kama Hawatuwezi, Ndiyo Zetu, Bang na Mchizi Wangu. Hizo ngoma na nyingine nyingi zilizidi kudhihirisha akili komavu ya akina Lord Eyes. Mara kikosi cha Mizinga wakaja na kampeni yao ya “Hip Hop Bila Madawa inawezekana”, na katika mabango yao wakamtaja Lord Eyes kuwa anatumia dawa za kulevya. Nani aliwaamini?

Mara Nako 2 Nako wakaanza kuchuja. Lord Eyes akachuja zaidi na ufalme wake ukahama na kwenda kwa G Nako. Bado watu hawakushtuka.

Taarifa zikaja za unga, tukataka kukataa ila uraibu wa Ray C ukawashawishi wakubali. Lord anaingia kwenye kundi la vijana wenye vipaji walioshindwa kuongozwa na kujiongoza. Inaumiza. Na kwa mwendo huu ni dhahiri jamii ya muziki inapungukiwa kitu. Weusi wako juu vile, lakini mtu mrefu mwenye mbavu nene haonekani kando yao.

Kila siku huwa tunalia na dawa za kulevya. Kama bila dawa unadhani ni wapi angekuwapo Lord Eyes? Hii dunia ya muziki ingekuwa chini ya soksi zake ikimuabudu Chalii huyu wa Arachuga.

Ni nyimbo ngapi za thamani na kiwango zingekuwa zimetengenezwa na Ray C pamoja na marehemu Langa na Mark II B. Ni mali ngapi angechuma Aisha Mbegu Madinda kwa kipaji na uwezo wake?

Kuwaonea huruma walioko magerezani iwe China au Tanzania, kwa sababu ya biashara za dawa za kulevya ni sehemu ya ushetani kama ushetani mwingine.

Sioni sababu ya kuwaonea huruma wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Ni sehemu ya Ibilisi tunaoishi nao hapa duniani huku tukiwaona mashujaa kwa mali wanazomiliki kupitia biashara ya kuua nguvu kazi ya Taifa.

Bila tamaa yenu ya fedha na utajiri wa haraka, leo Aisha Madinda huenda angekuwa na bendi yake, mgahawa wake au hata chuo chake cha unenguaji.

Wako wengi sana waliotoweka kwenye sanaa kwa sababu ya unga. Unapomtazama Profesa Jay leo, kuna mkali aliyemuhusudu hata kudiriki kupita kwenye njia zake za kuchana mistari Terry Fanani. Unga ulimchelewesha kupanda basi la mshahara.

Achana na unga, wasanii wengi wa filamu pamoja na kuigiza mapenzi kila siku kwenye filamu zao. Lakini, wameshindwa kujiongoza kwenye mapenzi katika maisha halisi. Wengi wanayumbishwa kisanaa katika daraja lile lile kama wala unga lakini wao ni kwa sababu ya mapenzi. Kipaji ni suala moja, kujiongoza ni suala lingine zito. Linahitaji akili kubwa zaidi ya kukaa location.

Ushindi wetu mkubwa siyo kukwepa kuanguka, bali kusimama kila wakati tukianguka.

Saturday, July 8, 2017

NDANI YA BOKSI: Ukimfuatilia Diamond... Utafeli

 

By Dk Levy

Kuna njia mbili pekee za kuishi maisha yako. Moja ni kama hakuna kitu cha miujiza. Nyingine ni kama kila kitu ni miujiza.

Watanzania na wanamuziki wote wa Bongo wamesimama wakimtazama Diamond katika kiwango chake cha juu kabisa cha muziki. Yuko juu sana.

Ukifanya kukaa na kubishana kila siku, unatoa maombi kwa shetani. Waliobishana mwanzoni wote wanaafiki kuwa yuko juu. Walioamini kuwa yuko juu tangu alipotoa wimbo wa ‘Nenda Kamwambie’ bado wanaamini yuko juu zaidi.

Wale masela wanaokaa maskani ambao muda wote wana akili ya ubishi, wanaamini yuko juu sana.

Sura yako itanuna, lakini moyo wako utakuwa unafuata mapigo ya ‘Fire Fire fire Baby... hebu cheka na sura ya kitoto...’. Mishipa yako ya damu itakuwa inafuata mapigo ya ‘Tanga kunani vurugu mechi Mkwakwani’. Mwishowe utashindwa kubana zaidi, hata sura itaanza kuimba ‘Sambaa chumbani yeye ndo Messi uwanjani, msiniibie Simba Yanga’.

Ifikie wakati tuache kuwafananisha wanamuziki wenzake wa hapa nyumbani na yeye. Tujifunze kama siyo kujilazimisha kumtofautisha nao.

Hii itawapa mizuka ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili wafikie kule aliko. Kusema mwanamuziki fulani wa Bongo Fleva ni zaidi ya Diamond ni kuikosea heshima biashara ya muziki.

Anataka nini zaidi? Ana gari la kifahari? Gari siyo ishu tena katika daraja lake. Anachotamani pengine ni kupata uhuru wa kuweza kupanda basi la mwendokasi. Nimetambua kwamba ukiyapenda maisha, maisha yatakupenda kwa usawia. Ndicho kinachotokea kwa Diamond.

Anapenda maisha. Ndiyo maana tangu aanze kupata umaarufu kwenye muziki wake hajawahi kukosea njia ya kupita.

Hataki kurudi Tandale. Anataka kuhama Madale. Anawafuata wenye maisha mazuri kama alivyofanya Bob Marley.

Bob Marley alipopata umaarufu na fedha hakutaka kuendelea kukaa ghetto za Jamaica na masela wake wa kitambo. Aliwamwaga kinomanoma.

Na jibu lake lilikuwa rahisi tu. Tunatafuta pesa ili tufanyeje? Akahamia zake Miami bata ndefu kwa rasta yule mpenda wanawake.

Kuna mamilionea wangapi katikati ya jiji la Dar es salaam hawatazamwi mara mbili? Kuna mamilionea wangapi katika ya jiji la Dar es salaam majina yao hayako midomoni mwa Watanzania? Mwishowe wanalazimishwa kuimbwa katika bendi.

Diamond Platinum yuko juu yao. Ngumu sana kushirikiana na Ne-Yo kama huna mtaji wa pesa na watu. Hasa watu. Inakuwa rahisi kwa staa mkubwa kushawishika kulingana na upana wa jina lako wewe unayetaka kufanya naye kazi toka Afrika Mashariki.

Diamond wa sasa anaacha kununua kiwanja Salasala au nyumba Sinza. Analipia kwa mtengenezaji wa video zake. Muziki unahitaji uwekezaji mkubwa.

Ni video ambazo hata Beyonce na Jay Z wanaweza kukaa sebuleni katika jumba lao la kifahari New York na kuzitazama.

Lakini Platinum mwenyewe anaamini hatakuwa juu ya kila mtu daima. Ndo maana unaona anavyozidi kuwekeza kwenye ardhi na biashara nje ya muziki. Anajua kuna wakati utafika ataanza kushuka chini. Atasimama katika kimo kile kile walichosimama wengi ambao walikuwepo wakapita, kama kina Awilo Longomba na wenzake.

Hakuna uchawi zaidi. Watu wana tabia ya kumchoka mtu. Si kwamba Diamond Platinumz atachokwa kwa kiwango chake, hapana. Diamond anaweza kuendelea kuwa yule yule. Katika ubora ule ule wa sauti, midundo na video.

Tatizo Watu hawapendi sana mtu mmoja akiwa juu kila siku. Wanamuziki wakubwa duniani yanawatokea haya. Kwa Bongo tena wataanza maneno ya chini chini kuwa ameisha. Baadaye watafanya kila wanaloweza kumnyanyua mtu mpya.

Kabla ya Diamond walimbeba zaidi Ally Kiba. Walipochoka walimuondoa, wakamkaribisha Platinumz.

Ndivyo maisha yetu wanadamu yalivyo. Hii ndio silika yetu watu wa ulimwengu huu. Tunapenda vitu vipya. Kitu cha muhimu zaidi kwa Platinumz ni kujitanua zaidi ya alipofika kibiashara. Atuache kabla hatujamuacha.

Kuisoma talaka yetu dhidi yake itakuwa ngumu kwake kuliko jinsi ilivyo rahisi kwake kuandika talaka dhidi yetu. Na kwa pale alipofikia Diamond siyo rahisi kushuka mpaka eneo alilokaa Mr Nice kwa sasa. Ni ngumu. Na inakuwa ngumu zaidi kutokana na namna ya uwekezaji wake kwenye muziki na biashara zingine.

Yatakuwa yaleyale ya kina R Kelly au Boys Two Men. Siyo kwamba wamefulia kimaisha bado wapo vizuri kiuchumi. Ila mazingira ya muziki yamewapa talaka wao.

Wapo kwao huko Marekani wanakula maisha, ila mboni zetu zimetengana nao kwenye runinga na jukwaani. Watu wanataka vitu vipya.

Ambwene Yessaya alitupa talaka Watanzania muda mrefu. Anaimba nyimbo na kutengeneza video zake kwa ajili ya watu wa mataifa ya nje ya Tanzania.

Haishangazi kuwa anabakia kuwa mwanamuziki wa kwanza kupata umaarufu zaidi nje ya mipaka yetu na wala hapandi jukwaa la Fiesta.

Nyimbo zake zipo kwa ajili ya Channel O, MTV Base, Trace na kwingineko. Angeendelea kuimba nyimbo kama ‘Yule’ na nyinginezo tungempa talaka kabla hajatupa talaka.

Lakini akaibuka kuwa mtu mjanja na makini akaachana na sisi mapema. Na siyo hayo tu, pia AY kwa kipindi kirefu alishaacha kutegemea pesa za shoo na albamu. Kitambo anafanya biashara ambazo pengine ndizo zinazomuingizia chapaa kwa wingi kuliko muziki.

Peter na Paul Okoye maarufu kama P Square walimjua AY kabla ya Diamond. Kuna watu wenye akili timamu wanaomzunguka Platinum. Ni hao hao wanaomkuza zaidi katika vyombo vya habari kiasi kwamba jina lake halitoweki kwa sababu mbaya au nzuri.

‘Diamond afumwa katika gari na Wema’.. ‘Diamond amsaidia maskini shilingi milioni moja’… ‘Diamond alala chumba cha mabilioni Malaysia’.

Watu wote walifanya kazi hii wakimuuza katika soko la ndani zaidi kwa wakati ule.

Achana na video yake ya Number One. Alitokea Mnijeria mmoja mfupi na mdogo kiumri kwa Diamond. David Adedeji Adeleke aliyezaliwa November 21, 1992 a.k.a Davido.

Huyu ndiye aliyechangia Diamond jina lake kutapakaa kwenye viunga vya majiji mengi Afrika. Ngumu sana kumtenga Davido na ustaa wa Diamond Afrika.

Hapa ndipo unapoona kuwa Diamond na watu wake wanaomzunguka wako makini sana kutumia fursa. Tofauti sana na wanamuziki wenzake wa Kitanzania.

Wengi wao wanaamini katika kipaji kuliko kujiongeza. Drama za Diamond na Wema na saga za Diamond na Zari wake. Ni mambo ambayo yanatufanya tushindwe kumuondoa Diamond kwenye vinywa na masikio yetu.

Mr Nice alishindwa katika hatua hii. Zaidi ya nchi ambazo zinazungumza Kiswahili, hakwenda mbali zaidi.

Na tatizo alitegemea nyimbo zake zijitangaze kuliko watu wake wa masuala ya biashara kumtangaza.

Platinumz hajapitia njia hii ya Mr Nice. Yeye kapitia njia za kina P Square, Davido, Jay Martins, Jose Chameleon, Cabo Snoop na wengineo.

Kinachoendelea hivi sasa ni stress tupu kwa wasanii wengi wa Bongo. Kuna vitu wanashindwa hata kupost mitandaoni kwa sababu kitakachopostiwa na Diamond kitatazamwa zaidi.

Akiposti gari yake atakuwa zaidi yao. Akiposti nyumba zake atakuwa zaidi yao. Akiposti video za shoo zake ni zaidi yao. Akiposti picha ya ofisi yake atakuwa zaidi yao. Kila kitu yuko hatua kumi mbele yao.

Diamond anapoingia kwenye kituo cha redio kufanyiwa interview, shughuli zote zinasimama. Kila kitu kinamuangalia yeye mpaka viyoyozi vya studio vinamnyenyekea.

Maiki zinatoa sauti kwa adabu. Zinajua kuna mwamba yupo mjengoni siku hiyo.

Hilo lipo kwa kituo chochote cha redio. Sasa aende msanii mwingine kwenye studio hizo. Atakavyotazamwa ni kama naye ni miongoni mwa wafanyakazi wa kituo hicho. Hakuna mtangazaji wala mfanyakazi anayeshituka.

Kuna tofauti kubwa sana kwa Diamond na wanamuziki wenzake wa Kitanzania. Anawapa wakati mgumu sana wa kuongeza bidii. Waache kuumizwa na kile kinachotokea kwa Diamond hivi sasa. Wafanye kazi bora na kujituma watanyenyekewa.

Badala kuwaza kuwa unastahili kuwa kama Diamond kimaisha. Fanya kazi kwanza kwa kujituma ili uanze kufikiria hilo. Huwezi kustahili kuishi maisha ya Diamond kwa kuendelea kuishi kama digidigi.

Jitokeze. Fanya kazi. Jitume. Usiogope kuwa kiherere. Usifuatilie kile anachofanya Diamond kwa sasa. Hakijaja kama bahati mbaya kwake aliyaandaa haya mazingira aliyonayo hivi sasa.

Ukiacha kujituma kivyako na kufuatilia hatua za Diamond wa sasa hivi... utafeli. Kuna wakati maisha yanahitaji kitu kingine zaidi.

Saturday, July 8, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: AK-47 v/s bakora ya mwembe

By Gaston Nunduma

Kuna mzee mmoja alitokea kule kwenye mwinuko mrefu kuliko mingine mingi duniani ambako wenyewe waliamini kuwa hakuna mahala pa juu kuliko hapo. Wakasema “hiki ni kiti cha Mungu” hivyo pakajulikana kama Mlima wa Mungu.

Huyu mzee aliingia kwenye maji kutega wavu wa samaki. Kwa bahati mbaya maji yakamshinda. Alimpigia kelele mwanaye aliyekuwa ukingoni, naye haraka akamwita mwokozi. Mwokozi alitaka walipane kabisa maana watu wa pande zile huwa hawanaga utani mbele ya “njuru”.

Dau lilikuwa laki tatu na dogo alikuwa na laki moja. Kama nilivyosema watu wa kitaa kile hawana soga hata chembe kwenye pesa. Nasikia ati yupo mmoja alikurupuka kwenye operesheni baada ya daktari kudondosha mkasi, akadhani amedondosha mia mbili. Kwa hiyo mwokozi aligoma kufanya kazi kwa malipo ya baadaye.

Huku majini mzee alizidi kutapatapa, akauliza “vipi sasa mbona hamji kuniokoa?” Mtoto akajibu hela haitoshi. Akauliza tena: “Kwani anataka shilingi ngapi huyo?” Akajibiwa laki tatu”.

“Kha!” Mzee alishtuka hadi maji yakaruka. “Achana naye! Mi mwenyewe huniuzi hata kwa elfu tano!” 

Kwa sasa si ajabu kwa mtu kuona pesa ina thamani kuliko maisha. Kila kukicha tunasikia watu wakichinjwa kama kuku kwa sababu ya hela ya kula tu. Uhalifu wa fedha umekuwa ukiongoza dhambi karibu zote ukizichanganya kwa pamoja.

Kama kawaida, vuli ni za mkulima lakini usiku ni wa mwizi. Maovu yote hufanyika usiku. Kama siku moja usiku utabadilika kuwa mchana kwa ghafla, unaweza kufa kwa utakayoyaona. Utashangaa kuona hata ndugu uliyezaliwa naye akikufukiza juju kitandani kwako.

Ni wazi kuwa ndugu zetu wana usalama huwa na kazi kubwa zaidi usiku. Zingatia kuwa paka shume huchagua kiza ili kuficha kucha zake, hivyo walinzi hulazimika kumtambua kwa namna nyingine. Ni lazima uwe umepita kwenye tasnia yao au umefunzwa ili kuwatambua. Ndiyo maana vikaanzishwa vyuo vya polisi.

Kwanza utafunzwa kumtambua mhalifu, kisha namna ya kumuingia. Unaweza kumsalimia tu ukapewa mkwaju. Ndiyo maana nasema paka wa ndani na yule wa jalalani wanatambuana kwa macho.

Baada ya kumtambua mhalifu, kuna namna ya kumdhibiti. Polisi hufunzwa matumizi ya nguvu nyepesi hadi za juu kulingana na mahitaji. Hawezi kumbebea bunduki mwizi wa kuku, au kumvaa jambazi sugu na bakora. Ukijifanya kifaru, wenzio tayari wanalo jeshi zima la vifaru.

Kumbuka kuwa raia anakubali kukatwa kodi ya kuwalipa walinzi wake kwa sababu ya mgawanyo wa majukumu kwenye jamii. Ili yeye na mali zake awe salama ni lazima awe na ulinzi. Vinginevyo wale watu wanaodhani kuwa pesa ni mali kuliko maisha watawachinja kama kuku wa mdondo.

Sasa wenye akili fupi watawaza: “Kama suala ni ulinzi basi kila mtu si afundishwe?” papo hapo wenye akili ndefu watajibu: “Ikitokea kila mmoja ni Polisi, nani atamlinda nani?”

Kwa hiyo mpaka hapo tumeelewana juu ya mgawanyo wa kazi. Tazama jinsi siafu walivyojipanga: hawa wanajenga, wale wanatafuta chakula, wale wanalinda himaya na wengine wanazalisha watoto. ndivyo jamii ya binadamu inavyoishi.

Hivi sasa wahalifu wamejiongeza. Wale wanaotumia nguvu sasa wanabeba silaha za kivita, na waporaji wa mtaani nao wanatembea katika vikundi almaarufu “Panya Road”. Hali sasa huku mitaani imekuwa ni ya kutisha kupita maelezo.

Niliamini kuwa Serikali ingebuni mbinu za ziada katika kukabiliana na hili. Lakini hakuna mtu wa ajabu kama Mtanzania. Akiwa mwembamba atashinda kwenye kitimoto ili anenepe, na akishanenepa atakunywa ndimu. kinyume chake tumerudi enzi zileeee kabla hata ya kuwepo kwa jeshi.

Mwanzoni raia walipewa mwito wa kujilinda wenyewe wakikumbushwa kauli mbiu ya “Kila mwananchi ni askari”. Ni kweli kabisa, lakini hata jeshini si wote washikao mitutu. Kuna wapagazi, wapishi, madakitari, vikosi vya mawasiliano, n.k.

Ikawa kila usiku raia wanajikusanya kwa mjumbe wao wa nyumba kumi wakiwa na bakora tayari kwa ulinzi. Katika miaka ya nyuma haikuwa hatari kwani wezi wa madirishani walikimbia mara tu walipohisi kuwa sungusungu wamewakaribia.

Si katika kizazi hiki cha digitali kinachojiapgredi automatikali. Sungusungu mwenye bakora anakutana na majambazi wenye zana za vita au panya road themanini wenye mapanga! Matokeo yake huyu raia anayetegemewa na Serikali pamoja na familia yake atapotezwa bila sababu za msingi.

Lakini kwa upande mwingine huyu sungusungu ni mfanyakazi aliyetoka kiwandani saa moja za usiku. Analazimika kutii sheria na kuingia lindoni saa sita hadi kumi na moja alfajiri. Atapumzika saa ngapi? Ataweza kufanya kazi vile anavyopaswa?

Wazo langu ni Serikali kulipa uwezo zaidi jeshi la polisi nchi nzima. Matukio kama yale yanayoendelea mkoani Pwani yawe changamoto ya kuharakisha utekelezaji. Kamwe tusitegemee sungusungu wala siafu ati watathubutu kuingiza pua katika mtiti kama ule.

Saturday, July 1, 2017

Unique Band na mpango wa kulikamata soko la burudani

 

By Aurea Simtowe,Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Ni vijana wanne  wasomi, wenye vipaji na ndoto za kufika mbali kupitia muziki wa kizazi kipya.

Wasanii wanne wanaunda kundi hilo ambao ni Herman Kibasso (Nicolass Nana), Rommy Romwad (Rommy The Base), Loyce Paul (Loichi) na Alex Exavery (Lexy Gitaa).

Vijana hao wanne wanapiga gitaa, kinanda na kuimba. Ukitaka kuujua umahiri wao tembelea Klabu ya Ground Zero iliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Kila siku ya Jumamosi, baada ya masomo ya wiki nzima hutumbuiza katika klabu hiyo.

Ni miezi miwili tangu kuanzishwa kwa kundi hili lakini umahiri wao katika kuimba na kupiga vyombo umewafanya wapewe kibali cha kutumbuiza kila mwisho wa wiki.

Meneja wa kundi hilo, Alex Exavery ‘Lexygitaa’ anasema lengo  la kuanzishwa kwa bendi yao ni kutaka kuonyesha mfano kwa kufanya kazi na watu kutoka sehemu yoyote duniani.

“Tunataka tuwe watu ambao tunaweza kufanya kazi na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, tuwe na vitu ambavyo watu wengine wameshindwa kuvifanya kwa mfano  hivi sasa tumeanzisha programu ya nyimbo mbalimbali za kigeni ikiwemo Kichina, Kijapani, Kikorea na Kiitaliano.” alisema Alex.

 Alisema lengo kubwa la kufanya hivyo ni kutaka kukusanya mashabiki kutoka sehemu mbalimbali na hata wageni watakapokuja kutoka nchi za nje basi bendi yao iwe moja kati ya wale watakaopewa kipaumbele katika kuwaburudisha  kwa lugha zao.

Alisema licha ya kufanya hivyo pia wao kama The Unique band wanafanya kazi sehemu yoyote ile ikiwa ni kwenye harusi,sherehe ya kuvalishwa pete,kuzaliwa.

Jinsi walivyokutana

Alex anasema yeye pamoja na Rommy wanasoma chuo kimoja cha utunzaji wa fedha IFM jambo ambalo liliwafanya kuwa karibu na kuamua kufanya kazi pamoja.

Ingawa kukutana kwake na Rommy ni tofauti na alivyokutana na Nicolass Nana kwani wao walikutana katika tamasha ambalo liliandaliwa na Aneth Kushaba na baada ya tamasha waliamua kukaa na kukubaliana kufanya kazi pamoja .

Kukutana kwao na mwanadada Loyce, aliletewa na mtu kutoka kundi la muungano wa wasanii wa chuo cha uhasibu(TIC) baada ya kuona The unique Band wana uhitaji wa msichana katika kundi lao.

“Siku ambayo tunamsikiliza Loyce akiimba alinivutia jambo lilifanya kumpatia nafasi ya kujiunga katika kundi hili,” alisema Alex.

Matarajio yao

Licha ya kukumbwa na changamoto nyingi katika shughuli za kimuziki kundi hili limejiwekea mikakati inayoweza kuwanufaisha na kuwafanya watu wote wafanikiwe kupitia vitu wanavyovipenda bila ya kundi kuvunjika.

Meneja Masoko kutoka The Unique band, ‘Nicolass Nana’ anasema ni ngumu kwa mtu kuendelea peke yake hivyo wanakaa katikakundi ili kuweza kusaidiana katika mambo mbalimbali ili kila mtu aweze kufanikisha kile anachokihitaji.

“Tunasaidiana kimawazo na mambo mbalimbali ili mwisho wa siku kila mmoja aweze kusimama na kitu chake lakini bendi ikiwa bado inaendelea” alisema Nicolass Nana na kuongeza kuwa

“Kukaa katika kundi kunafanya mambo kuwa mepesi kwa sababu kuna baadhi ya vitu mimi sivifahamu ila Alex anafahamu, mimi sijui kupiga gitaa ila Rommy anajua pia naweza kuwa sijui jinsi gani ya kukifanya kitu fulani lakini Loyce anafahamu hivyo tunajikuta tuna faida nyingi kuliko kuwa peke yangu,” alisema Nicolass Nana.

Mpaka sasa hawajaweza kutunga wimbo wao lakini wanaimba nyimbo za wasanii mbalimbali wa bongo flave na rnb wakati wakiwa katika mchakato wa kuandaa nyimbo zao.

Malengo yao ni kuwa bendi kubwa itakayotumbuiza katika majukwaa makubwa.

“Bado tunajijenga, unajua sasa hata watu kutuamini kutupa kazi inakuwa ngumu kwa sababu ndio tunaanza, lakini tumejipanga kulikamata soko la muziki,” alisema Loyce.

Changamoto

Kila kazi ina ugumu wake vivyo hivyo kundi hili limekuwa likipata vikwazo lakini haviwakatishi tamaa.

“Ugumu wa kazi hii ni wakati kama huu ukiwa ‘underground’ tunajitahidi kutafuta masoko zaidi ili angalau kwa  wiki tufanye kazi kwa siku tatu,” anasema Loyce.

Saturday, July 1, 2017

Wapo kina Rayvanny wengi tu tatizo ni kukaririJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

Siyo mashabiki na wadau waliokariri kuwa wanamuziki wanaoweza kufanya makubwa ni Diamond, Alikiba na labda Vanessa Mdee kwa mbali, hata wasanii wenyewe wanaamini hivyo.  Naamini hivyo kwa sababu hata kujaribu wamewaachia wao.

Wasanii wanaogopa kujaribu kushiriki wakiamini level hizo ni za wasanii fulani na wao hawahusiki kabisa. Wanaamini wanaandika nyimbo wapate shoo tu basi.

Wenye vipaji kama Rayvanny wapo wengi lakini vinaishia wapi? Hawa wanaojiita viongozi wanachoangalia ni kuingiza fedha lakini siyo kujaribu kupanua wigo kwa kushiriki tuzo za Kimataifa.

Wapo wapi kina Grace Matata, Vumilia, Beka, Hard Man na wengine? Muziki umewatema au kutokuthubutu kumewaweka benchi.

Zamani tuzo za Channel O ilikuwa dili yaani ukisikia msanii fulani amewahi kushinda unaona ni kitu kikubwa. Lakini mtoto kutoka Tandale, Diamond ndani ya usiku mmoja alizinyakua tatu. Hii inaonyesha kumbe hata sisi tunaweza sema basi tu uthubutu umekuwa butu.

AY pia amewahi kushinda tuzo ya Channelo O. Siyo tuzo za Channel O tu, MTV zipo nyumbani. Diamond amewahi kushinda tuzo za MTV Base na EMA. Alikiba kadhalka. Vannesa Mdee amewahi kushinda tuzo za Afrimma ambazo hutolewa kila mwaka nchini Nigeria.

Tuzo ya BET ni kubwa ambayo kwa Afrika Mashariki tuna ukame naye. Ukiitaja tuzo hiyo kwa Afrika Mashariki mbele yake litakuwapo jina la msanii wa Uganda, Eddy Kenzo.

