Friday, February 9, 2018

Mambo yatakayofanya uipende zaidi kazi yako

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Upo uhusiano mkubwa kati ya furaha na utendaji wako wa kazi. Unapofurahia kazi unayoifanya, utafiti unasema kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuzalisha zaidi, utakuwa na uhusiano mzuri zaidi na wafanyakazi wenzako na pia utajivunia kile unachokifanya kuliko mwenzako anayefanya kazi asiyoifurahia.

Mojawapo ya sababu za utendaji mbovu wa baadhi ya wafanyakazi kwenye taasisi za umma na zile za binafsi ni watu kufanya kazi wasizozifurahia.

Kutokufurahia kazi kunaweza kutokana na sababu mbalimbali kama uchaguzi mbaya wa kazi na mazingira mabovu ya kazi. Hata hivyo, bado unaweza kujifunza kuipenda kazi yako kwa kuelewa mambo matano tunayoyaangazia kwenye makala haya.

Unahitaji kuona unavyofikia malengo. Kufikia malengo kunachangia kukufanya uwe mtu mwenye furaha zaidi. Hili linawezekana ikiwa utaelewa ni malengo gani unajaribu kuyafikia kupitia kazi yako.

Ili kuona unavyofanikiwa kupitia kazi yako, jenga tabia ya kujiwekea malengo madogo unayoweza kuyafikia ndani ya muda mfupi. Kwa mfano, unafanya kazi ambayo matokeo yake yataonekana baada ya mwaka mzima, jiwekee malengo madogo madogo yanayoweza kupimika kila baada ya juma moja.

Kadiri unavyoona ukifikia malengo hayo, ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kufurahia kazi yako kuliko mtu anayefanya kazi asiyoona matokeo ya kazi yake.

Kwa kulielewa hili, mwajiri unaweza kuwa na utaratibu mzuri unaomwezesha mfanyakazi kupima utendaji wake kwa kipindi kifupi. Usiache mfanyakazi wako afanye kazi bila kuona matokeo yake kwa muda mfupi.

Unahitaji mfumo wa motisha

Motisha ina nafasi kubwa ya kukufanya uwe mtu mwenye furaha. Kwa hakika ni vigumu kuipenda kazi isiyokupa motisha.

Kupitia kutambuliwa kwa juhudi zako kwa maneno, vitendo, nyongeza ya mshahara au hata kupandishwa cheo, unaweza kuwa mfanyakazi mwenye furaha zaidi.

Inawezekana taasisi unayoifanyia kazi haina mfumo mzuri wa kutambua kazi unayoifanya kama mfanyakazi.

Hata hivyo, mara nyingine, hiyo haimaanishi hujafanya kazi kwa kiwango kinachotaiwa. Kuna uwezekano kuwa mwajiri wako hajajua tu umuhimu wa kukupa mrejesho.

Usisubiri kutambuliwa.

Unaweza kujipa motisha mwenyewe kwa kuangalia maeneo ambayo kazi yako inayagusa.

Mfano, angalia vile kazi yako inavyogusa maisha ya watu wa hali ya chini, hatua ulizopiga tangu umeanza kazi yako. Kupitia mambo kama hayo, unaweza kupata kiwango kikubwa cha motisha kuliko kile ambacho ungekipata kutoka kwa mwajiri.

INAENDELEA UK 24

Wapende wafanyakazi wenzako

Wafanyakazi wenye mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzao wanakuwa na uwezekano wa kuwa na furaha mara tatu zaidi ya wale wasioelewana na wenzao.

Aidha, unapokuwa na mahusiano ya karibu na wenzako unajiongezea asilimia zaidi ya 50 za kupata utoshelevu wa kazi yako.

Christine Carter, mwandishi wa kitabu cha The Sweet Spot: How to Find Your Groove at Home and Work aliwahi kuandika, “Katika kazi yoyote, mahusiano na watu ni kiashiria muhimu cha namna wafanyakazi watakavyofurahia kazi.”

Jenga tabia ya kuwa karibu na wenzako. Tafuta fursa za kushirikiana nao nje ya pilika pilika za ofisi. Kwa maneno mengine, usiwe mtu unayevaa sura ya kazi muda wote.

Tumia sehemu ya muda wako kuongea na wenzako, kufahamiana na wenzako nje ya maisha ya kazini.

Sasa unaweza kusema, mimi sina uwezo wa kujenga urafiki na watu. Ukweli ni kwamba sote tuna uwezo huo. Njia moja rahisi ya kuanzisha urafiki na watu ni kupenda yale wanayoyapenda wao.

Mtu anapoona unapenda mambo yake, inakuwa rahisi kwake kukufungulia milango ya kuwa karibu nae.

Kwa waajiri ni muhimu kuweka mazingira ambayo wafanyakazi wanakuwa na fursa ya kukutana nje ya ofisi. Buni shughuli za kawaida zinazowafanya wafanyakazi wako wafahamiane kwa karibu.

Unahitaji kiasi fulani cha uhuru

Binadamu kwa asili yake anapenda kuwa huru. Unapomnyang’anya uhuru wake umemnyang’anya furaha yake.

Hata kazini, tafiti zinaonesha kuwa kazi zinazowafanya wafanyakazi wajione wana nguvu fulani ya kufanya mambo yakaenda bila kusimamiwa kwa karibu sana wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na furaha zaidi.

Bahati mbaya, kazi zetu nyingi hazitupi kiasi cha uhuru tunaouhitaji. Ingawa tunatamani kuwa na mamlaka fulani ya kufanya tupendavyo, hatuwezi kwa sababu upo ukweli pia kuwa uhuru mkubwa nao hukwamisha kazi.

Kama unahitaji kuwa na uhuru fulani katika eneo lako la kazi lakini bosi wako hakuachi upumue, kuna njia unaweza kuzitumia kumridhisha bosi wako na bado ukawa na kiasi fulani cha uhuru.

Kwa mfano, wasimamizi wanaopenda kufuatilia sana watu kwa karibu, mara nyingi hupenda kuwa na uhakika kuwa kazi zinakwenda kama wanavyotaka. Namna nzuri ya kupunguza wasiwasi wao ni kufanya kazi kwa kiwango cha juu na kuwapa mrejesho mara kwa mara bila kusubiri waulizie.

Kwa ufanya hivyo, unajiwekea mazingira ya kuaminika zaidi na hivyo kupunguza haja ya kukubana.

Jitambulishe kwa kazi yako

Wafanyakazi wanaojisikia fahari na kazi wanazofanya, wanakuwa na uwezekano mara tatu zaidi ya kuwa wenye furaha kuliko wenzao wanaoonea haya kazi zao.

Hii pia ina maana ya kujisikia fahari kuwa sehemu ya utamaduni wa taasisi unayoifanyia kazi.

Kama hujawahi kujisikia fahari kusema unafanya wapi kazi, pengine unahitaji kutumia muda kidogo kufungua macho uone kitu gani kinasababisha ufiche mahali unakofanyia kazi.

Je, unafanya kazi usiyoipenda au basi pengine huoni sababu ya kujitambulisha na kazi yako?

Vyovyote iwavyo, tafuta thamani ya kazi unayoifanya kwa kuangalia aina ya matatizo yanayotatuliwa kupitia kazi yako. Kama wewe ni mlinzi, thamani ya kazi yako ni usalama wa watu na mali zao.

Kama wewe ni mwalimu, thamani ya kazi yako ni kufuta ujinga wa watoto wetu. Usijidharau.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

Friday, February 9, 2018

Wajua kustaafu kutakuongezea hatari ya kifo usipojipanga?

 

Katika hali ya kawaida mtu anapomaliza utumishi wake anatakiwa kufurahi kwa sababu maisha baada ya kustafu huonekana ni muda mzuri wa kujitua majukumu mengi mtu anakuwa na anapumzika.

Hakuna haja ya kuamka mapema ili kuwahi kazini, hakuna kukimbizana na ripoti za ofisini wala kupewa maelekezo na bosi wako. Kinadaharia, nadharia haya ni mazingira ambayo kila mtu huyatamani.

Lakini umeshawahi kujiuliza ajira yako ikikoma kwa sababu yoyote ile utakuwa unafanya shughuli gani? Mathalani, umefukuzwa kazi au muda wa kustaafu umefika nini kitafuata?

Kwa walio wengi hili swali huumiza kichwa na muda unapofika hujafanya maandalizi ya kutosha, ni dhahiri msongo wa mawazo hautakuacha salama. Utafiti unaonyesha watu wengi hufariki dunia muda mfupi baada ya kustaafu. Katika hali ya kawaida mtu anaweza kutetea kuwa hili si jambo la ajabu kwa sababu kadiri mwanadamu anavyoongezeka umri hatari ya kupoteza maisha inaongezeka kwa sababu ya uhusiano kati ya uzee na maradhi na sababu nyingine nyingi.

Utafiti uliofanywa kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Shell Oil ulibaini wengi wanaostaafu wakiwa na miaka 55 wapo kwenye hatari ya kupoteza maisha ndani ya miaka 10 kwa asilimia 89 zaidi ya wale wanao staafu wakiwa na miaka 65.

Kwa kifupi, utafiti huu unaonyesha mtu anapo acha kazi mapema anajiweka zaidi kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Ripoti ya utafiti iliyochapishwa mwaka 2013 na Chuo cha Masuala ya Kiuchumi cha London, ilibainisha kustaafu kazi kunaongeza hatari ya kupata tatizo la sonona kwa asilimia 40.

Hili ni moja ya tatizo kubwa kwenye afya ya akili na waathirika wa tatizo hilo hujikuta wakipata matatizo mengine yanayosababishwa na tatizo hili na hatimaye kupoteza maisha.

Sababu hatari ya kifo kuongezeka

Dk Mziray wa kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi anahusianisha vifo vya mapema vya wastaafu na kukosekana kwa maandalizi ya mapema.

Anasema wastaafu wanapomaliza muda wao wanakutana na mahitaji mengi ambayo yanashindwa kutimizwa vyema na kipato cha wakati huo. Hii huleta msongo wa mawazo, shinikizo la damu na baadaye vifo vya mapema.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kipindi hiki si rafiki kwa wale ambao wanakuwa hawajajiandaa vema.

Kipato kile ambacho mtu alizoea kukipata kila baada ya muda fulani kinapoondoka ghafla huku mahitaji yakiongezeka ni dhahiri maisha yanakuwa magumu kuyamudu.

Unaweza sema kuwa utalipwa mafao yako na hili ndilo litakuwa suluhisho, lakini ukweli ni kwamba, kwa wengi ni suluhisho la muda mfupi tu. Hebu fikiria mfano mdogo tu huu; mwajiri wako anakulipa Sh1,500,000 kwa mwezi unayoitumia kwa matumizi yako kwa mwezi na mara nyingi mishahara huwa haitoshi.

Baada ya kustaafu ukapewa mafao yako ya Sh100 milionioni.

Kwa haraka haraka hizi ni fedha nyingi waweza sema zitakutosha kumalizia maisha yako yaliyo baki duniani kwa amani.

Lakini ukitazama kiuhalisia utagundua hizi si fedha nyingi kama zinavyoonekana.

Mathalani utakuwa unatumia kiwango kile kile cha fedha ulizokuwa unatumia kwa mwezi. Hii inamaanisha itakuchukua takribani miezi 66 kuzimaliza fedha hizo ambayo ni sawa na miaka mitano tu. Ninachofahamu, watu wengi wakiwa na fedha nyingi kwa wakati mmoja matumizi huongezeka.

Hivyo kwa watu wasio makini, fedha hizo zinaweza kuisha hata ndani ya mwaka mmoja. Baada ya fedha kuishi kinachofuata huwa si kitu kizuri.

Vyanzo mbalimbali vinaonyesha kubadilika kwa mfumo wa maisha ni moja ya sababu kuu za kuongeza hatari ya kupoteza maisha.

Pamoja na ukweli kwamba ajira ni sehemu ya kupata ujira, lakini ni chanzo kikubwa cha furaha kupitia wale watu unaokutana nao kila siku. Watu hawa hugeuka kama familia ya karibu unayoshirikiana nayo kwenye mambo mengi na ukishaachana nayo kinachofuata ni upweke unaoweza kukuletea sonona (depression).

Ajira pia ni moja ya vitu vinavyofanya miili kuwa imara na hivyo kujikinga na maradhi mbalimbali. Kuwahi kuamka uwahi kazini na shughuli mbalimbali zinafanya mwili wako kuwa kwenye mjongeo muda wote, lakini unapostaafu na kuamua kukaa nyumbani na pengine kuamka muda unaotaka kunaongeza hatari ya kupata maradhi yanayoongeza hatari ya kupoteza maisha.

Ushauri

Ni vema kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto za maisha baada ya ajira. Siku ya kwanza niliposaini mkataba wangu wa ajira mzee mmoja aliniambia kwa mzaha, “mwanangu, maandalizi ya kustaafu yanaanza leo”. Ukifikiria kauli hii unawezadhani haina mantiki, lakini maandalizi ya kumaliza utumishi wako yanatakiwa yaanze siku unapoanza ajira.

Hii inajumuisha vyanzo vya mapato mbadala ili kuepukana na fedheha ya ukata na kujiandalia makazi mapema na mambo mengine ya kufanya.

Usipokuwa makini utamaliza utumishi ndiyo uanze kufikiria kujenga makazi yako hili nalo ni changamoto kwa watu wengi na huwa ni chanzo kikubwa cha kudholotesha afya ya akili.

Kujihusisha kwenye shughuli za kijamii kabla na baada ya utumishi kukoma ni jambo la muhimu pia. Hii itakusaidia kuwa na watu wa karibu na kuondoa upweke.

Kujihusisha na michezo na kujiunga na vilabu mbalimbali vya kijamii husaidia kuondoa upweke na kuushughulisha mwili wako.

Jambo la msingi pia ni kuishi na watu vizuri katika ajira au shughuli yoyote unayoifanya.

Wakati mwingine msongo wa mawazo huongezeka ukiwaona wale uliowatendea vibaya au kuwanyanyasa wakiendelea na kazi huku wewe utumishi wako ukiwa umekoma na pengine mambo mengine yanaenda kombo.

Maneno yatakayokuwa yakisemwa juu ya matendo yako mabaya uliyoyafanya katika utumishi wako yanaweza kukuumiza zaidi.

“Alikuwa anajifanya mbaguzi na mnyanyasaji, kiko wapi sasa, mbona kaiacha ofisi?” Wema ni mtaji mkubwa maishani.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kwa 0659 08 18 38, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com

Friday, February 2, 2018

Mambo matano yanayofanya mkataba wa ajira ujulikane kihalali na kisheria

 

By Christian Bwaya na Joel Kasanda bwaya@mwecau.ac.tz

Watu wengi wameajiriwa bila kuwa na mkataba wa ajira. Moja ya sababu ni ya baadhi ya waajiri na waajiriwa ambao kwa makusudi au kutokuelewa, hupendelea uhusiano wa ajira usio na nguvu ya kisheria.

Katika mazingira ambayo mwajiriwa anaamua kuacha kazi bila kufuata utaratibu, inakuwa vigumu kwa mwajiri kuchukua hatua za kisheria kwa sababu anakuwa hana ushahidi wa makubaliano ya kikazi kati yake na mwajiriwa.

Aidha, kwa upande wa mwajiriwa, inapotokea ajira yake imekoma kinyume cha utaratibu, anakuwa kwenye hatari ya kupoteza haki zake.

Kabla ya mwaka 2015 hatukuwa na tafsiri ya kisheria ya neno ‘ajira’ ingawa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura Na. 366 ya mwaka 2004 ilikuwapo.

Kifungu cha 4 cha Mabadiliko ya Sheria mbalimbali za Ajira na Kazi ya mwaka 2015 kinafafanua ajira ni; “utekelezaji wa mkataba wa ajira baina ya wahusika kwenye mkataba, chini ya uhusiano wa mwajiri–mwajiriwa.”

Kwa kifungu hiki haiwezekani kuwa na ajira bila kuwa na mkataba.

Maana ya mkataba

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, mkataba wa ajira ni makubaliano yanayofanyika kati ya mtu anayeitwa mwajiri, kwa upande mmoja na mwajiriwa kwa upande mwingine.

Lengo la mkataba ni kuweka utaratibu utakaoongoza uhusiano kati ya upande unaotoa huduma kwa mwajiri na upande mwingine ulinaolipa ujira kwa kazi inayofanywa na mwajiriwa.

Ili mkataba wa ajira uwe na nguvu ya kisheria lazima ukidhi vigezo vikuu vitano kama ifuatavyo.

Udhibiti wa ajira

Katika mkataba wa ajira, ni sharti uwapo upande unaokuwa na nguvu ya udhibiti wa majukumu ya mwajiriwa kwa maana ya uwezo wa kutoa maelekezo yanayoongoza utaratibu wa kutekeleza shughuli zinazohusiana na ajira. Tunafahamu yapo mazingira ambayo mtu hulipwa kwa kufanya kazi isiyomfunga.

INAENDFELEA UK 24

Chukulia kwa mfano, washauri waelekezi kama wahasibu, wakaguzi wa mahesabu, mawakili, wabunifu wa majengo na makandarasi. Hawa huuza ujuzi na uzoefu wao kwa mtu mwingine bila kulazimika kufuata maelezo ya kina ya yule anayelipia huduma yake na hivyo hatuwezi kusema mtu huyu ni mwajiriwa kwa sababu kiwango cha udhibiti hakikishi masharti ya sheria.

Ndio kusema ili mkataba uwe na nguvu ya kisheria, ni sharti uanishe wazi nani mwenye udhibiti wa ajira, kwa maana ya mwajiri, na upande unaofuata udhibiti wa upande mwingine, ambao ni mwajiriwa.

Kuwa sehemu ya taasisi

Katika siku za leo mazingira ya kazi yamebadilika. Waajiriwa leo, mathalani, hawalazimiki kuwepo eneo fulani ili kutekeleza majukumu yao. Waajiriwa wenye utaalam kama madaktari, wanasheria, mainjinia, wanaweza kuwa sehemu ya shughuli za mwajiriwa bila kulazimika kuwakufuata maelekezo ya moja kwa moja ya mwajiriwa kama tulivyoona hapo juu.

Mambo kama haya yamefanya sheria iweke kigezo cha mfanyakazi kutambulika kama sehemu ya taasisi hata kama halazimiki kuwepo kwenye taasisi kutekeleza kazi zake. Kigezo hiki husaidia mteja kudai haki kwa taasisi pale inapotokea mwajiriwa amefanya makosa yanayoleta madhara wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri wake.

Uthibitisho wa jumla

Ukiacha vigezo hivyo viwili, kuna vigezo zaidi vinavyotumika kupima uhalali wa mkataba kati ya mwajiri na mwajira. Hapa yanatazamwa masuala kama utaratibu unaotumiwa na mwajiri kumlipa mwajiriwa, utaratibu wa kulipa kodi na uanachama kwenye mifumo ya hifadhi ya jamii.

Masuala mengine ya kuzingatiwa ni utaratibu wa posho za likizo na ugonjwa, utaratibu wa mapumziko, upatikanaji wa vifaa vya kazi, masaa ya kazi; eneo linalotumika kufanyia kazi pamoja na uangalizi.

Kulingana na mazingira yenyewe, mambo kama haya hutumika kuangalia ikiwa kuna mahusiano ya kikazi kati ya pande mbili.

Maudhui ya mkataba

Hakuna mfumo mmoja unaofanya mkataba wa ajira uwe na nguvu ya kisheria. Mkataba unaweza kuwa kwa njia ya maandishi au kwa makubaliano yasiyo ya maandishi. Katika mazingira nadra, mkataba pia unaweza kutegemea mazoea yaliyopo kati ya pande mbili.

Hata hivyo, lazima mkataba ubainishe masuala kadhaa ya msingi. Kwa fano, lazima liwepo tamko la mwajiri kuahidi kumlipa mwajiriwa mshahara kama ujira wa ahadi ya mwajiriwa kufanya kazi fulani.

Lakini pia, lazima mkataba wa pande hizi mbili uwe wa hiari pasipo shurti wala kulazimishwa. Mkataba unapokosa kigezo cha uhiari unakosa nguvu ya kisheria.

Kadhalika, lazima mkataba uainishe majukumu yanayotekelezeka baina ya pande mbili. Mkataba unaoeleza majukumu yasiyotekelezeka katika mazingira ya kawaida, unakosa nguvu ya kisheria.

Vipengele vya lazima

Pamoja na kukubalika kwa makubaliano yasiyo ya kimaandishi kati ya pande pindi za ajira, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, sura Na. 366 bado maandishi yamepewa nafasi kubwa.

Kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria za Ajira na Kazi katika Sheria Na. 24 ya mwaka 2015, kifungu cha 14(2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kilirekebishwa na kumtaka mwajiri aweke kumbukumbu za mkataba wake na mwajiriwa kwa njia ya maandishi.

Vipengele hivi vinatofautiana kulingana na aina ya ajira lakini vilivyo muhimu ni jina la mwajiri na la mwajiriwa, siku ya kuanza kazi, ngazi au kiwango cha mshahara, jina la kazi na majukumu yake, eneo la kazi na mahali ambapo mwajiriwa alipatikana.

Masuala mengine ni utaratibu utakaotumika katika malipo ya mshahara/ujira, idadi ya saa za kufanya kazi, utaratibu wa likizo na nyakati za ugonjwa, mwongozo nyakati ambazo mwajiriwa atashindwa kufanya majukumu yake na utaratibu wa kufuata upande wowote unapotaka kuvunja makubaliano ya mkataba husika.

Joel Kasanda mwandishi mwalikwa wa makala haya ni Mwanasheria kitaaluma anayepatikana kwa namba +255 712 786 051.     

Friday, February 2, 2018

Uhusiano mbaya baina ya mwajiri na mwajiriwa unavyoathiri utendaji

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi

Moja ya vitu muhimu katika kujenga ustawi wa shirika lolote lile liwe la umma, binafsi, dogo au kubwa ni uhusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa.

Kwa upande wa mwajiri uhusiano huu unaweza kuwakilishwa na uongozi katika taasisi husika kwa ngazi tofauti tofauti kuanzia ya idara.

Hii inamaanisha wakuu wa taasisi, wizara na idara mbalimbali wapo kama wa wakilishi wa mwajiri na hutakiwa kuyalinda maslahi ya mwajiri.

Sababu nyingi zinazohusiana na watu kuacha ajira zao mara nyingi ni za mahusiano kazini na wala si ujira mdogo kama wengi wanavyodhani.

Tafiti nyingi zinaonyesha waajiriwa wengi hupenda taasisi zenye uhusiano mzuri na ujira mdogo kuliko zile zenye ujira mzuri na uhusiano mbaya hasa kati yao na waajiri.

Nini kinaharibu uhusiano?

Mara nyingi uhusiano uharibiwa na ubinafsi na wakati mwingine kukosa mbinu za kiungozi kwenye maeneo ya kazi. Waajiri wengi hufikiri zaidi katika kuongeza tija au faida bila kumfikiria mtu anayehusika moja kwa moja katika kuyafanikisha haya.

Migogoro mingi ya maeneo ya kazi chimbuko lake ni ubinafsi kwani waajiri wanashindwa kuwafikiria waajiriwa na hivyo kujikuta wanatunga sera, sheria na miongozo na wakati mwingine kufanya uamuzi unao athiri maslahi ya wafanyakazi.

Kukosa mbinu na ujuzi katika masuala ya kiongozi na menejimenti kumekuwa sababu kubwa ya waajiri kujikuta wakifanya mambo kwa mazoea huku wengine wakidhani pia wanachofanya ni sawa lakini wamekuwa wakiathiri utendaji wa wafanyakazi wao kwa kiasi kikubwa sana.

Waajiriwa pia uwa ni chanzo cha kuharibu uhusiano; si kweli kuwa waajiri uwa na shida wakati wote, bali waajiriwa pia husababisha uhusiano kuharibika na kuathiri utendajikazi.

Sababu za kinidhamu na kukosa umakini huwaingiza waajiri na waajiriwa katika migogoro inayoharibu uhusiano mzuri kazini.

Uhusiano mbaya katika maeneo ya kazi yana athari nyingi sana ambazo mara nyingi huwa matokeo ya mambo kadhaa, miongoni mwayo ni

Motisha

Kasumba miongoni wa watu wengi ni kuwa motisha kwenye ajira huletwa na fedha pekee kitu ambacho kinapingana na ukweli kutoka kwenye nadharia za menejimenti na tafiti mbalimbali.

Moja ya vitu vinavyo athiri motisha kwa wafanyakazi ni mahusiano mabaya kati yao na waajiri au mabosi wao.

Uhusiano uliojengwa kwenye misingi ya vitisho, uoga, uonevu na ubinafsi hufanya mazingira ya kazi yasiwe rafiki na hivyo kusababisha msongo wa mawazo, utoro, na kuacha kazi.

Kwa bahati mbaya sana, waajiri huweka mazingira haya kwa kutokujua madhara yake au kudhani hiyo ni njia sahihi ya kuongeza ufanisi na utendaji kazini.

Pia, taswira wanayodhani wanayo kwa waajiriwa ni tofauti na uhalisia kwani waajiriwa wengi huwaona kama ni kikwazo cha furaha yao na ufanisi kazini.

Utafiti uliochapishwa na Jarida la Forbes ulibaini asilimia 65 ya waajiriwa walipoambiwa wachangue kati ya kuongezewa mshahara au mabosi wao wafukuzwe kazi, walikuwa tayari kuona mabosi wakifukuzwa kazi kuliko kuongezewa mishahara.

Hii inaonyesha nguvu ya uhusiano ni kubwa katika kuleta furaha na kufanya mazingira ya kazi kuwa rafiki.

Mgawanyiko wa taasisi

Moja ya kanuni 14 za Menejimenti za mwanazuoni Henri Fayol inasisitiza kuweka maslahi ya taasisi mbele dhidi ya maslahi binafsi.

Kulifanikisha hili inahitaji waajiriwa wawe na mapenzi kwa taasisi yao kitu kinacho jengwa na uhusiano thabiti kati ya mwajiri na mwajiriwa.

Waajiri wanaoonyesha ubinafsi kwa kushindwa kuzingatia nini waajiriwa wanapenda, wanahitaji au wanajisikia kutokana na maneno na matendo yao huishia kuigawa timu au taasisi.

Ikifika kiwango watu wanafanya kazi ili wapate ujira pekee hii ni hatari sana kwa mustakabali wa taasisi husika.

Watu hawa hawatafanya shughuli zao kwa kujitoa na kwa ufanisi kwani wanaamini mafanikio ya taasisi siyo mafanikio yao bali na mfanikio ya mwajiri kutokana na ukuta uliyowekwa na mahusiano mabaya kati yao na mwajiri wao.

Nini Kifanyike?

Wakuu wa taasisi na idara wanawawakilisha waajiri hivyo wanatakiwa wafahamu kuwa vyeo ni dhamana na wanatakiwa kutumia nyadhfa zao vizuri na kuhakikisha hawanyanyasi na kuwaonea wafanyakazi.

Vyeo huja na kuondoka lakini utu unatakiwa ubaki palepale. Mabosi wahakikishe hawawi chanzo cha msongo wa mawazo bali kimbilio kwa wale wenye tatizo hilo.

Kiongozi mzuri anatakiwa awe rafiki. Urafiki huu unatafsiriwa kupitia kauli, maamuzi na matendo yake. Uongozi hautakiwi kuwa ukuta bali daraja kati ya kiongozi na wafuasi wake.

Kiongozi yoyote anatakiwa atambuwe kuwa kinachotakiwa kumtofautisha yeye na wengine ni ushawishi kwanza mamlaka baadaye.

Kiongozi anayeweka mamlaka mbele mara nyingi hujikuta katika wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yake na kuharibu mahusiano mema mahala pa kazi.

Waajiri wanatakiwa watambuwe umuhimu wa ushirikishaji katika utendaji wao.

Waajiriwa wanaoshirikishwa moja kwa moja au kupitia uwakilishi huthamini mahusiano yaliyojengwa kati yao na waajiri au mabosi wao hivyo kufanya maeneo ya kazi kuwa rafiki kitu kinachosaidia katika kuboresha utendaji.

Kwa kuzingaia kuwa mahusiano haya hujengwa na pande mbili ni vyema pia kwa waajiriwa kuhakikisha wanayalinda mahusiano haya kwa kuonesha jitihada mbali mbali ikiwemo kufuata taratibu na sheria na pia kuheshimu mikataba yao ya ajira.

Inapotokea kuna mambo hayaridhishi au yana athiri utendaji ni vyema kuyasema wazi ili kufikia malengo binafsi na yale ya taasisi.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kupitia 0659 08 18 38, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com     

Friday, January 19, 2018

Mambo ya kuzingatia ili kuongeza ufanisi kazini

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi

Moja ya changamoto zinazowakuta wengi katika shughuli zao ni kuwa na ufanisi usioridhisha.

Tafiti zinaonyesha wapo watu ambao kiasili wanahamasa kubwa ya kazi, hivyo kuwafanya wawe hodari zaidi katika kile wanachokifanya.

Pia, wapo wale ambao wanakipenda kile wanachokifanya, hivyo kufanya shughuli zao kwa moyo na kufikia viwango vinavyoridhisha.

Hii huwafanya watu hawa kuonekana wafanisi zaidi ya wengine hata kama wanafanya shughuli zao katika mazingira yanayofanana na wengine.

Ni ukweli usiopingika kuwa watu wenye ufanisi unaoridhisha kazini hufurahia shughuli hizo na kuwafanya wawe na furaha zaidi.

Wao hujiepusha na adhabu mbalimbali na kuwafanya kuwa watu wanaoaminiwa na kutegemewa katika maeneo yao ya kazi.

Teuzi nyingi katika taasisi mbalimbali pamoja na mambo mengine, huzingatia ufanisi wa kazi kama kigezo kikuu.

Hii inafanya suala hili kuwa muhimu katika shughuli yoyote ile.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayoweza kumuongezea ufanisi mtu kama atayazingatia mahala pakazi;

Malengo binafsi

Mara nyingi taasisi hujiwekea malengo yake ya muda mfupi na mrefu.

Idara katika taasisi husika nazo hujiwekea malengo madogomadogo ambayo kama yatafanikiwa yatawezesha malengo makubwa ya taasisi kufikiwa. Kila mtumishi hupewa malengo anayotakiwa kuyatimiza na wakati mwingine hupewa nyenzo za rasilimali zinazomuwezesha kuyafikia malengo haya.

Pamoja na hayo, bado ni muhimu kujiwekea malengo binafsi ya muda mfupi yatakayomsaidia kuyafikia malengo ya idara na kisha ya taasisi.

Si vyema kwenda kazini ukiwa haujapanga ni nini utafanya katika siku husika.

Kuwa na malengo ya siku, wiki, mwezi hadi mwaka katika shughuli yako yatakusaidia katika kuongeza ufanisi na kuyafikia malengo makuu ya taasisi kwa urahisi zaidi.

Matumizi ya Muda

Kwa bahati mbaya katika nchi zinazoendelea kwa kiasi kikubwa matumizi ya muda yamekuwa sio kitu kinachotiliwa mkazo na kuzingatiwa na wengi.

