Kasi ya kuzaliana nchini itatibua mipango kuelekea uchumi wa kati

Muktasari:

Kwa kila Watanzania 100 ni sita tu wenye kipato cha kuweza kujitegemea. Wengine hawana au wana vya ubabaishaji

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina watu milioni 44.9 huku idadi ya yao ikiwa inaongezeka kwa wastani wa asilimia 2.7 kila mwaka. Wataalamu wa masuala ya idadi ya watu wanakadiria kuwa ikiwa ongezeko hili la watu halitadhibitiwa idadi ya Watanzania itaongezeka maradufu na kufikia milioni 100 baada ya miaka 23 kabla ya mwaka 2050.

Ongezeko la idadi ya watu la asilimia 2.7 kwa nchi yetu ni kubwa kulinganisha nchi zenye uchumi wa kati barani Afrika kama vile Afrika Kusini, Algeria na Morocco ambako idadi ya watu inaongezeka kati ya asilimia 1.4 hadi asilimia 1.9.

Mataifa makubwa duniani, Marekani, China na Uingereza ongezeko la idadi ya watu kwa mujibu wa ripoti za Benki ya Dunia (WB) ni kati ya asilimia 0.5 hadi 0.7 na idadi ya watu katika nchi hizo inakadiriwa kuwa itaongezeka maradufu baada ya miaka 100 hadi 140.

Sababu za ongezeko la watu

Wataalamu hao wanataja sababu kadhaa. Katika makala haya yatajadili chache na nitaeleza ni kwa vipi zinachangia ongezeko la watu katika nchi yetu. Umri wa watu kuishi: Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, umri wa wastani wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka miaka 51 mwaka 2002 hadi miaka 62 mwaka 2012 huku wanawake wakikadiriwa kuishi muda mrefu zaidi wa miaka 64 kulinganisha na wanaume miaka 60. Kadiri watu wanavyoishi muda mrefu, idadi ya watu inaongezeka hasa kama sababu nyingine zinazosababisha ongezeko hilo mfano uzazi, vifo hazitabadilika.

Vifo vya watoto wachanga: Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, shukurani kwa miradi kabambe ya chanjo za utotoni, kuimarika kwa huduma za afya na upatikanaji wa dawa.

Ripoti ya hali ya demografia na afya ya mwaka 2010 iliripoti kupungua kwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka vifo 136 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 1996 hadi 81 mwaka 2010. Kupungua kwa vifo vya watoto wachanga kunachangia ongezeko la idadi ya watu hasa kama sababu nyingine zinazosababisha kuongezeka kwa idadi ya watu mfano uzazi hazitabadilika.

Uzazi: Idadi ya watoto wanaozaliwa ndio sababu kuu ya kuongezeka kwa idadi ya watu duniani. Nchini inakadiriwa kuwa wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke ni watano ambapo hali hii imekuwa hivi kwa miaka mingi. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini na iliyopita wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke imepungua kidogo kutoka watoto sita mwaka 1991 hadi watoto watano mwaka 2011.

Idadi kubwa ya wastani wa watoto kwa mwanamke inachangiwa pia na ndoa katika umri mdogo ambao inakadiriwa kuwa asilimia 37 ya wasichana wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Hali hii husababisha wasichana kupata ujauzito na kuanza kuzaa katika umri mdogo. Takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa Tanzania katika kila vizazi 1,000 kwa mwaka, vizazi 119 ni vya wasichana wenye umri hadi miaka 19.

Matumizi sahihi ya njia ya uzazi wa mpango yanawapa fursa wanawake na wenzi wao kupanga idadi ya watoto wanayoitaka na wakati gani wawapate. Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa njia kadhaa za kisasa za uzazi wa mpango, matumizi ya njia hizo bado ni madogo nchini.

Kwa mfano ni asilimia 27 tu ya wanandoa au wenza ndiyo wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango ikiwa ni pungufu ya asilimia 60 ambayo ndiyo mapendekezo ya Shirika la Afya la Duniani (WHO).

Uhamiaji: Duniani kote kumekuwa na ongezeko la watu kuhama kutoka nchi hususan zinazoendelea, zilizokumbwa na machafuko ya kivita, ukame na madhila mengine kuelekea za Ulaya na Amerika.

Changamoto za kiuchumi

Kama nilivyoeleza katika utangulizi wangu, taifa letu linakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watu na hali hii inaliweka njia panda kama nitakavyoeleza.

Ongezeko la uvunaji na matumizi ya rasilimali kama misitu, ardhi, maji na madini kutokana na idadi kubwa ya watu ni jambo ambalo linahatarisha ustawi wa taifa letu. Ongezeko la watu katika nchi yetu linalotokana na kuzaliwa watoto wengi limesababisha nchi yetu kuwa ya vijana weng, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

Karibu nusu ya Watanzania wote wako chini ya umri wa miaka 18, na zaidi ya asilimia 44 yao ni vijana chini ya 15. Hii maana yake ni kwamba nchi yetu ina idadi kubwa ya watu ambao ni vijana ‘tegemezi’ ama wako katika hatua za masomo shule ya msingi, sekondari, ufundi stadi, vyuo na nyumbani.

