MAONI YA MHARIRI: Serikali na Bunge wakutane, wajadili hili la Dk Kafumu, Kamata kujiuzulu

Muktasari:

Juzi, akiwa bungeni Dodoma, Dk Kafumu ambaye pia ni Mbunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuona kuna mwingiliano mkubwa wa majukumu yao kiasi cha kushindwa kutimiza malengo waliyokusudia.

Kwamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Dk Peter Kafumu na makamu wake, Vicky Kamata, wamejiuzulu nafasi zao kwa kile walichoeleza kuwa Serikali inaingilia majukumu yao, ni jambo ambalo limetushtua.

Juzi, akiwa bungeni Dodoma, Dk Kafumu ambaye pia ni Mbunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuona kuna mwingiliano mkubwa wa majukumu yao kiasi cha kushindwa kutimiza malengo waliyokusudia.

Bila kuingia kwa undani wa sababu za kuchukua hatua hiyo, Dk Kafumu alisema tangu achaguliwe, amekuwa akifanya kazi kwa uzalendo na wakati wote amekuwa na mawazo ya kuipeleka mbele Tanzania na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa viwanda, lakini akasema amekuwa akikutana na vikwazo vikubwa ambavyo vimekuwa vikimtoa nje ya mikakati hiyo na kujikuta akiyumba na kushindwa kufikia malengo yake.

Hatua ya viongozi hao imeibua maswali na minong’ono mingi juu ya kuingiliana kwa mihimili ya dola nchini.

Mwezi uliopita, tuliandika tahariri tukitaka mihimili hii ya dola kila mmoja utimize majukumu yake yaliyoainishwa vizuri kikatiba ili kuhakikisha kuwa hakuna mwingiliano kati yao.

Mihimili hii; Serikali ambayo wajibu wake wa ufupi ni kuendesha utawala na utekelezaji wa kila siku wa shughuli za umma, Bunge ambalo lina wajibu wa kuisimamia Serikali na kutunga sheria na Mahakama yenye wajibu wa kusikiliza na kuamua kesi na pia kutoa tafsiri ya sheria na Katiba ya nchi, inapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana lakini kila mmoja kwa uhuru wake. Chombo kimoja kisiingilie kazi za kingine.

Malalamiko ya kuingiliana kwa mihimili, kama tulivyoeleza inaelekea kushika mizizi na kwa siku za karibuni, kulitokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wabunge kuwa Serikali imekuwa ikiwakamata baadhi yao bila kufuata taratibu yaani bila kupitia ofisi ya Spika huku wakiilalamikia Mahakama kwamba imeshindwa kutoa dhamana kwa baadhi yao licha ya kuwa makosa wanayoshtakiwa kutoa fursa hiyo.

Baada ya hapo ukazuka mgogoro mwingine kati ya wabunge na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye anatuhumiwa kuwakashifu wabunge kuwa wakati mwingine hukosa cha kuzungumza na ndiyo maana husingizia bungeni.

Kauli hiyo ya Makonda ilitokana swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata ufafanuzi wa mali zake baada ya kutuhumiwa bungeni na Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’, aliyedai mkuu huyo wa mkoa anatumia gari aina ya Lexus lenye thamani ya Sh400 milioni, amekarabati ofisi yake kwa Sh400 milioni bila kufuata utaratibu wa ununuzi wa umma, ana gari aina ya Toyota V8 na amejenga maghorofa kwa mwaka mmoja tu.

Tulieleza katika tahariri yetu mwezi uliopita kwamba mizozo hii ya mihimili inaweza kuonekana kama midogo, lakini ukweli ni kwamba inakua na hili lililojitokeza juzi ni ushahidi wa kukua kwake.

Hivyo tunashauri kwamba pamoja na mambo mengine, kilichowafanya Dk Kafumu na Kamata kujiuzulu kijadiliwe na kufanyiwa kazi ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mihimili hii inapaswa kujua kwamba yote inajenga nyumba moja hivyo hakuna sababu wala haja ya kugombea fito.