Ili kuongeza ufanisi ni nyema kuzingatia matumizi bora ya muda wako ndani na hata nje ya ofisi yako.

Katika kupima ufanisi wa mfanyakazi hiki ni moja ya vigezo ambavyo hutazamwa kwa uzito wa kipekee.

Matumizi mazuri ya muda si kutumia muda wako wote kaika kufanya kazi bali ni kujua nini kifanyike kwa wakati gani yaani shughuli sahihi kwa wakati sahihi.

Fika kazini mapema; akili hufanya kazi vizuri zaidi wakati wa asubuhi. Pamoja na hayo zingatia kupumzisha akili na mwili wako pale vinapochoka.

Mafunzo

Ujuzi ni moja ya vitu muhimu sana katika kuongeza ufanisi wa shughuli yoyote ile.

Ni vyema kuhakikisha unajifunza vitu vipya kila unapopata fursa. Kila siku kuna jambo jipya la kujifunza. Kama unapata fursa ya kurudi chuoni kuongeza ujuzi fanya hivyo.

Ikumbukwe kuwa ujuzi haupatikani katika mfumo rasmi pekee. Jifunze kwa wenzako, soma vitabu, makala, tumia mtandao wa intaneti, udhulia semina na warsha mbali mbali; hii haitakupa ujuzi pekee bali itakuongezea hamasa ya kazi na hivyo kukuongezea ufanisi pia.

Vipaumbele

Moja ya changamoto inayowakumba wengi mahala pa kazi ni kutaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Hii hupunguza umakini na hivyo kufanya matokeo ya shughuli kuwa chini ya viwango vinavyotarajiwa.

Hakikisha vipaumbele vinafahamika katika kila unachofanya na kuanza kwa kuyafanya yale yenye umuhimu au uharaka zaidi kisha mengine yafuate.

Yale yasiyowezekana yaafutiwe ufumbuzi haraka iwezekanavyo na wakati mwingine ni vyema kukaimisha au kutafuta msaada kwa wengine kwani kujaribu kufanya jambo usilolijua au liweza kunaweza kuharibia kazi.

Mahusiano

Katika mazingira ya kazi ni vigumu kufanya kazi na kufikia malengo kama auhusiani vyema na wengine.

Hakikisha unaboresha na kudumisha mahusiano mema na kila mtu; kuanzia bosi wako mpaka yule muhudumu wa chini kabisa.

Hii ni siri kubwa sana katika kufanikisha malengo ya shughuli yoyote ile. Ukihusiana vyema na wengine inakujengea mtandao wa marafiki na timu kubwa ambayo inaweza kukusaidia pale unapohitaji msaada kazini na hata nje ya kazi yako.

Utulivu wa nafsi na akili

Shughuli tunazofanya zinahitaji kiwango kikubwa cha utulivu wa akili na amani nafsini mwetu.

Lakini vitu hivi uwa si rahisi kuvipata au uwa havipatikani kila tunapovihitaji.

Changamoto za nyumbani, ofisini, safarini, kwenye mahusiano na maisha kwa ujumla hutuletea msongo wa mawazo na huzuni.

Ni vyema kuhakikisha tunatafuta njia ya kuviepuka vile vinavyowezekana na kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha vile visivyoepukika havituathiri sana ili kuongeza umakini katika shughuli tunazozifanya.

Tathmini na pongezi binafsi

Shughuli yoyote inahitaji tathmini ili kujua kasi ya usahihi wa kile unachofanya.

Ni nyema kujitathimini na kuangalia wapi unafanya vyema na wapi unakosea.

Tathmini binafsi haitoshi hivyo ni vyema kuwapa nafasi watu wengine wakutathmini ili kujua mwenendo wako katika kile unachofanya.

Kubali kukusolewa na kuyachukulia mapungufu kama changamoto na kujirekebisha.

Pale ambapo unafanya vizuri hata kama hakuna atakayejitokeza kukupongeza usisite kujipongeza mwenyewe na kufurahia mafanikio yako. Ukisubiri kuambiwa na mtu ‘umefanya vizuri’ anaweza asitokee.

Uwiano wa kazi na maisha binafsi

Pamoja na umuhimu wa shughuli zinazotuingizia kipato bado tunahiaji muda wa kutosha katika kufanya mambo mengine hasa yale yakijamii.

Kuzipa shughuli zetu za kiuchumi muda mwingi zaidi na kusahau upande wa pili wa maisha kunaweza kupunguza ufanisi wa kazi hizo tunazoziangaikia usiku na mchana.

Ni vyema kukumbuka familia zetu, afya, imani na mambo mengine ya kufurahisha nafsi zetu.

Tenga muda kwa ajili ya michezo na burudani na kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.

Afya yako ikiyumba ajira yako itayumba pia, mahusiano yako na wengine yakiyumba shughuli zako nazo hazitabaki salama hivyo ni vyema kutenga muda wa kuangalia mambo mengine nje ya ajira zetu.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kwa 0659 081 838, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com     

Friday, January 19, 2018

Tabia tano zitakazokupa nidhamu ya muda kazini

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Mafanikio katika eneo lako la kazi, kwa kiasi kikubwa yanategemea matumizi ya muda ulionao kwa siku. Kile unachokifanya kati ya saa 6:00 usiku na saa 5:59 usiku wa siku inayofuata, ndicho kinachoamua utekelezaji wa majukumu yako.

Sote bila kujali aina ya kazi tunazofanya, mahali tunapoishi lakini tumepewa mtaji wa saa 24 kwa siku.

Tofauti ni namna tunavyoweza kutumia saa hizo kwa tija.

Makala haya yanakupa uzoefu wa watu ninaowajua wana shughuli nyingi lakini waliweza kujijengea tabia ya nidhamu ya muda. Watu hao wanatufundisha tabia tano muhimu.

Kuongozwa na malengo

Injinia Sylvanus Kamugisha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Sylcon Builders Limited anasema mahali pa kuanzia ni malengo ya mwaka uliyonayo:

Vipaumbele vinatokana na malengo ya mwaka niliyonayo.

Mfano, mwaka huu nimeazimia kuwa mtu wa sala. Kupunguza uzito kilo 20, kusoma vitabu 40 na mambo kama hayo. Kwa hiyo kwenye ratiba yangu ya siku pamoja na mambo mengine, inaanza na dakika 15 za sala, baadaye naenda kufanya mazoezi dakika 30 mpaka 45, baada ya hapo nasoma kurasa 10 hadi 15 za kitabu kilicho kwenye ratiba yangu na ratiba nyingine inaendelea.

INAENDFELEA UK 24

INATOKA UK 23

Aidha, namna unavyotafsiri malengo yako katika siku inayofuata ni muhimu kama anavyoeleza Prosper Mwakitalima, Mkurugenzi wa Ubunifu wa Brand Exponential: “Nina utaratibu wa kupangilia siku yangu siku moja kabla. Kisha ninaandaa mambo ya kutekeleza kesho kabla sijalala. Hii inanipa muda wa kuiona kesho kabla sijalala.”

Erick Mbogoro, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma naye anakubaliana naye: “Huwa naandaa abstract schedule (ratiba) yangu kabla ya kuanza siku.

Kwa hiyo nafanya kazi kulingana na muda niliojipangia.”

Kujiwekea vipaumbele

Erasto Kitia, Ofisa elimu vifaa na takwimu, Halmashauri ya Wilaya Singida, anasema lazima kuwa na vipaumbele vya siku, “Jambo la kwanza lazima uyakubali na kuyaelewa majukumu yako vizuri.

Tengeneza mpango wa kuyatekeleza majukumu hayo kwa kuweka vipaumbele na kuweka muda wa utekelezaji. Lakini muhimu sana kuwa na uwajibikaji binafsi na nidhamu ya kazi.”

“Katika kazi kuna mambo ambayo yakifanyika kwanza hurahisisha yajayo. Mengine yako ndani ya kipindi fulani tu kikipita hayawezekani tena. Kwa namna hiyo unaweza kujua kipi kianze na kipi kifuate,” anafafanua.

Dk Mwemezi Rwiza, mhadhiri katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha hupangilia vipaumbele kwa kuangalia uzito wa majukumu.

Anasema, “Ili kupangilia siku yangu, naangalia uzito. Kama VC (Makamu Mkuu wa Chuo) ameita kikao ofisini kwake na pia kuna muswada wa kukabidhi saa 10 jioni, nitaenda kwa VC kwanza. Naangalia pesa pia.

Kama ninaandika andiko la mradi na kuna kikao cha kamati ya miundo mbinu ya chuo, kipaumbele change kitakuwa andiko la mradi.”

Orodha ya mambo ya kufanya

Tumaini Stephen, Mwanasheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hutunza muda kwa kutengeneza orodha ya mambo ya kufanya kila siku:

“Kila mwisho wa siku huwa napanga vitu vya kufanya siku inayofuata. Huwa napanga vitu kuendana na uhalisia wa muda nilionao na nahakikisha kila nilichopanga nakifanya ndani ya muda niliopanga.”

Katika kupanga vipaumbele vya siku, Tumaini Stephen ana utaratibu wa kuangalia uharaka wa jambo. “Sisi watu wa mahakamani huwa tuna deadline (makataa) haswaa kwenye kuweka vizuri nyaraka.

Kama kesho ndio siku ya makataa na sijamaliza kuziandaa hilo lazima liwe jambo la kwanza kesho.”

Dk Rwiza naye anaunga mkono utaratibu huo, “Nahakikisha orodha hiyo ina uhalisia.

Siyo realistic (haiwezi kuwa na uhalisia) kusahihisha mitihani karatasi 15 za wanafunzi halafu pia niwe na muda wa kupitia dondoo za andiko la miradi mitatu tofauti.”

Kutengeneza ‘desturi’ ya siku

Bahiya Abdi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, anasema kwake nidhamu ya muda ni matokeo ya desturi ya siku aliyojijengea. Anasema, “Mimi ni mtu wa routine (kufanya mambo yale yale kila siku.)

Huwa nimeshapanga nini huwa ninafanya kwa wakati fulani kwa vitu ambavyo kila siku lazima nivifanye.

Sipotezi muda kupanga nini nitafanya saa ngapi wapi kwa sababu nina vitu ambavyo lazima nivifanye kwa wakati ule ule kila wakati.”

Lonyamali Morwo Mkurugenzi Mtendaji wa MultiSkills Business Consultancy naye ana desturi ya siku:

“Nina majukumu matano ya kutekeleza kila siku. Naenda kazini, nasoma vitabu, lazima nikae na familia na kukutana na marafiki na pia niwe na muda wa kufanya kazi zangu binafsi nje na ajira.

Kwa hiyo mimi huwa naamka saa 10 alfajiri na kuhakikisha hayo yote nimeyafanya kila siku.”

Kuongeza uzingativu katika kazi

Moja ya changamoto ya nidhamu ya muda ni kukosa uzingativu.

Bahiya Abdi hukabilianaje na changamoto hii? Anajibu, “Huwa sikubali kuwa disturbed (kusumbuliwa) wakati nafanya kazi muhimu zinazohitaji umakini.

Mfano, huwa naweka simu yangu mbali ili isinipe vishawishi vya kuitumia kufanya.”

Dk Rwiza, ambaye pia ana maelfu ya wafuasi wanaofuatilia anayoyaandika kwenye mtandao wa Twitter naye hutumia mbinu kama hiyo: “Huwa siendekezi sana inconveniences (mambo yanayoingilia shughuli) zisizo na msingi.

Kama nina kazi inayotakiwa mapema au niko na familia yangu huwa ninazima simu na hata kuchomoa waya wa internet.”

Ushauri

Lonyamali Morwo anamalizia kwa kutoa ushauri: “Matumizi sahihi ya muda ndio siri ya mafanikio.

Muda ni pesa na thamani ya pesa ipo kwenye muda. Unapata mshahara kwa kutoa muda, unapata mazao shambani kwa kutumia muda wako kuzalisha.

Muda ukipita umepita na haurudi tena. Tujifunze kutunza muda.”

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815     

Friday, January 5, 2018

Mbinu za kufanya mwaka 2018 uwe wa mafanikio kazini

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Sina shaka umeanza mwaka mpya kwa matumaini makubwa ya kupata mafanikio zaidi kazini kwako.

Swali hata hivyo, umejipangaje? Je, matumaini yasiyoambatana na mikakati madhubuti yanaweza kuzaa matunda unayoyatarajia?

Kwa kutambua kuwa mafanikio ni matokeo ya kujipanga vizuri mwanzoni mwa mwaka, makala haya yanaangazia maeneo matano yanayofaa kuyatazamwa vizuri na mfanyakazi mwenye shauku ya mafanikio kazini.

Kujiwekea malengo

Unapoanza mwaka mpya, ni muhimu kujiwekea malengo mahususi yatakayokuwa dira inayoongoza utendaji wako kama anavyoshauri Lonyamali Morwo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa MultiSkills Business Consultancy ya Arusha

Anasema: “Ili mfanyakazi ajipange vizuri kiutendaji, lazima ajue maono na dhima ya taasisi anayofanyia kazi. Mfanyakazi lazima auelewe mpango mkakati na malengo ya taasisi; ajue kile kinachotakiwa kufikiwa ndani ya mwaka na nini kinatarajiwa kutoka kwake.”

Anaongeza: “Mpango mkakati ndio lugha ya mawasiliano ya utendaji kazi kwa mfanyakazi. Taasisi isiyo na mpango mkakati ni sawa na gari linalounguruma lakini halitembei. Mafuta yataisha bila kwenda kokote.”

Hoja hiyo inaungwa mkono na Erasto Kitia, Ofisa elimu vifaa na takwimu wa Halmashauri ya Wilaya Singida, anayesema: “Wanafanyakazi waweke kipaumbele katika kuboresha huduma kwa kuzingatia mipango na vipaumbele katika sekta zao.”

Anaeleza kuwa wafanyakazi hawana budi kujiwekea malengo ya kuboresha ubunifu katika maeneo ya kazi kwa kutumia maarifa yao na kuanzisha vitu zaidi ya vile vilivyozoeleka.”

Kujiongeza kiuchumi

Mhadhiri wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela jijini Arusha, Dk Mwemezi Rwiza, anashauri kipaumbele kiwe akiba.

Anasema, “Kwa mwaka 2018 nadhani eneo muhimu ni kuweka akiba. Hapa nina maana kwamba mfanyakazi adhamirie kutunza asilimia fulani ya kila kipato chake katika mfuko maalum kwa ajili ya baadaye. Fedha ya akiba aikate na kuitunza kabla ya kufanya matumizi mengineyo. Asitumie kwanza halafu eti kinachobaki ndiyo kiwe akiba.”

Wafanyakazi wengi, hata hivyo, hushindwa kuweka akiba kwa kisingizio kuwa mshahara wenyewe hautoshi kwa matumizi ya kila siku. Dk Rwiza anatoa uzoefu wake: “Kila mwenye kipato anaweza kuweka akiba. Mimi na familia yangu tulipoanza jambo hili pia tulikwama kwa kipindi fulani kwa kisingizio kuwa kipato chetu kilikuwa hakitoshi.”

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Baadaye baada ya kuhangaika na kujisomea tukashawishika kuwa kipato chetu kilikuwa kinatosha ila sisi hatukuwa na matumizi mazuri. Tulidhani kuweka akiba ni jambo la ziada baada ya kufanya yale mengine tuliyodhani ni ya msingi. Tulipogundua kuwa akiba inaanza kwanza ndipo muujiza ulipoanza.”

Nidhamu kazini

Maranya Mayengo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma anafikiri mfanyakazi ajipange kuwa na nidhamu kazini: “Huu uwe mwaka wa kufanya kazi kwa ubora unaotarajiwa kwa kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi.”

Nidhamu yako hupimwa kwa namna tabia zako zinavyoleta tija kwenye eneo la kazi. Unapokuwa na tabia zinazozorotesha utendaji wako kama vile kuchelewa kuingia kazini, kuwahi kuondoka kazini, kuchelewesha kazi unazopaswa kuzikabidhi kwa wasimamizi wako, tafsiri yake ni kuwa huna nidhamu ya kazi.

Mwaka huu jipange kuwa na nidhamu zaidi. Pangilia majukumu yako ya siku kabla siku haijaanza. Fikiria kutumia shajara (diary) kuweka vipaumbele utakavyokuwa navyo kwa siku husika kama saa za vikao na mikutano, makataa (deadlines) yanayokaribia na shughuli nyingine unazotarajia kuzitekeleza nje ya eneo lako la kazi.

Uhusiano na wenzako

Huwezi kufanikiwa bila kuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako. Unaweza kuwa na uwezo mkubwa kazini lakini kama huna ujuzi wa kuishi na wenzako, itakuwia vigumu kupata mafanikio.

Mwaka huu weka maazimio ya kufanya kazi kama timu na wafanyakazi wenzako. Fanya jitihada za kuhakikisha unakuwa msaada wa kutatua changamoto za wenzako, badala ya kuendesha mashindano na misuguano isiyo ya lazima.

Kama sehemu ya kuboresha uhusiano wako na wengine, jifunze kuwasilisha mawazo yako kwa wengine bila kuwavunjia heshima. Hata katika mazingira ambayo hukubaliani na mawazo yao, linda hadhi zao.

Lakini pia Mayengo anafikiri uhusiano na familia ni muhimu pia: “Kazi zetu ziishie ofisini. Tusihamishie kazi nyumbani, familia zetu zinatuhitaji pia. Hatuwatendei haki tukirudi nyumbani tena tunakuwa tumetingwa na kazi za ofisini.”

Ongeza thamani yako

Gideon Obeid, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika anashauri uongeze thamani yako. Anasema: “Mwajiri wako anakuangalia wewe kama mzalishaji. Hiyo ndiyo thamani yako inayoamua mwajiri akulipe kiwango gani cha mshahara. Thamani yako inategemea vigezo vingi. Kimoja wapo ni kiwango chako cha elimu. Angalia kwenye kazi unayofanya uone mwaka huu ufanye nini ili uongeze thamani yako kazini.”

Fadhili Mtanga, mwandishi mashuhuri wa vitabu vya riwaya aliyeweza kusoma vitabu 1o7 mwaka uliopita, anafikiri mfanyakazi ajipange kujiongezea maarifa kupitia vitabu.

“Katika mwaka 2018, nashauri mfanyakazi ajikite kwenye kujiongezea maarifa kwenye maeneo mbalimbali kwa kupitia usomaji wa vitabu na machapisho mengineyo. Hii itasaidia kuwa na mtazamo mpana na uwezo wa juu katika kukabiliana na changamoto anazokumbana nazo mahali pa kazi,”anaeleza.

Hata hivyo, mara nyingi, wafanyakazi hutoa sababu ya kukosa muda wa kusoma vitabu.

Mtanga anashauri: “Muda unapatikana kama utaweka usomaji wa vitabu kuwa sehemu ya ratiba yako ya maisha. Kwa mfano, ukitenga saa mbili hadi nne kwa wiki, pengine nyakati za mwisho wa wiki, unaweza kusoma kurasa za kutosha.”

Usisahau wito wako

Tumia mwaka huu kuibua na kukuza uwezo na vipaji ambavyo Mwenyezi Mungu amevijaza ndani yako.

Thamani ya maisha haya ni zaidi ya kazi unayoifanya. Tafakari namna gani kazi yako inaweza kukusaidia kugusa maisha ya watu wengine. Heri ya Mwaka Mpya!

Christian Bwaya ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. 0754 870 815

Friday, January 5, 2018

Sifa hizi zitakusaidia kupata ajira

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mazingira ya kufanyia kazi yanabadilika kwa haraka zama hizi za sayansi na teknolojia.

Hali hii bila bila shaka inahitaji watu wanaoweza kwenda na mabadiliko hayo kwa kasi.

Watafuta ajira nao hawana budi kuyajua ya mabadiliko haya teknolojia na kisha kutafuta mbinu za kwenda nayo sambamba.

Huu siyo tena wakati wa kufanya vitu kizamani, unapaswa kutumia teknolojia kujiuza na kupata kile unachohitaji maishani.

Ili kujiweka katika nafasi nzuri katika soko la ajira na kurandana na hali halisi ya sasa, ni muhimu kwa wahitimu kuzingatia mambo kadhaa.

Uwezo wa kutumia zana za digitali

Vifaa vya digitali vimetengeneza nafasi ya watu kuingiliana na kuwa karibu zaidi na kupanua mianya ya ajira.

Katika dunia ya sasa, siyo lazima maombi ya kazi yafanywe kwa barua au siyo lazima kwa mtu kuhangaika na magazeti akitafuta ajira; haya yote sasa yanawezekana kwa kutumia njia za kisasa za vifaa vya kidigitali. Kwa sasa sio uamuzi wako kuamua kujifunza komputa au la, bali ni lazima mno ili uweze kuendana na uhalisia wa dunia kiteknolojia. Siyo kwa kutafutia ajira, lakini hata kazi sasa zinafanywa kiteknolojia zaidi.

Uwezo wa kufanya kazi na kuwasiliana na watu

Huombi ajira ili uje kujifungi chumbani ukifanya kazi peke yako, ni lazima uchangamane na wenzako katika ofisi moja au taasisi. Kuwa karibu na wenzako kwa kushirikiana kuhusu mambo yote muhimu kwa manufaa ya ofisi. Hakikisha unawashirikisha taarifa au maarifa mapya kutoka mahali kwingine ili kwa pamoja muweze kufikisha malengo kusudiwa.

Uwezo wa kuwasiliana ni muhimu kwa mfanyakazi mpya, kwani utakuwezesha kuwasilisha mawazo yako na kuyafanya yaeleweke vyema na kutumiwa na timu yako. Hivyo jifunze kuja na mawazo makubwa zaidi na kuwasilisha kwa unadhifu.

Elimu ya ujasiriamali

Huhitaji kumiliki biashara yako ili uwe na uwezo wa kupata mawazo makubwa na mapya, bali kupitia mabadiliko ya kiteknolojia yanaweza kukusaidia kujitambua na kujua unachopaswa kukifanya.

Ukijituma na kuwa mbunifu, ni dhahiri kuwa fursa zaidi zitakufuata mikononi mwako. Elewa kuwa hivi sasa kampuni nyingi hazihitaji wahitimu bali watu walio tayari kusababisha mabadiliko chanya na endelevu.

Kampuni zinataka mawazo mapya na watu wenye mipango stahiki walio na uthubutu wa kutenda kwa kuwa tayari wana tabia za kijasiriamali ndani yao.

Fahamiana na watu wengi kibiashara

Kuwa na mtandao mkubwa ambao umeutengeneza ni muhimu sana katika utendaji wa kisasa, kwani licha ya kuwa na msaada katika kuboresha biashara mauzo au huduma pia itakuwezesha wewe kujifunza mambo mbalimbali na kujiongezea uelewa jambo ambalo lina umuhimu mkubwa.

Mtandao ulionao una nguvu kubwa katika masoko yako hivyo kabla hujapata kazi jitahidi kuwa na watu sahihi. Pia, ni muhimu kujifunza namna ya kuwalinda na kuutunza urafiki wako na watu wako muhimu.

Uwezo wa kuchambua na kung’amua taarifa

Kuwa na taarifa nyingi na sahihi ni jambo kubwa mno katika karne hii. Kuwa na taarifa nyingi na maarifa ya kutoosha kutakusaidia kufanya jambo lolote kwa usahihi wake.

Unapaswa kuwa mchambuzi wa kilaa taarifaa unayoipata katikaa vyanzo mbalimbali. Kuwa makini na taarifa unayoichagua katika kutekeleza majukumu yako.

Kumbuka nyakati za kufanya kazi bila mpangilio na kwa kubahatisha zilishapita miaka mingi.

Uwezo wa kufikiri kwa mapana na usahihi

Ubunifu unathaminiwa na kampuni nyingi duniani. Ubunifu ndicho kitu pekee kinachosababisha kampuni kubakia kileleni katika ushindani wa dunia kibiashara.

Hivyo ni jambo zuri kuwa na watu ambao husugua akili zao kwa kujua nini kifanyike kwa maendeleo chanya ya namna ya kuboresha kazi au bidhaa.

Uwezo wa kujifunza kila siku

Kwa kadri teknolojia inavyokua na kubadilika, ndivyo unavyotakiwa kuendana nayo kama unataka kufanikiwa. Fungua akili yako na jifunze kwa watu wengine.

Hivi sasa watu hawajifunzi tena wakiwa darasani, zana za Tehama kama zimerahisisha watu kujifunza mambo mbalimbali, hivyo huna sababu ya kutojifunza.

Uwezo wa kutatua matatizo

Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, matatizo yanazaliwa kila kukicha na hakuna muda tena kumsubiri bosi kukuonyesha njia kama unakijua unachokifanya. Unatakiwa kuwa na uwezo kutambua matatizo na kuyatafutia ufumbuzi sanjari na kupendekeza nini kifanyike kwa haraka kadri matatio yalivyojitokeza.

Hii ina maana moja tu kuwa fikiria kwa njia yako kabla ya kulaumu. Wakati wote uwe mtu wa kuonyesha njia ya kutokea badala ya kukata tamaa.

Kama wewe ni mhitimu na unahitaji kufanya kazi ya ndoto yako ambayo umeisomea, hakikisha unajivika sifa hizi ili uwe mshindani wa kweli katika soko la ajira. Kumbuka kuna wengi wanatafuta kazi hiyohiyo unayoitafuta wewe.

Makala haya awali yalichapishwa katika tovuti ya Brighter Monday, ambayo ni tovuti namba moja ya ajira nchini.

Friday, December 15, 2017

Tabia tano unazozihitaji ili uishi vizuri na watu kazini

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Sehemu kubwa ya maisha ya kazi hutegemea vile unavyoweza kukaa na watu bila migongano.

Unapofanya kazi na watu msioelewana, unajiweka kwenye mazingira yanayoweza kukupunguzia si tu ari ya kufanya kazi, bali hata ufanisi wako.

Kama ilivyo mitaani tunakoishi, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya kila lililo kwenye uwezo wako, lakini bado wakaendelea kukuchukia.

Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa si mara zote watu hujenga chuki na wewe kwa sababu tu hawakupendi. Wakati mwingine, tabia ulizonazo (bila wewe kujua) zinaweza kuchochea hisia za wivu, uadui na hata mashindano yanayoweza kuathiri mahusiano yako na watu.

Katika makala haya, tunajifunza tabia tano zitakazokusaidia kuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako.

Kuwa tayari kuzidiwa

Katika mazingira ya kazi hisia za kuzidiana hazikosekani. Watu huweza kushindana kimyakimya kwa viwango vya elimu; uzoefu; utendaji wa kazi; ushawishi na hata tija waliyoileta kwa kampuni.

Usipokuwa makini unaweza kuingia kwenye mtego wa mashindano haya yanayoweza kuwa chanzo cha misuguano na wafanyakazi wenzako.

Mtu anayeona fahari kushindana na wenzake, mathalani, anaweza kuwa mtu wa kuzungumza sana kwenye vikao. Atashauri mahali ambako ushauri wake haujaombwa ilmradi tu aonekane ni mjuzi wa mambo.

Lakini pia, kwa kuwa anataka kuonekana anawazidi wengine hatakuwa tayari kujifunza kwa wenzake. Haya yote yatamtengenezea ufa wa uhusiano kati yake na wenzake.

Unahitaji kujifunza kuwa mnyenyekevu hata kama kweli inawezekana unawazidi watu. Jijengee mazingira ya kuomba msaada kwa watu wanaokuzidi uzoefu na ujuzi. Fanya hivyo kwa uangalifu bila kuwafanya watu wawe na wasiwasi na uwezo wako.

Sambamba na hilo, usiwe mwepesi wa kushauri kama ushauri wako haujahitajika. Badala yake jenga weledi utakaowafanya watu wakufuate wenyewe kwa ushauri.

Ukiweza kufanya hivyo, watu watakuchukulia kama rafiki asiye mshindani. Utajipunguzia maadui na mapambano yasiyo ya lazima.

Tatua changamoto za wengine

Kila mtu kazini huwa na malengo yake. Inawezekana, kwa mfano, kwa nafasi yako, ukawa na malengo ya kuongeza uzalishaji wa kampuni. Haya ni malengo ya kitaasisi.

Lakini pia unaweza kuwa na malengo yako binafsi kama kupanda cheo. Si jambo baya kuwa na malengo yako kama mfanyakazi anayejitambua.

Unapofanya hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa kila mfanyakazi naye ana malengo yake.

Wakati mwingine malengo yako yanaweza kuingilia na malengo ya mwingine.

Ukitaka kukaa na watu vizuri, jifunze kuongeza thamani yako kwa kufikiria namna unavyoweza kuwasaidia wenzako kufikia malengo yao.

Jambo la kukumbuka ni kuwasaidia wengine kufikia malengo yao, unaweza kujikuta wakati mwingine watu hao wanapata sifa kupitia mgongo wako.

Huna sababu ya kuumia wala kujiona umetumika.

Watu hao mbali na kuwawekea mazingira ya kukulipa fadhila siku nyingine utakapowahitaji, hawatakuwa na sababu ya kushindana na wewe.

Jifunze kuanzia chini

Kwa kawaida watu wanaoanza kazi huwa na matarajio makubwa. Inawezekana ni ndoto za kulipwa mishahara minono itakayobadilisha maisha yako ndani ya muda mfupi.

Ukiacha kipato, kuna mambo ya vyeo. Wafanyakazi wapya hufikiri ni rahisi kukwea ngazi na kupewa madaraka makubwa.

Fikra kuwa unaweza kuanzia juu haraka zinaweza kukuingiza kwenye matatizo yasiyo ya lazima. Kwanza, utakosa uvumilivu wa kufanya kazi chini ya watu wengine kwa kujiona una sifa za kutosha kukupandisha juu kimamlaka. Lakini pia tabia yako inaweza kuonesha papara na kiburi kisicho na sababu.

Unahitaji kuwa mtu wa subira

Jizuie kujipatia sifa za harakaharaka. Ukweli ni kwamba, mafanikio yoyote kazini ni matokeo ya jitihada na bidii zinazoweza kuchukua muda kulipa. Kila aliyefanikiwa leo alianza chini. Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na subira.

Kuwa mwaminifu kwa wenzako

Mazingira ya kazi hayakosi watu wanaopenda kueneza habari mbaya. Utakaa na mtu unayemheshimu wakati wa chai kisha ataanzisha mazungumzo yanayomhusu mtu asiyekuwepo kwenye mazungumzo hayo.

Mara nyingi mazungumzo haya huwa na lengo la kuwabomoa wengine. Tabia hii wakati mwingine hulenga kuimarisha makundi ya kimaslahi kazini.

Kwa kawaida, majungu ni kazi ya watu wasio na kazi; watu wasiojiamini au watu wanaolinda maslahi binafsi kwa kubomoa heshima za wengine. Jambo la kuzingatia ni kuwa hao hao unaopiga nao majungu hukosa imani na wewe.

Jenga utaratibu wa kulinda heshima ya wenzako hata wanapokuwa hawapo kwenye mazungumzo.

