Kilichotokea baada ya kufutwa Uchaguzi Mkuu Zanzibar kimerekebishwa?

Muktasari:

  • Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulifanyika kwa njia ya amani kuliko hata ule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania bara ambapo kuna maeneo kadhaa Jeshi la Polisi lililazimika kufyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi kutuliza ghasia jambo ambalo halikujitokeza sehemu yoyote Zanzibar.

Siku mbili zimebaki kutimiza mwaka mmoja  tangu Zanzibar ilipojiwekea historia ulimwenguni ya kuufuta Uchaguzi Mkuu kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na tume iliyosimamia uchaguzi huo.

Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 na siku moja baadaye, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salim Jecha Salim aliwatangazia waandishi wa habari kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Mbali na Jecha waangalizi wa ndani na wa kimataifa wote walieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na ulifanyika kwa njia ya amani katika utulivu bila mikwaruzo yoyote.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulifanyika kwa njia ya amani kuliko hata ule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania bara ambapo kuna maeneo kadhaa Jeshi la Polisi lililazimika kufyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi kutuliza ghasia jambo ambalo halikujitokeza sehemu yoyote Zanzibar.

 Mwafaka uliofikiwa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ndiyo sababu inayotajwa kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufanyika kwa amani na utulivu.

Muafaka huo ulisababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar iliyoongozwa na CCM na CUF kwa miaka mitano. Ushirikiano huo ulijenga mazingira mazuri kwa wananchi kuishi kwa umoja na amani.

Hata hivyo, Oktoba 28, 2015 wakati ZEC ikiwendelea kutaja matokeo ya kura wa wagombea kutoka majimbo mbalimbali, ghafla Jecha alionekana kwenye Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) akitangaza kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

Kwa bahati mbaya Jecha hakufuta Uchaguzi Mkuu wa rais pekee, badala yake aliyafuta matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

Wakati tangazo la kufutwa kwa matokeo linatolewa, washindi wa baadhi ya washindi wa viti vya wajumbe na Baraza la Wawakilishi na madiwani walishatangazwa na kukabidhiwa vyeti vyao na wasimamizi wa uchaguzi wa maeneo husika hatua ambayo hakuna mtu yeyote wala taasisi inayoweza kuhoji matokeo hayo isipokuwa mahakama.

Uhasama waibuka upya

Hatua hiyo ya Jecha iliibua upya uhasama kati ya wafuasi wa CCM na CUF ambao kwa mara ya kwanza ulianza baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, lakini ulikoma baada ya kufikiwa muafaka kati ya vyama hivyo mwaka 2009.

Kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu kuliko sababisha kufanyika uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu ambao ulisusiwa na CUF, mbali na kuua muafaka na Serikali ya Umoja wa Kitaifa umezua uhasama baina ya wananchi ambao wamefikia hatua ya kutokushirikiana hata katika shughuli za kijamii kutokana na itikadi za kisiasa.

Tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio mambo mengi yasiyofaa yamefanyika katika visiwa vya Unguja na Pemba huku viongozi na wanasiasa wakiwa hawachukui hatua madhubuti za kuyazuia.

Ni vigumu nchi kupiga hatua ya kimaendeleo iwapo hakuna maelewano kati ya wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa katika juhudi za kuiletea nchi yao maendeleo.

Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wakati ikiwa chini ya utawala wa SUK wananchi wake walikuwa wanashirikiana katika kila jambo na waliweka pembeni tofauti zao kisiasa.

Hata hivyo, kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu na kufanyika uchaguzi wa marudio kumeondoa sifa hizo pamoja na kuwapo kwa viongozi ambao wanadai Jecha anastahili kupongezwa na kupewa tuzo.

Kutokana na madhara ambayo yameikumba Zanzibar baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu na kufanyika uchaguzi wa marudio, itachukua muda mrefu kwa wananchi kumaliza tofauti zao iwapo viongozi hawatazimaliza kwa njia ya maridhiano.

