Saturday, July 7, 2018

Kutoka kuwa zao la chakula, Muhogo sasa wapaa kibiashara

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Kwa muda mrefu zao la muhogo limekuwa likilimwa nchini kama zao la chakula na jamii nyingi. Muhogo pia hulimwa na nchi zaidi ya 90 duniani.

Katika nchi nyingine mbali ya kuwa kinga ya njaa, muhogo pia ni zao la biashara na hutumika kutengeneza chakula cha mifugo na malighafi kwa viwanda.

Kwa Tanzania uzalishaji wa muhogo upo chini ya kiwango cha kimataifa, ambapo wakulima hupata kati ya tani tano hadi saba kwa hekta badala ya tani 10.

Habari njema kwa wakulima

Hivi karibuni, zao la muhogo limeibuka kuwa zao muhimu la biashara na huenda wakulima wengi wakatajirika. Hiyo ni kutokana na taarifa za kuwapo kwa soko la nchi ya China na mipango ya Serikali kufungua viwanda vya kuchakata.

Akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alisema Serikali ina mpango wa kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na soko la muhogo la China.

Alisema ili kufikia hatua hiyo, Mei,2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.

Amesema kufuatia hatua hiyo, Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo katika jimbo la Shandong, huku akisema kwa sasa nchi hiyo inahitaji tani150,000 kwa mwaka.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage anasema licha ya utata wa soko la China, tayari mwanga umeanza kuonekana. “Sisi ni miongoni mwa taasisi za Serikali tuliolifuatilia soko la muhogo la China kwa muda mrefu. Tatizo lao wana masharti magumu, lakini kuna ujanja tumeshaufanya na tumeshafanikiwa,” anasema Waziri Mwijage.

Anaongeza: “Shida ya Wachina wanataka wadhibiti zao tangu likiwa shambani. Wajue muhogo umelimwa wapi, umeanikwa wapi unauzwaje. Lakini tayari kuna mwanga umeonekana kwani kuna kontena moja limeshatumwa kwa majaribio na limekubaliwa. Baada ya hapo tutaanza kupeleka.”

Anasema tayari kuna itifaki ya afya iliyosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na China na Tanzania na kwamba kuna mkataba unaotakiwa kusainiwa na Wizara ya kilimo siku za usoni.

Wasemacho wakulima

Idd Omari anayelima zao hilo katika mikoa ya Tanga, Mtwara na Lindi anasema awali zao hilo walilitegemea kwa chakula lakini sasa liko kibiashara zaidi.

“Mimi niliamua kuzalisha muhogo kibiashara baada ya kupewa mafunzo ya taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation mkoani Mtwara yakihusisha pia Wakala wa kudhibiti mbegu Tanzania (Tosci),” anasema na kuongeza:

“Awali muhogo ulizalishwa kwa ajili ya chakula hasa kwenye mikoa yenye ukame na upungufu wa chakula. Wakulima wengi walitumia mbegu za kienyeji zisizo na sifa huku soko lenyewe likiwa halieleweki.’’

Anasema kuwa wakati huo wakulima waliuza muhogo shambani kwa matenga ya Sh25,000 hadi 40,000. Baadaye wakawa wanauza viroba vya kilo 50 na kilo 100 kwa Sh40,000 hadi 50,000.

Philipo Ntongolo ni mkulima wa muhogo mwenye shamba la ekari 60 katika kijiji cha Bungu wilayani Kibiti. Anasema endapo mikakati ya uhakika itafikiwa kwa soko la China, wana uhakika wa kupata muhogo wa kutosha kwani wakulima wamehamasika vya kutosha.

“Tumetembelea wakulima mbalimbali nchini, tumegundua wengi wamehamasika kulima muhogo. Kwa hiyo tuna uhakika wa kulisha soko la China. Isistoshe kwa sasa kuna mbegu ambayo shina moja linatoa kilo 45 kwa hiyo tunawahamasisha kutumia mbegu hiyo inayoitwa Kiroba,” anasema.

Hofu kwa wakulima na utata wa soko la China

Hata hivyo, baadhi ya wakulima hawajapata mwanga wa soko hilo, badala yake wamejikita kwenye soko la ndani linaloonekana pia kushika kasi.

Akizungumzia fursa ya soko la China, Omari anasema wamefanya uchunguzi na wakulima wenzake wakaona bado halijakaa sawa.

“Ni kweli kwamba zao la muhogo halijawekewa mfumo mzuri wa masoko kama vile mazao ya pamba, korosho na kahawa, lakini tumechunguza hilo soko la China, bado halijakaa vizuri. Ni bora tuendelee kuuza hapa hapa nchini,” anasema.

Omari ni miongoni mwa wakulima walioungana na kuunda kamati maalum ya kufuatilia masoko ya muhogo ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya wakulima wa muhogo, Philipo Ntongolo anasema utafiti walioufanya tangu Juni 7 mwaka huu umeonyesha bado soko la China halijakaa sawa hivyo wanalenga kuanza na masoko ya ndani kabla ya kulifikia.

“Kamati ilitaka kujua muhogo uliopelekwa China, ulikwendaje? Je, taarifa kuhusu nchi hiyo kuhitaji zaidi ya tani 100,000 na ni utaratibu gani unafuatwa kufikia soko hilo,” anasema.

Hata hivyo, anasema wakati wanatafakari soko hilo la China, wamebaini kuwa nchi ya Rwanda imekuwa ikinunua muhogo kutoka Mkoa wa Kigoma kwa Sh800 kwa kilo na kusafirisha katika nchi za Ubelgiji na Urusi.

Ushirika wa wakulima wa muhogo

Kutokana na unafuu wa soko la ndani, Ntongolo anasema wameamua kuunda ushirika wao, ili kukusanya mazao kwa wakulima na kutafuta masoko.

“Endapo ushirika utafanikiwa, wakulima tunaweza kujenga kiwanda chetu binafsi ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchakata makopa na wanga. Tunaweza kujenga viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo, soda, juisi na chakula cha samaki wa kufugwa,” anasema.

Jinsi ya kulima muhogo

Mambo ya kuzingatia katika kilimo cha muhogo ni pamoja na hali nzuri ya hewa na maeneo yenye udongo mzuri usiotuamisha maji. Mvua inayotakiwa ni ya wastani ambayo si kidogo sana na wala si nyingi sana.

Eneo linalolimwa muhogo linapaswa kuangaliwa historia yake ili kuelewa kama kuna magugu hatari na wadudu au magonjwa kwenye eneo hilo, ili kubuni mbinu za kuyazuia au kuyaangamiza mapema.

Epuka kupanda muhogo kwenye eneo lenye mwamba chini kwani hii husababisha mizizi kutonenepa na kuwa na mavuno hafifu. Shamba la muhogo linatakiwa kupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kupata mavuno mengi (Oktoba hadi Machi na Aprili).

Mbegu

Kipando kinatakiwa kiwe na urefu wa sentimeta 25-30 ili upate ustawi mzuri. Urefu wa kipando hutegemea na umbali kati ya jicho na jicho na idadi ya macho. Inashauriwa kipando kiwe na macho kati ya 5 hadi 7, kwani ndicho chanzo cha mizizi na majani.

Pingili zinatakiwa kukomaa vizuri kwani huchangia kwenye ubora na wingi wa mazao yatakayovunwa.

Mbegu haipaswi kuwa na dalili za mhatari, hivyo mkulima achague mimea isiyo na wadudu au magonjwa na zipandwe mapema baada ya kukatwa.

Saturday, July 7, 2018

Mfugaji bora ni yule anayemjua kuku wake

 

By CLEMENT FUMBUKA

Karibu tena kwenye makala kuhusu hatua za kupata mayai kabla hujaingia bandani kuyaokota. Ni elimu bora kwa mfugaji kujua namna gani mayai hutengenezwa kwenye mwili wa kuku kabla hajataga.

Lengo la makala haya ni kuweka mambo wazi kila mfugaji ajue jinsi ya kutunza kuku wenye kutaga kwa wingi.

Kimsingi, sio wafugaji wote wanajua mayai yanavyotengenezwa kwenye mwili wa kuku, japo idadi kubwa ya wafugaji wana mwanga fulani katika mambo mengi kwenye ufugaji.

Kwa mfano, kujua namna gani tumbo la kuku linazalisha mayai, ni hatua muhimu kwenye harakati za mtu kuwa mfugaji bora.

Tumbo la kuku ndiyo kiini cha mradi katika shamba la kuku wa mayai. Uzalishaji wa mayai unategemea hali ya afya ya mfuko wa uzazi wa kuku.

Mfugaji anatakiwa kufuga kwa lengo la kumfanya kuku atage mayai mengi. Lishe duni na magonjwa ya mara kwa mara kwa kuku, ni kuharibu ubora wa mfuko wa uzazi wa kuku anayetaga.

Ushauri wangu kwa wafugaji ni kuwa magonjwa mengi ya kuku yanatokana na mazingira wanayoishi kuku. Hali ya usafi wa banda au uchafu wa banda ndiyo sababu ya afya nzuri au mbya kwa kuku wako.

Ukiondoa uchafu wa kimazingira, lishe na huduma zingine za kiusimamizi huchangia uzalishaji kuwa mzuri au mbaya pia.

Hivyo ni vizuri kuchagua kuwa mfugaji bora kwa kuweka sawa mambo yote muhimu katika mahitaji ya kuku.

Kwa upande mwingine, mfugaji anaweza kufahamu mambo mengi katika ufugaji lakini kuna mambo mengine mengi hayajui.

Kutofahamu huko humfanya ashindwe kushughulikia ipasavyo matatizo yanayojitokeza shambani kwake.

Yajue mambo haya

Mambo matatu anapaswa mfugaji kujua kuhusu kuku. Moja, kuku ana ovari ya upande mmoja pekee kwenye mji wa uzazi inayofanya kazi.

Kuku anapotoka kwenye yai hukua akiwa na ovari zote mbili kulia na kushoto, lakini akifikia umri wa kuzalisha mayai ovari ya kushoto ndiyo hukomaa na kufanya kazi. Kwa hiyo mfugaji anatakiwa kujua kuwa kuku sio sawa na wanyama wengine kama vile ng’ombe, mbuzi na wengineo, ambayo matumbo yao ya uzazi hutumia ovari mbili kulia na kushoto ambazo hupokezana kutengeneza mayai.

Kutokana na sababu hiyo ya kuku kuwa na mfuko wa upande mmoja unaofanya kazi, hawezi kuzalisha mayai mawili kwa wakati mmoja kama ambavyo hutokea kwa wanyama wenye ovari mbili kuzaa pacha kwa kutumia ovari zote mbili.

Pacha wanaoweza kutokea kwa kuku ni yale ya yai moja kugawanyika ndani kwa ndani na kutengeneza viini viwili. Mgawanyiko huo wa yai unaweza kusababisha yai moja kutoa vifaranga wawili, lakini sio kuku mwenyewe kutoa mayai mawili yanayojitegemea kwa wakati mmoja.

Jambo hii huleta utata kwa watu wengi na wafugaji wengi kushindwa kujua kuwa kuku anataga yai moja tu kwa siku au zaidi?

Ukweli ni kwamba; mfumo wa uzazi wa kuku umeumbwa kufanya kazi moja baada ya nyingine; hivyo kalenda ya kuku pamoja na ndege wengine hutengeneza yai moja baada ya yai lililotangulia kutagwa. Hivyo kuku hawezi kutaga mayai zaidi ya moja kwa siku.

Pia sio rahisi kutokea kuku akawa na ovari zote mbili kulia na kushoto zinazotoa mayai. Endapo ovari ya kushoto ikiharibika kabla kuku hajaanza kutaga, ovari ya kulia inaweza kukomaa na kufanya kazi kama kawaida.

Jambo la pili asilolijua mfugaji ni kwamba; kuku akimaliza kutaga yai ndani ya dakika 30 hadi saa moja, mrija wa uzazi hufungua njia ya yai lingine kuanza kutengenezwa.

Hata hivyo, hilo linaweza lisitokee endapo kuku atakuwa ametaga muda wa jioni kuelekea usiku.

Kwa mfano, kuku anayetaga yai jioni ya saa tisa na kuendelea, mara nyingi mfuko wa uzazi hushindwa kufungua njia ya yai lingine kuanza kutengenezwa, badala yake husubiri hadi kesho yake mwanga wa jua umchangamshe na kisha njia kufunguka.

Kumbuka makala zilizopita zilisisitiza juu ya kuwa mwanga wa ziada kwa kuku wanaotaga angalau saa nne baada ya saa 12 za mwanga wa jua, ili homoni za kuzalisha mayai kwa kuku ziendelee kufanya kazi.

Homoni zinazoratibu uzalishaji wa mayai kwenye mwili wa kuku, hufanya kazi vizuri kuku akiwa macho.

Jambo la tatu lisilojulikana kwa mfugaji ni kwamba; kuku huchukua saa 25 hadi 26 kutengeneza yai na kutaga.

Sehemu ya kwanza kutengenezwa kwenye yai ni kiini cha njano ambacho hukuzwa na kuwa kikubwa. Tangu kuku akiwa kifaranga huwa anavyo vingi tayari kwenye ovari.

Sehemu ya pili inayoongezwa juu ya kiini hicho cha njano ni ute mweupe ambao yai likichemshwa ute huo hushikana na kuonekana kama sehemu ya ndani ya nazi inapovunjwa. Sehemu inayofuata ni mfano wa karatasi nyepesi ambayo hushikana na ganda gumu la nje.

Kila sehemu ya yai ina sehemu maalumu katika mlija wa uzazi wa kuku kutengenezwa. Sehemu zote za yai hutengenezwa kwa muda mfupi isipokuwa ganda la nje ya yai ambalo huchukua muda mwingi kuliko vyote.

Pia, ganda la nje ya yai hutumia madini mengi kuliko sehemu zote kwenye yai na huchukua saa 18 na zaidi kutengenezwa.

Upungufu wa madini ya kalshiamu na fosforasi husababisha kuku watage mayai yasiyo na ganda gumu.

Mayai mengi utakuta yametagwa yakiwa kwenye kikaratasi chepesi bila ganda gumu. Kuku wenye matatizo ya kutaga mayai laini mara kwa mara, hupatwa na shida ya kulemaa miguu na kushindwa kutaga kwa kukosa nguvu ya kusukuma yai wanapotaga.

Ili kutatua tatizo hili, boresha chakula chako upande wa madini.

Saturday, July 7, 2018

Lima nyanya kisasa-2

 

Katika makala ya wiki iliyopita, nukta ya mwisho ilihusu aina za nyanya. Endelea.

Nyanya zinazoonyesha kuwa na sifa ya kuhifadhika bila kuharibika mapema ni kama:

(a)Tengeru’97 ambayo ina sifa zifuatazo: Huzaa sana kutokana na wingi wa matunda na muda mrefu wa kuvuna, ambao hufikia michumo mikubwa kati ya sita hadi saba.

Aina hii ina sifa ya kuwa na ganda gumu, hivyo haziharibiki haraka wakati wa kusafirisha au kuhifadhi (wastani wa siku 20). Zina sifa ya kuvumilia baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kunyauka. Tengeru’97 hustahimili mashambulizi ya ugonjwa wa minyoo fundo (b) Tanya. Sifa kubwa ya Tanya ni kwamba nayo huzaa sana. Huwa na ganda/ngozi ngumu ambayo inazuia kuoza au kuharibika kwa urahisi wakati wa kusafirisha au wakati wa kuhifadhi kwa muda mrefu. Tanya nayo ina ladha nzuri inayopendelewa na walaji wengi.

Zingatia: Tatizo la Tanya na T97 ni kwamba si kubwa sana kama marglobe 2009. Lakini ukubwa ni karibu unge karibiana, haujapishana sana. Kwa ujumla, ukubwa na wingi wa mazao hutegemea sana matunzo, udongo, hali ya hewa na mazingira kwa jumla.

Maandalizi ya shamba la nyanya

Shamba la nyanya liandaliwe mwezi mmoja au miwili kabla ya kupanda miche. Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.

Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.

Andaa mashimo ya nyanya kutegemeana na idadi ya miche uliyonayo, nafasi na aina ya nyanya. Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita 50-60 na mistari ni 50-75 kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na nyanya.

Jinsi ya kupanda miche ya nyanya

Weka samadi viganja viwili au gram tano za mbolea ya kupandia kwenye shimo kabla ya kupanda mche. Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake. Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.

Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa kitaluni. Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kisha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.

Umwagiliaji wa nyanya

Nyanya kama ilivyo kwa mazao mengine, zinahitaji maji mengi ili kuzaa matunda yenye afya. Kutegemeana na aina ya udongo, unaweza kumwagilia nyanya mara mbili kwa wiki.

Hakikisha unapanga ratiba maalum ya kumwagilia na unaifuata ili kuepuka kumwagilia kiholela holela kwani umwagiliaji usio na mpangilio huathiri afya ya matunda ya nyanya na kupelekea nyanya kuoza kitako. Unapotumia vifaa kama keni au mpira, jitahidi sana usimwagilie kwenye majani ya mmea au matunda kwa sababu kulowesha mmea kunavutia wadudu na magonjwa ya ukungu yanayoharibu nyanya.

Zingatia: usituamishe maji kwenye bustani au shamba la nyanya.

Palizi: Kudhibiti magugu

Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini. Palilia shamba lako wiki ya pili au ya tatu baada ya kupandikiza miche,. Lakini pia unaweza kupalilia kila unapoona magugu kwani shamba linatakiwa kuwa safi muda wote. Unaweza kuondoa magugu kwa kutumia dawa za kuua magugu au jembe la mkono.

Magugu ni hatari kwa sababu yanashindana na mimea katika kuchukua nafasi na hivyo mimea kushindwa kujitanua. Pili: magugu huzuia mimea ya nyanya kupata mwanga wa jua wakutosha hivyo kuifanya mimea kushindwa kujitengenea chakula cha kutosha.

Imeandaliwa na Mogriculture. 0655-570-084. www.mogriculture.com

Saturday, June 30, 2018

Jua namna bora ya kuandaa chakula cha mifugoJinsi ya kuandaa chakula cha mifugo.

Jinsi ya kuandaa chakula cha mifugo. 

By Aurea Simtowe, Mwananchi

Sifa za utengenezaji wa chakula cha mifugo ni pamoja na mhusika kuwa na elimu ya lishe kwa mifugo na kujua virutubisho vinavyotakiwa kwa mifugo.

Mwamko wa kufuga umetamalaki kwa Watanzania wengi. Vijijini hata mijini, wananchi wanajihimu kuendesha miradi mbalimbali ya ufugaji hasa ule wa kuku ambao umekuwa kimbilio la walio wengi.

Hata hivyo, changamoto kubwa wanayokumbana nayo wafugaji wengi ni gharama kubwa ya vyakula vya mifugo, jambo wanalosema limekuwa likiwaingiza katika hasara.

Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika siku za karibuni, umebaini kuwa bei ya chakula cha kuku wa nyama na mayai aina ya ‘Starter’ huuzwa kuanzia Sh60,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Aina nyingine za chakula kama ‘Grower na Finisher zinauzwa kwa bei ya Sh40,000 na Sh50,000 mtawalia. Kwa wafugaji wadogo na wale wanaoanza, gharama hizi ni kubwa.

Kama njia ya kuondokana na changamoto hii, baadhi ya wafugaji wameamua kutengeneza vyakula kwa kutumia malighafi mbalimbali kama inavyoshauriwa na wataalamu. Lakini pia wapo wanaotengeneza vyakula hivyo kienyeji, hivyo kuathiri afya na ubora wa mifugo yao.

TAFMA yajitosa kuwasaidia wafugaji

Kuwepo kwa wafugaji wanaoandaa vyakula kimakosa, kumeifanya Jumuiya ya wazalishaji wa vyakula vya mifugo Tanzania (TAFMA), iwe inaandaa mafunzo kwa ajili ya kufundisha namna bora ya uchanganyaji wa vyakula vya mifugo.

Katibu wa jumuiya hiyo, Sufian Kyarua, anasema semina hizo hufanyika kutokana na kutambua kuwa katika utengenezaji wa chakula wafugaji wengi, wamekuwa wakitumia malighafi zisizofaa au zenye kiwango duni cha ubora, hivyo kupata hasara.

Anasema kimisngi, uzuri wa chakula, hutokana na ubora wa malighafi iliyotumika kuanzia katika uvunaji na namna ilivyohifadhiwa.

“Baadhi ya malighafi zinapochelewa kuvunwa au zilizovunwa kwa muda muafaka na kuhifadhiwa sehemu yenye unyevu, huwa zinatengeneza sumu kuvu ambayo hukinzana na ukuaji wa mifugo,” anaeleza.

Anaongeza: “Mtu anaweza kutumia pumba ambayo ilikobolewa kwa mfumo wa kutumia maji ili mahindi yakoboke vizuri, lakini baada ya hapo pumba inawezekana hazikuanikwa vizuri zikavunda, hivyo sumu kuvu inakuwa tayari ipo na endapo zitatumika kama chakula, zitaleta madhara kwa mifugo.’’

Pia anasema ubora wa malighafi wa sehemu moja hutofautiana na ule wa sehemu nyingine kulingana na rutuba ya udongo pamoja hali ya hewa.

Akifafanua hili, anasema:“Mahindi yanayolimwa Tanga yanaweza kutofautiana katika kiwango cha wanga na protini ikilinganishwa na yale yanayotoka Rukwa au Dodoma. Unapotengeneza chakula, lazima uzingatie madini yanayopatikana.’’

Anasema wafugaji wengi pia wamekuwa hawajui watumie kanuni gani katika kutengeneza chakula cha mifugo yao. Wengine anasema hutengeneza kanuni ambayo haiendani na aina ya mifugo waliyoikusudia jambo linaloathiri ukuaji wao.

“Mifugo ina mahitaji tofauti; ukimpa mnyama chakula ambacho hakiendani naye, uzalishaji utashuka. Kama ni kuku wa mayai atakuwa hatagi kwa kiwango kinachotakiwa; kama ni kuku wa nyama atashindwa kukua katika muda uliotarajiwa,” anasema Kyarua.

Njia bora za utengenezaji chakula

Anasema ili mfugaji aweze kutengeneza chakula kizuri kwa ajili ya mifugo yake, lazima atumie malighafi bora, awe na taaluma ya lishe ya wanyama ili kujua mnyama anayemtengenezea chakula anahitaji nini na kutambua virutubisho vinavyotakiwa.

“Ukishajua anahitaji nini utajua virutubisho hivyo vinapatikana katika malighafi gani na vimehifadhiwa katika sehemu inayostahili na hapo ndipo utatumia kanuni kujua uchanganye nini na nini kwa viwango unavyohitaji,” anasema Kyarua.

Baada ya kufanya uzalishaji, mfugaji anashauriwa kwenda kupima chakula maabara ili kujua utapata virutubisho vya aina gani na kama amefikia kile anachokihitaji. “Kila sampuli moja inapimwa kwa Sh20,000 hadi Sh25,000 na inaweka urahisi kwako kujua chakula hicho kinafaa kwa mfugo wa umri gani,” anaongeza kusema.

Uchanganyaji chakula cha mifugo

Uchanganyaji wa chakula ni maarifa yanayomwezesha mzalishaji kutengeneza chakula chenye virutubisho vinavyohitajiwa na miili ya wanyama mbalimbali katika ukuaji wao na uzalishaji.

Kwa mujibu wa Kyarua, kuna aina mbili za uchanganyaji wa chakula ambazo ni njia ya kisasa na ya kienyeji. Kwa njia ya kisasa, malighafi husagwa kwa viwango vilivyoshauriwa ili kufikia mchanganyiko ambao utakua na virutubisho vilivyokusudiwa.

“Kuna mashine za kisasa zinazofanya kazi hiyo, lakini kuna njia ya kienyeji ambayo hutumiwa na watu wenye kuku wachache. Hawa hutwanga chakula na kuchanganya kulingana na mahitaji yao,” anaeleza.

Miongoni mwa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa chakula cha mifugo ni mahindi, mtama, muhogo kwa ajili ya kutengeneza wanga.

Pia kuna mashudu ya soya, dagaa, pumba za mahindi na ngano, madini ya chokaa, vitamin na vichanganyio vingine kutoka viwandani ambavyo ni ‘premixes’ na ‘limestone’, ‘bone meal’,’ MCP’,’DCP’.

Tofauti ya vyakula

Anasema tofauti kubwa ya ubora wa chakula kinachotengenezwa na wafugaji wa kawaida na kile kinachotengenezwa viwandani ni utaalamu na utumiaji wa malighafi. “Watu wanaojishughulisha na utengenezaji wa chakula, wanakuwa na wataalamu wenye elimu ya lishe ya mifugo, vifaa, wanatumia maabara kuthibitisha ubora wa malighafi na wanajua ni chakula kipi kinafaa kwa kila aina ya mifugo,” anasema.

Lakini kwa walio wengi anasema ama wanakosa uelewa wa mbinu bora za ufugaji au kukosa mitaji kwa ajili ya kuandaa mazingira bora ya afya za mifugo yao.

“Wengi hawana taaluma ya lishe ya chakula hivyo inakuwa ni ngumu kutengeneza chakula kwa ajili ya mifugo yao. Uhifadhi wa malighafi pia unashusha viwango vya utengenezaji wa vyakula vya mifugo yao,” anaeleza.

Faida za kutumia vyakula bora

Kwa mujibu wa Kyarua, kuna faida kadhaa kama mfugaji atazingatia kanuni bora za ulishaji wa mifugo, ikiwamo matumizi madogo ya madawa, hivyo kuwa na uhakika wa kuzalisha mifugo iliyo salama kwa afya za walaji.

Anasema kuwa mnyama anayetumia dawa mara kwa mara, hudumaa katika ukuaji wake na faida zinazopatikana huwa ndogo ikilinganishwa na yule asiyetibiwa mara kwa mara.

“Gharama za uzalishaji zikipungua atafanikiwa kuongeza faida katika biashara yake na atamhakikishia mlaji kuwa bidhaa anazozalisha ni salama, kwa sababu hazitegemei madawa katika ukuaji,”

Saturday, June 30, 2018

Zijue siku 21 za kupata vifaranga kwenye mayai-2

 

By CLEMENT FUMBUKA

Ni mwendelezo wa mada ya kuzalisha vifaranga kutoka kwenye mayai ya kuku.

Makala yaliyopita yaligusia sehemu m uhimu katika utototeshaji, lakini mambo mengine mengi hayakuguswa.

Pengine kuna maswali mengi juu ya muda wa mayai kuanguliwa. Mtu anaweza asijue kuwa kila aina ya ndege ana siku zake za kuangua mayai.

Kwa mfano, mayai ya bata, njiwa, kware na kuku huanguliwa kwa siku tofauti. Njiwa huangua vifaranga baada ya siku 17 za kulalia mayai.

Kuku huangua baada ya siku siku 21 kulalia mayai, huku bata akiangua vifaranga baada ya siku 28 za kulalia mayai.

Wafugaji wanaotumia mashine kuangulisha wanatakiwa kufuata maelekezo kulingana na aina ya mayai ya ndege wanayotaka kutotolesha.

Iandae mashine vizuri kulingana na aina ya mayai unayotaka kuangulisha. Soma mwongozo wa mashine husika kwa sababu kila mashine huuzwa pamoja na mwongozo wake. Au pata ushauri wa kina kutoka kwa mtaalamu au mtu mwenye uzoefu wa mashine husika kwa muda mrefu.

Kama unatotolesha kwa njia ya asili, hakikisha aina ya ndege husika ndiye anayelalia mayai hayo. Ikiwa unatumia aina nyingine ya ndege kulalia mayai, hakikisha ndege anayelalia mayai ana asili ya kulalia kwa muda unaofanana na ndege mwenye mayai au zaidi.

Kwa mfano, bata anaweza kulalia mayai ya kuku, lakini kuku hawezi kulalia mayai ya bata, kwa kuwa atayaacha kabla hayajaanguliwa, kwa sababu kuku hulalia kwa siku 21, ilhali bata hulalia hadi siku 28 au 30.

Mambo muhimu katika utotoleshaji

Baada ya kuona tofauti hizo za uanguaji, tuangalie mambo mengine muhimu katika utotoleshaji baada ya kuona mambo matatu kwenye makala yaliyopita ikiwamo umuhimu wa mbegu ya jogoo kwenye mayai ya kuangulisha.

Jambo la nne ni maambukizi. Magonjwa huathiri afya ya kuku na ukuaji wa vifaranga walioko kwenye mayai. Ni jambo la kawaida kwa mayai kushindwa kuanguliwa hata kama yana mbegu za jogoo ndani endapo kuku waliotaga mayai hayo ni wagonjwa.

Yapo magonjwa ambayo huzuia ukuaji wa vifaranga kwenye mayai kabla hawajaanguliwa na mengine hushambulia vifaranga baada ya kuanguliwa.

Tano ni lishe. Kuku wenye lishe duni hawana virutubisho kwenye mayai vya kutosha, hivyo matokeo yake vifaranga hukosa nguvu na kufia kwenye mayai kabla ya kutoka.

Mfugaji anatakiwa kulisha chakula bora kwa kuku wanaotaga na kuwapa vitamini mara kwa mara hasa ikiwa ni kuku wanaofungiwa ndani.

Sita ni joto la mashine ya kuangulishia. Mfugaji anayeangua kwa njia ya asili, anategemea kuku wapashe joto mayai

Lakini kwa mtu anayetumia mashine, inatakiwa mashine itoe joto na unyevu unaotakiwa. Kupanda au kushuka kwa joto kuliko inavyotakiwa, kutasababisha mayai kutoanguliwa.

Ongezeko la joto kidogo zaidi ya kiwango mara nyingi huwahisha vifaranga kuanguliwa siku moja au mbili kabla ya siku ya 21 kwa mayai ya kuku.

Aidha, kupungua kwa joto kidogo chini ya kiwango huchelewesha mayai kuanguliwa. Vilevile unyevu ukipungua sana vifaranga hutoka wakiwa wadogo wadogo au pengine hushindwa kuvunja ganda la yai ambalo kifaranga hulazimika kulitoboa kwa kuligonga na mdomo wake.

Saba ni ukubwa wa mayai. Mayai makubwa sana hayafai kuangulisha. Mayai haya mara nyingi huwa na viini viwili ndani yake ambavyo hutoa mapacha.

Hata hivyo, sio rahisi vifaranga wawili kuishi hadi kuanguliwa wakiwa kwenye yai moja; mara nyingi hufia ndani kwa kukosa lishe, hewa na nafasi. Hivyo mayai yenye viini viwili hayafai kuanglisha.

Mbali na mayai yenye viini viwili, mayai yenye ganda gumu kama vile mayai ya kuku wazee hutagwa yakiwa na ganda gumu, hivyo vifaranga huchelewa kutoka ikilingalishwa na mayai ya kuku wanaoanza kutaga.

Nane ni kugeuza mayai. Mayai yanahitaji kugeuzwa mara kwa mara yakiwa yanapata joto la kuku au joto la mashine.

Ni kama mtu anayekaanga chapati kila baada ya muda anageuza chapati jikoni. Hivi ndivyo hata kwa kuku akiwa amelala kwenye mayai kila baada ya muda hugeuza mayai yote.

Kazi hiyo ya mayai kugeuzwa hufanyika pia kwenye utotoleshaji kwa njia ya mashine. Kila baada ya muda mashine hugeuza trei za mayai nyuzi 45 kulia na kushoto.

Mayai yakikaa bila kugeuzwa, hushindwa kuanguliwa hivyo vifaranga hugandia kwenye ganda walikolalia na kufa.

Tisa ni usafi. Safisha mashine kila mara kwa kuondoa mabaki ya mayai na vifaranga waliokufa. Pia puliza dawa kuondoa mazalia ya vimelea vya magonjwa. Safisha mashine kwa maji safi na sabuni na kuacha ikauke kabla ya kuweka mayai mengine mapya. Zingatia kanuni zote za afya ikiwemo kuwa na sehemu maalumu ya kufukia uchafu na kuchoma mabaki yote. Toa chanjo kwa vifaranga walioanguliwa kulingana na kalenda ya utoaji chanjo. Weka vitu vya kuzuia baridi na vipasha joto kwa vifaranga ili wasife kwa baridi.

Saturday, June 30, 2018

Lima nyanya kisasa-1

 

Nyanya ni zao la mboga linalolimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Nyanya ni aina ya mboga inayozalishwa kwa wingi sana duniani.

Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.

Kulingana na umuhimu wa zao hili kama chakula na pia kama zao linalomwingizia kipato mkulima, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wake.

Maeneo yanayolima nyanya

Inadhaniwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru au Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu. Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na Marekani, Italia na Mexico.

Kwa upande wa Afrika, nyanya hulimwa Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa upande wa Tanzania mikoa inayolima nyanya kwa wingi hasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Iringa, Tanga, Mbeya na Singida.

Mazingira yanayofaa kwa kilimo cha nyanya

Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa.

Udongo

Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiotuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 hadi 7.0.

Mwinuko

Nyanya hustawi vizuri kutoka sehemu za mwambao hadi kwenye mwinuko wa mita 400-1500 kutoka usawa wa bahari; yaani nyanda za chini kati hadi za juu kutoka usawa wa bahari. Nyanya zinazopandwa nyanda za juu sana hukumbwa na mvua za mara kwa mara ambazo huambatana na magonjwa ya jamii ya ukungu; kama Bakajani chelewa.

Aina za nyanya

Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

1.Aina ndefu: Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya shamba kitalu (green house). Uvunaji wake ni wa muda mrefu. Zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi sita. Mfano wa aina hizi ni ANNA F1, Tengeru 97, Marglobe (M2009).

2.Aina fupi: Mfano wa aina hizi za nyanya ni Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa).

Aidha, kulingana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

1. OPV (Open Pollinated Variety) - Hizi ni aina za kawaida

2. Hybrid - Chotara: Hizi ni nyanya zilizoboreshwa, aina hii zina mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.

Hata hivyo, katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazozaa sana na zenye ganda gumu, ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

Imeandaliwa na Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. 0655-570-084 www.mogriculture.com

Saturday, June 16, 2018

Mazao ya kilimo hai yalivyo na soko kitaifa na kimataifa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Kilimo hai ni kilimo kisichotumia mbolea wala dawa za viwandani katika uzalishaji wa mazao yake.

Mazao yanayozalishwa kwa kutumia kilimo hiki kwa kawaida huwa na bei ya juu, kutokana na ukweli kuwa ni salama zaidi kwa afya ya mlaji.

Aidha, mazao hayo hayana madhara ya muda mfupi wala mrefu, hivyo mtumiaji hana hofu ya kupatwa na magonjwa.

Utafiti unaonyesha kuwa katika soko la dunia bei ya mazao ambayo hayakutumia kemikali aina yoyote, imekuwa ikiongezeka kulinganisha na yale ambayo yamekuwa yakitumia kemikali hizo.

Wakati bei za mazao kama kahawa, pamba na sukari zimekuwa zikiyumba katika soko hilo, bei ya mbogamboga katika soko hilo imekuwa ikiongezeka na kuwapatia fedha nyingi wakulima wanaolima zao hilo kwa kutumia mfumo wa kilimo hai.

Hata hivyo, wanaharakati wa kuendeleza kilimo hai wamefanikiwa kuwashawishi wakulima kujihusisha na kilimo hai baada ya kuelezwa faida za kuuza kwa bei ya juu na umuhimu wa kutunza mazingira.

Wakulima wanasemaje?

Mkulima anayezalisha mazao kwa kufuata misingi ya kilimo hai, Zadock Kitomari anasema kuwa, unapoanza kujishughulisha na kilimo hai ambacho hakitumii kemikali unaona kuwa uzalishaji unakuwa mdogo, lakini kwa kadri unavyoendelea uzalishaji unakuwa mkubwa.

Anaeleza kuwa, kilimo hai ni aina ya kilimo kinachoangalia uhai wa mazingira, uhakika na usalama wa mlaji na usalama wa chakula, jambo linalomhakikishia mkulima kipato kwa kutumia fursa alizonazo.

Akizungumzia upatikanaji wa masoko ya kilimo hai, Kitomari anasema; “Masoko ya kilimo hai yapo, isipokuwa yanapatikana tu kwa wale wakulima waliothibitishwa na kufanyiwa utafiti kuwa ni kweli mazao yao yanazalishwa kwa misingi ya kilimo hai.”

Anasema kuwa, mashirika kama OICOS, na MESULA yamekuwa yakisaidia wakulima kwa kiasi kikubwa kujiingiza katika vikundi vya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai, kuwapa elimu sahihi kuhusu kilimo hai pamoja na kuwatafutia masoko ya pamoja.

Anaongeza kuwa, wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hakuna soko lakini tatizo kubwa hawajajikita hasa katika uzalishaji kwa kufuata misingi ya kilimo hai.

Aidha, wanatakiwa kuangalia jamii inayowazunguka kwanza kwani soko linaanzia nyumbani kabla ya kuingia katika masoko makubwa.

Sifa za shamba la kilimo hai

Moja, ni lazima eneo lako la kilimo liwe na mboji. Wakulima wengi wanadai kuwa wanafanya kilimo hai lakini ukitembelea maeneo yao hayana mboji.

Mbili, hakikisha unatengeneza mboji hiyo kila wakati kwa kutumia mabaki ya mifugo na mazalia mengine isipokuwa taka ngumu.

Tatu, Lazima shamba liwe na uzio kwa ajili ya kuzuia sumu kali zinazotoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali na dawa za viwandani na hata kuzuia wanyama waharibifu.

Nne, uzio wa mkulima wa kilimo hai lazima uwe na miti ya dawa, ambayo hukinga wadudu waharibifu na pia hutumiwa kutengenezea dawa.

Tano, mkulima wa mazao ya kilimo hai ni lazima awe na elimu ya kutosha juu ya kilimo hai na aweze kuwaelimisha na kuwashauri wakulima wenzake waliomzunguka kuhusu faida na hasara za kilimo hai.

Kauli ya wataalamu

Wataalamu mbalimbali wanaeleza kuwa, kwa sasa bidhaa zinazotokanana kilimo hai zinazidi kuongezeka na hii ni kutokana na baadhi ya wanajamii kufahamu kwa kiasi kikubwa madhara yanayotokana na mazao yanayozalishwa kwa kutumia madawa na kemikali za viwandani.

Lukas Rwechoka, anasema wakulima wamekuwa na mwamko mkubwa kuhusiana na uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo hai, ila tatizo kubwa limekuwa soko ambalo mara kwa mara limekuwa likiwakatisha tamaa ya kuendelea kuzalisha bidhaa hizo.

Je, wakulima wanatakiwa kufanya nini ili kuondokana na tatizo hili? Wakulima wa mazao ya kilimo hai wanatakiwa wawe waaminifu na wafuatae misingi yote ya uzalishaji wa mazao ya kilimo hai.

Aidha, wasiwe wadanganyifu katika shughuli nzima ya uzalishaji wa mazao na bidhaa zote zitokanazo na kilimo hai.

Uelewa kwa walaji wa ndani nao bado ni changamoto kubwa. Kuhusu walaji wa nje, wao wana uelewa mkubwa na wakisaidiwa na sera za nchi zao na ufafanuzi mzuri juu ya mazao yatokanayo na kilimo hai.

Je, kuna njia yoyote ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai wanazozalisha?

Rwechoka anasema: “Njia ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai ni kuwa wakweli na waaminifu katika shughuli zote za kilimo hai.

Anaongeza: ‘’Wanatakiwa kuwa na takwimu sahihi na kufahamu kwa ufasaha hatua za uzalishaji tangu kulima, kupanda, kuhudumia mazao, kuvuna na kuhifadhi mazao hayo. Ili kufanikisha hayo, hakuna budi kuwaruhusu wakaguzi (mawakala) wa kilimo hai walioidhinishwa wafanye ukaguzi na kutoa mwongozo na ushauri juu ya suala zima na kuwataarifu wanunuzi juu ya hatua sahihi zilizofuatwa katika kilimo hai.’’

Makala haya ni kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org

Saturday, June 16, 2018

Lima vitunguu kisasa-6

 

Nukta ya makala iliyopita ilikuwa uhifadhi wa vitunguu baada ya kuvuna. Endelea

Hifadhi kwa kuninginiza vitunguu kwenye banda

Hili ni banda lenye uwazi mkubwa, lenye upana usiozidi mita tano, na urefu toka chini hadi juu usizidi mita mbili na nusu.

Banda linajengwa kwa miti, fito, mbao au mianzi na vitunguu vinahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye fremu za fito ndani ya banda. Safu za vitunguu hupangwa kufuata urefu wa banda na kimo cha banda.

Urefu wa banda huelekezwa kwenye mkondo wa upepo ili kuruhusu upepo kuingia na kutoka. Banda liezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua. Kribu au banda vinahifadhi vitunguu vizuri kwa muda wa miezi sita bila kuharibika.

Upotevu wa vitunguu ghalani

Vitunguu vingi hupotea wakati wa kuhifadhi kwa sababu ya kuoza, kuota (toa majani na mizizi) na kupoteza uzito

Kuoza

Kuoza kwa vitunguu vikiwa ghalani kunasababishwa na vimeliea vya fangasi au bakteria. Joto pamoja na unyevunyevu ndani ya ghala, husababisha kuzaliana na kuongezeka kwa vimelea vya magonjwa.

Kudhibiti: Weka ghala katika hali ya usafi, kausha vizuri na chambua vitunguu kabla ya kuhifadhi.

Muozo kitako

Vimelea vya aina ya fungus vinavyoishi kwenye udongo, vinashambulia sehemu ya chini ya vitunguu. Vimelea vinapenya kwenye sehemu zenye michubuko inayotokea wakati wa palizi, kuvuna au kusafirishwa. Vitunguu vinaoza na baadaye vinakauka na kusinyaa.

