UCHAMBUZI: Kuanzisha soko ndani ya kituo cha mabasi siyo busara

Muktasari:

Hata kwenye vituo vya mabasi vya vijijini wapo wachuuzi wa vyakula na matunda ambao wanahangaika kuwauzia abiria mara gari linaposimama, lakini likiondoka wanakaa pembeni.

Kwa miaka mingi wachuuzi na wamachinga wameonekana wakiuza bidhaa zao kwenye vituo vya mabasi. Ni kawaida kuwaona wauzaji wa bidhaa za vinywaji baridi kama soda, maji na hata biskuti wakiyakimbilia magari kuuza bidhaa zao katika vituo vingi nchini.

Hata kwenye vituo vya mabasi vya vijijini wapo wachuuzi wa vyakula na matunda ambao wanahangaika kuwauzia abiria mara gari linaposimama, lakini likiondoka wanakaa pembeni.

Kwa Jiji la Mbeya mambo hayo sasa yameingia katika hatua mpya baada ya kuwarasimisha wachuuzi hao na kuwataka kuanzisha soko ndani ya kituo cha daladala cha Kabwe.

Wachuuzi waliokuwa wakipanga bidhaa zao pembeni mwa kituo hicho sasa wamerasimishwa baada ya kuwawekea utaratibu wa kutengeneza meza za kupanga bidhaa zao na kuuza ndani ya kituo hicho.

Tayari wafanyabiashara karibu 400 wametengenezewa meza na kupewa nafasi ndani ya kituo hicho ambacho ni cha tatu kwa ukubwa katika Jiji la Mbeya baada ya stendi kuu na kile cha Nanenane.

Kabwe ndicho kituo kikuu cha daladala nyingi zinazotoka miji midogo ya Mbalizi, Igawilo Uyole, Ituha pia kinapitiwa na daladala zote zinazosafiri jijini hapa kwenda katika vituo mbalimbali.

Hivi sasa abiria wakiteremka kwenye kituo hicho wanakumbana na meza zenye bidhaa mbalimbali za vyakula hususani matunda, mbogamboga, viazi mchele, samaki wa kukaanga na mitumba huku mamalishe nao wakijinafasi kutembeleza chai kwa makande, mihogo ya kuchemsha, vitumbua na vingine vingi.

Ukiwa eneo hilo, licha ya kuona vyakula hivyo, pia pua yako haitakosa harufu ya moshi wa daladala huku macho yakiangalia wapigadebe wanavyokunywa pombe kali za kwenye viroba mchana kweupe.

Kwa ujumla jambo hili linachekesha na kusikitisha kwa watu wastaarabu ingawa kwa wanasiasa linaonekana kama ni la kawaida.

Siyo kawaida vituo vya mabasi kuchanganywa na masoko kwani maeneo hayo yanatajwa kuwa yenye hatari kwa sababu ya uchafu wa kila aina.

Hali kadhalika haijawahi kutokea duniani soko likachanganyikana na kituo cha mabasi kwani ni hatari kwa wafanyabiashara gari linapokosa mwelekeo. Bila shaka ni hapa Mbeya pekee.

Mkurugenzi wa jiji, Nachoa Zakaria alipoulizwa kuhusu mchanganyiko huo anasema wanasiasa wameamua soko liwepo ndani ya kituo cha mabasi.

Zakaria anasema utaratibu huo unamkera zaidi kutokana na ukweli kwamba jiji lilikuwa na mpango wa kuwaondoa wachuuzi hao na kuwapeleka kwenye masoko ya Sido, Mwanjelwa na Nanenane ambako zaidi ya nafasi 700 zilipatikana.

Kibaya zaidi ni kwamba kituo cha Kabwe kipo mbele ya maduka mengi ambayo nyuma yake lipo soko kuu la Sido lenye wafanyabiashara zaidi ya 1,000 ambao wanauza bidhaa kwenye meza katika kituo cha mabasi.

Kwa ujumla watendaji wa jiji wamekata tamaa kwa uamuzi wa wanasiasa kuhusu mipango ya kuwasaidia wamachinga.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Mwanjelwa hivi karibuni alisisitiza kwamba anatekeleza maombi ya wafanyabiashara.

Anasema walimuomba wamachinga waingie ndani ya soko la Mwanjelwa, ndipo alipowaruhusu. Kwa maoni yangu ni mkanganyiko mkubwa kituo cha mabasi kutumika pia kama soko.

Lauden Mwambona anapatikana kwa barua pepe:[email protected] na simu namba 0784 338897