Je, nchi yetu ni ya wanafunzi? Takwimu za Benki ya Dunia (WB) za mwaka 2010 - 2015 zinakadiria kuwa hali ya utegemezi kwa Tanzania ni asilimia 94. Yaani katika kila Watanzania 100 wenye umri wa kufanya kazi, miaka 15-64, ni sita tu ambao wana kipato na wanaweza kujitegemea. Hii inaonyesha idadi kuwa ya Watanzania ama hawana kipato kwa maana ya kuzalisha au ni wabangaizaji wasio na uhakika wa kukidhi mahitaji ya kuishi.

Wategemezi ni wengi nchini

Taifa letu lina kundi kubwa la wategemezi wasio na ajira hivyo kutokulipa kodi na kufanya Serikali kukusanya kodi kutoka kwa watu wachache.

Vilevile, Serikali inalazimika kuelekeza sehemu kubwa ya pato la taifa kuhakikisha huduma za msingi za jamii zinapatikana kuhudumia idadi kubwa ya watu.

Hata hivyo, taifa lina nafasi ya kuigeuza hali hii ya idadi kubwa ya vijana, wategemezi na kuwa neema na kuvuna kile ambacho wachumi na wataalamu wa idadi ya watu na maendeleo wanakiita demographic dividend (kutumia takwimu za idadi ya watu katika rika fulani kwa faida za kiuchumi).

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Maendeleo, (UNFPA) linailezea dhana hii ya Demographic dividend kuwa ni kuimarika na kukua kwa uchumi kunakotokana na ongezeko la kasi ya ukuaji wa uchumi kufuatia kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, hivyo kulifanya taifa kuwa na idadi ndogo ya wategemezi.

Hali hii hulifanya taifa kupunguza uwekezaji katika huduma za jamii na kuwekeza zaidi katika kujenga uchumi.

Napenda nieleweke kuwa demographic dividend ili iweze ‘kuvunwa’ taifa linapaswa kufanya mambo makubwa yafuatayo:

Kwanza ni kuwekeza kwenye sera sahihi za afya zitakazowezesha vijana kupata taarifa na huduma ya afya ya uzazi na kupanga uzazi na kupunguza idadi ya watu.

Hali hiyo itasababisha wanawake kuwa na watoto wachache na kupata fursa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia shughuli za uzalishaji mali, Serikali kuokoa fedha ambazo zingekwenda kuhudumia watu wengi na kuzielekeza katika shughuli nyingine za ukuaji uchumi.

Pili ni kuimarisha mfumo wa elimu ili kuwezesha kutolewa kwa elimu bora itakayowapa vijana stadi na maarifa ya kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri kwenye kazi zenye staha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Tatu ni kutekelea sera za uchumi zitakazozalisha ajira na nguvu kazi kubwa ya vijana kutumika kukuza uchumi.

Nne ni kuzingatia na kuheshimu misingi ya utawala bora, kukuza ustawi wa jamii, kujenga utamaduni wa kulipa kodi, kuheshimu sheria na kuondoa vitendo vya ubadhirifu na rushwa.

Ningependa pia kutoa mifano michache ya nchi zilizovuna demographic dividend katika miaka ya 1955, Tanzania ilikuwa ikiwekwa kundi moja kwa kulinganishwa pato la ndani la taifa kwa mwaka (Gross domestic product) na Korea Kusini na nchi kadhaa za Asia ya mashariki kama Malaysia, Singapore.

Wakati huo wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke kwa Tanzania ilikuwa watoto saba na Korea watano.

Miaka sitini baadaye, pato la ndani la taifa kwa mwaka kwa Korea lilikuwa ni dola za Marekani 28,000 na wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke ni mtoto mmoja. Wakati huu Tanzania inakadiriwa kuwa na pato la taifa la Dola 960 za Marekani na wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke imeshuka kidogo ni watoto watano.

Nini kifanyike

Napenda kusisitiza kuwa taifa linakabiliwa na kasi ya ongezeko la watu na hali hii inaliweka njia panda. Hali hii kama nilivyoeleza inaweza kugeuzwa na kuwa neema kama uamuzi sahihi na kutekeleza sera zitakazochochea uwekezaji kwa idadi kubwa ya vijana iliyopo na hivyo tutaweza kuvuna demographic dividend. Ili tuweze kufanikiwa zinahitajika jitihada za pamoja kwa wizara na idara za Serikali wakijumuishwa pia wadau wa maendeleo kushirikiana, vinginevyo mtaji huu wa vijana usipowekewa mikakati madhubuti tutakaribisha majanga makubwa siku za usoni.

Dk Majaliwa Marwa ana shahada ya udaktari na uzamivu ya sayansi ya afya ya jamii. Ana uzoefu kwenye masuala ya UKIMWI, Afya ya mama na mtoto, maendeleo na vijana. Anapatikana 0784307055 au [email protected].