Njia zifuatazo zinadhibiti: mzunguko wa mazao, uchambuaji mzuri kabla ya kuhifadhi na

kuepuka michubuko wakati wa palizi na kuvuna

b) Ukungu mweusi (Black mould)

Ugonjwa huu unaletwa na vimelea vya fangasi vinavyoishi kwenye udongo. Vimelea vinazaliana katikati ya maganda na ukungu mweusi kama poda unaonekana. Baadaye maganda yanasinyaa na kuvunjika.

Kudhibiti

•Kutumia mzunguko wa mazao

•Kukagua ghala mara kwa mara na kuondoa vitunguu vilivyooza

•Kuweka ghala katika hali ya usafi.

•Kuondoa masalia ya vitunguu na kuchoma moto.

c) Kuoza shingo (Neck rot)

Vimelea vya fangasi vinashambulia vitunguu vikiwa shambani kabla ya kuvuna. Ugonjwa hauonekani mpaka vitunguu vikomae, vivunwe, vikaushwe na kuhifadhiwa ghalani, ndipo ugonjwa hujitokeza.

Ugonjwa unasababisha kuoza kwa vitunguu. Maganda ya vitunguu yanalainika kuanzia shingoni na nyama ya kitunguu huwa na sura ya maji maji. Vitunguu vilivyooza vinanyauka na kusinyaa.

Kudhibiti: kausha vitunguu vizuri kabla ya kuhifadhi, choma na kuharibu masalia ya vitunguu shambani na ghalani.

d) Muozo laini

Ugonjwa unasababishwa na vimelea vya bakteria. Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kulainika kwa vitunguu na kutoa harufu mbaya. Ukiminya kitunguu maji yenye harufu mbaya yanatoka kwenye shingo.

Muozo laini unatokea wakati hali ya hewa ikiwa na unyevunyevu na joto. Pia vitunguu vyenye shingo nene ambavyo havijakauka vizuri ni sehemu nzuri sana ya vimelea kuzaliana.

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture 0655-570-084. www.mogriculture.com

Saturday, June 16, 2018

Mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji-2

 

Makala haya ni mwendelezo wa makala yaliyopita juu ya mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji. Katika makala yaliyopita, tuliona mbinu sita za mwanzo na kubakiwa na mbinu sita nyingine kukamilisha mbinu zote ambazo makala haya ya leo yataongelea.

Hivyo ni fursa nyingine kupata ujuzi zaidi katika ufugaji kwa lengo la kuboresha biashara yako ya ufugaji.

Kabla ya kuendelea na mbinu sita zilizobaki, ni vema kujikumbusha mbinu sita zilizotangulia kwenye makala yaliyopita kupata mtiririko mzuri.

Kwanza tuliona mbinu ya kwanza katika kuzalisha mayai mengi ni kuchagua mbegu bora ya kuku yenye sifa za kutaga sana.

Mbinu ya pili ilikuwa ni kudhibiti vifo vya kuku shambani. Mbinu ya tatu ilikuwa kuzingatia umri wa kuku shambani. Mfugaji asikae na kuku wazee wasiozalisha.

Mbinu ya nne ilikuwa kudhibiti uzito wa kuku wanaotaga wasinenepe sana wala kukonda sana, kwani uzalishaji wa mayai utashuka.

Mbinu ya tano ilikuwa kujenga banda rafiki kwa maisha ya kuku na mfugaji mwenyewe. Mbinu ya sita ilikuwa kuondoa kabisa kuku wasiotaga kwa sababu mbalimbali kama vile vilema, wagonjwa wasiopona, wenye maumbo madogo kuliko kawaida, majogoo wasiohitajika na mbegu ya kuku ambayo sio kusudio la mfugaji.

Mbinu hizo hapo juu zilielezwa kwa kina kama ambavyo mbinu zilizobaki zitaelezwa kwa ufasaha kwenye makala haya ya leo.

Mbinu sita mpya

Mbinu ya saba ni matumizi ya mwanga wa jua na taa za usiku. Matumizi mazuri ya mwanga yanaweza kuongeza asilimia 20 hadi 30 kwenye uzalishaji wa mayai.

Kuku ni viumbe wanaopenda mwanga sana na uzalishaji wao wa mayai hutegemea urefu wa siku. Kuku wanaokaa kwenye mwanga kwa saa 16 huzalisha mayai zaidi kuliko kuku wanaokaa kwenye mwaga chini ya muda huo.

Kadiri muda wa mwanga unavyozidi kupungua ndivyo mayai yanavyopungua. Baada ya mwanga wa jua wa saa 12, inafaa kuwasha taa kuku wapate mwanga walau saa nne za ziada. Vilevile kuku wanahitaji kupumzika, hivyo zima taa wapate giza mara baada ya saa nne hizo kupita.

Mbinu ya nane ni chakula na ulishaji. Chakula bora na ulishaji unaotakiwa ndiyo uwezo wa kuku kutaga zaidi. Lisha mara mbili, mapema asubuhi na jioni jua likiwa limepoa. Zingatia kiasi kinachotakiwa kuku kula kwa siku.

Mbinu ya tisa ni kudhibiti joto bandani. Kuna wakati joto linakuwa kubwa kiasi cha kuku kushindwa kula vizuri au kunakuwapo na baridi kupita kiasi. Mabadiliko ya joto hushusha mayai sana, hivyo mfugaji anatakiwa kujua hili.

Wakati wa joto usiweke kuku wengi sana bandani, weka madirisha mengi ya kutosha, wape maji mengi ya kunywa pia lisha mapema alfajiri na jioni sana kukiwa kumepoa.

Epuka kunywesha maji yaliyokaa kwenye jua na kuchemka kama vile maji yaliyoko kwenye tanki la juu ya paa. Maji yaliyopata moto hayafai kunywesha kuku. Unaweza kufunika au kuweka kivuli kwenye tanki ili maji yasipate joto.

Mbinu ya 10 ni usimamizi. Kagua kila mara kujua kila kitu kwenye mabanda ya kuku kuanzia hali ya kiafya kwa kuku wako, kiasi cha chakula wanachopewa, muda wanaopewa chakula, usafi wa vyombo na mazingira

Pia, takwimu za idadi ya kuku bandani na mayai wanayotaga. Mambo haya ni muhimu sana kuziba mianya inayopunguza mayai kwenye shamba lako.

Mbinu ya 11 ni kuzingatia chanjo za kuku kwa magonjwa yenye chanjo na kuweka miundombinu yenye kuzuia magonjwa kuingia shambani kwako.

Kwa kiasi kikubwa magonjwa huletwa na binadamu na wanyama au ndege wanaoingia shambani. Kuweka uzio au chochote cha kuzuia watu au wanyama na ndege kufika shambani, ni njia salama kwenye mradi wako.

Kuweka kumbukumbu ya chanjo zote muhimu ni bora kuliko kusubiri kutibu kuku wakiugua. Baadhi ya magonjwa hayatibiki, hivyo suluhisho lake ni chanjo tu.

Mbinu ya 12 ni kutengeneza viota vya kutagia vilivyo safi na kuokota mayai kila mara bandani. Wafugaji wengi hupoteza mayai mengi kwa kuchelewa kuokota mayai, matokeo yake mayai huvunjika, kuchafuliwa na mbolea ya kuku na mengine kuliwa na kuku.

Okota mayai kila mara hasa muda wa asubuhi hadi saa sita mchana, kwani kuku hutaga zaidi. Kuacha mayai yajae kwenye vitagio ni kushawishi kuku kula mayai.

Usiache kuku watage kwenye sakafu, wala usiweke vitagio vichache bandani kwa kuwa kuku watavunja sana mayai. Kuku wakizoea kula mayai ni vigumu kuwazuia hata kama utaboresha chakula chao.

Ikiwa hali hii ya kula mayai imeshamiri, angalia viota vyako huenda sio rafiki kwa utagaji wa kuku kisha rekebisha.

Chunguza lishe ya chakula chao kama ina upungufu kwa sababu upugufu wa lishe hulazimu kuku kula mayai.

Ukifanya yote hayo lakini bado kuku wakawa wanakula mayai, basi kata midomo yao iwe butu. Kuwa mwangalifu wakati wa kukata; usikate sana wakashindwa kula. Tumia kifaa maalumu cha kukata na kupunguza damu isivuje.

Saturday, June 9, 2018

Umewahi kufikiria kulima mamung’unya?

 

By Asna kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Kwa wakazi wa mjini neno mung’unya huenda likawa geni kwao. Ukweli ni kwamba Tanzania kuna mazao mengi ambayo hayajulikani na wengi hali inayosababisha mazao hayo kuonekana hayana thamani.

Lakini kwa wale waliotambua thamani hiyo kwa sasa wanasema mazao hayo yanalipa tena mfano zao la Mung’unya ambalo halihitaji nguvu nyingi wala gharama katika kuwekeza bali akili na jitihada katika kulihudumia.

Jonathan Kadaso ni miongoni mwao, anasema baada ya kufanya tafiti amegundua kuwa zao hilo ni miongoni mwa mazao ya biashara ambayo yanaweza kumuingizia fedha za haraka.

Baada ya kufanya kazi katika kampuni mbalimbali ikiwemo za nje ya nchi katika kutoa ushauri wa kilimo aliamua kuacha baada ya kuona kazi hiyo kwake hailipi.

Kadaso aliyekuwa Bwana Shamba anasema alianza kilimo hicho mwaka 2015 baada ya kupata ushawishi kutoka kwa mwanafunzi wake aliyekuwa akimshauri masuala mbalimbali ya kilimo.

“Nilikuwa na mwanafunzi wangu ambaye nilikuwa namshauri katika masuala mbalimbali ya kilimo kama Bwana Shamba, lakini mwisho wa siku mwanafunzi akawa na mafanikio zaidi katika kilimo hapo ndipo nilipogundua kuwa kilimo ndiyo mpango mzima,”anasema.

Anasema zao kilimo cha mung’unywa hufanyika katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kwa ajili ya chakula tena halipewi kipaumbele kama ilivyo mahindi au mazao mengine.

Kwa yeye anasema kilimo hicho anakifanya katika kijiji cha Msata Wilaya ya bagamoyo mkoani Pwani na soko lake lipo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

“Ukweli ni kwamba baadhi watu hawajui thamani ya zao hili la Mung’unya kwa sababu hata unapoleta sokoni watu wengi hasa wa mjini huishia kulishangaa na kuuliza ni kitu gani hawajui kama zao hili ni zao la biashara pia,”anasema.

Mamung’unya ya kisasa (Butter nuts) ambayo ukubwa wake ni wawastani huuzwa moja kwa sh 1000 hadi 3000 kwa mkulima makini hakosi milioni 15 kwa heka moja.

“Nasema zao hili ni adimu kwa sababu watu wengi hawalijui, linachukuliwa kama zao ambalo linalimwa kwa uchache sana au linajiotea tu lenyewe porini. Habari njema ni kwamba zao hili linalimwa na zipo mbegu za kisasa achilia mbali hizo za kizamani,”anasema na kuongeza kuwa:

“Ukipata sehemu nzuri yenye rutuba, katika shina moja unaweza kukuta si chini ya mung’unya 20 zimezaliwa kwa hiyo kwa heka moja mkulima hakosi tani moja ama mbili,”anaongeza.

Kwa nini kilimo hicho

Anasema alifanya utafiti juu ya zao la Mung’unya nakubaini fursa nzuri kibiashara hususani maeneo ya mjini kwani mbali na vijijini baadhi ya walaji hupatikana huko.

“Kila kitu kinakuja kwa sababu na mimi niliwaza sana kwanini kuna zao hili lakini watu hawachangamkii fursa, huwezi amini nilianza na robo ekari lakini sasa nalima hadi ekari moja,”anasema.

“Nimefanya kazi mradi ya kilimo katika nchi mbalimbali kwa hiyo nilikuwa nafikiria baada ya kuacha kazi nitalima nini ambacho kitakuwa na faida katika maisha yangu, katika utafiti wangu nikagundua kuwa zao hili linasoko sana hasa nchini Kenya nikachangamkia fursa,”.

Lakini pia alijikita katika kilimo hicho baada ya kupata uhakika zaidi wa soko kutoka kwa rafiki yake anayeuza zao hilo nchini Kenya anasema kuanzia hapo akapata ujasiri wa kulima mamung’unya.

Kuhusu watumiaji wa zao hilo anasema zao hilo ni jipya kibiashara na hupendelewa kuliwa na watu jamii ya wahindi.

“Hivi sasa kidogo wanaanza kulitumia kama zao la biashara lakini kwa asilimia kubwa hulimwa kama chakula hasa kwa watu wenye kipato cha chini,”anaongeza.

Kilimo hichi ni kilimo ambacho hakina mambo mengi kama ilivyo mazao mengine cha msingi anasema kinachotakiwa lipatiwe maji ya kutosha na lisipandwe sehemu zenye joto.

“Zao hili linakubali zaidi mikoa yenye baridi mfano Lushoto Tanga,”anasema

Wito kwa wakulima.

Anatoa rai kwa wakulima kuwa hakuna kitu ambacho hakiuziki cha msingi ni kuwa na malengo na kile kitu ambacho mkulima anakusudia kufanya.

“Akili na malengo ndiyo vitu pekee ambavyo mtu akivifanyia kazi kamwe hawezi kujutia maamuzi yake mimi tangu nimeanza kulima japo kwa kiasi kidogo ninacholima lakini nayaona mafanikio yake,” anasema

Kuhusu soko anawaambia wakulima kwa kila kitu kinauzika cha msingi ajue unauza wapi na muda gani, kingine cha muhimu ni kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo ili kupata mwangaza zaidi.

“Wasilime kwa mazoea ya kusema kuwa wanalima kwa ajili ya chakula, kila zao ukilifanya kuwa la kisasa linalipa kibiashara, vijijini mang’umunya yapo lakini ukimueleza mkulima kuwa linaweza kuwa zao la biashara atashangaa,”anaongeza.

Kuhusu kumtoa mtu kimaisha anasema inategemea na soko: “Kama mtu anapata soko na akajitangaza anaweza kutoka kimaisha kwa sababu ni zao ambalo halihitaji uwekezaji mkubwa wala gharama nyingi lakini inazaa sana chamsingi ni maji na mbolea,”.

Wito kwa Serikali

Anatoa rai kwa Serikali kuweka utaratibu wa masoko kwa wakulima na kutoruhusu mazao kutoka nje ya nchi kwani hali hii inaathiri soko la mazao yanayozalishwa hapa nchini.

“Mbali na zao hili la mamung’unya (Butter nut) nalima pia mazao mengine hili suala la masoko huria linatuumiza sana wakulima wa ndani kwa sababu unakuta wananchi wengine wanapenda bidhaa za nje kuliko za ndani,”anasema.

“Msistizo utolewe kwa wakulima hasa katika kuongeza thamani ya mazao yao ili kuongeza ubora wa soko,”anaongeza.

Nchi nyingine kama Poland zao hili la Mung’unya wanaongeza thamani na wanasafirisha kuuza nje ya nchi hivyo anasema ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kuongeza mazao thamani kwa kusistiza wakulima.

“Unakuta tunalima nyanya lakini zinaharibika kwa sababu hata viwanda vya kusindika hatuna au kama vipo basi ni vichache,”anasema.

Kwa kuwa husafirisha mazao yake ktoka Mstata hadi Dar es Salaam ombi lake kwa Serikali ni kupunguziwa ushuru au tozo.

“Tuliambiwa ushuru wa mazao hakuna lakini ukienda vijijini bado tunatozwa wa hiyo suala hili liangaliwe upya,”anasema.

Kingine anasema Serikali itoe nafasi kwa wawekezaji hasa wakulima kuwekeza bila vikwazo kwani wanamchango katika kuleta maendeleo ya taifa.

Saturday, June 9, 2018

Zijue mbinu kumi na mbili za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji

 

By CLEMENT FUMBUKA

Tunaendelea kuibua na kuonyesha njia nyingi za kufanikiwa katika ufugaji wa kuku ambao ndiyo ndoto kubwa kwa wafugaji wengi. Fursa ya ufugaji inazidi kuchanua na kufanya vizuri kila kukicha kutokana na teknoloji kushamili.

Imekuwa kawaida kusikia mtu amejiajiri mwenyewe kupitia ufugaji wa kuku. Fursa nyingi za soko la kuku na mazao yake sambamba na elimu elekezi zinazotolewa mara kwa mara kwenye makongamano, warsha, semina na vyombo vya habari kama makala haya.

Mwendelezo huu wa uchambuzi wa leo unajikita katika kanuni bora za uboreshaji wa miradi yote ya kuku. Karibu upate kujuzwa mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi shambani kwako.

Kwa wale wasiopata makala haya kwa mwendelezo napenda kuwapa vidokezo vilivyopita kujadililiwa kwenye makala yaliyopita na kuwakumbusha kuwa makala haya hutolewa kila jumamosi.

Na hivi karibuni tulijadili juu ya sababu za kuku kunyonyoka manyoya, kukinga magonjwa hatarishi na sababu 10 za kukosa mayai kwa kuku. Leo ni mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji.

Mbinu ya kwanza ni Kuchagua mbegu ya kuku. Aina au mbegu ya kuku ndiyo siraha ya kwanza katika mbinu za kuzalisha mayai mengi shambani. Sio kila kuku anataga mayai mengi.

Zipo mbegu za kuku wanaotaga sana na nyingine zisizo taga mayai mengi. Ukiwa mfugaji mwenye lengo la kuzalisha mayai mengi kitu cha kwanza ni kupata mbegu ya kuku wenye asili ya kuzalisha mayai mengi.

Hata mkulima wa mazao shambani huchagua mbegu inayozaa sana shambani kwake. Hivyo chagua mbegu ya kuku inayotaga sana kama lengo lako ni kupata mayai mengi.

Mbinu ya pili ni kuzuia vifo vya kuku shambani. Kimsingi sio rahisi kuzuia vifo kwa sababu vifo ni sehemu ya maisha. Lakini vifo vingi hutokana na sababu zenye kuweza kuzuilika.

Zuia vifo kwa nguvu zote kwa kuziba mianya ya vifo kama vile kuimarisha kinga na tiba kwa magonjwa ya mlipuko, kuliwa na wanyama, kukosa hewa, joto kali na lishe. Vifo vikizidi kiwango huathili uzalishaji wa mayai na mavuno kwa mfugaji.

Mbinu ya tatu ni kuzingatia umri wa kuku. Kawaida kuku wa mayai wenye asili ya kuzalisha mayai mengi huanza kutaga wakiwa na umri wa wiki 20 na kuendelea hadi wiki 70 sawa na mwaka mmoja tangu kuanza kutaga kwao. Kipindi hiki cha utagaji ni kizuri kwa mfugaji kuvuna mayai.

Zaidi ya hapo mayai yatashuka kiasi cha kukosa faida. Hivyo uzalishaji uwe ndani na kipindi hiki kisha uza kuku wote na kuingiza wengine wapya. Ni vizuri kuingiza vifaranga watakaorithi mapema walau miezi sita kabla ya kuwauza wanaozalisha kwa wakati huo ili unapouza kuku wazee kuku wapya wawe tayari wameanza kutaga.

Mbinu ya nne ni kudhibiti uzito wa kuku. Wastani wa uzito wa kuku wenye kutaga sana ni kilo 1.5 zaidi au pungufu mno ya uzito huu kuku hatagi vizuri. Udhibiti huu wa uzito ufanyike katika ulishaji wa chakula. Mfugaji anashauriwa kulisha chakula kwa kipimo ili wasinenepe kuzidi kiasi au kuwapunja chakula chini ya kiasi wanachotakiwa kula wakakonda. Jambo la kuzingatia katika kudhibiti uzito ni kiasi na ubora wa chakula, chakula duni kuku watapungua uzito hata kama wanapewa kingi.

Mbinu ya tano ni kutengeneza banda rafiki kwa maisha ya kuku na mfugaji mwenyewe. Kwa kawaida kuku wanamahitaji yanayojulikana kama vile nafasi ya kutosha, hewa safi na joto la wastani bandani.

Ubunifu na uboreshaji zaidi wa mambo haya mfugaji anaweza kuongeza uzalishaji wa mayai. Kwa mfano mbinu ya kuweka kuku wengi kwenye chumba kidogo ni moja kati ya ubunifu.

Badala ya kufugia sakafuni mfugaji anaweza kuweka cages na kufuga kwa njia ya vizimba kuku wengi wakaingia kwenye chumba.

Mbinu ya sita ni kuondoa kuku wasiotaga. Katika kundi la kuku wengi, kuku wasiotaga hawakosi. Mfugaji anaweza kuchambua kuku wanaotaga na wasiotaga vizuri na kuwatenga.

Wasiotaga kabisa na wanaotaga kidogo anaweza kuwauza kuwauza kupunguza gharama ya chakula. Kwa mfano kuku wagonjwa bila dalili ya kupona, kuku walio wadogo sana kuliko kawaida kwenye kundi au kuku wasiohusika kama vila majogoo kwenye mitetea wanaotaga mayai ya kuuza bila kuangulisha au kuku wa kienye kwenye kundi la kuku wa mayai wa kisasa wote hao ni kuku wa kuchambuliwa na kuuzwa.

Kwa upande mwingine mfugaji anatakiwa kuwa mwangalifu anapotaka kufanya jambo lingine baada ya kukamilisha jambo la kwanza. Mara nyingi kila kitu unachotaka kufanya kinahitaji maandalizi na uchunguzi wa kujilithisha.

Pia mbinu hizi za kuzalisha mayai mengi kwa kuku hutegemeana hivyo inatakiwa kila mbinu kuifanyia mazoezi ya kutosha kiasi cha kuifanya vizuri. Au unaweza kujifunza kwa waliofanya mbinu hiyo mara kwa mara wakajua ufanisi wake.

Usijifunze kwa mtu aliyefanya kulipua ni rahisi kukukatisha tama na kukupoteza. Pata maelezo kwa wataalamu wenye kuaminika unapohitaji msaada wa maelekezo kufanya mbinu moja wapo kati ya mbinu hizo hapo juu utafauru vizuri.

Mbinu zingine sita juu ya kuzalisha mayai mengi zitakujia kwenye makala yajayo kukamilisha mbinu kumi na mbili.

Saturday, June 9, 2018

Lima vitunguu kisasa-5

 

Tunaendelea na mfululizo wa makala za kilimo cha vitunguu kama tulivyokianza wiki kadhaa zilizopita.

Kufungasha na kuweka vitambulisho

Vifungashio vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au magunia ya katani.

Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji. Magunia ya katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane. Pia yanachukua mzigo mzito na kuleta usumbufu wakati wa kupakia na kupakua.

Vitambulisho vinawekwa kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka na pia kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani.

Kwa soko la nje, utambulisho unatakiwa kujumuisha:

Jina la bidhaa mfano,vitunguu Mang’ola Red

Uzito kamili mfano kg20.

Jina na anuani ya mkulima au kikundi, jina na anwani ya msafirishaji

Jina la kijiji wilaya, mkoa na nchi mf. Igurusi, Mbarali, Mbeya, Tanzania Grade 1

Kwa soko la ndani utambulisho unajumuisha

Jina la bidhaa. mfano vitunguu Mang’ola Red

Uzito kamili mf. 20 kg

Jina la mkulima au kikundi na anuani John Geda au Jitegemee, Box 200, Mbarali Mbeya

Jina na anuani ya msambazaji mf: Mr. Saidi Mbaga Box 670, Mbeya

Usafirishaji

Uangalifu wakati wa kupakia, kusafirisha na kupakua ni muhimu ili kuepukana na uharibifu na upotevu wa vitunguu.

Mara nyingi vitunguu vinaharibika kutokana na ujazo kupita kiasi kwenye vifungashio na vyombo vya usafiri, pia kutokana na upakiaji na mpangilio mbaya, ambao unasababisha ugandamizaji na kubonyea kwa vitunguu.

Wakati wa usafirishaji yafuatayo yazingatiwe

Kutumia vyombo vya usafiri vinavyofaa hasa magari yenye nafasi ya kutosha na yenye kupitisha hewa.

Kupanga mifuko katika tabaka zenye safu zisizodi tatu

Mifuko isitupwe wakati wa kupakia na kupakua

Vitunguu visichanganywe na mazao mengine.

Namna ya kuhifadhi vitunguu

Vitunguu vinahifadhiwa kwenye maghala bora kama karibu au mabanda ambayo yanaruhusu hewa na paa kuezekwa kwa manyasi ili kupunguza joto.

Hifadhi kwenye kribu

Kribu inajengwa kwa fito au mianzi na kuinuliwa juu mita moja toka usawa wa aridhi. Upana wa kribu uwe kati ya sm 60 na 150 ili kuruhusu upepo kupita kwa urahisi.

Upepo unaondoa unyevu na joto kwenye vitunguu. Kribu igawanywe sehemu mbili zenye kina cha sm 60 kila moja na kutenganishwa na uwazi was m 30, ili kuruhusu mzunguko wa hewa.

Wakati wa kutengeneza kribu yaafutayo yazingatiwe

Kribu ijengwe kwenye sehemu yenye upepo

Kribu iezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua

Miguu ya kribi iwekwe vizuizi vya panya.

Weka vutunguu tabaka mbili na kina cha vitunguu kisizidi sm 60

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji.

0655-570-084

Saturday, June 2, 2018

Safari ya Mmakuwa kutoka ng’ombe mmoja hadi 20

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Alianza na ng’ombe mmoja, lakini sasa anao 20. Ni hivi, kumbe ng’ombe mmoja anaweza kukupa wengine 20.

Juma Mmakuwa, mkazi wa kijiji cha Mitwero mkoani Lindi, hatamani kufanya kazi nyingine zaidi ya ufugaji wa ng’ombe, shughuli anayosema inampatia kipato cha kuendesha maisha yake.

Muhimu ni uthubutu na kufuga kisasa, hizi ndizo siri za kufanikiwa katika kilimo. Haijalishi umeanza na idadi gani ya mifugo. Ukifuata kanuni, kicheko cha mafanikio ya ufugaji hakipo mbali.

Alivyoanza ufugaji

Anasema kuwa ufugaji huo unaofanya ndani ya banda nje ya nyumba yake, aliuanza tangu mwaka 2006 na idadi ilianza kuongezeka miaka miwili baadaye.

“Baada ya miaka miwili aliniongezea idadi na kuwa ng’ombe wawili na hufanya hivyo kila baada ya miaka miwili anazaa na kuifanya idadi kuongezeka maradufu. Biashara yangu ya maziwa nayo ikakua,”anasema.

Anasema aliamua kufuga baada ya kung’amua fursa iliyopo katika biashara ya maziwa kama anavyosimulia:

“Nilikuwa nafanya biashara zangu nyingine, hivyo katika mapato yangu nikaamua kununua ng’ombe, kwa kuwa niliambiwa biashara ya maziwa inalipa. Mara moja nikachangamkia fursa.’’

Mmakuwa mwenye ndoto ya kuwa mfugaji bora anasema lengo lake hivi sasa ni kuongeza mradi wake wa ufugaji kwa kwa na idadi kubwa zaidi ya ng’ombe.

“Lengo langu kubwa ni kuwa na kiwanda cha kusindika bidhaa zitokanazo na ng’ombe, ili kupanua wigo na kuajiri vijana wasio na ajira,”anasema.

Biashara ya maziwa

Kwa siku Mmakuwa anakamua lita 20 za maziwa na anasema isingekuwa magonjwa, angeweza kupata zaidi ya ujazo huo.

“Kiasi hicho cha maziwa ninachopata ni kwa sababu ng’ombe hawapati chakula maalumu kama vile pumba. Hapa wanakula tu majani na wakati mwingine vikipatikana virutubisho nawatengenezea kwenye pumba. Biashara hii kwa mwezi sikosi Sh500,000, anasema na kuongeza:

“Nauza maziwa lita moja kwa Sh1,500, ni kiasi kidogo kwangu kwa sababu wateja wa maziwa siyo wengi. Naamini kama soko lingekuwa zuri, ningepata zaidi ya Sh 1milioni kwa mwezi.’’

Mmakuwa hakuwahi kuajiriwa, lakini kupitia ufugaji wa ng’ombe amejenga nyumba nzuri huku akijinasibu kuwa nyumba hiyo haina tofauti na nyinginezo zinazomilikiwa na watu wenye ajira. Kikubwa ni malengo, wazo la kujenga lilikuja baada ya kufikisha ng’ombe watano. Niliuza watatu nikanunua kiwanja, nikasuburi tena kila wakiongezeka nauza, nilijenga taratibu kwa muda wa miaka sita hadi kukamilisha ujenzi kupitia mifugo yangu.’’

Changamoto

Mbali na kufurahia mafanikio yake, anasema changomoto aliyonayo ni eneo la kufugia na vyakula vyenye virutubisho. Anasema kwa sasa ng’ombe wake wanakula zaidi Majani tena katika maeneo asiyoyamiliki.

Magonjwa nayo ni moja ya changamoto katika safari ya mafanikio yake, kwani anasema mara nyingi ng’ombe wake hufa kwa ajili ya magonjwa mbalimbali.

“Kwa kweli kama sio magonjwa, ningekuwa na ng’ombe wengi. Kwa mfano, mwaka jana walifululiza kuzaa lakini walikufa kwa magonjwa ya kukatika mikia na kukohoa,” anaeleza.

Wito kwa Serikali

Mmakuwa anatoa rai kwa Serikali kusaidia wataalamu wa mifugo ili waweze kuhudumuia mifugo, kwani anasema kinachowakwamisha wafugaji kama yeye ni uhaba wa wataalamu ya afya ya mifugo.

“Wataalamu wapite mara kwa mara na ikiwezekana kila baada ya wiki moja, ili waweze kukagua na kutupatia ushauri wa namna ya kuepuka magonjwa ya mifugo na kushauri ng’ombe wa aina gani wanafaa kufuga.

Daktari wa mifugo

Rickey Zengele ni daktari wa mifugo kutoka kituo cha Bingwa Vet kilichopo mkoani Morogoro. Anasema, kinachowakwamisha wafugaji kupata faida ni kufuga bila kuwa na elimu ya kile wanachokifanya.

Anasema wapo wanaofuga kufuata mkumbo, lakini hawafahamu kuwa kufuga ng’ombe kunahitaji elimu ya kutosha, kwani bila ya hivyo mfugaji anaweza akachukia kabisa ufugaji

“Unakuta mtu anafuga ngombe lakini hajui ng’ombe anatakiwa kupewa tiba baada ya muda gani. Ifahamike kuwa mbali na ile chanjo ya kila mwaka mara moja, kuna chanjo nyingine ambazo zinatakiwa kila baada ya miezi mitatu ikiwemo ile ya minyoo” anasema.

Anasema mfugaji anatakiwa kufahamu kuwa kuna aina mbalimbali za magonjwa ambayo kama hayatatibiwa mapema yanaweza kudhoofisha afya ya mifugo na hata kusababisha kifo

Kwa wafugaji, kama wanahitaji kunufaika na ufugaji wa ng’ombe wanahitaji kuwa makini na magonjwa aina ya Ndigana kali, Ndorobo ugonjwa wa midomo na miguu kifua kikuu na ugonjwa wa chuchu. Anasema magonjwa hayo yanaweza kuathiri afya na uzalishaji wa maziwa na nyama.

“Hapa utakuta kama ng’ombe alikuwa anatoa maziwa lita tano atapunguza hadi lita moja au mbili. Kwa wale wanaofuga ng’ombe wa nyama, wanaweza kuathiri biashara yao, kwani ng’ombe mgojwa nyama yake sio nzuri hata kwa muonekano”

“Kwa kawaida ng’ombe anatakiwa kuchanjwa kwa mwaka mara moja, kuna zile kalenda ambazo zinatengenezwa na halmashauri husika au kila mkoa unakuwa na taratibu zake,”anaongeza.

Anatoa tahadhari kwa wafugaji wanaotamani kufuga ng’ombe wa kizungu….’’ Hawa ni wazuri, lakini wafugaji hawajui hali ya hewa inayotakiwa kwa mifugo hiyo. Unakuta wengine wanakufa na kusababisha hasara. Ng’ombe wa kizungu kwa asilimia 100 wanatakiwa waishi maeneo yenye baridi, kwa hapa Tanzania wanafugwa kwa wingi Makete.’’

Dk Zengele anasema kwa wale wafugaji wa maeneo ya joto kama vile Dar es Salaam, wanatakiwa kufuga ng’ombe aina ya chotara.

Saturday, June 2, 2018

TFS inavyoshughulika na rasilimali misitu nchini

 

By Tulizo Kilaga, TFS

Umuhimu wa wanyamapori na misitu ambao Taifa limeutambua tangu mwanzo wa uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), hivi sasa unazidi kuongezeka siyo tu katika kuwavutia watalii wengi hapa nchini, lakini pia katika kutunza mazingira.

Mazingira hayo ni yale yanayoyotuzunguka yanayojumuisha hewa, udongo na maji ili nchi yetu iweze kutoa mchango wake stahiki katika kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yameikumba sayari tunayoishi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, anasema kuwa uchumi wa Tanzania unategemea kwa kiasi kikubwa misitu iliyopo.

Anasema, misitu iliyopo inahitajika kwa matumizi ya vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo kuwapo kwake hutegemea zaidi uhifadhi wake na matumizi endelevu katika jamii inayotuzunguka.

Profesa Silayo anabainisha baadhi ya changamoto zilizopo kwa sasa kuwa ni pamoja na uvamizi wa misitu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu kama uvunaji na kilimo.

Mtendaji huyo anasema usafirishaji haramu wa mazao ya misitu na uvunaji wake, unafanyika katika maeneo yaliyoruhusiwa kuvunwa kisheria na maeneo ya hifadhi ambayo hayaruhusiwi shughuli za kibinadamu.

Sekta ya misitu na maliasili kwa jumla zinakabiliwa na changamoto kubwa katika uhifadhi, kutokana na kubadilika kwa mazingira ya kazi na mifumo ya kihalifu yanayosababisha mfumo wa utendaji wa sasa wa kiraia kushindwa kukabiliana na hali hiyo.

Profesa Silayo anasema, Serikali imeamua kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa wa jeshi usu (Paramilitary), ili kukabiliana na changamoto za uvunaji haramu lakini pia changamoto za kiusalama.

Hii ni kwa kuwa changamoto zilkuwa zinaongezeka kutokana na TFS kutokuwa na uwezo wa kumiliki silaha na kutumia mbinu nyingine za kijeshi, kwani katika ulinzi wa misitu kuna wahalifu wanaotumia silaha za kivita.

Hata hivyo kubadili mfumo wa kiutendaji na kwenda kwenye mfumo wa Jeshi Usu pekee hakutoshi. Wakala unaendelea kuchukua hatua kadhaa ili kuboresha mbinu za usimamizi wa misitu nchini. Hatua hizo ni pamoja na;

Kuongeza maeneo ya hifadhi

Jumla ya misitu 11 yenye wastani wa 280,000ha itahifadhiwa katika mwaka huu wa fedha. Misitu hii inapatikana katika wilaya za Chunya, Handeni, Singida, Chamwino, Mkinga, Nyasa, Buhigwe na Tunduru. Lengo ni kuhifadhi bionuai, kuhakikisha mapito ya wanyamapori na hifadhi ya maji.

Utatuzi wa migogoro

Uharibifu wa misitu ni mkubwa hasa maeneo ambayo vijiji vimeanzishwa ndani ya misitu bila kufuata sheria. TFS imeendelea kuzuia upanuzi zaidi wa vijiji hivyo, licha ya kuwa hadi sasa kuna vijiji 228 vinavyofahamika na miji kadhaa.

TFS inaendelea kutatua migogoro hiyo kwa kusaidia maandalizi ya mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 90 vinavyozunguka misitu ya hifadhi ya Serikali Kuu.

Upandaji miti

TFS imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuhakikisha miti inapandwa ili kuhuisha ardhi nchini. Kwa upande wa upandaji miti katika misitu ya Serikali, takribani miche milioni 18 itapandwa.

Kupunguza matumizi ya nishati ya mimea

Matumizi ya mkaa na kuni yanatishia ustawi wa misitu yetu. Matumizi yake yanatokana na ukweli kwamba hakuna nishati mbadala inayoweza kumudu jamii kubwa na pia usambazaji wa hizi zilizopo kama gesi bado ni kwa kiasi kidogo.

TFS inaratibu wizara tano na taasisi za Serikali nne pamoja na sekta binafsi katika kutatua tatizo hili. Tayari Utumishi na Utawala bora wametoa kinachoitwa ‘deduction code’ kwa kampuni za gesi ili watumishi wa Serikali waweze kukopeshwa gesi na vifaa vyake kutoka kwenye mishahara.

Aidha, TFS inashirikiana na kampuni ya KopaGAS kutafuta fedha kueneza teknolojia ya kuuza gesi rejareja kwa mfumo wa ‘Lipa Unavyotumia – LUKU’. Hii ni pamoja na kusaidia sekta binafsi kuzalisha mkaa mbadala.

Matumizi ya mifumo ya kisayansi, teknolojia

Professa Silayo anasema tayari matumizi ya ndege zisizotumia rubani, yameanza katika kusimamia misitu ya mikoko.

‘’Tumeanza katika Delta ya Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la Wetland International. Ndege zaidi zinategemewa kuletwa nchini muda wowote kusaidia doria za mwambao wa baharí,’’ anasema.

Jitihada nyingine

Profesa Silayo anataja jitihada nyingine kuwa ni kushirikisha vyombo vingine vya ulinzi katika kusimamia misitu kama Suma JKT, Polisi, kuwashirikisha wananchi katika maeneo mbalimbali, kurudisha misitu ya Serikali za mitaa iliyoharibika chini ya usimamizi wa serikali kuu (TFS)

Nyingine ni kuboresha ufugaji nyuki ili uwe chachu ya uhifadhi, kipato na utalii, pamoja na kutoa mafunzo ya uadilifu pamoja na kuchukua hatua kwa watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma. Hizi ni sehemu ya jitihada mbalimbali ambazo TFS inazochukua kuhakikisha usimamizi endelevu wa misitu.

Mwandishi wa makala haya ni ofisa habari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Saturday, June 2, 2018

Lima vitunguu kisasa-4

 

Tunaendelea na mwendelezo wa mada kuhusu ulimaji wa vitunguu kisasa

Kuvuna na uhifadhi wa vitunguu

Kabla ya kuvuna vitunguu kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Dalili ya vitunguu kukomaa ni majani kunyauka na kuanza kukauka, asilimia 75 hadi 100 ya mimea huangusha shingo na majani kukauka.

Kuvuna

Vitunguu huweza kuvunwa siku 90 mpaka 150 tangu kupanda mbegu kutegemeana na aina. Vitunguu vinavunwa kwa mikono. Mimea inang’olewa au kuchimbuliwa kwa kutumia rato (jembe uma).

Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na majani kukinga jua kali kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa.

Lengo ni kuimarisha ngozi ya vitunguu na kufanya michubuko na majeraha madogo madogo yanayotokea wakati wa kuvuna kuwa magumu na kutengeneza makovu ambayo yanazuia vimelea vya magonjwa kuingia ndani.

Pia kupunguza unyevu kwenye majani na mashina na kuruhusu sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo, vitunguu vichambuliwe na kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu nyingine.

Kuchambua

• Tenga vitunguu vilivyooza, kuchubuka na kupasuka. Vitunguu vizuri vikaushwe pekeyake.

• Iwapo vitunguu vitahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye chaga, basi shingo zisikatwe, bali zisukwe na kufungwa pamoja, na kuninginizwa.

Kukausha

Hatua hii ni muhimu ili kupunguza unyevu, kufanya vitunguu viwe vigumu na kuwa katika hali ya kulala bwete. Vitunguu vinaweza kukaushwa kwa kuning’iniza kwenye chaga zilizopangwa mfano wa dari ndani ya banda au kutandaza kwenye kichanja chenye kuruhusu mzunguko wa hewa pande zote, chini ya kivuli sehemu kavu.

Epuka kukausha vitunguu chini kwenye ardhi na hasa sehemu zenye jua kali. Jua linababusha vitunguu na kusababisha uharibifu. Ukaushaji huchukua muda wa siku saba au zaidi kutegemeana na hali ya hewa.

Kupanga madaraja

Vitunguu vinachambuliwa tena baada ya kukaushwa ili kuondoa vitunguu vyote vyenye ugonjwa au dalili za ugonjwa, vilivyoota na kutoa mizizi na vyenye shingo nene.

Vitunguu vinapangwa kwenye madaraja mbalimbali kufuata ukubwa, umbo au rangi. Hii inawezesha kupata soko zuri na kuepukana na upotevu mkubwa wakati wa kuhifadhi.

Kufungasha na kuweka vitambulisho

Vifungashio vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au magunia ya katani. Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji.

Magunia ya katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane pia vinachukua mzigo mzito na kuleta usumbufu wakati wa kupakia na kupakua. Vitambulisho vinawekwa kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka na pia kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani.

Makala haya yameandaliwa kwa hisani ya Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. 0655-570-084. www.mogriculture.com

Saturday, May 26, 2018

Kilimo cha pilipili ni fursa isiyojulikana na wengi

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Ni nadra kusikia wakulima wakizungumzia kilimo cha pilipili hasa pilipili aina ya ‘Bird’s eye chili’, kwa Kiswahili maarufu kwa jina la pilipili kichaa.

Wakulima wengi wanavutiwa na mazao wanayosema yanawapa fedha za ‘chapchap’ kama vile matikiti, nyanya na hata mbogamboga.

Wasichokijua ni kuwa kuna fursa katika kilimo cha pilipili. Na sio tu pilipili kichaa, lakini hata aina nyingine kama pilipili mbuzi, pilipili mtama na nyinginezo.

Tanga wachangamkia fursa

Katika kijiji cha Chongoleani mkoani Pwani, kuna ardhi mwanana yenye rutuba kwa kilimo cha jamii mbalimbali za mazao ya mbogamboga.

