Kampuni za simu zinaleta ushindani wa kweli kwenye sekta ya fedha

Muktasari:

Ubunifu huu umeshuhudia kampuni hizo zikitoa huduma za fedha na kuwa mhimili muhimu kwa baadhi ya watu ambao hawakufikiwa na mfumo rasmi.

Kampuni za simu za mkononi zimekuwa zikikimbizana na mabadiliko ya sanaa za mauzo na masoko kwa kwenda na wakati, hivyo kukidhi mahitaji ya wateja wao kwa ubunifu mzuri ambao umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Ubunifu huu umeshuhudia kampuni hizo zikitoa huduma za fedha na kuwa mhimili muhimu kwa baadhi ya watu ambao hawakufikiwa na mfumo rasmi.

Huduma hizi zinapunguza usumbufu na kuongeza kasi na uhakika wa miamala ya fedha kutoka kwa mawakala waliopo maeneno mengi yenye mzunguko wa biashara.

Wanapatikana sehemu nyingi jambo linalorahisisha malipo ya bidhaa au huduma kutoka kwa wauzaji tofauti bila kupoteza muda mwingi wa mteja.

Kama zilivyo benki za biashara, huduma zinazotumiwa na watu wengi bila kujali kipato ni kuhifadhi, kutuma fedha na kutoa mikopo. Kampuni za simu nazo zinafanya haya yote.

Wananchi wengi wanajumuishwa kwenye huduma za fedha wakiwa na fursa zote wanazozihitaji kwa miamala midogo inayokidhi mahitaji ya kila siku.

Mwanzoni tuliona kampuni za simu zikifanya huduma kuu za kuhifadhi na kutuma fedha, walidumu kwenye huduma hizi kwa muda mrefu sana na kuwafikia watu wengi mpaka vijijini na kutoa nafasi za ajira kwa vijana wengi pia kuingia kwenye shughuli za uwakala.

Tayari kampuni hizi zimeingia kwenye huduma kuu za fedha ambazo taasisi za fedha zinafanya, mfano zinatunza fedha na kutoa gawio kutokana na riba ya utunzaji na kuhamasisha wengi.

Lakini, huduma hizo zinafika maeneo ambayo miundombinu ya fedha bado ni michanga au hakuna kabisa, hivyo kujitengenezea mizizi ya kuendelea kutawala kwa muda mrefu ujao.

Jambo la msingi, ni uwezo wa kutoa mkopo wa fedha taslimu kwa mteja na kuzilipa kidogo kidogo. Kwa hakika, huu ni ushindani mkubwa na endelevu kwa taasisi za fedha kwa sababu bado miundombinu ya kufikisha huduma zao vijijini ni mdogo.

Mbali na hilo, taasisi hizi zimejikita kwenye kuwahudumia wateja wenye dhamana hasa kwa mikopo hivyo kuwatenga wasio na kipato ambao ndiyo wengi nchini.

Licha ya benki za biashara kuanzisha utaratibu wa kuwa na mawakala maeneo ya nje ya mji, bado hazina wigo mbana kama ilivyo kwa huduma za simu za mkononi ambazo wengi wanazitegemea.

Kwa tafsiri rahisi kampuni za simu zina watu makini, wabobezi, wazoefu, wenye ubunifu mkubwa kwenye masuala ya fedha na mipango ya kubuni na kusimamia bidhaa na huduma za fedha.

Zikitumika vizuri zitasaidia watu wenye kipato cha chini kupata mikopo midogo, kuhifadhi na kutuma fedha ambayo ni aina ya huduma yenye thamani kwa jamii ya Watanzania wengi.

Ushindani huu unaleta faida kubwa kwa mlaji au mtumiaji, jambo la msingi ni kuendeleza teknolojia hii ya uwekezaji hasa kwa jamii za vijijini ili kuongeza tija.

Kampuni za simu zinaweza kuwa na wataalamu wa fedha kwenye eneo hili la microfinance, ambao watakuwapo kwenye vituo vyao vya huduma vya mikoa ili kuwa karibu na wateja wao.

Uwepo wa wataalamu hawa utatoa nafasi kwa wateja kupata elimu ya fedha, uwekezaji na ujasiriamali wenye tija na kuisogeza kampuni husika karibu na jamii hivyo kutengeneza faida huku ikihamasisha watu kufanya kazi na kukuza uchumi binafsi na pato la taifa.

Uwepo wa mikopo midogo kutoka kampuni hizi ni fursa ya kipekee kwa wateja wenye biashara ndogo kukuza mitaji na kupanua biashara zao. Wateja hawa wanapaswa kutumia huduma hizi vizuri wakikopa na kuwekeza maeneo stahiki ili kuepuka hasara na matumizi mabaya ya fedha.

Kubwa na muhimu zaidi ni ulipaji wa uhakika wa mikopo ili huduma iendelee kukua na kuwafikia na kuwanufaisha watu wengi zaidi.

Wakati taasisi za fedha zikijielekeza kwa wateja wakubwa, wenye dhamana za kutosha kukopesheka, kampuni za simu ni vema zikajielekeza kwa watu wa chini.

Zitoe mikopo midogo ya kuanzia Sh100,000 au Sh500,000 mpaka milioni moja kwa wateja wanaochukua na kulipa vizuri. Hii itawasaidia kupata wateja wengi zaidi watakaokuza mzunguko wa mtaji na kuleta faida kubwa.

Zikifanya hivyo, zitakuwa nguzo imara ya fedha kwa wananchi na kujitengenezea nafasi kuendelea kuwapo kwenye soko la huduma za fedha kwa teknolojia ya kisasa isiyo na urasimu kwa mteja.

Ili ziendelee kudumu sokoni, benki za biashara zinatakiwa kubuni njia itakayowavutia wateja kufuata huduma na bidhaa zao. Huduma hizo hazina budi kutolewa kwa teknolojia rafiki na rahisi.

Tuwasiliane: 0657 157 122