Mwaka jana mwanamitindo Millen Magese aliitwaa tuzo ya BET kwa mchango wake kwa jamii katika kuielemisha kuhusiana na ugonjwa wa Endomitriosis.

Ushindi wa Rayvanny sio miujiza. Imetokana na uthubutu labda wa msanii mwenyewe au uongozi unaosimamia kazi zake.

Wasanii wenye vipaji sawa na Rayvanny au kumzidi wapo wengi lakini kinachowakwamisha ni hali ya kukariri kuwa wapo kina fulani wa kufanya hivyo.

Wapo ambao wamekaririshwa kuwa Diamond huwa anahonga ili ashinde tuzo. Kama hilo lingekuwa linawezekana angehonga aishinde hii maana ni kama imegoma kabisa kutua mikononi mwaka.

Mwaka jana tulishuhudia Black Coffee akimtoa kapa Diamond kwa kuinyakua. Kama angeipata sasa angekuwa anasubiri ya Grammy tu kuweka rekodi ya dunia kwa sababu tuzo kubwa zote angekuwa ameshazitwaa.

Rayvanny awafungue kuwa hakuna bahati wala uchawi katika mambo haya. Ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Kina Rayvanny wapo wengi tu sema hawajiamini.

Saturday, July 1, 2017

NDANI YA BOKSI: Dar es salaam bila King Kong...

 

By Dk Levy

Aboubakar Shaaban Katwila muite Chilla. Kama Chid Benz asingekaza yangetokea yale ya Jaffaray na wimbo wake wa ‘My Boo’. Chilla asingekubali kiitikio chache kielee elee juu ya mistari ya hovyo na vocal mbovu. ‘”Muda” bonge la wazo. Bonge la biti. Bonge la muunganiko wa sauti laini na ngumu. Kifupi ni ngoma lililotendewa haki. Wimbo usingekamilika bila Chilla na wazo la wimbo “Muda” lisingekuwa na maana kama lingeimbwa na mtu mwingine badala ya Chid Benz.

Katika wasanii ambao Diamond anamtazama kwa jicho la tofauti ni Chilla. Naamini anatamani pepo limtokee adondokee pale WCB kinuke tu. Kina Tekno na Pana wake wangejuta. Q Chilla ni tatizo sana.  Fundi. Yule ndiye picha  sahihi ya fleva za Kibongo. Wakati mwingine mtu unajiuliza amekwama wapi? Usipate jibu, na ukikutana naye akakueleza ya nyuma ya pazia unaishia kumuombea Mungu. Kamsikilize kwenye kiitikio cha wimbo wa Chid “Muda” unaweza kudhani ni msanii mpya maana zile kelele zilizounganishwa na midundo ambazo ndiyo nyingi kwa sasa huwezi kuzipata kwenye kinywa na kichwa cha Chilla.

Timing mbovu na mikwamo inayoleta stress kwa wanamuziki wengi ndo chanzo cha basi walilopanda kina Christian Bella na wenzake limuache njiani Chilla.

Bila hivyo wasingepata upenyo kibwegebwege na ‘kushaini’ kirahisi tu. Wangefanya kazi maana unapotoa kitu unamtazama aliye mbele yako. Mbele yako kuna Chilla utatoaje wimbo wa hovyo  ili utoboe?

Chilla leo hii anaingia kwenye jukwaa la wasanii ambao ni wakali kuliko ukali wenyewe lakini hawapati kile wanachostahili. Kamsikilize kwenye “Muda” maneno machache anayarudiarudia tu mtu unatamani angemaliza wimbo wote peke yake. Bahati nzuri kakutana na mtoto wa kihuni toka mitaa ya Ilala mwenye sauti yenye mamlaka na mitambao ya haja.

Hakutaka kuachwa na ladha ya Chilla katambaa naye na kuufanya wimbo kuwa wimbo na siyo jingo.

Kilichofanyika kwa Chilla na Benz ni muendelezo wa wanamuziki wa kitambo kile, kuamua kufanya kazi badala ya lawama nyingi na chuki kwa watoto wa sasa ambao wanakimbiza kama wamerogwa.

Umemsikiliza Mteule Jaymoe katika “Nisaidie Kushare”? Ni ngoma ya tani nyingi sana kuanzia ‘biti’ michano na kile anachoongelea. Yule ndiye Jaymoe halisi ambaye alitoweka kwenye “Pesa Madafu”. Wengine wanashindwa nini? Ni maswali ya watu wengi sana ambao wapo maofisini kwa sasa na kipindi kile walikuwa mashabiki wao wakiwa mashuleni.

Kuna ‘testi’ ya game ilitoweka hapo katikati kutokana na mafuriko ya staili za Kinijeria. Na wanamuziki wengi wakakaa kando kwa kushindwa kwenda na kasi iliyopo na wengine kuelemewa na matumizi ya dawa za kulevya na wengi wao ni stress tu.

Wenye stress wengi wao walijikuta wako kando ya game baada ya kukorifishana na wasimamizi wao. Bushoke katoweka kwa namna hiyo, siyo kuishiwa mashairi wala kukosa studio.

Utajiri wa sauti na uwezo wa kuandika wa Chilla ni mtaji mkubwa sana. Anachokosa ni akili ya kujiongeza iliyopo kwenye ubongo wa mtu mmoja tu kwa sasa ambaye ni Diamond. Chilla siyo kwamba kakosa usimamizi bali kakosa hata kujua tu nani anastahili kumsimamia.  Siku ubongo wake utakapoamka na kujua afanye nini na nani kwa njia ipi. Kuna watu watakimbia mji.

Jamaa mkali sana ni wale wanamuziki ambao wanaweza kuigeuza njano kuwa bluu kwa usiku mmoja.

Kasikilize wimbo wa “Taabasamu” wa Mr Blue achana na michano ya Blue na kiitikio cha Steve R&B. Kasikilize mwishoni kabisa mwa wimbo Chilla kavuruga kila kitu. Kaonyesha yeye ni nani na Steve RnB ni nani. Fundi sana na wengine watakuja kujua balaa lake mpaka siku atangulie mbele za haki. Lakini kwa sasa ni madini yanayozurula tu mitaa ya jiji la Dar we Salaam, badala ya kupishana na kina Davido kwenye maviwanja ya ndege na ‘kuselfika’ na watoto wazuri kwenye majukwaa makubwa nje ya mipaka ya Bongo.

Chilla ni madini kuliko wengi wanavyodhani. Bila ubora wa Chid Benz. Bila mitambao amazing ya KING KONG. Bila kukaza sauti na kujipindua kwa swaga kama za kwenye Jahazi na G Habashi baaaasi... yangemtokea ya Mteule Jafaray.

Miaka ya nyuma Chilla alitengeneza kiitikio cha wimbo wa “My Boo” wa Jafaray. Wakapishana kiswahili kidoogo. Chilla akabeba kiitikio chake na kuongeza maneno machache tu. Dunga amkanyongea ‘biti’ akaingiza  sauti na kuacha wimbo ujisambaze wenyewe. Ukawa mwisho wa wimbo wa Jafaray siyo kwa kutopigwa redioni bali kwa kutosikilizwa hata ukipigwa. Chilla fundi.

Kumsikiliza Chilla katika wimbo Subuhi wa  AY na FA ni zaidi ya kupokea nyongeza ya mshahara katika utawala wa Magu. Anaimba kama hataki. Hatari sana Chilla.

Saturday, July 1, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: Tusi la kikwenu linauma kuliko la kizungu

Kulikuwa na patashika ya kuingia kwenye orodha ya kuwania medali ya heshima baina ya nyota wa soka la daraja za juu. Ninaposema nyota nina maana ya nyota; siyo kimondo kinachowakawaka na kuzimikazimika. Ni zaidi ya Pele na Maradona. (Nilijua tu watu watanuna. Haya niseme zaidi ya Ronaldo na Messi).

Kitendawili kilikuwa baina ya wakali wawili waliolingana katika karibu kila sekta. Wote walikuwa sawa kwa magoli kumi ya kufunga, kadha ya kusababisha na kadha wa kadha ya kudhulumiwa kwa rafu na maamuzi mabovu. Iwapo mmoja wao angekuwa na goli moja tu la ziada, biashara ingekuwa ishakwisha.

Zoezi lilielekea kuwa gumu kwa mwaka huo. Lakini usiku mmoja kabla majaji hawajatoa tamko la kushindwa kuchagua kwa mwaka huo, nyota ya bahati ilimwangukia mmoja wao kwani alikuwa na mechi ya fainali. Akajifua na kuroga ili siku hiyo atupie japo moja tu litakalompa heshima na utajiri maishani.

Siku hiyo uwanja ulikuwa mdogo kwa mashabiki, maana waliopata nafasi walikuwa wachache kuliko waliotanda nje. Acha walioketi kando ya redio na TV.

Lakini kwa bahati mbaya mabeki wa timu hasimu walikula yamini juu ya nyota huyu. Na wao waliutaka ushindi kwa udi na uvumba. Hivyo ikawa rahisi kwa tembo kuingia kwenye shimo la panya kuliko yeye kulikaribia lango la washindani wake.

Kadiri muda ulivyoyoyoma ndivyo mzuka ulivyozidi kumpanda. Akawa anazunguka uwanja mzima: anakaba na kushambulia. Alitoka na mpira kwa kipa wake, akawapiga chenga wote bila kujali nani rafiki, nani adui. Hata ukimkata mtama hasikii: Kanzu… tobo… mbio… yeye na kipa… shuti… Dah, kagonga mwamba!

Akaona si bure. Hawa mabwege watakuwa nao walienda kuroga, tena kwa babake mganga wake.

Dakika chache kabla refa hajapuliza firimbi ya mwisho jamaa alibadilisha namba; akarudi kuwa mlinzi badala ya mshambuliaji. Kila mtu alishangaa lakini wengi walijua kuwa ameikubali hali halisi. Si wanasemaga kila ukifanya jambo na usione mafanikio, basi liache (let it go). Hadi dakika za majeruhi bado ngoma ilikuwa droo. Jamaa alionekana wazi kutojihangaisha tena, maana alikuwa akipiga danadana mbele ya kipa wake kusubiri mpira uishe.

Lakini wakati refarii anaangalia saa akijiandaa kumaliza mchezo jambo la ajabu zaidi likatukia. Jamaa yetu bila kutumia nguvu aliubetua mpira ulilojaa moja kwa moja wavuni kwa kipa wake. Wakati umati unaulizana ile sintofahamu. yeye alitokomea kusikojulikana!

Kila mtu alipigwa na butwaa. Tafsiri ya haraka ilikuwa: “huyu kaingia wazimu kwa kuikosa ile medali”. Lakini wenye akili wakabaini kuwa jamaa anakwenda kudai medali yake; si ameshafunga goli la ishirini na moja? Aisee watu walimfuata kwa mawe na magongo lakini hawakumpata. Tangu siku hiyo hakuonekana tena.

Ni sawa kuwa jamaa sasa aliongoza kwa goli moja la kufunga. Lakini lilikuwa goli sahihi?

Kila mtu anapaswa kufanya jambo ili maisha yaendelee. Lakini ni jambo la msingi pia kujua ni jambo gani, alifanye wakati gani na ni kwa nini anafanya jambo hilo. Maswali yote hayo huleta jibu la matokeo hasi au chanya baada ya kufanya jambo.

Wazungu wanasema “In every action there is a reaction”. Nadhani usemi huu ulitokana na utafiti wa bingwa wa fizikia, Sir Isaac Newton. Yeye alithibitisha kuwa maada yoyote itabaki katika hali yake hadi patokee nguvu ya nje na kuisumbua maada hiyo.

Nguvu inayotingisha maada inaweza kuwa nzuri au mbaya bila kujali ukubwa wala kasi yake. Unakumbuka mabishano baina ya upepo na jua? Walinuia kumvua mtu koti lake. Upepo ulizua tufani hadi kumwangusha mtu bila kufanikiwa. Lakini jua liliposababisha joto, mtu alivua koti bila shuruti.

Jamaa yetu alishatumia nguvu nyingi (maximum force) kwa muda mrefu bila kufanikiwa kuwainua watu uwanjani. Lakini katika dakika ya mwisho alipotumia nguvu ndogo (minimum force) alibadili hali ya hewa na kusababisha watu kumkimbiza ili wampe adhabu anayostahili mwizi.

Niliiona hali kama hii utotoni. Sisi watoto wa mjini tulivamiwa na jeba moja lililotoka bara. Inasemekana lililetwa kuja kuanza masomo wakati ule wa “hata kama umetimu miaka ishirini, lazima uanze shule”. Ukweli lilituzidi katika kila idara; lilienda hewani na lilikuwa mbavu nene zaidi ya sote kwa pamoja.

Mpirani lilikuwa maarufu kwa kupiga madochi. Sasa ukirogwa kulibambikia ndugu yangu, kazi unayo. Utakula makonzi hadi ukitingisha kichwa usikie kuchukucha kama nazi vile. Jamaa lilitutesa bila huruma hadi kalipoibuka kadogo janja kalikotoka naye kijiji kimoja.

Siku moja kwa bahati mbaya dogo aliikata manati ya jeba. Mwenyewe alipopata taarifa alikuja kama ngiri, akamnyakua yule dogo kwa hasira hadi tukajua atammeza bila maji. Ajabu eti yule dogo alikunja mikono kifuani na kuendelea kumtazama usoni kwa dharau.

 Jeba lilipoinua mkono kukunja konzi, dogo aling’aka kwa kilugha chao. Jeba likashtuka na kumwachia. Dogo akaongeza neno linguine la kilugha. Tukaona jeba hilooo linaondoka na machozi yakililenga! Niliamini kweli tusi la kikwenu litakuuma kuliko la Kizungu. Nguvu ndogo inaweza kuleta makubwa kutegemea matumizi yake tu.

Saturday, June 17, 2017

Gabo: Najengea daraja la kuelekea mafanikio mawe tunayopigwa

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. “Aliyeanzisha virusi kwenye simu, kompyuta, bila shaka alitafuta suluhisho la virusi hivyo akapata tiba yake (anti virus).

“Kwa sababu waigizaji ndiyo chanzo cha kufika hapa filamu zilipo, hatuna budi pia kutafuta suluhisho la tatizo, ” Hivyo ndivyo anavyoanza kueleza mwigizaji Gabo Zigamba.

Gabo anasema mashabiki wa filamu licha ya kupenda burudani wamechoshwa na mambo yanayotokea katika kazi hiyo iliyokuwa kivutio cha wengi.

Anafafanua kuwa wasanii wamesahau kuwa wanapimwa kwa kile wanachokifanya wakalewa majina jambo ambalo limeifikisha filamu hapa ilipo.

Anasema hataki kuelekeza lawama kwa yeyote miongoni mwao anachotamani kukiona ni kila mmoja kwa wakati wake anatafuta suluhisho la tatizo walilonalo.

“Kuna wanaosema hawaigizi tena, kuna wanaosema soko la filamu limevamiwa, hiyo siyo dawa, tunachotakiwa kufanya ni kufikiria kwa mapana yake nini tufanye ” anasema Gabo.

Gabo anasema kwa kuanza alipata wazo la kukutana na mashabiki kwa muda mfupi popote pale walipo, swali likawa anakutana nao vipi na siku hizi hakuna majukwaa ya kibisa?

Anasema akafanya utafiti mdogo kuona ni kitu gani kinawakutanisha watu wengi kwa wakati mmoja, akabaini ni mitandao ya simu.

“Nikaona hiyo kwangu ni fursa, nikakusanya mawe tunayopigwa kwa pamoja na kujenga daraja kuelekea kwenye mafanikio.

“Hatimaye nakutana na mashabiki wangu kupitia App ya Uhondo, filamu ya “kisogo” ni mwanzo tu zinakuja nyingi kama mvua, mashabiki wake mkao wa kula, ” anasema.

Anasema anavyowafahamu Watanzania wanapenda burudani na kuthamini vya kwao, isipokuwa wanahitaji kilicho bora zaidi ndiyo maana wamewaletea filamu hiyo fupi.

Anaeleza wazo lilikuwa ni kutafuta kuondoa manung’uniko kuhusu Bongo Movie, kwa kufuta makosa na kufanya kitu kitakachowavutia watizamaji na kuleta heshima.

Anasema filamu fupi zitakuwa na mashabiki wengi kutokana na kutotumia muda mwingi wa mtizamaji.

“Mwezi wa saba tunaweza kutizama bure iwapo mambo yatakwenda kama tulivyopanga na ifikapo mwezi wa nane nitaanza kuweka na tamthilia, kidogo kidogo hadi nitafika ninapopataka, ”anasema Gabo.

Anasema dunia imebadilika kuendelea kulaumu na kusubiri dunia irudi nyuma na kufanya vitu vile vile itabaki kuwa ni ndoto, hivyo la maana ni kuangalia jinsi ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya teknolojia.

Anafafanua pamoja na manung’uniko ya filamu kuwa na kiwango cha chini, kushuka kwa soko, bado ni ukweli usiopingika kuwa changamoto ya teknolojia inachangia kwa kiasi kikubwa.

Anasema ni ngumu kumlazimisha mtu aende kununua filamu kama hana nafasi hata kama ni nzuri kiasi gani, ilihali muda mchache anaoupata anaweza kufungua simu, kompyuta na kuona filamu zenye kiwango kutoka kila pembe ya dunia.

“Changamoto zipo nyingi, makosa yetu yapo mengi, jawabu la yote ni kujituma, kufikiri upya.

“Inawezekana walikuwa wakishangaa nguo nzuri walizokuwa wakivaa waigizaji hapo nyuma, na wao sasa wanazo, wanahitaji kuonyeshwa kitu kingine watakachoshangaa na kuvutiwa kutizama filamu zetu ” anasema.     

Saturday, May 27, 2017

Wasanii waanze kujifunza kuweka na kurekebisha taarifa mitandaoniJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

By Julieth Kulangwa

Wasanii wakubwa huwa wanachukua hatua pale anapoona mtandao au chombo cha habari kimetoa taarifa inayopotosha uhalisia.

Huwa wanalazimisha ziondolewe au marekebisho yafanyike. Huku ni kujijenga. Sina hakika na alichokifanya Benpol hivi karibuni kwa kuweka picha yake akiwa mtupu kama kinamjenga.

Miongoni mwa mambo mengi yanayowaangusha wasanii ni namna ya kutojua kutumia majukwaa mengine ili waendelee kudumu katika kazi ya sanaa. Wanamuziki wanaamini akisharekodi wimbo na kutoa video kazi imeisha.

Akimaliza kurekodi wimbo na video atazunguka katika vituo vya redio na televisheni kufanya promo baada ya hapo atakaa chini akisubiri mialiko ya matamasha.

Wanasahau kuwa majukwaa ya kujitangaza ni mengi na kila moja lina mbinu zake. Mbaya zaidi hawataki kujifunza au kujiuliza kwa nini fulani amefikia hapo.

Ukifuatilia kwa ukaribu hasa katika magazeti utaona wasanii wanaoandikwa ni wale wale kila siku na huenda unajiuliza inakuwaje hili linatokea.

Ukweli ni kuwa wasanii hawa ndiyo wale wanaofahamu umuhimu wa kuandikwa, iwe kwa uzuri au ubaya.  Hivi Kim Kardashian au Paris Hilton unaweza kuwaeleza tofauti ya kuandikwa kwa uzuri na ubaya? Umezuka mtindo hapa nchini pia wa wasanii kujitengenezea matukio mabaya au kutunga stori mbaya kuwahusu ili wazungumziwe.  Hapa ndiyo utakubaliana nami kuwa kuandikwa kwa mabaya au mazuri kote kuna faida.

Wapo wasanii ambao hawajui kutumia nafasi na pia ni kitu ambacho hakipo katika programu zao za kila siku. Kwa mfano msanii hajui umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii au gazeti kujikuza kisanii.

Wasanii wanaoandikwa ni walewale kila siku kwa kuwa ndio wanaopatikana na pia picha zao zinapatikana kwa urahisi. Unaweza kutafuta taarifa za msanii fulani kwenye mitandao au picha bila mafanikio.

Taarifa za msanii na picha vinapopatikana kwa urahisi ndivyo visababishi vikuu vya kuona wanaoandikwa ni walewale kila siku ndani na nje ya nchi.

Wasanii wanaotoa nyimbo nzuri na video ni walewale, mwisho wa siku huonekana wanabebwa lakini juhudi zao zinawafanya waonekane kila kukicha. Wajifunze kuwa ili uwe msanii ni lazima ukamilike kila idara. Kama taarifa zako zinatafutwa kwa tochi wewe ni ‘underground’.

Saturday, May 27, 2017

NDANI YA BOKSI: Tunasubiri wastaafu, wafe tuwape wanachostahili?

 

By Dk Levy; salaamzao@gmail.com ; 0744053111

Kuna wapendwa wetu wengi ambao tumebaki nao kwenye dunia hii kupitia sauti tu. Video ama maandishi yao. Ardhi inameza sana watu. Dogo Mfaume kishatangulia. Alipigania uhai wake kwa kupambana kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

Mpaka mauti yanamfika alikuwa ‘sobber house’, na aligoma kuondoka pale kurudi kitaa. Aliamini kuwa akirudi kitaa atashindwa kukwepa ushawishi wa kurudia tena ‘uduwanzi’ wa kubwia unga.

Alitaka kuwa salama. Na Mungu akataka awe salama zaidi kwa kumchukua jumla. Dogo Mfaume hatutamuona tena katika uso wa dunia hii.

Unaposoma hili andiko mchizi yupo ardhini kazungukwa na udongo. Mungu ampumzishe mahala anapostahili. Ameni.

Ni karibuni tu tumepoteza wadogo zetu huko Karatu kwa ajali ya gari, kifo tumeumbiwa na ni lazima kila mtu atakufa. Ila njia ya kupata umauti hutofautiana.

Mungu awape wapesi wale watoto majeruhi wanaoendelea na matibabu Marekani.

Kabla yake Dogo Mfaume, kuna wasanii wengi sana ambao walitangulia mbele ya haki lakini kabla ya umauti wao tuliwachukulia poa poa tu.

Walipoondoka jumla kwenye mboni za macho yetu kila mtu akajivisha ushahidi wa mema yao. Kila mtu alisifia na kufafanua ubora wa Ngwair, uwezo wa Kanumba, ukali wa Sharomilionea na wengine.

Lakini kabla ya mauti yao hakuna aliyesema sifa zao kwa kiwango sawa na kile baada ya mauti yao.

Tuache kusubiri wafe ndipo tuwasifie kana kwamba kutoa sifa kunaweza kuwarejeshea pumzi zao. Unafiki na akili za Waswahili ni kama mvua na Krismasi. Ni kulwa na doto. Hakuna sababu ya kusubiri afariki ili usifie uwezo wa kuandika wa Mwana FA kwenye muziki wa kizazi kipya.

Kutoka enzi za kina Miriam Odemba, Miriam Ikoa, Happyness Magesse mpaka katika utawala wa Flaviana Matata, Gigy Money, Lulu Diva, Linnah na kina Ruby. FA kaendelea kuwepo katika ubora ule ule.

Wako wapi waliokuwa na JB na Richie Richie, kwenye Mambo Hayo? Wao wameendelea kukomaa na sanaa kwa kiwango cha juu huku wakiutawala uwanja mbele ya wasanii wengi wapya. Lakini hizi sifa huwezi kuziona kwenye vinywa vya waswahili hawa jamaa wakiwa bado hai. Wanasubiri watangulie ndipo wamwage sifa nyingi, huku wengine wakishindana kwa mavazi na miwani ya giza misibani.

Ukitaka kujua kazi za msanii Bongo. Na ukitaka kumuelewa kwa mapana msanii wa Kitanzania. Subiri afariki.

Utajua kila kizuri chake na kuaminishwa kuwa hakuna tena kama yeye. Kabla ya hapo akiwa hai utayajua mabaya yake yote ya kweli na ya kusingiziwa.

Ufalme Bongo huletwa na waswahili baada ya mswahili mwenzao kufariki.

Akiwa hai huwezi kujua thamani yake. Huwezi kusikia kazi zake wala huwezi kuelezwa msaada wake kwa jamii inayomzunguka. Ndivyo ulivyokuwa kwa Ngwair. Wengi walijua ufalme wake na mengi juu yake baada ya kufariki. Alipambwa kila kona na nyimbo zake kupigwa kila dakika.

Wakati tayari tuliaminishwa na hao hao wapambaji kuwa amekwisha na hana jipya. Ndivyo ufalme ulivyokuwa hata kwa Kanumba, alikwezwa zaidi baada ya kufariki.

Kabla hajasukumwa usiku ule na kupelekea kufariki dunia, unadhani Kanumba alijua kuna watu wanaweza kuzimia kutokana na mapenzi yao kwake?

Aliishi kama msanii na kutambua ana thamani ila si kwa kiwango kile cha sifa za baada ya kufariki.

Unadhani marehemu Albert Mangwair alikuwa na uhakika kama bado thamani na ubora wa nyimbo zake unathaminiwa kwa kiwango hiki? Unadhani alikuwa anajua kama Mablogger wengi walikuwa wanajua uwezo wake kwa kina na kupelekea kuupamba kwa namna waliyompamba?

Wasanii wengi wana thamani kama hizi ila hatuzisemi na matokeo yake tunasubiri wafe tuseme. Wakifariki tunajivisha urafiki kwake na kujisingizia kuwa tuliwasiliana naye saa moja kabla ya mauti yake.

Unadhani baada ya kifo cha Kanumba hakuna msanii mkali mwingine wa filamu mwenye kuhusudiwa na kuthaminiwa kwa namna ile? Ila nani anasema?

Nani anaweza kusimamana na kuusifia uwezo wa Jacob Stephen katika upana na ubora wake? Tunaendelea kusemea chumbani kuwa jamaa mkali ila yakitokea ya kutokea kila mmoja atataka kusema. Wakati mwingine inauma sana kufa bila kujua thamani yako halisi.

Miezi kadhaa kabla Ngwair hajatangulia, tulimpita na tukadiriki kumbania nyimbo zake na wakati mwingine tulisema kachuja.

Ila vipi baada ya kifo chake? Hata zile redio zilizopiga nyimbo zake mwaka 2012 kwa mara ya mwisho zilipiga nyimbo zake saa 24, tena wakimwita mfalme. Inauma sana. Thamani hii anaipata akiwa katika maisha mengine kabisa! Akiwa chakula cha funza na mifupa kuwa sehemu ya udongo.

Leo kila mtu anamsema Diamond katika namna isiyofaa. Anaitwa mchawi, atasemwa hili atasemwa na lile. Ila ni nani anasema uwezo wa kuimba wa Diamond?

Nani anamtaja kama msanii aliyefanya mapinduzi katika suala la malipo na ubora wa shoo? Nani anapoteza muda wake kusema Diamond kaivusha boda Bongo Fleva kuliko yeyote hapo kabla? Hakuna!

Ila kama ingetokea la kutokea kila mmoja angemsema vizuri na kumuita kila jina bora analotamani kuitwa sasa na asiitwe.