Unaposikia habari mbaya za mfanyakazi mwenzako, usiwe mwepesi kushabikia. Habari mbaya zilizobomoa heshima ya mwenzako hazikusaidii kuongeza ufanisi wako.

Badala ya kushabikia mazungumzo yanayomharibia mwenzako asiyekuwepo, tafuta jambo jema na liseme kwa ujasiri. Watu wakikufahamu kwa tabia hiyo ya kukwepa kuwa sehemu ya makundi yanayofuga ‘siasa’ za maslahi kazini, utajenga kuaminika kazini. Mbinu chafu zinaposukwa dhidi yako, utakuwa na watu watakaokuwa tayari kukutetea.

Kubali kukosewa na watu

Unajisikiaje unapogundua mtu uliyemheshimu anasuka mpango wa kukuchafua na kukuharibia heshima yako? Je, utafikiria kulipa kisasi au kuachana naye na kuendelea na hamsini zako?

Ofisi hukutanisha watu wenye mawazo na hulka tofauti. Unaweza kujitahidi kuishi vizuri na watu, lakini bado wakawapo watu watakaochukulia wema huo kama sababu ya kukosana na wewe.

Hali hii isikuvunje moyo. Jichukulie kama binadamu anayeweza kuchukiwa bila sababu na mtu yeyote.

Jichukulie kama mtu anayeweza kufanyiwa visa na watu wenye kutumia mbinu chafu kufikia malengo yao. Ukielewa hivyo, hutapata shida unapogundua kuna watu wanakuzunguka.

Kufanya hivyo, hata hivyo, haimaanishi kukubali kuonewa bila sababu.

Hapana. Jenga ukomavu wa kufanya kazi na watu wasiokupenda bila kuathiri kazi zako.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

Friday, December 15, 2017

Zijue Faida za kuingia ubia kwenye biashara mbalimbali

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi kelvinmwita@gmail.com

Mwaka jana haukuwa mzuri kibiashara kwa marafiki wa karibu; Mushi na Brian ambao walikuwa wakifanya biashara zinazofanana katika maeneno tofauti mjini Moshi.

Wote walikuwa wakimiliki maduka ya kuuza nguo yaliyokuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

Gharama za uendeshaji zilikuwa zikiongezeka na faida ilikuwa ikipungua kila mwezi. Marafiki hawa walishauriana na kuamua kufunga biashara zao.

Je unadhani hilo lilikuwa suluhisho?

Jibu ni rahisi, hilo halikuwa suluhishi, bali moja ya njia ambayo Mushi na Brian wangeitumia ni kuunganisha mitaji yao ili biashara iendelee.

kuna methali ya Kiswahili isemayo kidole kimoja hakivunji chawa.

Kuanzisha na kufanya biashara kimekuwa siyo kitu rahisi kwa watu wengi kutokana na changamoto nyingi ikiwamo ya ushindani na gharama za uanzishaji na uendeshaji.

Watu wengi ukiwauliza kwa nini hawajaamua kuanzisha biashara ziwasaidie kutatua tatizo la ajira au kuwaongezea kipato kingine, sababu kubwa wanasema ni mtaji mdogo au kukosa mtaji wa biashara.

Ubia ni moja ya njia nzuri za kukabiliana na changamoto kama hizi.

Ubia ni mapatano ya kibiashara yanayohusisha zaidi ya mtu mmoja kwa kuchanga mtaji, rasilimali na nguvukazi kisha kugawana faida au hasara ya biashara hiyo.

Wabia huchanga mtaji au rasilimali kwa viwango sawa au vinavotofautiana na faida hugawanywa kulingana na mchango wa kila mbia.

Urasimu mdogo katika uanzishwaji wake

Moja ya mambo yanayokatisha tamaa katika kuanzisha biashara ni urasimu hasa katika mchakato wa usajiri.

Ukilinganisha na uanzishwaji wa kampuni, ubia hauna mahitaji mengi ya kisheria katika uanzishwaji wake. Hii inatoa fursa kwa watu wa kawaida kumiliki biashara kwa pamoja.

Kugawana gharama za uanzishaji na uendeshaji wa biashara.

Methali ya umoja ni nguvu inaelezea vizuri faida ya ubia katika biashara.

Gharama za kuanzisha biashara mara nyingi siyo rahisi kuzimudu kwa watu wengi, lakini ubia unatoa fursa kwa kila mbia kuchangia mtaji kutokana na makubaliano na kufanya upatikanaji wa rasilimali kuwa rahisi zaidi. Uendeshaji wa biashara pia una gharama zake nyingi kama kodi na ushuru, matangazo, malipo kwa wafanyakazi na mengineyo.

Kugawana kwa gharama hizi kwa wabia kunapunguza mzigo mkubwa wa gharama ambao mtu mmoja angeubeba peke yake.

Mchango wa mawazo na ujuzi kutoka kwa watu tofauti

Uwapo wa mtu zaidi ya mmoja kwenye biashara kunaongeza uwezekano wa kupata mawazo ya kibishara yaliyobora zaidi.

Kwa kuzingatia ukweli kwamba binadamu tumetofautiana na tumezidiana maarifa, uzoefu, uwezo wa kufikiria, ubunifu na mambo mengine mengi, wabia katika biashara wanaongeza uwezekano wa kufanya maamuzi bora na yenye tija kwenye mustakabali wa biashara zao.

Mgawanyo wa athari ya kushindwa kwa biashara

Biashara yoyote ile ina vihatarishi vyake. Si biashara zote ambazo hufanikiwa hivyo kunauwezekano wa kushindwa kuendelea. Endapo hili litatokea madhara au athari zake hugawanywa kwa wabia pia hivyo maumivu yake sio makubwa kama biashara hiyo ingefanywa na mtu mmoja.

Ulipaji wa kodi hautozwi kwenye biashara yenyewe

Katika ubia kodi hulipwa kama ilivo kawaida kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini utaratibu wa malipo ni wa tofauti ukilinganisha na ule unaofanywa na makampuni.

Wakati kampuni linalipa kodi kutokana na faida inayopata, kwenye ubia kila mbia hulipa kodi kutokana na gawiwo alilolipata kutokana na faida iliyopatikana kwenye ubia huo.

Hii inamaanisha kuwa kiwango cha kodi kitatofautina kwa kila mbia kutokana na faida aliyoipata ambayo nayo hutokana na kiwango cha mchango (hisa) katika ubia huo.

Urahisi katika utunzaji wa kumbukumbu za kifedha

Mahitaji katika uandishi na utunzaji wa kumbukumbu za kifedha unaohitajika katika makampuni ni mkubwa zaidi kwenye makampuni.

Katika ubia mchakazo hauhitaji urasimu mrefu na mgumu kwani mahesabu yanaweza kuandaliwa na wabia kwa mfumo ulio rahisi kuumudu.

Pamoja na ukweli kwamba ubia unafaida zake lakini pia una changamoto kadhaa zinakabili aina hii ya biashara.

Mbia anaweza kushtakiwa kama mtu binafsi kutokana na anachofanya hata kama kinahusiana na biashara.

Hii inamaanisha mbia mmoja anaweza kushitakiwa mahakamani na wengine kuachwa kwa sababu ya tuhma zozote zile.

Endapo biashara itafirisika au kuwa na madeni gharama zinaweza muathiri mbia moja kwa moja kwa kutakiwa kuzilipa gharama hizo.

Hii inaweza kupelekea hata kupigwa mnada kwa mali za mbia au wabia kulingana na kiwango cha umiliki katika biashara yao.

Biashara ya aina hii pia inaweza kuyumba na kumuathiri mbia moja kwa moja endapo mmoja wa wabia ataamua kujitoa au kupoteza maisha.

Angalizo

Mara nyingi mfumo huu kibiashara ili uweze kufanikiwa unahitaji watu wanaofahamiana na kuaminiana kwani kosa la mbia mmoja linaweza kuathiri biashara na kumuathiri mbia mwingine moja kwa moja.

Ubia unahitaji watu wenye moyo wa kujitoa na kuipenda biashara yao ili kuweza kuweka jitihada za kutosha kwenye kuifanya istawi na kuzidi kuendelea.

Uwazi katika kufanya maamuzi pia ni moja ya vitu muhimu katika mafanikio ya ubia kwani endapo mmoja ya wabia atahisi kuwa anatengwa au hashirikishwi kwenye maamuzi inaweza kumvunja moyo na kupunguza umoja na ushirikiano vitu ambavyo ni muhimu sana katika kufanikisha biashara ya aina hii.

Ikumbukwe kuwa aina hii ya biashara inahiataji usimamizi wa karibu sana hivyo wabia wanatakiwa wawe na kiwango cha juu cha nidhamu ya kibiashara na kuwa tayari kufanya ufuatiliaji wa karibu.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, 0659081838, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com

Friday, December 8, 2017

Uhusiano wa ufaulu wa darasani na mahitaji ya soko la ajira

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi kelvinmwita@gmail.com

Nilipokuwa nikianza masomo yangu ya Shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Mzumbe niliwatafuta watu kadhaa wanishauri. Lengo langu lilikuwa ni kujua nitumie mikakati ipi ili nifanye vizuri kwenye masomo yangu. Wapo walionishauri kuwa chuoni ufaulu sio kitu cha muhimu sana hasa katika kupata ajira, huku wakinipa mifano ya watu waliokuwa na matokeo ya kawaida lakini wameshapata kazi huku wale waliofanya vizuri wakiendelea kutafuta kazi mtaani. Wengine walinithibitishia hakuna uhusiano kati ya ufaulu mzuri na ufanisi kazini.

Nilifanikiwa pia kukutana na watu hasa wanafunzi waliokuwa mwaka wa pili na watatu walionishauri nisome kwa bidii ili nipate alama nzuri darasani. Watu hawa waliniambia ufaulu mzuri unafaida nyingi sana.

Baada ya muda niligundua walionishauri kuwa ufaulu mzuri hauna maana sana kwa ngazi ya chuo kikuu walikuwa hawafanyi vizuri sana darasani na wale walionishauri niweke bidii kwenye masomo, walikuwa na ufaulu mzuri.

Baada ya muda niligundua wanafunzi wengi hukosa watu wa kuwashauri hasa kwenye masomo yao au pengine hushauriwa vibaya na hivyo kukosa motisha ya kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Hivi sasa, vijana waliomaliza kidato cha sita na viwango vingine vya elimu wameshaanza masomo ya chuo kikuu katika ngazi mbalimbali huku wengine wakiendelea kujiunga na taasisi hizo.

Huu ni muda muafaka wa kuwashauri vijana hawa juu ya umuhimu wa kuwa na ufaulu mzuri.

Ufaulu na Upatikanaji wa ajira

Kuna vigezo kadhaa ambavyo waajiri huangalia pindi wanapotaka kumuajiri mtu yeyote, ufaulu ukiwa ni moja ya vigezo hivyo.

Ukweli ni kwamba, uzito wa vigezo unatofautiana kati ya kazi moja na nyingine.

INAENDELEA UK 24

INAENDELEA UK 24

Kwa kazi ambazo zinavutia watafutaji ajira wengi, ufaulu unaweza kutumika kama kigezo cha kuchuja watafuta ajira. Na zipo kazi ambazo huanisha kiwango cha ufaulu ambacho muombaji anatakiwa awenacho.

Yapo mashirika mengi sana ambayo huweka viwango vya ufaulu kama moja ya vigezo ambavyo waombaji wanatakiwa wawenavyo ili kupata ajira. Hii inaonesha kuwa watu wenye viwango vizuri vya ufaulu wana nafasi kubwa ya kupata ajira hizo kuliko wale ambao hawana viwango hivyo. Hii hupunguza ushindani katika kutafuta ajira ukizingatia kuwa soko la ajira limekuwa na ushindani zaidi ya kipindi chochote kwenye historia.

Ikumbukwe kuwa katika kusaili waombaji ajira mashirika mengi hutoa mitihani kabla ya usaili wa mahojiano. Hii pia inatoa fursa kwa watu wanaotia juhudi kwenye masomo yao na kujua mambo mengi juu ya taaluma zao na hata yale ya nje ya taaluma zao. Taasisi nyingi pia zinazotoa ufadhili katika ngazi mbali mbali za elimu huangalia ufaulu kama kigezo cha kutoa ufadhili.

Ufaulu na Uwezo wa Kujiajiri

Hivi karibuni kumezuka wimbi la watu wengi wanaobeza ufaulu kwa kusema kuwa mara nyingi hawa wanaofaulu vizuri mwisho wa siku huajiriwa na wale waliofanya vibaya darasani au wenye ufaulu wa wastani na wakati mwingine wale ambao hawakumaliza masomo yao kabisa. Wengine wamefika kiwango cha kuwakatisha tamaa wale wenye nia ya kufanya vizuri darasani kwamba eti hata wakifanya vibaya watajiajiri. Ushawishi wao umefika kiwango cha kutoa mifano ya watu walio katiza masomo yao kama Bill Gates (mwanzilishi wa Microsoft), Mark Zuckerberg (mwanzilishi wa facebook), Steve Jobs (Mwanzilishi wa kampuni ya Apple) na wengine bila kuwaelezea uwezo walikuwa nao watu hao katika ujuzi wa vitu walivokuwa wakivifanya ambavyo kwa kiwango kikubwa waliupata shuleni.

Katika mifano wanayotoa uwa hawataji waanzilishi wa makampuni na watu waliofanikiwa kupitia elimu zao na kutambua mchango wa elimu za watu wengi katika kufikia malengo yao. Wengi wanaojiajiri ni wale wenye elimu za kawaida au ufaulu wa wastani kwa sababu nyingi ikiwemo ukweli kwamba mara nyingi wenye ufaulu mzuri sana uwa ni wachache hivyo kwa namna yoyote tutarajie wengi watakao jiajiri ni wale wenye ufaulu mdogo au ule wa wastani.

Pamoja na hayo tukubaliane kuwa bado tunahitajiana katika suala zima ajira na kujiajiri. Mtu anayeanzisha hospitali atahitaji daktari msomi na pengine mbobezi hivyo kujiajiri kwa wenye uwezo mdogo au wastani kusitumike kubeza wale wenye uwezo mzuri darasani au walio ajiriwa. Tuwakumbushe vijana umuhimu wa kujiajiri na kuwatia moyo wengine wafanye vizuri kwenye masomo yao.

Ufaulu na ufanisi kazini

Mjadala wa uhusiano kati ya ufaulu na ufanisi kazini umekuwa ikiendelea kwa miaka mingi kiasi cha kuvutia watafiti mbalimbali. Zipo tafiti zilizoonesha kuwa hakuna uhusiano kati ya ufaulu mzuri na ufanisi kazini. Wapo waajiri wanaolalamika kuwa wale wenye ufaulu mzuri sana uwa hawafanyi vizuri katika maeneo ya kazi. Zipo tafiti pia zilizothibitisha ubora wa wale wenye ufaulu mzuri darasani.

Changamoto za utoaji wa madaraja katika taasisi za elimu ni moja ya maeneo ya kulaumiwa kwani mara nyingi hupima uwezo wa wanafunzi katika nadharia zaidi kuliko vitendo. Pamoja na hayo ikumbukwe kuwa kufanya vibaya darasani hakukupi sifa ya kuwa mfanisi kazini. Wapo wenye ufaulu mzuri na ni wafanisi pia kwani juhudi kwa kila jambo ni muhimu hasa katika kujifunza.

Ufaulu darasani sio kitu pekee chenye umuhimu lakini ni moja ya mambo mengi. Wanafunzi wanashauriwa kuhakikisha wanajiongezea ujuzi kwenye mambo mengi ikiwemo suala la ujuzi wa mawasiliano, ubunifu, ujasirimali na mambo mengine. Ufaulu darasani pekee hautoshi kwani tumeshuhudia wataalam wenye elimu zinazoheshimika wakitia hasara mashirika na hata nchi kwa kufanya maamuzi yasio na tija wala maslahi kwa taasisi zao.

Ifahamike kuwa kuajiriwa pekee hakutoshi katika kuwa na uhuru wa kifedha. Kuna haja ya kuhakikisha waajiriwa wanajiongezea vyanzo vingine vya mapato kama biashara na kilimo kwani mahitaji yameongezeka sana kiasi kwamba ujira kutoka kwenye kazi za kuajiriwa kushindwa kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.

Mwisho, lengo la elimu sio kutajirisha wanufaika wa elimu bali kuwapa uwezo wa kutatua changamoto mbali mbali katika jamii. Tusiangaike kutafuta uhusiano kati ya utajiri na elimu bali elimu na ufumbuzi wa changamoto tunazozikabili ajira ikiwa ni moja tu ya changamoto nyingi.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, 0659 081838, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com

Friday, December 8, 2017

Yajue makundi matano ya watu hatari kazini

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Tunaweza kukubaliana kwamba mafanikio anayoyapata mtu kazini kwake, mara nyingi yanategemea vile anavyoweza kutengeneza mazingira mazuri ya kupata ushirikiano wa karibu miongoni mwa wafanyakazi wenzake.

Mfanyakazi anapojichukulia kama ‘jeshi la mtu mmoja’ linalojitosheleza kila idara, anajiweka kwenye hatari ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu.

Pamoja na juhudi unazoweza kuzifanya katika kuhakikisha unashirikiana vizuri na wenzako kazini, zipo nyakati ambazo watu wanaokuzunguka wanaweza kuwa kikwazo cha kupiga hatua kwenda mbele.

Mara nyingi watu hawa huwa na tabia zinazochukuliwa kama za kawaida lakini zenye nguvu kubwa ya kumharibia mtu si tu mtazamo wake kazini, lakini pia hata utendaji wake wa kazi.

Makala haya yanaangazia makundi matano ya watu unaohitaji kukaa nao mbali kwenye eneo la kazi kuepuka kuhatarisha ufanisi wako.

‘Mwanaharakati’

Huyu ni mfanyakazi anayetafuta sifa nyepesi kwa kujipa kazi ya ‘kutetea’ haki za watu. Sifa yake kubwa ni ujasiri alionao wa kuwakosoa viongozi wake hadharani.

Ingawa kuna mazingira ambayo namna pekee ya kufikisha ujumbe inaweza kuwa ni ‘kumlipua’ bosi hadharani, lakini inapokuwa ndiyo tabia ya mtu kusubiri mikusanyiko ya wafanyakazi ‘kulipua’ mambo, hapo lazima kunakuwa na tatizo.

Lakini pia, ‘mwanaharakati’ ana tabia ya kufanya kampeni za chinichini kupingana na wakubwa zake kazini. Kinachomsumbua ni kiu ya kutaka kutumia matatizo ya kampuni kujipatia umaarufu.

Mara nyingi watu wa namna hii hawafiki mbali kwa sababu mbili. Kwanza, hutumia uanaharakati kuficha upungufu wao binafsi wa kikazi. Ili kujiweka kwenye mazingira salama, hutumia kichaka cha kuwabomoa wengine.

Lakini pia hawafiki mbali kwa sababu faida ya kuonekana wajuaji kwa muda mfupi, huwagharimu baadaye. Hujenga chuki isiyo ya lazima na wakubwa wa kazi na hivyo hujinyonga kwa mikono yao wenyewe.

Wakati mwingine wanaofanya uanaharakati maofisini ni watu wenye historia za siasa za vyuoni.

Wanafikiri kuwasema wakubwa mbele za watu kunasaidia kurekebisha hali ya mambo.

Pamoja na umuhimu wa kudai haki, kuna haja ya kujifunza kufuata utaratibu unaokubalika.

Hata katika mazingira ambayo taratibu rasmi hazionekani kuleta majibu, tafuta suluhu kwa njia zinazoheshimu utu na heshima ya unaowadai haki.

Maneno mengi

Hawa ni watu ambao ukiwasikiliza kwa haraka haraka utaamini ‘wanajua’ kila kitu.

Watakueleza kwa undani mambo usiyoyategemea lakini kwa kawaida huwa hawafanyii kazi kile wanachokisema.

‘Maneno mengi’ wanapenda sana kuongea vikaoni hata kama hakuna ulazima wowote wa kuongea. Hupenda kuchangia kila hoja muhimu ni kushibisha njaa ya kutambulika wanayokuwanayo.

Hawa ndio watu wanaoweza kukufuata ofisini muda wa kazi na kukaa wakizungumza kitu kisicho na dharura yoyote.

Wakati mwingine unaweza kuwaonesha ishara kwamba unahitaji kuendelea na kazi lakini wasielewe. Muhimu kwako ni kuongea.

Mtu wa namna hii ni hatari kwa sababu kubwa mbili.

Kwanza, anaweza kukujengea taswira ya maisha asiyoyaishi ukajikta unaiga kisichokuwepo.

Pili, ukimpa nafasi kubwa anaweza kupoteza muda wako kusikiliza mambo yasiyoongeza tija kwenye kazi yako.

Mlalamikaji

Si kazi rahisi kumridhisha mtu mlalamishi. Huyu ni mtu anayejiona ana haki ya kupata zaidi ya kile anachostahili.

Mara nyingi si mtu anayejituma sana lakini anatamani kuona watu wengine wakijituma kwa faida yake.

Hawa huwa wepesi kuwalaumu wengine mambo yanapokwenda mrama. Ukiongea naye kwa dakika mbili, atakwambia nani amemwonea, nani hamtakii mema, nani ni kikwazo kwake. Hata siku moja hawezi kukwambia yeye amechangia nini kwenye matatizo aliyonayo.

Mtu mlalamishi mara nyingi huwa hana majibu ya kile anachokilalamikia. Ukimwuuliza tufanye nini kurekebisha hali anayoinung’unikia, ataishia kutoa majibu ya jumla, “mfumo”, “Serikali”, “Kampuni” bila kusema ni kwa namna gani.

Ukimpa nafasi mtu wa namna hii, utajiingiza kwenye tabia ya uvivu hatua kwa hatua.

Utaanza kutarajia zaidi kwa wengine kuliko kuwajibika na utataka ufanyiwe kuliko unayotimiza wajibu wako. Huwezi kufanikiwa kwa mtindo huu.

Anayependa kukosoa

Huyu anaona mapungufu kwa karibu kila kitu na kila mtu.

Ni vigumu kumridhisha kwa sababu hana tabia ya kuona jema la mtu na akalikubali.

Hawa si walipuaji, kazi yao kubwa ni kukatisha tamaa watu. Ukikaa nae dakika mbili ameshakwambia ubaya wa kampuni, taasisi au mtu anayeonekana kufanya kazi kwa bidii.

Bila shaka unawafahamu watu wanaoweza kukwambia kwa nini mshahara mnaolipwa na kampuni hautoshi na kwamba kuna mahali wanalipa zaidi lakini ajabu hawaachi kazi.

Tabia ya mtu kulalamika mara nyingi hutokana na kukata tamaa kunakofanya wasiishi na uchungu usioisha.

Hawa ni watu wanaofanya kazi wasizozipenda na hawana namna ya kutimiza ndoto zao.

‘Jembe sifa’

Huyu ni mtu anayechapa sana kazi kwa lengo la kuonekana kwa wakubwa kazini. Mara nyingi ni mtu anayeonekana kujiamini sana kwa nje lakini ndani yake ana wasiwasi na usalama wake.

Huwa anakuwa na tabia ya kujikomba kwa bosi, mara nyingine kwa kuwasema vibaya wafanyakazi wenzake.

Katika mazingira ambayo bosi mwenyewe naye hajiamini, watu wa namna hii wana nafasi kubwa ya kuaminika sana kazini.

Tabia ya kupenda sifa huenda sambamba na tabia ya kushindana na watu ambao wakati mwingine hata hawashindani naye.

Mtu mshindani haridhiki kufanya vizuri bali hutaka kufanya vizuri kuliko wengine wote.

Unapokuwa karibu na mtu wa namna hii atakuharibia kazi kwa sababu si tu atakunyong’onyeza bila sababu, lakini pia atakufanya ujisikie huwezi, huna thamani unayofikiri unayo na utajiona dhalili.

Ambatana na watu wanaojituma kufanya kazi kwa bidii, lakini wasio na muda wa kusubiri sifa ili wafanye kile wanachokifanya.

Tafuta watu wasio na sababu ya kujilinganisha na wewe.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815

Friday, November 24, 2017

Malengo ya elimu yaoanishwe na mahitaji ya vijana kujiajiri

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

       Katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, kundi kubwa la vijana waliohitimu vyuo linaingia rasmi kwenye soko la ajira. Wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo hutumia kipindi hiki cha mahafali kuwaasa vijana ‘kufikiri nje ya boksi’ kwa maana ya kutafuta namna wanavyoweza kujiajiri.

Matamko haya ambayo mengi ni ya kisiasa, yanachochewa na tatizo kubwa la ajira linaloikabili nchi yetu.

Inakadiriwa kwa mfano, kila mwaka takribani watu wapya 1,000,000 huingia kwenye soko la ajira wakitafuta ajira.

Katika mazingira ambayo soko hili haliwezi kutengeneza nafasi za kazi kwa watu 100,000 kwa mwaka, ni wazi kwamba watunga sera na wafanya uamuzi wanalazimika kuwaasa vijana ‘kuacha kutegemea Serikali iwapatie ajira.’

Elimu inayowaandaa kuajiriwa

Pamoja na ushauri mzuri kwa vijana kujiajiri, ni vizuri tukijiuliza kama kweli tumewapa vijana elimu itakayowawezesha kujiajiri.

Chukulia kijana aliyesoma sayansi ya siasa. Tunapomshauri ajiajiri, tunakuwa na maana gani? Tunataka afungue biashara gani hasa inayoweza kuendeshwa kwa kutumia elimu yake aliyopata darasani?

Huo ni mfano mmoja. Tunafahamu, kwa mfano, program nyingi zinazotolewa kwenye vyuo vyetu haziwapi vijana mwangaza wa kujiajiri. Programu hizi, wakati mwingine huandikwa kwa lengo tu la kujaza orodha ya shahada zinazotolewa vyuoni, lakini hakuna utafiti wa kina unaofanyika kujua mahitaji halisi ya jamii.

Vijana huchagua kusoma programu hizo wakiwa na matarajio makubwa lakini kimsingi, hawajui watafanya nini na hicho wanachokijua nje ya darasa.

Tunapowaasa vijana watumie elimu yao kujiajiri, ni sawa na kuwadhihaki. Wapo vijana wenye uthubutu wanaoamua kuzitelekeza fani zao ili kufanya ujasiriamali na uchuuzi bila kutegemea ajira. Lakini hata wanapofanya hivyo, bado mazingira ya kazi huwakatisha tamaa tangu hatua za mwanzo.

Mlolongo wa tozo na kodi zisizozingatia mtaji mdogo ambao wakati mwingine analazimika kuazima kwa ndugu, jamaa na marafiki ni moja wapo ya orodha ndefu ya vikwazo anavyokabiliana navyo kijana mjasiriamali. Kwa maana hiyo, pamoja na nia njema ya kuwataka vijana wajiajiri ni vyema tukajiuliza ni kwa kiasi gani tumewaandalia mazingira ya kuitikia wito huo muhimu.

Elimu bora ni mtaji

Namna moja wapo ya kuwawezesha vijana kujiajiri ni kuwapa elimu inayokidhi matakwa ya wakati ulipo. Kijana aliyepatiwa elimu bora anaweza kuitumia kama mtaji utakaomwezesha kujiajiri.

Lakini je, elimu tunayompa kijana inamwandaa kujiajiri kama tunavyomshauri? Je, kijana aliyemaliza shahada ya kwanza anaweza kutumia maarifa aliyoyapata darasani kuendesha shughuli zake bila ajira?

Pamoja na ukweli kwamba dhima kuu ya elimu ni kupanua uelewa wa jumla wa kijana, pengine kuna haja ya kuifanya elimu yetu imsaidie kijana kujenga uwezo wa kuona matatizo yanayoikabili jamii na kuyatafutia ufumbuzi.

Ikiwa ndivyo hivyo, elimu inaweza kutumika kama mtaji.

Hivi sasa mwelekeo wa jumla wa elimu nchini ni ya kuchuja wanafunzi ili kupata wataalamu wachache watakaofikia ngazi ya juu zaidi ya elimu. Tunafikiri tija ya elimu inapatikana kwa kufika chuo kikuu. Mtazamo huo kwa bahati mbaya hauwezi kutatua tatizo kwa sababu kuu mbili.

Kwanza, wanafunzi wengi wanachujwa katika ngazi za chini na kuachwa bila ujuzi wowote wa maana.

Watu hawa ambao ndiyo wengi, wanalazimika kutafuta namna nyingine ya kuishi bila kutumia kile walichojifunza darasani.

Kadhalika, wale wachache wanaoendelea na elimu ya juu, wanajengewa mtazamo kwamba wao ni kundi maalumu katika jamii linalostahili ajira yenye hadhi.

Lakini bahati mbaya wengi wao humaliza shahada ama wakiwa na ujuzi nusu au hukosa kabisa ujuzi huo unaowezesha kufanya shughuli bila kuajiriwa lakini matokeo yake nao kama wale waliochujwa katika ngazi za chini, wanalazimika kutafuta nafasi za kazi kwa sababu msamiati wa kujiajiri hautekelezeki.

Elimu ya kujitegemea

Tunahitaji kubadili mwelekeo wa elimu yetu kutoka kumwandaa kijana kufanya kazi za mwajiri mpaka kujiajiri. Tangu mwanafunzi anapoanza masomo, aandaliwe kutumia hicho anachojifunza kama njia ya kujiongezea kipato hata pale anapojikuta nje ya mfumo wa ajira.

Mwalimu na mwanafunzi kwa pamoja wafanye kazi ya kutafsiri maudhui ya mitalaa yetu ili ngazi yoyote ya elimu imsaidie mwanafunzi kuona fursa katika mazingira yake bila kulazimika kupatiwa mafunzo mengine ya ziada.

Kijana anayejengewa uwezo wa kuona na kutatua changamoto, mkononi mwake anakuwa amekabidhiwa ufunguo unaobeba thamani yake. Kwa kuutumia ufunguo huo, kijana huyu hawezi kukosa kazi ya kufanya akirudi kwenye jamii.

Ili hilo liwezekane, mamlaka za elimu zinawajibika kufanya utafiti utakaowezesha kutengeneza programu zinazojibu matatizo halisi yanayoikabili jamii.

Ni kweli kwamba mahitaji ya jamii yana tabia ya kubadilika. Kinachoonekana muhimu leo, si lazima kiwe muhimu kesho. Maana yake ni kwamba, mwanafunzi hapaswi kutegemea kupata maarifa yaliyo tayari kwa matumizi.

Kazi ya kuyafanya maarifa hayo yatumike kutatua changamoto za kila siku zinazoikabili jamii inabaki kuwa ya mwanafunzi mwenyewe. Ni wajibu basi wa mwanafunzi mwenyewe kuhakikisha anajua kwa hakika kile anachokitaka ili aweze kuchagua eneo la kitaaluma linalokidhi wito alionao ndani yake.

Aidha, ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi kuoanisha mazingira halisi ya kazi na ujuzi unaotolewa darasani. Ufundishaji ulenge kuwafanya wanafunzi waione jamii yao wakiwa darasani badala ya kuwafundisha mambo ya kufikirika wasiyoyaona katika maisha yao ya kila siku.