Wakati wakazi wengi wa kijiji hicho wakijishughulisha na kilimo cha mazao kama mihogo, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Abdul Mkono, anawaongoza wenzake kulima pilipili kichaa baada ya kung’amua fursa ya soko iliyopo kuhusu zao hilo.

Ni soko endelevu kwa kuwa pilipili tofauti na mazao mengine ya mbogamboga, zina sifa ya kukaa kwa muda mrefu shambani. Kwa mwaka unaweza kuvuna zaidi ya mara nne na zao hilo linaweza kuishi kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja.

Mkono anasema kupitia zao hilo ameweza kufungua kampuni iitwayo Makaru Agro Limited, huku akishirikiana na wenzake 21.

Kwa nini pilipili?

Awali anasema walikuwa wanalima mazao mengine ya mbogamboga kama vile nyanya, tikiti maji na pilipili hoho. Lakini walipogundua fursa ya pilipili, mazao wakayaweka kando.

“Ukiangalia unaweza usiamini, lakini ukweli ni kwamba pilipili ni zao ambalo mkulima hatojutia maamuzi yake.

Sisi tumeanza na ekeri tano pekee lakini hatukosi Sh 25 milioni kila msimu wa kuvuna,”anasema.

Mkono anasema kilichowasukuma kuingia katika kilimo cha pilipili, ni uwezo wake wa kuweza kukaa kwa muda mrefu shambani.

“Tumegundua kuwa pilipili ni zao ambalo linazaa sana na hata uvunaji wake siyo kama mazao mengine kama tikiti maji ambalo ukivuna umevuna. Zao hili ukivuna linatoa maua mengine nakuzaa, kwa hiyo inaweza kufanya hivyo kama mara tano,” anaeleza.

Msukumo mwingine wa kulima anasema kuwa zao hilo linavumilia magonjwa, hivyo linapunguza gharama za mara kwa mara za kununua dawa.

“Ukishavuka zile hatua za awali na kama utalihudumia zao lako na kufuatilia kwa ukaribu, zao hili linapunguza gharama za mara kwa mara za kupiga dawa, ambazo mara nyingi zimekuwa zikisababisha usumbufu kwa wakulima wengi,” anasema.

Changamoto

Kila penye mafanikio hapakosi changamoto, Mkono anasema mbali na faida wanayopata kupitia zao hilo bado wanakumbana na kadhia ya uvivu wa wafanyakazi shambani.

Pilipili zinatakiwa kuvunwa kwa haraka kabla hazijaiva sana na kudondoka chini, kwani hali hii inaweza kusababisha hasara kwa hiyo inategemea na wavunaji,’’ anasema na kuongeza:

“Tunahitaji kuwa na mfanyakazi ambaye kwa siku anaweza kuvuna si chini ya kilo saba hadi 10, lakini kwa hawa waliopo wamevuna nyingi ni kilo nne.’’

Hali ya hewa nayo ni changamoto katika zao la pilipili, kwani anasema mvua inaponyesha zao hilo linaweza kupatwa na wadudu, jambo linalomlazimu mkulima kupiga dawa mara kwa mara.

“Mvua ikiwa kubwa ratiba ya upigaji dawa ya mara kwa mara inaweza kuwepo bila mkulima kupanga kwa ajili ya kinga dhidi ya magonjwa na wadudu,”anasema.

Matarajio

Anasema wanatarajia kuwa na mtandao wa Watanzania ambao watazalisha pilipili kwa kupata elimu na mwongozo kutoka kwao.

Mtandao huo anasema sio tu utachangia kutoa ajira, lakini utakuza wigo wa shughuli za kilimo hicho nchini kwa minajili ya kwenda katika soko la dunia.

Mkono anasema wakulima bado hawajachelewa, ni wakati kwa Watanzania kutafuta namna ya kuwekeza katika kilimo cha pilipili.

‘’ Wito wangu kwa Watanzania ni kuwa wasichague mazao ya kulima na pia wasilime bila kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu. Kilimo ndiyo sehemu ambayo mtu anaweza kufanikiwa kwa haraka,”anasema na kuongeza:

“Kilimo cha pilipili ni kilimo ambacho ukijitengenezea mazingira mazuri hutatamani kufanya kilimo kingine. Mimi nawasahauri wakulima wapambane, kilimo ni mkombozi.’’

Aidha, anawasihi Watanzania wanaotamani kujihusisha na kilimo, kufanya utafiti wa kutosha wa masoko ya mazao wanayotaka kuzalisha.

Wito kwa Serikali

Mkono anasema: “Naamini Serikali ina uwezo wa kuonyesha fursa mbalimbali, ikiwamo kuangalia soko gani ambalo linahitajika katika nchi mbalimbali za nje. Watusaidie iwe ni ndani ya nchi au nje tuweze kupata masoko na bei nzuri kwa ajili ya kumnufaisha mkulima.’’

Saturday, May 26, 2018

Zijue sababu za kuku kunyonyoka manyoya

 

Karibu tena katika ukurasa wa ufugaji wa kuku, ili ujue mengi kuhusu sekta hii inayopendwa na walio wengi.

Baada ya kutazama magonjwa yanayoshamiri zaidi wakati wa mvua kwenye makala yaliyopita, ni wito wangu kwa wafugaji wote kufuata kanuni za ukingaji magonjwa hasa kila inapotokea mabadiliko ya hali ya hewa.

Tuliona magonjwa mengi hulipuka wakati wa mvua, kipindi ambacho maeneo mengi yanajiandaa kutoka kuingia kwenye Kiangazi. Natumai msomaji wangu unafuatilia na kutunza kumbukumbu zinazokusaidia katika hatua za ufugaji.

Baadhji ya kumbukumbu muhimu ni pamoja na kutunza kalenda ya utoaji chanjo kwa magonjwa hatari ya kideri na gumboro.

Kideri na gumboro ni magonjwa ambayo husumbua sana nyakati zote na huenea haraka wakati wa kiangazi.

Kuku kunyonyoka manyoya

Makala ya leo yatajikita katika kuonyesha sababu zinazochangia kuku kunyonyoka manyoya.

Kwa kawaida kuku huwa hawanyonyoki manyoya wakiwa wadogo hadi wazeeke. Hivyo sababu ya kwanza kunyonyoka manyoya kwa kuku ni umri.

Kuku akiwa mzee, manyoya huharibika na kunyonyoka iwe mtetea au jogoo. Kunyonyoka kwa umri hutokea baada ya kipini kirefu cha kutaga kama ni mtetea baadaye kupumzika.

Manyoya huanza kunyonyoka kuanzia shingoni, mgongoni, mkiani na sehemu nyingine. Kunyonyoka huku hufuatiwa na kuota manyoya mengine.

Tatizo hili halina njia ya kulizuia; kama kuku wamefikia hatua hiyo, mfugaji anaweza kuwapa chakula bora cha kutosha na matunzo safi ili wawahi kutoka kwenye hali hiyo.

Kabla ya kuwapa huduma nzuri unaweza kuanza kwa kuwapunguzia chakula taratibu au kuwapa chakula chenye protini kidogo wapate mshituko na kuwahi kunyonyoka kwa pamoja.

Utatakiwa kuwapa huduma bora na chakula chenye protini kwa wingi zaidi kama vifaranga kwa muda wa wiki mbili na kuwarudisha kwenye chakula chao cha kawaida baada ya kuota manyoya mapya kwa asilimia 80. Kubadilisha chakula kufanyike taratibu sio ghafla, huku ukifuata kanuni za uzoeshaji wa chakula kila unapotaka kubadilisha kama ilivyoelezwa kwenye makala zilizopita.

Pili, kuku wanaweza kunyonyoka kwa kukosa virutubisho aina ya protini kwenye chakula chao.

Kuku wenye upungufu wa protini hunyonyoka manyoya sawa na kuku wazee hata kama ni kuku wadogo walio katika rika la kukua bila kujali mitetea au majogoo.

Kuku hunyonyoka manyoya ya mgongoni na mkiani kisha huanza kudonoana kama wanaishi kwenye sakafu bandani.

Kuku wanaoishi kwenye vizimba (cages) ni vigumu kudonoana kutokana na mazingira ya vizimba kutoruhusu kudonoana.

Suluhisho la tatizo hili ni kuhakikisha unawapa kuku chakula chenye makundi yote ya chakula kwa kiwango kinachatakiwa.

Katika mchanganyiko wa chakula cha kuku, weka walau vyakula vyenye protini itokanayo na wanyama na mimea.

Protini itokanayo na wanyama unaweza kuipata kwenye damu ya mifugo iliyokaushwa, dagaa au uduvi.

Protini ya mimea unaweza kuipata kwenye mashudu ya alizeti, pamba, karanga, mawese na mazao mengine ambayo hukamuliwa mafuta na kubaki mashudu.

Soya pia ni protini safi kwa mifugo ambayo husifika na kutumika hata bila ya protini itokanayo na wanyama kama itatumika vizuri, changamoto yake ni bei kuwa juu na upatikanaji wake pengine ni mgumu.

Lengo la kutumia mashudu au makapi ya vyakula, ni kupunguza gharama za uzalishaji wa zao la kuku.

Tatu, mitetea kupandwa na majogoo mara kwa mara husababisha manyoya ya kichwani, shingoni kunyonyoka kutokana na majogoo kuparua mgongo wa mtetea kwa makucha na mdomo kushika kichwani.

Weka idadi isiyozidi kiwango kwenye mitetea, jogoo mmoja anatosha kuhudumia mitetea tisa hadi 10. Kuweka majogoo mengi ni kusababisha fujo bandani na mitetea kupandwa bila kupumzika.

Epuka kuweka majogoo wenye rika tofauti kwenye banda moja. Majogoo wadogo watapigwa na jogoo wakubwa.

Kama unafuga kuku kwa ajili ya mayai pekee bila kuangulisha, hutakiwi kuweka jogoo yoyote bandani; waache mitetea wakae wenyewe watage bila bugudha.

Nne, kubadilisha chakula mara kwa mara. Chakula pia ni sababu ya kuku kunyonyoka manyoya kutokana na mpishano wa lishe katika vyakula hivyo.

Kama unatengeneza chakula chako mwenyewe ni vema kupima kiwango cha lishe yote kwenye chakula cha kuku wako, kwani maabara za kupima chakula cha mifugo zipo karibu sehemu nyingi na gharama zake ni nafuu.

Unaweza kuchukua sampuli ya chakula chako ulichochanganya na kwenda kupima kila kitu kikaonekana na kupata ushauri wa kitaalam.

Tano, joto kali, kubanana na kukosa hewa safi bandani husababisha mshituko na maisha yasiyo na furaha.

Mshituko wa muda mrefu, kukosa maji ya kutosha na chakula kwa kugombania, ni sababu za kuku kunyonyoka manyoya. Zingatia mahitaji bora ya kuku bandani, nafasi, hewa chakula na maji ya kutosha.

Sita, wadudu waishio juu ya ngozi ya kuku kama vile viroboto, chawa na utitiri husababisha kunyonyoka manyoya endapo wataishi nao kwa muda mrefu bila suluhisho.

Safisha mara kwa mara kwa kuondoa vumbi kwa maji na kupiga dawa kabla hujaingiza kuku wapya kwenye banda. Tumia dawa za kuua wadudu hao mara baada ya kuona dalili zao katika kuku wako.

Saturday, May 19, 2018

Utengenezaji na faida ya kutumia mboji shambani

 

By Steven Kibigili

Mboji ni aina ya mbolea ya asili yenye rangi nyeusi na harufu ya kidongo, ambayo hutokana na kuoza kwa mchanganyiko wa masalia ya mimea kunakosababishwa na wadudu rafiki wa mazao.

Muozo wa kutengeneza mbolea ya mboji ni tofauti na muozo wa kawaida, kwa sababu muozo wa mboji unahitaji usimamizi ili kupata matokeo mazuri, ambapo masalia ya mimea mbalimbali ambayo kwa pamoja hutambulika kama malighafi, hukusanywa na kutengeneza biwi au lundo litakalooza na kuwa mboji kamili.

Vitu vya msingi utengenezaji wa mboji

Vijidudu na wadudu: Sehemu kubwa ya lundo la mboji huozeshwa na vijidudu kama vile bakteria na fangasi ambavyo katika hali ya unyevu huhitaji Kaboni kama chanzo cha nishati na Naitrojeni kama kiungo muhimu cha protini, amino acid na enzymes muhimu kwa ukuaji wa seli zao na kuzaliana.

Vilevile baadhi ya wadudu rafiki wa mazao huhusika katika kumeng’enya malighafi wakati wa kutengeneza mboji. Wadudu hao ni kama vile jongoo, tandu, mnyoo mwekundu, kiwavi wa bito, siafu na wengineo.

Hewa: Vijidudu huhitaji hewa ya oksijeni ili viweze kuozesha malighafi kwa muozo unaohitaji hewa. Katika kiwango cha kutosha cha hewa ya oksijeni vijidudu huzaliana kwa kasi na hivyo biwi huoza kwa haraka.

Unyevu: Vijidudu vinahitaji unyevu ili viweze kuishi na hivyo kuozesha malighafi kwa urahisi. Shughuli za kibaiolojia za vijidudu zinaweza kusimama ikiwa biwi litakuwa katika hali ya ukavu uliopitiliza. Vilevile biwi linapokuwa limelowana sana hudidimia na kuzuia kuingia kwa hewa na hivyo kusababisha kutokea kwa muozo usiohitaji hewa.

Joto: Joto huchochea shughuli za kibaiolojia za vijidudu na kusafisha biwi kwa kuua mbegu za magugu na vimelea vya magonjwa vilivyo katika malighafi. Kiwango kikubwa cha joto huongezeka katika biwi kutokana na shughuli za kibaiolojia zinazofanywa na vijidudu katika kuozesha malighafi na kiwango fulani kutokana na mionzi ya jua.

Malighafi za kutengeneza mboji

Malighafi mbichi: Malighafi mbichi hujumuisha majani mabichi, mashina ya kijani ya mimea na mabaki ya jikoni kama vile maganda ya mbogamboga na matunda yaliyooza.

Malighafi mbichi huwekwa katika lundo kama chanzo cha Naitrojeni. Mfano: Mimea hapa inaweza kuwa majani ya mimea ya jamii ya mikunde, magugu mabichi, nyanya zilizooza, maganda ya kabichi, maganda ya ndizi, nyasi changa zisizo na mbegu, maganda ya kahawa, majani ya mlonge, majani ya mwembe na mengineyo.

Malighafi kavu: Malighafi kavu hujumuisha majani yaliyokauka ya mimea mbalimbali, vijiti na mabaki makavu ya mazao. Malighafi kavu huwekwa katika biwi kama chanzo cha Kaboni. Mfano wa Majani haya ni mabua ya mahindi, mabua ya mtama, mabua ya mpunga, majani makavu yaliyopukutika kutoka katika miti, magugu yaliyokauka, nyasi kavu, vijiti, makaratasi, maranda ya mbao.

Malighafi za ziada: Malighafi za ziada zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa mboji hujumuisha samadi, mboji iliyo tayari na udongo wa juu wa ardhi ya shamba linalolimwa. Malighafi hizi zote hutumika kama chanzo cha vijidudu vya kuozesha lundo la mboji. Vilevile majivu pia huweza kutumika kurekebisha kiwango cha tindikali katika lundo.

Matumizi ya mboji shambani

Mbolea ya mboji kama matandazo: Mboji ambayo haijaiva vizuri hutumika kama matandazo kwa kuwekwa na kutandazwa juu ya udongo katika shamba kabla au hata baada ya kupanda. Mbolea ya mboji iliyowekwa kama matandazo huendelea kuoza taratibu huku ikirutubisha udongo na mazao shambani.

Ukiweka mboji kama matandazo katika kitalu cha mboga husaidia miche kukua vizuri kwa kuwa sio tu kwamba itarutubisha miche, bali itaongeza pia uwepo wa hewa ya hewa ukaa inayozalishwa wakati wa kuoza kwa malighafi ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa chakula cha mmea.

Matumizi ya mbolea ya mboji kama matandazo, huharakisha matumizi ya mboji badala ya kusubiri kwa muda mrefu hadi iweze kuiva kabisa.

Mbolea ya mboji kama kiboresha udongo: Mboji inapotumika kama kiboresha udongo huchanganywa na udongo katika shamba ili kuboresha tabia za udongo muhimu kwa ustawi wa mazao.

Mbolea ya mboji iliyoiva vizuri isambazwe shamba zima kwa kiwango kitakachotegemeana na kiasi kilichopo kisha ilimiwe pamoja na udongo. Mboji ikitumika kama kiboresha udongo ni muhimu isambazwe katika shamba zima, kwa sababu lengo ni kuboresha tabia ya udongo.

Mbolea ya mboji inapotumika kama kiboresha udongo huweza pia kufanya kazi kama mbolea kwa kutoa virutubisho vinavyohitajika kwa ustawi wa mazao. Lakini inashauriwa usiache kuweka mbolea nyingine kama samadi au mbolea za viwandani ili kutosheleza mahitaji ya virutubisho.

Angalizo: Matumizi ya mbolea ya mboji ambayo haijaiva vizuri kama kiboresha udongo huweza kusababisha mimea kubadilika rangi kuwa ya njano na hivyo kuathiri ukuaji. Hii ni kwa sababu mbolea hii ya mboji bado inaendelea kuoza na hivyo kuwa kwake karibu na mizizi ya mmea kunasababisha ushindani wa kirutubisho cha Naitrojeni kati ya vimelea vinavyoozesha malighafi na mmea wenyewe.

Mboji kama mbolea; Mboji huweza kutumika kama mbolea kwa sababu ina virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mmea katika viwango tofauti hasa virutubisho vya msingi vya Naitrojen, Fosforasi na Potashi (N.P.K).

Mboji kama mbolea hutumika hata kabla ya kuiva vizuri kwa kuwekwa juu ya udongo kuzunguka shina la mmea au ikiwa imeiva kwa kuichanganya na udongo katika shamba zima au katika mashimo ya kupandia.

Mara nyingi ni vigumu kutengeneza mboji yenye wingi wa kutosha kusambazwa shamba zima hasa lenye ukubwa wa ekari moja au zaidi, hivyo ni busara kuweka mboji kama mbolea katika mashimo ya kupandia.

Faida za mbolea ya mboji

1.Utengenezaji wa mbolea ya mboji hauna gharama na ni rahisi, hivyo wakulima wa ngazi zote wanaweza kuumudu.

2.Mbolea ya mboji huboresha muundo wa udongo unaochangia kuwapo kwa mzunguko mzuri wa hewa na maji katika udongo.

3.Mbolea ya mboji huongeza virutubisho vinavyohitajika na mmea katika udongo na hivyo kuongeza mazao.

4.Mboji huongeza uwezo wa udongo kutunza maji na hivyo kupunguza kasi ya ukaukaji wa udongo hasa katika maeneo yenye hali ya joto na yasiyopata mvua za kutosha.

5.Mbolea ya mboji huweza kutumika kama mbadala wa mbolea ya samadi wakati wa kuandaa kitalu cha mboga.

6.Mbolea ya mboji huboresha afya ya mmea na kufanya uwe na uwezo wa kustahimili magonjwa.

Makala haya ni kwa hisani ya Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. www.mogriculture.com. 0655-570-084

Saturday, May 19, 2018

Magonjwa ya kuku ni mengi wakati wa mvua kuliko kiangazi

 

By CLEMENT FUMBUKA

Wakati nchi zilizoko ukanda wa Afrika Mashariki zikipokea mvua nyingi, kuna maeneo yameanza kuingia katika hali ya majira ya kiangazi.

Ilivyo ni kuwa hali ya hewa ina uhusiano wa moja kwa moja na magonjwa ya kuku, hivyo wafugaji wawe na tahadhari katika kukinga kuku wao wasidhulike na magonjwa.

Magonjwa mengi huambukizwa kwa njia ya hewa, maji na chakula. Ikumbukwe hewa, maji na chakula ndiyo mahitaji muhimu kwa kuku.

Wafugaji hupata hasara na taharuki ya kupoteza mifugo yao na pesa walizotumia kuwekeza miradi yao hiyo.

Ukijua sababu au chanzo cha maambukizi kwa kuku wako na njia ambayo ugonjwa unaingia kushambulia mifugo yako, huna budi kusema umepiga hatua.

Ili ugonjwa utokee lazima mazingira yaruhusu maambukizi kutokea. Bila hivyo ugonjwa hauwezi kuingia eneo hilo hata kama upo maeneo mengine.

Aina ya magonjwa

Magonjwa yanayosababishwa na vimelea aina ya bakteria: Magonjwa haya yana dawa na yanatibika. Kwa mfano, ugonjwa wa kipindupindu cha kuku na salmonella au mharo mweupe ni magonjwa ambayo hushamiri sana wakati wa mvua.

Kuku hudhoofika, kuharisha, kupumua kwa shida, kupoteza hamu ya kula na hatimaye kufa kama hawapati huduma ya haraka.

Wafugaji wengi husubiri kuona dalili za ugonjwa ndipo wanachukua hatua kudhibiti. Inatakiwa kujua mazingira yenye kuleta magonjwa na kudhibiti kwani kusubiri dalili ni kusubiri janga kubwa.

Unaposhughulikia ugonjwa wa bakteria ama kwa njia ya usafi au kwa dawa, ni vizuri kutumia dawa yenye kutibu walau magonjwa zaidi ya moja ili kuondoa hata ugonjwa ambao dalili zake zimemezwa na ugonjwa unaoonekana.

Magonjwa ya virusi

Ugonjwa wa kwanza ni Gumboro; ugonjwa huu husababishwa na virusi ambao hushambulia kuanzia kuku wenye umri wa wiki tatu hadi 18.

Ugonjwa huu hauna tiba ila kuku hukingwa kwa njia ya chanjo ambayo hupewa kuku wakiwa chini ya umri wa kuugua. Kinga yake ikitolewa sawa sawa inatosha kukinga maisha yote ya kuku.

Ugonjwa wa pili wa virusi ni Ndui ya kuku (fowl pox). Ugonjwa huu hauna tiba na kuku hukingwa kwa njia ya chanjo ambayo hutolewa kuku wakiwa na umri wa wiki sita hadi tisa au chini ya umri huo endapo kuna viashiria vya mbu au wadudu wengine wenye tabia za kunyonya damu kwa kuku.

Mbu huchangia ugonjwa kusambaa, hivyo kuku wanaweza kupata ugonjwa mapema wakiwa wadogo. Hakikisha hakuna maji yaliyotuama jirani na makazi ya kuku ili mbu wasizaliane. Pia, ukiona mazingira haya toa chanjo mapema kabla ya wiki ya sita ili kukinga maambukizi kwa tahadhari.

Dalili za ndui zinaonekana kwa kutoa vipele vyeusi kichwani sehemu zenye uwazi bila manyoya, utando mweupe kwenye ulimi lakini sio rahisi kuona dalili hizi kwa vifaranga wenye umri chini ya wiki nne kutokana na hali yao ya uchanga.

Kuku hupata homa kali kutokana na ugonjwa, huku vifaranga wakifa na wengine kuwa vipofu pindi vipele vinapotokea machoni.

Chanjo moja ikitolewa sawa sawa inatosha kuwakinga kuku maisha yao yote.

Ugonjwa wa tatu wa virusi ni Kideri (New castle disease) Ugonjwa huu hauna tiba na kuku hukingwa kwa chanjo ambayo hutolewa mapema siku saba baada ya vifaranga kuanguliwa. Kinga dhidi ya ugonjwa huu hushuka mara kwa mara.

Kuku wanahitaji kupewa chanjo kila baada ya miezi miwili au mitatu hadi maisha yao yatakapokoma. Ugonjwa huu huambukizwa hasa kwa njia ya hewa inayosambaa zaidi wakati wa kiangazi na majira ya upepo mkali.

Hiki ndicho kipindi ambacho watu wengi huita pepo za msimu mbaya kwa kuku. Ugonjwa huu ni hatari kwani huharibu na kushusha kinga ya mwili kwa magonjwa mengi ya bakteria na protozoa ambayo huongeza kazi ya kuua kuku.

Ugonjwa wa Kideri hautokani na upepo mbaya, bali ni vimelea wenye kushamiri wakati huo wa kiangazi na upepo ndiyo njia yao kusambaa.

Jipange kutoa chanjo mara kwa mara hasa kipindi cha kuhama kutoka masika kuingia kiangazi. Zuia kuku wako kuzagaa ovyo kwenda kwa majirani na epuka kununua kuku kutoka sehemu nyingine kwani utaingiza ugonjwa na kuku wako wataisha.

Ugonjwa mwingine ni kuhara damu unaosababishwa na vimelea aina ya protozoa na sio bakteria. Kuku huharisha damu, kupoteza hamu ya kula, kudhoofika na kufa ghafla kwa kujirusharusha kama amechinjwa.

Dawa zenye salfa hutibu haraka kuku wakiwa kwenye hali hii. Epuka unyevunyevu bandani au maranda kuganda.

Mwisho ni minyoo. Minyoo sio ugonjwa bali husababisha upungufu kutokana na kunyang’anyana chakula na kuku.

Minyoo huzaliana sana wakati wa mvua. Kuku hupata minyoo wakati huo kutokana na tabia yao ya kula vitu kutoka kwenye udongo.

Minyoo inatibika kwa dawa ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili au mitatu.

Dalili za minyoo kwa kuku ni pamoja na kuona minyoo kwenye kinyesi cha kuku, kuku kukohoa mara kwa mara, kupungua uzito au kupunguza uzalishaji kwa kuku wanaotaga.

Njia bora ya kudhibiti magonjwa nyakati zote ni usafi wa mazingira, vyombo vya maji na chakula.

Pia, kutoa chanjo kwa kufuata kalenda ya ugonjwa husika, hewa safi na nafasi ya kutosha bandani.

Hakikisha unawapa kuku chakula cha kutosha chenye ubora wa kuweza kuwapa kinga ya asili dhidi ya magonjwa na kuepuka kununua ovyo kuku na kuwaigiza bandani kwako.

Saturday, May 19, 2018

Lima vitunguu kisasa-3

 

Tunaendelea na hatua muhimu za kilimo cha vitunguu kwa njia za kisasa. Endelea

Matumizi ya mbolea ya CAN yanataka uangalifu sana. Mbolea ikizidi hufanya mimea kuwa teketeke, shingo ya vitunguu kuwa nene, kuchelewesha kukoma na kupunguza mazao na ubora wa vitunguu. Pia, kuoza kwa vitunguu ghalani kunaongezeka.

Kuzuia magugu

Miche ya vitungguu, huota taratibu, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen (Goal 2E).

Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikiza miche shambani.

Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyo wazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.

Magonjwa na wadudu waharibifu wa vitunguu

Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.

Magonjwa ya vitunguu

(a) Baka zambarau (Puple Blotch)

Ungonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi). Chanzo kikubwa cha ugonjwa ni mbegu zenye ugonjwa. Pia ugonjwa unajitokeza wakati kuna ukungu na unyevunyegu mwingi hewani hasa wakati wa masika. Kiasi cha asilimia 60-80 ya mazao yanaweza kupotea kama ugonjwa hautodhibitiwa.

Dalili za ugonjwa ni:

•Kujitokeza madoa meupe yaliyodidimia kwenye majani na kwenye mashina ya mbegu

•Rangi ya zambarau kuwepo katikati ya doa jeupe.

•Majani kuanguka

•Mashina ya mbegu kuanguka kabla ya mbegu kutengenezwa

Njia za kudhibiti:

•Kupanda mbegu safi

•Kupanda vitunguu kwa kutumia mzunguko wa mazao

•Kuteketeza masalia ya vitunguu baada ya kuvuna

•Kupulizia dawa zilizopendekezwa kama Dithane M45 na Ridomil MZ. Dawa hizi zinachanganywa na povu la sabuni ili zijishike kwenye majani.

(b) Ubwiri vinyoya (Downy Mildew)

Ugonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi) na kuenezwa na mbegu, hewa na masalia ya vitunguu. Unajitokeza wakati kuna unyevunyevu mwingi hewani hasa wakati wa masika na dalili zake ni kama zifuatazo:

•Madoa yenye umbo la yai, rangi ya njano iliyofifia hujitokeza kwenye majani makukuu na kusambaa mpaka kwenye majani machanga.

•Baada ya siku chache madoa ya njano yanafunikwa na ukungu wa rangi ya kijivu.

•Majani yanasinyaa na kufa kuanzia kwenye ncha.

•Shina la mbegu huzungukwa na vidonda na kusababisha kichwa cha mbegu kuanguka.

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. 0655-570-084. www.mogriculture.com

Saturday, May 12, 2018

Kwa Urasa kilimo sio ardhi kubwa, ni uthubutu

 

By Asna Kaniki, Mwananchi Akaniki@mwananchi.co.tz

Ni kijana mhitimu wa chuo kikuu, aliyeamua kufanya kilimo cha mbogamboga kwa kutumia chupa za plastiki

Zama za kilimo kutawaliwa na watu wasio na elimu zinaelekea ukingoni.

Hivi sasa kilimo kinachangamkiwa na watu wengi wakiwamo vijana wasomi, ambao miaka ya nyuma ilikuwa jambo gumu kwao kujihusisha na shughuli za kilimo.

Ukweli ni kuwa ugumu wa maisha hasa ukosefu wa ajira rasmi, unawasukuma vijana wasomi kutafuta njia za kujiajiri.

Wengi wamebaini fursa kwenye kilimo kama ilivyo kwa Aretas Urasa aliyeamua kuweka kabatini cheti cha elimu ya juu na kuamua kujiingiza kwenye kilimo.

Cha kutia moyo ni kuwa Urasa hakutaka kuanza kilimo kwa kutafuta ardhi kubwa vijijini kama wanavyofanya baadhi ya watu.

Uthubutu wa kutaka kulima kiubunifu, ukamsukuma kutembea mitaani na kuokota chupa za plastiki na kufanya kile anachokiita kwa jina la ‘kilimo cha mjini’

Hiki ni kilimo kisichohitaji ardhi kubwa kwa ajili ya kupanda mazao hasa yale ya jamii ya mbogamboga.

“Wakati mwingine nikiwa naokota chupa watu walinicheka na kunidharau kwa kigezo kuwa msomi tena kijana hawezi kufanya vitu kama hivyo,’’ anasema.

Hata hivyo, maneno ya watu hayakumkatisha tamaa Urasa mwenye miaka 23 na mkazi wa Morogoro. Sasa anasema kilimo ndiyo sehemu ya maisha yake na hafikirii tena kukiacha.

Kwa nini kilimo cha kwenye chupa?

“Wakati naanzisha kilimo hiki kwanza nililenga watu ambao wanaishi maeneo ya mjini hususan wanaoishi kwenye nyumba za kupanga ambao wanatamani kulima mbogamboga lakini wanashindwa kutokana na ufinyu wa ardhi,” anasema.

Anasema watu wengi wanaweza kufanya aina hiyo ya kilimo, kwani hakina gharama wala ugumu katika kukiendesha na kinaongeza upatikanaji na ulaji wa mboga za majani ambazo ni salama.

“Katika kilimo hiki mboga za majani zinapandwa katika mifuko au makopo ambayo ni salama kwa kuwa hazitumii dawa za kemikali kuua wadudu, bali katika kila kopo hupandwa mmea wa kitunguu ama tumbaku ambapo harufu ya mimea hiyo hufukuza wadudu waharibifu,” anasema.

Jinsi ya kutengeneza

Shamba hilo huandaliwa kwa vifaa mbalimbali ikiwemo mbao, misumari na chupa za maji. Hata hivyo, anasema zikikosekana mbao mkulima anaweza kutumia miti.

Vingine ni udongo na pumba za mpunga kwa kwa ajili ya kujaza kwenye chupa hizo za maji ambazo zimeshakatwa pamoja na mbolea ya samadi.

“Chupa au mifuko tunatoboa chini ili maji yasituame, bila kufanya hivyo mboga zitaharibika. Pia katika uoteshaji mboga, zinatakiwa zipandwe mwanzo na mwisho wa chupa ili kutoa nafasi ya kustawi vizuri,” anaeleza.

Alivyoanza kilimo

Tangu akiwa chuoni mkoani Morogoro, Urasa alikuwa akijihusisha na kilimo cha bustani japo hakuwa akifanya kwa kutumia chupa za plastiki.

“Kipindi hicho nilikuwa naishi hosteli nikawa nalima mbogamboga nauza. Kwa kuwa nilisomea kilimo, sikupata shida ya kuhudumia mbogamboga zangu,” anasema.

Urasa anasema alianza kukusanya chupa za maji kwa lengo la kufanya jaribio lake la kubuni kilimo cha mbogamboga kisichotumia ardhi kubwa

“Unajua kilimo kinafanywa kwa aina tofauti; kinachotakiwa ni mavuno pekee. Nimekaa nikafikiria kwa nini kila siku tunatumia jembe kulima mbogamboga, kwa nini nisitumie chupa kwa kuzijengea kichanja na kuotesha mbegu? anasema mkulima huyo.

“Nikaanza kuongea na wafanyakazi wanaofanya usafi hosteli wanikusanyie chupa kwa kuanza majaribio, hatimaye mboga zikakua, nikagundua kuwa kumbe watu wanaweza kuwa na shamba la mbogamboga bila kutumia nguvu, eneo wala gharama kubwa.”

Faida za kilimo hiki

Kilimo hiki hakina kikwazo cha mvua wala magonjwa yaletwayo na mvua, hivyo mkulima ana uhakika wa kupata mboga safi na salama.

“Mvua inaponyesha mara nyingi mboga zinajaa udongo hasa kwa mboga zilizotambaa ikiwemo matembele, lakini kwa kilimo hiki mvua itanyesha lakini mwishowe mboga itabaki kuwa safi na salama,” anasema. Kilimo cha mjini ni rahisi kusimamia kwa kuwa ni eneo dogo ambalo mkulima hawezi kumaliza nusu saa kulihudumia tofauti na ilivyo kwa mashamba ya kawaida ambapo muda mwingi unaweza kutumika kukagua mbogamboga.

Aidha, kilimo hicho ni rahisi kukihudumia, kwa kuwa hata inapotokea uvamizi wa wadudu, mkulima anaweza kuwadhibiti kwa urahisi.

Ni kilimo anachosema kinaweza kufanywa hata na mtu mwajiriwa asiye kuwa na muda mwingi wa kuhudumia shamba.

Kuhusu faida kifedha, Urasa anasema kwa siku anaingiza si chini ya Sh5,000 kwa kuuza mboga.

“Watu wanadharau, hizi Sh4,000 au 5,000 zinazoingia kutokana na kuuza mbogamboga, kwa mwezi sikosi Sh150,000 ambayo kwa kijana mtaani anayetegemea kuajiriwa hawezi kuipata kirahisi,” anasema mkulima huyo wa mjini.

Matarajio yake

Ndoto za Urasa siyo kuwa mkulima pekee, bali awe na mradi mkubwa wa kutengeneza mashamba ya aina hiyo na kukisambaza kilimo anachofanya katika maeneo mbalimbali hasa mijini.

Kwa ushauri wa aina hiyo ya kilimo wasiliana naye kwa kwa simu: 0753912159/ 0653584225

Saturday, May 12, 2018

Sababu 10 za kukosa mayai kwa kuku wanaotaga-2

 

By CLEMENT FUMBUKA

Makala haya ni mwendelezo wa kuangalia sababu 10 zinazosababisha kukosa mayai kutoka kwa kuku wanaotaga.

Hii ni baada ya kuangalia sababu nne kwenye makala yaliyopita na sasa tuangalie sababu sita zilizobaki.

Tukumbushane sababu nne zilizopita ambazo ni mabadiliko ya hali ya hewa kama vile baridi, giza, mvua na joto kali; umri wa kuku na mabadiliko ya mwili kutokana na hatua za ukuaji.

Sababu ya tatu ni chakula kinachotolewa kwa kuku kuwa duni au hakitoshi mahitaji ya mwili na kuzalisha. Sababu ya nne ni kukosa maji kwa muda mrefu na kusababisha mwili kuwa na mshituko mkubwa.

Makala hii ya leo itaendelea na sababu sita zilizobaki tukianza na sababu ya tano ambayo ni kubanana kwa kuku bandani. Kwa kawaida kuku wanahitaji nafasi ya kutosha kutembea kupata chakula na maji.

Kuku wakibanana bandani hushindwa kula na kunywa maji vizuri na matokeo yake hushindwa kushiba.

Kwa kawaida kuku mwenye umri wa kutaga, anatakiwa kula chakula gramu 120 hadi 140 kwa siku na eneo la kuishi linatakiwa kuwa mita moja ya mraba kukaa wastani wa kuku watano hadi sita kwa kuku wa mayai na kuku nane wa nyama.

Idadi kubwa ikiwekwa zaidi ya kiasi kinachotakiwa, kuku watachafua banda, kumwaga maji na kushindwa kukua vizuri na kushindwa kuzalisha.

Sababu ya sita ni uchafu. Banda la kuku linatakiwa kuwa safi bila harufu mbaya ya uozo au madawa yoyote. Kuku wanaokaa kwenye banda chafu hushambuliwa na magonjwa kutokana na kula uchafu ulioko kwenye sakafu au kunywa maji machafu.

Hali ya banda inatakiwa kuwa kavu na mbolea isigande au kuwa na unyevunyevu kama zizi la ng’ombe. Hali kama hiyo husababisha magonjwa mengi kwa kuku na kushindwa kutaga vizuri kama ni kuku wa mayai, kuhalisha na kudumaa kwa kuku wa nyama.

Sababu ya saba ni wadudu wanaoishi ndani au nje ya ngozi ya kuku kama vile minyoo, chawa, viroboto, kupe na utitiri. Wadudu hawa hufyonza damu kwenye ngozi ya kuku na kusababisha kuku wasitulie kwa kuwashwa. Muda mwingi kuku hutumia kuhangaika, matokeo yake uzalishaji hushuka kwa kushindwa kula vizuri, kutulia na kutaga.

Minyoo wa tumboni hutumia chakula kilekile ambacho kuku anahitaji kwa ajili ya mwili na kuzalisha mayai. Kuku wenye matatizo haya hudhoofika hata kama wanapewa chakula na dawa za kutibu.

Mfugaji anatakiwa kufuatilia na kujua tatizo kabla ya kuanza matibabu ili atumie dawa sahihi. Dawa za minyoo ni tofauti na dawa za wadudu wa nje kama vile utitiri, chawa kupe na viroboto. Minyoo huonekana kwenye kinyesi cha kuku. Kuku wenye utitiri, chawa, kupe na viroboto, wadudu hao huonekana kwenye ngozi.

Sababu ya nane ni vimelea. Mabanda mengi yanayofungwa kwa muda mrefu hutengeneza ngome ya vimelea vya magonjwa kuzaliana. Mara nyingi mfugaji utakuta anatibu ugonjwa huu, lakini punde ugonjwa mwingine tena unatokea.

Hii ni kutokana na sehemu hiyo kuwa na hifadhi kubwa ya vimelea. Mfugaji anatakiwa kufanya usafi wa kina kukusanya uchafu wote na kuchoma moto mabaki yote ya kuku waliopita.

Aoshe kuta na sakafu za banda baada ya kutoa mbolea na kupeleka shambani. Usihifadhi mbolea ya kuku jirani na banda la kuku unakofugia, kwani vimelea kutoka kwenye mbolea wataingia tena kwenye banda la kuku. Kinga bora dhidi ya magonjwa ni usafi wala sio chanjo au tiba. Chanjo na tiba zipo baada ya usafi kuzidiwa nguvu.

Sababu ya tisa ni wezi. Wezi sio ugonjwa wa hali ya hewa lakini ni sehemu ya kupunguza uzalishaji. Kama unamfanya kazi anayeiba mayai au kuku, madhara yake ni sawa na vifo vya kuku.

Mfugaji unashauriwa kuwa na mbinu thabiti kudhibiti wizi kwenye mabanda yako. Tengeneza mfumo wa kutunza kumbukumbu kila siku ujue idadi ya kuku au mayai kwa maandishi. Kuwa rafiki wa mhudumu wa banda kupanga na kutatua changamoto zote kwa pamoja.

Sababu ya tisa ni wanyama waharibifu. Kuna wanyama wanaopenda kula kuku au chakula cha kuku. Wanyama kama vile kenge, vichehe, nyoka, panya, paka na wengineo ni hatari kwa kuku na mayai. Tengeneza banda lenye uwezo wa kuwadhibiti.

Wanyama hawa pia husambaza magonjwa kwa kuku. Ni rahisi kuona unaokota mayai machache, lakini kila ukichunguza huoni sababu yoyote ya kupata mayai kidogo kumbe kuna panya, kenge, nyoka au paka wanaokula mayai kabla hujayaokota bandani.

Fanya uchunguzi kila mahali na tumia mitego safi kuwaua ili upunguze gharama za kupoteza kukua au mayai.

Sababu ya 10 ni kutojali na haraka ya kutaka kuona mambo makubwa kwa wakati mfupi kuliko uhalisia. Wafugaji wengi hukimbilia kutaka faida bila kuitafuta; matokeo yake huona wanachelewa na hata kutelekeza mradi.

Katika biashara zote ikiwamo ufugaji, faida ni matokeo ya kazi na hatua fulani. Wafugaji wengi huanza vizuri kwa huduma nzuri kwa kuku wao, ikifika sehemu wakaona kuku wanachelewa kutaga huamua kuwauza ghafla.

Maamuzi ya haraka bila kupata ushauri wa kitaalamu kwenye biashara yoyote ni kununua hasara kwa gharama yako mwenyewe.

Kabla hujaanza ufugaji, chukua hatua kujifunza kila kitu ili upate upeo wa kutosha na kuzingatia mambo yote muhimu.