Ni dhahiri kwamba wananchi ambao wamekumbwa na kadhia ya kususiwa maiti zao kuzikwa, kuharibiwa mashamba yao au kuchomewa moto nyumba zao kutokana na tofauti za kisiasa zilizoibuka baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu itawachukua muda mrefu zaidi kulisahau tukio hilo.

Mbali na hayo kuna wananchi kadhaa ambao wamepigwa na kundi la vijana lililojiita mazombi na wengine kukamatwa na kuadhibiwa na vyombo vya dola.

Hayo yote yanayotokea kutokana na kufa kwa muafaka wa CCM na CUF na kuvunjika kwa SUK ambao vyote viwili vilileta matumaini mapya Zanzibar na kama mipango ingekuwa mizuri Zanzibar ingepiga hatua kubwa ya maendeleo.

Iwapo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ingekuwapo mpaka hivi sasa, visiwa vya Zanzibar vingekuwa na maendeleo zaidi kama nchi ya Dubai kwa mujibu wa ahadi iliyokuwa imetolewa na Rais Ali Mohamed Shein kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Au visiwa hivyo vingekuwa kama Singapore kutokana na ahadi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar.

Kwa hali ilivyo sasa ni vigumu maendeleo ya kweli, maridhiano, amani na utulivu kupatikana Zanzibar katika mfumo wa utawala wa chama kimoja kinachopingwa na vyama vingine.

Uchaguzi Mkuu mwaka 1995

Ukiangalia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kuanzia ule wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995 ulikuwa na mvutano na upinzani mkali ambapo matokeo yaliyotangazwa na ZEC yalionyesha kuwa Dk Salmin Amour Juma wa CCM alimshinda Maalim Seif wa CUF kwa tofauti ya asilimia 0.4.

Kabla ya matokeo hayo kutangazwa baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza kuwa Maalim Seif ameshinda na hata aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohammed alitangaza hadharani kuwa hawaafiki matokeo ya uchaguzi huo.

Baada ya matokeo hayo Zanzibar iliingia katika uhasama mkubwa kati ya wafuasi wa CCM na CUF na vitendo kadhaa vya uvunjifu wa amani vya ukandamizaji wananchi viliibuka.

Njia za kurudisha umoja

Kuna baadhi ya watu wanadai kwamba baada ya uchaguzi wa marudio, Zanzibar inapaswa kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka huu, idadi ndogo ya watu walijitokeza kupiga kura. Hali hiyo ilisababishwa na uamuzi wa vyama vya siasa 14 kukataa kushiriki.

 Hata jumuiya ya kimataifa imetamka bayana kwamba haiutambui uchaguzi huo kwa vile haukuwa shirikishi na ulifanyika bila ya kuwapo maridhiano kati ya vyama vyote vya siasa vilivyotakiwa kushiriki.

Kuna njia mbili kuu ambazo zinaweza kutumika kurudisha umoja, amani na utulivu Zanzibar na kuwapa nafasi wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kujitafutia riziki zao na huku Serikali ikiwa katika fursa nzuri za kuleta kusimamia suala hilo.

Moja ya njia hizo ni kuundwa kwa serikali ya mpito itakayoongozwa na vyama vyote vya siasa chini ya CCM na CUF kwa miezi mitatu au miezi sita ili kujenga mazingira ya kufanya Uchaguzi Mkuu ambao utasimamiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Uchaguzi huo unaweza kusimamiwa na Umoja wa Kimataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU)  au kwa vyote kushirikiana katika kusimamia uchaguzi wa Zanzibar ili matokeo yake yakubalike kwa pande zote.

Njia nyingine ni kurudi kwenye kiti cha kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kumalizia pale ulipofikia kwa kumtangaza mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar na kuyarudisha matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika majimbo yote na madiwani.

Mwandishi ni mwanahabari mwandamizi na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]