Sambamba na hilo, tutafakari sababu iliyotufanya tupanue elimu ya juu na kupunguza uzito wa vyuo vya kati na vyuo vya ufundi. Kasumba kwamba kufika chuo kikuu ndiyo kipimo cha kuelimika, inachangia kukuza tatizo la ukosefu wa ajira.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815     

Friday, November 24, 2017

Unapaswa kulinda wasifu wako katika ushindani wa sasa wa ajira

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

       Dunia imetekwa na vita ya ushindani katika kila jambo hivi sasa. Hivyo, ni muhimu kwa kila mtu kutambua kila jambo unalofanya kuwa limezungukwa na mamilioni ya watu wenye uwezo wa kulifanya pengine kuliko ulionao.

Je umewahi kufikiria wasifu wako una uhusiano gani katika mwelekeo wa kufanikisha malengo, ndoto au mahitaji yako kwa hapo baadaye? Au umekuwa ni mwaathirika wa tamaa ya kuishi maisha ya watu wengine!

Wataalamu wa kazi wanasema kila mfanyakazi anabebwa na wasifu wake katika ajira yake.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuna makosa mengi yanayofanyika katika mbio za kusaka au kulinda ajira, pengine kwa kutokujua au kwa tamaa ya kujaribu kuishi wasifu wa wafanyakazi wengine.

Inawezekana wasifu wako haujatimiza ndoto zako licha ya juhudi za kujituma, uwezo na uchapakazi kwa miaka zaidi ya 20.

lakini kuna watu wengine wanafanya vizuri licha ya kuwa pamoja katika taaluma hiyo unayofanyia kazi.

Hatua hiyo inatokana na jinsi watu wanavyokufikiria, wanavyokuona na kukutafsiri katika utendaji wako wa kazi bila kujali unakubaliana nao au la.

Suala la utambulisho wa wasifu limeathiri maelfu ya wafanyakazi na wafanyabiashara.

Dosari hizo ni rahisi kuziepuka na kubadili mazingira yote yanayohusisha kuanzia mtazamo wa watu katika maisha yako, mazungumzo na vitendo au vinginevyo.

Katika makala haya, tutaangalia njia tatu zitakazosaidia kulinda au kutengeneza wasifu wako utakaosaidia kukutambulisha wewe ni nani, unaamini katika nini na unataka nini.

Watu watataka kufahamu kutoka kwako ili kujenga mtazamo chanya utakaokusaidia kufikia ndoto zako.

Kuwa wa kipekee

Hatua ya kwanza katika kutengeneza wasifu ni kuishi maisha yako. Kuna mabilioni ya watu duniani wanaoshindana kuitafuta ajira moja tu uliyonayo au mteja mmoja unayemtegemea katika bidhaa yako unayoiuza.

Lakini changamoto huja pale unapohitaji kujua ni kwa jinsi gani unahitaji kuwa wa tofauti katikati ya mabilioni ya hao.

Hata hivyo, tunaambiwa kutumia mbinu na ubunifu unaofanywa na wengi hauwezi kukufanya uonekane.

Kumekuwa na tatizo kwa mfano, kampuni X imekuwa bora katika ubunifu wa mavazi ya asili, lakini miezi kadhaa imehamia kwenye vazi linaloandaliwa na mbunifu mwingine eti kwa sababu limeteka soko kwa wakati huo.

Mfano mwingine ni mtangazaji Y wa vipindi vya Luninga ambaye leo ataonekana akitangaza kipindi cha ujasiriamali na kesho ataonekana akitangaza kipindi cha mitindo na urembo. Hii inaathiri kwa sehemu kubwa juhudi za kujenga wasifu.

Huu ni wakati wa kuanza kujitambulisha kwa upekee wako katikati ya ushindani wa maelfu ya wateja au wafanyakazi wenzako.

Hii pia inaweza kuwa muhimu katika jambo linalohusu ukuaji wako kibiashara au mahali pa kazi.

Hatua nyingine ni kuanza kuainisha vitu unavyodhani vinaweza kukufanya uwe wa tofauti kwa wengine.

Kwa mfano, unaweza kujitambulisha mbele ya umma kwa ukarimu, uaminifu, uchapakazi, ubunifu au uwazi.

Hakikisha njia hizo unazitumia katika kufanikisha malengo ya kukuza wasifu wako.

Kumbuka hatua hiyo ni sehemu ya kukutenganisha na wasifu wa wafanyakazi wengine ambao ni washindani wako.

Tafuta maarifa kwa njia mbalimbali yatakayokusaidia uwe wa tofauti kibiashara au mahali pa kazi.

Kuwa mbobezi wa jambo moja tu

Jambo hili ni muhimu unapojitambulisha kwa washindani au wafanyakazi wenzako kwamba, wategemee nini kutoka kwako.

Hauwezi kuwa bora kwa kila kitu, kwa hiyo, chagua eneo moja unaloamini kuwa bora zaidi na uanze kujisomea kila kinachohusika katika kuongeza thamani yako.

Kujitambulisha kama mtaalamu pekee haitoshi kukuza wasifu wako, lakini unahitaji kuthibitisha utalaamu huo kwa kushiriki maarifa hayo kwa wafanyakazi wenzako.

Kwa mfano, wewe ni mwandishi wa habari, umesoma taaluma ya habari lakini umechagua kuandika habari za biashara pekee.

Hakikisha unajitambulisha nafasi hiyo kwa wafanyakazi wenzako, rafiki, familia na jamaa wanaokuzunguka.

Utakapokuwa na utayari wa kufanya jambo hilo mahali pa kazi, ndiyo inavyokujengea ubobezi na wasifu wako.

Hautakosa washindani lakini ni muhimu kutafuta maarifa zaidi yanayohusiana na eneo hilo.

Kama ni fundi, hakikisha ni ufundi wa bidhaa gani. Hakikisha unakua mbunifu katika kila kitu unachotaka kukitengeneza.

Pia, hakikisha unapata taarifa za kutosha na mpya zinazoendana na mahitaji ya soko la kiatu chako. Kuna vyanzo mbalimbali vinavyosaidia kupata taarifa zinazokuhusu.

Unaweza kutumia tovuti au mitandao ya kijamii kujiunga na wafanyakazi wanaohusiana na kazi unayoifanya.Unaweza kujiunga na mitandao ya wawezeshaji, mitandao ya mashirika, wadau na ushiriki wa majukwaa mbalimbali yanayohusu eneo ulilochagua kufanyia kazi.

Mwisho katika kubobea kwenye eneo hilo, ni muhimu kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya kupata taarifa za wakati husika.

Hatua hiyo inahitaji kujitoa na kutenga muda ili uwe bora katika eneo unalohitaji kujenga wasifu wako.

Ishi katika jambo unalofanya

Hatua ya tatu ni mwendelezo wa kuuishi wasifu huo. Hatua hiyo imekuwa ni changamoto, kulinda wasifu usiporomoke au usiingie doa mahali pa kazi.

Kwa mfano, kumekuwa na makosa ya kujisahau au kutokutambua pale tunapokuwa tunajenga wasifu kupitia mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook, LinkedIn na tovuti.

Kwa bahati mbaya au kwa kutotambua, mfanyakazi au mfanyabiashara anayeweza kuweka picha nne zenye ujumbe na mitazamo tofauti katika mitandao ya kijamii.

Hii ni hatari kwa mtu anayetaka kulinda wasifu wake.

Kwani taarifa zozote utakazosambaza mitandaoni, lazima ziwe katika uhusiano na kazi au ajira unayoifanya.

Kwa maana ya kwamba, wasifu wako uakisi maisha yako halisi mitandaoni katika kila picha na ujumbe unaouweka.

Tuwasiliane kwa simu 0716186074     

Friday, October 6, 2017

Mambo matano yanayomfanya mfanyakazi afurahie kazi yake

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Nianze kwa kukuuliza swali rahisi. Kitu gani kinakupa motisha ya kuamka asubuhi na kwenda kazini?

Unafikiri nini hasa kinaongeza thamani ya kazi yako?

Kwa mujibu wa utafiti, takribani asilimia 80 ya watu wanaofanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri hawajitoshelezi.

Kuna mambo mengi yanachangia watu kutokupenda kazi zao. Kuna migororo kazini, kutokufikia matarajio waliyokuwa nayo na wakati mwingine mazingira hafifu ya kazi.

Sababu nyingine ni kutokuona namna gani kazi anayofanya mtu inakidhi malengo mapana ya maisha yake.

Katika mazingira haya, ni vigumu kuona thamani ya kazi yake na hivyo itakuwa vigumu kutosheka na kipato akipatacho.

Mtu anayependa kazi yake mara nyingi anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwa mbunifu, kuwa na bidii zaidi na hivyo kupata matokeo mazuri kuliko mtu anayesukumwa kufanya kitu asichoona thamani yake.

Kwa kuzingatia ukweli huo, katika makala haya tunaangazia maeneo matano yanayoweza kukusaidia kuelewa kwanini kazi unayoifanya inaweza kuwa na thamani usiyoiona.

Unajua wewe ni nani?

Swali hili linaonekana jepesi lakini si kila mtu anaweza kulijibu. Wengi wetu tunapoulizwa sisi ni nani, mawazo yetu yanakwenda kwenye majina yetu. Tunafikiri sisi ni majina yetu.

Lakini ukweli ni kwamba tungeweza kubadili majina yetu na bado tukabaki kuwa sisi. Maana yake sisi ni zaidi ya majina yetu.

Usipojua wewe ni nani, itakuwa vigumu kujua unachopaswa kukifanya.

Utajaribu kujifunza kila ujuzi, utafanya mambo mengi kwa wakati mmoja, matokeo yake hutajipambanua kwa jambo mahsusi litakalokufikisha kwenye kilele cha mafanikio.  

Hatua ya kwanza ya kujitambua ni kujua vitu maalumu ambavyo Mwenyezi Mungu ameviweka ndani yako.

Hapa tunazungumzia vipaji, ujuzi, maarifa na uzoefu ulionao.

Vitu hivi kimsingi ndivyo vinavyobeba utambulisho wako.

Unapolizwa wewe ni nani, maana yake unaulizwa kuubaini uwezo wa kipekee unaoishi ndani yako. Uwezo huu ndio uliobeba thamani yako.

Unafanya nini?

Ingawa sote tunafanya kazi kwa bidii, si kila mmoja wetu anajua kitu gani hasa mahsusi anachotakiwa kukifanya.

Tumezungukwa na mashinikizo ya kila aina yanayojaribu kutushawishi kuchukua uelekeo fulani katika maisha.

Mashinikizo haya, mara nyingi yanatufinyanga kufuata mkumbo unaotulazimisha kukidhi matarajio yasiyokidhi thamani yetu.

Kutokujua kitu kinachobeba thamani ya kazi tunazozifanya, hutufanya tukate tamaa na yale tunayoyafanya hali inayochangia kutukosesha furaha ya kazi.

Hata hivyo, ukizungumza na watu wanaojivunia kazi zao unagundua hawa ni wale wanaojua kwa hakika kitu gani hasa wanachokifanya.

Hawapati shida kujua eneo lipi la maisha wanaliweza zaidi kuliko maeneo mengine.

Wanajua kitu gani wanachokifanya kinachobeba thamani yao.

Hebu jiulize unazo sifa zipi maalumu unazodhani zinakuweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya watu wengine kujifunza kwako?

Je, kazi unayofanya inatumia uwezo na sifa hizo unazoamini unazo?

Unalinufaisha kundi lipi katika jamii?

Kwa asili binadamu ni mbinafsi anayejifikiria yeye na mahitaji yake.

Ndio maana tunapofikiria kazi gani tufanye, mara nyingi tunafikiria namna gani kazi hiyo itakavyotusaidia kuwazidi wengine.

Hakuna ubaya kuwa mbinafsi kwa sehemu. Hata hivyo, watu wanaofurahia kazi zao wanafanya tofauti.

Watu hawa wanakwenda mbele ya mahitaji yao binafsi.

Badala ya kujifikiria wenyewe, wanakuwa na aina fulani ya kundi la watu wanaolenga kulifikia kupitia kazi zao.

Kwa lugha nyingine, watu hawa wanajua nani ananufaika na kile wanachokifanya na hivyo wanatumia ujuzi na uzoefu walionao kuhakikisha watu hawa wananufaika.

Nikuulize swali, unalijua kundi mahsusi la watu wanaonufaika na kazi yako? Akina nani ni walengwa wa kazi yako?

Unatatua tatizo gani?

Furaha ya kazi yako inategemea pia namna gani unaamini kazi hiyo inakufanya kuwa jibu la matatizo yanayowakabili watu wengine.

Usipokuwa na uhakika kazi yako inakuwezesha kutatua tatizo gani kwa watu, kwa hakika, itakuwa vigumu kuifurahia.

Unaweza kuwa na madaraka, kipato, heshima na umaarufu, lakini kama huna hakika kazi yako inakusaidia kutatua shida gani za watu wanaokuzunguka, unaweza kuendelea kujisikia utupu ndani yako.

Je, kazi yako inakuwezesha kutatua tatizo gani? Je, watu unaowalenga wanakabiliwa na changamoto gani ambazo kwa uwezo, vipaji, ujuzi ulionao unaamini unaweza kuwasaidia kuzitatua?

Ukweli ni kwamba, kila kazi inaweza kukupa utoshelevu. Muhimu ni kujua aina ya matatizo unayoyatatua kwa kupitia kazi yako.

Utoshelevu wa polisi, kwa mfano, unategemea namna gani anajua vile anavyowezesha watu kuishi bila hofu ya uhalifu.

Unaleta tofauti gani kwa watu?

Tunaweza kupima mafanikio yetu kwa kipato, mamlaka tuliyonayo, umaarufu lakini kama vyote hivyo haviwasaidii watu wengine kuwa bora zaidi, itakuwa vigumu kujisikia utoshelevu.

Njia rahisi ya kujua nafasi uliyonayo katika jamii ni mchango unaoutoa kuboresha maisha ya watu unaowalenga.

Unapoona maisha ya watu yanabadilika kama matokeo ya kile unachokifanya kupitia kazi yako, ni wazi utapata utoshelevu zaidi.

Ukitaka kujua tofauti unayoileta kupitia kazi yako, jifunze kwenda mbele ya jina la kazi yako. Fikiria matokeo ya kazi unayoifanya katika jamii.

Kwa mfano, kama wewe ni mwalimu wa shule ya msingi, kazi yako ni kuwasaidia watoto kujitambua na kufikia ndoto zao.

Kazi yako ni zaidi ya ualimu. Ukianza kuitazama kazi yako kwa mtazamo huo, unaweza kushangaa namna utakavyokuwa na utoshelevu kuliko mtu anayesema, ‘Mimi ni mwalimu tu.’

Kama wewe ni muuguzi, badala kujibana kwenye jina la kazi yako, jione kama mtu anayefanya kazi ya kuwasaidia wagonjwa kuwa na furaha zaidi wanapopata huduma za daktari.

Kwa kifupi, tukiweza kuzitathimini kazi zetu kwa kuangalia nani tunayejaribu kumsaidia, tutajiongezea uwezekano wa kuwa watu wenye furaha zaidi.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815     

Friday, October 6, 2017

Mbinu mbadala zinazoweza kupaisha kazi za mjasiriamali

 

By Kelvin Matandiko,Mwananchi

Hakuna faida ya kuwa miongoni mwa wajasirimali wanaotengeneza bidhaa nzuri na zinazoweza kufanya vizuri katika ushindani wa soko la ndani na hata nje ya mipaka ya Tanzania, lakini bidhaa hizo hazifahamiki.

Inawezekana umekuwa mbunifu na mara kadhaa umekuwa ukitamani bidhaa yako iweze kufika mbali zaidi ya masoko ulionayo.

Unaweza kuwa na jina kubwa kuliko bidhaa lakini bidhaa yako haijulikani.

Hatua ya bidhaa kufikia watumiaji wengi ndiyo mafanikio ya kazi ya mjasirimali yeyote aliyejiajiri mwenyewe.

Kumbuka, katika ushindani wa soko, hakuna miujiza rafiki.Sasa umekata tamaa au unatumia njia gani kusukuma bidhaa yako iweze kuwafikia walengwa, uongeze kipato na kubadilisha maisha yako kiuchumi.

Kama unamiliki simu ya kisasa, inaweza kukufanya bilionea kupitia jukwaa la watumiaji wa mitandao.

Katika Makala haya, nitazungumzia jinsi gani mjasiriamali anavyoweza kupanua biashara yake kwa kufikia wateja wengi zaidi kupitia matumizi ya kurasa za mitandao ya kijamii.

Panga ratiba ya kazi zako vizuri

Katika saa 24 za siku moja, hakikisha unaweka ratiba itakayokuongoza kuweka na kupokea mrejesho wa matangazo ya bidhaa zako mitandaoni.

Utafiti unaonyesha kurasa zenye idadi kubwa ya watu ni Twitter, Facebook, Instagram. Unaweza kujisajili pia katika kurasa za LinkedIn na zaidi usikose kujiunga na majukwaa ya mawasiliano ya WhatsApp na Snapchat.

Unatakiwa kufungua akaunti hizo kwa sababu ni majukwaa yanayowakutanisha watu mbalimbali ndani ya Tanzania, Afrika na Duniani, watumiaji wa bidhaa na wazalishaji.

Weka ratiba ya kutembelea majukwaa hayo kwa dakika kadhaa asubuhi na jioni ili kupata taarifa mpya, kutuma na kujibu ujumbe. Usipofanya hivyo, dunia itakuacha hatua nyingi nyuma katika ushindani wa bidhaa zako.

Kalenda na muda wa kuingia ni siraha itakayokusaidia kuongeza idadi ya marafiki kwa sababu kuna utafiti mwingi unaonyesha muda wa idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka katika mitandao ya kijamii.

Hakikisha unaweka ratiba vizuri na kujua nini unachotakiwa kusambaza na kwa muda gani.

Kwa mfano, unaweza kufikiria nini unatakiwa kusambaza ndani ya mwezi mmoja ujao.

Unaweza kutumia softwea za kalenda kama eClincher au Hootsuite kwa ajili ya kuhifadhi taarifa zote muhimu kabla ya kuzisambaza mtandaoni.

Tafuta tovuti zinazokuhusu

Usipoteze muda mwingi kuandaa taarifa nyingi kuhusu bidhaa yako kwa ajili ya kutupia mitandaoni kwa wateja wapya unaowahitaji.

Jambo la muhimu ni kutafuta tovuti 10 au 15 zinazoaminika na zinazohusika na utengenezaji wa bidhaa zako.

Kwa mfano, unafanya biashara ya kuuza Korosho. Muhimu ni kuangalia tovuti zenye taarifa mbalimbali kuhusu biashara yako, mbinu za kibiashara ikiwamo namna ya kuyafikia masoko.

Tovuti hizo zitakusaidia kupata taarifa mpya, kuandika na kutupia katika kurasa zako mitandaoni ili kuongeza ushawishi kwa watumiaji.

Zingatia taarifa mpya zenye mashiko kuhusu bidhaa yako katika kila utakachohitaji kutupia kwenye ukurasa wako.

Tengeza ujumbe wa kusambaza

Baada ya kupata tovuti na vyanzo vya taarifa mpya, tengeza ujumbe wa bidhaa kabla ya kuitupia mtandaoni.

Kwa mfano, kama ni mjasirimali wa kuuza mafuta ya nazi, unataka watu wafahamu nini kuhusu ubora wa bidhaa hiyo.

Siyo kila kitu unatakiwa kutupia mtandaoni kuhusu bidhaa yako, hakikisha ujumbe au picha utakayotuma inavutia na inaibua hisia kuhusu ubora wa bidhaa yako.

Bidhaa yako inaweza kuwa bora lakini ujumbe ulioutuma haushawishi watumiaji wapya.

Maoni au mapendekezo, changamoto zitakazoibuliwa na wachangiaji, yatakusaidia kupata mrejesho na jinsi ya kufanyia kazi taarifa ulioituma mtandaoni.

Rudia kusambaza ujumbe tofauti wa bidhaa yako mara kadhaa katika kurasa zako mtandaoni na hakikisha unasambaza wastani wa asilimia 80 ya taarifa zinazohusu ubora na upatikanaji wa bidhaa zako.

Unaweza kusambaza picha, ujumbe mfupi wa kuvutia, vipande vya video ili watu waizoee bidhaa yako machoni.

Watalaamu wa Saikolojia wanasema kitu kinachojirudia kusikika maskioni au kuonekana machoni ndiyo hudumu kwenye akili ya mwanadamu.

Ndiyo maana utajiuliza kwanini matangazo ya simu za mkononi yanarushwa kila baada ya dakika redioni au katika televisheni, sababu kubwa ni hiyo.

Jiondoe kwa kundi lisilokunufaisha

Kumbuka kuna watu muhimu waliokosa mbadala wa kupata bidhaa nzuri kama unazotengeneza. Hivyo, ukifanikiwa kuwafikia maana yake utakuwa umeua soko la washindani wako na utakuwa umeingia kwenye mtandao mkubwa.

Kwa mantiki hiyo, hakikisha unakuwa na marafiki wanaoendana na mahitaji ya bidhaa zako wanaoweza kuguswa kwa karibu zaidi na kazi zako uzifanyazo.

Fanya utafiti wa mtandao kila mwezi

Mabadiliko hufanyika haraka kwa washindani wako wapya wanaoingia mitandaoni. Kila baada ya mwezi, unahitaji ripoti itakayokuonyesha ni posti gani zilifanya vizuri, nani aliyevutiwa zaidi na bidhaa zako, watakupataje, washindani wako ni akina nani na wanakuzidi nini. Usipoandaa ripoti, hautakuza soko la bidhaa yako kwa haraka.

Unaweza kushangazwa na taarifa unazozipata kama mrejesho, itakusaidia jinsi ya kuwa bora na kuongeza ubunifu katika mabadiliko ya soko la aina ya bidhaa yako.

Fuatilia wateja wako

Tafuta tovuti inayotoa takwimu za kimtandao kila wakati. Mtandao wa Swayy, ndiyo unaaminika zaidi katika utoaji wa taarifa za kimitandao ambazo zinaweza kusaidia ufuatiliaji wa karibu taarifa zinazosambazwa mitandaoni.

Wafuatilia hao na waratibu wa mitandao ya kijamii (Swayy), kazi kubwa wanayofanya ni kukusanya taarifa za watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii. Kwa takwimu zilizopo sasa, wanabainisha zaidi ya taarifa 4.75 bilioni zilizoko katika mfumo tofauti zinasambazwa katika mtandao wa Facebook kila siku huku milioni 500 zikisambazwa na twitter kila siku.

Kila mtumiaji anayetumia kibiashara hakosi kufuatilia taarifa zinazohusiana na maslahi yake. Kwa mfano, mameneja, maofisa masoko, maofisa uhusiano, washauri wa kuuza majina ya bidhaa, kampuni au mtu binafsi wanatumia zaidi fursa na wamesambaa kila ukurasa mtandaoni. Hivyo, anza sasa usingoje kesho.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0716186074     

Friday, September 29, 2017

Ijue ‘dawa’ sahihi ya kutokomeza uvivu sugu kazini

 

By Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Kila siku tunaamka asubuhi kwa ajili ya kuanza pilikapilika za kupambana na hali zetu za maisha. Katika mihangaiko hiyo ya kila siku, baadhi yetu wanafanikiwa kutimiza malengo yao na wengine hawafanikiwi.

Siyo kwamba wanaofanikiwa wanafanya kazi dunia nyingine la hasha. Sehemu kubwa ya wanaofanikiwa wanajituma zaidi kikazi kwa kuziishi ndoto zao huku wakitafuta suluhu mbadala kila wanapokumbana na vikwazo.

Upande wa pili wa wale wanaofeli kila mara kuna vitu wanavifanya kinyume na wanaofanikiwa.

Hata hivyo, miongoni mwa sababu kubwa zinazofanya watu wengi wasifanikiwe ni uvivu. Uvivu una hatua za ukuaji. Kuna uvivu unaochipukia, uvivu ‘kijana’ na uvivu sugu.

Kama ilivyo kwa tabia nyingine za binadamu, uvivu unajengwa na mtu husika kutoka ule unaochipukia hadi sugu.

Baadhi ya watu vivu sugu huanza tangu wakiwa watoto wadogo kutokana na malezi hafifu ya wazazi au walezi wao.

Madhara ya uvivu ni makubwa kwa maisha ya mwanadamu kiafya, kijamii na kiuchumi.

Mvivu yeyote anapata shida kuanzia kwenye kuutunza mwili wake hadi kazini kwake. Hakuna jambo litakalokuwa rahisi kwake.

Hata hivyo, uvivu unaweza kutokomezwa na kumrudisha mtu husika katika ari ya uchapakazi na kuchochea mafanikio yake. Miongoni mwa tabia zinazoweza kuutokomeza uvivu sugu ni kuwa na malengo.

Utaratibu wa kupanga malengo unasaidia kupata dira kwa kila myu akifanyacho. Panga malengo katika nyanja zote za maisha kuanzia mipango ya afya, kijamii na kiuchumi.

Weka muda pendekezwa utakaokuwa na ukomo wa kufikia malengo husika. Mfano, kama ni mfanyakazi ainisha malengo binafsi unayotaka kufikia kazini na maisha binafsi.

Kwa malengo ya kazini ambayo mara nyingi huwa na muda maalumu wa kuyafikia, yabainishe wazi na ikiwezekana punguza muda wa kuyafikia.

Fanya hivyo pia kwa malengo binafsi kama ni kuanzisha biashara ndani ya kipindi cha miezi mitatu, ufanye hivyo huku ukitekeleza mikakati ya kulifikia lengo hilo ikiwamo kutafuta mtaji na wateja. Malengo yenye ukomo wa muda wa kuyafikia yanaleta hamasa ya kujituma wakati wote na yanapunguza tabia ya ubongo kujisemea “aaah nitayafikia tu muda bado”.Hamasa hiyo inakufanya muda wote utafute mbadala kwa kila kitu kinachokukwamisha ili mradi ufikie malengo yako.

Tabia hii inaondoa moja kwa moja uvivu sugu unaochelewesha mafanikio kutokana na mawazo ya kuwa siku zote muda upo.

Amka mapema kila siku

Tabia ya kuchelewa kuamka ni moja ya kiashiria kikubwa cha uvivu sugu.

Huanza taratibu na mwisho huwa tabia inayomfanya mtu akose fursa lukuki katika maisha.

Uvivu wa kuchelewa kuamka huwafanya watu kuchelewa kazini na kwenye mikutano. Unafanya watu wafanye vitu kwa haraka bila umakini kwa kuwa wana muda mfupi wa kujiandaa na kutekeleza kazi zao.

Ili niwahi kazini na kupata muda wa kufanya mazoezi asubuhi, mapema mwaka huu nilipanga kuamka Saa 11 alfajiri.

Niliseti simu yangu iniamshe muda huo. Uamuzi huu ulikuja baada ya kujikuta nalala hadi Saa 12.30 asubuhi kiasi cha kunifanya nichelewe kazini siku kukiwa na foleni kubwa.

Nilibaini siku nikichelewa kuamka kiwango cha utendaji kazi pia kinashuka tofauti na siku ninazowahi kufika ofisini.

Japo inakuwa ngumu kwa siku za mwanzo, lakini ukizoea inakuwa sehemu ya maisha yako na unapata muda mwingi wa kufanya kazi.

Mtaalamu wa Baiolojia wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, Christoph Randler 2008 alibaini katika utafiti wake, watu wanaoamka mapema huwa makini zaidi na wanatumia muda mwingi kutekeleza malengo yao kuliko wale wanaochelewa kuamka.

Jihadhari na vikao vinavyopoteza muda

Unaweza kuwahi kuamka ukiwa na malengo madhubuti katika kazi na maisha yako, lakini kwa bahati mbaya mfumo wake wa kushiriki vikao vya kikazi au vya kijamii ukakufanya ushindwe kufikia mipango yako. Tabia ya kuendekeza vikao virefu visivyo na ulazima, hugeuka kuwa uvivu sugu.

Jaribu kufikiri, upo kazini umetingwa na majukumu na ghafla anakuja mtu aliyemaliza kazi zake anaanzisha mazungumzo yasiyo ya kikazi unayojikuta yanaenda zaidi ya nusu saa. Muda huo ambao umeupoteza hauwezi kurudi na haukuwa kwenye mipango yako.

Pia, kuna baadhi ya vikao ofisini huwa virefu bila ya ulazima. Jaribu kushauri wenzio kufupisha ili mpate muda wa kuyatekeleza mnayoyajadili. Jiwekeeni utaratibu wa kuwa na mtunza muda anayekumbusha kila wakati.

Kama wewe ni mwenyekiti wa kikao, hakikisha hamtoki nje ya mada ili kulinda muda. Wajumbe pia mnatakiwa kumkumbusha mwenyekiti juu ya jambo hilo. Ukikaa kimya, wewe ndiye utakayeathirika na upotevu huo wa muda ambao baadaye wakati wa tathmini ya kazi utahesabika kuwa ni sehemu ya uvivu sugu.

Ili kufanikiwa hili, ni vema ukapanga ratiba ya kazi zako na masuala ya kijamii.

Hakikisha kila kikao kipo kwenye ratiba isipokuwa vile vya dharura ambavyo kwa namna nyingine huwezi kuvikwepa.

Kwa vikao vinavyohusu watu wawili na vinahitaji kutoka nje ya ofisi, jaribu kuvifanya kwa kutumia teknolojia ya video kama Google Hangouts, Skype au Whatsapp.

Teknolojia kwa sasa inaokoa muda na fedha na inakufanya ufanye kazi nyingi na vikao vingi ndani ya muda mfupi.

Usipuuze vitu vidogo vidogo

Uvivu huanza na kupuuza vitu vidogo vidogo katika maisha na baadaye hugeuka kuwa tabia sugu inayopuuza mambo makubwa.

Mfano, ni rahisi mtu kuamka na kutotandika kitanda. Tabia hii inakua hadi kwenye maeneo mengine ya maisha. Anakunywa chai na kuacha kikombe juu meza nyumbani. Baadaye tabia ya kuacha vikombe bila kuosha inahamia ofisini. Anaweza kuacha vifaa vya kazi vimezagaa kwa sababu tu “kuviweka vizuri kutampotezea muda”.

Ufanyaji wa mambo unayodhani ni madogo unakufanya uwe mwajibikaji kila wakati.

Mtu anayepuuza vitu anavyodhani ni vidogo siku moja vitamgharimu kupata vikubwa. Uzembe huo ni matokeo ya uvivu.

Hivyo, ukitaka uondokane na uvivu sugu anza kufanya vitu unavyohisi ni vidogo. Amka asubuhi na utandike kitanda vema. Weka kila kitu mahali pake chumbani kwako.

Kwa wale waliooa au kuolewa hawana budi kusaidiana katika kujenga tabia hii ya uwajibikaji.

Baada ya muda mfupi uvivu utatoweka maeneo yote na utakuwa mtu mwenye kiwango kikubwa cha uzalishaji.