Saturday, May 12, 2018

Lima vitunguu kisasa-2

 

Tunaendelea na hatua muhimu za kilimo cha vitunguu kwa njia za kisasa. Endelea

Jinsi ya kuandaa kitalu na kuzalisha miche

Sehemu ya kitalu iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji. Tengeneza tuta la kubwa wa 1m x 2m. Urefu na idadi ya matuta hutegemea kiasi cha mbegu. Kiasi cha mbegu kwa hekta moja ni kilo sita au mbili kwa ekari. Weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha debe moja au mchanganyiko wa mbolea ya TSP na CAN (200gm) kwa uwiano wa 1:1 kwenye tuta kisha changanya vizuri na udongo. Sia mbegu kwenye mistari kwa nafasi ya 1 sm x 20 sm. Tawanya mbegu vizuri wakati wa kusia ili miche isisongamane.

Funika mbegu na weka matandazo ya nyasi kavu juu ya tuta na mwagilia maji. Udongo unatakiwa kuwa na unyevu kiasi mpaka mbegu ziote. Nyasi ziondolewe mara tu mbegu zikiota (siku 7-10 kutegemea hali ya hewa). Miche itunzwe vizuri na kitalu kiwe katika hali ya usafi. Miche imwagiliwe maji mpaka ifikie umri wa kupandikiza shambani (wiki 5-6).

Miche ikiwa kitaluni inaweza kukabiliwa na matatizo kadhaa kama vile kuoza kwa mbegu, kunyauka kwa miche kabla na baada ya kuota. Hali hii inasababishwa na ugonjwa wa ukungu “Kinyausi”. Dawa za ukungu kama Dithane M45 au Ridomil MZnk zinatumike kuzuia (changanya dawa na povu la sabuni ili dawa ijishike kwenye majani). Pia uangalifu uwepo wakati wa kumwagilia maji. Mwagilia maji wakati wa asubuhi au jioni.

Epuka kumwagilia maji wakati wa jua kali, kwani unyevunyevu hewani unaongeza na kusababisha vimelea vya magonjwa.

Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu ambao wanashambulia majani, Sota ambao hukata miche. Dawa za viwandani kama Thiodan, Selecron au Dusrban zinazuia na kudhibiti hawa wadudu.

Baada ya wiki ya tano au ya sita kutegemeana na hali ya hewa miche itakuwa tayari kupandikiza shambani. Miche iimarishwe kwa kusitisha maji, wiki moja kabla ya kupandikiza.

Kutayarisha shamba

Shamba litayarishwe sehemu isiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa vitunguu kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m. yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

Kupandikiza miche shambani na matumizi ya mbolea

Weka samadi debe mbili au mbolea ya TSP au DAP kwenye tuta au jaruba na kuchanganya na udongo. Mbolea kiasi cha mifuko miwili TSP au DAP kwa hekta au robo tatu ya mfuko kwa eka moja inashauriwa.

Chagua miche yenye afya, majani na mizizi ipunguzwe ili kurahisisha upandaji. Panda miche kwenye mistari kwa nafasi ya sm 20 kutoka mstari hadi mstari, na miche hadi mche kwa nafasi ya sm 8 au sm 10.

Tumia kijiti au kitu chochote chenye ncha kuchimba vijishimo vya kupandia miche. Mwagilia maji ya kutosha kila siku hasa sehemu zenye jua kali.

Mbolea ya kukuzia CAN kiasi cha mifuko miwili kwa hekta au robo tatu mfuko kwa eka moja iwekwe wiki mbili baada ya kupandikiza miche.

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. 0655-570-084. www.mogriculture.com

Saturday, May 5, 2018

Makosa wanayofanya wafugaji wa samaki

 

By Na Ayub Nnko

Ufugaji wa samaki ni kazi ya kupanda, kukuza na kutunza samaki katika bwawa au uzio uliotengenezwa kwa vyuma, miti pamoja na nyavu. Unaweza pia kufuga katika eneo lolote ambalo udhibiti wake uko chini ya mamlaka ya mfugaji mwenyewe. Mabwawa yanaweza yakawa ya kuchimbwa na watu au yale ya asili. Ufugaji wa samaki kwenye mabwawa si sawa na ukuaji wa samaki katika mito, maziwa na bahari.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya samaki wanaofugwa na wasiofugwa ipo katika huduma. Samaki wanaofugwa huwekwa kwa idadi maalumu ndani ya bwawa na kupatiwa chakula na kuhudumiwa kwa utaratibu maalumu.

Makosa ya wafugaji wa samaki

Kuna changamoto ya mabwawa kukumbwa na mafuriko. Hii ni changamoto kubwa kwa mabwawa ambayo yamechimbwa au kujengwa pasipo kufuata taratibu za ujenzi au uchimbaji wa mabwawa.

Kwa mfano, moja ya maeneo yaliyokumbwa na hali hii ni Ruvu mkoani Pwani, Morogoro, Mwanza na Mtwara. Hizi ni baadhi ya sehemu ambazo baadhi ya wafugaji wa samaki waliwahi kuathiriwa na changamoto hii.

Sababu kuu inayochangia mabwawa kukumbwa na mafurukio ni ujenzi usiozingatia tahadhari za kimazingira, ikiwemo watu kujenga mabwawa kandokando ya ziwa, mifereji mikubwa na mabondeni. Hili ni kosa la kwanza ambalo makala haya imelibaini.

Mara nyingi watu huchunguza eneo wakati ambao sio wa mvua, hivyo kufikiri ni maeneo salama kwao na kuanza kuchimba mabwawa. Wafugaji wanashauriwa kuchukua tahadhari kabla ya kuanza ujenzi wa bwawa.

Lazima eneo lifanyiwe uchunguzi wa kutosha kwa wakati wote iwe kiangazi au masika ili kubaini eneo lako kama

ni salama au sio salama kwa ufugaji wa samaki ili kuepuka hasara zinazoweza kutokea.

Wakulima waepuke kuchimba mabwawa kando kando ya vyanzo vikuu vya maji kama vile kujenga bwawa kandokando ya ziwa, mifereji au kwenye mabonde, kwani maeneo haya sio salama kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

Kutodhibiti maadui wa samaki kama ndege, kenge, fisi maji na nyoka

Changamoto hii ya uwepo wa ndege, kenge na fisi maji husababisha mfugaji kupata matokeo mabaya asiyoyatarajia. Hii ni kwa sababu samaki hupungua kutokana na kuliwa na maadui hao.

Kwa mfano, mfugaji anaweza akawa amepanda samaki 1,000 lakini wakati wa mavuno, hujikuta samaki wanaopatikana ni 400 kati ya 1,000, huku samaki wengine wakiwa wameshambuliwa na maadui hao.

Sababu kubwa za tatizo hili ni kujenga mabwawa sehemu zenye vichaka au kutofyeka majani kuzunguka bwawa la samaki, hivyo kushawishi maadui hao kama vile kenge, nyoka na fisi maji.

Baadhi ya mabwawa kutowekwa uzio na wavu wa juu kwa ajili ya kudhibiti maadui hao kupita na kushambulia samaki

kirahisi, ni sehemu ya mazingira yanayosababisha hasara kwa mfugaji.

Hakikisha eneo lako linakuwa safi. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa halina kichaka na kuweka uzio kuzunguka bwawa.

Hakikisha unaweka wavu juu ya bwawa kwa ajili ya kudhibiti ndege kutoingia ndani ya bwawa kirahisi.

Ugumu wa kukausha maji bwawani

Hii ni moja ya changamoto kubwa iliyobainika kwamba wafugaji wengi wamechimba mabwawa pasipo kuweka mfumo rafiki wa kutolea maji. Hali hii husababisha ubadilishwaji wa maji kuwa mgumu,jambo linalosababisha samaki kukaa na

maji machafu kwenye mabwawa kwa muda mrefu.

Madhara makubwa ya maji machafu kukaa kwa muda mrefu kwenye mabwawa, husababisha samaki kukumbwa na magonjwa kama vile fangasi au kufanya ukuaji hafifu kwa samaki.

Tatizo hili la ugumu wa utoaji wa maji husababishwa na ujenzi wa mabwawa bila kusimamiwa na wataalamu husika wa miradii ya ufugaji samaki na mabwawa. Pili husababishwa na bwawa kujengwa kwenye eneo la tambarare kiasi kuwa, hakuna uwezekano wa kutumia bomba au kukata kuta za bwawa kuondoa maji.

Utatuzi wa tatizo hili ni kuhakikisha kuwa unafuata kanuni zote muhimu za uchimbaji wa mabwawa, ikiwamo mfumo wa kutolea maji. Hakikisha unachimba bwawa kwa kuzingatia sehemu yenye mwinuko wa wastani ili kupata mlalo halisi utakaotiririsha maji yote kutoka bwawani na kufanya ufugaji mzuri unaozingatia kanuni bora za ufugaji samaki wenye tija.

Ugonjwa wa samaki kupasuka kichwa

Hii ni moja ya changamoto inayowakumba baadhi ya wafugaji wa samaki hususani wa kambale. Tatizo hili limeripotiwa na baadhi ya wafugaji hususani wenye mabwawa ya kujengea kwa tofali. Liligundulika baada ya wafugaji kuona samaki wao wanakufa hususani kambale.

Moja ya dalili za ugonjwa huu ni samaki kuvilia damu sehemu za juu ya kichwa, kisha hupasuka

na kutengeneza kidonda ambacho huanza kuwa kidogo kisha hukua na baadaye husababisha kifo cha samaki

Tatizo hili husababishwa zaidi na ukosefu au upungufu wa baadhi ya virutubisho. Moja ya virutubisho muhimu kwa kambale kuvipata ni vitamin C.

Uwepo wa vitamini hii humfanya kuimarisha mwili wake na kufanya utengemavu mzuri kwenye mfumo mzima wa mifupa yake. Hii hutokana na ulishaji usiozingatia kanuni bora za utengezaji wa chakula cha samaki kulingana na samaki husika.

Hali hii husababisha kutokea kwa tatizo hilo la samaki kupasuka kwenye sehemu ya mwili wake.

Unapoona tatizo hili limetokea, acha kutumia chakula ambacho kimesababisha kutokea kwa tatizo hilo. Tengeneza chakula au lisha chakula chenye virutubisho vya vitamin C na amino acid kwa ajili ya kurejesha hali ya samaki kwenye afya ya awali.

Wafugaji wengi kutokuwa na usimamizi mzuri kwenye miradi yao Ili mradi wowote ukue vizuri, tunahitaji uwepo wa usimamizi mzuri wa mradi. Moja ya changamoto kubwa ambayo imejitokeza ni hii ya usimamizi hafifu kwenye miradi.

Tunaposema usimamizi hafifu, tunamaanisha kwamba baadhi ya wafugaji wamepata matokeo ambayo sio ya kuridhisha, hasa kwenye mavuno kwa sababu hawana taratibu za kuweka kumbukumbu. Ni muhimu kuweka kumbukumbu kuanzia siku ya kuchimba bwawa, kuweka samaki, ulishaji wa samaki na na malipo ya vibarua. Hali hii itakusaidia kufahamu kuwa umetumia kiasi gani cha fedha na baada ya mavuno kufahamu umeingiza kiasi gani.

Ni vyema wafugaji kufuata na kuzingatia kanuni zote za ufugaji, ikiwamo ulishaji kwa wakati, ubadilishaji wa maji na usafi nje ya bwawa kwa ajili ya usalama. Haya yatasababisha kupata matokeo chanya zaidi na kufurahia biashara yaufugaji wa samaki.

Makala haya yaliyoboreshwa awali yalichapishwa katika jarida la Mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org. Wasiliana na mtaalamu wa ufugaji samaki

0718986328

Saturday, May 5, 2018

Lima vitunguu kisasa-1

 

Vitunguu ni zao muhimu hapa nchini. Mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya, Tanga, Singida, Kilimanjaro, Morogoro na Mara ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu na ni zao la chakula na biashara kwa mkulima mdogo.

Uzalishaji wa vitunguu bado ni mdogo na upotevu wa mazao baada ya kuvuna ni mkubwa ikikadiriwa kuwa asilimia 50 hadi 80, kutokana na hifadhi duni. Hivyo wakulima wanahitaji utaalamu wa kilimo bora na hifadhi ya vitunguu ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Uzalishaji wa vitunguu

Zao la vitunguu linazalishwa kutokana na mbegu na miche inayokuzwa kwenye kitalu kabla ya kupandikizawa shambani. Miche inakua na kuzaa vitunguu. Vitunguu vikikomaa, vinavunwa na kuhifadhiwa vikiwa katika hali ya kulala bwete.

Katika hali hii vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu ama kwa ajili ya kuzalisha mbegu msimu unaofuata au kwa kuuza.

Wingi na ubora wa zao la vitunguu hutegemea: hali ya hewa, aina ya vitunguu, upatikanaji wa mbegu bora, kilimo bora, uangalifu wakati wa kuvuna, usafirishaji na hifadhi bora.

Hali ya hewa na maji

Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu. Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji.

Maji mengi hasa wakati wa masika yanasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, hivyo vitunguu haviwezi kukomaa vizuri na kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu wakati wa kukomaa na kuvuna vitunguu.

Aina za vitunguu

Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Aina nyingine za vitunguu ni pamoja na Tropical Red F1 hybrid, Singida local na Pretoria Grano. Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi), msimu wa kupanda, uwezo wa kuzaa mazao mengi na uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Mbegu bora

Ubora wa mbegu ni muhimu , kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu zinapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa.

Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo: uotaji zaidi ya asilimia 80, safi zisizo na mchanganyiko na kufungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unjevu.

Mkulima azingatie yafuatayo anaponunua mbegu: chanzo cha mbegu, tarehe ya uzalishaji, tarehe ya kuisha muda wake na kifungashio cha mbegu.

Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja. Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: ALPHA Seed Co, Popvriend, Rotian Seed, Kibo Seed, East African Seed Company na wengineo. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.

Makala haya ni kwa hisani ya Mogriculture ambao ni washauri wa kilimo na ufugaji; 0655-570-084. infos@mogriculture.com

Saturday, May 5, 2018

Sababu 10 za kukosa mayai kwa kuku wanaotaga-1

 

Wapenzi wa makala haya ya ufugaji wa kuku nawakaribisha tena katika ukurasa wetu.

Bado tunayo fursa ya kuyajua mengi ya muhimu kwenye ufugaji. Makala haya ya leo yanakuletea mambo 10 ambayo yanaweza kusababisha usipate au upate mayai kidogo kutoka kwenye kuku wako wanaotaga.

Wafugaji wengi hupenda kuona mafanikio katika kazi zao, japo mambo fulani hujitokeza kuwakwamisha na kuwaacha bila kujua vyanzo vyake na nini cha kufanya.

Vikwazo kuku wanaotaga

Tuangalie vikwazo na njia ya kujinasua kutoka vikwazo hivyo kwa kuku wa mayai wa aina zote.

Kwanza; kubadilika kwa hali ya hewa ya siku kama vile hali ya joto ghafla kugeuka kuwa baridi, mvua kubwa na mawingu kutanda kuwa giza, baridi kali na kupungua kwa urefu wa saa za mwanga chini ya saa 14.

Hali hizo hubadilisha mwili wa kuku na mpangilio wa kazi za mwili wa kuku, huku athari kubwa ikiwa kwenye mfumo wa uzalishaji mayai.

Katika hali hizo mfugaji anashauriwa kuku wake awaongeze chakula cha kutoa baridi ili miili yao ipate nguvu ya kutosha kupasha mwili joto na kuendelea na uzalishaji.

Pia, mfugaji anaweza kushusha mapazia kwenye madirisha ili kupunguza baridi kuingia bandani. Hali ya giza bandani husababisha kuku wajisikie kama wantaka kulala wakati wa mchana kutokana na wingu zito kutanda. Washa taa za usiku kuku waendelee na shughuli zao za kula na kunywa. Kuku wanaweza kupewa vitamini mfululizo katika kipindi chote hicho kupunguza mshituko na kurejesha uzalishaji wa mayai.

Muda wa kuku kukaa kwenye mwanga usipungue saa 14 hadi 16 kwa siku. Kuku wanaofugwa ndani ni rahisi kuwadhibiti wakaendelea kutaga vizuri.

Pili; umri wa kuku wanaotaga. Kuku hutaga kuanzia wakiwa na umri wa wiki 18 hadi 22 na kuendelea kutaga hadi miaka miwili au mitatu, huku ikitegemea na mbegu ya kuku.

Kuku wenye uwezo mkubwa wa kutaga mayai mengi wakifika umri wa mwaka mmoja au zaidi (wiki 50 hadi 60), hushusha utagaji karibu nusu ya mayai waliyotaga wakiwa vijana kati ya wiki 27 na 40.

Katika umri huo wa wiki 50 hadi 60, kuku huanza kunyonyoka manyoya na kuota mengine. Hatua hiyo ni ishara ya kupumzisha mwili na kujiandaa tena kuendelea na utagaji baada ya wiki mbili au mwezi mmoja.

Hata hivyo, baada ya kunyonyoka na kuota manyoya mengine, hushindwa kurudia utagaji wa juu kama ilivyokuwa kabla kutokana na mwili kupungua nguvu.

Mfugaji unashauriwa kutoa chakula bora na cha kutosha kuwarudisha haraka kwenye utagaji baada ya kunyonyoka manyoya. Huu sio ugonjwa wala upungufu wa lishe kama wafugaji wengi wanavyodhani. Ni ishara ya mwili kuandaa nguvu nyingine.

Kuku wanaweza kuwahi kunyonyoka manyoya mapema kabla ya umri huo, endapo hawakuwa katika huduma bora ya chakula au kuwahi kutaga mayai kabla ya umri sahihi.

Kwa upande mwingine kuku wanaweza kunyonyoka manyoya kutokana na upungufu wa lishe lakini kunyonyoka huku sio sawa na vile wakiwa kwenye hali yao ya kawaida wiki ya 50 hadi 60. Kunyonyoka kwa upungufu wa lishe, hutokea bila kujali umri na pia huambatana na matatizo mbalimbali ikiwamo kudhoofika kiafya na ni rahisi mfugaji kujua.

Tatu; kuzidi au kupungua kwa virutubisho vya mwili. Kupungua kwa madini ya chokaa au kalshiamu kwa kuku anayetaga hushusha utagaji. Madini haya wakati wa utagaji, ni muhimu sana kwa afya ya kuku na uzalishaji wa mayai.

Bila madini haya mwilini, kuku hawezi kutaga kabisa. Upungufu wa madini haya kwa kuku anayetaga husababisha mifupa kukosa nguvu. Kuku wengi wanaotaga hukumbwa na tatizo la kushindwa kusimama na kutembea, kupooza miguu, mayai kuvunjikia tumboni na mayai kutagwa bila ganda gumu. Madini ya chumvi (chumvi ya mezani) ni muhimu katika uzalishaji wa mayai. Huongeza hamu ya kula, kusaga chakula na kumsaidia kuku kuwa mtulivu anapopata mshtuko au taharuki.

Kiasi kidogo sana cha chumvi huhitajika; usiweke chumvi bila kipimo kwenye chakula cha kuku. Chumvi ikizidi, kuku wataharisha, kupata upungufu na kushindwa kutaga vizuri.

Nne; kukosa maji na chakula kwa muda mrefu. Kuku wanaotaga wakikosa maji ya kunywa kwa muda mrefu, hupunguza kutaga mayai hasa nyakati za joto kali.

Sehemu kubwa ya yai ni maji, kwa hiyo kuku anahitaji maji ya kutumia mwilini na mengine zaidi kutengeneza yai. Weka maji safi na salama kwa kuku muda wote wapate maji bila shida.

Nyakati za joto, maji mengi ni sehemu ya kupunguza joto la mwili wa kuku na kuongeza hamu ya kula na kutaga zaidi. Wakati wa baridi kuku wenyewe hususia maji na kula chakula kingi kupandisha joto la mwili kuzalisha mayai.

Chakula cha kuku wanaotaga kina madini mengi ambayo huleta kiu kwa kuku. Mbali na madini, kuku wanapokaa muda mrefu bila kula, mwili hupunguza uzalishaji kutokana na kupungukiwa nguvu.

Kuku wa mayai inafaa wapewe chakula mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni ili wapate nguvu ya kutosha. Ulaji wa kuku ndiyo utagaji.

Mambo yote haya ni muhimu kuyafahamu. Kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya mahitaji ya kuku wako. Ukiacha utaalamu wa ndani wa kidaktari, mambo mengine unayaweza.

Weka kumbukumbu hizi kama rejea ya kutatua shida yako kwa uhakika, badala ya kutafuta mawazo kwa kila mtu. Ni rahisi kukutana na mtu asiyejua ukashauriwa vibaya au kupotezwa zaidi.

Sababu nyingine sita za kukosa mayai kwenye kuku wanaotaga zitaendelea kwenye makala ijayo.

Saturday, April 21, 2018

kuna fedha kwenye mabwawa haya ya maji

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Nani anajali akiona dimbwi la maji barabarani au mtaani kwake?

Katika maeneo mengi nchini, madimbwi hasa wakati wa misimu ya mvua japo ni kero, lakini kwa walio wengi ni jambo la kawaida. Yamezoeleka.

Kwa upande mwingine, kuna madimbwi ya maji ambayo binadamu anayatengeneza makusudi, lengo siyo kuleta kero kwa wengine, bali ni kusaka fedha kupitia madimbwi hayo.

Hivi sasa sekta ya samaki imekua, kutoka kutegemea samaki wa baharini, maziwa na mito pamoja na mabwawa makubwa, samaki sasa wanafugwa hata katika madimbwi na mabwawa ya kutengeneza.

Biashara ya ufugaji wa samaki

Ufugaji wa samaki ni moja ya maeneo ya uwekezaji ambayo Watanzania wanaweza kuwekeza na kujipatia fedha za kujikimu kimaisha na kufanya maendeleo makubwa.

Mtaalamu na mfugaji wa samaki, Musa Said anasema mtu akiamua kujitoa na kuwekeza katika ufugaji wa samaki kamwe hatojutia uamuzi wake. Said anasema ufugaji wa samaki hauna usumbufu wala gharama nyingi, isipokuwa wakati wa maandalizi.

“Uzuri wa samaki unaweza kufuga kwenye bwawa la kisasa au la kawaida, kinachotakiwa ni huduma muhimu ikiwemo chakula,”anasema.

Anasema biashara ya samaki wa kufugwa ina faida na inaweza kurudisha gharama zilizotumika katika kuwekeza pamoja na kumletea mfugaji faida.

“Inategemea na juhudi za mtu unajua suala la ufugaji wa samaki linachukuliwa kirahisi; watu hawajui faida zilizopo, ila wachache wameiona fursa na wanakuja kwangu nawapatia ushauri wa kitaalamu,”anasema.

Dk Dkt Aloyce Masanja ambaye ni Mkurugenzi wa chuo cha kilimo na ufugaji cha Canre, anasema alichogundua ni kwamba hakuna uwekezaji ambao hauhitaji gharama kubwa kama ufugaji wa samaki. Tofauti na uwekezaji mwingine anasema samaki wanaweza kumtoa mtu kutoka hatua moja kwenda nyingine kuliko watu wanavyodhani.

“Mfano mzuri hapa chuo napokea oda miezi miwili kabla; mtu akichelewa inabidi asubiri awamu nyingine kwa hiyo inaonyesha jinsi gani biashara hii inavyopendwa,”anasema.

Taratibu za ufugaji wa samaki

Hata hivyo, ufugaji wa samaki kibiashara siyo jambo la kukurupuka. Kuna utaratibu maalumu wa kufuatwa kwa mtu makini anayehitaji kutengeneza fedha.

Dk Masanja anasema taratibu hizo ni pamoja na kuangalia eneo gani sahihi kwa ajili ya kuanza ufugaji, kwani anasema kipengele hicho ni muhimu na wengi wao hukosea hapo.

Anasema sio lazima kwa mfugaji kutengeneza bwawa la kisasa kama eneo analofugia kuna udongo wa uvinyanzi ambao unahifadhi maji kwa muda mrefu.

“Kwa maeneo ambayo hakuna udongo wa ufinyanzi, mfugaji atalazimika kutengeneza bwawa kwa kutumia saruji, lakini kwa maeneo ambayo kuna udongo unaohifadhi maji, hakuna haja ya kutumia vibaya rasilimali fedha,” anasema.

Dk Masanja anasema mfugaji lazima angalie aina ya maji yaliyopo katika eneo analotaka kufuga hata. Hata hivyo, anasema maji sahihi kwa ajili ya kufugia samaki ni yale yaliyovunwa.

“Maji ya kuvuna ni mazuri kwa sababu hayana chumvi na kitaalamu maji ya chumvi siyo mazuri katika ufugaji wa samaki,”.

Anasema samaki akifugwa kwenye maji baridi anakua haraka kuliko maji chumvi.

Kingine cha kuzingatia ni chakula; anasema vipo vyakula vya ziada lakini chakula kikubwa cha samaki ni kijani iliyopo kwenye maji ambayo inatengenezwa kwa kuchanganywa na mbolea ya kuku, ng’ombe na sungura.

“Hivi vyakula vingine tunatengeneza wenyewe kama ziada kwa sababu hawawezi kutegemea tu huo ukijani,”.

Mfugaji pia anatakiwa kulifanyia usafi bwawa lake. Dk Masanja anasema ni kosa kufuga samaki kwa muda mrefu bila kubadilisha maji. Maji yabadilishwe kila baada ya mwezi,” anasema.

Anasema ili kuvuna samaki wengi na wenye afya mfugaji anatakiwa kuwekewa muda maalumu wa kuwalisha na wapewe vyakula vinavyohitajika.

“Kama ataongeza virutubisho vingine vya ziada siyo tatizo, lakini chakula kikuu ni kijani inayopatikana kwenye bwawa hivyo mbolea zaidi ya asili zinahitajika,”anaongeza.

Tatartibu nyingine kwa mujibu wa Said, ni kuhakikisha mfugaji anaweka samaki kulingana na ukubwa wa bwawa lake.

Pia. sehemu yenye bwawa inatakiwa kuwa na chanzo cha maji chenye uhakika.

Ujenzi wa bwawa

Kuhusu sifa za bwawa, Said anasema kwanza linatakiwa kuwa katika eneo lenye udongo wa ufinyanzi, kwani aina hii ya udongo inahifadhi maji kwa muda mrefu.

Anasema kwa anayetengeneza bwawa katika eneo hilo hatotumia kiasi kikubwa cha fedha.

“Kwa wale waliopo kwenye maeneo yenye changarawe, watalazimika kutengeneza kwa kutumia tofali japo ni gharama kwani inaweza kufika Sh milioni moja au zaidi,”anasema.

Anasema pia sehemu nzuri inayofaa kutengeneza bwawa ni ile yenye maji yanayotiririka kuliko yaliyotuama.

“Eneo lisiwe sehemu kwenye mteremko mkali ambayo mvua ikinyesha inaweza kusababisha mafuriko, ”anasema.

Aina za ufugaji wa samaki

Musa anasema kuna aina kuu tatu za ufugaji wa samaki, ambazo ni ufugaji mdogo,ufugaji wa kati na ufugaji mkubwa.

Anasema kinacho tofauutisha aina hizi za ufugaji ni ukubwa wa eneo, wingi wa maji uwezo wa chakula na uwekaji wa samaki katika bwawa

“Kwa anayefuga ufugaji mdogo hana majukumu mengi, kwani huu hufanywa na mtu ambaye kipato chake ni kidogo, lakini tunashauri afuge kwa kutoweka samaki wengi na huyu hatumii bwawa la kisasa mara nyingi anatumia bwawa la tope,”anaeleza.

Soko la samaki

Kwa kawaida samaki wa kufugwa wanachukua takriban miezi sita kabla ya kuvuliwa na kuuzwa.

Ni mradi wenye soko la uhakika kwa mfugaji anayefanya shughuli yake kwa kufuata miongozo ya wataalamu.

‘’Kwa mfano, hapa tunafuga kwa ajili ya kufundishia wanafunzi lakini wakifikia hatua ya kuvuna tunauza kilo hadi Sh8000 kwa samaki aina ya sato na kambale tunauza Sh10,000,”anaeleza Dk Massanja.

Saturday, April 21, 2018

Mbinu za kuzalisha mayai yenye soko

 

By CLEMENT FUMBUKA

Baada ya kujulishana mambo mengi juu ya mbinu na taratibu za kuzingatia kwenye ufugaji wa kuku kwa faida, bado tunahitaji kuendelea kuzijua hatua za uzalishaji bora wa kuku wa nyama na mayai.

Ni rahisi mtu kujiuliza swali hili; kwani kuku, nyama na mayai ni tofauti hadi tutofautishe kuku wa mayai na kuku wa nyama, ili hali nyama na mayai vyote vinatoka kwa kuku yuleyule?

Jibu ni kwamba; unaweza kuwa na kuku wakazalisha mayai na mwishowe ukavuna nyama kutoka kwa kuku aliyekuwa anataga mayai.

Lakini jambo linaloleta tofauti kati ya kuku hawa ni uzalishaji. Kuku wanaokua haraka, kuchinjwa na kutoa nyama nyingi huitwa kuku wa nyama.

Kwa upande mwingine, mbegu ya kuku wanaotaga mayai mengi, huitwa kuku wa mayai. Haina maana kuwa kuku wa nyama hawatagi mayai kabisa.

Vilevile haina maana kuwa kuku wa mayai hawaliwi nyama, wanaliwa na nyama yao ni tamu kama kawaida lakini hawana nyama nyingi kama kuku wa nyama.

Makala haya ni mwendelezo wa ufugaji na uzalishaji bora wa mayai

Makala yaliyopita, tulitaja mbinu muhimu za kufikia uzalishaji wenye tija wa mayai.

Kuwakumbusha, mbinu hizo ni; moja, kupunguza idadi ya kuku na kubaki wachache kwa ajili ya kuwahudumia ipasavyo.

Pili, boresha mazingira yao ya kuishi ndani na nje ya banda, chukua tahadhari dhidi ya magonjwa wakati wote.

Tatu, tumia kanuni bora za ulishaji kama inavyoshauriwa mara kwa mara kwenye makala hizi.

Nne, ondoa haraka ya kuwa na shamba kubwa sana kwa wakati mfupi ukiwa huna uwezo wa kulihudumia vizuri.

Mayai yenye soko

Baada ya kukumbushana hayo, turejee kwenye mada husika ya leo, ambayo ni uzalishaji wa mayai bora yanayojiuza sokoni.

Ni ukweli usiopingika kuwa uzalishaji wa mayai kwa kiasi kikubwa haujazingatia sifa, ndiyo maana wafugaji wengi hulalamikia soko kuwa gumu na kukataliwa kwa mayai.

Hata hivyo, wanaozalisha kwa ubora wanauza. Katika bidhaa yoyote, ubora ni sifa namba moja.

Baada ya bidhaa husika kuwa na ubora kinachofuata ni wingi wa uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Mtu anaweza kuwa na mayai safi yenye bora, lakini yakawa kidogo, hivyo kununuliwa mara moja na kumalizika na kuacha soko likiwa bado na mahitaji.

Hivyo mambo haya mawili; ubora na kiasi cha uzalishaji ndiyo vinara wa kuleta faida au hasara kwa mfugaji.

Mfugaji wa kuku anatakiwa kuweka vipaumbele vyake katika mambo haya mawili.

Kila bidhaa inapendwa kwa sababu fulani. Mayai nayo yatapendwa kulingana na vigezo vinavyotakiwa kama vile usafi ukubwa, ubora wa ndani na uhakika wa kutoharibika kwa muda ambao mnunuzi anategemea kuyatumia.

Mambo haya kwenye uzalishaji wa mayai ni muhimu, kwani utapata wateja wengi.

Aidha, watu wengi huangalia zaidi mazingira ya jinsi bidhaa inavyozalishiwa. Ukiwa na mazingira mabaya wateja watakimbia.

Kumbuka msemo: “tatizo sio mvinyo (kinywaji), tatizo ni kifungashio chake”. Ni vizuri kuwavuta wateja kwa ubora wa bidhaa yako na uhakika wa upatikanaji

Kama mfugaji umejiandaaje kumshawishi mteja wako wa mayai kupenda mayai yako na hata kukuletea wateja wengine?

Swali hili sio fumbo ni swali la wazi lenye majibu ya wazi; zalisha kwa ubora na idadi ya kutosha, utaona faida katika uzalishaji wako na mwishowe utaipenda biashara yako.

Sifa za mayai bora

Ukiondoa ukubwa na muonekano wa ganda la nje, kiini cha ndani kinatakiwa kuwa cha njano (rangi ya karoti).

Mjadala mkubwa huibuka kati ya kuku wa kienyeji na kuku wa kisasa; yupi mwenye kiini cha njano?

Majibu ya swali hili yapo kwenye chakula wanachokula kuku husika.

Rangi ya njano kwenye yai ni mrundikano wa virutubisho aina ya vitamini ‘A’ ambayo kuku husika huvipata kutoka kwenye malisho yake.

Kadri kuku anavyokula vyakula mbalimbali, ndivyo anavyoongeza uwezo wa kutengeneza yai lenye kiini cha njano.

Kuku wanaofunguliwa nje kujitafutia vyakula wao wenyewe hukutana na vyakula mbalimbali ikiwemo vyakula vyenye asili ya mbogambaga ambavyo ndiyo vyanzo vikuu vya vitamini A. Kuku anayepewa chakula akiwa ndani, hukosa fursa ya kupata mapochopocho mengi ya vyakula na kujikuta mwili unakuwa na kiasi kidogo cha virutubisho vinavyokwenda kutengeneza yai ikiwemo rangi ya njano kwenye kiini.

Hivyo kinachosababisha tofauti ya rangi ya kiini, ni mfumo wa ufugaji na wala sio mbegu au aina ya kuku wenyewe.

Kuku wa kienyeji akifungiwa ndani kama kuku wa kisasa na kupewa chakula kama kuku wa kisasa, mayai yake yatapoteza unjano uliokolea kwenye kiini, kutokana na kupungukiwa malisho aliyokuwa anapata nje.

Kwa upande mwingine, kuku wa kisasa wakifunguliwa na kujitafutia chakula kama kuku wa kienyeji, mayai yao yatakuwa na kiini cha njano sawa sawa na kuku wa kienyeji.

Hivyo mfugaji unaweza kuongeza ubora wa mayai hasa kwa kuongeza vitamini A kwenye viini vya mayai ya kuku wako kwa kuwapa vyakula vyenye asili ya mchicha.

Pia, unaweza kuweka vyakula vingine vyenye rangi ya karoti kama vile pumba ya dengu na mashudu ya pamba kwenye mchanganyiko wa vyakula vya kuku kulingana na uwiano wa makundi ya vyakula.

Aidha,, zingatia mchanganyiko wa vyakula vyote kama vile wanga, madini, protini na vitamini kwa kuku.

Wafugaji wanaojitengeneza vyakula vya kuku, wanashauriwa kabla ya kutengeneza wapate kwanza ushauri kutoka kwa wataalamu wa mifugo walio karibu.

Saturday, April 21, 2018

Kifahamu kilimo cha kisasa cha maharage-2

 

By Mtalula Mohamed

Makala ya wiki iliyopita iliishia katika kipengele kuhusu maandalizi ya mbegu. Endelea.

Kiasi cha mbegu

Ili kupanda ekari moja unahitaji kuwa na kiasi cha kilo 30 mpaka 40 za maharage. Hii ni sawasawa na kilo 80 hadi 90 za maharage kwa hekta.

Unaweza kupanda mbegu moja au mbili katika kila shimo, lakini mbegu mbili ni bora zaidi na huleta mavuno mengi kwa eneo.

Nafasi ya upandaji

Ikiwa utapanda mbegu mbili za maharage katika kila shimo tumia nafasi ya sm 50 kwa sm 20 yaani sm 50 kati ya mstari na mstari na sm 20 kati ya mmea na mmea (shimo na shimo).

Ukipanda mbegu moja katika kila shimo, tumia nafasi ya sm 50 kwa sm 10. Hii ikuletee mimea kati ya 150, 000 na 200, 000 katika hekta moja.

Kudhibiti magugu

Maharage yanahitaji palizi mbili za jembe la mkono. Katika palizi ya kwanza, ondoa magugu shambani mara tu yanapoonekana, lakini hili lifanyike angalau wiki ya pili tangu maharage kuota.

Palilia tena kabla maharage hayajachanua. Kupalilia maharage yanayochanua au yenye matunda, kunasababisha kupukutisha maua au matunda.

Lakini pia unaweza kutumia madawa ya kuuwa magugu kama vile Galex 500EC, Stomp 500EC, Dual gold, sateca.

Mahitaji ya mbolea

Maharage hayahitaji naitrojeni kwa wingi kwa sababu mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen.

Hata hivyo maharage yanahitaji madini ya fosforasi kwa ajili ya kuboresha mizizi na potashi kwa ajili ya kuuandaa mmea kwa ajili ya kutoa maua mengi na kuzaa matunda bora.

Ikiwa shamba lililimwa zao ambalo liliwekwa mbolea kama vile Urea au CAN, basi huna haja ya kuweka tena mbolea za naitrojeni, badala yake unaweza kuweka TSP au DAP Kg 60 kwa hekta wakati wa kupanda. Au mbolea ya minjingu (Minjingu Rock Phosphate) Kg 250 kwa hekta moja wakati wa kupanda.

Kama shamba limechoka sana au halikuwekwa mbolea za naitrojeni msimu uliopita, tumia NPK katika uwiano wa 5:10:10 kiasi cha Kg 30 kwa hekta; nayo iwekwe wakati wa kupanda.

Mbolea zote ziwekwe sentimita tano hadi 10 kutoka kwenye shina/shimo la mmea na urefu wa sentimita 3 hadi 5 kwenda chini. Pia unaweza kutumia mbolea samadi (tani 5 - 10 kwa hekta) au mbolea ya kijani (green manure, tani 5 kwa hekta).

Mwaga/tawanya samadi kwenye shamba lote halafu ichangane vizuri na udongo kwa kulima kwa plau la trekta au ng’ombe). Maana yake ni kwamba mwaga samadi kabla ya kulima shamba lako kwa trekta au ng’ombe.

Mbolea ya kijani inapatikana kwa kusafisha shamba halafu ukaliacha mpaka majani/magugu yakaota kisha ukalilima kwa trekta au ng’ombe likiwa na magugu hivyo hivyo, lakini kabla hayajatoa mbegu halafu ukapanda. Mbolea ya minjingu inaweza kutumika pamoja na samadi na mbolea ya kijani.

Maharage huhitaji mvua ya kutosha kipindi cha kabla ya uwekaji maua na kipindi cha ukuaji wa vitumba vya maharage (podding).

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture Tz, inayotoa mafunzo ya kilimo bora na ufugaji wa kuku. www.mogriculture.com. 0655570084

Saturday, April 14, 2018

Sifa za wasimamizi wa shamba na njia za kuwadhibiti

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Japo Watanzania sasa wanakichangamkia kilimo, ukweli ni kuwa wengi wanafanya kilimo kama ajira ya pili.

Hawa ni wale wakulima wenye ajira zao hasa mijini, lakini wameamua kulima kama njia ya kujiongeza katika kutafuta namna ya kujikimu kimaisha. Sifa kuu ya wakulima hawa ni kuwa menejimenti ya shamba liwe la mazao au mifugo, wamewaachia wafanyakazi wa shamba.

Makala haya yanajaribu kuangazia baadhi ya mambo muhimu kuhusu wasimamizi wa shamba, ambao uzoefu unaonyesha wengi wamekuwa wakiwaweka roho juu matajiri wao.

Unampataje msimamizi wa shamba, zipi sifa stahiki za mfanyakazi na nini maana ya menejimenti ya shamba, ni miongoni mwa masuala muhimu yanayoelezwa na wataalamu na wadau wa kilimo.

Menejimenti ya shamba

Wakulima wengi pamoja na dhamira na shauku kubwa walizo nazo, wanafeli kwenye miradi yao kwa kukosa maarifa kuhusu menejimenti ya shamba ambayo inahitaji ushiriki wa mwenye mali na msimamizi wa shamba.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), Adam Ngamange, menejimenti ya shamba, ni usimamizi madhubuti unaoanzia tangu shamba linapoandaliwa, ununuzi na matumizi ya mbegu, elimu ya ya udongo, matumizi sahihi ya pembejeo na usimamizi wa soko. “Anatakiwa msimamizi mwenye taaluma au uelewa kuhusu kulimo, kwa sababu hapa ndipo panapohitaji umakini wa hali ya juu, hivyo menejimenti ikiyumba hapa kila kitu kitaenda ndivyo sivyo,”anasema.

Kuhusu soko kama suala lenye changamoto kwa wakulima wengi, anasema: “Msimamizi ana jukumu la kusimamia upatikanaji wa soko, nah ii huja baada ya kuhudumia vizuri mazao, kwani mazao yakihudumiwa ipasavyo ni kivutio kizuri kwa mteja.”

Wasimamizi ni changamoto nchini

Ngamange anasema changamoto Tanzania ni kutokuwapo kwa taasisi wala vituo vinavyotoa elimu kwa wasimamizi wa shamba.

Anasema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu hakukuwapo na dhana ya kufanya kilimo kwa mtazamo wa kibiashara, ambayo kuwepo kwake kungejumuisha pia wasimamizi wa miradi ya kilimo anaosema wanahitaji kuandaliwa.

“Katika nchi zilizoendelea, vipo vituo na taasisi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wasimamizi wa mashamba; changamoto ni kwamba kupata msimamizi mzuri bado ni ndoto,”anasema.

Ni lazima kuwa na msimamizi wa shamba?

Mdau na mtaalamu wa kilimo, Abdul Mkono, anasema dhana ya kuwa na msimamizi wa shamba haikwepeki, kwa kuwa miradi ya kilimo ina mambo mengi yanayohitaji umakini na ufuatiliaji wa karibu.

Anasema baadhi ya miradi inaendeshwa na wakulima wasioishi mashambani, hivyo wanahitaji wasimamizi ambao pamoj na mambo mengine wanaweza kugundua changamoto za mazao. Kutokuwa na msimamizi, mkulima anaweza kupata hasara kwa karibu asilimia 90.

