Falsafa ya Msigwa ilivyochochea ukuaji wa maendeleo Iringa Mjini

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa. Picha na Said Ng'amilo

Muktasari:

Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka juzi, Chadema ilifanikiwa kuzoa viti vingi vya udiwani vilivyowawezesha kuongoza baraza la madiwani wa manispaa hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vyama vingi nchini.

Iringa Mjini ni kati ya majimbo yenye mvutano mkubwa wa kisiasa hasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka juzi, Chadema ilifanikiwa kuzoa viti vingi vya udiwani vilivyowawezesha kuongoza baraza la madiwani wa manispaa hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vyama vingi nchini.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anasema mvutano mkali wa kisiasa kwenye jimbo hilo siyo changamoto, isipokuwa ni fursa ya kukifanya chama chake kiendelee kuongoza.

Mchungaji huyo anasema jukumu kubwa walilonalo ni kutekeleza ahadi walizotoa kwenye kampeni ya mwaka juzi kwa vitendo na kwamba kazi kubwa kwao ni kuwafundisha wananchi kuvua samaki na siyo kuwapatia samaki waliovuliwa.

Yafuatayo ni mahojiano yaliyofanywa baina ya Msigwa na mwandishi wetu kuhusu hali ya kisiasa nchini na namna alivyoweza kutekeleza ahadi zake jimboni humo.

Mwandishi: Unauonaje mwelekeo wa siasa za Tanzania kwa sasa hivi?

Msigwa: Mwelekeo wa siasa za nchi yetu hivi sasa hasa kwa uongozi uliopo madarakani ni wa kudumaza demokrasia.

Kwa kifupi siasa zetu zinarudi nyuma badala ya kwenda mbele, hatuna demokrasia.

Mwandishi: Mambo gani ambayo Rais Magufuli anayafanya yanakufurahisha?

Msigwa: Jambo moja linalonifurahisha ni hatua yake ya kurejesha nidhamu kazini, pia namna alivyoweza kupambana na walarushwa na anavyoonyesha nia ya kuhamasisha watu kuipenda Tanzania, mambo haya yanafurahisha.

Mwandishi: Ni mambo gani usiyoyapenda kutoka kwa JPM na Serikali kwa ujumla?

Msigwa: Jambo la kwanza nisilopenda ni kukosekana kwa kauli za faraja. Rais anatakiwa kukemea lakini pia asikike akitoa kauli za faraja kwa wananchi.

Uongozi ni kuonyesha njia siyo amri. Nchi hii ni ya Watanzania na huwezi kuongoza nchi kwa amri.

Kitu nisichopenda katika Serikali hii ni kutoa takwimu za kuwaridhisha watu. Napenda waseme ukweli kama kweli tunataka kuendelea ili kama hali mbaya isemwe hivyo hivyo kama ilivyo.

Mwandishi: Nini maoni yako kuhusu kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa ya nje kwa vyama vya siasa?

Msigwa: Inaonekana wazi vyama vya upinzani tunaogopwa ndiyo maana mikutano imezuiwa. Hivi sasa tunashindwa kufanya kazi za mikutano kwa sababu ni kinyume cha sheria, lakini jambo hili halitazuia sisi kuendelea kufanya kazi zetu za kisiasa.

Mwandishi: Unatabiri nini kuhusu mwelekeo wa vikao vya Bunge mwaka huu?

Msigwa: Kwanza Bunge la bajeti la safari hii litakuwa gumu kwa Serikali na itakuwa na wakati mgumu. Hata wabunge wa CCM watasumbua kwa kuwa bajeti haijatekelezeka na haiwezi kutekelezeka.

Mwandishi: Unadhani kuzuiwa kwa Bunge ‘live’ kumeathiri?

Msigwa: Kuzuiwa kwa matangazo ya ‘live’ kumelifanya Bunge kukosa meno, wabunge wangependa kuona wananchi wawe wanasikia, kuona na kujua kinachoendelea bungeni.

Mwandishi: Ni kazi zipi umezifanya kwenye jimbo lako mpaka sasa?

Msigwa: Mtu yeyote mwenye akili timamu anaweza kuyaona mabadiliko makubwa kwenye Jimbo la Iringa Mjini tangu nilipoingia madarakani hadi hivi sasa tunapozungumza. Wakati naingia bungeni kwa mara ya kwanza tulikuwa na matatizo mengi kwenye manispaa yetu ikiwa pamoja na uhaba wa maji hasa katika maeneo ya Nduli, Kigonzile, Isakalilo na kwingineko.