Hii inasaidia hata kwa viongozi ofisini kubaini tabia za kizembe na kama zitaachwa, huigharimu kampuni kiutendaji au wakati mwingine huleta hasara kubwa ya fedha.

Kwa kuwa sehemu kubwa tunafanya kazi ama za kujiajiri au kuajiriwa ili kujiingizia vipato ni vema tukautokomeza uvivu.

Ukiukabili ni rahisi kufanya vema kwenye kila nyanja ya maisha.

Uvivu unatufanya tuziweke rehani afya zetu kwa kushindwa kufanya mazoezi kila wakati.

Unatufanya tukose fursa muhimu za maisha kwa kuchelewa kufika kwenye mikutano ama kazini.

Unafanya tuchelewe kutimiza ndoto zetu kwa dhana tu muda upo na kubwa kuliko yote unatufanya tuwe walalamikaji wakubwa na kujiaminisha kuwa hatukubarikiwa kuwa na maendeleo.Wachapakazi wanafanikiwa kwa sababu wana malengo, hawapotezi muda, wanajali kila kitu vikiwamo vile unavyoona ni vidogo na huamka mapema kwa kuwa kulala sana kwao ni kutafuta umaskini.

Nuzulack Dausen ni Mwandishi mwandamizi wa biashara na teknolojia wa Mwananchi Communications Ltd (MCL) +255714382434/ 0764176793

Friday, September 29, 2017

Mbinu ya kuchagua kazi itakayokupa utoshelevu

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Uamuzi wa kazi gani ufanye ni moja wapo ya mambo ya msingi yanayoathiri maisha ya mtu.

Kazi iwe ya kujiajiri au kuajiriwa ndiyo maisha yako.

Muda unaoutumia ukiwa kazini unaweza kuwa mwingi kuliko unaoutumia ukiwa kwingineko.

Maana yake ni kwamba unapofikiri kazi ipi uifanye kimsingi unafanya uamuzi utakaoathiri mfumo mzima wa maisha yako.

Uamuzi sahihi utakufanya uridhike zaidi na uwe mtu mwenye furaha na matumaini.

Uamuzi mbaya kwa upande mwingine, unaweza kukusababishia kukata tamaa ya maisha.

Ni dhahiri kufanya uamuzi wa kazi ni changamoto kubwa kwa sababu mara nyingi ni rahisi kuongozwa na msukumo wa nje.

Makala haya yanatathmini baadhi ya sababu unazoweza kuzitumia kufanya uamuzi unaohusu kazi.

Uzingatie kile unachokipenda?

Ukimsikiliza kijana anayefikiri afanye nini baada ya masomo yake, mara nyingi sababu anayoitoa ni mapenzi aliyonayo na kitu fulani.

Mfano, kijana anakwambia anataka kuwa mwanasheria, injinia, rubani, daktari kwa sababu hicho ndicho kinachomvutia.

Hata hivyo, changamoto ni kwamba, mambo yanayotuvutia hubadilika kulingana na umri.

Kila hatua ya maisha anayopitia binadamu hutengeneza mahitaji mapya ya kimaisha yanayoweza kubadili mambo yanayomvutia.

Kuna umri kwa mfano, anaweza kujikuta anavutiwa na vitu visivyo halisi.

Mashujaa unaowasikia kwenye vyombo vya habari, masimulizi unayokutana nayo mitaani, yanaweza kukufanya ukatamani kufanya kitu fulani kwa sababu tu umesikia kitu hicho kipo.

Leo unaweza kufikiri unapenda kuwa rubani na kurusha ndege ndiyo yakawa maisha yako.

Hata hivyo, shauku ya kuwa rubani inaweza kuwa imetokana na matamanio ya sifa tu ya kufanya kazi ya kipekee.

Kesho, kadri anavyokutana na uzoefu mpya, mvuto huo wa kurusha ndege unaweza kuhamia kwingine.

Kwa kuwa ni vigumu kujua atapenda nini kesho, kufanya uamuzi wa kazi ipi ufanye kwa kuangalia unapenda nini inaweza kuwa kosa la kiufundi.

Uige wanachofanya wengine?

Kwa namna fulani wapo watu wanaoathiri uamuzi wao. Wazazi, marafiki, watu tunaowaona kwenye vyombo vya habari wana nguvu ya kujenga ushawishi fulani kwenye maisha ya mtu.

Kuna uwezekano mkubwa, mtoto wa mwalimu naye atakuwa mwalimu. Mtoto wa daktari anaweza kuwa daktari kama mtoto wa mwanasiasa naye anaweza kuwa mwanasiasa.

Pia, marafiki ulionao nao wana nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo yako.

Unapoona wanafanikiwa kwenye eneo fulani la kimaisha, upo uwezekano na wewe ukatamani kujaribu eneo hilo.

Changamoto ni kwamba, kila mtu ana upekee wake. Si kila kinachofanywa vizuri na wengine na wewe unaweza kukifanya kwa uzuri ule ule.

Uamuzi wako wa kazi ukiathiriwa na yale tunayoyaona kwa watu wengine uwezekano wa kutokufanya vizuri ni mkubwa.

Ukubwa wa mshahara?

Nilipokuwa shuleni niliota kupata kazi itakayonilipa fedha nyingi.

Nilifikiri kazi yenye kipato kikubwa ndiyo mafanikio kwenye kazi.

Ndivyo wanavyofikiri vijana wengi wanaoanza maisha.

Hata hivyo, utoshelevu wa kazi ni zaidi ya kipato. Ingawa ni kweli moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kujipatia kipato, ni dhahiri kipato si sababu pekee.

Wapo watu wengi wanaopata kipato kikubwa lakini bado wanalamikia kazi zao.

Wengine wanaacha kazi zenye kipato kikubwa na kwenda kufanya kazi tofauti ikimaanisha kuwa kipato kikubwa si sababu inayotosha kuridhisha nafsi zao.

Unapofanya uamuzi wa kazi ukilenga kuwa tajiri pekee, unaweza kuishia kuwa mtu mwenye huzuni.

Pamoja na uzuri wa kuwa na fedha, bado kuna ukweli kwamba mafanikio yako kazini ni zaidi ya hitaji la kupata fedha.

Kugusa maisha ya watu?

Kulenga kugusa maisha ya watu ni kufanya kazi inayowanufaisha watu wengine.

Kwenda mbele ya mahitaji yako binafsi na kutumia ujuzi na muda wako kuangalia watu wengine wanahitaji nini kutoka kwako.

Changamoto kwa kizazi chetu, mara nyingi tunajiangalia sisi wenyewe na mahitaji yetu.

Tunataka kufanya kazi zitakazotufanya tuwe bora kuliko wengine na hata kuwatumia watu kwa maslahi yetu.

Ingawa ni vigumu kufikiria mahitaji ya wengine kwa asilimia mia, unapojaribu kufanya hivyo kimsingi unajiwekea akiba ya kundi la watu linalokutakia mema.

Ufanye uamuzi gani?

Jambo la kwanza ni kujidadisi. Hapa nina maana ya kujaribu kujichunguza ili kujua kitu gani unakiona kwenye jamii ambacho wewe unaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.

Kwa vyovyote vile, ufumbuzi wa tatizo huhitaji ujuzi.

Ikiwa unataka kuwatetea watu wanaonyang’anywa haki zao kwa mfano, ukiwa na ujuzi wa sheria au uandishi wa habari, itakuwa rahisi kufikia malengo yako.

Changamoto kama nilivyotangulia kusema, kile unachofikiri unaweza kukifanya leo, si lazima ukifanye kesho kwa sababu maisha yanabadilika.

Hata hivyo, tofauti na mtu anayeamua kuwa mwanasheria ili awe tajiri au maarufu, wewe utajifunza sheria ili uweze kutatua tatizo fulani unaloliona kwenye jamii inayokuzunguka.

Kutatua tatizo la mtu mwingine, ni utoshelevu usiobadilika. Katika kila hatua ya maisha yetu, sote tunatamani kuwa watu wenye manufaa kwa wengine.

Haya ndiyo matamanio ya kila mwanadamu anayejitambua.

Haitoshi kuwa na ujuzi fulani. Lazima kuutumia ujuzi huo kutatua matatizo halisi.

Utumie ujuzi huo kufanya kazi itakayopunguza tatizo unalofikiri linaisumbua jamii.

Hii ndiyo siri kubwa ya uamuzi bora wa kazi utakaokupa utoshelevu. Kutatua matatizo halisi yanayowasumbua watu wa jamii yako. Nenda katatue tatizo ambalo pengine limepuuzwa na jamii.

Kadri unavyotatua tatizo hilo, ndivyo thamani yako itakavyoongezeka na ndivyo utakavyoendelea kufurahia kile unachokifanya.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815

Friday, September 15, 2017

AJIRA&KAZI: Sababu za watu kufanya uchaguzi mbaya wa kazi

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Uchaguzi wa kazi ni uamuzi anaofanya mtu tangu anapopata wazo la kazi anayotaka kuifanya hadi atakapostaafu.

Ndoto za kimaisha ndizo zinazoongoza uamuzi wa mtu katika kipindi chote cha masomo yake.

Anapoomba kazi kwa mara ya kwanza na kuipata; anapobadilisha na hata anapofikia umri wa kustaafu.

Uamuzi huo unaposhindwa kukidhi matarajio na kumfanya mtu asifurahie kazi yake, tunaweza kusema hapo anakuwa amefanya uchaguzi mbaya wa kazi.

Uchaguzi wa namna hii unaweza kusababisha mtu asitumie uwezo wake wote kazini, hali inayoweza kuleta kutokuridhika na kazi.

Kwa kuwa kutokuridhika na kazi kunaweza kusababisha mtu aache kazi, au aendelee kufanya kazi yake kwa manung’uniko, makala haya yanaangazia sababu tano kubwa zinazochangia watu kufanya uchaguzi mbaya wa kazi.

Kukidhi matakwa ya soko

Mwenendo wa soko ni sababu moja kubwa inayoathiri uamuzi wa kazi anayoyafanya mtu.

Kwa kawaida, kazi zinazohitajika kwenye soko la ajira ndizo zinazowavutia watu wenye ndoto za kuajiriwa.

Hata hivyo, changamoto ya kuongozwa na soko ni pale mahitaji ya soko yanapobadilika ghafla kutokana na sababu mbalimbali ikiwapo ya kisera.

Hivi sasa kwa mfano, karibu kila chuo kikuu hapa nchini kina programu za ualimu.

Hiyo ni kwa sababu ya mahitaji makubwa ya walimu shuleni.

Wanafunzi wengi huona ni afadhali wasomee ualimu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo.

Huko tuendako tunaweza kujikuta tuna idadi kubwa ya wahitimu wa ualimu kuliko mahitaji halisi tutakayokuwa nayo wakati huo.

Ikitokea hivyo, wahitimu wengi wa ualimu watalazimika kutafuta ajira nyinginezo nje ya ualimu.

Hali hii inaweza kuleta changamoto kwa wanafunzi waliosoma kozi ya ualimu kwa lengo la kupata ajira mapema.

Kufurika kwa soko kunaathiri mustakabali wa wanafunzi wanaosomea ujuzi mahususi kwa ajili ya kazi fulani zinazopatikana hivi sasa kwenye soko la ajira.

Kazi hizo zinapojaa, wanafunzi wengi huaachwa wakitangatanga bila uelekeo unaoeleweka.

Kukidhi matarajio ya watu

Kuna kazi ambazo jamii huziheshimu kuliko nyingine.

Mfano, kazi zenye kuhitaji ujuzi na maarifa maalumu ambayo si watu wengi wanaweza kuwa nayo.

Huheshimika zaidi kuliko kazi zinazotegemea ujuzi wa jumla.

Aidha, mtu anayefanya kazi kama hizi huchukuliwa kama mwenye hadhi ya pekee kwenye jamii na watu humpa heshima kama mtu mwenye ujuzi maalumu.

Kwa kuwa binadamu kwa hulka yake anapenda heshima, ni rahisi kazi za namna hii kuwa chaguo la watu wengi hasa wasioutambua wito wao.

Mara nyingi watu hawa hujikuta wakitamani kukidhi matarajio ya jamii kwa kuchagua kazi wanazojua zinaheshimika. 

Hata hivyo, mara nyingine baada ya kufanya kazi hizi zisizoendana na wito, mtu huweza kubaini anafanya kitu kisichokidhi matarajio yake binafsi.

Hali ya kuchoka huweza kusababisha kuacha kazi na kutangatanga kutoka kwenye kazi moja kwenda nyingine.

Kuiga waliofanikiwa

Kuna kijana mmoja alivutiwa na kazi za wakili mmoja aliyekuwa maarufu mwishoni mwa miaka ya tisini.

Kwa sababu ya mafanikio makubwa aliyokuwa nayo wakili huyo, kijana yule aliamua kusomea sheria.

Baada ya kusomea sheria na hatimaye kufanya kazi za uhakimu kwa zaidi ya muongo mmoja, bado kijana yule anasema hajafikia mahali akajisikia ameridhika na kazi hiyo.

Juzi nilikutana naye akijaribu kufanya mipango ya kusomea kitu kingine kama jitihada za kutafuta utoshelevu.

Si jambo baya kuvutiwa na kujifunza kwa watu tunaofikiri wamefanikiwa kwenye kazi zao.

Hata hivyo, unapoiga uamuzi wa mtu mwingine unahitaji kuchukua tahadhari.

Mtu anaweza kufanya vizuri kwenye eneo fulani la utaalamu, lakini hiyo isimaanishe wewe ukifanya kitu hicho hicho utafanikiwa.

Kila mtu ana namna yake ya kufanikiwa.

Kupata kipato kikubwa

Upo ukweli kwamba moja wapo ya sababu kwa nini tunafanya kazi ni kutuwezesha kumudu maisha yetu.

Kwa sababu hiyo, kazi zenye uhakika wa kipato kikubwa, huwavutia watu wengi kuliko zenye heshima lakini hazina kipato kikubwa.

Si wakati wote suala la kipato huwa ni sababu iliyokamilika kueleza kwa nini tunafanya kazi.

Yapo mazingira ambayo kazi inaweza kuwa na kipato kikubwa lakini haimfanyi mtu atumie uwezo na ujuzi wake kikamilifu.

Inapotokea mtu analipwa vizuri lakini haoni namna gani kazi hiyo inakwenda sambamba na vipaji na haiba yake, ni rahisi mtu huyo kuanza kujisikia kudumaa na hivyo kukosa furaha ya kazi.

Ufaulu hafifu na uchumi duni

Katika mazingira yetu, kiwango cha ufaulu ndicho kinachoamua hatma ya mtu.

Mtu mwenye ufaulu mkubwa wa masomo kwa kidato cha nne au cha sita ndiye anayekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya uchaguzi unaokidhi ndoto zake kuliko mwingine mwenye ufaulu usioridhisha.

Zipo kazi ambazo ili mwanafunzi apate nafasi ya kuzisomea na kuzipata, anahitaji kuwa na ufaulu mkubwa.

Hizi ni zile kazi zenye kuchukuliwa kuwa nyeti mfano udaktari, sheria na uinjinia.

Ndiyo kusema, ufaulu dhaifu unaweza kuzima ndoto za mtu na kumfanya achague fani ambazo awali hakuwahi huzifikiria.

Pia, uwezo mdogo wa kiuchumi unaweza kuzima ndoto za maisha ya watu wengi.

Jitihada za kupata mkopo wa elimu ya juu huchangia wanafunzi wasio na uwezo  kufanya maamuzi yasiyozingatia matamanio yao.

Ingawa ni kweli uchaguzi mbaya wa kazi unaweza kumgharimu mtu, bado hata hivyo, kuna nafasi isiyo na kikomo ya kurekebisha uamuzi uliokwisha fanywa.

Lililo muhimu ni kujua kile unachokihitaji.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU).  0754870815

Friday, September 15, 2017

AJIRA&KAZI: Nyumba za ibada zinavyojenga kizazi cha watu wavivu nchini

Biblia inasema asiyefanya kazi na asile,

Biblia inasema asiyefanya kazi na asile, haikusema asiyeombewa na asile. Maombi yana umuhimu lakini waumini wanatakiwa wakumbushwe kumtumikia Mungu, kuanzisha biashara zao, kufanyakazi kwa bidii na kuwa na maadili. 

By Kelvin Mwita, Mwananchi

Asilimia kubwa ya Watanzania ni waumini wa dini na dhehebu fulani.

Idadi ya wanaoingia sehemu za ibada ni kubwa kuliko ile inayoingia shuleni na vyuoni.

Hii inatoa picha kuwa viongozi wa dini wananafasi kubwa ya kushawishi na kufanya mageuzi ya kifikra na kimtazamo.

Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea duniani, ina changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa ajira kutokana na ukweli kwamba Serikali inatoa nafasi chache zisizotosheleza mahitaji ya wanaotafuta ajira.

Pamoja na hayo, mmomonyoko wa maadili maeneo ya kazi pia ni changamoto ya muda mrefu huku rushwa ikitajwa kuwa moja ya matatizo makubwa nchini.

Hii imesababisha watu kuonewa na wengine kukosa haki na mahitaji yao ya msingi.

Nyumba za ibada zinaweza kuchangia katika kutengeneza kizazi cha wazembe na wavivu au wachapakazi na wenye juhudi.

Miujiza na mahubiri ya mafanikio

Sehemu kubwa ya mahubiri hasa makanisani yamekuwa ni ya kupata mafanikio ya fedha, nyumba, magari na vitu vingine vya thamani.

Wahubiri wanaegemea zaidi upande wa mambo ambayo waumini wao wanapenda kuyasikia.

 Mahubiri ya kuwataka wafanye kazi kwa bidii, waanzishe biashara na kutafuta mali kwa njia zilizo halali hayapewi nafasi kubwa.

Mchungaji Hosea Magelenga wa Kanisa la First Love Discipleship la jijini Dar er Salaam anakiri kuna tatizo katika mafundisho ya makanisani, kwani mengi  yanatengeneza kizazi kivivu na kizembe.

Mchungaji Hosea anasema wapo watu wanaoacha hata ajira zao kwa ushawishi wa wachungaji wanao watabiria mambo makubwa zaidi ya kile wanachopata kwenye ajira zao.

Anasema tamaa ya fedha na umaarufu kwa wachungaji wa baadhi ya madhehebu umesababisha mpaka waanze kutengeneza shuhuda za uongo za mafanikio na miujiza ili kuvuta waumini wengi katika makanisa yao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na Mkufunzi wa Dini ya Kislam, Bilal Ramadhani anasema misikiti haina shida kama ilivyo kwa makanisa mengi kuhusiana na mafundisho juu ya kufanya kazi kwa bidii.

Anasema Mtume Muhamad pamoja na mitume wengine walikuwa wakifanya kazi na wengine walikuwa wafanyabiashara.

Lakini anasema nguzo ya tatu ya Uislam inahusu zaka na hauwezi kutoa zaka kama haujafanya kazi na kupata kipato halali.

Anasisitiza Sala pekee haitoshi kukuongezea kipato bila kuvuja jasho na mafundisho misikitini huegemea zaidi kwenye juhudu ya kazi ili mtu ajipatie kipato.

Hassan Mnyone, muumini wa Dini ya Kiislam anasema kuna aya nyingi kwenye Msaafu ambazo zihimiza watu kufanya kazi.

Mnyone ametolea mfano Surat Al-Jumua: Ayat 10 inaeleza wazi:  “Na itakapokwisha sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu na  mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi (ili msipate kufanya mabaya), ili mpate kufaulu”.

Anaongeza kuwa Dini ya Kiislam inapinga njia za mkato za kupata fedha hivyo ni vema watu kuvuja jasho ili kupata kipato halali.

Padri, Calistus Msuri wa Jimbo Katoliki la Moshi anasema tabia ya wahubiri wengi kutoa mahubiri yanayoweza kusababisha watu kutozingatia bidii ya kufanya kazi yanatokana na sababu kuu mbili.

Mosi, kuwa na wahubiri watafuta fursa za kujipatia kipato, hivyo kuacha kuhubiri misingi mingine ya kiimani na kuhubiri kile waumini wanachotaka kukisikia ili wawashawishi kutoa fedha zinazonufaisha mahubiri na kuwatajirisha huku waumini wakibaki na ufukara.

Sababu nyingine ni wahubiri kutokuwa na elimu ya kutosha ya teolojia.

Anasema Kanisa Katoliki limejiwekea mfumo mzuri wa kupata wahubiri wake wanaozingatia taaluma na weeledi.

Anasema kuna baadhi ya makanisa hasa ya kipentekosti yanaanzishwa na watu wasio na elimu ya kutosha ihusuyo teolojia.

Hata hivyo, padri huyo anasema  hali hiyo inasababisha makanisa yawe ya kibiashara zaidi badala ya  kiimani.

“Biblia inasema asiyefanya kazi na asile, haikusema asiyeombewa na asile. Maombi yana umuhimu lakini waumini wanatakiwa wakumbushwe kumtumikia Mungu, kuanzisha biashara zao, kufanyakazi kwa bidii na kuwa na maadili.”

“Haya ni mambo ya kiroho, lakini yapo makanisa mengi yanawataka waumini watoe fedha ili wapate miujiza ya fedha, kazi, magari, nyumba, ndoa na menginyeyo, hii si sahihi,” anasisitiza Padri Msuri.

Nini Kifanyike?

Nyumba za ibada zina nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko ya kifikra kwa jamii.

Ni vema viongozi wa dini wakahakikisha pamoja na maombi, waumini wao wanahamasishwa kuchukua hatua za kufanya shughuli mbali mbali zinazoweza kuwaingizia au kuwaongezea kipato.

Siyo kitu cha ajabu wala cha kushangaza kwa nyumba za ibada kuratibu semina kwa waumini wao zenye lengo la kuwaongezea maarifa ya jinsi ya kuongeza vipato vyao kupitia biashara na ujasiriamali.

Hii itaonyesha zinajali maendeleo ya kimwili na kiroho ya waumini wao.

Yapo makanisa nchini yaliyoamua kuwaiunua waumini wao kwa kufungua vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) na kuendesha mafunzo ya ujasirimali ili waweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi.

Hakuna imani yoyote ya dini inayoruhusu uvivu na uzembe; wahubiri watumie fursa ya kuwa na ushawishi kwa jamii, kwa kukemea uzembe, uvivu na matendo mengine yanayosababisha mmomonyoko wa maadili kuliko kuhubiri miujiza pekee.

Waumini nao wawe makini na kujua wapo viongozi wa dini wanaoutumia mianya ya umasikini, ukosefu wa ajira na matatizo mengine kama fursa ya kujiongezea umaarufu na kujitajirisha.

Pamoja na umuhimu wa sala na maombezi katika kutatua changamoto, bidii nayo inanafasi kubwa katika kutatua changamoto. Hakuna haja ya kubweteka nyumbani ukisubiri muujiza wa fedha wakati una nguvu, uwezo, rasilimali na maarifa.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Mzumbe, 0659 081838, kelvinmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com

Friday, September 8, 2017

Namna ya kutambua kazi ya wito wako

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Vijana wengi siku hizi hujikuta wakipandikizwa mawazo kwamba mafanikio hayaji bila mtu kufanya aina fulani ya kazi. Wahubiri wa mawazo haya wanapima tija na heshima ya kazi kwa mizani ya kipato.

Mtazamo huu hasi  kwa kiasi kikubwa unachochewa na mfumo wa kibepari unaotukuza faida anayopata mtu binafsi dhidi ya manufaa mapana ya jamii.

Katika mfumo huo, mtu anaweza kufanya kazi yoyote ambayo inamnufaisha yeye binafsi.

Mawazo hayo ya kuweka mbele fedha, yanakwenda kinyume na utamaduni wa kijamaa unaopima ufanisi wa mtu kwa kutazama mchango alionao katika kuwasaidia wengine.

Wengi wanatambua wazee wengi waliitumikia jamii kwa uadilifu lakini walistaafu wakiwa na maisha ya kawaida.

Heshima yao haikuwa namna walivyojitengenezea himaya zao za kimaslahi, bali walivyoweza kutumikia wito wao. Kizazi hiki cha sasa kinaanza kuupa mkono utamaduni huo.

Vijana wa mjini wanasema, ‘Sasa tunapambana na hali zetu.’ Kila mtu anapigania maslahi yake kwa kutumia njia zozote halali na haramu ili mradi maisha yaendelee.

Mwelekeo huu umefanya watu wavamie kazi zisizo za wito wao kwa sababu tu zina harufu ya kuwaharakishia mafanikio ya kifedha. Watu hawa hujikuta wakifubaza uwezekano wa kufanikiwa kinyume na matamanio yao. Sababu ni kufanya kitu sahihi lakini kisichokuza ile mbegu inayoishi ndani yao.

Katika makala haya, naiita mbegu hii wito na ninapendekeza mbinu nne unazoweza kuzitumia kuibaini na kuikuza kupitia kazi unayoifanya.

Kitu gani kinakugusa?

Kila mtu analo eneo la maisha linamvutia kulifuatilia kwa karibu. Kuna kitu ambacho ukikisikia kinazunguzwa mahali moyo wako unasisimka. Unapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine, masikio yako yanasikia kitu hicho hata kama watu wengine hawakisikii. Unanunua vitabu, unafuatilia televisheni na mitandao na karibu kila unachokifanya kinazunguka zaidi kwenye eneo hilo hilo.

Unapoendelea kusoma hapa tayari kuna kitu kinakujia kichwani. Inawezekana ni matatizo fulani ya watu, hitaji fulani unalofikiri jamii yetu inalo au ubunifu fulani unaoamini bado jamii haijauona.

Pia, huenda ni masuala ya teknolojia. Inawezekana ni mfumo fulani wa maisha, imani au fikra katika jamii unazofikiri ungepewa nafasi ungezibadilisha. Chochote kile kinachogusa fikra zako, hicho ndicho kinachoweza kuwa wito wako. Ukifanya kazi zinazogusa eneo hilo unaweza kufanya vizuri zaidi.

Unajitambulisha na kitu gani?

Kwa kawaida, kuna vitu tukivifanya vikaleta matokeo fulani tunajisikia fahari. Kila mtu ana eneo lake akilifanya vizuri anajisikia kuridhika.  Kuna watu wanajisikia fahari wanapotetea haki za watu; wengine kufundisha; wengine uandishi; kubuni vitu vipya; kuongoza wengine; kushauri, kuendesha biashara, kutaja kwa uchache.

Kile kinachokuletea ufahari, mara nyingi, utapenda kujitambulisha nacho. Utatumia muda mwingi kukielewa kuliko unavyofanya kwenye maeneo mengine.

Nina rafiki yangu daktari mzuri lakini mara zote hujitambulisha kama mwandishi. Mazungumzo yake mengi hujikita kwenye uandishi kuliko udaktari na sisi tunamtambua kama mwandishi kuliko daktari. Hii ndiyo sifa ya wito. Unaweza kufanya kazi nyingine lakini kinachokupa hali ya utoshelevu kikawa kitu kingine kabisa.

Jiulize, kitu gani ukikifanya vizuri unajisikia fahari? Je, watu wanakusifia na kukutambua kwa kitu gani? Ukiweza kuuoanisha uwezo huo na kazi unayoifanya itakuwa rahisi kupata mafanikio makubwa zaidi.

Unayatazamaje mafanikio?

Mafanikio ni dhana pana isiyo na jibu moja. Kila mtu ana namna yake ya kutafsiri kile kinachoitwa mafanikio. Wapo wanaochukulia mafanikio kama uwezo wa kujikusanyia mali. Hawa huridhika wanapokuwa wamefikia kiwango cha kujitosheleza na vitu vinavyowawezesha kuishi maisha mazuri.

Wengine mafanikio yao ni umaarufu katika jamii. Vitu vinavyowafanya wajulikane ndivyo wanavyovichukulia kama mafanikio. Wengine wanakwenda mbali zaidi. Hawaridhiki na fedha wala umaarufu bali mamlaka. Wasipopata madaraka yanayowapa nguvu ya kuwatawala wengine, bado hawajisikii kufanikiwa.

Pamoja na hao, wapo pia wanaopima mafanikio yao kwa namna wanavyotatua matatizo ya watu wanaowazunguka. Hawa, hawaishii kuridhika na maisha mazuri bali kuona  maisha yao yanagusa watu wengine.

Tafsiri ya mafanikio uliyonayo, ni kiashiria kimojawapo cha wito ulionao katika maisha. Wito wako hutengeneza mtazamo fulani wa mafanikio. Ukiweza kuoanisha tafsiri uliyonayo ya mafanikio na kazi unayoifanya uwezekano ni mkubwa kuwa kufanya vizuri zaidi.

Maamuzi gani unayafurahia?

Kipimo cha juu cha wito ni aina ya maamuzi unayoyafanya. Kuna nyakati unaweza kufanya maamuzi ambayo si kila mtu anaweza kukuelewa lakini wewe mwenyewe ukawa na amani na kile unachokifanya.

Kuna kijana aliwahi kuacha kazi yenye kipato kikubwa ili akafanye kitu alichoamini kinabeba thamani yake. Aliacha kazi ambayo watu wengi wangetamani kuipata na akaenda kuanzisha biashara. Mtu wa namna hii kwa vyovyote anakuwa na wito wa ujasiriamali ndani yake. Ili wito huo ukamilike inakuwa ni lazima afanye maamuzi magumu.

Jiulize, umewahi kufanya maamuzi gani yaliyobadili mwelekeo wa maisha yako? Ikiwa kuna maamuzi unatamani kuyachukua ukiamini yatabadili maisha yako, huo inawezekana ndio wito wako.

Wito hubeba mafanikio yako

Mafanikio katika kazi mara nyingi hujipua kama mbegu inayoota kwenye wito alionao mtu. Kila mtu ana mbegu yake. Kwa mfano, hata tungependa kujiajiri si kila mtu anaweza. Wapo watu ambao hata wangewezeshwa kujiajiri bado hawatafanya vizuri. Kujiajiri si wito wao.

Kadhalika, si kila mtu anaweza kuajiriwa. Kuna watu wana wito ndani yao wa kutengeneza mifumo inayoajiri watu wengine. Wito wao ni kusimamia mawazo yao na kuyageuza kuwa ajira. Ndio maana ni muhimu kuutambua wito wako.

Unapoutambua wito wako unajiweka kwenye nafasi ya kujitoa kikamilifu kwenye eneo lililobeba thamani yako. Hutajaribu kufanya vitu vingi kwa sababu unajua iliko thamani yako na wapi pa kuelekeza nguvu zako.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815

Friday, July 28, 2017Picha na Mtandao wa Crafthubs.com 

Picha na Mtandao wa Crafthubs.com  

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Ni ndoto ya kila aliyeajiriwa kupata mafanikio katika kazi anayofanya.

Iwe umeanza kazi hivi karibuni au upo katika ajira kwa muda mrefu, kumbuka unaweza kupata mafanikio katika kazi unayofanya.

Dhana nzima ya mafanikio katika muktadha huu simaanishi kuwa tajiri au kupata cheo kikubwa sana katika kampuni.