“Nasema ni muhimu kwa sababu msimamzi anaweza kugundua matatizo mbalimbali

“Shambani kuna mambo mengi, hasa magonjwa ya mimea ambayo yanatakiwa kufuatiliwa kwa karibu. Kwa hiyo mmiliki pekee hawezi kuzunguka shamba lote na pengine hafiki shambani hapo mara kwa mara kwa sababu ana majukumu mengine,”anasema na kuongeza:

“Hii inatokea shamba likiwa kwa mfano liko mbali na mwenye shamba yupo mjini kwa ajili ya kazi nyingine, hivyo ni muhimu msimamizi awepo ili kujua hatua kwa hatua maendeleo ya mazao shambani.’’

Hata hivyo, Mkono anawatanabahisha wakulima kuwa makini katika kuwapata wasimamizi wa miradi shambani. Anaeleza: ‘’ Kuwa na msimamizi asiye na taaluma au maarifa yoyote kuhusu kilimo, ndiyo sababu ya wengi kuboronga na wakati mwingine kumsababisha mwenye shamba akate tamaa ya kuendelea na kilimo.

Omba ushauri

Kuna umuhimu mkubwa hasa kwa mkulima makini kushirikisha wataalamu katika masuala mbalimbali ikiwamo kutafuta wasimamizi wa shamba.

Ngamange anasema wataalamu wanafahamu ni msimamizi wa aina gani anafaa na yupi hafai na pia wanajua njia za kuwapata.

“Kwa hiyo njia pekee ndiyo hiyo, kwani wao ndiyo watakueleza kuwa huyu ni msimamizi mzuri au la, kwa sababu imezoeleka kuwa wasimamizi wa shamba ni wale wasio na kazi, waliofeli maisha; kumbe hapana,”anasema.

Mbinu za kuwadhibiti wasimamizi wa shamba

Ngamange anaamini moja ya silaha za kudhibiti wasimamizi wa shamba ni kuwapa fursa ya kupata maarifa zaidi yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika kazi zake.

“Kama kuna vitu havijui ni vizuri ukampa maarifa kupitia njia hii, atakupenda lakini pia utakuwa mwalimu wake ambaye kamwe hawezi kukusahau,”anasema.

Mbinu nyingine anataja ni malipo mazuri…’’Kila mfanyakazi anahitaji malipo mazuri tena yanayoendana na kazi anayofanya. Msimamizi hawezi kufanya udanganyifu kama mkulima anamjali na kumlipa vizuri.’’

Anasema pia mkulima anatakiwa kuwa karibu na msimamizi wake kwa kuwa wakulima wengi wanadhani msimamizi wa shamba ni mtu asiye na thamani kwao.

Kwa upande wake, Mkono anawataka wakulima kuwa na jicho la huruma kwa wasimamizi wao wa shamba, ikiwamo kuwasaidia wanapokuwa na matatizo binafsi.

“Unakuta mwingine kwa sababu tu yupo msimamizi basi atakaa mwaka mzima bila kumtembelea mfanyakazi wake wa shamba, kwa hiyo unapokuwa karibu naye na kumtembelea mara kwa mara unamtengenezea utendaji mzuri wa kazi,’’ anaeleza.

Usikate tamaa

Pamoja na wataalamu kushauri mbinu za kudhibiti wasimamizi wa shamba kwa kuwalipa vizuri, huduma bora na hata fursa za kielimu na nyinginezo kimaisha, baadhi ya wasimamizi ni sawa na sikio la kufa lisilosikia dawa. Hawa ni watu waliokosa fadhila ambao pamoja na mema wanayofanyiwa bado wamekuwa wakiwatenda matajiri wao.

Katika hali kama hii mkulima hapaswi kukata tamaa, njia muhimu zaidi kwake ni kujichunguza namna anavyowapata wasimamizi.

Baadhi ya mbinu zinapendekezwa hapa kuhusu kupunguza matatizo yanayoweza kusababishwa na wasimamizi wasio waaminifu.

Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na kujua mahala anapotoka mfanyakazi, kupata watu wanaoweza kumdhamini, kuhusisha mamlaka za kiserikali kama vile Serikali za vijiji na mitaa na kuingia nao mikataba ya kimaandishi.

Badilika

Baadhi ya wakulima wanawachukulia wafanyakazi wao kama mashine au wanyama wa kazi. Kibaya zaidi mfanyakazi huyu anayetumikishwa kama mashine halipwi vizuri au anaishi katika mazingira ya kusikitisha.

Huu ni udhaifu ambao kama mkulima makini unapaswa kuuepuka kama unatarajia mafanikio yenye tija katika mradi wako.

Saturday, April 14, 2018

Kifahamu kilimo cha kisasa cha maharage

By Mtalula Mohamed

Karibu katika safu hii mpya tuliyoipa jina la Jifunze kilimo. Nikiwa mtaalamu wa kilimo na ufugaji, makala katika mfululizo wa safu hii zitalenga kutoa mafunzo ya ulimaji wa kisasa wa mazao mbalimbali. Leo tunafungua safu yetu kwa kuangalia zao maarufu la maharage.

Maharage ni moja kati ya mazao ya jamii ya mikunde. Jamii ya mikunde hujumuisha mazao kama kunde, mbaazi, karanga, soya, choroko na maharage yenyewe.

Maharage pamoja na mazao mengine ya jamii hiyo, yana sifa moja kuu ya kuwa na vinundu kwenye mizizi yake. Vinundu hivyo vinawahifadhi bakteria maalumu wanaotengeneza naitrojeni. Hii ndio sababu ya jamii hii kufahamika kwa sifa ya kujitengenezea mbolea yake.

Zao la maharage linapendwa na wakulima wengi kwa sababu kwanza linachukua muda mfupi kukomaa, pili halina gharama kubwa katika uzalishaji wake na tatu lina bei nzuri sokoni karibu nyakati zote hata wakati wa mavuno.

Mkulima anaweza kulima maharage kwa matumizi ya chakula tu nyumbani kwake au kwa biashara rejareja au kwa jumla. Urahisi wa kulima maharage na faida zake lukuki, ni kivutio kwa watu wengi lakini bila kufuata muongozo wa kitaalamu ni ndoto kwa mkulima kupata mavuno anayotarajia.

Mazingira ya kilimo na hali ya hewa

Hustawi vizuri maeneo yenye mwinuko wa mita 800 hadi 2000 kutoka usawa wa bahari.

Kwa Tanzania maharage hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Kigoma, Arusha, Morogoro, Kagera, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma na Rukwa.

Udongo unaofaa

Maharage hustawi vizuri katika udongo wa tifutifu au tifutifu yenye mchanganyiko na kichanga wenye rutuba na usiotuamisha maji. Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya 5.5 - 7.0 kwa kipimo vya pH ingawa maharage yanaweza kuvumilia hata pH ya 4.5.

Mbegu bora za maharage

Mbegu bora ni zile zilizofanyiwa utafiti na taasisi zinazotambulika kisheria na zikapitishwa na Kamati ya Taifa ya Mbegu. Miongoni mwa mbegu bora za maharage zilizozalishwa katika nyakati tofauti tofauti na sasa zinatumiwa na wakulima ni pamoja na Uyole, Zawadi, Lyamungu 85 & 90, Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90, Bilfa na Canadian wonder.

Mbali na hizi zipo pia mbegu zinazozalishwa na wakulima wenyewe lakini chini ya usimamizi wa taasisi ya ithibati ya mbegu.

Wakati wa kupanda

Katika mikoa ya Mashariki, muda wa kupanda ni Machi/Aprili. Mikoa ya kanda ya ziwa ni Agosti/Septemba na Januari/Februari. Nyanda za juu kusini: Novemba/Desemba, Februari/ Machi Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike wakati muafaka kwa eneo husika kutegemeana na upatikanaji wa maji ya kutosha au mvua.

Pia maamuzi ya wakati wa kupanda maharage yazingatie kuwa wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.

Maji mengi yaliyotuama siyo mazuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza. Ukame nao haufai kwani unaweza kukausha mazao na kukuletea hasara. Hivyo kabla ya kupanda hakikisha una chanzo cha uhakika cha maji.

Maandalizi ya mbegu

Kuna aina nyingi za mbegu za maharage. Ni juu yako kufanya maamuzi ya mbegu unayoitaka lakini ni vizuri kutumia mbegu. Mbegu bora za maharage zinapatikana katika ofisi za wakala wa mbegu mkoani Morogoro, lakini wana matawi Arusha, Mwanza na Njombe. Pia unaweza kuuliza kwenye maduka ya mbegu yaliyo jirani.

Makala haya yameandaliwa na Mogriculture Tz, inayotoa mafunzo ya kilimo bora cha mazao na ufugaji wa kuku. www.mogriculture.com. 0655-570-084

Saturday, April 14, 2018

Ujue uzalishaji wa mayai ya kuku

 

By CLEMENT FUMBUKA

Safu hii imekuwa ikiangazia mambo mengi muhimu katika ufugaji wa kuku, ikiwemo kutambua fursa ya ufugaji, kanuni za ufugaji na ujasiriamali.

Sasa tunaweza kwenda sehemu nyingine ya mavuno ya mazao ya kuku shambani.

Ukiondoa mbolea, mayai na nyama ndio dhamira kuu ya biashara ya ufugaji wa kuku. Na kwa kuwa somo la leo ni juu ya uzalishaji wa mayai, ni vizuri tukajua mayai huanzia wapi kwenye mwili wa kuku.

Kuku ni sawa na wanyama au ndege wengine majike. Huzaliwa au kuanguliwa kutoka kwenye mayai wakiwa na mayai (via vya uzazi) matumboni mwao.

Baada ya kuanguliwa, viungo muhimu kwenye maisha kama vile moyo, figo, mapafu, ini na mfumo wa fahamu huanza kazi mara moja.

Ukuaji wa viungo vyote hupangiliwa kulingana na matumizi yake mwilini. Katika viungo vyote, via vya uzazi hukomaa mwishoni baada ya viungo vingine vyote kukomaa.

Nimependa kuleta ufafanuzi huu kwako mfugaji, ili ujue matokeo ya huduma unayoitoa kwa kuku wako. Kimsingi, kuku ni sawa na viumbe wengine; huhitaji nguvu kutoka kwenye chakula ili waweze kukua na hatimaye kuzalisha.

Afya na uzalishaji wa kuku ni matokeo ya chakula anachopewa kukuza viungo vyake vyote, ikiwemo via vya uzazi ambavyo ndiyo huzalisha mayai. Mbali na hilo, via vya uzazi hutegemea viungo vyote vya mwili vifanye kazi. Ndiyo maana shida ndogo kwenye mwili wa kuku, husababisha uzalishaji wa mayai kupungua.

Msomaji, unaweza kushangaa mada ya leo ni uzalishaji wa mayai lakini viungo visivyohusika na mayai vinaingiaje hapa?

Hii ni kwa sababu mayai hutokana na hali ya kiungo kimoja kimoja hata kabla ya kukomaa kwa ovari ambao ni mji wa uzazi wa kuku.

Hivyo ni vema kuonyesha chimbuko la huo uzalishaji wa mayai kwa wafugaji wakaelewa na kuufanya ufugaji wao kwa misingi bora.

Kwa nini kazi ya uzalishaji wa mayai inasubiri kazi ya ukuaji ikamilike kwanza mwilini, badala ya kuendesha mambo yote pamoja ukuaji na uzalishaji wa mayai?

Via vya uzazi huhitaji nguvu nyingi kukua, kukomaa na kufanya kazi. Kiumbe chochote (akiwemo binadamu) kikichanganya mambo ya uzazi kingali bado kinakua, kiumbe hicho lazima kidumae na kuwa na afya mbaya maisha yake yote.

Uzalishaji na ukuaji vikitokea kwa pamoja kabla kiumbe husika hakija komaa, ukuaji husimama na nguvu yote ya mwili huhamia kuhudumia via vya uzazi na kusababisha upungufu mwingi kwa kuku.

Hivyo mfugaji alenge kutoa huduma nzuri kwa kuku wake ili wafikie kutaga mwili ukiwa umekomaa, hivyo ibaki shughuli ya kuzalisha mayai pekee.

Vilevile napenda mfugaji afahamu kwamba uzalishaji unahitaji nguvu kubwa kuliko nguvu ya ukuaji.

Ndiyo maana kuchanganya ukuaji na uzalishaji mwili wa kuku, kutasababisha kudhoofika kiafya maisha yote. Na kwa sababu hiyo kwa mfugaji, si jambo la kufurahi kuona kuku wanataga mapema kuliko umri unaotakiwa kuanza kutaga.

Ikitokea hivyo, tambua kwamba kuku wako hawatofanya vizuri maisha yao yote. Kwa msaada juu ya hili, kagua uzito wa kuku wako, kwani umri wa kuku, uzito na uzalishaji wake huendana.

Unaweza kutumia kigezo cha uzito wa kuku kujua uzalishaji wa mayai kabla na baada ya kuanza kutaga.

Kuku wepesi hutaga mayai yenye umbo dogo na utagaji wao ni wa kubahatisha. Kuku wenye uzito wa wastani hutaga mayai yenye ukubwa wa wastani na utagaji wao ni mzuri.

Kuku wenye uzito mkubwa hutaga mayai makubwa, wakati mwingine hushindwa kutaga kwa sababu ya yai kushindwa kupita.

Kuku wenye uzito mkubwa hutokana na kulishwa sana pia sio watagaji wazuri.

Mfugaji anatakiwa kujali zaidi afya ya kuku wake kabla hawajafikia kutaga, ili wakue vizuri na kukomaa vema. Hapo atavuna mayai mengi kwa muda mrefu.

Ni vizuri mfugaji kupangilia huduma zake kwa kuku, baada ya kujua mahitaji yao ya msingi wakati wa makuzi na wakati wa uzalishaji. Zingatia ugawaji chakula bora kwa kiasi kinachotakiwa kulingana na umri wa kuku.

Kagua uzito wa kuku wako mara kwa mara kabla na baada ya kuanza kutaga mayai. Makala haya yanakuonyesha sehemu ambayo unaweza kuingilia kati, kuokoa mradi wako na kufuga kwa faida.

Ili taaluma yako hii unayoipata humu iweze kufanya kazi, anza kuitumia kila unapopata ujumbe huu muhimu. Kama ulianza kufuga bila kujua haya, huu ndio muda wako kubadilisha mambo na kufuga kwa tija. Na kama bado hujaanza kufuga lakini unategemea kufuga ni wakati wako mzuri kuanza kwa ujuzi bora.

Mbinu za kuzalisha mayai mengi kwa faida

Kwanza, punguza idadi ya kuku wako na kubakia wachache ikiwa huna uwezo wa kuwahudumia.

Pili, boresha mazingira yao ya kuishi ndani na nje ya banda. Chukua tahadhari dhidi ya magonjwa wakati wote.

Tatu, tumia kanuni bora za ulishaji kama inavyoshauriwa mara kwa mara kwenye makala hizi.

Nne, ondoa haraka ya kuwa na shamba kubwa sana kwa wakati mfupi ilhali huna uwezo wa kulihudumia vizuri.

Tano, epuka kufuga kwa hasara, kwani inachosha, kuudhi na kukatisha tamaa.

Wapo wafugaji wengi wameanza kwa mitaji kidogo na kuku wachache, lakini kwa kufuata kanuni za utoaji huduma bora, wamefanikiwa kuwa wafugaji wakubwa.

Saturday, March 24, 2018

Mambo muhimu ya kuzingatia kilimo cha bustani

 

By Flora Laanyuni

Kilimo cha bustani kinahusika na uzalishaji wa mazao ya aina ya mboga, matunda, viungo na mimea ya mapambo.

Kilimo cha bustani ni chanzo cha ajira na pato kwa wakulima na watu wengine. Mboga na matunda vinatupatia virutubisho vya kujenga, kutia nguvu na kulinda mwili.

Zaidi ya hivyo, mimea ya mapambo hutumika katika kuremba na kuboresha sehemu za makazi, majengo, barabara na sehemu nyingine za wazi za jumuia.

Hata hivyo, unapowaangalia wakulima wengi mazao ya bustani hasa yale ya mbogamboga, utagundua wengi wamejikita katika uzalishaji wa mazao hayo, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya familia pekee.

Hawa ni wakulima wasio na wigo mpana wa kuzalisha kwa kulenga soko kubwa na kupata kipato cha kudumu, japo mazao hayo yana sifa ya kuwa na soko zuri.

Ni muhimu kuhakikisha kunakuwapo mifumo mizuri kuanzia kwenye uzalishaji, uhifadhi, usindikaji na upatikanaji wa taarifa sahihi za masoko.

Haya yakifanyika, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa faida kubwa na kuwawezesha kukua kiuchumi.

Mambo muhimu ya kuzingatia katika uzalishaji

Hata hivyo, ili kuzalisha kwa kiwango kikubwa, mkulima wa mazao ya bustani anapaswa kuzingatia baadhi ya mambo muhimu ikiwamo kuwa na taarifa sahihi na za kutosha kuhusu zao analolima.

Mkulima anatakiwa kuwa na taarifa zote muhimu zinazohusiana na zao analotegemea kushughulika nalo.

Taarifa hizi zinajumuisha upatikanaji wa mbegu bora, hali ya hewa inayopendekezwa kwa zao husika.

Mengine ni taarifa kuhusu magonjwa na wadudu wanaoweza kulishambulia zao hilo na namna ya kuyakabili, pamoja na uhitaji wake katika soko la ndani na la nje.

2.Misingi ya uzalishaji: Ili mkulima aweze kuzalisha kwa tija na kwa gharama nafuu wakati huo

huo akilinda afya yake na ya walaji, ni muhimu kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai.

Fanya uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia misingi hii kuanzia kwenye mbegu kwa kutumia mbegu zilizozalishwa kwa misingi ya kilimo hai, matumizi ya mbolea hai, dawa za kudhibiti magonjwa na wadudu pamoja na uhifadhi wa mavuno au mazao yako ghalani au katika usindikaji.

Kilimo hai ni aina ya kilimo kisichotumia madawa wale kemikali za viwandani. Bidhaa zitokanazo na kilimo hai zinaelezwa kuwa na ubora maradufu kuliko bidhaa zitokanazo na madawa na mbolea za viwandani.

3.Eneo na hali ya hewa:

Kabla mkulima hajafikiria juu ya kulima zao fulani, ni lazima ahakikishe kuwa ana eneo la kutosha kwa ajili ya mazao yake

Lakini pia ahakikishe kuwa hali ya hewa ya eneo hilo inaoana na zao analotaka kulima.

4.Gharama za uzalishaji:

Jambo hili ni la msingi kwani huwezi kufanya kilimo bila kuingia katika gharama za uzalishaji.

Gharama hizi ni pamoja na ununuzi wa mbegu, maandalizi ya shamba, utunzaji wa zao shambani kwa kudhibiti wadudu na magonjwa, uvunaji na upelekaji sokoni au usindikaji.

5.Upatikanaji wa soko

Suala la soko ni la msingi na ni la wakati wote, kuanzia kipindi cha utafutaji taarifa ya zao husika, wakati zao likiwa katika hatua ya awali ya uzalishaji na hata linapokuwa tayari kwenda sokoni.

Ni muhimu kwa mkulima kutafuta soko la mazao yake ili aweze kuuza kwa bei iliyopo sokoni na ikiwa bei

imeshuka kwa ghalfa bila kutarajiwa, aweze kufikiri namna nyingine ya kutatua tatizo hilo hasa kwa kutumia njia mbadala kama vile kufanya usindikaji wa zao lake.

6.Mikataba ya ununuzi:

Mbali na upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakulima wa bustani, ni muhimu pia wakulima kuhakikisha kunakuwapo mikataba inayoeleweka baina yao na wanunuzi.

Mikataba hii itawawezesha kujua wanazalisha nini, watapata huduma wapi, watauza wapi, watauza kwa nani na watauza kwa bei gani.

Aidha, kabla wakulima hawajaingia katika kufanya mikataba, ni muhimu wakawa na uelewa mkubwa wa namna ya uuzaji wa mazao hayo ya bustani ndani ya nchi na hata nje ya nchi, bila kudanganywa na bila kudidimizwa ili kuendeleza uchumi wao wenyewe na wa nchi kwa jumla.

7: Kulima kulingana na uhitaji

Hili linawagusa wakulima wengi hasa wanaolima kwa kufuata mkumbo kama ilivyozoeleka hivi sasa katika jamii zetu.

Ni kweli hamasa za kutaka watu wajiingize kwenye kilimo ni nyingi, kubwa na zina umuhimu, lakini wakulima hawana budi kutafakari kabla ya kuamua kuingia kwenye kilimo fulani.

Lazima wakulima wahakikishe wanalima kulingana na uhitaji wa walaji na si kulima kwa mazoea au kwa vile kila mmoja analima.

Kwa mfano, sio busara kutaka kulima matikiti kwa kuwa ndilo zao linalolimwa na kila mtu eneo uliopo. Tatuta zao ambalo mahitaji yake ni makubwa, kwa kuwa unakuwa na uhakika wa soko lake.

Makala haya yaliyoboreshwa ni kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org


Saturday, March 24, 2018

Mbinu bora za utoaji wa chakula kwa kuku

Mfugaji akilisha kuku wake chakula. Wafundishe

Mfugaji akilisha kuku wake chakula. Wafundishe kuku wako kula chakula chote kiishe asubuhi ili jioni wapate hamu tena ya kula chakula chote. Picha na mtandao wa livestocking. net 

By Clement Fumbuka

Napenda kuwapongeza wote wanaofuatilia kwa karibu makala haya ya ufugaji wa kuku kwa muda mrefu. Bado naguswa kuendelea na harakati hizi za kutoa elimu juu ya ufugaji wa kuku kwa wafugaji na kuongeza ufanisi zaidi kwenye biashara hii.

Nawakaribisha watu wote wenye nia na biashara hii waendelee kunufaika na makala hizi za mara kwa mara kujifunza mbinu na kanuni mbali mbali kuboresha kazi ya ufugaji.

Ukizingatia makala hizi na kuzifanyia kazi, ni dhahiri kwamba unaweza kubadilisha hali yako ya uzalishaji shambani kutoka kuzalisha kwa faida ndogo na kuingia kwenye uzalishaji wenye faida kubwa.

Kosa dogo katika biashara huleta upungufu mkubwa kwenye uzalishaji na faida kwa ujumla.

Kila siku biashara hubadilika kulingana na mazingira, teknolojia, upeo wa watu na mahitaji ya jamii.

Kuna wakati unahitaji kupata mawazo mengine mapya na kupanua fikra zaidi ili kuendana na hali ya ushindani katika soko la biashara.

Kampuni kubwa na mashirika mbali mbali wanajua kuwa kila baada ya muda watumishi wao wanahitaji kupewa elimu kwenye kazi zao, ili kuongezewa upeo na namna ya kufikiri na kutoa huduma bora kila wakati.

Hivyo hivyo katika ufugaji kwani ni sekta kubwa inayoweza kuajiri watu na kuwalipa vizuri sawa na biashara nyingine kubwa za mashirika au kampuni.

Hakuna shirika au kampuni inayoweza kusimama bila kuanguka kama elimu haitolewi kwa wafanyakazi wake.

Ndiyo maana utaona semina zikitolewa mara kwa mara kwenye mashirika na kampuni bila kujali gharama kubwa ya kuendesha semina au mafunzo ya mara kwa mara.

Pengine wanafanya hivyo kwa sababu wanajua faida ya kutoa elimu kuimarisha usimamizi na utoaji huduma bora katika mambo yao wanayofanya.

Ukienda kupata ushauri wa kuanzisha biashara fulani kwa mtu swali la kwanza atakuuliza ‘una uzoefu gani au una mtaalamu wa kukuongoza?’

Elimu ni mwongozo kwa mtu ili asikosee jambo kwenye kazi yake na kupata hasara. Makala haya ni mwongozo mzuri kwa mfugaji, ni semina au mafunzo ya kuongeza upeo wa kufikiri kuendana na mazingira ya uzalishaji kwa faida. Maendeleo katika jambo lolote yanakuja baada ya kupangwa na kutafutwa kwa kufuata maelekezo ya watu wenye ujuzi, kusoma maandiko au kuhudhuria semina zinazofundisha mambo hayo. Ukurasa huu kwa wafugaji ni sehemu ya kupata elimu kwa urahisi.

Ulishaji kuku

Katika makala yaliyopita tuliona ni namna gani ulishaji kwa kuweka vyombo vichache bandani, unavyosababisha kuku kukua kwa matabaka.

Tuliona kuku au vifaranga wenye nguvu hutangulia kula chakula chote chenye virutubisho na kuacha vifaranga wanyonge wakila mabaki.

Ili kuepuka tatizo hilo tuliona kuwa ni vema mfugaji aweke vifaa vya kutosha ili kuku wote wapate chakula kwa pamoja tangu siku ya kwanza vifaranga wanapoingia bandani.

Hii itawasaidia kukua kwa pamoja bila kutokea wa kumpiga mwenzake wakati wa kulisha.

Moja kati ya matokeo mazuri ambayo tuliona endapo mfugaji atafuata kanuni hizi za ulishaji bora, ni pamoja na kuku kufikia umri wa kutaga mayai au kuuzwa wakiwa wote wanalingana.

Faida ya kulingana kwa kuku wanapofikia umri wa kuzalisha ni kubwa kwani hata uzalishaji wao utakuwa mzuri.

Kama ni kuku wa mayai watataga mayai mengi; kama ni kuku wa kuuzwa kwa ajili ya nyama mteja hatochagua kuku kwa sababu wote wanalingana hivyo mfugaji anaweza kuuza mara moja na kuingiza wengine.

Sehemu hii katika ulishaji ni muhimu na inatakiwa kuangaliwa na wafugaji wote kwenye mifugo yote.

Mbali na ulishaji na idadi ya vyombo vya kulishia, leo tuangalie namna ya utoaji wa chakula kwa kuku.

Kuku ni mifugo wenye kuzoea haraka mazingira. Mfugaji wa kuku anatakiwa kuwa na muda maalumu wa kulisha kuku wake; sio kila wakati unafaa kulisha kuku.

Lisha chakula mapema asubuhi kuku wanapoamka na jioni wakati jua limepoa. Weka utaratibu unaojulikana ili kuku waelewe saa ya kula na saa isiyo ya kula.

Usilishe chakula wakati wa mchana jua likiwa kali au usiku kuku wakiwa wamelala.

Kuku ni sawa na ndege wengine tabia zao hupangiliwa kwa muda hivyo ni vizuri kutoa huduma kulingana na wakati.

Kama kuku wamefikia umri wa kupimiwa chakula, hakikisha unawapa chakula nusu asubuhi mapema na nusu iliyobaki jioni na ratiba hiyo waizoee.

Kuku wasiolishwa kwa utaratibu hukosa hamu ya kula na kujikuta kila siku chakula kinabaki kwenye vyombo vya kulishia na uzalishaji au ukuaji kushuka. Wafundishe kuku wako kula chakula chote kiishe asubuhi ili jioni wapate hamu tena ya kula chakula chote.

Hii itasaidia kuongeza uzalishaji na ukuaji wakiwa wote wamelingana tangu wakiwa wadogo. Wakati wa kulisha hakisha unatumia ndoo na bakuli la kuchotea na kuweka kwenye vyombo vya kulishia.

Weka chakula kidogokidogo kwanza kwenye vyombo vyote ili vipate chakula na kuku wasambae kwenye vyombo vyote kisha rudia kujazia kwenye vyombo kadiri inavyotakiwa.

Usiweke chakula kikaishia njiani na vyombo vingine vikabaki tupu; utasababisha fujo na kugombania nafasi bila sababu.

Mara baada ya kuweka chakula kwenye vyombo vya kulishia, toa vyombo vya maji na vioshe kwa maji safi na kurudishia maji haraka. Kuku hawatakiwi kukosa maji kwa muda mrefu.

Epuka kulisha chakula kisichofaa. Hata kama utafuata kanuni za utoaji chakula kwa wakati, itakuwa kazi bure kwa sababu kuku watakosa lishe ndani ya chakula na kubaki hawana uwezo wa kuzalisha ipasavyo.

Lisha mchanganyiko wenye makundi yote ya chakula uliochanganywa kwa uwiano sahihi kwa kila kundi la virutubisho.


Saturday, March 17, 2018

Sababu ya Dk Masanja kuanzisha chuo cha kilimo

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Wakati mtazamo wa wawekezaji wengi katika sekta ya elimu ukiwa ni kufungua shule au taasisi zinazotoa kozi ambazo kwa wengi ni kozi zinazolipa, wapo wenye mtazamo tofauti.

Uzoefu unaonyesha ili ujihakikishie wanafunzi wa kutosha unapofungua chuo nchini, huna budi kutoa kozi kama kompyuta, uhasibu, afya, uandishi wa habari, utawala na nyinginezo. Huko ndipo walipowekeza wawekezaji wengi binafsi.

Hata hivyo, kuna wawekezaji wachache wanaoona fursa kwenye sekta ya kilimo. Miongoni mwao ni Dk Aloyce Masanja aliyeamua kuanzisha chuo cha masuala ya kilimo na ufugaji.

Kwa muda mrefu Serikali ndiyo imekuwa mwekezaji pekee kwenye sekta hiyo, lakini sasa nguvu imeongezeka kwa kuwapo taasisi binafsi kikiwamo chuo hiki.

Dk Masanja ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chuo kijulikanacho kwa jina la Canre, anasema haikuwa kazi rahisi kuwavutia wanafunzi kusoma kozi za kilimo lakini sasa mwitikio umekuwa mkubwa.

Chuo hicho kilichopo Bonyokwa, Segerea jijini Dar es Salaam, kilianzishwa mwaka 2006 huku kikiwa na wanafunzi wawili, lakini sasa kina zaidi ya wanafunzi 600.

“Mwitikio ulikuwa mdogo sana kwa wanafunzi kusomea masomo ya kilimo; kuna wakati nilikuwa najiuliza hivi mimi nitaweza kweli mana niliona kama masomo haya ya kilimo hayapendwi hata hivyo sikukaata tama,”anasema.

Anasema baada ya chuo hicho kusajiliwa mwaka 2010 wanafunzi waliongezeka huku mwitikio kwa wasichana kusomea kilimo ukiwa mdogo.

“Lakini sasa hivi naona vijana wanaongezaka na kwa mtazamo huu natarajia kuona wataalamu wengi wa kilimo wanatoka hapa na kwenda kukomboa wananchi katika masuala ya kilimo na ufugaji,”anaongeza.

Kilichomsukuma kuanzisha chuo cha kilimo

Anasema wazo la kuanzisha chuo cha kilimo lilikuja baada ya kuona sekta ya kilimo haina maendeleo ya kuridhisha kwa maana kwamba watu wengi wanaikimbia na hata waliokuwa wakilima na kufuga, hawakufanya kitaalamu.

Anasema kilimo ni uti mgongo lakini hakiwezi kuwa na tija kama hakutakuwa na wataalamu wa kutosha watakoashauri wakulima hasa katika maeneo ya vijijini.

Kabla ya hapo alikuwa na utaratibu wa kwenda kutembelea nchi mbalimbali kuona maeneo gani yanakwamisha Watanzania wenye nia ya kufanya kilimo na ufugaji.

“Mfano nilipokwenda Japani nilikuta watu wanalima tena kwa kutumia enao dogo tu lakini wanavuna mazao mengi, nikasema kwani sisi Tanzania tunashindwaje?

Nikaweka nia kwamba lazima niikomboe nchi yangu katika masuala ya kilimo,”anasema.

Anasema pia kilichomvuta kuanza chuo hicho ni kwamba alizaliwa kwenye familia ya wakulima hivyo kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi chuo alijikita zaidi katika masomo ya kilimo.

“Nimefikiria sana nikaona hapa nchini vyuo vingi vya binafsi ni vya fani nyigine nikaona kwa nini nisianzishe chuo cha kilimo ili kuongeza nguvu kile cha Serikali tuweze kuzalisha wataalamu wa kutosha,” anasema.

Anasema alichokiona ni kwamba jamii inashindwa kutambua kuwa kilimo ni sehemu ya ajira. Wapo wanaolima zao la aina moja tu wakidhani kwamba mazao mangine hayana faida.

“Sasa hivi kilimo ni biashara, nchi za wenzetu wanafanya kilimo hadi cha maua lakini kinalipa lakini kwa Tanzania mtu anaona maua ni kwa ajili ya kupendezesha nyumba yake tu lakini kumbe maua ni mtaji,”anasema.

Alivyoanzisha chuo hicho

Kwa kuwa alikuwa mwajiriwa katika Wizara ya Kilimo kwa miaka 20, hakutaka kupoteza ujuzi wake hivyo wazo la kuanzisha chuo hicho likaanzia hapo.

“Katika eneo hili kulikuwa pori kubwa kwa bahati nzuri nilikuwa nalima mahindi, migomba, nilikuwa pia nafuga kuku na samaki nikaona ni vyema nianzishe chuo cha kilimo na ufugaji,”anasema Dk Masanja.

Hata alipokuwa masomoni nje ya nchi akichukua Shahada ya Uzamivu, aalijikita kwenye masuala ya kilimo na ufugaji, lengo likiwa kuja kuisaidia jamii nchini baada ya kuona haijahamasika katika sekta hiyo.

“Basi baada ya hapo nilianza na wanafunzi wawili na walimu wawili nilienda nao hivyo hivyo japo mwanzo ulikuwa mgumu lakini sikukata tamaa na safari yangu ya kuwakomboa wakulima,”anasema.

Kwa nini watu wanakimbia kilimo?

Dk Massanja anasema: “Nilichokiona hapa ni mtazamo wa wengi kufikiria kwamba kiilimo ni cha wazee na hata ukiangalia asilimia kubwa watu wanaishi kijijini kwa hiyo huku mjini mtu anaona kilimo hakina tija.’’

Kutokana na zana zinazotumika kutokuwa za kisasa ndiyo maana wengi wanasema kilimo hakilipi.

“Mkulima anatakiwa kujua kilimo kina maana gani kwake, wengi wanalima kimazoea na wengi wanashindwa kwa sababu hawajapata elimu ya kutosha kilimo kina maana kubwa sana ndani ya jamii,”anasema.

Anasema uwepo wa vyuo vya kilimo nchini utakiongezea tija kilimo kwani ni wachache wenye mwamko na kutambua umuhimu wa kilimo, hivyo ni vyema Serikali ikaongeza juhudi ikiwemo kuongeza sehemu za mafunzo.

“Lakini pia hata sera ya Serikali ya kilimo ya mwaka 2013 mimi nilivyoiona imetoa mwelekeo mzuri na imegusa karibu maeneo yote muhimu, kwa hiyo sasa hivi watu wameanza kupata ufahamu kuwa kilimo sio kwa ajili ya chakula tu bali kilimo ni biashara,”anaongeza.

Changamoto

Dk Masanja anasema tangu ameanzisha chuo hicho amepitia changamoto mbalimbali ambazo kama sio ujasiri wake zingeweza kumkatisha tamaa na kurudisha nyuma malengo yake ya kukomboa wakulima.

Moja ya changamoto hizo ni kutoaminiwa na taasisi za kifedha wakati wa kuomba mkopo, kwani anasema kutokana na chuo hicho kuwa na wanafunzi wachache walihisi asingeweza kulipa.

Changamoto nyingine ni kutoungwa mkono na Serikali.

Anasema mbali na chuo hicho ni kuiinua sekta ya kilimo kwa kuzalisha wataalamu wa kilimo, lakini bado Serikali haiungi mkono juhudi zao.

“Mimi sikufichi nimetoa zaidi ya wanafunzi 2000 tangu naanzisha hiki chuo, lakini hakuna hata kiongozi mmoja aliyekuja kuona wala kuangalia ninachokifanya. Ningefarijika pengine hata masuala ya kodi wangenipunguzia,” anaeleza

Anasema suala la kodi lina mtesa kwani wakati mwingine hadi vifaa anavyopatiwa kama msaada analazimika kuvilipia kodi.

Mbali na changamoto hizo anasema kwa kuwa amedhamiria kuwa mkombozi wa kilimo na ufugaji. Anasema mbali na kutoa elimu kwa ngazi ya astashahada na stashahada, ana lengo la kuanzisha chuo kikuu.

“Mimi sitoishia hapa, nitaenda mbali zaidi kwa kuanzisha shahada ya kilimo na mifugo na tayari eneo nimeshalitenga kwa ajili hiyo,”anasema.

Mafanikio yake

Masanja anajivunia kuona wanafunzi waliotoka chuoni kwake wakiajiriwa katika halmasahauri mbalimbali wakitoa huduma ya masuala ya kilimo kwa Watanzania.

“Hayo ndiyo mafanikio yangu mimi, siwezi kujivunia nyumba wala mali nilizonazo kwa kuwa lengo langu ni kutoa elimu ya kilimo kwa vijana kwa hiyo najivunia kupiga hatua kubwa,” anasema.

Saturday, March 3, 2018

Mbinu za kuwaepuka madalali wa mazao

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Wiki iliyopita jarida hili lilichapisha makala kuhusu kilio cha wakulima, wakiwalalamikia madalali wa mazao kuwa ni kikwazo cha maendeleo yao.

Katika makala haya, wakulima wanaeleza jinsi ambavyo baadhi ya nyakati, wanavyoweza kuwaepuka madalali hao ambao uwepo wao katika masoko unaonekana kuwa kama mfumo rasmi wa uendeshaji wa masoko nchini.

Mkulima wa matunda kutoka wilayani Bagamoyo, Lucy Salema anasema : “Hawa mbona kuwaepuka ni kazi rahisi tu ilimradi tu kuwepo na utaratibu maalum kwenye haya masoko makubwa mfano Kariakoo ili madalali wasiwepo kabisa.”

Anasema kuwa kinachotakiwa kwa mkulima ni kutoa taarifa mapema kwa kiongozi wa soko kabla hajapeleka mazao sokoni, ili kiongozi huyo ajue kwamba ni wakulima wangapi wataingiza mazao sokoni na taarifa hiyo itolewe mwezi mmoja kabla.

Utaratibu huo utampa nafasi kiongozi wa soko kujua ni wakulima wangapi wataleta mazao ya aina moja na wangapi wataleta aina nyingine. Ni utaratibu ambao utasaidia kuondoa msongamano wa wingi wa watu wanaopeleka mazao.

“Wakulima tukienda sokoni wengi, madalali wanapata nafasi nzuri ya kutuumiza, kwa sababu wanajua mkulima hawezi kumkataa maana matunda ukikaa nayo sana yanaharibika, lakini kiongozi wa soko akisimama imara hatuwezi kunyanyaswa na watu hawa,” anasema.

Kwa mkulima, Salim Magege anayeishi mkoani Mwanza, anasema kinachotakiwa kufanywa ni ushirikiano kati ya mkulima, kiongozi wa soko na mnunuzi bila hivyo hawawezi kumaliza tatizo hilo la madalali sokoni wanaokandamiza haki za wakulima.

“Uwezekano wa kutotumia madalali sokoni upo tena mkubwa tu, yaani ni bora kama kuna ushuru mkulima nilipe moja kwa moja kwa uongozi wa soko na uongozi wa soko unikutanishe moja kwa moja na mnunuzi,” anasema.

Anasema kinachofanyika sasa ni kwamba madalali wanachukua fedha, uongozi wa soko nao wanachukua fedha kwa hiyo kuna mlolongo mkubwa ambao mkulima anapitia.

“Ukiangalia kiashiria kikubwa kuwa madalali wanatudhulumu ni kushusha bei. Kwa mfano, mkulima anaenda soko kuu la Kariakoo kwa lengo la kuuza vitunguu Sh 150,000 kwa gunia, lakini ukikutana na dalali unaambiwa uuze kwa 130,000,”anaeleza.

Anasema kuwa madalali wakipanga bei, hawataki mabishano kwani ukifanya hivyo huwezi kupata mteja na bidhaa yako itaoza.

Viongozi wa masoko wawazungumzia madalali

Saidi Mzuzure ni mjumbe wa kamati ya soko la Sterio wilayani Temeke anasema: “Sio kweli kuwa tunawabeba madalali kwa sababu kiongozi wa soko ni kiongozi wa mteja na mkulima kwani bila wao hakuna soko.’’

Akielezea taratibu za soko lao, anasema madalali nao ni wakusanya kodi, kwa kuwa mkulima anapouza bila ya kumtumia dalali Serikali ya wilaya inakosa mapato.

“Tukisema pia hawa wakulima wauze bila kupitia kwa dalali hatuwezi kukusanya ushuru, kwa sababu mkulima anapokuja hapa na kuuza mazao yake bila dalali akipata tu mtu akamuuzia utakuta mkulima yule anaondoka na yule mnunuzi anaondoka na mwishowe Manispaa haipati mapato,”anasema.

Isihaka Ofiole ambaye ni Kaimu Katibu wa soko la Buguruni, anasema wanatambua uwepo wa madalali katika soko hilo ila kuhusu wakulima kudhulumiwa hawalitambui hilo kwani makubaliano hufanywa kati ya wakulima wenyewe na madalali.

“Hilo la kudhulumiwa sijapata malalamiko, lakini kwa kucheleweshewa malipo inatokea mara kwa mara na hii ni kutokana na wakulima na madalali kutotoa taarifa kwa uongozi wa soko pindi wanapokabidhiana mazao yao,” anasema.

Ofiole hata hivyo, anasema madalali wanatokana na wakulima wenyewe kwa kuwa ndio wanaowapa mzigo. Anasema kilichozoeleka ni ule utamaduni waliojiwekea wakulima wa kuuza kupitia kwa dalali hasa kwa wale wanaoleata mzigo mkubwa.

“Lakini pia wakati mwingine mkulima ni mgeni, labda ametokea mkoani kwa hiyo huyu huwezi tu ukamwachia auze vinginevyo watu watamzunguka huko nje na hatimaye matapeli watamuibia, ndiyo maana tunamkabidhi kwa dalali,” anasema.