Wakati mwingine ni vyema tukajifunza kutoa pongezi wakati huu bado wanatumia pumzi zao, tukiwa nao mitaani, tukiwatazama majukwaani na runingani.

Kama tunavyosahau mabaya yao wakifa, pia wakati mwingine tutoe pongezi wakiwa bado wako hai.

Ndiyo, tuwakosoe ila pia tuwapongeze inapobidi. Kama ilivyo sasa kwa nini usitoe pongezi kwa mtu kama Ray? Mtu kama JB, mtu anayeonekana kama anatembea na ufunguo wa soko la filamu? Wanafanya vizuri na wanafaa kupongezwa.

Leo vijana wengi wanatamani kufanya muziki. Unajua kwa nini? Wengi wameguswa katika nafsi zao na uwezo pamoja na mafanikio ya kina Diamond.

Kama kina Nature walivyofanya kina Godzilla kurap ndivyo umahiri wa akina Diamond unavyofanya leo kina Rayvanny wafanye wanachokifanya. Sasa kwa nini tusiwape sifa wanazostahili kwa wakati huu? Najua katika mioyo ya wengi kuna thamani na ubora wa Nature. Najua katika upande wa ukweli watangazaji wengi wanajua umuhimu wa kupiga nyimbo za Lady Jaydee. Ila kwa nini sasa hawapigi?

Tuache unafiki, tuishi katika dunia ya kweli na haki. Ni vyema kila anayestahili kupewa na apewe. Hii imekuwa sifa kuu ya Wabongo. Hata Jakaya Kikwete ubora wake tunauona baada ya kupumzika Msoga.

Alipokuwa Magogoni na lile tabasamu lake tulimtupia kila aina ya neno lisilofaa. Tulimuonea vya kutosha. Akatuacha. Tunamtamani leo.

Ilikuwa hivyo kwa Mkapa, kwa Mwinyi na mtangulizi wao Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Wote baada ya kustaafu tukaona umuhimu wao.

Haifai kuacha kupiga nyimbo nzuri ya Nature. Kisa? Jamaa yuko katika game kitambo apishe na wengine. Haifai! Anayestahili na apewe.

Kuna mengi yanazungumzwa baada ya vifo vya wasanii. Kama ni ya kweli kwa nini katika uhai wao wasipewe sifa hizo?

Dogo Mfaume ukikutana na Ngwair mpe sifa alizopewa baada ya kifo chake ajue thamani aliyoiacha nyuma yake. 

Saturday, May 27, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: Mchango wa harusi umejengea choo?

Nilisema, ninasema na nitasema daima kuwa panya anatuzidi akili kwenye chakula. Anajua na kuheshimu sana virutubisho kuliko harufu au nakshi ya chakula hicho. Mfano hai utauona kwenye ghala la mahindi lililotembelewa na panya.

Mwenyewe utajipa moyo na kusema “Akh! Wajinga wakubwa. Wamedonyoa donyoa...” Lakini kumbe wenzio ndo washakula. Wanadili na vikonyo na magamba tu ambavyo ndivyo vinavyobeba utajiri wa chakula, na kukuachia boya la chokaa.

Kinyume chake hata panya asipofanya ziara ya kushtukiza humo ghalani, binadamu kwa hiyari yake hukoboa mahindi (kuondoa gamba na kikonyo) na kula ile chaki iliyobaki! Pengine anapendezwa na ugali mweupe kama pamba.

Katika miaka ya 1980 tuliletewa msaada wa mahindi ya njano wakati tulipokumbwa na kinenge. Watu waliokuwa na uwezo au nyadhifa waliugomea ugali wa “yanga” kwa kuamini siyo wa hadhi yao. Wengi ni wale wanaoamini kwamba paka mweusi ni mchawi na mweupe ndiye rafiki. Au malaika ni weupe kama theluji bali shetani ni mweusi kama mkaa. Imani kitu cha ajabu sana!

Lakini wataalamu wa chakula walikuja na ukweli wa kushangaza. Walisema kulingana na tafiti zao, ukiguguna pande moja kubwa cha muhindi wa njano uliochemshwa unapata gramu nne za protini, 3.5 za ung’ong’o (nyuzi) lishe, 30 za wanga, 1.5 za mafuta, 3.6 za sukari na 100 za maji.

Kwa maana hiyo ukila ugali wa njano, hata kama umelumagia picha ya nguru bado utakuwa juu zaidi ya aliyekula chipsi yai miksa na kuku.

Ukweli huu unathibitisha kuwa binadamu anaishi kwa imani. Haiwezekani kula chaki (unga wa kukoboa) kwa samaki wa maboksi au viazi kwa mayai yasiyo na baba halafu bado ukaishi. Wengine wanakula mchele uliotengenezwa kwa tambi na kuku asiye na wazazi lakini anaendelea kunenepa tu.

Ni maajabu ya imani. Inaeleweka kuwa mgonjwa anayedanganywa kuwa afya yake inaimarika anaweza kuishi zaidi ya yule anayeambiwa ukweli kuwa afya yake inazidi kuporomoka.

Lakini imani ina uzuri na ubaya wake. Kule Mashariki ya Kati kulipandikizwa imani za chuki baina ya koo mbili. Tangu akiwa mdogo, mtoto wa Kiyahudi alifundishwa kulenga shabaha juu ya picha ya Mpalestina. Upande wa pili nao ukafanya vivyo hivyo. Babu wa babu zetu walishuhudia, na vining’ina wa kizazi hiki kama watakuwepo basi watashuhudia vita ya ndugu hawa isiyo na mwisho.

Mafundisho ya imani za mila, desturi na dini za pande zile mbili yalisisitiza chuki dhidi ya adui; kwani ni machukizo kwao, kwa wahenga na hata kwa Mungu. Katika hali ya namna hiyo, usipofuata mafundisho hayo nawe unageuka kuwa chukizo!

Silaha hii bado ingali inatumika kwa nguvu nyingi kwenye nchi changa (kiuchumi) kama yetu. Wapo viongozi wanaotumia mchezo mchafu wa kuwapotosha raia wao imani. Mtu anaanza kuwagawa watu kwa fedha, dini na ukabila ili kupata kundi atakalolifunga nira na kulipeleka atakako.

Watu werevu wanapoona hali hii, huanza kuwatahadharisha wenzi wao kuwa “huko tunakokwenda siko”. Lakini haraka wale viongozi wasio na weledi huwatangaza werevu hawa kuwa wachochezi na wanaokusudia kuleta vita.

Hakuna mtu anayeweza kuhimili kuona watoto wake wakiuana na kutiana vilema katika vita. Hivyo haraka anajitenga na werevu kwa nia ya kuepusha majanga. Ni afadhali kuongopewa kuliko kuletewa vita. Na kwa vile imani hufunga macho, masikio na hisia. Yule mwerevu akisema “Unapelekwa korongoni” hutakubali kufumbua macho.

Matokeo yake kunakosekana ushirikishwaji. Yanakuwa maamuzi ya mmoja na majibu ya ‘ndiyo’ na ‘sawa’ kutoka kwa umma.

Hata kama katiba na sheria zitavunjwa, kitendo cha kuhoji kitakutupa kwenye kundi la ‘machukizo’.

Kwa bahati mbaya viongozi wetu wanafanya kazi kwa mazoea. Wanaamini raia ni kuku wa kuchinjwa alfajiri, hawahangaiki kukimbizana naye. Wameshatufukisha imani za kutosha, sasa wamefikia mahala pa kutuamulia jinsi mpya ya kuishi nyumbani kwetu hata kama mila na desturi zinakiukwa.

Sisi tunajua kuishi kama jamii bila kuvunja sheria. Hatuvunji sheria tunapopeana zawadi, misaada, hongera na pole. Kama ndugu, tuna kawaida ya kushirikishana kwenye shughuli zetu. Iwapo ninatarajia kumuoza mwanangu, nitasambaza jumbe kwa ndugu, jamaa na marafiki, ili tukijaaliwa tumsherehekee kwa pamoja kijana wetu.

Wapo watakaonipa michango ili kufanikisha shughuli hiyo adhimu. Najua kwamba nikisema “Asanteni lakini michango yenu nimekarabati choo cha shule” nitachafua hali ya hewa. Maadamu nilichangisha kwa minajili ya kufungisha ndoa, basi ilibidi nifanye hivyo japo shule ni kitu cha msingi zaidi.

Hili lililotokea Arusha limenishangaza sana. Nikadhani Wameru na Wamasai wana tamaduni tofauti na zetu. Iweje watu watoe rambirambi kwa wenzi wao baada ya msiba mkubwa wa wanafunzi, walimu na dereva, kisha mamlaka ziamue kutumia rambirambi hizo kukarabati Hospitali?

Tunaamini mfarijiwa ndiye mtu wa mwisho katika maamuzi ya faraja anazopewa. Kama Serikali ya Mkoa ilishindwa kuliombea fedha tatizo lao kutoka Serikali kuu, ingetangaza harambee nasi tungeichangia. Lakini siyo kwenye kampeni mnatuahidi ukarabati kisha mnangojea watoto wetu wafe ili mje kukamatia rambirambi.

Mmeitia doa Serikali yenu iliyoweka rekodi nzuri ya kukusanya kodi kwa maendeleo ya wananchi wake.

Saturday, May 20, 2017

Kama Bongo Movie vile, Bongo Fleva nayo inaanza kurudi ilipotokaJulie Kulangwa

Julie Kulangwa 

By Julie jkulangwa@mwananchi.co.tz

Wimbi la kutegemea video nzuri kuwa zitaubeba wimbo linaanza kupungua kasi. Kama wimbi hilo liliweza kupindua meli basi sasa linaonekana hata mashua itakuwa kazi ngumu kuizamisha.

Miaka miwili au mitatu nyuma ulizuka mtindo wa wasanii kutegemea video kuzibeba nyimbo zao, lakini kwa mifano michache tu ya hivi karibuni utaona utamaduni huo unaanza kufa.

Wiki mbili zilizopita Darassa baada ya kusumbua sana na wimbo wake Muziki, alitoa mwingine Hasara Roho. Niliwahi kuandika hapa kuwa mwanamuziki huyu ana deni kubwa pengine kuliko wasanii wote kwa mashabiki wake.

“Muziki” ulikuwa wimbo wa taifa uliotambaa na kuambukiza nchi jirani. Ukweli ni kwamba kama kuna mtu ametengeneza fedha katika kipindi hiki ambacho wengine tunalia njaa ni Darassa. Nyomi lake katika kila kiwanja au nchi anayotia miguu halikuwa la nchi hii.

Turudi kwenye wimbo mpya wa Hasara Roho. Ukweli haifikii viwango vya Muziki kwa kila kitu na mbaya zaidi sasa hivi sisi mashabiki tunausikiliza huu mpya kwa kuulinganisha na uliotangulia. Labda angeyajua haya angeutanguliza Hasara Roho halafu Muziki utoke sasa. Yote kwa yote muziki ni biashara ya kubahatisha. Alipotoa wimbo huo kuna mtu nilimsikia akisema baada ya kuusikiliza: “Si mkali lakini ngoja niisubiri video.” Video ni nzuri lakini ukweli ni kuwa tumeshazoea kuona vitu vya aina hii.

Wasanii wa WCB, Rich Mavoko, Harmonize na Rayvanny wametoa nyimbo mfululizo na kama kawaida yao ni safi kama jina lao, lakini je, video zimewasadia kwa kiasi gani kuzikuza nyimbo zao?

Bongo Movie imetoka huko sasa wanalazimishwa kurudi katika misingi yake. Walijisahau wakiamini kuwa sura yenye mvuto, picha zilizopigwa vizuri zinaweza kuwafanya washindane na japo Nollywood…imeshindikana.

Sasa wanaambiwa kuwa wakitaka kufanya vizuri sokoni lazima wawe na hadithi nzuri iliyopangiliwa kwa ustadi, picha zilizopigwa vyema na sauti isiyoumiza masikio au kumlazimisha mtazamaji akae karibu na rimoti yake.

Niionavyo Bongo Fleva inaanza kurudi kwenye misingi yake kwamba wimbo mzuri ndio kila kitu. Mashabiki wanaanza kupotezea video au tuseme nazo zimefika mwisho wa ubunifu wake. Hata mwanamuziki ‘underground’ naye anakwenda Afrika Kusini kurekodi video. Imekuwa kawaida sana. Sana.

Saturday, May 20, 2017

Dakika 10 za uso kwa uso na Future

 

Rapa wa Marekani, Future atatua Bongo mwaka huu na kutumbuiza Julai 22 katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Future ni msanii ambaye kwa sasa anawika zaidi duniani kote na mtindo wa kurap kwa kuzungumza maarufu kama Trap. Mtindo ambao baada yake kumekuwa na wasanii wengi wameamua kufanya muziki kwa namna hiyo kiasi kwamba sasa Future anaonekana kama ndiye muanzilishi.

Mtandao wa E ulifanya mahojiano katika kipindi cha Ten Minute With a Star na haya yalikuwa mazungumzo yao:

Wakati unaandaa albamu yako ya Hendrix hukuwa ukiposti picha kwenye mitandao ya kijamii wala ukiandika chochote kwa ajili ya mashabiki wako. Inadaiwa uliachana na matumizi ya mitandao kipindi hicho. Je, hili lina ukweli.

Ni kweli, nilifanya hivyo kwa sababu nilikuwa nahitaji muda wa kutosha kwa ajili ya kufikiria mambo mengine, kufikiria cha kuandika katika nyimbo zangu na kufikiria jinsi ya kufanya kitu kipya na bora.

Unajua, mitandao ya kijamii ni mizuri lakini inatafuna muda mwingi, unapotaka ku-post picha ni lazima utumie muda kuipiga na kuandika ‘caption’, kabla picha haijaenda kwenye mtandao. Kwa hiyo niliamua kupumzika.

Kama mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii. Ulijisikiaje kuacha kuitumia kwa muda?

Kwangu ilikuwa ni kitu kizuri kwa sababu sikuwa nikihitajika kumjibu yeyote aliyeandika kitu kuhusu mimi, wala sikuwa nikihitaji kuandaa kitu chochote kwa ajili ya kuzungumza na mashabiki wangu. Zaidi nilikuwa napata muda mwingi wa kuwa studio, muda mwingi wa kuwa na watoto wangu na familia kwa ujumla.

Kwa nini umeamua kuiita albamu yako jina la msanii mwingine?

Unamzungumzia Hendrix sio? Ni kwa sababu namkubali Jimi Hendrix, napenda alichokuwa anakifanya enzi za uhai wake, alikuwa ni nyota ingawa watu wa asili yake (weusi) hawakutaka kukubaliana na hili.

Na hicho ni kitu kinachonifanya nijione kama tunafanana hivi kwa sababu naamini nafanya vitu vikubwa, ila kuna watu hawataki kukubaliana na mimi, wengine wanadai nimeuharibu muziki kabisa kwa hiki ninachokifanya.

Ni msanii gani ambaye huwa unamsikiliza sana?

Mimi huwa simsikilizi msanii yeyote, huwa najifunza muziki tu. Na huwa najifunza kupitia kusikiliza muziki mzuri uliofanikiwa kibiashara bila kuangalia ni nani aliyeimba. Nasikiliza mistari, midundo, melodi na kila kitu?

Nini malengo yako kwa siku za usoni?

Nimepanga kuacha kila kitu kuhusu muziki katika siku za usoni, nitakuwa nafanya mambo binafsi tu. Na ndio maana kwa kipindi hiki najitahidi sana kufanya kazi kwa bidii ili muda wa kuachana na muziki ukifika niwe nilishajenga msingi imara na niweze kusimama kiuchumi.

Saturday, May 20, 2017

Muziki na siasa ni ndugu mojaMsanii Roma Mkatoliki

Msanii Roma Mkatoliki 

By Ericky Boniphace, Mwananchi

Wakati mashabiki na wasanii wakisubiri hatma ya tukio la utekaji wa wasanii Roma Mkatoliki, Moni Centrozone na Imma, hili ni pigo lingine kwa msanii mwenye wazo au aliyerekodi nyimbo zenye ujumbe wa siasa kutokana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwataka wasijihusishe na siasa.

Dk Mwakyembe ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Nape Nnauye alitoa tamko hilo alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule ambaye pia ni mwanamuziki maarufu kwa jina la Profesa J, kuhusu unyanyasaji wa wasanii wanaoimba nyimbo za siasa.

Kauli ya Dk Mwakyembe imeibua hoja katika mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa wasanii kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kisiasa ambapo baadhi ya wadau na mashabiki wanakiri kauli hiyo itabana uhuru wa wasanii katika kazi zao huku wengine wakihoji ni siasa gani ambazo wasanii hawapaswi kujihusisha.

Binafsi naungana na kundi la watu wanaohoji kuhusu utata wa kauli hii kuingilia uhuru wa msanii suala lililofanya nijiulize mara kadhaa kwa nini sasa? Kwa nini umuhimu wa wasanii kutojihusisha na siasa uonekane sasa? Ni kipi hasa kimelazimu Waziri kutoa kauli hii? Au ni mafanikio ya wasanii wasioimba muziki wa siasa kama anavyodai?

Alipokuwa akijenga hoja hii Dk Mwakyembe alisema hakuna msanii aliyefanikiwa kwa kuimba siasa huku alimtaja Fella Kuti pekee kama msanii aliyeimba muziki wa siasa lakini aliishia pabaya. Imenishangaza Waziri kusahau kuwa Mbunge aliyemuuliza swali hilo Joseph Haule ndiye muasisi wa nyimbo za siasa hasa kwa tungo zake za ‘Ndio Mzee’ , Nang’atuka na ‘Sio Mzee’ zilizobadilisha mtazamo wa jamii kuhusu muziki wa kizazi kipya. Je, Profesa J sio mwanamuziki mwenye mafanikio au Waziri anapima vipi mafanikio ya msanii?

Ni siasa zipi hasa Dk Mwakyembe anataka wasanii wasijihusishe ikiwa chama chake cha CCM kinachoongoza dola kinamiliki bendi ya muziki inayotunga nyimbo zinazosifu siasa za chama hicho, kwani wale sio wasanii? Kama ni sawa kwa msanii kuimba nyimbo za kusifu uongozi kwa nini isiwe hivyo wanapohoji utendaji wa kazi za viongozi hao? Najua Mwanasiasa si mwenye ukamilifu usiohitaji kukosolewa hivyo wasanii waachwe wafanye kazi yao bila kuchaguliwa nini cha kuimba bali wasimamiwe katika maudhui ya nyimbo zao na ndio maana kuna Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Kuna mifano mingi ya wasanii waliofanikiwa kwa kuimba tungo zenye ujumbe wa siasa, mwaka 2012 msanii Roma Mkatoliki alikuwa miongoni mwa wasanii waliofanya shoo nyingi nchini kuliko wengine na ndani ya mwaka huo alikabidhiwa tuzo ya Wimbo bora wa mwaka na Mwanamuziki bora wa Hip Hop katika tuzo za Muziki za Kilimanjaro kupitia wimbo wa Mathematics wenye maudhui ya siasa na utawala.

Ukitaja wasanii waliofanikiwa kimuziki nchini huwezi kumuweka pembeni Nay wa Mitego katika orodha hiyo, ni juzi tu Mwanamuziki wa nchini Marekani Katy Perry ameachia wimbo wa ‘Chained to the Rhythm’ unaofanya vizuri sokoni licha ya kuwa na ujumbe unaopinga siasa za Rais wa taifa hilo, Donald Trump.

Hata hivyo, nimkumbushe Waziri mafanikio ya msanii hayapimwi kimasilahi pekee, Muziki wa Hip hop una uzao tofauti ‘Genre’ kama Conscious, Rap na Trap katika Conscious ‘ngumu’ msanii hulenga kufikisha ujumbe katika jamii kuhusu mtazamo fulani alionao hapa msanii hutumia kipaji chake katika uchoraji wa mashairi kuliko kubuni mdundo na melodi ambavyo vina mvuto katika muziki wa biashara. Wasanii wanaofanya aina hii ya muziki ni kama Common wa nchini Marekani, Niki Mbishi, One the Incredible pamoja na Solo Thang katika wimbo wake wa Miss Tanzania.

Rai yangu kwa Waziri Mwakyembe, msanii hafanikiwi kwa kutokuimba siasa bali ni ubunifu anaoutumia katika kazi zake ndio utakaompatia mafanikio, kumchagulia msanii nini cha kuimba ni kubana uhuru wake utakaosababisha kuua vipaji vya wasanii wengi ambao asilimia kubwa ni vijana wanaotegemea kupata kipato kupitia muziki.

0755068131

Saturday, May 20, 2017

HEKAYA YA MLEVI : ‘Buta nikubutue’ si suluhuGASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Kabla sanaa na michezo kuwa kazi ilikuwapo kwa ajili ya burudani tu. Ilifanywa wakati wa mapumziko ya kazi au baada ya kazi. Hakukuwa na viwanja maalumu, hivyo mchezo uliweza kuanzishwa kondeni, shambani kiwandani muda ambao watu wanapumzika. Wanaporudi kazini waliuacha mchezo ukiendelezwa na watu wengine.

Mpira ungeweza kuanzishwa Januari pale Keko ukaenda kuisha Desemba huko Kitonga kwa kutumbukia korongoni. Najua mnashangaa. Lakini ni lazima muelewe kuwa hakukuwa na timu; Wewe uliye Msamvu unaupokea kutoka Chalinze, ambako waliupokea kutoka Ubungo. Tuache hayo.

Ukitaka kuwa mshindi usiwaze kupaa, ila fuata nyayo za washindi. Yeyote aweza kuwa nyota kwenye jambo kama ataiga mafanikio ya waliomtangulia. Muhammad Ali alimfuata Sugar Ray na alifanikiwa kumkaribia kama si kumzidi. Michael Jackson alimkopi Elvis Presley kuanzia kuimba hadi kujikoboa sura. Lakini alifanikisha malengo yake.

Sijawahi kusikia kiongozi yeyote anayefuata nyayo za Adolf Hitler. Hata yeye sijui alifuata nyayo za nani, kwa maana hata kama angezaliwa upya, asingekubali kuzifuata nyayo zake mwenyewe. Huyu jamaa alikuwa hafai hata kwa kulumagia. Hafai hata senti.

Yeyote anayetaka kufanikiwa kwenye uongozi huyaiga mafanikio ya viongozi walioweka historia za uadilifu na uongozi uliotukuka. Tangu kuumbwa kwa dunia kulikuwa na viongozi; lakini walitofautiana sana katika njia zao. Vitabu vya dini vinatusimulia nyakati za Adam, Nuhu na Musa kama viongozi waadilifu. Lakini pia Farao (Firauni) na wenzake waliokuwa viongozi wabadhirifu. Vitabu hivi vinahitimisha ukweli juu ya unyenyekevu kushinda kiburi.

Kutoka wakati huo hadi sasa hakuna yeyote anayependa kuongozwa kifirauni. Viongozi wa dini na wa Serikali kwa pamoja wanasisitiza maridhiano. Ili kutia mkazo, wanasheria pia wameshirikishwa kuyahariri na kuyaweka kwenye kumbukumbu kama herufi zilizochongwa juu ya mawe, si kuandikwa juu ya mchanga.

Kiongozi apende au asipende huwajibika na maandiko hayo. Hulazimika kutoa haki na fursa sawa kwa wote bila kujali tofauti zao. Mwalimu Nyerere alisema akipita mtaani na kukuta ombaomba, majambazi na makahaba, alijua kwamba ni wa kwake hao. Kazi yake ni kubeba shida hizo pamoja nao na kuuelekea unafuu.

Nchi ni sawa na mwili wa binadamu. Ina mchanganyiko wa ngurumbili wa kila aina. Hivi karibuni mitandao ya kijamii ilionyesha picha za marais wa Marekani wakati wakiapishwa, na wakati wakistaafu. Wote waliingia wakiwa vijana watanashati, lakini miaka minane ya uongozi iliwatoa wakiwa wamechoka hasa! Uongozi ni mgumu jamani.

Endapo ungeweza kuona timbwili linalofanywa kila siku mwilini mwako ungekufa kwa mshtuko. Kuna zaidi ya debe la minyoo iliyo bize kwelikweli usiku na mchana. Kama ukikasirika na kuua minyoo wote, bila shaka nawe ungekufa saa hiyo. Kwani kuna minyoo yenye kazi ya kumeng’enya chakula mwilini ili uendelee kuishi.

Mgonjwa hupata tiba. Lakini kuna wakati tiba zote zinakataa. Hapo kwa kujijali mgonjwa hutafuta tiba mbadala. Atakwenda kwa matabibu wa asilia, wanasaikolojia, wazee wa mila ama kwenye maombezi.

Anaweza kuwa ameshakunywa dawa zenye ujazo wa kontena mbili bila nafuu. Lakini siku moja akakutana na mzee anayetibu kwa ushauri tu, na akapona.

Kwa mfano, mmoja baada ya kuhojiwa aligundulika kuwa anafanya kazi zinazotumia akili nyingi kiasi cha kumchosha akili.

Sasa ili kesho aweze kuendelea na kazi, alikunywa pombe nyingi kwa lengo la kupunguza misongo akilini mwake. Siku alipoumwa alikwenda kutibiwa na tiba haikufanya kazi. Alirudia na kurudia dozi bila nafuu. Madaktari wakasema ana ugonjwa mpya, waombezi wakasema kapandwa na pepo na masangoma wakadai amerogwa…

Kwa bahati alikutana na daktari anayetibu kwa ushauri. Akaisikiliza hadithi yake kwa makini sana, kisha akamwambia: “Dawa yako ni maji. Kunywa maji glasi moja kila baada ya dakika tano.” Jamaa akang’aka: “Mi nshakunywa hadi mkojo, maji kitu gani!” Mtaalamu akabaki kimya akimtazama.

Kwa vile mgonjwa hakatai dawa, alikunywa maji kwa fujo sana na maradhi yakaisha. Wenye akili tunajua kuwa mapombe makali aliyotumia yalimtia sumu nyingi mwilini, alipoumwa na kumeza dawa zilikutana na sumu ile navyo kushindwa kufanya kazi au kugeuzwa sumu. Usione mganga akikuchanganyia dawa, pengine ni maji tu hayo.

Dawa ya aina hii ndiyo niliyotaka kuwashauri Wizara ya Mambo ya Ndani.

Tumeambiwa kuwa polisi hawapati ushirikiano kutoka kwa raia juu ya sakata linaloendelea mkoani Pwani. Kabla ya mganga kutoa dozi ni lazima atazame historia ya mgonjwa, hivyo uchunguzi wa kadhia hii ungeanza na “kwa nini hatupati ushirikiano wa raia?”

Bila shaka hakuna askari Polisi anayefurahia kuua. Pia, hakuna raia hata mmoja anayeshangilia kuuawa kwa mlinzi wake. Hivyo, basi ni lazima kuna pazia linalotakiwa kufunuliwa ili pande zote zionane. Ushauri wangu mkubwa ni viongozi kwenda kukaa na wazee, akinamama na kisha vijana wa kule.