Mafanikio ninayoyazungumzia yamejikita katika mawanda kama vile kuwa na uwezo wa kuifanya kazi yako vizuri na kwa ufanisi, kujihisi kuwa umetimiza na kukamilisha malengo na majukumu yako kazini, kuboresha thamani yako katika soko la ajira na hivyo kuwa na uwezo wa kunufaika kiuchumi, pamoja na kutambulika na kuheshimiwa na bosi wako na wafanyakazi wenzako.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio katika ajira. Ikumbukwe kuwa mafanikio kazini si kitu rahisi ambacho kila mtu anaweza kukipata.

Kuna siri nyingi za kuyafikia mafanikio katika ajira. Baadhi ya siri hizo ni kama zifuatazo:

Moja, jitihada na bidii kazini ni ufunguo wa mafanikio kazini. Watu wenye kupenda mafanikio daima huwa na tabia za kufanya mambo ambayo daima watu wavivu hawapendi kuyafanya.

Katika zama tulizo nazo imekuwa ni vigumu kupata wafanyakazi waaminifu na wenye kujituma. Wengi wamekuwa ni watu wa kutafuta fursa ziwe nzuri au mbaya za kujinufaisha binafsi.

Katika mazingira kama haya ili ufanikiwe inakubidi ujipambanue kama mpambanaji usiyekubali kushindwa. Tekeleza majukumu yako kwa viwango vya juu na daima pigania kuwa wa kwanza kwa ufanisi.

Katika kuyafanya haya unaweza kujijengea maadui kazini kwani baadhi ya wafanyakazi wanaweza kukuona unajipendekeza au una kiherehere cha kazi.

Tambua kuwa upo ofisini kwa faida yako na ya mwajiri, kwa hiyo maneno ya mtu yasikupe presha. Hata hivyo, waheshimu wafanyakazi wenzako, pokea ushauri wao na msaidiane katika kazi zenu za kila siku.

Usijisifu kuhusu utendaji wako bali waache watu watambue na wayaeleze mafanikio yako kazini.

Tabia njema ni moja ya siri kubwa za mafanikio kazini. Ukiwa na tabia mbaya hata kama ni mchapakazi kiasi gani, hakuna mwajiri atakayeridhika na wewe. Kiburi, dharau na kujifanya unajua kila kitu vinaweza kukuharibia maisha yako ya ajira.

Kuna wafanyakazi ambao siku zote hulalamika tu kana kwamba hawajawahi kutendewa jema hata moja na waajiri wao!

Kama una malalamiko yanayokwaza utendaji wako kazini, yafikishe mahali husika ili yatafutiwe ufumbuzi badala ya kuendekeza majungu.

Wafanyakazi wenye ufanisi daima hufanya mambo mawili: hufanya kazi zao vizuri na huziwekea vipaumbele. Usifanye tu kazi bali jitahidi uifanye kazi yako vizuri na kwa weledi.

Kazi bora itatambuliwa tu kwani itajipambanua na zile zilizofanywa chini ya kiwango. Acha kazi iongee. Fanya kazi kwa kufuata kanuni na siyo kwa njia za mkato zinazoweza kukugharimu.

Tambua kuwa mteja ni mtu muhimu sana kwa uhai wa kampuni au taasisi. Bila mteja hakuna biashara. Wafanye wateja wajihisi kuwa unafurahi kuwahudumia.

Ninaposema wateja hapa ni kila unayemhudumia katika utekelezaji wa majukumu yako kazini. Dhana ya mteja haishii kwa wafanyabiashara pekee.

Tafuta mbinu ambazo zitawafanya wateja waridhike na huduma yako. Wateja ni watu muhimu sana kwani wanaweza kuyatangaza mafanikio yako mbali na eneo lako la kazi.

Unatakiwa kuwajali wateja kama ni watu muhimu sana na hawa ndio watakaopeperusha bendera ya mafanikio yako.

Usiogope kufanya zaidi ya kile ulichopangiwa. Kama unaweza kufanya na ziada kwa manufaa ya ofisi na wafanyakazi wenzako fanya badala ya kutekeleza yale majukumu machache uliyopangiwa.

Unapoajiriwa unakuwa sehemu ya kampuni, jitahidi uwe mwanafamilia bora badala ya kuwa mnafiki unayeisimulia vibaya ofisi, kwa kuwa tu matakwa yako fulani hayakamilishwa.

Kwa nini ubaki kuwa mnafiki katika ofisi unayodhani haikujali? Tafuta njia ya kutoka hapo na kwenda unapoona kuna masilahi zaidi.     

Friday, July 28, 2017

Elimu yetu inatuandaa kukabiliana na tatizo la ajira?

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

“Kijana wangu amesoma shahada ya ujasiriamali. Huu sasa ni mwaka wa pili sioni kitu anachofanya na huo ujasiriamali wake aliousomea. Hawezi kujiajiri, hawezi chochote; mpaka nauli ananitegemea.” Ni kauli aliyonieleza mzazi mmoja hivi karibuni.

Inavyoonekana, mzazi huyu kama wazazi wengine, alikuwa na matarajio makubwa alipomsomesha mwanawe. Kwake, mafanikio ya elimu yanatafsirika katika uwezo wa kujiajiri au kupata ajira.

Hata hivyo, hali ni tofauti kidogo. Wahitimu  wengi wanapomaliza masomo yao, wanashindwa kuutumia ujuzi walionao kutengeneza ajira kama anavyoeleza  mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Maranya Mayengo:

“Elimu yetu haimuandai mwanafunzi kukabiliana na tatizo la ajira, bali inamuandaa kuwa tatizo anapokosa ajira.”

Mayengo anafikiri, tatizo hili halianzii kwa wanafunzi bali ni suala la mtazamo wa jumla wa jamii kuhusu ajira na kazi.

Anasema, “Watu wengi hawana ujasiri wa kujiajiri, sio tu kwa wahitimu wetu bali hata kwa walimu wao. Msamiati wa kujiajiri ni mwepesi kuzungumzwa na watu walioko kwenye ajira, wanasiasa na maofisa wa Serikali ambao kimsingi wao hawana ujasiri huo.”

Imekuwa kawaida kusikia watu waliofanikiwa, ikiwa ni pamoja na wanasiasa, wakitoa wito kwa vijana kujiajiri na kuacha kuisubiri Serikali iwape ajira. Hata hivyo, ni vyema tukatafakari namna tunavyowawezesha vijana kuitikia wito huo.

 

Elimu inawajengea uwezo wahitimu?

Katika enzi za elimu ya ujamaa na kujitegemea, kwa kiasi kikubwa, kila ngazi ya elimu iliandaa watu wanaoweza kuzalisha kazi bila kulazimika kuwa na elimu ya juu. Mwanafunzi wa ngazi yoyote ya elimu alipatiwa maarifa yaliyomwezesha kufanya kazi bila kulazimika kupitia mafunzo mengine maalum.

Mwalimu Pamela Challo wa Shule ya Sekondari Viwandani, Dodoma anasema aina ya elimu wanayopata wanafunzi inaweza kuwa kikwazo cha kujiajiri kwa wahitimu wengi.

“ “Shule za mapishi, ushonaji, ufundi, zilisaidia kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri wenyewe bila shida. Tulipofuta masomo kama hayo tulitengeneza tatizo. Sasa hivi watoto hawajengewi ujuzi, wanaandaliwa kufaulu mitihani na kusubiri ajira,” anaeleza.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mwalimu Morice Missanga wa mkoani Arusha, anayesema:

“Mfumo wetu wa ufundishaji umejikita zaidi kwenye content coverage (kumaliza yanayotakiwa kufundishwa) zaidi kuliko kwenye ujuzi. Ujuzi ndio unaoweza kuibua ajira zisizoonekana kwa macho ya darasani.”

Anaongeza: “Kama elimu yetu ingetambua nafasi ya ajira zisizo rasmi na kuziingiza kwenye ufundishaji kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, huku kunakoitwa juu (elimu ya juu) kusingesongwa kwa maana ya kuwa na wahitimu wengi kuliko mahitaji. Fedha zinazotumika kuwasomesha elimu ya juu, zingekuwa ndio mtaji wa kuingia kwenye stadi za kazi na ubunifu.”

Tunachuja badala ya kukuza

Kwa muda mrefu, tumelenga kuwachuja wanafunzi kwa vigezo, ambavyo wakati mwingine havina uhusiano wa moja kwa moja na kazi watakazozifanya baada ya kumaliza masomo yao.

Kwa mfano, mwanafunzi mwenye kipaji cha kuigiza au kuimba anaposhindwa kufaulu Fizikia anaambiwa hana akili ya kuendelea na masomo.

Kwa utaratibu huu, idadi kubwa ya wanafunzi wenye uwezo usiotambuliwa kwa mitihani wanakosa fursa ya kukuzwa, ili wawe watu wanaofanana na uwezo uliomo ndani yao.

Badala ya kukuza uwezo wa wanafunzi, tunatumia rasilimali nyingi kuwahudumia watu wachache tunaofikiri ndio wenye tija. Lakini mwisho wake wanaishia kuidai Serikali iwaajiri, kwa sababu hawajui wanavyoweza kutumia maarifa waliyofikiri wanayo.

Kwa nini tusiweke utaratibu wa kuwajenga wanafunzi wote kadri ya uwezo walionao? Elimu ikiweza kuibua na kukuza uwezo binafsi wa mwanafunzi, ni dhahiri tatizo la ajira litapungua.

Kukuza thamani ya wahitimu

Dhima kuu ya elimu ni kupanua uelewa wa watu kuhusu matatizo yanayoikabili jamii yao. Hata hivyo, ni muhimu uelewa huo uwasaidie wahitimu kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili jamii.

Kijana anayejengewa uwezo wa kuona na kutatua changamoto, mkononi mwake anakuwa amekabidhiwa ufunguo unaobeba thamani yake.

Kwa kuutumia ufunguo huo, kijana huyu hawezi kukosa kazi ya kufanya akirudi kwenye jamii.

Ili hilo liwezekane, mamlaka za elimu zinawajibika kufanya utafiti kujua shida halisi zinazowakabili watu ili kutengeneza programu zinazojibu changamoto halisi katika jamii.

Hata hivyo, mahitaji ya jamii yanabadilika kila siku. Changamoto ni namna ya tunavyoweza kukabiliana na mabadiliko haya.

Lakini pia, upo ukweli kwamba mazingira yanavilazimisha vyuo kutoa maarifa ya jumla kwa lengo la kuchokoza uelewa. Kazi ya kuyafanya maarifa hayo yajibu matarajio binafsi ya mwanafunzi, inabaki kuwa ya mwanafunzi mwenyewe na mazingira yake.

Hivyo ni wajibu wa mwanafunzi binafsi kuhakikisha anajua kwa hakika kile anachokitaka, ili aweze kuchagua eneo la kitaaluma linalokidhi wito alionao ndani yake.

Tuthamini ujuzi

Wahitimu wengi hawaajiriki, kwa sababu wakati mwingine wanakosa ujuzi. Wanashindwa kutafsiri ufaulu mkubwa wa darasani katika utendaji. Kutojua wafanye kutokana na yale wanayoyajua, kunafanya lugha ya kujiajiri iwe ngumu kwao.

Kasoro hii inaweza kurekebishwa ikiwa tutaanza kuthamini ujuzi na si maarifa pekee. Badala ya walimu kuuliza maswali yanayolenga kupima uelewa wa mambo darasani, waende hatua moja mbele.

Mwanafunzi apimwe namna anavyoweza kutumia maarifa aliyonayo kuboresha hali ya mambo katika jamii yake.

Aidha, ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi za kuoanisha mazingira halisi ya kazi na ujuzi unaotolewa darasani. Ufundishaji ulenge kuwafanya wanafunzi waione jamii yao wakiwa darasani badala ya kuwafundisha mambo ya kufikirika wasiyoyaona katika maisha yao ya kila siku.

Pia, tutafakari sababu iliyotufanya tupanue elimu ya juu na kupunguza uzito wa vyuo vya kati na vyuo vya ufundi.

Kasumba kwamba kufika chuo kikuu ndio kipimo cha kuelimika, inachangia kukuza tatizo la ukosefu wa ajira.

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815

 

Friday, June 2, 2017

Sifa muhimu kwa wahitimu wanaotafuta ajira

 

By Colnely Joseph, Mwananchi

Mazingira ya kufanyia kazi yanabadilika kwa haraka zama hizi za sayansi na teknolojia.

Hali hii bila bila shaka inahitaji watu wanaoweza kwenda na mabadiliko hayo kwa kasi.

Watafuta ajira nao hawana budi kuyajua ya mabadiliko haya teknolojia na kisha kutafuta mbinu za kwenda nayo sambamba.

Huu siyo tena wakati wa kufanya vitu kizamani, unapaswa kutumia teknolojia kujiuza na kupata kile unachohitaji maishani.

Ili kujiweka katika nafasi nzuri katika soko la ajira na kurandana na hali halisi ya sasa, ni muhimu kwa wahitimu kuzingatia mambo kadhaa.

Uwezo wa kutumia zana za digitali

Vifaa vya digitali vimetengeneza nafasi ya watu kuingiliana na kuwa karibu zaidi na kupanua mianya ya ajira.

Katika dunia ya sasa, siyo lazima maombi ya kazi yafanywe kwa barua au siyo lazima kwa mtu kuhangaika na magazeti akitafuta ajira; haya yote sasa yanawezekana kwa kutumia njia za kisasa za vifaa vya kidigitali.

Kwa sasa sio uamuzi wako kuamua kujifunza komputa au la, bali ni lazima mno ili uweze kuendana na uhalisia wa dunia kiteknolojia. Siyo kwa kutafutia ajira, lakini hata kazi sasa zinafanywa kiteknolojia zaidi.

Uwezo wa kufanya kazi na kuwasiliana na watu

Huombi ajira ili uje kujifungi chumbani ukifanya kazi peke yako, ni lazima uchangamane na wenzako katika ofisi moja au taasisi. Kuwa karibu na wenzako kwa kushirikiana kuhusu mambo yote muhimu kwa manufaa ya ofisi. Hakikisha unawashirikisha taarifa au maarifa mapya kutoka mahali kwingine ili kwa pamoja muweze kufikisha malengo kusudiwa.

Uwezo wa kuwasiliana ni muhimu kwa mfanyakazi mpya, kwani utakuwezesha kuwasilisha mawazo yako na kuyafanya yaeleweke vyema na kutumiwa na timu yako. Hivyo jifunze kuja na mawazo makubwa zaidi na kuwasilisha kwa unadhifu.

Elimu ya ujasiriamali

Huhitaji kumiliki biashara yako ili uwe na uwezo wa kupata mawazo makubwa na mapya, bali kupitia mabadiliko ya kiteknolojia yanaweza kukusaidia kujitambua na kujua unachopaswa kukifanya.

Ukijituma na kuwa mbunifu, ni dhahiri kuwa fursa zaidi zitakufuata mikononi mwako. Elewa kuwa hivi sasa kampuni nyingi hazihitaji wahitimu bali watu walio tayari kusababisha mabadiliko chanya na endelevu.

Kampuni zinataka mawazo mapya na watu wenye mipango stahiki walio na uthubutu wa kutenda kwa kuwa tayari wana tabia za kijasiriamali ndani yao.

Fahamiana na watu wengi kibiashara

Kuwa na mtandao mkubwa ambao umeutengeneza ni muhimu sana katika utendaji wa kisasa, kwani licha ya kuwa na msaada katika kuboresha biashara mauzo au huduma pia itakuwezesha wewe kujifunza mambo mbalimbali na kujiongezea uelewa jambo ambalo lina umuhimu mkubwa.

Mtandao ulionao una nguvu kubwa katika masoko yako hivyo kabla hujapata kazi jitahidi kuwa na watu sahihi. Pia, ni muhimu kujifunza namna ya kuwalinda na kuutunza urafiki wako na watu wako muhimu.

Uwezo wa kuchambua na kung’amua taarifa

Kuwa na taarifa nyingi na sahihi ni jambo kubwa mno katika karne hii. Kuwa na taarifa nyingi na maarifa ya kutoosha kutakusaidia kufanya jambo lolote kwa usahihi wake.

Unapaswa kuwa mchambuzi wa kilaa taarifaa unayoipata katikaa vyanzo mbalimbali. Kuwa makini na taarifa unayoichagua katika kutekeleza majukumu yako.

Kumbuka nyakati za kufanya kazi bila mpangilio na kwa kubahatisha zilishapita miaka mingi.

Uwezo wa kufikiri kwa mapana na usahihi

Ubunifu unathaminiwa na kampuni nyingi duniani. Ubunifu ndicho kitu pekee kinachosababisha kampuni kubakia kileleni katika ushindani wa dunia kibiashara.

Hivyo ni jambo zuri kuwa na watu ambao husugua akili zao kwa kujua nini kifanyike kwa maendeleo chanya ya namna ya kuboresha kazi au bidhaa.

Uwezo wa kujifunza kila siku

Kwa kadri teknolojia inavyokua na kubadilika, ndivyo unavyotakiwa kuendana nayo kama unataka kufanikiwa. Fungua akili yako na jifunze kwa watu wengine.

Hivi sasa watu hawajifunzi tena wakiwa darasani, zana za Tehama kama zimerahisisha watu kujifunza mambo mbalimbali, hivyo huna sababu ya kutojifunza.

Uwezo wa kutatua matatizo

Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, matatizo yanazaliwa kila kukicha na hakuna muda tena kumsubiri bosi kukuonyesha njia kama unakijua unachokifanya. Unatakiwa kuwa na uwezo kutambua matatizo na kuyatafutia ufumbuzi sanjari na kupendekeza nini kifanyike kwa haraka kadri matatio yalivyojitokeza.

Hii ina maana moja tu kuwa fikiria kwa njia yako kabla ya kulaumu. Wakati wote uwe mtu wa kuonyesha njia ya kutokea badala ya kukata tamaa.

Kama wewe ni mhitimu na unahitaji kufanya kazi ya ndoto yako ambayo umeisomea, hakikisha unajivika sifa hizi ili uwe mshindani wa kweli katika soko la ajira. Kumbuka kuna wengi wanatafuta kazi hiyohiyo unayoitafuta wewe.

Makala haya awali yalichapishwa katika tovuti ya Brighter Monday, ambayo ni tovuti namba moja ya ajira nchini.     

Friday, June 2, 2017

Mambo yanayokuza motisha kwa wafanyakazi

 

By Christina Bwaya,Mwananchibwaya@mwecau.ac.tz

Jenga Uaminifu

Moja ya vitu vinavyotufanya tuonekane watu wa kawaida au pengine tuepukwe na wafanyakazi wenzetu katika mambo mengi ni kukosa uaminifu.

Uaminifu haupimwi kwa kuangalia matumizi ya rasilimali mbalimbali ikiwamo mali za ofisi na hata muda.

Hakikisha kile chochote unachopewa kukitumia kama nyenzo ya kukuwezesha kufanya kazi vizuri unakitumia kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuepuka kutoa ahadi za uongo au zisizotekelezeka.

Fahamu kuwa kurudisha uaminifu ni kazi sana pale mtu anapoupoteza kwa namna moja ama nyingine.

Matendo kama rushwa, ubadhilifu, uongo na mengineyo ni ya kuepukwa ili usivunje uaminifu kwa wengine.

Tenda haki

Katika kila jambo unalotakiwa kulifanya hasa katika kutoa maamuzi hakikisha unatenda haki.

Hii inaenda sawia na kutoa maoni juu ya mambo au watu wengine kwani watu kupenda kutathmini kama kweli wewe ni mtenda haki hata kupitia maoni unayotoa juu ya wengine.

Ubaguzi na upendeleo hupunguza au huondoa kabisa ushawishi wa mtu kwa wengine.

Hakikisha maamuzi yoyote unayoyafanya ni matokeo ya uchambuzi na fikra sahihi juu ya jambo husika.

Maamuzi ya kukurupuka husababisha kutoa maamuzi yasio sahihi yanayoweza kusababisha kumnyima mtu haki yake pengine hata bila kukusudia.

Shirikiana

Watu humuunga mkono yule wanayedhani kuwa yupo pamoja nao. Kwa sababu mbalimbali wapo wanafanyakazi katika taasisi ambao huamua kujitenga na wenzao.

Wapo wanaoamini kuwa na cheo ni sababu ya kuweka ukuta na wengine bila kujua kuwa cheo ni daraja linaloweza kutumika     

Friday, March 10, 2017

Kanuni nne za kufurahia kazi yako

 

Kwa nini unaamka asubuhi kwenda kazini? Kitu gani kinakupa sababu ya msingi ya kwenda kazini?

Ni dhahiri vigezo tunavyovitumia kufurahia kazi haviwezi kufanana. Wapo wanaofurahia kiwango kikubwa cha mshahara.

Thamani ya kazi inategemea na ukubwa wa kipato. Wengine wanaridhika na kazi inayowajengea hadhi katika jamii. Kazi inayowaongezea hadhi inawafanya waridhike.

Pia, wapo wanaoridhika na kazi inayowapa utulivu. Hawa hata kama kazi yenyewe hailipi, wala haiwapi heshima kubwa katika jamii, ikiwa tu inaweza kuwapa uhakika wa kuishi bila kuwa na wasiwasi wa kukosa kazi kesho, wanatulia.

Ingawa kila mmoja ana sababu zake, kwa ujumla, namna gani mwajiri wako amekuwekea mazingira yanayokuwezesha kutekeleza majukumu yako, kwa kukulipa kiwango kinacholingana na thamani yako, kukutambua, kukupa uhakika wa kazi ni baadhi ya mambo yanayoweza kukuongezea furaha ya kazi.

Hata hivyo, tafiti za ajira na kazi zinaonyesha kuwa mtazamo binafsi wa mfanyakazi una nafasi kubwa ya kumwongezea furaha ya kazi anayoifanya. Makala haya yanaangazia kanuni nne unazoweza kuzitumia kufurahia kazi unayofanya na hivyo kuongeza tija yako kazini.

 

Fahamu kinachokuridhisha

Kuelewa kitu gani kinakufanya uone thamani ya kazi unayoifanya kunaweza kukuongezea furaha ya kazi. Watu wasio na hakika ya kitu mahususi kinachowapa furaha maishani mwao, ni vigumu kuridhika na kazi.


Jiulize, kitu gani kilikuhamasisha kuomba kazi uliyonayo leo? Je, msukumo gani hasa unakufanya uendelee kwenda kazini? Je, usingekuwa na kazi uliyonayo, ungekuwa na furaha zaidi?

Majibu ya maswali haya yanaweza kukusaidia kutathmini kiwango chako cha kuridhika na kazi uliyonayo. Ni dhahiri pia kuwa ari na msisimko wa kazi hupungua kadri mtu anavyoizoea kazi yake. Kadhalika, mahitaji yetu ya kisaikolojia, kiuchumi na kijamii hubadilika kadri miaka inavyokwenda.

Hata hivyo, unapotambua kiwango chako cha kuridhika na kazi, unaweza kuchukua hatua stahiki. Siyo mara zote unapokosa msisimko wa kazi maana yake uache kazi.

Wakati mwingine kubadili namna unavyoitazama kazi yako kunaweza kukusaidia. Kazi unayoona haina maana leo, wapo watu maelfu ambao pengine wanaota siku moja wangeipata.

 

Jitambulishe na kazi yako

Ujasiri wa kujitambulisha na kazi yako ya sasa unakusaidia kuipenda zaidi kazi yako. Kufurahia kazi yako ya sasa haimaanishi usiwe na ndoto za kufanya kazi nyingine. Siyo watu wengi wanafanya kazi walizotamani kuzifanya.

Hata hivyo, kutoridhika na kazi uliyonayo tayari kwa kiasi kikubwa, kunaathiri ufanisi wako. Unapokosa furaha na kazi yako, inakuwa rahisi kwako kukosa hamasa ya kuwa mbunifu; hutajituma na inaweza kuwa vigumu kwako kuleta matokeo yanayoweza kukupeleka kule unakotaka kwenda.

Jizoeshe kujitambulisha na kampuni yako. Jione kama sehemu muhimu ya kampuni au taasisi unayoifanyia kazi badala ya kujichukulia kama mpitaji. Kuwa tayari kuitetea kampuni au taasisi yako mbele ya macho ya umma.

Kutojisikia fahari na kazi unayoifanya kunakuondolea furaha ya kazi. Kadri unavyoendelea kudanganya mahali unakofanya kazi, kwa sababu ya imani kuwa ikifahamika itakupunguzia heshima unayopata kwa kutofahamika, ndivyo unayokuwa kwenye mazingira ya kukosa amani na hapo ulipo.

Fanya kinyume. Jitambulishe waziwazi hata kama unajua wapo watu wenye mtazamo hasi na aina ya kazi unayoifanya. Kujiamini kutakuongezea furaha.

 

Kuwa na bidii na ushirikiano

Heshima inayotokana na kazi ya mtu, kwa kawaida inaongeza furaha ya kazi. Kule kujisikia kuwa mchango wako unatambuliwa, uwepo wako unahitajika, inakupa heshima. Lakini ili uweze kuheshimiwa kazini, unahitaji kujituma. Fanya kazi kwa bidii. Ione kazi yako kama njia halali ya kukusaidia kupata heshima unayohitaji kuwa nayo.

Ni kweli kuwa wakati mwingine unaweza usijikie kujituma kwa sababu labda mazingira ya kazi sio rafiki. Hakuna kazi inayoweza kukujengea mazingira yasiyo na kasoro yoyote. Pengine hujioni ukitumia vipaji vyako ipasavyo. Hakuna kazi yoyote unayoweza kuifanya na ikatumia vipaji ulivyonavyo kikamilifu.

Vipaji vyako vinaweza kutumiwa na karibu kila kazi unayoifanya. Labda hujajituma vya kutosha. Ukiweza kujituma kikamilifu kwenye kazi hiyo unayoifanya, unaweza kushangaa namna utakavyotumia vipaji usivyovutumia hivi sasa. Kadri unavyovitumia vipaji vyako, ndivyo utakavyojisikia kuridhika zaidi.

Jenga uhusiano mzuri na wenzako. Uhusiano mbaya kazini unachangia kuondoa furaha ya kazi. Huwezi kuridhika na kazi inayokukutanisha na watu msioelewana. Shirikiana na wenzako badala ya kushindana nao. Wape msaada wanaouhitaji kukamilisha kazi zao. Kwa kufanya hivyo, utashangaa namna wanavyofurahia kufanya kazi na wewe na hiyo itakuongezea furaha ya kazi.

 

Rekebisha namna unavyoyachukulia maisha

Mtu asiye na furaha na maisha yake ya kawaida, anakuwa na uwezekano mdogo wa kufurahia kazi yake. Unapokuwa na utulivu na mtazamo chanya na maisha, inakuwa rahisi kwako kuipenda kazi yako. Kinyume chake pia ni kweli. Usipokuwa na furaha na maisha, hutafurahia kazi yoyote utakayopewa.

Tafsiri yake ni kuwa unahitaji kurekebisha mtazamo wako wa jumla na maisha ili uweze kuona thamani ya kazi unayoifanya. Pengine unashindana na watu. Kila unachokifanya unakiweka kwenye mizani ya kile unachofikiri watu wengine wanakifanya.

Pengine unajifikiria mwenyewe kuliko mchango unaoutoa kwa watu wengine. Labda ni wakati wa kufikiri upya. Je, maisha ni kujifikiria mwenyewe? Je, fedha na mali ndilo lengo kuu la maisha? Hakuna kusudi jingine kubwa zaidi ya kupata mahitaji yako ya kila siku?

Pengine vile unavyoyachukulia maisha ndiyo tatizo. Ukibadili mtazamo wako wa jumla wa maisha, unaweza kugundua namna kazi yako ilivyo na thamani kubwa kuliko unavyofikiri.

 

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

Friday, March 10, 2017

Wanatakiwa kuchangamkia fursa hizi

 

By Julieth Kulangwa, Mwananchi

Ni ndoto ya kila mjasiriamali kukuza mtaji wake. Zipo mbinu mbalimbali ambazo anaweza kutumia kufanikisha malengo haya.

Anaweza kukuza mtaji mdogo alionao ili kufanikisha ndoto kubwa uliyonayo, lakini inaweza kuchukua muda mrefu. Unaweza kuomba mtaji kwa ndugu na jamaa, lakini njia hii haina uhakika kwa kuwa inategemea na hali.

Kuna njia mbadala inayotumiwa na wajasiriamali wengi duniani ambayo ni ufadhili wa mitaji (fellowships and grants) inayotolewa na mashirika mbalimbali duniani.

Kwa wajasiriamali wanaoperuzi mitandaoni mara kwa mara huenda wameshakutana na fursa hizi na huenda wapo wanufaika. Kwa wale ambao ndio kwanza wanasikia habari hizi, wakati ndio huu wa kujaribu bahati yao katika hizi chache.

 

1.Microsoft #INSIDERS4GOOD East Africa Fellowship 2017

Kampuni ya Microsoft inafahamika kwa kusaidia kupitia Taasisi yake ya Bill & Melinda Gates Foundation. Taasisi hii ipo katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kuwezesha mapinduzi ya wajasiriamali wanaojihusisha na ugunduzi (innovation).

Wajasiriamali 25 watachaguliwa katika mradi huo wa miezi sita na baada ya hapo wataunganishwa katika masoko ya dunia.

Kama unadhani unakidhi mahitaji ya ufadhili huu tembelea tovuti hii:

https://windowsinsiders.azurewebsites.net/Fellowship/EastAfrica

 

 

2.African Entrepreneurship Award

Hii ni nafasi nyingine kwa wajasiriamali wanaotaka kuanzisha biashara zao.

The African entrepreneurship inatafuta mawazo ya biashara kutoka barani Afrika. Unachotakiwa kufanya ni kuingia katika tovuti yao na kuwasilisha wazo lako la biashara.

Mawazo yote ya biashara yatapitia mchujo mara nne na watakaopita wataitwa nchini Morocco kuwasilisha mawazo yao na kupewa mtaji.

Unaweza kuwasilisha wazo tembelea: https://africanentrepreneurshipaward.com/eligibility/

 

 

3. The Tony Elumelu Foundation Entrepreneurship Programme

Mfanyabiashara wa Nigeria, Tony Elumelu ameanzisha mpango wake wa miaka 10 wa kuwawezesha wajasiriliamali 10,000 kwa kuwapa mitaji.

Alianzisha The Tony Elumelu Entrepreneurship Programme 2010 kwa kutenga dola za marekani 100.

Kila mwaka wajasiriliamli 1,000 hupewa mitaji kwa wajisiliamli wenye mawazo ya biashara au biashara zenye umri usiozidi miaka mitatu.

Programu hii hutoa mtaji wa dola za Marekani 5,000 ambazo ni wastani wa Sh10,000. Unachotakiwa kufanya ni kuwasilisha wazo lako kabla ya Machi 1, mwaka huu.

Omba fedha hizo hapa: http://tonyelumelufoundation.org/Programme/


4. Anzisha Prize for African Youth Entrepreneurs

Vijana 15 wa umri kati ya miaka 15 na 22 wananafasi ya kujishindia dola za Marekani 100,000 ambazo ni wastani wa Sh250 milioni kwa ajili ya kuendeleza mawazo au biashara zao.