Anasema dalali anapokabidhiwa mzigo na mkulima na kuuhifadhi anabeba jukumu la kuulinda, kuuhifadhi na hata kulipia ushuru. Ni jukumu lake kwa kuwa yeye ndiye muuzaji.

Ofiole anawashauri wakulima kuwaona viongozi wa masoko kabla ya kuwapa mzigo madalali. Anasema kosa wanalolifanya wakulima ni kukabidhi mzigo kwa dalali bila kuwa na hati ya maandishi, hivyo uongozi unashindwa kuingilia kati kwa sababu hakuna uthibitisho unao onyesha kuwa wawili hao walikabidhiana mzigo.

Wenyewe wajitetea

Dalali wa mbogamboga katika soko la Temeke Sterio, Amosi Kimbute, anasema wanachakifanya wao ni utekelezaji wa majukumu yao, kwani hata kama wasingekwepo bado wakulima wangelalamika.

‘’Ukweli ni kwamba bila sisi hawawezi kuuza mazao yao. Nasema hivyo kwa sababu madalali tuna mtandao mkubwa na tunajua wapi kuna wanunuzi na yupi mnunuuzi wa kweli,”anasema.

Kuhusu bei anasema ni suala la makubaliano kati yao na wakulima na hata wanapopanga wao madalali, lazima wawaulize wenyewe wakulima kama wameridhia au hawajaridhia.

“Sawa tunapanga bei lakini huwa hatulazimishi mtu kukubaliana na bei ile kama akikataa basi na mara nyingi wakikataa tukiwaacha wanaanza kulalamika na ku tubembeleza,”anaongeza.

Anasema kwa mkulima anayelalamika kutapeliwa basi amekutana na dalali ambaye hatambuliki katika soko, kwa sababu madalali wanajuana na wanahakikisha hakuna mkulima anayedhulumiwa.

‘’Unakuta mkulima analeta tikiti zaidi ya 2000 na unapomtafutia mteja dalali anachukua Sh200 pekee sasa hapo namdhulumu vipi?anahoji.

Naye Omari Othman ambaye ni dalali wa matunda katika soko la Buguruni, anasema madalali hawapangi bei ila wanapanga pamoja kati yao na mkulima.

“Kwa wale wanaokwenda shamba sawa lakini sisi wa sokoni inategemea ila mara nyingi bei tunapanga pamoja na mkulima na tunauza pamoja hadi pale matunda yatakapokwisha,”anasema Othman na kuongeza:

“Changamoto iliyopo ni kwamba wanunuzi wanachelewa kulipa fedha, lakini pia hata matunda yanayokuja mengine hayana viwango hivyo unakuta tunayagawanya katika madaraja. Sasa lawama zinakuja unapomweleza kuwa matunda yako yapo daraja la mwisho, hivyo unatakiwa kuuza kwa bei hii. Sisi huwa tunayagawa katika madaraja matatu yaani la kwanza la pili na la tatu”


Saturday, March 3, 2018

Mpe kuku chakula bora akupe faida

Chakula kwa kuku kama hawa, kinaelezwa kuchukua

Chakula kwa kuku kama hawa, kinaelezwa kuchukua asilimia zaidi ya 80 ya gharama za ufugaji. Kuwa makini na chakula. 

By Clement Fumbuka

Chakula cha kuku ni muhimu kuangaliwa kabla ya kununua na kulisha.

Tunajua kwamba makapi na masalia ya vyakula vya binadamu ndiyo hutumika kwa chakula cha mifugo.

Makapi haya hupatikana kutokana na kupembua nafaka, kukoboa au kukamua mafuta. Katika uchakataji wa mazao kuyafanya yafae kwa matumizi ya bunadamu, kuyaongeza thamani na kurahisisha utunzaji tunapata vyakula vya mifugo.

Mazao kama vile alizeti, pamba, mawese, karanga na mengine hukamuliwa na kutoa mafuta ya kupikia na kuacha makapi yake (mashudu) yakitumika kwa chakula cha mifugo.

Makapi haya kwa mifugo hutoa virutubisho aina ya protini ambayo hujenga mwili na kutoa kinga dhidi ya magonjwa. Mazao kama vile mahindi, mpunga, ngano na mengine hukobolewa na kutoa pumba ambazo ni chakula cha wanga chenye kutoa nguvu ya kukua na kwa mifugo.

Kwa kiasi kikubwa, mifugo wote ikiwamo kuku hutegemea mabaki haya ambayo kwa binadamu hayana lishe ya kutosha au pengine huenguliwa kutokana na tumbo la binadamu kukosa kemikali za kusaga makapi haya.

Tumbo la binadamu sio sawa na matumbo ya wanyama yenye uwezo mkubwa kusaga aina nyingi za mazao ghafi.

Kutokana na hatua hiyo binadamu hupata fursa ya kuhakikisha kila kitu chake hakipotei ikiwemo makapi ya vyakula yaliyoshindikana kwake, hivyo huyalisha mifugo na kuyageuza kuwa chakula chake tena baada ya kuliwa na mifugo. Hapa ndio tunapata nyama, maziwa na mayai.

Wafugaji wengi wanafahamu faida wanazopata kutoka kwenye makapi au masalia ya mazao ya mimea wakilisha mifugo yao, na wanaweza kusema vizuri zaidi kuliko makala haya yanavyoeleza.

Chaguo la kutumia makapi kulisha mifugo badala ya kutumia mazao halisi yanayoliwa na binadamu ni kutokana na bei nafuu ya kununua makapi hayo. Pili mifugo ina uwezo mkubwa wa kubadilisha makapi hayo kuwa nyama, mayai au maziwa.

Tatu kuepusha uhaba wa mazao ya chakula kwa binadamu na kuruhusu chenye thamani kitumike kwa ajili ya binadamu na chenye thamani ndogo kutumika kwa ajili ya mifugo.

Na hii ndiyo siri pekee inayotakiwa ya mkulima na mfugaji kuwa marafiki. Makapi ya mazao ni chakula cha mifugo lakini pia makapi hayo ni mbolea ya mimea ya mkulima shambani.

Hivi ndivyo tunavyotakiwa kuishi na kutembea pamoja katika kuzisaka fursa za maisha. “Kidole kimoja hakivunji chawa” leo tunajua thamani ya ufugaji imetokana na mchanganyiko wa mawazo mbalimbali ya wafugaji, wakulima na wadau wengine wakiwamo wataalamu wanaotoa miongozo kuinua sekta hii. Mtu aliyebuni kutengeneza chakula cha kuku na mifugo wengine alibuni kutumia malighafi yenye gharama nafuu, ili kupunguza gharama za uendeshaji. Katika ufugaji gharama ya chakula huchukua zaidi ya asilimia 80 ya gharama zote kwenye mradi wa ufugaji wa kuku na mifugo wengine.

Huduma ya chakula kwa kuku

Punguza gharama za ulishaji kwa kuzingatia mambo muhimu yafuatayo: Kwanza, mchanganyiko wa vyakula uhusishe makundi yote ya vyakula.

Pili, lisha kiasi cha chakula kinachotakiwa kulingana na umri wa kuku wako. Tatu, tumia makapi au mabaki ya mazao au vyakula yaliyo karibu nawe. Nne, chunguza mwenendo wa afaya ya kuku wako baada ya kuanza kutumia chakula kipya ukilinganisha na chakula cha hapo awali, uzito wa kuku na ukuaji wake huonekana haraka ndani ya wiki moja baada ya kubadilisha chakula kwa mifugo.

Katika makala zilizopita tuliona ni namna gani mfugaji anaweza kuanza kutengeneza faida yake tangu akiwa analea vifaranga.

Katika hatua hizo muhimu tuliona umuhimu wa kukinga magonjwa kwa chanjo na dawa tiba, lakini msisitizo ulikuwa juu ya chakula bora.

Chakula kinaweza kuwa bora lakini mfugaji akashindwa kupangilia namna ya kuwapatia kuku wake hivyo akakosa matokeo mazuri. Makala haya yamelenga kuonyesha mambo muhimu katika ulishaji ikiwemo kulenga kuku wote wakue wakiwa wamelingana.

Kuku wakipishana maumbo wakiwa chini ya wiki nane wataendelea kupishana hadi umri wa kuzalisha mayai au nyama, hivyo lisha kwa lengo la kuku wote wafanane ukubwa na uzito.

Kuku wa mayai malezi yao huishia wiki ya 18 hadi 19 na kuingia kwenye uzalishaji wa mayai. Wakati huo kabla ya umri huo mfugaji azingatie kuwa na vifaa vingi kiasi cha kuku wote bandani wale na kushiba kwa pamoja bila kupigana angalau kwa asilimia 90 ya banda wakue pamoja.

Kuku wakikua pamoja huanza kutaga pamoja na kufikia kilelele cha kutaga wakiwa na uwezo mkubwa sana wa kuzalisha na mfugaji kupata faida inayotakiwa.

Kuna shida kubwa katika malezi ya kuku na kipengele hiki, wafugaji wengi hawakijui au wanaokijua kipengele hiki hawakitekelezi kwa kina.

Unapoweka vyombo vya kulishia angalia kuku wakati wa kula utaona baadhi ya kuku wanahangaika kutafuta sehemu ya kulia lakini wanakosa kutokana na wenzao kujaa kwenye vyombo vya kulishia.

Kitendo hicho kikuongoze kujua kuwa unatakiwa kuongeza vifaa vya kulishia hadi hapo watakapokula wote kwa pamoja.

Anza na mfumo huu tangu kuku wakiwa vifaranga na kuendelea kuongeza vyombo kadiri wanavyokuwa hadi kutaga au kuwauza kama ni kuku wa nyama.

Pia weka vyombo vya maji vya kutosha na maji yakae muda wote. Kumbuka baada ya kula chakula kuku wanapenda kunywa maji huku wakistarehe. Usafi wa vyombo vya maji unatakiwa ili kuepusha maambukizi ya magonjwa.

Vifaa vyote vya chakula na maji vi-ning’inizwe usawa wa migongo ya kuku ili kuepusha kumwaga chakula na maji wakati wa kula na kunywa.

Mfugaji tambua kuwa chakula na ulishaji ndiyo mradi wenyewe na ndiyo faida yako. Chakula na ulishaji vinaweza kukufanya uendelee kufuga kwa faida au ushindwe kufuga


Saturday, February 17, 2018

Fursa hiyo kwa wakulima wa pilipili kichaa

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

Pilipili kichaa ni zao lililoanza kushika kasi ya mauzo na kufanya vizuri sokoni miongoni mwa mazao ya biashara katika soko la dunia.

Pilipili kichaa kutoka katika bara la Afrika maarufu kama ‘African Bird’s Eye Chilli’ ndizo zinazoonekana kupendelewa zaidi katika anga za kimataifa.

Cha ajabu ni kwamba wakulima wengi wa Tanzania hawajachangamkia fursa hiyo adhimu ambayo kwa sasa imefunguka zaidi barani Ulaya.

Mkurugenzi wa kampuni yaVegrab Organic Farming inayojihusisha na kilimo cha mboga mboga na matunda, Gladness Nyangi anasema soko la zao hilo lipo vizuri na sasa nchi za Ujerumani na Uingereza zimeonyesha uhitaji.

“Tuliona kuna fursa katika kilimo hiki lakini kabla ya kuanza tulifanya utafiti kujua ni wapi hasa tutapata soko na kuona kama mkulima atapata faida,”

“Matokeo yalionyesha kuwa faida ipo na kwa kuanzia soko la Kenya lilikuwa wazi; tukawaomba waje kutusaidia kutuelekeza namna ya kulima pilipili hizo kisasa hilo likafanyika sasa mambo yanakwenda vizuri zaidi,”

“Tatizo ni kwamba bado Watanzania wengi hawajaamka na kuona faida ambayo inaweza kupatikana kupitia kilimo hiki, ila ninachoweza kuwaambia kuwa kina manufaa makubwa na biashara nzuri,”anasema Nyangi

Mtaalamu wa kilimo wa kampuni hiyo Josephat Lingodo anasema bei ya pilipili kichaa kwa sasa imefikia Sh 4500 kwa kilo moja huku katika shamba la ukubwa wa ekari moja zinaweza kuvunwa hadi kilo 150.

Kwa mujibu wa Lingoda, shamba la ekari moja linaweza kupandwa miche 10,000 ya pilipili aina hiyo.

Anasema tofauti na wanavyofikiria wengi kuwa huenda kuna masharti makubwa kujiunga na kampuni hiyo, Lingodo anasema mkulima akishanunua mbegu anakuwa tayari mwanachama.

Anasema. “Mkulima akishakuja kununua mbegu kwetu tunaanza kumpatia mafunzo ya namna sahihi ya kulima pilipili zinazohitajika katika soko la kimataifa na tunakuwa tunafualia maendeleo ya zao hilo hadi pale linapofungashwa,”

“Wakulima wachangamkie fursa hii, soko lipo tayari kazi inabaki kwetu tunahitaji pilipili za kutosha hakuna namna ya kuzipata zaidi ya wakulima kujikita kwenye zao hilo, tukaachana na masuala ya kulalamika,”

Matumizi ya zao hili

Ingawa wengi hutumia pilipili kama kiungo kwenye chakula, yapo matumizi mengine ya zao hilo ikiwa ni pamoja na kutumika kama mojawapo ya malighafi ya kutengenezea dawa za kuchua misuli na dawa nyingine za hospitali.

Pilipili hutumika pia kama malighafi katika kutengeneza bidhaa za viwandani.

Unga unga unaotokana na pilipili kichaa unatumika katika utengenezaji wa mabomu ya machozi.

Lingoda anasema zao hilo pia ni malighafi katika rangi za midomo maarufu kama lipstick.

Faida za pilipili kichaa kwa afya ya binadamu

Pilipili kichaa ni zao lenye wingi wa vitamini A na limebarikiwa pia kuwa na virutubisho vya vitamini B, vitamini E, vitamini C, Riboflavin, Potassium na Manganese.

Virutubisho hivyo vyote vina manufaa katika mwili wa mwanadamu na ndiyo sababu ulaji wa pilipili hizi unatajwa kuwa na faida kiafya.

Ndani ya mwili wa binadamu zinafanya kazi ya kusafisha damu, kutoa sumu , kusisimua mzunguko wa damu na kuweka sawa uwiano wa tindikali(acid)mwilini.

Pilipili kichaa pia husaidia kufungua kwa haraka na kwa ufanisi pua zilizoziba kwa mafua na kukufanya upumue kwa urahisi.

Aidha, mlaji wa pilipili kichaa anajiondolea uwezekano wa kupatwa na saratani ya utumbo.

Kilimo cha pilipili kichaa

Zao hili lina sifa kubwa ya kuvumilia hali yoyote ya hewa ikiwamo ukame, joto na mvua za kiasi kati ya mililimita 600 hadi 1200 kwa mwaka.

Pamoja na sifa hiyo, mkulima unapaswa kuwa makini ukame unapozidi sana unasababisha kuanguka kwa maua hivyo ni muhimu kunyunyuzia maji.

Pilipili huhitaji joto la kiasi cha nyuzi 20 hadi 30 na udongo tifutifu wenye kiwango cha tindikali yaani Ph 6.0 hadi 6.5.

Zao hili linapaswa kuoteshwa kwanza kwenye vitalu kabla ya kuipeleka shambani. Tengeneza vitalu vya upana wa mita moja.

Tumia mbolea ya kinyesi cha ng’ombe au mboji

Weka mistari ya mbegu upana wa sentimita 10 kwa kila mstari hadi mstari.

Baada ya kuweka mbegu weka udongo kiasi na weka nyasi kutunza unyevu nyevu na mwagilia maji mara kwa mara.

Mbegu zikiota toa nyasi na nyunyizia dawa ya kuua wadudu, iache iendelee kukua hadi kufikia unene wa sentimita 2-3 kwa urefu sentimita 8-10 ndipo uipeleke shambani.

Ndani ya miezi mitatu zikiwa shambani pilipili zitakuwa zimebadilika rangi na kuwa nyekundu hapo zinakuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa na huvunwa mfululizo kwa miezi mitatu hadi minne.

Inashauriwa uvunaji huu ufanyike kila baada ya wiki mbili na haitakiwi kuvunwa pamoja na vikonyo vyake.

Changamoto

Lingodo anasema pamoja na mafanikio makubwa yanayotokana na kilimo hicho, uwepo wa wadudu waharibifu ni kikwazo kikubwa kwao.

Anasema kuna wadudu wadogo wadogo ambao ni nadra kuonekana kwa macho, wao hufanya kazi ya kuharibu maua ambayo yanategemewa kuzalisha pilipili.

Utitiri ni changamoto nyingine pamoja na uwepo wa wadudu wanaoshambulia mizizi.

Kukabiliana na changamoto hizo mkulima anashauriwa kupalilia mapema kukabiliana na na maficho ya wadudu ambao wanaonekana kwa macho.

Mkulima anashauriwa kabla ya kujitosa kwenye kilimo hiki awe na uhakika wa soko, hivyo ni muhimu kuingia mkataba wa makubaliano ili mazao yakitoka shambani moja kwa moja yaende sokoni.

Saturday, February 17, 2018

Malezi ya vifaranga wanaokua

 

Katika biashara hakuna mchawi zaidi ya huduma nzuri na usimamizi wa kutosha.

Shamba lolote au mradi wowote usipohakikishwa kwenye kipengele cha usimamizi, mambo mengine hayana nguvu kuleta faida kwenye mradi huo.

Mfugaji anaweza kuweka wasimamizi wa kumsaidia anapokuwa katika majukumu mengine, lakini ahakikishe anatembelea na kukagua mara zote kwani atagundua mambo mengi yatakayomuongezea akili ya kuboresha biashara yake na kumletea faida kubwa.

Makala hizi za ufugaji wa kuku hutoka kila mara na kuelimisha eneo fulani kwenye ufugaji, ni vizuri kwa mtu mwenye uthubutu kufanyia kazi kila kipengele kinachoongelewa.

‘Haba na haba hujaza kibaba’, usiache jambo la ufugaji linalozungumziwa hapa likupite kama unayo nia ya kufanya vizuri au kujiajiri kupitia ufugaji hasa ufugaji wa kuku.

Kimsingi, kila jambo linahitaji kuandaliwa vizuri ili kuleta matokeo mazuri. Kuandaa na kulea vizuri vifaranga wa kuku ni kuandaa mavuno mazuri ya mayai au nyama ya kuku baadaye. Waswahili husema ‘ ukitaka kuzitumia zichange kwanza, lakini mimi nasema ukitaka kufanikiwa kwenye biashara yako jipange kufanana na biashara yako kwanza.

Mtu anayetaka kuwa na ng’ombe wengi kesho anatakiwa kuwa na ndama wengi leo, sawa sawa na mtu anayetaka kuwa na mradi mkubwa wa kuku kesho anatakiwa kuwa na vifaranga wenye malezi bora leo.

Kila kitu ni kushawishika, usiposhawishika na malezi kwenye mradi wako hutashawishika na hatua ya uzalishaji mwishowe ni kusema haijakulipa Tuangalie mwendelezo wa malezi ya vifaranga wenye umri wa wiki nane na kuendelea baada ya kutazama malezi ya vifaranga wenye umri wa wiki sifuri hadi saba katika makala yaliyopita.

Tuliona namna gani vifaranga wanahitaji chanjo za mara kwa mara kipindi wangali wadogo, joto na chakula chao kuwa na ubora kuwapa kinga dhidi ya magonjwa na kukua kwa haraka.

Katika umri wa wiki nane au zaidi vifaranga hufikia hatua ya pili katika malezi na kuhitaji kubadilishiwa huduma za chakula, joto na tiba.

Katika umri huu vifaranga huitwa (growers) badala ya (chicks) walipokuwa na umri wa chini ya wiki nane.

Hapa mambo mengi hubadilika na vifaranga kuwa wamechangamka sana na kuonyesha tabia nyingi mbalimbali ambazo hapo awali hawakuonekana kuwa nazo.

Kwanza hutambuana kwa harufu na rangi ya manyoya kwa kila kifaranga aliyemo kwenye banda. Kila kifaranga hutambua kuwa ana uwezo hivyo huanza kutafuta utawala dhidi ya wengine na fujo nyingi hujitokeza mara kwa mara wakipigana bandani.

Hali hii husababisha vifaranga wadogo kupigwa na kunyanyaswa hasa wakati wa kula chakula.

Katika umri huu mfugaji awe makini tangu wiki ya kwanza ahakikishe kuna vifaa vingi vya kutosha vifaranga wote wapate chakula kwa pamoja na kukua wakiwa wote wana miili yenye ukubwa sawa ili hapo baadaye mapigano yakianza watatoshana nguvu na kuamua kuwa wapole na kuacha kudonoana au fujo zozote za wao kwa wao bandani hukoma.

Pili, nafasi bandani iwe ya kutosha wasibanane tangu wakiwa wachanga. Hali hii huwapa nafasi ya kustarehe na kukimbizana au kufanya michezo inayawajengea urafiki usioleta ghadhabu ya kudonoana kwa nia ya kutafuta uhuru wa nafasi.

Tatu, usichanganye vifaranga wenye rika tofauti waliopishana kwa zaidi ya umri wa wiki moja.

Kuwachanganya vifaranga wenye rika tofauti ni kusababisha vifaranga wadogo kupigwa muda wote bandani na kushindwa kukua vizuri au kufa kutokana na majeraha ya kudonolewa au kutoshiba.

Usichanganye vifaranga wenye rangi tofauti labda itokee vifaranga hao wamechanganyika tangu awali wakiwa hawajapata akili ya kubaguana.

Endapo umepanga kuchanganya vifaranga waliolelewa tofauti wachanganye usiku wakiwa hawana uwezo wa kupigana ili kufikia kesho watakuwa wameambukizana harufu na kuwa sio rahisi kutambuana na kupigana.

Pia hakikisha banda lako sio kubwa sana kiasi cha kuruhusu vifaranga wageni kujitenga sehemu yao na wenyeji sehemu yao kwani mapigano yataendelea.

Katika umri huu vifaranga hujifunza kila kitu ambacho hushindwa kusahau hadi wanafikia umri wa kutaga kama ni kuku wa mayai.

Tabia ambazo husababisha hasara kwa mfugaji hukomeshwa kwa namna mbali mbali ikiwamo kukatwa midomo ili kukomesha kudonoana na kuuana.

Ukataji wa midomo ufanyike kwa kuzingatia kanuni za afya kwa vifaranga, kwani vifaranga wanaweza kuvuja damu nyingi na kufa endapo mkataji atatumia mkasi, kisu au wembe.

Tumia kitu cha moto kukata na kuunguza mdomo dawa isivuje. Ikumbukwe kila tabia inayojitokeza kwa vifaranga husababishwa na kitu fulani ambacho mfugaji hakukigundua mapema.

Vifaranga wakibanana au kupungukiwa na lishe kwenye chakula husababisha kudonoana.

Mfugaji afuatilie kila hatua kwa kutoa huduma zinazotakiwa kulingana na umri wa kuku wake.

Mbali na huduma hizi kwa vifaranya wenye umri huu, chakula chao hubadilika kutoka chakula cha kuanzia (chickmash) na kupewa chakula cha kukuzia (growers mash).

Chanjo za mara kwa mara huachwa na kufuata kalenda ya chanjo ya kideri (Newcastle disease vaccine) ya kuku wakubwa ambayo hutolewa kila baada ya miezi miwili hadi mitatu.

Pia, katika umri huu vifaranga huanza kupimiwa chakula wanachokula kila siku kwa kipimo ambacho huongezwa kila wiki kulingana na umri unavyo kwenda na mahitaji ya mwili, ili wasinenepe na kujaa mafuta na kushindwa kutaga hapo baadaye.

Saturday, November 25, 2017

Mwaka wa kicheko kwa wakulima wa korosho

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaninki@mwananchi.co.tz

Msimu wa korosho ulioshia Februari mwaka huu katika mikoa ya Lindi na Mtwara, umeleta furaha kwa wakulima wa zao hilo.

Ndio maana haikuwa ajabu kuona utani katika mitandao ya kijamii ikionyesha vituko kadhaa vinavyofanywa na wakulima wa zao hilo. Yote ni kwa sababu wana fedha mifukoni.

Mwaka huu unatajwa kuwa msimu bora kuliko yote iliyopita baada ya mauzo ya bidhaa hiyo kupaa kwa zaidi ya mara mbili.

Hadi shughuli za minada zinafungwa… bei ya korosho katika mikoa hiyo ilifikia zaidi ya Sh 4000. Kicheko zaidi kilitokana na kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyesema hata kukiwa na makato kwa wakulima, mwishowe mkulima asiondoke na chini ya Sh3500 kwa kilo.

Kwa hakika kilimo cha korosho hasa mikoa ya Kusini, sasa ni kama lulu. Korosho ni mali, korosho inaweza kuwakomboa watu wengi na umasikini.

Tofauti na ilivyokuwa zamani, kilichowakatisha tamaa wakulima wengi wa korosho miaka ya nyuma ni utaratibu wa kuuza zao hilo katika mnada mmoja, huku kiwango kikubwa kikiuzwa kwa utaratibu usioratibiwa.

Hata hivyo, Serikali ilifuta machozi ya wakulima hao baada ya kuanzisha mfumo mpya wa mauzo ya korosho kwa kuendesha minada kila wilaya.

Aidha, matumaini ya wakulima pia yalikuja baada ya Serikali kupunguza baadhi ya makato yaliyokuwa yanakwenda kwa vyama vya ushirika kwa kuweka udhibiti unaoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia korosho kuuzwa kiholela.

Ushuhuda wa Hassan Yakub

Huyu ni mmoja wa wanufaika wa zao la korosho, anasema kwa faida aliyopata katika msimu uliopita, imempa nguvu ya kukipenda kilimo hicho.

Yakub anayefanya kilimo hicho huko wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, anasema alianza kulima mwaka 2016 akitumia shamba la kukodi lenye ukubwa wa ekari tano.

Wapo walioanza kilimo hicho miaka mingi kidogo hali iliyosababisha kukata tamaa kwa kutoona faida, lakini kwake ilikuwa kama bahati kwani hakutarajia kuwa angefaidika.

Baada ya mavuno kupitia ekari hizo alizokodi zikiwa na mikorosho, alijiongeza na kununua shamba lake mwenyewe lenye ukubwa wa ekeri 23.

“Asikwa ambie mtu hivi sasa kilimo cha korosho kina lipa, mimi nilianza na ekari tano tena kwa kujaribu tu Faida niliyoipata sikutaka kupoteza muda ndiyo maana nikanunua shamba langu mwenyewe,”anasema.

Kilimo cha korosho sio kilimo cha muda mfupi kama kwani zao hilo hudumu kwa miaka takriban mitatu na hiyo ndiyo sababu ya Yakub kujikita katika kilimo hicho

Anasema hana tena shaka na soko la korosho kwa kuwa kinachowaumiza wakulima nchini ni soko, hivyo analima akiwa na uhakika wa kuuza korosho zake.“Hivi sasa hatuna shaka na zao hili kwa sababu linasimamiwa kwa weledi na Serikali. Kwa kweli tunashukuru kwa kushikwa mkono kwani sasa tunaona matunda ya kilimo cha korosho,”anaeleza. Na kuongeza:

“Uzuri wa zao hili ukivuna inaanza kuzaa tena, kinachotakiwa ni kuihudumia kila inapohitajika, Ni zao la kudumu lakini uzaaji wake ni wa muda mfupi.

Kicheko cha korosho anacho pia Peter Majinzi aliyeanza kulima zao hilo miaka kumi aliyopita. Anasema tofauti na miaka ya nyuma hivi sasa kilimo cha korosho kupitia usimamizi wa Serikali kimeweza kuwafuta machozi wakulima wengi.

“Kwa bei hii sisi kwetu tunasema ‘Kusini kuchele’ hivi sasa tunauza kilo Sh 4000. Bei hii tunaifurahia na inatupa nguvu wakulima kuendelea kulima na kuongeza mashamba zaidi, mimi kwa msimu huu nimeuza gunia 30”

Anasema amefanikiwa kuongeza mashamba mawili na kufanya idadi ya mashamba yake kuwa matatu.

“Nilianza na ekari moja tu lakini kupitia manufaa niliyopata nimeweza kuongeza ekari nne zikiwa na mikorosho. Nina mikorosho 200 kwa mashamba yangu yote,”anasema.

Mambo ya kuzingatia katika klimo cha korosho

Ili mkulima apate mafanikio katika kilimo hiki, Yakub anasema hana budi kuwa na shamba analomiliki badala ya kukodi.

“Ili uwe huru na kilimo cha korosho mkulima, unatakiwa kuwa na shamba lako mwenyewe ambalo litakupa uhuru zaidi kwa kuwa zao la korosho ni la kudumu, kuliko kukodi halafu baadaye unarudisha shamba kwa mwenyewe,” anasema.

Jambo la pili anasema ni kutambua aina bora ya mbegu kati ya zile za kienyeji na za kisasa. Anapendekeza wakulima kuchagua mbegu za kisasa zinazochukua muda mdogo (karibu miaka mitatu) kuanza kutoa mavuno.

Uhudumiaji wa shamba hasa katika uwekaji wa dawa za kuua wadudu na magonjwa, ni suala jingine muhimu kwa mkulima wa korosho. Hata hivyo, huduma hii inahitaji utambuzi wa kitaalamu wa mbinu za kutunza shamba, madawa na upigaji wake katika miti.

“Mikorosho inatakiwa kuhudumiwa ili iweze kuzaa, Kuna upuliziaji wa dawa ili kudhibiti wadudu wasiharibu maua, bila kufanya hivyo mkulima hatoweza kupata mafanikio katika zao la korosho,” anaongeza.

Pembejeo bado tatizo

Kila penye mafanikio changamoto hazikosi, Yakub anasema pamoja na neema iliyowashukia mwaka huu, bado suala la upatikanaji wa pembejeo, linawapasua kichwa wakulima. Anasema kinachowatesa zaidi ni kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa bei zake.

“Bado Serikali haijaweza kusimamia bei, kwani kila muuzaji anauza kwa bei anayojiamulia yeye, hali inayotuumiza sisi wakulima,”anasema na kuongeza:

“Ni jukumu la viongozi waliopewa dhamana na Serikali kufahamu kuwa zile pembejeo walizosema tupewe bure je zinatufikia kulingana na idadi iliyopelekwa?’’ Changamoto nyingine ni pembejeo kutotolewa kwa wakati.“Unapomwambia mkulima kuwa unamletea ruzuku na inachukua muda mrefu hii ina maana kuwa mazao yake yatashambuliwa na magonjwa.’’

Wito wa kubangua korosho

Pamoja na changamoto hizo,Yakub anawasisitiza Watanzania kuingia katika kilimo hicho na hatimaye kubangua korosho badala ya kuziuza zikiwa ghafi.

“Mfano hivi sasa kilo moja ya korosho iliyobanguliwa ni sh 25,000 kwa soko la ndani wakati isiyobanguliwa kwa soko la ndani ni Sh 4000 hapa unagundua kuwa korosho ambayo haijabanguliwa haina thamani kama iliyobanguliwa,”anasema.

Zao la korosho Tanzania

Licha ya ukweli kuwa mikoa ya Kusini hasa Lindi na Mtwara ndio kinara wa zao hilo, zao hilo limeshafanyiwa utafiti na kubainika kuwa linaweza kulimwa katika mikoa kama Ruvuma, Tanga, Dodoma, Singida, Kigoma, Kilimanjaro na Mbeya.

Mkoa mwingine maarufu kwa zao la korosho ni Pwani hasa wilaya ya Kisarawe. Hata hivyo, wataalamu wanasema zao hilo linaweza kuzalishwa karibu nusu ya mikoa ya Tanzania.

Korosho ni kati ya mazao ya muda mrefu yanayostahmili ukame na kuzaa kwa miaka mingi.

Bodi ya Korosho

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Hassan Jarufu anasema baada ya kuona wakulima wengi wa korosho wanadhulumiwa kwa kuuza korosho zao kiholela, Serikali iliamua

kuingilia kati kwa kuagiza korosho zinunuliwe kwenye minada.

Anasema hiyo ndiyo sababu ya bei ya korosho kuwa nzuri kwa kuwa wanunuzi kutoka nchini Vitenam wanatufuata wenyewe tofauti na ilivyo mwanzo walipokuwa wakipelekewa na wafanyabiashara kutoka India.

“Zamani wakulima walidhulumiwa, kwani wanunuzi walikwenda shamba wenyewe na kununua kwa bei wanazotaka wao hivyo kusababisha wakulima kukiona kilimo cha korosho hakina thamani,” anasema”.

Miliki shamba lako sasa

Njia bora ya kufaidi matunda ya zao hili ni kuwa na shamba lisilipungua miti 100 yenye afya. Hii ni kwa mkulima mdogo. Kwa mikoa ya Kusini, unaweza kununua ardhi na kulima, lakini wapo wanaokodi mashamba yenye mikorosho.

Njia bora ya kupata maarifa ya zao hili ni kuwatumia maofisa kilimo karibu nawe, kuwauliza wazoefu wa zao hili. Pia, unaweza kupata tarifa za kina kutoka bodi ya korosho ( www.cashew@go.tz).

Kwa ushauri zaidi:0716508848

Saturday, November 25, 2017

Njia mbili za kulea kuku bandani

Mfugaji Saria Munisi wa Bomang’ombe mkoani

Mfugaji Saria Munisi wa Bomang’ombe mkoani Kilimanjaro, akiwahudumia kuku anaowafuga katika mabanda maalumu (cages). Hii ni mojawapo ya njia mbili za kulea kuku wakiwa bandani. Picha na Clement Fumbuka 

By Clement Fumbuka

Banda la kuku linaweza kulea kuku kwa namna nyingi. Leo tutangalia namna mfugaji anavyoweza kutumia banda kulea kuku kwa namna mbili.

Ukiondoa kanuni za ujenzi wa banda zinazoelekeza sehemu ya kujenga banda na vigezo vyake, ufugaji wa kuku kwa njia ya kisasa unafaa uzingatiwe katika matumizi ya banda.

Katika ufugaji wa kuku kwa njia ya kienyeji, kuku huenda bandani kulala wakati wa usiku, huku wakitumia muda mwingi kuzagaa nje wakitafuta chakula na maji wakati wa mchana.

Lakini ufugaji wa kuku kwa njia ya kisasa, kuku hukaa bandani muda wote wakipatiwa mahitaji yao yote bandani. Ni muhimu kuzingatia ujenzi wa banda na njia utakayotumia kulea kuku wako bandani. Faida ya ufugaji wa kuku kwa njia ya kisasa hutegemea matumizi ya banda lako.

Kulea kwenye sakafu

Njia ya kwanza katika matumizi ya banda kwa ufugaji wa kuku kwa njia ya kisasa ni kulelea kuku kwenye sakafu. Kuku kwa njia hii huishi kwenye sakafu iliyowekwa maranda au pumba ngumu ya mpunga. Kwa muda mrefu njia hii imezoeleka na inatumika mara kwa mara na ni teknolojia ya muda mrefu.

Ufanisi wake hutegemea vigezo bora vya banda kama vile nafasi ya kutosha ndani ya banda ili kuku waishi bila kubanana.

Vingine ni hewa safi na ya kutosha itakayofanya kuku wakue vizuri na kuzuia magonjwa au vifo vya mrundikano na kukosa hewa. Mwanga wa kutosha ili kuku wale na kunywa vizuri bila kuhitaji taa wakati wa mchana.

Pia, kuwapo kwa ukuta, milango, na madirisha imara ili kuzuia wizi na banda kutumika kwa muda mrefu bila kuharibika. Uelekeo sahihi wa madirisha ili kuwakinga dhidi ya mvua, jua na upepo.

Kuwe na sakafu imara iliyonyanyuliwa chini ili kuepuka kuku kuchimba mashimo ndani ya banda na hatimaye vimelea vya magonjwa kuathiri kuku mara kwa mara.

Njia ya mabanda maalumu

Njia ya pili ni ya mabanda maalumu maarufu kwa jina la ‘cages’. Kuku huwekwa kwenye banda wakiwa ndani ya waya uliotengenEzwa kwa vyuma. Waya huo unaweza kubebeshwa juu ya mwingine kitaalamu na kutengeneza mfano wa ghorofa kama makreti ya soda ndani ya banda.

Katika teknolojia hii, kuku huwa wasafi muda wote kutokana na kinyesi chao kudondoka moja kwa moja sakafuni bila kukikanyaga.

Pia, kuku hupewa chakula sehemu safi na kula chakula bila kumwaga. Mayai hutagwa na kujikusanya yenyewe sehemu moja. Njia ni bora zaidi katika kuepuka matatizo ya kuku kula mayai, kudonoana na kupatwa na magonjwa ya mara kwa mara.

Aidha, banda linaweza kulea kuku wengi mara nne hadi tano zaidi ya idadi ya kuku wanalelewa kwa njia ya kulelea kwenye sakafu.

Uzalishaji wa kuku kwa kutumia cages ni nafuu kwani mfugaji akifunga cages zake atazitumia kwa muda mrefu na gharama zake ni za kawaida kuliko kujenga banda.

Kwa mfano, mfugaji akijenga banda la kufugia kuku 100 kwa njia ya kufugia sakafuni, banda hilo hilo anaweza kufugia kuku wa mayai 450 kwa njia ya cages. Kufanya usafi kwenye banda la ‘cages’ ni rahisi kuliko kufanya usafi kwenye banda lililofugiwa kuku kwa njia ya sakafuni na kuwekwa maranda.

Mfugaji anaweza kutathmini kwa kulinganisha njia zote mbili ili kubaini tofauti zake katika gharama na faida kabla hajaamua kutumia njia mojawapo..

Ufugaji wa kuku ni biashara sawa na biashara nyingine zenye kuhitaji bidhaa iliyoboreshwa kuvutia wateja kutengeneza soko na hatimaye kuleta faida.

Katika ufugaji, ubunifu upo katika kutumia vizuri rasilimali kama chakula, maji, eneo, mtaji, utaalamu na nguvu kazi.

Matumizi mabaya au kutotumia ipasavyo rasilimali hizi ni kupoteza mapato katika biashara yako. Jambo lolote linahitaji mazingira fulani ili liende vizuri.

Ufugaji nao unahitaji kuandaliwa mazingira rafiki ili kupata mavuno mengi. Watu wengi huchukua mambo kwa historia kitu ambacho hakipaswi kuwa hivyo. Jambo zuri hutokea kutokana na usimamizi wenye kujali kila kipengele kinachohusiana na kuleta matokeo tarajiwa.

Mambo haya yaliyotajwa katika mwongozo huu wa ufugaji wa kuku ni mambo ya msingi kama tofali katika ujenzi wa nyumba.

Huwezi kujenga nyumba bila kuwa na matofali. Kadhalika huwezi kuzungumzia faida katika biashara ya ufugaji wa kuku bila kuzingatia matumizi bora ya rasilimali unazotumia kuendeshea biashara yako.

Banda la kuku ni sawa na shamba kwa mkulima. Mkulima hawezi kupanda mazao yake hewani lazima atahitaji shamba.

Kwa mfano huo mfugaji hawezi kufuga bila banda; lazima ajenge banda bora lenye vigezo kama ambavyo mkulima atatafuta shamba lenye rutuba nzuri ili kupata mavuno mengi.

Kuna aina nyingi za matumizi ya banda kulingana na mfumo aliojiandalia mfugaji. Banda linaweza kutumika kulingana na ubunifu wa mfugaji. Mabanda mengi hujengwa kulingana na mipango ya mfugaji.

Ramani ya banda na malighafi iliyotumika kujengea vina maana kubwa sana katika uzalishaji wa kuku. Mazingira ni kitu muhimu cha kutazamwa hasa mfugaji anapotaka kuchagua njia ya ufugaji wake.

Kwa kuwa faida ni kipaumbele cha mambo yote, kila kitu kifanyike kwa kulenga faida. Biashara yoyote inalenga kupata faida, ndiyo maana mfugaji anashauriwa kuwa na mazingira yenye kuleta faida katika biashara yake.

Mfugaji ahusishe wataalamu katika kubuni ramani ya mradi wake ili kuepuka gharama zinazoweza kuepukika.

Saturday, November 18, 2017

Mmea wa mchicha nafaka ni zaidi ya mboga

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Kama unafikiri majani ya mchicha ndicho chakula pekee, unakosea.

Mbegu zake zinaelezwa kuwa na virutubisho mbalimbali kwa ujenzi wa mwili wa binadamu.

Mtu anayetumia chakula kitokanacho na mbegu hizi, huwezi kumsikia akilalamika magonjwa ya aina mbalimbali wala maumivu; na yote ni kutokana na nguvu inayopatikana katika chakula hicho.

Taarifa njema kwa wajasiriamali

Mbegu hizi ni taarifa njema kwa wakulima nchini, kwa kuwa sasa wanaweza kulima mchicha siyo kwa minajili ya kuuza majani kama mboga, lakini pia kuuza mbegu.

Tangu mwaka 1995, mjasiriamali wa mkoani Dar es Salaam, Consolata Haule, amekuwa akijishughulisha na matumizi ya mbegu za mchicha nafaka kutengeneza bidhaa kama vile kashata, bisi, keki maandazi na bidhaa nyinginezo.

Amefungua kampuni maalumu iitwayo Jacoli inayojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mbegu za mchicha.

Kwa mujibu wa Consolata ambaye zamani alikuwa ofisa lishe serikalini, kabla ya kustaafu, mbegu za mchicha zina uwezo wa kuwasaidia wagonjwa wa saratani zote, kisukari, shinikizo la damu, ukimwi, wazee, watoto, wajawazito na wanaonyonyesha.

