Msiba wa mbunge Macha ulivyowafunda wabunge wa CCM, wapinzani

Muktasari:

Kauli hii ya Mbowe ambayo iliungwa mkono na viongozi na wabunge kadhaa, ilimaanisha jambo kubwa nyuma yake, alikuwa akimaanisha upo mpasuko miongoni mwa wabunge uliotokana na itikadi zao.

“Msiba huu uwe funzo kwetu sote kwamba tunahitajiana, urafiki huu usiishie leo, bali uwe somo kwetu katika maisha yetu ya kila siku,” hiyo ni kauli ya Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani wakati wa kumuaga mbunge wa Viti Maalumu, Marehemu Dk Elly Macha.

Kauli hii ya Mbowe ambayo iliungwa mkono na viongozi na wabunge kadhaa, ilimaanisha jambo kubwa nyuma yake, alikuwa akimaanisha upo mpasuko miongoni mwa wabunge uliotokana na itikadi zao.

Tofauti na ilivyokuwa kwenye mkusanyiko wa juzi msibani, kila wakati wabunge wakikaa wamekuwa wanalumbana kulingana na masilahi ya vyama vyao lakini juzi waliunganishwa na msiba.

Mbowe anasema kifo cha Dk Macha kinapaswa kuwaunganisha na kuwakumbusha wote kuhusu safari ya mwisho ya mwanadamu na namna anavyotakiwa kuishi hapa duniani.

“Alikuwa ni zaidi ya mtu na aliweza kujitoa kwa ajili ya wengine na hasa wenye mahitaji bila ya kujali kwamba alikuwa ni mlemavu, hakika kifo chake ni pigo kwa familia pamoja na chama chetu cha Chadema kwani alikuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu,” anasema Mbowe.

Kifo chake

Dk Macha alifariki dunia Machi 31, mwaka huu katika Hospitali ya New Cross nchini Uingereza, alikokwenda kwenye matibabu ya ugonjwa wa kupungukiwa damu.

Mwili wa mbunge huyo uliwasili nchini Aprili 20 katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kabla ya kupelekwa Dodoma juzi, na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwake mkoani Arusha kabla ya kupumzishwa katika Kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Mbali na Mbowe, wabunge na viongozi waliopata nafasi ya kutoa salamu zao za rambirambi walisema kuwa kuna umuhimu wanasiasa hao kuungana wakati wote.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alizungumzia suala la umoja miongoni mwa wabunge huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akifafanua kuwa hakuna ubaguzi wowote kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba ambayo Dk Macha alikuwa mjumbe, alisema kila mara aliposimama bungeni kuchangia hakuzungumzia kuhusu vyama.

“Tunaletwa na vyama (bungeni), tupendane na tunapokuwa na mambo magumu hatutakiwi kukata tamaa.

Kauli ambayo iliungwa mkono na Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza ambaye anasema Dk Macha alikuwa mchapakazi na hakuwa na majungu.

INAENDELEA UK26

INATOKA UK25

“Alikuwa hazungumzi mambo ya vyama na ilikuwa vigumu sana kugundua kuwa ni mpinzani (mbunge kutoka upinzani) alikuwa si mbunge anayebishana katika mambo ambayo si ya msingi kama wengine, alikuwa mbunge wa Tanzania,” anasema.

Elimu na upofu

Mbali na ushirikiano na umoja bila kujali itikadi, msiba huo ulitoa funzo jingine kutafuta elimu bila kuchoka wala kujali vikwanzo ambavyo havina maana.

Elimu aliyoipata Dk Macha hadi ngazi ya uzamivu huku akiwa mwanamke mwenye changamoto ya ulemavu wa kutokuona ilikuwa moja ya sifa lukuki alizopewa wakati wa salamu za rambirambi.