Hiyo ndiyo gharama ya uongozi, lakini ikumbukwe kuwa ukivaa shati la masikini utajua sehemu ya shida zake. Na hii ndiyo moja ya silaha kubwa iliyotumiwa na muasisi wa Tanzania katika kudumisha mshikamano.

Kwa mtindo huu wa ‘Buta Nikubutue’ nyasi zote zitaungua.

Saturday, May 20, 2017

NDANI YA BOKSI : Anguko la Bongo Movie lilitabirika

 

By James Gayo

Inasemekana soko la filamu za Kitanzania linadoda kila uchao. Katika harakati la kuliokoa, Aprili 19 mwaka huu, wasanii wa filamu waliandamana na kufanya mkutano mkubwa kuwahi kuratibiwa.

Hata hivyo, mkutano huo ulidhihirisha pia kuwa wasanii wenyewe hawajui nini hasa kiini cha kuanguka kwa tasnia yao.

Kwa mfano wakati wakiandamana na kuimba vibwagizo vya “Hatutaki movie za nje au movie za nje bai bai”. Mpaka leo wasikilizaji tumeshindwa kuelewa mwingiliano wa ujumbe huo.

Wazungumzaji katika mkutano huo walikuwa kama walenga shabaha waliorusha risasi zao gizani. Wengine wakikazia uharamia wa kazi za filamu, wengine marufuku ya kazi za nje, wengine maadili ya Kitanzania katika utengenezaji wa filamu. Mkutano haukua na maudhui maalumu. Kwenye mitandao ya kijamii mkutano huo umedhihakiwa vya kutosha. Wachangiaji wengi wakiapa kutoangalia sinema mbovu za Kitanzania.

Kisichoeleweka pengine ni kwamba, hata huko Nigeria kulikosifika, soko la sinema zinazotengenezwa nchini humo limeanguka vibaya. Wanigeria wanajiuliza kitu gani kimeisibu tasnia waliyowahi kujivunia kama ya pili kwa ukubwa duniani. Tasnia iliyowahi kutajwa na tafiti nyingi za kimataifa kama sekta namba mbili katika utoaji wa ajira nchini.

Hapa Tanzania pia, kushamiri kwa biashara ya sinema kulivutia tafiti nyingi toka mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Kilichovutia watafiti wa kimatafa kufanya tafiti si umahiri wa filamu zilizokuwa zikitengenezwa Nigeria au hapa Tanzania bali ni ujio nadra wa tasnia za filamu zinayojiendesha kibiashara. Ikumbukwe kwamba katika nchi nyingi, hata zilizoendelea, sinema bado zinatengezwa na fedha za mifuko mbalimbali ya utamaduni na si mauzo.

Kwa hiyo basi, kitu gani kilifanya biashara ya filamu hizo kushamiri awali na kitu gani kimetokea hiyo inaanguka? Kwa maoni yangu, tasnia hii ulikuwa ni ujenzi wa ghorofa ndefu katika msingi wa tope; anguko lake lilikuwa likitabirika.

Filamu ni taaluma rasmi, ikifundishwa katika vyuo na kutolewa shahada zote kama taaluma zingine. Je, tungetegemea utengenezaji wa filamu zetu ujiendee hivyohivyo bila misingi yoyote ya kitaaluma kwa miaka mingapi? Je, ingewezekana kuwa na madaktari wetu ambao, mbali na kutosomea, wangeendelea kutibu bila kufuatisha mbinu za utoaji tiba zilizojaribiwa kwa miongo mingi na kukubalika ulimwenguni pote?

Kwa hiyo fursa moja muhimu ambayo haikuendana na kustawi kwa kwa utengenezaji wa filamu ilikuwa ni fursa ya elimu. Mara kadhaa chuo mahiri cha filamu duniani New York Film Accademy, kilitembelea Nigeria na kuwasihi vijana wanaonuia kutengeneza sinema zitakazovuka mipaka kusomea ujuzi wa kazi hiyo. Hapa nyumbani ninafahamu pamekuwa na fursa nyingi za stadi za utengenezaji wa filamu kutoka kwa wataalamu wa nje lakini naambiwa wasanii mahiri wa filamu zetu huwa hawaitikii mialiko hii.

Watengeneza sinema wetu wanahitaji kutanua uwezo wao, kama si kwa kwenda vyuoni basi kwa kusoma vitabu vya taaluma au kuhudhuria warsha mbalimbali.

Sababu nyingine ya msingi inayodororesha sinema zetu inaweza kuwa ndiyo iliyobeba kiini cha tatizo. Sinema ni tanzu moja tu ya sanaa za masimulizi. Imekuja wakati sanaa za uchoraji wa picha, muziki, mashairi, ngano, maigizo au riwaya zikiwepo tayari. Umashuhuri wa filamu umetokana na uwezo wake wa kujumuisha na kutumia sanaa zote nilizozitaja hapo juu. Uwezo wa kutumia hadithi zilizoandikwa vizuri, kupangilia picha, matumizi ya lugha ya kishairi, muziki na kadhalika. Kwa maneno mengine msingi sinema ni sanaa hizo zingine.

Ndio maana basi wasanii wa sinema karibu wote huko nje, ukisoma, utagundua awali walikuwa ni wasanii wa aina fulani. Au walikuwa wachoraji, waandishi, wapiga picha, wasanifu wa majengo, wabunifu wa mitindo, waigizaji wa jukwaani au wanamuziki. Hapa kwetu wasanii wengi wa sinema wameibuka tu kama uyoga. Ni ngumu mno kutengeneza sinema zenye mashiko ikiwa jamii haina msingi wa riwaya na ngano, ushairi, uchoraji na sanaa zingine za masimulizi. Sinema zinazotengenezwa kutokana na hadithi za vitabu ni ushahidi mmoja tu wa mwingiliano wa sanaa za awali na sinema.

Kwa maoni yangu kozi inayohitajika kufundishwa haraka ni ya stadi za kuandika hadithi katika mfumo wa sinema. Umuhimu wa tungo zilizoandikwa vizuri kisinema ndio msingi wa sinema duniani kote na haukwepeki. Sisemi kwamba maeneo mengine si ya muhimu ila najaribu kufikiria mahali pa dharura pa kuanzia. Sinema nyingi mno za Kiafrika zinaangukia katika kaburi hili. Hadithi za sinema zina muundo na sayansi yake ili kuhakikisha zinamvutia mtazamaji mwanzo hadi mwisho. Ukihudhuria warsha za misingi ya uandishi wa miswada ya sinema utagundua kumbe sinema zetu wala hazina hadithi.

Mkusanyiko wa mawazo tu (yasiyowiana wakati mwingine) hayawezi kutumika kama muswada. Stadi ya uandishi wa sinema inahitaji nidhamu maalumu kuhakikisha kuwa mtazamaji hachoki wala kupotea katikati ya hadithi. Haishangazi hamasa ya watazamaji imefikia ukomo na soko kudorora baada ya kubaini kuwa hakuna jipya katika tungo hizi.

Pengine Bongo Movie, kama wenyewe wanavyoiita, inaweza kufa lakini sinema kama sanaa tanzu ya masimulizi haiwezi kufa kamwe. Huu unaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuchipua tasnia inayokua taratibu huku ikizingatia misingi ya taaluma. Vijana wenye vipaji waingie kwenye tasnia wakijua kuwa hii ni taaluma kamili na si mahala pa kupatia umaarufu, kutembea kwenye mazuria mekundu na kupata fursa za kuongea na wanasiasa tu. Watafute namna ya kujiongezea ujuzi kila siku.

Kila ninapokutana na vijana waliobahatika kupata fursa ya kwenda kusoma nje huniambia wanaenda kusomea IT au biashara, sijawahi kusikia kijana anaenda kusomea filamu. Bado wengi tunadhani kuwa kigezo cha kutengeneza filamu ni kipaji na uwezo wa kununua kamera tu.

Kwa kuelewa mvuto wa sinema katika jamii wanasiasa wamejenga uswahiba mkubwa na wasanii wa filamu. Wamewatumika kwenye kampeni, wanawasiliana nao moja kwa moja. Viongozi hawa wana fursa nzuri zaidi si tu ya kuinua sanaa bali kukuza uchumi kama ilivyoshuhudiwa Nigeria kwa kuwekeza katika elimu ya utengenezaji wa filamu. Soko la nje lina njaa kubwa ya kununua filamu za kigeni endapo tu zitakidhi viwango vya kitaaluma.

Hitimisho

Juhudi iliyofanywa na watengeneza sinema wetu ni uthubutu mzuri na wa kupongeza. Vipaji vingi vimeonekana lakini hatuna budi kufikiria namna ya kutoka hapa na kufikia viwango vya kidunia. Ninawajua Watanzania wachache ambao ama wamesoma kwenye vyuo vya filamu au wamejiendeleza kwa namna mbalimbali lakini baada ya kurejea na kuona mazingira ya kienyeji ya utengenezaji wa filamu yanakinzana na elimu yao, wameamua kukaa pembeni na kuponda sinema zilizopo. Udhuru wao una mashiko lakini unanikumbusha swali lililowahi kuulizwa na mtu mmoja: Je, daktari asiyekubaliana na mazingira ya kazi akae pembeni na kuwaangalia waganga wa kienyeji wakiua watu?

James Gayo ni shabiki wa filamu

Saturday, May 13, 2017

Flaviana Matata: Mwanamitindo, mjasiriamali na mwanaharakati

Flaviana Matata

June 9, 1988

Wilhelmina

Flaviana Matata June 9, 1988 Wilhelmina Models 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Miaka 10 iliyopita  Flaviana Matata aliibuka mshindi katika mashindano ya Miss Universe nchini. Huenda wengi walimchukulia kama washindi wengine ambao hufurahia umaarufu na zawadi kisha hupotea.

Miaka 10 baadaye Flaviana si tu jina maarufu nchini kama yalivyo mengine, ni super model, mjasiriamali na mwanaharakati anayesaidia wenye uhitaji.

Amefanyakazi na makampuni makubwa katika kazi yake ya uanamitindo na dili la hivi karibuni la kutangaza bidhaa za kampuni ya American Express ni mfano hai wa ukubwa wake katika  biashara yake.

Wengi wanamtaja Flaviana kama mwanamitindo wa aina yake kuwahi kutokea katika nchi hii kwamba anaibeba nchi na kuitangaza vilivyo.

Ametoka mbali, lakini anasema anaendelea kujifunza na kupigania ndoto zake za kupanda katika majukwaa ya wabunifu nguli duniani– Alexander McQueen, Tory Burch na Vivienne Westwood.

Kwa hadhi yake anaweza kukutana na yeyote mfano, mzuri ni picha zinazomuonyesha akiwa na Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump.

 “Ninakuwa mtu tofauti ninapokua kazini lakini baada ya hapo mke, dada na mtoto. Kaka zangu na baba wananikumbusha hivyo,” anasema Flaviana ambaye mama yake alifariki katika ajali ya meli ya MV Bukoba miaka 22 iliyopita.

Anasema miaka mitano ya mwanzo baada ya kushinda taji la Miss Universe ilikuwa ya kipindi cha mpito: “Nilikuwa najifunza mbinu za biashara ya mitindo. Nilianzia Afrika Kusini baadaye nikahamia New York Marekani.”

Kuhusu ndoa

Kwa wengi hasa walio katika biashara ya burudani ndoa inaweza kuwa kikwazo lakini kwa Flaviana ni tofauti na mwenyewe kwa neno moja tu anasema ni Baraka.

Anasema imekuwa chachu ya kuendelea kufanya vizuri kwani mume wake anamuunga mkono na kumsukuma kufanya kazi zaidi tofauti na awali.

 “Kazi ya uanamitindo ina changamoto nyingi mwanamke asipopata mume anayeielewa biashara hii atakwama, anahitaji kuungwa mkono,” anasema.

Pamoja na kuwa ameolewa anasema bado anafuata miiko ya kazi yake na mume wake anamuunga mkono kwa kuwa anaelewa hiyo ni kazi yake.

 “Nafanya kazi ya mitindo kama ajira, nina biashara ya rangi za kucha na mfuko wa kusaidia wenye uhitaji The Flaviana Matata Foundation (FMF), vyote hivi vinanihitaji.”

Kuhusu kuanzisha familia kwa maana ya kupata watoto anasema ni baraka na kwamba watakapokuja atawapokea kwa kuwa hawatakuwa kikwazo katika kazi zake.

 “Siwezi kusema moja kwa moja ni lini lakini watoto ni baraka ambazo kila mmoja anafurahia kuzipata. Tofauti na watu wanavyofikiria wapo watu ninaowafahamu wanafanya vizuri katika kazi pamoja na kuwa na watoto. Unapokuwa mjamzito au kulea unaweza kuendelea na kazi. Hata hapa ninapoongea si kwamba huwa nafanya mitindo ya kuonyesha mavazi jukwaani, nafanya mara chache sana,” anasema.

 

Kuhusu Lavy

Mwaka 2015 Flaviana alifungua ukurasa mwingine kwa kujiingiza rasmi katika ujasiriliamali kwa kuingiza sokoni rangi zake za kucha ziiitwazo Lavy.

Anasema mzigo wake wa kwanza kuuingiza nchini uliisha ndani ya wiki mbili: “Nilitamani kufanya biashara muda mrefu lakini niliogopa soko, nilijiuliza namna watu watakavyozipokea bidhaa zangu.”

Anasema kilichomwogopesha ni ukweli kwamba watu wengi nchini huichagua bidhaa kutokana na bei yake na si ubora.

Anaongeza: “Nilitaka kutengeneza kitu tofauti. Nilichukua muda kutengeneza rangi ambayo inaweza kutumiwa na kila mtu kuanzia mama mjamzito mpaka mtoto.”

Rangi hizo zimepokelewa vizuri katika soko: “Zinapendwa na kununuliwa sana, kwa hilo namshukuru Mungu na watu wote wanaoniunga mkono.”

Trump na Russell

Kipara na nywele fupi ndizo zinazomtambulisha katika ulimwengu wa mitindo na kwamba hana mpango wa kuubadili mtindo huo kwa sasa.

Kupata dili za kufanya kazi na kampuni kubwa kumemfanya ajikute akiwa karibu na watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa duniani.

Anasema alikutana na Donald Trump kabla hajawa Rais wa Marekani: “Ni mtu anayependa watu wake pamoja na kuzungukwa na watu wengi lakini anakumbuka majina ya kila mmoja.”

Kuhusu Russell Simmons ambaye amewahi kuwa mume wa mwanamitindo Kimora Lee, anasema wamekuwa ndugu kutokana ukaribu walionao.

Kuhusu FMF

Mbali na kazi anapenda kusaidia wenye uhitaji. Katika kipindi kifupi alichofanya kazi Marekani alirudi nyumbani kuanzisha taasisi ya kusaidia wasichana  nchini ya Flaviana Matata Foundation.

“Hii ndiyo namna pekee ya kuwasaidia wenye uhitaji, hata kama ni wasichana 20 tu basi ninahakikisha wanakaa darasani wakipata mahitaji yote muhimu ya shule,” anasema.

Anasema wasichana ndio taa ya Taifa lolote ndio maana anawahimiza kuweka bidii katika masomo yao.

Saturday, May 13, 2017

Nahitaji darasa kuielewa orodha ya wasanii ‘bankable’JULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

By Julieth Kulangwa

Kwa mujibu wa kamusi niliyosoma neno ‘bankable’ ni kivumishi kinachomaanisha mtu au bidhaa fulani inafaa kwa uwekezaji kutokana na kile anachokifanya.

Kwa mfano ukiwekeza kwa Davido, Wizkid una uhakika kuwa fedha zako zitarudi kwa sababu ukichungulia mialiko wanayopata kwa mwaka mzima unaiona hela yako ikielekea benki na faida juu.

Nimeisoma orodha ya wasanii kumi Afrika ambao ni ‘bankable’ kwa mujibu wa Forbes. Wamo Davido, Wizkid, Don Jazzy, Sarkodie, Hugh Masekela, Black Coffee, Don Jazzy, Tinashe, Jedanne na Oliver Mtukudzi.

Orodha hii ina majina ambayo yanaleta sintofahamu. Huenda kuna vigezo vimatumika kuipata orodha hii lakini wengine wanatafsiri kama hawa ndio wasanii matajiri Afrika.

Nakubali kwamba Akon ni Mwafrika. Nakubali kwamba ni mwanamuziki mzuri. Nakubali kwamba kutokana na uzuri wa kazi zake anauzika na anastahili kuwa bilionea.

Nakubali kwamba anastahili kuwa bilionea kwa sababu yupo katika nchi ya fursa. Akitoa wimbo mmoja tu na robo ya raia wa nchi yake wakaununua kwenye mitandao na kuutazama Vevo au Youtube atapata pesa nyingi kuliko mwanamuziki wa Bongo atakayoipata atakapozunguka nchi nzima kufanya matamasha.

Akon ni Mwafrika aliyebahatika kuzaliwa Marekani na shughuli zake za muziki anafanyia kule. Ni tofauti na Sarkodie aliyezaliwa Ghana au Diamond aliyekulia Tandale. Hawa wakienda Marekani wanakwenda kuwaburudisha Waafrika wenzao.

Siku zote hapa tunasema wanakwenda kufanya shoo sebuleni sijui nini wakati Akon katika nchi hiyo hiyo anaweza kufanya shoo ya peke yake ya watu 60,000.

Ninahitaji maelezo zaidi kujua Don Jazzy anaingiaje katika orodha hii. Huenda maelezo yalipaswa kuwa marefu kidogo kwamba utajiri huu kaupata kwa kuwasimamia kina Tiwa Savage na Ricado Banks au biashara nyingine.

Namuona Don Jazzy kama mfanyabiashara wa muziki  na si mwanamuziki. Hata utajiri anaotajwa kuwa nao hakuupata kwa kushika maiki. Ni mwekezaji katika muziki ambaye naye mara moja moja anafanya muziki.

Naona si sahihi kumshindanisha mtu anayefanya biashara ya muziki na mwanamuziki. Wengine wanajituma jukwaani, wanakata viuno halafu wanashindanishwa na mtu anayeimba kujifurahisha si sahihi. Diamond na Don Jazzy ni watu wawili wanaounganishwa na uwekezaji katika muziki lakini Diamond ni mwanamuziki hodari kuliko Don Jazzy.

Sitaki kumzungumzia Jedanne  na Tinashe walioingia katika orodha hii kwa sababu nachanganyikiwa ziaidi.

Saturday, May 13, 2017

NDANI YA BOKSI: Mkubwa Fella njoo tunywe kahawa...

 

By Dk Levy, salaamzao@gmail.com Simu no 0744053111

Muziki wa Bongo Fleva umepitia mengi sana. Kuna watu waliishia njiani na kuamua kufanya mengine. Wapo ambao wameamua kukomaa mpaka leo hii. Mungu awarehemu waliotangulia mbele za haki.

Inasikitisha kuna wengine muziki ulipita kushoto wao kulia na kuishi kubwia unga. Mjanja yeyote havuti unga. Lakini kila jambo lina sababu tusichoke kuwaombea warudi kwenye mstari.

Kuna wanamuziki na wadau wa muziki ambao nalazimika kuwaheshimu kwenye hili game la Bongo Fleva. Walifanya mambo kwenye nafasi zao na kujenga himaya kubwa.

FA. Akiwa kwenye ubora wake. Kwenye umaarufu wenye umaarufu wa kuzimiwa na totozi za mjini.

Akashindwa kuendekeza ‘hagi’ na mitego ya totozi. Akaangalia kesho yake. Akaamua kurudi darasani. Shule inamfanya awe FA unayemuona hii leo.

Ukitaka kujua linganisha kati yake na wengine. Elimu ilimfanya atafute njia ya namna ya kupambana na game linavyokwenda. Alijua kula na kipofu.

Fid Q. Hawa kina Darassa, Billinas na wenzao. Bila uwepo wa Fid Q wangekata tamaa. Kukomaa kwenye misingi yake na kuitwa Ngosha. Kulifanya hata Joh Makini aamini kuwa ‘any thing can happen’ (lolote lawezekana) kwenye hip hop. Fid alisimama mwenyewe katikati ya wimbi la muziki wa kuimbaimba kama ndio muziki bora. Akakomaa bila kujali kuwa Mchizi Mox, D Knob na kina Jaymoe wamesanda. Ndipo wakaibuka kina Young Killer na wenzake na kuona kuwa mbona inawezekana? Kumbuka kuwa watu kama kina Solo Thang waliimba mpaka Mduara. Wakaamua kukimbia nchi kwa kukwama ila Fid akakomaa.

JIDE. Moja kati ya wasichana ambao waliwafanya wasichana wajue kuwa kuna maisha nje ya kujiuza. Nje ya kupata digrii na nje ya ajira ya rushwa ya ngono. Uwepo wake na kukomaa kwake kuliwazalisha wengi mpaka kina Shilole. Snura. Linnah na wenzao.

Maisha ya Jide ni daraja moja na kina Shy-Rose Bhanji na wenzake ila yeye akaunti yake inatuna kwa sauti na tungo zake.

Bila yeye wengi wao wangeishia sehemu mbaya kimaisha ila muziki umewaondoa huku na kuwaweka sehemu moja na Ester Bulaya.

AY. Ni wanamuziki wa mwanzo kabisa ambao walianza kuupaisha muziki wa Bongo Fleva nje ya mipaka ya Tanzania.

Aliwateka Uganda na Kenya miaka mingi iliyopita. Wanamuziki wa mwanzo kabisa ambao walianza kuonesha njia ambazo wanapita kina Diamond kwa sasa.

Na zaidi ana akili ya biashara. Hategemei pesa za shoo tu ana miradi mingi kupitia muziki na wanamuziki.

ALI KIBA. Wakati Diamond anaanza ‘swaga’ zake yeye alikuwepo. Ila alikuwepo kama hayupo. Fujo za Diamond zilimuamsha na kufanya kitu kilichomfanya awe mpinzani wa Diamond.

Kitu kilichowashinda Q Chillah na wengineo kama kina Matonya na wenzake. Kiba aliamka akasimama. Leo hii Mwakyembe akimtaja Diamond lazima amhusishe na Ali Kiba. Si jambo dogo kushindana na Diamond mwenye Ruge, Fella, Babu Tale na Sallam. Waandishi na watangazaji kibao waliokuwa upande wa Diamond.

JOH MAKINI. Huyu Mweusi toka Kaskazini siyo mtu wa kumchukulia poa poa. Hata kama mdogo wake ila kuwa ‘role model’ wa msomi kama Nikki wa Pili siyo kitu kidogo. Nikki kusema hataki kazi ni kwa sababu ya uwepo wa kakaake kwenye game la muziki.

Kama Joh angekuwa kwenye hali kama ya wenzake wengi walioshindwa kuugeuza muziki kuwa pesa. Hata Nikki wa Pili asingethubutu kusema hataki kazi.

RUGE. Huyu kiumbe ngumu sana kumuongelea kwenye huu muziki. Aliufanya huu muziki. Rasta za wanamuziki. Kwato za wanamuziki na harufu za vikwapa za wanamuziki wa Bongo Fleva kufika kwenye viunga vya Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam.

Ushawishi wake na kuitumia vyema Clouds FM, waliupandisha muziki huu na kutengeneza ajira kubwa sana kwa vijana wengi.

DIAMOND. Bado anaendelea kufanya miujiza yake. Miujiza iliyomshinda Mr Nice na wenzake. Kutoka Tandale ambako na mvua hii hakukaliki mpaka kupiga stori na kufanya kazi na NE-YO? Nahisi kuna mengi zaidi kutoka kwake. Tusubiri.

FELLA. Mkubwa Fella hakudandia treni kwa mbele kama wengi wanavyodhani. Ni mtu kati ya watu wanaohitaji heshima kwenye huu muziki.

Aliowasimamia wakasimama ni ushahidi kamili. Waliokwama kwa kukataa kusimamiwa naye pia ni ushahidi tosha.

Tofauti ya Fella na Sallam. Ni Sallam kumsukuma aliyejisukuma. Na Fella ni kugeuza karanga kuwa dhahabu. Yamoto Band inatosha.

Mae West anasema “Kuishi ni mara moja pekee, lakini ukifanya vema, mara moja yatosha”. Fella muziki unaudai haukudai. NI wakati wa kufurahia maisha. Njoo tunywe kahawa.

Sugu na Profesa Jay kuwaelezea wanahitaji WARAKA KAMA WA MTUME PAULO. Tuwaache kwanza.

Saturday, May 13, 2017

Mambo yanayoupandisha muziki na kuushusha kwa wakati mmoja

By Kelvin Kagambo, Mwananchi

Kila chenye faida kwa namna moja huwa na hasara kwa namna nyingine. Hata kwenye muziki, kuna mambo lukuki ambayo yana faidia katika kuijenga tasnia, lakini mambo hayo hayo ukiyatazama kwa upande mwingine yamekuwa ni chachu ya kuharibu sanaa hiyo na  yafuatayo ni miongoni mwao.

Duniani kote, muziki wa kisasa unabebwa sana na video nzuri. Yaani hata kama msanii akiwa mahiri namna gani kwenye uimbaji, kama nyimbo zake hazina video zilizotengenezwa kwa ubunifu zenye kuvutia basi ‘ataula wa chuya’.

Hata wasanii wa nyumbani Tanzania wameshtukia mabadaliko haya, na kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakiwekeza kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanatengeneza video nzuri jambo ambalo limesaidia kuutangaza muziki wa Tanzania nje ya mipaka.

Lakini mbali na kwamba video zimekuwa na mchango mkubwa, pia zimekuwa ni sehemu kuu za kuuporomosha muziki. Wasanii wengi wameyapokea vibaya mabadiliko ya nguvu ya video katika muziki wa kisasa kiasi kwamba wasahau kuhusu audio (nyimbo). Matokeo yake tumekuwa na video nyingi nzuri za muziki lakini nyimbo ni za ovyo.

Kiki

Kamusi ya Kiingereza – Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, toleo la mwaka 2000 inatafsiri neno ‘Kick’ au Kiki kama ilivyozoeleka mitaani kwa maana zaidi ya nne. Huku maana moja kati ya hizo, ambayo hutumika kwenye uzungumzaji ikimaanisha ‘nguvu’.

Neno hili limesikika likizungumzwa sana na wasanii, likiwa na maana ya kwamba kutafuta nguvu ya kuvuma. Wasanii wengi wamekuwa wakitengeneza matukio kadha wa kadha yenye kushangaza ili kuwafanya mashabiki waendelee kuwazungumzia.

Kimsingi Kick zimekuwa zikiwasaidia sana wasanii wa enzi hizi duniani kote, lakini mbali na hiyo pia zimekuwa zikiwaangusha na hata kuwapoteza kabisa, kwa sababu kuna baadhi ya matukio wanayoyatengeneza yanawaharibia taswira nzima kwa jamii na kuwapotezea baadhi ya mashabiki.