Washindi watapewa mafunzo katika nchi mbalimbali kabla ya kukabidhiwa fedha zao kwaajili ya kuanzisha biashara.

Kijana anayetaka kushiriki anaweza kutembelea tovuti ya Anzisha:

http://youtheconomicopportunities.org/announcement/8474/fellowship-anzisha-prize-african-youth-entrepreneurs

 

 

5. Unreasonable East AFrica Fellowship

Ni programu inayowezesha kutoa mafunzo na misaada kwa biashara zinazoanza kuchipua na mashirika yasiyojiendesha kwa faida. Kila mwaka kwa miezi 10 huendesha mafunzo, kuyaktuanisha mashirika ba wafadhili na kuendesha harambee kwa ajili ya kuyasaidia mashirika hayo.

Kwa mashirika yanayohitaji mafunzo na misaada hii ndiyo sehemu sahihi ya kuwamo kwaajili ya kukukua na yanayojiendesha kwa faida ni sehemu sahihi ya kukutana na wadau.

Kwa namna ya kujiunga tembelea: http://unreasonableeastafrica.org/

Friday, January 27, 2017

AJIRA NA KAZI: Mambo ya kuzingatia kwa waajiriwa mwaka 2017

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

Inawezekana kila mwaka umekuwa miongoni mwa mamilioni ya Watanzania wanaonza mwaka mpya kwa mikogo na mbwembwe nyingi

Unaweza kuwa katika kundi la watu wenye utamaduni wa kushiriki mwaka mpya, kwa tafsiri ya kusamehe yaliyopita, kujitathmini na kuweka malengo mapya.

Kuna kundi linalosherehekea baada ya kuongeza idadi ya miaka, wapo wanaoshereheka kwa kushinda vikwazo vya mwaka uliopita.

Katika makala haya naangazia mambo sita ambayo mwajiriwa anapaswa kuyazingatia tunapoanza mwaka mpya wa 2017.Inawezekana mwaka 2016 ulibakia nyuma kwa sababu ya wengine au kwa makosa yako mwenyewe, lakini ukijaribu mambo haya, mwaka huu unaweza kuwa wa mafanikio kwako.

Ongeza thamani

Kuna mambo matatu yanayoweza kuongeza thamani ya mwajiriwa kazini bila kujali uzoefu.Kwanza ni muhimu kuongeza mbunifu. Inawezekana umekuwa ukifanya hivyo au hukuwahi kujihusisha lakini ni jambo la msingi.

Ubunifu unahusisha zaidi kufikiria mambo mapya au mawazo yanayohusiana na ofisi yako ili kuongeza thamani yako kazini.

Pili, ni muhimu kuongeza kiwango cha elimu yako. Hii inatofautiana na suala la ubunifu kwani unaweza kuwa mbunifu licha ya elimu ndogo uliyonayo na ukawa bora kuliko wenzako wanaokuzidi elimu

Unaweza kujisomea mambo yanayohusu taaluma yako kwa njia ya mtandao au kuhudhuria madarasa ya baada ya muda wa kazi. Kimsingi, tengeneza muda na ratiba isiyoweza kuathiri ajira yako.

Tatu, unatakiwa kuendelea kuonyesha uwezo zaidi wa kile unachokijua mbele ya wafanyakazi wenzako ili wakutambue.Tumia njia chanya kuwasilisha ili kuepuka kuwakwaza.

Kumbuka ajira yako inawindwa na watu wengine wenye uwezo na hata uzoefu kuliko hata ulionao. Mchango wako ofisini ni sawa na mchezaji wa soka, ambaye kiwango chako ndiyo kinakutengenezea thamani katika soko la usajili.

Linda hadhi yako

Je wewe ni muongo, mbabaishaji au haupo makini? Umewahi kujiuliza ofisi na wafanyakazi wenzako wanakutambua kwa utambulisho wa mtu makini, mwelevu, mchapakazi, mbishi, mjuaji, mchekeshaji tu au mzigo tu.

Ziko sababu za kimazingira zinazoweza kusababisha ukaonekana una au hauna mchango. Lakini kwa sehemu kubwa hupaswi kumnyooshea kidole mfanyakazi mwenzako.

Kumbuka uwezo wako ni jambo moja na hadhi yako ni jambo lingine. Lakini baada ya kuona hivyo umefanya nini? Umewahi kujitathmini kati yako na ofisi unayofanya kazi ni upande gani ulionufaika zaidi ya mwenzake?

Je, umeinyonya ofisi yako au imekunyonya? Je, umekuwa na matokeo gani kwako binafsi.Unadhani kwa miaka uliopo ofisini, elimu na uzoefu vina uhusiano na nafasi au kipato ulichonacho. Ni mambo gani yamekwamisha. Umemshirikisha nani na kwa namna gani.Ulipata mrejesho?

Pengine una tatizo la aina ya mavazi au mazungumzo yako. Unadhani umeathiriwa na ulevi au sifa mbaya kama udokozi, uzinzi, uchafu na tabia nyinginezo zinazokera?

Kama ulifanya hivyo mwaka 2016, hakikisha unabadilika haraka, vinginevyo, utaendelea kukosa raha. Jitathmini kwa kuuliza marafiki zako, waulize wewe ni mfanyakazi wa aina gani? Waulize viongozi unatakiwa kufanya nini ili kujenga taswira mpya.

Vumilia

Umekuwa mtu wa kulalamika kila jambo. Wakati mwingine unahisi unatengwa au kutopewa nafasi.Umejaribu pengine njia kadhaa kupata faraja lakini hujafanikiwa.

Jiulize matatizo yanayokusonga ni jambo la kujitakia au unatengenezewa mazingira hayo. Jitathmini ili kujua endapo umetengenezewa na ni kwa nini. Kumbuka unaishi katikati ya binadamu bila kujali anayekuongoza, lakini jaribu kutambua zaidi bosi wako anataka nini na kwa wakati gani.

Epuka kumkwaza kwa jambo lisilokuwa na ulazima. Mambo mengine kaa kimya na usionyesha chuki ukitofautiana japo ni vyema kutumia busara kuwashirikisha wafanyakazi wenzako kwa mrengo chanya.

Ongeza kujiamini kwako

Tafsiri ya kujiamini ndiyo inayozaa kuaminika.Kuaminika ndiyo kunazalisha mafanikio yako. Na hali ya kujiamini haijitokezi kwa bahati mbaya ila ni muhimu kwanza kuwa mjuzi wa mambo. Ili kuishi katika dunia mpya ya taaluma, ni lazima kujenga uwezo wa kujiamini katika kile unachokiamini.Hali hiyo itakujengea heshima ofisini kwako.

Mwaka 2017, jaribu kuhakikisha unatenga muda wako kwa ajili ya kuongeza maarifa kupitia usomaji wa vitabu na makala mbalimbali zinazohusu ajira yako. Kujiamini pekee haitoshi lakini kujiridhisha na unachoambiwa na kutetea unachokiona kwa macho yako.

Rekebisha makosa yako

Kuna makosa ya kutengenezewa na kuna makosa ya kutengeneza mfanyakazi mwenyewe. Kufanya makosa yanayokuwa kinyume na kanuni za ofisi yako kunaweza kuathiri ajira yako moja kwa moja. Ni kigezo cha kwanza kutofanikiwa.

Lakini kuna makosa mengine yanayohusiana kwa karibu na taaluma ikiwemo mwenendo wa tabia yako, uhusiano wako na wafanyakazi wenzako.

Pengine hata unavyovaa mavazi yako na unavyoishi kwa matendo yako na jamii nje ya ofisi. Ujumbe unaoweka mitandaoni vina uhusiano mkubwa na ajira yako.

Makosa hayaepukiki lakini ni muhimu kuwa makini ili kujilinda zaidi na kibarua chako, utambulisho wako. Jitathmini 2016 umefanya makosa ya aina gani, umeyashughulikia au bado na kwa nini imekuwa vigumu.

Angalia uhusiano wako na wengine

Nguzo ya mfanyakazi yeyote kufanikiwa ni uhusiano mzuri na wengine.Uhusiano kazini utakusaidia kupata ushirikiano wa mambo kadhaa usiyoyafahamu na mengine yaliyofichika.

Siyo rahisi kuwa na uhusiano na kila mtu, lakini jaribu kuwa makini na vikwazo na uwatambue wanaoweza kuwa watetezi wako pale inapotokea changamoto ya kikazi.

Angalia watu walioshikilia maslahi yako na upime changamoto za vikwazo vinavyoweza kukutenganisha nao. Kuwa mtulivu lakini isiwe kwa kiwango cha kupitiliza na ukabadilika asili yako ya awali.

Tumia busara kuwasiliana na wenzako.Usijifanye wa tofauti au kundi la watu muhimu zaidi ofisini kwa sababu ya utofauti wa kipato, elimu au ajira yako.

Nje ya ofisi yako angalia tena uhusiano wako. Unatambuliwa na nani na kwa mtazamo upi.Fursa unazipata au zimejificha nyuma yako kwa sababu ya kujitenga kwako? Tumia maarifa yako kwa mwaka 2017 kujenga taswira yako mpya.

Friday, January 27, 2017

Hatua za kuchukua unapoamua kuacha kazi -2

 

By Christian Bwaya, Mwananchi bwaya@mwecau.ac.tz

Katika makala yaliyopita tuliona sababu za watu kuacha kazi na hatua za awali za kuchukuliwa na mtu anayefikiria kufanya maamuzi ya kuacha kazi. Tuliona ni muhimu kuwa na utulivu unapofanya maamuzi mazito.

Mtu mtulivu anayejitambua hafanyi maamuzi yanayoongozwa na hasira au hata furaha isiyo na kiasi.

Hutafuta ushauri wa kitaalamu ili kufikia maamuzi yanayotokana na uelewa sahihi wa mambo.

Kuna faida ya kuacha kazi kwa kufuata taratibu rasmi. Kwanza, inakusaidia kudai haki zako unazostahili kwa mujibu wa sheria.

Ili uweze kupata haki zako, ikiwa ni pamoja na mafao yoyote unayostahili kwa mujibu wa mkataba wa kazi, zitahitajika nyaraka rasmi kuthibitisha uliacha kazi.

Aidha, kuheshimu mkataba kunakuepusha na uwezekano wa kujiingiza kwenye matatizo baada ya kuondoka kazini.

Unapoondoka kienyeji kazini kwa sababu yoyote ile, mwajiri mkorofi anaweza kukuhesabu kuwa mtoro kazini na kukubebesha tuhuma za kuiba mali za ofisi zilizokuwa chini ya uangalizi wako.

Wapo wafanyakazi ambao, mara baada tu ya kupata kazi nzuri, waliondoka kwa mbwembwe na dharau kwa waajiri wao.

Wengine waliacha kazi kwa notisi ya saa 24 kwa kuamini hawana cha kupoteza tena. Haikuwa kama walivyofikiri.

Ondoka kazini kwa namna inayolinda uhusiano wako wa kikazi na mwajiri. Unaweza usione faida hiyo leo lakini baadaye uhusiano mbaya unaweza kukugharimu.

Mwajiri mpya anaweza kuwasiliana na mwajiri wako wa zamani kujiridhisha kama ni kweli uliacha kazi.

Kama hukuondoka kwa utaratibu, unaweza kujikuta ukipoteza kazi uliyofurahia kuipata.

Katika makala haya tunapendekeza namna nzuri ya kutoa taarifa ya kuacha kazi kwa mwajiri wako wa sasa na wafanyakazi wenzako.

Kutoa taarifa rasmi kwa mwajiri

Baada ya kujiridhisha kuwa umezingatia taratibu za kuacha kazi kwa mujibu wa mkataba, hatua inayofuata ni kufanya mawasiliano rasmi na mwajiri kuwa sasa unaacha kazi.

Siyo waajiri wengi wanaweza kufurahia kukutana na tetesi za mfanyakazi kuacha kazi kwenye vikao vya chai. Epuka kueneza taarifa hizo kabla hujawasiliana rasmi na mwajiri.

Taarifa rasmi ya kuacha kazi ni muhimu, kama inawezekana, itanguliwe na mazungumzo ya ana kwa ana na mwajiri.

Katika mazungumzo hayo, mwajiri wako anapata nafasi ya kuzipokea habari mbaya katika mazingira yasiyo rasmi kabla hajasoma barua rasmi.

Katika kuandika barua ya kuacha kazi, yapo mambo kadhaa ya kuzingatia. Mosi, ni kuweka wazi kuwa nia yako kuwa unaacha kazi.

Kwa mfano, barua yako inaweza kuwa na kichwa cha habari kinachosema;

‘YAH: KUACHA KAZI’.

Maneno kama, ‘Kuhama kazi’, ‘Kuchoka na mazingira ya kazi’ ‘Kubadili kazi’ yanaweza kuwa na tafsiri nyingi. Epuka maneno yenye tafsiri nyingi.

Baada ya kuainisha lengo la barua yako, andika sentensi inayotaja tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako.

Kwa mfano, ‘Ninakuarifu kuwa baada ya kutafakari kwa kina, kwa hiari yangu, nimeamua kufanya maamuzi ya kuacha kazi ili kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo. Siku ya mwisho kufanya kazi inategemewa kuwa Ijumaa ya tarehe 31/3/2017.’

Baada ya kutaja siku ya mwisho kufanya kazi, shukuru kwa kutambua mchango wa mwajiri wako katika kuboresha ujuzi wako.

Taja kwa ufupi fursa ulizopata tangu umeanza kazi unazoamini zilizokujenga kiuweledi na kiuzoefu.

Inawezekana kweli kuna mambo hukuyapenda katika kampuni/taasisi unayoondoka. Labda ulikuwa na mgogoro na mkubwa wako wa kazi.

Huu si wakati wa kulalamika wala kukumbushia maumivu yaliyopita. Tumia lugha chanya isiyoonyesha hisia hasi.

Sambamba na hilo, epuka kumtaja mwajiri wako mpya wala unakokusudia kwenda. Mwajiri haitaji kujua mipango yako baada ya kuachana nae.

Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi.

Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi.

Unaweza pia kuonyesha uko tayari kwa usaili wa kuacha kazi kumpa fursa mwajiri kukudadisi sababu zilizokufanya uondoke; namna utakavyopewa haki zako; utaratibu wa makabidhiano ya ofisi; utayari wako katika kumsaidia mtu mpya atakayepatikana kuchukua nafasi yako na mambo mengineyo.

Kuwajulisha wafanyakazi wenzako

Baada ya makubaliano rasmi na mwajiri wako kwamba sasa unaacha kazi, kinachofuata ni kuwajulisha wafanyakazi wenzako.

Taarifa kuwa sasa unaondoka zinaweza kuibua hisia za wivu. Unapowajulisha, heshimu hisia zao.

Ni kweli umeacha kazi na unakwenda mahali bora zaidi. Pengine hata wafanyakazi wenzako wangependa kwenda huko unakokwenda wewe.

Usiwafanye wajione hawana mahali pa kwenda kwa kuendelea kubaki na mwajiri unayeachana naye.

Huna sababu ya kufanya majigambo ya maneno na vitendo kabla na baada ya kuondoka kwenye kituo cha kazi.

Hakuna sababu ya msingi kueleza kwa nini umeondoka na kwamba unakokwenda kuna maslahi zaidi.

Pia, usihatarishe uhusiano wako na mwajiri unayemwacha kwa kumsema vibaya kwa wafanyakazi unaowaacha. Hata kama ni kweli ana upungufu wake; hata kama mazingira ya kazi unayoyaacha hayafai; huna sababu ya kuyaeleza hayo kwa wafanyakazi unaowaacha.

Sema maneno chanya. Toa sababu za kawaida kwa nini unaondoka. Ondoka kwa namna ambayo itakufanya uendelee kuwa na uhusiano mzuri na hao unaowaacha. Kumbuka kuna kesho!

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. 0754 870 815

Friday, January 13, 2017

AJIRA NA KAZI: Muongozo wa maisha ya kazi kwa mfanyakazi mgeni

 

By Luqman Maloto, Mwananchi

Unapokuwa mfanyakazi mpya kazini kuna vitu viwili utakutana navyo. Kwanza ni changamoto ya kimazingira, pili ni uzuri wa mazingira.

Changamoto ni kuwa utakutana na mazingira ambayo hujawahi kukutana nayo. Utajikuta unatakiwa kuanza kuelewana kikazi na watu ambao hukuwa ukijuana nao hapo kabla.

Uzuri wake ni kuwa utakutana na mazingira mapya utakayotakiwa kuyazoea, pamoja na watu wapya ambao utajenga nao urafiki mpya wa kikazi.

Watu wapya na mazingira mapya kwa kawaida huwa na mambo yake mazuri kuliko uliyozoea, vilevile kutakuwapo changamoto mpya ambazo hukuwahi kuzikabili.

Faida kubwa unapoanza kazi ni kuwa viongozi wako wanakuwa na imani kubwa nawe kuwa utatenda kazi bora kwa jinsi ambavyo uliweza kufaulu vizuri usaili wako.

Unapoingia kazini ni rahisi kupendwa. Mkuu wako wa idara hawezi kuzungumza na wewe kwa ukali, lugha itakayotumika ni ya majadiliano zaidi kuliko amri. Unachotakiwa ni kuichukua tabia hiyo ili iendelee kila siku.

Kutoka lugha ya majadiliano mpaka kuanza kufokeana kazini hapo ujue tayari kuna vitu ambavyo vimeshakaribishwa. Ni wewe kama mfanyakazi unakuwa umetengeneza mazingira ya kufokewa kutokana na utendaji wako mbaya au nidhamu mbovu.

Shika muongozo ufuatao ili ukusaidie kujenga mazingira bora ya kazi kuanzia ukiwa mpya kazini mpaka utakapotajwa kuwa mfanyakazi mzoefu miongoni mwa wazoefu

Nidhamu binafsi na kazi

Kila siku unatakiwa ujiheshimu na uiheshimu kazi yako. Kipindi ambacho viongozi wako wanakulea kutokana na upya wako kazini, wewe thibitisha kwa vitendo nidhamu yako binafsi na ya kazi.

Wafanye viongozi wako wabadili nyakati za kukupenda kwa upya wako mpaka kuvutiwa na wewe kwa utendaji na nidhamu yako binafsi.

Utashangaa maisha yako kazini yanakuwa mepesi kila siku. Unaweza kustaajabu bosi ambaye kila mtu anamwogopa kwa ukali na usumbufu mwingine, akija kwako mnazungumza kwa upendo na kuheshimiana.

Hivyo, jiheshimu, heshimu viongozi pamoja na wafanyakazi wenzako. Hakikisha uvaaji wako ni mzuri wenye kuendana na mazingira ya kazi yako, kisha uchape kazi kuzidi kiwango ambacho watu wangekitarajia kutoka kwako.

Unapaswa kuwa mtu mwenye malengo. Jiwekee malengo ya kazi na uyafikie. Njia hiyo itakufanya uonekane mtu bora zaidi kazini na utamvutia mwajiri kila siku.

Kuwa sehemu ya wafanyakazi

Ukiingia kazini, usitake kujionyesha kuwa wewe ni jeshi la mtu mmoja. Ni kweli unatakiwa uzingatie zaidi kile ambacho kimekufanya uajiriwe, lakini hapo kazini kuna wafanyakazi wenzako ambao kwa namna moja au nyingine utahitaji ushirikiano wao.

Unaweza kujiona unajitosheleza kikazi, kwa hiyo ukaona huhitaji kuuliza wala kumshirikisha yeyote kile unachofanya, lakini wewe ni binadamu. Unaweza kuumwa ghafla kazini na wafanyakazi wenzako ndiyo watakaotakiwa kukupa msaada.

Hivyo, ukiingia kazini jambo la kwanza hakikisha unafahamiana na wafanyakazi wenzako. Hakikisha unajuana nao majina, na umwite unayemhitaji kwa jina lake. Ni kosa kumaliza wiki nzima kazini ukiwa hujachukua hatua yoyote kujua majina ya wafanyakazi wenzako.

Ukiwa mgeni kazini, hakikisha kila siku katika siku zako za mwanzo, uwe unatumia angalau dakika 20 kuzungumza na wafanyakazi wenzako japo wawili, mbadilishane uzoefu kuhusu kazi. Upate kile ambacho wamekuwa wakifanya kila siku, nawe utoe ulichonacho.

Mazungumzo na wafanyakazi wenzako, yatakusaidia kujua mwajiri wako anapenda nini na mambo gani hapendi. Utakachokipata kitakusaidia kujitengenezea njia za kuishi ukiwa kazini.

Hakikisha mahudhurio mazuri

Siku za mwanzo ingia kazini mapema na ujitahidi kutoka kazini ukiwa umechelewa. Baada ya hapo, hakikisha hiyo ndiyo inakuwa tabia yako siku zote.

Ukiwa mpya kazini epuka visingizio na maombi ya ruhusa ya hapa na pale. Onyesha kuwa umeanza kazi rasmi na upo tayari kiakili na kimwili. Ukianza kutia doa mapema, utamfanya mwajiri wako akuone una upungufu.

Weka vizuri rekodi yako ya mahudhurio. Kumbukumbu za kiofisi zikitazamwa wewe uonekane hukosi kazini na muda wako wa kuingia ni mapema kisha huchelewa kutoka.

Una wagonjwa? Watembelee katika muda ambao unakuwa umeshatoka kazini. Safari nyingine fanya siku zako za mapumziko. Fanya hivyo ili kutetea rekodi zako za kiofisi hasa kwenye eneo la mahudhurio.

Usishiriki majungu, siasa

Kila ofisi majungu na mazungumzo ya siasa yapo, ni kutokana na kukutanisha watu wa aina tofauti. Unachotakiwa kutambua ni kuwa umeingia kazini kufanya kazi na siyo kupiga soga, kusengenya watu na kuendekeza ubishi wa kisiasa.

Onyesha tofauti kwa kujiweka mbali na vitendo hivyo. Hakuna mwajiri ambaye anaweza kuwapenda watu ambao muda wa kazi wanakuwa wanabishania siasa. Ukijiunga nao, unamfanya mwajiri akuchukie ukiwa bado mgeni kazini.

Kama una damu ya siasa na unapenda kuzijadili, siyo vibaya kama utazipangia muda wake, nyakati za mapumziko ya chakula au kipindi cha kuupoza ubongo. Siyo unaingia kazini kabla hujashika faili lolote au hujawasha hata kompyuta unaanza siasa. Ukiwa mtu wa aina hiyo, utayaona mazingira ya kazi ni magumu na utajishushia heshima mbele ya mwajiri.

Mazungumzo na wafanyakazi wenzako muda wa kazi yawe yanahusu kazi. Siyo kujadili mfanyakazi mwenzako ana uhusiano wa kimapenzi na nani. Hayo siyo ambayo yaliwavutia wasaili wako kisha wakakuona unafaa kupewa kazi.

Tengeneza mtandao mzuri

Ni mtandao wa kazi. Ndani ya ofisi na nje. Hiyo ni kukusaidia kutimiza wajibu wako inavyotakiwa. Itakusaidia wakati wowote pale unapojiona umekwama kupata msaada wa haraka.

Waajiri wengi wana nongwa, hawapendi kuona mtu anasimama na kutembea kutoka meza moja kwenda nyingine akiwa kazini. Kwa hiyo, unapohitaji msaada kutoka kwa mfanyakazi mwenzako, mtumie barua pepe au ujumbe wa simu, kisha naye akujibu.

Mtambue mfanyakazi mzuri

Ukiwa mgeni kazini unatakiwa kumtambua mfanyakazi mzuri, anayetimiza wajibu wake na ambaye anamvutia hata mwajiri wako. Ukimshamjua mfanye kuwa rafiki na mshauri wako wa mambo ya kazi.

Friday, January 13, 2017

Jadili unachotaka kulipwa na mwajiri

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Huwezi kupata malipo unayostahili bila kujadili mshahara.

Watu wengi hupumbazwa na furaha ya kupata ofa ya kazi waliyokua wanataka, kiasi cha kuwasababishia kukubali masharti yanayokuja na ofa bila kuyaafiki.

Unatakiwa ukumbuke kupata ofa ya kazi sio mwisho wa mahojiano na badala yake unaingia kwenye sehemu ngumu zaidi ambayo ni makubaliano kuhusu malipo ya mshahara na marupurupu mengine.

Unaweza kuwaza kwamba labda mwajiri wako atabadili mawazo ukiomba fedha zaidi, au usubiri mpaka uthibitishe uwezo wako ndio uombe mshahara unaotaka.

Lakini kupata mshahara unaotaka, kunategemea kwa kiwango kikubwa na jinsi unavyojiamini. Kama unajua ujuzi utakaoleta kwenye kampuni na thamani yake, lazima uwasilishe pendekezo zuri kuhusu malipo yako.

Hata hivyo, zaidi ya kujiamini kuna njia unazoweza kutumia kuafikiana mshahara baada ya kupata ofa ya kazi.

Fanya utafiti katika sekta

Kufanya utafiti wa kiwango cha mshahara kilichopo kwenye sekta ya kazi unayoomba, ni suala muhimu kabla ya kwenda kufanya usaili wa kazi.

Hii ni kwa sababu waajiri wengi watakuuliza kuhusu mshahara unaotegemea kulipwa.

Uliza kwa jamaa na marafiki au fanya utafiti mtandaoni na ukishajua kiwango, ongeza asilimia 30 ili upate nafasi ya kufanya maelewano na wahusika.

Jadili bima, mifuko ya jamii na faida nyingine. Ukishapata ofa ya kazi mwajiri wako atakupa mgawanyo wa mshahara wako, michango na bonasi. Akishafanya hivi sasa ni zamu yako kuleta mahitaji yako, usianze na mshahara au bonasi badala yake uliza maswali kama mchango wako katika mfuko wa jamii. Asilimia ngapi ya mshahara itatumika na mwajiri atachangia kiasi gani.

Aina ya bima ya afya, gharama yake na kama utarudishiwa gharama za usafiri kwenda kwenye mikutano ya kikazi.

Useme nini wakati wa maafikiano ya mshahara?

Kusaidia kufikisha maombi yako kwa urahisi, unaweza kusema kitu kama; “Nina furaha ya dhati kuanza kufanya kazi na nyinyi, Ninaamini nitaleta mchango na mafanikio makubwa hapa. Nimetathmini ofa yenu ya Sh2,000,000 lakini kutokana na uzoefu wangu wa miaka mitano katika sekta hii

na wateja ambao nitawaleta hapa, nilikua nategemea ofa ya Sh3,500,000.’’

Kumbuka mwajiri wako anategemea majadiliano haya, hivyo kistaaarabu sisitiza kuhusu mshahara uliokuwa unategemea. Atakapokupa jibu kwamba hawezi kuongeza mshahara na ukajiridhisha kwamba hawezi, omba muda wa kufikiria.

Usisahau kuhusu bonasi

Ukiondoa mshahara, unaweza pia kujadiliana na mwajiri kuhusu bonasi. Tumia utaratibu kama uliotumia wakati mnaelewana kuhusu mshahara. Hapa kumbuka kuuliza bonasi yako itakokotolewa vipi? Nani atakuwa na wajibu wa kutathmini na kuamua bonasi yako na utaipata kila baada ya muda gani?

Usipouliza hutojua

Watanzania ni watu wastaarabu, wengi tunaona aibu kuongelea ni fedha kiasi gani tunahisi tunafaa kulipwa. Lakini hakuna ambaye atakataa kulipwa zaidi ya anacholipwa sasa.

Kwa hiyo, njia bora ya kupata fedha zaidi kutoka kwa mwajiri wako ni kumwambia kiasi unachotamani kutokana na majukumu anayotarajia kukupa.

Makala haya yameandaliwa kwa hisani ya shirika la Brighter Monday. www.brightermonday.co.tz

Mak.brightermonday.co.tz

Friday, January 6, 2017

Ukiona dalili hizi acha kazi

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Kuacha kazi kunaweza kuwa ni jambo zuri katika maisha yako. Ukweli ni kuwa ni vigumu kupata kazi uipendayo kwa asilimia 100.

Hata hivyo, kama unapenda kuwa na kazi ambayo inatimiza matakwa yako, kwa hakika hutokubali kufanya kazi usiyoipenda. Na hata kama upo kwenye kazi unayoipenda, kuna matatizo ambayo ukikutana nayo ni ishara kwamba umefikia muda wa kusonga mbele kwingine.

Zifuatazo ni dalili 10 zinazokuonyesha kwamba umefikia muda wa kuacha kazi unayofanya sasa.

 

Ujuzi wako hautumiki ipasavyo

Watu wengi wenye motisha huanza kutoridhika kama wanatumia muda wao mwingi kwenye kazi ambayo haitumii ujuzi wao ipasavyo. Kama wewe ni mmoja wa watu hawa ni bora ukatumia muda wako kutafuta kazi ambayo itatumia ujuzi wako ipasavyo.

 

Unafanyishwa kazi kupita kiasi bila kulipwa fidia

Waajiri wengi Tanzania hawalipi wafanyakazi wao wanapofanya kazi ndani ya muda wa nyongeza.

Ingawa kila kazi ina wakati ambao wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi nje ya muda wa kazi, hautakiwi kufanya hivyo mara kwa mara kwani itakusababishia kuwa mchovu na kushindwa kufanya kazi vizuri.

 

Umechoka na huna motisha

Hutokea wakati mwingine kazi au kampuni inakua sio sahihi kwako. Aidha, huamini ujumbe au maadili ya kampuni au huridhishwi na kazi unayofanya. Hii ni dalili kuwa hapo hapakustahili kwa sasa.

 

Humheshimu au kumuamini bosi wako

Moja ya sababu kubwa za watu kuacha kazi ni kumchukia bosi wao, na hili ni kweli hasa kama bosi huyo anafanya haya: anachukua sifa kwa kazi uliyofanya wewe bila kukiri mchango wako, haangalii maslahi yako anapofanya makubaliano ya kazi na mabosi wake, anajifanya kukusikiliza lakini hafanyii kazi maoni au malalamiko yako au hakuheshimu.

 

Ujuzi wako umezidi kazi unayofanya

Wakati mwingine unakuta umejifunza vyote ambavyo unaweza kujifunza kutoka kwenye nafasi uliyopo, hivyo hupati changamoto zozote. Kama hakuna nafasi ya kuhamia sehemu nyingine kwenye kampuni hiyohiyo basi ni muda wa kuhama kampuni.

 

Hupendi utamaduni wa kampuni

Ni muhimu kupenda mazingira yako ya kazi. Kwa mfano, baadhi ya ofisi zinaweza kuwa na kelele mno au kuwa na sheria kali. Mwenyewe unajijua vizuri na unajua ni mazingira gani yatakufaa zaidi.

 

 

Unalipwa chini ya kiwango

Pesa haitakiwi kuwa sababu kuu ya wewe kufanya kazi ufanyayo. Lakini kazi yako inatakiwa ikuwezeshe kumudu gharama za msingi za maisha hasa kama unaishi maeneo ya miji mikuu ambayo maisha yako juu.