Hakukuwa na barabara za lami za kutosha, pia hatukuwa na hospitali ya wilaya hivyo watu walitegemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kupata matibabu.

Hivi sasa Jimbo la Iringa Mjini limekuwa moja kati ya majimbo machache nchini yenye uhakika wa maji. Asilimia 95 ya wakazi wa jimbo langu wana uhakika wa maji safi na salama, jambo hili kwangu ni mafanikio makubwa. Pia, tumefanikiwa kujenga hospitali ya wilaya katika eneo la Frelimo na imeshaanza huduma kwa wananchi, hivyo hatutegemei hospitali ya rufaa peke yake. Eneo ilikojengwa hospitali ya manispaa hakukuwa na barabara, lakini hivi sasa barabara ya lami inajengwa.

Mji wa Iringa ni msafi na umepangika vizuri na kikubwa zaidi mara kadhaa tumekuwa tukipata tuzo za usafi na hilo linaonekana kwa macho kwani watu wanaoingia na kutoka wanaushangaa na kuupongeza kwa mpangilio wake na hata usafi.

Tumefanikiwa kujenga machinjio ya kisasa ambayo siku siyo nyingi yataanza kufanya kazi vizuri. Nimeweza kushiriki shughuli nyingi za kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu.

Mwaka jana nilikabidhi madawati 537 ili kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya kusoma katika mrundikano mkubwa na baadhi yao walikuwa wanakaa sakafuni.

Sipendi kuona wanafunzi wanaosoma katika shule za jimbo langu wanakaa chini, kitendo hiki huwa kinaniumiza ndiyo maana nimeamua kupambana kutafuta madawati ili kufanikisha azima yangu ya kukuza elimu kwa wanafunzi wa Jimbo la Iringa Mjini.

Tumeweza kuongeza vyumba vya madarasa, vituo vya afya na miundombinu imara. Kwa kifupi ni kwamba maendeleo Iringa yanakua kwa kasi kubwa. Jambo zuri zaidi ni kuwa wananchi wa Iringa wanaelewa nini maana ya maendeleo na wanashiriki kwa vitendo katika kupambana na umaskini. Hivi sasa tunaendelea na ujenzi wa Daraja la Igumbilo sehemu ambayo watu hasa watoto walikuwa wakifa kwa kusombwa na maji kwa sababu ya kukosa daraja. Haya ni mafanikio makubwa kwetu.

Tunaanza ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi Igumbilo ambacho kukamilika kwake kutasaidia kuinua uchumi wa jimbo langu.

Kifupi ni kwamba zipo kazi nyingi kama mbunge nimezifanya Iringa na sitaacha kukiri kwamba, mji huu uliojaa watu wengi umebadilika kwenye kila sekta.

Mwandishi: Changamoto zipi unakutana nazo kwenye utekelezaji wa majukumu yako?

Msigwa: Zipo changamoto nyingi lakini kwa kifupi ni namna fedha za maendeleo zinavyoshindwa kufika kwa wakati kwenye manispaa yangu. Tunahangaika kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kutekeleza kazi za maendeleo kwa wananchi. Changamoto hizi nyingine za kisiasa ni nyepesi na hazikatishi tamaa kwa sababu tumeshazizoea.

Mwandishi: Unaonaje mwelekeo wa hali ya uchumi wa nchi kwa miaka mitano ijayo?

Msigwa: Mpaka sasa tunavyoongea hali inaonyesha kuwa kuna hali ngumu ya kiuchumi japo kitakwimu hali inaonekana kuwa nzuri. Kiuhalisia hali ya uchumi ni mbaya kwenye maisha ya watu. Kila kona wanalia hali ngumu, hakuna fedha.

Watu wanakabiliwa na mikopo, wamefunga biashara zao kwa kushindwa kurejesha fedha waliyokopa kwenye taasisi mbalimbali zikiwamo benki. Imefikia hatua wameamua kufunga biashara zao na hivyo kuathili hata mzunguko wa kifedha.

Mzunguko wa fedha umekuwa siyo mzuri na hautabiriki matokeo yake wanazodaiwa fedha wameshindwa kulipa. Hali ikiendelea kama ilivyo kwa siku zijazo ni ngumu kwa Watanzania, wengi watashindwa kusomesha watoto wala kupata mahitaji ya msingi ya chakula.