Urafiki wa msanii na vyombo vya habari

Vyombo vya habari ndiyo kila kitu tangu enzi na enzi, vina uwezo wa kutengeneza jamii kwa namna vinavyoamua. Yaani taswira ya Tanzania unayoiona leo, imechangiwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari nchini pamoja na vile vya nje. Kwa upande wa sanaa hasa ya muziki, wasanii wakubwa na maarufu ni wale ambao wamefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya habari, kwa sababu hii hutoa nafasi kwao kupewa kipaumbele wanapofanya mambo yao, aidha kuachia wimbo mpya na kadhalika.

Hata hivyo licha ya kwamba urafiki baina ya msanii na vyombo vya habari husaidia kumjenga msanii, pia kuna nafasi kubwa ya kumporomosha kwa sababu, kuna wakati, watu wanaounda hivyo vyombo vya habari, kama binadamu hujikuta wakilazimika kusifia kazi za wasanii hata kama ni za ovyo.

Hii inatokana na falsafa ya kwamba, mtu anayekupenda (rafiki yako), mara nyingi huwa tayari kukudanganya ili asikuumize. Kwahiyo hata msanii akiboronga, mtangazaji atasifia ili kuhakikisha ule  ukaribu wao hauporomoki.

Teknolojia

Maendeleo ya teknolojia ni kitu ambacho hatuwezi kukipinga, tunakihitaji katika dunia ili kuendelea kuyafanya maisha rahisi na saa 24 tulizo nazo ndani ya siku moja ziweze kututosha.

Katika muziki, maendeleo ya teknolojia yamechangia kwa kiasi kikubwa mno ambapo awali, kabla ya utaratibu wa kurekodi muziki haujawa kama ilivyo sasa, muziki ulikuwa unatumia muda mwingi, idadi kubwa ya watu na nguvu nyingi katika kutengenezwa kwake jambo ambalo liliwanyima fursa watu waliokuwa na vipaji vikubwa lakini hawakuwa na uwezo wa kugharamikia muda, nguvu na idadi kubwa ya watu katika kuandaa nyimbo zao .

Hata hivyo teknolojia ilipoendelea ikarahisisha mambo kiasi kwamba kwa sasa, idadi ya watu wawili tu inatosha kutengeneza wimbo mzuri ndani ya muda mfupi. Aidha, nyenzo za  kutengenezea muziki zimekuwa rahisi kiasi kwamba ukiwa na kompyuta unaweza kutengeneza mdundo (beat) mahali popote ulipo ikabaki kazi ya kurekodi tu hali hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwatengeneza kina Diamond na Alikiba tulionao leo.

Hata hivyo, mbali na kwamba teknolojia hii inasaidia kuukuza muziki kwa kiasi kikubwa, pia imekuwa na sehemu fulani ya kuuporomosha muziki, kwa sababu kila kitu kimekuwa rahisi, mtu yeyote mwenye kompyuta tu anaweza kutengeza muziki na matokeo yake ni kwamba tumekuwa na idadi kubwa ya waandaji wa muziki na wasanii ambao wamejikita kwenye sanaa si kwa sababu wana vipaji, bali ni kwa sababu wana nyenzo za kufanya kazi.

Saturday, May 6, 2017

NDANI YA BOKSI: Bongo Fleva inapoishi kwa matukio

 

By Dk Levy

Msimu wa Fiesta unakaribia. Tegemea nyimbo nyingi za Bongo Fleva kuachiwa kipindi hiki. Kwa msukumo wa tukio la Fiesta ili wapate nafasi ya kupanda majukwaani katika mikoa mbalimbali. Shoo zilizokuwa zikiandaliwa na kina Nyau kule Morogoro na mwenzake Ngedere hazipo hivi sasa hata kama zipo siyo kama zamani kimapato na msisimko.

Mdosi wa Shinyanga sidhani kama ana namba ya Young Killer na kina Shilole. Ndivyo ambavyo Kampuni ya 5 Stars Entertainment ya Tanga imetoweka kwenye masikio ya wadau wa Bongo Fleva.

Kusema muziki umekua inabidi utoe ufafanuzi mkubwa. Kinachoendelea ni muziki kutengeneza matukio zaidi huku wasanii wawili watatu wakitanuka na kuacha pengo kubwa la mafanikio kwa wenzao.

Muziki umekua kwa mwanamuziki mmoja kuwa staa pekee kwa mwaka wa saba sasa? Tusidanganyane muziki umekata ringi unaenda kama gari la mkaa, tripu moja porini moja gereji.

 Utaniaminisha vipi kuwa muziki umekua kwa kuwatazama wawili tu Dai na Kiba? Ni kama soka la Bongo kutawaliwa na Simba na Yanga tu. Katika ubora wake muziki ulikuwa juu. Watangazaji wa vipindi vya Bongo Fleva redioni walikuwa juu kwa umaarufu ule ule kama wa wanamuziki.

Venture alikuwa staa kama Mr Blue. Steve B alikuwa staa kama alivyokuwa Noorah. Leo hii watangazaji wa vipindi vya umbea kama Shilawadu wanakuwa maarufu kuliko wanamuziki. Ndo maana wanamuziki wa sasa wanawategemea Shilawadu kupeleka umbea ili wazungumziwe kwenye vipindi hivyo kwa mambo ya nje ya muziki.

Muziki umekuwa wa matukio wanategemea matukio ya uhusiano wa kingono na totoz za Bongo Movie ili wapande chati na si  ubora wa tungo na sauti.

Wakati zamani watu walikuwa wanatega sikio redioni kusikia wimbo mpya, leo wanatega sikio na macho ili wasikie na kuona muendelezo wa penzi la Wolper na Harmonize. Muziki na wanamuziki wanaishi kwa matukio.

Harmonize anatumia tukio la penzi lake na Jack Wolper ili kuwafanya watu watege sikio juu yake kabla hajaachia wimbo mpya. Na ndo maana wanamuziki wanasubiri msimu wa Fiesta ili waachie nyimbo wapate shavu kwa tukio la Fiesta.

Muziki umeyumba. Huu si wakati wa Bongo Fleva kutamba Afrika kwa jina la mwanamuziki mmoja tu. Tunahitaji kuwa na kina Diamond wa kutosha kwa ubora na kipato kama ilivyo kwa Wanaijeria. Lakini kinachoendelea ni uwepo wa daraja kubwa la kipato na umaarufu kwa Diamond na wenzake. Shoo anazofanya Diamond huko Zambia, Mr Nice alifanya miaka 15 iliyopita. Si kitu kipya. Na maisha ya Nice na Ferouz hayakuwa na utofauti sana kama Diamond na Belle 9 kwa sasa.

Maana yake ni kwamba Ferouz aliishi vizuri kama Mr Nice kwa shoo za ndani ya nchi bila kutoka nje ya mipaka. Sasa mtazame Diamond na Fid Q, ni Vogue na Bodaboda. Tofauti ni kubwa.

Lakini wakati ule Nice alikodi ndege kwenda kwenye shoo Comoro huku Profesa Jay akiendelea na shoo zake za Sitimbi na Makorokochoni vizuri tu. Na maisha yao yalikuwa hayana utofauti kuanzia magari ya kutembelea mpaka bili za pombe kwenye kaunta za klabu za usiku.

Kama mtu utajidanganya kuwa Mr Nice alikuwa analipwa pesa kidogo kwa shoo za nje kuliko Diamond wa leo utakuwa unakosea. Tunamuongelea Mr Nice aliyekwenda Japan badala ya Twanga Pepeta kwenye shoo siyo tafrija ya Wabongo. Tunamuongelea Nice ambaye alipiga shoo Zambia, Malawi, Msumbiji, Uganda, Kenya na Comoro kwa dau la dola elfu 20 kwa shoo mara kwa mara katika utawala wa Mkapa. Ogopa.Ndiyo maana pesa ilimtia uchizi.

Kilichopo ni Diamond kuzichanga karata zake vyema kwenye maisha tofauti na Nice. Bongo Fleva si mtu mmoja au wawili. Ni kitu ambacho kilikuwa kinazalisha ajira ndani ya ajira. Mwenye ukumbi alipata pesa, promota na wasaidizi wake na washereheshaji wa shughuli walipata pesa. Na zaidi kampuni za vinywaji zilipata pesa kupitia muziki huu. Kuna watu mikoani walijenga nyumba kusomesha watoto shule nzuri kupitia muziki huu. Bongo Fleva haikuwa faida kwa wanamuziki tu. Leo hii miaka mingi imetoweka bila msanii kutoa albamu. Ni vipi nikuamini unaponambia muziki unakua? Wenye ‘stationary’ walipata pesa kwa kutengeneza vipeperushi vya shoo na posters. Ndivyo ilivyokuwa kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni. Ulikuwa ukisikia Afande Sele yuko Tabora, Blue yuko Tanga, Daz Baba yuko Kahama na Gangwe Mobb wako Mtwara na Soggy yuko Kilombero. Na wote walijaza watu na kupata pesa.

Hii leo wote hao utasikia wapo Instagram si kwenye shoo. Leo hii wanamuziki wako bize kujibu shutuma kwenye vipindi vya Shilawadu na kuposti vinywaji Instagram.

Wanaishi kwa matukio na kina Nay wa Mitego wanabamba kwa nyimbo za matukio. Roma anaongelewa kwa tukio la kutekwa kuliko kazi yake. Chid Benz anaongelewa kwa tukio la uteja na kutoka rehab muziki wake umewekwa kando. Linah tukio la ujauzito wake ndiyo habari ya mjini na siyo sauti yake. Ndivyo ilivyo kwa Barnaba na tukio la kutelekezwa na mkewe limeuteka muziki wake. Muziki wa Bongo Fleva uko pale pale ila akili ya Diamond imejiongeza.

Kusema kuwa muziki huu umekua kwa ubora, umaarufu na mafanikio ya Diamond ni sawa kabisa na kumtazama Champion Boy Mbwana Samatta na kusema soka la Bongo limepanda wakati bado linaendeshwa kwa kamati za saa 72 huku timu ikililia pointi za mezani.

Diamond anaenda kuchukua tuzo nje ya nchi. Kwenye korido akitazama kushoto anamuona Sallam. Kulia Mose Iyobo. Wakipishana na wanamuziki wa Kinaijeria kibao. Tunawahitaji kina Diamond wa kutosha badala ya kutuletea stori za Baraka Da Prince na Naj. Muziki na wanamuziki wahame kwenye matukio. Mwenye mawasiliano na Asha Baraka, Ally Choki na Nyoshi wapeni salamu. Muziki unaishi kwa matukio hivi sasa.

Saturday, May 6, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: Machinga anayelala ni ‘Slipinga’

Kipindi cha nyuma nikiwa Unyakyusani nilipata kumfahamu mzee mmoja aliyekuwa maarufu sana. Hakuwa mwenye uwezo mkubwa lakini sikuwahi kumwona akiwa nje ya vazi la suti. Nilikuja kufahamu baadaye kwamba aliitwa Kima kya Mbwele”. Sikushangaa hata kidogo.

Jina hili lilimtafsiri moja kwa moja kama ‘makalio ya nzi’. Kama tujuavyo, nyuma ya koti la suti kuna mchano mdogo kwa chini. Unaweza kuufananisha na mabawa ya nzi yanapokutana chini ya mgongo wake. Hivyo anapovaa suti alifanana na nzi kutokea kwa nyuma.

Watu hawataki kuuma meno katika kutaja majina. Ukiwa mnene utaitwa bonge, mrefu ataitwa ‘tall’. Yupo rafiki yetu tuliyecheza naye mpira aliitwa ‘kijino’; bila shaka unajua ni kwa sababu gani.

Tumeshaongea mara nyingi majina ya ‘baiskeli’, ‘pikipiki’, ‘tukutuku’ na ‘gari’. Tukakubaliana yote haya yalizalishwa na Waswahili kwa kutotaka kuuma ndimi zao.

Na si Waswahili pekee. Wazungu walitamka “Bagamoyo” badala ya Bwaga Moyo, Wamakonde wakasema “nchachani” na Mzungu “Msasani” badala ya Mussa Hassan. Wahindi wakasema “gali ya mogo” kumaanisha ugali wa muhogo. Ebu jaribu kuwaiga Waarabu wanavyotamka “chuma kingali moto”, halafu nijulishe kama ungali salama.

Huku mitaa ya kwetu kuna mtaa maarufu unaojulikana kama Wachawacha. Nilipouliza asili ya jina hili nikaambiwa kuwa mwenye mtaa alitambaliwa na wadudu wanaowasha. Sasa kwa vile wengi wa wakazi wa eneo hilo ni wa asili ya ‘ukipanda nchale, ukichuka nchale’, neno washawasha likawa jina ‘Wachawacha’.

Ni ya kawaida tu. Hata ‘Mtoto nyamaza’, kwa Mwinyi Amani sasa ni Mwananyamala kwa Mnyamani.

Kabla ya kuwapo kwa sehemu maalumu za kufanyia biashara, watu walikuwa wakifanya mabadilishano ya bidhaa. Mwenye nguo alimfuata mkulima na kubadilishana naye kwa kiroba cha mahindi. Hakukuwa na benki wala sim pesa wakati huo.

Hata maduka yalipoanza kutumika utamaduni wa kupelekeana bidhaa haukufutika. Moja ya faida kuu ikiwa ni kukutana moja kwa moja na mteja. Kama wewe ni mvuvi wa papa hutakosa chochote ukimpelekea Mzaramo anayekula ugali kwa papa kila asubuhi.

Kwa kawaida wachuuzi huwa na mitaji midogo au kutokuwa na mtaji kabisa. Anaweza kwenda kukopa mashati manne dukani kwa Mhindi, akazungusha mtaani na baada ya muda mfupi akaja na pesa za mauzo, akarudisha mtaji na kubaki na faida yake.

Wakati wa jua kali kila chinga atatembeza leso na vitaulo vya kukaushia jasho. Hali ikibadilika na mvua kunyesha, haraka sana atarudisha leso dukani na kutoka na miavuli. Daktari mjanja hufungua zahanati kwenye kitongoji cha wagonjwa. 

Kule ughaibuni mchuuzi wa aina hii aliitwa Marching Guy. Matamshi ya jina hilo kwetu yanasomeka kama Machinga. Machinga si kabila, jinsia, rika wala dini. Ni kijana yeyote aliyetafuta riziki kwa kuwafuata wateja walipo au kuzurura. Si lengo langu kumwita ‘mzururaji, lakini kazi yake ni kuwafuata wateja popote walipo.

Kwa jinsi ninavyomfahamu Machinga, simtofautishi na kunguru. Mfuge kwenye mazingira bora kuliko tausi, umpe kila anachokihitaji (minofu kwa mizoga) lakini ataona kuwa hapo si mahala stahiki kwake. Ukimwachia mlango wazi kwa sekunde tu, atakimbia.

Kamkamate chinga uchochoroni, umpe fremu kubwa katikati ya jiji na mtaji wa kutosha, atamwachia mwingine biashara na yeye kurudi mtaani.

Kutokana na hali tete ya uchumi, Machinga walifanikiwa kuzoa wateja wengi sana kuanzia jijini Dar es Salaam. Muda mfupi baadaye wakaanza kupata wateja kutoka nje ya jiji. Iliwabidi sasa pamoja na kuzurura, waweke makao makuu katika mitaa ya Kariakoo ili kukutana na wateja wa mikoani.

Kila kilichouzwa dukani kilipatikana kwa machinga kwa bei ya maafikiano. Mitaa ya jiji ikawa bize sana, viongozi wakaanza kuumia vichwa kutokana na hali hii. Kila mara tukawa tukishuhudia mshikemshike kati ya askari wa jiji na machinga.

Likaja wazo la kuwajengea nyumba za biashara maarufu Machinga Complex.

Hapo sasa ukaja mshangao mwingine. Chinga huyuhuyu asiye na elimu ya biashara wala mtaji, anayetegemea kuzurura kumtafuta mteja. Huyuhuyu ambaye hajaweza kulipia hata pango la nyumba ya kuishi? Ati unamkopea jengo kwa karibu Sh13 bilioni ukitarajia atazilipa!

Ni machinga yupi anayemudu kukaa mahala pamoja akilipa kodi ya vizimba, umeme, usafi na kadhalika? Nadhani angelifanana na simu ya kiganjani iliyofungiwa mezani.

Lakini mambo hayakuharibika moja kwa moja. Watu wenye mitaji ya biashara walikwenda kupanga vizimba na kuanza kazi.

Ajabu ni kwamba viongozi wetu wakatangaza kuwa ‘wafanya biashara wafukuzwe’ kwa sababu lile ni jengo la machinga. Marching guy wa aina gani?

Ningeshauri kuwa machinga angeandaliwa kwa elimu ya biashara na mitaji kabla ya kupokea deni kubwa asilolimudu. Akifuzu ataweza kukuza mtaji na kuhama kutoka kwenye mfumo wake hadi kutulia mjengoni. Ashirikishwe juu ya mustakabali wake.

Tumeambiwa ati mkopeshaji (NSSF) alimtingishia fedha akisema, “Hizi ni bilioni 12.7. Nampa fundi akujengee kisha utanilipa na riba.”

Kanuni za biashara si rahisi kama wengi wanavyochukulia. Machinga akifundishwa BITWA (Business, Insurance, Transportation, Warehousing na Advertisements) tunaweza kupata kizazi bora cha wafanyabiashara. Tutasahau kabisa habari ya kukimbizana nao huko mtaani.

Tuesday, April 25, 2017

NDANI YA BOKSI: Mnalazimisha kuuza kitimoto Saudi Arabia !

 

By Dk Levy

Kuna kitu kinaendelea Dar es Salaam kwa sasa. Ukikifikiria sana unaweza kulia. Vituko vya Harmorapa vina tija na mvuto kuliko haya ya Bongo Movie. Yaani ni filamu tosha inatengenezwa.

Bongo Movie wanachofanya ni kuliua zaidi soko la filamu zao. Pamoja na kelele za wadau mbalimbali hawasikii la muadhini wala mnadi swala. Wameweka pamba sikioni na kudumisha ule msemo wa “Sikio la kufa halisikii dawa”.

Wameamua kushika kisu na kuchinja shingo zao. Kuna tatizo kubwa kwenye mishipa ya fahamu. Dah!

Tatizo si Wamachinga. Tatizo ni kutaka tununue filamu ya mtu kaigiza kama malaika kwenye filamu halafu anamwambia mtu mwenye matatizo kuwa “Usijali ndugu, yupo Mungu juu atakusaidia.” Malaika huyo eti. Tatizo wasanii wetu wameamua kutulisha matango pori. Halafu tunaoshindwa kula wanatulazimisha tumeze bila kutafuna. Kweli imefika wakati wasanii wetu wameshindwa kucheza uhusika kwenye filamu zao. Wameshindwa kuandika stori nzuri. Wameshindwa kuandika miswada bora. Na zaidi wameshindwa kabisa kujua kwa nini soko lao limetoweka kama magagulo. Dah!

Mtu anafyatua risasi kwenye filamu halafu inachukua dakika kadhaa kumfikia mhusika. Risasi yenyewe mlio wake kama mtu kawasha njiti ya kiberiti. Inampata mhusika kifuani na damu inatoka kama ile ya kipimo cha malaria.

Mtu yupo na demu wake supermarket nusu saa nzima wanachagua na kutazama vitu, halafu filamu ina saa moja na nusu tu. Dah!  Hivi haya mapungufu hawayaoni kabisa Kwenye filamu zao mpaka kuwaonea vijana wanaovuja jasho mitaani wakisaka hela ya kula? Dah!

Haya mambo ndiyo yaliyofanya mioyo ya watu ikinai kazi za wasanii wetu siyo filamu kutoka nje. Eti mtu akipigwa ngumi anaangalia sehemu ya kuangukia kwa usalama wake asije kiumia. Dah!         

Kahaba lazima avute sigara, jambazi lazima avae koti refu na miwani ya giza. Hamuoni majambazi wanaokamatwa na jeshi la polisi kila siku kwenye taarifa za habari na magazeti? Wanavaa mnachoigiza? Dah!

Eti mganga wa kienyeji lazima awe porini, mchafu, halafu anaongea kwa ukali kutoa maelekezo kwa mgonjwa.

Inakuaje kwenye filamu jini anavuka barabara kwa kuangalia usalama kwanza kulia na kushoto asigongwe na bodaboda? Huyo ni jini kweli? Dah!

Filamu moja inaonesha mjini ni usiku, kijijini inaonekana ni mchana ila ni siku moja hiyo hiyo na muda ni huo huo. Hakuna uhalisia, wasanii hawavai ule uhusika kabisa.

Ni bora kuwatazama kina Mzee Majuto na Joti kwenye matangazo ya biashara kuliko filamu hizi ambazo wanataka kutulazimisha tununue kinguvu. Sawa hamtaki tuuziwe filamu za nje, kwa lengo la kutuuzia filamu ambazo jambazi anavua viatu akivamia kwenye nyumba ya mtu? Dah!

Katika mapambano ndani ya filamu mnazotaka tununue kinguvu unaweza kuzuia risasi kwa viti au meza za plastiki. Pia Mtanga au mchekeshaji yeyote ni lazima awe mlinzi kila filamu. Na siyo mlinzi tu pia awe mwehu. Taahira au zuzu.

Yaani mtu fulani fyatu asiyejielewa. Kweli Mzee Mengi analindwa na mataahira? Mnatulazimisha tuamini kuwa Mohamed Dewji analindwa na mapunguani. Wasiojielewa? Ndo somo mnalotupa kwenye filamu zenu hizo mnazotaka tununue kwa lazima? Dah!

Hapana kina JB tupeni ‘breki’. Sisi si makoro kiasi hicho, rudini nyuma kajiulizeni kwanza na hata jini ni lazima awe mwanamke?

Nadhani wanapita kwenye mfereji ule aliopita Jini Kabula na kupata umaarufu kwenye Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu. Dah!

Kutokana na haraka ya kucheza filamu nyingi kwa wakati mmoja na kubana matumizi. Siyo ajabu JB kuonekana na shati la aina moja kwenye filamu tatu. Halafu kwenye kila filamu anaachama mdomo wake (kucheka eti) kwenye kila ‘sini’. Naona hiyo ‘swaga’ imekuwa sehemu ya kiungo chake mwilini.

Hakuna uhalisia. Wasanii wetu wanaigiza tu ili mradi. Sasa usishangae filamu inayochezwa ni matukio yaliyokea mwaka 1977 lakini ndani ya ofisi husika ukutani kuna picha ya Rais wa sasa Dk John Magufuli. Bora liende. Dah!

Kila mtu akichomwa kisu lazima iwe tumboni. Familia ya kitajiri lazima waongee kizungu, dadiiii, mamiiiii. Wanatuaminisha kuwa matajiri na watu wenye uwezo wote wanastahili kuwa na tamaduni za Wazungu. Wakati nchi hii matajiri wengi ni Waarabu na Wahindi.

Ukiangalia hizi filamu tunazotakiwa kuzinunua tutake tusitake lazima ukae na ‘rimoti’ karibu maana sehemu ya kugombana sauti inapaaa hadi inakera lazima upunguze, likivuka hilo tukio ndipo uongeze tena sauti. Dah!

Kama filamu waliigizia juani utakiona kivuli cha mtu aliyeshika ‘maiki’ kinatokelezea.

Mama wa kijijini ana mkufu wa dhahabu shingoni na hereni kisha ana kilemba kichwani na kubeba kuni kachakaa nguo na kutinda nyusi na kucha za bandia. Anaongea na simu kizungu kitupu “Okay baby thanks... miss u honey”. Mama wa kijijini huyo. Dah!

Dada anaigiza kama mwanasheria anaenda mahakamani kumtetea mtu na nguo za kutokea usiku, yaani lazima akikaa mapaja yote nje. Dah!

Kituo cha polisi ni kimoja tu. Hata kama wanaishi maeneo tofauti kukiwa na kesi kituo ndio hicho hicho. Na sare zao unaweza kudhani ni askari wa Malawi na wa Comoro.Na wanajitambulisha “Sisi ni askari polisi kutoka kituo cha kati”. Ni hivyo hivyo kila filamu yenye tukio la kipolisi.

Kila anayetoa habari za maisha yake ya nyuma lazima anyanyue uso juu kisha kamera imuoneshe macho. Au lazima asogee dirishani kakunja mikono kifuani, usipoigiza hivyo kwenye filamu hizi tunazolazimishwa kununua hupewi ‘sini’.

Mwanamke amelala kapaka lip shine na make up. Mtunzi, muongozaji, mtayarishaji, mwandishi wa muswada, editor, location manager, mwigizaji mkuu na mtu wa sauti ni mtu  mmoja. Dah!

Ukute sasa wanapigana na yale makelele yao “Hwaaaaaaa... Hiyaaaaaaaaa”.

Halafu anayekuja kulipiza kisasi anafika ameshika bastola kisha anaangalia juu huku kamuelekezea mbaya wake bastola. Kamera inaonesha macho yake akikumbuka mabaya aliyotendewa nusu saa nzima, mbaya wake yupo palepale anatetemeka akisubiri kuuliwa. Dah!

Mume na mke wapo ndani ya nyumba yao lakini ukutani kuna picha ya mume na mke mwingine.

Stori zao ni kama hadithi za Madenge tu.

Baba: Madenge nikusimulie hadithi?

Madenge: Ndio baba.

Baba: Hapo zamani za kale palitokea sungura na fisi.

Madenge: Aaaah! Hiyo nishaijua, mwisho wa siku sungura atamzidi ujanja fisi!

Hizo ndo filamu tunazolazimishwa kununua sasa. Dah!

Badilikeni. Fanyeni kazi bora badala ya kuandamana kuwaumiza vijana wanaotafuta pesa za mafuta ya kupakaa watoto wao wanapoenda shule.

Suala hapa siyo filamu kutoka nje. Hapa cha kufanya ni kuwalisha walaji chakula bora. Huo upuuzi wa Wakorea utatoweka automatically kama Babu wa Loliondo. Endeleeni kuigiza mpaka namna ya kurudisha soko lenu. Mtachonga viazi.

Saturday, April 15, 2017

NDANI YA BOKSI: Mchawi wa bongo movie ni bongo movie...

 

Kim Kardashian anaweza kuwa na mpango wa kupiga picha za utupu katika jarida maarufu la PlayBoy. Ameshafanya hivyo mara kadhaa.

Na zaidi dunia nzima iliwahi kumuona akifanya ngono na Ray J, kupitia mkanda wa video waliojirekodi pamoja. Lakini haijawahi kumyumbusha akili yake na kushindwa kuendelea na mambo yake na zaidi umaarufu ukaongezeka zaidi. Biashara zake zikaendelea kubamba.

Tanzania na Marekani ni mbingu na ardhi. Hatufanani kwa kila kitu. Kuanzia maadili, uchumi na utamaduni.  Katika mpango wake huo wa kupiga picha za utupu meneja wake atamuunga mkono. Atamsisitiza. Atampa mbinu zaidi za namna ya kukamata akili za watu. Na zaidi yeye ndiye aatayesimamia shughuli nzima ya namna na kiasi cha fedha watakacholipwa. Unamfahamu meneja wake?