 

Kampuni yako haiwekezi kwako

Ni muhimu kwenda na wakati kwa kujua yanayojiri katika sekta yako ili uongeze uwezo wako wa kufanya kazi. Lakini kama kampuni yako haiko tayari kulipia kozi zitakazokusaidia kuongeza ujuzi wako kazini, hii ni dalili kwamba hawakuthamini. Tafuta sehemu nyingine.

 

Unahisi kwamba hii ni ‘kwa ajili ya sasa’

Kama unahisi ajira yako ni ya muda na haikufai kwa muda mrefu, ni bora uache hasa kama ni kazi usiyoitaka.

 

Umepata ofa nzuri kwingine

Kama umepata ofa ya kazi ambayo itakufaa zaidi, Hiyo ni sababu rahisi ya kukufanya uache kazi uliyo nayo sasa.

 

Kumbuka

Watu wengi hutafuta kazi nyingine pale tu wanapoacha kazi au kwa kutoridhishwa na kazi walizonazo, hili lina hasara kwako kwa sababu itasababisha kukubali kazi isiyo kufaa.

Muda wote tafuta kazi, hii itakuonyesha nafasi zilizopo na utakapopata ofa au kuitwa kwenye mahojiano itakujulisha thamani yako kwenye soko la ajira.

Makala haya yamenadaliwa kwa hisani ya shirika la Brighter Monday.

Friday, January 6, 2017

Mbinu za kushinda maswali ya usaili wa kazi - 3

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Katika makala yaliyopita tuliona maeneo manne muhimu ya kuzingatia unapoingia kwenye usaili.

Pamoja na maswali mengine, unaweza kuulizwa maswali kuhusu uzoefu wako wa kikazi huko ulikotoka.

Tuliona kuwa unapoulizwa maswali kama hayo, lengo ni kupima namna unavyoweza kuwa mkweli.

Usikimbilie kumponda mwajiri wako wa zamani kwa kutoa sababu za kutoridhika na mshahara, migogoro ya kazi uliyokuwa na mwajiri wako, kutoelewana na wakubwa wako wa kazi au watu uliokuwa unawasimamia.Ukifanya hivyo utaonekana wewe ni mtu wa matatizo.

Badala yake, toa sababu chanya zinazoleta picha ya mtu mkomavu kazini. Kwa mfano, unaweza kuonyesha kuwa uliacha kazi uliyokuwa nayo kwa sababu ulipata fursa ya kutumia vipaji vyako vizuri zaidi kwingineko, au kwamba kazi uliyoipata ingekuwezesha kukua kiujuzi zaidi. Katika makala haya, tutatazama maeneo mengine manne unayohitaji kujiandaa ili kushinda maswali utakayoulizwa kwa mafanikio.

 

Matarajio yako kwa mwajiri

‘Unadhani tukulipe mshahara kiasi gani?’

Hili swali linatafuta kujua vipaumbele vyako ukiwa kazini. Ni kweli unatafuta kazi ili upate fedha uboreshe maisha yako. Lakini kuonyesha kuwa ari na kujituma kwako kazini kunategemea na kiasi cha pesa unacholipwa ni kosa la kiufundi. Kosa hili linaweza kuwa kikwazo cha kukukosesha kazi.

Unahitaji kuonyesha ukomavu kwa kuelewa kuwa taasisi bora kama hiyo unayotaka ikuajiri, zina utaratibu rasmi wa kuwalipa wafanyakazi wake. Mtu hulipwa kwa sifa alizonazo. Kwa uelewa huo, utapata alama za ziada.

Hata hivyo, pamoja na majibu hayo wapo wasaili wanaoweza kukubana uwaambie matarajio yako. Fahamu kuwa kujadili mshahara wa kazi ambayo bado hauna uhakika nayo, haiwezi kukusaidia.

Ikiwa utalazimika kutaja tarakimu, inatarajiwa kuwa tayari utakuwa umeshafanya utafiti wa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na viwango vya mishahara.

Taja kiwango ambacho hakitaonyesha huna thamani, lakini pia usitaje kiwango kitakachoonyesha kujikweza kupita kiasi.

 

Uelewa wa mambo na ujuzi wa kazi

Unaweza kuulizwa maswali yanayopima uelewa wako wa kawaida kwa mambo yanayofahamika. Lakini pia unaweza kuulizwa masuala ya moja kwa moja yanayohusiana na kazi unayoomba.

Wakati mwingine, baadhi ya wasaili hutumia mtihani wa kuandika kujaribu kuthibitisha kama kweli una uwezo na ujuzi uliouonyesha kwenye wasifu wa kazi.

Maswali yanayoulizwa yanaweza kupima moja kwa moja utaalamu uliousomea darasani au namna unavyoweza kutatua changamoto halisi za kazi. Jiandae ipasavyo kwenye maeneo muhimu.

Kilicho muhimu ni namna unavyoweza kutafsiri nadharia zako katika mazingira ya kazi.

Kwa mfano, unaomba kazi ya uhasibu msaili mmoja anakuuliza, ‘Chukulia ofisini kwako kumetokea wizi wa fedha. Utachukua hatua gani?’ Au unaomba kazi inayohusika na utawala, ‘Chukulia kama kiongozi umesikia wafanyakazi wa chini yako wana mpango wa kugoma. Utafanyaje?’

Hayo ni maswali ya uchokozi. Usitumie muda mrefu kutafuta masuluhisho yasiyokuwepo. Jibu kwa ujasiri kuwa hutarajii kuwa matatizo ya namna hiyo yatajitokeza. Lengo ni kuonyesha una uwezo wa kuikinga taasisi yako na changamoto kama hizo.

 

Malengo yako ya baadaye

‘Unajiona ukifanya nini baada ya miaka 10 ijayo?’

‘Una malengo gani ndani ya miaka mitano ijayo?’

Hapa unahitajika kuonyesha ari ya kukua kiujuzi na kiuweledi. Ongelea mipango ya kujifunza zaidi kufikia kwenye malengo makubwa yanayoendana na malengo mapana ya kitaasisi. Kuzungumzia malengo yasiyoendana na kazi unayoomba kutakupunguzia alama.

‘Umeomba kazi kwingine?’ Wanahitaji kuwa na uhakika na maamuzi yako. Ni kweli inawezekana utakuwa umeomba kazi maeneo mengine. Lakini utaonekana mkomavu ukiweza kuonyesha kuwa kazi hii unayosailiwa ndio chaguo la kwanza.

 

‘Utafanya kazi na sisi kwa muda gani?’

Hapa wanataka kujua kama wewe ni mpita njia au la. Inawezekana kweli unaweza kuwa na mpango wa kufanya kazi kwa muda mfupi na utafute njia nyingine. Lakini kuonyesha wazi kuwa unapita wakati hata kazi hujapata si busara. Onyesha ungependa kufanya kazi kwa muda mrefu kadri utakavyohitajika.

‘Unaota kufanya kazi gani nzuri baadae?’ Ukitaja kazi nyingine mbali na hiyo unayoomba, unaleta wasiwasi kuwa hutaridhika na kazi unayoomba. Ongelea mazingira ya kazi bila kutaja kazi mahususi. Kwa mfano, kazi inayokufanya utumie vipaji vyako na ujuzi ulionao. Kazi inayokufanya ukue kiujuzi na kiuzoefu.

‘Uko tayari kuanza kazi lini?’Kama huna kazi, ukisema uko tayari kuanza kazi mara moja inaonyesha utayari ulionao. Lakini kama unabadilisha kazi, kuonyesha utahitaji muda mfupi wa kukamilisha taratibu za kukabidhi majukumu uliyonayo na kuaga, itakupa alama.

 

Fursa ya kuuliza swali

Kwa kawaida, baada ya kuulizwa maswali mengi, kikao cha usaili kitahitimishwa kwa kukukaribisha kuuliza swali. Kama tulivyosema, kila swali lina maana. Unapoulizwa, ‘Je, una swali ungependa kuuliza?’ lengo ni kutaka kujua ulivyo na ari ya kufanya kazi na taasisi hiyo.

Usipouliza swali lolote, maana yake ama huna uelewa wa mambo mengi au huna ari ya kutosha. Uliza swali kuhusu taasisi hiyo. Waliuze wanatarajia nini kwa mtu atakayepata kazi hiyo. Pia unaweza kuulizia mambo yanayohusiana na fursa wanazoweza kutoa kukuza ujuzi wako kama mfanyakazi wao.

Epuka kuuliza maswali ya kimaslahi kama kuuliza’ mtanilipa bei gani?’ Hii inaonyesha huna mtazamo mpana wa kazi. Unaweza hata usijibiwe au ukajibiwa jibu litakalokunyong’onyeza.

Shukrani kwa Fr Aldalbert Donge, Mkurugenzi wa Raslimali Watu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenye kwa kuchangia uzoefu wake katika makala haya. 0754 870 815

Friday, December 23, 2016

Mbinu za kujiongezea thamani kaziniPicha na Citizen Tv

Picha na Citizen Tv 

By Luqman Maloto, Mwananchi

Kupata kazi ni jambo la kwanza lakini muhimu ni namna unavyoweza kuilinda ajira yako.

Ndani ya mashirika binafsi na serikalini, wapo watu waliofanya kazi kwa muda mrefu, lakini kufanya kazi kwa kipindi kirefu hakusaidii kama huendi na mabadiliko ya nyakati.

Vijana wapya wanaingia kwenye soko la ajira wanakuwa na thamani kubwa, kwa sababu wanaingia kazini wakiwa ni rasilimali inayotosheleza mahitaji ya wakati. Mtu ambaye alikuwa kazini zaidi ya miaka 20 anaonekana si mali kitu.

Kwa nini ufike wakati uonekane una thamani ndogo kwenye kazi ambayo umekuwa ukiitumikia kwa miaka mingi na unaiweza? Kwa nini vijana wadogo wageuke rasilimali ghali kwenye kazi ambayo wewe umeifanya kwa miaka mingi?

Haiwezi kukuvutia hata kidogo, kijana ambaye wakati wewe ulipokuwa unaanza kazi na kusifiwa na viongozi wako kutokana na uwezo wako, yeye hakuwa ameanza hata shule.

Utaumia kupewa kijana sawa na mwanao au mdogo wako wa mbali awe kiongozi wako, huku mshahara wake ukiwa mkubwa hata kuzidi mara tatu wa ule wa kwako. Lakini huyu anabebwa na thamani aliyoingia nayo kazini. Wewe ni rasilimali inayoshuka thamani kwa kasi.

Hivyo basi, zingatia mambo matatu; mosi ni kupata kazi, pili kuilinda hiyo kazi yako, tatu na muhimu zaidi ni kuhakikisha unajiongezea thamani ukiwa kazini. Unapoweza kujiongezea thamani kazini unapata faida mbili, kuilinda ajira na kuendelea kuwa rasilimali muhimu ofisini kwako.

Zipo mbinu tatu ambazo ukizitumia vizuri utaitetea thamani yako kazini kila wakati. Na ukiwa na thamani kazini kwako hutakuwa na wasiwasi wa kushushwa cheo wala kuondolewa kazini.

Nenda na wakati

Katika eneo la kazi yako kuna mabadiliko gani? Tupo kwenye ulimwengu wa teknolojia, wagunduzi wanaingiza ugunduzi mpya kila kukicha. Unatakiwa kufungua macho na masikio kuhusu taaluma yako.

Haitakiwi watu wa idara nyingine wajue kuwa sasa hivi kuna ugunduzi mpya wa namna ya ufanyaji kazi katika idara yako, wakati wewe mwenyewe huna habari. Utaonekana huendi na wakati. Siku zote wakati ndiyo hushusha au kupandisha thamani ya mfanyakazi.

Mathalan wewe ni mhasibu na siku zote unatumia programu ya Microsoft Excel kuweka sawa mahesabu yako na takwimu za kiofisi kuhusiana na masuala yote ya kifedha. Hupaswi kubaki nyuma kufahamu kuwa kuna programu toleo la mwaka 2016 (v16.0).

Huo ni mfano tu. Inatakiwa kila mmoja kwa nafasi yake aonekane anakwenda na wakati. Ukiwa mkusanya kodi, unapaswa kufahamu njia mbalimbali mpya ambazo wakwepa kodi huzitumia.

Umeajiriwa kwenye kampuni ya kudai madeni, kwa hiyo unatakiwa ujitume kutafuta maarifa mapya ambayo wadaiwa sugu hutumia ili kuendelea kutolipa madeni wanayodaiwa.

Eneo la kwenda na wakati lina maana ya kuwa na maarifa mapya yenye kwenda na wakati. Unapaswa kujua dunia inavyokwenda kuhusiana na kazi yako. Unatakiwa uwe mfuatiliaji.

Kama wewe ni msanifu kurasa katika magazeti, vitabu, majarida na kadhalika na unatumia programu ya Adobe InDesign, unatakiwa uwe na taarifa kuwa kuna toleo jipya la Novemba 2, mwaka huu la CC 2017.

Hata kama ni mwajiriwa katika kampuni ya ulinzi, unahitaji kufahamu mbinu mpya ambazo wezi wanazitumia kuiba.

Jitahidi kujifunza

Ukishajua mambo mapya kuhusiana na kazi yako anza kujisomea. Unaweza kwenda darasani au kujisomea wewe mwenyewe kupitia vitabu na mitandao. Maarifa utakayoyapata hakikisha unayaingiza kazini kwako ili uonyeshe tofauti.

Viongozi wako watakuheshimu zaidi kutokana na maarifa mapya ambayo unayaingiza kazini kwako kila wakati. Wataingia vijana wapya kutoka vyuoni lakini wanachoingia nacho tayari unacho na baada ya muda unawapita kwa kasi kutokana na tabia yako ya kupenda kujifunza.

Tupo kwenye ulimwengu ambao watu wanaamini zaidi vyeti kuliko maarifa ndani ya kichwa. Kwa maana hiyo unapopata nafasi ya kurejea darasani ili uwe na cheti chenye kuonekana, utakuwa unajiongezea thamani thamani kubwa zaidi.

Amua kuwa mtu wa kutafuta maarifa mapya na kuyaingiza kichwani kwako. Hilo siyo tu litakusaidia kukuongezea thamani kazini kwako, bali pia hata taasisi nyingine ni rahisi kukumulika na kutamani kufanya kazi na wewe kama rasilimali ya wakati mwafaka.

Kuwa mbunifu

Hakikisha huzoeleki kazini kwa namna unavyofanya kazi zako. Ukiwepo na usipokuwepo lazima tofauti yako ionekane. Si kwa sababu ya kuficha maarifa yako ili wenzako wasiyatumie, hapana. Ni kutokana na ubunifu ambao unakuwa nao kila siku katika utendaji wako.

KIla unapotoka kazini, unarejea nyumbani na kulala. Usiku unaamua kujinyima hata dakika chache kuifikiria kazi yako hasa jinsi ya kuifanya tofauti.

Ukiwa mbunifu unaweza kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuchokwa. Na kila mara utafikiriwa kuongezewa maslahi kwa sababu unahitajika zaidi.

Kwa kawaida wafanyakazi wabunifu thamani yao huwa juu. Pale taasisi inapofikiria kupunguza wafanyakazi ili kuondokana na mzigo wa uendeshaji, mfanyakazi mbunifu hubaki kutokana na umuhimu wake kimaarifa.

Luqman Maloto ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius www.luqmanmaloto.com

Friday, December 23, 2016

Mambo muhimu unapojiandaa na usaili wa kazi - 1

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Kuitwa kwenye usaili wa kazi ni hatua ya mwisho kuelekea kupata ajira uipendayo.

Mara nyingi, kazi inapotangazwa waombaji wa kazi hiyo huwa ni wengi. Baada ya kupokea maombi ya kazi, shughuli inayofuata ni kufanya uchambuzi wa kuwatambua waombaji wanaokaribia vigezo vinavyohitajika.

Matokeo ya uchambuzi ni kupatikana kwa orodha ya watu wachache wanaoitwa kwa hatua ya mwisho ya uombaji wa kazi.

Kwa kuwa siyo watu wengi hufikia hatua hii, unapopata taarifa rasmi kuwa umeitwa kwenye usaili wa kazi uliyoiomba, ni jambo la kujivunia. Kushindana na kundi la watu wengi waliohitaji kazi hiyo na hawakuitwa, siyo jambo dogo.

Hata hivyo, ni vizuri kutambua kuwa usaili wa kazi sio kupata kazi. Wapo watu waliowahi kuitwa kwenye usaili mara nyingi lakini hawakupata kazi. Makala haya yanakupa dondoo chache za kukusaidia kufanya usaili kwa mafanikio.

Lengo la makala haya si kujadili makosa wanayofanya watu kwenye usaili. Tutajitahidi kujadili mambo halisi ya kukuwezesha kushinda usaili na kupata kazi.

Elewa malengo ya usaili

Huwezi kujiandaa vizuri na usaili bila kuelewa malengo ya usaili. Kwa kawaida, usaili ni mahojiano kati ya mwombaji wa kazi na mwajiri kwa lengo la kutathmini uwezo wa kikazi alionao mwombaji. Mahojiano haya aghalabu hufanyika kwa mazungumzo au maandishi katika chumba au eneo lolote linaloteuliwa na mwajiri kwa kazi hiyo.

Hata hivyo, si lazima mwajiri awepo kwenye usaili. Wakati mwingine mwajiri hukasimu mamlaka yake kwa watu anaowaamini kwa kazi hiyo. Jopo hilo hufanya kazi ya kukusanya taarifa zinazotumika kufanya maamuzi ya ikiwa mwombaji wa kazi anaweza kuajiriwa ama la. Kwa muktadha huu, kinachoamuliwa na jopo hilo halali, kinawakilisha matakwa halisi ya mwajiri.

Jambo la msingi kuzingatia ni kuwa unapokwenda kwenye usaili wa kazi, una wajibu wa kuthibitisha kuwa unafaa kwa nafasi unayoomba. Hilo litawezekana ikiwa utaonyesha namna uwezo wako, maarifa yako, na ujuzi ulionao yanavyowazidi watu wengine wanaoshindana kupata nafasi hiyo unayoiomba.

Fanya utafiti wa taasisi

Maandalizi yanaanza kwa kufanya utafiti wa taasisi unayotarajia ikupe kazi. Uelewa wa taasisi ni muhimu kwa sababu maswali mengi utakayokabiliana nayo siku ya usaili, kwa kiasi kikubwa yanategemea namna unavyoielewa taasisi unayotaka ikuajiri.

Katika kufanya utafiti, unahitaji kuelewa historia ya taasisi, dira na malengo yake, mfumo wa utendaji wake, uongozi wake, walengwa katika huduma zake na mambo kama hayo. Uelewa wa kina maeneo hayo utakusaidia kujibu kwa ufasaha maswali yanayoweza kujitokeza siku ya usaili.

Ili uweze kufanya utafiti, unahitaji kufuatilia tovuti ya taasisi hiyo, kurasa za taasisi katika mitandao ya kijamii na machapisho mbalimbali yanayopatikana mtandaoni. Pia, unaweza kuwasiliana na watu wanaoifahamu taasisi husika na kujaribu kupata taarifa zitakazokusaidia.

Jiandae kisaikolojia

Sambamba na kufanya utafiti wa taasisi husika, unahitaji kuiandaa akili yako kwa ajili ya siku ya usaili. Amini kuwa upo uwezekano mkubwa wa kupata kazi uliyoitiwa. Unapokuwa na mawazo chanya, ni rahisi kujenga hali ya kujiamini itakayokusaidia kufanya vizuri zaidi kwenye usaili.

Ni makosa kwenda kwenye usaili hali ukiamini hutapata kazi. Hisia kuwa unatimiza mradi tu, zitakuondolea nguvu za kufanya vizuri.

Hata kama ni kweli mara nyingi umeitwa kwenye usaili wa kazi na hukufanikiwa, amini kuwa safari hii utapata kazi. Imani inajenga kujiamini, kujiamini kunajenga ujasiri.

Kama una wasiwasi na kujiamini kwako, tafuta watu wenye maneno ya kuinua moyo wakusaidie. Soma maandiko yanayokuinua moyo. Kwa kusikia na kusoma maneno yanayokujenga, utaimarika kisaikolojia na kuwa jasiri zaidi.

Sambamba na hilo, epuka kuongea na watu wanaokukatisha tamaa wanaokuonyesha kuwa hutapata kazi. Ukijiruhusu kukutana na watu wa namna hii, utaishia kuvunjika moyo na utashindwa kufanya vizuri.

Hakiki muda na mahali pa usaili

Kosa kubwa unaloweza kufanya siku ya usaili ni kuchelewa. Unaweza kuchelewa kwa sababu nyingi. Mosi, kutokukumbuka muda halisi wa kuanza kwa usaili. Ni rahisi kuchelewa unapokuwa huna hakika na muda halisi wa kuanza usaili.

Pili, unaweza kuchelewa kwa sababu huna uhakika na mahali patakapofanyikia usaili. Kubahatisha namna ya kufika eneo la usaili siku ya usaili, unajiweka kwenye hatari ya kuchelewa, na wakati mwingine, hata kushindwa kufika.

Tafuta ramani ya eneo mapema, jiridhishe na namna utakavyoweza kufika. Hiyo itakusaidia kukadiria muda wa kuondoka nyumbani au mahali ulikofikia ili uweze kuwahi usaili.

Ikiwa unahitaji kusafiri umbali mrefu, usisubiri siku ya mwisho kuanza safari. Fika mapema kwenye eneo lililo karibu na mahali patakapofanyikia usaili, ili upate muda wa kupumzika na kutulia kifikra.

Maandalizi ya mwisho

Unahitaji kuonekana nadhifu siku ya usaili. Ingawa hulazimiki kuvaa mavazi ya gharama na ya namna fulani, hata hivyo unahitaji kuvaa nguo za heshima. Epuka kuvaa nguo zitakazotoa picha ya mtu asiye rasmi. Mavazi mafupi, yanayobana, milegezo, mitindo inayozidi kiasi na mavazi yenye maandishi hayawezi kuwa chaguo sahihi.

Andaa nyaraka muhimu kama vyeti halisi, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, barua ya kuitwa kwenye usaili kama umepewa na nyaraka nyingine kama ulivyoelekezwa. Ingawa nyaraka hizi zinaweza zisihitajike, lakini unapokuwa nazo unakuwa na utulivu wa nafsi na akili.

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

Friday, December 2, 2016

Anza sasa kujiandaa kuishi bila ajira uzeeni

 

“Wapi unapokwenda?” Peter alipaza sauti kwa mkewe, Maria aliyekuwa akijiandaa kwenda kazini. Ilikuwa siku ya Jumatatu asubuhi Maria alifanya kila kitu kumfanya Peter ajisikie furaha awapo nyumbani peke yake.

Peter alistaafu kazi mwaka mmoja kabla uliopita. Aliamua kustaafu mapema kutokana na maumivu ya mgongo. Miezi 10 tangu astaafu kazi ilikuwa ya furaha kwake. Hakuwa anaamka asubuhi kuwahi kazini na mara kwa mara alitumia muda wake mwingi kukaa nyumbani akiangalia mpira kwenye runinga.

Utaratibu huo wa kupumzika muda mwili ulimsababishia Peter uzembe, ambapo mara nyingi alimshuhudia mkewe akijiandaa kwenda kazini huku nyuma akibaki peke yake.

Kwa upande wake, hali hiyo hatimaye iligeuka karaha hasa alipofikiria mkewe alikuwa na miaka kadhaa ya kuendelea kuwa kazini, jambo ambalo lingewatenganisha muda mwingi wa mchana katika kipindi kirefu cha maisha yao.

Ingawa Peter alikuwa na mawasiliano ya karibu na wafanyakazi wenzake wa zamani, hakuna simu alizokuwa akipigiwa mara kwa mara. Kuna wakati alishangaa kwa nini hakukuwa na yeyote mahali alikofanya kazi miaka mingi aliyekuwa akiukosa uwapo wake na hivyo kumpigia simu kama zamani.

Watu wengi hawapendi kuyaona madhara ya kustaafu mpaka wanapojikuta ndani ya hali hiyo. Ustaafu ni zaidi ya baridi kali ambayo humtenganisha mwajiriwa na taasisi aliyoitumikia.

Ni wazi kwamba, watu hutumia muda mwingi wa maisha yao katika sehemu zao za kazi. Hubuni urafiki fulani sehemu hizo, hupata vyeo, utambulisho na taswira ya kuvutia. Kwa wengi mahali pa kazi huwapatia kila wakitakacho. Pia huwapatia heshima na thamani maishani.

Hiyo ndiyo sababu inayoelezea uhusiano uliopo kati ya sehemu ya kazi na ustaafu pamoja, na madhara ya kisaikolojia anayokumbana nayo mstaafu, jambo ambalo watu wengi hawajiandai mapema kulikabili.

Sababu ya kustaafu au kuacha kazi pamoja na kiwango cha maandalizi baada ya kuondoka kwenye ajira hueleza uchungu anaokuwa nao mstaafu. Hata hivyo, muhimu kwa mwajiriwa ni maandalizi ya kustaafu.

 

Maandalizi kwa ajili ya kustaafu maana yake ni tathmini ya mambo kadhaa maishani - kubwa kuliko yote maandalizi ya kiuchumi (kifedha) kumwezesha mstaafu mtarajiwa kukabiliana na maisha yasiyokuwa na mshahara au posho anazopata kazini ambazo hatazipata.

Pia suala hilo huambatana na mipango ya awali ili hatimaye usiwe tegemezi wa kipato kilichokuwa kinakuja chenyewe kila baada ya kipindi fulani (hasa mshahara au posho).

Kustaafu huibua mambo mengi ambayo hata hivyo unaweza kuyakabili mapema. Chuki ya Peter iliyotokana na kuachwa nyumbani na Maria ilitokana na kutojiandaa mapema, maana aligeuka kuwa ‘mlinzi’ wa nyumba badala ya kuamkia katika kazi zingine binafsi.

Badala yake, licha ya ukweli kwamba alikuwa na tatizo la kiafya ambalo hata hivyo halikutishia maisha yake, alijikuta akishinda nyumbani bila kazi yoyote.

Pia hali ya ‘kutengwa’ kulikotokana na waliokuwa wafanyakazi wenzake ilimuongezea mzigo wa mawazo. Hali hiyo mara nyingi husababisha msongo wa mawazo na iwapo hutachukua hatua za kuikabili mapema inaweza kusababisha madhara zaidi ya kiafya.

Japokuwa katika ustaafu watu wengine huzowea unafuu na uhuru wa kufanya mambo yao zaidi kuliko ilivyo katika fungate la wanandoa, lakini athari zinazotokana na maadalizi duni pamoja na kutojiamini maishani husababisha afya za wastaafu wengi kuzorota baada ya muda mfupi.

Hali hiyo husababishwa mara nyingi na wastaafu hao kutokuwa na kazi nyingine ya kufanya wala mahali pa kujishikiza panapoweza kuifanya akili ifanye kazi ya ziada kuushurutisha mwili ujione uko kazini.

Ndiyo maana wakati huo (kwa wasiojiandaa mapema wawapo kazini) huanza kujiona hawana maana wala utambulisho waliouzowea na kuanza kuhoji uwapo wao duniani.

Hatua hiyo huashiria kwamba watu hao wanapaswa kurejea au kusaka malisho na utambulisho mpya. Kupata ajira na utambulisho mwingine humfanya mtu aondokane na upweke wa kukaa nyumbani akitazama runinga.

Hata hivyo, iwapo umri wake umegota na hawezi kupata kazi kwa urahisi, huo ndio unaweza kuwa mwisho wa kutamba au kuonekana kwa mstaafu.

Tofauti na wanaume, wanawake huweza kutengeneza mzunguko wa uhusiano na utambulisho nje ya kazi, ikiwamo kujiunga katika vyama vya kinamama vya kuendelezana, kusaidiana au urafiki. Uzoefu unaonyesha kwamba hata baada ya ajira, wanawake wanaweza kuendeleza uhusiano huo.

 

Pangilia maisha yako mapema

Hata hivyo lililo dhahiri ni kuwa mipango mizuri ya kustaafu inamtaka mfanyakazi aanze kujipanga na kupangilia maisha ya ustaafu tangu siku yake ya kwanza kazini.

Inashauriwa kwamba unapopata barua ya ajira pangilia pato lako utakavyoligawa kila linapoingia. Fahamu jinsi gani unavyopaswa ‘kusevu’ na kuwekeza ili kujiandalia ajira nyingine baada ya kuondoka kazini.

Watafiti wa mambo ya maisha wanasema kustaafu hakuwahusu wazee pekee, bali hata vijana maana kwa kuwekeza, kujinyima na kuanzisha miradi kunaweza kukufanya ukaachana mapema na ‘utumwa’ wa kuwatumikia watu wengine.

Hiyo ina maana kuwa mipango ya kustaafu ni kufanya maandalizi ya muda mrefu ya kifedha, kiafya na mambo mengine muhimu ya maisha.

Ni vyema ukajua kwamba matumizi yako ya fedha yatakuja kukuweka katika nafasi gani utakapofikia wakati wa kuondoka kazini. Pesa nyingi au chache unazopata wakati huu zitakuja kuamua hatma ya uzee wako iwapo utaishi miaka mingi zaidi (baada ya ajira) ama la.

Mara nyingi rika la ujana huwadanganya watu. Maneno ya “wakati ukifika nitafanya...”, “bado bado nipo” na “ngoja nipate milioni 50 ndipo nianze au niwekeze” huwasumbua na baada ya kujikuta hawana pa kushika, huanza kujuta. Ni vyema ikaeleweka kuwa, kila shilingi moja uipatayo unaweza kuigawa ikaja kukunufaisha zaidi uzeeni.

Ipo hoja nyingine katika maisha ya ustaafu. Hoja hiyo inahusiana na umri, jambo ambalo halikwepeki. Kila mtu umri wake unapofika miaka ya kuondoka kazini kisheria huondoka au kujiondoa katika ajira. Hata hivyo anapokuwa amefanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha hatatetereka huko aendako, anaweza kuishi kama alivyokuwa kazini.

Shirika la Kazi duniani (ILO) liliwahi kupendekeza kwa mataifa wanachama kuwa na ukomo wa umri wa wafanyakazi. Katika mapendekezo hayo, ILO ilizitaka nchi hizo kusimamia matakwa ya ukomo wa ajira kisheria.

Suala hilo liliifanya Serikali ya Tanzania kuridhia na kutunga sheria mbalimbali za kazi, ikiwamo ya Ajira na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004, Sheria ya Taasisi za Usimamizi wa Kazi namba 7 ya mwaka 2004, Sheria ya Afya na Usalama Kazini namba 5 ya mwaka 2003 na Sheria ya Hifadhi za Jamii ya mwaka 2008.

Hata hivyo, changamoto inabaki katika maandalizi ya kustaafu, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watumishi, kwani wengi hawajiandalii mazingira hayo mapema.

Inawezekana uzembe au matanuzi yakawa chanzo, lakini maisha ya baada ya ajira ndiyo ‘yanayomuanika’ mtu anapoondoka kazini. Huu ni wakati wako mfanyakazi kujiandaa kustaafu.

-->