Azma Mponda: Msomi anayeamini mafanikio yapo kwenye muziki

Muktasari:

Azma Mponda ni miongoni mwa wasanii walioamua kubadilika akisema kabla ya kutoka kwenye kundi la Tamaduni hakuona umuhimu wa kufanya hivyo kulingana na mazingira waliyokuwa wamejiwekea.

Dar es Salaam. Mabadiliko katika sekta ya burudani yameenda mbali zaidi na muziki wa Hip Hop ukibebwa na wimbi hilo.

Dume Suruali, Muziki, Kemosabe, Sumu, OG, Sweet Mangi, Mungu  na Astara Vaste.

Azma Mponda ni miongoni mwa wasanii walioamua kubadilika akisema kabla ya kutoka kwenye kundi la Tamaduni hakuona umuhimu wa kufanya hivyo kulingana na mazingira waliyokuwa wamejiwekea.

Kwa nini alitoka Tamaduni Music?

Anasema ilifikia kipindi hata walipokuwa wakifuatwa na waandishi wa habari hawakuwa tayari kuzungumza nao kwa madai ya kufanya Hip Hop ya harakati ya chini kwa chini.

Anafafanua kuwa baada ya muda alihisi anapotea na kuamua kuachana nao kwa sababu Dunia haiwezi kumtambua mtu kama hajajitambulisha.

“Niliona kabisa nahitaji kutoka nje, kuachia ngoma kwenye mitandao. Kuachia ngoma mpya kadri niwezavyo, ndiyo sababu hasa iliyonitoa Tamaduni.

Azma ni nani?

Anasema hajaanza muziki leo wala jana , kwani tangu mwaka 2008 alikuwa tayari amefanya kazi nzuri na za maana ikiwamo  “Kipimo cha Penzi”,

Anasema wanaojua muziki anaoimba wanaukumbuka wimbo huo na jinsi ulivyofanya vizuri.

Anawataja baadhi ya wasanii waliowahi kuusifia wimbo huo kuwa ni pamoja na Belle 9  aliyetamka wazi kuwa Azma ni mwimbaji mwenye uwezo wa kuandika nyimbo za mapenzi, na msanii Chindo alidiriki kumfananisha na mwanamuziki LL cool J wa Marekani.

Anasema siyo jambo rahisi kwa mwimbaji mkongwe kama Profesa J kukubali kazi zako, lakini kwake hilo limeshafanyika.

Anazikubali kazi zake zipi?

Azma anasema pamoja na kuwa na kazi nyingi na bora kama “Astara Vaste”, anazikubali zaidi “Utata wa Katiba” na  “Jinsi ya Kumfikisha Mpenzi”.

Anasema wimbo uliomng’arisha zaidi kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kufikisha watazamaji milioni moja kwenye mtandao wa Youtube (kwa wakati huo kabla ya Darasa alikuwa msanii wa kwanza wa Hip Hop kufikisha watizamaji hao), kutokana na ujumbe uliomo.

Kwa nini aliimba mapenzi?

Anasema kwa uelewa wake aligundua wanandoa wengi wanahitaji elimu ya uhusiano, hivyo kupitia kalamu na sauti yake akaamua kuwaelimisha kidogo.

Anafafanua kuwa tofauti na matarajio yake wimbo huo ulipokelewa vizuri na mashabiki, licha ya kuiachia mtandaoni na anaamini wengi walijifunza.

Hip Hop kwa nini inahitaji mabadiliko

Anasema kuwa wasanii wa hip hop wanaimba nyimbo ngumu na za harakati, hivyo wanahitaji mabadiliko wakiangalia zaidi   mashabiki wanataka nini.

 Anasema mashabiki wanataka vitu laini ambavyo vitakaa vichwani mwao na mabadiliko yanahitajika ili tufike tunapopataka.

Anafafanua kuwa kuna aina nyingi za harakati ambazo zinaweza kuwa kivutio kwa wasikilizaji na zikafikisha ujumbe, badala ya kung’ang’ania vitu vigumu vinavyokosa mashabiki.

Anaeleza kufanya vitu vigumu, kufanya mapambano kwenye nchi isiyokuwa na machafuko ni ngumu kuvutia mashabiki na ndiyo maana wasanii wa muziki huo wanaotea nyimbo moja na kupotea.

Kwa nini ameweka shahada kabatini?

Azma anasema licha ya kusoma shahada ya usimaizi wa fedha, hajaona haja ya kuifanyia kazi kwa sababu anaamini katika muziki.

Anasema kama muziki ukikaa vema anaweza kuifanyia kazi shahada yake kupitia muziki.

Analielezea hilo kuwa kuna wasanii wanaofanya vizuri wanalazimika kuajiri watu wa mahesabu, hivyo akifika hatua hiyo hatakuwa na haja ya kumuajiri mtu.

Anasema tangu akiwa mdogo hakuwa na hamu ya kuajiriwa wala kufikiria kufanya hivyo zaidi ya kujiajiri.