Ni mama yake mzazi. Marekani akili zao wanazijua wenyewe. Ndiyo utofauti wetu Tanzania na Marekani. Wakati huko mama mtu anamuunga mkono mwanaye kupiga picha za utupu, huku Tanzania mama yake Wema analumbana na waandishi wa udaku. Kwa habari yenye kichwa cha habari kisemacho “Wema, Diamond wana kwichi kwichi kisiri”.

Tuko tofauti sana na Wamarekani. Wazungu wote wako hivyo, naitaja Marekani kwa sababu sisi tunawaiga zaidi wao kuliko Wapoland au Wahispania. Kwa utofauti huo tunawaacha na utamaduni wao sisi tufanye yetu.

Msanii wa Tanzania ni tofauti na wa Marekani. Kiuchumi aina ya maisha yao na kila kitu. Kuna kitu kimoja tu tulichowazidi. Aibu ya utu.

Video ya Ndindindi ya Jide inaweza kutazamwa popote duniani. Lakini Morocco wanaweza kupiga marufuku nchi kwao video ya Rude Boy ya Rihanna. Iko hivyo. Msanii wa Kitanzania inabidi aitazame jamii yake kwanza kabla ya kuingia ‘location’ au studio kufanya yake.

Kuna wendawazimu umewaangia wasanii wetu sijui ni ushamba au kuyojitambua.

Katika ardhi ya Tanzania kutaka kufanya kile anachofanya Kardashian utachekesha watu. Utawakera. Utawapoteza. Na watakutenga.

Leo hii tunawaona wasanii wetu wakipiga picha za utupu mitandaoni. Wakiacha miili yao wazi ili tuone tattoo walizojichora mpaka sehemu nyeti.

Na hawaoni kama ni kosa kubwa kwa siku za usoni. Ila wanachoona wao ni ushamba na ubwege wa kiboya wa sisi tunaoshangaa wanachofanya. Wanawaiga kina Kim Kardashian wakati wako katika ardhi tofauti kwa kila kitu. Kardashian anaangalia jamii yake inataka nini. Ndo maana Jarida la PlayBoy linauzwa ndani ya nchi yake bila vikwazo. Huku PlayBoy zetu zimekuwa Instagram.

Wasanii wa Bongo Movie hivi sasa wana haha. Soko lao limetoweka kama ‘kaseti’ za Marehemu Lufufu. Hawatazamwi tena kwa kazi zao. Wanatazamwa kama midoli ya kwenye maduka ya nguo. Watu watanunuaje filamu zao. Kama vituko vyao watu wanavyoviona kwenye vipindi vya Shilawadu ni filamu tosha? Wasanii wa filamu wametengeneza mazingira mabovu ya soko lao wao wenyewe.

Wamewalazimisha watu wafuatilie maisha yao zaidi badala ya kazi yao. Maisha ya mitandaoni kwa wasanii wetu ni filamu tosha. Wataenda vipi kunua movie ya elfu tano wakati matukio ya kwenye filamu yapo Instagram. Unazama mitandaoni unakutana na video ya Jack Wolper akiigiza kulia chozi linamtoka anajirekodi anapost Instagram kisha anawaomba watu wampe pole kafiwa sijui na shost yake huku mtaani anakojua yeye.

Kila siku unasikia fulani ana kwichi kwichi na fulani. Habari zao zinaanzia mitandaoni redioni mpaka magazetini. Na kibaya zaidi habari zao zina mvuto kwa watu kuliko filamu zao. Habari zao za mapenzi zinasambaa kuliko filamu zao. Na stori zao ni za ukweli na zinavutia kusoma na kusikiliza kuliko stori zao za kwenye filamu ambazo ni za uongo halafu mbaya.

Watu hawawezi kununua stori za uongo ambazo hazina mvuto kwenye filamu, wakati wakitega sikio kwenye Shilawadu na kuperuzi mitandaoni wanakutana na stori zao za ukweli halafu zinavutia kwa kuzisikiliza na kutazama. Maisha yao wameyageuza kama filamu halafu filamu wamegeuza kama mikanda ya Kipaimara. Komonio. Harusi au Birthday.

Lazima soko liyumbe. Na mwenye akili ni ngumu kushangaa Monalisa na Rose Ndauka kuwa watangazaji maarufu badala ya waigizaji maarufu. Kwa sababu soko la filamu limepauka kama ukuta wa uwanja wa Kaunda pale Jangwani.

Bongo Movie punguzeni ‘vicheche’ kwenye tasnia yenu. Ondoeni wauza sura wanaotaka kulelewa kwa umaarufu. Ingizeni wasanii bora na siyo bora wasanii kwenye tasnia ya filamu.

Namna ya kupunguza siyo kuwatimua waliopo bali jiwekeeni miiko maadili taratibu na kanuni zitakazowabana wasanii ambao hawana lengo zuri na tasnia yenu.

Hakuna sababu ya kulalamikia filamu za kutoka nje ya nchi kwamba zinaharibu soko lenu.  Huo utakuwa uvivu wa kufikiri na kutenda. Ukweli ni kwamba mazingira haya ya ubovu wa soko mmeyatengeneza na kuyatukuza wenyewe.  Na bado mnayalea kwa kuyapalilia na kuyamwagilia kama mazao mashambani.

Kanumba waliingia kwenye game filamu za Kinaijeria zikiwa juu nchini. Ilikuwa ngumu sana watu kuwahamisha kwenye filamu za Kinijeria. Kwa sababu hizo ndizo zilizoua hata soko ka tamthiliya zetu.

Taratibu kwa ubora wa kazi za hapa nyumbani Wanigeria wakaondolewa kwenye soko. Wakabaki kina Kanumba. Wakasomba watu. Wakawateka ‘Wadosi’ kisha wakapiga fedha nyingi sana.

Kwa nini ishindikane leo? Ondoeni magugu maji. Achaneni na maisha ya siasa. Kulalamikia filamu za nje ni maneno ya kisiasa.

Unataka kuondoka kitu bora kinachopendwa na watu ili kuwalazimisha waangalie mikanda ya Vipaimara na Komonio mnazoita movie? Kinachowaponza Bongo Movie ni maisha ya kwenye filamu kuyaleta mtaani.

Kila kitu wanaigiza. Wanaigiza kuvaa nguo. Wanaigiza kulia hata kwenye misiba inayowahusu kwa damu kabisa. Wanaigiza kuishi kana kwamba wana kipato kikubwa sana. Na wanaigiza mpaka kwenye mapenzi. Bongo Movie vigumu sana kumuamini kwenye uhusiano wa mapenzi kwa sababu wanaigiza sana. Naamini huigiza hata kuoga na kwenda msalani.

Maisha yao ya filamu wameyaweka mitandaoni. Msanii wa Bongo Movie siyo bidhaa adimu tena. Wanapatikana sana kama mabasi ya mwendokasi. Kila dakika utamsikia redioni. Utamuona mitandaoni. Gazetini au runingani akihojiwa siyo kwa kazi yake mpya au iliyopo. Bali kwa kituko alichofanya. Mahojiano ya mastaa wetu hivi sasa ni ya nani anatoka na nani. Nani kamtema nani. Nani kaingilia penzi la nani.

Iko hivyo lakini suala la kazi yao huwezi kulisikia. Na mashabiki nao wanaenda vile unavyotaka wewe nao wanafuatilia zaidi vituko vyao kuliko kazi zao. Akiandikwa gazetini anaenda kujibu mitandaoni. Hivi hamjiulizi kwamba watu bado wanawapenda ndiyo maana wanafuatilia kila kitu mnachopost mitandaoni na kuandikwa magazetini?

Sasa kwa nini hawafuatilii wala kununua kazi zenu? Manaake ni kwamba matukio yenu ya kila siku ni rafiki kwa macho na masikio ya mashabiki wenu kuliko uongo wenu wa kwenye filamu. Shitukeni.

Ni vigumu watu kuwa na hamu na wewe au kazi yako. Wanajisifia kuwa magazeti ya udaku siku hizi hayana soko kwa sababu kila kitu kipo Instagram. Sawa ni kweli ila Instagram inakusaidia nini? Kama una wafuasi milioni mbili halafu kazi yako ya filamu huwezi kuuza hata kopi mia tano mtaani? Si kichaa hicho? Unafurahia likes na comments tu. Una wafuasi mamilioni mitandaoni ukurasa wako hauna tangazo hata moja la biashara ambalo linakuingizia pesa.

Watu wenye akili zetu tulishituka mapema sana baada ya kuona Steve Nyerere anapewa madaraka ya kumuongoza JB na Ray kwenye kikundi cha Bongo Movie. Siasa ikateka akili zao wakawaza posho za kampeni kuliko kile kilichowapa heshima na pesa kwa miaka mingi.

Kichaa kinatofautiana ila hiki nacho ni kichaa mtambuka.

Saturday, April 8, 2017

Uaminifu unazidi kuwa bidhaa iliyopitwa na wakatiJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

By Julie jkulangwa@mwananchi.co.tz

Labda umeshawahi kukutana na visa kama hivi. Ndugu au jamaa ana kupigia simu akikuomba umkopeshe kiasi fulani cha fedha na kuahidi kukurudishia siku tatu baadaye. Kwa mfano, anakupigia simu Alhamisi na kuahidi kuwa Jumamosi atakurudishia.

Huenda nawe huna kitu siku hiyo na kwa kuwa unataka kumsaidia kweli, unamwambia asikilizie kidogo ili na wewe utafute. Inapita siku, kesho yake anakupigia kuuliza kama umefanikiwa unamwambia bado unatafuta.

Ijumaa nayo inapita hakijaeleweka, inaingia Jumamosi ambayo alikuahidi kukulipa kama ungemkopesha kwa kuwa mipango yake ingetiki siku hiyo, lakini la kustaajabisha anakupigia simu kuulizia ule mtonyo uliomwahidi kumkopesha.

Sasa mtu alikuahidi kuwa angerudishia fedha hizo Jumamosi halafu siku hiyo anakupigia kukuulizia kama umepata. Maana yake alipanga kukudanganya na inawezekana hana kabisa mpango wa kukulipa. Mimi na wewe ni mashahidi kwa kiasi gani madeni yamevunja urafiki na kuwafarakanisha ndugu.

Kuchukuliana wapenzi sasa hivi ni fasheni, yale mambo ya kumwamini rafiki yako kuwa mlinzi wa penzi lako yamepitwa na wakati.

Zamani kulikuwa na msemo kuwa mtoto ni wa jamii nzima lakini siyo sasa. Mtoto anachungwa kuliko kitu chochote kwa sababu ukizubaa utakuja kulia kwa kitakachomtokea. Siyo mtu baki, hata ndugu haaminiki kuachiwa mtoto siku hizi.

Sasa hivi unapiga tu kura kwa kuwa hakuna jinsi. Unaanzaje sasa kumuamini mwanasiasa! Kwa kuwa hakuna namna inabidi ukubali tu kumpa mtu ulaji huku ukijua kabisa unapigwa changa la macho.

Ukisikia ving’ora vya gari la wagonjwa  barabarani unalipisha tu lakini moyoni unajisemea inawezekana hakuna hata mgonjwa.

Ndio. Tumeshazisikia sana hadithi za watu kutumia magari hayo kufanikisha shughuli zao za kila siku kwa hadaa kuwa wanawawahisha wagonjwa mahututi.

Umuamini nani? Polisi, daktari,  hakimu au kiongozi wa dini? Kila mmoja ana jibu lake lakini imefikia mahali hata majibu ya daktari inabidi ukajiridhishe kwa kupima katika hospitali nyinyine, kwa nini? Kwa sababu biashara imeondoa utu.

Yaani daktari hajali madhara ya dawa atakazokuandikia kwa afya yako kwa kuwa anachotaka kufanya ni kuona anaingiza fedha.

Wangapi wapo magerezani kwa makosa ya kusingiziwa. Wangapi wanaishi kwa hofu kwa sababu wakisema ukweli wataumia? Wengi tu.
Sms 0744 053 111

Saturday, April 8, 2017

NDANI YA BOKSI: Shoo ya milioni 10, shingoni cheni ya milioni 100!

 

By Dk Levy

Hasira. Inatia hasira. Kuchukuliana poa poa maisha haya. Jay Z ni mtoto wa maskini tu, aliyelelewa na mama. Atake asitake ni mtoto wa maskini. Aliyekulia sehemu za kipumbavu. Kipuuzi na kila aina ya ushenzi. Wendawazimu uliotopea.

Ila binti yake Blue Ivy, atabaki kuwa mtoto wa tajiri na atakufa akijulikana kama mtoto wa tajiri.

Jay Z kabla ya kuingia kwenye muziki aliuza sana unga. Huu unga ambao hapa katikati ulivuruga nchi.

Aliingia kwenye muziki akiwa tayari akaunti yake inasoma pesa nyingi sana. Zaidi ya dola milioni 3. Muziki ukatunisha zaidi akaunti. Akili yake ikamuweka pale alipo. Mpaka kuingia kwenye biashara ya unga ni kutokana na maisha mabovu aliyokulia. Akawa na hasira na pesa. Mungu akamuongoza na kuingia kwenye muziki na kuachana na mchongo wa kuua vijana wenzake kwa unga.

Diamond Platinumz wetu ambaye aliuza mpaka mitumba, lakini hakupata pesa, akaamua kujiingiza kwenye muziki ili apate unafuu wa maisha.

Naye kakulia kwenye umaskini kama vijana wengi ambao muziki au soka limekuwa kimbilio lao.

Kaingia kwenye muziki akiwa hana kitu tofauti na Jay Z. Hivi sasa unapoongelea Diamond Platinumz, ni kijana mdogo mwenye pesa ya kufanya afanye analotaka kwenye maisha yake katika uso wa dunia hii.

Mungu kamjaalia. ‘Of coz’ bidii yake na kujielewa ni vyanzo na sababu ya kipato chake. Kuna kitu kimoja tuwekane sawa hapa. Muziki wa sasa hivi dunia nzima, kutokana na utandawazi una maisha mafupi kuliko funza.

Pesa ya muziki kama ya soka ukishindwa kuwekeza unapokuwa kwenye chati, siku si nyingi utachekwa na hawa wanaokuzunguka kwa sasa kama mfalme. Unapopata nafasi ya kupenya na kupiga pesa. Piga pesa kila inayokatiza mbele yako. Fanya muziki ukiwa na akili ya Mangi Mchaga wa Kibosho kwenye hela.

Kusanya fedha zote kuliko serikali ya Magufuli. Huku ukilinda heshima yako. Usiichekee pesa hata sekunde. Kamata.

Angalia wanamuziki wote wa kimataifa waliokuja kutumbuiza hapa Bongo. Ni wale ambao wanapatikana kirahisi. Kwa bei nafuu. Ndo maana humuoni Justin Bieber akija. Beyonce wala Rihanna.

Kwa sababu hao na wengineo wapo ila hawapatikani kirahisi. Jay Z alikuja Bongo miaka kumi iliyopita. Eleweni nyie kizazi cha Kikwete. Jay Z hakuja kufanya shoo. Ni kama Diamond apelekwe na Tamwa au Tasaf huko Mbamba Bay, kwenye shughuli ya kijamii halafu jamii ya huko imbembeleze atumbuize kidogo.

Jay Z alikuja kwa suala tofauti na muziki. Ndiyo maana hata shoo yake ilikuwa na ‘complimentary’ nyingi zaidi kupata kutokea.

Ingetangazwa kuwa ni bure usalama ungekuwa mdogo. Ndiyo maana kiingilio kilikuwa kidogo na ‘complimentary’ zikawa nyingi kuliko taksi za Dar es Salaam.

Mwanamuziki ambaye yuko juu ndani ya Amerika huwezi kumleta aje kushika maiki na kulala kwenye hotel za Dar es Salaam kirahisi rahisi atumbuize jukwaa moja na Man Fongo na Snura. Haiwezekani.

Kwa sababu wanakuwa na ratiba ngumu na ya fedha nyingi huko huko kwao Marekani.

Msanii ambaye yuko juu ndani ya Amerika hakamatiki kirahisi hata kwenye nchi za Ulaya. Kwa sababu Marekani yenyewe inajitegemea kwa kila kitu. Li nchi kubwa kama bara la Afrika. Kuna Tanzania 50 ndani yake. Dar es Salaam kama elfu tatu. Mpaka amalizane na Wamarekani wenzake siyo leo. Asikudanganye mtu.

Wengi wa wanamuziki wanaokuja Bongo wanakuwa wamekata ‘ringi’ kwao inakuwa rahisi kuja kuambulia chochote Afrika. Kutokana na muziki kuwa na maisha mafupi. Baadhi ya wanamuziki wameamua kujikita kwenye shughuli za filamu. 50 Cent na Ice Cube ni miongoni mwao.

Wanaendelea kupiga hela huko Hollywood. Muziki umekuwa bidhaa ya Kichina. Haudumu. Ukiwa juu piga hela kama vile kesho unakufa. Piga pesa. Kusanya pesa. Kisha itunze mpaka ishike adabu. Usicheke na kima utachekwa wewe keshokutwa.

Ukitambua kuwa umetoka kwenye umasikini, kuwa na adabu na kila senti inayoingia mfukoni. Unaweza kuwa siyo mtu wa club. Siyo mlevi wala mpenda starehe za kidunia. Lakini, ukawa na udhaifu fulani ambao unateketeza pesa katika daraja lile lile la mlevi au zaidi. Kama mzinzi na mpenda anasa za kila aina.

Kama mambo ambayo mtoto wa maskini unatakiwa kuyakwepa ili kujenga baadaye yako. Hasa kwa ajili ya watoto wako. Baraka ya 40 ya mtoto kutumia mamilioni ya pesa kana kwamba ni tukio la kitaifa. Fanya kitu kingine cha kutunisha akaunti yako.

Inahitaji moyo wa kiwendawazimu kidogo. Hata kama wapo wadhamini wa shughuli kama hiyo ya 40 komonio au birthday kama siyo kipaimara. Unaweza kufanya shughuli ya kuingiza pesa zaidi na wadhamini hao hao wakadhamini na wakajitangaza.

Siri ya utajiri ni kuingiza kingi na kutumia kwa kiasi. Hakuna uchawi zaidi ya huo. Kuna shughuli za kujionesha kwa watu ambazo hazifanani na mtoto aliyekulia katika umasikini. Haya mambo yatafanywa na watoto wako ambao kwa wakati huo wataitwa watoto wa matajiri kutokana na namna ulivyowatengenezea maisha kabla.

Huu ni wakati wa kupiga pesa, siyo kuteketeza pesa.  Kuna wanamuziki wengine wanataka kuwa sehemu alipo Diamond, bila kupitia njia alizopita. Wanapata matajiri wawezeshaji wanaomba pesa za video ya soko la Afrika.

Wakati hata Tandale hajajulikana bado. Matokeo yake video ya milioni 50 inaenda kuingiza Sh3 milioni kwa shoo za Fiesta. Kutaka tu awe na video sawa na Diamond, ambaye soko lake limesambaa mpaka Sierra Leone.

Wasanii mlio nyuma ya Diamond pigeni kazi kwanza hapa Tanzania. Kamata pesa mashabiki wa hapa kabla ya kuwawaza kina Davido.

Kabla ya kuwaza kuwa na video kama ya Diamond, tengeneza himaya yako nyumbani. Kuwa na wafuasi wako unakotoka kabla ya kutafuta wafuasi kwa majirani.

Diamond hakuanza ghafla. Aliiteka Bongo, akaiteka Afrika Mashariki. Kabla hajaanza kuwakalisha kina Davido kwenye vibaraza vya mama zao huko Abuja na Lagos. Jenga himaya yako nyumbani kwanza.

Hili tatizo analo Shetta. Ni mhanga wa kutaka kuwa Diamond kabla ya kupambana kuwa Daz Baba.

Shetta alikuwa na haraka sana, na haraka hiyo imemponza. Hivi leo wawezeshaji ni ngumu kutoa mamilioni ya pesa kwa mtu ambaye hata Arusha hawezi kufanya shoo ya milioni sita peke yake. Alisahau kuwekeza mtaani kwao akataka kuwekeza kwa jirani kama Diamond.

Haraka ya matumizi makubwa ya pesa bila mipango.

Pesa za kwenda kutengenezea video Afrika Kusini, tumieni kujijenga Tanzania kwanza.

Wakati una mshangaa Shetta hata anayemuiga naye anataka kuishi dunia ya kina Mike Tyson. Anakataa shoo ya milioni 10 huku akinunua cheni ya milioni 100.

Ni pesa yake. Ni haki yake anavyotaka kuitumia. Ila tunataka kuzalisha kina Mo Dewji kupitia muziki huu.

Na hawawezi kupatikana kama wanaopata wanataka kuvaa na kuishi kama Myweither. Pigeni pesa. Wekeza vya kutosha haya maisha unayotaka kuishi watakuja kuyaishi watoto wetu.

Hasira za kuishi kwenye maisha duni lipiza kwa watoto wako. Sisi hata tutajirike vipi bado tutatambulika kama watoto wa masikini mpaka tunakata roho.

Na wadau wa muziki nchini wanahitaji kubadilika kifikra. Huu siyo muda wa kukandamizana ili wapate kikubwa kuliko wavuja jasho ambao ni wanamuziki.

Kama rahisi hivyo waambieni watoto wenu waingie studio. Wafanye kile wanachofanya kina Dimpoz, kisha wafanyisheni shoo za kujitolea kwenu.

Ni wakati wa kuwaeleza ukweli waandaaji wa shoo za nyumbani. Kwamba kabla ya kumuita Diamond kwanza ujue ukumbi gani wa kumfanyisha shoo ya kuzidi Milioni 100.

Na wasaidizi wake (Mameneja) si busara kufanya mazungumzo na mtu ambaye anataka kufanya shoo Mbagala.

Unafanya mazungumzo na mtu anayetaka kufanya shoo Vingunguti kwa ukumbi gani wa kumpeleka Diamond? Mnapotezeana muda mreefu wakati mnajua siyo tu Mbagala, Dar es Salaam hii hakuna ukumbi wa kufanya shoo ya milioni 100 kumlipa mwanamuziki tu. ‘Mapromota’ kokote mliko Bongo hii. Akili zenu zijilazimishe kuamini kuwa Diamond siyo wa nchi hii.

Hamtaki? Unafanya mazungumzo na meneja wa mtu ambaye shingoni ana cheni ya milioni 100, wewe ukatake kumpa milioni 10 kwa shoo?  Wakati miaka mitatu iliyopita alimzawadia Wema gari ya milioni 40? Mnachekesha.

salaamzao@gmail.com
Simu no  0744053111

Saturday, April 1, 2017

Miaka 17 ya Tamasha la Pasaka

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Kwa mara ya kwanza mwaka 2000 Tamasha la Pasaka liliburudisha ‘wapendwa’ jijini Dar es Salaam. Mbele ya watu  700,  waimbaji nane tu walitumbuiza kwa zaidi ya saa tano . Baadhi ya waimbaji waliotumbuiza ni Marehemu Vuyo Makohera, Faustine Munishi, Mzungu Soo na Kwaya Nuru Mtoni.

Miaka 17 baadaye Tamasha la Pasaka limejijengea heshima na kuwa  miongoni mwa yale ambayo husubiriwa kwa hamu kila mwaka. Zaidi ya wahudhuriaji 40,000 hushuhudia tamasha hilo kila mwaka katika kipindi cha miaka 10.

Tangu kuwa jukwaa linalowapa nafasi wasanii nane tu mpaka kufikia 25 haikuwa kazi rahisi. Wasanii mahiri Afrika wamewahi kutumbuiza katika tamasha hilo akiwamo Rebecca Malope, Solly Mahlangu na Sipho Makabane   wa Afrika Kusini, Ephraem Sekeleti  wa Zambia, Annastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa  wa Kenya, Kwetu Pazuri (Rwanda) na Faraja Ntaboba  wa DR Congo.

Mwanzilishi wa Tamasha hilo, Alex Msama anazungumzia safari hiyo alipokutana katika mahojiano na mwandishi wa Gazeti hili Julieth Kulangwa.

Kwa maneno machache unawezaje kuielezea safari ya miaka 17 ya Tamasha la Pasaka?

Haikuwa rahisi na kama isingekuwa wito huenda ningeishia njiani. Namshukuru Mungu ndoto yangu imetimia kwani unapozungumzia muziki wa Injili unamzungumzia Alex Msama.

Ni kwa kiasi gani Tamasha linachangia kukuza ajira nchini?

Mchango wake ni mkubwa kwa sababu kwa wastani kila mwaka huwa linatoa ajira za muda kwa watu wasiopungua 500. Kumbuka hawa ni vibarua tu kwa sababu wapo wale ambao nimewaajiri.

 Tamasha linatoa ajira kwa watengenezaji wa majukwaa, wenye vyombo vya muziki, taa, magari na wenye mapambo.  Mbali na kutoa ajira za muda lakini huwanufaisha wajasiriamali  wenye mahoteli, migahawa, usafiri ambao hunufaika unapofika msimu wa pasaka.

Mchango wa  Tamasha kwenye sanaa?

Sanaa imewaajiri wanamuziki wengi. Kama siyo muziki kwa ujumla huenda vijana wasio na kazi wangekuwa wengi mtaani. Muziki wa Injili umeajiri watu wengi pia. Tamasha linawapa jukwaa wasanii hasa wale wasiofahamika na kuwaingiza katika mfumo wa ajira za sanaa. Kwa mfano Bonny Mwaitege, Christina Shusho, Rose Muhando umaarufu wao umekuja katika jukwaa la Tamasha hili. Siyo tu linawapa umaarufu lakini linawaongezea mapato kwani baada ya hapo mashabiki wanazitafuta kazi zao hasa albamu na kuzinunua.

Mchango wa tamasha katika kukuza pato la Taifa?

Ni mkubwa. Kumbuka pale patauzwa maji ya kunywa, soda, vitafunwa, albamu za wasanii, vitabu na vitu vingine vingi. Hivi vyote vinazalishwa katika viwanda vyetu maana yake watu wanaponunua Serikali inapata kodi yake. Lakini viwanja tunakofanyia matamasha tunakodi. Tunatoa karibu shilingi milioni 20 kwa Dar es Salaam peke yake maana yake kodi inayoingia ni kubwa. Kuna wageni kutoka nje wanaingia nchini. Hapa Serikali inaanza kupata fedha kuanzia kwenye viza na vibali vya kufanya kazi nchini katika msimu wa Tamasha.

Basata wananufaika vipi na Tamasha hili?           

Kwa kifupi kazi tunayoifanya ni kuisadia Basata. Wao ndio wenye jukumu la kuwatafutia majukwaa wasanii na kuwatangaza, lakini sisi tunawafanyia kazi hiyo. Bila uwepo wa matamasha kama haya unalifanya Baraza lipate kazi ya kufanya. Tunawasaidia kuibua vipaji kazi ambayo ilibidi waifanye.

