SAIKOLOJIA : Fahamu jinsi ya kuwafundisha watoto thamani ya fedha

Muktasari:

  • Lakini baada ya muda mfupi huwa anaviharibu au kuvipoteza. Mama yake husema, “Mwanangu usijali, nitakununulia vingine.” Kweli humnunulia vingine lakini kuwa hajirekebishi. Mara tu huviharibu au kuvipoteza vile vipya na hununuliwa tena.

Jirani na ninakoishi kuna familia yenye mtoto wa miaka nane anayependwa na wazazi wake. Hawa wanamnunulia vitu vya shule kama mkebe wa vifaa vya hesabu, chupa ya juisi na vinginevyo.

Lakini baada ya muda mfupi huwa anaviharibu au kuvipoteza. Mama yake husema, “Mwanangu usijali, nitakununulia vingine.” Kweli humnunulia vingine lakini kuwa hajirekebishi. Mara tu huviharibu au kuvipoteza vile vipya na hununuliwa tena.

Jirani zetu wengine pia wana binti kama yule wa kwanza. Yeye hupewa fedha kidogo tu anapokwenda shule. Ingawa ni pesa kidogo kila siku anabakiza chache na kuweka akiba. Alimuomba mama yake amtengenezee kisanduku kidogo cha kutumbukiza akiba yake kila siku. Baada ya ya muda huchukua fedha hizo na kununua vitu anavyohitaji ambavyo wazazi wake hawajamnunulia kama vile saa ya mkononi, kikokoteo na vinginevyo . Baada ya hapo huanza tena kuweka akiba.

Nilipokuwa kazini kuna wakati tuliajiri vijana waliomaliza sekondari moja kwa moja. Wengine walipopokea mshahara mara ya kwanza walifika nyumbani ukiwa umebaki nusu. Njiani walinunua vitu vidogo walivyotamani kama vile biskuti na chokoleti. Wengine walinunua viatu vya raba ghali na mafulana ya bei mbaya yenye picha, marembo na maandishi.

Kuna mmoja alikuwa akitumia mshahara wake na kuumaliza baada ya siku chache kutokana na matumizi mabaya, Mwezi uliofuata aliishi kwa kukopa kwa wafanyakazi wenzake ili kupata hata nauli ya kwenda kazini. Mwisho wa mwezi ulipofika alipojipanga kupokea mashahara ulikuwa ukiishia pale pale kwa kulipa madeni.

Kutokana na visa hivi inafaa tujiulize tunawezaje kuwafundisha watoto wetu maana na thamani ya fedha. Tunaweza kufanya hivyo kwa kuwaweka katika mazingira ya kuwafahamisha fedha ni kitu gani na kuwaelekeza kwa maneno na vitendo jinsi fedha zinavyopatikana na zinavyofanya kazi.

Hawana budi kutambua kuwa inabidi watumie fedha kwa makini, busara na uangalifu kwa kuwa huwa hazipatikani kwa urahisi. Tukifanya hivyo tutawajengea uelewa utakaowasaidia kuyamudu maisha ya sasa yenye uchumi mgumu. Zifuatazo ni njia zinazoweza kutusaidia kuwafundisha:-

•Kuwazoesha kuweka akiba

Ni muhimu kuwafundisha watoto tangu wakiwa wadogo, umuhimu wa kuweka akiba ya fedha. Huko Ulaya kuna vitu vya aina mbalimbali vinavyotengenezwa maalumu kwa ajili ya watoto kutumbukiza sarafu za fedha kila mara. Baada ya muda kitu hicho hufunguliwa kuona zimepatikana fedha kiasi gani. Inafaa kuwazoesha watoto kufanya hivyo na wanapopata umri wa kuanzia miaka minane kuwafungulia akaunti ya akiba katika benki na kuwafahamisha kuwa wana akaunti hiyo.

•Kuwapatia posho

Wazoeshe watoto wako kuwapatia posho ya fedha wanapokwenda shuleni au hata wakati wa sikukuu. Kiwango cha posho kitategemea umri wa mtoto. Mtindo huu huwawezesha watoto kuwa na fedha zao kwa ajili ya matumizi yao wao wenyewe.

Aidha, huwawezesha kupata zoezi la kushika pesa, kutambua thamani yake na kuamua jinsi ya kuzitumia kufuatana na mahitaji. Tena huwasaidia kujua namna ya kupiga hesabu za fedha.

•Kutotumia fedha kama hongo Kuna wazazi wamezoea kutumia fedha kama kichocheo cha kuwahamasisha watoto kufanya kazi za nyumbani kwa mfano mzazi anamwamba mtoto kuwa akisafisha chumba chake vizuri atampa fedha. Tabia hii siyo nzuri kwa sababu huwafanya watoto wapate mawazo kuwa kazi zote nzuri anazofanya mtu ni lazima alipwe fedha hata kama ni wajibu wake.

Kuna wazazi ambao huwapa fedha watoto kwa kuwaamkia wakubwa au kuwapenda wadogo zao na kuwatendea mema. Wakati mwingine mzazi mmoja humwongezea mtoto pesa za shule na kumwambia asimwambie baba au mama.

Hapa mzazi huwa anajaribu kununua upendo kwa mtoto kwa kutumia fedha. Jambo hili ni baya sana kwa sababu huweza kusababisha mfarakano katika familia, baina ya mzazi mmoja na mwingine, kati ya wazazi na watoto na hata watoto kwa watoto.

Kanuni hii haizuii kuwapongeza watoto wanapofanya mambo mazuri ila inazuia kufanya hivyo kwa kutumia fedha. Wanaweza kupongezwa kwa kupewa zawadi mbalimbali hata kuwapeleka kutembelea sehemu wanazozitamani sana. Aidha, ni vibaya kutumia fedha kama adhabu kama vile mtoto asipotimiza jambo fulani, kumnyima fedha ya kwenda nayo shule. Jambo hili humdhalilisha mtoto wa wakati mwingine kumfanya aibe au kurubuniwa kwa urahisi na watu wabaya kwa kutumia pesa.

•Kutowaficha bajeti ya familia

Wazazi wengine huwa hawapendi kuwafahamisha watoto bajeti ya familia kwa sababu mbalimbali. Baadhi ya wazazi huhofu kuwa watoto wanaweza kutoa siri za familia nje wengine huogopa kuwa watoto wanaweza kuwachagiza kwa kutaka watekelezewe mambo yao ya ujana ambayo pengine huwa hayana maana. Lakini wazazi wakianza mapema kuwashirikisha watoto wao wala hawatapata hayo mawazo potovu. Kutowashirikisha watoto katika matumizi ya familia huweza kuwafanya wastahamili hali inapokuwa ngumu.

Wanapopata umri mkubwa kidogo ni vyema hata kuwashirikisha katika kupanga bajeti ya familia. Hatua hii haitawapatia tu stadi za kuandaa bajeti bali inaweza kuwafanya wafikirie wao wataweza kuchangia vipi katika kupambana na makali ya maisha.

•Kuwafahamisha watoto kazi zao

Watoto wanapoanza kuelewa mambo mbalimbali ni muhimu wazazi wawafahamishe kazi wanazofanya zinazowaingizia kipato wanachotumia kwa kuindesha familia. Watakapoelewa kazi ya baba na ya mama wataweza kuelewa uhusiano uliopo kati ya kazi na mapato.