Ili kuona kama zinaweza kufanya kazi, alilazimika kufanya majaribio kwa wagonjwa ambao walimpatia matokeo yanayotia moyo kuwa walipata nafuu

“Watu wenye sukari walikiri kuwa ilishuka na kuwa kawaida, presha ikashuka na wazee waliokua wana maumivu ya misuli na miguu walipoitumia, walisema wamepata nafuu huku watoto wakiweza kukaa hadi miezi sita bila kuugua,” anasema.

Inaendelea uk 28

Inatoka uk 27

Anasema baada ya sifa na maajabu waliyopata wagonjwa, wateja waliweza kuongezeka ndani ya muda mfupi jambo lililomfanya kuongeza uzalishaji.

“Kutoka kilo mbili nilianza kusaga kilo 20 za mbegu za mchicha ili niweze kukidhi mahitaji ya wateja,” anaongeza.

Anasema anajivunia kuwa mtu anayeboresha afya ya jamii kwa kuwapunguzia magonjwa, huku akitumia biashara hiyo kuongeza kipato yeye mwenyewe na wakulima kwa jumla. Anasema hivi sasa kwa mwezi anaweza kutengeneza kiasi cha Sh 700,000 hadi 1,000,000.

Tiba ya magonjwa mengi

Kwa mujibu wa taarifa ya kitaalamu iliyomo kwenye blogu ya mazingiranp,

mchicha nafaka una vitamin E sawa na mafuta ya mzeituni, huku mmea huo ukiwa na uwezo wa kutibu magonjwa kama kisukari, magonjwa ya moyo, maumivu ya magoti, maumivu ya vidonda vya koo (mdomoni), baridi yabisi, minyoo aina ya tegu, kansa ya tumbo, maziwa, koo, mapafu, kupunguza uzee, magonjwa ya ngozi

Mengine ni kuzuia meno kupata kutu, shinikizo la damu, kuzuia mwili kufa ganzi, udhaifu wa misuli, lehemu,

Atoa mafunzo

Mwaka 2005 alipatiwa mafunzo kutoka Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) ya namna ya kuwafundisha wakulima faida za fursa zinazopatikana katika mchicha nafaka baada ya kuonekana ana uzoefu.

“Niliweza kutoa mafunzo katika maeneo ya Mbeya, Mufindi na Morogoro. Baada ya kuwafundisha wakulima waliomba niwe nanunua mbegu hizo ili wao wapate soko,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa wakulima wananufaika kwa sababu tangu mwaka 2010, kilo moja ya mbegu za mchicha imepanda hadi kufikia Sh5,000 kutoka 2,500 mwaka 1997 na hiyo ni baada ya wafanyabiashara wa Kenya kuanza kuzitafuta,” anasema.

Anasema kuongezeka kwa mikoa inayolima mbegu hizo kumepunguza changamoto ya upatikanaji wa malighafi kwa wafanyabiashara tofauti na hapo awali walipokuwa wakitegemea wilaya ya Same pekee kama mzalishaji mkuu.

Changamoto

Consolata anasema moja kati ya changamoto kubwa zinazomkwamish ni kukosa vibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA() na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambazo ni taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali vya ubora wa bidhaa.

“Niliwahi kupata wateja kutoka nje, mmoja China na mwingine Uholanzi wakiwa na uhitaji wa bidhaa hizi, lakini walishindwa kuchukua kwa sababu sikuwa na nembo ya TBS,” anaeleza.

Anasema masharti yaliyowekwa na TFDA kwa wajasiriamali ni magumu na hawawezi kuyamudu kutokana na mitaji yao kuwa midogo.

“Wao wanataka eneo utakalotumia kutengeneza bidhaa lisitumike kwa shughuli nyingine, lakini hiyo ni ngumu na hata wakisema tukatengenezee SIDO bado ni vigumu,” anasema Consolata.

Ulimaji wa mbegu za mchicha

Anasema mbegu hizo hutumia miezi miwili hadi kukomaa tangu kupandwa, hulimwa kiangazi na baada ya kuvunwa hupepetwa na kusafishwa.

Ili mtu aweze kulima mchicha nafaka, lazima atayarishe shamba mwezi mmoja kabla ya kupanda na kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri ili kuongeza rutuba ya udongo.

Mbolea hiyo hufanya udongo ushikamane vizuri na kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu. Kiasi cha ndoo moja ya lita 20 ya mbolea kinatosha katika eneo la mita moja ya mraba na baada ya kumwaga, udongo ni lazima uchanganywe na mbolea hiyo.

Wiki mbili kabla ya kupanda, lainisha tena eneo shamba lako kwa kupigapiga mabonge makubwa na sawazisha.

Kuna aina mbili za upandaji mchicha huu. Aina ya kwanza ni kupanda moja kwa moja na nyingine ni kupandikiza miche.

Upandaji wa mbegu

Kumwaga mbegu: Mbegu hupandwa katika shamba la kudumu kwa kumwagwa baada ya kuchanganywa na mchanga ilio kiwango sawa na mbegu ili kuweka urahisi na kuepusha mbegu nyingi kukaa katika eneo moja.

Baada ya wiki mbili hadi tatu, mimea hupunguzwa na kuachwa mmoja mmoja kwa nafasi ya sentimita 15 hadi 23 na inaweza kupandwa katika sesa au matuta.

Lengo la kuacha sentimita hizo kati ya mmea mmoja na mwingine, ni kuipa nafasi ya kuchanua na kuzaliana kwa sababu miche hiyo huwa na matawi makubwa.

Kiasi cha kilo moja hadi mbili za mbegu kinatosha kuotesha katika eneo la hekta moja.

Kuotesha miche: Kupitia njia hii, miche huoteshwa katika kitalu kingine kabla ya kuhamishiwa katika shamba la kudumu.

Baada ya wiki mbili au tatu, miche hiyo hupandwa mmoja baada ya mwingine kwa kufuata mstari kwa upana ule wa awali katika shamba ambalo tayari limekwishaandaliwa mwezi mmoja kabla.

Saturday, November 18, 2017

Fahamu ujenzi wa banda bora la kuku

 

Kuku wanahitaji sehemu nzuri ya kuishi na kukua vizuri.

Mfugaji wa kuku ana jukumu la kuhakikisha kuku wake wanaishi katika mazingira mazuri kiasi cha kutosha kufanya uzalishaji kwa faida.

Katika mchakato wa ufugaji kuku, ujenzi wa banda ni hatua muhimu na nyeti kwa kuwa inachangia katika uzalishaji wa kuku wako.

Kabla ya kufanya chochote mfugaji anatakiwa kujiridhisha kuwa banda lake linafaa au la.

Mfugaji yeyote mwenye uchungu na mifugo yake hawezi kukwepa kuwa na mahali salama kutunzia mifugo hiyo. Hivyo kabla ya kutoa fedha mfukoni kununua mbegu ya kuku, ni lazima uwe na uhakika na sehemu unayokwenda kuweka kuku wako.

Aidha, mfugaji anaweza kuchagua ufugaji kwa njia ya kienyeji ambayo kuku wanajitafutia chakula. Lakini bado akalazimika kuwa na banda la kuwatunza kuku wake wakati wa usiku.

Hitajio la banda kwa mfugaji yeyote ni la lazima bila kujali anafuga nini au anafuga kwa njia gani. Ieleweke kuwa kuku ni viumbe hai wenye mahitaji sawa na binadamu.

Mtu anayefuga kuku anatakiwa kujua bidhaa yake kuwa ni viumbe hai wenye mahitaji yote. Kama ilivyo kwa binadamu mwili wa kuku ukikosa hata moja kati ya mahitaji yake muhimu utaona upungufu kwenye ukuaji na uzalishaji wake.

Kwa kuzingatia hayo ni vizuri kutengeneza mazingira bora kwa kuku, ili kuepusha gharama za kuanzisha biashara isiyokuwa na faida.

Faida katika ufugaji hutegemea malezi bora kwa mifugo. Ukiondoa gharama nyingine kama vile matibabu, chakula, maji, katika ufugaji wa kuku, gharama ya kujenga banda hufanyika mara moja. Mfugaji akijenga banda imara hawezi kurudia kujenga banda lake kila wakati kama atakavyogharimia maji, umeme, chakula na dawa.

Gharama ya kujenga banda ikipita, imepita hairudi tena hadi mfugaji atakapopata wazo jipya kuongeza banda lingine kupanua biashara.

Kwa mantiki hii mtu akisema nataka kujenga banda ajue kuwa anafanya kitu cha kudumu sio leo na kesho kinaharibika. Na kama wewe ni mmoja kati ya wale wanaoona fursa katika ufugaji wa kuku hakuna sababu ya kuogopa kufuga.

Nakushauri itendee haki biashara yako kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya kuku wako, ikiwamo sehemu nzuri ya maisha yao bandani ili uone faida zaidi.

Sifa za banda bora

1.Sehemu ya kujenga banda: Chagua sehemu sahihi isiyo na vikwazo kufikiwa na huduma kama vile watoa huduma za maji, chakula, ulinzi, wanunuzi. Mambo haya na mengine yenye kufanana na hayo ni muhimu kuzingatiwa.

Epuka kujenga sehemu yenye kutuama maji utasababisha mafuriko ya maji bandani, unyevu nyevu wa mara kwa mara na magonjwa yasiyoisha hasa wakati wa mvua.

2.Uelekeo wa banda: Jenga banda pande za marefu ya banda zitizame Kusini na Kaskazini ili kuepusha tabu ya mvua, upepo na jua kupiga kuku bandani. Kitaalamu dunia hujizungusha kutoka Magharibi kwenda Mashariki na pepo huvuma kinyume na uelekeo wa dunia, hiyo pepo nyingi huvuma kutoka Mashariki kuelekea Magharibi.

Mvua hunyesha kwa kutegemea uelekeo wa upepo. Aidha, jua huchomoza Mashariki na kuzama Magharibi. Kama mfugaji atajenga banda lake marefu ya banda yakaelekea Mashariki na Magharibi ajue kuwa madirisha yake yataelekea Mashariki na Magharibi, hivyo mvua itanyesha bandani, upepo utavuma na kusumbua kuku.

Pia, jua litapiga bandani asubuhi na wakati wa jioni. Ili kuepukana na tatizo hili, ni vema mapana ya banda yatizame Mashariki na Magharibi na pasiwe na dirisha lolote kwenye mapana yote kuepuka adha ya mvua, upepo na jua.

3.Usalama wa kuku bandani: Hakikisha banda ni imara kuepusha wizi kwa kuvunja mlango, madirisha au kubomoa ukuta.

Mfugaji anaweza kutumia wavu imara kwenye madirisha, ukuta wa tofali au miti imara na kuezeka vizuri banda lisivuje wakati wa mvua.

4.Nafasi ndani ya banda: Jenga banda kulingana na wingi wa kuku watakao ingia na kuishi humo. Nafasi nzuri katika ufugaji wa kisasa ni: kuku wa mayai wanne kwa kila mita moja ya mraba. Kuku wa kisasa wanaweza kukaa watano hadi sita. 5 – 6.

Kuku wakijaa, hushindwa kula vizuri, hudumaa, kumwaga maji bandani, kupata maradhi mengi, kujenga tabia ya kudonoana na kushindwa kutaga vizuri au kula mayai kwa wale kuku wa mayai.

5.Hewa na mwanga: Kuku wanahitaji hewa safi na mwanga wa kutosha ili wakue na kuzalisha vizuri.

Mfugaji anatakiwa kujenga banda lenye madirisha makubwa na mengi ya kutosha ili hewa safi na mwanga vipate kuingia bandani. Kuku hutengeneza joto la wao wenyewe kutokana na kupumua wakiwa bandani.

Mbolea yao na majimaji wanapojisaidia au kunywa maji vinahitaji kukaushwa kwa hewa inayotoka nje na kuondoa harufu mbaya.

Banda lenye mwanga hafifu na hewa nzito, huwafanya kuku waugue mara kwa mara kutokana na vimelea wa magonjwa hupenda mazingira hayo. Banda lenye hewa safi ya kutosha na mwanga hupunguza gharama za kutibu kuku mara kwa mara.

6.Sakafu ya banda na urefu wake kwenda juu: Banda linaweza kujengwa kwa urefu wowote kwenda juu lakini lisipungue futi nane kutoka sakafuni hadi kwenye paa lake.

Sakafu yake inyanyuliwe kimo cha inchi sita hadi 10 kutoka usawa wa ardhi ili kuepuka maradhi kwa kuku. Udongo ni makazi ya wadudu wengi na vimelea vya magonjwa.

Kimo cha ukuta wa tofali kutoka sakafu hadi mwanzo wa madirisha kisizidi futi tatu, ili kuku wasionekane na mtu akiwa nje, huku ikiruhusu hewa nyingi na mwanga vipite.

Madirisha makubwa yenye wavu imara ni fahari katika ufugaji wa kuku. Usifunge madirisha kama nyumba ya kuishi. Madirisha yakae wazi usiku na mchana kwa kuku wakubwa.

Kwa vifaranga, madirisha yanaweza kuwekwa mapazia kupunguza baridi (inategemea na hali ya hewa). Sakafu ya banda isakafiwe ili kuku wasichimbe mashimo bandani. Pia, usitengeneze sakafu laini yenye kuteleza kama nyumba ya kuishi.

Saturday, September 23, 2017

Beatrice: Mrembo aliyeamua kushika jembe kukuza kipato

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Tofauti na vijana wengi wa rika lake, huwezi kuamini kwa ajira aliyonayo kama Batrice Haule angekuwa na hamu ya kujishughulisha na kilimo.

Umuonapo kazini au barabarani, mwonekano wake ni kama ule wa wanawake wengi wanaoijipenda ambao muda mwingi wanafikiria kuonekana warembo.

Lakini msichana huyu ana sifa ya ziada, siku za mwisho wa wiki au likizo, badala ya kupumzika nyumbani, yeye anatumia nafasi hiyo kusimamia miradi kadhaa ya kilimo anayoiendesha mkoani Ruvuma.

Beatrice mwenye umri wa miaka 28 anaishi Njombe na anafanya kazi katika shirika moja la kimataifa kama ofisa takwimu.

Pamoja na kuwa na ajira ambayo kwa baadhi ya watu ingetosha kumtuliza kimaisha, yeye anaamini katika dhana ya kuwekeza. Kwake maisha kama anavyosema; ‘’…ni kuwekeza, ni kupambana.’’

Ili kutekeleza dhana ya maisha ni kuwekeza akaamua kuwekeza mtaji wa akili na fedha zake kwenye sekta ya kilimo anayosema inalipa kuliko hata ajira rasmi. Anaamini kilimo ni zaidi ya ajira, kwani faida anazozipapata kutoka shambani ni kubwa mno

‘’Kwa zama hizi kama mtu anataka kufanikiwa katika maisha yake ni kilimo pekee. Kilimo ni fursa nzuri ambayo kijana anaweza kuifanya na kumpa mafanikio. ‘’ anasema na kuongeza:

‘’Kama upo kwenye ajira, hakikisha hiyo ajira yako iwe mbegu na anza kwa kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji. Mshahara haununui gari, mshahara haujengi nyumba, mshahara hausomeshi watoto shule nzuri, ila mshahara unaweza kuwa chanzo cha kufanya hayo yote.’’

Tangu mwaka 2015, Beatrice amekuwa akijishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali, na sasa anaendesha miradi yake mitatu ya kilimo na usambazaji wa maziwa aina ya mtindi.

Hii ni kwa sababu alibaini kuwa ajira pekee haitoshi kuendesha maisha yake.

Shauku ya kilimo

Zao la ufuta ndilo liloanza kumpa shauku ya kulima kama anavyosema:

“’Kwa mara ya kwanza nilianza kulima ufuta Chalinze mkoani Pwani, baada ya kuona mafanikio katika zao hilo nikaona kumbe fursa ipo kwenye kilimo,”, anasema.

Kwa kuwa kilimo kwake ni biashara, hakuridhika na zao moja la ufuta baada ya hapo aliongeza miradi mingine miwili ya mazao ya soya na tangawizi mkoani Songea.

INAENDELEA UK 28

INATOKA UK 25

“Mwaka jana nilipata taarifa kuwa kijiji cha Mkongo kuna ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo cha soya, sikutaka kupoteza muda nilikwenda kuona hali halisi baada ya kujiridhisha nikaanza na heka 20,”anasema.

Anasema mbali na ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo hicho alifanya utafiti kujua soko la soya na wateja wake. Baada ya hapo alilima akiwa na uhakika wa soko kwa asilimia 100.

“Kosa tunalolifanya sisi wakulima ni kulima bila kujua soko likoje; mazao haya ni ya biashara hivyo kabla ya kulima cha kwanza kujua ni soko na ndivyo nilivyofanya mimi” anaeleza.

Anasema sababu ya kulima zao zaidi ya moja na katika maeneo tofauti, ni kufanya kilimo kama sehemu ya biashara hivyo anaangalia mazao yenye faida na ambayo hata soko lake halisumbui.

Kwa zao kama soya ambalo hutumiwa na watu kama lishe na hata chakula cha kuku, wake soko kubwa anakouzia ni katika kampuni ya kutengeneza chakula cha mifugo ya Silverland Intrenation iliyopo iringa.

Mkulima hachoki

Kama ilivyo kawaida, mtafutaji hachoki, Beatrice aliamua tena kuongeza mradi mwingine kwa kulima zao la tangawizi hukohuko mkoani Songea katika kijiji cha cha Mkongotema kwa kulima heka moja pekee.

“Hili zao nilijaribu tu, kuna ndugu yangu mmoja alinieleza katika kijiji hicho tangawizi inakubali sana nikasema ngoja nikajaribu, kwa kweli sikutarajia mana zao limekubali hadi nikajuta kulima heka moja,” anaeleza.

Anavyomudu kilimo na ajira

Pamoja na kuwa mwajiriwa, lakini ajira yake haimzuii kufanya shughuli zake za kilimo, kwa kuwa hupangilia ratiba zake vizuri ili kilimo kisiathiri majukumu mengine ya kazi.

“Huwa naingia kazini asubuhi hadi saa nane mchana, hivyo kwa siku za wiki sipati muda mzuri wa kutembelea miradi yangu hivyo natumia vyema siku za mapumziko kwenda shambani, ‘’ anasema na kuongeza:

“Pia wakati wa likizo ndio muda mzuri kwangu kishirikiana na vijana wangu walioko shambani.’’

Changamoto

Kwa sasa mapenzi yake yameelemea kwenye kilimo, lakini kwa kuwa bado ni mwajiriwa, anajikuta katika mtanziko mkubwa wa kusimama miradi yake kiasi cha kufikiria kuacha kazi.

Kwa kuwa miradi yake ipo katika maeneo tofauti, anasema wakati mwingine anashindwa kuitembelea yote, kitu ambacho ni kosa kwa mkulima makini kama yeye.

“Raha ya miradi yako uwe nayo karibu, lakini inapokuwa mbali sina Amani, hivyo natamani siku moja nihamie katika mashamba yangu” anasema.

Ajivunia kilimo

Kwake kilimo sio tu kwa ajili ya kuvuna mazao mengi na kujipatia kipato. Anasema kupitia kilimo amejifunza mengi.

“Sasa hivi nimekuwa kama bwanashamba, kwani najua aina mbalimbali za dawa za kilimo,’’ anaeleza.

Anasema kipato anachokipata kupitia kilimo, asingeweza kukipata kama angetegemea ajira pekee. Kilimo hicho kwa sasa kimemwezesha kusomesha wadogo zake

“Asikwambie mtu hakuna njia nyingine ya mafanikio kama kilimo, yaani najivunia kutunza familia yangu kupitia kulimo lakini pia hata mahitaji yangu nayamudu sio kama zamani” anasema.

Kufahamiana na watu ni moja ya mafanikia kwa Beatrice, anasema kupitia kilimo amefahamiana na watu mbalimbali ambao hakutarajia kuonana nao ambao wamechangia mafanikio yake hasa kwa kutoa ushauri juu ya kilimo.

“Nimejenga jina kupitia kilimo hivi sasa ukiuliza Beatrice watakuambia yule mkulima, kwa hiyo jina limekua kupitia kilimo na sio cheo changu kazini” anaongeza.

Ndoto zake

Ukiondoa shauku ya kutaka kuwa mkulima mkubwa Afrika na duniani kwa jumla, Beatrice ana ndoto ya kuwasukuma wanawake kuingia kwenye kilimo.

“Nataka wanawake sasa waone kuwa kushika jembe sio ushamba, tusitegemee tu ajira ambazo hata kipato chake ni mara tatu zaidi ya kile kinachopatikana shambani”.

Aidha, anatamani kuwa mjasiriamali mkubwa kwani mbali na kilimo ana mradi wake wa kuuza maziwa mahala anapoishi.

“Katika hili nawaambia Wanawake wenzangu tusimame imara kwani tunaweza na tusikate tamaa mapema, tusichague kazi, hivi sasa kutegemea ajira pekee utachelewa kimaendeleo,’’ anasema.

Saturday, September 23, 2017

Sailo teknolojia bora ya kuhifadhi nafaka

Huu ndio mwonekano wa maghala ya kisasa

Huu ndio mwonekano wa maghala ya kisasa yaitwayo sailo yanayoweza kutumika kuhifadhia mazao ya nafaka na yale ya jamii ya mikunde. Picha na mtandao 

By Beatrice Moses, Mwananchi bkabojoka@mwananchi.co.tz

Hawalimi, hawana uwezo wa kulima wala kuvuna lakini wana afya njema.

Wakati wote wamenawiri kuliko hata wakulima hutumia nguvu kubwa kulima kwa ajili yao wanawiri.

Hawa ni wadudu waharibifu wa mazao ambao ni adui mkubwa wa wakulima. Hujineemesha kwa kushambulia mazao tangu shambani mpaka nafaka zinapohifadhiwa ghalani.

Wadudu hao ni pamoja na dumuzi na kiwavi chake wanaoathiri mazao kama mahindi.

Ni wazi kwamba wadudu hao na wengine wamekuwa wakisababisha mateso kwa wakulima wengi, licha ya juhudi za kuwadhibiti ambazo zimekuwa zinafanywa.

Pamoja na kuwepo viuatilifu ambavyo hutumika katika kuwadhibiti wadudu wasishambulie mazao shambani, bado wengine hufanikiwa kushambulia baada ya kuvunwa.

Sailo kama mkombozi kwa wakulima

Wadudu wharibifu wakiwa kero kwa wakulima kwa kuwapa hasara, wataalamu hawapo nyuma kuwasaidia wakulima. Wamekuwa wakijitahidi kubuni mbinu mbalimbali za kuwadhibiti wadudu hao.

Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na vifaa vya kiteknolojia vya kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa ikiwamo ghala la kisasa liitwalo Sailo.

Kwa mujibu wa kitabu cha Teknolojia za Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Nafaka baada ya Kuvuna kilichoandikwa na wataalam wa Wizara ya Kilimo mwaka 2013, kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi nafaka kwenye ghala bora kama sailo.

Wataalamu wanasema sailo ni maghala yanayojengwa kwa dhana ya kutokuwepo na mzunguko wa kawaida wa hewa ndani yake.

Hatua hiyo husaidia wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa kutoweza kustawi na kuharibu nafaka kwa sababu wanakosa hewa.

Wataalamu hao wanabainisha kuwa Sailo hujengwa kwa kutumia bati la chuma ngumu kisha kusiribwa kwa matofali ya kuchoma au ya saruji.

Hata hivyo, wanabainisha kuwa Sailo za bati hazifai kujengwa katika maeneo ambayo mabadiliko ya vipindi vya joto na vya baridi ni makubwa kwa sababu wakati wa joto bati linapata joto kwa haraka.

Aidha, wakati wa baridi bati hupoa kwa haraka na kupa

ta unyevu kwa ndani, jambo ambalo husababisha nafaka au mazao jamii mikunde iliyohifadhiwa kuoza.

“Lengo la uandaaji wa kitabu hiki ni kuelimisha jamii kuhusu teknolojia sahihi za uvunaji, utayarishaji, ufungashaji, usindikaji na hifadhi ya mazao ya nafaka baada ya kuvuna,” inaelezwa.

Wanabainisha kuwa uwezo mdogo na maghala duni yanayotumiwa na wakulima vijijini kwa kuhifadhi, huruhusu upotevu wa nafaka hadi asilimia 10

“Huu ni mwongozo kwa wakulima na wadau wengine, ili kuziweka bayana teknolojia sahihi na mbinu bora za kutunza baadhi ya mazao ya nafaka baada ya kuvuna ili kupunguza

upotevu,” kinasema kitabu hicho.

Wanaeleza kuwa wakulima wengi nchini huhifadhi nafaka kwa kutumia njia za asili kama vile vilindo, mitungi au vibuyu ambazo ni duni na husababisha upotevu wa nafaka kwa kiasi kikubwa.

“Pia hifadhi ya namna hii mara nyingi haikidhi mahitaji ya kaya, ili kuepuka upotevu wa mazao wakati wa kuhifadhi, hivyo ni muhimu kutumia maghala bora yanayokidhi mahitaji ya mkulima.

Faida za Sailo

Hupunguza gharama kwa mkulima kununua magunia kila mwaka. Hutumia nafasi ndogo ya eneo la kuhifadhi. Huzuia wadudu waharibifu na wanyama kama vile pannya kuharibu nafaka.

Ni nzuri kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya nafaka ambayo ni pamoja na mahindi, kunde, maharage na choroko. Lina sehemu ya juu ya kuwekea na sehemu ya chini ya kutolea nafaka.

Faida nyingine ni kudhibiti matumizi kwa kuweka kufuli, bei nafuu ili kumwezesha mkulima kumiliki na kuwa na usalama wa chakula. Linapatikana kwa ujazo mbalimbali kuanzia Kg250 hadi Kg 2000 kulingana na mahitaji.

Vyakula vya nafaka vinaaminika kuwa vinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu ikilinganishwa na mazao mengine ya chakula.

Inabainishwa kuwa iwapo wakulima wakiitikia wito na kutumia teknolojia hiyo ya kisasa ambayo imefanyiwa utafiti, vyakula vyao vitakuwa salama .

Mwitikio wa wakulima kuhusu teknolojia hii

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ulaya, wilayani Kilosa Julius Lumambo anaeleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipoteza sehemu kubwa ya vyakula baada ya kuvuna kutokana na kukosa elimu.

“Kuna wakati tuliwekwa kwenye mradi wa kuzuia upotevu wa nafaka,lakini hakukuwa na mwitikio mzuri kwa wakulima, pengine wengi hupenda kuuza muda mfupi baada ya kuuza,” anasema.

Anasema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwatesa wakulima wengi kwa njaa hasa inapozuka mabadiliko ya hali ya hewa, mvua ikiwa nyingi au ikichelewa kunyesha kwa wakati.

Mkulima Malekela Kayombo wa kijiji cha Malangali mkoani Iringa anaeleza kuwa anahifadhi mazao yake kwenye viroba.

“ Kuna watu wamepita kuja kutuelimisha kuhusu uhifadhi wa mazao kwenye Sailo, nimevutiwa nayo kwa sababu sitohitaji kunyunyuzia dawa kwenye mahindi au mazao mengine ya nafaka, jambo ambalo ni la kiafya zaidi,”anasema.

Kayombo anabainisha kuwa ameshindwa kuwa na kifaa hicho kwa sasa kwa sababu kinauzwa kwa gharama ya Sh190,000 ambapo ukubwa wake ni sasa na gunia 40, hivyo amejipanga kununua msimu mwingine wa mavuno.

Mkulima mwingine Laurian Mbale wa Kijiji cha Msolwa wilayani Kilosa, anasema kuwa kwa sasa amekuwa anahifadhi mazao yake kwa kutegemea kunyunyuzia dawa, lakini ana lengo la kununua kifaa hicho.

“ Natamani kununua kwa ajili ya kuhifadhi mahindi maana pamoja na kwamba nalima na mpunga, lakini wadudu wanashambulia zaidi mahindi ingawa huwa najitahidi kuhakikisha yamekauka vizuri lakini bado wanasumbua,” anasema Mbale.

Saturday, September 9, 2017

Mtunze mbuzi akutunze

 

By Flora Laanyuni, Mwananchi

Ufugaji wa wanyama kama mbuzi, kondoo, ng’ombe na wengineo, unalipa hasa ikiwa mfugaji atafuata kanuni na miongozo ya ufugaji kwa njia za kisasa.

Unapofuga wanyama kama mbuzi, una uhakika wa kutengeneza mfumo imara wa kukuingiza kipato. Unaweza kufuga mbuzi kwa ajili ya maziwa au nyama.

Lakini ili kujihakikishia una mfumo mzuri wa kuingiza kipato kupitia ufugaji wa mbuzi, matunzo ya wanyama hawa ni muhimu ili nao wawe na tija kwako kiuchumi. Makala haya yanaangazia baadhi ya vitu muhimu katika ufugaji wa mbuzi.

Ili kuwa na mbuzi wenye afya nzuri ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo:

Moja, chagua mbuzi ambao wanakabaliana na hali ya hewa na magonjwa kwenye ukanda wako. Hawa watahitaji matunzo kidogo ya kiafya.

Mbili, mbuzi ni lazima walishwe vizuri kulingana na mahitaji yao. Malisho bora na ya kutosha ni muhimu kwa

afya ya wanyama wote. Lishe hiyo ni lazima iwe ya kiasili kwa asilimia kubwa inavyowezekana.

Tatu, mbuzi wote wanahitaji kupata maji safi.

Nne, mfugaji lazima awe makini katika kupunguza kiasi cha minyoo, kwa kuweka banda la mbuzi katika hali

ya usafi. Hakikisha kuwa kihondi, matandiko na banda kwa ujumla ni safi na kavu wakati wote.

Tano, banda la mbuzi lazima liwe na sehemu ya malazi, mwanga, sehemu nzuri za kupitisha hewa na eneo la kutosha la kuzunguka. Ni lazima msongamano uepukwe.

Sita, mbuzi wanahitaji eneo la kutosha kuzunguka kwa uhuru. Mazoezi mfano kwenda machungani ni muhimu.

Saba, utunzaji wa mbarika: Ni rahisi sana mbarika kudhuriwa na wadudu na magonjwa. Dang’a (maziwa ya

awali) yanasaidia kulinda wanyama wadogo baada ya kuzaliwa katika wiki za mwanzo. Mbarika wanahitaji malazi, mazingira safi, maziwa ya kutosha, malisho mazuri ili kujijengea ulinzi wanapokua.

Nane, kukata kwato mara kwa mara na kutunza miguu ni muhimu kwa wanyama wote wanaocheua. Angalia kwato zote kabla na baada ya mvua na ukate kama ni lazima.

Tisa, kudhibiti wadudu. Udhibiti mzuri wa wadudu ni pamoja na ratiba nzuri ya kuchunga. Epuka eneo lenye tindiga na wape dawa ya minyoo mara kwa mara na kudhibiti kupe.

Kuchunga kijamaa kunaweza kuepukwa, vinginevyo kama jamii inafanya shughuli zao kwa karibu sana, ili kukabiliana na mazingira hatarishi.

Kumi, Chanja mbuzi wako kulingana na mapendekezo yanayotolewa katika ukanda wako ili kuepuka hasara

isiyo ya lazima. Chanjo hukinga wanyama vizuri kutokana na magonjwa ambayo kwa kawaida hayawezi kutibiwa.

Chunguza mbuzi wako

Kwa kiasi kikubwa, mbuzi husumbuliwa na wadudu na magonjwa sawa na kondoo na ng’ombe. Mbuzi huathiriwa zaidi na wadudu waliomo ardhini wakati wa kula. Pia, wanapata na kuathiriwa kirahisi na homa ya mapafu na kukohoa, hivyo kamwe wasiachwe kwenye mvua au nyumba isiyokuwa na nafasi ya kutosha, hewa na sehemu za wazi kupitisha hewa.

Dalili za kuumwa

Moja, mbuzi anakuwa amezubaa na asiyechangamka kama ilivyo kawaida, huwa na tahadhari, masikio na mkia

huanguka badala ya kuwa juu.

Mbili, hujitenga na wanyama wengine, na hajishughulishi na shughuli za wengine kama vile kula na kunywa, hupungua kwa kasi.

Tatu, Kinyesi kinakuwa si laini au unaweza kuona akiharisha.

Nne, mbuzi hukohoa, kutetemeka, au kupumua kwa haraka kuliko ilivyo kawaida.

Tano, mbuzi anakuwa na matongotongo au makamasi.

Sita, mbuzi hulala au kusimama katika mtindo ambao si wa kawaida.

Saba, manyoya kutokuwa katika mpangilio mzuri wa kawaida.

Nane, unaweza kugundua uvimbe au ugumu fulani mwilini mwake

Dalili za maumivu

Yafuatayo yatakuongoza kujua kama mbuzi wako ana maumivu; kulia, kuhangaika, kutafuna meno,

kutoa sauti kidogo au hafifu, hujigusagusa na kupiga mateke.

Tiba kwa mbuzi mgonjwa

Mnyama anayeumwa, lazima atibiwe mara moja. Kwa kawaida mbuzi huwa na msongo wanapoumwa na wanahitaji kusaidiwa haraka. Muone mtaalamu wa mifugo endapo una wasiwasi na anachoumwa mbuzi.

Mwache mbuzi mgonjwa apumzike kivulini, palipotulia na pasafi, na uhakikishe anapata maji na majani mabichi. Anaweza kupona haraka kama hatasumbuliwa.

Asilimia kubwa ya magonjwa na vifo vya mbuzi vinaweza kuzuilika.

Kwa maswali unaweza kuwasiliana na mtaalamu kwa simu: 0754 511 805

Makala haya ni kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org

Saturday, September 9, 2017

Teknolojia ya Aflasafe inavyoondoa sumu kuvu kwenye mazao

Mtafiti mshiriki wa sumu kuvu, Jacob Njela,

Mtafiti mshiriki wa sumu kuvu, Jacob Njela, akielezea jinsi teknolojia ya Aflasafe inavyofanya kazi kwenye mazao. Picha na Asna Kaniki 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Wakulima wengi hasa wa mazao ya nafaka, wanatambua namna wadudu wanavyosumbua mazao yao.

Mazao kama karanga, mahindi na yale ya jamii ya mizizi na kunde, mara nyingi wanalalamika mazao yao kushambuliwa na fangasi ambao huzalisha kemikali za sumu, maarufu sumu kuvu.

Hii ni sumu na watumiaji wasipochukua tahadhari, afya zao ziko shakani na pengine wanaweza kupoteza maisha.

Habari njema

Baada ya tatizo hili kuonekana kuwa kubwa kwa wakulima nchini timu ya wanasayansi kutoka Taasisi ya kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (Ukanda wa joto) (IITA, imeegundua teknolojia itwayo Aflasafe kama tiba ya changamoto hiyo.

Kupitia teknolojia hiyo, sasa mkulima anaweza kulima mazao yake huku akiwa na uhakika wa kuvuna yakiwa salama.

Wataalamu hawa wanatengeneza Aflasafe kwa kutumia mchanganyiko wa mtama mweupe , rangi ya bluu, gundi pamoja na fangasi asilia wajulikanao kama “A.flavus” ambao hawazalishi sumu na ni salama kwa mkulima.

Jacob Njela ni mtafiti mshiriki wa kudhibiti sumu kuvu kwenye mimea amesema teknolojia hiyo ina uwezo wa kupunguza sumu kuvu katika mazao kwa asilimia 80 hadi 99.

“Mwaka jana tuliijaribu katika wilaya za Babati, Masasi, Kilombero, Nanyumbu, Mpwapwa, Kilosa, na Kongwa na ikaleta matokeo mazuri na sasa tupo katika jaribio la pili,”anasema.

Anasema kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) wameongeza wilaya nyingine nne ambazi ni Chemba, Kondoa, Kiteto na Chamwino katika jaribia la pili la msimu wa pili.

Anasema kwa kuwa fangasi wanaotengeneza sumu kuvu huingia shambani kipindi mazao yanapotoa maua,hivyo ili kudhibiti wadudu hao wasiingie Aflasafe inapelekwa shambani wiki mbili kabla ya mazao kutoa maua.

Lengo la wataalamu hao kupeleka Aflasafe shambani mapema ni kutoa nafasi kwa fangasi hao wasiozalisha sumu, ya kuzaliana wakiwa shambani hapo ili wakue na kukomaa tayari kwa ajili ya kuthibiti sumu kuvu.

“Kwa kipindi hiki tuna uhakika kabisa kwamba sumu kuvu haitakuwa na uwezo kabisa wa kuingia shamba kwani hawezi kushindana na Aflasafe kwa chakula, kwa hewa na hatimaye watakimbia kwa kuwa hawatapata nafasi ya kuwepo shambani,” anaeleza

Njela anasema kwa mkulima mwenye ekari moja atapaswa kutumia kilo 10 tu za Aflasafe.

Sababu ya kugunduliwa teknolojia hii

Madhara makubwa yatokanayo na sumu kuvu ndio hasa sababu ya wataalamu hawa kubuni teknolojia hiyo ambayo itakuwa suluhisho la madhara hayo kwa wakulima lakini pia hata kwa wale ambao wanatumia mazao hayo kama chakula.

Anasema sumu kuvu haiathiri afya pekee bali hata soko kwa mkulima, mazao yaliyoshambuliwa na sumu kuvu hayafanyi vizuri sokoni hasa masoko ya nje kama vile Ulaya.

Mbali na soko la nje, Njela anasema hata hapa nchini ni vigumu kwa mkulima kupata kipato kwa kuuza mazao ambayo tayari yamekwisha shambuliwa na sumu kuvu.

“Teknolojia hii ya Aflasafe kama itatumika vizuri na kwa usahihi itamsaidia mkulima katika kudhibiti sumu kuvu ambao ndio adui wa maendeleo ya mkulima nchini kiafaya na kimasoko” anasema

Anasema lengo la teknolojia hii sio kibishara ila lengo ni kuona wananchi wanakuwa salama dhidi ya sumu hatari ambao wanaweza kusababisha magonjwa mbalimbali ya hatari ikiwemo kansa.

Anasema pia Aflasafe ikitumika vizuri itaweza kupunguza fangasi wanaozalisha sumu na itaongeza wale wasiozalisha sumu na wasio na madhara kwa mkulima na jamii kwa jumla.

Tamko la Serikali kuhusu Aflasafe

Beatrice Pallangyo ni Ofisa mfawidhi wa udhibiti wa visumbufu uvamizi wa mimea kutoka Wizara ya Kilimo, anayesema kama nchi itafanikiwa kupunguza sumu kuvu, itaboresha afya pamoja na kipato kwa wakulima.

Anasema teknolojia hiyo ya aflasafe itasaidia kupunguza hatari za sumu kuvu kufuatia kufanya vizuri katika jaribio la kwanza katika wilaya saba hapa nchini.

“Aflasafe imesajiliwa na inatumika pia katika nchi za Marekani, Nigeria na Kenya hivyo kwa kuwa sumu kuvu ni tatizo hapa nchini na sisi tupo katika hatua ya kusajili bidhaa hiyo ili iweze kutumika mashambani kama njia ya kudhibiti,”anasema na kuongeza:

“Katika kufanikisha hili, Serikali itafanya utafiti kupita katika maeneo yote yanayosumbuliwa na tatizo hili, ili kuwarahisishia kutambua mapema kabla ya kuanza kusambaza bidhaa hiyo,”.

Hii ni habari njema kwa wakulima Kwani kwa miaka kadhaa suala hili la sumu kuvu limekuwa likidhoofisha mazao yao pamoja na mifugo kwani nayo hufa kwa sumu kuvu.

Kama ilivyo ada, matumizi ya teknolojia bila elimu hayawezi kuleta mafanikio mazuri.

Pallangyo anasema kwa kuwa bidhaa hii imethibitika kudhibiti sumu kuvu, Serikali itaenda sambamba na kutoa elimu kwa wakulimu juu ya umuhimu wa Aflasafe.

Saturday, September 9, 2017

Kilimo hai kinahitaji mbolea za asili

Mbolea kama hii ya asali ndiyo inayotakiwa

Mbolea kama hii ya asali ndiyo inayotakiwa kutumika katika kilimo hai.Picha nma Mkulima mbunifu 

By Patrick Jonathan

Ni ukweli usiofichika kuwa watu wengi wangependa kutumia bidhaa za mazao yasiyozalishwa na madawa na mbolea za kemikali zinazotengenezwa viwandani.

Kwa walio wengi, suluhisho ni kutumia mazao yanayozalishwa kupitia kilimo hai.

Hiki ni kilimo kisichotumia madawa wala kemikali za viwandani. Bidhaa zake zinaelezwa kuwa ni bora maradufu ya bidhaa zinazozalishwa na mbolea za viwandani.

Lakini kilimo hiki kinafanyikaje? Ili uweze kufanya kilimo hai ni lazima uwe na mbolea za asili. Bila mbolea za asili huwezi kufanya kilimo cha aina yoyote kwa misingi ya kilimo hai.

Mbolea za asili zipo za aina mbalimbali au huweza kutengenezwa kwa njia mbalimbali na kwa kutumia malighafi kama vile samadi, majani ya kurundika na nyinginezo.

Baadhi ya mbolea za asili na njia za kuzalisha mbolea za asili ambazo mkulima wa kilimo hai huweza kutumia katika kilimo kwa ajili ya uzalishaji bora, ni pamoja na mabaki ya mazao, mazao funikizi, matandazo, samadi na mboji.

Mbolea za asili zina faida kuu mbili, moja huongeza na kushamirisha viumbe hai katika udongo na pia ni huru kwa maana kuwa mkulima unaweza kuotesha au kutengeneza mwenyewe nyumbani au shambani kwako.

Aidha, ikiwa utakuwa na mbolea nyingi kupita mahitaji yako, unaweza kuuza na kujipatia fedha.

Hata hivyo, baadhi ya mbolea za asili zinakosa kirutubisho muhimu cha kutosha cha fosiforasi ambayo mmea huhitaji kwa ajili ya kukua.