Kupitia  Tamasha waimbaji wametambulika nje ya mipaka kiasi cha kupata mialiko ya kutumbuiza huko. Rose Muhando ni mfano kwani ameshawahi kupata mkataba wa Sony na hivi karibuni atakwenda Marekani kufanya kazi.  Zote ni jukumu la Tamasha.

Katika Tamasha la mwaka huu watatumbuiza wangapi?

Tunatarajia waimbaji zaidi ya 25 kwa sababu wapo wengi wanaochipukia tunaotaka kuwapa nafasi.

Vipi kuhusu kusaidia wasiojiweza?

Kwenye kutoa misaada hatuchagui dini isipokuwa uhitaji. Tumesaidia yatima, wajane , wazee na wengine wenye uhitaji. Na siyo kwamba misaada yote ninatoa kutokana na mapato ya tamasha.

Ndugu yetu Reginald Mengi ametusaidia sana. Tukimwomba pale kunapokuwa na uhitaji wa kuwasaidia hawa wenye uhitaji anatusikia na kutusaidia. Wakati mwingine huwa anatupa matangazo bure katika media zake.

Mwingine aliyekuwa msaada mkubwa kwetu ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alikuwa karibu na sisi baada ya kugundua kuwa tuna nia njema ya kuwasaidia Watanzania wenzetu. Ninaamini Rais wetu John Magufuli atatuunga mkono.

Kumbukumbu nzuri kuhusu Tamasha la Pasaka?

Kubwa ambalo siwezi kuisahau ni pale tulipomwalika Rais Jakaya Kikwete mwaka 2011. Baada ya kumwandikia barua na kukubali kuna watu walitubeza kuwa hatakuja bali atamtuma mwakilishi.

Alitushangaza alipokuja na tulipomlilia kuhusu vibali vya wasanii kutoka nje kuwa ghali na tangu hapo tumeanza kulipa nusu.

Naweza kusema yeye ndiye aliyebadilisha upepo wa Tamasha la  Pasaka kwa kuwa nakumbuka kabla ya hapo tulikuwa tukilifanyia Diamond Jubilee ikabidi sasa tulihamishie Uwanja wa Taifa kutokana na mwamko wa watu kuhudhuria.

Kumbukumbu mbaya uliyokuwa nayo?

Sitasahau mwaka 2013 tulipata changamoto ya kukutana na mvua kila tulipokwenda kufanya Tamasha.  Maeneo tuliyotembelea watu walishindwa kutoka kwa kuwa mvua ilinyesha sana. Iringa tulipata watu 11, Songea tulipata watu kama 100 na Shinyanga watu 20. Tuliishiwa hela, tukakopa mpaka ikabidi tumuweke mtu rehani. Huyo mtu alikaa wiki ikabidi atoroke.

Kwa mara ya kwanza nilikopa mpaka nikawa na madeni yasiyolipika. Kuna wakati magari yaliishiwa mafuta ikabidi mpaka waimbaji na wao wachangie.

Kitu gani kilikusukuma kwenye muziki wa Injili?

Niliamua kutoa huduma hii kumshukuru Mungu kwa aliponitoa katika maisha yangu. Ukweli kabisa kutoka moyoni mwangu ni kwamba sipati faida yoyote katika kuendesha Tamasha, lakini nimejitoa kuhudumia. Najua Mungu ananishushia  baraka kutokana na huduma hii ninayoitoa.

Wizi wa kazi za sanaa ni kilio cha muda mrefu, nini mtazamo wako katika hili?

Serikali haijalivalia njuga suala hili. Ni jukumu la Serikali kulivalia njuga kwa sababu leo hii Rais magufuli akisema sitaki kuona cd feki mtaani zitapotea. Leo hii kila mtu anauza tu kwa sababu anajua hawezi kufanywa chochote.

Kuhusu Tamasha la mwaka huu

Tamasha la mwaka huu litazinduliwa  Aprili 16 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kuhusu maandalizi Msama anasema yamekamilika kwa asilimia 90 kwani baadhi ya waimbaji wamethibitisha kushiriki.

Waliothibitisha kushiriki ni pamoja na  Christina Shusho, Martha Mwaipaja, Jesca ‘BM’ na Goodluck Gosbert.

Wengine ni  Kwaya ya Ulyankuru Tabora, maarufu kama Kwa Viumbe Vyote iliyowahi kutikisa vilivyo katika miaka ya 1990.

Kwaya nyingine ni Kinondoni Revival Choir ambayo italitumia tamasha hilo kuzindua albamu yake mpya huku malkia wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando naye akitarajiwa kuzindua albamu yake ya Ruth.

Kiingilio

Kiingilio katika viwanja vyote litakapofanyika tamasha hilo, viti maalumu ni Sh10,000 na wakubwa ni Sh5,000 na watoto ni Sh3,000.

Saturday, April 1, 2017

Kuna tofauti kati ya msanii anayetaka kurudi na yule anayetaka kuweka heshima kwenye gemuJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

By Julie Kulangwa; jkulangwa@mwananchi.co.tz

Miaka 10 nyuma niliwahi kuwaambia marafiki zangu kuwa nitakuwa shabiki wa mwanamuziki Lady Jay Dee siku zote hata kama angeacha kuimba wakati ule.

Nakumbuka nilikuwa nasikiliza nyimbo zake kama Binti, Rafiki wa Mashaka, Mawazo, Umuhimu Wako, Siri Yangu, makini na nyingine nyingi ambazo vijana waliozaliwa enzi za utawala wa Rais Benjamin Mkapa hawazijui.

Nyakati zimebadilika na muziki haukubaki nyuma. Bongo Fleva kama kawaida huwa inasukumwa na upepo. Nakumbuka kuna wakati kwaito na sasa tumetekwa na Nigeria.

Kuna wanamuziki wanaibuka na kupotea. Wanapendwa, wanatengeneza mamilioni ya fedha na baadaye wanapotea kabisa. Lakini Lady Jay Dee yupo na heshima yake ipo palepale.

Siyo kwamba amependelewa, lah hasha, isipokuwa ipo siri moja ambayo wanamuzii wengi wangeijua kamwe wasiongepotea kwenye muziki.

Tatizo huwa linakuja pale mwanamuziki anapoondoka kwenye chati halafu akawa hana kitu na kutaka kufanya muziki wa ushindani.

Kumbuka kuna mahali ukifika unabaki kwenye ligi yako mwenyewe. Unaimba kujenga heshima na kilinda hadhi lakini siyo kushindana na wengine. Mashabiki wanakiburi sana, hasa wanapojua jamaa anataka kurudi. Wanasikiliza wimbo kwa kulinganisha.

Kuna wasanii unaona wanavyohangaika kutoka tena, lakini wanarudi kwa staili zilezile za zamani wakati muziki umeshapiga hatua umekwenda mbali.

Ukifanya muziki ‘kidon’ kama Lady Jay Dee, AY, MwanaFA, Profesa Jay na wengine inakulindia heshima yako na watu wanasikiliza au kununua kazi kama legend. Hushindani na mtu wala hushindanii ligi iliyopo.

Wanamuziki wajifunze kuwa kuna wakati hawatatakiwa kufanya muziki wa njaa. Ifike mahali jina lako liuze kazi. Yaani unaamka asubuhi unatupia sokoni albamu ya kushtukiza na ikifika saa saba mchana umemaliza mzigo.

Lady Jay Dee sasa hivi akifanya shoo wala hatumii nguvu nyingi kujitangaza kwa sababu amejijengea heshima na mashabiki wa kudumu.

Asikwambie mtu njaa mbaya na inapunguza uwezo wa kufikiri. Ukiwa na mkwanja ni rahisi pia kufanya kazi inayoendana na hadhi ya jina lako ndio maana unaona leo wasanii wanaruka viwanja kwenda kutengeneza kazi nzuri.

Muhimu wasanii wajijengee heshima na wafanye uwekezaji kwenye bisahara nyingine ili waache kuimba kwa sababu ya njaa. Watakesha.

Saturday, April 1, 2017

NDANI YA BOKSI: Darassa kazimwa na Rais Magufuli...

 

By Dk Levy, salaamzao@gmail.com , 0744053111

255 champion boy niite Mbwana Samatta haaa...” Ngoma linaanza kibabe. Linaisha kindava. Na ‘biti’ ya kikatili kama sound track ya movie la kimafia. Lazima ukae.

Alikuwa yeye tu kwa kipindi kirefu. Aliwafunika wanamuziki wote mpaka mashabiki wao. Miaka mingi imepita bila wimbo wa kutikisa nchi hii kutoka. Darassa alipokuja na ngoma yake ya “Muziki” alishitua watu na wanamuziki wenzake.

Kadiri muda ulivyokwenda ndivyo vituko vilizidi kuongezeka kupitia wimbo wake.

Achana na yule dereva huko Singida aliyeachia usukani gari ikiwa kasi kwa sababu ya mizuka ya wimbo wa Darassa. Hapo kati yalitokea ya kutokea. Totoz mitandaoni zilijirekodi zikiucheza muziki wake. Ilivutia sana.

Hata maneno kwenye wimbo yake yakageuka misemo mitaani. Ni maneno ya kila siku lakini wimbo huu ni kama ulifufua vinywa vya watu kuyatumia.

Bampa to bampa. Ni kama yale ya Nature ya “Weka kigingi niweke jiwe, weka ugoko niweke chuma”.

Ni maneno yanayotumika sana kwa watu wa mpira viwanjani na mitaani. Yapo sana ila kwa utamu wa wimbo wake yakawa kama maneno mapya.

Wimbo ulipendwa na watoto wazee na zaidi vijana. Na kilichotia chumvi zaidi ni watoto wazuri wa mjini kujirekodi wakiucheza na kutupia mitandaoni, ilizidi kunogesha utamu wa wimbo.

Ungetamani kumuona Lulu alipojirekodi akiucheza wimbo huo, kwa namna ya pekee akifuatisha midundo na maneno kwa maringo. Ilivutia.

Na ungedata na Jokate, naye alijirekodi kwa namna ya kujidekesha kama mtoto mdogo anayefundishwa kuucheza. Ilitia raha kumtazama.

 Kuna binti mzuri zaidi na mdogo zaidi ambaye alijirekodi ndani ya duka la nguo. Kila mwanaume mkware mitandaoni alitamani kumfahamu yule binti.

Umbile lake sura na namna alivyokuwa akiufuatisha wimbo huo uliwachanganya akili. Hasa pale anaposema “Waote mapembe waongezee mkia”.

Kila mtu alimuongelea Darassa na wimbo wake. Ni kama ulikuwa wimbo wake wa kwanza kumbe ana nyimbo kibao kabla.

Ndiye mwanamuziki pekee ambaye alipita katikati ya msitu mzito wa Diamond na Kiba. Akapasua na kuwaacha wakiwa hawaamini kinachotokea. Ikawa ngumu sana watu kusikiliza wimbo mpya.

Ujio wake lilikuwa pigo kwa Ommy Dimpoz na “Kajiandae” akiwa na Kiba. Rich Mavoko na “Kokoro” akiwa na Diamond. Mwana FA na “Dume Suruali” akiwa na Vanessa Mdee.

Wote hao nyimbo zao zilizimwa ghafla. Wakatoweka.

Masikio ya Watanzania yalielekezwa kwa Darassa. Bila Darassa wimbo wa FA “Dume suruali” ungekuwa habari ya mjini. Hata Dimpoz na Mavoko walikuwa na ngoma kali wakiwa wamewashirikisha miamba mikubwa. Lakini haikuwasaidia kuepuka kikombe kichungu cha Darassa. Ulikuwa wimbo wa Taifa unaoanza kindava. Unaisha kibabe. Na mdundo ni wa kikatili. Lazima unyooshe mikono juu.

Kama una roho nyepesi unaweza kulisusa na game lenyewe la muziki. Ujio wake kwenye wimbo huu hauna tofauti na ule ujio wa marehemu Ngwair na “Mikasi”. Ferouz na “Starehe”. Profesa Jay na “Ndiyo Mzee”. Nature na “Sitaki demu”.

Hapo katikati ulipita muda mrefu bila kutoka wimbo wa kushitua watu na kusambaa kwenye mioyo ya watu wa rika zote mpaka balaa la Darassa lilipotua kama bomu la nyuklia mwaka jana.

Ukatili aliofanya kwa wanamuziki wenzake hauna tofauti na ule wa Inspector Haroun na “Mtoto wa Geti Kali”. Watu walitaka kumsikiliza Inspector kila wakati kuliko taarifa ya habari.

Darassa baada ya wimbo wake huo, alichoshwa na safari kwenda kwenye shoo. Alikerwa na simu yake kwa mapromota na waandishi. Akaumizwa bega kwa ‘hagi’ za mashabiki hasa totoz.

Wanawake wepesi kutoa heshima kwa mtu maarufu kwa salamu au kuomba kupiga naye picha. Tofauti na wanaume wanapenda kukaza bila sababu ya msingi hasa Wabongo wanapokutana na staa.

Kila kona ni Darassa. Lakini hii leo unamsikia tena Darassa? Ni rahisi kumsikia Harmorapa kuliko yeye. Muda hauna fadhila na mtu.  Muda wa wimbo wake umeshapita. Leo hii Nay Wa Mitego ndo kitu kinachoendelea kwenye vinywa vya watu.

Kama zali tu, wimbo wa kawaida. Maneno ya wimbo huo ndo tunayoyaona kwenye post za watu mitandaoni.

Wakati watu wakifurahia comments na likes za watu mitandaoni. Yeye alichofanya ni kuchukua maneno hayo akayatengeneza kwenye mtindo wa mashairi, midundo na kutiririka nayo. Kitu kimeitika.

Hafurahii likes na comments kama za wale wa mitandaoni. Ila anachekelea pesa anayoingiza kupitia wimbo huu.

Ukitaka ‘stress’ za kujitakia kwa sasa, fanya shoo moja na Nay. Shangwe atakazopata unaweza kutamani kuacha muziki na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji.

Masikio ya Watanzania wanataka kusikia kile alichoimba Nay. Huu siyo muda rafiki na nyimbo za kubembelezana kimapenzi. Serikali yenyewe haibembelezani na mtu. Ni kanyaga twende siyo muda wa ‘Ala za Roho’ na kina Diva.

‘Dai’ na Kiba wakomae kimataifa tu. Kwa sasa muziki wa Bongo unataka kile alichofanya Nay. Huu ni mwanzo tu kuna mipini kibao inakuja.

Watu walikuwa wanasubiri tobo wazame. Alianza Darassa kila mtu mpenzi wa muziki aliona kwamba Hip Hop imerudi kupitia akili ya Darassa, sasa kuna Nay naye kadondosha fataki. Subiri mabomu zaidi na mkuu karuhusu watoto wa ‘kihuni’ wafanye kile roho inataka kwa sasa. Kama Nay alichosema kichaa kapewa rungu.

Ni kama fisi aliyekutana na mzoga. Kuna kundi la ‘wahuni’ wanapishana kwenye milango ya studio kuandaa ngoma. Unadhani wimbo wa Darassa “Muziki” ulikuwa bora kuliko nyimbo zake zote alizowahi kutoa? Usijidanganye, unaweza kuwa ndo wimbo wake wa kawaida ambao hakutumia akili nyingi na muda mrefu kuandaa. Ni wakati tu na ukifika hakuna wa kuzuia.

Watu walichoka na mwendelezo wa watu wawili tu kila siku ndiyo ukweli. Masikio yalikuwa yanataka kitu kipya tatizo waliokuwa kwenye mtiririko hawakuweza kufanya kitu bora zaidi ya wawili hao.

Darassa akaja kuvunja mwiko kibabe. Ndivyo ilivyo kwa Nay. Wimbo wake wa “Wapo” siyo bora sana kuliko nyimbo ambazo amewahi kutoa huko nyuma ila katoa kitu muafaka kwa wakati muafaka. Mwache apige pesa. “Wapo” ndo kitu pekee kinachosikilizwa kwa sasa Tanzania.

Siyo kwamba “Wapo” ni bora sana kuliko “Muziki” yawezekana “Muziki” ukawa bora zaidi ila wakati hauna ndoa na mtu.

Nay kapata zari kubwa na ni miongoni mwa Watanzania wenye bahati kubwa na utawala wa Magufuli kwa kilichotokea.

Kazi ngumu sana katika sanaa ya muziki inayochukua muda na pesa kuifanya, yeye imefanyika ndani ya saa 24 tu.

Promo ya wimbo kwa sasa si jambo dogo, ila Mheshimiwa Mwakyembe na Rais Magufuli wamemrahisishia kazi huyu Mchagga nusu na Mnyakyusa.

Wimbo wake ungepita tu kama upepo wa feni. Kama ilivyo post za watu mitandaoni. Kukamatwa kwake kumefanya kila mtu atake kujua sababu. Alipoambiwa sababu ni wimbo, akataka kujua hiyo sababu ya wimbo ikoje.

Matokeo yake ni kila mtu hata ambaye hana muda na Bongo Fleva akataka kusikiliza. Akasikilizwa.  Bao kubwa zaidi ni kitendo cha Rais Magufuli kuufagilia na kuamuru aachiwe na wimbo wake upigwe kila sehemu na aongeze vionjo.

Hii ni bahati ya mtende kuota Jangwani. Ni shangwe na kicheko tu kwa Nay. Hana muda tena wa kupiga simu kwa watangazaji na madj kuwaomba waupige. Ila Kazi inabaki kwao kumsaka Nay kwa ‘intavyuu’ kila siku.

Magufuli ni kama kocha ambaye kamtoa mchezaji uwanjani aliyeanza kukata pumzi na kumuingiza mchezaji kwenda kuziba nafasi yake.

Kasaidia kumeweka kando Darassa ili kumpisha Nay.

Darassa tatizo ni Magufuli siyo Nay.

Saturday, April 1, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: Uking’wafua ni lazima ugugumie

By Gaston Nunduma

Wafalme wa zamani walikuwa na mambo ya ajabu sana. Walikuwa wakibuni mambo ya hatari sana kwa nia ya kujifurahisha tu. Yupo mmoja alishurutisha kushonewa vazi ambalo lingeonekana kwa watu wema na wenye akili tu. Mwingine ati alitaka kupigiwa hadithi isiyokwisha; vinginevyo angechinja watu!

Siku hiyo alikusudia kuanza kupokea posa za harusi ya binti yake. Sasa kwa kuwa alikuwa tajiri wa fedha na mali, akasema “sihitaji ng’ombe wala dhahabu. Atakayeweza kunisimulia hadithi isiyo na mwisho ndiye atakayekuwa mkwe wangu. Lakini nitawachinja wote watakaojaribu na kushindwa”.

Basi kwa urembo wa binti, vijana wengi walipoteza vichwa. Kila mmoja alifanya mazoezi ya hadithi isiyo mwisho, lakini bila kutaraji akajikuta akiimaliza kwa kusinzia mbele ya Mfalme tajiri. Matokeo yakawa ni yaleyale yaliyokusudiwa: vichwa vyao vikatenganishwa na viwiliwili.

Kijana mmoja baada ya kuusoma mchezo vizuri alikwenda kwa Mfalme. Akakaribishwa kama wenzake waliotangulia kwa maakuli na vinywaji. Jua lilipozama aliketishwa mbele ya baraza ya Mfalme, mchinjaji akaitwa na kijana akaamuriwa kuanza hadithi, naye akaanza:

“Hapo kale paliondokea sisimizi mdogo. Aliishi kwa amani na utulivu akicheza peke yake kando ya njia kuu. Siku moja alipokuwa mchezoni alisikia vishindo vikubwa. Akakimbilia kujificha nyuma ya chembe ya mchanga.

“Kwa mbali alimshuhudia kiumbe mkubwa aliyebeba mzigo mkubwa na mzito sana. Yule kiumbe alikanyaga kando ya mchanga uliomkinga sisimizi mdogo. Guu lake liliacha shimo kubwa na matone mawili ya mfano wa mchanga yaliangukia humo.

“Sisimizi aliogopa sana. Alikimbia hadi nyumbani kuwaeleza wazazi jinsi alivyonusurika. Akawaeleza juu ya matone yale mawili yaliyong’ara mithili ya vito vya thamani. Wazazi wakaingia shauku ya kutaka kujua zaidi kuhusu alichokiona mwana wao.

“Waliondoka naye mpaka kwenye eneo la tukio. Hammadi! Walikuta ni matone ya sukari. Walijitwisha na kurudi nayo mbio hadi kambini. Kamanda wa zamu alipiga mbinja na kuamuru sisimizi wa kazi waingie kufanya msako katika eneo lile.

“Basi bwana... kikosi kikaingia kazini. Kilikagua mashimo yaliyoachwa na kiumbe yule na kugundua kuwa zilikuwa nyayo za binadamu. Sisimizi mzee aliwakumbusha wenzake kuwa huyo alikuwa mkulima mwenye ghala kubwa. Akawaongoza wana kikosi hadi ghalani ambako walikuta shehena kubwa ya magunia ya sukari.

“Hapo sasa kazi ikawa ni moja tu: kuhamishia shehena ile kambini kwao…

“Kila mmoja alibeba donge moja la sukari na kulipeleka kambini. Kiongozi wa msafara aliamua kuanza na madonge yaliyotawanyika sakafuni kabla ya kuingia kwenye magunia. Maafisa wengine walibaki kambini kwa ajili ya upokeaji na upangaji wa sukari.

“Wakarudi tena, kila mmoja akabeba donge na kuondoka…”

Basi kutokea hapo kijana msimulizi wa hadithi aliishikilia sentensi ya mwisho, akainakili na kuibandika tena na tena. Wacheza disko watanielewa nikisema “alifanya looping” ila tu aliongeza vionjo vya kuchoka kwa kikosi kimoja na kupokewa kazi hiyo na kikosi kingine.

Mfalme akaanza kusinzia maana chupa tatu za kahawa zilishamshinda. Akauliza; “Baada ya hapo kulitokea nini? Akajibiwa: “Walirudi tena, wakachukua madonge yao na kuondoka”. Kila aliposinzia, Mfalme aliamshwa na maneno yaleyale: “Wakarudi tena, kila mmoja akabeba donge moja na kuondoka…”

Mfalme sasa akawa na hali mbaya. Kila mmoja anaelewa jinsi usingizi unavyowasha na kulevya. Kama huelewi mtazame mtoto aliyeshikwa na usingizi jinsi anavyojikuna na kupiga mayowe. Hivyo Bwana Mkubwa aliona ni bora yaishe, kijana akafanikiwa kumuoa binti Mfalme.

Usipoangalia unaweza kumcheka Mfalme huyu. Lakini ukifikiri sana utajionea huruma kwa jinsi nawe unavyoamshwa na kupewa tamthilia isiyo na mwisho. Tumekuwa mabingwa wa kuanzisha mambo, kuyakatiza na kuanzisha mapya.

Wakati huu tunaopania kuwa na Tanzania ya Viwanda hatukutegemea kuhangaika na mwanga wa vibatari. Tunakumbuka kipande cha hadithi kilichokopiwa na kupestiwa katika kitabu kizima: “Tukifungua vituo vya Kinyerezi, shida ya umeme itakuwa historia…”

Lakini, kila leo umeme unakatika. Nimejaribu kuwauliza hawa ndugu zangu waliojitwisha au kutwishwa dhamana hii kubwa wakanijibu: “Kwani huoni tunabadili nguzo chakavu? Au hujui kuwa transfoma zenu zimepitwa na wakati? Hivi unadhani hizo nyaya zipo salama?

Huwezi kusema unaendelea kwa kufaulisha Walimu wazuri bila kujenga Shule stahiki kwa ajili yao. Vinginevyo utawaacha wakizurura wakati ukifikiria namna ya kupata fedha za ujenzi wa Shule hizo. Hali kadhalika unapojenga Shule za Mkoa, Manispaa, Tarafa hadi Kata bila kuwa na Walimu ni kazi bure.

Mfano mzuri zaidi ni pale unapohesabu maendeleo kwa wingi wa magari yanayoingia nchini kwako. Kabla hujakaa sawa unaanza kuweweseka na wingi wa foleni katika kila mtaa. Jawabu litakujia kuwa kumbe kila gari huchukua nafasi ya barabara. Hivyo ni jukumu lisiloepukika kuboresha miundombinu ya barabara sanjari na wingi wa magari yanayoingia.

Hata ukijenga wodi zenye viyoyozi kwenye Hospitali za Serikali, bila kuwa na Madakitari wa kutosha utakuwa umefanya kazi ya bure.

Ni jambo la lazima kuanzia chini wakati ukienda juu. Huwezi kujenga nyumba pasi na kuanzia kwenye misingi. Na hakika ukijenga juu ya mchanga nyumba itaondoka na upepo. Vilevile ukijenga nyumba imara juu ya msingi imara ni lazima upaue kabla ya kufikiria kununua magari.

Maendeleo ni kwenda juu ukitokea chini. Kama unaanzia juu kwenda chini, tafadhali tafuta neno la kinyume cha maendeleo kabla sijakutafutia.

Maswali na majibu piga na sms kwa simu: 0713-248943

Saturday, March 25, 2017

Dj Sinyorita kutoka XXL mpaka redioni kwakoAkiwajibika jukwaani

Akiwajibika jukwaani 

By Kelvin Kagambo, Mwananchi

Madj ni watu muhimu kwenye muziki. Ni mfano wa ngazi zenye uwezo wa kushusha au kuupandisha wimbo wowote pale wanapoamua. Ili kuthibitisha umuhimu wao jua kwamba, u-Dj ni moja ya nguzo za  muziki wa Hip Hop.

Hata hivyo, duniani kuna idadi kubwa ya ma-Dj wa kiume kuzidi wa kike na hii imesababisha kazi hii kuonekana ni ya kuime, ingawa kuna baadhi ya wanawake wamevunja fikra hizo kwa kuamua kujitosa kwenye tasnia na kufanya u-Dj,  miongoni mwao ni Dj Sinyorita.

Jina lake halisi ni Aisha Said. Ni Dj katika kituo cha redio Clouds FM na kazi zake zinasikika mara nyingi kwenye kipindi cha XXL kinachoruka kuanzia saa 7.00  mchana mpaka saa 10.00  alasiri kuanzia Jumatatu hadi  Ijumaa.

Kutokana na upekee wa kazi anayoifanya, Starehe ilimtafuta na kufanya mahojiano naye ambapo amezungumzia mengi kuhusu kazi na maisha yake.

Starehe: Lini uligundua una wito wa kuwa Dj?

Dj Sinyorita: Muda mrefu sana, tangu nikiwa shule. Nilikuwa napenda sana kusikiliza muziki na kwa kipindi kile Dj wa kike Tanzania niliyekuwa namsikia alikuwa ni Dj Fetty tu. Kupitia yeye nikajikuta natamani sana kuwa Dj na nikahisi kwamba natosha kabisa kuingia katika taaluma hii.

Starehe: Kwa hiyo safari yako kwa ujumla ilikuwaje mpaka kufikia hapa ulipo?