Enzi za utoto wake, mbunge huyo aliugua ugonjwa wa surua ambao ulisababisha apoteze uoni wake hadi mauti yanamkuta. Hata hivyo kutoona hakukumzuia kupata elimu hadi ngazi ya Shahada ya Uzamivu.

Elimu hiyo, unyenyekevu na kutojikweza, vilimpa mbunge huyo fursa ya kupata nafasi mbalimbali na amekuwa akitoa mchango wenye hoja katika maisha yake mafupi ya ubunge tangu aapishwe 2015.

Wanavyomkumbuka

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai, anasema Dk Macha hakuwahi kumkwaza yeyote katika kambi yao kwenye Bunge la 11.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ambaye anasema amejifunza unyenyekevu kutoka kwa Dk Macha.

“Kwa umri aliokuwa nao kama tulivyosikia katika historia yake, angetaka kufanya kiburi angeweza kufanya hivyo lakini alikuwa ni msikivu, mnyenyekevu,” anasema Dk Tulia.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake nchini (TWPG), Margaret Sitta anamzungumzia kuwa mpiganaji wa haki za wanawake na watu wenye ulemavu.

“Alikuwa mtu mwenye kuwatetea watu wenye ulemavu, haki zao na wajibu wao. Alisema kweli, tumepata pengo tulikuwa wabunge wanawake 145 sasa tumebaki 144,” anasema Sitta.

Anasema wamepoteza mtu mahiri na mwenye mchango kwa jamii, kuthubutu na ujasiri na kuwataka wabunge kupendana, kufanya mambo yenye manufaa kwa Taifa na yanayompendeza Mungu.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Mollel anasema yeye na wabunge wenye ulemavu wamepata pigo kwa sababu licha ya changamoto za ulemavu na tofauti za kiitikadi, waliungana pamoja kuhakikisha kuwa wanatetea haki za watu walemavu.

“Ili kumuenzi marehemu Dk Macha tuhakikishe yale yote aliyokuwa akiyasema yanatekelezwa,” anasema Amina.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wabunge washikamane wakati wote na isiwe katika misiba pekee.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anasema ulemavu haukuwahi kuwa kikwazo kwa Dk Macha kwani aliweza kufanya jambo lolote lilokuwa ndani ya uwezo wake.

“Dk Macha alipenda sana elimu na hakutaka changamoto yoyote katika maisha yake iwe kizuizi cha kufikia ndoto zake,” anasema Msigwa.

Mbunge huyo alijitoa kuwatetea watu wenye ulemavu na miongoni mwa maswali yake ambayo yatakumbukwa katika kipindi chake alichokuwapo bungeni ni swali la papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mei 2016.

“Tanzania ilisaini mkataba wa kimataifa wa mwaka 2006 kuhusu haki za watu wenye ulemavu, utaratibu ni kwamba baada ya miaka miwili baada ya kuridhia Serikali inatakiwa kuandika State Report (ripoti ya nchi), kwanini Serikali haijapeleka hiyo ripoti hadi leo kuhusu watu wenye ulemavu?” alihoji Macha.

Akijibu Majaliwa alisema, “Serikali yetu imedhamiria kufungua milango na kutoa huduma na kuwafanya ndugu zetu wenye mahitaji maalumukuwa ni sehemu ya wachangiaji wakubwa wa shughuli za kimaendeleo nchini.”

“Mikataba hii baada ya kuwa tumeunda Serikali yetu tutafanya mapitio ya kazi zote za awamu ya nne ambazo zilikuwa zimefikiwa na tuweze kuunganisha mkakati ambao Rais ameuweka ikiwa ni pamoja na hili ambalo Dk Macha umelieleza.

“Nikuhakikishie, kwa kuwa tayari tunaye Waziri mwenye dhamana ya watu wenye mahitaji maalumu basi wakati wowote kuanzia sasa jambo hili litakamilika na nimtake Dokta Abdallah Poss aanze mchakato wa kuwakusanya wadau wote ili tuanze kuyapitia mahitaji hayo.”