Thursday, January 12, 2017

TAFAKURI YA ABU IDD: CCM inahitaji kura za Kagera 2020?

 

By Abuu Iddi,Mwananchi

Watanzania wenzetu wa Mkoa wa Kagera wamekumbwa na tetemeko la ardhi liliowaletea madhara makubwa, ikiwamo baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha, uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu na kadhalika.

Viongozi kadhaa wa Serikali pamoja na wa vyama vya siasa walijitokeza kuwafariji waathirika hao pamoja na kuwapa misaada ya awali. Hata baadhi ya nchi na asasi za kiraia ‘zilikunjua mikono yake’ ili kuwafariji wana Kagera.

Pamoja na yote hayo, Watanzania tulisubiri kwa hamu kubwa ziara ya Kiongozi wetu Mkuu wa nchi, Rais John Magufuli, katika mkoa huo kwani kwa sasa ndiye ‘Baba’ wa Watanzania wote bila ya kujali dini zao, rangi zao, makabila yao, kanda zao na itikadi zao za kisiasa.

Hatimaye Rais Magufuli alifika mkoani Kagera na kutembelea baadhi ya sehemu zilizokumbwa na tetemeko hilo pamoja na kuzungumza na baadhi ya waathirika. Kwa bahati mbaya, matarajio ya Watanzania na haswa wana Kagera kutoka kwa Rais Magufuli hayakupatikana na kibaya zaidi wameongezewa uchungu juu ya uchungu walio nao.

Baadhi ya lugha zilizotamkwa katika kuwasilisha msimamo wa Serikali kwa wana Kagera zimekosa hekima, busara na huruma kwa waathirika wale. Ni ukweli ulio wazi na usiohitaji kufikiri kwamba wana Kagera wamejawa na huzuni, hasira na mshangao mkubwa kutokana na kauli hizo.

Jambo muhimu la kujiuliza ni; Je, ni nini kimejificha katika nyoyo za wana Kagera baada ya majumuisho ya yote yaliyotokea? Jawabu la swali hili tuliache kwa wana Kagera wenyewe.

Kuhusu tafakuri yetu ya leo yenye swali linalouliza juu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuzihitaji kura za wana Kagera katika chaguzi zijazo, msingi wake ni kwamba CCM ni chama cha siasa ambacho kwa sasa ndicho kinachoongoza nchi. Hivyo, kinapaswa kutafakari kuanzia sasa ni nguvu ipi kwao itawapa ushindi na ni udhaifu upi kwao ni kikwazo cha ushindi katika chaguzi zijazo.

Yapo maeneo kadhaa CCM inatakiwa ijitafakari na kujiuliza yenyewe na hatimaye kupata majibu kabla ya wakati wa chama hicho kufikiriwa na wananchi haujafika. CCM inatakiwa kutafakari ni maeneo yapi inachukiwa na nini kilichopelekea kuchukiwa huko na ni maeneo yapi inapendwa na nini kilichopelekea kupendwa huko.

Matayarisho ya ushindi wa CCM yanatakiwa yazingatie msemo mashuhuri usemao “Kanzu ya Ijumaa huandaliwa Alhamisi”. Kwa kura za wana Kagera, CCM ijiweke wazi mapema kama wanazihitaji na wasitamke tu kuzihitaji bali waonyeshe kwa vitendo kama ni kweli wanazihitaji kura hizo.

Kama CCM wametafakari na wakaona kwa dhati kwamba wanazihitaji kura za wana Kagera wafanye mambo yafuatayo:

Waiombe Serikali itoe tamko kuielezea kadhia nzima ya Kagera lililosheheni lugha zilizopoa na zenye staha zinazoonyesha huruma na kuguswa kwa yaliyowatokea wana Kagera.

Wawaombe wana Kagera kufuta maumivu yaliyosababishwa na lugha zilizopoteza mwelekeo katika nyoyo zao na wazichukulie lugha hizo kama matokeo ya ‘kuteleza’ kwa ulimi kwani Waswahili wanasema: “ulimi hauna mfupa”.

Waiombe Serikali inayoongozwa na chama chao ibatilishe kauli yake kwa wana Kagera juu ya kutokuwajengea waathirika na kuwataka wajenge wenyewe nyumba zao na ifanye kila juhudi iliyo ndani ya uwezo wake kuwasaidia kufanikisha kupata makazi mapya.

Ukweli ni kwamba wachangiaji wengi wa kitaifa na kimataifa wameguswa na maisha binafsi ya waathirika wa tetemeko la ardhi Kagera na ndipo wakapata msukumo wa kuchangia na hata kauli zao zilionyesha kusikitishwa na madhara ya kuharibika kwa makazi ya baadhi ya wana Kagera.

Serikali inapaswa kurejesha miundombinu ya barabara, shule, hospitali na ofisi za umma kupitia mifuko yake ya maafa na kodi za Watanzania haswa ikizingatiwa kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli imefanya vyema katika kukusanya kodi pengine kuliko awamu zote zilizopita.

Fedha zilizochangwa na Serikali za mataifa mbalimbali, mashirika binafsi ya ndani na nje ya nchi pamoja na watu binafsi kama msaada kutokana na maafa hayo ya tetemeko la ardhi Kagera ziwaendee walengwa kwa kuzingatia viwango vya athari zao.

Serikali itamke wazi kwamba katika majanga yote yaliyoorodheshwa kutokea mkoani Kagera, hayakutokea kwa matakwa wala uzembe wa wana Kagera bali ni mapenzi ya Mola Muumba ambaye amewapa mitihani hiyo mikubwa waja wake. Hivyo si vyema kwa kiongozi wa Serikali au chama kuyatumia matukio hayo (ambayo wana Kagera wanayakumbuka kwa huzuni) kama ‘fimbo’ ya kuwakejeli wana Kagera.

Nihitimishe tafakuri ya wiki hii kwa kuwakumbusha wanaCCM kwamba CCM ni mali ya wanachama hivyo wao kama wenye chama chao wanapoyaona mazingira ya kutengenezewa udhaifu ili chama kikiingia kwenye ushindani kishindwe, wanapaswa kusimama na kuirekebisha hali hiyo ili chama kibakie katika nguvu yake ya asili na viongozi wawe ‘wasikivu’ kupokea marekebisho hayo.

Ni vyema CCM ikajifunza kupitia vyama viwili vilivyokuwa maarufu katika nchi jirani ambavyo baada ya kupoteza ‘mvuto’ vilikataliwa na wapigakura na sasa vimekuwa vyama vya upinzani na si tawala tena. Hivyo si vyema CCM ikajiona kwamba ‘haikataliki’.

Aidha, CCM inapaswa kutafakari mara kwa mara juu ya tofauti ya kura milioni mbili zilizokiwezesha chama hicho kushinda kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2015 kama ishara ya ‘taa ya njano’ inayotoa taarifa kwamba chama kimepoteza mvuto kwa kiasi kikubwa.

CCM inazihitaji kura za Kagera katika uchaguzi ujao? Haya na tutafakari.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.

-->