Dj Sinyorita: Kwanza niseme tu mimi nimekulia na kusomea Dodoma na ili kutimiza ndoto yangu nilihisi kuna ulazima wa kutoka kule kwenda Dar es Salaam. Nilipofika nikaunganishwa na bosi mmoja wa ‘Maisha Club’, nikamueleza shida yangu kwamba nahitaji kujifunza u-Dj, na akanisaidia kwa kunikabidhi kwa Dj wa hapohapo ili anifundishe. Nakumbuka mtihani wa kwanza kupewa niliambiwa nikatafute nyimbo zisizopungua 200 niziweke kwenye CD na nilipewa mtihani huu kama kipimo cha kwamba najua muziki kwa sababu Dj yeyote silaha yake ni nyimbo nzuri.

Baada ya pale nikaendelea kufundishwa jinsi ya kuchanganya nyimbo na vitu vingine muhimu. Kipindi hicho nilikuwa naishi Ubungo na Maisha Club ipo Masaki, kwahiyo nilikuwa naenda kila siku kujifunza. Baada ya kuweza kidogo nikajiunga na kundi moja la ma-Dj. Huko walikuwa wanafundisha lakini pia walikuwa wanapiga muziki kwenye kumbi za starehe kila mwisho wa wiki, kwa hiyo na mimi nilikuwa nazunguka nao na kuna wakati nilikuwa napata fursa ya kupiga. Baada ya pale nikaingia kwenye mashindano ya u-Dj ya Street Music, huko nilikuwa Dj wa kike peke yangu na nakumbuka nilifika mpaka fainali lakini sikufanikiwa kushinda. Kisha baadae nikapata kazi Samaki Samaki na hapo sasa watu ndiyo wakaanza kunijua, na chaneli zangu zilipokomaa nikapata ajira ‘East Africa Radio’; nilipotoka hapo ndo nikapata nafasi hapa Clouds Fm.

Starehe: Wazazi wako wana maoni gani kuhusu hiki unachokifanya?

Dj Sinyorita: Mimi kwanza wazazi wangu wametengana na hata kule Dodoma nilikuwa naishi na mama tu; baba yangu yupo huku Dar. Na nikushangaze tu kwamba mpaka leo hii, baba yangu anasikia juu juu tu kwamba mimi ni Dj, sijawahi kumwambia. Mama yangu yeye anafahamu kwa sasa lakini mwanzo ilikuwa ni ngumu sana kunielewa.

Starehe: Unamaanisha nini unaposema hujawahi kumwambia baba yako kuhusu kazi unayofanya; kwani huna mawasiliano naye?

Dj Sinyorita: Nina mawasiliano naye lakini hatuna ukaribu namna hiyo, si unajua tena haya mambo ya wazazi kutengana?

 Starehe:  Katika konakona zote ulizopitia kuelekea ndoto yako, umekutana na changamoto gani kama Dj wa kike?

Dj Sinyorita: Kuwa Dj mwanamke kuna changamoto kwa kweli na moja kubwa niliyokumbana nayo ni kutoheshimiwa na baadhi ya watu. Yaani kuna mtu mwingine kwa sababu wewe ni mwanamke na unafanya u-Dj basi anakuchukulia poa tu, anakuwa na mtazamo hasi juu yako. Lakini changamoto nyingine ni kwamba kwa Tanzania bado u-Dj haujawa kazi ya kuthaminiwa, ingawa kuna baadhi ya watu na makampuni wanafahamu umuhimu wetu ikiwemo Clouds Media, lakini wengi wanatuchukulia kama watu wa kawaida tu wakati sisi ni watu muhimu kwa ajili ya kukuza muziki.

Starehe: Je unafikiria kwenda shule kuongeza utaalaamu zaidi juu ya hiki unachokifanya?

Dj Sinyorita: Ndiyo nina mpango huo, lakini nikienda sitasoma u-Dj pekee, nafikiria kwenda kusoma muziki kwa ujumla kwa sababu nina mpango wa kuwa mtayarishaji wa muziki.

Starehe: Jina la Sinyorita limetoka wapi?

Dj Sinyorita: Sinyorita ni neno kutoka katika lugha ya Kihispaniola na linamaanisha ‘mwanamke’;  kwa hiyo mimi niliamua kuongezea Dj hapo mbele ili limaanishe Dj Mwanamke.

Starehe: Kila binadamu ana uwezo na mapungufu katika kazi anayoifanya. Wewe uwezo wako katika u-Dj upo kwenye nini na mapungufu yako yapo kwenye nini?

Dj Sinyorita: Mapungufu yangu ni kwenye baadhi ya ujuzi tu, yaani kuna mambo ma-Dj wenzangu wanafanya lakini mimi bado sijayaweza. Na uwezo wangu ni kwamba najua kuchagua nyimbo nzuri, najua kuchanganya nyimbo lakini pia nina muonekano mzuri.

Starehe: Vipi kuhusu uhusiano?

Dj Sinyorita: Aaah! Mimi sina mchumba wala sijaolewa, ila nina mpenzi na tupo katika uhusiano kwa muda mrefu, karibu miaka mitano sasa.

Starehe: Huyu mpenzi uliyenaye anaichukuliaji kazi yako?

Dj Sinyorita: Hana tatizo kwa sababu hata yeye ni Dj pia na ndiye aliyepewa kazi ya kunifundisha kipindi nilipofika Dar es Salaam kutoka Dodoma.

Starehe: Nje ya u-Dj unafanya nini kingine cha kukuongezea kipato?

Dj Sinyorita: Sifanyi kwa kweli, lakini nina mipango ya kujaribu ujasiriamali siku za usoni.

Starehe: Mtaani kuna ma-Dj wa kike ingawa ni wachache, Je wewe umeshawahi kufikiria kuwasaidia labda kwa kuanzisha lebo ya ma-Dj wa kike?

Dj Sinyorita: Nimewahi kufikiria lakini kwa sasa hivi hicho kitu siwezi kukifanya kwa sababu kwa mtazamo wangu hata mimi bado sijawa imara kiasi cha kuweza kuwabeba wengine. Labda tu ninachokifanya kwa sasa ni kuwasaidia ushauri.

Swali: Madj wa Tanzania mnalalamikiwa kwamba mnapiga nyimbo nyingi za nje hasa Nigeria kuliko mnavyopiga za nyumbani. Wewe unalizungumziaje suala hili?

Dj Sinyorita: Tatizo letu Watanzania hatupendi kuukubali ukweli; na naomba nisieleweke vibaya katika hili. Hivi kama wimbo wa Nigeria umetengenezwa vizuri kuzidi wa Tanzania kwa nini mimi kama Dj nisiucheze wa Nigeria? Katika hili dawa si kulalamika, ni wasanii kujituma ili kazi zao zivutie. Lakini kwa kuongeza ni kwamba, Dj mwenye maadili hapigi nyimbo kwa upendeleo, anapiga nyimbo yoyote nzuri.

Swali: Je, una mtoto au labda umeshawahi kubeba ujauzito?

Dj Sinyorita: Sina mtoto, ila nilishawahi kupata ujauzito zamani. Lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa kujifungua, mimba ilitoka.

Swali: Mikono yako ina uwezo wa kufanya kazi gani mbali na u-Dj?

Dj Sinyorita:  Kusuka siwezi  ila nafanya kazi zote za nyumbani. Nafua, naosha vyombo na napika pia. Tena hapa kwenye kupika ndio usiseme, naweza kupika pilau, biriani, wali, chapati, maandazi, dagaa, mlenda na ninaposema kupika namaanisha kupika, yaani nikiingia jikoni vinanukia si mchezo.

Swali:  Unaweza kueleza jinsi unavyokumbana na usumbufu kutoka kwa wanaume wanaokutaka kimapenzi?

Dj Sinyorita: Ishu ya mtoto wa kike kusumbuliwa na wanaume  ni jambo la kawaida, si kwa ma-Dj wa kike tu, kila mwanamke mzuri. Na kwa taarifa yako mtoto wa kike usipokuwa unatongozwatongozwa unaweza kujikuta unakwenda kwa babu ukidhani labda una gundu. Binafsi nasumbuliwa lakini najua jinsi gani ya ‘kudeal’ nao.

Starehe: Mashabiki walikuwa wanamshindanisha Diamond na Alikiba, lakini mara wakamletea Diamond mpinzani mwingine ambaye ni Darassa. Kwa mtazamo wako unahisi nafasi ya Diamond inafikika?

Dj Sinyorita: Inafikika kabisa  lakini ni lazima huyo msanii anayetaka kumfikia Diamond aongeze juhudi mno kwa sababu Diamond ni msanii mkubwa  na kila siku anazidi kufanya vitu vikubwa, anazidi kwenda juu, hashuki, kumfikia ni kazi ngumu lakini inawezakana kwa asilimia mia moja.

Saturday, March 25, 2017

Samahani naombeni ‘mnisaidie kushea’ makala hiiJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

By Julie ; jkulangwa@mwananchi.co.tz Sms 0744 053 111

Mitandao ya simu nadhani ndizo kampuni pekee nchini zinazoendelea kupata faida kubwa katika mauzo ya data. Kwa Mtanzania mwenye smartphone wakati huu sidhani kama anaweza kukaa siku moja bila kununua data. Kuliko kupitwa na ubuyu mitandaoni ni bora kukosa kula.

Mambo yamekuwa mengi kiasi kwamba kuna vitu vizuri vinatokea katika tasnia ya burudani halafu havipati tena kiki au nafasi ya kung’aa katika media zetu na mitandao ya kijamii.

Darassa na muziki wake wamesumbua kwa miezi minne kama sikosei, kila aliyejaribu kutoa wimbo alibuma  au kama alipata airtime basi ilikuwa kidogo tu.

Nakumbuka kuusikia wimbo wa Darassa ukipigwa hata mara tano kwa siku katika kituo kimoja cha redio au televisheni na huko klabu usiseme.

Lakini hapo katikati upepo wa mjadala ukabadilika, kiki zikachukuliwa na wenye kiki zao. Kwa miezi miwili sasa ni watu wachache wanaofuatilia burudani ndiyo wanaweza kuwa na taarifa sahihi za kinachotokea katika tasnia hiyo.

Kuna mapinduzi yamefanyika katika filamu lakini ni kama vile sicho tulichokuwa tukikipigania. Filamu ya Homecoming imezinduliwa kwa kishindo lakini mwangwi wake umeshindwa kuakisi kutokana na kinachoendelea nchini.

Nimeamua kuandika kuwakumbusha na kuweka kumbukumbu kuwa katikati ya yanayotokea nchini, kwenye burudani kuna vitu vinaendelea.

Jay Mo ametoa wimbo wake Nisaidie Kushare, Profesa Jay ametoa wimbo wake alioubatiza jina Kibabe, Shishi Trump naye ameachia ngoma yake Hatutoi Kiki na Baraka The Prince ameingiza mtaani wimbo wake Niende.

WCB nao wameathirika katika hili kwani Harmonize naye ametoa wimbo Niambie na bila kusahau Rockonolo wa Lomino ambao Diamond ameshirikishwa nao upo hewani.

Ollah wa Christian Bella akishirikiana na Kalighaph Jones wa Kenya  nao upo kwenye chati mbalimbali nchini hivyo ni vyema kuliweka katika kumbukumbu zetu.

Najua zimetoka nyimbo nyingi na video za kutosha hivyo sitaweza kuziweka katika kumbukumbu hii lakini ikumbukwe kuwa kuna mambo yanafanyika katika tasnia nyingine nchini na mimi kama mdau inabidi nisaidie kuwakumbusha.

Katika kuweka sawa kumbukumbu nyingine ni kwamba Baraza la Sanaa (Basata) limetangaza kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sanaa ili kuwahamasisha waendeleze vipaji.

Huenda kuna mengine yamenipita kwa sababu na mimi sipo nyuma katika kufuatilia yanayojiri nchini.

Saturday, March 25, 2017

NDANI YA BOKSI: Jide anapogeuza mapenzi kuwa pesa...

By Dk Levy; salaamzao@gmail.com Simu no 0744053111

Mtoto mmoja wa Kikurya yupo mjini miaka mingi. Umbo lake halina uhusiano mwema na uzito wa jina lake.

Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’. Ukiwa mvivu wa kutanua mashavu yako muite Jide.

Miamba mingi kwenye muziki imedondoka kwa kujitakia au kwa mapenzi ya Mungu.

Wapo ambao wapo kama hawapo, yaani wapo hai kwa jina kubwa bila kufanya vitendo vilivyowapa majina makubwa.

Yeye yupo, anaendelea kufanya kilichompatia jina, fedha na kundi la marafiki. Wakati wengi walioanza naye muziki wakiwa hawana tofauti na mateja na wengine wakiingiza fedha kwa njia zingine, yeye kakomaa kama ruba na muziki.

Muziki umemfanya awe daraja moja na Mwamvita Makamba, kimo kimoja na Shy-Rose Bhanji pia ni ngumu kumtenga Jide na Madam Rita Paulsen, wakati wao wakiingiza fedha, wakijenga nyumba, wakisukuma ndinga za maana kwa ajira, biashara na siasa. Yeye yupo kwenye foleni yao kupitia muziki.

Anasukuma ‘ndinga’ anayostahili mwenye PhD. Anaishi kwenye nyumba kama ya mwenye Masters na anakula chakula anachostahili Profesa. Kama anatumia kinywaji bila shaka bili yake haiendi mbali na ile ya Andrew Chenge. Ni mule mule ila yeye anatunisha akaunti kwa muziki.

Miaka kati ya 2000 hadi 2010 kuna mwanamuziki ambaye kwa sasa ni marehemu, alikwenda kupokea fedha nyingi kwa ‘Wadosi’ pale Kariakoo kando ya Kituo cha Polisi Msimbazi. Ni fedha za mauzo ya albamu yake.

Aliondoka na pesa taslimu mkononi. Unategemea nini? Wakati mwingine tusiwalaumu hawa vijana. Walikosa muongozo na elimu mbadala nje ya kazi yao ya muziki. Aliondoka na ‘keshi’ si kwa kupenda au kwa kuwa mtoto wa mjini. Au alikuwa rafiki na majambazi kiasi cha kutoweza kumpora. Hapana. Hakuwa na akaunti benki.

Fedha iliisha kirahisi kama alivyoibeba, huwezi kupanga matumizi ya pesa ikiwa mkononi, mipango hufanikiwa ukiwa huna fedha mkononi.

Ukiwa nayo mkononi matumizi yana nguvu kuliko mipango. Vijana wengi wa Bongo Fleva wakati ule fedha zao zilitafunika kirahisi kwa kukosa usimamizi. Si yeye tu, staa mwingine wa kitambo kwenye muziki alipata dili la kutengeneza wimbo wa taasisi moja ya Kijerumani. Alipewa milioni tatu ‘keshi’ kwa wimbo mmoja. Enzi za Mkapa ni kama milioni 30 kwa sasa. Alipewa Ijumaa, akawa na shoo Dodoma Jumamosi, kwa kutokuwa na akaunti akamuachia yote mdogo wake amtunzie mpaka akirudi siku ya Jumapili.

Aliporudi alikuta chupa tupu za bia mezani, mdogo wake na wapambe wakiwa hawajitambui, wamezima kwa pombe za siku tatu mfululizo. Akaishia kuwatengenezea Wazungu wimbo bure.

Wengi wao fedha zilitoweka kiwepesi kama walivyozipata. Hilo Jide aliliona, wakati kaka zake wakikosa muelekeo yeye alikuwa ananunua kinanda, maiki, spika na tumba kimya kimya. Chini ya usimamizi wa kiumbe kinachoijua fedha ya burudani kuliko bafu lake, Ruge Mutahaba.

Kwa miaka mingi alikuwa chini ya Ruge na akili yake ilikubali kuongozwa na ikatii. Hata kama faida ya kuongozwa ilikuwa kubwa kuliko dhuluma au maumivu ya kutumikishwa kwake.

Ambao hawakuwa na usimamizi mzuri fedha za shoo walichukulia baa na kuziacha baa.

Hata ‘kopi’ za albamu zao waligongea mihuri baa, wangeacha deni la bia kaunta mbio kwa ‘Wadosi’ kufuata fedha za mauzo ya albamu na kuzipeleka kaunta. Totoz na nyama choma.

Starehe ni shimo la mauti ya mafanikio ya wanamuziki wengi wa kizazi kipya.

Ungeweza kuwakuta wanamuziki Rose Garden vifua wazi jasho linawatoka, wanagonga bia na kugonga mihuri ya kopi zao za albamu.

Kwa waliomfuatilia Jide toka anaanza muziki wana vitu vya kumhusudu; sauti nzuri, utunzi bora na aina ya maisha anavyoyaendesha na kujikuta ni mwanamke na nusu. Haikushangaza kumiliki bendi ya Machozi.

Wema anapita kwenye kivuli cha Jide ila njia tofauti, Jide anapita kulia Wema kushoto, majina yao yanaendelea kung’ang’ania kwenye kilele cha umaarufu kwa sababu ya mapenzi.

Wema vituko na ‘drama’ zake za uhusiano wa kimapenzi zinamfanya aendelee kuongelewa kwenye vyombo vya habari na mitandaoni.

Jide ni tofauti. Ni mapenzi yale yale ila kwake yanamfanya aendelee kutengeneza fedha. Moja ya sifa ya Jide ni kutopenda habari za uhusiano wake kuandikwa magazetini. Hajawahi kuwa rafiki na magazeti ya udaku, mambo yake ya mapenzi anayapeleka chini chini.

Akitaka kutoa albamu au wimbo mpya ndipo utamjua Jide wa upande wa pili. Utajua kumbe anaishi na mwanaume kama binti. Kumbe anaishi na ‘marioo’ anayetumia gari zake kuchukulia vicheche. Atakusimulia matatizo ya mwanaume wake ambaye simu yake iko ‘bize’ nusu saa akiongea na michepuko.

Kwa sauti tamu na midundo mizuri, utaburudika na kujifunza kitu kupitia tungo zake. Utalipa pesa, anakusimulia matatizo yake kwa malipo.

Ni mara moja tu katika historia yake kimuziki kutoa albamu kwa ‘kiki’ ya nje ya mapenzi.

Ni ‘Joto Hasira’ ndipo alipokamata akili za mashabiki kwa mgogoro wake na kituo kimoja cha radio. Aliungwa mkono na wengi kwa kilichoaminika anaonewa. Si kuonewa tu, bali kwa kuwa yeye ni mwanamke sapoti ya kutisha aliipata.  Kabla na baada ya hapo, amekuwa akitumia matatizo yake kwenye uhusiano wa mapenzi kutengeneza pesa kupitia muziki. Ni akili.

Na inatufundisha kuwa kuna fursa nyingi ya kupata pesa bila kubebeshwa madawa ya kulevya. Jide anatumia mapenzi kupiga pesa.

Mapenzi ni kama dawa za kulevya. Yanamgusa kila mtu, ni maisha yetu ya kila siku. Na Jide anakamata watu kwa kuwa anawaimbia watu. Kila mwanadamu ana matatizo kwenye uhusiano ndani na nje ya ndoa. Ila si kila binadamu ana fursa ya kueleza hadharani matatizo yake.

Jide amekuwa kama daraja la kuelezea hisia za mapenzi kwa mamilioni ya wanawake na wasichana. Kifupi ni kwamba amekuwa faraja kwao, matatizo ya mapenzi ni sehemu ya dawa za kulevya. Mapenzi yanalevya, yanaua, yanaharibu vijana wengi.

Saturday, March 25, 2017

TEKNOLOJIA: Unavyoweza kuweka password katika flash

Kama unatumia kompyuta bila shaka unatumia flash kama kifaa cha kuhamisha nyaraka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Si hivyo tu, flash ambazo pia hujulikana kama USB, au USB stick zimekuwa kiunganishi muhimu kwa wapenzi wa muziki na filamu duniani kote kutokana na umuhimu wake katika kuhamisha taarifa.

Kukua kwa teknolojia kumefanya mahitaji ya CD yapungue kwa kiasi kikubwa na flash kuchua nafasi yake kutokana na urahisi wa kufuta na kuweka taarifa mpya.

Leo hii ukipita mitaani si jambo la kustaajabisha kukuta vijana wakiuza flash zilizojazwa nyimbo au video za muziki.

Hata hivyo, kila chenye uzuri kina ubaya wake na hivi ndivyo ilivyo kwa flash ambazo kutokana na udogo wake ni rahisi kupotea au hata kuibwa.

Hili linaifanya flash kuwa moja kati ya vifaa vinavyohitaji kuwekewa ulinzi hasa inapokuwa imebeba nyaraka muhimu.

Kama ilivyo kwa simu, kompyuta na vifaa vingine vya kielektroniki inaweza kuwekewa neno la siri (password).

Kila mtumiaji atakapoingiza kifaa hiki katika kompyuta hakitafunguka mpaka atakapoweka neno hili la siri.

Zipo software mbalimbali unazoweza kuzitumia kuifunga flash yako kama vile VeraCrypt,  DiskCryptor, Rohos Disk Encryption na LaCie Private-Public.

Kati ya hizo zote Bitlocker  ni rahisi kwa kuwa ipo katika kompyuta nyingi zinazotumia muundo wa Window.

Unachotakiwa kufanya ni kuichomeka flash katika kompyuta yako na kisha right click katika kiendesha kompyuta chako (mouse) kisha chagua Turn on Bitlocker.

Baada ya hapo itakueletea maelezo ya kutengeneza neno la siri kwa ajili ya flash yako na baada ya hatua tatu itakuwa tayari.

Angalizo ni kwamba flash iliyowekwa  neno la siri haiwezi kutumika katika redio au kifaa kingine cha kielectoniki ambacho hakikupi chaguo la kuingiza neno la siri.

Utaweza kuondoa neno la siri kwa kufuta taarifa zote (format) katika flash yako.

Saturday, March 25, 2017

HEKAYA ZA MLEVI: Usidharau togwa, soda ni za mpito

By Gaston Nunduma

Mimi hupenda sana hadithi zenye mwisho mzuri. Kila mara nilikuwa nikirudia visa vya “Kunyenge”, “Wagagagigikoko” na vingine vinavyofanana na hivyo.

Hadithi hizi zimekuwa zikifundisha namna ya kujikwamua na kuyashinda matatizo yanayokukabili. Unaweza kusoma kwa taabu jinsi watu wanavyoteswa na wababe hadi walipojikomboa na kuushinda udhalimu. Hatimaye utajikuta ukimaliza hadithi kwa machozi ya furaha.

Kwa kuwa watu wa mataifa hubadilishana tamaduni zao, waliweza kuchukua hadithi njema na kuwapelekea watoto wao. Tulibadilishana na Waajemi na Waghaibu na kuzijua tungo mahiri kama “Binti Matlai Shem”. “Cinderella”, “Sindbad”, “The Beast and the Beautiful” na “Sleeping Princess”.

Kama nilivyosema kila Taifa lina hadithi za namna hii zinazoanza kusimuliwa utotoni. Lengo ni kuwakuza watoto katika tumaini la wema kuushinda uovu. Hatimaye matumaini haya huwajenga kuwa jamii ya wafanyakazi inayoweza kuvumiliana, kusaidiana na kuishi kwenye misingi ya haki na usawa.

Tofauti kubwa nililoliona mimi ni kwamba watoto wa wenzetu walijifunza namna ya kufikia mafanikio wakati sisi tunajifunza kuishi ndani ya mafanikio. Mtoto wa Kihindi anajifunza kutengeneza saa na baiskeli, lakini wa kwetu hulilia kuveshwa sanamu ya saa na kuendesha baiskeli za watoto.

Juma lililopita nilisema kuwa sisi ni mabingwa wa kuwaiga waliofanikiwa bila kufuata njia walizopita. Tunapenda kutembelea magari mazuri kama alivyofanya Mike Tyson huku tukikwepa kutazama changamoto alizopitia kwenda kwenye mafanikio.

Ulaya na Marekani walihangaika sana kufika kwenye starehe. Walianza kutumia kuni kuchemsha maji ili kupata mvuke uliosukuma gari moshi na meli (steamers). Baadaye hatua kwa hatua wakaanza kutumia umeme wa maji, upepo, gesi na sasa mwanga wa jua.

Kinachonishangaza ni sisi baada ya kutengeneza jiko la mkaa, tunavunja vibubu kuingia kwenye treni za umeme. Hatujaweka nguvu kwenye majiko ya mafuta, umeme wala gesi. Na hivi sasa tumeshaanza kupiga marufuku matumizi ya mkaa ili tutumie ya gesi.

Siyapingi maendeleo hayo ila naona tunakimbia kwa kuruka viunzi, kisha tunarudi nyuma kutembea pale tuliporuka. Bado tunaweza kuwa Tanzania ya viwanda inayoweza kuimarisha uchumi, hata tukamudu kuiendesha treni ya umeme iwapo ni lazima kuwa nayo. Nasema hivi kwa sababu treni hiyo itahitaji gharama za uendeshaji na matengenezo pale itakapokwazika.

Hivi sasa ni marufuku kusafirisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda ingine. Kwa maana hii matumizi ya mkaa yataharamishwa katika siku za karibuni. Wananchi wa kawaida wataishi kwa mashaka.

Wote wamezoeshwa matumizi ya nishati hiyo kwa karne nyingi. Ingebidi waizoee gesi kabla ya kuachana na kuni. 

Wangali wakikumbuka tangazo la Tanesco lililosema “baada ya kufungua vituo vya Kinyerezi, hakutakuwa na shida ya umeme asilani”. Vituo vikafunguliwa na bado umeme ukaendelea kukatika hali wao wakilala na kandili.

Hivi ndivyo tunavyoruka viunzi na kurudi kutambaa pale tuliporuka. Roma haikujengwa kwa siku moja. Wakati tunasafiri kwa umeme tusisahau kutengeneza majiko ya mafuta.

Maswali na majibu piga na sms kwa simu:: 0713-248943

Saturday, March 18, 2017

Kuna tofauti kati ya uwezo na kipaji cha mtuJULIETH KULANGWA

JULIETH KULANGWA 

Unaweza kuwa mzuri katika kitu fulani bila hata kuwa na kipawa. Kukipenda kitu na kukifanyia bidii kunaweza kukufanya uonekane ulizaliwa kufanya hivyo.

Mara nyingi tunapomuona mtu anafanya maajabu katika jambo fulani huwa tunashangazwa na kuona kama miujiza au ni kipaji tu, lakini ukweli inawezekana nyuma yake kuna miaka mingi ameitumia kujibidiisha. Wanariadha wanaojishindia medali katika mashindano ya olimpiki, hutumia muda mwingi katika mazoezi kuanzia alfajiri wakati watu wengine wakiwa wamejifunika mablanketi  na kukoroma katika usingizi mororo.

Mwanamuziki bingwa wa kupiga gitaa, huenda alijifunza mpaka vidole vyake kutoa damu na bingwa wa mahesabu huenda alikaribia kuwehuka kwa mapenzi yake kwa namba.

Wapo wasanii wengi wameingia kwenye sanaa kwa sababu tofauti ya kuwa na kipaji lakini wanaendelea kupiga shoo. Nani alijua Shilole, Lulu Diva na Snura wanaweza kutajwa katika kundi la wanamuziki nchini, lakini mdogomdo