Lakini upungufu huu unaweza kufanyiwa kazi kwa kuongeza mimea yenye virutubishi vya fosifirasi kwa wingi.

Mabaki ya mimea

Mabua na majani ya baadhi ya mazao ni mazuri sana kwa matandazo. Stover kutoka kwenye mahindi na mtama huanza kuoza taratibu na hivyo hukaa juu ya ardhi kwa muda mrefu kidogo na kufunika udongo.

Aidha, mabua na majani ya mikunde yana wingi wa naitrojeni na huoza kwa haraka hivyo kuwezesha virutubishi kutumika kwa haraka kwa mimea itakayofuata kuoteshwa.

Mazao funikizi

Mazao funikizi yanahitajika kuoteshwa mapema yakiwa yanafaa katika mseto wa kilimo, hivyo kuwezesha kukua na kufunika udongo. Baada ya kuota, yafyeke na kuacha juu ya ardhi kama masalia kabla ya kuotesha zao kuu linalofuata.

Mazao funikizi jamii ya mikunde ni muhimu sana kwani yanakusanya

naitrojeni kutoka hewani na kuifanya kutumika kwa mazao mengine.

Nyasi na magugu

Unaweza kukata na kukusanya nyasi na magugu kutoka pembezoni mwa shamba au kutoka katika eneo lingine na kuyatandaza shambani kama matandazo.

Hata hivyo, kuwa na tahadhari usichukue nyasi au magusu yenye mbegu kwani baadaye huota na kusababisha kuwapo kwa magugu shambani.

Kupogoa majani kutoka kwenye miti na vichaka

Unaweza kupogoa majani ya miti na vichaka ulivyovikata kisha kuweka kama matandazo shambani.

Miti na vichaka jamii ya mikunde ni mizuri zaidi kwa kuwa ina kiwango kikubwa cha naitrojeni na unaweza kuvuna vichaka katika kipindi chochote cha mwaka.

Aidha, baadhi ya mimea huoza haraka wakati mingine ikichukua muda kidogo, hivyo ni muhimu kutumia aina mbalimbali ya mimea ili kupata mchanganyiko mzuri wa kufunika udongo na hatimaye uweze kuozesha mimea kwa haraka wakati utakapohitaji.

Kinyesi cha wanyama (samadi)

Samadi inayotokana na kinyesi cha wanyama ni mbolea nzuri katika kilimo hai. Ni muhimu unapokusanya mbolea hii kuiacha kwa muda wa miezi kadhaa ili iweze kuoza kabla ya kupeleka shambani.

Unapoitumia mbolea hii moja kwa moja baada ya kutoka kwa wanyama, unahatarisha mimea yako kwa kuwa mbolea mbichi ina tabia ya kuunguza mimea.

Unashauriwa kutumia samadi inayotokana na na kuku kama kipaumbele cha kwanza. Unapokosa samadi ya kuku, unaweza kutumia kinyesi cha mbuzi, kondoo na kinyesi cha ng’ombe.

Mboji

Hii inajumuisha mabaki ya vitu mbalimbali. Unaweza kutengeneza mboji kutokana na majani, magugu, samadi, majivu, mabaki kutoka jikoni au malighafi yoyote ya asili yanayopatikana katika eneo lako.

Wakati wa kutengeneza mboji, jaribu kutumia malighafi inayooza haraka na kuzalisha mboji mapema kama vile nyasi na majani.

Unaweza pia ukatengeneza mboji kwa kuweka malighafi kwenye shimo hasa katika maeneo yenye mvua kidogo au za wastani.

Makala haya ni kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu.www.mkulimambunifu.org

Saturday, September 9, 2017

Fuata hatua hizi kama unataka kulima kilimo chenye tija

By Abuu Mkono

Naomba katika safu hii leo tujifunze mambo ya msingi yanayoweza kukupa uhakika wa kupata mavuno katika shughuli zako za kilimo.

Kwa kawaida ikiwa mkulima utasimamia vyema kulikinga shamba dhidi ya wadudu na magonjwa pamoja na usimamizi mzuri wa uwekaji mbolea, una uhakika wa kupata mavuno mazuri.

Unaweza ukauliza itakuaje kama una mavuno mazuri lakini sokoni hali ni mbaya. Ninachotaka kukueleza ni kuwa kama una bidhaa bora, unao uhakika wa kurudisha fedha yako uliyowekeza katika mradi wako wa kilimo.

Kumbuka kuwa kilimo huwa na faida mara mbili au mara tatu ya fedha zako za mtaji kama utalima kisasa.

Kulima kisasa kunamaanisha mambo yafuatayo;

1.Kupima udongo

2. Kuwa na maji ya uhakika shambani

3.Una nguvu kazi ya kusimamia shamba yenye maarifa sahihi kuhusu kilimo unachofanya.

4. Unafuatilia kila hatua shambani kwako. Kwa mtu mwenye majukumu mengine kama vile wafanyakazi, wanapaswa angalau kila wiki watenge siku kadhaa za kuwa shambani.

5. Una ratiba nzuri ya upigaji dawa na unaifuata. Kumbuka ni kosa kuacha mimea ikiwa imeathiriwa kwa zaidi ya asilimia 60 kisha unakumbuka kuanza kutafuta tiba.

Hapa utakuwa unacheza mchezo hatari, kwa sababu kuna magonjwa kama ya virusi ambayo yakiingia shambani na ukachelewa kuyashughulikia, unaweza kupoteza mazao yako yote.

6. Una mtaji uliozidi na unaokutosha kwa ajili mradi wako wa kilimo.

7. Umenunua dawa na zenye sifa kwa ajili ya kuikinga na kuitibu mimea yako. Ununuzi huu lazima uende sambamba na mbegu bora.

Mazao bora huanzia katika ununuzi wa mbegu bora na zilizokingwa dhidi ya magonjwa.

8. Una mbolea ya uhakika na inayotosheleza mahitaji ya shamba lako. Mbolea inaweza kuwa zile za kiasili kama samadi, mboji na nyinginezo au hata mbolea za viwandani kama DAP na NPK.

9. Umefanya utafiti wa soko na kujua nguvu na udhaifu wake. Ni muhimu kujua muda mzuri wa soko la zao unalotaka kulima. Tembelea masoko na zungumza na wachuuzi, madalali na kila mtu mwenye taarifa kuhusu soko la zao hilo.

Hizi ni hatua muhimu za kufuata kwa mkulima anayetaka maendeleo na tija katika kilimo. Ukitekeleza haya, una uhakika mkubwa wa kufanya vema katika kilimo.

Lakini pia kumbuka kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kuwa yapo mambo yako nje ya uwezo wa kibinadamu.

Sababu ya mazao kuuzwa kwa bei ndogo

Nikiwa mtaalamu naweza kulielezea hili kwa kuangalia vipenegele vifuatavyo:

1.Kuwapo kwa mazao mengi sokoni

2.Kuuza mazao kwa madalali

3. Kuvuna mazao madogo na dhaifu (mazao yasiyokuwa na ubora)

Unavyoweza kudhibiti wadudu shamba

Nitawagawa wadudu hawa katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni wadudu wadogo kama vile mites na leafminor

Kundi la pili ni la wadudu wakubwa kiasi kama nzi weupe, nyigu na wengineo. Kundi la tatu ni wadudu wakubwa zaidi kama vile panya na hata ndege wanaingia katika kundi hili.

Wadudu hawa kwa pamoja wanahusika kwa kiasi kikubwa kupoteza thamani ya mazao yako na kuyafanya yakumbane na bei ndogo sokoni.

Kwa mfano, nyigu na nzi weupe wanaweza kuathiri matunda kama kama matikiti maji kwa kuyagonga mwishowe yanakosa umbile zuri na kutoa madoa meusi. Yakifika sokoni, bila shaka bei itapungua.

Makosa katika upigaji wa dawa

Baadhi ya wakulima hukosea kwa kuchanganya madawa na maji yasiyokuwa safi. Siyo kila maji yana sifa ya kuchanganywa na madawa.

Fuata maelekezo ya madawa kama inavyoelezwa na wataalamu, wauzaji au maelezo yaliyomo kwenye chupa za dawa.

Epuka kuchanganya dawa zaidi ya moja katika maji . Unapolazimika kutumia dawa tofauti, andaa dawa tofauti na piga kwa wakati tofauti.

Abuu Mkono ni mtaalamu wa kilimo. 0767359818

Saturday, August 26, 2017

Kilimo cha uyoga kinavyoweza kukuingizia kipato kizuri

 

By Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Umewahi kula keki ya uyoga? Je, unafahamu kama uyoga unaweza kukupa supu maridhawa ukafurahia chakula chako mezani?

Hivi sasa uyoga sio tena zao adimu, zao ambalo zamani wengi tulizoea kuona likijiotea tu. Hivi sasa uyoga unalimwa tena kwa njia za kisasa kiasi cha kuwa chanzo kizuri cha mapato kama ilivyo kwa mkulima Ruth Samwel.

Anasema alianza kulima zao hilo lenye virutubisho lukuki kwa afya ya binadamu tangu Mei mwaka huu.

Tofauti na aina nyingine za mazao, kilimo cha uyoga hufanyika ndani. Kwa Ruth yeye anatumia kibanda cha udongo kilichoezekwa na makuti kwani anasema uyoga haupatani na joto na hustawi sehemu yenye giza.

Kwa kupitia mifuko ya plastiki ambayo ndio mashamba yatumikayo kuotesha uyoga, huweka vimeng’enya ambavyo ni mahususi kwa ajili ya uyoga wake.

“Nikishaandaa vimeng’enya naviweka kwa muda wa wiki moja kwa kuvifunika vizuri ili visipate mwanga, baada ya hapo najaza kwenye mifuko yangu na hatua inayofuata ni kuchemsha kwa kutumia mvuke ili kuua bakteria”

Anasema vimeng’enya hivyo vyenye mchanganyiko wa majani makavu ya mgomba, taka zitokanazo na mbao, pumba za mahindi, pamoja na sukari, huchanganya na mbolea ya itokanayo na kinyesi cha kuku kwa ajili ya ukuaji mzuri wa uyoga.

“Inategemea na wingi wa mashamba yangu. Kwa mfano, yaliyopo sasa ni mashamba 500 hivyo natumia mbolea kilo tano. Kama mifuko ni 1,000 mbolea inabidi iwe kilo 10” anaeleza. Kwake kila mfuko mmoja wenye vimeng’enya ni sawa na shamba moja kama anavyoita yeye mwenyewe.

Anasema kilimo cha uyoga pamoja na kuwa ni cha kisasa, lakini kinaweza kutumiwa na mtu yeyote kutokana na njia zinazotumika kutotumia gharama kubwa.

INAENDELEA NUK 28

INATOKA UK 27

“Kilimo hiki nimejifunza ndani ya miezi mitatu tu, na kilichonisukuma kuingia kwenye kilimo hiki ni baada ya kuona wengi wanakidharau kwa kigezo kwamba watu hawapendi uyoga” anasema.

Baada ya kuona faida katika kilimo hicho, Ruth hakutaka kuingia katika kilimo kingine , alijikita moja kwa moja kama sehemu ya ajira kwake.

“Niliona kuwa wakulima nchini wanapenda kufanya vitu vya kufanana, mfano hivi sasa wakulima wengi wamejikita kwenye kilimo cha matunda kwa hiyo mimi nimetumia fursa hii kuwa tofauti,” anasema.

Ruth anayeendesha mradi wake Tuangoma wilayani Temeke, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, anasema uyoga aina ya aina ya ‘Mamama’ (Oyster mushroom) huchukua miezi miwili kuwa tayari kwa ajili ya kuwauzia wateja wake ambao ni wa jumla na rejareja.

“Nauza kilo moja kwa Sh10,000 na wateja wangu wa jumla hununua kuanzia kilo 10, huku wengine wakinunua bei ya rejareja kuanzia robo hadi kilo moja” anasema.

Anasema kupitia kilimo hicho sio tu amefanikiwa kufahamiana na wafanyabiasha mbalimbali na kumjengea mwanzo mzuri kibiashara, lakini uyoga unampatia kipato cha kuendesha familia yake.

“Kwangu mimi haya ni mafanikio pamoja na kwamba kilimo hiki sajakianza muda mrefu, lakini napata moyo wa kuendelea nacho kutokana na faida nipatazo,” anaongeza.

Faida ya uyoga kwa binadamu

Kila chakula kina umuhimu katika mwili wa binadamu, ndiyo maana wataalamu hushauri ulaji wa vyakula vyenye virutubisho ili kujikinga na maradhi.

Tofauti na vyakula vingine, uyoga una vitamin D nyingi ambayo hakuna matunda wala mbogamboga ambazo zinazoweza kufikia kiwango cha hicho.

Dk Sajjad Fazel ni mtaalamu wa dawa na tiba kutoka hospitali ya Sanitas jijini Dar es Salaam, anashauri jamii kujenga mazoea ya kula uyoga kutokana na faida zake kiafya.

Mbali na vurutubisho vipatikanavyo kwenye uyoga, anasema uyoga una madini mengi ya chuma, potashi na shaba.

Anasema mazoea ya kula uyoga mara kwa mara, huimarisha kinga ya mwili ambayo itasaidia mlaji kumkinga na magonjwa mbalimbali na kupitia vitamini D, mlaji ataimarisha ngozi yake na kuboresha mifupa.

Wito kwa Serikali

Anatoa rai kwa Serikali, pamoja na wataalamu wa afya kutoa elimu juu ya umuhimu wa kula uyoga kwani wengi hawana mwamko juu ya matumizi ya uyoga kiafya.

“Kama elimu itatolewa vizuri walaji wataongezeka, wengine bado wanadhani uyoga ni mimea inayojiotea, kwa hiyo wanatakiwa wajue umuhimu wa uyoga na faida zake kiafya na kiuchumi,’’ anasema.

Aidha, anaiomba Serikali kuunga mkono jitihada za wajasiriamali na wakulima wanaobuni mbinu mbalimbali za kilimo.

Anasema kama kilimo hiki kitapewa kipaumbele kina uwezo wa kumbadilisha mtu kutoka kipato cha kawaida hadi kipato cha juu.

‘’ Ikiwezekana Serikali ianzishe mashamba kwa ajili ya vijana ili kuepuka wimbi la vijana wasio na ajira,” anashauri.

Saturday, August 26, 2017

Tanzania kinara wa uzalishaji muhogo kiteknolojia Afrika

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha muhogo barani Afrika.

Muhogo ni muhimu kwa kinga ya njaa na biashara na pia hutumika kutengeneza chakula cha mifugo malighafi kwa viwanda.

Hata hivyo, kwa muda mrefu, wakulima wamekuwa wakishindwa kupata mazao ya kutosha, kutokana na magonjwa, hali ya hewa na uelewa mdogo wa mbinu za kilimo.

Uzalishaji wa wa zao la muhogo hapa Tanzania upo chini ya kiwango cha kimataifa, kwani wakulima hupata kati ya tani tano hadi saba kwa hekta ukilinganisha na uzalishaji wa kimataifa wa tani 10 kwa hekta.

Utafiti unaonyesha kuwa muhogo unaweza kutoa mazao kuanzia tani 20 hadi 50 kwa ekari kama kanuni za kilimo bora zikifuatwa na wakulima wakatumia mbegu bora za muhogo.

Kwa kuzingatia changamoto hizo, wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Mikocheni (Mari), wamefanya tafiti za uzalishaji wa muhogo zilizoleta matokeo mazuri na kusambaza kwa baadhi ya nchi za Afrika.

Mkuu wa kituo hicho na mratibu wa tafiti za bayoteknolojia nchini, Dk Joseph Ndunguru anasema kuna tafiti zilizokamilika na zimeshaonyesha mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi na sasa utafiti wa uzalishaji muhogo kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO), unaendelea.

Swali: Yakoje maendeleo ya utafiti mnaoufanya kuhusu zao la muhogo?

Jibu: Kwanza ieleweke kwamba tafiti hizi zina lengo kubwa la kupambana na magonjwa yanayosumbua zao la muhogo na kuongeza mazao.

Magonjwa makubwa yanayosumbua muhogo ni batobato na michirizi ya kahawia.

Tunachokifanya hapa ni kuzalisha mbegu zisizo na magonjwa na zenye ukinzani wa magonjwa.

Katika utafiti wetu wa kwanza tumesafisha mbegu za muhogo na kuzisambaza katika maeneo ya kanda ya Pwani, kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.

Swali: Mnazisafishaje mbegu?

Jibu: Kinachofanyika ni kuchukua kipande cha mche (tissue) kutoka kwenye shina au tawi kisha tunakiotesha kwenye chupa kikiwa na chakula maalum (media). Baada ya muda kipande hicho huchipua matawi na mizizi.

Baadaye mbegu hiyo huhamishiwa kwenye vitalu maalum kwa uangalifu ili hali ya hewa isije kuviathiri. Vikishamea kwenye udongo, tayari tunakuwa tumepata mbegu safi isiyo na ugonjwa. Njia hii inasaidia kuepuka magonjwa.

Swali: Kwa kuwa uzalishaji wa muhogo nchini umekuwa chini kwa muda mrefu, utafiti huu umeleta mafanikio gani katika uzalishaji?

Jibu: Kwanza umetusaidia kuepuka magonjwa sugu yaliyokuwa yakisumbua wakulima kwa muda mrefu. Pili, uzalishaji wa muhogo umeongezeka kutoka tani tano hadi tani 40 kwa hekta moja. Haya ni mafanikio makubwa katika kupambana na njaa nchini.

Swali: Mnawafikiaje wakulima ili wafaidike na teknolojia hii?

Jibu: Kama nilivyosema tumeshapeleka mbegu tulizosafisha katika kanda ya Pwani, kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini. Huko tuna vikundi vya wakulima vyenye mashamba ya mfano.

Kwa mfano, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, tuna vikundi 16 na kila kikundi kina wakulima 20, ambao tunawapatia mbegu zilizosafishwa.

Tunawaelekeza wakulima kupanda vipande 4,000 vya miti ya muhogo katika ekari moja. Baada ya miezi minane kila mche utatoa mbegu nyingine 20, kwa hiyo kila ekari moja itatoa mbegu 80,000 ambazo watasambaza kwa wakulima wengine.

Tumeziomba halmashauri kutenga bajeti ya kununua mbegu kwa vikundi vya wakulima ili wafaidi teknolojia hiyo.

Kanda ya Ziwa katika wilaya za Rorya na Butiama, tuna mashamba 18 ya kuzalishia mbegu kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima.

Wilaya ya Mbiga (Ruvuma) ilikuwa imeathirika na magonjwa, lakini sasa tuna vikundi 67 vya wakulima vinavyopata mbegu safi.

Swali: Je, katika utafiti huu mmepata uzoefu wowote kutoka nchi nyingine?

Jibu: Tanzania ndiyo tumekuwa chachu ya utafiti wa muhogo Afrika. Tumeshakwenda nchini Rwanda ambako pia tulikuta magonjwa ya muhogo yamewaathiri.

Tumetoa mafunzo ya uzalishaji wa mbegu safi na kuanzisha mashamba ya mfano. Kwa sasa wamepata mafanikio makubwa. Tumeshakwenda pia Zambia, nako tumeanzisha mashamba ya mfano na uzalishaji wa muhogo unaendelea.

Kwa sasa tumealikwa Afrika Magharibi kwenye nchi za Nigeria, Ghana, Benin, Togo na Burkina Faso. Kote huko wameshaona mafanikio yetu nao wanataka kuonja.

Tunashukuru mfuko wa Bill and Melinda Gates pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) wanaotusaidia katika tafiti zetu.

Swali: Ulitaja awali kuhusu teknolojia ya uhandisi jeni (GMO), hiyo nayo mmefikia wapi?

Jibu: Teknolojia hii ni ya uhakika zaidi kuliko hii ya sasa. Kwa sasa tuko kwenye hatua ya maabara tangu mwaka 2013.

Tunachokifanya ni kuchukua mbegu zilezile za kienyeji ambazo wakulima wanazipenda na kuziainisha kijenetiki. Ni lazima kuzitambulisha mbegu hizo kwa kutofautisha seli zake.

Lengo letu ni kuwashirikisha wakulima kwa kutumia mbegu zao kuliko kutumia mbegu mpya ambazo hawajazizoea; wanaweza kuzikataa.

Baada ya utafiti wa kimaabara unaoweza kutumia miaka mitano, tutaomba kibali cha kuendelea na majaribio shambani.

Lengo letu ni kufikisha tani 21 milioni za muhogo kwa mwaka badala ya tani milioni saba zinazozalishwa kwa mwaka.

Swali: Kuna changamoto gani mnazokumbana nazo katika tafiti hizi?

Jibu: Tatizo kubwa ni idadi kubwa ya wakulima tunaotakiwa kuwafikia ukilinganisha na rasilimali tulizonazo. Ndiyo maana tunaziomba halmashauri zisaidie kuwafikia wakulima.

Hata baada ya kuwawezesha wakulima kuzalisha muhogo kwa wingi, kumekuwa na changamoto ya masoko. Hapa ndipo tunapowaomba wataalamu wa viwanda na masoko waingilie kwa kufundisha jinsi ya kuchakata muhogo ili hatimaye wazalishe unga, biskuti, tambi na bidhaa nyinginezo.

Friday, July 21, 2017

KONA YA KILIMO : Mafuta ya nje yanaathiri soko la alizeti nchini

 

By Tonny Addams

Ukitaka kujua umuhimu na thamani halisi ya zao la alizeti, pitia mizania yetu ya biashara ya nje na ya kimataifa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Lipo utakalojifunza.
Zao hili lilipuuzwa  kwa kipindi kirefu kilichopita; licha ya ukweli kuwa  mahitaji ya mafuta ya kupikia au kukaangiza (edible vegetable cooking oil) yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kila mwaka kutokana na kuboreka kwa kipato na maisha ya Watanzania,.
Ni kwa sababu hii, wafanyabiashara na wasindikaji wa mafuta ya kuupikia wakapata mwanya wa kuagiza mafuta ghafi ya mawese  kwa kiasi kikubwa kutoka nchi za nje hasa  Indonesia na Malaysia ili kuziba pengo la mahitaji.
Mahitaji ya mafuta ya kupikia au kukaangiza hapa nchini kwa makadirio ya watu milioni 55  na kipimo cha matumizi ya kilo 11 za mafuta kwa mtu kwa mwaka, yanaweza kufikia tani 605,000 za mafuta ya kupikia kwa mwaka.
Matumizi hayo ni wastani wa vijiko viwili vya chai vya mafuta ya kupikia kwa mtu mmoja kwa siku. Wengi tunajua matumizi yao ni makubwa zaidi ya kiwango hiki kilichowekwa na wataalamu wa masuala ya lishe.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO), uzalishaji wa mbegu za alizeti ulikadiriwa kufikia tani milioni moja  mwaka 2013, ingawa takwimu za kilimo zilionyesha kiwango kikubwa zaidi.
Kwa ukamuaji wa mafuta wa kiwango cha lita 30 hadi 38 za mafuta kwa kila kilo 100 za mbegu za alizeti, uzalishaji wa mbegu kwa mwaka 2013 uliweza kutoa tani 380,000 za mafuta ya alizeti.
Ukweli ni kwamba, bado kuna kiasi kikubwa cha mbegu ghafi za alizeti zilizouzwa nchi za nje, hususan katika soko la India. Kwa hiyo, uzalishaji halisi wa mafuta ya alizeti ulikuwa chini ya makadirio hayo.
Kiasi cha mafuta ya alizeti kilichozalishwa hapa nchini kiliweza kutosheleza asilimia 40 tu ya mahitaji ya nchi. Asilimia 60 ya mahitaji ya mafuta nchini ilibidi yaagizwe kutoka nchi za nje ili kufidia pengo.
Utafiti mmoja wa FAO uliofanyika mwaka 2010 kwa awamu awamu mbili tofauti, ulibainisha kwamba iwapo fursa zote zilizopo nchini zitatumika kikamilifu na kwa tija ya hali ya juu, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani milioni 100 za mbegu za alizeti kwa mwaka.
 Kiasi hicho cha uzalishaji kingeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kwa uzalishaji wa mbegu za alizeti.
Tukirudi kwenye mizania yetu ya biashara ya nje katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, inabainisha kwamba bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilikuwa katika kundi la bidhaa 10 za juu katika orodha ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje  kwa thamani.
Katika mwaka 2011 kwa mfano, bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilishika nafasi ya 3 katika orodha ya bidhaa zilizo agizwa kutoka nje, na iligharimu Dola za Marekani milioni 274.6 baada ya mafuta ya petrol yaliyoshika mafasi ya kwanza, yakifuatiwa na ngano.
Mwaka 2012, bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilishika nafasi ya nne  katika orodha ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje na iligharimu Dola za Marekani milioni 247.7 baada ya bidhaa za mafuta ya petroli na magari mchanganyiko.
Unaweza kuendelea na orodha hiyo, lakini ukweli utabakia kwamba mafuta ghafi ya mawese kutoka nje, yamekuwa yakiligharimu Taifa fedha nyingi za kigeni kwa kipindi kirefu.
Tukiangalia upande mwingine,  uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini ni wa kiwango cha chini na umekuwa ukisuasua kutokana na changamoto mbalimbali.
Wadau katika sekta ya alizeti wamekuwa wakilalamika kwamba, kuondolewa kabisa kwa ushuru wa forodha katika bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese kutoka nje, na bidhaa hiyo ikiwa imeshapata ruzuku huko ilikozalishwa, kumeifanya shughuli nzima ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini kutolipa.

Friday, July 21, 2017

Mbeya, Tabora vinara wa kuzalisha kuku wa kienyeji

 

By Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam na baadhi ya mikoa, wakisikia kuku wa kienyeji wazo la kwanza mara nyingi ni huwa ni wale waliotoka Singida au Dodoma.

Sehemu kubwa ya wananchi hili wanaamini mikoa hiyo ndiyo inayozalisha kuku hao kwa wingi.

Hata hivyo, walichokuwa wanafikiri sicho. Mikoa hiyo haipo hata kwenye orodha ya mikoa 10 inayozalisha zaidi kuku wa kienyeji. Lakini Dodoma ina sifa tofauti ambayo ni kuongoza katika kuzalisha kuku wa kisasa.

Takwimu za utafiti wa kilimo kwa mwaka 2014-15 zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Februari mwaka huu zinaonyesha kuwa mkoa wa Mbeya ndiyo unaoongeza kwa kuwa na kuku wengi wa kienyeji ambao ni zaidi ya milioni 2.5.

Idadi ya kuku wa kienyeji waliopo katika mkoa huo uliopo nyanda za juu Kusini ni takriban mara mbili ya wale waliopo mkoani Dodoma ambao ni milioni 1.4.

Mbeya inafuatiwa kwa karibu na Tabora yenye kuku wa aina hiyo zaidi ya milioni 2.49.

Fursa muhimu

Uwepo wa idadi kubwa ya mifugo hiyo ni fursa ya kibiashara kwa wafugaji wa mikoa hiyo iwapo watatumia vizuri rasilimali hizo kujitangaza ili kujiingizia kipato.

Pia, kufahamika kwa mikoa yenye kuku wengi wa kienyeji, ni fursa ya soko kwa wafanyabiashara wa mifugo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, hasa kwa kuzingatia kuwa kuku wa kienyeji wanapendwa zaidi na watu kuliko wale wa kisasa.

Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya chakula na magonjwa uliofanyika Novemba, 2010 nchini Marekani, kuku wa kienyeji wana faida lukuki ikiwamo ladha nzuri tofauti na wale wa kisasa.

Ripoti ya utafiti huo unaoitwa kwa Kiingereza ‘Foodborne Pathogens and Disease study’ inaeleza kuwa nyama ya kuku hao ina kiwango kidogo cha sumu kwa kuwa hazitumii dawa nyingi za kuwakuza na pia haina mafuta mengi ikilinganishwa na wale wa kisasa.

Kuku wa kienyeji ni miongoni mwa vitoweo ghali jijini Dar es Salaam akiuzwa kuanzia Sh18,000 kwa kuku wadogo huku wakubwa wakiuzwa hadi kufikia Sh40,000.

Pamoja na Dar es Salaam kuwa na bei ya juu ya kuku, mkoani Dodoma kuku wa kienyeji huuzwa kati ya Sh9, 000 hadi Sh12, 000 bei inayoelekeana na ile ya mkoani Mbeya.

Kuku wa kisasa wa nyama huuzwa wa wastani wa Sh5,000 hadi Sh7,000 kutegemeana na ukubwa na uzito.

Lakini hali ni tofauti kwa kuku wa kisasa. Utafiti uliofanywa na Kevin Queenan na wenzie watano hapa nchini na Zambia na kuchapishwa mwaka jana, unaonyesha kuwa bei ya kuku wa kisasa inafanana kabisa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa sababu gharama za uendeshaji zinafanana.

Utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la kilimo liitwalo Utafiti wa Mifugo kwa Maendeleo Vijijini toleo la 28, (Livestock Research for Rural Development 28 (10) 2016), unaeleza kuwa sehemu kubwa ya kuku hao wa kienyeji wanafugwa kwa ajili ya kitoweo nyumbani na wachache hufugwa kwa ajili ya biashara.

Hata wakati baadhi ya mikoa ya Tanzania kuongoza kwa kuku hao wa kienyeji bado sehemu kubwa ya wafugaji wanafuga kienyeji zaidi jambo linalofanya wapate mavuno kidogo na yasiyo na afya imara.

Friday, July 21, 2017

Fuata kanuni hizi ufanikiwe katika mradi wako wa kilimo-1

 

By Abdul Mkono

Kilimo ni uzalishaji wa mazao kwenye mashamba. Kilimo kina maana pana inayojumuisha mifumo ya uzalishaji mimea, ufugaji wa wanyama na uvuvi wa samaki. Mara nyingi kilimo cha mimea kinakwenda sambamba na ufugaji wa wanyama.

Watu hupanda mimea na kuitunza hadi mavuno hasa kwa uzalishaji wa chakula cha binadamu na lishe ya wanyama, lakini pia kwa shabaha ya kupata malighafi mbalimbali zinazotumiwa kwa kutengeneza nguo za watu.

Kilimo biashara kwa sasa kimekuwa kikifanywa na Watanzania wengi. Wengi wakiwa ni watu wenye kipato na waajiriwa katika maeneo mbalimbali. Wapo wanaojiandaa kuanza, wengine wameshaanza, wengine wakiwa na uzoefu wa hali ya juu. Lakini wapo pia wanaolima kwa mazoea na wengine wakitaka kukiacha kutokana na kushindwa kupata faida ya kilimo chao.

Makala ya leo yanaangazia kanuni kadhaa muhimu ambazo ni mwongozo kwa mkulima anayetaka kulima kwa mafanikio.

Fanya kilimo cha umwagiliaji

Kwa sasa kuna tatizo kubwa la ukame, yaani unapanda mazao yako lakini mwishowe yanakauka au yanakosa afya nzuri, hali inayosababisha mavuno kidogo. Kulima kwa kutegemea mvua ni mchezo wa kubahatisha, hivyo wakulima wanapaswa kuhakikisha wana maji, tena masafi yasiyokuwa na chumvi nyingi kwa sababu chumvi inapozidi huathiri ukuaji wa mimea.

Lakini pia mmea huhitaji maji kutokana na ukuaji wake. Unapopandwa unahitaji maji mengi, unapoanza kukua huhitaji maji pia, unapotoa matunda ambayo huelekea kukomaa maji hupunguzwa; hili nalo mkulima anapaswa kujua.

Kwa ufupi kujua kiwango cha umwagiliaji katika zao lako shambani itategemeana na aina ya udongo, aina ya zao, ukuaji wa zao na urefu wa mizizi na hali ya hewa ya eneo. Kwa haya washirikishe wataalamu kabla ya kukurupuka kama wengine.

Wengi humwagulia maji asubuhi na jioni kimazoea bila kujali aina ya udongo mwishowe maji yanazidi na kukumbana na magonjwa ya fangasi. Hivyo kuna haja ya kujifunza na kufahamu ratiba sahihi yaumwagiliaji.

Pima udongo wa shamba lako

Wakulima wengi huingia katika kilimo bila kupima udongo. Hali hii huleta madhara makubwa hasa katika kupunguza uzalishaji. Mmea unahitaji virutubisho 16 ili uweze kukua. Katika virutubisho hivyo kuna ambavyo huhitajika kiasi kikubwa ambavyo ni naitrojeni, fosiforasi na potasiamu. Kutokana na umuhimu wa virutubisho hivi mkulima anahitajika aweke mbolea mara kwa mara ili aweze kuvirudisha kwa kuwa hupotea kwa kuchukuliwa na mmea kila anapolima.

Kwa mfano, ili uweze kuota na kuwa na mizizi yenye nguvu na shina lenye nguvu, fosiforasi huhitajika. Hapa ndipo tunapomshauri mkulima aweke mbolea ya DAP. Mmea ukiwa unakua unahitaji naitrojen wa wingi ili jani lisiwe la njano na kusababisha mmea kushindwa kutengeneza chakula chake.

Mmea huhitaji pia potasiam na kalshamu hasa katika kuukinga mmea na magonjwa lakini pia kusaidia tunda kutengenezwa na kuliepusha na kuoza kitako. Hivyo huwa tunashauri kuweka mbolea ya NPK kipindi cha ukuaji. Pia unaweza kuweka mbolea za asili mara kwa mara.

Pima udongo wako na uache kubahatisha katika kilimo. Huwezi kujua uchachu wa udongo (ph) kama hujapima udongo. Ukipima udongo utajua aina ya mazao ya kulima, kiwango cha mbolea na ratiba ya umwagiliaji.

Panda kwa vipimo sahihi

Mkulima anapoambiwa ekari moja ya mahindi inaweza kuingia miche 55,000 haamini hata kidogo. Mkulima utakuta ana ekari 10, lakini kiuhalisia utakuta amelima kama ekari nne au tano.

Hii ni kutokana na sababu muhimu ya kutozingatia nafasi za upandaji. Kila zao hapa duniani lina nafasi yake maalumu ambayo shambani inapaswa kuzingatiwa kwa malengo maalumu.

Kupunguza nafasi hizo elekezi au kuzidisha kunasababisha madhara makubwa hasa katika uzalishaji wa mazao, kudhibiti magonjwa hatari na ugumu katika kuhudumia shamba. Kumbuka miche ikiwa michache, mazao hupungua wakati wa mavuno.

Simamia kwa karibu mradi wako

Kuna mkulima mmoja mkubwa na aliyefanikiwa katika kilimo. Yeye huzingatia usimamizi wake shambani. Aliwahi kusema: ‘‘Pale pesa yako ilipo nawe uwepo la sivyo utaibiwa au itapotea.’’

Anachokisema hapa ni kuwa kama mkulima makini lazima uwepo siku zote muhimu za mradi wako kama vile wakati wa upandaji, uwekaji dawa, uvunaji,uuzaji na nyinginezo.

Wengi hapa tumekwama kwa sababu tunafanya kilimo kwa njia ya simu. Tunajisahau kuwa kijana wa kazi hajui maumivu ya pesa ya bosi wake. Kwa mfano, usipokuwepo anaweza asimwagilie maji, au anaweza kupanda kwa utaratibu usiokubalika.

Tafuta soko kabla hujalima

Ili mkulima afaidike na kilimo anapaswa kukumbana na bei nzuri sana sokoni ambayo itamsaidia kurudisha gharama zake za kilimo. Ikiwa bei itakuwa chini anapaswa kuhifadhi mazao yake mpaka bei itakapopanda. Hata hivyo, changamoto wanayokumbana nayo wakulima wengi ni kuharibika kwa mazao yao kwa muda mfupi.

Unashauriwa kufanya utafiti wa soko na muda mwafaka wa kulima ili usikumbane na kadhia niliyotaja hapo juu.

Jifunze kutambua pembejeo bora

Kushindwa kuchagua mbegu bora tayari ni dalili ya hasara katika kilimo, kushindwa kutambua dawa nzuri ya wadudu au ya ukungu hilo nalo ni kosa litakalosababisha kupata hasara kubwa katika kilimo. Hapa wakulima mnahitajika kudadisi ili kupata ukweli. Unapoona wadudu mfano inzi weupe unapaswa kujua dawa gani sahihi kwa kumuua mdudu huyo. Kukosea kujua dawa kwanza utapata gharama ya kununua dawa ambayo sio sahihi..

Friday, July 21, 2017

Fursa za masoko kwa wakulima wa papai

Mkurugenzi wa  kampuni JOG Agri-consult and

Mkurugenzi wa  kampuni JOG Agri-consult and Solution ya jijini Dar es Salaam, Grace Mzoo akiwa katika shamba la mipapai. Na Mpigapicha wetu 

By Mwandishi wetu, Mwananchi

Kilimo cha matunda kimekuwa kikiwavutia Watanzania wengi. Mojawapo ya mazao yanayopendwa kwa sasa ni kilimo cha mipapai.

Achilia mbali virutubisho vingi vinavyopatikana katika mapapai katika kuboresha afya ya binadamu, wengi wanataka kuwa wakulima wa zao hili kwa sababu ni moja ya mazao yasiyochukua muda mrefu kuvuna.

Ni zao unaloweza kuvuna kuanzia miezi sita kwa uchache tangu kupandwa na hata sokoni bei yake inatia matumaini.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha wanaovutika na kilimo hiki wanakosa taarifa sahihi hasa kuhusu maarifa ya kilimo chenyewe, menejimenti ya kilimo na masoko.

Kwa sababu hii, baadhi ya wadau wa kilimo ambao ni wataalamu wa mazao ya mbogamboga na matunda, wamebuni mkakati wa kuwasaidia wakulima wa papai wakiamini zao hilo pekee linaweza kuwatoa wengi kutoka katika umasikini.

Wataalamu wa kampuni ya JOG Agri-consult and Solution ya jijini Dar es Salaam, wanasema kwa sasa wana masoko mkononi. Kinachohitajika ni wakulima kujitokeza kwa minajili ya kupewa maarifa na hatimaye kunufaika na kilimo cha mipapai.

Mwandishi wetu amefanya mahojiano na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Grace Mzoo anayesema kilimo cha papai ni utajiri tosha ikiwa wakulima watakuwa tayari kufuata kanuni za kisayansi zinazoendesha kilimo cha kisasa.

Swali: Unawezaje kuwahakikishia Watanzania kuwa zao hili linalipa kwa maana ya kuwaingizia kipato kizuri?

Jibu: Nathibitisha kuwa kilimo cha papai ni utajiri mkubwa, kwani mahitaji yake kwa masoko ya ndani ni makubwa kwa matumizi ya kula na kusindika. Acha nionyeshe namna unavyoweza kupata fedha nyingi kupitia kilimo hiki.

Katika eneo la ekari moja ukizingatia vipimo sahihi unaweza kupanda miche 800 hadi 1000,ambayo ina uwezo wa kuzalisha matunda 100,000. Ukiamua kuuza kwa bei ya chini ya Sh 500, utakuwa na kiasi cha milioni 50 kwa mwaka mmoja. Kumbuka zao hili linakaa kwa muda wa miaka mitatu shambani.

Watanzania tujaribu kutafakari namna gani tunaweza kuuondoa umaskini kwa kuheshimu kilimo kama sehemu ya utajiri.

Tuache kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa ya msingi, bali tujikite kwenye kilimo maana kuna fedha nyingi kulinganisha na biashara nyingine hapa duniani.

Swali: Zao hili siyo geni, wakulima wamekuwa wakilima kwa muda mrefu, pengine wanakosea wapi kiasi cha kutofanya vizuri?

Jibu: Wakulima wengi hawafanyi kilimo biashara, wanalima kwa mazoea, kwa maana hawatumii mbinu bora za kisasa kuzalisha mipapai.

Mbinu hizi ni kama upimaji wa udongo, uandaaji mzuri wa shamba, matumizi ya mbegu bora, matumizi mazuri ya mbolea yanayozingatia aina ya mbolea na wakati mzuri wa kutumia. Pia, matumizi ya madawa ya kuua wadudu na kudhibiti magonjwa.

Swali: Kuna madai kuwa zao hili halina soko, hivyo wengi wanalikimbia?

Jibu: Ni kweli zao hili halipo kwa wingi sokoni kutokana na Watanzania kutoelewa umuhimu wake mwilini na virutubisho vinavyotokana na papai. Pia, kuna hofu ya wakulima kuogopa kuzalisha kwa kuogopa masoko.

Swali: Umesema mna mkakati wa kuwasaidia wakulima wa zao hili, ni upi huo?

Jibu: Tunatangaza kuwa masoko ya zao hili tunayo mikononi mwetu. Soko lililopatikana ni la nje na zinahitajika tani nyingi,hivyo kama kampuni tunawakaribisha watu wa kuanza nao.

Kwa Tanzania tunahitaji wakulima 300 ambao tutaanza nao awamu ya kwanza. Papai zinazohitajika ni zile ambazo tutakushauri kuzilima maana tumepewa masharti ya hizo aina za papai. Pia, kilimo tutakachokifanya ni kilimo hai kwa maana ya kuwa hatutatumia kemikali za viwandani.

Kwa kupitia mpango huu wa kilimo biashara, zipo fursa za mazao mengi ukitoa papai, ila tumeanza na papai kwa maana soko lake limeshapatikana,hivyo kadri tupatapo masoko tutakuwa tayari kuwapa fursa Watanzania wenzetu.

Swali: ukoje utaratibu ikiwa mkulima atahitaji kufanya kazi na nyinyi?

Jibu: Mkulima anapotaka kufanya kazi na sisi ni lazima akubali taratibu zetu zikiwamo kujisajili kwenye orodha, akubali kukaguliwa miradi yake na kusimamiwa na timu ya wataalamu wetu na akubali kusaini mkataba wetu wa masoko.

Mhariri: Wataalamu hawa wanapatikana kwa simu 0715500136 /0768279408.